MIAKA MIWILI YA RAIS KIKWETE MADARAKANI:

MASWALI MENGI KULIKO MAJIBU
Na Happiness Katabazi

ALIPOINGIA Ikulu Desemba 21 mwaka 2005 Rais Jakaya Kikwete alikuwa mtu mwenye tabasamu lenye matumaini kwa taifa lake. Alikuwa anajivunia ushindi wa Tsunami wa zaidi ya asilimia 80.

Yeye alionekana ametimiza ndoto yake ya muda mrefu ya kuwa Rais wa Tanzania, ndoto ambayo ilififia mwaka 1995 aliposhindwa na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa.

Kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita Rais Kikwete alijizatiti kuwa rais wa taifa hili, inaelezwa alikusanya fedha na kujenga mtandao ili kushinda ndani ya chama chake na kushinda kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Pamoja na maandalizi hayo ambayo yaliingiza Taifa kwa mara ya kwanza katika matumizi makubwa ya kupindukia katika uchaguzi ilisadikiwa kwamba Rais Kikwete aliandaa timu ya wanamtandao, itakayompelekea Ikulu.

Miaka miwili sasa inatimia Ijumaa ijayo aiingie ikulu,Je Kikwete anatabasamu lilelile lenye matumaini kwa watanzania lenye kupatia maisha bora kila mmoja wao, milo mitatu kwa siku, ajira milioni moja kwa vijana,wanawake watawezeshwa?

Je wale wanamtandao wote walikuwa wakijitapa kuwa wameaidiwa vyeo na fursa za biashara wamevuna walichoaidiwa?.Na je watanzania waliompigia kura kwa asilimia 80 bado wapo nyuma ya rais wao?

Ili kujibu maswali haya yafaa kuiweka serikali ya awamu ya nne ya ari,nguvu na kasi mpya kwenye mizani na vitendo.Lazima tujue kama ahadi zile zilikuwa danganya toto au kweli na rais wetu na chama chake walikuwa wamejizatiti kuzitekeleza kwa vitendo.

Mtandao uliomweka madarakani una wana CCM na wasio wana CCM.Wasio kuwa wana CCM walijikuta wanakimbilia kadi haraka ili kujiweka imara kwenye mkao wa kula.

Na hao walikuwa wengi mno wenye elimu na wasiyo na taaluma na matapeli wa mtaani,wafanyabiashara, waandishi wa habari hata baadhi ya viongozi wa dini wote walijikuta wana matumani ya kufanyiwa hiki au kile kama walivyokuwa wakijitapa vichochoroni na kwenye mabar kwamba wameaidiwa na rais wetu.

Matokeo ya mategemeo haya yalikuwa kuteuliwa kwa baraza la mawaziri lenye wingi wa mawaziri kama darasa la chekechea.

Kweli mawaziri 61 ni wengi mno hawana tija kwa taifa ni kero,hasara kubwa na gharama.Hakuna jambo ambalo baraza hili kubwa limeweza kukamilisha katika kipindi hiki cha miaka miwili kwa sifa na unafisi ila baraza hili limejipatia sifa yakuwa wafalme wa matumizi ambao wamekiuka vigezo vyote vya matumizi makubwa ya fedha.

Kwa upande mwingine vyeo vya ukuu wa wilaya, Ukuu wa mkoa na makatibu wa kuu maana ni vichache mno kuwatosha wanamtandao walioaidiwa vyeo hivyo.

Hata tukiongeza vyeo vya mabalozi na wakurugenzi wa mashiriki bado haviwatoshi ,hivyo waliokosa wamekosa na waliopata wamepata,wanaomba ‘reshaffle’wanaomba lakini huo ndiyo ukomo wa mtandao.

Yawezekana tumejionea uroho na ugomvi wa madaraka ndani ya anachokiongoza rais wetu jambo ambalo alijawahi kutokea katika historia ya chama hicho tangu kianzishwe.
Wazee wamejikuta wakipigwa mweleka na vijana wadogo kwa jina la wanamtandao.Neno Mtandao limegeuka kuwa itikadi ya CCM ,ukiwa mwanamtandao unanafasi,ukiwa si mwanamtandao huna nafasi.

