Header Ads

MTIKILA NILIKUPENDA NAWE ULINIPENDA



Na Happiness Katabazi

OKTOBA 4 Mwaka huu, saa mbili asubuhi Nikiwa nyumbani Sinza Dar Es Salaam,nilipigwa simu na Mwandishi wa Gazeti la Habari Leo,Regina Kumba ambaye akitaka kuthibitisha taarifa alizozisikia Kuwa swahiba wangu  Mwenyekiti wa Chama cha Democraty(DP),Mchungaji Christopher Mtikila Kuwa amefariki kwa ajali zina ukweli kwasababu Mtikila ni mtu wa karibu yangu sana.

Mtikila tulimpachika jina la 'KANA KWAMBA' kwasababu ukifuatilia maongezi yote ya Mtikila akiwa anazungumza lazima utamsikia akitumia neno 'KANA KWAMBA'. 

Nilishtuka,nikamjibu sina taarifa hizo ila nikamtaka asubiri nimpigie simu Mtikila.

Kweli nilipiga simu za Mtikila zote mbili za Voda na Tigo zote zikawa hazipatikani lakini Nikaendelea kujipa moyo Kuwa uenda Mtikila amezima hizo simu kwasababu labda anaendesha Ibada kanisani kwake.

Nikaamua kupiga simu ya Mke wake Georgia Inaitaji bila majibu.Ghafla nikaanza kupokea simu na ujumbe wa pole kutoka kwa watu Mbali wakiwemo waandishi wenzangu wa Habari wakinipa pole na kunitania Kuwa ndiyo tayari nimeishakuwa mjane Mume wangu Mtikila amefariki kwa ajali.

Bado sikutaka kuamini hadi pale nilipotumiwa taarifa ya Televisheni TBC 1 ,Ikimnukuu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani akithibitisha Kuwa ni kweli Mtikila amefariki.

Nilikuwa chumbani na mwanangu Queen ,nilipatwa na uchungu Mkali sana na donge kunikaba Kwenye Koo huku nikizunguka zunguka humu ndani bila Sababu za Msingi nikarudi chumbani nikaanza kulia kwa uchungu nisijue nifanye nini ?

Na baada ya kukutwa Hali hiyo Mbaya ambayo ilisababisha nisiende kanisani nilifika uamuzi wa kwenda nyumbani kwa marehemu Mtikila Mikocheni karibuni na Shule ya Msingi Ushindi Dar Es Salaam, ili nijiridhishe tena Kuwa kweli amekufa swahiba wangu Mtikila?

Saa nne asubuhi siku hiyo ya Oktoba 4 Mwaka huu,nilifika nyumbani kwa Mtikila,wakati anaingia ndani ya geti kulia Kwangu ndiyo Bendera ya Tanganyika uwa imesimamishwa pale siku zote,nikaona imeshushwa nusu mlingoti.

Na nikaingia ndani Moja kwa Moja nikatokea uwani Ndipo nilipo mkuta Mke wa Marehemu Mtikila,Georgia akiwa amesimama kashikilia kitenge analia huku kasimama analazimisha tu mpeleke alipo mume wake Mtikila ambae katika mapenzi yao walikuwa wakiitana 'Darking'.

Nililia pamoja na Mama Mtikila alinikumbatia maana ananifahamu sana.Mimi pamoja na  wanawake wengine na Naibu Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge na watu wengine tuli mbembeleza sana mama Mtikila ambaye alikuwa Kama Mithili ya mtu aliyerukwa na akili aingie ndani akae alikataa alisema akiingia ndani inamaanisha ni kweli mume wake amefariki Dunia anachotaka tumlete Mtikila pale nyumbani  muda ule au tu mpeleke alipo Mtikila akamuone ama sivyo hatoingia ndani Kamwe na ataendelea kulia huku amesimama.

Kama mnavyomfahamu Georgia naye ni Mtu mwenye misimamo mikali  ,kweli kwa zaidi ya saa nne alikuwa analia kwa kupiga mayowe huku akiwa amesimama uwani  hukum akisikika akisema:

' Mume wangu Mtikila alikuwa akidekeza,akinipenda...
leo amefariki nani atanidekeza? Leo nipo Tayari nilie nionekane Kituko na Happiness Katabazi mwanangu endelea kunipiga picha misijali hata nikioneka  chizi ,sawa...mi namlilia Darling wangu Mtikila....nani atanidekeza tena yooooo' alisema Geogia Mtikila.

Geogia aliendelea kuweka mgomo wa kulia huku akiwa amesimama,kuto ingia ndani kwake wala kuingia chumbani kwake hadi saa nane mchana hali iliyosababisha niende walipokuwa wameketi wanaume waliokuwa wamekaa na Naibu Meya Songoro Mnyonge nikatoa wazo la ama afungwe Kamba aingizwe ndani kwa Nguvu,achomwe sindano ya usingizi au apelekwe  Katika Hospitali ya Tumbi - Kibaha akaione hiyo maiti ya mume wake ili aache kulia sana.

Kweli wanaume wale zaidi ya saba wakiongozwa na Songoro wakainuka na kwenda uwani alipokuwa amesimama Mke wa Mtikila  tangu asubuhi akilia mithili ya mtu  aliyerukwa na akili wakambeleleza aingie  ndani aka wagomea.

Ndio  ikabidi itumike mbinu ya tatu ambapo Mzee mmoja akalazimika  kutoa Gari lake lim peleka Mke wa Mtikila , Geogia  na baadhi ya wanawake watatu Katika Hospitali ya Tumbi - Kibaha ,Mkoani Pwani, ili akashuhudie maiti ya mume wake .

Na kweli alipopanda katika Hilo Gari kuelekea Hospitali ya Tumbi ,Kibaha Majira ya saa nane mchana ndipo alipoacha kulia na walianza safari ya kuelekea Tumbi Hospitali , wakiwa wametuacha baadhi ya Kwenye msiba   ambapo baadae viongozi Mbalimbali walifika msibani hapo akiwemo Msajili wa Vyama Vya Siasa nchini,Jaji Francis Mutungi.

Baadhi ya Waandishi wa habari Mtikila tulimpachika jina la 'KANA KWAMBA' kwasababu ukifuatilia maongezi yote ya Mtikila akiwa anazungumza lazima utamsikia akitumia neno 'KANA KWAMBA'. 

Aidha Enzi za Uhai wake Mtikila tukasalimiana naye alikuwa akipenda kutumia salamu ya Chama Chake CHA DP, alikuwa akisema hivi ( saa ya ukombozi ni sasa).

Nirudi kwenye historia ya jinsi Mimi nilivyomfahamu Mtikila kwa zaidi ya miaka 13 na nilivyokuwa karibu nae   ,mke wake kikazi na kifamilia.

