Kumbe Wanamageuzi ni wakombozi wa kweli wa taifa hili

Na Happiness Katabazi

WACHUNGUZI wa mambo ya siasa wanaoitazama Tanzania leo wataona kuwa mfumo wa Kidemokrasia unaojengeka na uchumi wa soko unaendelea kushamiri nchini ni mwendelezo wa sera za chama kimoja.

Mtizamo huo kwa hakika ni potofu kwakuwa sababu kubwa ya Tanzania kuondoka kwenye mfumo wa chama kimoja na kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi ni kuzorota kwa uchumi uliyokuwa unatawaliwa na sekta ya umma.

Harakati za wanamageuzi kudai demokrasia vya vyama vingi zilizaliwa katika mchakato huo.Baba wa Taifa Mwalimu Julias Nyerere, alikiri ukweli huo na kukishinikiza Chama Cha Mapinduzi(CCM), kiridhie mabadiliko ya vyama vingi kuliko kingoje kung’olewa madarakani kwa shari.

Kwa mantiki ya Mwalimu Nyerere, moja wapo ya majukumu makubwa ya wanamageuzi ni kukiweka chama tawala macho ili kisinzie wala kubweteka.

Tukitazama Ilani za vyama vya Mageuzi tutaona kwamba mengi mazuri tunayoshuhudia leo hapa nchini kwetu, ni matokea ya juhudi za wana mageuzi, wanamageuzi ndani ya vyama visivyo madarakani na wanamageuzi nje ya vyama hivyo wameibua hoja nyingi nzuri za kulisaidia taifa letu ambalo zimewazindua wana CCM kwenye usingizi mnono na kuanza kuzitekeleza.

Tatizo ni kwamba walipoanza harakati zao wanamageuzi miaka ya 1980, walionekana kuwa wapinzani wa serikali na chama tawala,wahuni, vichaa,waroho wa madaraka na maadui,wanaharamu.

Mara nyingi viongozi wa CCM walitumia na wanaendelea nguvu za dola kuwahujumu na kuwadhibiti na alitumia baadhi ya vyombo vya habari kuwapaka matope ili waonekane kuwa ni wenye njaa kali, wasiro na sera na ambao wataleta vita endapo watachaguliwa kuongoza taifa hili.

Sambamba na mtizamo huo, viongozi wa CCM walijaribu kutoelewa hoja za wanamageuzi kwa kuzibeza kwa kujitapa kuwa CCM ni namba moja.

Lakini tukitizama basi baadhi ya sera au mambo muhimu ambayo wanamageuzi wamelitetea taifa, wanamageuzi walipinga ubinafsishaji holela wa Mashirika ya Umma na kutuambia kwa taifa sio nchi ya kwanza kubinafsisha sekta ya umma, hivyo hapana haja ya kukurupuka kufanya ubinafsishaji bila kujali maslahi ya taifa letu.

Wanamageuzi waliona kuwa ingekuwa vyema taifa livute pumzi na kupanga ratiba ya ubinafsishaji itakayowapa wananchi kipaumbelea katika umilikaji wa sehemu kubwa ya sekta ya sekta inatakayobinafsishwa badala ya kukabidhili hatamu wageni.

Je! tungewasikiliza wanamageuzi, tungeshuhudia Benki ya Taifa ya Biashara(NBC) ingeuzwa kwa bei ya nazi sokoni?

Ebu tujiulize thamani ya Jengo la Millenium Tower ambalo limejengwa kwa bilioni 35, ni kubwa kuliko benki ya NBC iliyouzwa kwa bilioni 15?

Ebu tuangalie wanamageuzi kuhusu sekta ya madini, tukisoma sera na Ilani zaom wengi wao wanasema si halali wa Tanzania kuambulia mrahaba 3% kutokana na madini ya nchi wakati wageni wakiruhusiwa kuondoka na 97%.

Duniani kote utajiri wa nchi ni rasilimali zake za asili.Waarabu ni matajiri kwasababu wana mafuta,Makaburu wa Afrika Kusini ni matajari kwasababu wana dhahabu.

Iweje Tanzania ni nchi ya tatu kuzalisha dhahabu Barani Afrika na ni nchi pekee duniani kuwa na madini ya Tanzanite, iitwe nchi maskini?

Tunachokiona hapa ni kwamba CCM haijui itendalo,ingekuwa vyema chama hicho na serikali yake kingekuwa kinasikiliza wanamageuzi katika suala hilo.

Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete, amekiri upungufu wa sera ya madini na mikataba yake na ameaidi serikali yake itatazama upya mikataba hiyo nakuongeza kuwa serikali haitaruhusu kusainiwa mikatana mipya ya madini hadi hiyo iliyopo ipitiwe.

Lakini cha ajabu ambacho watanzania wamekishuhudia wiki iliyopita Mbunge wa Kigoma Kaskazi Kabwe Zitto, amewafungua maskio wananchi kupitia bunge, kuwa Waziri wa Nishati na Madini Nazir Karamagi, amesaini mkataba mpya licha mikataba ya zamani haijamalizwa kupitiwa.Wamesaini mkataba wa Buzwagi ,nchini London, Uingereza na kuliomba bunge liunde tume,na alichoambulia sote tunajua kwamba hoja yake ilitupiliwa mbali na kushughulikiwa kikamilifu na wabunge wa CCM na kusimamishwa kuudhulia vikao vya bunge hadi Januari mwaka 2008.

Ila kinachofurahisha ni kwamba Rais Kikwete, mwenyewe ni mhusika wa karibu na sera hizo na mikataba hiyo kwakuwa alikuwa Waziri wa Nishati na Madini,Waziri wa Mambo na nje na Kada mahiri wa chama tawala.

Suala ni kwamba ahadi za Rais Kikwete zitatekelezwa lini?Je ataruhusu serikali yake iendelee kuingia mikataba mipya na makampuni za madini kabla mikataba ya awali atujaalifiwa kama imeishamalizwa kupitiwa?

Kwahiyo tunasema wanamageuzi waendelee kuvuta kamba kwani hatujui nani ni nani katika mikataba ya madini bila shaka harakati na kelele za wana mageuzi zitalikomboa taifa.

