AZIZA MURSALI

Kamishna wa kwanza mwanamke wa Jeshi la Magereza
*Ndiye alikuwa Naibu Kamishna Mwanamke Pekee
*Aeleza siri ya mafanikio yake jeshini
*Awaonya wanawake kutojilegeza

AZIZA Mursali (58) ni mmoja kati ya wanawake wachache waliopata mafanikio makubwa yaliyotokana na bidii na kujituma katika kazi. Akiwa miongoni mwa askari wachache wa kike waliojiunga na Jeshi la Magereza mwishoni mwa miaka ya 1960, alifanikiwa kupanda ngazi za kijeshi hadi kufikia cheo cha Kamishna na kuwa mwanamke wa kwanza katika historia ya jeshi hilo kutunukiwa wadhifa huo. Katika makala hii, Mwandishi Wetu Happiness Katabazi, anamuhoji mwanamama huyo siri ya mafanikio na misukosuko aliyokutana nayo katika maisha yake ya kazi ndani ya jeshi hilo.

Swali: Kitu gani kilikusukuma kujiunga na Jeshi la Magereza?

Jibu: Nilikuwa na mapenzi ya Jeshi la Magereza tangu nilipokuwa msichana mdogo bila kujua ni kwa sababu gani, lakini ilitokea tu nikawa napenda kuwa Askari wa Magereza.
Kama Mungu alijua kuwa nalipenda jeshi, baada tu ya kumaliza masomo yangu nililetewa barua ya kutakiwa kujiunga na Jeshi la Magereza kutoka iliyokuwa Idara ya Kazi wakati huo. Enzi hizo kulikuwa na utaratibu wa vijana wanaomaliza shule kupangwa kufanya kazi katika idara mbalimbali au kujiunga na kozi. Bila kusita niliikubali nafasi hiyo, ndiyo hivyo.

Swali: Wewe ni mwanamke mwenye mafanikio makubwa ndani ya Jeshi la Magereza, siri ya mafanikio yako ni nini?

Jibu: Siri ya mafanikio yangu ni utii, uaminifu, ukweli, juhudi na bidii kazini, lakini kikubwa ni kujiendeleza. Katika maisha yangu nimekuwa nikijiendeleza bila kuchoka, imani niliyojijengea kuwa elimu haina mwisho ndiyo iliyonisaidia na kufika hapa nilipo.

Swali: Wewe ni kiongozi wa kijeshi, kwa cheo chako haina shaka una majukumu mengi na makubwa, unaweza kumudu kazi yako na kutunza familia yako?

Jibu: Ukitaka mafanikio katika kazi yoyote ni lazima ujiwekee taratibu ambazo ni lazima uzifuate, kwa kuzingatia taratibu nilizojiwekea nimekuwa nikipanga ratiba ya kazi zangu na za familia yangu. Ninachofanya ni kuhakikisha ratiba zangu za nyumbani hazivurugi taratibu ya kazi za mwajiri wangu. Ingawa kazi za jeshi ni amri, lakini ninao muda mwafaka wa kuwa na familia yangu, mara nyingi natumia muda wa jioni, siku za sikukuu na likizo.

Mwanamke hatakiwi kubweteka, kama tunapiga kelele za usawa ni lazima tuonyeshe kweli tunaweza, na nimekuwa nikifanya kazi kwa bidii siku zote ili kuthibitisha hilo.
Imenisaidia na hata kama ningekuwa si askari na kuwa ninaishi kijiji, ningelima kwa bidii, ni mpangalio tu na uamuzi, kama mtu umeamua kweli kufanya na kazi kuachana na uzembe na utegemezi hakuna kinachoshindikana.

Swali: Kuna madai kuwa nafasi za kujiunga na jeshi zinatolewa kwa upendeleo, ni lazima muombaji awe na mtu anayemjua wa kumfanyia mpango, unalizungumziaje hili?

Jibu: Huo ni uongo. Ajira kwa vijana wanaotaka kujiunga na jeshi zinatangazwa magazetini, pia kuna matangazo mbalimbali yanayobandikwa hadi vijijini kuelezea sifa zinazotakiwa kwa waombaji.Waombaji hujadiliwa na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na wanaochaguliwa huchujwa na Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa, wenye sifa huchaguliwa na Magereza huwa hawabadili uamuzi wa vikao vya Ulinzi na Usalama vya mikoa.

