Twahitaji Usalama wa Taifa si Uhasama wa Taifa

Na Happiness Katabazi

KISWAHILI kama zilivyo lugha nyingine, kina maneno kadhaa ambayo ama yana maana ya kitu kimoja au maana yake inashabihiana.

Mfano wa maneno haya ni hili ‘taifa’ waweza kulifananisha na neno ‘nchi’ na pengine neno ‘dola’. Taifa au dola kama inavyojulikana ni jumuiya ya watu wanaolikalia pande la ardhi yenye mipaka inayotambulika rasmi kwa mataifa au dola nyingine.

Hivyo taifa au dola hufanya mambo yake ndani ya mipaka yake na hutumia vyombo kadhaa kuendesha shughuli hizo na kulinda masilahi ya wanataifa dhidi ya maadui wa ndani na nje.

Wataalamu wanatanabaisha kwamba dola/taifa lina mihimili mitatu (Serikali, Bunge na Mahakama), wengine huongeza mhimili wa nne, yaani vyombo vya habari. Mhimili wa Serikali ndiyo wa kiutendaji na hivyo husimamia vyombo kadhaa katika utendaji huo. Hivi huitwa vyombo vya dola, ambavyo ni pamoja na majeshi ya ulinzi na usalama.

Hapa Tanzania tunalo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) linalohusika sana katika kulinda nchi yetu na mipaka yetu dhidi ya maadui wa nje na pale inapobidi kuingia vitani kulinda nchi.

Katika hili twaweza kutoa mfano jinsi JWTZ walivyofanya kazi ya barabara mnamo mwaka 1978/1979 dhidi ya majeshi ya adui Idd Amini Dada wa Uganda (sasa marehemu).

JWTZ katika vita iliyopiganwa mwaka huo walifanya kazi iliyotukuka, kiasi kwamba sitarajii itakuja kusahaulika miongoni mwa Watanzania na katika historia ya nchi hii.

Naam! JWTZ walitimiza wajibu nyeti ambao si mwingine, bali kulihakikishia taifa letu usalama.

Tunalo jeshi jingine, Polisi, hawa tunaambiwa siku zote wako kwa ajili ya usalama wetu sisi raia na usalama wa mali zetu tulizojaliwa kuzimiliki.

Nao kazi yao si haba. Mara kadhaa wametuweka salama dhidi ya vibaka wakwapuaji, majambazi wa kutumia silaha, wavunja sheria za nchi na wengineo.

Hata hivyo pamoja na jitihada zao nzuri, matukio ya uhalifu bado yapo nchini na pengine wanashindwa kwa sababu zilizo nje ya uwezo wao, mathalani vifaa duni na mengineyo.
Lakini hatuwezi kusita kusema kwamba, vitendo vya baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi si tu ni kero bali vinaondoa maana ya dhana nzima ya wao kuwa chombo cha usalama wa raia na mali.

Kwa muda mrefu baadhi ya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani (Traffic) wameendelea kuwanyanyasa wenye magari kwa rushwa.

Aidha, udhaifu mwingine wa Jeshi la Polisi umejikita katika namna ambavyo watu fulani wenye mamlaka huamua kukitumia chombo hiki ndivyo sivyo, mathalani, katika matukio kadhaa badala ya polisi kuwalinda raia walitumiwa kuwatesa raia.

Asiyeelewa hili awaulize vijana wa vyuo vikuu walivyotandikwa mara kadhaa na FFU, au wamuulize Profesa Ibrahim Lipumba kisa cha kujeruhiwa mkono wake na askari waliopaswa wamlinde.

Kama hilo halitoshi, kumbukumbu ziwapeleke huko Zanzibar ambako askari polisi
walitumika kuwamwagia maji ya ‘washawasha’ raia wema. Polisi wasinielewe vibaya, kazi yao ni nzuri sana ila kasoro za ufisadi na unyanyasaji ni mbaya. Isije ikawa mnatimiza lile neno lililonenwa na nabii akisema ‘chachu kidogo inachachua donge zima’.

Naam!, kwa ujumla twaweza kusema, mipaka yetu ni salama (heko JWTZ), raia tuko salama kiasi chake (asante polisi). Lakini je, kama tutatumia usalama katika maana yake kamili, taifa letu Tanzania liko salama? Na hili si swali la kipima joto hata lijibiwe kwa kusema tu ndiyo, hapana au sijui. Jibu linahitaji fikra pana.

Tangu tukingali watoto wadogo tumekuwa tukisikia uwepo wa chombo kiitwacho Usalama wa Taifa.

Wengi tunaweza kuwa tunafahamu majukumu ya chombo hiki kinadharia tu, maana shughuli kinazozifanya hazionekani moja kwa moja hadharani mara zote.

Yamkini kazi za wanausalama wa taifa hufanyika kwa usiri mkubwa. Ndiyo maana inakuwa hata si rahisi kujua nani mwajiriwa katika chombo hiki. Watu wanaishia kutuhumiana tu, mara utasikia ‘ooh, fulani ni usalama wa taifa na fulani naye…’ lakini hakuna uthibitisho, ni siri kwelikweli.

Hawa wanaodhaniwa kuwa ni wanausalama wa taifa wako katika vyama vya siasa, taasisi kama vile vyuo vikuu na kwingineko, ambako kama pasipochungwa huenda patahatarisha masilahi ya vigogo.

Kinachoshangaza hapa ni kwamba inakuwaje mtu wa usalama wa taifa afanye kazi ya kudhibiti jitihada za chama fulani kisiweze kushika madaraka ya dola kihalali?

Inakuwaje mtu wa usalama wa taifa atumiwe kudhibiti midomo ya wasomi katika vyuo vikuu wasiseme ukweli, wasiwe na uhuru wa fikra bali wahubiri tu na kukariri yale yaliyo matakwa ya vigogo?

Inakuwaje usalama wa taifa kufanya kazi ya kudhibiti vyombo vya habari ili viandike yale tu ambayo wakubwa wanataka na si vinginevyo!

Inakuwaje usalama wa taifa uone kwamba kazi inayotakiwa ni kuwadhibiti waandishi wa habari wasifanye kazi yao, kama ilivyotokea wiki mbili zilizopita pale Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere kati ya wapiga picha hadi Rais Jakaya Kikwete, akaingilia kati!

Katika hili, sina budi kumsifu Rais Kikwete. Ama kwa hakika kitendo chake cha kuwakataza walinzi wasiwazuie waandishi kufanya kazi zao ni cha upeo wa hali ya juu wa uelewa na ni funzo kwa wanausalama ambao wanasahau majukumu yao ya msingi na kujishughulisha na vitu ambavyo wala si hatari kwa usalama wa taifa.

Kudhibiti vyombo vya habari, wasomi na wanasiasa wa kambi ya upinzani, wanausalama wetu mfahamu fika kwamba uko si kulinda usalama wa taifa bali ni kujenga uhasama wa kitaifa.

Usalama wa taifa mkitambua hilo, rejeeni katika shughuli za kimsingi mnazopaswa kuzifanya hususan zama hizi ambapo usalama wa taifa letu na wa wakati ujao unazidi kuwa shakani.

Hamisheni nyenzo zenu pale Chuo Kikuu Mlimani mzielekeze kwenye maofisi ambako wizi wa kalamu unazidi kushamiri, ufisadi unaoota vitambi na uzandiki unastawi kupitia mikataba ya kishenzi inayosainiwa kati ya wezi wa ughaibuni na wenzetu wachache wanaokosa hata lepe la uzalendo, wanaiuza nchi hii kila uchao mchana kweupe na nyie mpo eti usalama wa taifa…usalama upi?

Tuseme hamjasikia hayo yanayotokea katika Benki Kuu ya nchi hii, kwanza mlikuwa wapi hata msiyadhibiti yasitokee? Au mlikuwa Tanzania Daima na MwanaHalisi mkiangalia nani anawaandikia wananchi ukweli ili ashughulikiwe?

Mmelala usingizi upi mpaka madini ya nchi hii na rasilimani nyinginezo vinachotwa na wageni kwa ‘raha zao’. Yamkini mlikuwa kwenye lecture rooms pale Mzumbe au SUA mkidhibiti wahadhiri wasitoe mihadhara ya takwimu za uporaji huo.

Mlikuwa wapi wakati hao wezi wakifanya mambo yanayowahusisha na kashfa nzito pengine kuliko zote nchini (ya BoT, Meremeta Gold Company, Kampuni ya Alex Stewarts, Akaunti ya madeni ya nje, Bank-M na kwingineko?).

Au mlikuwa kwenye mikutano ya hadhara ya ushirikiano wa vyama vya upinzani ili kukusanya ni hoja gani za nguvu wamezijenga mkawaripoti kwa vigogo watafute namna ya kuwajibu?
Ni usalama wa taifa upi mnaoshughulika nao ndani ya nchi ambayo wengi wanazidi kufukarika wachache wananeemeka kwa kasi ya roketi?

Ama hamjui kwamba hapana usalama palipo na wingi wa fukara, maana wajapokata tamaa amani itayeyuka kama barafu wakati wa jua kali.

Yatosha mliojishughulisha na masilahi ya wachache wala nchi, oneni uchungu, rejeeni maadili ya taaluma yenu, liokoeni taifa lenu, watumikieni wananchi, turejesheeni usalama wa taifa.

Watanzania tunautamani usalama wa taifa unaomlenga kila mmoja wetu, unaolenga uhifadhi wa rasilimali zetu na unaolinda haki ya kila mmoja wetu, awe raia huru au raia anayetumikia kifungo (pengine kwa kuvunja sheria au kubambikiziwa, au kushindwa kutoa rushwa kwa hakimu na karani mahakamani).

Katika hilo mawazo yananirejesha kukitazama chombo kingine cha dola, Jeshi la Magereza. Chombo hiki nacho kilipewa jukumu zuri, kuwahifadhi wahalifu wanapotumikia vifungo vyao na kuwafanya warejee katika tabia njema zinazofaa katika jamii (re-socialization). Jukumu hili nalo lililenga usalama wa jamii.

Cha ajabu ni kwamba, wafungwa kadhaa wanapomaliza kutumikia vifungo vyao badala ya kurejea uraiani wakiwa watu wema waliobadilika, wazingativu wa maadili ndiyo kwanza huja na mbinu kali zaidi za uhalifu.

Msomaji usishangae bali tushirikiane kuliambia Jeshi la Magereza litufafanulie; bangi na pengine dawa za kulevya zinapenyaje na ulinzi wenu mkali na kuwafikia wafungwa? Au baadhi yenu mna masilahi katika hiyo miradi?

Inakuwaje huko magereza wafungwa ‘wanashikishana ukuta’ (wanaingiliana kinyume cha maumbile), au kwenu ninyi hiyo ni haki ya mfungwa?

Hao chawa wataisha lini kwenye virago wanavyolalia wafungwa, wataacha lini kulala mzungu wa pili na kwa msongamano katika vyumba vidogo.

Au hamjui kwamba kwa kuwaweka wafungwa katika mazingira ya kinyama namna hiyo ndiyo kwanza mnawajengea moyo wa ‘kihayawani’ na kikatili badala ya kuwarejesha katika uadilifu.

Mtueleze wazi mnakuwa wapi hadi wafungwa wa kike wanapachikwa mimba wakiwa magerezani?

Jeshi la Magereza, ebu jiulizeni leo hao wafungwa mnaowahifadhi wakimaliza vifungo vyao usalama wa taifa utakuwa katika hali gani?

Mama yetu Tanzania, leo wewe si taifa salama, waambie wanao (wananchi) wajue hali uliyonayo, washiriki kilio chako ili tumbo lako lisizidi kuwa shimo tupu lililotolewa utumbo wote (mali asili) kwa manufaa ya wageni; lisiendelee kupata uchungu wa kuzaa wana mafisadi na wahalifu, mwite mwanao serikali akishtue chombo chake Usalama wa Taifa kisiendelee kubweteka ilhali usalama wako unazidi kutokewa.

Mungu ibariki Afrika, Mungu inusuru Tanzania.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu: 0755 312 859 au barua pepe; katabazihappy@yahoo.com. Au www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili,Uk 6, Juali 22, 2007

Huyu ndiye Augustino Ramadhani; Jaji Mkuu Mteule wa Tanzania


Mapema wiki hii Rais Jakaya Kikwete, alimteua aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Augustino Ramadhani (62) kuwa Jaji Mkuu mpya, Mwandishi Wetu Happiness Katabazi, alifanya mahojiano maalumu na Jaji Mkuu huyo mteule na katika makala hii amezungumzia historia ya maisha yake kwa mapana na masuala mengine mbalimbali yanayohusu Mahakama ambayo ni mhimili mahususi.

Swali: Umepokeaje uteuzi wa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania?

Jibu: Nimepokea uteuzi huu kwa furaha. Na nimechukulia kwamba Rais Kikwete ana imani nami na pia ameridhishwa na utendaji kazi wangu na kabla ameamini kuwa mimi nitaendeleza yaliyofanywa na watangulizi wangu yaani Jaji Augustino Saidi, Jaji Francis Nyalali na Jaji Barnabas Samatta.
Sikutazamia, uteuzi umenijia ghafla. Hivyo nataka nipate muda wa kujipanga ili siku za usoni aliyeniteua asione alichagua mtu asiyestahili kushika wadhifa huu.

Swali: Watanzania wangependa kusikia kauli yako kwamba ni mambo yapi umejipanga kuyafanya katika uongozi wako?

Jibu: Ni mapema mno kusema nimejipanga kuanza kukabiliana na jambo gani maana nafasi hii ni ya kuteuliwa, labda kama nafasi hii ingekuwa ya kisiasa ningeweza kutamka mapema namna hii kwamba nimejipanga kufanya nini.
Sipendi kuwadanganya Watanzania kwamba ooh, nitafanya ili na lile, kwakuwa mimi ni mwanasheria mwandamizi, hivyo leo hii nikurupuke na kusema kitu ambacho sijakifanyia utafiti, nitakuwa nadhalilisha taaluma ya sheria na Mahakama kwa ujumla.
Nitakapoingia ofisi mpya nakuona ofisi hiyo mambo yanaendeshwaje, kuna ‘miba gani’, na kushirikisha wenzangu hapo ninaweza kutoa kauli ya nini tumejipanga kukifanya.
Ila ninachoweza kuwahakikishia wananchi ni kwamba, nimelenga kusimamia mambo matatu. Moja nitahakikisha haki inapatikana haraka iwezekanavyo, maana imekuwa ni tatizo linalolalamikiwa na watu wengi wanapotafuta haki katika vyombo vya sheria.
Nitahakikisha pia haki inapatikana bila rushwa na kwamba nitajipanga na watendaji wenzangu kuona ni jinsi gani tutakabiliana na tatizo hilo.
Pia nitahakikisha haki inapatikana kwa gharama nafuu, maana haki imekuwa ikipatikana kwa gharama kubwa hasa inapokuja gharama za kuwalipa mawakili, lakini nitaweka mipango na wenzangu na kuandaa mazingira ya kupatikana haki kwa gharama nafuu.

Swali: Kuna malalamiko mengi ya ucheleweshwaji wa usikilizaji wa kesi hasa za mauaji, hili umelipangia mkakati gani?