Tukiangalia suala la umaskini, sera ya CCM ilikuwa ni ujamaa na kujitegema, sera hizo zilishindwa na wenyewe CCM walizitumbukiza baharini kule Zanzibar wakati Baba wa Taifa, aking’ali hai.

Sera za uchumi wa soko, ni sera za wanamageuzi sera hizo sasa zimetekwa na ccm ndizo rasmi sera zake.

Lakini tofauti ya wenye sera na waigaji wa sera ni kubwa,ccm imkumbayia sera za soko huria za Shirika la Fedha Duniani.

Hivyo CCM inazungumzia Mpango wa Taifa wa Kupunguza Umaskini ifikapo mwaka 2025(MKUKUTA).Wanamageuzi kwa upande wao wanazungumzia uchumi wa soko unaoendeshwa na kutawaliwa na wazawa hivyo kwa upande wao, suala si kupunguza umaskini bali ni kufuta umaskini haraka iwezekano.

Kwahiyo wanamageuzi kwa mujibu wa Ilani zao wanatoa kipaumbele katika kuwawezesha wazawa kwa makusudi.
Suala linajitokeza sasa ni kama ni sera hipi kati ya hizi mbili zitalikomboa taifa.

Tukitazama mifano hai ya nchi za Bara la Asia kama vile Marasia,Taiwan,Korea Kusini tunaona kwamba wenzetu wameamua kufuta umaskini badala ya kupunguza makali yake.

Tunatamani sana kama wanamageuzi wangevuta kamba na kushinikiza taifa likubali kufuta umaskini badala ya kupunguza.
Kinachoshangaza ni taifa kukubali kuuza taasisi za fedha.

Je ni busara gani kuuza benki ya Taifa ya Biashara kwa wageni na wakati huo huo kuanza kampeni ya kuanzisha Benki ya Wananchi?

Je ni busara gani kuanzisha Benki ya NMB kwa juhudi kubwa ya wananchi wenyewe bila mtaji wowote na mara ilipoanza kufanikiwa ikauzwa kwa wageni?

Je! Ni busara gani taifa kupoteza muda wake kuimiza na kuanzisha SACCOS wakati linakataa kuendesha benki ya Microfinance?Aina hii ya uchumi wa kundunduliza kamwe haiwezi kufuta umaskini.

Kwahiyo kilio cha wanamageuzi kutetea benki ya Microfinance isiuzwe ni kilio cha taifa na ndiyo mkombozi wa taifa kiuchumi.

Wanamageuzi walipambana kweli kweli na sera ya elimu ya ccm na serikali yake ,waheshimiwa wa ccm,waliamua kufuta masomo ya biashara,kilimo,uraia,michezo na wakaamua kuunganisha somoa Kemia na Fizikia bila mantiki yoyote.

Mantiki ya kufuta masomo hayo ni kuzalisha taifa la mambumbubu wasio na uwezo wa kukabaliana na utandawazi ili wakoloni waje kutatawala tena.

Hata taasisi zisizoza kiserikali zizilizo jaribu kupambana na aina hiyo ya elimu ,mfano,Haki Elimu, zilijikuta zikitishiwa kufungiwa.

Sera za mageuzi sio tu zilidai kurejeshwa kwa mtaala wa zamani ila pia zilidai kuboresga mtaala huo ili kumudu changamoto za utandawazi.

Wanamageuzi pia wamekuwa wakihoji wingi wa viajan wanaomaliza darasa la saba bila kupata nafasi ya kwenda sekondari.Ilani nyingi za vyama vya mageuzi zinaonyesha kwamba elimu ya msingi kwa mtanzania ingefaa ipandishwe kitado cha nne.

Nakiri mantiki na ubora wa nchi hii,kinachofurahisha ni kwamba tayari serikali ya ccm imekiri ubora wa hoja hiyo hii na kuanza kuitekeleza japo kwa 50%.
Tatizo ni kwamba CCM imekurupuka kuitekeleza hoja hii bila maandalizi ya kutosha.

Ipo mifano mingi inayoonyesha kwamba ccm sasa imeachana na sera zake na Ilani yake na inatekeleza kinyemelea sera na ilani za vyama vya mageuzi, tunaisifu CCM kwakuwa wepesi kukiri na kuiga kwani hiyo ina maana na faida ya kuwa na Vyama Vingi vya Siasa hapa nchini.

Tusibaguane kwa sera wala itikadi ila tujali maslahi ya taifa letu.Wazo bora la wanamageuzi,wanaharakati,wataalam,wanyonge na sisi wanahabari lichukuliwe na kufanyiwa kazi kwa umakini.

Mwandishi wa makala hii anapatika kwa simu namba 0755 312 859 na barua pepe katabazihappy@yahoo.com na tovuti. www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili,Agosti 26,2007

Hoja ya Zitto Kabwe:Bunge limesigina demokrasia!

Na Happiness Katabazi

JUMANNE ya wiki hii, tulishuhudia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, likimwadhibu Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Zuberi Kabwe (CHADEMA), kwa kumsimamisha kuhudhuria vikao vya Bunge hadi Januari 2008 baada ya kumtia hatiani na kosa la kulidanganya Bunge.

Hoja binafsi iliyowasilishwa na mbunge huyo kijana kuliko wote kutoka katika majimbo ya uchaguzi, ya kuliomba Bunge liunde kamati teule kuchunguza uharaka uliosababisha Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Mustafa Karamagi, kusaini mkataba wa madini nje ya nchi, siku hiyo iligeuzwa na wabunge wa CCM na kuwa jambia kali kwa mbunge huyo kijana machachari, ambaye anajiamini na kusimamia yale anayoyaamini.

Katika hoja yake, Zitto alihoji sababu za Karamagi kusaini mkataba mpya wa madini wa mgodi huo London, Uingereza na kwa nini mkataba huo ulisainiwa wakati serikali ikiendelea kudurusu mikataba kama ilivyoagizwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Hoja ya Zitto kusimamishwa ubunge, ilijengwa na Mbunge wa Mchinga, Mudhihir Mudhihir na Bunge likalazimika kuongeza muda wake ili kutekeleza adhabu hiyo, ambayo Zitto mwenyewe alipotakiwa kujitetea alisema yuko tayari kwa lolote.
Awali Zitto wakati akiwasilisha hoja hiyo, alitaka kujua sababu za kuondolewa kwa kipengele katika sheria ya kodi ya mapato ya mwaka 1973 kuhusu asilimia 15 bila ya kibali cha Bunge.

