BABA WA TAIFA TUNAENDELEA KUKUENZI


Na Happiness Katabazi

MWALIMU Julias Nyerere Baba wa Taifa letu,leo tunaadhimisha miaka nane tangu ulipotutoka Oktoba 14,1999, na tukakupumzisha kwa amani katika Kijiji ulichozaliwa cha Butiama.

Tunaendelea kukuenzi baba japo kwa staili mbalimbali.Tukikuita baba kwa sababu wewe ni mwasisi wa taifa letu la Tanzania .Baba,ulikuwa Mwalimu wetu na hata leo hii inaendelea kutufundisha katika yale yote uliyotuusia.

Nakuomba baba uchungulie toka uliko utuangalie hapa duniani katika taifa lako la Tanzania uone tunavyokuenzi hususan katika yale mambo kuntu(masuala mazito) sana uliyotufundisha na kutuhusia.

Wasia wako uliukita katika mtindo wako wa maisha binafsi,uongozi wako uliotukuka,matamshi na matendo yako.Miongoni mwa mambo uliyotuusia yanahusu elimu.Ulipenda watu wote wapate elimu na ukatuambia kila apataye elimu afanye nini.

Baba, uliwahi kutuambia kwamba;aliyepata bahati ya kusoma na akapata elimu ni kama mtu ambaye kijiji kimempa chakula chote kilichopo ili ale ashibe,avuke ng’ambo akakiletee kijiji chote chakula ,na asipofanya hivyo akajenga kiburi ni sawa na msaliti.Baba tunakuenzi kwa hilo.

Tunakuenzi kuanzia katika suala la elimu, ambalo baba ulibobea katika hilo ukiwa mwalimu na mwanafalsafa. Ulitufundisha falsafa ya Elimu ya Kujitegemea, uliyoiasisi mwenyewe; ulituusia kwamba elimu itujengee akili za udadisi.Leo tunakuenzi baba kupuuza kuwa wadadisi na wabunifu.Shuleni tunasoma kwa kukariri ili tufaulu mitihani.Baba,hata udadisi wa kisiasa umepigwa marufuku katika taasisi za elimu ya juu, ili tuwe mbumbumbu,mazumbuku,mzungu wa reli,wasioweza kuhoji lolote.

Hukuishia hapo ukaanzisha elimu ya watu wazima. Tunakuenzi baba kwa mipango na mikakati lukuki ya elimu.Baba, kupitia mipango mbalimbali ya elimu kuanzia ya msingi (MMEM), sekondari (MMES) na kadhalika, tumeongeza idadi ya shule nchini hususan za sekondari ambazo baadhi ya wajukuu zako wanaziita eti sekondari za Lowassa,na walimu wake wanaitwa ni ‘voda fasta’ bila shaka utamkumbuka huyu kijana wako,ndiye waziri wetu mkuu wa sasa.

Baba ukichungulia huwezi kuamini wingi wa shule hizo. Si unakumbuka idadi ya kata katika nchi hii uliotuachia. Tumekuenzi kwa kufungua sekondari kwa kutumia kanuni ya kata moja shule moja kama ulivyoacha tumekusudia katika sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 1995. yaani baba tumeanzisha shule nyingi kwelikweli kiasi kwamba hazina walimu.

Hilo baba usidhani ni tatizo si afadhali tunazo shule angalau tupate mahali ambapo wajukuu zako watakaa wapige soga kuliko kukaa bure nyumbani. Alafu baba kama tusingezifungua si wagombea uongozi wetu watakosa kura katika uchaguzi ujao.

Baba usijali masuala ya kitaaluma, tunaenzi uanasiasa wako kwa kuanzisha shule za kisiasa. Hata zisipozalisha wataalam, si wawekezaji wataendelea kuja na wataalam wao.

Tunajitahidi kwa kuhakikisha angalau kila shule tuliyoianzisha ina mwalimu mmoja,tena huyo huyo ndio mkuu wa shule, wasaidizi wake viranja. Kwa kawaida huyu mwalimu akisafiri usiwe na wasiwasi, anakabidhi mafaili ya ofisi na majukumu yote ya kufundisha kidato cha kwanza hadi cha nne kwa kiranja mkuu.

Usiwe na wasiwasi baba, viranja wanaimudu kazi hiyo vizuri sana, hii ni katika kuakikisha tunaienzi vyema taaluma yako ya ualimu kwa kuifanya si taaluma tena bali kichwa cha mwenda wazimu ambacho hata asiyejua kushika wembe anaweza kukinyoa, kwani baba, lazima mtu ajue kusoma ndio awe mwalimu?