Jibu: Maoni yangu. Si ucheleweshwaji wa kesi za mauaji tu, bali kesi zote zinacheleweshwa. Kwa upande wa kesi za jinai, kuna sababu tatu ninaweza kuzitaja kuwa zinachangia ucheleweshwaji wa kusikiliza, upande wa kwanza ni serikali ambao waendesha mashitaka huwa wanasema upelelezi kwa kesi fulani bado haujakamilika.
Na sisi kama Mahakama ni vigumu kujua ni matatizo gani yanawakabili katika upelelezi, kwa kweli hili ni tatizo kubwa na kila kukicha limekuwa likipigiwa kelele.
Upande wa pili ni mshitakiwa mwenyewe, wakati mwingine unachelewesha kuleta mashahidi mahakamani ila hali hiyo katika upende huu wa mshitakiwa hutokea mara chache mno.
Upande wa tatu ni Mahakama yenyewe, sasa kwenye Mahakama yenyewe kuna mambo ambayo yanasababisha kesi kuchelewa kusikilizwa. Uchache wa vyumba vya kuendeshea kesi na mfano halisi pale Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ina vyumba vinne tu vya kuendeshea kesi, hapa Mahakama ya Rufani ina vyumba viwili vya kuendeshea kesi. Sasa majaji ina wabidi wasubiriane kuendesha kesi na kesi nyingine zinachukua muda mrefu wakati zikiendeshwa.
Jingine linalochangia ucheleweshwaji wa kusikiliza kesi ni uhaba wa majaji na mahakimu, hili ni tatizo na hata kama unao mahakimu na majaji wengi, lakini vyumba vya kuendeshea kesi ni vichache kama ilivyo sasa hapa nchini, bado tatizo kesi kuchelewa kusikilizwa litakuwa pale pale.
Tatizo jingine la ucheleweshwaji ni uhaba wa nyenzo, leo hii hapa majaji na mahakimu kurekodi mienendo ya kesi kwa mkono badala ya kutumia teknolojia ya kisasa ya kurekodi sauti kama ilivyo kwa mahakama za nje. Kwa hiyo muda mwingi sisi majaji na mahakimu kuandika. Mfano Mahakama ya Afrika Mashariki, majaji wake wanatumia teknolojia ya kisasa ya kurekodi sauti.
Halafu pia katika hili la nyenzo, kutokuwepo kwa mfumo wa kompyuta ‘computerization’, unakuta jaji anaandika hukumu kwa mkono kisha hukumu hiyo inapelekwa kuchapwa kwa mchapaji sasa unakuta hukumu moja inaandikwa mara mbili.
Kwa hiyo hayo matatizo niliyoyataja hapo juu yanachukua muda mwingi na si siri yanachangia ucheleweshwaji wa usikilizaji wa kesi kwa wakati.

Swali: Mahakama yako ina majaji, mahakimu na wataalamu wa kutosha kuweza kukabiliana na changamoto zinazoikabili sasa?

Jibu: Majaji, mahakimu na watalaamu katika mhimili wa Mahakama hawatoshi na kuna haja waongezwe kwa kuwa uchache wao nao ni sababu moja wapo inayopelekea ucheleweshwaji wa kesi.

Swali: Unazungumziaje madai kwamba kuna mahakimu hawana ujuzi wa kutosha na kwamba mishahara midogo wanayopata inawafanya baadhi yao wajihusishe na vitendo vya rushwa?

Jibu: Wakisema mahakimu hawana uzoefu wa kutosha nitawaelewa, siyo hawana uzoefu, hili nakataa kwakuwa mahakimu wote wamehudhuria kozi katika vyuo husika na kozi zao zinatofautiana kwa muda, kwani mahakimu wa mahakama za mwanzo na wilaya kozi zao huwa ni za muda mfupi tofauti na mahakimu wa Mahakama za Hakimu Mkazi, kwakuwa hao ni wanasheria kamili, ila nasema hivi kinachotakiwa hapa ni kwa mahakimu hao kupenda kujifunza zaidi kila mara bila kuchoka kwa kuwa elimu haina mwisho na mtu au kiongozi yeyote anayependa kujifunza mara kwa mara anapata fursa ya kujua vitu vingi na uzoefu wake unaongezeka na ninatoa changamoto kwa watendaji wote wa mahakama kupenda kujisomea na kuifunza.
Kweli mishahara ni midogo kama ilivyo sekta nyingi nyingine, lakini mishahara kuwa midogo siyo sababu ya mfanyakazi wa Mahakama kuchukua rushwa kwa sababu kuna wanaopata mishahara minono na kila kukicha wanapokea na kudai rushwa. Binafsi yangu nasema hivi rushwa ni urafi wa mtu binafsi.

Swali: Unaridhika na mfumo wa Mahakama ya Tanzania?

Jibu: Hadi sasa mfumo wa Mahakama hapa nchini unaridhisha ila nitahakikisha ninakaa na wenzangu kuona ni jinsi gani tunaweza kuuboresha zaidi.

Swali: Ni tukio gani unalikumbuka, liwe zuri ama baya katika maisha yako?

Jibu: Tukio ambalo sitalisahau lilikuwa ni kule kufiwa na baba yangu mzazi, Mathew Douglas Ramadhani, Machi mosi mwaka 1962, nilikuwa na umri wa mika 15, tukio hili lilinishtua sana na siwezi kulisahau kwa sababu nilikuwa bado mtoto mdogo, nilikuwa nikiwaza nani angenisomeshwa.
Tukio lililonifurahisha ni siku nilipomuoa mke wangu kipenzi Luteni Kanali Saada Mbarouk, ambaye anafanya kazi Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Nilifunga naye ndoa Novemba mosi mwaka 1975.

Swali: Ni kitu gani kilikutuma kujiunga na fani ya sheria?

Jibu: Nilipenda kusoma sheria kwanza pale Tabora Sekondari (Tabora School) nilipokuwa nasoma kuliwa na mwalimu akiitwa Butterworth, alikuwa akitufundisha somo la historia tangu kidato cha kwanza hadi cha sita, yeye alikuwa mwanasheria, sasa huyu vile alivyokuwa anazungumza ni tofauti na walimu wengine kwa namna alivyokuwa anabishana na kuchukulia mambo tofauti na walimu wengine.
Basi tangu hapo alinivutia na zaidi ya hapo marehemu baba yangu alisomea somo la sheria, alichukua shahada ya BA na moja ya masomo ya hiyo digrii ilikuwa ni sheria na nyumbani kulikuwa na vitabu vya sheria na katika maktaba ya nyumbani.
Lakini si hivyo tu baba yangu mzaa mama, Masoud Than, alikuwa mkalimani wa mahakama na babu alimlea mama Justine Dodo naye alikuwa mkalimani wa jaji enzi za ukoloni na kutembea naye miji mingi hapa Tanganyika. Sasa haya yote nalazimika kusema yalifanya nipende sheria na hadi nikaenda kuisoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Swali: Unafikiri idadi ya wanawake waliobahatika kuchaguliwa kuwa mahakimu na kuteuliwa kuwa majaji wanatosha na kama hawatoshi nini kifanyike?

Jibu: Majaji na mahakimu wanawake hawatoshi na chakufanya Mahakama iwezeshe wanawake ili waweze kufikia vigezo vinavyotakiwa ili siku moja wateuliwe kuwa majaji au wachaguliwe kuwa mahakimu.
Nasema kuwa idadi ya majaji wanawake ni ndogo, kwa mifano hai, mfano mmoja wapo unapatikana hapa Mahakama ya Rufani, mahakama hii ina jumla ya majaji 13 na watatu kati yao ni wanawake waliosalia ni majaji wanaume. Sasa hii ni tofauti kubwa sana.
Hapo awali Mahakama ya Rufaa ilikuwa na jaji mwanamke mmoja tu ambaye pia ni mwanamke wa kwanza kuwa hakimu hapa nchini anaitwa Eusebio Mnuo, na Rais Jakaya Kikwete alivyoingia madarakani akateua majaji wawili katika mahakama hii nao ni Jaji Natalia Kimaro na Engela Kileo.

Swali: Ni changamoto zipi zinaikabili Mahakama ya Tanzania?

Jibu: Changamoto ni nyingi, moja ya changamoto kubwa inayotukabili ni kutoa haki zote katika mashauri ya jinai na madai haraka, kupiga vita rushwa na suala la rushwa nalitazama katika sehemu mbili ya kwanza ni rushwa ya kweli na ya pili rushwa ya kudhaniwa.
Hivyo watendaji wa Mahakama wanatakiwa waweke juhudi kwamba kusiwepo na mazingira ya rushwa ya kweli na ya kudhaniwa. Na changamoto ya tatu inayoikabili mhimili mahususi wa Mahakama ni kuhakikisha haki inapatikana kwa watu wengi kwakuwa haki ina gharimu hasa inapokuja suala la mawakili, sasa tuhakikishe haki inapatikana kwa wote wenye madai yao mahakamani.

Swali: Hivi sasa kuna mchakato wa waumini na taasisi ya dini ya Kiislamu wanataka irejeshwe Mahakama ya Kadhi, nini msimamo wako na kama ikija itakaaje katika mtiririko wa mahakama?

Jibu: Kwa kweli kuhusu hili la Mahakama ya Kadhi siwezi kulizungumzia kwakuwa ninavyofahamu mimi suala hili lipo kwenye mchakato katika ngazi husika hata hivyo sina taarifa rasmi kama utekelezaji wa suala hilo umefikia wapi, hivyo binafsi siwezi kuzungumzia jambo kama sina taarifa za uhakika.

Swali: Huoni wakati umefika wa shughuli za Mahakama ya Tanzania kuendeshwa kwa Kiswahili ili wananchi waridhike na maamuzi yanayotolewa, kwakuwa hivi sasa mahakama zinaendeshwa kwa lugha ya Kiingereza na wananchi wengi wanaona hawatendewi haki na hasa unapofikwa wakati wa mawakili wa pande mbili wanapobishana kisheria wawapo mahakamani?

Jibu: Nakubali kwamba ipo haja ya kuendesha shughuli za mahakama kwa lugha ya Kiswahili. Na kwakweli tayari limefanyika hilo la kuendesha mahakama kwa kutumia lugha ya taifa, sasa hivi mahakama za mwanzo zinaendeshwa kwa lugha ya Kiswahili na sehemu kubwa ya Mahakama za Wilaya.
Lakini hata Mahakama ya Rufani tunaendesha Kiswahili inapobidi kuwa kanuni za Mahakama ya Rufani zinaruhusu kuendesha mashauri kwa Kiswahili au Kiingereza ila kumbukumbu lazima ziandikwe kwa lugha ya Kiingereza.
Na ninaamini ikitumika lugha ya Kiswahili mahakamani itaondoa manung’uniko ya wananchi na itasaidia watu waone haki inavyotendeka.

Swali: Huoni wakati umefika sheria zote za nchi ziandikwe kwa lugha ya Kiswahili kama ilivyo Katiba ya Tanzania ambayo ndiyo pekee imeandikwa kwa lugha ya taifa?

Jibu: Katika hili siwezi kusema wakati umefika kwa sababu hadi sasa hakuna maneno ya Kiswahili yaliyowekwa katika lugha ya kitaaluma ya sheria (many legal technical terms yet produced) yakipatikana hapo tunaweza kusema wakati umefika sheria za nchi ziandikwe katika lugha ya Kiswahili.

Swali: Wadhifa huu mpya wa ujaji mkuu, huoni kwamba unaweza kukuzuia usiendelee kupiga kinanda kanisani?

Jibu: Kwanza kabisa kupiga kinanda nachukulia kama ibada, yaani kama vile ninavyokuwa na uhuru wa kwenda kusali hivyo ninao uhuru wa kuingia kanisani na kupiga kinanda.
Kwahiyo ieleweke uteuzi huu hautanizuia kupiga kinanda kwani hata nilivyokuwa Jaji Mkuu Zanzibar nilikuwa nahudhuria ibada na kupiga kinanda hata Jumapili ijayo (leo) nitakwenda kanisani St. Albano kusali na kisha nitapiga kinanda kama kawaida.
Enzi nasoma Tabora School ndipo nilipojifunza kupiga kinanda na mwanangu aitwaye Francis ndiye anayeonyesha kufuata nyayo zangu katika upigaji kinanda.
Licha ya kupendelea kupiga kinanda pia napenda kucheza mpira wa kikapu, na nimeanza kucheza mchezo huu tangu nasoma hadi nilivyokuwa ndani ya JWTZ niliupenda sana mchezo huu hadi nilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Tanzania Basketball Association (TABA, sasa BFT baada ya kuwa shirikisho) na mimi na wanamichezo wengine akiwemo Ofisa Habari na ofisa Utamaduni Manispaa ya Kinondoni Iddi Chaulembo, mwaka 1972 tulifufua chama hicho mkoani Iringa kitaifa.

Swali: Tueleze historia ya maisha yako kwa mapana?

Jibu: Nimezaliwa Desemba 28, mwaka 1945 Zanzibar mjini nikiwa ni mtoto wa pili kati ya watoto wanane, wa kike wanne na wanaume wanne. Ni Mkristo wa dhehebu la Anglikana.
Nimesoma shule mbalimbali za msingi Mpwapwa mkoani Dodoma 1952 -1953 nikaenda Town School-Tabora nikasoma darasa la tatu hadi la nne mwaka 1954-1956 na darasa la sita na saba nilisoma Kazel Hill sasa inatwa Shule ya Msingi Itetemia mwaka 1957-1958. Na darasa la nane tu mwaka 1959 nikarudi kusoma Mpwawa.
Mwaka 1960-1965 nilijiunga na Tabora School kwa ajili ya masomo ya kidato cha kwanza hadi cha sita. Kwakuwa nilifaulu nilichaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1966, na nilisoma shahada yangu ya Sheria na ilipofika Machi 1970 nilihitimu masomo.
Na mwishoni mwa Machi mwaka huo huo wa 1970 nikajiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), niliingia jeshini kama mwanasheria raia mpaka kipindi cha mafunzo ya kijeshi nikaenda kwenye mafunzo na kisha nikarudi kuitumikia JWTZ.
Ilipofika mwaka 1971 nikapewa kamisheni kambi ya Mgulani nikawa Luteni (nyota mbili). Nikaendelea na jeshi hadi mwaka 1977, nikahamishiwa Brigedi ya Faru-Tabora nikiwa na cheo cha Meja.
Sasa mwaka 1978, wewe mwandishi ulikuwa hujazaliwa, ndiyo mzee Aboud Jumbe Mwinyi, wakati huo akiwa ni rais akaniita Zanzibar na kuniteua kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar na kipindi hicho Mwanasheria Mkuu wa Serikali alikuwa ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Damian Lubuva.
Aidha Oktoba 1978 niliteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar. Na ilipofika Machi 1979 nilirudishwa JWTZ na baada ya muda mfupi nikapelekwa kwenye vita ya Uganda , nikiwa na cheo cha Luteni Kanali na kwenye vita hiyo nilikuwa naendesha mahakama za kijeshi.
Vita ilipokwisha nikarudi Zanzibar. Januari 8 mwaka 1980 nikaapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, wakati huo nikiwa na cheo cha Luteni Kanali. Nikaendelea na Ujaji Mkuu Zanzibar hadi Septemba 1989 alipoapishwa Jaji Mkuu Zanzibar Hamid Mahamod Hamid.
Hata hivyo Juni 23 mwaka 1989 niliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania hadi mapema wiki hii nilivyoteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania.
Nilipoteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani hapa Bara ndiyo sababu ya kuacha ujaji Mkuu Zanzibar.
Januari 1993 niliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na niliendelea na nafasi hiyo hadi Januari 2003 na Oktoba 2002 niliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ambapo kipindi changu cha miaka mitano katika tume ZEC kinamalizika Oktoba mwaka huu.

Mwaka 1997 nilistaafu JWTZ nikiwa na cheo cha Brigedia, na niliagwa kwa heshima zote za kijeshi licha sikupewa mafao yangu kwakuwa mafao hayo yameunganishwa kwenye kazi yangu ya ujaji hivyo mafao yangu yote nitalipwa wakati nikistaafu kazi hii ya Ujaji Mkuu, kama mungu atanipa uzima.

Novemba 2001, niliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Afrika Mashariki nafasi ambayo natakiwa nimalize kipindi changu cha miaka sita Novemba mwaka huu.
Nina mke mmoja ambaye Mungu ametujalia tumebahatika kupata watoto wanne, wawili ni wasichana na wawili ni wavulana.
Mtoto wangu wa kwanza anaitwa Francis (30) huyu ni mwanasheria na anafanyakazi ya uwakili Manchester, Uingereza, Brigeth, huyu ana shahada ya Uandishi wa Habari na anafanyakazi ICAP hapa nchini, Marina ni mfamasia, yuko Liverpool, Uingereza na Mathew naye ni mfamasia, anafanya kazi Liverpool.”

