RAIS KIKWETE JIHADHARI NA UDANGANYIFU, HUTOAMINIKA



Na Happiness Katabazi

RAIS Jakaya Kikwete amewaahidi Watanzania kuwa serikali yake iko vitani dhidi ya ufisadi. Amesisitiza taifa limpe fursa kuifanya kazi hiyo kwa umakini na umahiri unaostahili.

Ili kuonyesha azima yake hiyo, aliviagiza vyombo vyake vya utendaji, ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Jeshi la Polisi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuunda timu ya pamoja kushughulikia ufisadi uliojitokeza BoT, hasa ule wa akaunti ya malipo ya madeni ya nje (EPA).

Katika utekelezaji wao, kamati hiyo hivi karibuni imezungumza na wahariri wa vyombo vya habari kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika na IGP Said Mwema, wakisema kwamba kazi wanayoifanya ni nzuri, imeanza kuzaa matunda na fedha zimeanza kurejeshwa, wanahitaji muda na usiri mkubwa.

Kwa wananchi wa kawaida tatizo si usiri wala muda, hayo tunajua ni mahitaji ya lazima ili kazi yao iweze kufanyika vizuri. Tatizo kubwa ni kwamba Rais Kikwete hakuvisafisha vyombo hivi vikawa safi ili kuviwezesha kupambana na ufisadi.

Tunajua kwamba ni kesi ya ngedere amelekewa nyani.Kama vyombo hivi vyenyewe vinatuhumiwa kushiriki kwenye ufisadi kama ambavyo kamati ya uchunguzi wa mkataba wa kufua umeme wa Richmond iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe, ilieleza Bunge, vitakuwa na uhalali gani wa kusimama na kuwanyooshea kidole mafisadi wenzao?

Tatizo la pili ni ufisadi wenyewe: Ni nani wa kuaminika aliye kwenye kamati hiyo inayoendesha mahojiano na mafisadi, anayeweza kuaminiwa na Watanzania hata kuthibitisha kwamba fedha zimerejeshwa?

Huu ni mchezo wa nyani kula kula mahindi mabichi. Kusingizia fedha zimetoka mfuko huu kuziingiza kwenye mfuko wa pili bila kujua huu mfuko wa kwanza ulipataje hizo fedha.

Watanzania tumechoka na viinimacho vya baadhi ya viongozi kuleta fedha chafu za mihadarati au za ufisadi mwingine na kuwagawia washirika wao kwa siri, ili waje kuzitoa kwenye harambee wanazozisimamia.

Vivyo hivyo, fedha chafu zinaweza kusafishwa kwa kurejeshwa serikalini kupitia dirisha hilo la kashfa ya EPA. Kama Rais angependa tumuamini angelazimika kuweka wajumbe wenye sifa za kutukuka na ambao ni huru wanaoweza kuaminika na wananchi.

Lakini ilivyo hivi sasa hata tungeambiwa sh billion 133 zote zimerejeshwa, haitaondoa shaka kuwa fedha hizo zimepatikana kutoka kwenye fedha chafu ama za mihadarati au za uharamia mwingine.

Tunamwomba Rais Kikwete asilifumbie macho hili kwa sababu linakera na kuwaletea wananchi kichefuchefu na likiendelea hivi litamchafua.
Ifike mahala Watanzania tujiulize; hizi fedha zinazorejeshwa na hawa mafisadi, tena kwa kipindi kifupi, zilikuwa wapi?

Hawa mafisadi katika kipindi hiki kifupi wamefanya biashara gani iliyowaingizia fedha hizi?

Na hii ndiyo maana tunasema ni vizuri wananchi waelezwe kosa la jinai lilitendwa, mtu aliyetenda ili hata kama ikiamriwa asifikishwe mahakamani tujue kwamba huyu ni fisadi.

