MWAHALISI ALUTA CONTINUA

Na Happiness Katabazi

UBAYA ni kama kutu, kutu inayoharibu chuma huota kwenye chuma chenyewe. Na ndivyo ubaya uotavyo ndani ya moyo wa binadamu na kuuharibu.

Nimelazimika kutumia msemo huo kwani mada yangu ya leo nitakayoichambua inaenda kabisa na maana nzima ya msemo huo.

Mada hiyo inahusu tukio la kishenzi lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo watu wasiyofahamika walivamia katika ofisi za gazeti la Mwanahalisi na Mseto na kuwajeruhiwa kwa mapanga na kuwamwagia tindikali usoni wanahabari mahiri nchini Saed Kubenea na Ndimara Tegambwage.

Siku zote ubaya ni mbaya na ubaya haufanywi na wanyama bali ufanywa na binadamu wenywe ambao binadamu hao kutokana na akili zao kuwa finyu ufikiri kwamba mungu ni wao peke yao na wanasahau kwamba ipo siku nao ubaya huo utawarudia ikiwezekana mara dufu.

Ubaya uliofanywa dhidi ya wanahabari wenzetu endapo hautakomeshwa ipo siku utaota mizizi katika mioyo ya binadamu wa jamii yetu na hatimaye tutaanza kuumiza wenye kwa wenyewe.

Tukio hilo hakika ni la kwanza tangu nchi yetu ilipopata uhuru mwaka 1961 na hakika limeweka historia mbaya ndani na nje ya nchi kwani kila kukicha viongozi wetu wamekuwa wakitamba Tanzania ina uhuru wa habari lakini cha kushanga kama si kustaajabisha tambo hizo tayari zimeanza kuingiwa na dosari.

Dosari hizo hasa hasa zimeanza kujitokeza katika kipindi cha serikali ya awamu ya nne muda mfupi kabla ya kuingia madarakani na hadi ilivyoingia.

Baadhi ya viongozi wa awamu nne ambao katika mchakato wa kumtafuta mgombea urais kupitia chama chao cha CCM, hakuna kificho kundi maarufu la wanamtandao’ ambalo linaelezwa lilikuwa likimunga mkono Rais Jakaya Kikwete, lilikuwa mstari wa mbele kununua baadhi ya waandishi wa habari waandamizi toka vyombo mbalimbali vya habari ili viweze kuwaandika kwa mazuri na kuficha maovu yao.

Waliokuwa wakifuatilia mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, walibaini hilo kwani kundi la Mtandao liliwaweka kwapani wanahabari wakiwemo baadhi ya wahariri kwa kuwapatia safari za ndani na nje ya nchi,fedha na hata kuwaidi vyeo vya ukuu wa mkoa, wilaya na ubalozi na hadi sasa baadhi ya wanahabari hao wanaendelea kutumiwa na wanasiasa wa kundi hilo kwa maslahi yao na si jamii tena wala maadili ya taaluma ya uandishi inavyotaka.

Waanahabari ambao walikataa kugeuzwa vibaraka wa kundi hilo, walionekana kuwa ni maadui na kusakamwa sambamba na kutishiwa usalama wao na wengine walifukuzwa kazi kutokana na misimamo yao.

Baada ya jamii kugundua uzandiki huu, ilianza kuwalaumu wanahabari hao sambamba na kuwaanika majina yao kwenye tovuti mbalimbali hali iliyosababisha vibaraka hao heshima yao kuporomoka kwenye jamii ya wanahabari.

Nalazimika kusema hali hiyo ilisaidia kidogo kwani hata mbwembwe na ngebe walizokuwa nazo awali wanahabari hao ambao nao wakalewa ujinga na kujiita nao ‘wanamtandao’ hivi sasa zimekwisha kwani kwenye mijumuiko ya wanahabari makini wamekuwa wakionekana kwa nadra na hivyo vyeo waliyoaidiwa wengi wao wametoswa.

Baada ya wanahabari na wadau wa habari kugundua njama ya wanahabari hawa vibaraka waliamua kusimama kidete kwa kuanza kupambana na vibaraka hawa ambapo walianza kuandika ukweli kuhusu mwenendo wa serikali ya awamu ya nne na viongozi wake sambamba na kuikosoa na hatimaye hivi sasa wamefanikiwa kuwazidi nguvu vibaraka hao.

Na kutokana na mapambano hayo, serikali ikaondoka kwenye lindi la ulevi wa sifa za ushindi wa Tsunami na hatimaye imeanza kuchapa kazi kwa uwezo wake licha katika nyanja nyinge utendaji umekuwa ukizolota na hiyo yote imesababishwa na changamoto mbalimbali zinazotolewa na vyombo mbalimbali vya habari uhuru.

Licha vyombo hivyo vya habari uhuru kuipa changamoto serikali, baadhi ya viongozi wa juu wa serikali ambao kila kukichwa wanataka wasifiwe kama ‘mabibi harusi’ huku jamii inawafahamu kuwa ni wachafu ,wamekuwa wakitoa maelekezo katika taasisi za serikali zisitoe matangazo kwa magazeti hayo likiwemo gazeti la Tanzania Daima, Mwanahalisi ,kwa sababu magazeti haya yamekuwa yakiandika habari zisowasifia.

Ukiona kiongozi wa serikali amefikia hatua hiyo, ama anatumwa na kiongozi wanchi au ameamua kufanya hivyo kwa matakwa yake kwa kutumia wadhifa wake, ujue kabisa kiongozi huyo hanatofauti na madikteta kwani Dikteta anakasumba ya kutotaka kukosolewa na kupokea changamoto na kwa bahati nzuri kwa hapa kuna viongozi wa aina hiyo na wanafanywa mchezo huo ,tunawajua ,wanajijua tena wamepewa dhamana ya kutuongoza.

Nimeeleza hilo ili wadau wa habari watambue kwamba uhuru wa habari pia unapigwa vita na baadhi ya viongozi wa juu wa serikali tuliyoiweka madarakani, na hali hii aikubaliki hata kidogo kwani hatuwezi kuona mambo yanaenda mlama kisha tukae kimya kwani tutakuwa hatuitendei haki jamii na siku wa siku tuje kulaumiwa.

Ukibaraka uliokuwa ukifanywa na unaendelea kufanywa na wanahabari wenzetu ambao wanaelimu kubwa tu, naweza kusema ni mianya ambayo inawapa fursa mabazazi wasiyopenda kuona uhuru wa habari ukiendelea kukua hapa nchini , kutuangamiza kirahisi.

