JWTZ MSIPIGE RAIA

Na Happiness Katabazi

JESHI la Ulinzi katika nchi yoyote ile ni chombo maarufu na muhimu. Hakuna njia nyingine ya kumwelezea shujaa wa nchi isipokuwa kupitia taswira ya mwanajeshi.

Na ndiyo maana Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ni chombo cha kujivunia kwa kuwa huliletea taifa sifa ya ukakamavu, nidhamu na uwezo mkubwa wa ulinzi wa mipaka ya nchi.
Panapotokea maafa, mara zote tegemeo kubwa la raia ni jeshi lao la ulinzi, kwa kuwa wanajeshi wa jeshi hilo ndio wenye sifa, maarifa, mbinu na vifaa vya kuokoa. Na kwa kawaida wanajeshi ni vipenzi wakubwa wa wananchi wao.

Kitendo kilichofanywa na askari wa JWTZ wiki iliyopita cha kuvamia ofisi za DAWASCO, kuwapiga na kuwanyanyasa watendaji wa shirika hilo na kupora kamera ya mwandishi wa habari wa Gazeti la Mwananchi, ni kitendo cha aibu kwa jeshi hilo na hakiwezi kupita bila kujadiliwa.

Kwanza, raia si saizi ya wanajeshi katika makabiliano ya kivita na matumizi ya mitulinga (mabavu).

Kitendo kile ni sawa na kaka mkubwa kuvamia wadogo zake chekechea katika patashika ya kugombea chakula mezani, kwa vyovyote vile vitoto hivyo vya chekechea vitashindwa.

Lakini kitendo kile kinaonyesha jeshi letu bado lina wanajeshi wasio na nidhamu, kwa sababu hata kama wangekuwa wameudhiwa kwa kitendo cha kukatiwa maji, ufumbuzi wake usingekuwa kuvamia na kuwapiga watendaji wa Dawasco, bali kutuma mmoja wao kwenda na hundi ya malipo kwenye shirika hilo na kurejesha huduma ya maji.

Kuwapiga watendaji wa DAWASCO, hakuondoi ukweli kwamba JWTZ ni mdaiwa sugu. Kumbe ilikuwa ni upungufu wa busara uliopita kiasi kwa vijana wetu waliovaa sare za kivita wakiwa kwenye gari la kivita kufanya uvunjaji wa amani, kujeruhi na kunajisi sheria za nchi.

Labda JWTZ huheshimu tu Wazungu wanapoajiriwa kudai madeni kama ilivyokuwa kwa Net Group Solutions ya Afrika Kusini.

Kampuni hii ilidai madeni ya umeme yaliyokuwa yameshikiliwa na idara zote za serikali ikiwa ni pamoja na JWTZ na hatukuona akipigwa mtu! Kumbe mnyonge ni mmatumbi, Mzungu huogopwa kama simba!

Sasa hawa ndio mashujaa kweli wa nchi yetu? Labda suala zima la wanajeshi kutoka kambini na kuvamia raia kwa visingizio mbalimbali, kama vile kunyang’anyana ‘mabibi’ na raia vimekuwa vikilaaniwa mara kwa mara na taasisi za kutetea haki za binadamu nchini.

Kwa vyovyote vile tabia hii ina maanisha kuwa hatuheshimiani. Raia akienda kwenye kambi ya jeshi anatakiwa atii na kuheshimu sehemu ile kwa jinsi wanavyotaka wanajeshi. Lakini mwanajeshi akiingia uraiani na hata ofisini hataki kutii na kuheshimu ofisi za wengine. Hakika, kwa hali hii hatufiki!

Septemba 15,2007 , alipokula kiapo cha utii mbele ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete, Mkuu wa Jeshi la Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, alishutumu na kulaani vikali tabia hiyo na kuahidi kwamba uongozi wake utaikomesha.

Kwa kuwa sasa hili limetokea, wananchi wana hamu sana kumsikia ana lipi la kuwaeleza kuhusu utovu wa nidhamu uliofanywa na wanajeshi wake wiki iliyopita katika ofisi za shirika linalomilikiwa na serikali la - Dawasco.

Ili wananchi waendelee kumheshimu, kumuamini na kutolinganisha kauli yake hiyo na porojo za kisiasa, tunamtaka Jenerali Mwamunyange atetee sasa heshima ya JWTZ.

Tunataka atuthibitishie kwamba wanajeshi wetu si genge la wahuni wanaochukua sheria mikononi mwao. Ikiwa atashindwa kufanya hivyo, raia watashindwa kumwamini na kuiheshimu JWTZ.