Kama watanzania wanajiuliza ni kwanini serikali ya awamu ya nne inaonekana kupoteza dira na sifa basi jibu watalipata kwa kuangalia taswira mpya ya CCM, chama hicho sasa ni zizi la viongozi wa ovyo ovyo na baadhi yao wapo kwaajili ya kujilimbikizia mali. Hiyo ndiyo CCM mpya tuliyonayo hivi sasa.

Tuhuma za ufisadi, miaka miwili ya uongozi wa rais Kikwete, aikupambwa na vitendo vya kikakamavu vinavyoliletea taifa tija kimaendeleo badala yake imekuwa ni miaka miwili iliyogubikwa na habari za vitendo vya ufisadi vinavyotuhumiwa kufanywa na viongozi.

Tulianza na kashfa ya mkataba wa Richmond ambapo wakati taifa linaumia kiuchumi kwakukosa nishati serikali ilijikuta ikipiga magoti mbele ya mafisadi waliotoka kujitoa mabilioni ya fedha kuleta vinu vya umeme hewa kutoka Marekani.

Mpaka leo kashfa hii haijapatiwa ufumbuzi.Inasadikika kuwa baadhi ya vigogo walio ndani ya serikali waliusika kwenye kashfa hiyo.

Imelichukua bunge muda mrefu mno kuunda kamati kuchunguza kashfa hiyo.Wakati kashfa ya Richmond ikitokea wananchi walijikuta wakilipukiwa na bomu jingine la ufisadi ambapo ilielezwa kwamba wanunuzi wa Rada iliyopingwa vikali na wananchi.

Inadaiwa kuwa walijipatia rushwa ya dola milioni 12 ambazo zinasadikiwa kuwa zilitolewa kama bahasha kwa vigogo ndani ya serikali.Hili nalo lipo na wala alijapatiwa ufumbuzi.

Kana kwamba kashfa hizo azitoshi hivi sasa tunazo kashfa mbili kubwa moja, ubadhirifu wa fedha ndani ya Benki Kuu (BOT) na nyingine kuhusu mikataba ya madini.

Kashfa ya BOT, ni ufisadi uliopita kipimo, hakuna Mtanzania anayeweza kuelewa jinsi gani taasisi hiyo ilijiingiza kwenye ubadhirifu kwa kiwango kile. Kweli kuwaambia wananchi kwamba vile viminara viwili vina thamani ya Sh milioni 523, ni jambo lisilowezekana.

Pia ukweli kwamba BOT imejiingiza katika bodi za makampuni yanayotajwa kuwa ni ya kifisadi ya Meremeta, Tangolg, Kagoda na Mwananchi Golg ambazo zimeingiza serikali kwenye hasara za mabilioni ya fedha za walipa kodi ni dhambi isiyosameheka.

Hata ilipogundilika Waziri wa Madini Nazir Karamagi amekiuka agizo la Rais Kikwete na kuweka saini katika mkataba wa madini unaolileta taifa hasara ya mabilioni ya fedha ni jambo lisilosameheka.

Tujiulize sasa sera ya awamu nne ni kuliangamiza taifa kiuchumi kwa ari,nguvu na kasi mpya? Haya siyo matumaini tuliyokuwa nayo tulivyompigia rais wetu kura katika uchunguzi mkuu wa mwaka 2005.

Inabidi sasa Rais Kikwete atueleze kama kweli yeye ni msafi na hana ushirika na hawa wanaoliangamiza taifa.Alisipofanya hivyo basi itakuwa alali kuamini na yeye ni mmoja wao, kwani mbona hatuoni Gavana wa Benki Kuu Daudi Balali akiguswa, mbona hatuoni Karamagi akiguswa?

