Header Ads

MAAMUZI MABOVU YA VIONGOZI WETU NI MATOKEO YA KUTOFIKIRI SAWA SAWA!



Na Happiness Katabazi

MAPEMA mwaka huu Rais Jakaya Kikwete alisema tunaingia mikataba mibovu kutokana na kukosa wataalamu wazuri.

Tunao ushaidi wa kutosha wa kuonyesha serikali yetu ni bingwa na mahiri katika kuingia mikataba kadhaa iliyoiletea na inayoendelea kuliletea hasara kubwa taifa hili.

Mikataba kama ya Valambhia, IPTL, rada, ndege ya Rais, ununuzi wa benki ya NBC, mkataba wa mauzo ya mashamba ya sukari ya Kilombero na Richmond yenye kampuni dada sasa iitwayo Dowans.

Sasa tunaweza kusema Tanzania tumebobea na ni magwiji hasa katika uingiaji/upitishaji mikataba mibovu. Wanasheria wakuu wa serikali kwa awamu zote zilizopita na sasa hawajawai kutetea katika hili kwa kuwa mikataba yote kabla serikali haijaingia taasisi hiyo inashirikishwa kikamilifu.

Kwa hiyo Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba na viongozi wetu wapo kimya katika hilo na ukimya huo labda unaashiria kukubali kauli ya Rais Kikwete aliposema kwamba tunaingia mikataba mibovu kutokana na kukosa wataalamu.

Lakini mikataba hii imetokana na sera ya chama kinachotawala hapa nchini CCM, na chama hicho hakijawahi kusema kwamba mikataba hiyo mibovu imo kwenye sera zake au Ilani yake za uchaguzi.

Rais Kikwete na viongozi wengine wa serikali pia hajawahi kusema mikataba hiyo ni mibovu au ina dosari zozote. Kwa hiyo inawezekana kabisa kwamba ubovu uliomo ndani ya mikataba hiyo unatokana na sera zenyewe za chama kinachotawala zisizokidhi haja.

Kwa kuwa kuna Watanzania waliokwishawahi kukosoa mikataba hiyo, basi ni lazima tukubali kwamba kama CCM na serikali yake vinaongozwa na watu makini, basi dosari hizo zingesahihishwa.

Lakini kwa vile hayo hayakutokea na kwa sababu hakuna dalili za masahihisho kufanywa kwa siku za usoni, lazima tutilie shaka uwezo wa viongozi wa CCM na serikali kufikiri.

Tuna shaka kwamba huenda baadhi ya viongozi wetu wana kasoro - ama hawafikirii sana kesho kutatokea nini au wanaweka maslahi yao mbele kuliko ya taifa. Na hapo moja kwa moja panagusa maradhi makubwa yaliyo na yanayowatafuna viongozi wengi - rushwa.

Na hapa ndipo ninapokumbuka usemi wa waziri mstaafu Arcado Ntagazwa alioutoa bungeni Dodoma, mwaka 1993 alipokuwa mbunge wa Jimbo la Kibondo. Alisema: “Tutakapokufa vizazi vijavyo vitafukua makaburi yetu ili vione vichwa vyetu viongozi vilikuwa na ubongo wa aina gani kwa sababu yaelekea hatufikiri sawa sawa,” mwisho wa kunukuu.

Ntagazwa alilazimika kutoa kauli hiyo baada ya kuona kwamba baadhi ya maamuzi yanayofikiwa na serikali hayana maslahi kwa taifa, na ni ya kibinafsi. Nampongeza kwa kauli hiyo na ninaamini kuwa ipo siku vizazi vijavyo si tu kwamba vitafukua makaburi kutazama ubongo, bali pia vitatulaani.

Tusipokuwa wakali katika kujadili hoja ya utawala mbovu tulionao hivi sasa tutakuwa tunashiriki au kujihusisha katika kero hii ya kuwa na viongozi wanaotoa maamuzi kama watu wenye mtindio wa akili.

Hivi Tanzania itakuwa kichekesho hadi lini? Kwa nini utawala wetu ni wa kubabaishababaisha tu na kamwe hatuoni uongozi unaotuletea tija na maendeleo?

Inakuwaje Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, Rais wa nchi inayotawala na kumiliki migodi yetu ya dhahabu na tanzanite, atusute kuwa sisi ni wazembe wa kufikiri na tuone kwamba ametusifu?

Rais Mbeki alipozungumzia madini ya tanzanite alisema japo biashara ya tanzanite inatoa dola milioni 500 kwa mwaka duniani, Tanzania, nchi pekee duniani yenye madini hayo, inapata dola milioni 80 tu.

Aliuliza kwa nini tunamtafuta mchawi wakati sheria ya uchimbaji madini tumeitunga wenyewe inayoruhusu wageni waondoke na asilimia kubwa ya madini hayo?

Sasa kwa hakika bila kufichana ukweli, baadhi ya viongozi Tanzania na wataalamu wake ni bomu na wengine kati yao wanafikiria ama kughushi vyeti ama kuwaibiwa walipa kodi kwa kuingia mikataba ‘feki’.

Hawa hawafikirii kamwe maslahi ya nchi yetu, kwani hata walipoambiwa na Chama cha Wanasheria nchini wasiridhie mabadiliko ya mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa mabadiliko hayo hayana maslahi ya taifa, hawakujali wala kusikiliza.

Waliitana kama Kamati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuamua kuridhia mkataba huo kulingana na sera za chama chao bila kufikiria kutatokea nini baadaye.

Kudumaa huku kwa fikra kumetufikisha mahali pabaya na sasa taifa letu linayumbishwa bila wananchi kupewa fursa kuzuia jambo hilo.

Hiyo ndiyo gharama na matokeo ya kuongozwa na viongozi na wataalamu wasio na chembe ya uzalendo wa nchi yao. Huenda hawafikiri sawasawa kwa sababu kiongozi mwenye uzalendo wa kweli na yupo kwa ajili ya Watanzania wenzake anaweza kukubali kuliingiza taifa kwenye mikataba mibovu kila kukicha.

Mungu ibariki Afrika, Mungu inusuru Tanzania

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili April 22,2007

No comments:

Powered by Blogger.