Kwani endapo wanahabari wote wakifanyakazi yao kwakuzingatia matakwa ya taaluma zao bila kujikomba kwa wanasiasa,wafanyabishara, viongozi wa juu wa serikali ,kamwe hakutakuwa na kundi la watu watakaothubutu kuchezea wanahabari wala kutikisa uhuru wa habari.

Ni sisi wenyewe kwa njaa zetu ambazo tumeamua ‘kuzifungulia feni’tumekuwa mstari wa mbele kulamba viatu vya viongozi na kuchomana wenyewe kwa wenyewe kwa hao mabazazi.Hatuna umoja wa kweli miongoni wetu, wengi wetu tumetanguliza maslahi binafsi mbele kuliko ya taifa.

Ni sisi miongoni mwetu tumekuwa tukitumiwa na baadhi ya watu ili kuhujumiana kwa kubambikiana habari ili ikiichapisha gazeti lake lishitakiwe au kufungiwa. Ni sisi si tumekuwa tukio siri tumekuwa tukivujisha siri za vyumba vyetu vya habari kwa mabazazi.

Wanahabari wamekuwa wamoja wakati wa kipindi cha uchaguzi kikikiwa kimemalizika , ila umoja huo uenda likizo pindi mchakato wa uchaguzi mkuu unapoanza kwani kipindi hiki waandishi vibaraka ugeuka kuwa ni kipindi cha neema na mavuno kwao.

Hivyo katika kipindi hiki cha majonzi kutokana na yaliyowakumba wanahabari wenzetu , tukae chini tufikiri kwamba ukibaraka siyo chanzo cha kuzika uhuru wa habari?.Miongoni mwetu kujirahisha kwetu kwa wakubwa na kuchomana wenyewe kwa wenye kwa mabazazi siyo sababu inayosababisha sisi kutishwa,kujeruhiwa na hata kutaka kutolewa uhai na watu hao?

Kila mmoja wetu akiacha unafki na kuyatafakari hayo kwa kina naamini atakubali kwamba mapungufu hayo yanatoa mianya kwa ‘mabazazi’ wasiotaka kukosolewa kutudhuru kwa urahisi na kuangamiza uhuru wa habari ambao sisi kama wanataaluma ndiyo tunatakiwa tuwe wa mstari wa mbele kuutetea na kuusimamia.

Lakini nawataka wale wote ambao hawataki kuguswa na kalamu zetu basi wajirekebishe ,waache ufisadi na na wachape kazi, wasifikiri kututisha na kujeruhi ni dawa, hiyo siyo dawa kwani hata wakifanikiwa kutoa uhai miongoni mwetu bado, watazaliwa watu wengine ambao nao watakuwa na fikra za kimapinduzi na wataendeleza kazi iliyokwishaanza kufanywa na watu wa taifa hili tangu lilipopata uhuru wake.

Na mtambue kwamba wanao sisi tunawaokoa kwa hoja nikiwemo mimi, siyo maadui wa taifa hili bali tunalitakia mema taifa na viongozi wake ila hao wanaowasifia na kuwajaza ujinga kila kukicha hawawatakii mema kwani wanawageuza ‘wanasesere’ machoni kwa jamii, wanachokitaka kutoka kwenu ni msaada unaowanufaisha matumbo na familia zao na si jamii.

Nikiligeukia jeshi la polisi ambalo limetuaidi kuwa limeunda timu ya uchunguzi kuchunguza waliosika na tukio hilo la uvamizi, nataka nimwambie IGP-Said Mwema kwamba tunaomba uhakikishe vijana wako wanawakamata watu sahihi waliohusika na tukio hilo na si vinginevyo.

Kwani endapo watawakamata watu wasiyohusika sisi kama wanahabari ambao miongoni mwetu ni mahiri kabisa katika kuandika habari za uchunguzi ambazo zinahusu serikali, majeshi yetu na ambazo zimekuwa zikichapishwa magazetini, na baada ya kuchapishwa habari hizo taasisi hizo zimekuwa zikishindwa kuzikanusha kutoka na habari hizo kujaa ukweli.

Hivyo sisi wanahabari ni askari kasoro magandwa,na endapo vijana wako watafanya ujanjaujanja ili kutaka kufunika- kombe mwanaharu apite- tutajua na tukijua tutauanika ujanja huo kwenye vyombo vyetu vya habari .

Jambo litashusha adhi na heshima ya Jeshi la Polisi ambalo kwa muda mfupi tangu uanze kuliongoza ,limeanza kurejesha heshima na matumaini kwa jamii kwani siyo siri lilikuwa limepoteza sifa, heshima kutokana na baadhi ya askari wake waliokuwa wamekubuhu kwa rushwa,kubambikia raia kesi na wengine kujihusisha na uharifu wa kutumia silaha.

Nimalizie kwa kuwapa salamu hao mahalamia ambao wamefanikiwa kuwajeruhi mpiganaji Kubenea na Ndimara, ni hivi wapiganaji wengine bado wapo ndani na nje ya nchi licha wapiganaji hao ni wachache ukilinganisha na idadi ya mafisadi lakini tunawaakikishia kwamba tutaendelea kupigania maslahi ya walio wengi, kuandika na kusema ukweli bila kumhofia mtu yoyote kwani tuliumbwa siku moja na tutakufa siku moja.

Na rejeeni msemo huu ambao uwapa moyo wa ujasiri wapigania haki wote,unasema hivi “Makalio ya chungu hayaogopi moto kwani yakiogopa moto ugali hautaiva’.Hivyo haturidi nyuma,tunasonga mbele na wala hatuogopi vitisho vyenu na kwa tafsiri rahisi ya msemo huo, wanahabari tukiogopa kufichua uovu, jamii na serikali kwa ujumla itakwenda mlama.

Enyi mnaotuma watu kutufanyia uharamia mkae mkijua ipo siku hizo fedha zinazowatia uchizi na hayo madaraka mnayolingia ipo siku mungu atawanyang’anya atawapatia wengine.

Naamini katika dunia hii sote tunapita na tuendako atukujui na kila mtu aliyepo hapa duniani, mungu anajua amemleta kwa makusudi gani hivyo hila na ubaya ufanywao na binadamu dhidi ya binadamu wenzao ipo siku mungu atawaadhibu.