Urafiki wangu na Mtikila Ulianza Mwaka 2000 nilipokuwa Mwandisi wa Habari wa Gazeti la Mwananchi Enzi hizo Gazeti la Mwananchi lilikuwa na Ofisi zake jengo la CCM Mkoa wa Dar Es Salaam.

Kabla ya Agosti Mosi Mwaka 2014 kuacha Kazi uandishi wa Habari Katika Gazeti la Tanzania Daima, nilipenda  sana kuandika Habari,makala za siasa,kisheria na kuripoti Kesi Katika Mahakama mbalimbali zilizopo Katika  Mkoa  wa Dar Es Salaam na Pwani  tangu nilipoanza Kazi yangu ya uandishi wa Habari Mwaka 1999.

Enzi hizo Mtikila alikuwa akiishi Ilala Katika maghorofa ya NHC. Urafiki wangu na Mtikila Ulianza kushika kasi wakati nikiripoti kesi ya kutoa maneno ya uchochezi ambayo ilifunguliwa na Jamhuri dhidi ya Mtikila Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam. 

Katika Kesi hiyo upande wa jamhuri Ulidai Mtikila alienda kosa Hilo kufuati Kauli yake aliyoitoa hadharani siku Chache baada ya Mhasisi wa Taifa la Tanzania, Julias Nyerere kufariki Dunia Oktoba 14 Mwaka 1999 ambapo Mtikila alitamka maneno yafutatayo:

 ' Marehemu Rais Julias Nyerere alifariki kwa ugonjwa wa Ukimwi,ni mzoga,nyamagu na ameenda jehanamu" alisema Mtikila.

Mtikila amekuwa akisema maneno hayo siku zote za Maisha yake.Kesi hiyo niliiripoti mwanzo hadi mwisho na mwisho wa siku Kesi hiyo ilifutwa.

Kesi nyingine ya kutoa maneno ya uchochezi alivyoshitakiwa nayo Mtikila Enzi za Uhai wake ni Jamhuri dhidi ya Christopher Mtikila .

Mtikila alishitakiwa kwa Kesi nyingine ya uchochezi   ambapo ilidaiwa na upande wa jamhuri kuwa Mtikila wakati  akihutubia mkutano Katika Viwanja vya Jangwani Dar Es Salaam ,Alisema maneno yafutatayo ambayo yao ichapishwa Katika Gazeti la Mtanzania na miongoni wa mashahidi wa upande wa jamhuri alikuwa ni Mhariri wa Gazeti Hilo Badra Masoud ambaye kwasasa ni Mkuu wa Kitengo cha Habari Cha Wizara ya Nishati na Madini na Askari Polisi .

Maneno hayo yaliyotolewa na Mtikila ambayo upande wa jamhuri Ulidai ni ya kichochezi ni haya hapa nchini;  "Rais Mkapa siyo Raia wa Tanzania ni Raia wa Msumbiji '.

Kesi hiyo iliunguruma na mwisho wa siku Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilifuta Kesi hiyo dhidi ya Mtikila kwasababu ilichukua muda mrefu kumalizika na mashahidi upande jamhuri ukawa auleti mashahidi.

Mtikila Katika Kesi hii wakati ikisikilizwa ,mapolisi walipokuwa wakija kutoa ushahidi ,Mtikili alikuwa Mara kwa Mara akiomba Mahakama isipokee ushahidi wa mapolisi wale kwasababu wao sio Rais Mkapa.Yeye (Mtikila) Kama mshitakiwa aliomba Mahakama itoe hati ya kumlazimisha Rais Mkapa aje Mahakamani atoe ushahidi wake wa kupinga yeye siyo Raia wa Msumbiji.

" Mweshimiwa Hakimu ,huyu Rais Mkapa anaishi hapo nyumbani kwake SVU -Upanga,ni karibu kabisa na hapa Mahakama ya Kisutu .Kwanini  asipelekewe Samansi  aje hapa mahakamani maana ni karibu na anaweza kutembea hata kwa miguu aje akatae Kuwa yeye siyo Raia wa Msumbuji...mini Nina ushahidi Rais Mkapa ni Raia wa Msumbiji Ndio maana Hana uchungu na taifa hili anauza Viwanda vyetu kwa Wazungu ovyo ovyo.

Wakati Mtikila akitoa Maombi hayo akiwa amesimama kizimbani tena Mkapa akiwa bado ni rais wa nchi wakati huo,waandishi tuliokuwa tumeketi mahakamani tunaofuatilia Kesi hiyo tulikuwa tunainama huku Tukicheka bila kutoa sauti.

Pia Mtikila mitamkumbuka Katika Kesi nyingine ya uchochezi  Na.132/2011. Jamhuri dhidi ya Mtikila ambapo Mtikila alikuwa akidaiwa Kutoa  maneno ya uchochezi na kashfa dhidi ya Rais Kikwete kwa kumuita gaidi kwa madai kuwa serikali anayoiongoza inataka kuanzisha Mahakama ya Kadhi, jambo ambalo ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya   Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977. 

Ilidaiwa kuwa kati ya Januari mwaka 2009 na Aprili 17, mwaka 2010 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya uchochezi mshitakiwa alisambaza kwa umma nyaraka zilizosema 'Kikwete kuuangamiza ukristo', 'wakristo waungane kuweka mtu Ikulu' alinukuliwa Mtikila.

Katika shitaka la pili, Aprili 16, mwaka 2010 eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam, bila kibali alikutwa akimiliki waraka wenye uchochezi kwa jamii.Na katika kesi hii Mtikila hana wakili wa kumtetea na anajitetea mwenyewe.

Nakumbuka siku Polisi wamevamia nyumbani kwa Mtikila alfajiri kufanya upekuzi kwa Lengo la kusaka Waraka huo na kumkamata, Nilipigiwa simu saa 12 asubuhi na Mkewe Mtikila akiniarifu Kuwa baba yangu (Mtikila) amekamatwa na Polisi hivyo niandike Habari na kuharifu umma Kuwa Mtetezi wa walalahoi (Mtikila) amekamatwa na Polisi kweli Nilifanya hivyo nakusambaza taarifa kwa waaandishi wenzake na umma kwa ujumla.

Kesi hiyo ambayo ilisikilizwa na Mahakimu watatu tofauti ambao ni Waliarwande Lema,  Sundi Fimbo  ambao Walilazimika wajitoe Katika Kesi hiyo kwasababu Mtikila aliwaomba mahakimu wawili wajitoe kwasababu anaamini hawana hadhi na hawawezi kumtendea Haki na mwisho wa siku Kesi hiyo akapangiwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo kwa wakati huo Elvin Mugeta ambaye aliisikiliza Kesi hiyo na Septemba 25 Mwaka 2012 ,alitoa hukumu ya kumuachilia huru Mtikila baada ya upande wa jamhuri kushindwa kuthibitisha kesi yao.