Wapenzi wasomaji, tukumbuke sakata la Mbunge wa Mkuranga, Adam Kighoma Ali Malima na mfanyabiashara Reginald Abraham Mengi ambalo lilikuwa ni la kibinafsi na halikuwa na maslahi ya taifa, liliundiwa Kamati ya Bunge kuchunguza ukweli kwa sababu tu suala hilo lilisemwa bungeni na likaligharimu serikali zaidi ya sh milioni 100, ukweli ukabainika.

Tulitegemea Bunge lingemwadhibu aidha Mengi au Malima, lakini suala hilo liliishia kusemwa na Spika Samuel John Sitta kwamba, imetumika busara na mjadala ukafungwa.

Inakuwaje suala la Zitto Kabwe ambaye hoja yake ni ya msingi, ina maslahi kwa taifa, Bunge hilo hilo likamwadhibu, tena katika kipindi kifupi bila kuunda kamati ya kuchunguza wala kumpa nafasi ya kujitetea kwa sababu tu ya kutoa hoja bungeni?

Hata kama aliambiwa ajitetee wakati huohuo alipomaliza kutoa hoja, muda aliopewa haukutosha kwa yeye kujiandaa kutoa utetezi wake dhidi ya hoja ya Mudhihir, kwani kanuni za utoaji haki zinahitaji mtu kupewa mashitaka au tuhuma zake, ili azisome na kuzielewa, na hatimaye apewe muda wa kutosha kutoa majibu yake dhidi ya tuhuma hizo. Bila shaka hizi ni sheria za mwituni, za mbabe ndiye mwenye haki, ndizo zilizotumika.

Naamini Zitto alitumia uhuru wake wa kutoa maoni yake juu ya suala hilo kwa mujibu wa ibara ya 18 ya katiba inayohusu uhuru wa maoni na ibara ya 100 ya uhuru wa majadiliano bungeni kama ibara hizo zilivyoainishwa kwenye katiba ya nchi ya kuibua mambo yaliyokuwa yamejificha na yenye utata.

Kumwadhibu Zitto kwa hoja ya mbunge aliyetaka aadhibiwe, bila kuwa na kikao chochote cha kutoa maamuzi hayo kisheria, ni kukiuka kanuni za msingi za utoaji hoja.

Kwamba mtu aadhibiwe, asihukumiwe bila kupewa nafasi ya kujitetea na hilo Spika Sitta analijua, lakini kalipuuzia na kutengeneza kosa jipya linaloitwa 'kutoa hoja binafsi bungeni' ikipingwa mtoaji ana kosa anastahili adhabu na kila anayeshitaki na kushindwa kesi anastahili adhabu.

Mheshimiwa Sitta ni mwanasheria, tena ni wakili wa kujitegemea na aliyeahidi kuliendesha Bunge kwa ‘standards and speed’, na kwamba atawabana sana mawaziri watakaotoa majibu mepesi kwa maswali magumu.

Je, anataka Watanzania tuamini kwamba hafahamu kanuni za msingi za utoaji haki (rules of natural justice)? Je, anataka kuweka historia (precedent) kwamba mtu yeyote au wakili atakayeshitaki mahakamani na kushindwa kesi kwa hoja, ni muongo na anapaswa kwenda jela? Hata kidogo siamini kama hii ndiyo tafsiri ya sheria, naungana na Wakili wa kujitegemea, Sambwe Shitambala kwamba, ingekuwa hivyo, mawakili wote wanaoshindwa kesi kwa sasa wangekuwa ndani.

Mimi ninajiuliza, kuna ubaya gani kwa mtu kutoa hoja? (what’s wrong with putting up an argument?).

Ninaamini kwamba Spika anapokuwa anaendesha Bunge, yeye si wakili wala hakimu au jaji, hivyo basi maoni ya kina Mudhirhir kuwa Mhe. Zitto asimamishwe, hayawezi kuchukuliwa moja kwa moja kuwa ni uamuzi pasipo kuangalia ushahidi wa pande zote mbili, kwani hata Mungu mwenyewe katika bustani ya Eden hakuwaadhibu Adam na Eva bila kuwasikiliza, kila mmoja alipewa mashitaka yake akajitetea na mwishowe akapitisha adhabu.

Vivyo hivyo, wananchi, tulitegemea Bunge lingeunda kamati kuchunguza aliyoyasema Kabwe, kuona kama ni uongo ama kweli na baadaye kumwadhibu au kumwachia. Pia kitendo cha kumwadhibu Kabwe kinakwenda kinyume cha kanuni za haki za binadamu, zinazotaka usawa mbele ya sheria na kuondoa ubaguzi. Hivi inakuwaje kwa kosa hilohilo la kusema uongo, Malima hakuadhibiwa, lakini Zitto akaadhibiwa? Hata pale alipoambiwa amwombe msamaha Spika akakataa, na spika kujifanya kutumia busara kumaliza mgogoro?

Hivi tuseme kwamba kwa sababu Mhe. Malima hakuwa kambi ya upinzani ndiyo maana hakustahili adhabu hata ilipothibitika kuwa amedanganya? Ziko wapi standards and speed za Spika Sitta.

Zaidi ya hayo, wananchi tunajiuliza kuwa, hivi Bunge letu halina adhabu nyingine ya kuwapa wabunge zaidi ya hiyo ya kuwasimamisha kwa muda? Kanuni za Bunge toleo la mwaka 2004 zinaeleza wazi utaratibu utakaotumika pindi mbunge anapotuhumiwa kusema uongo na adhabu zake. Sasa ilikuwaje kumsimamisha Zitto bila kufuata utaratibu huo ambao Bunge limejiwekea lenyewe?

Je, Bunge halioni kwamba kwa kumsimamisha mbunge ni kuwaadhibu wananchi wasio na hatia, kwani matatizo yao na mapendekezo yao yatakosa uwakilishi? Poleni wananchi wa Kigoma, poleni Watanzania wenzangu, poleni vijana.

