Mgomo wa Vyuo Vikuu ni Matokeo ya Uzembe wa Watawala

Na Happiness Katabazi

JUMAMOSI iliyopita, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Pro.Rwekaza Mukandara alitoa tamko la Chuo hicho la kuruhusu wanafunzi wote kurejea masomoni isipokuwa viongozi wao 56.

Kwa kiasi kikubwa uamuzi huo umetekeleza masharti yaliyotolewa na vyama vya siasa kwamba wanafunzi warejeshwe vyuoni bila masharti.

Tamko la chuo lilisema kwamba japokuwa asilimia 41 tu ya wananchuo wote ndiyo waliotekeleza masharti yaliyokuwa yametolewa na chuo na chuo sasa kimeamua kuwarejesha masomoni wanafunzi wote bila kujali kama wamelipa au hawajalipa asilimia 40 ya ada kwa wale wa mwaka wa kwanza na fedha za matibabu kwa wote.

Kulingana na tamko hilo chuo kiko tayari sasa kushirikiana na bodi ya mikopo kuchuja wanafunzi ili wapatiwe mikopo kulingana na mahitaji.

Kwa wachunguzi wa mambo tamko hilo la Professa Mukandara limeonyesha wazi jinsi gani uzembe wa watawala unavyoweza kuliletea taifa hasara.

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, peke yake kimepata hasara ya Sh Milioni 100 kila siku tangu kilipofungwa April 17 mwaka huu.Kiasi hicho ni jumla ya bilioni tatu.Hiki ni kiasi kikubwa sana ukilinganisha na Sh Milioni 500 ambazo wangelipwa wanafunzi kama madai yao ya gharama ya mafunzo kwa vitendo walipwe.

Ni jambo la kushangaza kama watawala wa chuo au hata serikali wanaamini kuwa dai la nyongeza ya gharama ya elimu kwa vitendo kutoka sh 3,500 hadi 6,500 wanazodai hazilingani na gharama halisi.Ukweli ni kwamba kiasi walichodai wanafunzi ni kidogo mno kulingana na gharama halisi za maisha.

Tujadili hoja ya gharama za elimu ya Juu sera ya kuchangia haipo tena.Wanafunzi na wazazi wao wanalipia asilimia 100 na serikali haichangii chochote.

Hayo ndiyo mantiki ya sheria ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ya mwaka 2004.Kwa mujibu wa sheria hiyo gharama yote ya elimu ya juu itabebwa na mwanafunzi mwenyewe na mzazi wake mfadhili wake.

Serikali inawajibika kuipatia bodi ya mkopo kiasi cha fedha kinachotosha mikopo ya wanafunzi waliodahiliwa na vyuo vikuu.

Mgogoro uliopo hivi sasa ni matokeo ya uongozi wa serikali ya awamu ya nne kukiuka sheria ya uanzishwaji wa bodi ya mikopo ya mwaka 2004.Serikali ya awamu ya nne imetafsiri mikopo ya wanafunzi kuwa ni ufadhili(scholarship) na hivyo kuamuru kuwa kigezo cha kutoa mkopo kiwe daraja kwanza kwa jinsia zote na daraja la kwanza na pili kwa jinsia ya kike.

Sasa sio tu kwamba serikali haikuwa na mwelekeo wa kutoa amri hiyo kwa mujibu wa sheria ya bodi ya mikopo bali amri hiyo ilinyang’anya bodi ya mikopo madaraka na wajibu wake wa kuchuja na maombi ya mikopo ya wanafunzi walikanga na kigezo cha mhitaji.

Matokeo ya hili ni kwamba serikali kupitia bodi ya mikopo ilijikuta inatoa mikopo kwa waombaji wasiyostahili na kuwanyima wake wanaostahili.

Tamko la Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mukandara kuwa sasa kigezo kilichowekwa na sheria ya mikopo ya wanafunzi kitafuatiwa au kuzingatiwa ni jambo jema lakini pia ni ushaidi kuwa utawala wa chuo na serikali unakiri makosa yake.

Hivi ndiyo inatufanya tuone kwamba kuzuiliwa au kufukuzwa kwa viongozi 56, si sahii na ni mwendelezo wa kiburi cha watalawa.Wao wanataka ‘Kondoo wa kafara’ watakaoikosha serikali na uongozi wa chuo ili wasionekane kuwa wamekosea au kushindwa.