Nakumbuka Siku Mtikila alipotoa utetezi wake Katika Kesi hii Nilikuwepo ,Mtikila Kama kawaida alikanusha Madai ya upande wa jamhuri Kuwa ule Waraka wake uliokuwa na kichwa cha Habari kisemacho ( KIKWETE KUANGAMIZA UKRISTO) Kuwa ni wa uchochezi,na alikubali Kuwa ule   Waraka ni wake na aliundaa yeye na siyo wa uchochezi na kwamba hawezi Kuukana Waraka ule kwasababu Kuukana Walaka ule ni sawa na kumkana  YESU KRISTO.

Nilicheka sana kwasababu wakati akiuandaa Waraka ule na Nyaraka  zingine mbalimbali za kukemea maovu alikuwa akiniita nyumbani kwake akiniarifu Kuwa anaandaa mabomu ya Eroshima dhidi ya serikali ya 'Msanii ' Rais Jakaya Kikwete.Mtikila Kabla na baada ya Kikwete awe rais ,yeye pindi nikikutana naye amekuwa akimuita Kikwete ni 'RAIS MSANII', Chadema,Reginald Mengi ,Rostam Aziz na wengine.Nilikuwa nacheka sana.'

Badaa ya hukumu ya Kesi hiyo kutolewa Mtikila akiwa kizimbani alipaza sauti akisema 'Aleluya'. 

Wafuasi wake walishangilia na baadhi ya Polisi wenye vyeo Vya chini walijipanga nje ya Chamba za Mahakama hiyo Wakataka kumuweka chini ya Ulinzi ambapo Mtikila aliwaeleza maneno yafutatayo ambayo yalisababisha jaribio lile la Polisi kutinga Mwamba:

" Nyie Polisi hamna uwezo wa kunikamata kwanza mnavyeo Vya chini sana....Kama mnataka kanifungulia Kesi nyingine nitakwenda Mwenyewe Kituo cha Polisi kuripoti .Hata boss wenu IGP- Said Mwema ananiita kwa heshima kwa kunipigia   simu naenda Mwenyewe Polisi,ebu toeni Ujinga wenu hapa" alisema Mtikila na kusababisha watu kuangua vicheko na Polisi wale waliokuwa wamepanga kumkamata kutuacha Mtikila aende zake nyumbani.

Itakumbukwa Kesi hiyo ya kumtolea kashfa rais Kikwete mwanzo alipangiwa Hakimu Mkazi Waliarwande Lema , ambapo Januari 11 mwaka 2010 alitoa amri ya kumfutia dhamana Mtikila kwa madai ya kushindwa kujiheshimu.

Amri hiyo ya kumfutia dhamana ilitolewa na Hakimu Mkazi Waliarwande Lema baada ya kusikiliza utetezi wa mshitakiwa ambaye alifika katika viwanja vya mahakama hiyo saa tano asubuhi akiwa amechelewa na ghafla alijikuta akikamatwa na askari polisi wa mahakamani hapo.

 Mtikila alipaswa kufika mahakamani hapo majira ya saa tatu asubuhi wakati kesi hiyo ilipotajwa, lakini hakuwepo, ndipo Wakili wa Serikali, Beatrice Mpangala aliomba hati ya kukamatwa kwa mshitakiwa.

Kabla ya Mtikila kukamatwa, aliambi a mahakama kwamba alidamka mapema na kumtafuta daktari wake aliyemtaja kwa jina moja la Katembo, ambaye alimfanyia upasuaji baada ya kugongwa na nyoka aina ya kobra wakati alipokuwa katika shughuli za kidini nchini Zimbabwe mwaka jana.

Alisema alijitahidi kuwatafuta wadhamini wake ili wafike mahakamani kwa niaba yake, lakini hakuweza kuwapata, ndiyo maana alikuja mwenyewe mahakamani hapo akiwa na maumivu makali mwilini mwake.

Hata hivyo hakimu Lema alieleza kutoridhishwa na utetezi huo na kuamuru Mtikila atupwe rumande hadi Januari 25 mwaka 2010 kesi yake itakapotajwa tena.

Hii ni mara ya pili kwa Mchungaji Mtikila kushindwa kufika mahakamani wala wadhamini wake. Mara ya kwanza ilikuwa Oktoba 22 Mwaka 2009.Mchungaji Mtikila aliwaku akikabiliwa na kesi hiyo ya uchochezi  Na.132/2011


Ilipofika saa saa tano mchana ,Mtikila aliwasili mahakamani hapo nanilipomuona anashida Kwenye Bajaji nilimuwahi kule kule Kwenye bajaji Kuwa Hakimu Lema ametoa Hati ya yeye Kukamatwa hivyo mapolisi Wakimuona watamkamata .

Hata hivyo utetezi wake huo haukumsaidia Mtikila ,Hakimu Lema aliamuru aepelekwe mahabusu.

Mtikila alienda mahabusu na alipotoka Kesho yake alinipigia simu Kuwa anakusudia Kuwasilisha ombi la Kumkataa Hakimu Lema ajitoe Kwenye Kesi yake kwasababu Hana utu na mwisho wa siku Hakimu Lema alijitoa .

Pia Kesi hiyo ilipohamishiwa kwa  Hakimu Sundi Fimbo pia ,Mtikila kupitia barua yake aliyoiwasilisha mahakamani hapo alimuomba  hakimu Fimbo ajitoe kwenye kesi yake kwasababu amebaini hawezi kumtendea haki kwasababu wakati kesi hiyo ikiendelea Mtikila ambaye ni mshtakiwa katika kesi hiyo aliwasilisha ombi la kuomba usikilizwaji wa kesi hiyo usimame hadi kesi ya Kikatiba iliyopo mbele ya Jopo la Majaji wa tatu wa mahakama Kuu wanaongozwa na Jaji Fakhi Jundu na Profesa Ibrahim Juma ambapo katika kesi hiyo anaiomba mahakama hiyo izifute sheria za makosa ya uchochezi kwakuwa zinanyima haki wananachi ya kutoa maoni yao itakapotolewa uamuzi lakini huyo alilikataa ombi lake.

Mtikila alidai kuna kesi tatu za Kikatiba zilizokuwa zimefunguliwa mahakama kuu na washtakiwa wanaokabiliwa na kesi za jinai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambao ni Jayantkumar Patel ‘Jeetu Patel’, Profesa Costa Mahalu na mahakama ya Kisutu ilisitisha usikilizwaji wa kesi zinazowakabili hadio mahakama kuu ilipozitolea uamuzi kesi zao za Kikatiba.