Hakika hii inatuonyesha kwamba wananchi tuna thamani wakati wa uchaguzi tu, na si baada ya hapo kwani bungeni anaguswa mbunge kama mbunge na si wananchi wake.

Imefika wakati sasa kwa Bunge kurekebisha kanuni zake ili kutofautisha adhabu zinazoweza kutolewa kwa mbunge kama mbunge kwa utovu wa nidhamu aliounyesha bungeni au uongo na adhabu ya mbunge na wananchi wake.

Hivi ni kweli Bunge limeshindwa kutofautisha maana ya uongo na maana ya kosa kwa maana ya ‘error’ au kupitiwa, au kuchanganya vitu viwili tofauti?

Kwa uelewa wangu mdogo, uongo ni hali ya kusema jambo unaloamini kuwa si la kweli au kusema jambo la kubuni kwa lengo la kuwaaminisha wengine ili kuwapotosha ‘knowingly misrepresenting facts’.

Lakini kuchanganya ni hali ya kutaja kitu kimoja kinachofanana na kingine kama vile ndiyo kile ulichokitaja ‘citing wrong provision’, ni vitu vya kawaida sana katika maisha ya binadamu. Tatizo hapa si nani mkweli nani mwongo, suala ni utaratibu mbovu usio wa kibinadamu uliotumika.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kwenye vyombo vya habari, Jumatano wiki hii, zilitueleza kwamba kitendo cha Zitto kuchanganya sheria ya madini, vipengele vya sheria ya kodi hali akiamini anayoyasema ya kweli, hiyo si tafsiri nyingine ya uongo, labda angetaja kitu ambacho hakipo kabisa katika ukweli na uhalisia wake.

Tatizo kubwa hapa lilikuwa ni kusainiwa haraka kwa mkataba; (a) nje ya nchi, (b) kwa kutofuata taratibu zilizowekwa, (c) kinyume cha kauli ya Rais Kikwete na aliyekuwa Waziri wa Nishati Dk. Ibrahim Msabaha, ambao waliwahi kusema kwamba serikali haitasaini mikataba mingine ya madini hadi mikataba ya madini iliyopo itakapomaliza kupitiwa, kauli ambazo hazijafutwa hadi leo, na hivyo tunaamini kauli hizo bado ni hai.

Ingekuwa ni busara kwa Bunge kuchunguza mambo hayo matatu kwa kuzingatia hoja zilizotolewa na Zitto na majibu ya hoja yaliyotolewa na Karamagi, kwani Mhe. Karamagi alikiri kusaini mkataba nje ya nchi na kitendo hicho ni kweli kilikuwa kinyume chaa kauli za rais na aliyekuwa Waziri wa Madini wakati huo.

Jambo lililokuwa limebaki hapa, ni kuthibitisha tu endapo utaratibu ulifuatwa ama haukufuatwa, na kama ingeonekana ulifuatwa, huo ndiyo ungekuwa mwisho wa jambo, kwani Mhe. Zitto angekuwa ametoshelezwa majibu kwa wasiwasi aliokuwa nao.

Tofauti na tulivyotarajia, umechukuliwa uamuzi wa haraka bila kuzingatia mambo tuliyotaja hapo juu, kwa maslahi ambayo tunaamini si maslahi ya taifa, bali ni maslahi ya ki-CCM zaidi.

Dhahama hili lililomkumba Zitto, litasababisha wabunge wetu wengi kuwa mabubu wanapokuwa bungeni au kuishia kuunga mkono hoja, hata iwe dhaifu kwa hofu ya kwamba akiuliza sana uenda akazikosa posho bungeni.

Tunafikiri kwamba hali hii ni kinyume cha nia ya ibara ya 100 ya katiba ya nchi, inayotoa haki ya uhuru wa majadiliano bungeni.

Endapo kungekuwa na chombo kingine cha kukata rufaa, tunaamini maamuzi ya namna hii yangetenguliwa. Lakini kwa kuwa Bunge lina mamlaka makubwa sana, tunaobaki kuumia ni sisi wananchi, hasa sisi walalahoi.

Uamuzi huu wa Zitto kusimamishwa hautufurahishi, si siri, haujawafurahisha Watanzania wengi, kwani hoja iliyokuwepo mezani haikuwa na maslahi kwa CHADEMA, CUF, CCM, TLP na vyama vingine, ni taifa zima.

Na kumwadhibu mbunge huyo hakujaweza kuondoa ukweli kwamba kuna mikataba ya kishenzi inayoingiwa na serikali na suala la Buzwagi ni mfano tu kati ya mikataba mingi mibovu iliyoingiwa, hasa ya madini.

Si siri tena, wabunge wengi wanaonyesha kuwa hawana utashi wa kulinda maslahi ya wananchi, na ndiyo maana wakakataa kuunda kamati kujadili suala lile muhimu. Na kwa jinsi Mhe. Mudhihir alivyoanza kutoa hoja ya kusimamishwa Zitto, na baadaye kuchangiwa na wabunge wengine, akiwemo Mheshimiwa John Samuel Malecela, inaonyesha kuwa mpango wa kumuondoa Zitto ulikuwa umepangwa mapema kabisa, tangu Zitto alipoanza kudadisi hotuba ya Karamagi.

Ikumbukwe kuzimwa kwa jambo lile bungeni si tiba, na wala kumuadhibu Zitto kwa kuonyesha uzalendo wake, kwani hakusaidii kuziba tatizo, bali kilichofanyika ni kudhihirisha tu kwamba Bunge limetumika kusigina demokrasia na uhuru wa majadiliano bungeni.

Tukubaliane kimsingi maswali ya Zitto hayajajibiwa, kwani jibu la kuwa kulikuwa na ulazima wa kuharakisha mkataba si jibu lenye mantiki hata kidogo, kwani sote tunaelewa kwamba hizo dola milioni 800 si za kwetu na kwamba sisi tunanufaika na asilimia tatu tu ya mapato ya madini.

Bei za mafuta zinavyopanda, mikataba ya kishenzi kama ya IPTL, ununuzi wa rada na kadhalika, haiwaumizi wanachama wa vyama vya upinzani tu, bali inamgusa na kumuumiza kila Mtanzania, hata wanachama wa CCM inayotawala nchi.

