BILA KAZI YA ZIADA,HADHI YA MAHAKAMA YA TANZANIA INAKWISHA!

Na Happiness Katabazi

JULAI mwaka huu Rais Jakaya Kikwete alimteua Jaji Augustine Ramadhani(62) kuwa Jaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Jaji Mkuu, Barnabas Samatta, aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.

Na ni kwa mabadiliko ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Mahakama iliongezewa nguvu na kubadilishwa jina kutoka kuwa Idara tu ndani ya Wizara ya Katiba na Sheria na kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania.

Mabadiliko haya yalikuwa na maana kwamba sasa mahakama inatambilika rasmi kama muhimili wa dola. Muhimili ambao kwa muda mrefu ulikuwa umegandamizwa na serikali(executive) kwani mahakama ilikuwa inapangiwa kila kitu ikiwemo bajeti yake.

Pamoja na dhana ya uhuru wa mahakama lakini bado katika mazingira ya utendaji wake isingeweza kujidadavua na kufanya mambo yake kama inavyotaka.

Kwa hali ilivyo sasa mahakama yetu ya Tanzania ina kazi kubwa sana ya kufanya. Zipo changamoto nyingi ambazo inabidi izitatue ili kufikia uhuru wa kweli wa mahakama na utaoaji wa haki kwa haraka na pasipo malalamiko.

Ni miaka 28 sasa tangu Mahakama ya Rufani ilipoanzishwa lakini hadi sasa bado hakuna mabadiliko makubwa. Mh.Jaji Mkuu; mahakama nyingi za mwanzo huko vijijini zinatisha ukiyaangalia majengo yake, ukiachilia mbali samani zilizomo humo ndani.

Hakuna sehemu za kuweka mafaili, vitendea kazi hakuna,nyumba za mahakimu n.k. ambapo hakimu anatembea umbali mrefu kufika kazini na mara nyingine hakimu anapoendelea na kesi kunyeshewa na mvua au upepo.

Hali hii imetokea pia huko Biharamulo ambako pia wakati mwingine mahakama hufanyika kwenye wodi la zamani la hospitali ya Biharamulo. Haya yote yanafanya mahakama zetu zikose uhuru wake na ukiachia hayo mahakimu wengi kutoripoti vituo vya kazi walivyopangiwa au kuhama hasa kipindi hiki ambacho mahakimu wengi wanaoenda huko ni wale wenye Stashahada.

Ifike wakati sasa mahakama hizi za mwanzo ziangaliwe na kwa kuwa pesa za serikali kuu hazitoshi basi nashauri iendeshwe harambee na Mahakama Kuu kuwahamasisha wananchi kujenga mahakama kama inavyokuwa kwa vituo vya polisi ili wajijengee mahakama zao wenyewe.

Aidha, katika mahakama zetu za chini kuna ukosefu mkubwa wa samani,vitendea kazi kama vile karatasi,n.k na upungufu wa majengo ambao unafanya mahakimu na wengine kukosa mahali pa kukaa, mifumo ya maji taka ni mibovu, vyoo vinatia kinyaa.

Ukienda mathalani pale Kisutu utakuta mahakimu wawili wanakaa chumba kimoja, hakimu mwingine hata kiti anachokalia utamwonea huruma aidha hata chumba cha kukaa mawakili nacho hakitoshi, hali inayofanya utendaji kazi kuwa mgumu sana.

Katika mahakama nyingine kama huko Kigoma Hakimu Mfawidhi anawajibika kutembea umbali mrefu na saa nyingine kupanda treni wakati anapokwenda kukagua mahakama za mwanzo. Mambo haya yote yanaathiri sana uhuru wa mahakama.

Kutokana na kukosekana mazingira mazuri ya kufanyia kazi unakuta mahakimu wengi wanaamua kutokwenda wanakopangiwa kazi au kuwa wavivu au saa nyingine kupewa lifti na wadaiwa katika kesi, au kufadhiliwa mahitaji muhimu kitu ambacho kinaathiri utoaji haki.

Unategemea nini hakimu ambaye anatoka Bunju na kuja kuendesha mahakama ya Kisutu huku akitumia usafiri wa daladala?

Humo humo kwenye daladala wamepanda watuhumiwa au wadaiwa ambapo saa nyingine anajikuta amelipiwa nauli au mwenye nyumba wake. Naam! yaweza kuwa ni ukarimu lakini kwa nini uwe kwa hakimu?

Je unategemea mwenye nyumba huyu au mtu aliyemlipia nauli ya daladala hakimu mara atakapopatwa na kosa kuhukumiwa kwa haki?

Hali hii ndivyo ilivyo hata kwa makarani wetu ambao mishahara yao ni midogo, wakati kazi wanayofanya ni kubwa sana. Kila kukicha wanacheza na mafaili ambayo pamoja na vumbi wanalolipata hawapati hata ‘allowance’ ya maziwa.

Hali hiyo inapelekea kuanza kuwaomba wateja pesa, mara nyingine kwa nia njema tu si kwa lengo la rushwa. Mara nyingi hata rushwa zinazolalamikiwa mahakamani si za mahakimu kama mahakimu ni bali nyingi zinapokelewa na makarani kwa kisingizio kwamba mahakimu wanataka chochote ili wateja washinde kesi zao.

Mara nyingine makarani wamekuwa wakituhumiwa kwa makusudi kuwa wanaficha majalada ya wateja ili tu kulazimisha rushwa kwani mteja akisumbuka sana mwisho huamua kutoa chochote.
Mara nyingi rushwa hizi ni za kati ya Sh. mia tano, elfu moja, elfu mbili hadi elfu tano.Inasikitisha sana kuona kwamba hukumu imetolewa lakini inachukua miezi mitano hadi sita kupata hukumu yake, na bado hukumu ikishachapwa kule kukabidhiwa tu na karani utasugua viatu weeeee mpaka uchoke.

Baadhi ya Makarani hata imefikia wanathubutu kuwaacha wateja na kwenda kunywa chai au kupiga soga tu na ndugu zao kwa zaidi ya masaa mawili huku wananchi wakisota tu kwenye korido za mahakama.

Kisingizio kompyuta mbovu mara mafaili mengi n.k.Yupo rafiki yangu mmoja ambaye alifungua kesi yake katika mahakama ya Kisutu hapa Dar-es-salaam, ilichukua zaidi ya mwezi kupata tu wito wa mahakama(summons) kila siku anaambiwa njoo mchana mara njoo asubuhi.Cha ajabu kesi hii ilikuwa kwa Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi kabisa,lakini utendaji wa makarani wake ukaongoza kuwa mbovu. Watumishi wa mahakama hawajali kabisa.

Wengine wamefikia hatua kuomba rushwa mchana kweupe pee hata kwa kulazimisha kana kwamba ni halali. Tatizo kubwa linalotokea hapa ni kwamba hakuna hata mfumo mzuri wa kupeleka malalamiko katika mahakama zetu.

Ukiachilia malalamiko ya rushwa hakuna mfumo mzuri wa kiutendaji wa kupeleka malamiko yanayohusu utendaji wa watumishi wa mahakama,na hata kama upo basi au haujulikani au walio na wajibu hawataki kufanya wajibu wao, kwani utakuta baadhi ya wakuu wa makarani wenyewe ndiyo wanaongoza kwa kupokea rushwa au kulalamikiwa kwa utendaji mbovu.