“Na huyu Hakimu Fimbo anafahamu fika nimefungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu kuzipinga sheria za uchochezi ambao sheria hizo ndizo zimetumika kunifungulia kesi ya uchochezi iliyopo mbele yake na anafahamu fika kesi ya aina hiyo ikishafunguliwa mahakama ya juu, mahakama ya chini inatakiwa isitishe usikilizaji wa yangu hadi mahakama hiyo ya juu itakapotoa uamuzi lakini yeye amekuwa akilikataa ombi langu na kwa kitendo chake hicho minasema amevunja mwenendo wa kesi na ukiukwajili wa maadili ya sheria za nchi na haki na nimuomba ajitoe kwenye kesi yangu kwani tayari ameishaonyesha hawezi kunitendea haki ”alidai Mtikila.

Aidha Mtikila alidai sababu nyingine ya kumkataa hakimu Fimbo, ni kwamba wakati kesi hiyo ikiendeshwa aliwai kuwasilisha ombi la kutaka afutiwe kesi hiyo ya uchochezi kwasababu kesi hiyo ilifunguliwa nje ya muda kwani kesi za uchochezi zinatakiwa zifunguliwe mahakamani ndani ya miezi sita tangu mshtakiwa alituhumiwa kutenda kosa hilo na kwamba kesi hiyo inafanana na kesi ya madai ya fidia Na.166/2004 inayosikilizwa na Jaji Robert Makaramba , ambapo katika kesi hiyo anamdai Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa alikamatwa kinyume na sheria na kwamba kesi ile ambayo nayo ni ya uchochezi iliyokuwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni ilifunguliwa nje ya muda.

Na kweli Ilipofika Machi 22 Mwaka 2013 Hakimu Fimbo alitangaza Kujitoa kusikiliza Kesi hiyo ikapangwa kwa Hakimu Mugeta ambaye aliisikiliza Kesi hiyo hadi akatoa hukumu ya kumwachilia huru Mtikila.

Juni 2013 , Mchungaji, Christopher Mtikila, aliibwaga  serikali katika kesi namba 009 & 011/2011, aliyokuwa ameigungua Katika  Mahakama ya Haki za Binadamu Afrika (AfCHPR) ya kutaka kuruhusiwa kwa mgombea binafsi, nafasi mbalimbali ikiwamo urais.

Mtikila alifikia uamuzi wa Kufungua Kesi hiyo Katika Mahakama hiyo Kimataifa baada ya Juni 17 Mwaka 2010 , Mahakama ya Rufani ya Tanzania, kutoa hukumu ya rufaa ya Madai Na.  45/2009 ambayo ilifunguliwa mahakamani hapo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Mchungaji Christopher Mtikila.

Mrufani( Mwanasheria Mkuu wa serikali) ambaye alikuwa akitetewa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye kwasasa ndiyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju Katika rufaa hiyo alikuwa akiomba Mahakama hiyo ya juu kabisa nchini kutengua hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar Es Salaam katika kesi ya madai Na.10/2005 

Mbele ya jopo la Majaji wa Tatu ,Amir Manento(Mstaafu), Salum Massati(Jaji wa Mahakama ya Rufaa hivi sasa ) na Thomas Mihayo(Mstaafu) ambayo ilitangaza  Ibara ya 39,67,77 zinavunja Haki ya za watu wasiokuwa wanachama wa vyama vyovyote  vya siasa kugombea urais na hivyo hukumu ile  ikaruhusu mgombea binafsi.

Juni 17 Mwaka 2010 ndipo jopo  la Majaji Saba wa Mahakama ya Rufani Tanzania lilokuwa likiongozwa na Jaji Mkuu wa Kipindi hicho ambaye kwasasa  amestaafu,Augustino Ramadhani ,Eusebio Mnuo(Mstaafu),Nataria Kimaro,Mbarouk Mbarouk ,Sauda Mjasiri,January Msoffe ,Bernad Luhanda walitoa hukumu ya rufaa hiyo ambapo walitangua hukumu ya Mahakama Kuu kwa maelezo Kuwa Mahakama haina mamlaka ya kutunga Sheria ,Mhimili wenye mamlaka ya kufanyia marekebisho Katiba ni Bunge   hivyo suala la kuwepo kwa mgombea binafsi litapelekwa bungeni kwasababu Mhimili wa Mahakama haina mamlaka ya kufanyia marekebisho Katiba ya nchi.

 Ieleweke Kuwa Katiba ya Tanzania hadi sasa hairuhusu kuwepo kwa mgombea binafsi kwasababu Ibara ya 39(1) (c) inasomeka hivi : " (c) ni mwanachama, na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa.

Nakumbuka siku hukumu ya rufaa ya mgombea binafsi Imetolewa ambapo ili mkataa mgombea binafsi , Mtikila a likasirika  sana na alihojiwa na vyombo Vya Habari na nilizungumza nae Ana kwa Ana na siku nyingine nilikuwa nilizungumza  nae kwa njia ya simu na email, alikuwa akisema Majaji wote Saba waliokataa kuhurusu mgombea binafsi   ni  Yuda Eskalioti na vibaraka wa serikali yaani wasaliti wakubwa. 

Basi kila nilipokuwa namuona Mzee wangu Jaji Mkuu Augustino Ramadhani na wenzake nacheka peke yangu  nakumbuka Lile jina walilopachikwa na Mtikila la Yuda Eskalioti.

Aidha Kesi nyingine ambaye ili zidisha ukaribu wangu na Mtikila ni ile Kesi ya Madai ya fidia ya Sh.Bilioni Moja ambayo anataka Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Dk.Valentino Mokiwa Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Katika Kesi hiyo Mtikila Anadai Mokiwa alimdhalilisha kwa kumshika   makalio Mtikila na kwamba kitendo hicho kilichotokea Juni 25 mwaka 2013.

.Mtikila alikuwa ameitwa na Askofu kujadili tamko la la Mtikila kwamba Kanisa la Anglican linajihusisha na ufisadi, ukiwemo wizi wa vifaa vya Hospitali ya Mission ya Millo iliyoko Ludewa mkoani Njombe.

Mtikila alisema kuwa alivyoitwa na Askofu Mokiwa ili kujadili hilo alifika na wenzake watatu wa taasisi ya Liberty International Foundation na wakakaribishwa kwenye moja ya jengo la dayosisi ya St. Nicholous, usiku wa saa 03:00.

Muda mfupi baada ya kikao kuanza, Askofu Mokiwa ambaye alikuwa na wenzake saba, alisimama na kuwataka wajumbe wote wakaguliwe kama kuna mtu ana kinasa sauti. 

Baadaye Askofu Mokiwa nae alisimama na kuungana na wenzie kuwakagua kina Mtikila baada ya kuhakikisha mlango umefungwa.Katika upekuzi huo ndipo tuhuma hizo zilipopatikana kutokana na madai kwamba operesheni hiyo ilienda mbali zaidi ya lengo la kawaida.

