Bunge Lisilo Meno Halitufai!

Na Happiness Katabazi

AWALI ya yote namshukuru Mungu kwa kunifikisha siku ya leo salama, ninamshukuru kwa kunipa nguvu ya kuandika makala hii.

Baada ya kushukuru, sasa nipaze sauti yangu, niwapigie kelele kwanza wabunge na kisha Bunge kwa ujumla wake na mwisho serikali yetu.

Kwa muda wote ambao nimekuwa nikifuatilia shughuli za Bunge letu, nimekuwa nikiliona kama taasisi isiyokuwa na nguvu hata ya kufanya yale ambayo inaruhusiwa kisheria, Bunge lisilokuwa na haki ya kukagua na kujadili mikataba kati ya serikali na wawekezaji.

Katika kikao cha Bunge kilichomalizika wiki iliyopita, Watanzania walisubiri kwa hamu kusikia wabunge wakijadili mkataba mbovu kabisa uliosaniwa hivi karibuni kati ya serikali na kampuni ya Richmond.

Pamoja na huo, ipo mikataba mingine ambayo naamini Watanzania walikuwa na hamu ya kuwasikia wawakilishi wao wakiijadili mikataba kuwa ni pamoja na ile ya wawekeaji wa sekta ya madini ambayo Rais Jakaya Kikwete alikwishakiri kuwa ina upungufu na akaahidi kuwa itafanyiwa marekebisho.

Nimejiridhisha kabisa kuwa serikali inafanya makusudi kukataa kuitoa mikataba hii kwa wabunge, kwa sababu inatambua kuna 'madudu' ya ajabu katika mikataba hiyo, ndiyo maana ilikataa kutoa mkataba wa kampuni ya Richmond licha ya Kamati ya Uwezeshaji na Biashara kuagiza ipewe mkataba huo.

Cha ajabu, wakati kamati hiyo ikinyimwa mkataba huo, maudhui ya mkataba huo yalichapishwa katika magazeti binafsi.

Sote tunajua misingi ya demokrasia na utawala bora ni kuwa na Bunge huru na lenye meno.

Kitendo cha kuwanyima wabunge haki ya kujadili mikataba ambayo serikali inaingia na wawekezaji ni ishara kwamba, mhimili mmoja wa dola unaoitwa serikali, unakaidi na kukataa kudhibitiwa au kuwajibika kwa chombo cha uwakilishi wa wananchi kinachoitwa Bunge. Huu ndiyo mwanzo wa ufisadi.

Sasa tunajua kwamba mikataba bomu inayoruhusu rasilimali ya nchi hii kuporwa na wageni ni kitendo cha makusudi chenye maslahi binafsi ya baadhi ya viongozi wakuu wa dola walio katika serikali.

Tuchukulie mfano wa Richmond. Kampuni hii inasadikiwa kuwa ilipewa mkataba na serikali kinyume cha sheria ya manunuzi ya umma ya mwaka 2004.

Wote tunajua kwamba Richmond haikuwa na uwezo wa kujenga vinu vya umeme, ingawa serikali iliipatia mkataba wa dola zaidi ya milion 178.Matokeo ya Kampuni ya Richmond kushindwa kukidhi matakwa ya mkataba, ni kukosekana kwa umeme.

Ili kukwepa aibu hii, wafadhili wa kashfa hii waliibua Kampuni ya Dowans.
Hawa eti wamenunua mkataba wa Kampuni ya Richmond. Hata Mtanzania wa kijijini kabisa sasa anajua kinachochezewa hapa ni kodi ya wananchi kutokana na kutokuwa na watu makini wa kutetea maslahi yao.

Tuukumbuke msemo wa ‘kikulacho ki nguoni mwako’. Msemo huu ni kielelezo cha vitendo vinavyofanywa na watendaji wa serikali yetu ambao baadhi yao sasa wanaonekana kuingiwa na roho ya ufisadi wa kuiba fedha za wananchi kwa kiwango cha kutisha.

Ni hawa ndiyo wasiotaka mkataba baina na Richmond na serikali ujadiliwe bungeni na wanataka vyombo vya habari viwashangilie na kuwasifu kwa ufisadi huu.

Matarajio ya Watanzania ya kusikia kilichomo katika mkataba kupitia kwa wawakilishi wao bungeni yameyeyuka, wawakilishi wao hawawezi kufanya kile wanachokitaka wananchi kwa sababu tu wamenaswa katika ndoano waliyojiingiza ya uanamtandao.

Hawako tayari kuwapigania wananchi wao waliowatuma wakawawakilishe bungeni, badala yake wanaonekana ku0shindana kuwaramba miguu viongozi serikalini katika kile kinachoonekana kusaka uteuele katika bodi za mashirika na tume mbalimbali.

Midomo yao wameitia gundi kali (super glue) na wanaisifu serikali bungeni, lakini 'uswahilini' wakiwa katika vijiwe vyao vya moja baridi na moja moto huku wakibadilisha mawazo na wananchi wa kawaida, wanakuwa vinara wa kuiponda kwa kila aina ya maneno ya kashfa na wakati mwingine matusi kabisa.

Najiuliza, hawa ni wawakilishi wa namna gani kama si wanafiki na watu waliojaa nidhamu za woga, watu wanaoishi kwa staili ya mbwa anayebweka kukiwa shwari, lakini akiona mwizi anakimbia na kufyata mkia?

Nimetafakari na kujiuliza kwa muda mrefu kidogo kuhusu wabunge hawa. Hivi tatizo lao ni nini? Ni kukosa elimu ya kutosha au ni uwoga na njaa? Imani niliyonayo sasa ni kwamba inawezekana kuna rundo la wabunge walio na upeo mdogo wa kusoma na kuielewa miswada mingi iliyondikwa kwa lugha ya Kiingereza ambayo hawataki hata kuisikia. Naamini udhaifu wao huu ndiyo kiini cha tatizo hili.

