Kasi ya ujenzi wa Sekondari na wosia wa Mwl.Nyerere

(SAUTI YA JUMAPILI)

Kasi ya ujenzi wa sekondari na wosia wa Mwl. Nyerere

Na Happiness Katabazi

INGAWA sikuwahi kumsikia au kumwelewa kutokana na umri wangu kuwa mdogo, bado naukumbuka vizuri wosia wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuhusiana na elimu.
Akizungumzia hali na changamoto ya elimu Oktoba 22 mwaka 1984, Mwalimu Nyerere alisema: “Tunapoongelea kupanua elimu ya sekondari, tunaharakisha sana kusema kwamba watu watachangia ujenzi kwa juhudi zao. Lakini majengo hayana umuhimu kwanza vitu muhimu katika elimu ni walimu, vitabu na kwa sayansi ni maabara”.
Nimeikumbuka kauli hii isiyochuja kutokana na kampeni iliyoshika kasi ya nchi nzima kuhakikisha shule za sekondari zinajengwa kwa kasi, lengo likiwa kuwapa nafasi wanafunzi waliofaulu darasa la saba mwaka 2006, lakini wakakosa shule za kujiunga nazo.
Kampeni imepamba moto, kiasi cha serikali kuwaamuru manaibu waziri wote 30 katika Serikali ya Awamu ya Nne, kwenda mikoani kukagua ujenzi wa shule hizo.
Agizo la kuzunguka kote nchini limetolewa na Waziri Mkuu, Edward Lowassa, ambaye pia anazunguka mikoani kuangalia mwelekeo wa utendaji.
Kwa hakika, dhamira ya kutaka shule zijengwe kwa mithili ya uyoga nchini nzima si baya, ingawa kuna mengi yanayoonyesha kwamba, serikali imekurupuka.
Haikufanya maandalizi yoyote, kuanzia mikakati na hata walimu watakaohusika katika kuwapa elimu watoto waliokwama kuingia kidato cha kwanza mwaka huu na wale wa miaka inayofuata, wala vifaa, ndiyo maana tunashuhudia shule zilizokamilika wanafunzi wakikalia mifuko ya madaftari yao, kanga na hata vitenge!
Lakini kikubwa zaidi, nadhani uamuzi wa serikali wa kuwachukua manaibu waziri wote kwenda mikoani kukagua ujenzi wa madarasa ni matumizi mabaya ya madaraka.
Si matumizi mabaya ya madaraka ya kiongozi aliyetoa agizo hilo, bali pia agizo hilo linaonyesha kwamba, manaibu waziri hawana majukumu mazito ya kikazi katika ofisi zao.
Inawezekanaje mtu mwenye wizara yake aondolewe kazini kwa zaidi ya wiki mbili kufanya kazi ya ukaguzi katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi?
Ikiwa Wizara ya Elimu ina wakaguzi, ina maana wakaguzi hawa hawafanyi kazi ya kumridhisha Waziri Mkuu, basi ilibidi awafukuze kazi kwanza ndipo awateue hawa manaibu mawaziri kuwa wakaguzi wa shule.
Lakini kitendo cha kutoa kazi kwa jozi (pair) mbili tofauti jozi ya Wanasiasa na jozi ya watawala/watendaji wa kiserikali ni utawala mbovu.
Sijui ni kipi kimemkuta Waziri Mkuu wetu katika haya mawili. Suala la elimu ni suala la kitaaluma, hivyo linahitaji umakini na si suala la amri, suala la elimu haliwezi kutekelezwa kwa serikali kupeleka wanasiasa kukagua shule ambao hawana taaluma, kanuni za ukaguzi wa mashule.
Sasa aliwapeleka kufanya nini huko? Tukumbushane kwamba tangu awamu ya nne iingie madarakani kulikuwa na taarifa ambazo hadi sasa hazijathibitishwa polisi au mahakamani kwamba kuna baadhi ya wabunge na mawaziri vyeti vyao ni vya kughushi ama vya kununua, sasa kwa shaka ya namna hii wana uhalali wa kukagua shule?
Mheshimiwa Lowassa, ebu fanya kwanza zoezi la kukagua vyeti vya hilo baraza lako la mawaziri na wabunge bungeni kwani hofu yetu ni kwamba kuna viongozi wanasemwa vibaya mitaani.