Kwa vyovyote vile, hakuna chombo cha kuwasafisha hawa isipokuwa mahakama. Hatutaki tuambiwe utaratibu wa utendaji wa BoT ni wa kizembe kiasi kwamba mtu yeyote anaweza kujichotea mamilioni ya fedha kutoka benki hiyo. Na hili ndilo Rais analokwepa kuwaeleza Watanzania.

Yawezekana kabisa kwamba vigogo ndani ya CCM na serikali ‘walikatiwa pochi’ ya fedha za EPA na inawezekana pia kuwa hiyo ndiyo sababu ya kukwepa kutaja majina ya mafisadi.

Yawezekana pia fedha za EPA zilitumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 kuiweka Serikali ya Awamu ya Nne madarakani.

Lakini hayo ndiyo maswali magumu na machungu ambayo ni lazima taifa liambiwe, ili kesho na keshokutwa vyama vya upinzani vinapolalamika kuhusu gharama za uchaguzi, tuweze kuvielewa kwa sura mpya.

Lazima Watanzania waelewe CCM hailalamikii gharama za uchaguzi kwa sababu zina njia za kifisadi za kuchofa fedha.

Tusipoyasema haya taifa hili halitashinda vita ya ufisadi kwa sababu ufisadi umefungamana na siasa za CCM na jinsi chama hicho kinavyoendesha nchi.

0755 312859
katabazihappy@yahoo.com:www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Machi 26 mwaka 2008

WANA MTANDAO NA MAFISADI NI KUNDI MOJA

Na Happiness Katabazi

KATIKA uwanja wa siasa Tanzania, yamezuka maneno ‘mtandao’ na ‘ufisadi’. Hapa kuna jukumu la kutosha kuoanisha dhana zinazobebwa na maneno haya mawili.

Neno mtandao lilizuka kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, likikusanya watu katika nyanja mbalimbali, wakiwemo wasomi, wafanyabaishara, wanahabari, wafanyakazi serikalini na matapeli ambao walikuwa na tamaa ya kupindua wazee katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kutumia chama hicho kuingia Ikulu.

Kwa asilimia 95, kundi hili lilifaulu kuiteka CCM kwa kuwapiga bakora wazee na kuwagaragaza katika chaguzi za ndani za chama na kushika madaraka serikalini.

Ujana ulioanishwa na kundi hili na itikadi yake ikawa ni Ari mpya, Nguvu mpya na Kasi mpya. Na kwa itikadi hii kundi hili likaingia Ikulu.

Kitu ambacho Watanzania hawakujiuliza ni wapi vijana hawa walipata mabilioni ya fedha walizokuwa wakizitumia kwenye kampeni za uchaguzi wa ndani ya chama na katika uchaguzi mkuu uliopita.

Zilizuka tetesi kuwa kundi hili lilikusanya fedha nyingi toka nje ya nchi, hasa kutoka Iran na Libya.

Watanzania hawakubaini kwamba kundi hili lilikuwa limejijenga ndani ya nchi katika taasisi nyeti za fedha na Benki Kuu (BoT).

Imewachukua Watanzania miaka miwili ya utawala wa kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya kugundua kwamba kundi hili ni la kifisadi au limetenda ufisadi mkubwa ndani ya nchi yetu.

Mikataba ya serikali na kampuni hewa iliwezesha kundi hili kuchukua mabilioni ya fedha kutoka bajeti ya serikali. Ikumbukwe kwamba kundi hili lilikamata viongozi wakuu wa serikali katika kila sekta na lilifanya kazi kwa kusaidiwa kwa karibu na baadhi ya maofisa toka vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.

Inadaiwa mikataba ya serikali kwenye sekta ya maliasili iliwezesha kundi hili kupata mabilioni ya fedha kwenye asilimia 10 walizokuwa wanapewa na kampuni hizo, lakini pia katika michango waliyochangiwa na kampuni hizo kwa visingizio mbalimbali.