Tunakuenzi baba kwa kuendelea kusoma tukiwa watu wazima na katika siku zote za maisha yetu. Chungulia baba uone jinsi wengi wetu walivyofanikiwa kusoma ukubwani na kujipatia shahada za juu kabisa. Tangia uondoke baba idadi ya wanao wenye shahada za falsafa (PhD) imeongezeka kwa kasi. Usishangae baba tumewezaje hilo, siku hizi kuna shahada tunazipata kiurahiiisi kwenye mtandao. Wenyewe baba wanaziita za ‘on line’.

Kwahiyo tunakuenzi baba kwa kurahisisha mambo, tunatafuta wenzetu wenye uwezo kichwani tunawapa visenti kidogo wanatufanyia ‘assignments’ na kutuandikia thesis, tunawasilisha kwenye vyuo vya ughaibuni, kisha kufumba na kufumbua tunaitwa ‘madokita’. Hicho cheo baba tunakitumia vilivyo kukuenzi katika siasa , maana kitaaluma hatuwezi kukitumia, samahani baba hatuna ujuzi wowote katika nyanja za shahada tunazotunukiwa.

Kukuenzi kwetu hakuishii hapo baba. Si unakumbuka ulituachia vyuo vikuu. Tumekuenzi si tu kwa kuviboresha bali tumeongeza na vingine vingi baba. Kwa sasa baba tuna universities zisizopungua therathini(30). Zaidi baba tumekuenzi kwa kuongeza kwa kiasi kikubwa udahili katika vyuo hivyo.

Hiyo ni mojawapo ya mikakati tunayoitumia kukuenzi kwa kuuporomosha kwa kasi ya roketi ubora wa elimu ya juu uliyotuanzishia baba. Kwa mfano baba katika chuo kikuu cha mlimani, tumekuenzi kwa kukigeuza mfano wa sekondari kuubwa!

Nikufafanulie kidogo baba, chungulia baba uone jinsi tulivyokuenzi kwa kuboresha mazingira ya kazi ya wafanyakazi wa chuo hicho kwa kuwarundika waadhiri na maprofesa watatu watatu au wawili wawili karibu katika kila chumba kinachofanana ofisi japo ni vyumba vidogo vidogo baba. Si unafahamu baba kwamba ualimu ni wito na uadhiri ni wito mkuu na afterall hatuna fedha zilizobaki baada ya kununua mashangingi hata tuwajengee ofisi zenye ‘vipupwe’ na nafasi.

Baba, fedha zimetutindikia tunawalipa mishahara ambayo haina tofauti sana na posho ya siku nne ya mheshimiwa mmoja anayetuwakilisha bungeni. Tumekuenzi enzi baba kwa kutambua kuwa siku moja ya mbunge aliyesinzia kwenye kiti cha kuzunguka kule dodoma ina thamani sawa na wiki nzima ya mhadhiri anayesugua kichwa na kula vumbi la vitabu akitoka jasho kuwaelimisha wanao.

Lakini baba, nisiseme sana maana wahadiri wenyewe baadhi yao wameamua kukuenzi kwa kuweka chaki chini na kukimbilia kuomba kura za wananchi. Wana ka-msemo eti siasa inalipa vizuri hasa ukiweza kupata takrima ya ‘kuinvest’ humo. Wengine wao wanakuenzi kwa kukalia kimya makosa ya watawala.

Wanachelea kufungua midomo yao wasije wakaikosa ahadi ya maisha bora waliyoahidiwa na kijana wako, japo wengi wao hawana nyumba za kuishi tuankaa nao mitaani ‘uswazi’ au ‘madongo poromoka’. Tunashangaa baba,wanawezaje kukaa chini wakafikiri na kuandika mambo ya akili,ya kisomi wakiwa wanaishi huku uswahilini kwetu ambako kila mpangaji ufungulia redio yake.

Wameshindwa baba kuandika chochote cha maana, wanakuenzi kwa kuwaelezea kila siku mawazo yako uliyoandika,wakitoka hapo wanahubiri na kukariri tu nadharia na mawazo ya wasomi wenzao wa nchi za ughaibuni. Si kosa lao baba, hivyo ndivyo watawala wamewataka wawe labda wasije wakahatarisha maslahi ya wenye nacho.

Baba, kwa kushindwa kuwajengea wasomi wetu hawa nyumba za kuishi, hatuwezi kukulaumu wewe,maana enzi zako nyumba zilijengwa pale mlimani zilizowatosheleza waliokuwepo. Na kwa kuona mbali baba ulitenga eneo kubwa la mlima ule kwa ajili ya ujenzi wa baadaye, bila shaka wa vyumba vya mihadhara, ofisi, makazi ya wahadhiri na wanafunzi wao.