Ninamini hivyo kwa sababu nina hakika mbunge aliyeghushi vyeti vya elimu yake hana ubavu wa kumdhibiti kiongozi anayeghushi au kuweka saini mikataba bomu. Nayakumbuka maneno ya karibuni kabisa ya mbunge mmoja aliyediriki kusema; ‘Bunge lina meno ya plastiki’.

Mungu ibariki Afrika, Mungu inusuru Tanzania.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili April 29,2009

Kamishna wa kwanza mwanamke wa Jeshi la Magereza Tanzania

Aziza Mursali
Kamishna wa kwanza mwanamke wa Jeshi la Magereza
*Ndiye alikuwa Naibu Kamishna Mwanamke Pekee
*Aeleza siri ya mafanikio yake jeshini
*Awaonya wanawake kutojilegeza

AZIZA Mursali (57) ni mmoja kati ya wanawake wachache waliopata mafanikio makubwa yaliyotokana na bidii na kujituma katika kazi. Akiwa miongoni mwa askari wachache wa kike waliojiunga na Jeshi la Magereza mwishoni mwa miaka ya 1960, alifanikiwa kupanda ngazi za kijeshi hadi kufikia cheo cha Kamishan na kuwa mwanamke wa kwanza katika historia ya jeshi hilo kutunukiwa wadhifa huo. Katika makala hii, Mwandishi Wetu Happiness Katabazi, anamuhoji mwanamama huyo siri ya mafanikio na misukosuko aliyokutana nayo katika maisha yake ya kazi ndani ya jeshi hilo.

Swali: Kitu gani kilikusukuma kujiunga na Jeshi la Magereza?

Jibu: Nilikuwa na mapenzi ya Jeshi la Magereza tangu nilipokuwa msichana mdogo bila kujua ni kwa sababu gani, lakini ilitokea tu nikawa napenda kuwa Askari wa Magereza.
Kama Mungu alijua kuwa nalipenda jeshi, baada tu ya kumaliza masomo yangu nililetewa barua ya kutakiwa kujiunga na Jeshi la Magereza kutoka iliyokuwa Idara ya Kazi wakati huo. Enzi hizo kulikuwa na utaratibu wa vijana wanaomaliza shule kupangwa kufanya kazi katika idara mbalimbali au kujiunga na kozi. Bila kusita niliikubali nafasi hiyo, ndiyo hivyo.

Swali: Wewe ni mwanamke mwenye mafanikio makubwa ndani ya Jeshi la Magereza, siri ya mafanikio yako ni nini?

Jibu: Siri ya mafanikio yangu ni utii, uaminifu, ukweli, juhudi na bidii kazini, lakini kikubwa ni kujiendeleza. Katika maisha yangu nimekuwa nikijiendeleza bila kuchoka, imani niliyojijengea kuwa elimu haina mwisho ndiyo iliyonisaidia na kufika hapa nilipo.

Swali: Wewe ni kiongozi wa kijeshi, kwa cheo chako haina shaka una majukumu mengi na makubwa, unaweza kumudu kazi yako na kutunza familia yako?

Jibu: Ukitaka mafanikio katika kazi yoyote ni lazima ujiwekee taratibu ambazo ni lazima uzifuate, kwa kuzingatia taratibu nilizojiwekea nimekuwa nikipanga ratiba ya kazi zangu na za familia yangu. Ninachofanya ni kuhakikisha ratiba zangu za nyumbani hazivurugi taratibu ya kazi za mwajiri wangu. Ingawa kazi za jeshi ni amri, lakini ninao muda mwafaka wa kuwa na familia yangu, mara nyingi natumia muda wa jioni, siku za sikukuu na likizo. Mwanamke hatakiwi kubweteka, kama tunapiga kelele za usawa ni lazima tuonyeshe kweli tunaweza, na nimekuwa nikifanya kazi kwa bidii siku zote ili kuthibitisha hilo.
Imenisaidia na hata kama ningekuwa si askari na kuwa ninaishi kijiji, ningelima kwa bidii, ni mpangalio tu na uamuzi, kama mtu umeamua kweli kufanya na kazi kuachana na uzembe na utegemezi hakuna kinachoshindikana.

Swali: Kuna madai kuwa nafasi za kujiunga na jeshi zinatolewa kwa upendeleo, ni lazima muombaji awe na mtu anayemjua wa kumfanyia mpango, unalizungumziaje hili?

Jibu: Huo ni uongo. Ajira kwa vijana wanaotaka kujiunga na jeshi zinatangazwa magazetini, pia kuna matangazo mbalimbali yanayobandikwa hadi vijijini kuelezea sifa zinazotakiwa kwa waombaji.
Waombaji hujadiliwa na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na wanaochaguliwa huchujwa na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa, wenye sifa huchaguliwa na Magereza huwa hawabadili uamuzi wa vikao vya Ulinzi na Usalama vya mikoa.

Swali: Kwa mtizamo wako, viongozi wanawake ndani na nje ya jeshi hapa wanatosha?

Jibu: Idadi ya wanawake viongozi hapa nchini haina uwiano sawa na wanaume, hilo liko wazi. Wito wangu kwa Watanzania, kila mtu kwa nafasi yake aone umuhimu wa kuwapa elimu wasichana. Ni lazima tukubali kuwa wanawake wanaweza kuwa viongozi wazuri, inategemea na malezi na jinsi wanavyowezeshwa. Mfano hai ni mimi. Pamoja na wengine ambao tunalitumikia taifa letu katika ngazi mbalimbali za uongozi, wanawake tupo na hivi sasa tunajivunia kuwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro. Kikubwa, nasisitiza hili, ni malezi na kuwezeshwa.

Swali: Ukiangalia enzi ulizojiunga na jeshi na sasa, ukakamavu mliokuwa nao wanawake wakati huo ni sawa na walionao wasichana wa sasa.

