Header Ads

KESI YA KAKOBE YAZUA MAZITO

Na Happiness Katabazi

KESI inayomkabili Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zakaria Kakobe, imechukua sura mpya baada ya mama mzazi wa Jaji Agustine Shangwa anayesikiliza shauri hilo kumvaa mwanaye na kumtaka ajieleze kwa nini amekataliwa na walalamikaji.


Jaji Shangwa alisema kesi hiyo imemletea mzozo na mama yake mzazi anayeishi Bukoba ambaye baada ya kusoma taarifa za kukataliwa kusikiliza shauri hilo zilizochapishwa na gazeti moja la kila siku (sio Tanzania Daima), alimpigia simu na kumhoji kwa nini hawatendei haki walalamikaji.

Alidai kuwa kitendo cha walalamikaji kukimbilia katika vyombo vya habari hakikuwa cha kistaarabu kwa kuwa yeye katika kesi hiyo ni mshauri tu na sio msikilizaji.
Pamoja na kutoa siri hiyo, Jaji Sangwa amechukua uamuzi mwingine mzito wa kukataa kujitoa katika kesi hiyo kama alivyotakiwa na walalamikaji waliodai kutokuwa na imani naye kwa vile alionyesha upendeleo kwa mshtakiwa.

“Jamani mimi nilikuwa nikiwashauri tu nyie walalamikaji lakini mkaenda kwenye gazeti hilo na sijui na kwa watu gani wengine kulalamika kuwa siwatendei haki, hadi mama yangu akaniuliza, sasa nendeni mkaseme tena kuwa leo nimerudia kutowatendea haki, maana hao waandishi wana vinasa sauti vinarekodi kila kitu,” alisema Jaji Shangwa na kusababisha watu kucheka.

Akieleza sababu za kugoma kujitoa, Jaji Shangwa alisema walalamikaji wameshindwa kutoa hoja za maana ambazo zingeweza kumfanya ajiondoe kwenye kesi hiyo.

Jaji Shangwa alitoa uamuzi huo mwishoni mwa wiki akisema amefikia uamuzi huo wa kukataa kujiondoa kwenye kesi hiyo kwa kuwa yeye si msikilizaji bali ni msuluhishi.

“Msisononeshwe na uamuzi huo, mimi ni Jaji Msuluhishi tu katika kesi hii na si Jaji Msikilizaji. Hivyo kama usuluhishi wa kesi hii ukishindikana jalada litarudishwa kwa Jaji Mfawidhi ili ampange jaji mwingine wa kuisikiliza kesi hii,” alisema Jaji Shangwa.

Walalamikaji katika kesi hiyo ya tuhuma za ubadhirifu wa mali na pesa zaidi ya shilingi bilioni 14 pamoja na ukiukwaji wa katiba ya kanisa hilo, Dezedelius Patrick, Angelo Mutasingwa na Benedict Kaduma walimtaka Jaji Shangwa ajiondoe mwenyewe katika kesi hiyo kwa madai kuwa hawana imani naye.

Walalamikaji hao walimwandikia barua Msajili wa Mahakama Kuu Dar es Salaam, Agosti 26, mwaka huu, wakimtaka Jaji Shangwa ajiondoe mwenyewe katika kesi hiyo wakidai kuwa amekiuka maadili ya kitaaluma, taratibu na heshima ya mahakama na ameonyesha upendeleo kwa mlalamikiwa.

Wanadai kuwa mlalamikiwa hakuwasilisha maelezo yake ya maandishi (WSD) ndani ya siku 21 na kwamba siku ya kutajwa kwa kesi hiyo wakili wake Miriam Majamba alitoa sababu za uongo lakini jaji hakutilia maanani na badala yake Agosti 2, 2011 yeye alitoa hukumu dhidi yao wakati kesi hiyo haijafikia hatua hiyo.

Walalamikaji hao wanadai maneno ya jaji huyo yalikuwa na upendeleo wa waziwazi kwa Kakobe. Katika ushauri wake katika kesi hiyo, jaji huyo alisema, “Nyie walalamikaji nasema bila kumung’unya maneno kuwa madai yenu yote ni majungu… Kakobe ni mungu wa kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, kanisa ni mali yake… kwa hiyo kama anakula fedha za kanisa anakula fedha zake, hakuna wa kumhoji kwani lile ni kanisa lake na ni mali yake,” alisema.

Walalamikaji hao wananukuu maneno ya jaji huyo aliyedai: “Kakobe atawashinda kesi hii na kuwadai pesa nyingi, kwa hiyo futeni kesi, kama na ninyi mnataka kaanzisheni makanisa yenu, uaskofu wake alijipa mwenyewe sio kama makanisa mengine wanaosomea.”
Kwa mujibu wa hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani, walalamikaji hao wanamtuhumu Kakobe kuwa amekuwa akikusanya fedha kutoka kwa waumini wake kwa madai ya kufanyia shughuli na miradi mbalimbali ya kanisa na kuzitumia isivyo halali.

Mbali na kufuja fedha hizo kama vile kugharamia kampeni za kisiasa, pia wanadai kuwa amekuwa hatoi taarifa ya mapato na matumizi ya fedha anazozikusanya.
Miongoni mwa madai hayo ni makusanyo ya shilingi milioni 800 kwa ajili ya kununulia vifaa vya kuanzisha televisheni.

Hata hivyo wanadai kuwa badala yake Kakobe anadai kuwa vifaa hiyo amevirudisha Marekani alikovinunua kwa kuwa eneo la mradi huo limeathiriwa na mradi wa umeme wa msongo mkubwa na kwamba kwa sasa anataka kuhamia jijini Boston Marekani.

Kuhusu ukiukwaji wa katiba ya kanisa hilo, walalamikaji hao wanadai kuwa katiba inataka kuitishwa kwa mkutano mkuu kila baada ya miaka mitano ambacho ndicho chombo cha juu cha maamuzi lakini Kakobe hajawahi kuitisha mkutano huo tangu mwaka 1989.

Pia wanadai kuwa katiba hiyo inataka kanisa liwe na Katibu Mkuu na Mweka Hazina ambao ndio watakaolinda mali za kanisa lakini Kakobe amekuwa akifanya maamuzi na shughuli zote peke yake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Oktoba 24 mwaka 2011.

No comments:

Powered by Blogger.