Ukichunguza sana utakuta kama vile makarani hawawajibiki kwa mahakimu na hivyo wanakuwa hawawaheshimu. Kwa ufupi makarani wanaharibu sifa ya mahakama kuliko mahakimu wenyewe hasa wanapokuwa na ujuzi kidogo wa sheria basi hapo hujifanya mahakimu au majaji wenyewe.Ukimkuta karani mzuri basi ni yule aliye chini ya hakimu aliyemakini na mkali sana,vinginevyo karani atakuchezea anavyoweza.

Unakuta hadi saa nyingine wanashindana na wanasheria kwa kukosoa hati zao mbalimbali wanazoziwasilisha mahakamani kana kwamba wao ndio wataalamu wa sheria.

Kundi jingine linaliochangia kuipaka matope na kuharibu uhuru wa mahakama ni Waendesha Mashitaka (PP)ambao ni watumishi wa Jeshi la Polisi chini ya IGP-Said Mwema, lakini wanafanya kazi za ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini inayoongozwa na Eliezer Feleshi,chini ya utaratibu wan chi uliopo.

Yaani baadhi ya Waendesha Mashitaka Mahakamani wanaongoza katika kuomba na kuporushwa mahakamani toka kwa ndugu na jamaa wa washtakiwa.

Hali hii hujitokeza sana pale ambapo Hakimu ametoa dhamana tena ya wazi na bure kabisa lakini mara akiachiwa tu anapokwenda kusaini na kukamilisha taratibu nyingine za polisi kama kutaka waandikiwe amri ya kutolewa gerezani, baadhi ya Waendesha Mashtaka(PP) na ndiyo huchukua nafasi yao wakishirikiana na karani husika kuwazungushazungusha na kuweka urasimu kibao na hata mara nyingine kuwatishia ndugu kwamba karandinga linakuja ili tu ndugu watoe chochote.

Pia Baadhi ya Waendesha Mashitaka wamekuwa wakituhumiwa kuaribu ushaidi katika kesi mbalimbali pindi wanapopewa rushwa na washitakwa, nasijawai kusikia wakikanusha hili, hakika ili ni tatizo na viongozi wao hawana budi kulikemea hili ili lisiendelee kuichafua mahakama zetu.

Mahakama zetu zinahitaji mabadiliko makubwa ili kukabiliana na changamoto hizi.

Ofisi za Mahakimu Wafawidhi zinapaswa kuwa wazi ili kukaribisha malalamiko ya watu na kupewa uwezo wa kudhibiti makarani wasio waaminifu katika kazi zao.

Na siyo ofisi za mahakama za Wafawidhi tu bali kuanzia ngazi zote za mahakama ziwe wazi kupokea malalamiko pia mahakama zote zitengeneze masanduku ya maoni ambayo yatawezesha raia kutumbukiza maoni na malalamiko kuhusu watumishi mbalimbali wa mahakama.

Na kuwe na tume au kamati ya utumishi wa mahakama ambayo itachukua maoni hayo na kuyafanyiakazi kama alivyokuwa kuwa akifanya Jaji wa Mahakama ya Rufaa Jaji Laurian Kalegeya, alipokuwa Jaji wa Mahakama Kuu na Mfawidhi wa Mahakama za Dar es Salaam.

Jaji Kalegeya enzi akiwa Jaji Mfawidhi alisaidia sana kuleta nidhamu mahakamani kwa kuzitembelea mahakama mara kwa mara hasa za mwanzo,kuongea na watumishi na kupokea malalamiko ya wananchi dhidi ya watumishi wake wasiyowaaminifu na kuwashughulikia kikamilifu,na ili ninaushaidi nalo.

Kazi ya kudhibiti rushwa ni kweli wanaweza kuachiwa (TAKUKURU) lakini hata masuala ya kiutendaji nayo mathalani uzembe wa makarani kupoteza mafaili tunahitaji kuwaachia TAKUKURU? La hasha huu ni wajibu wa mahakama moja kwa moja na haukwepeki.

Mahakama zetu zinapaswa kuwa na kompyuta za kutosha, printa, magari au walau hata pikipiki kwa mahakimu na vitendea kazi vingine ili kazi ziweze kufanyika kwa urahisi. Aidha ilipaswa kila hakimu wa mahakama ya wilaya kuwa na kompyuta kwajili ya kurahisisha ufanisi wake wa kazi mathalani uchapaji wa maamuzi madogo madogo ya mahakama kama vile ruling na order mbalimbali.

Aidha ni jambo la aibu sana hadi sasa kwa mahakama kutokuwa na tovuti(website) ambayo maamuzi na hukumu mbalimbali za mahakama zingekuwa zinapatikana.

Nasema ni jambo la aibu kwa sababu mahakama nyingi duniani tayari zina mitandao na tovuti na idara nyingi za serikali yakiwamo mashirika na taasisi binafsi yana tovuti kwaajili ya kutolea na kupokelea taarifa mbalimbali.

Leo hii hakimu au jaji anataka asome hukumu labda ya kesi ya Takrima, mgombea binafsi nk. ina mlazimu atafute ‘Law report’ au aingie gharama ya kuja Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,ndiyo apate nakala hizo za hukumu.Mahakama ingekuwa imefungua tofuti yake hakimu au jaji huyo asingelazimika kufunga safari kuja hapa hapa na badala yake kule mkoani alipo angefungua tovuti ya Mahakama ya Tanzania na angeweza kupata na kuisoma vema hukumu hizo na nyingine nyingi.

Je, nini kinashindikana kwa mahakama zetu, je,ni kukosekana kwa vipaumbele au kutojua?

Kuwepo kwa mtandao wa kompyuta, tovuti(website) kungesaidia mambo mengi sana kwani mahakama zilizoko wilayani na mikoani zingeweza kupata mawasiliano moja kwa moja na Mahakama Kuu.Mahakimu wangeweza kupata rejea za kesi mbali mbali ambazo hazijaripotiwa kupitia katika mtandao huu.

Aidha kusingekuwa na haja ya kusubiri muda mrefu uamuzi utoke kwani ukishasomwa tu unawekwa kwenye mtandao,mtumiaji anaufungua na kuutumia.
Vilevile Jaji wa chumba kimoja angeweza kujua jaji mwenzie ameamua nini na hivyo kuepusha mlundikano wa maamuzi mengi yanayotofautiana kuhusu jambo moja.

Baadhi ya ufisadi nilioutaja katika makala hii si wa kubuni wala kutunga.Upo na unatokea kila siku mashaidi ni wananchi wanao hudumiwa na mahakama hizo ,mimi mwenyewe ni Mwandishi wa Habari wa gazeti hili kwa miaka zaidi ya mitano sasa nimekuwa nikiandika habari za mahakamani toka mahakama za Mwanzo hadi mahakama ya Rufaa hivi sasa nimeshuudia baadhi ya ufisadi huo na hasa umekithiri katika mahakama za chini ukiachilia mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa.

Naweza kusema kwamba kupungua kwa matatizo niliyokwisha yataja hapo juu kunatokana kwa namna moja na udhibiti na usimamizi wa karibu uliopo kutoka kwa Majaji,Wasajili wa mahakama na uchache wa mashauri yanayofika Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu.

Kwa aina nyingine uwepo wa vitendea kazi vya kisasa japo havikidhi maitaji, umechangia sana kuleta ufanisi katika mahakama hizo mbili .Hivyo niimani yangu kwamba iwapo maslahi ya watumishi wa mahakama yataboreshwa kama ya wenzao wa mahakama Kuu na Rufaa,vifaa vikaongezwa,mazingira ya utendaji kazi yakaboreshwa na usimamizi mzuri ukawepo basi hata mahakama za chini zitakuwa na ufanisi mzuri ukilinganisha na sasa.