Jibu: Sioni tofauti kubwa kati ya askari wa kike wa karne ya 20 na wa karne ya 21, tofauti ndogo iliyopo ni kwamba askari wa kike wa enzi zetu ni wavumilivu sana. Unajua wakati huo wasichana wengi wasomi hawakutaka kujiunga na Magereza, tuliojiunga tulikuwa na nia na dhamira ya kweli ya kulitumikia jeshi, ndio maana tumefanya kazi katika mazingira magumu kwa miaka mingi kwa uaminifu bila kukata tamaa. Lakini kwa hivi sasa watu wanaangalia maslahi kwanza, ule moyo wa kujituma kizalendo umefifia.

Swali: Ni tukio gani kubwa katika maisha yako jeshini au kabla hujajiunga na jeshi ulilokutana nalo ambalo hutalisahau.

Jibu: Ni kifo cha Mwalimu Julius Nyerere…Unajua yule alikuwa kiongozi kweli, ninaweza kusema hata moyo wa kujiunga na jeshi mimi na baadhi ya wenzangu tuliupata kwake. Alikuwa kiongozi aliyekuwa akiwajenga vijana wa Kitanzania kuipinda nchi yao, kuwa na moyo wa kizalendo, tulikuwa tunaipenda kweli Tanzania yetu.

Swali: Kuna haya madai ya kuwapo kwa unyanyasaji wa kijinsia kwa askari wa kike kunakofanywa na askari wa kiume jeshini. Je, madai haya yana ukweli wowote?

Jibu: Ninalolifahamu mimi ni Jeshi la Magereza, hivyo nitalizungumzia hilo. Kwanza kunyanyaswa kijinsia ni udhaifu binafsi. Ukweli ni kwamba ndani ya Jeshi la Magereza hakuna huo unyanyasaji, wala askari wa kike kunyanyaswa na askari wa kiume hakuna Tatizo hapo ni moja nililoligundua mimi - kudeka! Baadhi ya wanawake wanapenda kudeka, na jeshini ni amri ndugu yangu, sasa kama mtu ana tabia ya kudekadeka au kujirahisirahisi, popote pale watadhani kuwa ananyanyaswa.

Swali: Mabadiliko yanayofanywa sasa na serikali katika Jeshi la Magereza unayaonaje, yanawaridhisha ninyi askari?

Jibu: Sana, tena kwa kiasi kikubwa sana. Unajua mahali popote kama unawataka watu wafanye kazi vizuri, ni lazima uwawezesha, si siri, hapo nyuma askari tulikuwa na hali mbaya sana lakini sasa hali imebadilika, serikali inawatupia jicho askari wake na ninaomba iendelee kufanya hivyo.
Tuna mafanikio mengi, mfano tumepewa zabuni ya ujenzi wa nyumba za serikali na tumemudu kuzijenga kwa ubora wa hali juu, magereza mapya yamejengwa sehemu mbalimbali nchini sambamba na upanuzi na ukarabati wa magereza ya zamani.
Lakini hata wafungwa hali zao zimeboreshwa, sasa wanavaa shati na suruali badala ya kaptura zilizokuwa zinadhalilisha utu wao, sasa magereza yana radio za kisasa na televisheni zinazotoa mafunzo burudani kwa wafungwa, haya yote ni mafanikio.
Lakini pia serikali imewakumbuka zaidi wanawake. Sasa yupo mkuu wa Magereza wa mkoa mmoja - Boharia Mkuu wa Jeshi la Magereza mmoja ambaye ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi Edith Malya, Mkuu wa Chuo cha Udereva mmoja, yeye ni Kamishna Msaidizi Grace Ungani, pia yupo Katibu wa Bodi ya Parole Magereza nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Simfroza Bondo pamoja na maofisa nidhamu wa mikoa wawili. Hizi zote ni jitihada za serikali kulifanyia mabadiliko Jeshi la Magereza.

Swali: Tueleze historia ya maisha yako.

Jibu: Nizaliwa 1950 katika Kijiji cha Mazombe, Wilaya ya Iringa Vijijini. Mimi pamoja na ndugu zangu tisa tulilelewa na mama baada ya baba kufariki mwaka 1958 tukiwa bado wadogo.
Mama ni mkulima, aliolewa na mwanamume mwingine baadaye, baba yetu huyo wa kambo alitusomesha mimi, kaka yangu na wadogo zangu watatu hadi elimu ya sekondari, huwa tunamshukuru sana baba huyu.
Nilihitimu masomo ya sekondari mwaka 1968 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara. Na mwaka huo huo nilijiunga na Jeshi la Magereza. Kituo changu cha kwanza cha kazi kilikuwa Gereza la Wanawake KPF – Morogoro.
Mwaka 1969 nilihudhuria mafunzo ya uaskari katika Chuo cha Magereza Ukonga kwa muda wa mwaka mmoja. Mwaka 1971 nilirudi tena katika Chuo cha Magereza Ukonga kwa kozi fupi ya uongozi na mwaka huo huo nilikwenda kusoma Elimu ya Siasa katika Chuo cha Kivukoni. Baadaye mwaka 1974 nilijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama mwanafunzi wa nje wa chuo, ambako nilisoma kozi ya sheria na nilihitimu na kutunukiwa cheti mwaka 1976.
Mwaka 1976 nilikwenda tena Ukonga kusoma kozi ya Gazzetted Officer na baadaye mwaka 1981 nikarudi Kivukoni kwa ajili ya kozi ndefu elimu ya siasa na kisha mwaka 1984 nilikwenda nchini Burgaria kwa ajili ya kozi ya mwaka mmoja ya Social Science & Management course.
Hivi sasa ninasomea Shahada ya Sheria (LLB) katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania nikiwa mwaka wa mwisho.
Katika kipindi changu cha utumishi ndani ya Jeshi la Magereza nilishika pia wadhifa wa Katibu Msaidizi Mkuu wa Chama wa Mkoa wa Majeshi kwa muda wa miaka mitano Nilikuwa Katibu Mkuu Msaidizi wa Chama wa Mkoa wa Majeshi kabla ya Tanzania haijaingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa 1992.
Mkoa wa Majeshi ilikuwa ukiundwa na vikosi vya Ulinzi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Polisi na Magereza.
Katika vipindi tofauti nimefundisha katika vyuo vya kijeshi kikiwamo Chuo cha Usalama Moshi na Chuo cha Maofisa wa Magereza Ukonga. Aidha, nimewahi kuwa Mkuu wa viwanda vya Magereza nchini, hivyo naamini nina sifa za kuwa kiongozi.
Niliteuliwa kuwa Kamanda wa Magereza Mkoa wa Kagera Oktoba 17, 2003. Nimeolewa na Said Kangwi, mwenyeji wa Kijiji cha Mkanyageni, Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga. Nina watoto wanne - wasichana watatu na mvulana mmoja.
Katika maisha yangu ya utumishi jeshini nimetunukiwa medali mbalimbali ikiwamo ya utumishi uliotukuka niliyotunukiwa mwaka 1996 na nishani ya utumishi wa muda mrefu mwaka 1999.Na Agosti mwaka huu nilipandishwa cheo na kuwa Kamishna mwanamke pekee magereza, kabla ya kupandishwa cheo hiki nilikuwa na Cheo cha Naibu Kamishna ambacho nimedumu nacho kwa miaka mitatu na wakati wote nikiwa na cheo hicho cha DCP nilikuwa nacho mwanamke peke yangu.