Namalizia kwa kuungana na wadau wenzangu wa habari kulaani tukio hilo .Na kuwataka wadau wa habari wenzangu kuacha ubinafsi na kutanguliza maslahi ya taifa mbele naamini tutawashinda manyang’au haulitakii mema taifa hili kwani wanatumia fedha na madaraka yao kutaka kuua uhuru wa habari ambapo tuna fahamu kwamba taifa ambalo uhuru wake wa habari umekufa ni taifa ambalo shughuli zake za maendeleo zinadolola.Nyie manyang’au wa Tanzania hatutaki mtufikishe huko na kamwe hatutakubali mtufikishe kwa hali yoyote ile.

Mungu ibariki Afrika, Mungu inusuru Tanzania
0755312859:katabazihappy@yahoo.com:www.katabazihappy.blogspot.com

UFISADI WA TANZANIA NI TISHIO HATA KWA SHETANI

Na Happiness Katabazi

KASHFA ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ni kashfa kubwa ya ufisadi kuliko zote zilizowahi kutokea katika Bara la Afrika.

Kashfa za ufisadi ambazo zilikuwa zimetokea kwa nchi kamamNaigeria, ziliwahusu viongozi wa serikali kuibia serikali bila kuhusisha vyombo vya serikali.

Hivyo kila mara serikali na vyombo vyake nchini humo vilibaki katika ulingo wa kutetea Katiba na sheria za nchi.

Lakini katika kashfa hii ya BOT vyombo vya serikali ya Tanzania vimetumika kufanya ufisadi na hivyo kuvunja sheria za nchi.Kwahiyo tatizo siyo mfuko wa EPA kwa EPA ni tone katika bahari ya ufisadi inayogubika kwenye jiko letu la uchumi (BOT).

Sheria ya BOT inakataza BOT kushiriki au kujihusisha katika biashara.Je iliwezekanaje vifungu hivyo kukiukwa wakati bodi ya taasisi hiyo ipo,vyombo vya kuzuia rushwa na polisi vipo?. Kama bodi ya BOT iliona na kuidhinisha uvunjaji wa sheria huo utajiwajibisha wenyewe?

Mfano Dk. Balali ambaye alikuwa ni gavana amekuwa ni mjumbe katika makampuni yanayotajwa ni ya kifisadi ya Meremeta,Tangolg na mengineyo,Gavana huyo huyo ni Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa BOT iliyodhamini na kutoa fedha kwa makampuni hayo ya kifisadi.Makampuni hayo yamegundulika kuwa ni ya kifisadi yalifunguliwa ‘off show’ kwa maana ya kukimbia na kukwepa kodi.

Kumbe basi kwa makamuni haya kufunguliwa kwa ‘off show’,BOT ilikuwa inaidhinisha ufisadi wa kukwepa kodi na kukwepa mkono wa sheria ya Tanzania kwa vile Tangold ilifunguliwa Mortius na Meremeta ilifunguliwa Uingereza.

Yalipofilisika sheria ya ufilisi haikutumika kuteua mfilisi na wala hapakuwa na ushaidi wa mahesabu kwamba makampuni hayo yalifilisika kweli wala hapakuwa na wadai waliodai kwamba walifanyabiashara na makampuni hayo lakini BOT ililipoa gharama za madai hewa yatokanayo na kufilisa kwa Meremeta na Tangold.

Huu ni mfano tu kwamba bodi ya sasa ya BOT haina uwezo wa kukabili aina ya ufisadi uliojitokezakatika taasisi hiyo kwasababu bodi hiyo ni sehemu ya ufisadi huo.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali amu iliyopita alikuwa Andrew Chenge ambaye kwa sasa ni Waziri wa Miundo Mbinu na alikuwa ni mjumbe wa bodi ya Meremeta na Tangold, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Gray Mgonja alikuwa mhumbe wa bodi hizo.

Sasa Rais Jakaya Kikwete anapompa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kazi ya kudhibiti kuchunguza maovu yaliyotokea BOT, Mwanasheria Mkuu ana ubavu wa kumdhibiti mwanasheria mkuu aliyemtangulia hadi aombe vyombo

Vyambo vya dola vichunguze na kuchukua hatua za kisheria?

RaisKikwete ameangalia hoja ya EPA na kutengua uteuzi si sawa na kumfukuza kazi mtu. Hii na maana kwamba Balali bado ni mtumishi wa BOT na ana pata malupulupu sambambana kutibiwa kwa kuwa hajatuhumiwa na kosa lolote lile.

Hao wanaoumsifu rais kwa uamuzi wake wanamsifu kwalipi?.Pia rais katazama hoja ya EPA,akutazama hoja zingine ambazo ni kubwa kuliko hoja hiyo.

Hoja ya EPA inausu ubadhilifu wa sh bil.133 lakini hoja moja inayohusu Minara pacha inaubadhilifu wa billion 523.Kwanini rais anawinda sungura badala ya kuiwinda tembo?.Au hana ubavu wakukabiliana na tuhuma hii?

Tuhuma ya kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd ni tuhuma ya aibu kwasababu inaelezwa kuwa wakurugenzi ni maswahiba wa arais,ambaye anasemekana ni wanatamtandao kigogo,ambaye alitoa fedha nyingi katika uchaguzi Mkuu uliopita Yawezeekana kweli jina la mwanatanda huyu kigogo halipo kwenye wakurugenzi wa kampuni hiyo lakini kasoro hii ya kiufundi aiondoi tuhuma kubwa ya kwamba dola milioni 30,732,658.82 sawa na sh billion 40 walizopewa kampuni ya Kagoda wakati wa uchaguzi zilitumika kwa shughuli nyeti’kununulia kura’.

Kama hili lina ubishi basi waziri wa Fedha Zakia Meghji atuambie hizo shughuli nyeti za serikali zilizo gharamiwa na fedha hizo ni zipi?.

Kagoda ilisajiliwa Septemba 29 mwaka 2005 na kupewa hati ya usajili namba 54040 na ilichotewa mabilion wiki tano baadae kwa amri ya serikali.

Hata hivyo tangu lini kampuni binafsi yenye wakurugenzi wasiyojulikana uaminifu wao ikatumika kufanya shughu nyeti za siri za serikali?.