Na kwa kuwa hakuna kiongozi yeyote wa JWTZ aliyekanusha kwamba waliofanya kitendo kile cha ovyo si wanajeshi, inatazamiwa jeshi litoe maelezo ya kuridhisha sambamba na kuwaomba radhi wananchi na litegemee pia kwamba uvamizi ule unaweza ukazua kesi kubwa ya madai ya fidia yanayoweza kuliletea taifa hasara kubwa.

Izingatiwe kwamba ule wakati ambapo raia walikuwa hawajui haki zao na ni waoga kutetea haki zao umekwisha. Serikali itajikuta ikidaiwa mabilioni ya fedha kwa kutozingatia kanuni za utawala bora.

Tuanelewa kwamba walioathirika katika kitendo kile ni pamoja na waandishi wa habari ambao mmoja alinyang’anywa kamera ili asiweze kutimiza wajibu wake. Hii ni mara ya pili kwa majeshi yetu kuwahujumu waandishi wa habari wakiwa kazini.

Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2005, askari wa Jeshi la Magereza waliwapiga waandishi wa habari na kuwajeruhi, eneo la Ukonga.

Wakati umefika sasa kuuliza kama majeshi yetu ni adui au rafiki wa haki za raia? Je, tuwatofautishe vipi waliotenda ushenzi ule na wale wahuni waliotumiwa kuwahujumu waandishi mahiri wa habari, Ndimara Tegambwage na Saed Kubenea wa gazeti la Mwanahalisi?

Kwa ujumla tunajua kama ilivyo ada ya taasisi za serikali zinapokutwa zimevunja haki za wananchi, kutakuwa na kulindana ili kuhakikisha kwamba waliofanya vitendo hivyo hawapatikani, hawakamatwi na hawachukuliwi hatua za kisheria.

Ikiwa hilo litaendelea, basi Tanzania itakuwa imejijengea utamaduni ambao majeshi yake ni ‘miungu watu’ wanaoweza kufanya udhalimu wa aina yoyote dhidi ya haki na uhai wa raia bila kukanywa wala kudhibitiwa.

Tutakuwa tunajijengea jehenamu ya aina yake na Tanzania haitakuwa tofauti na kambi za Al Ghareb, Iraq au Guantanamo Bay, Cuba.

Tukubali makosa, tukubali kusahihishwa na kama taifa tumrejee Mungu kama wimbo wetu wa
taifa unavyotuasa.

JWTZ itimize wajibu wake wa kulinda nchi na si kupiga raia. DAWASCO fanyeni kazi bila upendeleo na epukeni ufisadi. Hata hivyo kipigo mlichokipata kisiwakatishe tamaa, poleni na jengeni taifa lenu bila woga.

0755 312859katabazihappy@yahoo.com www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumatano la Februari 27,2008

IDARA YA USALAMA WA TAIFA NI SEHEMU YA UFISADI?

Na Happiness Katabazi

BAADHI ya Watanzania wakiwemo viongozi mbalimbali wastaafu na wale wa vyama vya upinzani,wamekuwa wakiliambia taifa kwamba limepungukiwa na viongozi waadilifu na wakaona kwamba umaskini unaolikabili taifa letu ni wa kujitakia.

Kwakuwa licha ya rasilimali kubwa tulizonazo hatuna viongozi wenye upeo wa kutuonyesha njia ya kuzitumia vyema ili tupate maendeleo.

Badala yake tunaona kuwa tunao viongozi wasiyo waadilifu,mafisadi,wazandiki na wababaishaji wa kutupwa.

Uongozi wa taifa una mfumo wa kitaasisi ambao wengi wanaita ‘system’.Kwa lugha ya kawaida system inamaanisha mfumo wa Idara ya Usalama wa Taifa katika kuchagua na kudhibiti ubora wa viongozi na mwenendo wao.
Moja ya wajibu mkubwa wa Idara ya hiyo ni kulipatia taifa viongozi bora,wazalendo na waliofundwa vya kutosha kutumia madaraka yao kutetea maslahi ya taifa.Lakini wimbi la ufisadi lililojitokeza nchini ni ishara kwamba idara yetu ya usalama wa taifa imeshindwa kazi.

Moja,idara hiyo imegeuka kuwa ni sehemu ya CCM kwahiyo badala ya kutekeleza wajibu wake tulioujata kulingana na Katiba na sheria za nchi, ikiangalia vyama vyote,taasisi zote za kijamii nk.

Baadhi yao wamejifanya ni watendaji wa CCM na wanapotenda hivyo kazi yao kubwa inakuwa ni kuhujumu viongozi walio kwenye vyama shindani kana kwamba hawa si watanzania na ila ni maadui wa nchi.