0755 312859:katabazihappy@yahoo.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima, la Jumapili April 29,2007

DPP kijana anayeingia ofisini na msahafu wa Sheria


ELIEZER MBUKI FELESHI

.Ndiye DPP mpya Tanzania, ana miaka 39
.Apania kumfuta tongotongo Rais Kikwete
.Aliungurumisha kesi ya MV Bukoba
.Adai ilijaa mambo ya ajabu, ataka kutungia kitabu
.Uhaba wa wanasheria wampasua kichwa

HIVI karibuni Rais Jakaya Kikwete, alimteua mwanasheria mwandamizi wa serikali, Eliezer Mbuki Feleshi (39), kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP). Uteuzi wa Feleshi ambaye alijizoelea sifa nyingi wakati wa kesi ya MV Bukoba aliposhiriki kama mwendesha mashitaka msaidizi na mchango mkubwa alioutoa katika tume ya kuchunguza mauaji ya wafanyabishara wanne wakazi wa Mahenge, ambayo iliwatia hatiani polisi, umekuwa ukielezwa na baadhi ya watu kama muarobaini wa ofisi hiyo. Katika makala hii MWANDISHI WETU HAPPINESS KATABAZI, anamuhoji jinsi alivyoupokea uteuzi huo, na pia alivyojiandaa kukabiliana na changamoto za ofisi hiyo.

Swali: Kuteuliwa kwako na Rais Jakaya Kikwete, kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) katika umri mdogo ulionao, kumedhihirisha jinsi rais alivyo na imani na utendaji kazi wako, umeupokeaje uteuzi huo?
Jibu: Nimeupokea kwa heshima kubwa. Natambua kuwa rais ananiamini na ndio maana akafikia uamuzi wa kunitwisha mzigo huu mzito katika umri mdogo nilionao.
Lakini uteuzi wangu nina hakika umezingatia sifa zilizowekwa kikatiba za mtu anayestahili kuteuliwa kushika wadhifa huu, binafsi ninafarijika kwamba, Mheshimiwa Rais aliisoma katiba kabla ya kuniteua, na aliporidhika, ndipo akaniteua.
Ni fahari kwangu, familia yangu, vijana wenzangu na taifa kwa ujumla, kuwa na vijana wanaoweza kuaminiwa na kukabidhiwa majukumu makubwa kama hili la kuongoza ofisi nyeti na kubwa.
Kazi iliyopo ni kuhakikisha kuwa simuangushi rais wangu na Watanzania kwa ujumla, nimepania kuwaonyesha kuwa vijana tunaweza kazi.

Swali: Umejipanga vipi kuthibitisha kuwa unaweza?

Jibu: Jambo la msingi ambalo nitalizingatia siku zote, nitakapokuwa katika ofisi hii, ni kutekeleza majukumu yangu kwa kuzingatia taratibu na misingi ya sheria ambayo ndio muhimili mkuu wa ofisi hii.
Misahafu ya sheria haidanganyi hata siku moja, na mimi ni muumini wake mkubwa, siku zote nimekuwa muumini wa sheria na ninaziishi, na kwa imani yangu hiyo ambayo imenipa mafanikio tangu nikiwa ngazi za chini, naamini nitafanya kitu kitakachomtoa tongotongo rais wangu.
Mimi na wenzangu tumeshajipanga, na bado tunaendelea kujipanga, sina cha kueleza zaidi katika hili…, unajua ofisi kama hizi ndugu yangu mambo mengine yanabaki ya kiofisi, lakini ninachotaka kuwaambia Watanzania ni kwamba, nitaiendesha ofisi hii kwa kufuata taratibu na sheria za nchi.
Bahati nzuri ni kwamba, kuna maofisa wengi tu hapa waliobobea katika fani ya sheria ambao utendaji wao, ninaamini kabisa kuwa hauna shaka hata kidogo, na tangu awali nilikuwa nikifanya nao kazi pamoja, na kwa ushirikiano wa dhati.
Majukumu tuliyokuwa tukitekeleza pamoja hapo awali, si kwamba yatabadilika baada ya mimi kuingia ofisini hapa, hapana, kimsingi ni yale yale, lakini ninachotaka tufanye kwa sasa ni kuhakikisha tunasonga mbele kukabiliana na changamoto zilizopo kwa kuwa nyakati zinabadilika kwa kasi sana.
Na ieleweke kuwa ofisi ya DPP ni ya kikatiba, si ya mtu binafsi, wala haitawaliwi kwa msingi wa umri, bali inaongozwa na mtu anayeonekana kuwa na sifa ya kupewa wadhifa huo. Watangulizi wangu waliteuliwa kushika wadhifa huo si kwa kuwa na umri mkubwa, bali kwa kuwa walikuwa na sifa za kuongoza ofisi hii.

Swali: Kuna malalamiko mengi ya kucheleweshwa kwa upelelezi wa kesi, hasa za mauaji, hili umelipangia mkakati gani?