Binafsi nina imani na Jaji Mkuu Agustine Ramadhani ambaye pia ni Brigedia Mstaafu wa Jeshi la Wananchi(JWTZ) ambaye kabla ya kuapishwa nilifanya naye mahojiano maalum ofisini kwake kuhusu historia ya maisha yake na amejipanga vipi kuongoza Mahakama ya Tanzania, ambapo aliniambia kwamba kwake ni mapema mno kutamka kuwa amepanga kufanya jambo gani na kuomba Watanzania wampe muda aingie kwenye ofisi mpya ya (Ujaji Mkuu),aangalie ofisi hiyo ina miba gani, na akae na wenzake wajadiliane mambo mbalimbali kisha anaweza kutamka kwamba amejipanga kufanya mambo gani.

Jaji Mkuu umeishaingia ofisi mpya na kiti umeishakikalia na sasa umeishaanza kukizoea na hata ile miba uliyosema nafikiri umeishaanza kuiona.

Sisi kama wananchi tuna wajibu wa kukusaidia kwa kukuonesha wapi uozo ulipo, na wapi panatukera na kutuchefua ili wewe na timu yako mjue pa kuanzia. Ombi letu kwako ni hili mahakama ifungue Tovuti yake,itandaze masanduku ya maoni katika kila makahakama na watumishi wasiyowaaminifu washughulikiwe mara moja bila kuoneana haya.

Hizo ni changamoto zinazokabili mahakama zetu na Jaji Mkuu Ramadhan unapaswa kuzifanyiakazi ili hadi ya mahakama iweze kuwepo kama ilivyoelezwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Bila kazi ya ziada,hadhi ya mahakama ya Tanzania inakwisha.

Mungu Afrika,Mungu inusuru Tanzania

0755 312859; Email:katabazihappy@yahoo.com,website:www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Jumapili Septemba 30, mwaka 2007

LOWASSA AMENICHANGANYA


Na Happiness Katabazi

BABA wa Taifa Mwalimu Julias Kambarage Nyerere aliwai kusema ili nchi iendelee yahitaji mambo manne, nayo ni watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.

Wahaya na sisi Wanyambo tuna msemo: “Omukama ainduka anketo tainduka alulimi.” Kwa Kiswahili: “Mfalme hujigeuza kitini, si katika ulimi (kauli).”

Kwa kawaida kiongozi anatakiwa kuwa na kauli thabiti na msimamo katika ayasemayo.
Uchumi unapaa ni kauli iliyotolewa na Waziri Mkuu Edward Lowassa aliyoitoa kabla na wakati wa kufunga kikao cha Bunge la bajeti, la mwaka wa fedha 2007/2008, mjini Dodoma.

Waziri Mkuu Lowassa, akisoma hotuba yake ya kufunga kikao cha Bunge, alilalamika kuwa kuna baadhi ya waandishi wa habari, wachora katuni na wanaharakati wamekuwa wakipinga hilo.

Alisisitiza tena kuwa uchumi unapaa, kutoa vigezo na kuwataka wanaopinga hoja hiyo pia kuleta vigezo vya kupingana na hali hiyo.

Lakini mwishoni mwa wiki akiwa kwenye ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza, akijibu swali la wananchi wa Sengerema waliotaka kujua ni kwanini mfumko wa bei umeshika kasi katika kipindi kifupi tangu Rais Benjamin Mkapa aondoke madarakani.

Pia walitaka kujua ni lini ahadi ya maisha bora kwa kila Mtanzania itatimizwa.
Lowassa akijibu swali hilo alisema mfumuko wa bei unaoendelea hivi sasa umesababishwa na uchumi wa nchi kutokuwa mzuri. Na kuhusu ahadi ya maisha bora itatimizwa lini, aliwajibu kuwa maisha bora hayaji kwa wananchi wake kutofanya kazi kikamilifu katika sehemu zao za kazi.

Hapa waziri mkuu amenichanganya, kwani ni yeye aliyeuambia umma kupitia Bunge kuwa uchumi wa nchi unapaa kwa kasi ya ndege, lakini mwishoni mwa wiki iliyopita anawaambia wananchi wa Sengerema walipodai awaonjeshe huo uchumi unao paa, anasema vinginevyo.

Hivi waziri mkuu tukuelewe vipi? Ni mtu yuleyule uliyezungumza bungeni ndiye uliyezungumza Sengerema mwishoni mwa wiki?

Tuambizane ukweli kwamba wataalamu wako walilidanganya taifa kwa kukupa taarifa zisizo sahihi na hali halisi ya uchumi.

Kumbuka wakati wa kampeni jinsi CCM walivyoliimbia taifa ngonjera ambazo kiutekelezaji ni sawa na ndoto za Abunuasi. kwani hazitekelezeki.

Kwa jinsi hali ya mambo inavyokwenda, unaweza kuona kabisa uwezekano wa serikali kuleta maisha bora kwa kila Mtanzania.

Mfano, nia njema ya kujenga shule lazima iendane na taaluma ya elimu katika kujenga shule. Shule ni walimu wanafunzi, majengo, madawati, mahabara, vitabu n.k.
Sasa kila kimoja kwa nafasi yake. Tukijenga darasa, tukaweka wanafunzi ndani bila kupata walimu, tukae tukijua tunajenga genge la wahuni.

Na hizo ndizo shule zako Lowassa tunazoambiwa kwamba hazina walimu wa kutosha, hao ni wale walimu wako wa wiki nne. Tuambizane ukweli la sivyo taifa hili tutalipeleka pabaya.

Hao Watanzania wenzetu wanaojazwa upumbavu katika shule za kata bila walimu, watalipeleka taifa hili kuzimu.

Shule bila vitabu, madaftari, karamu, chaki, na vifaa vya maabara, si shule, hawa wanafunzi ni kiwango gani cha elimu ambacho wanapata?

Twende kwenye vyuo vikuu, serikali ina vyuo vikuu vinne, Mzumbe, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sokoine na Chuo Kikuu Uhuria. Hivyo vyuo vikuu kwanza ni vidogo na serikali haifanyi juhudi ya kupanua ili viweze kupokea wanafunzi wengi.

Uwezo wa vyuo vikuu hivyo kuvipanua ni mkubwa na unahitaji ongezeko la walimu, mishahara waboreshewe, inahitaji vifaa vya elimu ya juu, kompyuta na maabara za kisayansi.

Badala ya kulifanya hili, serikali inakurupuka na kuanzisha chuo kikuu kipya cha Dodoma. Ili kuanzisha Chuo Kikuu cha Dodoma, serikali imelazimika kuchukua baadhi ya wahadhiri kutoka kwenye vyuo vikuu hivyo vine, ingawa vyuo vyenyewe havina walimu wa kutosha.

Je, hayo maendeleo yako wapi kama una bomoa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sokoine, Mzumbe na Chuo Kikuu Huria ili ujenge Chuo Kikuu cha Dodoma maana yake nini? Au tunataka utitiri wa vyuo vikuu usio na viwango?

Twende kwenye sekta ya afya, huko vijijini tunaowajua ni waganga wa kienyeji na wakunga wa jadi, si madaktari ambao serikali inawasomesha kwenye vyuo vikuu na ndio wanaozalisha kina mama huko vijijini.