Tujiulize kama hao viongozi wa chuo wana elimu mwafaka kuhusu Utawala Bora?. Je si wakati mwafaka sasa wa kuanzisha chuo cha viongozi?.

Tunajua fika uongozi wa sasa wa wanafunzi wa UDSM ni mpya na bila shaka usio na uzoefu na maharifa ya uongozi.'Kubangaiza' kama ambavyo uongozi huo umefanya sasa katika suala hili la mgomo wa wanafunzi kunaweza kiliangamiza taifa au kuliletea hasara kubwa.

Tuwaombe sasa viongozi Chuo wameze wembe au kiburi chao kwa kuwarejesha viongozi wa wanafunzi na kisha kukaa nao kujadili matatizo ya wanafunzi ili ufumbuzi unaokubalika na pande zote upatikane.

Tunachokiona hivi sasa ni kuzuka kwa mtafaruku mpya pale wanafunzi watakaporejea na kujikuta hawana viongozi na hivyo kuanza madai kuwa viongozi wao warejeshwe.

Mlipuko utakaotokana na hili unaweza ukawa mbaya zaidi kwakuwa viongozi halali wa wanafunzi watakuwa hawapo na hivyo harakati hizo zinaweza kukosa nidhamu na zikaleta uharibifu,ghasia,majeruhi na hata vifo.

Ieleweke wazi kwamba nyakati zimebadilika na akili na mioyo ya watu imebadilika.Huu siyo wakati wa utawala wa kidkteta na huu siyo wakati wa kutishiana na ‘mashushushu’ kujaza makachero UDSM au hata FFU kunaweza kukawa chanzo cha hali ya wasiwasi na kuhatarisha amani na utulivu ndani ya vyuo vikuu.

Busara na hekima iwarejee watawala wa Chuo Kikuu watambue wajibu wao wakuwalea vijana na kuwaelimisha.Busara na hekima hiyo hiyo iwarejee viongozi wa Wizara ya Elimu ya Juu na serikalini kutambua wajibu wao wa kutumia kodi ya wananchi kuakikisha kwamba watoto wa Tanzania wanapata elimu.

Hasirani isiwe utamaduni wetu kwa kiongozi au raia kufikiri kwamba nchi hii inaweza kuongozwa kwa vitisho kwa mfano, wapo viongozi wamesikika wakisema mgomo wa wanafunzi wa vyuo vikuu umechochewa na vyama vya upinzani.Hao ni wazushi ,wasanii na wachochezi wakubwa.

Hawa hawaoni mzizi wa mgomo huu katika kushindwa kwa serikali kutekeleza sheria ya nchi kuhusu mikopo ya wanafunzi.Hawa hawana hata busara ya kuona kuwa ahadi ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Rais Jakaya Kikwete, pale Dimond Jubilee ilikuwa ndiyo kichocheo kikubwa cha mgomo huu.

Je ni vyama vya upinzani vilitoa ahadi alioitoa Rais Kikwete, kuwa hakuna mtoto wa maskini atakayefukuzwa kwa kukosa ada?. Je ni vyama vya upinzani vilivyowakusanya wanachuo 2500 pale Dimond Jubilee kuwa kirimu kwa kapero na fulana zenye rangi ya njano na kijani na kuwazawadia wasomi hao kadi za kujiunga na UVCCM?

Je Professa Mkandara na Waziri wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msolwa hawakuudhulia tukio hilo?Nani sasa anafanya siasa vyuoni au chama gani kinafanya siasa vyuoni?

Tuelewane watoto wanaosoma vyuo vikuu wengi wao ni watoto wa Watanzania,wanaweza kuwa na vyama au wasiwe navyo lakini itakuwa ni Uhayawani mkubwa kuwanyanyasa na kuwavunjia haki zao za kibinadamu kwa sababu yoyote ile.

Mungu ibariki Afrika,Mungu inusuru Tanzania

O755312859:katabazihappy@yahoo.com:www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano Mei 16,2007

Viongozi wetu wamefilisika kisiasa kiasi kwamba sasa ngono ndiyo siasa?