Jibu: Kesi ni ushahidi, na ushahidi unapatikana kwa kuukusanya. Jamii inao wajibu wa kushirikiana na taasisi zinazofanya upelelezi ili kuharakisha kazi ya kukusanya ushahidi. Kwa nyakati fulani wananchi wamekuwa waoga kutoa ushahidi au wakati mwingine kuutoa kwa wasiwasi.
Kuna wakati wapelelezi wamezorota kufanya kazi zao na kuna wakati wamejitahidi, ila wanakwamishwa na nyenzo.
Kwa sababu hiyo, sipingi kuwa kuna malalamiko kama hayo kutoka kwa jamii, yapo, na ili kukabiliana na hali hiyo, nitaanza kwa kulifanyia kazi tatizo la vitendea kazi, pili ofisi yangu itafanya jitihada za makusudi za kuwaomba wananchi kushirikiana na waendesha mashitaka katika kukusanya ushahidi.
Kikubwa ni kuwaelimisha wananchi kuwa, wanayo sehemu yao ya kutoa taarifa dhidi ya wapelelezi wasio waadilifu, hasa kama wapelelezi wanawazungusha kupokea ushahidi wanaowapelekea, ninaamini nitafanikiwa kuondoa malalamiko hayo.

Swali: Idara yako ina wataalamu mahiri wa kutosha kuweza kukabiliana na changamoto zinazoikabili sasa?

Jibu: Wataalamu wazuri wapo, ila ukweli ni kwamba, hawatoshi. Hili ni tatizo. Mmmm, ni tatizo hili... Nchi ni kubwa na inayo mahitaji mengi. Na idara hii ni eneo lenye changamoto nyingi na kubwa. Hivyo kuna kila sababu ya kuwatambua kwa karibu wataalamu wachache waliopo na kuwathamini, na hili ni kwa idara zote zilizo chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Swali: Kuna mpango wa kutenganishwa kwa wapelelezi wa kesi za jinai na waendeshaji wa kesi za jinai, utekelezaji wake utaanza hili?

Jibu: Inatakiwa ieleweke kuwa, hapatakuwa na wakati wa mpelelezi na mwendesha mashitaka kufanya kazi bila ushirikiano wa karibu, kutokana na kutegemeana kwa kazi zao.
Kinachokusudiwa kufanyika ni kuiwezesha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka kuwa na waendesha mashitaka wa kutosha ili wao kama waendesha mashitaka, wafanye kazi ya kuendesha mashitaka na wapelelezi waimarishe kazi ya kupeleleza na kuwasaidia waendesha mashitaka kupata ushahidi.
Hivyo askari polisi wanaoendesha kesi leo kwa kupewa kazi hiyo na DPP, watapata fursa nzuri ya kufanya kazi za kupeleleza kesi za watuhumiwa mbalimbali.
Uimarishaji wa mkakati huu ulishaanza, na mwaka ujao wa fedha tunatumaini, baadhi ya maeneo ya nchi yetu, wataanza kushuhudia kesi zikiendeshwa na maofisa kutoka ofisi ya DPP, kuanzia ngazi ya wilaya.

Swali: Hili la kutengenisha majukumu haya likifanyika, ofisi yako itakuwa na mamlaka gani ya kuhakikisha kesi zinaendeshwa katika muda unaotakiwa?

Jibu: Upelelezi ni taaluma iliyo na mafunzo, mbinu na miiko yake, na haitegemei zoezi la kutenganisha kazi ya upelelezi na uendeshaji mashitaka. Hivyo tangu awali wapelelezi wanatakiwa kupeleleza kesi kwa umahiri na haraka.
Lakini ni matarajio yangu kuwa Ofisi ya DPP itakapoanza kuendesha kesi nchi nzima au katika maeneo machache, polisi waliokuwa awali wanahusika kwenye zoezi la kuendesha mashitaka, watapata fursa nzuri ya kuongeza nguvu kwenye eneo la upelelezi.

Swali: Unazungumziaje madai kuwa baadhi ya mawakili wa serikali hawana ujuzi wa kutosha, na kwamba mishahara midogo inawafanya baadhi yao, wajihusishe na vitendo vya rushwa?

Jibu: Ujuzi haununuliwi, unatokana na mafunzo na utendaji wa mtu mwenye bidii ya kujifunza, kuna mawakili wengi wanafanya kazi vizuri ingawa wana mishahara midogo.
Mshahara mdogo si kigezo cha kula rushwa. La msingi ni kuangalia jinsi ya kumwezesha wakili awe na mshahara mzuri, utakaomwezesha kupangilia mambo yake kwa uhakika, aweze kununulia vitabu vya kujisomea na nyenzo nyingine za kazi, jambo ambalo viongozi wetu wanapaswa kuliangalia kwa jicho makini.

Swali: Una maoni gani kuhusu watu wanaopinga mamlaka makubwa aliyonayo DPP?

Jibu: Katiba iko wazi, na sioni sababu ya kuliongelea hili. Huenda kinachoweza kuangaliwa ni kama kuna ukiukwaji au matumizi mabaya ya madaraka ya DPP. Unajua DPP kama taasisi, hawezi kuwa na tatizo, ila tatizo linaweza kuwa kwa mtu anayeweza kutumia madaraka hayo vibaya, kitu ambacho kitahitaji ushahidi.

Swali: Unaridhika na mfumo wa uendeshaji mashitaka hapa nchini?

Jibu: Siyo mmbaya, naweza kusema unaridhisha, lakini pia ni lazima nikiri kuwa kuna mapungufu yanayosababishwa na uhaba wa vitendea kazi.
Kama nilivyoeleza awali, wataalamu hawatoshi na kuna tatizo la mashahidi kutokupatikana kuja kutoa ushahidi, na hasa katika maeneo yaliyo na mila na desturi za kufanya mapatano ya kutozana fidia.

Swali: Ni tukio gani unalolikumbuka, liwe zuri ama baya katika maisha yako?