Je serikali ilishindwa kuunda kampuni za umma kwa madhumuni hayo?.Tunachokijua ni kwamba katika demokrasia haki ya kutumia fedha za walipa kodi inaendana na uwajibikaji wa wazi.

Aiwezekani ukaibuka ukiwa umejificha katika koti la usiri nyeti ya shughuli za serikali.

Rais aache unafki amevalia njuga fedha za EPA kwasababu zinawagusa wafadhili mwaka jana walichachama kwamba fedha zao zifanyiwe ukaguzi,ameacha fedha nyingi za Watanzania zitafunwe na washirika wake watafune wanavyotaka.Huu ni unafki na inauma kweli kweli.

Ninachosema ni kwamba mafisadi Watanzania ni wabaya kuliko shetani na wana tishia cheo cha shetani Mkuu ajulikanae kwa jina la Lusiferi.

Mungu ibariki Afrika Mungu inusuru Tanzania

0755312859;katabazihappy@yahoo.com;www.katabazihappy.blogspot.com.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 23, 2008

MEJA JENERALI MARWA:KAMANDA ALIYEONGOZA VITA YA IDI AMIN


Na Happiness Katabazi

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ndilo lenye dhamana ya kuhakikisha ulinzi na usalama wa nchi na mipaka yake.

Kwa mantiki hiyo inapotokea nchi yetu haielewani na majirani au kujitengenezea maadui wa nje, ni JWTZ lililo na jukumu zito la kuhakikisha linapambana kikamilifu dhidi ya maaduni hao.

Hii inaweza kumaanisha ama kuingia vitani kikamilifu au kufanya operesheni maalumu kwa ajili ya kutokomeza hali ya wasiwasi ili nchi isiingie katika vita kamili.Katika hili twaweza kutoa mfano jinsi JWTZ walivyofanya kazi mwaka 1978/1979 dhidi ya majeshi ya adui Idi Amin Dada wa Uganda.

JWTZ katika vita walifanya kazi iliyotukuka kiasi kwamba sitarajii itakuja kusahaulika miongoni mwa Watanzania na katika historia ya nchi hii. Naam! JWTZ walitimiza wajibu wa kuhakikisha kwamba taifa letu linakuwa usalama.

Sifa hizo kwa jeshi letu hazikuja hivi hivi, bali zililetwa na askari waliotoa maisha yao kwa ajili ya taifa letu, na miongoni mwa watu hao ni marehemu Meja Jenerali mstaafu Michael Mwita Marwa (78).

Kwa wale wanaofuatilia kwa karibu shughuli zifanywazo na JWTZ na historia ya jeshi hilo, jina hilo haliwi geni masikioni mwao.

Meja Jenerali Marwa ni mmoja wa makamanda mashuhuru wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania aliyeongoza majeshi kuteka miji ya Masaka na Entebbe wakati wa Vita ya Kagera.

Marwa maarufu kwa jina la ‘Kambale’ , wakati wa vita alikuwa mmoja wa makamanda waasisi wa kutegemewa wa JWTZ. Hivi karibuni alipelekwa Kenya na Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu kabla ya kufikwa na mauti.

Meja Jenerali Marwa atakumbukwa pamoja na wengine kwa mchango wake alioutoa wakati wa Vita ya Kagera yaani ‘Operesheni Chakaza”. Kwa nyakati tofauti aliongoza Brigedi za 207 na 208 na kutoa kipigo kikali kwa majeshi ya Idi Amin na kufanikisha kuiteka miji ya Masaka na Entebbe.

Mara baada ya Vita ya Kagera, Meja Jenerali Marwa aliteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali jeshini na serikali ikiwamo Kamanda wa Divisheni ya 20 Tabora (1979), Mkuu wa Mkoa wa Singida (1983-1993) wadhifa alioendelea nao hata baada ya kustaafu utumishi jeshini Januari 1, 1990.

Marwa aliyetumikia JWTZ kwa uadilifu mkubwa kwa miaka 36, miezi mitatu na siku 21, alizaliwa Januari 1, 1930 katika Kijiji cha Mogabiri, Wilayani Tarime, mkoani Mara. Alijiunga na jeshi la kikoloni la King’s African Rifles (KAR) mwaka 1953 baada ya kuhitimu elimu ya msingi.

Akiwa jeshini, alijiendeleza kielimu na aliteuliwa kuhudhuria kozi ya maofisa Uingereza mwaka 1962 na baada ya kuhitimu na kurejea nchini, alihudhuria kozi nyingine ikiwamo ya ukamanda wa platuni, kamanda kombania na mafunzo ya siasa katika Chuo cha Chama Kivukoni, Dar es Salaam, mwaka 1970. Pia aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Moja ya sifa ambazo Meja Jenerali Marwa ameacha jeshini ni ujenzi wa kambi na mabwalo. Alisimamia kikamilifu ujenzi wa bwalo la maofisa wa JWTZ lililopo Migombani, Zanzibar akiwa Mkuu wa Brigedi ya Nyuki. Sehemu hii hadi sasa inaitwa Kwa Marwa.

Kwa kutambua na kuthamini mchango wake katika kulinda taifa, Rais na Amiri Jeshi Mkuu alimtunukia medali nane ikiwamo medali ya Vita, Kagera, Uhuru, Jamhuri, Muungano, Miaka 20 ya JWTZ, Utumishi wa Muda Mrefu na Utumishi uliotukuka Tanzania.

Alipanda vyeo jeshini kwa ngazi akianzia na cheo cha askari. Baada ya uhuru mwaka 1961 alipewa kamisheni na kuwa Ofisa wa cheo cha Luteni Usu. Mtiririko wa kupanda vyeo kama ofisa ni kama ifuatavyo: Julai 28, 1962 alipandishwa cheo na kuwa Luteni.

Februari 1, 1964 alipandishwa cheo na kuwa Kapteni, Machi 28, 1965 alipandishwa cheo na kuwa Meja, Januari 1, 1967 na Juni 19, 1973 tarehe ambayo alikuwa akikumbuka siku yake ya kuzaliwa, alipandishwa cheo cha Luteni Kanali. Februari 12, 1974 alipandishwa tena cheo na kuwa Brigedia Jenerali.

Hakuishia hapo kwani Januari 10, 1979 alipandishwa cheo na kuwa Meja Jenerali, cheo alichodumu nacho hadi alipostaafu jeshi.