Tulishuhudia wagombea wa CCM wakichangiwa kwenye mikoa mbalimbali ya nchi mamilioni ya fedha. Jambo la kushangaza ni pale ilipogundulika mifuko ya pensheni imetumika kuchangia kampeni za CCM na mauzo ya majengo yalifanywa kwa kutumia taasisi ya ubinafsishaji na taasisi za umma kupitia mifuko hiyo kuwaneemesha wafanyabiashara makuadi ambao kazi yao ilikuwa kulikusanyia fedha kundi la mtandao.

Kana kwamba hiyo haitoshi, imedhiirika sasa miradi ya majengo mbalimbali kama vile minara pacha ya BoT ilitumika pia kuiba mabilioni ya fedha kupitia kandarasi.

Mfano jengo ambalo lilipangwa kugharimu sh bilioni 83, sasa limegharimu sh bilioni 523. Hilo halijachunguzwa na hakuna anayethubutu kulichunguza kwa sababu haiyumkini hizo ndizo baadhi ya fedha zilizoiingiza serikali ya awamu ya nne madarakani.

Hivi sasa mtandao umekamilika kwa kuwa wamegawana vyeo vyote serikalini kama walivyoahidiana kwenye kampeni. Aliyeahidiwa u-DC, u-RC alipata na hilo tulilithibitisha tulivyokuwa na baraza kubwa la mawaziri mithili ya darasa la chekechea.

Tatizo kubwa linaloukabili mtandao leo hii ni vyeo vimekwisha kwenye chama na serikali, ambaye hakupata analia na kusaga meno na anashauriwa asubiri mwaka 2010.

Lakini upo pia msambaratiko utokanao na wale wanamtandao wanaotaka kula sasa na si kungoja 2010.

Matokeo yake wanalaumiana, kuchomeana nguru na kusalitiana, hasa pale ambapo mwanamtandao aliyekabidhiwa madaraka amefanya kosa au kashfa.

Hilo tumeliona wakati aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, aliyejiuzulu, alipojitetea bungeni kwamba kuna wanaotaka cheo chake. Kumbe uwaziri mkuu ulikuwa ni wake lije jua ije mvua, akosee asikosee! Jambo hili linasikitisha sana.

Hivi sasa katika vyombo vya habari inaonekana wazi kwamba upo mgawanyiko kati ya vyombo vya habari vinavyounga mkono kundi moja la mtandao dhidi ya jingine.

Swali ni kwamba, kwani wanamtandao ni watu wema? Mbona inadhihirika wazi kwa vitendo vyao kwamba hakuna tofauti kati ya mtandao na ufisadi?

Je, mafisadi wanapogombana kundi moja likisema kwamba kundi jingine ni fisadi zaidi sisi Watanzania tunafaidika nini?

Tunachosema ni kwamba, mtandao ni ufisadi na yeyote aliyeshiriki kwenye kundi hili la mtandao kwa namna yoyote ile ajue wazi ameshiriki kikamilifu kujenga na kuimarisha ufisadi hapa nchini.

Kila mmoja ajichunguze alishiriki vipi kusaidia kundi hili kuingia Ikulu. Tunaweza kulaumiana bila sababu, tukubaliane kwamba kundi la mtandao halikuwa jema ndani ya CCM na si jambo jema ndani ya Tanzania kwani ni mwanzo wa mwisho wa CCM.

0755 312859
katabazihappy@yahoo.com
www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Machi 19 mwaka 2008

RAIS ANZA KUREJESHA NYUMBA YAKO SERIKALINI

Na Happiness Katabazi

UADILIFU wa serikali hautokani na hotuba nzuri za viongozi bali vitendo ambavyo viongozi hao wamevifanya na vinaonekana kwa wananchi.

Hapa nchini, ipo kanuni ya maadili ya viongozi inayosema uongozi ni dhamana.

Maana halisi ya kanuni hii ni kwamba, uongozi si mali ya mtu, wala nchi hii si mali ya kiongozi, bali vyote viwili ni mali ya wananchi.

Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), hasa Serikali ya Awamu ya Tatu na Awamu ya Nne, imeshindwa kutafsiri kanuni hii kwa kivitendo, badala yake viongozi wa CCM wanaamini kwamba uongozi wa nchi ni mali yao, na hakuna binadamu mwingine anayestahili kuupata. Pia nchi hii ni mali yao na wanaweza kufanya watakavyo.

Wanaweza kuuza mali ya serikali na kuuza nchi yenyewe bila kuulizwa na mtu. Aina hii ya mtazamo tumeiona katika uamuzi wa kuuza nyumba za serikali.

Jambo hili limepigiwa kelele sana na watu wenye heshima na maadili mema, wakisema mtumishi wa umma, hawezi kuchukua nyumba ya mwajiri wake na kuifanya yake au hata kuiuza.

Kitendo cha viongozi wa serikali ya CCM kujigawia nyumba za serikali ni aina nyingine ya ufisadi.

Nyumba zile zilianza kujengwa wakati wa mkoloni, zikaongezewa na uongozi wa Awamu ya Kwanza wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Awamu ya Pili.

Haikumithilika kamwe katika awamu hizo mtu kujiuzia nyumba za serikali, lakini, Rais mstaafu Benjamin Mkapa, tuliyeambiwa kuwa ni ‘Bwana Msafi’, ndiye aliyekuwa wa kwanza kuvunja mwiko huo.

Alijichukulia nyumba iliyopo pale Sea View, Upanga na kisha akawaruhusu wenzake wachukue nyumba walizokuwa wanakaa.

Mawaziri, makatibu wakuu, majaji na wakurugenzi, kila mmoja kwa nafasi yake alitafuta nyumba na kuinunua. Nyumba nyingine zilikarabatiwa kwa mamilioni ya fedha za walipa kodi na kisha zikauzwa kwa bei chee.

Je, ni halali nyumba ikarabatiwe kwa sh milioni 300 halafu ije kuuzwa kwa mtumishi wa serikali kwa milioni 30 au 40, tena fedha zenyewe anazilipa kwa awamu?

Kichekesho zaidi ni pale familia nzima, yaani baba, mama na watoto wawili eti kwa vile wote wanafanya kazi serikalini, kila mmoja amenunua nyumba ya serikali. Huu kama si ufisadi ni nini?

Jambo hili lilifanyika kwa usiri mkubwa bila kupata idhini ya Bunge. Tunashangaa hadi sasa hakuna hoja iliyowasilishwa bungeni kujadili ufisadi huu.

Tuelezane ukweli kwamba nyumba za serikali zimejengwa kwa kodi ya wananchi. Si halali watumishi wa serikali kugawana nyumba hizo kwa madai kuwa eti wameuziwa. Huo ni wizi.

Rais Jakaya Kikwete aliiga kampeni za washindani wake wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 kwamba endapo ataingia Ikulu, atazirejesha nyumba hizo.

Mara baada ya kuchaguliwa, Kikwete alilitangazia taifa kuwa yeye amekubali kuuziwa nyumba ya serikali baada ya kulazimishwa, lakini alilaani mpango mzima wa kuuza nyumba za serikali, kwamba ulikuwa mbovu.

Kwa kukubali kuchukua nyumba ya serikali, rais naye alishiriki kwenye dhambi hiyo, akawa mmoja wa waliozawadiwa nyumba hizo.

Rais aonyeshe mfano, aanze kwanza kurejesha serikalini nyumba yake ili wengine wafuate. Watanzania wamechoka kuwalipia viongozi na watendaji wa serikali mabilioni ya fedha kwa kuishi mahotelini, kwani wapo wanaolipiwa sh 300,000 kwa siku kwa kukaa hotelini baada ya serikali kukosa nyumba ya kuwaweka..

Hivi huo ubadhirifu wa kodi ya wananchi utaisha lini? Je, ni lini umaskini tutaupiga vita?

Mara ya mwisho wakati akiadhimisha miaka miwili ya kuwa Ikulu, Rais Kikwete alisema, serikali bado inaendelea na utafiti wa jinsi ya kurejesha nyumba hizo. Napenda kumuuliza, lini utafiti huo utakwisha na lini kazi ya kuanza kurejesha nyumba hizo itaanza?