Hivyo, binafsi naamini kwamba hata wale wanachama wa CCM wanaoafiki kuondolewa kwa Zitto, ni kwa sababu ya unafiki tu, si kwamba hawajui ukweli, na baadhi wanaojua ukweli wamebaki kukaa kimya ama kuteta kwa chinichini tu, wakiogopa kama wataonwa watafukuzwa uanachama au majina yao kutopitishwa kugombea uongozi msimu ujao.

Ifike wakati kuwa, kunapokuwa na hoja yenye maslahi ya taifa, wabunge wote na wananchi tuweke itikadi zetu pembeni, tutetee hoja hizo au kupinga kama hazina maslahi kwetu.

Namaliza kwa kusema kwamba, kanuni za Bunge zinatumika au kutafsiriwa vibaya na baadhi ya wabunge. Sidhani kama Bunge la Kenya au Uganda, wanasimamishana ovyo, licha ya kwamba Bunge la Kenya limekuwa likisifika kwamba wabunge wake hata hufikia kupigana pindi wanapotofautiana katika hoja yenye masilahi ya taifa, lakini hatujasikia wakisimamishana kwa mtindo kama uliotumiwa na Bunge letu wiki hii.

Je, uhuru wa majadiliano bungeni na demokrasia ni mkubwa Kenya kuliko Tanzania?
Watanzania ebu tuamke usingizini, tuache itikadi zetu na woga tutetee maswala yanayohusu maslahi ya taifa zima na si vyama vyetu.

Wosia wangu kwa shujaa Zitto, sasa arudi jimboni kwake akaongee kwa ukaribu na wananchi waliomtuma bungeni, akawaeleze sababu zilizosababisha Bunge limsimamishe ubunge kwa kuwa wao ndio watakaomuhukumu, kwamba ndiyo waliyomtuma au amekiuka maagizo yao.

Aidha, atumie nafasi hii kuzungumza na wapiga kura wake na kupumzika na kuhimiza maendeleo ndani ya jimbo analoliongoza. Na asisahau kunusanusa na kupeleleza ufisadi unaofanywa chini chini kisha auanike bungeni atakaporudi.

Na uamuzi huu wa kusimamishwa naomba umtie nguvu zaidi na arudi na moto mkubwa panapo majaliwa Januari mwaka 2008, kwa maslahi ya wapiga kura wa Jimbo la Kigoma Kaskazini na Watanzania kwa ujumla. Tunakuombea Mungu akupe afya njema ili uweze kulitetea taifa hili kwa ujasiri ule ule. Tupo nyuma yake.
Mungu ibariki Afrika, Mungu inusuru Tanzania.

Mwandishi wa wa makala hii anapatikana kwa simu; 0755 312 859; baruapepe: katabazihappy@yahoo.com au www.katabazihapppy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Agosti 19,2007

Hatuna budi kuwabaini wadau wa ujambazi


IGP-Said Mwema

Na Happiness Katabazi

MWANZONI wa utawala wa serikali ya awamu ya nne, chini ya amiri jeshi mkuu Rais Jakaya Kikwete na mkuu mpya wa jeshi la polisi IGP Said Mwema, Watanzania tuliona mwanga wa matumaini katika ncha ya mwisho wa handaki lenye kiza kinene cha kushamiri kwa ujambazi hususan wa utumiaji wa silaha na mwingineo.

IGP mpya- mambo mapya, mathalani utumiaji wa helkopta kama teknolojia yenye tija katika kusaka majambazi na wahalifu kwa ujumla; heko ‘Njagu Mkuu’- Mwema.

Ama kweli kabla ya awamu ya nne matukio ya uporaji wa abiria wakiwa safarini, uvamizi wa mabenki, sehemu za starehe na majumba ya makazi pamoja na wizi wa magari yaligeuka kuwa ada siku hadi siku.

Katika kile kinachomaanisha kurejea kwa kasi mpya kwa uhalifu wa aina hiyo, mwaka huu matukio ya ujambazi yameshamiri upya kama ilivyoripotiwa na vyombo mbali mbali vya habari hususan mwezi Julai, 2007.

Ni katika mwezi huo wa Julai watalii wameporwa kule Mto wa Mbu, majambazi yaliiba nyumbani kwa mkuu wa polisi wilaya ya Kahama, yakakwapua kwenye ATM mbalimbali, mengine yakakwapua kitita cha milioni ya shilingi katika benki ya NMB tawi la Mwanga,waliokuwa wanapata Tusker baridi baada ya kazi katika baa tatu za Changanyikeni nao yamewafika. Huko Geita nako nyumba ya wageni imevamiwa na wakora… loo, orodha ni ndefu kweli kweli!

Maswali kuhusu ujambazi huu ni mengi kuliko majibu. Miongoni mwa maswali hayo ni kwa nini ujambazi uongezeke na je majambazi wanamuduje kazi zao kwa msaada wa nani, ama nani hasa yuko nyuma yao akiwawezesha moja kwa moja ama kwa namna nyingine?

Wataalam kadhaa wa Sosholojia wanatwambia kuwa jambazi ni zao la jamii. Pengine ni kweli kwa kuwa majambazi nao wamezaliwa, yaani wana Baba na Mama, shangazi, wajomba, mahawala na wanandugu. Ama kwa hakika mtu hawi jambazi hivi hivi ila kwa sababu fulani fulani.

Wapo ambao wamekuwa majambazi kwa sababu walizaliwa na walikulia katika mazingira magumu, wakakosa mahitaji muhimu, wakakosa kufunzwa maadili, wakakosa kulindwa dhidi ya kujifunza tabia mbaya wakingali makinda.

Hivyo jamii yoyote iliyo makini haiwezi kupata usingizi endapo watoto yatima wanaongezeka, watoto wa mitaani wanarudufika idadi na wasioenda shule inashamiri.

Watoto wa jinsi hiyo ndio hugeuka kuwa vibaka na hatimaye majambazi kadri umri unavyoongezeka waongezekea na kadri matumbo yao yanavyozidi kuuma njaa.

Upo usemi wa kifalsafa kwamba kinga ni bora kuliko tiba. Yafaa basi viongozi wetu na wanajamii sote kwa ujumla tuone haja ya kudhibiti ongezeko la watoto wa jinsi hii mitaani ili bomu walilobeba lisizidi kuongezeka petroli na utambi.