Pili,kuzuka kwa kundi la wanamtandao ambalo linadaiwa kumuweka madarakani rais Kikwete kunaashiria ushiriki mkubwa wa idara hiyo kupanga mtandao kuhusisha sekta zote za jamii na kuhusisha watendaji muhimu serikali ili wote kwa pamoja watekeleze azimima ya CCM kubaki madarakani.

Inasemakana kwamba nyuma ya ufisadi unafichuliwa yapo makampuni ya kifisadi ambayo hayumkini yalioanzishwa na idara ya usalama wa taifa kukusanya mabilioni ya fedha yaliyotumika na wanamtandao na CCM kwenye uchaguzi wa 2005.

Hakika yeyote anayependa kusema ukweli atakiri kwamba mabilioni ya fedha yaliyotumika kwenye mchakato ndani ya CCM na mabilioni ya fedha yaliyotumika na ccm katika uchaguzi uliopita hayana maelezo au chanzo kingine kama si makampuni hayo ya kifisadi ya kupora fedha za umma.

Sasa tujiulize taasisi hii ina uadilifu kiasi gani na Je aijashiriki katika ufisadi kwa namna yoyote ile?. Ikiwa watetezi wa usalama wa taifa watasema inatenda kazi zake kwa mujibu Katiba na sheria za nchi Je walilala wapi BOT ilipohujumiwa?

Je ilikuwa wapi maslahi ya nchi katika uzalishaji wa umeme yalipohujumiwa katika mradi wa IPTL na Richmond?

Je walikuwepo wapi maslahi ya nchi yalipohujumiwa katika ubinafsishaji wa Benki ya Taifa ya Biashara,TTCL, na makampuni mengine mbalimbali ya umma?

Tunachokiona sisi Idara ya Usalama wa taifa isiyojua wajibu wake na ambayo ufisadi ni sehemu kuu ya kazi yake. Pia tunachokiona sisi ni idara hii isiyojua kutetea maslahi ya ya nchi ambayo ipo tayari kuona rasilimali za nchi zikihujumuiwa ili mradi wanafanya hivyo ni marafiki zao.

Kazi kubwa ni kulindana, kupeana vyeo bila kuwa na sifa na pia kuwapiga vita wale wanaojitokeza kupingana na mwenendo wa kifisadi.

Tumefikishana mahala watu sasa wanamwagiwa tindikali,wanahushishwa kwenye ajali za kupangwa na bila shaka siku si nyingi tutashuhudia mauaji ya watu kwa mtindo wa kijambazi unaotumika na Mafia.

Inapotokea kwamba viongozi wa taifa ama serikali wanapata nyadhifa au kuajiliwa kazini kwa sifa za ubabaishaji au kughushi na hilo likafumbiwa macho,basi hakuna usalama wa taifa.

Kwa maana kwamba ikiwa uongozi utawekwa mikononi mwa matapeli walioghushi sifa za elimu basi hatima ya taifa itakuwa hatarini.

Je viongozi wa aina hii wataelewa nini kinachoendelea kuhusiana na mikataba ya biashara ya madini au mikataba ya umma? Kwa hiyo tusishangae serikali yetu inaendeshwa sawa kama viongozi hawajaenda shule kwani siyo kila anayejiita Daktari ni Daktari wa kweli.

Mfano ilikuwaje kampuni ya kihuni ya Richmond kupewa mkataba wa mabilioni ya fedha kununua majenereta ya umeme bila usalama wa taifa kujua?

Je kukosekana kwa umeme Je si jambo nyeti na hatari kwa usalama wa taifa?Au labda idara hii inaona Watanzania wamelala usingizi na wako tayari kufanyiwa vitendo viovu na wako tayari kulipishwa kodi na kubebeshwa gharama kubwa za maisha bila kulalamika au hata kufanya maandamano?

Labda Watanzania wamekuwa wapole mno katika kutetea haki zao.Bila shaka usalama wa taifa utaona ugumu wa maisha wanaopata wananchi pale tutakapokuwa tayari kuandamana na kuwatoa maofisini na kuwafukuza kwa bakora hao mafisadi?

Kwa ujumla , vyombo vyetu vya ulinzi na usalama tulivyonavyo, chombo ambacho akijatufanyia haki ni Idara hii ya usalama wa taifa.Hawa wamelala usingizi wa pono nchi ina hujumiwa,wananchi tunapata taabu .JWTZ,Magereza,JKT na Polisi wanafanyakazi nzuri, tunawapongeza, licha ya kwamba wamekuwa wakilalamika bajeti za wizara zao ni finyu kuliko bajeti ya Idara ya usalama wa Taifa.

Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) chini ya Jenerali Davis Mwamunyange, wanafanyakazi nzuri na ndiyo maana hadi sasa nchi yetu haijavamiwa na maadui.

Polisi chini ya IGP-Said Mwema,nao wamejitahidi kwa kiasi kikubwa kupunguza wimbi la uhalifu.

Magereza chini Kamishna Mkuu, Agustino Nanyaro nao wamejitahidi, kwani hadi sasa hatujasikia wafungwa wamevunja magereza na kutoraka. JKT na wanajitaidi kuwalea vijana na kuzalisha mali.

Wakati umefika sasa watendaji wa Idara ya Usalama wa Taifa wawajibike kikamilifu bila kumuonea haya kiongozi yeyote, ama sivyo itabidi idara hii ivunjwe tuunde jipya na hilo linawezekana kama tuna uchungu wa kweli na Tanzania yetu.

Mungu ibariki Afrika,Mungu ibariki Tanzania

katabazihappy@yahoo.com:www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano Februari 13 mwaka 2008

HAPPINESS NA BALOZI CHOKARA


Pichani nikiwa na rafiki yangu Balozi wa Tanzania nchini Urusi Patrick Chokala, nje ya Mahakama ya Rufaa Dar es Salaam, tukibadilishana mawazo.Picha hii ilipigwa Siku ya Sheria Tanzania Februari 4,2008 na mpiga picha Francis Dande.

JWTZ ISISUBIRI WAKATI WA MAJANGA TU




Na Happiness Katabazi

JUKUMU mojawapo la msingi la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakati wa amani, ni kusaidia mamlaka za kiraia kulinda usalama wa wananchi na mali zao na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kutoa misaada ya uokoaji wakati wa majanga na kukarabati miundombinu inapoharibika.

Katika kusaidia shughuli za kijamii, JWTZ kwa muda wote wa uhai wake, imeweza kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi mkubwa na kujipatia sifa kemkem kutokana na mchango wake, hasa katika uokoaji na urejeshaji miundombinu ya barabara na madaraja wakati wa mvua.

Jukumu hilo limekuwa likifanywa na wanajeshi wote, wakiongozwa na wahandisi wa medani wa JWTZ wenye makao makuu yao eneo la Sangasanga mkoani Morogoro, ambao wamebobea katika fani hiyo.

Wahandisi wa medani ndio watalaamu ambao wakati wa vita huwezesha vikosi kusonga mbele kwa kuonyesha njia, kwa kufanya doria na kuchagua sehemu nzuri ya kupitisha vikosi, zana na vifaa. Wao pia husafisha njia kwa kutegua mabomu, kujenga barabara, madaraja na viwanja vya ndege.

Kwa misingi hiyo basi, naona kuna haja kwa taifa letu kuanzisha utaratibu wa kuwatumia wahandisi wa JWTZ wakati wa amani ili taifa liweze kupiga hatua ya maendeleo katika sekta ya miundombinu.

Jeshi letu hivi sasa lina hazina ya wataalam wa kila fani, lakini baadhi yao taaluma zao hawazitumii ipasavyo kutokana na serikali kutowapa fursa ya kutumia ujuzi wao wakati wa amani.

Sote ni mashaidi kwamba inapotekea maafa, wahandisi wa JWTZ wamekuwa wakisukumizwa kutengeneza barabara, kuokoa majeruhi nk., lakini hali hiyo ya pilikapilika hawaipati wakati wa amani.

Pamoja na kuwa na fani ya uhandisi, lakini wanajeshi wote wamefundishwa ukakamavu na kazi zao huzifanya ndani ya muda unaotakiwa.

Ni barabara, madaraja mengi tunayashuhudia yamejengwa na raia wa kawaida, tena kwa gharama kubwa, lakini yamekuwa yakichukua muda mrefu kukamilika, na mara nyingine tunaambiwa serikali ndiyo imekuwa ikichelewesha fedha za kuwalipa makandarasi na wakati mwingine tunaambiwa makandarasi hao ni wazembe.

Hakika habari kama hizi hazipendezi kusikiwa maskioni mwa mwananchi yeyote mpenda maendeleo, kwani sote tunafahamu taifa lisilo na miundombinu ya uhakika ni wazi litakuwa linajirudisha nyuma kimaendeleo kwani shughuli za uzalishaji zitakwama kwa kuwa mazao au mawasiliano hayasafirishwi kwa wakati muafaka, hivyo kufanya pato la wananchi na taifa kwa ujumla kukosekana na bidhaa kukosekana sokoni.