" Mokiwa alianza kupenyeza mikono yake kwenye shingo yangu kuelekea chini kisha huko chini mikono ya mlalamikiwa ilionekana waziwazi ikipapasa makalio ya yangu ".alidai Mchungaji Mtikila .

Mtikila aliomba  Mahakama imwamuru Askofu Mokiwa amlipe kiasi hicho cha fidia kwasababu mdaiwa alimdhalilisha na alimletea madhara  zaidi ya kitendo hicho ni pamoja na mfadhaiko, masikitiko, wasiwasi, aibu katika jamii na kupata shinikizao la damu la mara kwa mara na matatizo ya moyo kila anapokumbuka kitendo hicho.

Nilipokuwa ni kuhudhuria kuripoti kesi hiyo dhidi ya Askofu Mokiwa pindi tunapotoka katia chemba ya mahakama, Mtikila alikuwa akinishika mkono na kujadiliana naye mambo mbalimbali na kusema kuwa anashahuku kubwa siku ifike aanze kutoa utetezi wake katika kesi hiyo maana atavua nguo zote na sijui huyo wakili wa Mokiwa ambaye ni kijana wangu atakuwa tayari kunishuhudia mimi mzee wake nikivua nguo zote mahakamani kumuonyesha hakimu makalio yangu maana akinishuhudia nipo uchi nikimuonyesha hakimu makalio yangu atakuwa amepata laana huyo wakili wa Askofu Mokiwa ambaye ni kijana wangu..Nilicheka sana.

Mtikila Enzi za Uhai wake  alikuwa anataka Shirika la uchunguzi la Scotland Yard Lije Tanzania, ichunguze kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba aliyefariki ghafla kwasababu Mtikila alikuwa akiamini Kolimba aliuwawa na CCM Hali  iliyosababisha kufunguliwa Kesi Katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni Dar Es Salaam, ambapo Hakimu Gabriel Mirumbe (Hakimu huyo ambaye ni marehemu kwasasa ambapo alipofariki nilimjulisha Mtikila na Mtikila alisema amefuraishwa na kifo hicho kwasbabu hakimu hiyo alimfunga gerezani kwa kumuonea kifungo cha mwaka mmoja gerezani  ambapo alitumikia kifungo hicho katika gereza la Keko.

Aidha vibekwa vingine Vya Mtikila ambavyo sitavisahau ni Kwenye ombi lakuomba Mahakama ya Kisutu itoe amri ya kutolewa rumande  ( Habeas copus) lilowasilishwa mahakamani hapo na Wakili wa kujitegemea Hurbet Nyange dhidi ya Jamhuri Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Nyange alikuwa akimtetea aliyekuwa mgombea urais nchini Burundi Katika awamu ya kwanza ambaye alikuwa ni Mtangazaji Katika Redio Moja huko Burundi, Sinduije.

Sinduije alikuwa ni rafiki wa Mtikila na aliposhindwa uchaguzi nchini Burundi alikimbilia Tanzania kujificha  maana serikali ya Burundi ilikuwa ikimsaka kwa kutenda makosa ya jinai wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu nchini Burundi na alipokamatwa na Askari wa Interpol na kuwekwa Rumande ili upande wa jamhuri uwasilishe ombi la Mahakama itoe Kibali cha kumrejesha nchini Kwao Sinduije ( Extradition request) .

Mtikila alikuwa akifika Katika Mahakama hiyo na kujaribu kukaa karibu na eneo la mahabusu ya Mahakama hiyo lakini Askari Magereza walikuwa wakimtimua wakimtaka akae Mbali na eneo Hilo Mtikila.

Waandishi wa Habari za mahakamani tulikuwa tunaenda kuchekea Mbali ili Mtikila asituone maana angetuona tunacheka anget ushughulikia kwa maneno makali.Mwisho wa siku Mahakama ilitoa Kibali cha Sinduije kurudishwa chini kwako wakati Mtikila Mimi Nilipokuwa naongea nae nje ya Mahakama alikuwa anasema yeye anataka Sinduije abaki hapa nchini kwasababu endapo atarudishwa Burundi, serikali ya Burundi itaenda Kumkata kichwa Sinduije.Nikacheka sana.

Waandishi wa Habari walikuwa wamejipachika  jina la 'Mama Mtikila' ,kwasababu ya ukaribu wangu  na Mtikila.Hata pindi watakapo namba zake za simu au kupata taarifa zozote kuhusu Mtikila walikuwa walinipigia simu yangu Mara kwa Mara kuniomba namba zake.

Ndio maana Askari wa upelelezi walipokuwa wanapata taarifa za Siri Kuwa Mtikila yupo nyumbani wake anaandaa Waraka wa maneno makali dhidi ya viongozi wa serikali,Mtikila alipokuwa akiona Polisi wamevamia nyumbani wake cha kwanza alikuwa akimtaka   Mke wake Geogia anipigie simu Mimi ili nipate taarifa nianze kuisambaza Kwenye Jamii ili Jamii ifahamu Polisi wamemkamata.

Mtikila yeye alikuwa alilipachika jina la 'Mgodi' Kesi zote za Madai alipokuwa amezifungua.Alisema ameamua kuzipachika jina la mdodi kwasababu anaamini atashinda na akishinda na Mahakama itaamuru wadaiwa wamlipe fidia ya Fedha kwahiyo Fedha ndiyo mgodi.

Mtikila aliniamini na kunipenda sana nami nilimpenda sana.Mambo mengi aliyokuwa aliyafanya na kukusudia kuyafanya alikuwa akinieleza na kuniambia baadhi ya watu ambao wamehaidi kumsaidia wakiwemo baadhi ya Wanasheria.

Sebuleni kwa Mtikila makochi yake na meza zilikuwa zimepambwa na vitambaa Vya kufumwa mwenye rangi za Bendera ya Tanganyika.Na nje ya nyumba yake alikuwa ametundika Bendera ya Tanganyika maana alikuwa akiamini na kuipenda serikali ya Tanganyika.

Mtikila chai yake ya asubuhi alikuwa akipenda kula chapati na Samaki wa kukaanga.Na kweli Mara kwa Mara Nilipokuwa nikienda kumtembelea nyumbani kwake asubuhi na kupiga nae stori za siasa za nchini nilikuwa nikimkuta akinywa chai yenye vitu hivyo.

Mtikila alilipenda  sana vazi la suti na muda mwingi Katika harakati zake alikuwa akivalia vazi Hilo la suti na Saspenda. 

Pia niliwahi kumuuliza kwanini anavaa vazi la Sasipenda ,aliniambia Miaka ya nyuma alienda Marekani Kwenye mkutano wa watumishi wa Mungu akiwa bado hajaanza kuvaa Sasipenda na aliwakuta watumishi wenzake wa Mungu wakiwa wamevalia vazi la Sasipenda na aliwauliza kwanini wanapenda kuvaa Saspenda.