Basi linapozungumzwa suala la kusaidia yatima na watoto waishio katika mazingira magumu asiyejua umuhimu na maana yake afunguke macho sasa na asikie.

Kadhalika kisababishi kingine cha uwepo wa majambazi ni umaskini ambao unazidi kuota mizizi miongoni mwa wananchi tulio wengi. Hakika ni hatari kwa nchi tunapoendelea kushuhudia bila kuchukua hatua stahili za kudhibiti ongezeko la tofauti ya kipato kati ya wakwasi na mafukara.

Tofauti hiyo kubwa licha ya kuwa kichocheo cha tamaa ya mali kwa wale walio maskini ni chimbuko la chuki ya wasionacho dhidi ya walionacho. Maskini anapoendelea kuwa fukara ni rahisi sana kujiingiza katika ujambazi ili ajipatie cha kujaza tumbo lake.

Yamkini ujambazi mwingine ni vita vya chuki kati ya maskini wa kizazi hadi kizazi na tajiri wa enzi na enzi.

Hivyo, baadhi ya majambazi wanapoamua kubeba silaha wanaongeza kiwango cha kufyatua risasi wakiongozwa na chuki hii, na siombei mabaya ila tayari kuna kila dalili za kuzuka vita kati ya maskini na matajiri hapa nchini.

Baadhi ya mataifa makubwa duniani yameibaini chuki hii na wanajua wazi kwamba kadri dunia itakavyozidi kugawanyika kati ya wenye nacho na wasio nacho, ugaidi utaongezeka na uhalifu wa kimataifa utakomaa, na vita baina ya mataifa zitaongezeka.

Kwa kifupi ili tajiri ale kwa raha zake sharti ahakikishe maskini aketiye mlangoni pake naye kapata ukoko na makombo, vinginevyo kama wasemavyo waswahili pataendelea kuwa ‘hapatoshi/kujichimbika’, ujambazi utakuwa ni kila uchao tena kwa ari, nguvu na kasi ya chombo cha anga za mbali.

Ujumbe ni kwetu sote tunaofikiria kudhibiti ujambazi, imetupasa kutambua kuwa kadri tunavoendelea kuwa na sera zinazomtajirisha zaidi bepari (kwa mgongo wa ubinafsishaji na uwekezaji) ndivyo hivyo hivyo tunazalisha makabwela wasio na mbele wala nyuma.

Wenzetu wenye busara na akili timamu kama hayati Baba wa Taifa Julias Nyerere na Prof. Chachage wa Chachage waliutanabahisha kuwa nchi yetu sasa imetekwa na utandawizi ambao ni ubeberu katika lugha ya danganya jinga isemayo “utandawazi”. (Je ni kweli sisi watanzania ni mabwege hata kuliko yule Chifu Mangungo wa Msovero aliyeuza nchi kwa bei ya shanga na vipande vya nguo ya kaniki?).

Tujue wazi tunazidi kuongeza ‘makuruta’ katika jeshi hatari sana la ujambazi wa kujikwamua na kuelezea chuki iliyoko moyoni. Pengine lugha ya maneno ya kuwataka kubadilisha sera mbovu na mgawano mbaya wa keki ya taifa watawala wetu hamuielewi, eleweni basi lugha ya risasi za moto. Huko ndiko tunapoelekea sote, hata tukiachilia mbali hayo ya majambazi!

Chanzo kingine cha ujambazi kinachoshabihiana na niliyokwisha yataja, ni ukosefu wa ajira. Ni nani asiyejua kwamba matokeo ya mhitimu wa darasa la saba, kidato cha nne au cha sita na pengine chuo kikuu kukosa kazi ni kujiingiza katika vitendo vya uhalifu?.

Naam, asomaye na afahamu kwamba vita dhidi ya ujambazi haianzii katika kutisha wakazi wa ardhini kwa kurusha chombo cha usafiri kinachofanana na cha Mhe. Freeman Mbowe hewani, bali vita hii inaanzia katika kuwatafutia vijana ajira lakini kila mwaka shule zinapowaruhusu kuingia katika ulimwengu wa utafutaji.

Kwa ujumla jamii inao wajibu wa kudhibiti vyanzo hivi, na kwa maana hiyo jamii ni mdau katika suala zima la ujambazi.

Wengine ambao waweza kutajwa katika orodha ya wadau ni pamoja na vyombo vya dola, serikali na watu binafsi mmoja mmoja.

Udau huu uko katika namna ambayo wadau wengine wanao wajibu wa kutimiza ili kuiondolea jamii kero ya ujambazi, ilihali wadau wengine ni washirika wa majambazi. Ushirika wao umejikita katika kuwasaidia na kuwawezesha majambazi kuwepo na kufanya kazi zao.

Jambazi hawezi kutumia silaha hususan bunduki za kisasa, mabomu na silaha nyingine kali za kivita mpaka jambazi huyo awe amepata mafunzo mazuri ya kufanya hivyo.

Yawezekana majambazi wenyewe kwa wenyewe wanafundishana matumizi ya silaha katika makambi yao ya kificho, lakini hatuwezi kupuuza uwezekano kwamba majambazi wengine, yamkini walio wengi wana ujuzi wa matumizi ya silaha kutokana na mafunzo rasmi ya kijeshi.

Mara kadhaa matukio ya ujambazi yamebainika kuwahusisha moja kwa moja ama baadhi ya askari wa JWTZ au jeshi la polisi. Kwa upande mwingine, kitendo cha kufunzwa matumizi ya silaha kwa vijana wa kitanzania halafu wasipewe ajira yoyote iwe jeshini au kwingineko, ni cha hatari kabisa kwani ni mojawapo ya chimbuko la utaalam wa majambazi.

Kama nilivyosema mwanzo, ujambazi una uhusiano na ukosefu wa ajira na hivyo ni hatari zaidi kwa aliyefunzwa mbinu za kivita kukosa ajira.

Wakati umefika kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kufikiria upya kuhusu mafunzo ya kijeshi wanayoyatoa kwa vijana kwa kipindi cha miaka miwili huku wakipewa matumaini kwamba JWTZ itawachukua kwenda katika mafunzo zaidi (depo) na hatimaye waajiriwe katika jeshi hilo.