Na Happiness Katabazi

HIVI karibuni kumekuwa na habari kubwa kuhusu kinachosadikiwa kuwa ni mahusiano yasiyofaa baina ya wabunge wawili wa jinsia tofauti. Mahusiano hayo ya kimapenzi yamekuwa yanaandikwa na kupewa nafasi kubwa kama habari za kitaifa.

Yawezekana kuwa habari kama hizi zikielezea ngono haramu au hata isiyo haramu miongoni mwa habari zinazovutia wasomaji na kuzua minong'ono ya hapa na pale.

Lakini tukumbuke kwamba sisi taifa linaloitaji kujenga misingi imara ya utamaduni.Taifa lisilo na mipaka kuhusu mahusiano ya jinsia na ngono ni taifa la hayawani.

Kumbe basi misingi ya kimaadili inayofundishwa na taasisi za dini itasaidia kulielekeza taifa kuwa na tabia njema.
Yapata miaka mitatu imepita sasa Mama Terry Ghamudu, aliwai kukemea utamaduni wa machangudoa kuamia Dodoma wakati wa vikao vya bunge.

Badala ya kusifiwa mwanaharakati huyo alidhibitiwa na kuitwa mbele ya Kamati ya Maadili ya Bunge akidaiwa kwamba amewadharilisha wabunge.

Na muda mfupi tangu mwanaharakati huyo kukemewa na kamati hiyo, baadhi ya vyombo vya habari viliendelea kuripoti habari za ngono zinazowahusu baadhi ya wawakilishi wetu na viongozi wengine waliopo kwenye medani ya siasa na kwingineko.

Leo zimechapishwa habari zinazoonyesha utovu wa nidhamu na maadili miongoni mwa baadhi ya wabunge hata kama wahusikawataweza kudhibiti kwamba habari hizo si za kweli kisheria, bado mjadala kuhusu maadili ya taifa kuhusu mahusiano ya kijinsia unabakia pale pale.

Imefika sasa wakati kujiuliza kama viongozi wetu wamefilisika kisiasa kiasi kwamba sasa ngono ndiyo siasa.?Labda ngono yaweza kutumiwa kisiasa na makundi yanayo hasimiana.

Kwa hilo la ngono tunaweza kujiuliza kama habari zilizochapishwa hivi karibuni kuhusu Mbunge wa CHADEMA, Zitto Kabwe na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Amina Chifupa, kuwa na mahusiano ya kingono si mchezo mchafu wa kisiasa baina ya makundi yanayosadikiwa kuwa yatagombea kiti cha Uenyekiti wa UVCCM mwaka kesho?.

Sitaki kumtetea mtu yoyote kati ya Zitto na Chifupa katika hili ila ni vyema kutaadharisha kuhusu mmonyoko wa maadili ya viongozi unaojionyesha sasa miongoni mwa viongozi wetu.

Tuchepuke kidogo tujikumbushe habari tuhuma za ngono na hata za kusambaratisha ndoa kadhaa zilizokuwa zikiripotiwa kwenye vyombo vya habari siku za nyuma ambazo habari hizo zilikuwa zikimhusisha Chifupa moja kwa moja.

Tangu akiwa Mtangazaji wa Redio Clouds, Chifupa amekuwa akiandamwa na kashfa za ngono na katika kumbukumbu zangu hazionyeshi kwamba alikuwa akikanusha madai hayo zaidi ya akiwa kwenye kipindi cha Bambataa, kutumia muda mrefu kurusha vijembe kwa maasimu wake.

Kashfa hizo za kuvuruga ndoa za watu, zilisababisha mwaka 2005, wananchi wengi kuitaadharisha UVCCM, isipitishe jina la Chifupa awe mbunge kwa maelezo kwamba endapo atachaguliwa ,atapeleka mipasho bungeni, bunge litakuwa halina heshima machoni mwa wananchi wake kwakuwa waliamini na kusadiki kwamba mbunge huyo angeenda kuendeleza tabia hiyo kwenye bunge hilo tukufu.