Swali: Kwa mtizamo wako, viongozi wanawake ndani na nje ya jeshi hapa wanatosha?

Jibu: Idadi ya wanawake viongozi hapa nchini haina uwiano sawa na wanaume, hilo liko wazi. Wito wangu kwa Watanzania, kila mtu kwa nafasi yake aone umuhimu wa kuwapa elimu wasichana. Ni lazima tukubali kuwa wanawake wanaweza kuwa viongozi wazuri, inategemea na malezi na jinsi wanavyowezeshwa. Mfano hai ni mimi. Pamoja na wengine ambao tunalitumikia taifa letu katika ngazi mbalimbali za uongozi, wanawake tupo na hivi sasa tunajivunia kuwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro. Kikubwa, nasisitiza hili, ni malezi na kuwezeshwa.

Swali: Ukiangalia enzi ulizojiunga na jeshi na sasa, ukakamavu mliokuwa nao wanawake wakati huo ni sawa na walionao wasichana wa sasa.

Jibu: Sioni tofauti kubwa kati ya askari wa kike wa karne ya 20 na wa karne ya 21, tofauti ndogo iliyopo ni kwamba askari wa kike wa enzi zetu ni wavumilivu sana. Unajua wakati huo wasichana wengi wasomi hawakutaka kujiunga na Magereza, tuliojiunga tulikuwa na nia na dhamira ya kweli ya kulitumikia jeshi, ndio maana tumefanya kazi katika mazingira magumu kwa miaka mingi kwa uaminifu bila kukata tamaa. Lakini kwa hivi sasa watu wanaangalia maslahi kwanza, ule moyo wa kujituma kizalendo umefifia.

Swali: Ni tukio gani kubwa katika maisha yako jeshini au kabla hujajiunga na jeshi ulilokutana nalo ambalo hutalisahau.

Jibu: Ni kifo cha Mwalimu Julius Nyerere...Unajua yule alikuwa kiongozi kweli, ninaweza kusema hata moyo wa kujiunga na jeshi mimi na baadhi ya wenzangu tuliupata kwake. Alikuwa kiongozi aliyekuwa akiwajenga vijana wa Kitanzania kuipinda nchi yao, kuwa na moyo wa kizalendo, tulikuwa tunaipenda kweli Tanzania yetu.

Swali: Kuna haya madai ya kuwapo kwa unyanyasaji wa kijinsia kwa askari wa kike kunakofanywa na askari wa kiume jeshini. Je, madai haya yana ukweli wowote?

Jibu: Ninalolifahamu mimi ni Jeshi la Magereza, hivyo nitalizungumzia hilo. Kwanza kunyanyaswa kijinsia ni udhaifu binafsi. Ukweli ni kwamba ndani ya Jeshi la Magereza hakuna huo unyanyasaji, wala askari wa kike kunyanyaswa na askari wa kiume hakuna Tatizo hapo ni moja nililoligundua mimi - kudeka! Baadhi ya wanawake wanapenda kudeka, na jeshini ni amri ndugu yangu, sasa kama mtu ana tabia ya kudekadeka au kujirahisirahisi, popote pale watadhani kuwa ananyanyaswa.

Swali: Mabadiliko yanayofanywa sasa na serikali katika Jeshi la Magereza unayaonaje, yanawaridhisha ninyi askari?

Jibu: Sana, tena kwa kiasi kikubwa sana. Unajua mahali popote kama unawataka watu wafanye kazi vizuri, ni lazima uwawezesha, si siri, hapo nyuma askari tulikuwa na hali mbaya sana lakini sasa hali imebadilika, serikali inawatupia jicho askari wake na ninaomba iendelee kufanya hivyo.

Tuna mafanikio mengi, mfano tumepewa zabuni ya ujenzi wa nyumba za serikali na tumemudu kuzijenga kwa ubora wa hali juu, magereza mapya yamejengwa sehemu mbalimbali nchini sambamba na upanuzi na ukarabati wa magereza ya zamani.