Badala hata ya kuwasaidia wakatoe huduma bora zaidi, mnakimbilia kujenga majengo ya zahanati bila kuweka wataalamu wa kutosha na dawa.

Wenzetu wa Kenya wanatengeneza dawa za mitishamba, tena wakati mwingine miti hiyo wanaivuna hapa kwetu na kwenda kutengeneza dawa hizo nchini mwao na kisha wanakuja kutuuzia hapa, na katika hili tukae tukijua tunapoteza na kukosa teknolojia.

Miti tunayo, waganga wa jadi na wakunga tunao, kitengo cha miti shamba kipo lakini akipewi fedha za kutosha badala yake fedha za walipa kodi zinanunulia mashangingi na kuishia kwenye ziara za viongozi.

Viongozi wakipata ajali wanapelekwa kutibiwa Afika Kusini, kwa matibabu ambayo waganga wetu wa hapa kupitia kitengo hicho cha tiba asilia kitengo cha MOI, kinaweza kutoa matibabu hayo.

Mheshimiwa Lowassa, wewe unawaambia wananchi wa Sengerema kwamba serikali ina mikakati ya kuboresha maisha yao, mikakati hiyo ni ipi tusiyoijua?
Au unataka kuzungumzia MKUKUTA, MKURABITA na mabilioni ya Kikwete? Kweli hiyo mikakati itatutoa kwenye umaskini?

MKURABITA ni mkakati wa walionacho na wanarasimisha mali walizonazo, kwa maana kama hauna mali, MKURABITA haukufikii.

MKUKUTA ni mpango wa kupunguza makali ya umaskini lakini umaskini una baki pale pale, hautuhakikishii kama tutaondoka kwenye umaskini kwa mikopo ya sh 50,000 au sh 100,000. Serikali itaondoaje umaskini kwa mikopo hiyo midogo?

Mabilioni ya Rais Kikwete hayawezi kutokomeza umaskini kwa sababu mikopo hii inatolewa kwa masharti na maskini hawezi kutekeleza masharti hayo, na si kila anayeomba anapata kutokana na masharti ya kibenki.Hata fedha hizo zingetolewa bila masharti, pia hazitoshi.

Kwa hiyo sisi tunachokusii Lowassa, usijalibu kupotosha wananchi kwasababu tayari wameishagundua siri ya sifuri.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima,Jumatano Septemba 26 mwaka 2007

KINGUNGE,MARMO TUMECHOSHWA NA POROJO!


Na Happiness Katabazi

SEPTEMBA 15, mwaka huu, nilikuwa miongoni mwa waandishi wa habari waliohudhuria mkutano wa hadhara viwanja vya Mwembe Yanga, Tandika, Dar es Salaam na kumshuhudia Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, akitaja orodha ya vigogo 11 aliowaita mafisadi.

Baada ya Dk. Slaa kuanika majina ya vigogo hao, mapema wiki hii vyombo vya habari vilimkariri Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Philip Marmo, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Siasa na Uhusiano wa Jamii), Kingunge Ngombale – Mwiru, wakiwataka wapinzani kuwasilisha ushahidi wa tuhuma hizo kwenye vyombo husika.

Mzee Kingunge aliwaambia waandishi wa habari Ikulu, Jumanne, kwamba tuhuma hizo ni za ‘uongo na uchochezi’ na kwamba wapinzani wanataka kuilazimisha serikali kuwakamata na aliwataka wananchi na umma uwapuuze wapinzani.

Binafsi nasema matamshi hayo ya viongozi hao wawili ni ya wanasiasa waliochoka.

Kwanza, wanasema viongozi wa upinzani wanapotosha wananchi kwa orodha ile ya vigogo 11. Sasa hatuoni ni jinsi gani usemi usio na mantiki unaweza kutolewa na kiongozi mwenye busara.

Hawa wana mageuzi wametaja vigogo na hawa wameeleza hilo hadharani kweupe. Hawa wametoa vigezo vya kisheria vya kumtaja kila mmoja kati yao.
Kuna waliotajwa kwa sababu walifanya vitendo vya kifisadi na kujineemesha na ufisadi huo. Kuna waliotajwa kutokana na maamuzi ya kifisadi waliyoyafanya.

Makundi haya yote mawili ni mafisadi. Mtu anayetaka kukanusha hilo, sharti athibitishe kuwa hakuna hata mmoja miongoni mwa vigogo waliotajwa kuwa si mafisadi.

Lakini kitendo cha Kingunge kuamka na kusema kwamba habari hizo zimepotosha umma, ni kuamini kwamba umma ni ‘wapumbavu’ na hauna uwezo wa kufikiri.

Labda tuangalie asiye na uwezo wa kufikiri kati ya umma na Kingunge ni yupi. Lalamiko la huyu bingwa wa propaganda Kingunge ni kwamba wapinzani wangeviarifu vyombo vya dola, hivyo vyombo ni vipi?

Kingunge na Marmo watutajie chombo kimoja cha dola chenye uwezo kisheria kumchunguza Rais Jakaya Kikwete au Rais mstaafu, Benjamin Mkapa.

Sheria inayounda (TAKUKURU) ya mwaka 2007 inampa uwezo rais wa nchi kumteua Mkurugenzi wa (TAKUKURU), hii ina maana kwamba mkurugenzi wa chombo hicho hawezi kufanya kazi dhidi ya rais, kwa sababu si tu kifungu hicho cha 6 (2), rais ana mamlaka ya kumteua, lakini kifungu cha 14 kinaweka masharti kwamba kila mwaka Machi 31, taasisi hiyo ya kupambana na rushwa itoe ripoti ya utendaji wake wa kazi kwa rais.

Kwa hiyo, kuwaambia wapinzani waende kulalamika (TAKUKURU) na kwenye vyombo vingine vya dola ni kudhania kwamba wananchi hawajui kwamba taasisi hiyo haina mamlaka ya kumchunguza rais.

Na kama Rais Kikwete ambaye naye ni miongoni mwa waliotajwa kwenye orodha ile hatachunguzwa, basi na hao vigogo waliobaki hawatachunguzwa. Ikiwa madai kwamba kampuni ya Kagoda ilianzishwa na kupewa sh bilioni 30 na Benki Kuu (BoT) ili zitumike kama ‘rushwa’ wakati wa uchaguzi, usafi wa rais uko wapi?

Ikiwa rais mstaafu Mkapa tunaelezwa alijigeuza kuwa mjasiriamali na akaanza kufanya biashara badala ya kuongoza taifa, usafi wa mstaafu huyu tulioambiwa na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere utakuwa wapi?

Ikiwa huyo Mkapa alipokuwa rais, familia yake pamoja na washirika wake wa karibu, wapinzani wanamtuhumu kwamba alijiuzia migodi ya machimbo ya makaa ya mawe ya Kiwira Coals Mines Ltd ili ajipatie mamilioni ya fedha kutoka TANESCO, usafi wa uongozi uko wapi?

Ikiwa BoT na gavana wake wanadaiwa kujiingiza katika makampuni yanayotajwa na wapinzani kuwa ni ya kitapeli ya Meremeta Ltd na Tangold Ltd, kwanini tusiamini wahusika wa makampuni haya ni mafisadi na matapeli wakubwa?.