Na sasa tunaweza kusema kwamba utabiri huo uliotabiriwa na wananchi hao pamoja na magazeti kadhaa, umetimia kwani ni kipindi cha mwaka mmoja nanusu tangu akiingie bungeni tayari ameishakumbwa na kashfa ya ngono na mbunge Zitto, hali iliyopelekea mumewe kumtwanga talaka.

Binafsi sipendi kufurahia matatizo ya wenzangu lakini Amina, alipoteuliwa kuwa mbunge alipaswa akumbuke alitabiriwa mambo gani na wanachi na pia aachane na mambo ambayo hayafai kufanywa na kiongozi kama yeye na mama wa familia kama yeye.

Pamoja na kuteuliwa kuwa mbunge,Chifupa, tulikuwa tukimsikia kwenye vyombo vya habari akiomba apigiwe nyimbo za mipasho zilizojaa vijembe, akitamba yeye na mumewe Mpakanjia hawaachani kamwe na kwamba yeye ndiye mwenye hati miliki na wanawake wengine ni wapita njia lakini wakati binadamu anapanga yake na mungu anapanga yake pia Mei 3, mwaka huu mbunge huyo aliyekuwa akijigamba hayo yote alitwanga talaka na mumewe huyo ambaye alikuwa akisema anampenda sana.

Ni huyu huyu Chifupa tulisikia taarifa zake kwamba alikwenda kigamboni kumpora picha za harusi baba wa msichana ambaye Mohamed Mpakanjia, hivi karibuni alidaiwa kuwa amefunga naye ndoa kinyemelewa wakati mkewe akiwa bungeni.Ni huyu huyu Amina tulimsikia kwamba yeye ni kiongozi wa kikundi cha Alqaida ambapo alithubutu kwenda kumfanyia vurugu msanii mmoja wa luninga akimtuhumu kuwa alikuwa akitembea na mumewe pale Chuo Cha Uandishi wa Habari DSJ Dar es Saalam.

Sasa sisi watanzania tunaamini wawakilishi wetu hawawezi kufanya mambo kama hayo adharani sasa inapotokea ndani ya bunge letu tunakuwa na viongozi wanaofanya mambo kama hayo siyo siri bunge linadharaulika na pia hata UVCCM iliyopitisha jina la Chifupa awe mbunge.

Chifupa tambua, kashfa kama hizo ambazo zinaelekezwa kwako ni mbaya na ukae ukijua hazitakuathiri peke yako kwani zitamuathiri hata mtoto wako katika maisha yake kwakuwa mtoto wako atakuwa anakwenda shule kule shule atakutana na wanafunzi wenzake wataanza kumdhalau au kumtolea maneno ya kejeli ya kuhusu wewe,huoni kwamba mtoto ataaribikiwa Kisaikolojia kwa kashfa zako na pia hata kukosa raha ya kusoma?

Na pia kwa kashfa kama hizo pia zinaleta sifa mbaya kwa familia ya wazazi wako.Leo watu wataogopa kukejeli adharani lakini pindi utakapotoka madarakani watakukejeli adharani na usiwafanye lolote. Ushauri wa bure kwako ni kwamba jiepushe na mambo ambayo kiongozi kama wewe upaswi kuyafanya na pia kaa chini utafakari ni kwanini wewe umekuwa ukiandamwa na kashfa za namna hiyo kisha fungua ukurasa mpya naamini mungu atakuongoza.

Hata hizi kashfa zikibainika si za kweli lakini kwanini mke wa Mfalme awe anatuhumiwa kutokua mwaminifu katika jamii inayomzunguka kila kukicha?

Hebu turejee kwenye mada yetu, upo usemi kwamba rushwa yaweza kuwa fedha,mali au mapenzi.Je ni viongozi wangapi wako madarakani kutokana na nguvu ya rushwa ya fedha,mali au ngono?.

Kwenye mantiki ya kijinsia taifa letu lina utamaduni butu kuhusu mahusiano ya kingono.Ngono kati ya mwanaume na wanawake wengi inachukuliwa kuwa ni sifa kwa maana kuwa mwanamme huyo anadhihirisha kuwa yeye lijali.Hiyo ni sifa.

Lakini ngono kati ya mwanamke na wanaume wengi inadhiirisha kuwa mwanamke huyo ni malaya tena kahaba aliyepindukia.Hiyo ni sifa mbaya na mwanamke wa namna hiyo udhalilishwa na kuoneka ni mchafu mbele ya jamii.