Mtikila alisema watumishi wale wa Mungu walimweleza Kuwa wanapenda kuvaa vazi Hilo la susipenda kwasababu wao upenda Kufunga ili wawe karibu na Mungu ,sasa wanaomaliza Kufunga ,uzito upungua na kusababisha nguo kuwapwaya na kuwaletea Usumbufu wa kwenda kwa fundi kupunguza nguo zao Mara kwa Mara .

Sasa hili kuondokona na tatizo Hilo la kupeleka kwa fundi kupunguza nguo,wanaamua kuvaa Sasipenda ambazo zinasaidia nguo zile zinazowapya wakutowalegea mwilini.

 Mtikila alikuwa na komputa na printa nyumbani kwake tangu alipokuwa akiishi Ilala na Mikocheni na alikuwa na chumba chake kimoja amekitenga kama ofisi ambacho alikuwa akikitumia kufanyia shughuli zake ikiwemo shughuli kubwa aliyokuwa akiipenda sana ya uandishi wa nyaraka mbalimbali ambazo zimebeba maovu ambayo ameyachunguza na kuyabaini na pindi akimaliza kuandika nyaraka hizo mara kwa mara amekuwa akinipigia simu kunishirikisha kuniambia alichokiandika na amekuwa akinitukia nyaraka kadhaa kwenye email yangu nasoma hayo maovu ya watu .

Licha nyaraka zake hizo za maovu aliyokuwa anadai ameyagundua yalikuwa na maneno makali ambayo wahariri wengi walikuwa wakiogopa kutumia habari zinatokana na nyaraka zile alizokuwa akiziandika kwa zaidi ya miaka 10 sasa,ila mkewe atakuwa amezitunza.

Sasa askari polisi pindi wapatapo taarifa za siri kuwa Mtikila anaandaa waraka mbalimbali za kuja kuwavua nguo viongozi wa serikali ,walikuwa wakivamia nyumba yake asubuhi sana na kufanya upekuzi ndani ya nyumba yake kwasababu wamepewa maelezo kutoka kwa viongozi wao wa juu.

Hata hivyo Mtikila alikuwa akiniambia baadhi ya polisi waliokuwa wanatumwa kumkamata walikuwa wakipenda harakati zake za kuiletea changamoto serikali, wakati wanampekua na kukamata nyaraka, askari wengine walikuwa wakimfuata bila askari wenzao kuwaona na kumtaka nyaraka zingine azifiche ili asiwe na Kesi nyingi .

Kwa tuliokuwa karibu sana na Mtikila alikuwa akinieleza mambo mengi mazito ambayo sikuwahi kuthubutu kuyaandika Kwenye magazeti.

Kuna siku Mtikila akifurahi alikuwa akinieleza Kuwa kuna baadhi ya watumishi wa serikali wazalendo ambao wanakerwa na baadhi ya ufisadi ndani ya serikali tena wengine walikuwa wakimuita Faragha Na Kumpa taarifa zote za uchafu unaoendelea  ndani ya serikali ili Mtikila akauanike hadharani ikibidi hata Kufungua Kesi mahakamani na Mtikila alisema alikuwa akifanya hivyo.

Kibweka kingine cha Mtikila alichokifanya Enzi za Uhai wake,kuna siku alifika getini Katika Ofisi za Msajili wa Vyama Vya Siasa Enzi hizo Msajili wa vyama akiwa JohTendwa ,Mtikila Mlinzi aliyekuwa akilinda zamu walipishana Kiswahili ,Mtikila alikuwa anataka Aingie kuona na Msajili Yule Mlinzi Akawa anamkatalia, Mtikila alimpiga kofi Yule Mlinzi na Kuzua mjadala .

Kibweka kingine cha Mtikila , yeye alikuwa akimuita Rais Jakaya Kikwete ni Rais Msainii.
Katika kampeni za ndani ya CCM Mwaka 2005 kumpata mgombea urais,mtakumbuka Mtikila alimvalia njuga aliyekuwa mgombea urais ndani ya CCM ambaye pia alikuwa waziri Mkuu ,Fredrick Sumaye Kuwa ni mwizi mkubwa na hafai Kuwa rais.

Wiki Tatu zilizopita Mtikila alikuwa akihojiwa na Televisheni ya Star Tv ,Kuwa maoni yake ni yapi kuhusu Mwenendo wa Hali ya uchaguzi nchini ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba 25 Mwaka huu.

Mtikila alitoa maoni yake mengi lakini kubwa liloacha gumzo Katika Jamii alipo sema wale wote wanaomshabika mgombea urais kupitia Chadema,Edward Lowassa, anautahira nusu/ apedomia yaani undani na kwamba Lowassa hafai Kuwa rais Kwani ni fisadi na mgonjwa sana na kwamba bangi imekuwa ndiyo sakrementi ya wanachama Wengi wa Chadema.Nilicheka sana.

Aidha vibweka vingine ambavyo sitavisahau ni baadhi ya wahariri wa vyombo Vya Habari walinitisha azimio la kutochapisha Habari zinazotolewa na Mtikila kimya kimya, Mtikila alivyopata taarifa hizo alitembelea baadhi ya vyombo Vya Habari na kuwakuta wahariri na kuanza kuwasemea ovyo .

Aidha siku zote Mtikila alikuwa anasema Aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, siyo Raia wa Tanzania, ni Raia wa Iran na anaitwa Sakalili na alikuwa akifanya Biashara ya ngozi eti ni Mtu hatari sana Katika hii nchini.

Hili jina la Sakalili wakati Nikiwa mfanyakazi wa Gazeti la Tanzania Daima, waandishi wa Habari wenzangu tulikuwa tukilitaja jina la Sakalili na kucheka sana kwa sauti .

Waandishi ambao wanacheka sana pindi wakumbukapo jina Hilo la Sakalili ni Absalom Kibanda( Mtanzania), Alfred Lucas(Jamhuri), ,Iren Mark(Tanzania Daima),Mobini Sarya na Martin Malela( Tanzania Daima). 

Waaandishi wote hawa pindi tulipokuwa Tukimjadili Rostam Aziz,tulikuwa hatumtaji kwa jina la Rostam tunamtaja kwa jina la Sakalili Kisha tunacheka sana.

Kesi ya kupinga Kuuzwa jengo la Mahakama ya Rufaa hivi sasa, Kesi ya Kikatiba ya kuomba Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), apunguziwe mamlaka  kwasababu kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya ya Jinai ya Mwaka 2002, DPP amepewa mamlaka makubwa sana Kwani Kifungu 91(1) cha Sheria hiyo kinatoa madaraka kwa DPP kumfutia Kesi mshitakiwa wa kesi ya jinai bila kuhojiwa na Mtu wala Taasisi yoyote ile.