Jibu; Ninayo mambo mengi, lakini kubwa ni kesi ya MV Bukoba ambayo nilikuwa mwendesha mashitaka, nikimsaidia Wakili Mkuu wa Serikali W.C. Magoma.
Kesi hii ilikuwa ya mauaji, mamia ya watu walipoteza maisha yao, mashahidi wengi walipokuja mahakamani na kutoa ushahidi, ilinibidi kuwa makini sana, kulikuwa na mambo ya ajabu sana katika kesi hiyo, ni vigumu kuelezea, labda kama kuna siku nitaandika kitabu, nitaeleza kwa unaga ubaga.
Mahakama ilikuwa ikigubikwa na simanzi kila siku kesi hii ilipokuwa ikisikilizwa, kama binadamu, hata mwendesha mashitaka kuna wakati unakuwa na majonzi kama hao waliofiwa na ndugu na jamaa zao, lakini kazi kwanza, nilikuwa natakiwa kusimamia ukweli.

Swali: Tueleze historia ya maisha yako kwa mapana zaidi.

Jibu: Nimezaliwa Julai mosi, mwaka 1967, katika Kijiji cha Malya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, nikiwa mtoto wa mwisho kati ya watoto tisa wa familia yetu ya mzee Mussa Mbuki Feleshi na mama yangu Ruth N’gweshemi.
Baba yangu alikuwa mchungaji wa Kanisa la African Inland Church na mama alikuwa mama wa nyumbani.

Baba yangu alifariki mwaka 1973 kwa ajali ya gari na mama yeye alifariki mwaka 1991, wakati huo nikiwa mwanafunzi wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Nimesoma Shule ya Sekondari Shinyanga, baadaye nilijiunga na Shule ya Sekondari Galanos mkoani Tanga ambako nilisoma kidato cha tano na sita.

Baada ya kumaliza kidato sita nilijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT Ruvu).
Nilijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1991, nikichukua shahada ya kwanza ya sheria na kuhitimu mwaka 1994. mwaka 2003 nilirudi tena Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusoma shahada ya uzamili ya sheria (Masters in Law), nilihitimu mwaka 2005.
Kabla ya kuteuliwa kuwa DDP, nilikuwa Mwanasheria wa Serikali na kituo changu cha kazi kilikuwa mkoani Mwanza.

Hivi sasa ninasoma Shaha ya Udaktari wan Sheria PhD in Law Criminology and Penology. Nina mke mmoja, Suzana Majija, ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Nyamagana mkoani Mwanza na tuna watoto wanne.

0755 312859:katabazihappy@yahoo.com:www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo;Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, April 15,2007

Ukimya wa wazazi wa wanafunzi wa elimu ya juu unamaanisha nini?

Na Happiness Katabazi

ELIMU, kama zilivyo sekta nyingine ina wadau ambao si haba. Wadau hao uhusika kwa namna moja au nyingine katika kuamua mustakabari wa sekta husika.

Hapa nchini, wadau wa Elimu ni pamoja na Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Jumuiya za wahisani, Taasisi na Mashirika mbalimbali, Taasisi za elimu, Wazazi, walimu na wanafunzi,asasi za kidini.

Mchango wa kila mdau katika ya elimu katu haupuuziki kwa kuwa ni mkubwa na wa maana sana. Matharani, wadau hawa wanawajibika kugharimia elimu, kuendesha mchakato wa siku hadi siku mashuleni au vyuoni, na vilevile kushawishi (influence) mitaala itumikayo mashuleni.

Lakini, mara kadhaa baadhi ya wadau wameonekana kusahau wajibu wao huo na kukaa pembeni, hata wasijihusishe katika mambo yanayoipata sekta ya Elimu kana kwamba ama hayawahusu au hakuna umuhimu wa wao kuyashughulikia.

Nitoe mfano wa ambayo yamekuwa yakijiri hapa nchini katika vyuo vyetu vya Elimu ya Juu. Vyuo hivi vimekumbwa na matatizo mengi tokea enzi za uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julias Nyerere hata leo. Kumekuwa na matatizo kama vile migomo ya wanafunzi ambavyo sasa imegeuka kuwa kana kwamba ni moja ya sifa kuu za vyuo vikuu vya Tanzania.

Katika tukio la hivi karibuni (mwezi huu April, 2007), wanafunzi wa vyuo hivyo waligoma kuingia madarasani wakipinga kulipia moja kwa moja asilimia arobaini (40%) ya karo yao ya kila mwaka wa masomo. Mgomo huo ulisababisha vyuo vifungwe na baadaye wanafunzi wakatangaziwa masharti mazito yapatayo tisa (9) ambayo pasipo kutimizwa kuyatimiza, katu mwanafunzi asiote kurejea masomomi katika chuo husika.

Naam, nafasi za baadhi ya wadau wa Elimu katika kushughulikia masuala ya elimu ilijionesha wazi katika hili. Mdau serikali, kipitia mamlaka aliyopewa Makamu Mkuu wa Chuo aliwatimua wanafunzi, kisha kupitia Naibu waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia na Waziri Mkuu, mdau Serikali akawalaumu wanafunzi kwa kugoma na akabariki hatua ya kutimuliwa kwao.

Kwa upande wake wadau taasisi na mashirika, matharani vyama vya siasa CUF, TLP, NCCR, CHADEMA na NGOs kama TANLET, wakapinga kufukuzwa kwa wanafunzi na kuwataka wahusika wavifungue vyuo bila masharti.
Kinachogomba hapa ni kwamba, yu wapi mdau/wadau wakuu waitwao WAZAZI katika hili? Mbona wazazi mko kimya mara zote katika matatizo ya watoto wenu wanaosoma vyuo vikuu?

Siamini kwamba nafasi yenu wazazi inaishia katika kuwagombeza wana wenu wanaporejeshwa mara kwa mara majumbani mwenu eti kisa wamegoma. Haiingii akilini mwa mtu anayefikiri vizuri kwamba wazazi mnaona ni vyema kunyamaza kimya ilihali mnajua kabisa kwamba baadhi yenu watoto wenu hamjawaona huko nyumbani tokea wafukuzwe.