Kampuni ya Meremeta kwa mujibu wa orodha ile inaonyesha ni kampuni ya kigeni iliyosajiliwa nje ya nchi kama kampuni ya wafanyabiashara wakwepa kodi. Je, wanaweza kutueleza Serikali ya Tanzania ilikuwa inakwepa kodi ya nchi gani, ya Tanzania, Mauritius au Afrika Kusini?

Je, huu ni uadilifu? Na mahesabu yaliyokaguliwa na Mkaguzi wa Serikali yako wapi? Na mbona imefilisika bila kufanya biashara yoyote licha ya kupewa mabilioni ya fedha na BoT?

Je, ni sahihi kuanzisha kampuni nje ya nchi, kuzipelekea mamilioni ya fedha nje ya nchi, kisha kuzifilisi na kuzipelekea tena fedha za walipa kodi kulipa madeni? Je, huu si ufisadi wa kupindukia?

Sasa wapinzani wanapotosha nini katika hili? Tunadhani kwamba serikali ina deni kubwa la kutoa maelezo sahihi kwa Watanzania badala ya viongozi wake kuropoka ovyo, ikifikiria bado wananchi wanaweza kurubuniwa kwa ombi lao la kutaka wananchi wawapuuze wapinzani?

Pia tunadhani watuhumiwa hao wa ufisadi nao wanapaswa wajitetee kwa umma.

Jambo li wazi kwamba Serikali ya Awamu ya Nne inayoongozwa na Rais Kikwete imeweka rekodi katika awamu zote kwa kuingia katika kashfa kubwa ya ufisadi katika kipindi cha miaka miwili ya utawala wake.

Hoja ya Kingunge ina maanisha kwamba wapinzani wana wajibu wa kufanya kazi za upelelezi badala ya taasisi za serikali. Taasisi hizo zenye wajibu wa kupeleleza rushwa, zipo na watumishi wake wanalipwa mishahara kwa kazi hiyo na hawana sababu ya kualala usingizi.

Rais Kikwete muda mfupi baada ya kuingia madarakani alitangaza baraza lake la mawaziri na alinukuliwa kwenye vyombo vya habari kwamba baraza lake haliwezi kuwa na vijana peke yao kwakuwa bila wazee moto unaweza kuwaka, akimaanisha kwamba wazee ni ‘grisi’ inayoweza kulainisha mambo yanapokuwa magumu, akimaanisha kwamba amemteua Kingunge kwa kuwa ana uzoefu mkubwa katika serikali na chama licha ana umri mkubwa.

Kutokana na matamshi ya Kingunge, Watanzania tujiulize hii ndiyo grisi tuliyoelezwa na rais wetu wakati akitangaza baraza lake la mawaziri?.

Sasa kwanini wangoje wapinzani wafanye kazi wawaletee ushaidi, kwani wapinzani wanalipwa kwa hiyo kazi? Huo ni uzembe wa serikali na hakika unawatia hasira walipa kodi.

Na kwa sababu ya uzembe huo, serikali haiwezi kuwatwisha mzigo wapinzani wa kuleta ushaidi. Kwa wajibu gani? Uwezeshwaji gani?
Hivi hizo taasisi za upelelezi zipo chini ya mamlaka ya wapinzani? Ieleweke wazi matamshi ya Marmo ya kutaka wapinzani wapeleke ushahidi na matamshi ya Kingunge kuwa tuhuma hizo ni za uongo na uchochezi na kwamba wapinzani wanataka kuilazimisha serikali kuwakamata na kuutaka umma upuuze tuhuma za wapinzani, ni matamshi yanayodhihirisha kukingia kifua ufisadi.

Na matamshi kama haya yaliyotolewa na viongozi hawa wa serikali, si mageni masikioni mwetu, kwani tulishawahi kuyasikia ya kitolewa na Rais mstaafu, Mkapa, enzi za uongozi wake, alipowaambia waandishi wa habari wathibitishe kuwa serikali yake ni ya wala rushwa na aliwanyoshea kidole waandishi kwamba hawaandiki rushwa ya wanahabari badala yake wanaandika rushwa ya viongozi wa serikali yake.

Aidha, lugha ya kutaka wananchi kuleta ushahidi kuhusu madai ya rushwa dhidi ya baadhi ya viongozi pia tumeishawahi kuyasikia sana kwa Mkapa.

Nasema tumechoka na porojo, tunataka kuona taasisi husika zinachukua hatua ili serikali iendelee kuaminiwa na kuheshimiwa ndani na nje ya nchi.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu 0755 312 859; barua pepe;katabazihappy@yahoo.com; tovuti;www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili la Septemba 23, 2007

HAPPINESS&MWANAMKE WA SHOKA JESHI LA POLISI


Nikifanya mahojiano maalum na Mkuu wa Kitengo cha Makosa dhidi ya Binadamu katika Jeshi la Polisi Tanzania ,Kamishna Msaidizi Mwandamizi(SACP)Sydney Mkumbi,Dar es Salaam,Juni 14 mwaka 2007.

WAITARA:SITAKI SIASA

*Asema ataendelea kuishi Dar

Na Happiness Katabazi

MKUU wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) mstaafu, Jenerali George Marwa Waitara (57), amesema hana mpango wa kushiriki katika siasa.

Jenerali Waitara alisema hayo jana kwenye lango la kutokea la Kambi ya Jenerali Twalipo, Mgulani jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kusukumwa na maofisa wakuu wanane wenye vyeo vya meja jenerali na brigedia jenerali, kama ishara ya kuagwa rasmi jeshini.

Jenerali Waitara ambaye aliagwa kwa kishindo na heshima zote za kijeshi, alisema hata baada ya kustaafu rasmi Septemba 15, ataendelea kuishi Dar es Salaam kwa kuwa familia yake ina makazi ndani ya jiji.

“Ndiyo nimestaafu lakini nitaendelea kuishi hapa hapa jijini kwa kuwa familia yangu ipo hapa, ila wakati mwingine nitakuwa nikienda Tarime ambako nilizaliwa… ila sihami jijini, nitaendelea kuishi hapa hapa,” alisisitiza Jenerali Waitara, huku akicheka na kusababisha maofisa wa jeshi hilo waliokuwa karibu yake na waandishi wa habari kuangua kicheko pia.

Akijibu mwaswali ya mwandishi wa gazeti hili kwamba ana mpango wa kuingia kwenye medani ya siasa na anatarajia kufanya shughuli gani, alisema kazi anayoijua yeye ni moja, na kuitaja kazi hiyo kuwa ni jeshi.

Alisema hana mpango wa kujitumbukiza kwenye siasa kwa kuwa kazi anayoijua yeye ni jeshi, na kuwa tangu azaliwe hajawahi kufikiria wala kuota ndoto ya kujiunga katika siasa.

Kuhusu shughuli gani ya kumuingizia kipato anayotarajia kuifanya baada ya kustaafu, alisema hadi wakati anastaafu alikuwa hajapanga atafanya shughuli gani na akaongeza kuwa, baada ya mapumziko ataangalia na kushauriana na ndugu na jamaa zake kuhusu shughuli atakayoifanya.

Mkuu mpya wa JWTZ, Jenerali Davis Mwamunyage, alimkabidhi mstaafu huyo kitambulisho cha kustaafu, ikiwa ni ishara ya kumuaga na Waitara naye alimkabidhi kitambulisho chake cha kazi, alichokuwa akikitumia kabla ya kustaafu.