Lakini hata wafungwa hali zao zimeboreshwa, sasa wanavaa shati na suruali badala ya kaptura zilizokuwa zinadhalilisha utu wao, sasa magereza yana radio za kisasa na televisheni zinazotoa mafunzo burudani kwa wafungwa, haya yote ni mafanikio.

Lakini pia serikali imewakumbuka zaidi wanawake. Sasa yupo mkuu wa Magereza wa mkoa mmoja - Boharia Mkuu wa Jeshi la Magereza mmoja ambaye ni Kamishna Msaidizi Mwandamizi Edith Malya, Mkuu wa Chuo cha Udereva mmoja, yeye ni Kamishna Msaidizi Grace Ungani, pia yupo Katibu wa Bodi ya Parole Magereza nchini, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Simfroza Bondo pamoja na maofisa nidhamu wa mikoa wawili. Hizi zote ni jitihada za serikali kulifanyia mabadiliko Jeshi la Magereza.

Swali: Tueleze historia ya maisha yako.

Jibu: Nizaliwa 1950 katika Kijiji cha Mazombe, Wilaya ya Iringa Vijijini. Mimi pamoja na ndugu zangu tisa tulilelewa na mama baada ya baba kufariki mwaka 1958 tukiwa bado wadogo.
Mama ni mkulima, aliolewa na mwanamume mwingine baadaye, baba yetu huyo wa kambo alitusomesha mimi, kaka yangu na wadogo zangu watatu hadi elimu ya sekondari, huwa tunamshukuru sana baba huyu.

Nilihitimu masomo ya sekondari mwaka 1968 katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara. Na mwaka huo huo nilijiunga na Jeshi la Magereza. Kituo changu cha kwanza cha kazi kilikuwa Gereza la Wanawake KPF - Morogoro.

Mwaka 1969 nilihudhuria mafunzo ya uaskari katika Chuo cha Magereza Ukonga kwa muda wa mwaka mmoja. Mwaka 1971 nilirudi tena katika Chuo cha Magereza Ukonga kwa kozi fupi ya uongozi na mwaka huo huo nilikwenda kusoma Elimu ya Siasa katika Chuo cha Kivukoni.

Baadaye mwaka 1974 nilijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama mwanafunzi wa nje wa chuo, ambako nilisoma kozi ya sheria na nilihitimu na kutunukiwa cheti mwaka 1976.

Mwaka 1976 nilikwenda tena Ukonga kusoma kozi ya Gazzetted Officer na baadaye mwaka 1981 nikarudi Kivukoni kwa ajili ya kozi ndefu elimu ya siasa na kisha mwaka 1984 nilikwenda nchini Burgaria kwa ajili ya kozi ya mwaka mmoja ya Social Science & Management course.

Hivi sasa ninasomea Shahada ya Sheria (LLB) katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania nikiwa mwaka wa mwisho.

Katika kipindi changu cha utumishi ndani ya Jeshi la Magereza nilishika pia wadhifa wa Katibu Msaidizi Mkuu wa Chama wa Mkoa wa Majeshi kwa muda wa miaka mitano Nilikuwa Katibu Mkuu Msaidizi wa Chama wa Mkoa wa Majeshi kabla ya Tanzania haijaingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa 1992.

Mkoa wa Majeshi ilikuwa ukiundwa na vikosi vya Ulinzi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Polisi na Magereza.

Katika vipindi tofauti nimefundisha katika vyuo vya kijeshi kikiwamo Chuo cha Usalama Moshi na Chuo cha Maofisa wa Magereza Ukonga. Aidha, nimewahi kuwa Mkuu wa viwanda vya Magereza nchini, hivyo naamini nina sifa za kuwa kiongozi.

Niliteuliwa kuwa Kamanda wa Magereza Mkoa wa Kagera Oktoba 17, 2003. Nimeolewa na Said Kangwi, mwenyeji wa Kijiji cha Mkanyageni, Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga. Nina watoto wanne - wasichana watatu na mvulana mmoja.