Hivyo basi wakati umefika sasa kuangalia upya utamaduni wetu na kuweka misingi sawa na udhibiti sawa kwenye maadili yetu yanayohusiana na ngono.

Lakini pia tutaadharishe kila mwananchi /viongozi kuhusu usemi usemao 'kila mla cha mwenzie na chake pia huliwa' gwiji wa muziki wa taarabu nchini Marehemu Issa Matona, alishawai kutoa usemi huo katika moja ya nyimbo zake.

Hivyo basi kwa wanaume na wanawake wanaoshiriki kuvunja ndoa za wenzao wasisikitike hapo kesho wanapokuta ndoa zao zimeingiliwa, zimevunjika na kusambaratishwa.Hayo ndiyo tunayoyaona katika habari hizi zinazozagaa kuhusu ngono za viongozi.

Mungu ibariki Afrika,Mungu inusuru Tanzania
0755312859:katabazihappy@yahoo.com:www.katabazihappy.blogspot.com

ELIMU YA TANZANIA NA WALIMU WA WIKI NNE

(MAKALA)

Happiness Katabazi

SERIKALI ya awamu ya nne, imekuja na mkakati mpya wa kuinua elimu kwa kuimiza ujenzi wa shule za sekondari katika kila kata kiasi kwamba, kwa sasa tumekuwa na shule za aina tatu. Aina hizo ni sekondari za kitaifa, kata na za binafsi.

Kwa hiyo, katika kila sekondari za kata, mhudumu mkubwa katika hizo shule ni halmashauri na manispaa. Serikali Kuu kwa upande wake itakuwa inatoa ruzuku katika shule hizo.

Hatua hiyo inalazimu kuongezeka kwa idadi ya walimu, vifaa vya kufundishia, mahabara na samani.

Katika kutatua tatizo la upungufu wa walimu, serikali ya awamu ya nne imekuja na mbinu ambayo wamejinadi kuwa ni dawa ya kukabiliana na tatizo la uhaba wa walimu, hasa ukichukulia wingi wa shule zilizojengwa.

Hatua hizo ni pamoja na kuwachukua walimu wote wenye diploma walio katika shule za msingi na kuwapeleka kufundisha sekondari za kata.

Hatua ya pili ni kuajiri wanataaluma wengine wasio walimu kujaza nafasi za walimu, na hatua ya tatu ni kuajiri walimu wa diploma na hatua ya mwisho ni kuajiri walimu wa leseni (crush programe), ambao kwa sasa huko mitaani wamepachikwa jina la ‘Voda Fasta’. Kwa hiyo, makala hii nitachambua nafasi ya walimu hawa wa leseni (Voda Fasta).

Tuangalie kwa sasa watoto wameandikishwa shule wakiwa na umri wa miaka 6 au 7. Kwahiyo tuchukulie mtoto ambaye ameanza shule na miaka 6, ina maana kidato cha sita atamaliza akiwa na umri wa miaka 19.

Sasa huyu mtoto mwenye umri wa miaka 19, tunafikiria hata masuala ya kubalehe hayajamtoka bado, hajui saikolojia ya malezi, hajafundishwa malezi na mbinu ya kufundishia.

Na wanafunzi hawa hawa, wanapohitimu kidato cha sita serikali inawachukua na kuwapeleka kwenye mafunzo ya wiki nne katika vyuo mbalimbali vya ualimu kwa kuwafundisha (mafunzo ya muda mfupi ya ualimu) na kuwaajiri kwa leseni, tayari kwa kutufundishia watoto wetu.

Watanzania tujiulize hawa walimu (Voda Fasta) wataweza kutekeleza majukumu ipasavyo ikiwa wenyewe bado ni watoto na walivyokuwa kidato cha tano na sita hawakufundishwa na walimu wao saikolojia na uongozi?

Na matokeo ambayo tumeishaanza kuyashuhudia ni mahusiano kati ya walimu na wanafunzi kwa lugha ya mitaani yanakuwa ya ‘kishikaji’, hakuna nidhamu, ufundishaji ni wa kukariri na vile vile kwa sababu walimu wengi hawa wa ‘Voda Fasta’ wanakuwa hawajatokwa vizuri na hali ya kubalehe, matokeo yake ni kutongoza wanafunzi na si muda mrefu tutashuhudia mimba nyingi mashuleni.