Naona wakati umefika kwa serikali ya awamu ya nne ambayo kwa bahati nzuri inaongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye kabla ya kuingia kwenye ulingo wa siasa alikuwa ni ofisa wa jeshi hili, iketi na kwa kushirikiana na Wizara ya Miundombinu ione jinsi ya kuwashirikisha wahandishi wa jeshi kwenye ujenzi wa miundombinu ya taifa hata wakati wa amani.

Kwani hivi sasa serikali inatumia fedha nyingi kuleta makandarasi toka nje ya nchi kwa ajili ya ujenzi wa barabara wakati jeshi lina wahandisi wengi tu wasiotumiwa ipasavyo. Endapo serikali itakubali kuwatumia wahandisi medani, ni wazi kwamba serikali itatumia fedha kidogo kwa ajili ya kulipa gharama za uhuduma hiyo.

Yawezekana wakawapo watakaosema kuwa jeshi halina vifaa vya kutosha vya kuweza kufanya shughuli hiyo, sawa, lakini hatuoni sababu ya JWTZ kutowezeshwa ili waweze kununua vifaa hivyo ambavyo vitakuwa ni mali yetu ya kudumu na tutakuwa tukivitumia muda wowote tunapovihitaji kuliko hali ilivyo hivi sasa ambako tunatoa tenda kwa wahandisi wa nje ambao huongeza gharama kwa kuingiza vifaa vya ujenzi na bado hujinufaisha kwa kuviuza mara wanapomaliza kazi zao.

Tujiulize kipi bora, kuendelea kuwatumia makandarasi toka nje ya nchi kwa gharama kubwa ambao wakimaliza kazi wanaondoka na vifaa vyao au taifa lijinyime na kununua vifaa vyake na kutumia wahandisi wake katika ujenzi wa miundombinu ya taifa letu?

Lengo langu si kupiga vita makandarasi wa nje ili wasipewe tenda, la hasha! Ila kwa kuwa serikali kila kukicha imekuwa ikilia kuwa haina fedha za kutosha kutokana na bajeti ya taifa kuwa tegemezi kwa wafadhali, sasa kwanini hicho kidogo tulichonacho kisizunguke humu ndani ili wananchi na taasisi nyingine za serikali ziweze kufaidika nacho?

Naamini fedha za kununulia vifaa vya ujenzi wa miundombinu kote nchini tukiwa na nia ya dhati tunaweza kuzipata, kwani nchi yetu ina utajiri mwingi wa rasilimali, ambao tukiutumia vizuri, unaweza kutupatia haraka fedha hizo.

Nitoe pia changamoto kwa JWTZ kwamba, kama kweli nayo ina nia njema na taifa hili na inapenda kuona miundombinu ya taifa lao ikiimarika, pia nayo ina jukumu la kuiomba serikali iiwezeshe na kisha iwaruhusu kufanya kazi za kuboresha miundombinu wakati wa amani.

Huu ni wakati wa zama za maendeleo ya sayansi na teknolojia na hivyo vinapaswa kulikumba jeshi pia na njia mojawapo ya kulifanya liende sambamba na maendeleo hayo, ni kupanua wigo wa utendaji wake na ninafikiri njia mojawapo ni kwa kujishughulisha katika ujenzi wa taifa kwa kutumia wataalamu lililonao.

Hizi si zama za wanajeshi wetu kutembea na silaha wakati wote, bali kubadilika ili liwe jeshi la ujenzi wa taifa, huku likihakikisha amani na usalama kwa nchi yetu.

Rais Kikwete haitoshi kuona ukiteua baadhi ya maofisa wa JWTZ kuwa wakuu wa mikoa na wilaya. Kama ulivyoweza kuteua maofisa hao kuja uraiani kufanya kazi, vivyo hivyo tunataka kuona wahandisi medani wa jeshi hilo wakitumiwa na serikali yako katika shughuli za ukarabati na ujenzi wa miundombinu ili taifa lipate maendeleo kwa kukimbia kama sote tunavyotamani.

Wanajeshi madaktari na fani nyingine ndani ya jeshi hilo, tunaona hivi sasa wamekuwa wakitumia fani zao vizuri kwa sababu kuna hospitali zinazoeleweka ndani ya jeshi hilo ambazo zimekuwa zikitoa uhuduma ya matibabu hata kwa raia. Na mfano halisi ni Hospitali ya Jeshi Lugalo Dar es Salaam.

Ni vyema tutambue kuwa, mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe, hivyo basi Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe na si wageni. Sote kwa pamoja tujifunge mkanda bila kubaguana katika kushiriki kwenye shughuli za ujenzi wa taifa na naamini tutafanikiwa.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi Februari 2, 2007