Sijui mnajisikiaje mnaposikia kwamba baadhi ya wanafunzi hao wanazagaa jijini Dar es Salaam ama wakiuza mali zao na pengine miili yao ili wajikimu katika kipindi ambacho hata hawajui ni kirefu kiasi gani.

Dhalau (kudharirishwa) hii inayowapata wana na mabinti zenu si tu itakiongezea kizazi hiki laana bali itawafanya hao wanafunzi wajapohitimu, virusi vya ukimwi wanavyovichota katika kipindi hiki havitawaruhusu walitumikie taifa na wala hawatakuwa na nguvu za kurejesha hiyo mikopo wanayopewa ili wasome.

Sidhani mko tayari kuuza mashamba yenu ili mlipe, mikopo waliyopewa watoto wakaaga dunia kabla ya kuirejesha kupitia nguvu kazi zao.Pengine kwa kuwa kuna baadhi ya watanzania hatupendi kufikiri juu ya kesho, hayo madhara ya baadaye twaweza kuyapuuza.

Lakini lipo ambalo wazazi hamtalipuuza maana linawahusu ninyi moja kwa moja; nalo ni masharti 9 waliyopewa wanafunzi.Mojawapo ya masharti hayo ni kwamba watoto wenu hawatarejea vyuoni hadi walipe 40%.

Ukweli ni kwamba sharti hii hawajapewa wanafunzi bali ninyi wazazi na walezi. Kazi kwenu, mnatakiwa mlipe hizo fedha japo watoto wenu waligoma wakidai ninyi wazazi mlio wengi hamna uwezo wa kulipa kiasi hicho.

Pengine baadhi yenu mmeshaanza kulipa au mnakusudia kufanya hivyo. Fanyeni hima basi ili ithibitike kwamba wanafunzi ni waongo na wakorofi tu maana kumbe wazazi mnao uwezo wa kulipa bila matatizo.

Au ithibitike vinginevyo, kwamba wanafunzi walisema ukweli maana wanazijua fika hali za familia walikotokea. Naamini katika upande wa kwamba, wanafunzi walisema UKWELI. Ni mtanzania yupi asiyejua kwamba nchi hii licha ya kubarikiwa kwa utajiri wa Rasilimali, wanaoufaidi utajiri huo ni tabaka dogo la walanchi na maswahiba wao kutoka nchi za nje, wanaoifyonza nchi hii hadi inyauke kwa kisingizio cha soko huria na uwekezaji.
Wazazi (wananchi) wa kitanzania walio wengi ni wakulima hohehahe ambao licha ya uduni wa zana zao za uzalishaji, kizalishwacho mashambani kinakosa soko, kiasi kwamba kumudu maisha ya kila siku ni msamiati mgumu kwa familia nyingi, sembuse kulipia elimu ya chuo kikuu!

Ama si ninyi wazazi mlioshindwa kulipa UPE na UMITASHUMTA wa shilingi 2000/= tu hata ada hiyo ikafutwa, mtayaweza ya laki tano (500.000/=) na ushehe, jumlisha na mkopo wa asilimia sitini (60%) juu?Yamkini yote haya wazazi hamyaoni hata mngali mwaendelea kunyamaza. Mjapo lipa hiyo 40% kumbukeni yafuatayo.

Mosi, mtakuwa mmebariki Serikali ijitoe moja kwa moja katika kugharimia elimu ya juu maana sasa kila mzazi atamsomesha mwanae chuo kikuu kwa kugharimia asilimia 100% ya mahitaji, wakati huo huo mkilipa Serikali kodi sijui ikatumie fungu hilo kufanyia ziara za ughaibuni na manunuzi ya mashangingi,kujenga mahekaru,rada butu na madege ya anasa.

Pili, kwa kuwa alipiaye kilo moja ya Sukari dukani hamtarajii mwenye duka ampimie nusu kilo, na katu hata mtoto mdogo hataondoka penye dirisha la duka hadi apewe kiasi timilifu cha bidhaa aliyolipia, ni wakati wenu sasa wazazi kwa kushirikiana na wanafunzi watoto wenu, kuhakikisha kwamba hiyo elimu mtakayokubali kuilipia 100% ubora wake usiwe chini ya thamani hiyo. Itakuwa ni “uzumbukuku” endapo mtagharimika kiasi hicho alafu watoto wenu waendele kupatiwa elimu isiyowawesha kuajirika au kujiajiri.

Eti mlipe gharama hizo, alafu wana na mabinti zenu waendelee kujifunza wakiwa wamesimama nje ya vyumba vya madarasa wanasikiliza Mhadhara (Lecture) kwa kuwa madarasa yamejaa pomoni!

Ati mlipe mamilioni, alafu katika mabweni watoto wenu walale ‘mzungu mchongoma’ kana kwamba wako gerezani. Mtoe fedha lukuki alafu wanafunzi wapatiwe muda kichele wa mafunzo kwa vitendo. Waulizeni wakupeni ‘orodha mnyororo’ ya matatizo yanayowasibu wawapo masomoni.

Mjikamue kisawasawa alafu kizazi chenu kipate huduma mbovu za maktaba zenye vitabu na vifaa visivyotosheleza. Mjitoe mhanga kugharimia alafu wasomi wenu wagombanie komputa chache zilizopo vyuoni kana kwamba ni wa cheza mpira na refa kaamuru kona. Mtoe fedha za kilo moja ya mchele, mnyamaze kimya msiwaulize wana wenu iwapo mwenye duka ni kweli kapima kila moja, sufuria jikoni ikipwaya msimlaumu mtu bali ukimya wenu.

Nikusihi au nikuulize ewe mzazi, wapi udau wako katika elimu; ni upi msimamo wako kuhusu migomo ya wanafunzi na hatua ambazo serikali inawachukulia. Wapi sauti ya Jumuiya ya Wazazi Tanzania , wapi kauli ya umma wa watanzania. Mwathubutuje kunyamaza wakati mustakabari wa watoto wenu na taifa kwa ujumla uko mashakani! Haifai mkanyamaza kama kwamba kuna mliyemwajiri awasemee.