“Leo nina furaha kubwa sana ya kukukabidhi hati hii ambayo utaitumia baada ya kustaafu… na ninakukabidhi hati hii kwa niaba ya JWTZ kama ishara ya kutambua na kuheshimu utumishi ndani ya jeshi hili… hongera sana na nina furaha sana kuona unastaafu kwa amani na kuliacha jeshi likiwa imara,” alisema Jenerali Mwamunyange.

“Nami nakukabidhi kitambulisho changu ambacho nilikuwa nikitumia kabla ya kustaafu kazi ya jeshi kama ishara ya kitambulisho hicho kwisha muda wake,” alisema Jenerali mstaafu Waitara.

Sherehe za kuagwa kwa mstaafu huyo zilianza saa 2:30 asubuhi katika Kambi ya Jenerali Twalipo, Mgulani kwa gwaride lililokuwa na gadi sita.

Awali, gadi hizo zilifanya gwaride la kumkaribisha Mkuu mpya wa jeshi hilo, Jenerali Mwamunyange, ambaye aliapishwa Jumamosi iliyopita na Amiri Jeshi Mkuu, Rais Jakaya Kikwete, na kisha kupita mbele kwa ukakamavu na kisha kutoa heshima kwa mwendo wa pole na haraka.

Baada ya kumaliza kutoa heshima, gwaride hilo lililokuwa likiongozwa na Kanali Raphael Mataba, liliumba umbo la Omega ikiwa ni ishara ya utumishi wa mwisho wa Waitara katika jeshi hilo.

Baada ya tukio hilo kumalizika, Waitara alipakiwa kwenye gari maalumu la wazi lililokuwa lilisukumwa na maofisa wa jeshi taratibu. Maofisa hao waliongozwa na mameja jenerali wawili. Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Martin Madatta na Meja Jenerali Sylvester Rioba.

Wengine sita waliomsukuma ni wenye vyeo vya brigedia jenerali, Said S. Omar ambaye ni Mkuu wa Kikosi cha Wanamaji (Navy), Seni Hinda, Charles Makakala, Rasul Kilonzo, Kamaro Ileti na Albert Balati.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na Kaimu Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Aziza Murhsal, Waziri wa Fedha, Zakia Meghji, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Profesa Juma Kapuya, majenerali wastaafu, waambata wa kijeshi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini na wananchi wa kawaida.

Wakati huo huo, maofisa na askari wa kawaida walimmwagia sifa Waitara wakimtaja kama kiongozi imara aliyeliongoza jeshi katika misingi ya haki na maadili mema.

Waitara alistaafu rasmi Septemba 15 mwaka huu. Alizaliwa Septemba 15 mwaka 1950 katika Kijiji cha Itirya, Wilaya ya Tarime, mkoani Mara. Alimaliza masomo yake ya Sekondari katika Shule ya Sekondari ya Minaki mwaka 1969.

Alijiunga rasmi na jeshi hilo mwaka 1970 akiwa ofisa mwanafunzi, na alipata kamisheni mwaka 1971, na kuhudhuria mafunzo mbalimbali ya kijeshi.

Mwaka 1978, katika vita ya Tanzania na Uganda, Waitara alikuwa miongoni mwa makamanda walioongoza vikosi katika vita hiyo.

Wakuu wa majeshi wengine waliomtangulia Waitara ni Sam Hagai, Mrisho Sarakikya, marehemu Abdallah Twalipo, David Musuguri, Ernest Mwita Kiaro na Robert Mboma.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima,Septemba 18,mwaka 2007

HAPPINESS & JENERALI MWAMUNYANGE


Nikiwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania(JWTZ)Jenerali Davis Adolf Mwamnyange,muda mfupi baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete,Ikulu Dar es Salaam, Septemba 15,2007. Picha na Mpoki Bukuku.

CCM IJIFUNZE ALAMA ZA NYAKATI

Na Happiness Katabazi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimetokana na chama cha TANU na Afro-Shiraz, vilivyokuwa vikiamini na kuhubiri kuwa rushwa ni adui wa haki.

Wakati wazee wetu wakipigania uhuru na hata baada ya kupatikana, mahubiri ya viongozi wetu wa CCM na serikali yao yalikuwa yakikisitiza kuwa rushwa ni adui wa haki.

Miaka michache iliyopita, CCM iliwashangaza Watanzania iliposema rushwa ni takrima. Hili liliwashangaza wengi kwa sababu katika historia ya taifa hili na katika miaka 45 ya uhuru wa nchi yetu, hakujawahi kutokea mabadiliko ya kuhalalisha rushwa mpaka hivi majuzi CCM ilipotamka kuwa rushwa ni takrima, na kwamba ni utaratibu wa Kiafrika kumkarimu mtu.

CCM ililivalia hili njuga na kulipeleka bungeni, na kwa sababu ndiyo chama dola, likapita, ikawa sheria ya nchi. Kwa kuwa wapinzani bungeni ni wachache, hawakuweza kuuzuia muswada ule usiwe sheria, ikatumika turufu ya wengi wape.

Wanaharakati wakaichachamalia sheria ile na kuipeleka mahakamani, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na Nola vikapaza sauti kwa nguvu kuipinga sheria hiyo. Mahakama ikasikia kelele hizo, ikatamka kwamba vipengele vya takrima kwenye sheria ya uchaguzi vinahalalisha rushwa, na hivyo ni kinyume cha katiba ya nchi.

Hii maana yake ni kwamba, CCM na serikali yake, vilikuwa vimehalalisha rushwa, na kwa maana nyingine ni kwamba, wale wote walio bungeni walikuwa wamepata uongozi kwa rushwa.

Ukiihalalisha rushwa kwenye uchaguzi, utapata viongozi wa aina gani? Ikiwa uongozi unaweza kupatikana kwa fulana, kofia, pilau, fedha n.k je, unaweza kusema tuna uongozi wa kiadilifu?

Siku zote uongozi uliopatikana kwa rushwa, huzaa serikali ya wala rushwa. Takrima iliyohalalishwa na serikali yetu, ndiyo matokeo ya ufisadi unaojionyesha hivi sasa serikalini. Tujiulize, kama tuna viongozi walioingia madarakani kwa kutoa takrima, ufisadi unaoiandama serikali yetu utakwisha?

Unaweza kuueleza vipi uongozi unaopora nyumba za serikali, kisha kuanza kupangisha maofisa wa serikali kwenye mahoteli ya kitalii kwa mabilioni ya fedha za walipa kodi?

Sasa Watanzania wanajiuliza, kwa nini mikataba ya madini inatiwa saini kwa siri? Wanajiuliza kwa nini madini kama dhahabu, tanzanite n.k hayawaletei manufaa Watanzania, badala yake yanawanufaisha wageni na makuadi wao wenyeji?

Lakini Watanzania tunasahau wale tuliowakabidhi madaraka, wanahitaji kurejesha fedha zao walizonunulia uongozi. Hii ndiyo siri ya mikataba kuwekwa saini kwa siri vichochoroni na katika mahoteli ughaibuni.

Hivyo hakuna sababu ya kushangaa kwanini serikali inashiriki kwenye rushwa, kwa sababu hao tuliowakabidhi madaraka wanatumia nafasi zao za uongozi kufanya biashara za kifisadi ili pesa yao irudi katika kipindi kifupi, na wajilimbikizie nyingine za kununulia kura kwenye uchaguzi ujao.

Leo hii tunapigia kelele rushwa ndani ya CCM, lakini ile kashfa ya rushwa na ufisadi katika ununuzi wa rada, IPTL, BoT zimeishia wapi? Tunapigia kelele rushwa katika uchaguzi wa CCM wakati tumefumbia macho rushwa ya Richmond.