Meja Jenerali Marwa alifariki dunia Januari 7, mwaka huu, katika hospitali ya Med-Clinic Heart, Pretoria, Afrika Kusini. Mwili wake ulirejeshwa nchini Januari 9 na juzi uliagwa na mamia ya wakazi wa Dar es Salaam walioongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Makamanda wenzake wastaafu walijitokeza kutoa heshima zao za mwisho kwa mpendwa wao huyo na kisha mwili wake ulisafirishwa jana jioni kwenda kijijini kwake Mogabiri, wilayani Tarime, mkoani Mara na amezikwa leo kwa heshima zote za kijeshi.

Meja Jenerali Marwa atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa ndani na nje ya jeshi. Alionyesha njia ambayo bila shaka askari wa jeshi hili watazifuata kwa vitendo.

Bwana alitoa na Bwana alitwaa, jina la Bwana libarikiwe na upumzike kwa amani.

*0755312859
katabazihappy@yahoo.com
http://www.katabazihappy@yahoo.com/

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi,Januari 11,2007.

POLE KUBENEA ,HAYO NDIYO MATOKEO YA KUTETEA HAKI


Nikimsikiliza kwa makini Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Halihalisi Publishers, inayotoa gazeti la Mwanahalisi na Mseto, Saed Kubenea, Januari 6 mwaka huu, wakati akizungumza na waandishi wa habari ambao tulifika katika wodi ya Sewahaji ambako alilazwa baada ya kujeruhiwa na kumwagiwa tindikali usoni na watu wasiofahamika Januari 5 mwaka huu, ofisini kwake Kinondoni. (Picha na Francis Dande)

MWANAHALISI WAVAMIWA OFISINI


Nikimjulia hali Mshauri Mkuu wa Habari wa Gazeti la Mwanahalisi , Ndimara Tegambwage nyumbani kwakwe Tegeta Machakani ,ambaye Januari 5 mwaka huu, alijeruhiwa kwa mapanga na watu wasiofahamika wakati wakiwa katika ofisi za gazeti hilo zilizopo katika eneo la Kinondoni Vijana Dar es Salaam,ofisini wakiandaa gazeti hilo.(Picha na Francis Dande)

KIKWETE ANAPONZWA NA WASAIDIZI WAKE



Na Happiness Katabazi

MWANASESERE ni sanamu inayotumiwa na watoto kwa kuchezea. Kwa mtoto mwanasesere anawakilisha kitu halisi. Katika uhalisia mwanasesere ni hali kwa uanasesere wake lakini kwa kweli si kile hasa anachokiwakilisha.

Kwa mfano, mwanaserere mwenye umbo la simba, atabakia kuwa mwanasesere na si simba halisi.Nimeanza makala yangu na mfano huu nikiamini kuwa utasaidia kufikisha ujumbe wangu kwa watu wa marika yote.

Nitazungumzia tabia isiyopendeza inayoanza kuota mizizi kwa baadhi ya watendaji wa serikali na wasaidizi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete.

Inaonekana kuwa Rais Kikwete amekuwa akidanganywa katika taarifa anazopewa na wasaidizi wake na hata watendaji wa serikali. Kwa bahati nzuri na kwa sababu anawaamini, taarifa hizo amekuwa akizitumia anapozungumza na wananchi na kuwataka waziamini, wakati wananchi wengi wanajua kuwa taarifa hizo si sahihi.

Hili ni moja ya sababu zilizompunguzia umaarufu wake yeye binafsi na serikali yake kwa mwaka mmoja uliopita kama jinsi ripoti ya Taasisi ya Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) katika utafiti wake ilivyoeleza.

Kwa mujibu wa kumbukumbu zangu, Rais Kikwete alianza kutofautiana na wananchi katika hotuba yake aliyoitoa mkoani Mwanza mapema mwaka jana, aliposema wakazi wa mkoa huo hawali mabaki ya samaki – kule Jiji la Miamba wanaojulikana kama mapanki - na kwamba hakukuwa na wasichana ‘wanaojiuza’ mkoani humo.

Rais Kikwete aliyatamka hayo baada ya mtunzi wa filamu ya ‘Darwin’s Nightmare’, raia wa Australia, Hubert Sauper, kutengeneza filamu iliyokuwa ikionyesha jinsi wananchi wanavyoishi katika lindi la umasikini huku rasilimali yao - samaki - ikiwanufaisha wawekezaji kutoka nje.

Katika filamu hiyo, mtunzi alionyesha jinsi wananchi hao masikini wanavyopona kwa kula mabaki ya samaki.

Katika hili, Rais Kikwete alipingwa kwa ushahidi. Wananchi waliikosoa kauli yake hii na vyombo vya habari viliandika vikithibitisha kuwa yaliyokuwa katika filamu ya ‘Darwin’s Nightmare’ yalikuwa ya kweli.

Katika hali ya kushangaza serikali iliibuka na kutumia nguvu nyingi na fedha za walipa kodi kutengeza tovuti ya kupinga maudhui yaliyokuwa kwenye filamu hiyo.

Hata hivyo, haikufanikiwa sana kwa sababu mapanki yamebaki kuwa kitoweo muhimu kwa wakazi wa Kanda ya Ziwa na Sauper anaendelea kuwa mkweli kuliko Rais Kikwete kuhusu ulaji mapanki.

Ingawa Rais Kikwete ni kiongozi mwenye sifa ya pekee ya kujua zaidi matatizo ya wananchi wake kutokana na staili ya maisha yake wakati akiwa waziri ya kujichanganya zaidi na watu wa kawaida, akiwa rais sifa hiyo hana, anawategemea zaidi wasaidizi wake kumpa taarifa za hali ya maisha ya watu wake.

Hivyo, waliomwandalia taarifa hiyo kwamba Mwanza hawali mapanki walimdanganya na kumuabisha mbele ya wananchi wake na jumuiya ya kimataifa inayoufahamu ukweli huu. Nilidhani alipaswa kuwafuta kazi wasaidizi hawa mara moja kutokana na kumpotosha.

Mwaka jana huo huo, Rais Kikwete alijikuta katika tukio jingine la aibu baada ya picha yake kuchapishwa katika vyombo vya habari ikimwonyesha akiwa anapokea hundi kutoka kwa maofisa wa juu wa Benki ya Dunia.