Sisi baba, tumeamua kukuenzi kwa kulitumia eneo hilo ulilotutengea kwa staili mbadala kabisaa! Tumewekeza baba kwa kutumia sehemu ya eneo hilo kuwapa wageni makaburu; hapana ni ndugu zetu wa sauzi, wanyonyaji; sio – ni wawekezaji, makupe; no! ni wajasiriamali, tumewapa wajenge maduka ya kisasa ya bei mabaya kwa ajili ya wenyenazo kufanya shoping na walalahoi kwenda kujionea mambo! Usishangae baba, katika maduka hayo miwani ya jua bei yake ni sawa na mshahara wa kima cha chini ongeza noti kadhaa!

Tunaendelea kukuenzi baba kwa kutojali tena mwanafunzi wa chuo kikuu anaishi wapi,ni mtu mzima atajua mwenyewe. Anasomasomaje ‘madesa’ au vitabu shauri yake, anakula au ‘anadeshi’,kalala pazuri au ‘kabebwa’ no bode keaz. Samahani baba hiyo misamiati mitatu hukutuachia,imetungwa na wasomi wenyewe kutokana na maisha magumu yanayowakabili kutokana na harakati za kukuenzi.

Madesa wanasema ni makaratasi ya kuokoteza yanayofanana na kile kilichomo kwenye vitabu wasivyoweza kuvipata; kudeshi baba ni kushinda bila kula nakokufanya msomi ili aweze kumudu uchangiaji wa gharama za elimu ya juu. Wanachangia baba kwa mujibu wa sera iliyotungwa na wale wanaokuenzi kwa vile uliwasomesha bure elimu bora,ukawalisha bure chakula bora, ukawapatia vitabu bora na walimu bora. Wanakuenzi baba kwa kutanguliza adjective bora kabla ya nomino.

Baba, kule Dodoma ulikotuambia viongozi wetu wahamie wakakuenzi kwa kukataa kwenda huko hadi leo,sasa tunapatumia kukuenzi kwa mtindo mpya. Tumeanzisha Chuo Kikuu kipya huko. Hatukupata shida ya majengo ya kuanzia, tumetumia yale yale ambayo waliyatelekeza uliowaagiza waame Magogoni waende Ugogoni.

Eeh, tumetumia na mojawapo ya majengo ya chama ambayo awali kilikataa kuyarejesha kwa umma baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama ulivyotwambia visiwe utitiri,mpaka sasa havijawa utitiri baba, tunavyo kumi na saba tu japo vingi vina tatizo la utapiaruzuku.

Baba, ulituachia uhuru wa kutoa kauli na ukavifanya vyuo vikuu mahali huru pa kujieleza. Tunakuenzi baba kwa kuua moyo huo. Kila anpojitokeza anyethubutu kuwa jasiri kama wewe tunamnyamazisha ili wewe tu ubakie mwenye kuenziwa. Kuna mjukuu wako mmoja, labda humjui vizuri kwani ni mdogo sana. Tumemwekea breki ya kuongea kwa niaba ya wananchi katika chombo cha uwakilishi. Haikutosha baba,juzi tu alialikwa chuo kikuu,lakini tukafanikiwa kumdhibiti maana tuliona ana fikra huru kama zako tukakuenzi kwa kumkatalia kuingia chuoni. Chungulia baba umwone huyo kijana.

Vilevile katika uwanja huo huo wa elimu,tunaendelea kukuenzi kwa kufanya midahalo isiyo na tija. Tunatajataja jina la lako,tunakunywa maji ya kilimanjaro,tunagahawana posho,tayari tunakuwa tumekuenzi.

Baba ulituhusia pia tuwe na umoja wa kitaifa,watoto wa baba mmoja wasiokuwa na ubaguzi wa kidini wala kikabila.Baba ukasema katika karne ya 20,wanangu mnazungumzia ukabila,ukatuuliza iwapo tunaka kutambika?Tunakuenzi baba,hasa linapokuja suala la uchaguzi.

Ni hivi juzi tu tu limchagua Rais wa Awamu ya Nne,Jakaya Kikwete, bila wewe kuwepo.Tunakuenzi kwa kukataa ukabila, lakini wapo baadhi ya wanao wanaouendekeza.Baba unamkumbuka yule motto wako kipenzi Dk.Salim Ahmed Salim? Wapo waliompigia kumbo asigombee kiti cha urais kwa sababu ya asili yake, ngozi ya rangi yake.Eti yeye ni Mwarabu,eti alikuwa mwanachama wa Hizbu!

Pia yule mwanao Joseph Mungai ambaye ni waziri tangu enzi za utawala wako hadi sasa, naye ameambia yeye si Mtanzania ni ‘mkikuyu’, na aliambia hivyo baada ya kugombea nafasi ya NEC kupitia mkoa Iringa ambapo mwaka huu chama chako ulichokiasisi kinafanya uchaguzi mkuu.