Katika maisha yangu ya utumishi jeshini nimetunukiwa medali mbalimbali ikiwamo ya utumishi uliotukuka niliyotunukiwa mwaka 1996 na nishani ya utumishi wa muda mrefu mwaka 1999.Na Agosti mwaka jana nilipandishwa cheo na kuwa Kamishna mwanamke pekee magereza, kabla ya kupandishwa cheo hiki nilikuwa na Cheo cha Naibu Kamishna ambacho nimedumu nacho kwa miaka mitatu na wakati wote nikiwa na cheo hicho cha DCP nilikuwa nacho mwanamke peke yangu.

0755 312859:
katabazihappy@yahoo.com
www.katabazihappy.blogspot.com

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima, la Jumapili April 2008

TUME YA MAADILI NI KICHAKA CHA UFISADI

Na Happiness Katabazi

IJUMAA iliyopita, asasi tano zisizokuwa za kiserikali zilifungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, kupinga kanuni ya 6(1) na 2 na 7(2)(c) ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Kanuni ya 6(1) na (2) inakataza vipengele ambavyo vinaweka pingamizi visivyo vya lazima, vya kumzuia mwananchi kuwa na haki ya kupata taarifa zinazotolewa na viongozi wa umma kuhusu rasilimali, mapato au madeni yao.

Asasi zilizofungua kesi hiyo ni Mtandao wa Asasi zilizo Kusini mwa Afrika zinazojishughulisha na Masuala ya Haki za Binadamu (SAHRINGON), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISATAN), Asasi inayojishughulisha na Haki za Wanawake (KIVULINI) na Shirika la Kitaifa la Msaada wa Sheria (nola) na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA).

Hati ya madai ya asasi hizo, inadai kwamba kifungu cha 7(2) (c) kinachozuia mtu aliyepata fursa ya kuona mali za kiongozi wa umma kuzitangaza hadharani, kinapingana kabisa na Ibara ya 18 ya katiba ya nchi yenye vipengele (a), (b), (c) na (d) ambavyo vinampa raia wa Tanzania haki ya kupata habari.

“Vifungu hivyo vinavunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 132 kifungu kidogo cha 4 na cha 5(b), na pia kwenye sheria hiyo ya maadili kanuni ya 9, kifungu kidogo cha (1) na kanuni ya 14, ambavyo vinatoa mwanya wa kufunguliwa kesi ya jinai kwa mtu au chombo chochote kitakachotoa taarifa kuhusu mapato, rasilimali na madeni ya viongozi wa umma,” ilisema sehemu ya hati hiyo ya madai.

Kutokana na hali hiyo, asasi hizo zimefungua kesi hiyo kuomba tafsiri ya mahakama na pia kuitaka mahakama itamke kuwa kanuni hizo za Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1995 ni batili kwa kuwa inapingana na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambayo ndiyo sheria mama ya nchi yetu.

Hii ina maana kwamba yeyote anayetaka kujua ni lazima aende mwenyewe kwa Kamishna wa Tume ya Maadili alipe ada ya sh 1,000 na akishapata habari hizo arejee nyumbani akalale usingizi. Kwa kifupi vipengele hivyo vinatumika kama kichaka cha kuficha ufisadi.

Sisi Watanzania tuna wajibu wa kutumia kila njia kujenga miundombinu ya kiutawala na kisheria itakayoweza kuzuia ufisadi.

Moja ya miundombinu ya kisheria ni Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, lakini sheria hiyo kwa kuweka vipengele hivyo ni kukumbatia ufisadi kwa maana ingekuwa mali za viongozi zinawekwa hadharani, leo hii tungejua wazi Andrew Chenge ana vijisenti kwenye akaunti yake huko Kisiwa cha New Jersey au bingo aliyopata.

Kutoturuhusu tujue hilo, ni kutunyima fursa ya kumpima huyu kiongozi kama ni mkweli au mlaghai.

Na hii ina maana kwamba Chenge hajataja akaunti yake hiyo kama sehemu ya akaunti zake. Ameidanganya tume na anastahili kufunguliwa mashtaka.

Vivyo hivyo sheria hii imetunyima fursa ya kujua kwamba Rais mstaafu Benjamín Mkapa ‘Bwana Msafi’ na washirika wake, walitangaza mali zao na kuwa wanamiliki Kampuni ya Tanpower.
Ukweli ni kwamba lipo kosa la jinai kama viongozi hawa hawakuandikisha mali zao hizo kwa Kamishna wa Tume hiyo na wanastahili kushtakiwa haraka iwezekanavyo.

