Header Ads

MTUHUMIWA EPA ASHINDWA KUFIKISHWA MAHAKAMANI KWA MARA NYINGINE

Na Happiness Katabazi

KWA mara ya pili sasa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana imejikuta ikishindwa kuendelea kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya wizi wa sh milioni 207 katika Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu kwa sababu mshtakiwa wa tano katika kesi hiyo, Bosco Kimela, ameshindwa kuletwa mahakamani hapo na Jeshi la Magereza kwa sababu zisizojulikana.


Kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi, Ignas Kitusi, anayesaidiwa na Eva Nkya na John Utamwa juzi na jana walilazimika kuahirisha kusikilizaji kesi hiyo kwa sababu mshtakiwa huyo ambaye yuko mahabusu ameshindwa kuletwa mahakamani hapo na Jeshi la Magereza licha ya jopo hilo kuandika hati ya kutaka aletwe mahakamani.

Hakimu Mkazi Kitusi alimsikiliza kwa makini Wakili Mwandamizi wa Serikali, Fredrick Manuyanda, aliyesema wao walikuwa tayari kuendelea na kesi hiyo licha ya mshtakiwa huyo kwa mara nyingine kushindwa kuletwa mahakamani hapo.

Katika hilo, hakimu huyo alilazimika kumuita askari mmoja wa Jeshi la Magereza na kumhoji ni kwa nini mshtakiwa huyo hajaletwa mahakamani.

Askari huyo alimjibu kuwa hafahamu ni kwa nini; na wala hati iliyotolewa na mahakama juzi ya kulitaka jeshi hilo limlete mshtakiwa jana hakukabidhiwa yeye.

“Hili tatizo liko juu ya uwezo wetu, yaani mahakama na upande wa mashtaka na utetezi, hivyo kwa mara nyingine naiahirisha kesi hii ambayo ilipangwa kusikilizwa kwa siku nne mfululizo kuanzia juzi hadi Aprili mosi, na ninauamrisha upande wa mashtaka ulete mashahidi wake siku hiyo ya Aprili Mosi,” alisema Utamwa.

Mbali na Bosco ambaye alikuwa katibu wa BoT wengine ni Rajabu Maranda na Farijala Hussein ambao ni wafanyabiashara; maofisa wa BoT ni Iman Mwakosya na Ester Komu ambao wanatetewa na Majura Magafu, Ademba Agomba na Gabrile Mnyele.

Wakati huo huo, upande wa utetezi katika kesi ya wizi wa sh bilioni 3.9 katika akaunti ya EPA inayomkabili mfanyabiashara maarufu nchini Jayantkumar Patel na wenzake watatu jana uliwasilisha ombi la kutaka mahakama hiyo itoe amri ya kusimamisha usikilizaji wa kesi hiyo hadi ombi Na.3/2010 la mapitio ya uamuzi uliotolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Semistocles Kaijage, litakapotolewa uamuzi na Mahakama ya Rufani nchini.

Ombi hilo liliwasilishwa jana na wakili wa utetezi Martin Matunda ambaye alidai upande wa utetezi haujaridhishwa na uamuzi wa Jaji Kaijage ambao alitoa amri ya kurudishwa majarada ya kesi nne zinazowakabili washtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kesi hizo ziendelee kama kawaida kwa sababu amebaini kwamba maombi ya utetezi yanafanana na kesi ya Kikatiba waliyofungua washtakiwa hao dhidi ya Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginard Mengi, DPP na AG.

“Kwa sababu hatujaridhishwa na uamuzi huo wa Jaji Kaijage ndiyo maana tayari tumeishawasilisha ombi katika Mahakama ya Rufani nchini la kutaka mahakama hiyo ipitie upya uamuzi wa Mahakama Kuu na wakati mchakato huo ukiendelea tunaiomba mahakama hii itoe amri ya usikilizwaji wa kesi ya msingi iliyopo mahakamani hapa hadi Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi wake,” alidai Matunda.

Hata hivyo kwa upande wake wakili wa serikali, Manyanda, alidai hakuwa amejiandaa kujibu hoja hizo na akaomba apewe muda lakini hata hivyo wakili Matunda alisema kuwa hoja hiyo haina nia njema kwani Septemba 21 na Septemba 25 mwaka jana, waliwasilisha maombi ya aina hiyo mbele ya mahakimu hao hao na mawakili hao hao wa serikali hivyo haoni sababu ya wakili huyo kutaka apewe muda wa kwenda kutafuta hoja.

Hata hivyo Hakimu Kitusi aliutaka upande wa mashtaka ulete hoja zake Aprili mosi mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Machi 31 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.