Dhambi ya pili baba tumetenda,utusamehe na utuombee kama ulivyotuahidi kabla hujatutoka, kuwa unajua tungelia sana baada ya kifo chako,lakini kwamba utatuombea.

Vile vile baba ulituasa kwamba serikali haina dini,na kila mtu awe na uhuru wa kufuata dini anayoipenda.Kwamba dini kamwe isitutenganishe.Baba ulikuwa Mkatoliki mwaminifu, lakini uliwapenda na kuwaheshimu wanao Waislamu na hata wengine waliofikia wakakubatiza jina la Musa!

Baba mwaka huu tunakuenzi kwa kukwaruzana kidini.Tunabisaha juu ya Mahakama ya Kadhi na kunyoosheana vidole machini huku chama ulichokiasisi mwenyewe kikiwa ndicho kinachokonoa udini huu kwa kuwaahidi dada na kaka zetu wa Kiislamu kwamba kina sera ya kuanzisha Mahakama ya Kadhi.Tuombee baba,amani uliyotuachia tusiipoteze kwa kuanzisha taasisi ambazo hukuturithisha na ambazo ni hatari.

Baba katika suala la uchumi tunaendelea kukuenzi kwa kuuza kila raslimali uliyotuachia. Ahsante baba kwa kutuachia mali. Alhamdulilahi hatujaanza kutoana roho – yarabi kwa mali ulizoacha baba. Ila tumeziuza kisawasawa.
Baba zile nyumba ulizotuachia ukasema wakae humo watumishi wa umma tumeziuza na pesa tulizopata tukazitumia kuwapangishia viongozi wetu vyumba katika mahoteli makubwa. Si unaona mwenyewe tulivyo na akili.

Baba yale mabenki uliyotuachia tunaendelea kuyauza, viwanda tunaendelea kuvinadi, mashirika hatujaacha kuyapiga bei, mahoteli hatujachoka kuyabinafsisha na madini tuayatoa zawadi kwa marafiki zetu wa ughaibuni kwa njia ya mikataba yenye kamrabaha. Baba, katika miaka michache ijayo almasi,dhahabu,tanzanite,,bati, uranium na vito vingine vya thamani ulivyotuachia tutakuwa hatunavyo tena. Hizo zote ni harakati za kukuenzi maana ulituachia mali nyingi kiasi kwamba zinatulewesha.

Tunakuenzi baba hata katika suala zima la uongozi bora.Baba,unamkumbuka yule kijana wako uliyempenda sana kwa tabia yake ya utanashati na usafi wa mwili na roho,hata akaitwa Mr.Clean?Naye amekuenzi hivyo.

Amekuenzi Baba kwa kutuhumiwa kufanya Ikulu ni mahala pa ujasiriamali japo wewe ulimhusia kwamba Ikulu ni mahala patakatifu.Uliuliza baba, ikulu pana biashara gani?’ Swali lako .Baba kijana wako kakuenzi kwa kulijibu kwamba ikulu pana biashara ya kutumia dhamana ya ukuu wa nchi kujipatia mikopo bila kuulizwa ulizwa ili ujasiriamali.Tunakuenzi baba,kwa kuisigina vilivyo sheria ya Maadili ya Viongozi.Baba,kalianzisha kaka, wadogo zake unatarajia wafanyeje?

Na wadogo nao wameamua kukuenzi.Wewe baba ulituambia ,’watu safi katika nchi hii wapo chungu nzima’ utuwie radhi baba mpaka sasa hatujaweza kuwatambua.Ila angalau tumewatambua hao wengine.Tumekuenzi baba kwa kuunda timu ya mchezo wa ufisadi, inaitwa”The list of shame’ aka “Jk eleven’.Hii timu inakuenzi vizuri sana baba,kwa kuongeza harufu chafu uliyoisikia uliposema ‘kanchi kananuka rushwa!’. Siku hizi baba siyo kunuka tu, bali ka-nchi kamevunda ufisadi’ kuanzia sebuleni hadi jikoni.Yaani baba huwezi kuamini, uvundo umefika hadi kwenye jiko la uchumi(Benki Kuu ya Tanzania).

Baba ungekuwepo endapo wala rushwa wangetiwa hatiani na vyombo vya sheria ungeamuru wachapwe viboko wakati wakuingia gerezani na wakati wa kutoka ili wakawaonyeshe wake zao makovu ya bakora hizo.Lakini sasa hakuna wakuamuru hilo.

Tunakuenzi Baba, tukikumbuka ulitufundisha hata kutunga mashairi, mfano ni tunaposoma kile kitabu chako cha ‘Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania’.usibishe baba ebu soma shairi hili uone tunavyofuata nyanyo zako:

“Mkataba wa Buzwagi, alisaini Karamagi,
Umezua hoja nyingi,tena hoja za msingi
Kulikoni Karamagi,akaiuza Buzwagi
Mbona hanywi Konyagi,na wala havuti Bangi”?