Isitoshe, shule nyingi ambazo voda fasta wamekwenda, kumeanza kutokea misuguano kati yao na wanajamii wanaoishi maeneo yanazozunguka shule na walimu wakongwe.

Tunavyosema msuguano katika jamii unatokana na kwamba, mwonekano wa voda fasta kama walimu, haupo kati ya walimu wakongwe wanaojua ualimu na maadili yake, wanakuwa wanakinzana sana na hawa Voda fasta na hivyo kuonekana kama wananyanyaswa kumbe ni kutokana na kutojua masharti na maadili ya kazi yao kama walimu, walezi na wazazi mbadala.

Kiutawala, hawa Voda fasta hawajui uongozi wa shule (School Administration) na kukabiliana na migogoro (crisis Management), mathalani migomo ya wanafunzi, matatizo ya kinidhamu na kisaikolojia, utendaji wa kiutawala. Mfano, majukumu ya mkuu wa shule, mwalimu wa taaluma, mwalimu wa malezi hata mwalimu anayesimamia miradi ya shule.

Hawa Voda fasta wamejikuta wakikabidhiwa madaraka ambayo hawajui miongozo na miiko yake na kulazimika kukabilina nayo ghafla bila kuwa na kiongozi au uzoefu kazini, hasa ukichukulia wakuu wengi wa shule mpya za kata ni walimu wenye diploma waliokuwa shule za misingi ambao nao pia hawana uzoefu au ujuzi wa uongozi kwa ngazi za sekondari.

Waliosomea diploma zao kama sehemu ya kujiendeleza tu kwa ajili ya kupandisha madaraja yao ya mishahara pasipo kuwa na nia ya ya kufundisha shule za sekondari.

Ili kuhakikisha malengo ya kila mtoto anapata elimu ya sekondari, serikali haina budi kuweka mikakati madhubuti ya kupata walimu wananaokidhi, si kupeleka bora walimu kufundisha watoto wetu hawa.

email:katabazihappy@yahoo.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamis April 3,2007

MAAMUZI MABOVU YA VIONGOZI WETU NI MATOKEO YA KUTOFIKIRI SAWA SAWA!



Na Happiness Katabazi

MAPEMA mwaka huu Rais Jakaya Kikwete alisema tunaingia mikataba mibovu kutokana na kukosa wataalamu wazuri.

Tunao ushaidi wa kutosha wa kuonyesha serikali yetu ni bingwa na mahiri katika kuingia mikataba kadhaa iliyoiletea na inayoendelea kuliletea hasara kubwa taifa hili.

Mikataba kama ya Valambhia, IPTL, rada, ndege ya Rais, ununuzi wa benki ya NBC, mkataba wa mauzo ya mashamba ya sukari ya Kilombero na Richmond yenye kampuni dada sasa iitwayo Dowans.

Sasa tunaweza kusema Tanzania tumebobea na ni magwiji hasa katika uingiaji/upitishaji mikataba mibovu. Wanasheria wakuu wa serikali kwa awamu zote zilizopita na sasa hawajawai kutetea katika hili kwa kuwa mikataba yote kabla serikali haijaingia taasisi hiyo inashirikishwa kikamilifu.

Kwa hiyo Wizara ya Sheria na Mambo ya Katiba na viongozi wetu wapo kimya katika hilo na ukimya huo labda unaashiria kukubali kauli ya Rais Kikwete aliposema kwamba tunaingia mikataba mibovu kutokana na kukosa wataalamu.

Lakini mikataba hii imetokana na sera ya chama kinachotawala hapa nchini CCM, na chama hicho hakijawahi kusema kwamba mikataba hiyo mibovu imo kwenye sera zake au Ilani yake za uchaguzi.

Rais Kikwete na viongozi wengine wa serikali pia hajawahi kusema mikataba hiyo ni mibovu au ina dosari zozote. Kwa hiyo inawezekana kabisa kwamba ubovu uliomo ndani ya mikataba hiyo unatokana na sera zenyewe za chama kinachotawala zisizokidhi haja.