Hii ni sehemu tu ya mashtaka ambayo yanaweza kuwakabili waheshimiwa hawa kama Rais Jakaya Kikwete ataacha tabia yake ya kuwakumbatia mafisadi na badala yake kusimamia sheria na katiba kama alivyoahidi kwenye kiapo chake pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Desemba 21 mwaka 2005.

Vipengele viwili tunavyovijadili vya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ni vichache tu kati ya sheria nyingi mbovu zinazowaletea wananchi wasiwasi na mkanganyiko wanapojadili uvunjwaji wa katiba na ufisadi.

Mfano, tunajua kwamba katiba inamlinda rais aliye madarakani na mstaafu na kuwawekea kinga wasishtakiwe kwa makosa yatokanayo na utekelezaji wa madaraka yao ya urais.

Swali ni je, pale rais aliyepo madarakani au mstaafu wanapogundulika kwamba wametumia madaraka kujinufaisha binafsi, kinga hiyo bado itasimama?

Kwa fikra zangu, naona kinga hiyo haiwezi kuwalinda viongozi wanaotumia nafasi zao za uongozi kwa maslahi yao binafsi.

Hivyo sitaki kusikia ile hoja ya Rais Kikwete aliyoitoa mwaka jana, kwamba ‘hatafuatilia tuhuma za ufisadi au uvunjwaji wa sheria na katiba zinazomkabili mtangulizi wake Mkapa.’

Naamini kwamba hoja hiyo ya rais si sahihi kwa kuwa tumeanza kugundua kwamba, Rais mstaafu Mkapa, hakuwa mwadilifu kwa taifa letu.

Itatusaidia sana kupambana na ufisadi kama uchunguzi huru ungefanyika kuthibitisha kama kweli Mkapa alitumia muda wake wa urais kujilimbikizia mali, yeye na familia yake.

Kwa vyovyote vile, hilo lisipoeleweka, vita dhidi ya ufisadi itakuwa imetushinda. Lakini vile vile tujadili hoja ya mwenendo wa hivi sasa wa viongozi waliotuhumiwa kuhusika na ufisadi, kung’ang’ania madaraka mpaka walazimishwe kujiuzulu.

Kweli hiyo inathibitisha kwamba utamaduni wa uwajibikaji unaozingatia usafi usiotiliwa shaka wa viongozi wa umma, haujajengeka bado hapa Tanzania.
Kwa hiyo, kiongozi anapotuhumiwa anawajibu kwa kiburi, dharau, kejeli wale wanaomtuhumu kana kwamba wamemzulia kashfa zisizo na msingi.

Hii ni tamaa na ulafi wa madaraka, na ni ushahidi tosha kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshindwa kulea viongozi waadilifu na wenye kuheshimu wananchi.

Kero hii inaenda sambamba na kero ya Rais Kikwete kushindwa kufanya maamuzi na kuchukua hatua kali na kuwawajibisha viongozi wa aina hii.

Rais Kikwete amekuwa mtumwa wa tume za uchunguzi, kana kwamba hana vyombo vya dola vya kumshauri. Pia kwa tabia hii ya kuwaruhusu mafisadi wajiuzulu, inathibitisha kwamba rais anawakumbatia, na kwamba hayuko tayari kuwawajibisha.

Lakini athari za hili ni kwamba, viongozi wanaondoka na marupurupu yao na haki zingine ambazo wangenyimwa kama wangefukuzwa kazi.

Pia inaonekana kana kwamba kwa kujiuzulu, viongozi hawa wamekwepa msumeno wa sheria ambao ni kufunguliwa mashtaka mahakamani na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria.

Kwa mantiki hiyo, mawaziri wanapojiuzulu kwa kashfa za ufisadi, wamekuwa na tabia ya kutojiuzulu ubunge kana kwamba ni jambo la heri kuwa na wabunge mafisadi.

Sifa za uongozi na maadili ya uongozi yanayowabana mawaziri, ni sawa na yale yanayowabana wabunge. Kwa hiyo, haitoshi kujiuzulu uwaziri ukabaki kuwa mbunge.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0755 312859
katabazihappy@yahoo.com

Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, April 30, 2008