Buzwagi unaijua baba;ni eneo moja lenye utajiri wa madini uliyotuachia, kijana wako Karamgi kawagawia wazungu kwa kusaini mkataba ambao ukisoma baba utalia machozi.

Baba tunazidi kukuenzi kwelikweli, hadi ndani ya chama ulichotuachia.Baba ulituambia chama kiwe na matawi imara.Tumekuenzi baba kwa kuimarisha matawi hayo., ila si kama yale matawi ya kizamani, tumeanzisha matawi yanayoendana na wakati.Nikutajie matawi hayo Baba japo machache?Haya…moja linaitwa,mtandao-maslahi,jingine mtandao-halisi, la tatu mtandao-matumaini, la nne mtandao-dhuluma—yako mengi baba.

Halafu Baba unajua tunakuenzije kuhusu suala la alama za chama?Baba uliturithisha jembe na nyundo ukasema kwa maana hiyo chama ni cha wakulima na wafanyakazi.

Lakini tumekuenzi Baba, kwa kugundua kwamba hizo alama haziendi na wakati.Hatujazifuta,ila tumekigeuza chama kuwa cha wenye uwezo ,wafanyabiashara na mafisadi.Baba, hakuna wa kukwambia kwamba hili si kweli.

Akikwambia hivyo muulize mweka hazina wa sasa wa chama ni mkulima au mfanyakazi?Je hayumo kwenye Jk eleven? Muulize nini kilitokea kuhusu ufisadi wakati wa uchaguzi ndani ya chama.

Baba , watoto wadogo ambao hakukuona,wanachanganywa sana juu ya sura yazo.Kuna sanamu za ajabu kabisa zinachongwa na kuwekwa mitaani sasa, hadi wengine wakubwa wanakaribia kuisahau sura yako halisi.Wahurumie hao baba, njaa zao zinawatuma vibaya.

Baba, niruhusu niwakumbushe wanao wote kwamba hatuwezi kujivunia wewe kuwa baba yetu na kusema kwamba tunakuenzi, wakati kile tunachokifanya ni kinyume cha mafundisho,wasia na imani yako.

Tuombee baba, ili mfumo wa elimu yetu ukuenzi,ili mfumo wa uchumi wetu nao ukuenzi na mfumo wa siasa ukuenzi.Kadhalika viongozi wetu wakuenzi kwa maneno yao,mawazo yao na matendo yao.

Baba ,viongozi wetu inabidi wakumbuke maneno ya Yesu Kristo aliyowaambia watu wa taifa la Uyahudi,kwamba “Hamjui kwamba mnaye baba mwingine,ninyi si watoto wa Ibrahim,ninyi ni watoto wa ibili,kwa kuwa ibilisi amekuwa mwongo na mnafiki tangu mwanzo,nanyi mnayatenda hayo hayo kama baba yenu”.

Sasa baba ,wanao tunapojivunia ubaba wako,baadhi ya yetu wanaye baba mwingine ambaye si wewe!Baba yao ni beberu(bepari aliyekomaa),kwani bepari amekuwa mnonyaji,tangu mwanzo hata leo hii,angali akinyonya kwa kutumia utandawazi,unafsishaji na kuendekeza masilahi binafsi.

Viongozi wetu wa leo mnamuenzi baba yupi?Baba Mungu alikuumba na ukiisha kuifanya kazi yake hapa kwetu,akakutwaa.Jina la Bwana lihimidiwe na aipumzishe roho yako mahali pema peponi.Amina.

0755 312859:katabazihappy@yahoo.com;www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili , Oktoba 14, 2007

KWANINI MAWAZIRI WANAZOMEWA?

Na Happiness Katabazi

MTAJI Mkubwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake ni uoga na ukondoo wa Watanzania. CCM imekuwa ikidumisha ukondoo huo ili wananchi wabaki mbumbumbu wasio na uwezo wa kuona ukweli wa mambo na kuweza kukosoa sera, sheria na vitendo viovu wanavyofanyiwa na serikali.

Ningependa kuwapongeza Watanzania kwamba wameweza kuthibitisha katika wiki mbili hizi kwamba wamepevuka, si mbumbu tena kama baadhi ya viongozi walivyofikiria.
Wananchi wa Tanzania wameweza kuelewa hoja ya ufisadi iliyotolewa na Watanzania wenzao ambao nao wanaipenda nchi yao.

Pili, Watanzania wameweza kuwaadhibu viongozi wa serikali na CCM waliokwenda mikoani kubeza hoja ya wapinzani kwa kuwazomea adharani. Nawapongeza sana wananchi hasa wa Mkoa wa Mbeya.