Waziri Mkuu wetu anapaswa kutueleza, hawa manaibu waziri walikwenda kumkagua nani na kwa vigezo vipi au ni ‘watalii’ ambao wanakwenda kuangalia uzuri wa majengo kwa sababu wanaweza kufikiri shule ni majengo!
Waziri Mkuu atueleze hii misafara ya manaibu waziri kwa ujumla inaligharimu taifa shilingi ngapi? Na je, matunda yake ni ya kiasi gani? Kwa vyovyote vile, misafara ya wakaguzi wa elimu isingekuwa na gharama kama hii ya manaibu waziri lakini matokeo yake katika kukagua ujenzi wa madarasa yangekuwa makubwa zaidi.
Na kama ni kuhamasisha michango, kwanini wasitumike wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi, tena kila mbunge angekwenda kuhamasisha katika jimbo lake?
Je, serikali sasa imekuwa wizara moja ya elimu? Waziri Magraret Sitta anafanya kazi gani na watendaji wake?
Kama kigezo ni kutekeleza maagizo ya rais kuhusu elimu, lini hawa manaibu waziri watatekeleza maagizo ya Rais Jakaya Kikwete aliyoyatoa katika wizara zao mahususi?
Naibu Waziri wa Fedha atasimamia lini kikamilifu ukusanyaji wa kodi ili tupate fedha za kuwekeza kwenye elimu? Na yule wa Nishati na Madini atahakikisha vipi kama tuna nishati na kwamba tunanufaika vyema na mapato ya rasilimali zetu kama muda mwingi atautumia kukagua ujenzi wa madarasa? Lini atasimamia kuhakikisha Kampuni kama Dowans inatekeleza mkataba wake kwa wakati? Mifano kama hii ipo kwa kila wizara!
Hebu tuelezwe hawa manaibu, waziri watakaguaje taaluma ya elimu ambayo vifaa vya kufundishia hawavijui na hawana ujuzi navyo, hata utendaji kazi wa walimu?
Basi, kwa kuwa kila jambo lina busara yake, bila shaka hili ni jambo lisilo na busara, kwa kuwa tutakuwa tunatumia fedha za walipa kodi bila tija kwa taifa.
Hata hivyo nazipongeza jitihada za serikali za kuongeza ujenzi wa madarasa katika shule za sekondari nchini, suala ambalo naweza kusema Lowassa, amelivalia njuga, lakini ninamwomba auelezee umma kwamba kuna mikakati gani ya kufanya maandalizi kwa walimu na kuhakikisha kwamba kuna vifaa vya kufundishia, vikiwamo vitabu na hata maabara?
Ni kwa kiasi gani mikakati inayotekelezwa hivi sasa inatimiza azima hii? Tukizingatia serikali tayari imetangaza kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa ‘halaiki ya walimu’ na kuwamwaga katika shule hizi. Je, si ishara ya kuingia tena katika mtego wa Ualimu Pasipo Elimu (UPE)?
Kwa upande mwingine, kuna maandalizi gani ya kuwapokea hao wanafunzi katika vyuo vikuu vya hapa nchini? Kwakuwa hawa wanafunzi waliopo vyuoni ni wachache na serikali inashindwa kuwalipia karo.
Je, wahadhiri wanaandaliwaje na serikali kuwapokea wanafunzi hao pindi watakapoingia chuo kikuu, ilhali serikali imekataa kabisa kusomesha watu wa zaidi ya digrii ya kwanza?
Namaliza kwa kusema kuwa historia ya nchi hii inaonyesha baadhi ya viongozi wetu wamekuwa wakianzisha mipango ambayo si endelevu, ambayo inaligharimu taifa fedha nyingi.
Hata hivyo nataka Waziri Mkuu ajue kwamba tayari wataalamu wa ujenzi wameishaanza kukosoa kasi ya ujenzi wa shule hizi, wakidai kitaalamu ni dhambi kubwa kujenga jengo kwa muda mfupi kama ilivyo kwa majengo haya ya sekondari!
Tukumbuke wosia wa Baba wa Taifa kwamba, elimu si madarasa pekee, bali yanahitajika mambo mengi kwa wakati mmoja, yaani walimu, vitabu na hata maabara. Alamsiki!
Mungu ibariki Afrika.
Mungu inusuru Tanzania.

0755 312 859, katabazihappy@yahoo.com, www.katabazihapppy.blogspot.com