Mbona Watanzania tumekuwa taifa linaloongozwa kwa jazba za msimu, kwa maana kwamba tumekuwa wepesi kusahau haraka hoja ya leo mara jambo jipya linapoibuka.

Hebu turudi kwenye hoja yetu ya msingi, hawa wanachama wa CCM wanaolalamika kuwa wenzao wametoa rushwa, akiwemo Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Dk. Juma Ngasongwa na Katibu Mkuu wa CCM, mstaafu Philip Mangula ni vyema tuwasikilize.

Wanachosema ni kweli, kwa vile tunawajua ni watu wazito ndani ya CCM, hatuhitaji ushahidi mkubwa zaidi kwamba CCM inanuka rushwa.

Lakini mbona waheshimiwa hawa wanatetea haki hiyo ndani ya chaguzi za CCM tu? Mbona kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, udiwani, ubunge na urais hatukuwaona makada na wanachama wa CCM wakivalia njuga kupiga vita rushwa? Au mkuki kwa nguruwe mtamu, lakini kwa binadamu mchungu?

TAKUKURU sasa imewakamata na imesema itaendelea kuwakamata watoa rushwa na tayari imeishawafikisha mahakamani baadhi ya wabunge wa chama hicho na wengine kuwaachia, hilo ni jambo zuri na la kusifiwa kwa sababu unapokuwa na chama tawala kilichojaa wala rushwa, ni dhahiri kitazaa serikali ya wala rushwa.

Lakini TAKUKURU mbona haikufanya hivyo kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka juzi? Au wanafanya hivyo kwa sababu Rais Jakaya Kikwete kasema hataki rushwa? Je, Kikwete asingesema wangefanya kamatakamata hiyo?

Jambo jingine ambalo ni jema lililotokana na uchaguzi ndani ya CCM, limetuonyesha kwamba kile ambacho CCM imekuwa ikiwashutumu wapinzani kuwa wanaking’ang’ania kimejidhihirisha kuwa kweli, kwamba kumbe hata miongoni mwa wanachama wake wakiwemo viongozi ni walafi wa madaraka.

Hawakubali kung’atuka, wanahodhi vyeo ndani ya CCM kama vile wameumbiwa na Mungu vyeo hivyo na hakuna mwanachama mwingine mwenye haki ya kuvishika vyeo hivyo.

Inashangaza kwa Katibu Mkuu mstaafu wa CCM - Taifa, Philip Mangula, ambaye alitangaza kung’atuka katika siasa kwenda kugombea uenyekiti wa CCM Mkoa Iringa, pia wapo ambao walikwishakuwa na nyadhifa za Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Katibu Mwenezi Mkoa au Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa zaidi ya miaka kumi, lakini bado wanang’ang’ania na kugombea tena.

Ingawa ni haki yao kugombea, lakini wanaong’ang’ania kufanya hivyo ili kulinda maslahi binafsi, hawa kamwe hawapaswi kuvumiliwa.

Kimsingi matokeo ya vigogo kugaragazwa, ni karamu ya wapiga kura, ni ushindi kwa wanademokrasia ndani ya CCM.

Lakini pia inawezekana ikawa hizi ni dalili za mwanzo za chama hiki kumeguka na kuwa
katika kambi mbalimbali zinazogombea madaraka, ikizingatiwa kuwa wanamtandao wana haraka ya kujijenga na kutwaa hatamu za uongozi wa chama wakati wakongwe hawajawa tayari kung’atuka.

Uchaguzi wa CCM haujaonyesha kama chama sasa kitakuwa bora kuliko kilivyokuwa awali, ubora wa viongozi wapya bado haujaonekana, hivyo hatuna sababu ya kuwaweka katika mizani ya juu kwa sifa, hatutajua wanatofautiana nini na waliowatangulia.

Nashawishika kuamini kuwa, viongozi wapya hawana agenda ya kuliletea taifa hili heri. Tunachokiona ni mabadiliko ya sura na jinsia, lakini wanachopigania ni kupata fursa ya kupora, kujilimbikizia mali na vyeo.

Kwani waziri kuwa mjumbe wa NEC, ni ajabu, kwa sababu haifahamiki atawasaidia vipi wananchi, kama si kujiimarisha ndani ya chama chake ili awe kwenye kinyang’anyiro cha urais?

Tunachokiona ni wabunge, manaibu waziri na mawaziri wengi kuomba uongozi ndani ya chama, hasa nafasi ya ujumbe wa NEC ili waweze kujilimbikizia madaraka vizuri, hawa nawaita walafi na hawana jipya, isipokuwa kuweka sawa matumbo yao.

Natuma salamu zangu kwa wanasiasa wakongwe walioangushwa kwenye uchaguzi huu, akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani na Mbunge wa Mufindi Kaskazini, Joseph Mungai, ambaye amekuwa mwanachama wa TANU tangu mwaka 1960 hadi 1977 na mwanachama mwanzilishi wa CCM .

Pia amewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo kwa miaka 37 sasa, pamoja na nyadhifa nyingine za juu alizowahi kushika tangu serikali ya awamu ya kwanza mpaka sasa.

Pia Philip Mangula, aliyekuwa mwalimu wa siasa katika kilichokuwa Chuo cha Itikadi Kivukoni, baadaye Mkuu wa Mkoa na kisha akawa Katibu Mkuu wa CCM Taifa kwa kipindi chote cha uongozi wa Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Benjamin Mkapa. Na wengine wote waliongushwa katika kinyang’anyiro huku wakiwa wamekaa madarakani kwa muda mrefu, someni alama za nyakati!

Nawapa pole kwa vile ninyi ni wahanga wa ari, nguvu na kasi mpya. Msife moyo, kwani hao waliowagalagaza nao siku yao inakuja, waswahili wanasema “mwosha huoshwa, tena akioshwa hulipuliwa”. Kama waliwaondoa kwenye kinyang’anyiro kwa hila, basi ipo siku nao watafanyiwa hivyo hivyo au zaidi ya hivyo.

Mungu Ibariki Afrika, Mungu inusuru Tanzania.

0755 312 859;katabazihappy@yahoo.com;
www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Septemba 16,2007

KWANINI WATU WANAHAMA VYAMA?

Na Happiness Katabazi

KILA penye nguvu hasi, pana nguvu chanya, kwa hiyo kila penye mrisho pana mrejesho.

Ukiweka nadharia hiyo ya kisayansi katika suala la watu kuhama kwenye vyama vyao vya siasa, ni dhahiri kwamba kama kuna watu watahama CCM kwenda vyama vya upinzani, basi ni lazima kutakuwepo na watu kuhama vyama vya upinzani kwenda CCM.

Leo nazitaja sababu ambazo nimezigawa kwenye makundi matatu ambayo binafsi naamini yamekuwa yakisababisha watu kuhama CCM kwenda kujiunga na vyama vingine.

Kundi la kwanza ni waliohama CCM , waliona kule hapatoshi, hapafai au hapawawezeshi kufanya mambo au mabadiliko waliyotaka kwa masilahi ya nchi yao.

Kundi la pili ni kwa sababu watu hao walishindwa kutekeleza misingi, malengo na nidhamu ndani ya CCM, kwa hiyo chama hicho tawala kikawatema na wao wakaona kwa sababu wametemwa, wakaamua kujiunga na upinzani.