Viongozi wa serikali wamekuwa wakitisha na kusema kwamba wapinzani ni wachochezi na hata vyombo vya habari vilivyoandika habari za ufisadi vimeitwa kuwa ni vya uchochezi.

Hii inamaanisha kwamba serikali ya CCM ina amini kwamba wenye haki ya kuwaambia Watanzania ukweli ni wao pekee.

Kwa hiyo, mtu mwingine yeyote akienda kuwaeleza wananchi taarifa zozote zile anaitwa mchochezi, mzushi, hana kazi za kufanya, asiye na hoja.

Lakini upo usemi unaosema kwamba unaweza kuwadanganya watu wote kwa muda fulani, lakini huwezi kuwadanganya watu wote kwa muda wote, kwani ukweli unaposimama, uongo hujitenga.

Sisi Watanzania tuna uwezo sasa wa kuchambua mchele na pumba, si mahala pake sasa kulishwa kasumba na propaganda za CCM wakati fedha zetu zinaporwa, mali na rasilimali zetu zinafujwa na nchi inakwenda mrama na gharama za maisha zimepanda.

Jambo la kusikitisha ni kwamba serikali inawasikia wageni au wafadhili, lakini haiwasikilizi wananchi wake. Kwa hiyo serikali imeanza kuzijibu hoja za wapinzani kijuujuu baada ya wafadhili kuchachamaa.

Hii inamaanisha kwamba wafadhili wasingechachamaa, hoja za wapinzani zingepuuzwa, ukweli ungefichwa na ufisadi ungeendelea.

Kipimo cha heshima ya serikali yoyote duniani na viongozi wake, ni jinsi wananchi wanavyowapokea na kuwa tayari kuwasikiliza. Wimbi la zomeazomea ni ‘tsunami’ inayoizengea CCM na serikali yake.

Ipo hatari serikali hii ikasombwa na tsunami hiyo, kwani wananchi wanapokosa imani nayo, hawaiheshimu tena na wala viongozi wake hawaonekani kuwa viongozi wenye heshima.

Ukiangalia uendeshaji wa dola, mihimili mikuu ya dola imepoteza sifa. Mhimili wa kwanza ni Bunge, limepoteza umaarufu na sifa yake baada ya kujigeuza kuwa kama kamati tendaji ya CCM.

Matukio kadhaa ya hivi karibuni, yamedhihirisha kuwa Bunge letu kwa kiasi fulani halisikilizi hoja wala kufuata kanuni, kwa kuwa CCM ina vita ya kuangamiza wapinzani.

Kumbe fursa ya sauti ya wanyonge kusikika bungeni imepotea na mfano halisi ni jinsi Bunge lilivyojadili hoja ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, kuhusu utata wa mkataba wa Buzwagi.

Mbunge huyu kijana alifikisha hoja bungeni akimtuhumu Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, alivyotia saini mkataba huo hotelini nchini Uingereza.

Basi, hata kama Bunge lingeona hakuna haja ya kuunda tume huru ya uchunguzi wa mkataba ule, basi hoja hii isingesababisha Zitto kuadhibiwa, maana hakuwa amemdhalilisha mtu.

Mhimili wa pili ni serikali, nao umepoteza sifa kwa kujiingiza kwenye kashfa nyingi za kiutendaji, kashfa za namna hiyo zinaashiria ufisadi mkubwa ndani ya serikali yetu.

Mhimili huu una kashfa nyingi, ikiwemo kashfa ya IPTL ambayo hadi sasa tunaendelea kuilipa kampuni hiyo dola 100,000 kila siku, kwa mradi wa ovyo, na hatujui ni lini kashfa ya Richmond itachunguzwa ili wananchi waambiwe ukweli.

Kwa mtazamo wangu, hata chombo cha kukabiliana na rushwa kimekuwa chombo cha kusafisha na kupaka rangi ufisadi, kama kilivyofanya kwenye Richmond, baada ya Watanzania kuteseka sana kwa kukosa umeme na fedha nyingi kulipwa kwenye makampuni yasiyo na uwezo wa kuzalisha umeme.

Na hata hatujaambiwa nani amewajibishwa, tulichoambiwa ni kwamba hapakuwepo na rushwa. Hivi nani anaamini maelezo hayo?

Takukuru sasa inachunguza kashfa ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) na mkataba wa Buzwagi. Hivi Takukuru ina ubavu wa kuchunguza kashfa hizo? Watanzania tungoje tu kuambiwa Buzwagi na BOT hapakuwa na vitendo vya rushwa wala ufisadi.

Sasa matokeo ya aina hii ya utendaji wa dola ndiyo yanayopelekea wananchi kukosa imani na serikali, CCM na viongozi wake na kuamua kuwazomea na kuwapiga mawe.