Mwandishi wa makala hii anapatika kwa simu: 0755 312 859, barua pepe: katabazihappy@yahoo.com au www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Julai 22,2007

NCCR-Mageuzi imestahimili mawimbi ya kisiasa-Mbatia



MWENYEKITI wa Chama NCCR-Mageuzi, James Mbatia, anasema kutokana na kurekebishwa kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutungwa kwa sheria Na. 5 ya mwaka 1992 na sheria nyingine zinazoruhusu kuundwa kwa vyama vingi vya siasa nchini, taifa letu limeshuhudia kuibuka kwa vyama ambavyo kwa kiasi fulani vimeleta changamoto na kuchochea maendeleo katika ngazi za jamii ungana na Mwandishi Wetu ,Happiness Katabazi , ambaye alifanya naye mahojiano na kiongozi hivi karibuni.

James Mbatia anasema kutokana na uamuzi huo, vyama 13 vilivyopata usajili wa kudumu kutoka kwa Msajili wa Vyama ni pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), National Convetion for Construction and Reform – Mageuzi (NCCR-Mageuzi), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Civic United Front (CUF) na United Democratic Party (UDP).

Vyama vingine vilikuwa ni TADEA, NRA, UMD, Tanzania Labour Party (TLP), UPDP, PONA na Tanzania Peoples Party (TPP); vyama vingine viliendelea kuandikishwa na kupata usajili wa kudumu baadaye na kujiunga rasmi kwenye mchakato huo wa kisiasa.

Anasema licha ya uchanga wa vyama vya siasa vilivyoundwa kufuatia kutungwa kwa sheria hiyo, chama kikongwe na kinachotawala, Chama cha Mapinduzi ambacho kimekuwa na historia ndefu ya kutoka mwaka 1954, kimekiri kwa nyakati tofauti kutikiswa na chagamoto zilizotokana na vyama hivi vichanga.

Leo hii tunapotafakari kutimia kwa miaka 15 baada ya kuruhusiwa kwa mfumo huo demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania, ni lazima kama wananchi wa taifa hili kuangalia kwa makini tulikotoka, kuanzia enzi za Uhuru chini ya vyama vingi, kufutwa kwa mfumo huo na kuingizwa kwenye mfumo wa utawala wa chama kimoja na baadaye kurejea tena kwenye mfumo huu.

“Historia ni ndefu, na matukio muhimu yaliyotokea katika kipindi hicho ni mengi, lakini lililo la umuhimu wa kipekee na swali la msingi la kujiuliza ni Je, mfumo huu umetimiza kwa kiasi gani matarajio ya watanzania ambao licha ya asilimia 80 kukataa mfumo huo lakini serikali ikaamua kuufuata”anasema James Mbatia.

Anasema kumetokea matukio kadhaa katika historia ya mfumo huu kati ya Julai 1992 na Oktoba 1995 ambapo katika uchaguzi wa kwanza uliofanyika 1993, CCM ilishinda kwa asilimia 97 kwenye kinyang’anyiro cha kutafuta wenyeviti wa vitongoji, vijiji na wajumbe wa serikali za vijiji, chama hicho kiliendelea kuvinyanyasa vyama vingine hadi mwishoni mwa 1995.

Aidha Oktoba 1994, kulikuwa na uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa kwa maana ya madiwani ambapo kati ya nafasi 2,411 zilizokuwepo, ni nafasi 1,226 zilizoshindaniwa na vyama mbalimbali kutokana na nafasi zingine kunyakuliwa na wagombea wa CCM bila ya kupingwa na mwisho CCM ikajikusanyia viti 2,336 huku vyama vya upinzani vikiambulia viti 75 sawa na asilimia 3.11.

Oktoba mwaka 1995, uchaguzi mkuu wa kwanza uliendeshwa nchini kwa mara ya kwanza na vyama vingi vikashiriki na kupata matokeo kama ifuatavyo kwenye uchaguzi wa Rais wa Jamhuri; CCM 61.96%, NCCR – Mageuzi 27.8%, CUF 6.4% na UDP 4.0%; hii ni kutokana na kura 6,512,745 zilizopigwa.

Na katika uchaguzi wa wabunge jumla ya vyama siasa 13 vilishiriki kuwania kura 6,440,913 zilizopigwa na kupata matokeo kama ifuatavyo; CCM 59.22%, NCCR-Mageuzi 21.83%, CHADEMA 6.16%, CUF 5.02%, UDP 3.32%, TADEA 1.19%, NRA 0.94%, UMD 0.64%, TLP 0.41%, NLD 0.41%, UPDP 0.31%, PONA 0.28% na TPP 0.24%.

Anaeleza kuwa kwa vyovyote vile kutokana na matokeo hayo, chama cha NCCR-Mageuzi kilionekana dhahiri kuwa na ushawishi mkubwa miongoni mwa wapiga kura na kilitoa changamoto kubwa katika siasa na mfumo mpya wa vyama vingi vya siasa nchini; changamoto ambayo miaka takriban 15 baadaye imeonekana kufifia na kukosa matumaini makubwa.

“Nakumbuka tukio moja nililolishuhudia wakati wa kampeni hizo ambazo wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa endapo Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Julius Nyerere, asingelichukua hatua ya kukisaidia CCM katika kampeni zake, basi leo historia ingekuwa inasema mambo mengine,” anasema Mbatia.

Mbatia anasema ndicho kipindi ambacho mgombea urais kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, Augustine Mrema, alikuwa ameingia kwenye nyoyo za watanzania kwa kiwango kikubwa nami nilishuhudia hilo kwenye mji mdogo wa Shirati wilayani Tarime, wakati mashabiki na wanachama wa chama hicho walivyojitokeza bila ya woga kumpokea Nyerere wakiwa na bendera na mavazi rasmi ya NCCR-Mageuzi.

“Hakukuwepo na woga tena, walikuwa wakikimbia pande zote mbili za barabara wakiwa na bendera na mabango yanayoonyesha kuwa hawamtaki mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa na Nyerere mwenyewe na kufurika kwenye uwanja wa Obwere kumdhihirishia Nyerere kuwa chama chake kimewachosha’ anasema.

Aidha anasema baada ya uchaguzi, chama hicho kilichoasisiwa na Mabere Marando na ambacho kilichoonekana kuwa chama mbadala kwa CCM kilighubikwa na mtafaruku uliopelekea kusambaratika kwa viongozi wake waandamizi na kujikuta kikiwa njia panda kisiasa, jinamizi ambalo licha ya kudhibitisha uongozi uliopo wa chama hicho limeacha kovu kubwa la kisiasa nchini.

Matukio, kupanda na kuporomoka kwa NCCR-Mageuzi katika ulingo wa kiasiasa ni changamoto kwa viongozi wa vyama mbalimbali vya kisiasa nchini, ingawaje yeye binafsi na wanachama na wapenzi wa NCCR , chama hicho kimestahimili mawimbi ya kisiasa na kiko imara zaidi ya kipindi cha nyuma.

Hata hivyo anasema Watanzania ambao walikuwa na matumaini makubwa na mfumo wa vyama vingi, kwa kiasi fulani wameanza kupoteza imani kwa vyama hivyo na walishuhudia wimbi kubwa la wanachama mahiri waliokuwa kwenye upinzani wakikimbilia tena kurejea CCM.

Wanachama na viongozi hawa kwa mujibu wa kiongozi mwandamizi wa NCCR-Mageuzi, Dk. Sengondo Mvungi, wamesahau au hawajui maana ya chama cha kisiasa na ndiyo maana wamekosa misimamo na kuwa ‘malaya’ wa kisiasa.

Itakumbukwa kwamba kwenye semina ya wajumbe wa halmashauri mjumbe akiwasilisha mada kweye semina ya wajumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho kwenye hoteli ya Bahari Beach Dar es Salaam mwaka 2006, Dk. Mvungi alisema kuwa chama cha kisiasa ni mjumuiko wa hiari wa wananchi wenye mtizamo mmoja wa kiitikadi ya kisiasa wenye nia ya kujenga hoja ndani ya jamii ili kupata ridhaa ya uongozi wa jamii kwa misingi na malengo ya itikadi yao.

Kwamba chama cha siasa huundwa kwa hiari ya wanachama bila ya shuruti, hivyo wanachama waliobakia ndani ya chama hicho ni wale wanaotekeleza mtazamo wao na hawayumbishwi na matakwa ya viongozi.

Mrema alipofarakana na Marando na baadaye akakihama chama hicho, wanachama wengi walimfuata Mrema na kujiunga na chama cha TLP bila ya kubaini na kukubaliana na itikadi ya chama hicho, matokeo yake tumeshuhudia wanachama hao wakikihama tena TLP na kujiunga na vyama vingine au kurejea CCM.

Aidha kuhama kwa Mrema, kuliangaliwa na baadhi ya watanzania kama mwisho wa NCCR-Mageuzi, lakini chama hicho kikastahimili matokeo ya mtafaruku huo na kuendelea kufanya uchaguzi mkuu ndani ya chama ambapo Mbatia alimshinda muasisi wa chama hicho kwenye uchaguzi wa kidemokrasia.

“NCCR-Mageuzi chini uongozi wa wangu imeendelea kughubikwa na matatizo mbalimbali ndani na nje ya chama, matatizo ambayo kwa kiasi fulani yameonyesha ukomavu wa kisiasa wa chama hicho ukilinganisha na vyama vingine,” anasema.

Chama hiki cho kinaongozwa kwa kufuata itikadi ya demokrasia ya kijamii ambayo lengo lake ni ujenzi wa jamii yenye uhuru, haki za binadamu, usawa na ustawi wa jamii na inayokubali kutegemeana kwa binadamu katika msingi wa mmoja kwa wote na wote kwa mmoja kimeweza kujiendesha bila ya kutegemea ruzuku toka serikali toka mwaka 2000 hadi leo.

Kutokana na mtafaruku uliokikumba, chama hicho kilishindwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 na kuambulia mbunge mmoja, Gulam Hussein Kiffu, toka jimbo la Kigoma Kusini ambaye hata hivyo aliondolewa katika nafasi hiyo baada ya kupingwa kwa matokeo hayo mahamakani na hivyo kukosa uhalali wa kupatiwa ruzuku na serikali.

“NCCR- Mageuzi imeweza kuweka historia ya kudai mabadiliko ya katiba wakati huo kikundi cha wanaharakati, tulifanikiwa na serikali ikaruhusu mfumo huo, lakini pia tuna historia ya kuwa na mtandao mkubwa nchini baada ya uchaguzi mkuu wa kwanza 1995”. Anasema Mbatia na kuongeza kuwa chama chake ndicho chama pekee kilichoweza kuendesha chaguzi za kidemokrasia ndani ya chama kisheria.

Mbatia anasema hali ya vyama vya upinzani nchini bado inafanana na hali ndani ya CCM ambapo kiongozi wa chama haruhusu kushindana na wanachama wengine wakati wa uchaguzi mkuu, hali ambayo inadhoofisha demokrasia na kuendekeza udumishwaji wa fikra za baadhi ya watu.

Chama hicho kikongwe, pia kimeweza kuandika historia ya kuwa chama cha kwanza cha upinzani kutoa mbunge, Mabere Marando, kuwakilisha kwenye bunge la Afrika Mashariki huku kikiwa kimetumia vizuri michango ya wanachama wake na kununua rasilimali nyingi za kudumu kwenye maeneo mbalimbali nchini.

“Bila ya ruzuku ya serikali, chama chetu kimeweza kutumia michango ya wanachama kuendesha mikutano mikuu ndani ya chama, kampeni kwenye chaguzi mbalimbali, tumenunua magari kadhaa na kununua majengo kwenye wilaya mbalimbali nchini likiwemo jengo la kisasa la ofisi za makao makuu na kununua ardhi kwa ajili ya kujenga chuo kikuu,” anasema Mbatia.

Akizungumzia changamoto kubwa zilizokikabili chama hicho kipindi cha uongozi wake, Mbatia anaeleza kuwa alipata wakati mgumu sana wakati NCCR-Mageuzi kilipoamua kuwawekea pingamizi wagombea wa CUF kwenye uchaguzi wa marudio kwenye mikoa ya Pemba ambapo wananchi walikihukumu chama hicho kuwa ni wakala wa CCM.

Anasema kuwa mbele ya sheria, vyama vyote ni sawa na vyote vinawania kupata ridhaa ya kuongoza na hakuna chama chochote chenye ubia na chama kingine, hivyo kwa kuweka pingamizi dhidi ya wagombea wa CUF, NCCR-Mageuzi ilikuwa ikitekeleza haki yake ya kikatiba na kisheria na kwamba chama hicho kilikuwa na haki zote za kisheria kuwafanya hivyo.

“CUF waliwahi kumuwekea pingamizi mgombea wetu kwenye uchaguzi wa kule Kagera, wananchi hawakulalamika, na hata wakati walipomzuia Mhe. Naila Jidawi kugombea urais wa Zanzibar kupitia chama chetu pia watu walinyamaza, lakini sisi tulipotekeleza wajibu wetu wa kikatiba kuwawekea wagombea wao pingamizi basi tukaonekana wanaCCM, huu ni upuuzi!”. Amesisitiza Mbatia.

Kiongozi huyo amesema kuwa Tanzania ni ya watanzania wote ya vyama vyote, hakuna ngome ya chama Fulani kwasababu vyama vyote vina haki mbele ya sheria na kikatiba hivyo dhana ya kwamba Zanzibar ni ngome ya CCM na CUF pekee inadumaza demokrasia ya vyama vingi na haistahili kuendekezwa.

Licha ya CCM kuhodhi rasilimali nyingi zilizochangiwa na watanzania wote na kutumia fursa ya kuwepo madarakani kwa kipindi kirefu kuvinyanyasa vyama vya upinzani, lakini Mbatia anaamini kuwa mageuzi ya kisiasa yanawezekana kutokana na nguvu za wananchi endapo watazijua haki zao na kusimama kidete kuzidai kwa kujiunga na vyama vya upinzani na kuvipatia nguvu na kutokana na hilo chama chake kimefanya marekebisho kadhaa kwenye katiba yake ya 1992 ili kukiwezesha kujiendesha kisayansi zaidi.

Wananchi wanavikataa vyama vya upinzani nyakati za uchaguzi kutokana na rushwa na vitisho na kutokana na dola kutumiwa na chama hicho tawala lakini mara baada ya uchaguzi wanaanza kukilaani chama hicho kutokana na ubadhirifu na kuingia mikataba mibovu na kutumia vibaya mamlaka zake.

“CCM inatumia mabavu kuvinyanyasa vyama vya upinzani, inatumia vitisho kuwanyakua wanachama wetu, kuna mfano niloutoa wa Mkuu wa wilaya, ya Sumbawanga, C.F.Mwali, alivyotumia madaraka yake vibaya na kupokea vitendea kazi vya NCCR- Mageuzi na kuvikabidhi rasmi kwa Katibu wa CCM kwa barua yenye Kumb. Na. SUMB/SS.20/1 ya 11/11/2003”. Amesema na kuongeza kuwa watanzania wameshuhudia jinsi marais ambao ni viongozi wa CCM wanavyokusanya bendera na mali nyingine za vyama na kuvirundika kwenye ofisi za CCM.

Licha ya vyama vya upinzani kukosa umaarufu uliotarajiwa kutokana na uongozi mbovu kwenye baadhi ya vyama, lakini kumekuwepo na malalamiko mengi kuhusu matumizi ya nguvu za dola katika kuvidhoofisha vyama hivi, hii imetumika mara kadhaa wakati viongozi wa vyama hivyo kikiwemo NCCR-Mageuzi walipopigwa na polisi wakati wa maandamano.

Upungufu wa kutokuwepo kwa katiba mpya pia ni dosari kwasababu mara baada ya madadiliko ya kisiasa kuridhiwa, kulitakiwa kuwepo na katiba mpya ambayo inakidhi matakwa na hali ya kisiasa.