0755312859;katabazihappy@yahoo.com;www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Tanzania Daima la Jumatano, April 25,2007.

Ukaidi wa Malima,unabomoa nguvu za Bunge?

(Sauti ya Jumapili) April 8,2007,Easter day

Na Happiness Katabazi

HIVI karibuni baadhi ya vyombo vya habari vilimkariri Mbunge wa Mkuranga Adamu Malima, kwamba hayupo tayari kwenda ofisini kwa Spika wa Bunge Samwel Sitta, kwaajili ya kupatanishwa na Mwenyekiti wa Makapuni ya IPP, Reginald Mengi, kwakuwa hana ugomvi naye.

Vyombo hivyo vya habari kwa nyakati tofauti pia vilimkariri Mbunge huyo, kwamba akubaliani na uamuzi wa Spika, na badala yake amewasilisha malalamiko yako kwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuf Makamba, ya kwamba amezalishwa na uamuzi ulitolewa Spika Sitta bungeni hivi karibuni.

Pia vyombo hivyo vilimkariri Makamba, ambaye alikiri kupokea malalamiko ya Malima, dhidi ya Spika Sitta kwakuwa hawa wote ni viongozi ndani ya CCM, ambaye hata hivyo alisema lalamiko hilo litaongelewa katika vikao husika vya chama.

Kwa wale kama mimi tunaofuatilia masuala ya siasa za hapa nchini na mustakabali wanchi yetu mtakuwa mmesikia na kuzisoma kauli za viongozi hao kupitia vyombo vya habari hivi karibuni.

Uamuzi uliotolewa bungeni hauwezi kupingwa kwenye chombo cha chama siasa na hilo likifaulu ni kuvunja mamlaka ya bunge na kufanya bunge letu tukufu kuwa ni kichekesho kubwa sana.

Ieleweke kwamba wabunge na hata Spika wa bunge ni wanachama wa vyama vyao lakini ikiwa vikundi ndani ya Chama Tawala (CCM) , kinatumika kudhoofisha mamlaka ya bunge ni hatari kwa demokrasia hapa nchini.

Inawezekana kwamba uamuzi wa Sitta, kuhusu sakata la mbunge huyo na Mengi,aliutoa bungeni mapema mwaka huu, haukukubaliwi na kundi la Malima ambaye hivi sasa anatazamwa kuwa yeye ni chambo,kuadi wa vigogo ndani ya CCM katika kupigania madaraka siku za usoni.

Lakini kubomolewa kwa Spika Sitta ni kubomolewa kwa mamlaka ya bunge na inawezekana kuleta mtafaruku mkubwa ndani ya CCM.Na si mtafaruku pekee, pia linadharirisha CCM, na viongozi wa chama hicho ambao wengine ni viongozi wa kuu ndani ya serikali.

Pia kutaitimisha minong'ono inayoongelewa chini chini hivi sasa,ya kwamba viongozi wengi wa awamu hii ni wasanii na wanaendesha nchi hii kisanii na ambao nyoyo zao zimejawa na uchu wa madaraka na wapo madarakani kwaajili ya maslahi yao binafsi.

Lile sakata la Malima na Mengi, lilionyesha mgawanyiko mkubwa katika vigogo ndani ya CCM na kilichokuwa kinaonekana wazi ni makundi ambayo yalikuwa yanajipendekeza na kujikomba kwa Rais Jakaya Kikwete, kwa kisingizio cha kumtetea Rais hatangazwi vizuri na apewi muda wa kutosha na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Mengi.

Sasa kama Malima anafikiri hilo linaweza kutatuliwa kwa siri ndani ya CCM amekosea sana.Binafisi si mtetei Sitta wala Mengi, lakini umbeya na uzandiki wa jambo lenyewe hautoshi katika vita vya kumng’oa Sitta katika cheo chake cha Uspika.

Na ninashanga hadi sasa Sitta kutomchukulia hatua mbunge huyo baada ya kukaidi amri ya bunge. Kwa hili Malima kukataa amri ya Sitta inavyoonekana vita vya kugombea urais ndani ya CCM vimeanza na bila shaka Malima ni kuadi au mpiga debe wa mgombea urais ajaye na ndiye anayempa jeuri na kibri.

Viongozi wetu mtambue hili kwamba lengo la kuwa viongozi ni kuongoza wananchi ili wajiletee maendeleo na kazi ya kiongozi ni kuwafikisha hapo wananchi.

Sasa kiongozi anapozua mjadala ya kitaifa isiyo na kichwa wala miguu ni kuiletea taifa hasara.Watanzania ebu tufikirie hoja ya Malima na Mengi imetughalimu fedha kisasi gani za walipa kodi? Ebu angalia Taifa limetumia muda gani wa watu walioshiriki katika hoja hiyo?.

Ebu fikiria tu wananchi huko mitaani walioshiriki katika hoja hiyo badala ya kufanya shughuli za maendeleo. Narudia tena Malima hoja yako siyo ya msingi na kamwe haileti tija kwa taifa hili.

Malima alikuwa akimtuhumu Mengi kuwa anatumia muda mwingi kujitangaza yeye kwenye Televisheni yake ya ITV kuliko viongozi wa nchi, lakini kwasasa tunachokishuhudia kufanywa na mbunge huyo ni anatumia muda mwingi wa wananchi kumjadili tena yeye anatumia vyombo vingi vikiwemo vya habari na CCM.

Nimalizie kwakumwambia Malima, kuwa mwisho wa ubaya ni aibu kwahiyo usipoangalia utakuja kuumia kwa aibu kwani unaweza kuwa unatumiwa bila wewe kujua na wajanja wakawa wamevuna wakakuacha kwenye mataa.

Mungu ibariki Afrika, Mungu inusuru Tanzania
0755 312859;katabazihappy@yahoo.com;www.katabazihappy@blogspot.com

Chanzo;Gazeti la Tanzania Daima