Kama viongozi wetu wa serikali wasipobadili tabia na wakashirikiana na wananchi kutokomeza ufisadi na kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli, nasisitiza tena viongozi wa CCM na serikali wasije kushaanga wakicharazwa bakora mitaani.

Wananchi wamechoshwa na ufisadi unaofanywa na baadhi ya viongozi, wamechoka na uroho wao wa mali usio na kipimo. Na hakika nasema, wakiacha kuzomea, watabeba bakora na kuanza kuwacharaza viongozi wetu, hatua ambayo sitaki tuifikie.

Mungu Ibariki Afrika,Inusuru Tanzania

Chanzo:Gazeti la Tanzania la Alhamis ya Oktoba 11,2007

WAANDISHI WA HABARI WAKIWA KAZINI


Pichani nipo na Mwanahabari mwenzagu toka gazeti la The Citzen,Bernad James, nje ya jesngo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam,kufuatilia wa kesi ya madai iliyofunguliwa Ijumaa ya Oktoba 5 mwaka 2007, na vyama vinne vya siasa dhidi ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. James ni mwandishi mwenzangu ninayeripoti naye kesi mbalimbali katika mahakama hiyo.(Picha na Kassim Mbarouk wa Gazeti la Mwananchi).

ZIARA ZA MAWAZIRI SI JIBU LA HOJA ZA WAPINZANI

Na Happiness Katabazi

HOJA ya wapinzani kuhusu tuhuma za ufisadi, ukiukwaji wa maadili kwa viongozi, ugumu wa bajeti na ufujwaji wa rasilimali za nchi, zimeichanganya Serikali kiasi cha mawaziri na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenda mikoani kujaribu kuondoa sumu hiyo.

Utetezi unaotakiwa utolewe na serikali si kwenda kuhutubia wananchi mikoani, ni kukaa chini na kuangalia wapinzani wametoa hoja zipi na serikali kuzijibu kwa vitendo na kitaaluma.

Mfano, Mbunge wa Karatu Dk. Willibrod Slaa, (CHADEMA) anaposema kwamba Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), alinyimwa mikataba ya ujenzi wa minara pacha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), hawezi kujibiwa kwa mawaziri, manaibu wao na makada wa CCM kwenda kuwahutubia wananchi.

Nasisitiza na kutoa ushauri wa bure kwa Serikali, dawa ya hoja za wapinzani si kuwatoa viongozi hao wa serikali katika ofisi zao na kwenda kutangatanga mitaani kuhutubia wananchi, tena kwa kutumia fedha za walipa kodi na fedha za CCM wakati baadhi ya wana CCM wanalia njaa.

Na hata hivi karibuni vyombo vya habari viliripoti habari kwamba uchaguzi wa CCM Mkoa wa Mara ulishindwa kufanyika baada ya kukosekana kwa posho za wajumbe hadi kada mmoja na mfanyabiashara wa mkoa huo, kuokoa jahazi kwa kutoa mamilioni ya fedha zake kwa ajili ya posho za wajumbe wa mkutano huo na hatimaye ukafanyika.

Ziara hizo hazina maana yoyote zaidi ya ufujaji wa fedha za umma. Binafsi najiuliza kama ni kwenda kunadi Ilani ya CCM leo hii, ina maana wakati wa uchaguzi wa mwaka 2005, iIlani hiyo haikunadiwa, na kama haikunadiwa vizuri ni vipi CCM ilishinda kwa kishindo?

Serikali ijibu hoja na kama inaona wapinzani hususan Dk. Slaa amechafua jina la viongozi, basi akamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Hiyo ndiyo dawa ya kujibu hoja za wapinzani.

Dk. Slaa anaposema Kampuni ya Meremeta haimilikiwi kwa asilimia 100 na serikali, badala yake inamilikiwa kwa asilimia 50 na asilimia 50 iliyobaki inamilikiwa na Kampuni ya Trinex ya Afrika Kusini, je, uzushi uko wapi katika hili?
Je, hati ya Brela ya kutambua usajili wa kampuni hiyo uliofanywa kwenye visiwa vya wakwepa kodi huko Uingereza je, ni uongo?

Dk. Slaa ameuliza katika hoja yake kwamba, je, Serikali ya Tanzania haikushiriki kwenye ufisadi kwa kufungua kampuni ya wakwepa kodi, kwanini serikali haitaki kueleza ilipofungua kampuni Uingereza katika visiwa vya Ilse of Man ilikuwa inakwepa kodi ya nani?

Na je, ni halali kwa serikali yetu kuanzisha kampuni hizo zinazotuhumiwa kuwa ni za kifisadi? Hoja kama hii isipojibiwa vizuri Watanzania tutaichoka serikali.
Labda ni vizuri pia kuuliza Kampuni ya Meremeta ilifanya biashara gani kustahili kulipwa mabilioni kutoka BoT na iliingizia taifa faida gani?