Kwa kuwa kuna Watanzania waliokwishawahi kukosoa mikataba hiyo, basi ni lazima tukubali kwamba kama CCM na serikali yake vinaongozwa na watu makini, basi dosari hizo zingesahihishwa.

Lakini kwa vile hayo hayakutokea na kwa sababu hakuna dalili za masahihisho kufanywa kwa siku za usoni, lazima tutilie shaka uwezo wa viongozi wa CCM na serikali kufikiri.

Tuna shaka kwamba huenda baadhi ya viongozi wetu wana kasoro - ama hawafikirii sana kesho kutatokea nini au wanaweka maslahi yao mbele kuliko ya taifa. Na hapo moja kwa moja panagusa maradhi makubwa yaliyo na yanayowatafuna viongozi wengi - rushwa.

Na hapa ndipo ninapokumbuka usemi wa waziri mstaafu Arcado Ntagazwa alioutoa bungeni Dodoma, mwaka 1993 alipokuwa mbunge wa Jimbo la Kibondo. Alisema: “Tutakapokufa vizazi vijavyo vitafukua makaburi yetu ili vione vichwa vyetu viongozi vilikuwa na ubongo wa aina gani kwa sababu yaelekea hatufikiri sawa sawa,” mwisho wa kunukuu.

Ntagazwa alilazimika kutoa kauli hiyo baada ya kuona kwamba baadhi ya maamuzi yanayofikiwa na serikali hayana maslahi kwa taifa, na ni ya kibinafsi. Nampongeza kwa kauli hiyo na ninaamini kuwa ipo siku vizazi vijavyo si tu kwamba vitafukua makaburi kutazama ubongo, bali pia vitatulaani.

Tusipokuwa wakali katika kujadili hoja ya utawala mbovu tulionao hivi sasa tutakuwa tunashiriki au kujihusisha katika kero hii ya kuwa na viongozi wanaotoa maamuzi kama watu wenye mtindio wa akili.

Hivi Tanzania itakuwa kichekesho hadi lini? Kwa nini utawala wetu ni wa kubabaishababaisha tu na kamwe hatuoni uongozi unaotuletea tija na maendeleo?

Inakuwaje Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, Rais wa nchi inayotawala na kumiliki migodi yetu ya dhahabu na tanzanite, atusute kuwa sisi ni wazembe wa kufikiri na tuone kwamba ametusifu?

Rais Mbeki alipozungumzia madini ya tanzanite alisema japo biashara ya tanzanite inatoa dola milioni 500 kwa mwaka duniani, Tanzania, nchi pekee duniani yenye madini hayo, inapata dola milioni 80 tu.

Aliuliza kwa nini tunamtafuta mchawi wakati sheria ya uchimbaji madini tumeitunga wenyewe inayoruhusu wageni waondoke na asilimia kubwa ya madini hayo?

Sasa kwa hakika bila kufichana ukweli, baadhi ya viongozi Tanzania na wataalamu wake ni bomu na wengine kati yao wanafikiria ama kughushi vyeti ama kuwaibiwa walipa kodi kwa kuingia mikataba ‘feki’.

Hawa hawafikirii kamwe maslahi ya nchi yetu, kwani hata walipoambiwa na Chama cha Wanasheria nchini wasiridhie mabadiliko ya mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa mabadiliko hayo hayana maslahi ya taifa, hawakujali wala kusikiliza.

Waliitana kama Kamati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuamua kuridhia mkataba huo kulingana na sera za chama chao bila kufikiria kutatokea nini baadaye.

Kudumaa huku kwa fikra kumetufikisha mahali pabaya na sasa taifa letu linayumbishwa bila wananchi kupewa fursa kuzuia jambo hilo.

Hiyo ndiyo gharama na matokeo ya kuongozwa na viongozi na wataalamu wasio na chembe ya uzalendo wa nchi yao. Huenda hawafikiri sawasawa kwa sababu kiongozi mwenye uzalendo wa kweli na yupo kwa ajili ya Watanzania wenzake anaweza kukubali kuliingiza taifa kwenye mikataba mibovu kila kukicha.

Mungu ibariki Afrika, Mungu inusuru Tanzania

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili April 22,2007