Kundi la tatu, ni walioona kuwa walipokuwa CCM hawakuwa na fursa au matumaini ya kujiendeleza kimasilahi au kupanda juu kisiasa.
Sasa makundi hayo matatu yapo kwenye vyama vya upinzani kuelekea CCM.

Kwenye vyama vya upinzani kuna jambo la ziada kwamba kwenda CCM ni fursa mpya ya wao kupanda juu au kujineemesha kimasilahi, kwa kuwa ukiondoka upinzani na kwenda CCM, utaridhisha wale walio chama tawala kwamba wameweza kubomoa upinzani.

Ikumbukwe mtu akitoka CCM kwenda kujiunga na upinzani, sifa ni wapinzani wameweza kuibomoa CCM. Ebu tujiulize pande hizi mbili kifikra ziko sawa?

Si sawa kwa sababu mwanasiasa ni mtumishi na utumishi huo utatukuka tu kama utatumikia masilahi ya umma. Hivyo kundi lile la pili na la tatu, ambayo nimeyataja hapo juu, yasingekuwepo tungekuwa na kundi la kwanza, basi.

Lakini ukweli ulio wazi, hivi sasa watu wanahama vyama kwa sababu ya dhiki zao walizoamua kuzifungulia feni, ukosefu wa nidhamu, ubinafsi, ulafi wa madaraka, yaani mtu anataka miaka yote awe kiongozi, siku akikosa uongozi anahama chama.

Lakini sasa kiupembuzi, tuliangalie jambo la watu kuhama vyama kwa njia nyingine. Mtu au kikundi kinaweza kuhama na kujiunga na chama kingine ili kukiteka au kukiharibu chama wanachohamia au kukiimarisha.

Katika kuliangalia hili, tuiangalie Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambayo inamruhusu mtu kuchagua chama anachokitaka kujiunga nacho na hakuna atakayelazimishwa kujiunga na chama asichokitaka.

Kwa hiyo, waliohama kwenye vyama vya upinzani, tunaweza kuwaweka kwenye makundi hayo matatu niliyokwisha kuyataja hapo juu kwenye makala hii.
Na ili kuthibitisha hayo makundi, rejea sababu mbalimbali walizotoa wanachama waliohama vyama vyao.

Ni mara chache mno kusikia mtu aliyehama chama na kusema sababu yake ya msingi ni kutekeleza haki yake ya kibinadamu ya kuchagua chama anachokitaka.

Dk. Masumbuko Lamwai, ambaye hivi sasa amefungiwa kufanya kazi ya uwakili na Mahakama Kuu ya Tanzania, Mei mwaka huu, baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kukiuka maadili ya uwakili, enzi hizo alipokihama Chama cha NCCR –Mageuzi kwenda CCM, alisema alirubuniwa na aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho wakati huo, ambaye ni Mwenyekiti wa TLP sasa, Augustine Mrema, na atazunguka nchi nzima kubomoa mageuzi kama alivyoshiriki kuyajenga.
Na zawadi aliyopewa Dk. Lamwai muda mfupi tu baada ya kurejea kwa kishindo CCM ni ubunge wa kuteuliwa.

Aliyekuwa Mweka hazina wa NCCR-Mageuzi enzi hizo James Nyakyoma, alipohamia CCM alisema anarudi nyumbani, akimaanisha CCM, kwa kuwa kule kwa wana mageuzi kuna baridi kali. Na wengine wengi walitoa kauli tofauti.

Nitakuwa sijakosea kama nikisema kauli hiyo iliyotolewa na Dk. Masumbuko Lamwai, si ya kiungwana, kwa kuwa kauli yake hiyo inaonyesha alivyokuwa ameahidiwa ubunge na kutaka kubomoa mageuzi yaliyojengwa kwa nguvu na akili nyingi za Watanzania, ambao waliweka maisha yao rehani.

Jamii inayotuzunguka inakuwa na kasumba ya kulaumu mno, si kwa medani ya kisiasa pekee, tena bila kuangalia hali halisi ya utendaji wa kisiasa.

Kwa maana gani? Watu wanapenda kuamini kwamba kila mwanasiasa awaye chama tawala au vyama vya upinzani analipwa na serikali.

Wanapomuona mwanachama au kiongozi wa CCM wanajua analipwa, jambo ambalo si kweli. Wanamuona kiongozi wa upinzani wanajua analipwa na serikali kupitia chama chake.

Hizi ni fikra potofu ambazo hazina ukweli wowote, kwa sababu viongozi wengi wa vyama vya siasa hawalipwi mishahara na wachache tu waliopo CCM na vyama vya upinzani vinavyolipwa ruzuku ndio wanaweza kulipwa hata posho.

Ukitaka katibu wa CCM awe na maisha ya uhakika, inabidi ateuliwe kuwa mbunge ili apate mshahara na posho. Je, makatibu wa vyama vya upinzani nao mbona hawajateuliwa kuwa wabunge ili nao wawe na maisha ya uhakika?

Wananchi wengi wana fikra nyingine potofu, wanafikiri mazingira ya utendaji wa kazi za siasa ni sawa kwa vyama vyote, wanasahau kwamba kuna vyama vinavyopata ruzuku na visivyopata ruzuku.

Wanasahau kwamba ukubwa wa ruzuku unategemeana na kura na nafasi ambazo chama kinapata kwenye uchaguzi. Kwa hiyo uwezo wa chama kutumia ruzuku kuendesha shughuli za siasa utakuwa mkubwa au mdogo kutokana na ruzuku. Na chama kisicho na ruzuku hakitakuwa na uwezo wowote ule.

Wananchi wanasahau pia kuwa chama tawala kina maanisha kuwa na uwezo wa kujichotea fedha katika serikali kwa visingizio mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuanzisha makampuni ya kifisadi ambayo hupewa mikopo isiyo na dhamana na serikali na kisha kuzifilisi kampuni hizo kwa visingizio mbalimbali baada ya kufaulu kuchota mabilioni ya fedha za wananchi.

Pia wananchi wanasahau ukweli kwamba wafanyabiashara wakubwa wengi hudhamini na kufadhili chama tawala ili wapewe misamaha ya kodi, wapewe hati na serikali inayowatambulisha kwamba wana rekodi nzuri ya kulipa kodi na mizigo yao hata ikiwa ni ya magendo haitakaguliwa na wapewe tenda nono za serikali.

Kutokana na hayo yote, ni rahisi kwa chama tawala kokote duniani kurubuni na hata kununua viongozi kutoka vyama vya upinzani kwa kuwa fedha na vyeo inavyo.

Kwa ujumla viongozi wengi walio kwenye vyama vya upinzani hawana kazi, biashara zozote na pia hakuna jinsi ambavyo wanaweza kujipatia riziki yao kutokana na kazi yao ya kisiasa.

Hili ni jeshi la kujitolea, wananchi wanatizamia hawa wajitolee kwa kiwango gani na mpaka lini? Na je, wakati wa kujitolea, wao na familia zao wanaishi vipi?

Tusipofikiria hilo, siasa za upinzani Afrika lazima zianzie msituni, hiyo ndiyo njia pekee ya kuharakisha mchakato wa mageuzi ya wale walio msituni kuja kuwang’oa walio madarakani kabla ya wapinzani kudhoofu kwa njaa.

Mwandishi wa makala hii anapatika kwa simu 0755 312 859;barua pepe ;katabazihappy@yahoo.com ; na kwenye tovuti ya www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima Jumatano, Septemba 12, 2007