Sisi wananchi wa kawaida tukiamini kwamba Kampuni ya Meremeta iliundwa kwa madhumuni ya kuchota fedha za BoT na kuzipeleka nje ya nchi, tutakuwa tumekosea?
Kwaninii hata ilipofilisika hatuambiwi nani aliteuliwa kama mufilisi wa kampuni hii? Kwani serikali haijaeleza kuhusu madeni yote ya kampuni hiyo mufilisi.

Watanzania tunataka kujua, hiyo Trinex ya Afrika Kusini iliyolipwa kwa fedha za walipa kodi ni ya nani? Sasa haisaidii serikali kutapatapa na kukurupuka kujibu kashfa hii wala kuwahutubia wananchi hakutasaidia serikali kujikosha.

Hoja ya Dk.Slaa tumeielewa na hii ni mara ya pili nasisitiza inahijati majibu thabiti na si ya ‘mipasho’. Serikali ijue kwamba wananchi si mbumbu kiasi cha kutong’amua ukweli wa mambo.

Alipozungumza na waandishi wa habari Ikulu Dar es Salaam, Mzee Kingunge Ngombare-Mwiru, aliwabeza wapinzani na kusema hoja zao zimejaa uzushi, uongo na wana wivu, kwa sababu CCM iliwashinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, na sasa wanaona wivu kwamba serikali inatekeleza ahadi za kuleta maisha bora, imejenga shule nyingi za sekondari.

Kitu ambacho mzee Kingunge amesahau ni kwamba tayari serikali ipo madarakani na yeye ni waziri na hakuna mpinzani aliyekwenda mahakamani kupinga kutokuitambua serikali iliyopo madarakani.

Kwa hiyo, hoja ya Kingunge hata kama alitumwa na serikali kama alivyodai, ni ya kukurupuka na ailengi wala kujibu hoja ya vigogo wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Kwa kuwa hoja ya wapinzani ni ufisadi, wizi wa mali za umma na uvunjwaji wa maadili ya viongozi unaofanywa na viongozi wakuu wa ngazi za juu za serikali na CCM, jibu la mzee Kingunge liko nje ya mada.

Hata pale Kingunge alipo wadharau na kusema serikali ina mengi ya kufanya na kwamba haitawafuatilia wapinzani mikoani kujieleza kwa wananchi, tayari serikali hiyo hiyo ya kina mzee Kingunge imesalimu amri na imeteua timu yake ya viongozi kwenda kuzima moto wa wapinzani.

Kwani Mawaziri, Manaibu Waziri na Bendi ya TOT-Plus, Katibu Mkuu wa CMM Yusuf Makamba na makada wengine , wamepangwa mikoani wakijaribu bila mafanikio makubwa kujikosha mbele ya wananchi na kujaribu kukanusha hoja za wapinzani.

Kinachojidhiirisha ni jinsi serikali inavyojikang’anya katika suala hili. Haionekani serikali ina majibu yanayoeleweka kukanusha hoja za wapinzani. Hivyo kila kigogo aliyeguswa na tuhuma hizo anakurupuka na kutoa maelezo yake yanayopingana na vigogo wenzake kana kwamba serikali haina msemaji mmoja wa kueleweka.

Chakuchekesha zaidi ni pale baadhi ya watuhumiwa wa ufisadi walipotishia bila mafanikio makubwa kumshitaki Dk. Slaa, gazeti la Mwanahalisi na Mbunge wa Kigoma Kaskazini Kabwe Zitto.

Kitendo cha kutotimiza vitisho vyao kinaonyesha uwoga walionao wa siri nyingi zinazowahusu kufichuliwa mahakamani.

Tunawapa ushauri waheshimiwa watuhumiwa wa ufisadi kwamba wakubali kujiuzulu badala ya kungoja wananchi kufumuka kwa maandamano yanayoweza kusababisha ghasia na wao wenyewe kucharazwa bakora na umma wenye 'hasira takatifu'.

Ieleweke wazi kwamba japo Watanzania wanasemekana kuwa ni binadamu ambao nyonga yao ya hasira iliondolewa na wakunga walipozaliwa, itafika siku vifuko vyao ya nyonga vitajaa nyongo ya hasira takatifu na watakapoanza maandamano itakuwa ni vigumu kuwadhibiti.

Tunaamini bado nchi yetu ina viongozi angalau wachache wenye busara ya kutambua ukweli, hivyo kuwashauri watuhumiwa wa ufisadi kung’oka madarakani.

0755 312859;katabazihappy@yahoo.com;www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Alhamisi ya Oktoba 4,mwaka 2007