Katika picha hiyo, Rais Kikwete akiwa ndani ya mavazi nadhifu na uso wake ukiwa umepambwa na tabasamu, alionekana akipokea hundi ambayo kiasi cha fedha kilichoandikwa kwa maneno kilikuwa tofauti na kile kilichoandikwa kwa tarakimu.





Hundi hiyo iliandikwa kiasi cha fedha kwa maneno, dola za Kimarekani laki mbili ilhali katika tarakimu iliandikwa dola 300,000. Wakati Rais akipokea hundi hiyo na kupigwa picha na waandishi wa habari, wasaidizi wake lukuki walikuwapo.





Hawa ni watu wanaoaminika kuwa makini, lakini katika hilo la hundi umakini wao uliyeyuka. Rais akawa amepokea hundi yenye shaka kwa kila hali.





Maswali yaliibuka baada ya Rais Kikwete kuonekana katika vyombo vya habari akiwa amekamata hundi hiyo. Wapo waliohoji kama maofisa wa Benki ya Dunia waliamua kumdhalilisha Rais wetu ili ionekane kuwa ni kiongozi anayeweza kupokea chochote kile ilimradi tu kinahusu fedha. Na wengine walibaki wakihoji umakini wa wasaidizi wa Rais.





Tukio hili liliibua hisia kwamba viongozi wa serikali hawako makini na hata udhaifu ulioko kwenye mikataba mbalimbali inayolitia hasara taifa inatokana na umakini mdogo wa viongozi wetu.




Nami niliamini hivyo na kulingana na tukio lenyewe, sidhani kama yupo anayeweza kupingana na imani hii. Hilo nalo lilipita.





Lakini siku chache kabla ya mwisho wa mwaka 2007, alijikuta akiingia tena katika mtego ule ule wa kupewa taarifa za uongo na yeye kutoa tamko ambalo baadaye lilikuja thibitika kuwa si la kweli.





Safari hii Rais Kikwete alikutana uso kwa uso na mahujaji waliokuwa wamekwama Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, baada ya mahujaji hao kukosa ndege ya kuwapeleke Makka kwa ibada ya Hijja.





Rais Kikwete alifika uwanjani hapo akiwa njiani kwenda zake Marekani. Akawakuta mahujaji waliokata tamaa wakiwa uwanjani hapo, hawajui safari yao itakuwa lini licha ya kulipa fedha kwa ajili ya safari hiyo.





Tunaambiwa kwamba Rais alipowahoji wasaidizi wake alitaarifiwa kwamba tayari kuna ndege imeandaliwa kwa ajili ya kuwasafirisha mahujaji hao. Katika kumsadikisha hilo baadhi ya mahujaji walichukuliwa na kupakizwa kwenye ndege kuonyesha kama kwamba wako tayari kwa safari.





Ilikuwa kama sarakasi. Mheshimiwa akapata moyo, akawafuata kuwaaga huku akiwatakia safari njema ya Hijja. Akaigeukia ndege iliyokuwa imepangwa kumpelekea Marekani, akapaa.





Kituko! Alipoondoka tu, mahujaji waliopakizwa kwenye ndege kwa ajili ya safari wakateremshwa. Kisa? Eti ndege hiyo iligundulika kuwa na hitilafu! Si rahisi kuamini, lakini hivyo ndivyo ilivyokuwa.





Rais Kikwete kwa mara nyingine akawa ameingizwa katika mtego wa kusema uongo, kwamba alikwenda kuwaaga mahujaji hao baada ya kudanganywa kuwa safari imeiva, naye akadanganyika na kuwaaga mahujaji. Hiki ni kitendo cha aibu kwa Rais wetu.





Kwa kumbukumbu ya matukio haya yaliyotokea mwaka jana, nadhani Rais Kikwete ana kila sababu ya kuipanga upya safu ya wasaidizi wake ili kuondokana na aibu ya kutoa kauli zenye utata kila mara kwa wapiga kura wake.





Naamini Rais Kikwete anaweza kusahihisha hali hii kutokana na rekodi yake kiutendeji na kutovumilia watumishi wazembe. Watumishi wanaomwangusha mbele ya wananchi wake.




Kwa matendo yote haya hatuoni kwamba Mheshimiwa Rais wetu anageuzwa mwanasesere?





Wito wangu kwa Rais Kikwete ni kwamba naye awe anajiridhisha kwanza na hotuba anazoandaliwa kabla ya yeye kwenda kuzisoma hadharani, kwa sababu mifano hiyo hai imetuonyesha wazi baadhi ya watendaji wake ambao aliwaamini akawapa dhamana ya kumsaidia si makini.





Wanachokifanya ni kumfurahisha Rais lakini kumbe wanampoteza na kumwingiza mkenge kama watoto wa mjini wasemavyo.





Mungu ibariki afrika, mungu inusuru Tanzania





Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Januari 6, 2007


KAAYA:NiTALETA MAPINDUZI YA KIUCHUMI CCM ARUSHA

.Apania kupambana makada mamluki
.Ndiye Mkurugenzi Mwendeshaji wa AICC

Na Happiness Katabazi

Swali: Nini kilikusukuma ukajiunga na kwenye ulingo wa siasa?
Jibu:
Kama ujuavyo hakuna mtu ambaye siyo mwanasiasa. Hata wewe nakufahamu kwamba ni mawanasiasa!. Hata hivyo mimi ninajifahamu kama mshiriki katika siasa tangu nikiwa mtoto mdogo. Tunzi zangu za mashairi zimejaa siasa. Niliandika sana hasa kupitia magazeti ya Sunday news na daily news makala zilizohusiana na vita vya ukombozi.Nilikuwa mshiriki mkuu katika madadiliano ya midahalo ihusuyo siasa shuleni na vyuoni. Kwa hiyo kujihusisha kwangu katika siasa sikuhusihanishi na uamuzi wangu wa karibuni wa kugombea nafasi ya NEC Mkoa wa Arusha. Matokeo ya uchaguzi huo yalikuwa dhahiri. Nilishinda kwa kiushindo na Mkoa wa Arusha kuweka historia ya kumchagua mgombea wa nafasi ya juu kama hiyo bila yeye mwenyew kuwepo. Nilikuwa safarini nje ya nchi lakini wajumbe walidhihirisha mapenzi yao!