Inasikitisha kuona kwamba wanaofundishwa JKT ni wengi sana, na wanaochukuliwa na JWTZ na majeshi mengine ni wachache sana miongoni mwao. Yafaa JKT na taifa kwa ujumla tujiulize wanaobaki wanaingia katika sekta gani ya uhakika. Ya nini tujinase kwa tego letu sisi wenyewe. Nisikieni JKT; huo ndio udau wenu katika ujambazi.

Vile vile, jambazi hatumii silaha kali bila kuwa nayo. Swali la kujiuliza hapa ni je, majambazi wanapata wapi silaha. Baadhi ya majibu yako wazi kwani mara kadhaa majambazi wamekamatwa wakiwa na silaha zinazomilikiwa na vyombo vyetu vya dola.

Na hiyo ndio sura nyingine ya udau wa vyombo hivi katika ujambazi. Jeshi la polisi linapoendelea kukaza buti katika kupambana na majambazi yafaa pia lijigeukie lenyewe na kuondoa kabisa ushirika wa baadhi yao katika kuwapatia majambazi silaha, kuwasindikiza majambazi kufanya uhalifu na kisha kuwatorosha.

Hatua za kuchukua ni pamoja na kuboresha maslahi ya askari wenyewe, ili isiwe kwao rahisi kushawishika kuchukua rushwa toka kwa majambazi na au kuwakodisha silaha wakafanyie uhalifu.

Kadhalika, jambazi hapati silaha na hatimaye kufanya uhalifu mpaka pawepo na udhaifu katika mfumo mzima wa uhifadhi silaha zenyewe na ulinzi thabiti wa maeneo tete. Enzi za Mwalimu Nyerere ilikuwa ni nadra sana mtu kukamatwa na risasi japo moja.

Lakini katika wakati tulionao mtu kukutwa na bunduki ,silaha na mabomu ni fasheni kana kwamba wahusika wanapata risasi kiurahisi kama vile kununua peremende kwenye kioski! Inakuwaje mambo haya…,maduka na maghala yetu yakuifadhia silaha na viambata vyake kwa nini yavuje kiurahisi namna hiyo?. Nitakuwa nimekosea wapi nikiwaorodhesha askari watunza maghala haya miongoni mwao ni wadau wa ujambazi nchini.

Suala la kwamba chanzo kingine cha majambazi na silaha wanazozitumia ni nchi jirani zetu. Lakini haitatosha kuwatupia lawama (japo za kweli) majirani hawa, maana laiti kama ulinzi wa mipaka yetu ungekuwa imara hao Wakenya wanaopora benki zetu huko Arusha, Mwanga na hata Dar es Salaam wasingefurukuta.

Wiki mbili zilizopita niliandika kwamba nchi yetu si salama japo tuna chombo kinaitwa Usalama wa Taifa na Idara ya Uhamiaji. Usalama wa Taifa kivipi ilihali mipaka yetu inapenyeka kiurahisi na majambazi kama maji yapenyavyo kwenye tenga la nyanya.

Na asante sana wasomaji wote mlionitumia pongezi kutokana na makala hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Twahitaji Usalama wa Taifa siyo Uhasama wa Taifa’.

Kumradhi walinzi wetu mipakani, udau wenu katika ujambazi ni udhaifu (pengine uzembe) huo katika kuifanyia doria thabiti mipaka yetu na kuwa makini katika vituo vya mipakani wanakopitia wageni kutoka na kuingia nchini.

Vile vile, jambazi mara nyingi havamii sehemu pasipokuwa na taarifa kwamba mahali fulani kipo anachokihitaji. Majambazi wanajua lini pesa zinasafirishwa, gari gani lina abiria wenye pesa, mahali gani wanalala watalii wenye vitu vya thamani, ni mfumo gani wa ulinzi uko mahali fulani.

Taarifa hizi wanazipata si kwa mzizi wala hirizi bali kutoka kwa wadau wao ambao pengine ni wafanyakazi wa taasisi itakayovamiwa au ni watu wa karibu wa wenye mali wanayoilenga majambazi.

Hapa ndipo udau wa mtu mmoja mmoja unapoingilia.Yafaa basi hatua za kudhibiti ujambazi zilenge pia kuwashughulikia wadau wa upashaji habari nyeti kwa majambazi.

Tochi itakayotumika hapa isikose kuwamulika wafanyakazi katika taasisi za fedha ambao uaminifu wao ni wa mashaka, walinzi ambao tabia zao ni walakini mtupu na wengineo.

Jambazi hafanyi shughuli zake bila kuwa na kambi/makao (base). Mara kadhaa imebainika majambazi ni wapangaji wa kawaida katika nyumba zinazomilikiwa na watu binafsi.

Tuwaulize wenye nyumba hizi, inakuwaje mtu usiyejua shughuli inayompatia riziki unaingia naye mkataba wa kupanga nyumba. Udau wa wamiliki wa nyumba katika ujambazi ndio huo. Lakini tuiulize pia serikali, mbona sheria ya ukaazi na ulazima wa mfumo wa wenye nyumba kuoanishwa na mfumo wa polisi hatujauibua?

Wenye nyumba jamani kuweni makini na watu mnao wapangisha, labda kama mnafanya mnachokijua endapo ninyi ni washirika wa majambazi.

Pia baadhi ya Madalali wa nyumba,vyumba nao kwa njia moja au nyingine ni wadau wa ujambazi kwani kupitia hiyo kazi yao ya udalali wamekuwa wakiwafahamu wahamiaji haramu na majambazi wanapoishi ila kwasababu wanazozijua wao wamekuwa hawataki kuisaidia polisi kuwafichua.

Nasema hivyo kwasababu mfano jambazi anaishi Kinondoni na akaona watu wameishaanza kujua nyendo zake anatafuta dalali anayemjua kisha anampa kazi ya kumtafutia nyumba katika maeneo mengine , ambapo katika eneo hilo atakuwa ni mgeni na hivyo itawachukua muda mrefu wananchi wa eneo hili kujua kazi anayoifanya.