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

Simu: 0755 312859.
katabazihappy@yahoo.com;www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Machi 12 mwaka 2008

RAIS HAFANYI MAAMUZI BILA KUUNDA TUME

Na Happiness Katabazi

NI miaka miwili tangu Rais Jakaya Kikwete aingie Ikulu, na katika kipindi hicho, hajawahi kufanya maamuzi yoyote kuhusu kero zinazowagusa wananchi bila kuunda tume.

Ni stahili nzuri ya uongozi unaojali misingi ya utawala bora na kuheshimu haki za binadamu, lakini si mara zote stahili hiyo inaweza kutumika. Kuna wakati Rais Kikwete alipofanya ziara kwenye wizara mbalimbali, alipofika Wizara ya Fedha, alisema ushahidi wa mazingira unatosha kumchukulia hatua mtumishi
bila kuthibitishwa na mahakama.

Lakini leo, hafanyi maamuzi mazito bila kwanza kuunda tume au kamati, hata kwa mambo yaliyo wazi kabisa, inawezekana stahili hiyo inatokana na kuwaonea aibu baadhi ya watendaji walio na uhusiano naye wa karibu.

Nikirejea kwenye hoja yangu ya uundwaji wa tume, wakati Watanzania walipokuwa wanakerwa na mwenendo wa Jeshi la Polisi ambalo lilikuwa limepoteza mwelekeo na kuwa sehemu ya ujambazi, rais aliunda tume iliyoongozwa na Jaji Mussa Kipenka, kuchunguza mauaji ya watu wanne wakazi wa Mahenge, mkoani Morogoro.

Tume hiyo ilifanya kazi nzuri na ilimtia matatani pamoja na watu wengine ACP-Abdallah Zombe ambaye hadi sasa anakabiliwa na kesi ya mauaji.

Tunakumbuka pia rais aliunda tume ya kuchunguza mikataba na sheria ya madini baada ya vilio vya Watanzania, akiwemo Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), kuwasilisha hoja binafsi bungeni, lakini Bunge likakengeuka na kutoa adhabu kwa kile walichokiita kulidanganya Bunge na kusema uongo dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi.

Alipofukuzwa Zitto, wananchi walihamaki, wakamuunga mkono rais naye akawageuka wabunge wa CCM kama kinyonga na kuunda tume kupitia upya mikataba ya madini na sheria zake. Tume hiyo ambayo pia yumo Zitto, bado inaendelea na kazi yake.

Hii ina maana kwamba rais hajui nini kinatokea kwenye sekta ya madini, wala kuna tatizo gani licha ya ukweli kwamba aliwahi kuongoza Wizara ya Nishati na Madini, hivyo anangojea tume aliyoiunda imletee mapendekezo.

Hivi majuzi tu, Bunge liliunda tume ya kuchunguza mkataba wa Richmond, uamuzi wa kuunda tume hiyo ulifanyika baada ya hoja hiyo iliyoasisiwa na upinzani, kuletwa na mbunge wa CCM.

Hoja hiyo ingeletwa na mbunge wa upinzani lazima ingepingwa kama ilivyopingwa hoja ya Buzwagi iliyowasilishwa na Zitto. Kwa hiyo Bunge letu lisijisifu sana eti limebadilika na kuanza kutetea maslahi ya wananchi.

Ukweli ni kwamba halijabadilika, ni Bunge lilelile la CCM, isipokuwa safari hii, lilikuwa na mpango maalum wa kujinusuru kutokana na tuhuma na kashfa nyingi zilizokuwa zikiikabili serikali.

Lakini tukirudi kwenye hoja, baada ya Dk. Harrison Mwakyembe kuwasilisha ripoti yake na aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa kulazimishwa kujiudhulu, kumekuwa na usemi kwamba rais alivunja Baraza la Mawaziri. Kwa hakika hilo halikutokea.