Aidha Mtikila alifungue Kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dar Es Salaam, akiomba Mahakama izuie uuzwaji wa jengo la Mahakama ya Rufani Dar Es Salaam.Maana kulikuwa na taarifa kuwa uongozi wa mahakama nchini unampango wa kuliuza jengo hilo la Mahakama ya Rufani nchini ambalo ni jengo la kihistoria ambalo zamani jengo hilo lilikuwa likijulikana kama Forodhani Hoteli.

Aidha  Machi 2015 Mtikila, alifungue Kesi Na.14/2015 Mahakama Kuu Kanda ya Dar Es Salaam  kupinga muswada wa mabadiliko ya sheria kwa ajili ya kuitambua rasmi Mahakama ya Kadhi.   Muswada huo umepangwa kuwasilishwa, kujadiliwa bungeni lakini hata hivyo baadae muswaada huo haukuweza kuruhusiwa kujadiliwa bungeni .

Binafsi namuelezea  Mtikila alikuwa Mwanasiasa ,kiongozi wa dini ambaye ni Mtanzania  pekee  mwenye msimamo usiyoyumba kwani alikuwa Tayari  kusimamia msimamo wake Katika kukemea baadhi ya mambo ambayo aliyaamini siyo sahihi  hata akibaki peke yake .

Mtikila ambaye ni Mhasisi wa neno la "Magabacholi",yaani Wahindi ambapo Mtikila alikuwa anataka Wahindi wote wanaokaa Katika maghorofa ya NHC Katikati ya Jiji la Dar Es Salaam waondolewe na Watanganyika Ndio waishi Katika maghorofa hayo.

Kulikuwepo na Madai  Kuwa kutokana na ujasiri na misimamo mikali aliyokuwa nayo Mtikila ambayo alikuwa akionyesha Kwenye Jamii  tangu  zamani ,yalisababisha Kutengenezewa kwa pro panda yakuwaaminisha  Watanzania wapuuze yote yanayosemwa na Mtikila kwasababu Mtikila ni kichaa.

Kweli mwanzoni propaganda  hiyo iliwangia watu waliikubali ila kadri siku zilivyokuwa zinaenda watu walipuuza propaganda hiyo dhidi ya Mtikila na Kusema Mtikila ni mzima siyo chizi anasema ukweli ila serikali haitaki kusikia ukweli huo.

Mtikila naye pia ni miongoni mwa baba wa Mageuzi ambayo ambao wameacha historia Katika siasa za upinzani hapa nchini .

Kwasababu tangu Nyerere alipokuwa hai,Mtikila ambaye alifariki Oktiba 4 mwaka huu, kwa ajali ya gari huko Chalinze Mkoani Pwani wakati akitoka kwenye shughuli za kisiasa alionyesha alikuwa ni mtu mwenye misimamo mikali na kusimamia yale anamisimamo yake mikali wazi wazi na Enzi hizo Demokrasia ya vyama Vingi ilikuwa haijashamili.

Hakuna ubishi kuwa uthubutu  na ujasiri aliokuwa nao Mtikila ambao alikuwa akionyesha kwa vitendo kwa kusema hadharani,kufungua kesi mbalimbali mahakamani ndiko kulikosababisha kwa namna fulani kukuza demokrasia ya vyama vingi, wananchi Wengi kujitokeza kwa Wingi kuikosoa serikali , kufungua kukuza utawala wa sheria nchini.

Hatua ya Mtikila kwenda mahakamani Mara kwa Mara Kufungua Kesi mbalimbali dhidi ya serikali, na serikali kumfungulia Kesi za jinai Mtikali mahakamani, pia kumesababisha kukuza Utawala wa Sheria nchini.

Aidha baadhi ya Kesi zilizofunguliwa na Mtikila zimekuwa zikitumiwa Na wahadhiri wa Sheria Katika Vyuo Vikuu kufundishia wanafunzi wa kozi ya Sheria hususani Katika somo la Sheria ya Katiba (Constitution Law).

Nikiwa mwanafunzi wa fani ya Sheria wahadhiri wangu wa fani ya Sheria wamekuwa wakitufundisha masomo mbalimbali ya Sheria Inafika somo la Sheria ya Katiba,wahadhiri hao ututaka wanafunzi wa Sheria tu some na kuelewa Kesi ya Mtikila one na Mtikila Two.

Kesi ya Mtikila one ni kesi Na.10/2015 ambayo Mahakama Kuu Kanda ya Dar Es Salaam, iliruhurusu uwepo wa mgombea binafsi.Na Kesi ya Mtikila Two , rufaa ya Madai Na.45/2009 ambayo Mahakama ya Rufaa ilitengua hukumu ya Mahakama Kuu iliyoruhusu uwepo wa mgombea binafsi nchini kwasababu Mahakama haina mamlaka ya kufanyia marekebisho Katiba ya nchi, na kwamba Bunge peke yake ndiyo yenye mamlaka ya kufanyia marekebisho Katiba ya nchi hivyo suala la kuruhusu mgombea binafsi Mhimili wa Mahakama unalirudisha Katika Mhimili wa Bunge.

Katika sherehe za siku ya Sheria nchini ( Law Day), Mtikila Mara kwa Mara amekuwa alishiriki Katika sherehe hiyo kwasababu naye ni mdau wa Mahakama na Mara zote amekuwa akishangiliwa umma ambao umekuwa umeshiriki Katika Sheria hiyo ya Law Day.

Kingine nilichompendea Mtikila alikuwa Akizungumza lugha ya Kiingereza kwa ufasaha utafikiri ni Muingereza tena kwa mapozi .Na pindi azungumzapo lugha hiyo ya Kiingereza alipenda sana kutamka tena hili hili la Kiingereza ' WELL' .

Mtikila hakuwa Mwoga, alikuwa ni jasiri sana na binafsi sijatarajii taifa kupata Mtanzania ,Mwanasiasa aina ya Mtikila kwa kizazi hiki labda pengine Miaka 50 ijayo.

Kwasababu  wanasiasa Wengi wakorofi hasa wa upinzani wamekuwa wakianzisha vurugu, maandamano haramu, ajenda wakianza kusakwa na Polisi wanakimbia wengine kwenye maandamano haramu waliyoyaitisha hawatokei wanaamua kuwatanguliza mstari wa mbele  vijana  lakini swahiba wangu Mtikila alikuwa haogopi Polisi, Mahakama na dola kwa ujumla ,mtu yoyote awe rais ,yeye alikuwa Akiamua kuanzisha  jambo lake ananipigania hadi mwisho hata Kama kulikuwa na watu waliokuwa wakimuunga  mkono mwanzo wakati analianzisha jambo Hilo wakija kumsaliti katikati ya harakati hizo.