Hata hivyo Rais Kikwete, akiwa anatimiza miaka miwili tangu aingie madarakani, napenda kumpongeza yeye binafsi kwa kuruhusu uhuru wa habari kupanuka katika muda mfupi tangu aingie madarakani, naomba aendelee na moyo huo kwani umedhiirisha ni jinsi gani ameiva kidplomasia na anaheshimu demokrasia.Hongera sana.

Lakini bado kuna viongozi wachache wamekuwa wakilitumia jina la rais kujaribu kuviziba mdomo vyombo vya habari huru visifichue maovu wala kumkosoa rais panapostahili hata hivyo kadri siku zinavyozidi kwenda jitihada hizo zinagongwa mwamba.

Kwenu nyie viongozi ambao nadiriki kusema ni wachafu kwani mngekuwa wasafi msingethubutu kupitapita na kupiga simu kwenye vyombo vya habari kwamba habari fulani isichapishwe, acheni tabia hiyo kwani April mwaka jana, rais aliutangazia umma kwamba yupo tayari kukosolewa kupitia vyombo vya habari na kupongezwa na baadhi ya watu wasigeuke kuwa wasemaji wake na mkumbuke huyu ni rais wa wananchi wote na siyo kikundi cha wanamtandao maslahi.

Mwisho Rais Kikwete,kumbuka wananchi tulikuamini tukakuweka madarakani kwanjia ya demokrasia, hivyo tunapenda kuona wewe na serikali yako mkisikiliza shida zetu na kuzitatua na pia viongozi wazembe ambao huo uzembe wao unakwamisha ufanisi wapumzishe,weka wengine ambao wanaipenda nchi yao na wako tayari kuilitumikia taifa hili wakati wowote.

Mungu ibariki Afrika,mungu inusuru Tanzania

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili Desemba 16,2007

BURIANI KANALI GODFREY MAKAYA


Kanali Makaya afariki dunia
Na Happiness Katabazi

ALIYEWAHI kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kinondoni enzi hizo wilaya hiyo ilikuwa ikiitwa Mzizima, Kanali Mstaafu Godfrey Kajana Makaya(63) amefariki dunia.
Akizungunza ba gazeti hili nyumbani kwa marehemu Sinza Madukani Dar es Salaam, jana, mtoto wa marehemu Doreen Makaya alisema kwamba baba yake alifariki Ijumaa iliyopita saa 4:20 katika hospitali ya Agha Khan Jijini Dare-es salaam. Kanali Mstaafu Godfrey Makaya alifanyiwa upasuaji mdogo wa Henia mapema Novemba 19 mwaka huu, na kuruhusiwa kutoka hospitali Novemba 25 Mwaka huu.

Hali yake ya afya ilibadilika ghafla Ijumaa, akiwa katika hospitali ya Agha Khan alipokwenda kwa ajili ya kuangaliwa maendeleo ya operesheni yake aliyokuwa amefanyiwa.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa alitakiwa arudi baadaye ili kumuona daktari majira ya saa nane mchana lakini akiwa anatembea kurudi kwenye gari, hali yake ilibadilika ghafla na kufariki muda mfupi baadaye saa nne asubuhi hospitalini hapo.

Kanali Mstaafu Makaya aliiongoza Wilaya ya Mzimzima sasa Kinondoni kwa Kipindi cha zaidi ya miaka 17 mfululizo kwa kuchaguliwa na wananchi na hadi mauti yalipomkuta alikuwa mjumbe wa Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Kinondoni na Mjumbe wa Tawi la Sinza D.
Kanali Mstaafu Makaya alizaliwa Septemba mosi mwaka 1944. Alijiunga na jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) na kustaafu kazi Desemba 9 mwaka1997 akiwa Mkuu wa Chuo cha Mgambo Mbeya.
Aidha mazishi yatafanyika kesho katika makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na hataazikwa kwa heshima zote za kijeshi baada ya baada ya kutolewa heshima za mwisho nyumbani kwake Sinza Madukani.Marehemu ameacha watoto kumi na sita na wajuu 29.
Mungu ametoa na bwana ametwa jina la bwana liimidiwe.