Kilichotokea ni kwamba Waziri Mkuu akijiudhulu, Baraza la Mawaziri linavunjika. Kwa hiyo hilo ni tukio la kawaida la kikatiba na wala Kikwete hastahili kupongezwa eti amevunja Baraza la Mawaziri.

Tatizo kubwa ni kwamba, rais aliyajua haya yote ya Richmond na Dowans, lakini hakuchukua hatua kwa kuwa wahusika walikuwa ni watu wake wa karibu, na ndiyo maana amekaririwa akisema yaliyompata Lowassa ni ajali ya kisiasa.

Maneno dhidi ya Richmond yalikuwa mengi kiasi cha kutohitaji hata kuunda tume kuchunguza tuhuma hizo. Je, ina maana kwamba rais hakuwa na uamuzi wowote hadi kuunda tume na itoe mapendekezo?

Kwenye fedha za EPA, kelele zilipigwa nyingi, lakini rais alinyamaza hadi taarifa ya Enrest &Young iliposema kuwa zaidi ya sh bilioni 133 zimeporwa, ndipo alipochukua hatua ya kubadilisha uteuzi wa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu (BoT), Daud Ballali ambaye hadi sasa hajulikani alipo.

Tukumbuke kuwa uchunguzi huo ulifanywa kutokana na shinikizo la wafadhili, kwani wizi huo pia ulibainishwa na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali, lakini serikali ilifumbia macho, hadi ilipopewa amri na wafadhili.

Zipo kashfa nyingi ambazo kwa stahili ya Rais Kikwete, kila moja inasubiri iundiwe tume na kutoa mapendekezo yake, jambo ambalo binafsi naliona si jema kwani kuna tuhuma ambazo hazihitaji kumaliza hela za walipa kodi kuundia tume.

Je, Rais Kikwete anangojea ashinikizwe ndipo uchunguzi ufanyike kuhusu kashfa zilizosalia? Kwa mfano lini tutaambiwa ukweli kuhusu gharama za ujenzi wa minara pacha ya BoT?

Je, ni kweli kwamba gharama hizo zilipandishwa kitapeli kutoka sh bilioni 83 hadi kufikia sh bilioni 523? .

Kama hoja hii inabeba ukweli wowote, basi Watanzania tujiandae kusikia habari kuhusu kashfa hii kubwa kuliko zote zilizowahi kuikabili Benki Kuu yoyote duniani.

Naamini hasira za Watanzania zitakuwa maradufu ya zile walizokuwa nazo kuhusu kashfa ya Richmond. Tatizo ni kwamba hakuna tume ilishaundwa na rais kuchunguza kashfa hii. Je, Rais Kikwete anangoja nini?

Kuhusu ufisadi utokanao na kashfa ya EPA, tayari tumeelezwa na serikali kwamba mafisadi hao wameanza kurejesha fedha. Tatizo lililopo ni njia ambayo serikali inataka kutumia kuwashughulikia mafisadi hao.

Nchi ina sheria ya jinai ambayo ikivunjwa, mtuhumiwa hufunguliwa mashitaka na kuamriwa na mahakama ya wazi kurejesha mali aliyoiba na pia kutumikia adhabu. Katika sheria zetu hatuna utaratibu wa mahakama za siri zinazoendeshwa na makachero wa Usalama wa Taifa.

Tukiruhusu mafisadi wakahukumiwa na mahakama za siri za aina hii, tutakuwa tumevunja msingi mkuu wa utawala wa katiba na sheria za nchi.

Lazima kila raia achukuliwe kuwa ni raia mwema na mtiifu wa sheria mpaka mahakama itakapothibitisha pasipo shaka kwamba ana hatia.

Hivyo, hatuko tayari kusikia kwamba mafisadi wanarejesha fedha kwa siri na kuachwa wakiendelea kutamba mitaani. Lazima sheria ichuke mkondo wake.


Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika
0755 312859
katabazihappy@yahoo.com
www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazei la Tanzania Daima la Alhamisi Machi 6,2008