Swali: Hivi karibuni umechaguliwa kuwa Mjumbe wa NEC-Arusha, umejipangaje kwenye ulingo huo wa wadhifa huo mpya ndani ya CCM?.
Jibu:
Arusha tumeanza vema, ten sana. Nilichuguliwa kwa kufahamika utendaji wangu ndani na nje ya chama. Nimatarajio yangu kwamba sitaisaliti imani hiyo iliyoonyeshwa kwangu na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Arusha.
Moja, nitatumia uwezo wangu wote wa Kitaaluma na elimu yangu ambayo niliipata kupitia sera sahihi za CCM na misingi iliwekwa na Baba wa Taifa kukishauri chama katika ngazi zote kuendeleza rasilimali zilizozopo na kuwekeza kukiepusha chama na adha ya kuwa ombaomba. Hili litawezekana kwani Mwenyekiti wa Taifa wa CCM na Rais wetu amebainisha nia yake kulishughulikia hili.

Nitashiriki kuhakikisha kwamba adhima hii inakuwa kweli na siyo nadharia. Nimepania kuifanya CCM iepuke fedha ya aibu kutoka kwa wanaoigiza kukipenda chama kumbe wako katika biashara. CCM imara itajengwa na wanachama na Watanzania wenye mapenzi ya kweli na uzalendo na sio watafutaji wanaowania nafasi katika chama ili kuweza kulinda masilahi yao. CCM ni ya wakulima,wafanyakazi, wafanyabiashara lakini wanoongozwa na sifa moja tu nayo ni mapenzi kwa nchi na uzalendo. Mwenye sifa hizi hataweza kamwe kubomo sifa iliyotukuka ambayo CCM imejijengea kwa miaka mingi.

Mbili, kwa kuwa wanachama na wajumbe wamenipa heshima ya kunichagua kwa kutumia kigezo cha uadilifu na mapenzi kwa chama, ninabakia na deni kubwa. Nitalilipa deni hilo kwa kuwaheshimu na kutekeleza watakayonituma kwa unyenyekevu, uadilifu na bila upendeleo kwa yeyote. Nitakuwa kichocheo cha kuisafisha hali ya hewa katika Mkoa wetu ambayo siyo ya kufurahisha sana. Nitajitahidi kuwashawishi wanachama kukienzi tu Chama Cha Mapinduzi na kwamba makundi ndani ya chama ni sumu ya utengamano. Nitafanya kazi ya kushona pale ninapobaini kuna dalili za kuendeleza makundi kwa kuwa mkweli, nisiye na upendeleo, muwazi na muunini wa falsafa ya Mwalimu ambayo ndiyo falsafa ya CCM.

Nitamuunga mkono Mwenyekiti wa Taifa wa CCM na chama changu kwa vitendo katika mradi mkubwa wa Chama wa kupapambana na adui rushwa. Rushwa ikisafishwa ndani ya Chama, serikalini itakuwa ni kutelezea tu.

Tatu, nitaitumia nafasi yangu katika Halmashauri kuu ya Taifa kufafanua kinagaubaga ni kwa namna gani Utaklii wa Mikutano, sekta ambayo niifahamu vilivyo inaweza kuwa injini KUBWA ya kukua kwa uchumi wa Taifa letu. Somo hili likifahamika vema ndani ya Chama, basi serikali itapiga kasi katika kulipa msukumo sahihi. Hata hivyo nilifurahi sana pale Mwenyekiti wa CCM Taifa alipolitaja bayana katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Nane wa CCM pale Kizota Dodoma.

Swali: Unafikiria idadi ya wanawake waliobahatika kupata a uongozi ndani ya CCM katika uchaguzi mkuu ulifanyika mwaka huu, wanatosha na kama hawatoshi nini kifanyike?
Jibu:
Kwanza kabisa hauitafika wakati ambapo tunaweza kusema kwamba idadi ya viongozi wanawake ndani ya CCM na hata serikalini inatosha. Changamoto kubwa ni kuwahamasisha wanawake wote wenye uwezo ambao ni wengi kujitokeza zaidi na zaidi kushiriki katika mchakato. Mimi ninaamini wanawake wana uwezo mkubwa kiuongozi, hata zaidi ya wanaume kwa hiyo uwino kwangu siyo hoja ya msingi. CCM imetoa kipaumbele kwa wanawake na wajitokezo ili Taifa lifaidike na uwezo, umakini na uwelewa wao mkubwa wa masuala ya kijamii, kiuchumi, kisiasa. “The sky is not the limit”. Ikiwezekana wachukue hata nafasi zote kwani bado tutabakia katika mikono salama. Mwanamke wa kulibomoa Taifa letu mimi simfahamu. Wanawake ni waumbaji. Watiwe moyo.

Swali: Ni nini matarajio yako kwenye medani ya siasa, Je unatarajia kuwania madaraka makubwa ndani ya CCM katika uchaguzi ujao?
Jibu:
unajua kuna tatizo moja kubwa sana katika uelewa wa wansiasa wetu. Wengi wanatekeleza majukumu yao siyo kwa nia ya kufanya yawapasayo kuitendea jamii na Taifa bali kwa kukukotoa namna ya kuendelea kuwa viongozi. Hata ikiwezekana kwa kufanya mambo yanayoiachia jamii majeraha makubwa, kama vile rushwa. Kipaumbele ni ushindi wao na siyo vyama vyao. Kigezo na uamuzi wa mimi kuendelea kuwania madaraka ndani ya CCM kitakuwa utendaji wangu katika nafasi ambayo wanachama wamenipa tena bure. Uitikio wao kwa utendaji wangu ndicho kitakachokuwa kigezo changu kutamani kuwania nafasi siku za usoni. Kwa sasa hivi siwazi kukosa usingizi kuwawazia uongozi katika uchaguzi ujao. Ukumbuke pia kwamba cheo ni dhamana. Cheo ni deni.Cheo ni changamoto na ni mzigio mkubwa kwa yule anaepania kweli kweli kuwatumikia wananchi kwa moyo wake wote. Kuwania nafasi katika uchaguzi ujao siyo ajenda ya msingi kwa kiongozi mwenye nia ya kweli. Utendaji wake na mafanikio ya chama chake vitakuwa kigezo cha maamuzi kwa wakati muafaka.