Marekebisho ya katiba yaliyofanywa yalifanywa na bunge lililokuwa limesheheni wabunge wa CCM, hivyo kukubalika kwake na wadau wengine kisiasa ni vigumu kwasababu bunge halina mamlaka ya kuunda katiba kwavile linakuwepo kutokana na katiba iliyotungwa na wadau wote.

Kwa mujibu wa mwanasheria mmoja ambaye sina haja ya kutaja jina lake, Katiba yoyote katika nchi inayotawaliwa kidemokrasia hufaqnyiwa mabadiliko kutokana na mabadiliko ya kiuchumi au kisiasa na sio vinginevyo; hivyo kutokana na badiliko kuu la mfumo wa kisiasa tulilopitia kuna haja kubwa ya kuwepo kwa katiba mpya inayokidhi haja za hali ya sasa ya kisiasa na kiuchumi.

Mfano mmoja wa mabadiliko ya kikatiba kutokana na hali ya kiuchumi ni kuwepo na baadhi ya sheria ambazo zinatoza faini ya sh.200, katika mazingira ya sasa kama mtuhumiwa atatozwa faini ya kiwango hicho kitasaidia nini.

Katika hili, NCCR-Mageuzi inadai kuwepo kwa katiba mpya isiyowekewa viraka ili iweze kukidhi mahitaji na matakwa ya mfumo uliopo, kama chama tawala kitaendelea kung’ang’ania katiba iliyopo basi itashuhudia vyama vya upinzani vikifa kifo vya mende na kurejesha nchi kwenye mfumo wa chama kimoja.

Kuhusu matarajio ya baadaye ya chama, James Mbatia anasema kuwa NCCR-Mageuzi ni chama pekee nchini kilichoandaa Mpango Mkakati wa chama cha umma kwa ajili ya mageuzi ya kidemokrasia nchini Tanzania, mpango ambao umeanza kutekelezwa toka mwaka 2006 kufikia lengo lake 2010 na kwamba mpango huo umekuwa ukiendelea kutekelezwa kama ulivyopangwa.

0755 312859
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano Julai 18,2007

Tendwa:Sheria ya kuungana ni kikwazo




JULAI mosi mwaka huu, Tanzania imetimiza miaka 15 tangu ianzishe mfumo wa vyama vingi vya siasa. Katika mahojihano na Mwandishi Wetu Happiness Katabazi, Msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa, anaeleza kwa mapana historia, changamoto na mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa mfumo huo.

Swali: Tunaomba utueleze kwa mapana historia ya mfumo wa vyama vingi.

Jibu: Mfumo wa vyama vingi vya siasa hapa nchini ulianza rasmi Julai mosi, 1992, kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992.
Lakini kabla ya hapo, kulikuwa na vuguvugu la wanajamii la kuleta msukumo wa kutaka mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Msukumo huo uliungwa mkono na mabadiliko ya kiulimwengu ya kisiasa, hasa kuanguka kwa dola za Kisoshalisti (dola la Ulaya Mashariki) iliyokuwa ikiongozwa na Urusi ambao ndiyo walikuwa na siasa za Usoshalisti (Ujamaa).
Sasa kuanguka kwa dola hizi ndio kulifanya jumuiya za Ulaya Mashariki kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi.

Mabadiliko hayo ya nchi za Ulaya, yaliungwa mkono na nguvu ya soko huria (free economic) ambapo nchi zilikuwa na uwezo wa kuuza na kununua badala ya uchumi kuwa hodhi ya serikali.

Kwa hiyo mambo yote haya yalileta mabadiliko yakaingia kwenye mfumo wa vyama vingi. Hivyo uamuzi wa Tanzania kujiunga na mfumo huu si wa kushangaza.

Na muda mfupi baada ya mfumo huo kuanzishwa nchini, taasisi nyingi zilituma maombi ya kutaka kuanzishwa kwa vyama vya siasa kwa mujibu wa sheria.
Hadi mwaka 1993, kulikuwa na maombi 51 ya usajili, lakini kutokana na mchujo uliofanyika kwa mujibu wa sheria, ni vyama 13 vilikubaliwa.

Vyama hivi 13 vilianza kushiriki chaguzi ndogo mwaka 1994, kama za nafasi ya ubunge, udiwani endapo tu wabunge au madiwani walikuwa wamefariki au wamepoteza sifa za kuendelea kushika nyadhifa hizo.
Kwa hiyo mwaka 1995 ndipo ulipofanyika uchaguzi mkuu wa kwanza ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Swali: Hali ya kisiasa wakati huo ilikuwaje?

Jibu: Kulikuwa na hali ya vuguvugu la kutaka kutoka katika mfumo wa chama kimoja na nifananishe vuguvugu hilo lilikuwa sawa na ndege au wanyama waliokuwa wamefungiwa sehemu moja, sasa wanataka kufunguliwa wakimbie.

Kimsingi, dira na mwelekeo wa mfumo wa vyama vingi havikuwapo wakati huo mwaka 1995.
Kwa mfano, sheria ilikuwapo na ilikuwa imerekebishwa, lakini wananchi hawakupata nafasi ya uelewa kwamba sheria hiyo ilikuwa imesema nini na hawakupata nafasi ya kupata elimu ya uraia kuhusu mfumo wa vyama vingi na matokeo yake vyama vingi vya siasa vilitoka na hoja ya sheria 40 zilizotamkwa kuwa ni mbovu na kandamizi na Tume ya Jaji Francis Nyalali.

Na hii ikageuka kuwa hoja ya kampeni katika uchaguzi wa mwaka 1995. Kimsingi katika kipindi hicho hali ya kisiasa ilikuwa inatafuta mwelekeo kama maji yanavyotafuta mkondo wa kutokea.
Ili kukidhi matakwa ya mfumo huo, katika uchaguzi wa 1995, vyama vilipata fedha kwa ajili ya kampeni toka serikalini.

Sasa baadhi ya wabunge na madiwani hawakufanya kampeni kama ilivyokusudiwa, kwa hiyo walikuwa wakiganga njaa na hakukuwa na marejesho ya fedha hizo serikalini.

Tunaweza kusema kipindi hicho wale waliokuwa na dhamira ya kisiasa walifanikiwa. Kivipi? Kulikuwa na uwakilishi mkubwa wa upinzani bungeni na vile vile madiwani wengi kwa kuwa halmashauri nyingine ziliongozwa na wapinzani na halmashauri zilizoongozwa na wapinzani wakati huo ni Bariadi, Karatu na Kigoma.

Swali: Baada ya uchaguzi wa mwaka 1995 nini kilitokea?

Jibu: Vyama vilitulia, hakukuwa na vuguvugu kama lilivyokuwa awali, vyama vilivyoshindwa uchaguzi vilitafakari nini cha kufanya kwa sababu mfumo wa vyama vingi ulishaanza.

Kwa hiyo utaona vyama vingi viliingia kwenye uchaguzi huo vikashindwa kukamata dola.
Kwa hiyo mwaka 1996-2000, kikawa kipindi cha mtawanyiko wa wanachama toka chama kimoja hadi kingine na pia kilikuwa ni kipindi cha migogoro ndani ya vyama vya siasa ama kwa kukosa uongozi au hata kugombea ruzuku ambayo ilikuwa ikigombewa sana.

Pia kilikuwa kipindi cha vyama kujizatiti, na kujijenga upya. Mfano ni kipindi ambacho viongozi kama Augustine Mrema alitoka chama cha NCCR-Mageuzi na kwenda Tanzania Labour Party (TLP).

Ni kipindi ambacho vijana walichukua uongozi wa juu kama Mwenyekiti wa sasa wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia.Vyama vilikuwa na sifa kama CHADEMA vilivyopwaya kipindi cha nyuma, lakini pia kilikuwa ni kipindi cha kujiimarisha.

Vyama vikongwe kama UMD baada ya viongozi wake wa juu kuondoka, kama Abdallah Fundikira na kujiunga na CCM, vililala usingizi. Kwa ujumla hakikuwa kipindi cha mikikimikiki na hekaheka kama ilivyokuwa mwaka 1995.

Swali: Uchaguzi wa pili ndani ya mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 2000, ulikuwaje kwa upande wa Tanzania Bara?

Jibu: Ulikuwa ni uchaguzi wa pili wa vyama vingi. Kipindi hiki serikali haikutoa ruzuku kwa vyama, kwa sababu sheria ya vyama vingi Namba 5 ya mwaka 1992 ilifanyiwa marekebisho na kuweka vigezo vya chama kufanikiwa kupata ruzuku.
Baadhi ya vigezo ni chama lazima kishinde uchaguzi ngazi ya diwani na ubunge au chama kupata asilimia 5 katika kura zilizopigwa kitaifa.

Japokuwa vyama vyote 13 vilishiriki katika uchaguzi, lakini kampeni zilidorora kwa kuwa hawakuweza kufika katika maeneo yote waliyokusudia na matokeo yake ni kwamba, vyama havikupata uwakilishi mkubwa ndani ya Bunge na serikali za mitaa dhidi ya CCM.
Pia kilikuwa ni kipindi ambacho wabunge waliofanikiwa katika chama tawala (CCM), ni wale waliotoka vyama vya upinzani.

Kwa hiyo vyama vingi vya upinzani vilikosa wagombea wenye uwezo wa kufanya kampeni na wale wachache waliopata ubunge kwa kupitia vyama vya upinzani, walienguliwa toka CCM baada ya kufanyika kwa kura za maoni ndani ya chama hicho.
Na hawa walikuwa wasemaji wazuri sana wa kambi ya upinzani ndani ya Bunge.

Swali: Uchaguzi wa pili ndani ya mfumo wa vyama vingi mwaka 2000, kwa upande wa Zanzibar, ulikuwaje?

Jibu: Ni kipindi ambapo Chama cha Wananchi (CUF) kilikuwa na mategemeo makubwa ya kushinda, hasa upande wa kiti cha urais, lakini CCM ilipata ushindi ambapo Rais Abeid Amani Karume, alianza kipindi chake cha kwanza cha urais.

Katika kipindi hiki, kulikuwa na mgogoro mkubwa wa kisiasa ambapo matokeo yake kulitokea vurugu za Januari 26, 2001 ambapo matokeo yake watu kadhaa walipoteza maisha yao.
Huu ulikuwa ni mwendelezo wa mgogoro wa kisiasa Zanzibar uliotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 1995.
Kipindi hiki kwa ujumla kilikuwa ni cha mgongano wa kiitikadi baina ya vyama vya CCM na CUF. Lakini pia ni kipindi cha maelewano baada ya makubaliano (policatal diolog) yaliyojengwa na utashi wa kisiasa.

CCM na CUF vikaungwa mkono na wanajamii na vyama vingine vya siasa ili kuleta mwafaka na hali bora ya kisiasa Zanzibar.

Mazungumzo haya yalichukua takribani miezi sita na Oktoba 21 mwaka 2001, vyama vya CCM na CUF viliwekeana saini na kuwa mwafaka wa makubaliano ya kisiasa hapa nchini.
Hiki ni kipindi cha ukomavu wa kisiasa ulioanza kujitokeza nchini kwa vyama vinavyogongana kuwa na mazungumzo na kuelewana bila kutafuta msaada wa usuluishi nje ya nchi.

Swali: Tueleze kipindi cha mwaka 2000-2005 vuguvugu la kisiasa lilikuwaje?

Jibu: Vyama vya siasa viliongezeka toka 13 hadi 18 na vyama viwili kupoteza usajili wa kudumu ambavyo ni PONA na TPP, vilivyofutwa kwa kukiuka matakwa ya sheria. Huu ni wakati ambapo demokrasia ilionekana kukomaa katika nchi yetu.

Kwa upande wa CCM, kilikuwa ni kipindi cha kujizatiti ili kuendelea kushika uongozi na kilikuwa ni kipindi cha mwisho wa serikali ya awamu ya tatu kushika uongozi.

Kwa kufuata dhana ya muungano wa vyama vya siasa Kenya na kuunda NARC, baadhi ya vyama vya siasa hapa Tanzania wanajaribu kuunda muungano wa kisiasa, lakini masharti yanawashinda kwa sababu sheria ya vyama vya siasa ya hapa nchini haiwaruhusu kuungana bila kupoteza sifa za vyama vyao.

Dhamana yao pia haikuwa ya kisiasa japo kuwa wangeweza kushirikiana katika chaguzi za serikali za mitaa na baadaye uchaguzi mkuu 2005.

Swali: Uchaguzi wa mwaka 2005 umewafundisha nini Watanzania na vyama vya siasa kwa ujumla?

Jibu: Uchaguzi huu ulikuwa ni kipimo cha sheria ya uchaguzi ya mwaka 1992 na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo imefanyiwa marekebisho mara kadhaa, hasa eneo lililofanyiwa marekebisho ni la mgombea mwenza.

Uchaguzi huu japo ulikwenda vizuri, lakini ulifikwa na kasoro kutokana na kifo cha mgombea mwenza wa CHADEMA, ambacho kilitokea siku tatu kabla ya kupiga kura. Hali hii ilifanya uchaguzi kuahirishwa kwa siku 51 na vyama vya siasa viliathirika kifedha na kupungukiwa na ari ya kufanya kampeni.

Serikali nayo ilipungukiwa na fedha kibajeti kwa ajili ya kununulia vifaa, usafiri wa vifaa vya kupigia kura nk. Baada ya uchaguzi CCM ilipata ushindi kwa asilimia 80.28.

Chama cha CUF japokuwa kilipata ushindi mkubwa Tanzania visiwani, lakini Tanzania bara haikupata hata kiti kimoja cha ubunge, viti vyote vya ubunge vilipatikana Zanzibar na hasa Pemba vilikopatikana viti 17 na Unguja Mji Mkongwe kilipatikana kiti kimoja.
CHADEMA kilifuatia kwa ushindi wa viti vitano vya ubunge na UDP na TLP vilipata kiti kimoja kimoja.
Huu haukuwa ushindi mzuri kwa vyama vya upinzani, ni matokeo ya mambo yaliyotokea katika uchaguzi wa mwaka 2000, kwa hiyo vyama havikuwa vimejizatiti kisiasa.

Na hivyo uchaguzi wa mwaka 2005 ulikuwa ni fundisho kwa vyama vya upinzani. Ni vyema sasa wakajipanga vizuri na wawafikie wananchi wengi waliopo vijijini kwa kuwa asilimia 80 ya Watanzania wanaishi vijijini.

Swali: Hadi hivi sasa Tanzania ina vyama vingapi vya siasa ambavyo vina usajili wa kudumu?

Jibu: Hadi sasa Tanzania ina jumla ya vyama vya siasa 18 ambavyo vina usajili wa kudumu.
Vyama hivyo ni Chama cha Mapinduzi (CCM), National Convention for Construction and Reform (NCCR-Mageuzi), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), The Civic United Front (CUF), Union for Multiparty Democracy (UMD), National League for Democracy (NLD) na United People’s Democratic Party (UPDP).
Vingine ni National Reconstruction Alliance (NRA), Tanzania Democratic Alliance (TADEA), Tanzania Labour Party (TLP), United Democratic Party (UDP) na Demokrasia Makini (MAKINI).

Pia kuna The Forum for Restoration of Democracy (FORD), Chama cha Haki na Ustawi (CHAUSTA), Democratic Party (DP), Progressive Party of Tanzania (PPT-Maendeleo), Jahazi Asilia na Sauti ya Umma (SAU).

Licha ya kuwa na vyama hivyo, ofisi yangu ipo mbioni kuifuta FORD, kwa kuwa imekiuka katiba yake yenyewe, sheria ya vyama vingi ya mwaka 1992 na cha kustaajabisha hadi hivi tunavyozungumza chama hicho hakijafanya uchaguzi wa ndani.

Swali: Tueleze hali ya kisiasa kwa ujumla hivi sasa Tanzania bara na visiwani ikoje?

Jibu: Kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano ni nzuri. Vyama vya siasa hivi sasa vimekuwa na mwelekeo mzuri kiitikadi.

Migongano na migogoro ya kisiasa ndani ya vyama imepungua, vyama hivi sasa vimejiimarisha kiuongozi na vingi vimeishafanya chaguzi ndani ya vyama vyao na vingine vinajiandaa kufanya chaguzi ndani ya vyama vyao, ikiwemo CCM.

Hivi sasa vyama ya upinzani, vimejenga uhusiano wa kushirikiana kwa nia ya kuungana na hapo baadaye kidemokrasia. Hakika hili ni jambo jema kwa vyama hivi kuwa na mawazo ya pamoja, mwelekeo na mtazamo wa pamoja.

Ila tatizo lililopo ni sheria ya vyama vingi ya mwaka 1992, ambayo hairuhusu vyama kuungana, lakini sheria hiyo hiyo inaruhusu vyama hivyo kushirikiana katika kampeni. mfano chama kimoja kumuunga mkono mgombea wa chama kingine.

Nakiri sheria hii ni tatizo, lakini ofisi yangu ilikwishapeleka mapendekezo serikalini ya kutaka sheria hiyo ifanyiwe marekebisho licha ya kwamba hadi sasa bado marekebisho hayajafanyika.

Swali: Mfumo wa vyama vingi vya siasa umetuletea nini Watanzania?

Jibu: Hakuna ubishi, mfumo wa vyama vingi umetutoa katika mgando wa chama kimoja, ambao ulikuwa hautoi nafasi ya wenye kero kukosoa serikali na kuweka hoja mbadala.
Hivi sasa wananchi wana mwamko mkubwa katika masuala mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii. Leo hii Bunge si chombo tena cha utekelezaji wa matakwa ya chama kama ilivyokuwa awali.

Sasa hivi Bunge ni chombo chenye nguvu ya kuielekeza serikali nini cha kufanya ili kukidhi matakwa ya wananchi. Hapo awali Bunge lilikuwa likifuata maelekezo ya chama. Dhamana kubwa ilikuwa watu wote walikuwa ni wanachama wa CCM kwa hiyo ilikuwa ni demokrasia ya chama kimoja.

Leo hii wananchi hata bila kupitia Bunge wanaweza kutoa maoni yao kupitia taasisi mbalimbali kutokana na uhuru wa kutoa mawazo yao. Hakika ni jambo la kujipongeza.

Serikali nayo inakubali kukosolewa na kufanya marekebisho ili kukidhi matakwa ya wananchi. CCM nayo inakubali kukosolewa na kujikosoa ili iweze kuendelea kubaki madarakani kwa kuheshimu na kufuata sheria.

Ukilinganisha mfumo wa vyama vingi vya siasa na ule wa chama kimoja, ukiweka kwenye mizani utaona mfumo wa vyama vingi ni mzuri na umeleta fikra za kimapinduzi na maendeleo makubwa katika taifa letu.

0755 312 859
katabazihappy@yahoo.com
www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Tanzania Daima Jumatano Julai 18,2007

NCCR-Mageuzi imestahimili mawimbi ya kisiasa-Mbatia

MWENYEKITI wa Chama NCCR-Mageuzi, James Mbatia, anasema kutokana na kurekebishwa kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutungwa kwa sheria Na. 5 ya mwaka 1992 na sheria nyingine zinazoruhusu kuundwa kwa vyama vingi vya siasa nchini, taifa letu limeshuhudia kuibuka kwa vyama ambavyo kwa kiasi fulani vimeleta changamoto na kuchochea maendeleo katika ngazi za jamii ungana na Mwandishi Wetu ,Happiness Katabazi , ambaye alifanya naye mahojiano na kiongozi hivi karibuni.

James Mbatia anasema kutokana na uamuzi huo, vyama 13 vilivyopata usajili wa kudumu kutoka kwa Msajili wa Vyama ni pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM), National Convetion for Construction and Reform – Mageuzi (NCCR-Mageuzi), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Civic United Front (CUF) na United Democratic Party (UDP).

Vyama vingine vilikuwa ni TADEA, NRA, UMD, Tanzania Labour Party (TLP), UPDP, PONA na Tanzania Peoples Party (TPP); vyama vingine viliendelea kuandikishwa na kupata usajili wa kudumu baadaye na kujiunga rasmi kwenye mchakato huo wa kisiasa.

Anasema licha ya uchanga wa vyama vya siasa vilivyoundwa kufuatia kutungwa kwa sheria hiyo, chama kikongwe na kinachotawala, Chama cha Mapinduzi ambacho kimekuwa na historia ndefu ya kutoka mwaka 1954, kimekiri kwa nyakati tofauti kutikiswa na chagamoto zilizotokana na vyama hivi vichanga.

Leo hii tunapotafakari kutimia kwa miaka 15 baada ya kuruhusiwa kwa mfumo huo demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania, ni lazima kama wananchi wa taifa hili kuangalia kwa makini tulikotoka, kuanzia enzi za Uhuru chini ya vyama vingi, kufutwa kwa mfumo huo na kuingizwa kwenye mfumo wa utawala wa chama kimoja na baadaye kurejea tena kwenye mfumo huu.

“Historia ni ndefu, na matukio muhimu yaliyotokea katika kipindi hicho ni mengi, lakini lililo la umuhimu wa kipekee na swali la msingi la kujiuliza ni Je, mfumo huu umetimiza kwa kiasi gani matarajio ya watanzania ambao licha ya asilimia 80 kukataa mfumo huo lakini serikali ikaamua kuufuata”anasema James Mbatia.

Anasema kumetokea matukio kadhaa katika historia ya mfumo huu kati ya Julai 1992 na Oktoba 1995 ambapo katika uchaguzi wa kwanza uliofanyika 1993, CCM ilishinda kwa asilimia 97 kwenye kinyang’anyiro cha kutafuta wenyeviti wa vitongoji, vijiji na wajumbe wa serikali za vijiji, chama hicho kiliendelea kuvinyanyasa vyama vingine hadi mwishoni mwa 1995.

Aidha Oktoba 1994, kulikuwa na uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa kwa maana ya madiwani ambapo kati ya nafasi 2,411 zilizokuwepo, ni nafasi 1,226 zilizoshindaniwa na vyama mbalimbali kutokana na nafasi zingine kunyakuliwa na wagombea wa CCM bila ya kupingwa na mwisho CCM ikajikusanyia viti 2,336 huku vyama vya upinzani vikiambulia viti 75 sawa na asilimia 3.11.

Oktoba mwaka 1995, uchaguzi mkuu wa kwanza uliendeshwa nchini kwa mara ya kwanza na vyama vingi vikashiriki na kupata matokeo kama ifuatavyo kwenye uchaguzi wa Rais wa Jamhuri; CCM 61.96%, NCCR – Mageuzi 27.8%, CUF 6.4% na UDP 4.0%; hii ni kutokana na kura 6,512,745 zilizopigwa.

Na katika uchaguzi wa wabunge jumla ya vyama siasa 13 vilishiriki kuwania kura 6,440,913 zilizopigwa na kupata matokeo kama ifuatavyo; CCM 59.22%, NCCR-Mageuzi 21.83%, CHADEMA 6.16%, CUF 5.02%, UDP 3.32%, TADEA 1.19%, NRA 0.94%, UMD 0.64%, TLP 0.41%, NLD 0.41%, UPDP 0.31%, PONA 0.28% na TPP 0.24%.

Anaeleza kuwa kwa vyovyote vile kutokana na matokeo hayo, chama cha NCCR-Mageuzi kilionekana dhahiri kuwa na ushawishi mkubwa miongoni mwa wapiga kura na kilitoa changamoto kubwa katika siasa na mfumo mpya wa vyama vingi vya siasa nchini; changamoto ambayo miaka takriban 15 baadaye imeonekana kufifia na kukosa matumaini makubwa.

“Nakumbuka tukio moja nililolishuhudia wakati wa kampeni hizo ambazo wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa endapo Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Julius Nyerere, asingelichukua hatua ya kukisaidia CCM katika kampeni zake, basi leo historia ingekuwa inasema mambo mengine,” anasema Mbatia.

Mbatia anasema ndicho kipindi ambacho mgombea urais kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, Augustine Mrema, alikuwa ameingia kwenye nyoyo za watanzania kwa kiwango kikubwa nami nilishuhudia hilo kwenye mji mdogo wa Shirati wilayani Tarime, wakati mashabiki na wanachama wa chama hicho walivyojitokeza bila ya woga kumpokea Nyerere wakiwa na bendera na mavazi rasmi ya NCCR-Mageuzi.

“Hakukuwepo na woga tena, walikuwa wakikimbia pande zote mbili za barabara wakiwa na bendera na mabango yanayoonyesha kuwa hawamtaki mgombea wa CCM, Benjamin Mkapa na Nyerere mwenyewe na kufurika kwenye uwanja wa Obwere kumdhihirishia Nyerere kuwa chama chake kimewachosha’ anasema.

Aidha anasema baada ya uchaguzi, chama hicho kilichoasisiwa na Mabere Marando na ambacho kilichoonekana kuwa chama mbadala kwa CCM kilighubikwa na mtafaruku uliopelekea kusambaratika kwa viongozi wake waandamizi na kujikuta kikiwa njia panda kisiasa, jinamizi ambalo licha ya kudhibitisha uongozi uliopo wa chama hicho limeacha kovu kubwa la kisiasa nchini.

Matukio, kupanda na kuporomoka kwa NCCR-Mageuzi katika ulingo wa kiasiasa ni changamoto kwa viongozi wa vyama mbalimbali vya kisiasa nchini, ingawaje yeye binafsi na wanachama na wapenzi wa NCCR , chama hicho kimestahimili mawimbi ya kisiasa na kiko imara zaidi ya kipindi cha nyuma.

Hata hivyo anasema Watanzania ambao walikuwa na matumaini makubwa na mfumo wa vyama vingi, kwa kiasi fulani wameanza kupoteza imani kwa vyama hivyo na walishuhudia wimbi kubwa la wanachama mahiri waliokuwa kwenye upinzani wakikimbilia tena kurejea CCM.

Wanachama na viongozi hawa kwa mujibu wa kiongozi mwandamizi wa NCCR-Mageuzi, Dk. Sengondo Mvungi, wamesahau au hawajui maana ya chama cha kisiasa na ndiyo maana wamekosa misimamo na kuwa ‘malaya’ wa kisiasa.

Itakumbukwa kwamba kwenye semina ya wajumbe wa halmashauri mjumbe akiwasilisha mada kweye semina ya wajumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho kwenye hoteli ya Bahari Beach Dar es Salaam mwaka 2006, Dk. Mvungi alisema kuwa chama cha kisiasa ni mjumuiko wa hiari wa wananchi wenye mtizamo mmoja wa kiitikadi ya kisiasa wenye nia ya kujenga hoja ndani ya jamii ili kupata ridhaa ya uongozi wa jamii kwa misingi na malengo ya itikadi yao.

Kwamba chama cha siasa huundwa kwa hiari ya wanachama bila ya shuruti, hivyo wanachama waliobakia ndani ya chama hicho ni wale wanaotekeleza mtazamo wao na hawayumbishwi na matakwa ya viongozi.

Mrema alipofarakana na Marando na baadaye akakihama chama hicho, wanachama wengi walimfuata Mrema na kujiunga na chama cha TLP bila ya kubaini na kukubaliana na itikadi ya chama hicho, matokeo yake tumeshuhudia wanachama hao wakikihama tena TLP na kujiunga na vyama vingine au kurejea CCM.

Aidha kuhama kwa Mrema, kuliangaliwa na baadhi ya watanzania kama mwisho wa NCCR-Mageuzi, lakini chama hicho kikastahimili matokeo ya mtafaruku huo na kuendelea kufanya uchaguzi mkuu ndani ya chama ambapo Mbatia alimshinda muasisi wa chama hicho kwenye uchaguzi wa kidemokrasia.

“NCCR-Mageuzi chini uongozi wa wangu imeendelea kughubikwa na matatizo mbalimbali ndani na nje ya chama, matatizo ambayo kwa kiasi fulani yameonyesha ukomavu wa kisiasa wa chama hicho ukilinganisha na vyama vingine,” anasema.

Chama hiki cho kinaongozwa kwa kufuata itikadi ya demokrasia ya kijamii ambayo lengo lake ni ujenzi wa jamii yenye uhuru, haki za binadamu, usawa na ustawi wa jamii na inayokubali kutegemeana kwa binadamu katika msingi wa mmoja kwa wote na wote kwa mmoja kimeweza kujiendesha bila ya kutegemea ruzuku toka serikali toka mwaka 2000 hadi leo.

Kutokana na mtafaruku uliokikumba, chama hicho kilishindwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 na kuambulia mbunge mmoja, Gulam Hussein Kiffu, toka jimbo la Kigoma Kusini ambaye hata hivyo aliondolewa katika nafasi hiyo baada ya kupingwa kwa matokeo hayo mahamakani na hivyo kukosa uhalali wa kupatiwa ruzuku na serikali.

“NCCR- Mageuzi imeweza kuweka historia ya kudai mabadiliko ya katiba wakati huo kikundi cha wanaharakati, tulifanikiwa na serikali ikaruhusu mfumo huo, lakini pia tuna historia ya kuwa na mtandao mkubwa nchini baada ya uchaguzi mkuu wa kwanza 1995”. Anasema Mbatia na kuongeza kuwa chama chake ndicho chama pekee kilichoweza kuendesha chaguzi za kidemokrasia ndani ya chama kisheria.

Mbatia anasema hali ya vyama vya upinzani nchini bado inafanana na hali ndani ya CCM ambapo kiongozi wa chama haruhusu kushindana na wanachama wengine wakati wa uchaguzi mkuu, hali ambayo inadhoofisha demokrasia na kuendekeza udumishwaji wa fikra za baadhi ya watu.

Chama hicho kikongwe, pia kimeweza kuandika historia ya kuwa chama cha kwanza cha upinzani kutoa mbunge, Mabere Marando, kuwakilisha kwenye bunge la Afrika Mashariki huku kikiwa kimetumia vizuri michango ya wanachama wake na kununua rasilimali nyingi za kudumu kwenye maeneo mbalimbali nchini.

“Bila ya ruzuku ya serikali, chama chetu kimeweza kutumia michango ya wanachama kuendesha mikutano mikuu ndani ya chama, kampeni kwenye chaguzi mbalimbali, tumenunua magari kadhaa na kununua majengo kwenye wilaya mbalimbali nchini likiwemo jengo la kisasa la ofisi za makao makuu na kununua ardhi kwa ajili ya kujenga chuo kikuu,” anasema Mbatia.

Akizungumzia changamoto kubwa zilizokikabili chama hicho kipindi cha uongozi wake, Mbatia anaeleza kuwa alipata wakati mgumu sana wakati NCCR-Mageuzi kilipoamua kuwawekea pingamizi wagombea wa CUF kwenye uchaguzi wa marudio kwenye mikoa ya Pemba ambapo wananchi walikihukumu chama hicho kuwa ni wakala wa CCM.

Anasema kuwa mbele ya sheria, vyama vyote ni sawa na vyote vinawania kupata ridhaa ya kuongoza na hakuna chama chochote chenye ubia na chama kingine, hivyo kwa kuweka pingamizi dhidi ya wagombea wa CUF, NCCR-Mageuzi ilikuwa ikitekeleza haki yake ya kikatiba na kisheria na kwamba chama hicho kilikuwa na haki zote za kisheria kuwafanya hivyo.

“CUF waliwahi kumuwekea pingamizi mgombea wetu kwenye uchaguzi wa kule Kagera, wananchi hawakulalamika, na hata wakati walipomzuia Mhe. Naila Jidawi kugombea urais wa Zanzibar kupitia chama chetu pia watu walinyamaza, lakini sisi tulipotekeleza wajibu wetu wa kikatiba kuwawekea wagombea wao pingamizi basi tukaonekana wanaCCM, huu ni upuuzi!”. Amesisitiza Mbatia.

Kiongozi huyo amesema kuwa Tanzania ni ya watanzania wote ya vyama vyote, hakuna ngome ya chama Fulani kwasababu vyama vyote vina haki mbele ya sheria na kikatiba hivyo dhana ya kwamba Zanzibar ni ngome ya CCM na CUF pekee inadumaza demokrasia ya vyama vingi na haistahili kuendekezwa.

Licha ya CCM kuhodhi rasilimali nyingi zilizochangiwa na watanzania wote na kutumia fursa ya kuwepo madarakani kwa kipindi kirefu kuvinyanyasa vyama vya upinzani, lakini Mbatia anaamini kuwa mageuzi ya kisiasa yanawezekana kutokana na nguvu za wananchi endapo watazijua haki zao na kusimama kidete kuzidai kwa kujiunga na vyama vya upinzani na kuvipatia nguvu na kutokana na hilo chama chake kimefanya marekebisho kadhaa kwenye katiba yake ya 1992 ili kukiwezesha kujiendesha kisayansi zaidi.

Wananchi wanavikataa vyama vya upinzani nyakati za uchaguzi kutokana na rushwa na vitisho na kutokana na dola kutumiwa na chama hicho tawala lakini mara baada ya uchaguzi wanaanza kukilaani chama hicho kutokana na ubadhirifu na kuingia mikataba mibovu na kutumia vibaya mamlaka zake.

“CCM inatumia mabavu kuvinyanyasa vyama vya upinzani, inatumia vitisho kuwanyakua wanachama wetu, kuna mfano niloutoa wa Mkuu wa wilaya, ya Sumbawanga, C.F.Mwali, alivyotumia madaraka yake vibaya na kupokea vitendea kazi vya NCCR- Mageuzi na kuvikabidhi rasmi kwa Katibu wa CCM kwa barua yenye Kumb. Na. SUMB/SS.20/1 ya 11/11/2003”. Amesema na kuongeza kuwa watanzania wameshuhudia jinsi marais ambao ni viongozi wa CCM wanavyokusanya bendera na mali nyingine za vyama na kuvirundika kwenye ofisi za CCM.

Licha ya vyama vya upinzani kukosa umaarufu uliotarajiwa kutokana na uongozi mbovu kwenye baadhi ya vyama, lakini kumekuwepo na malalamiko mengi kuhusu matumizi ya nguvu za dola katika kuvidhoofisha vyama hivi, hii imetumika mara kadhaa wakati viongozi wa vyama hivyo kikiwemo NCCR-Mageuzi walipopigwa na polisi wakati wa maandamano.

Upungufu wa kutokuwepo kwa katiba mpya pia ni dosari kwasababu mara baada ya madadiliko ya kisiasa kuridhiwa, kulitakiwa kuwepo na katiba mpya ambayo inakidhi matakwa na hali ya kisiasa.

Marekebisho ya katiba yaliyofanywa yalifanywa na bunge lililokuwa limesheheni wabunge wa CCM, hivyo kukubalika kwake na wadau wengine kisiasa ni vigumu kwasababu bunge halina mamlaka ya kuunda katiba kwavile linakuwepo kutokana na katiba iliyotungwa na wadau wote.

Kwa mujibu wa mwanasheria mmoja ambaye sina haja ya kutaja jina lake, Katiba yoyote katika nchi inayotawaliwa kidemokrasia hufaqnyiwa mabadiliko kutokana na mabadiliko ya kiuchumi au kisiasa na sio vinginevyo; hivyo kutokana na badiliko kuu la mfumo wa kisiasa tulilopitia kuna haja kubwa ya kuwepo kwa katiba mpya inayokidhi haja za hali ya sasa ya kisiasa na kiuchumi.

Mfano mmoja wa mabadiliko ya kikatiba kutokana na hali ya kiuchumi ni kuwepo na baadhi ya sheria ambazo zinatoza faini ya sh.200, katika mazingira ya sasa kama mtuhumiwa atatozwa faini ya kiwango hicho kitasaidia nini.

Katika hili, NCCR-Mageuzi inadai kuwepo kwa katiba mpya isiyowekewa viraka ili iweze kukidhi mahitaji na matakwa ya mfumo uliopo, kama chama tawala kitaendelea kung’ang’ania katiba iliyopo basi itashuhudia vyama vya upinzani vikifa kifo vya mende na kurejesha nchi kwenye mfumo wa chama kimoja.

Kuhusu matarajio ya baadaye ya chama, James Mbatia anasema kuwa NCCR-Mageuzi ni chama pekee nchini kilichoandaa Mpango Mkakati wa chama cha umma kwa ajili ya mageuzi ya kidemokrasia nchini Tanzania, mpango ambao umeanza kutekelezwa toka mwaka 2006 kufikia lengo lake 2010 na kwamba mpango huo umekuwa ukiendelea kutekelezwa kama ulivyopangwa.

0755 312859
katabazihappy@yahoo.com;www.katabazihappy.blogspot.com
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano Julai 18,2007

Dk.Slaa-Serikali inatekeleza changamoto za wapinzani?

Na Happiness Katabazi

MIAKA 15 sasa tangu Tanzania iruhusu mfumo wa vyama vingi, ambao wataalamu wa masuala ya kisiasa wanakiri kuwa umeleta changamoto kwa chama kilichopo madarakani mbali na wananchi kuwa huru kutoa maoni yao, lakini changamoto nyingine iliyotokana na mfumo huo ni uanzishwaji wa taasisi ambazo zimekuwa msaada kwa wananchi. Wakati imetimia miaka 15, ni utamaduni wetu kutafakari na kutathimini kule tulikotoka na hali ya sasa ikoje hususani kwa kuangalia mabadiliko na changamoto zilizoko. Katika mahojiana na Mwandishi Wetu HAPPINESS KATABAZI, Mbunge wa Karatu na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, anaelezea hali ya demokrasia ya vyama vingi nchini.

Swali: Je, ndani ya Bunge kuna mabadiliko gani tangu mfumo wa vyama vingi uanzishwe hapa nchini mwaka 1992?

Jibu: Kwanza lazima tukiri kwamba idadi ya wabunge wa upinzani ni ndogo.
Wabunge wa upinzani wapo 45 kati ya wabunge 320. Wabunge wa CHADEMA ni 11 kati ya hao 45 wa upinzani.
Lakini uchache si hoja japo maamuzi bungeni yanafanyika kwa kura na hivyo yote yanapitishwa kwa wingi wa wabunge wa CCM hata kama maamuzi hayo hayana maslahi kwa taifa.
Hasa suala la ongezeko la kodi na ushuru wa mafuta ambalo ni dhahiri kabisa halina maslahi kwa wananchi wa kawaida na kwa vyovyote ongezeko hilo litapandisha gharama ya maisha, hoja ambayo iliungwa mkono na wabunge wote wa CCM.
Pamoja na hali hiyo, kambi ya upinzani imetoa changamoto nyingi ndani ya Bunge.
Watanzania sasa wana nafasi ya kujua hali halisi ya mambo yalivyo katika uendeshaji wa nchi yao.
Hata wabunge wa chama tawala wakifungwa mdomo, wabunge wa kambi ya upinzani hakuna wa kuwafunga mdomo, watapasua mabomu tu.
Mfano, tuhuma za ubadhirifu ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambazo Gavana wa benki hiyo, Daudi Balali anauhusishwa, kwa mara ya kwanza sasa wananchi wa nchi hii wamejua kwamba ndani ya chombo kikubwa kama BoT kuna shutuma nzito kama hizo.
Aidha, Watanzania wamejua sasa kwamba kuna uwezekano wa kutengeneza bajeti mbadala kutoka kwenye rasilimali ya nchi yetu kama madini, misitu, uvuvi ambao kwa mara ya kwanza kambi ya upinzani imeonyesha kwamba taifa linaweza kupata sh trilioni 8 ikilinganishwa na sh trilioni 6 za serikali bila kuongeza mzigo wa ushuru na kodi kwa mwananchi wa kawaida.
Aidha, kutokana na rasilimali hizo, tungeweza kuwekeza zaidi kwenye huduma za jamii kama elimu ambayo tungeweza kuifanya kuwa bure hadi chuo kikuu, matibabu na yakalipiwa na serikali kikamilifu bila ya kumbughudhi mwananchi.

Swali: Unafikiri mchanganuo wa hoja za wabunge wa kambi ya upinzani zimeleta changamoto ndani ya Bunge?

Jibu: Siyo siri, tena mchanganuo wa hoja za kambi ya upinzani zimeleta changamoto ndani ya Bunge na zinaendelea kuleta changamoto wa utajiri wa mawazo, ambazo serikali ikizizingatia zitaleta unafuu kwa wananchi wa taifa hili kwa ujumla.
Kwa kuwa wapinzani hawawezi kufungwa midomo, serikali hivi sasa hailali tena, inajiandaa vizuri zaidi kwa maovu yanayoibuliwa na wapinzani ambayo wanayafanyia pamoja na uchache wao.
Naweza kusema ni sawa na mbwa mdogo ambaye kwa kupiga kelele tu, mwenye nyumba ataamka na kuchukua hatua za kulinda nyumba na mali zake.
Sasa kama wananchi hamtaamka baada ya kuamshwa na mbwa mdogo ili msaidiane naye kulinda rasilimali za nchi yenu, ipo siku mtajuta.

Swali: Manufaa na malengo ya mfumo wa vyama vingi nini?

Jibu: Lengo la msingi la vyama vingi vya siasa ni kushindanisha sera na ilani za vyama lengo likiwa ni kumnufaisha mwananchi apate kuchagua chama chenye sera bora.
Sura ya kwanza ya manufaa ya mfumo wa vyama vingi, ni kwamba umeleta utajirisho wa mawazo ambao huwezi kupata kwenye chama kimoja.
Hata kama vyama hivi havishiki madaraka kwa kuwa chama kimoja tu ndiyo kinatakiwa kiingie Ikulu, lakini kwa kuwa utajirisho huo si wa chama peke yake bali ni kwa wananchi wote, chama kina jukumu la kuchapisha na kutangaza sera zake, na mwisho wa hayo yote anayenufaika ni mwananchi.
Kwa hiyo, chama kinachotawala kinatakiwa kiwe na masikio ya kusikiliza sera za vyama vilivyoshindwa kutwaa madaraka na kisha izichukue na kuzifanyia kazi kwa maslahi ya wananchi wote bila kujali itikadi za vyama vyao.
Kwa mfano mwaka 1992, ukiona sera ya kwanza kabisa ya CHADEMA ilisema jengo la Chimwaga lililopo Dodoma ligeuzwe kuwa Chuo Kikuu kwa kuwa mji huo kuwa makao makuu ya nchi ni ngumu na badala yake ugeuzwe na uwe mji wa kitaaluma.
Nchi zilizoendelea kama Uingereza, kuna mji mmoja umekuwa kwa sababu serikali ya nchi hiyo ilitenga mji huo kuwa wa kitaaluma na kujengwa maduka makubwa ya kuuza bidhaa mbalimbali.
Serikali yetu ilikalia kimya sera hiyo hadi hivi sasa ndiyo imekubali jengo la Chimwaga liwe chuo kikuu, kwa hiyo jambo hili ni la kihistoria na kama serikali ingetekeleza tangu mwanzo hiyo sera yetu, mkoa huo hivi sasa ungekuwa mbali kimaendeleo.
Hivyo wananchi wanaweza kuangalia ushindani wa sera za vyama katika uchaguzi wa mwaka 2000, Serikali ya CCM ilikuwa inasema elimu ya msingi inalipiwa na wazazi, lakini vyama vya upinzani viliibuka na sera kwamba huwezi kumsomesha mtoto kwa kutegemea mchango wa wazazi ambao wengi wanaishi chini ya dola moja kwa siku na tulipendekeza elimu ya msingi itolewe bure.
Ilipotimu mwaka 2001, serikali ilipokea hayo mawazo na kuanza kutekeleza licha ya kuwa Ilani ya CCM ilikuwa haisemi kwamba watoto wasome bure na mara moja ikafuta UPE, ikapunguza ada na sasa taifa libeba mzigo wa gharama za wanafunzi.
Badala ya mzazi mmoja kuchangia, wanachangishwa wanajamii kwa kuchangia ujenzi wa madarasa.
Sasa huu ni utajirisho uliotokana na vyama vingi. Chama makini kinapaswa kuchukua sera za vyama vingine na si chama tawala tu ndiyo kichukue sera nzuri, la hasha, hata vyama ambavyo havijashika dola.
Asilimia 95 ya Watanzania wanaishi chini ya dola moja na hizi ni takwimu za serikali. Sasa taifa linapokuwa na idadi hiyo ya maskini kisha unawawekea kodi nyingi, hatuoni kwamba anakandamizwa mwananchi hapo?
Sasa kwa upande wa ilani za vyama vya upinzani, vilipunguza kodi za kichwa, kodi za usumbufu katika Jimbo la Hai, Karatu, Bariadi Mashariki na Kigoma, majimbo haya yanaongozwa na wabunge wa vyama vya upinzani.
Hata hivyo Julai 2002, serikali ilitangaza rasmi kufuta kodi zote za kichwa na usumbufu.
Hivyo hapa utabaini kwamba wapinzani baada ya kupunguza kodi hizo, serikali ikazifuta kabisa kwa hiyo, bila kuwepo ushindani katika hili la kodi serikali isingezifuta.
Hata hivyo, dhana ya vyama kuingia Ikulu katika utendaji, hili si muhimu kwa wananchi, mwananchi anachoangalia atapata faida gani. Na kitu kitakachomwondoa madarakani aliyepo madarakani, ni jinsi atakavyotekeleza yale aliyoyaahidi.
Sasa utekelezaji ni yale aliyobuni kiongozi anayeongoza na sera na ilani ya chama chake.
Sura ya pili ya mfumo huu, ukichukulia miaka 40 iliyopita iliyokuwa chini ya mfumo wa chama kimoja uhuru wa mawazo uliminywa kwa kiwango kikubwa.
Taifa lilitawaliwa na hofu kubwa hadi kwenye mfumo wa vyama vingi ulipoanza. Leo hii Watanzania tunaweza kutembea kifua mbele kwamba kwa kiasi kikubwa hofu imeondoka.
Lakini kwanini imeondoka? Imeondoka kwa sababu sisi wanachama wa vyama vingi hatuogopi, tunawatangulia wananchi katika kuonyesha njia kuondoa hofu.
Na baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wamefunguliwa kesi nyingi za kubambikizwa.
Hadi vituo vya polisi, mahakama vimekuwa sebule za nyumba za viongozi wa vyama vya upinzani.
Watanzania watakumbuka Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo katika kampeni yeye na wafuasi wake walipigwa mabomu na marungu na kisha kuangukia kwenye mitaro kwa ajili ya kufanya maandamano na mkutano wa amani.
Sasa leo hii hayo yote yatabaki kuwa ni historia kwa kuwa hivi sasa tupo huru kufanya mikutano ya hadhara kwa kutoa taarifa tu kwa polisi, si kuomba tena kibali kwa Mkuu wa Wilaya yeyote na polisi anawajibika kutoa ulinzi kwa sababu wapinzani na wafuasi wa vyama vyao hivyo ni sehemu ya jamii.
Hakika ni mabadiliko makubwa sana na mtu atakayebeza vyama vya upinzani havijaleta mabadiliko tangu vianzishwe, basi mtu huyo atakuwa ni hayawani.
Nenda kwenye utawala bora, watendaji wa vijiji na wa kata enzi hizo waligeuka miungu watu, wananchi walipigwa kwa kukosa fedha za kuchangia mbio za Mwenge, wakaporwa mali zao na viongozi hao.
Hivi ninavyosema, manyanyaso hayo yamepungua, hasa jimbo ninaloliongoza la Karatu, na sehemu nyingine kama Bariadi Mashariki, Tarime na Kigoma.
Katika miaka hiyo ya nyuma, watendaji wa vijiji walikuwa wanakwenda kwa wanavijiji wanataka ng’ombe kinguvu na mwanakijiji akikataa kutoa anabambikiwa kesi za mauaji ambazo hazina dhamana. Kwa sababu upinzani umeimarisha utawala bora, watu hawanyamazi wanaongea yanayowakera, kwa hiyo haya nayo ni mabadiliko ya msingi.
Uhuru wa magazeti baada ya mfumo wa vyama vingi vya siasa kuanzishwa umepanuka, leo magazeti, redio na televisheni ni nyingi sana.
Zamani tulikuwa tunasikiliza habari zinazohusu nchi yetu kupitia BBC ya Uingereza na Deutschewelle ya Ujerumani.
Sisi kama CHADEMA tupo mstari wa mbele tangu kuanzishwa mfumo huu, hasa uchaguzi wa mwaka 1995, baada ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi, chama chetu kiliingia bungeni na kutumia nafasi yetu nje ya Bunge.
Kazi tuliyoifanya, matokeo yake CHADEMA ilikubalika kwa wananchi na hatimaye kupata halmashauri tatu za Hai, Karatu na Kigoma. Na katika maeneo hayo, kulifanya CCM kuwa chama cha upinzani jambo ambalo ni mabadiliko kama ilivyokuwa miaka 40 iliyopita ya enzi ya mfumo wa chama kimoja.
Kazi ya maendeleo iliyofanyika Karatu, wananchi walikichagua tena CHADEMA kwa sababu kilileta maendeleo.
Mwaka 2000 Karatu ilikuwa na sekondari moja iliyokuwa imejengwa kwa nguvu za wananchi.
“Leo Karatu inakamilisha sekondari 22… wakati Serikali ya CCM inazungumzia ujenzi wa sekondari katika kata, chama chetu Karatu kimeishamaliza ujenzi wa sekondari katika kila kata,” anasema.
Wakati leo serikali inazungumzia ujenzi wa zahanati kwenye kata, mpango ambao haujaanza, Karatu mwaka 2001 imetekeleza ujenzi wa zahanati katika vijiiji kwa mujibu wa sera ya chama chetu.
Kimsingi serikali tumeionyesha njia katika mambo mengi na inatufuata. Ndiyo manufaa ya ushindani na mfumo wa vyama vingi.
Vivyo hivyo vjiiji vya Karatu karibu vyote vinapata mradi wa maji na kimsingi si kwa mkono wa serikali na isipokuwa vijiji 10 kati ya 45 ndani ya jimbo hilo vinapata maji toka mradi wa Benki ya Dunia (WB).
Nasisitiza haya ni matokeo ya kushindanisha, Karatu haisubiri serikali, tunatafuta kwa njia zetu na ndiyo maana tangu nimeingia bungeni sijawai kuiomba serikali inijengee zahanati wala shule, ila serikali kuu inaposaidia pale ni jukumu lake.
Leo hii mbunge anasimama analialia na kuomba serikali imjengee shule, anapewa jibu na wizara husika arudi kwenye halmashauri yake jambo ambalo ni tusi, kana kwamba mbunge amekurupuka kutoa ombi hilo bila kupitia au kuwasiliana na halmashauri yake.
Sasa kulialia huko hakuwezi kutokea kwa mbunge toka kambi ya upinzani, kwa sababu anajua kabisa anachokitaka kwa serikali.
Ni wajibu wa Serikali Kuu kutekeleza mahitaji ya wananchi wa jimbo husika kwa kuwa wananchi hao ni sehemu ya walipa kodi wa nchi hii.
Na hali ya kulialia ufanywa na wabunge wengi wa CCM kutokana na mfumo wa chama chao ulivyo.

0755 312 859
katabazihappy@yahoo.com
www.katabazihappy.blogspot.com
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima,Jumatano Julai 18,2007

Tukubali, si kila mtu anafaa kuwa kiongozi



Na Happiness Katabazi

KWA muda mrefu miongoni mwa wasomi na wananchi wa kawaida wamekuwa na mawazo tofauti kuhusu viongozi wanapatikanaje na ni hasa anastahili kuwa kiongozi.

Wapo wanaoamini kwamba uongozi ni karama au kipaji anachozaliwa nacho mtu, lakini kuna wengine wanaamini mtu anaweza kufundishwa kuwa kiongozi.

Kwa upande mwingine wapo wanaoamini kwamba akiwa na sifa za kuzaliwa na akapewa mafunzo ya uongozi huyo ndiye kiongozi anayefaa.
Lakini wote hawa hikubaliana jambo moja kwamba sikila mtu hata asiyekuwa na sifa anaweza kuwa kiongozi. Kimsingi kiongozi lazima awe na sifa zinastahili ikiwa ni pamoja na uelewa wa mambo, maono, awe ni mfano bora kwa wanaowaongoza na asiyetanguliza maslahi yake binafsi kabla ya awali anaowaongoza na kadhalika.

Dunia imebahatika kupata viongozi wenye sifa za namna hii na mifano hao viongozi si ya kutafuta kwa maana ni wengi. Kule Afrika Kusini, kulikuwa na Nelson Mandela, alikuwa na uelewa wa mambo na msomi wa hali ya juu alitanguliza maslahi ya watu wa taifa lake weupe kwa weusi hata akafungwa gerezani miaka 27 kwa sababu hiyo.

Waliopata fursa ya kuisoma hotuba yake aliyoitoa mwaka 1964 kabla ya kuingizwa gerezani alisema hivi. :” My life time I have dedicated my self to this struggle of the Afrivan people. There fought again in black domination, I have ideal of decratic and free society in which al persons live together in hormony and with equal opputunities.
“It is an ideal which hope to live for and achive.But if I needs be, it is an ideal for which I am prepares to die.” mwisho wa nukuu.
Tunaweza kuchukua mfano wa Alexander The Great, aliyeishi kati ya mwaka 356-323, ambaye wakati fulani akiwa kwenye mapambano na vikosi vyake alikataa kunywa maji kidogo yaliyokuwepo kwa sababu yasingewatosha yeye na na askari wake na akaamuru vikosi visonge mbele katika mstari wa mapambano na askari wake walimtii baada ya kuona ana moyo wa kutanguliza maslahi ya watu wake badala ya maslahi yake binafsi.
Sasa tukirejea Tanzania tunaweza kumtaja Baba wa Taifa Julius Nyerere, ambaye aliipenda watu na taifa lake na hata muda mfupi ya kuaga dunia alitamka wazi atawaombea wananchi wa taifa hili kwa mwenyezi mungu.

Vile vile Nyerere aliwahi kusema Ikulu ni mahali patakatifu na pana mzigo mzito wa kuwatumikia wananchi waliona matatizo mbalimbali kama umaskini na kadhalika.

Nyerere alikuwa msomi aliyebobea na mwenye shahada kadhaa za vyuo vikuu, mwenye maono na mwenye msimamo dhabiti katika yale aliyoyaamini. Kiongozi huyu aliyeweza kuibua viongozi wengine wenye sifa kama za kwake na pengine ni za kipekee mathalani marehemu Moringe Sokoine, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa nchi hii.

Mwalimu alifikia hatua ya kuwafunza watu uongozi akijua kwamba anatengeneza uongozi wa baadaye wa taifa lake kwa bahati wanafunzi wake wengi (kwa leo sitawataja ila wanajijua), wamesaliti mafunzo aliyowapa. Taifa letu la Tanzania lilipata bahati kubwa wakati wa uongozi wa Nyerere, viongozi waliheshimika ndani na nje ya nchi.

Waliheshimika kwa sababu walijiheshimu, walifuata maadili, walikuwa na moyo wazalendo na kutanguliza maslahi ya taifa mbele na hawakuwa wabinafsi. Viongozi hawa walipokuwa wakitamka jambo au kutoa maelekezo kwa watendakazi chini yao, wananchi kwa ujumla walisikilizwa na maelekezo yalikuwa yakitekelezwa bila kupuuzwa.

Leo hii viongozi wetu wanatoa maelekezo wanaishiwa kukosolewa na wananchi na watalaamu mbalimbali.

Enzi hizo lilipotangazwa Azimio la Arusha, Musoma na Nyerere taifa zima lilizima na kuitikia wito wa kiongozi muda mfupi na utekelezaji ulioneka hadharani.

Lakini kama alivyoimba mwanamuziki maarufu wa muziki wa kizazi kipya Lady J Dee, ‘Siku hazigandi’, enzi za uongozi na viongozi walio na uwezo wa kutupeleka kule kunakostahili hivi leo zinaoneka kama zimetoweka.
Leo hii sifa na vigezo vya mtu kuchaguliwa kuwa kiongozi si tena zile sifa njema, taifa hili sasa linashuhudia watu wakipata uongozi kwa sababu ya mahusiano yao na watu fulani wenye sauti katika jamii.

Mifano si ya kutafuta viongozi wetu wa ngazi ya kitaifa, mikoa, wilaya hata kata na wataasisi mbalimbali wametumia mgongo wa ‘uana mtandao’ kukalia viti vya uongozi walivyonavyo sasa.

Wengine wana kuwa viongozi kwa sababu hapo zamani au hata sasa wana uhusiano wa kimapenzi na wenye mamlaka ya kuteua. Kwa upande mwingine wapo viongozi ambao madaraka yao yametokana na undugu na kiongozi fulani mkubwa, wengine kwa kisingizio cha kufuata nyayo za wazazi wao, waume zao au wake zao.

Kadhalika wapo waliopewa uongozi kwa sababu sifa za kung’ara katika sanaa za maonyesho mathalani uimbaji kwaya, maigizo, mashairi, mipasho na au kwa sifa ya kupiga porojo na kuwa bingwa wa fitna.

Wengine wameteuliwa, kuchaguliwa kwa sababu ya kutoa michango mikubwa katika misiba, nyumba za ibada, kweye vyama vya siasa hususani chama tawala hata hakuna aliye na uhakika kama mapesa hayo wanayochangia hayatokani na baishara za haramu ya dawa za kulevya na hujuma zingine.

Maadamu hizi ndizo zimekuwa ni kisasa za kupata uongozi katika taifa letu hii leo tunashuhudia uongozi uliolegalega kwa namna ambayo haijawahi kutokea katika historia ya nchi yetu.

Leo hii viongozi wetu hawasemi kitu kikasikilizwa na watendaji waliopo chini yao wala kikatekelezwa na wananchi ipasavyo. Viongozi wengi wanaonekana kupwaya katika nafasi zao, kwani wengi wanadaiwa hawana uwezo kuwashawishi utendaji kazi na wao wenyewe hawaonekani kumudu majukumu yao.

Hali hiyo inaipa taifa letu hasara za siku hadi siku maana tunalazimika kuingia gharama zisizokoma za kuwakumbusha na kuwafundisha viongozi waandamizi majukumu yao.
Cha kustaabisha zaidi hata viongozi wakuu wa nchi hawaonekani kuwa na mvuto tena wa kusikilizwa na kupata utii unaostahili kutoka kwa wananchi.
Hayo yote ni kwa sababu ya viongozi wetu kukosa sifa machoni pa jamii na katika viongozi wengi tulionao si viongozi wenye uelewa mpana wa mambo, maono, uzalendo na maadili.

Katika hali hii ni dhahiri taifa linakoelekea ni kubaya sana kama vile ilivyo meli baharini inapokosa nahodha mahiri itapoteza dira na mwelekeo kama alivyowahi kusema aliyekuwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba, siku chache kabla ya kutoweka ghafla bin vuu duniani ambalo alisema “CCM imepoteza dira”.

Ni kama vile mashirika na makampuni ya umma yalivyokosa dira na mwelekeo hadi serikali ikaamua kubinafsisha kwa wageni. Kwa bahati mbaya hatuwezi kulibinafsisha taifa japo zipo dalili za kutuletea uchuro huo.
Tutajisikiaje watanzania, viongozi wa taifa hili watakuwa ni wageni na wafanya maamuzi muhimu wa nchi hii watakuwa si wazawa tena bali wageni?

Endapo tutaendelea kuwa na viongozi wanaopwaya kiasi hiki, taifa letu litasahau habari ya kutokomeza umaskini na kusonga mbele kimaendeleo sana sana tutapiga hatua kurudi nyuma siku hadi hadi siku.

Lakini hatima ya nchi hii katika suala la uongozi lipo mikononi mwa wananchi,wananchi ndiyo tunatakiwa tusimame sasa na kusema uongozi usio na sifa sasa basi.

Tufike mahali ambapo hatutamchagua kamwe kiongozi mbinafsi, fisadi, mlaghai, mbumbumbu, asiye na dira wa mwelekeo eti kwasababu tu ana uwezo wa kuwapatia wapiga kura sukaru kilo moja, doti za kanga, kapelo, fulana na vijisenti.

Tena sasa hivi imeibuka mchezo wa baadhi ya watu wenye fedha zao utoa fedha kidogo kwa wanamuziki wa bendi za dansi hapa nchi, ma DJ wa redio mbalimbali kuwarusha hewani, ili majina yao yazoeleke mbele ya jamii na kujipatia umaarufu wa chee, ili wakati wa uchaguzi waweze kutumia umaarufu huo kugombea nafasi za uongozi na kweli wanafanikiwa, Tuwakatae kwa nguvu zote viongozi wa aina .

Tufike mahala wananchi tumkatae kiongozi yoyote atakayeteuliwa ati kwa sababu ni mpenzi, ndugu au swahiba wa karibu wa anayemteua.

Kama wananchi hatutajali, tukumbuke kuwa dereva asiye na sifa za kuwa dereva akiendelea kupewa usukuni siku atakaposababisha ajali likawa janga la kitaifa, tutakaopoteza uhai ni sisi wananchi na dereva (kiongozi) huyo atatokomea kusikojulikana atakimbilia kule alikohifadhi fedha ambazo yeye na wenzake waliuibia umma.

Nasi tutabaki kuoza katika makaburi ya upweke ilhali vizazi vyetu vya baadaye vikaendelea kuteseka katika ufukara, dhiki kuu na aibu ya kutawaliwa na wageni kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.

Hatuna budi kusimama na kuwakemea sasa viongozi wanaotaka kuturejesha katika enzi za utawala wa Kifalme ambapo uongozi uliaminiwa upo kwenye damu na ukoo au nasaba ya mhusika badala ya sifa zinazostahili.

Wakati umefika kila aliyempiga kura asiliangamize taifa kwa kumchagua mtu eti ni kwa sababu ni mtoto au mjukuu wa fulani. Wakati umefika viongozi wote mliochaguliwa kwa mizengwe kwa namna isiyostahili muone haja ya kujiuzulu na wa wananchi tutawaheshimu kwa kitendo hicho cha kiungwana.

Ni kweli jamii za wanadamu zinahitaji viongozi na viongozi hao lazima wawe watu. Hivyo ingawa viongozi wote ni watu lakini kila si kila mtu anafaa kuwa kiongozi.

Yule ambaye hawawezi kufikiri kwamba jamii anayokusudia kuiongoza atafanyia nini, bali anafikiri jamii imfanyie nini hatufai. Yule ambaye yupo tayari kuuza mwili wake ili apate nafasi ya uongozi hatufai. Yule ambaye yupo tayari kutoa na kupokea rushwa ili apate uongozi hatufai.

Yule ambaye anaghushi vyeti na kujipachika shahada za udaktari wa Falsafa (PhD) hatufai. Hakika Watanzania tumechoka kulaghaiwa na vyeo vya kitaaluma ilhali uongozi wenu kiutendaji ni sawa tu na mtu aliyeishia darasa la pili, tena katika shule isiyokuwa na walimu wala viti,vitabu na chaki.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu inusuru Tanzania

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili Uk.10. Julai 8,2007

Profesa Chachage:Mbegu itakayoota kesho



Na Happiness Katabazi

KWA binadamu wanaozaliwa na mwanamke, wakaishi, wakafanya mambo yao, wakifa inaleta kihoro na msiba kwa watu wengi.

Lakini wapo wengine ambao utamani kuamini walizaliwa na mwanamke wakaishi katika jamii ya binadamu wakifa japo si mila njema kushangilia kifo, watu ukaa na kusema afadhali shetani kachukua mtu wake. Labda kila binadamu upenda kujua lipi kati ya haya mawili yatatokea siku ya kifo chake.

Na Julai 12 mwaka jana, katika Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, walikusanyika watu wa matabaka yote, wenye hadhi, makabila na jinsia zote wakiongozwa na Rais Jakaya Kikwete, walikuja kutoa heshima za mwisho kwa msomi.

Ni nani huyo? Si mwingine ni hayati Profesa Chachage Chachage (51).Chachage ni nani? Alifanya nini hata makundi hayo yakaitwa na kifo chake? Hakuna msomi mwingine ndani ya nchi hii ambaye kifo chake kilivuta wingi wa watu kama hawa.

Nilimfahamu Profesa Chachage. Naweza nikasema mimi nilikuwa ni mwandishi wa mwisho kuzungumza naye kuhusu fikra zake wakati alipokaribia kuhitimisha safari yake hapa duniani.

Ilikuwa ni Jumamosi, siku moja kabla ya kufa kwake, kiasi cha saa 4:30 hivi usiku nikiwa sebuleni nyumbani kwetu Sinza ‘C’. Nilipatwa na mshawasha wa kuzungumza kwa njia ya simu yangu ya mkononi na Profesa Chachage, ambaye alikuwa ni miongoni mwa vyanzo vyangu vya habari nyeti.

Ambaye kabla ya kukumbwa na mauti alikuwa akiniambia ataki katu katu kuitwa mwanaharakati, akitaka aitwe Mwanamapinduzi, kwa maelezo kwamba wanaharakati wengi ni wanafki na wasanii. Na kweli nikazoea kumwita jina hilo.

Kwa nini nilipata mshawasha wa kuzungumza naye siku hiyo? Mezani kwake, kulikuwa na maswali kadhaa ambayo nilikuwa nimemwandikia, nikitaka kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali kwa ajili ya habari na makala, ambavyo nilitarajia kuchapisha katika gazeti.

Nilizungumza naye kwa takriban dakika tano, kabla ya kuniambia kwamba muda huo alikuwa Kibaha, mkoani Pwani, kikazi. Baada ya kuniambia yuko Kibaha , nilipata hamu ya kutaka kujua kazi anayoifanya huko.

Hata hivyo, hakutaka kuweka wazi juu ya shughuli iliyokuwa imempeleka huko. Hata hivyo kabla ya kumaliza mazungumzo yetu, alinidokeza kwamba katika safari hiyo alikuwa ameongozana na rafiki yake mkubwa, na ambaye pia alikuwa mtu muhimu kwangu katika kazi yangu ya uandishi wa habari, Dk. Abuu Mvungi.

Bila hiana, nilimwomba Profesa Chachage kunipatia simu yake ili naye nimsalimie. Alifanya hivyo, tukaanza kutupiana ‘madongo’ ya utani kama ilivyokuwa ada yetu pindi tunapokutana katika mihangaiko mbalimbali.

Baada ya kumalizana na Dk. Mvungi, Profesa Chachage alirudisha simu yake katika masikio yake, huku nikiendelea kumdadisi ni nini hasa kilichokuwa kimewafanya wanamapinduzi hao wawe Kibaha muda huo.

“Happiness, Jumanne nitakuwa ofisini. Usijali, njoo nakuahidi, kisha nitajibu maswali yako ambayo uliniletea wiki tatu zilizopita, usijali, ” aliserma.

Hiyo ndiyo ilikuwa kauli ya mwisho ya Profesa Chachage.
Wapo waliomfahamu marehemu kama mwandishi wa vitabu, mwanafalsafa na mpenzi wa muziku wa Bongo Flavor.

Mimi nilimfahamu kama mtu mwenye fikra za kimapinduzi, mwandishi wa vitabu na mpigania haki na masilahi ya umma, mkweli.
Leo Watanzania wa kada mbalimbali hususan jumuiya ya wasomi, tunaadhimisha mwaka mmoja tangu kufariki kwake, Professa Chachage Seith Chachage.

Professa Chachage alifariki dunia ghafla Julai 9 mwaka jana, saa 5:00 usiku, akiwa katika ukumbi wa mikutano Kibaha, ambako alikuwa ameongozana na jopo la wasomi wanne waliopewa kazi mahususi, ya kuandika ripoti kuhusu hali ya Muungano na migogoro ya kisiasa Zanzibar na namna serikali inavyoweza kuitatua.

Kazi hiyo walikuwa wametumwa na serikali zote mbili, ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Kabla ya kifo chake, habari zilisema Profesa Chachage alianza kulalamika kuhusu hali ya joto iliyokuwa katika chumba hicho cha mikutano, ingawa inaelezwa kwamba wasomi wenzake hao walimwona kama anatania kutokana na ukweli kwamba chumba hicho kilikuwa na ubaridi unaotokana na viyoyozi vilivyomo ndani ya chumba hicho, na vyote vikiwa vinafanya kazi barabara kiasi cha baadhi ya waliokuwamo kuhisi baridi kali.

Katika malalamiko hayo, ilielezwa kwamba Professa Chachage alichukua chupa ya maji, baada ya kunywa maji, habari zinasema aliendelea kutokwa jasho jingi, hali iliyomfanya asimame kitini kwake, akijaribu kujikongoja ili atoke nje kupata upepo.

Hata hivyo, kabla hajafika nje, ghafla alianguka na kupoteza fahamu. Hapo ndipo wenzake walizinduka na kuanza kushika hiki na kile kwa nia ya kunusuru uhai wake.

Kama wasemavyo wahenga, ‘siku ya kufa nyani miti yote huteleza’.
Siku na muda ambao Mwenyezi Mungu amepanga kuchukua roho ya mja wake, binadamu hawezi kuukwepa.

Akiwa njiani akipelekwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha, alikata roho.
Huo ndio ukawa mwisho wa safari ya maisha yake duniani, Profesa Chachage, kipenzi si cha jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wanafunzi wa Idara ya Sosiolojia waliopo na waliopita.

Nikiri kwamba pamoja na kulisikia jina la Profesa Chachage tangu nikiwa katika Shule ya Msingi Mugabe, jijini Dar es Salaam, kwa mara ya kwanza nilishikana mikono na profesa huyo mwaka jana kabla ya kifo chake.

Ilikuwa Jumamosi moja, Januari mwaka jana, saa moja jioni, pale UDASA Club. Aliyenikutanisha ana kwa ana na bingwa huyu wa sosiolojia ni aliyekuwa Mkuu wa Kitivo cha Sheria wakati huo, Dk. Sengondo Mvungi.

Tangu siku hiyo, hadi kifo chake, Profesa Chachage na mimi, tuliishi kama chanda na pete.

Katika mambo ambayo sitayasahau, ni msimamo wake kuhusu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Uhandisi ndani ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo Rais Kikwete alikifungua mwaka jana.

Enzi ya uhai wake, alitaka kuwe na utaratibu mzuri unaolinda masilahi ya wasomi kwa maana kwamba wasomi walipwe vizuri ili waweze kuishi kutoka na utaalamu wao badala ya hali ilivyo hivi sasa, ambapo wasomi wanajikuta wakiwa wabangaiza mitaani, wakifanya biashara ya kuuza machungwa, mchicha au kufuga kuku, ng’ombe na nguruwe ili waweze kujikimu.

Kwa hiyo, ndiyo maana hayati Profesa Chachage alisimamia kidete suala la mishahara na masurufi ya wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Tunaweza kusema kwamba wasomi wa UDSM walimtambua kwa hilo na walimuunga mkono, na hadi sasa wameshapata awamu ya kwanza ya nyongeza ya mishahara waliyoahidiwa na serikali.

Kuhusu suala la wasomi kulitumikia taifa lao kizalendo, huo ndio ulikuwa msimamo wake kiitikadi kwamba katika kila taifa wasomi lazima wawe wana mageuzi wanaotetea haki za walio wengi.

Hilo hata yeye mwenyewe katika uhai wake hakuweza kulifanikisha, japo aliandika mengi akilipigania hilo. Hakulifanikisha kwa sababu linahitaji pawepo idadi ya kutosha ya wasomi wenye msimamo huo ili waweze kulitekeleza.

Hivi sasa wasomi walio wengi wanapendelea kujiunga ama na CCM, kuunga mkono sera zake, au kukaa kimya ili kutetea masilahi yao binafsi na kushibisha matumbo yao na familia zao.

Wasomi wengi hivi sasa wanadhalilisha taaluma zao kwa kuunga mkono au kutumika kubuni miradi ya kifisadi na ya kuuza nchi, na wanafahamika.

Nitaendelea kumkumbuka na kuheshimu mchango wa Profesa Chachage kwa vitendo, kwani nakumbuka katika uhai wake alijaribu kutetea nafasi ya vyuo vikuu kuhusu mfumo wa elimu.

Yeye alisimama kidete kupambana na mrengo wa kibwanyenye unaotaka kugeuza vyuo vikuu kuwa taasisi za kufanyia miradi ya kiuchumi.

Na katika hili, alipambana na katiba mpya ya chuo iliyokuwa ikipendekezwa na enzi za uongozi wa Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa Methew Luhanga, ambayo ingekigeuza chuo kuwa taasisi ya kibiashara badala ya wajibu wake wa kutoa elimu ya juu na kufanya utafiti.

Katika harakati zake hizo aliwaongoza na kuwashawishi wasomi katika chama chao cha (UDASA) na katika chama cha wafanyakazi wa (RAAWU) kupinga katiba hiyo.

Hata hivyo katiba mpya ya chuo hicho imepatikana baada ya yeye kufariki.

Wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walionyesha dhahiri kumkubali na kumuenzi mwanamapinduzi huyu kwa sababu walikubali kuanzisha Mfuko wa Profesa Chachage, kwakukatwa mishahara yao.

Wasomi wa UDSM wana haki ya kumuenzi marehemu Chachage, labda enzi za uhai wake alifahamika kwa watu wengi lakini mambo yalivyo, mwanamapinduzi huyu atapendwa zaidi na Watanzania baada ya kifo chake.

Yale aliyoyapigania na hayakupatikana katika uhai wake na wala Tanzania ya leo haitapa faida ya mchango wake.

Hata hivyo kesho watapatikana kina Profesa Chachage wengine watakao chukua kurunzi aliyoiwasha kuwaangazia Watanzania wa kizazi chao kuona njia ya kufika kwenye maendeleo.

Profesa Chachage, sasa marehemu ametoka wapi?
Alizaliwa Januari 8, mwaka 1955 katika Kijiji cha Mtwango, wilayani Njombe, Iringa.

Kwa asili, yeye ni kutoka kabila la Wabena, ambalo ni moja ya makabila makubwa mkoani humo, ukiacha Wahehe.

Si siri, marehemu alikuwa ni mwanamapinduzi wa kweli na asiye na woga katika kutetea haki na masilahi ya umma na itachukua muda mrefu kumpata msomi mwenye sifa kama za marehemu.

Pia kifo chake ni pigo kwa jumuiya ya wanachuo, duru za wasomi ndani na nje ya nchi.

Profesa Chachage, ambaye ameacha mjane na watoto wanne, kwa mara ya kwanza alitunukiwa shahada ya kwanza ya Sosiolojia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1982.

Baada ya ya kuhitimu, na kuwa miongoni mwa wanafunzi bora alipewa kazi ya kufundisha shuleni hapo akiwa kama Mkufunzi Msaidizi, kabla ya kuendelea na masomo ya shahada ya pili na ya uzamili chuoni hapo katika fani yake hiyo mwaka uliofuata.

Mwaka huo wa 2000, akiwa na cheo chake hicho cha Profesa Mshiriki, Chachage alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na akakabidhiwa dhamana ya kuongoza kitengo cha Utafiti na Uchapishaji cha chuo kikuu hicho hadi 2003.

Kuanzia mwaka 2003 hadi anafariki dunia, Profesa Chachage alikuwa ni Mkuu wa Kitivo cha Sosiolojia na pia Mwenyekiti wa UDASA.
Lakini pia, Profesa Chachage ameandika mada na vitabu kadhaa, ambavyo vitatumika katika vyuo vikuu na vyuo vingine vya elimu ya juu nchini.

Moja ya vitabu na mada zake zilizotia fora katika ulimwengu wa mazingira ya Tanzania, ni Makuadi wa soko huria, ambacho, pamoja na mambo mengine, Profesa Chachage anayaangalia madhira ya wakulima wa korosho wanayoyapata kutokana na sera mbovu za nchi, dhidi ya wanunuzi wa zao hilo.

Vitabu vingine ni pamoja na Honourable Teacher (Mheshimiwa Mwalimu), Dhima ya Fasihi na Sudi ya Yohana, ambavyo amevitunga katika mfumo wa hadithi. Pia vipo Fasihi na sanaa na uhusiano wake na Kiswahili, Kivuli na almasi za bandia.

Profesa Chachage, binafsi nakutakia mapumziko mema huko uliko. Najua utakutana na wana mapinduzi magwiji, kama Mwalimu Julius Nyerere, Kwame Nkrumah, Patrice Lumumba na wengine wengi.
Usisahau kuwaeleza mbinu mpya ya ukoloni unaolinyemelea Bara la Afrika.

Pia umweleze Mwalimu Nyerere kile chama chake alichokiasisi cha CCM, kimejaa makundi madogo na makubwa, lililoyafunika kwa sasa ni kundi la ‘wanamtandao’ na si tena chama cha wakulima na wafanyakazi, bali hivi sasa chama hicho ni cha wafanyabiasha na matajiri.

Aidha, umweleze kwamba makada wa chama chake wengi wao hawawezi kugombea nafasi za uongozi bila kupewa baraka na ‘sangoma’.

Pia hivi sasa ni nadra sana kuwa kiongozi kama si mwanamtandao, mpika majungu, mfitini na bingwa wa kutumia vyombo vya habari ili vikupambe.

Nilazima pia uwe hodari na mahiri wa kujikomba kwa wakubwa na kuwasifia hata kama utendaji wao ni mbovu.Tafadhari usisahau kumweleza haya.

Umweleze ile migomo ya vyuo vikuu inaendelea kama kawaida na ubinafsishaji na uingiaji wa mikataba yenye utata imeshika kasi.

Pia umweleze hivi sasa tofauti kati ya maskini na wenye nacho, ambayo alikuwa akiipinga kila siku hivi sasa imeanza kuota mizizi.

Najua umekutana na wasomi wenzako kutoka pande nne za dunia pamoja na walalahoi kadhaa waliopoteza maisha kutokana na taabu walizozipata katika harakati zao za kutetea mazingira mazuri na bora ya elimu, ambayo sasa yameanza kuharibiwa na mitazamo pamoja na sera mbovu za wanasiasa na watunga sheria.

Mwisho kabisa, pamoja na pengo kubwa uliloliacha kwa Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na familia yako, lakini kumbuka kwamba wale marafiki zako tuliokuwa tukikata karibu usiku mzima kutakiana heri kwa kugongeana bilauri, nasi umetuacha taabani.

Mimi nitaendelea kukuenzi daima kwa kuandika ukweli na kukemea maovu kama ulivyokuwa ukiniusia kila mara.

Naahidi kuwa jasiri kwa kusema na kuandika ukweli katika kutetea masilahi ya wanyonge wa nchi yetu.

Profesa Chachage ambaye alizikwa kijijini kwake Mtwango, Njombe, mkoani Iringa, atakumbukwa pia na wale aliokuwa akichangia nao katika ‘upigaji pafu’ wa sigara.

Hao nao wataendelea kukulia na kuuenzi mchango wako, umewaacha bila mlezi wala mshauri. Watakukumbuka daima.

Mungu alikuumba na akakutwaa. Jina la Bwana lihimidiwe na aipumzishe roho yako mahala pema peponi.

Amina.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu Julai 9,2007