Nasema hivi kwasababu mimi ni Mkazi wa Sinza C, na Kata ya Sinza ni eneo lilikuwa likisifika sana kwa kukaliwa na wahamiaji haramu na majambazi kuishi katika eneo hili,lakini mwaka jana Kamati ya Ulinzi na Usalama Kata ya Sinza,ilikaa kikao pale Ukumbi Dulex, nami nilikuwa nimiongoni mwa wananchi walioudhulia kikao kile na ajenda kubwa ya kikao ilikuwa ni kupanga mikakati ya kutokomeza uhalifu na kuimarisha ulinzi Sinza.

Kama ilivyoada Polisi kituo cha Urafiki na Mabati, waliudhuria kikao hicho na kweli walishirikiana bega kwa bega na wananchi na ikatolewa azimio kwamba madalali nao washirikiane na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mitaa iliyopo Kata ya Sinza, na kweli baadhi ya Madalali kwa siri kubwa walishirikiana na kamati hizo ambao walitaja namba za nyumba wanazoishi wahamiaji haramu na watu waowashuku kuwa ni wahalifu na hatimaye Afisa Mtendaji wa Kata hiyo akishirikiana na Diwani wa Kata ya Sinza Salum Mwaking’inda, waliwasilisha orodha hiyo kwenye vituo hivyo vya polisi na kweli nilishuudia kwa macho yangu Defenda za polisi kila mara zilikuwa zikikatiza kwenye mitaa yetu nyakati za usiku na kuwakamata wahamiaji haramu kwenye nyumba walizokuwa wamepanga.

Hivi sasa wakazi wa ‘Sinza kwa wajanja’ tunaweza kusema idadi ya wahamiaji haramu na matukio ya uhalifu kwa kiasi fulani umepungua.heko polisi.

Wito kwa Manjagu wetu (Polisi), watumieni Madalali kupata taarifa za wahalifu wanapoishi na pia wahaamiaji haramu naamini mtafanikiwa.

Nisisitize hapa kwamba, kazi inayofanywa na jeshi la polisi kushughulikia majambazi kwa ufupi ni nzuri, kinachotakiwa ni utambuzi mpana wa wadau wa ujambazi na kuwashughulikia ipasavyo. Hatimaye wafikishwe mbele ya sheria, wakabidhiwe magerezani wakarekebishwe tabia (kama kweli Magereza yanafanya hivyo, na si kuwafunza wahalifu mbinu za nyongeza).

Naam, polisi dhibitini ujambazi wa kutumia silaha ila msisahau kwamba upo ujambazi mwingine unaozidi huu kwa mapana na makali yake, uko maofisini, unatendwa na wavaa kola nyeupe, suti na kubeba briefcase na, watu wenye haiba na staha mbele ya jamii. Kama waimbavyo wana bongo flava; ‘machoni kama watu moyoni hawana utu’, kina nani hawa… majambazi wanaotumia kalamu, na wadau wao.

Mwisho kabisa niiambie serikali kwamba hatuwezi kufanikiwa ikiwa tunaendesha mambo kishikaji. Tuanze kuthamini wataalamu wetu waliobobea katika taaluma husika kwenye taasisi binafsi na za umma hasa walio kwenye vyuo vya elimu ya juu. Pia tuwasikilize jeshi la polisi wanapoiomba serikali iwaongezee fungu ili iweze kufanyakazi yake kikamilifu kwani kitendo cha serikali kuendelea kuziba maskio na kutoa visingio kwamba serikali haina fedha huku serikali hiyo hiyo inaizinisha mamilioni ya hela kununulia mashangi ikome kuanzia sasa.

Watanzania tunataka tuishi kwa usalama katika nchi yetu, na polisi ndiyo wamekabidhiwa jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zetu hivyo hatuko radhi kuona ‘polisi njaa’ wanaotumia zana duni. Jeshi la polisi linapoiomba serikali itenge fedha za kutosha tunaomba wasikilizwe na kutekelezewa mara moja maombi yao.

Kwa kuwa sisi wananchi tumechoka kuona askari wetu wanaishi kwenye nyumba zisizoeleweka, sare zao zimepauka kama 'mashuka ya gesti', kuona askari wetu wamevalia ndani fulana ziliozoandikwa 'chagua ccm' badala ya kuvalishwa vikinga risasi 'bullet proof.

Umefiika wakati wa Jeshi la Polisi kutengeneza fulana zenye nembo ya Jeshi hilo ambazo zitavaliwa na askari wake wala moja kwa wiki kama ilivyo kwa askari wa JWTZ na JKT.Natumaini kwa uwelewa mkubwa alionao IGP Mwema na Makamishna wake swala hili watalifanyia kazi haraka.

Umefika wakati wa kuwa na jeshi dogo la polisi,bora na lenye vifaa vya kisasa vinavyowawezesha kufanyakazi katika mazingira yoyote yawe ya hatari au amani.

Pia umefika wakati nao polisi na makamanda wao kuungana pamoja kuikomalia serikali bila woga ili maslahi yao yaboreshwe kama ilivyo wafanyakazi wa majeshi mengine na sekta nyingine za serikali kwa kuwa askari wetu bila kuboreshewa maslahi yao ni wazi watavunjika moyo wa kulitumikia taifa hili. Hata hivyo napenda kumalizia kwa kuwaasa ndugu zetu kwenye jeshi la polisi wajihadhari sana na tabia ya kutumiwa na chama tawala hasa nyakati za uchaguzi.

Hivi mmeishawahi kujiuliza kama ninyi ni Umoja wa Vijana wa CCM au jeshi la usalama wa raia wa Tanzania? Tuhuma za nyie kutumika kuiba masanduku kura na kuwapiga raia wanapounga mkono wanamageuzi zitaisha lini? Hii kazi ya kuwabambikia kesi raia wanaounga mkono mageuzi amewapa nani na anawalipa nani kwa kazi hiyo? Hivi ninyi mnaona sisi raia hatujui wala hatuoni mnachokifanya? Basi endeleeni kuvaa vesti za “changua CCM” badala ya vesti za kukinga risasi tuone kama mtafika.

Sisi wananchi tunawapenda na kuwatetea kwa kuwa tunajua wajibu wa polisi kwa taifa lao lakini kwa tuhuma hizi, hatuwaungi mkono.

Mungu ibariki Afrika,Mungu inusuru Tanzania
0755312859; katabazihappy@yahoo.com;www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili,Uk.7. Agosti 5,2007