Mwili wa marehemu Mtikila ambaye Mwaka 2014  aliteuliwa Kuwa mjumbe wa Bunge Maalum la  Katiba ambapo alileta Changamoto ndani ya Bunge Hilo ulitolewa heshima za mwisho Oktoba 7 Mwaka 2015  Katika Viwanja Vya Karimjee na Rais Jakaya Kikwete na Makamu wa Rais Dk.Mohammed Gharib Bilal waliongoza  watu wa Kada  mbalimbali kuaga mwili wa marehemu Mtikila ambao ulisafirishwa jana hiyo kwenda Ludewa Mkoani Njombe kwaajili ya mazishi .

Faida niliyoipata baada ya Kuwa karibu kikazi na kijamii na Mtikia Enzi za Uhai wake, kwanza kumtukuza Mungu,kuacha woga wakati nikifanya baadhi ya mambo yangu kwasababu kama Unaamini Katika Mungu haogopi kitu.

Pia Mtikila naye alikuwa ni miongoni mwa watu walionishawishi nikasome Sheria Kwani Mtikila alikuwa akipenda sana kufahamu mambo ya kisheria hasa Katiba ya nchi licha hajawahi kusoma kozi ya Sheria .

Mtikila jinsi alipenda kufanya mambo ya kisheria ikiwemo Kufungua Kesi mahakamani na Kesi nyingine alikuwa akijitetea Mwenyewe bila kuweka Mawakili wa kumtetea na alikuwa akishinda na mfano mzuri ni Kesi ya uchochezi dhidi ya Rais Kikwete ambapo Hakimu Elvin Mugeta alimuachilia huru.

Niliwahi kumhoji Kama aliwahi kusoma kozi ya Sheria ,alinijibu hajawahi ila aliyekuwa Msajili wa Vyama Vya Siasa, Christopher Lihundi (marehemu kwa sasa) ndiye hasa Nyakati za jioni mwishoni mwa Miaka 1980 na mwanzoni mwa  Miaka 1990 walikuwa wakakutana na Mtikila sehemu anamfundisha kuvisoma vifungu naIbara za Katiba na kumuelimisha zilikuwa zinataka Mwananchi afanye nini na jinsi ya kuzidai Haki zake.

Katika mazungumzo yangu Mimi na yeye Mara Kadhaa alikuwa anasema a namuombea kwa Mungu awape Maisha Marefu Mawakili hawa Richard Rweyongeza na Mpare Mpoki kwasababu Ndio walikuwa wakijitolea Kumpa msaada wa kisheria hata kama alikuwa Hana Fedha za kuwalipia nakwambia wakimwakilisha vyema Katika Kesi ya kutaka kuwepo na mgombea binafsi hala nchini.Nilibahati Kujifunza mambo mengi kutoka mwanasiasa Huyo wa upinzani.

Sioni Sababu ya kujadili kifo cha Mtikila kwasababu Tayari Jeshi la Polisi Mkoani Pwani limeishatoa taarifa ya Chanzo cha kifo cha marehemu Kuwa ni ajali.

Ninaposema Mtikila alikuwa ni Chanzo changu cha Habari (source) cha aina yake na mwanasiasa wa aina yake Kwani hata siku Moja hawezi Kumruka  Mwandishi aliye andika taarifa inayomnukuu yeye Kuwa hajampa hiyo taarifa.

Kwa sababu baadhi ya Vyanzo Vyetu vya Habari siyo majasiri ,ni Waoga wanaweza kutoa Habari kwa Mwandishi wa Habari na Mwandishi kaenda kuiandika hiyo Habari magazeti ni lakini baada ya Habari hiyo kuchapishwa Kwenye Gazeti kile Chanzo cha Habari kinamruka Yule mwandishi wa Habari aliye andika taarifa ile.

Mtikila alikuwa na mchezo wakuandika Waraka kuhusu tuhuma za mtu Fulani kwa urefu wenye maneno makali Nakisha anaitisha  mkutano na waandishi wa Habari Anaongea Na wakara huo lakini baadhi ya vyombo ya Habari vilikuwa vikisita kutumia Waraka wa Mtikila kwasababu Una maneno makali na baadhi ya wahariri hawana uelewa wa Sheria hivyo walikuwa wakihofia kuchapisha Habari za Mtikila ,Gazeti linaweza kushitakiwa.

Baada mitandao ya kijamii kuanza kutumika kwa Wingi Mtikila Alichokuwa akijifanya anaandaa Waraka wake Kisha anawatumia watu Kwenye email zao wasome .

Mtikila ambaye alikuwa hajui kuficha hisia zake, alikuwa anawapasha ukweli waandishi wa Habari nchini Kuwa hawataki kutoa Habari zake,kuhudhuria mikutano yake na waandishi wa Habari kwasababu Chama Chake ni masikini Hakina uwezo wa kuwapatia Fedha 'mashiko" waandishi wa Habari kama vyama vingine vinavyofanya jambo ambalo Mimi kama mwanadishi wa Habari Mwandamizi nchini siku zote nimekuwa nikiliunga mkono Kwani waandishi Wengi siku hizo wanapenda kwenda Kwenye kuripoti Habari za vyama Vya siasa ambazo zinawapatia mishiko.

Kingine Nilichojifunza Katika harakati za Mtikila ni kwamba Watanzania Wengi ni wanafki sana Kwasababu wakati Mtikila anapambana Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma na Mahakama Kuu Kanda ya Dar Es Salaam kutaka mgombea binafsi aruhusiwe walikuwa Wakimuona Mwendawazimu na wala walikuwa hawa thamani, lakini siku Mahakama Kuu Kanda ya Dar Es Salaam ,iliporuhusu uwepo wa mgombea binafsi wale wote waliokuwa Wakimuona Mtikila ni chizi walianza kumthamini na kumuona Mtu wa maana sana.

Jambo la Msingi kwa wale wapenda Demokrasia ,Mageuzi ,Haki tumuenzi Mtikila aliyezaliwa 9/6/1950 na kufariki 4/10/2015 kwa kuendeleza Yale yote aliyoaacha  kwa maslahi ya taifa letu.

Mtikila ambaye ulinipachika jina la ' Mpambanaji' nitakuenzi na kukumbuka na nitakapokuwa nakukumbuka  nacheka sana maana ulikuwa ni Mpiganaji mwenye vibweka Vingi.

Tangu ukipofariki sikuoni tena naishia kukutazama  Kwenye video mtandaoni ulivyokuwa ukishambulia mafisadi nacheka sana na kujifunza baadhi ya vitu kutoka kwako.

Mungu aiweke roho ya marehemu Mtikila mahali panapostahili.  Mtikila Nilikupenda nawe ulinipenda. Amina.

Facebook: Happy Katabazi
8/10/2015.






1 comment:

Anonymous said...

Nice

Powered by Blogger.