Swali: Ni changamoto zipi zinakukabili katika uongozi wako?
Jibu:
Kama nilivyosema, ndani ya Chama nitapenda kutumia elimu yangu na hekima nitakayojaliwa na Mwenyenzi Mungu kujenda mshikamano ndani ya chama Mkoani mwetu Arusha. Yanayobakia yatatekelezeka kwa kuisimamia ilani ya Miaka mitano ya Chama Cha Mapinduzi

Swali: Unazungumziaje utawala wako hapo AICC? Unafikiri umeleta mabadiliko ya kimaendeleo?
Jibu:
Jibu la swali hili sinalo. Watu sahihi wa kukujibu hili ni wafanyakazi wa AICC, Wakazi wa Arusha na kwa hakika Watanzania wote. Siyo busara kujipia mbiu mwenyewe kwani mbiu utakayojipigia ni ya kujisifu. Nafikiri siyo utaratibu na ustaarabu.

Swali:Tunaomba kufahamu historia ya Ukumbi wa AICC.
Jibu:
AICC ilizaliwa baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya awali Afrika Masharika. Serikali ilifanya uamuzi wa makusudi mwaka 1978 kuiunda AICC kama shirika la umma chini ya Wizara ya Mambo ya nje na Ushiukiano wa Kimataifa ili kuridhi mali zote zilizoachwa na Jumuia na pia kuendesha shughuli za mikutano na kupangisha ofisi kwa taasisi mbalimbali za ndani na nje.Haya ndiyo majukumu tunayoendelea nayo. Hata hivyo jukumu la mikutano ndilo jukumu mama na kupitia jukumu hili AICC imeendelea kupeperusha bendara ya taifa ndani na nje ya nchi.

Swali: AICC inakabiliana vipi na changamoto za kibiashara na kumbi zingine za mikutano katika kuakikisha inaendelea kutoa huduma bora zaidi ya kumbi nyingine za kimataifa katika nchi za Afrika Mashariki?
Jibu:
Biashara ya mikutano inaendelea kubadilika siku hadi siku. Kwa kuzingatia ukweli kwamba AICC haikujengwa hususan kwa ajili ya Mikutano bali kwa shughuli za ofisi, tutajikita vema katika ushindani kimataifa na kikanda hapo ndoto ya ujenzi wa Kituo sahihi itakapotimia. Hata hivyo tunaendelea kuboresha kilichopo na kushindana vilivyo pamoja na vipingamizi vya mzingi vilivyopo (structural limitations).

Swali: Nataka kujua kuhusu mguu wako,nini kilikusibu hadi mguu wako mmoja ukawa katika hali hiyo?
Jibu;
Naam, hili kali. Hata hivyo linadhihirisha uhalisi wako katika kazi ya uandishi wa habari. Wengi huwaza vichwani mwao maswali fulafulani na kuandika watakavyo. Ninakupongeza kwa kuwa muwazi. Mimi niliugua ugojwa wa polio utotoni mwangu. Kwa sababu hiyo mguu wangu wa kushoto uliadhirika. Wazazi wangu, ambao ninaendelea kuwashukuru katika maisha nitakayojaliwa na Mwenyenzi Mungu walilishughulikia tatizo langu kwa uwezo wao wote. Nilifanyiwa upasuaji mara nyingi na katika vipindi mbalimbali vya umri wangu kuniwezesha kuwa katika hali njema zaidi.Ninamshukuru Mungu kwa mafanikio yaliyofikiwa. Lakini hali ndivyo ilivyo kama ulivyoona wewe.

Hata hivyo, sijawahi kujihisi kwamba nina tatizo kwani sivyo nilivyolelewa. Nafikiri unajione mwenyewe. Niko “very sober”. Ninafurahia maisha yangu na kuendelea kutoa mchango wa wangu katika dunia yetu. Zipo dhana mbalimbali zinanzowalenga watu wenye tatizo kama langu. Kwa bahati mbaya wapo hata viongozi, wengine wakubwa tu ambao wamekuwa waumini wa dhana hizo za kipuuzi. Kwa hakika hata kuamini kwamba jamii zao haziwezi kuwapa nafasi za uongozi watu wenye tatizo kama langu. Hawa ni wa kisamehe bure. Ninawashukuru wazazi wangu kwa kunilea vema. Ninalishukuru Taifa langu kwa kubaini uwezo wangu na kunipa dhamana ya kuwa kiongozi. Ninakishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kuhuburi na kutenda kwa vitendo imani yake kwamba binadamu wote ni sawa.

Swali: Naomba kufahamu historia ya maisha yako mapana.
Jibu: Mimi nilizaliwa katika Kijiji cha Mikungani, Tarafa ya Mbuguni Mkoa wa Arusha na Wilaya ya Arusha kwa wakati ule, ambayo kwa sasa hivi inajulikana kamam Wilaya ya Arumeru mnamo tarehe 23 Augusiti 1962. Ni mtoto wa tano wa Mzee Daniel Saitore Kaaya, ambaye kwa wakati huo alikuwa ndiye Jumbe( kumbuka ukolon!) wa eneo lile. Elimu yangu ya Msingi hadi kidato cha nne ilikuwa hapahapo mkoani Arusha na nilimalizia kidato cha sita huko Tosamaganga Iringa Vijijini. Elimu ya juu nilipatie Dar-es salaam, Arusha na baadaye huko Uholanzi ambako nilihitimu shahadi ya uzamili. Nimeudhuria mafunzo mbali mbali ya kitaalamu na kiutawala nje na ndani ya nchi.

Kama ujuavyo fani yangu ni mhasibu nikiwa nimehitimu shahada ya Juu kabisa ya kitaalamu ijulikanayo kama CPA. Nimefanya kazi za kihasibu na ukaguzi AICC. Nimesajiliwa na Bodi ya Wakurugenzi ya Wahasibu na wakaguzi wa Hesabu NBAA. Nimeongoza idara ya fedha na baadae idara ya Fedha na Utawala AICC kwa muda Mrefu. Nimekaimu mara mbili nafasi ya juu kabisa ya uongozi wa Kituo hadi hapo tarehe 4.4. 2007 Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania aliponiteua rasmi kuwa Mkurugenzi Mwendeshaji wa AICC.

Kama sehemu ya Historia yangu sisiti kusema kwamba mimi na mtuzi wa muda mrefu wsa mashairi ya Kingereza. Mwaka 2003 nilitunukiwa medani ya heshima kama mtuzi bora wa Mashairi duniani, nishani ambayo nilikabidhiwa huko Washngton DC, Marekani na International Society of Poets (ISP)

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu 0755312859:katabazihappy@yahoo.com:www.katabazihappy@yahoo.com: