MJUMBE WA NEC CCM MATATANI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Biashara jijini Dar es Salaam, imemwamuru mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (CCM), Ramadhani Madabida na wadaiwa wengine wanne kulipa zaidi ya sh milioni 699 walizojipatia kama mkopo kutoka Benki ya Stanbic jijini Dar es Salaam.

Uamuzi huo ulitolewa hivi karibuni na Jaji Frederick Werema, ambaye alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuridhishwa na hoja na ushahidi uliotolewa na mlalamikaji, Dilip Kesaria na Meneja wa benki hiyo, Charles Daniel.

Kwa mujibu wa nakala ya hukumu hiyo, wadaiwa wengine mbali na Madabida ambao nao wametiwa hatiani baada ya kushindwa kurejesha sh 699,860,717 kama mkopo walioupata kutoka kwa benki hiyo ni Kampuni ya Pharmaceutical Investment, Mpewani Trading, Global Trading na Mkurugenzi wa Kampuni ya Pharmaceutical, Salum Shamte.

Jaji Werema alisema mbali ya kuwaamuru wadaiwa hao kurejesha mkopo huo, pia amewaamuru walipe fidia ya asilimia 15 kwa mwaka, kuanzia Septemba mosi 2007 hadi Mei 22, mwaka huu, ambapo hukumu hiyo ilitolewa, na asilimia saba tangu siku ya kutolewa kwa hukumu.

Aidha, Jaji Werema amemtaka Madabida na mwenzake kulipa gharama za uendeshaji wa kesi hiyo kwa Benki ya Stanbic, ambaye ndiye mlalamikaji katika kesi hiyo.

Ilidaiwa kuwa Benki ya Stanibic katika shughuli zake za kibenki ilitoa mkopo kwenye Kampuni ya Pharmaceutical na baada ya Madabida na wenzake kuweka dhamana (guarantee). Hadi kufikia Oktoba 31, 2003 deni lilifikia sh 1,110,444,611 na baadaye kupunguzwa na kufikia sh 971,861,074/-.

“Pamoja na hayo, benki ilipunguza tena deni hilo na kufikia sh milioni 800 Mei 2004 . Na kwakuwa Kampuni ya Pharmaceutical haikuwa na uwezo wa kulipa deni hilo, benki ilipunguza tena deni hilo na kufikia sh milioni 529 ambazo zingelipwa kwa miezi 24, ambapo kila mwezi wadaiwa wangelipa sh 25,649,436 pamoja na faida.

Hata hivyo, wadaiwa walishindwa kurejesha deni hilo, hali iliyosababisha benki kutoa taarifa kadhaa za kuwakumbusha wadaiwa kulipa deni hilo na ilipofika Agosti mosi 2007 deni lilifikia sh 699,807,717, jambo ambalo liliilazimu benki hiyo kufungua kesi katika mahakama hiyo.

Katika hukumu yake, Jaji Werema alisema ameridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo kuwa Benki ya Stanibic ilitoa mkopo kwa Kampuni ya Pharmaceutical, hivyo kutokubaliana na wadaiwa, ambapo Madabiba na wadaiwa wengine walipinga vikali kuhusika na deni hilo.

“Baada ya kupitia kwa hoja na ushahidi uliotolewa na pande mbili katika kesi hii nimebaini kuwa kulikuwepo na majadiliano kadhaa kati ya pande zote mbili, ambapo nyaraka zilizoletwa mbele yangu zimebainisha kuwapo kwa mkopo ambao ulipunguzwa na kufikia sh milioni 529, ambazo zingelipwa kwa kipindi cha miezi 24.

Aidha, Jaji Werema alisema katika nyaraka hizo zimeonyesha makubaliano ambayo yalisainiwa na Madabida kama Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Pharmaceutical ambayo ndiyo ilikuwa mkopaji mkuu na pia Madabida alisaini kama Mkurugenzi na mtoa dhamana (guarantor) wakati Shamte na mkewe Madabida anayeitwa Zarina Madabida, ambaye ni Mwenyekiti wa UWT-CCM Mkoa wa Dar es Salaam, ambao wote ni wakurugenzi wa kampuni hiyo walisaini kama watoa dhamana (guarantors).

Kwenye utetezi wao, wadaiwa kupitia Madabida walikana kuhusika na deni hilo na badala yake alidai benki ndiyo iliyopaswa kumlipa fidia ya dola za Marekani 105,000, ambazo alitozwa na Medical Store Department (MSD), baada ya benki hiyo kuchelewa kufungua kile alichokiita Local Letters of Credit.

Alidai kuwa Kampuni ya Pharmaceutical iliingia mkataba na MSD ya kusambaza au kuwapatia dawa mbalimbali za thamani ya dola za Marekani milioni 5.1, ambazo wangeziagiza kutoka nje ya nchi na kwa kuwa kampuni hiyo haikuwa na mtaji wa kutosha, iliiomba MSD ifungue hiyo Local Letters of Credit ambapo wangeitumia kufungua kile alichokiita ‘Slave Letters of Credit’.

Madabida aliiambia mahakama kuwa MDS ilitimiza utaratibu huo mwaka 1997 lakini Benki ya Stanbic ilikataa utaratibu huo na baadaye kubadili uamuzi wake na kuikubalia MSD kufungua hiyo Local Letters of Credit mwaka mmoja baadaye na hivyo kuchelewesha usambazaji wa dawa hizo, kitendo kilichoigharimu kampuni na kutozwa kiasi hicho cha pesa kama fidia.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Juni 1, 2009

RAUNDI YA KWANZA LIYUMBA KIDEDEA,DOLA IMEJIFUNZA NINI?

Na Happiness Katabazi

VITA ya dhidi ya ufisadi vilianza kwa kishindi.Kwa kishindo hicho hicho vita ya ufisadi itaisha kwani.Kwani ni ufisadi mtupu na usanii mtupu.


Sheria ya TAKUKURU ya 2006 ilitungwa kwa shinikizo la wafadhili, serikali iliburuzwa miguu kwa miaka kadhaa lakini hatimaye ilisalimu amri pale wafadhali walipotishia kuwa hawatatoa mikopo, misaada katika nchi ambazo hazitaaonyesha nia ya kupambana na rushwa(ufisadi sasa), dawa za kulevya na ugaidi.

Tanzania ilisalimu amri moja kwa moja ikatunga sheria ya Ugaidi ambayo ni kinyume kabisa na haki za binadamu na ikatunga sheria ya rushwa iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2006 ambayo inatumika hivi sasa.

Kwahiyo serikali yetu haikuwa na nia ya dhati ya kupambana na majanga hayo, sheria hizo zilitungwa kishabiki,kishikaji na kisanii.

Mawazo ya wananchi ya kutaka ziundwe taasisi huru ya kijamii zenye uwezo wa kupambana na majanga hayo ziligonga mwamba hiovyo nleo hii sheria hizo hazimgusi rais na makamu wake, ,rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu.

Hivyo ikiwa rais ni gaidi au ikiwa rais ni fisadi hakuna njia ya kumdhibiti.Taasisi ya Takukuru ni mbwa asiye na meno mbele ya viongozi hao.

Vivyo hivyo sheria za nchi kama ile ya Kanuni ya Adhabu(Penal Code),hazikubadilishwa kuunda dhana na makosa mapya yanayoendana na hali halisi ya majanga hayo yakiwemo wizi wa kutumia mitandao.

Hata neno ufisadi ulikuti katika sheria hizo.Sasa kesi zilizofunguliwa dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi na zitakazofunguliwa zitajikuta hazina mguu wa kusimama kisheria.

Hivyo Watanzania wasije kushangaa watuhumiwa kwa kesi za aina hiyo wakiachiwa huru kwa makosa ya kiufundi yaliyofanywa au yatakayofanywa na mawakili wa serikali bila hata kujibu kesi zenyewe.

Hii inatufanya tuamini kwamba baadhi ya watuhumiwa walipelekwa mahakamani kiusanii tu ili kukidhi haja ya kuwwarisha wafadhali kwamba serikali ya awamu ya nne ni makini ni shupavu katika vita dhidi ya rushwa,ufisadi,dawa za kulevya na ugaidi.

Ndiyo maana Rais wetu Jakaya Kikwete sasa ni rais bora wa Afrika ana haki ya kukaribishwa Ikulu ya Marekani,Ikulu ya Elysee-Ufaransa ,Ikulu ya Uingereza Buck Gham , kwasababu huyu sasa ni shujaa wa Afrika katika vita dhidi ya ufisadi ,ugaidi na dawa za kulevya.

Haijalishi kwamba ukweli usiopingika ni kwamba aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala(BoT) Amatus Liyumba na Meneja Mradi wa benki hiyo, Deogratius Kweka waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya jinai namba 27/2009 iliyokuwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Alhamisi wiki hii, walishinda mzunguko wa kwanza katika vita hivyo vya ufisadi dhidi ya Serikali, baada ya mahakama hiyo kuwaachilia huru baada ya kubaini hati ya mashtaka imekosewa.

Haijalishi kwamba mtandao wa dawa za kulevya umeongezeka na Mafisadi Papa wanaotumia vijana wetu kusafirisha dawa hizo ndani na nje ya nchi hawajakamatwa.


Jeshi la Polisi wanawajua,Rais alisema anawajua hao mafisadi papa wa dawa za kulevya.Je tuseme kwamba hawa ni ndege wa mabawa yanayofanana na hivyo wanaruka pamoja?

Hiki kimya cha kuficha mapapa wa dawa za kulevya serikali ya awamu ya nne imekipata wapi?

Rais wetu alivyoingia madarakani alitutangazia kuwa ana orodha ya mapapa hao na kuwa angewataja na wangeshughulikiwa, mbona ajamtaja hata mmoja?

Wasiwasi wetu mkubwa ni kwamba Liyumba ,anayedaiwa kuwa ni marehemu ambaye alikuwa ni Gavana wa BoT, Daud Balali, Danile Yona, Basil Mramba,Gray Mgonja na wale wote ambao wanatuhumiwa kwa kashfa za ufisadi ambazo zipo kesi mahakamani au hazipo mahakamani wanaoenekana ni watu wa serikali na wanachama wa Chama cha Mapinduzi(CCM).

Rais Kikwete na serikali yake na chama chake hawana haja ya kuomba tena kuchaguliwa ikiwa hawataweza kulimaliza hili sakata la ufisadi.

Lakini Watanzania tujiulize pia kama ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)inayoongozwa na Johnson Mwanyika na ile ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)inayoongozwa na Eliezer Feleshi zimejipanga inavyostahili kupambana na ufisadi unaotishia ulinzi na usalama wa dola hivi sasa?

Kilichojionyesha katika kuachiliwa huru kwa Liyumba na kisha kukamatwa kwa muda mfupi na Alhamisi kufunguliwa kesi upya, ni udhaifu katika taaluma ya uendeshaji mashtaka kwa mujibu wa Sheria za Jinai.

Pamoja na kwamba mawakili wa serikali wanaoendesha kesi hizo waandamizi,inadhiirika kwamba taaluma yao kisheria haitoshi.

Je hii siyo ishara mbaya katika kesi zote za matumuzi mabaya ya ofisi za umma na wizi wa EPA zilizopo mahakamani hivi sasa?

Je hivi sasa si kweli kuwa mafisadi ambao hawajafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kashfa ya ununuzi wa Rada, ndege ya rais, , helkopta za JWTZ, Kagoda, Kiwira,Meremeta,Tangold, wanasherehekea na kugonganisha glasi zao za mvinyo?

Tayari upande wa serikali katika baadhi ya kesi zilizopo katika Mahakama ya Kisutu kwa sisi ambao siku tano za juma tunashinda hapo ,tumeshuhudia wameonyesha kubabaika kwa kubadilishabalisha hati za mashtaka kwa kuongeza au kupunguza mashtaka.

Je itakapotekea watuhumiwa wa kuachiriwa huru si kesi zitakuwa zimekwisha kwa kishindo kile kile kama zilivyofunguliwa kwa kishindo?

Tuseme nini sasa.usanii mtupu au ufisadi mtupu unaofanywa na mawakili wetu wa serikali?

Kama mawakili wa serikali hawana taaluma ya kutosha kwanini wasiombe ushirikiano wa kitaalum toka kwa mawakili wengine wenye ujuzi ambao mawakili wengine binafsi walikuwa walimu wenu vyuoni?

Serikali sasa iache uchoyo na ukiritimba katika mambo ya kitaaluma, ipende kushirika wanataluuma wenye uwezo kwenye maeno yao. Naomba kutoa hoja.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Mei 31, 2009

LIYUMBA MWIBA MKALI

.Sasa apumua .aweza kutoka sero Juni Jumatatu

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, jana imelegezea masharti ya dhamana kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, ambaye anakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.


Hatua hiyo inatoa uwezekano mkubwa kwa mshitakiwa huyo, aliyesota mahabusu kwa siku 114, kuwa nje kwa dhamana Jumatatu ijayo - Juni Mosi mwaka huu, endapo atakamilisha masharti mapya ya dhamana.

Uamuzi wa kulegeza masharti ya dhamana mpya, ulitolewa jana na Hakimu Nyigumalile Mwaseba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambaye kabla ya kusoma uamuzi huo, alikumbusha kuwa katika shauri hilo dhamana ilikuwa haibishaniwi bali kilichokuwa kikibishaniwa ni masharti ya dhamana.

Kwa uamuzi huo, Liyumba sasa atatakiwa atoe fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya sh milioni 300, wadhamini wawili watakaosaini bondi ya sh milioni 50 kila mmoja, kutotoka nje ya Dar es Salaam hadi kwa kibali maalum na kusalimisha hati ya kusafiria mahakamani.

Masharti hayo ni tofauti na awali, ambapo alitakiwa awe na wadhamini wawili wa kuaminika, ambao wangesaini bondi au kuwasilisha hati yenye thamani ya nusu ya kiasi cha sh bilioni sh 221, anachotuhumiwa kuisababishia serikali hasara.

Sharti lingine la awali lilikuwa kuacha hati za kusafiria mahakamani, kuripoti katika ofisi za Takukuru kila siku ya Ijumaa na kutotoka nje ya Dar es Salaam bila ya kibali cha mahakama.

Juzi, mawakili wa serikali, wakiongozwa na Justus Mulokozi, John Wabuhanga na Prosper Mwangamila, waliiomba mahakama itoe dhamana kwa mujibu wa kifungu Na. 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho 2002.
Kifungu hicho kinasema ili mshitakiwa apate dhamana, lazima awasilishe mahakamani nusu ya fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya nusu ya mali ya mtuhumiwa anayodaiwa kuiba.

Akitoa uamuzi ambao umemfanya Liyumba apumue, Hakimu Mwaseba alisema amesikiliza hoja za pande zote mbili na kulazimika kukubaliana na hoja za mawakili wa utetezi kwamba, ni kweli kifungu hicho kamwe hakipaswi kutumika katika mashitaka mapya yanayomkabili mshitakiwa huyo.

Alisema, hakuna ubishi kwamba mashitaka yanayomkabili Liyumba ni yale ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia hasara serikali ya sh bilioni 221, hivyo mashitaka hayo ni tofauti kabisa na yanayoainishwa kwenye kifungu hicho.

Akisoma kwa makini uamuzi huo, Mwaseba ambaye ni mmoja wa mahakimu vijana wa mahakama hiyo, alisema ameamua kutupa ombi la upande wa mashitaka la kutaka kifungu hicho kitumike kumpa dhamana Liyumba.

“Nakubaliana na hoja za mawakili wa utetezi kuwa kifungu hicho kamwe hakipaswi kutumika katika mashitaka yanayomkabili mshitakiwa na kwa sababu hiyo natupilia mbali ombi la upande wa mashitaka lililotaka mahakama hii itumie kifungu hicho katika kumpatia dhamana mshitakiwa na endapo upande wa mashitaka haujaridhika na uamuzi wake, unaweza kukata rufaa,” alisema Mwaseba na kusababisha mawakili wa serikali kujiinamia.

Baada ya kumaliza kutoa uamuzi huo, wakili Magafu aliomba mahakama kuahirisha kwa muda kesi hiyo hadi saa saba mchana jana ili mteja wake aweze kukamilisha masharti hayo.

Lakini wakili wa serikali, Mulokozi alipinga hoja hiyo kwa madai kuwa, wana shughuli nyingine na kupendekeza iahirishwe hadi tarehe nyingine.

Hata hivyo, Mwaseba alikubaliana na Mulokozi na kuahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu ijayo ambapo itakuja kwa ajili ya kukamilisha masharti ya dhamana na kama yatakamilika, Liyumba atakuwa nje kwa dhamana.

Baada ya hakimu kuondoka katika chumba cha mahakama, ndugu na jamaa wa Liyumba waliruka kwa furaha, huku wengine wakienda kizimbani kumbusu mshitakiwa huyo pamoja na kuwapongeza mawakili wake kwa kupambana katika kesi hiyo hadi kufikia hatua hiyo.

Wakati hayo yakifanyika, mawakili wa serikali walionekana kupooza na kuamua kubeba makabrasha yao na kuanza kuondoka.

Juzi, Liyumba alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka upya ambapo wakili wa serikali, Mwangamila, alidai kuwa kesi hiyo ya jinai imepewa namba 105/2009 na ina mashitaka mawili tofauti na awali ambapo ilikuwa na mashitaka matatu.

Kwa mujibu wa Mwangamila, katika shitaka la kwanza, Liyumba anakabiliwa na kosa la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma ambapo anadaiwa kuwa kati ya mwaka 2001-2006, akiwa mwajiriwa wa serikali, aliidhinisha ujenzi wa minara pacha, bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu.

Mwangamila alidai kuwa, shitaka la pili ni kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 kwa uamuzi wake wa kuidhinisha ujenzi wa minara hiyo pacha.

Liyumba alisomewa mashitaka mapya baada ya Hakimu Mkazi Walirwande Lema, aliyekuwa akisikiliza kesi namba 27/2009 iliyokuwa ikimkabili mshitakiwa huyo na Meneja Miradi wa BoT, Deogratius Kweka, kuwaachia huru baada ya kubaini hati ya mashitaka ilikuwa ina makosa kisheria.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye, Liyumba na Kweka walikamatwa tena na Liyumba kusomewa mashitaka mapya, huku Kweka akiendelea kuhojiwa na Takukuru.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Mei 30,2009

LIYUMBA KUTOKA SELO JUNI MOSI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, jana imelegezea masharti ya dhamana kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, ambaye anakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Hatua hiyo inatoa uwezekano mkubwa kwa mshitakiwa huyo, aliyesota mahabusu kwa siku 114, kuwa nje kwa dhamana Jumatatu ijayo - Juni Mosi mwaka huu, endapo atakamilisha masharti mapya ya dhamana.

Uamuzi wa kulegeza masharti ya dhamana mpya, ulitolewa jana na Hakimu Nyigumalile Mwaseba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambaye kabla ya kusoma uamuzi huo, alikumbusha kuwa katika shauri hilo dhamana ilikuwa haibishaniwi bali kilichokuwa kikibishaniwa ni masharti ya dhamana.

Kwa uamuzi huo, Liyumba sasa atatakiwa atoe fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya sh milioni 300, wadhamini wawili watakaosaini bondi ya sh milioni 50 kila mmoja, kutotoka nje ya Dar es Salaam hadi kwa kibali maalum na kusalimisha hati ya kusafiria mahakamani.

Masharti hayo ni tofauti na awali, ambapo alitakiwa awe na wadhamini wawili wa kuaminika, ambao wangesaini bondi au kuwasilisha hati yenye thamani ya nusu ya kiasi cha sh bilioni sh 221, anachotuhumiwa kuisababishia serikali hasara.

Sharti lingine la awali lilikuwa kuacha hati za kusafiria mahakamani, kuripoti katika ofisi za Takukuru kila siku ya Ijumaa na kutotoka nje ya Dar es Salaam bila ya kibali cha mahakama.

Juzi, mawakili wa serikali, wakiongozwa na Justus Mulokozi, John Wabuhanga na Prosper Mwangamila, waliiomba mahakama itoe dhamana kwa mujibu wa kifungu Na. 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho 2002.
Kifungu hicho kinasema ili mshitakiwa apate dhamana, lazima awasilishe mahakamani nusu ya fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya nusu ya mali ya mtuhumiwa anayodaiwa kuiba.

Akitoa uamuzi ambao umemfanya Liyumba apumue, Hakimu Mwaseba alisema amesikiliza hoja za pande zote mbili na kulazimika kukubaliana na hoja za mawakili wa utetezi kwamba, ni kweli kifungu hicho kamwe hakipaswi kutumika katika mashitaka mapya yanayomkabili mshitakiwa huyo.

Alisema, hakuna ubishi kwamba mashitaka yanayomkabili Liyumba ni yale ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia hasara serikali ya sh bilioni 221, hivyo mashitaka hayo ni tofauti kabisa na yanayoainishwa kwenye kifungu hicho.

Akisoma kwa makini uamuzi huo, Mwaseba ambaye ni mmoja wa mahakimu vijana wa mahakama hiyo, alisema ameamua kutupa ombi la upande wa mashitaka la kutaka kifungu hicho kitumike kumpa dhamana Liyumba.

“Nakubaliana na hoja za mawakili wa utetezi kuwa kifungu hicho kamwe hakipaswi kutumika katika mashitaka yanayomkabili mshitakiwa na kwa sababu hiyo natupilia mbali ombi la upande wa mashitaka lililotaka mahakama hii itumie kifungu hicho katika kumpatia dhamana mshitakiwa na endapo upande wa mashitaka haujaridhika na uamuzi wake, unaweza kukata rufaa,” alisema Mwaseba na kusababisha mawakili wa serikali kujiinamia.

Baada ya kumaliza kutoa uamuzi huo, wakili Magafu aliomba mahakama kuahirisha kwa muda kesi hiyo hadi saa saba mchana jana ili mteja wake aweze kukamilisha masharti hayo.

Lakini wakili wa serikali, Mulokozi alipinga hoja hiyo kwa madai kuwa, wana shughuli nyingine na kupendekeza iahirishwe hadi tarehe nyingine.

Hata hivyo, Mwaseba alikubaliana na Mulokozi na kuahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu ijayo ambapo itakuja kwa ajili ya kukamilisha masharti ya dhamana na kama yatakamilika, Liyumba atakuwa nje kwa dhamana.

Baada ya hakimu kuondoka katika chumba cha mahakama, ndugu na jamaa wa Liyumba waliruka kwa furaha, huku wengine wakienda kizimbani kumbusu mshitakiwa huyo pamoja na kuwapongeza mawakili wake kwa kupambana katika kesi hiyo hadi kufikia hatua hiyo.

Wakati hayo yakifanyika, mawakili wa serikali walionekana kupooza na kuamua kubeba makabrasha yao na kuanza kuondoka.

Juzi, Liyumba alifikishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka upya ambapo wakili wa serikali, Mwangamila, alidai kuwa kesi hiyo ya jinai imepewa namba 105/2009 na ina mashitaka mawili tofauti na awali ambapo ilikuwa na mashitaka matatu.

Kwa mujibu wa Mwangamila, katika shitaka la kwanza, Liyumba anakabiliwa na kosa la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma ambapo anadaiwa kuwa kati ya mwaka 2001-2006, akiwa mwajiriwa wa serikali, aliidhinisha ujenzi wa minara pacha, bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu.

Mwangamila alidai kuwa, shitaka la pili ni kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 kwa uamuzi wake wa kuidhinisha ujenzi wa minara hiyo pacha.

Liyumba alisomewa mashitaka mapya baada ya Hakimu Mkazi Walirwande Lema, aliyekuwa akisikiliza kesi namba 27/2009 iliyokuwa ikimkabili mshitakiwa huyo na Meneja Miradi wa BoT, Deogratius Kweka, kuwaachia huru baada ya kubaini hati ya mashitaka ilikuwa ina makosa kisheria.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye, Liyumba na Kweka walikamatwa tena na Liyumba kusomewa mashitaka mapya, huku Kweka akiendelea kuhojiwa na Takukuru.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Mei 30,2009

MAHAKAMA YAZUIA UCHAGUZI TUCTA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imetoa amri ya kuzuia kufanyika kwa uchaguzi wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi nchini (TUCTA), hadi kesi ya msingi iliyofunguliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Nestory Ngula, itakapotolewa uamuzi.
Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Mkazi, B. Mashabara, aliyesema amekubalina na ombi moja la Ngulla anayetetewa na Dk. Sengondo Mvungi na Deo Mwarabu, kuwa endapo TUCTA itafanya uchaguzi, bila kesi ya msingi kumalizika, ataathirika.

“Nakubaliana na hoja za mawakili wa mwombaji kuwa endapo uchaguzi utafanyika bila kesi ya msingi iliyopo mahakamani kuamriwa ni wazi kabisa Ngulla ataathirika zaidi kuliko mdaiwa na kwa sababu hiyo natoa amri kwa mdaiwa ambaye ni rais wa TUCTA, kumzuia kuitisha uchaguzi huo.

Hata hivyo Hakimu Mashabara alishindwa kutolea uamuzi wa ombi la pili la Ngulla aliyetaka mahakama itoe amri ya kutozuiliwa kuingia ofisini na kufanya kazi zake kama Katibu Mkuu hadi kesi ya msingi, itakaposikilizwa.

Katika kesi ya msingi iliyopo mahakamani hapo, Ngulla anapinga kuwa amejiuzulu wadhifa huo na kuwa taarifa za vikao viwili vya Kamati ya Utendaji ya TUCTA vilivyofanyika Machi 30 mwaka huu, vilivyoibuka na maazimio kuwa yeye amejizulu si sahihi kwani hajawahi kutangaza hivyo.

Kwa mujibu wa hati hiyo ya kesi ya msingi, Ngulla anaeleza kisheria Katibu Mkuu anajiuzulu kwa barua na kwa mujibu wa Katiba ya TUCTA; barua hiyo inapelekwa kwa Baraza Kuu la Shirikisho hilo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Mei 29,2009

LIYUMBA AITIKISA SERIKALI

Na Happiness Katabazi

‘FILAMU’ ya kumkamata na kukumuachilia huru aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, jana iliendelea tena baada ya mshitakiwa huyo kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashitaka mapya.

Liyumba alifikishwa mahakamani hapo jana, majira ya saa 8:00 mchana, chini ya ulinzi wa polisi akiwa amepakizwa kwenye gari aina ya Yundai, yenye namba za usajili T 450 ARU ambalo lilikuwa likiongozwa na Defender lenye namba za usajili T 220 AMV na Land Cruiser yenye namba T 120 AZD.

Baada ya kushushwa, mshitakiwa huyo alipitishiwa mlango wa nyuma na kisha kuingizwa kwenye chumba cha Mwendesha Mashitaka Mkuu Kanda ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Charles Kenyela alikokaa kwa dakika takriban 20.

Baadaye, alitolewa na kuingizwa katika mahakama ya wazi kwa ajili ya kusomewa mashitaka mapya.

Wakili wa Serikali, Prosper Mwangamila, akisaidiana na John Wabuhanga na Justus Mlokozi mbele ya Hakimu Mkazi, Nyigumalila Mwaseba, alidai kuwa Liyumba amefungulia kesi mpya ya jinai yenye mashitaka mawili na imepewa namba 105/2009.

Katika shitaka la kwanza, Liyumba anakabiliwa na kosa la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma ambapo anadaiwa kuwa kati ya mwaka 2001-2006, akiwa mwajiriwa wa serikali, aliidhinisha ujenzi wa minara pacha, bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu.

Mwangamila alidai kuwa, shitaka la pili ni kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 kwa uamuzi wake wa kuidhinisha ujenzi wa minara hiyo pacha.

Hata hivyo, mashitaka hayo katika hati mpya yanafanana na yale waliyoshitakiwa katika hati ya mashitaka iliyofutwa na kilichobadilika ni yeye kushitakiwa kwa makosa mawili wakati hati ya mashitaka ya awali ilikuwa na mashitaka matatu.

Hata hivyo, Liyumba alikana mashitaka yote, lakini upande wa mashitaka uliiomba mahakama itoe dhamana kwa mujibu wa kifungu Na. 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho 2002.

Kifungu hicho kinasema ili mshitakiwa apate dhamana, lazima awasilishe mahakamani nusu ya fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya nusu ya mali ya mtuhumiwa anayodaiwa kuiba.

Hata hivyo, kiongozi wa jopo la mawakili linalomtetea Liyumba, Majura Magafu, aliibua hoja mpya ya kisheria akidai kuwa kifungu hicho hakipaswi kutumika katika kesi hiyo.

Akiwasilisha hoja hiyo, Magafu aliiambia mahakama kuwa, mashitaka yanayomkabili mteja wake ni ya matumizi mabaya ya ofisi za umma na kuisababishia hasara serikali na kuongeza kuwa, kifungu hicho kinasema masharti hayo yatatumika kwa mshitakiwa anayetuhumiwa kuiba au mali inayoonekana ya mamlaka husika yenye zaidi ya thamani ya sh milioni 10.

“Shitaka la kusababisha hasara halimaanishi mteja wangu alichukua sh bilioni 221 za BoT au mali yenye thamani hiyo.

“Kwa kuwa upande wa mashitaka umetaka tuwakumbushe historia ya kifungu hicho kilianzia wapi, nalazimika kuwakumbusha;

“Ni hivi, kifungu hicho kiliingizwa kwenye Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, baada ya miaka ya 1980 baada ya serikali ya awamu ya kwanza kutangaza vita dhidi ya wahujumu uchumi na serikali ilisema, kama mtu anatuhumiwa kuiba zaidi ya milioni 10, na miaka michache baadaye ndiyo kifungu hicho kiliingizwa kwenye Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na kuanza kutumika.

“Hakimu, ni rai yetu kwamba hiki kifungu cha 148(5)(e) cha CPA kisitumike kabisa kwenye kesi hii kwani mteja wangu hakuiba fedha wala mali…na hiki kifungu ni mtego wa panya, na katika uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya Daud Pete dhidi ya DPP ya mwaka 1991, mahakama ilikataa sheria za nchi kutumika kama mtego wa panya,” alidai Magafu.

Aidha Magafu alidai wanasikitishwa na upande wa mashitaka kutaka kutumia kifungu hicho kwa ajili ya dhamana, kwani ni hatari kwa watumishi wa umma ambao wamestaafu baada ya kulitumikia taifa kwa uaminifu. Lakini kwa sababu ya chuki tu, wanaamua kutumia kifungu hicho ili kuwatesa.

Hakimu Mwaseba aliamua kuahirisha kesi hiyo hadi leo kwa ajili ya kutoa uamuzi kuhusu utata wa masharti hayo ya dhamana.

Baada ya kuahirishwa, Liyumba alichukuliwa na maofisa usalama na kuingizwa kwenye gari lililomleta na kisha kupelekwa mahabusu.

Juzi, Hakimu Mkazi Walirwande Lema, aliyekuwa akisikiliza kesi namba 27/2009 iliyokuwa ikimkabili Liyumba na Meneja Miradi wa BoT, Deogratius Kweka, aliwaachilia huru baada ya kubaini hati ya mashitaka ilikuwa imekosewa, lakini muda mfupi baadaye walikamatwa tena mahakamani hapo.

Wakati huo huo, vyanzo vya kuaminika toka Makao Makuu ya Takukuru na Jeshi la Polisi, vimelihakikishia gazeti hili kuwa, Kweka ambaye awali alishitakiwa na Liyumba kwenye kesi ya jinai namba 27/2009, iliyofutwa na mahakama hiyo, anaendelea kuhojiwa na maofisa wa Takukuru.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Mei 29, 2009

CASS:CHUO CHENYE MKAKATI WA KULETA UFANISI KWENYE UONGOZI


MEI 11 mwaka huu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinachoongozwa na Profesa Rwekaza Mukandala, kiliandika historia nyingine ya kimaendeleo baada ya Chuo cha Fani ya Sayansi za Jamii (CASS) kuzinduliwa na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni. Katika makala hii, Mkuu wa Chuo hicho kipya, Profesa Bertram Mapunda (52), anazungumzia kwa mapana madhumuni ya kuanzishwa kwa chuo hicho na masuala mengine ya kitaalumu. Mwandishi Wetu HAPPINESS KATABAZI anaelezea zaidi.
Swali: Tueleze kwa nini Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiliamua kuanzisha CASS?

JIBU: Asante. Kwanza ieleweke wazi kuwa mkutano wa 180 uliofanyika Agosti mosi, 2008, Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam liliidhinisha muundo mpya wa utawala wa Chuo pamoja na muunganisho wa vitengo vyake vya kitaaluma. Baraza liliidhinisha ngazi tatu za kiutawala kwenye shughuli za kitaaluma ambazo ni idara (ngazi ya chini), vyuo vya kampasi/skuli/taasisi (ngazi ya kati) na utawala wa juu wa chuo.
Kwa muundo huo, vitivo vilivyokuwapo Kampasi ya Mlimani vinafutwa isipokuwa kwa Kitivo cha Sheria ambacho mchakato wake wa mabadiliko umepewa muda. Katika mabadiliko, baraza liliidhinisha kuanzishwa kwa vyuo vya kampasi yaani Campus Colleges tatu ambazo ni Chuo cha Uhandishi na Teknolojia.
Chuo hiki kilikuwapo kwa hivyo kinaendelea, Chuo cha Fani ya Sayansi za Jamii (Collage of Arts and Social Sciences) ambacho kinatokana na idara zilizokuwa chini ya Kitivo cha Fani na Sayansi za Jamii, Chuo cha Sayansi Asilia na Sayansi Tumizi (Collage of Natural and Applied Sciences) kitachojumuisha idara zilizokuwa chini ya Kitivo cha Sayansi na Kitivo cha Sayansi na Teknolojia za Majini. Hivyo kimsingi CASS imeanzishwa ili kuleta ufanisi kwenye uongozi na utawala.
Lengo hasa la kuanzishwa kwa chuo hiki ni kupunguza urasimu wa kiuongozi uliokuwapo, kwani mfumo wa zamani wa kiutawala chuoni hapo ulikuwa ni wa ngazi nne ambazo ni idara, kitivo, chuo na chuo kikuu. Kwa utaratibu huo mpya ngazi ya kitivo imefutwa. Na ndani ya chuo hicho kipya kuna idara kumi nazo ni Idara ya Uchumi, Sanaa za Maonyesho, Lugha za Kigeni na Isimu. Nyingine ni Fasihi, Geografia, Historia na Akiolojia, elimu ya Siasa na Utawala,Takwimu, Filosofia, Socialojia na Anthropology, elimu ya dini idara ambayo bado haijaanza kufanyakazi.
Kwa hiyo, CASS sasa itakuwa na madaraka ya kufanya maamuzi mbali mbali yatakayotatuliwa kwa haraka, na kwa mfumo huu mpya chuo hiki kimepewa madaraka zaidi kuliko kilivyokuwa kitivo kwa maana hiyo maamuzi ambazo zamani yaliyokuwa yanafanywa na uongozi wa UDSM sasa yatafanywa na CASS. Hili ni jambo la kujivunia sana, kwa hiyo tunatarajia kwa muundo huu mpya kutakuwepo na mabadiliko ya kiutendaji yatakayoleta ufanisi na tija.

Swali: Ni changamoto zipi CASS inakabiliana nazo licha ya kuzinduliwa hivi karibuni?

Jibu: Bado miundombinu ni tatizo hususani ofisi za walimu bado hazijitoshelezi, vyumba vya wanafunzi tungependa wanafunzi wawe wanaishi karibu na chuo hasa ukizingatia masomo yanaanza asubuhi. Hakuna sehemu ya kupumzikia wanafunzi. Pia tunatatizo jingine la wafanyakazi kutokana na uamuzi wa ulitolewa na serikali ya awamu ya pili iliyokuwa ikiongozwa na Rais Ali Hassan Mwinyi, iliposimamisha ajira za serikali wakiwamo watendaji wa UDSM kutokana na kile kilichoelezwa matatizo ya uchumi. Kwa hiyo muda mrefu chuo kikuu hakikuajiri wafanyakazi tangu kipindi kile cha mwaka 1990. Matokeo yake leo hii UDSM ina idadi kubwa ya wahadhiri wenye umri wa kustaafu. Kwa hiyo hapa katikati kuna pengo kati ya wahadhiri wenye umri wa kustaafu na wale wanaoajiriwa. Asilimia 50 ya wahadhiri ni wale walioajiriwa miaka ya 2000 ambao wapo katika ngazi ya wahadhiri wasaidizi na Tutor Assistan.

Swali: Hali hiyo ina madhara gani?

Jibu: Wapo wahadhiri wenye uzoefu ndiyo wanastaafu sasa, ile hali ya wahadhiri wasaidizi kurithi uzoefu kwa wahadhiri waandamizi ambao wapo kwenye umri wa kustaafu inashindikana. Matokeo yake wahadhiri wasaidizi wanakosa uzoefu wa kitaaluma.

Swali: Una shauri nini kifanyike kuepuka hali hiyo?

Jibu: Wahadhiri wanaostafu serikali ione haja ya kuwapatia mikataba ya muda mrefu kama miaka mitano kwa wahadhiri hao wastaafu, ili waweze kuendeleza mchango wao katika vyuo vyetu. Kama hilo litashindikana basi pendekezo jingine naiomba serikali itoe upendeleo maalum kwa wahadhili hao wanaostaafu, waruhusiwe kustaafu wakiwa na umri wa miaka 65 badala ya 60 kama ilivyo sasa. Ikumbukwe kuwa historia ya chuo hicho anachokiongoza kwa sasa kilianzishwa 1964 wakati huo ndipo Kitivo cha Fani ya Sayansi ya Jamii kilipozalishwa. Kwa hiyo, hadi leo kitivo hicho kilipobadilika na kuwa chuo Mei 11 mwaka huu, kina umri wa miaka 45.

Alikotokea Profesa Mapunda

Profesa Mapunda kabla ya kuwa mkuu wa chuo hicho kipya, alikuwa Mkuu wa Idara ya Historia iliyokuwa chini ya Kitivo cha Fani na Sayansi za Jamii, Aliongoza idara hiyo tangu mwaka 2003 hadi Mei 2009.

Aliajiriwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Agosti 1989 kama Tutor Assistant ikiwa ni miezi michache kuhitimu Shahada ya Kwanza ya Elimu ya Malikale (Archaeology), lakini hakuweza kufanya kazi hiyo kwa muda mrefu, kwani mwezi mmoja baadaye alikwenda Marekani kuchukua shahada ya pili na ya tatu ya fani hiyo hiyo. Alirejea nchini 1995 na kuanza kufundisha historia chuoni hapo.

Alitenda kazi zake vizuri na kujiamini kwake ndiko kulikosababisha kupandishwa vyeo na wakuu wake wa kazi.

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Mei 28,2009

LIYUMBA AIZIDI AKIRI SERIKALI MAHAKAMANI

*Yeye, Kweka wafutiwa mashitaka, dola yawakamata
*Furaha ya ndugu zao yadumu kwa dakika tano tu
*Waandaliwa mashitaka mapya, kutinga kortini leo

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilimwachilia huru aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba na Meneja Mradi wa benki hiyo, Deogratius Kweka, baada ya kubaini hati ya mashitaka imekosewa.

Lakini wakati Liyumba na mwanzeke wakifurahia uamuzi huo, walikamatwa tena na makachero wa polisi waliofurika mahakamani hapo, muda mfupi baada ya kuachiwa na kupelekwa katika kituo cha polisi Salender Bridge walikowekwa mahabusu.

Uamuzi wa kesi hiyo iliyovuta hisia za wengi kila ilipotajwa mahakamani, ulitolewa jana saa 4:47 asubuhi na Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema, baada ya kuahirisha kutoa uamuzi huo kwa mara tatu mfululizo.

Alisema amefikia uamuzi wa kuwaachia washitakiwa baada ya kukubaliana na maombi ya mawakili wa utetezi kuwa, hati ya mashitaka katika kesi hiyo, ina dosari za kisheria.

Februari 25, mwaka huu, wakili wa utetezi, Majura Magafu, ambaye alikuwa akisaidiana na Hudson Ndusyepo na Profesa Gamalieli Mgongo Fimbo, waliwasilisha maombi mahakamani hapo wakitaka wateja wao waachiliwe na kufutiwa mashitaka kwa madai kuwa kibali cha Mkurugenzi wa Mahitaka (DPP), kilichotumika kufungua kesi hiyo, kina makosa.

Pia walidai kuwa, shitaka katika kesi ya msingi, namba 27/2008, linalodai kuwa washitakiwa hao waliisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, halionyeshi ni aina gani ya kosa lililotendwa na watuhumiwa hao.

Alisema shitaka hilo limeandaliwa kinyume na kifungu cha 135 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Lema akisoma uamuzi huo, alisema kisheria hati ya mashitaka ndiyo inayojenga msingi wa kesi yoyote iliyopo mbele ya mahakama, hivyo inapobaini kuwa ina dosari za kisheria, inalazimika kuifuta na kisha kuwaachilia huru washitakiwa.

“Baada ya kupitia kwa kina hoja za pande zote mbili, mahakama hii inakubaliana na maombi ya utetezi kuwa, hati hiyo ina dosari na kwamba kosa la tatu halionyeshi ni kosa gani limetendwa na washitakiwa, hivyo nawaachia washitakiwa chini ya kifungu Na. 135 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai 2002.

“Nimewaachilia huru washitakiwa chini ya kifungu hicho baada ya mahakama kubaini kuwa hati ya mashitaka iliyofikishwa mahakamani na upande wa mashitaka ni ‘hopeless’,” alisema Lema na kusababisha makachero waliokuwa wameketi viti vya nyuma, kuanza kusogea karibu na kizimba waliposimama washitakiwa ili kuwakamata tena.

Tangu saa moja asubuhi, makachero hao kutoka Idara ya Usalama wa Taifa, Takukuru na Polisi, walikuwa wamezingira mahakama hiyo, huku makachero wa polisi toka Kitengo cha Kupambana na Ujambazi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, ambao waliliambia gazeti hili kuwa walikuwa na taarifa za washitakiwa kuachiwa huru, wakiwa wamebeba silaha aina ya SMG, tayari kwa ajili ya kuwakamata washitakiwa hao.

Mara baada ya Lema kumaliza kutoa uamuzi wake, maofisa usalama walimwamuru Liyumba na Kweka washuke kizimbani na kuwataka waketi kwenye viti vinavyotumiwa na mawakili wakati wakiendesha kesi mahakamani hapo.

Washitakiwa hao ambao walionekana kuwa na furaha, walitii amri hiyo, kisha Mwendesha Mashitaka Mkuu Kanda ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Charles Kenyella, aliutangazia umati wa watu uliofurika kufuatilia kesi hiyo, kutoka nje ili maofisa usalama hao na mawakili wa utetezi, wabaki na washitakiwa.

Baada ya umati huo kutoka, ndipo maofisa hao wakiwamo wa Jeshi la Magereza, waliwakabidhi rasmi watuhumiwa hao mikononi mwa polisi.

Ilipofika majira ya saa 5:28 asubuhi, polisi waliwapakiza watuhumiwa hao kwenye gari la polisi aina ya Defender lenye namba za usajili T 337 AKV, huku maofisa usalama wengine wakipanda kwenye gari aina Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili T 319 ATD na kuwapeleka katika Kituo cha Polisi cha Salender Bridge, chini ya ulinzi mkali, na kuwaacha ndugu na jamaa wa washitakiwa hao, wakipigwa na butwaa.

Licha ya wanausalama kufurika mahakamani hapo, pia ndugu na jamaa wa washitakiwa hao walifurika kwa wingi kusikiliza hukumu hiyo, huku eneo lote la mahakama linalotumika kuegeshea magari, likiwa limefurika magari.

Baadhi ya ndugu wa washitakiwa hao, walishindwa kuficha hisia, kwani walikuwa wakibubujikwa na machozi, huku wengine sura zao zikiwa zimejawa na simanzi.

Dalili za Liyumba kuachiwa na kukamatwa tena, zilionekana tangu uamuzi wa kesi hiyo ulipokuwa ukiahirishwa kutokana na idadi kubwa ya watu wa usalama na polisi waliokuwa wakifurika kwenye kesi hiyo.

Awali, Aprili 23, mwaka huu, Lema alitupilia mbali ombi la utetezi lililowasilishwa mahakamani hapo na wakili Magafu, lililokuwa likiomba mahakama hiyo itumie kifungu 225(1-4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai 2002, kinachotamka kuwa, ndani ya siku 60, upelelezi katika kesi husika uwe umekamilika, vinginevyo ifutwe.

Lema katika uamuzi wake alisema, hatafuta kesi hiyo kwa sababu amebaini kuwa licha ya siku 60 kupita na upalelezi wa kesi hiyo kutokamilika, haoni kama haki za msingi za washitakiwa zimevunjwa, na alitoa amri ya kuongeza muda kwa upande wa mashitaka ili uweze kukamilisha ushahidi wake.

Machi 30, mwaka huu, Hakimu Mkazi Lema ndipo alipoanza kuendesha kesi hiyo baada ya Hakimu Mkazi, Hadija Msongo aliyeanza nayo awali, kujiondoa rasmi Januari 26, mwaka huu kwa madai kuwa jamii kupitia vyombo vya habari, imekuwa ikilalamikia dhamana ya Liyumba.

Februari 17, mwaka huu, hakimu Msongo alimwachia kwa dhamana Liyumba na kuibua utata kutokana na kutotimiza masharti.

Moja ya masharti ambayo hayakutimizwa na Liyumba, ni kuwasilisha mahakamani hati zenye thamani ya sh bilioni 55, wadhamini wawili wa serikali wakiwa na barua kutoka kwa waajiri wao na kukabidhi hati za kusafiria mahakamani hapo.

Siku hiyo, Liyumba aliwasilisha hati yenye thamani ya sh milioni 882, hati ya kusafiria ambayo muda wake wa matumizi umekwisha, huku wadhamini wawili wakiwa hawana barua zilizosainiwa na mwajiri wao kama masharti yalivyotolewa na mahakama.

Na wakati hakimu Msongo akitoa dhamana hiyo, alipingana na masharti ya dhamana aliyoyaweka mwenyewe wakati washitakiwa walipofikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, na pia alipingana na uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ambayo ilisikiliza maombi ya Liyumba ya kutaka wapunguziwe dhamana.

Lakini siku mbili baadaye, Msongo alitoa hati ya kukamatwa Liyumba na wadhamini wake baada ya kubainika hati 10 zilizotumika kumdhamini zilikuwa na makosa, na pia barua za wadhamini wake hazikuwa zimesainiwa na mwajiri wao na kwamba Liyumba alikuwa amewasilisha hati ya kusafiria iliyokwisha muda wake.

Liyumba na mwenzake walipanda kizimbani mara ya kwanza Januari 26 mwaka huu, wakikabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia hasara serikali.

Ilidaiwa mahakamani hapo na Wakili Mwandamizi wa Serikali, John Wabuhanga ambaye alikuwa akisaidiana na Fredrick Manyanda kuwa, washitakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka yaliyoisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Wakili Wabuhanga alidai kuwa, washitakiwa hao wanadaiwa kutumia vibaya fedha za umma kwa kuidhinisha ujenzi wa Minara Pacha ya BoT maarufu kama ‘Twin Tower’ na kwamba wanakabiliwa na mashitaka matatu.

Shitaka la kwanza linamkabili mshitakiwa wa kwanza, Liyumba, ambalo ni matumizi mabaya ya ofisi ya umma. Kwamba kati ya mwaka 2001-2006, akiwa mwajiri wa serikali, aliidhinisha ujenzi wa minara pacha bila baraka za uongozi wa juu wa benki hiyo.

Shitaka la pili, linamkabili mshitakiwa wa kwanza peke yake, ambalo ni kuidhinisha malipo ya ujenzi huo bila kibali cha Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu.

Wabuhanga alidai kuwa, shitaka la tatu ni kuisababishia serikali hasara, ambalo liliwahusu washitakiwa wote ambapo wanadaiwa kuwa kati ya mwaka 2001-2006, wakiwa watumishi wa umma, kwa makusudi au kwa kushindwa kuwa makini na kazi yao, waliisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Msongo alisema ili mshitakiwa apate dhamana, ni lazima kila mmoja awe na wadhamini wawili wa kuaminika ambao watasaini bondi au kuwasilisha hati yenye thamani ya nusu ya kiasi wanachotuhumiwa kuisababishia serikali hasara.

Sharti jingine ni washitakiwa kuacha hati za kusafiria mahakamani na kila Ijumaa watahitajika kuripoti ofisi za Takukuru na kutotoka nje ya Dar es Salaam bila ya kibali cha korti.

Nusu ya kiwango wanachodaiwa kuisababishia serikali ni sh bilioni 110, hivyo kila mmoja wao atapaswa kusaini bondi au kuwasilisha hati yenye thamani ya sh bilioni 50.

Wakati huo huo, vyanzo vya kuaminika toka Jeshi la Polisi na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, vimeliambia Tanzania Daima kuwa, Liyumba atafikishwa mahakamani hapo leo na kusomewa mashitaka mapya kwa kuwa tayari hati ya mashitaka imeishaandaaliwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Mei 28, 2009

DPP-ELIEZER FELESHI AKIELEZA MAFANIKIO




Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi akielezea mafanikio yaliyopatikana tangu waendesha mashtaka wa kiraia toka ofisi yake waanze kuendesha mashtaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu pamoja na changamoto zinazowakabili. (katikati) Waziri wa Katika na Sheria Mathias Chikawe na ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Lameck Mlacha, wakati waziri Chikawe alipofanya ziara katika mahakama hiyo, leo Mei 25,2009. (Picha na Happiness Katabazi).

TUMEDHITI HATI ZA KUGHUSHI-DPP

Na Happiness Katabazi

OFISI ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini(DPP) imesema tangu waendesha mashtaka wa kiraia waanze kuendesha kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imeweza kudhibiti tatizo sugu la hati za dhamana feki mahakamani hapo.

Mafanikio hayo yalielezwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Winfrida Koroso kwaniaba ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)Eliezer Feleshi mbele ya Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe, ambaye jana alifanyaziara katika mahakama hiyo kwaajili ya kuzungumza na mahakimu wakazi na mawakili wa serikali sambamba kusikiliza mafanikio na changamoto zinazowakabili watendaji wa mahakama hiyo kwa ujumla.

Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka,Koroso alisema mawakili hao ambao wanatoka katika ofisi yake walianza kufanyakazi Septemba mosi mwaka jana, na kwamba tangu waanze kufanyakazi hiyo ambayo awali ilikuwa ikifanywa na Waendesha Mashtaka toka Jeshi la Polisi wameweza kukabiliana na wimbi la wadhamini wanaowasilisha hati za mali zisizoamishika ambazo ni za kugushiwa ili waweze kuwadhamini ndugu na jamaa zao na nyaraka nyingine za kipelelezi.

Koroso alisema mafanikio hayo yametokana na mawakili hao wa kiraia kushirikiana na kikamilifu na Jeshi la Polisi ambapo wameweza kuzibaini hati nyingi kuwa ni za kughushiwa. Akitaja mafanikio mengine tangu mfumo huo uanze kufanyakazi alisema umewezesha kuboresha uendeshaji mashtaka ,kwani kabla ya mawakili kuanza kazi kulikuwa na mafaili ya kesi 800 yalilikuwa hayaonekani lakini tangu wameanza kufanyakazi mafaili hayo yamepatikana.

“Hata hivyo mchakato huo pia umeleta mafaniko kwani umeweza kupanua wigo wa uwazi katika kesi mbalimbali kwani katika mahakama tumeanzisha kitengo cha kupokea malalamiko ya wananchi wenye kesi zao mahakamani ambao wanaona hawatendewi haki….pia mchakato huu umeweza kututunganisha na wadau ambao ni Polisi, Takukuru na mahakama” alisema Koroso.

Hata hivyo alisema changamoto zinazowakabili ni kukosekana kwa majarada ya kesi, mahabusu kushindwa kutimiza masharti ya dhamana na kwamba vyumba vya waendesha mashtaka katika mahakamani hapo havitoshi hivyo kumuomba Waziri Chikawe awasaidie kutatua tatizo hilo.

Wakichangia mada kwenye mkutano huo, Hakimu Mkazi Henzron Mwankenja, Waliarwande Lema, Mkuu wa Waendesha Mashtaka Kanda ya Dar es Salaam, (ACP) Charles Kenyela walipongeza mfumo huo wa waendeshamashtaka wa kiraia ila walishauri pia bado kuna haja waendesha mashtaka wa polisi waongezewe muda ili waweze kuwapatia uzoefu waendesha mashtaka wa kiraia kwani ni wazi kabisa waendesha mashtaka wa kirai bado hawajapata uzoefu wa kutosha katika kuendesha kesi mbalimbali.

Kwa upande wake Kenyela alisema alisema hali ya ulinzi na usalama katika mahakama hiyo ni finyu kwani hata askari polisi wanaolinda mahakamani hapo hawana vifaa vya kisasa vya kuweza kukabiliana na wahalifu ambao wanaweza kufika mahakamani hapo na visu au mabomu hivyo kuomba mamlaka husika liangalie ni jinsi gani linaweza kutenga fedha kwaajili ya kuweka mfumo ulinzi wa kisasa mahakamani hapo.

‘Ebu fikiria askari wangu wanavirungu tu na bastola wakati mwingine ndiyo wanalinda hapa mahakamani lakini lazima tukubali wahalifu hivi sasa nao kila kukicha nao wanafanya uhalifu wao kisayansi…..atuombei mabaya leo hii mhalifu aje na bomu kaficha au kisu askari wangu hawawezi kumtambua hivyo basi mahakama iwekewe uzio na geti moja ambapo kila anayeingia na kutoka anapekuliwa na kifaa maalum naamini tutakabiliana na hali hiyo” alisema Kenyela huku akionyesha kujiamini.

Kwa upande wake Waziri Chikawe alisema amesikilia maelezo ya waliochangia na kusema ameteembelea mahakama hiyo amejionea kuwa mahakama hiyo ipo katika hali mbaya na kwamba imechoka na akamwelekeza Hakimu Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Addy Lyamuya kushirikiana na mtaalum toka wizarani yake ambapo watampa mchoro wa jinsi wanavyotaka mahakama hiyo ijengwe.

Chakawe hata hivyo alionekana kuguswa na tatizo la upatikanaji wa mashahidi na jinsi ya kuwatunza , alisema tatizo hilo ni kubwa na kuongeza kuwa ndiyo maana wameamua kuamishia mashahidi wa kesi mbalimbali katika ofisi ya DPP kwasababu ofisi hiyo ndiyo inayowahitaji mashahidi na tayari serikali imekusudia kutoa fungu kwenye ofisi ya DPP kwaajili ya mashahidi.

“Nimesikiliza matatizo yenu na pia napongeza ofisi ya DPP kwa mafanikio mliyoyapata ila haya matatizo nitayapeleka kwa wakubwa wenzangu ili tuone tunatumia utaratibu upi kuyapatia ufumbuzi” alisema Chikawe.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei 26,2009

JWTZ HUU SIYO UUNGWANA

Na Happiness Katabazi

JESHI la Ulinzi katika nchi yoyote ile ni chombo maarufu na nyeti katika masuala ya ulinzi na usalama, mtu anayefanya vitendo vya kishujaa hupewa taswira ya jeshi.

Heshima hiyo iliyonayo Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ilijengwa zaidi na ukakamavu, nidhamu na uwezo mkubwa wa utendaji wake wa kazi ndani na nje ya mipaka ya nchi.

Panapotokea maafa, mara nyingi tegemeo kubwa la raia ni jeshi lao la ulinzi, kwa kuwa wanajeshi wa jeshi hilo ndio wenye sifa, maarifa, mbinu na vifaa vya kuokoa maisha ya watu au mali zao. Uwajibikaji wao katika maafa kumewafanya wapendwe na wananchi.

Uhuni uliofanywa na askari wa JWTZ mapema wiki hii katika Makutano ya barabara za Morogoro na,Mandela na Sam Nujoma,dhidi ya askari wa Usalama wa Barabarani (Trafiki), Sajini Thomas Mayapila.

Kwa kile eti walichokidai kucheleweshwa na Trafiki huyo aliyekuwa akiongoza magari katika eneo hilo maarufu kama Ubungo Mataa.

Lakini tayari JWTZ imeshatoa taarifa kwa umma kuwa tayari limemkamata Koplo Steven Sagana kwa kuhusika na kosa la kuongoza kufanya uhuni huo na kwamba Jeshi la Polisi nchini limeishaunda timu ya pamoja kuchunguza na kubaini undani wa mazingira ya tukio hilo.

Hata hivyo kuundwa kwa timu hiyo na kukamatwa kwa Kolo Sagana, hakutuzui kulijadili kwa kina tukio hilo la kishenzi ambalo linaendelea kuweka rekodi mbaya kwa JWTZ ya kuwa baadhi ya wajeshi wake wamekuwa ni vinara wa kuvunja sheria za nchi kwa kujiona wapo juu ya sheria.

Tukio hilo limetudhihirishia kuwa jeshi letu bado lina wanajeshi wasio na nidhamu, kwa sababu hata kama wangekuwa wamegadhabika kwa kitendo cha kucheleweshwa bado suluhisho lake si kumvamia na kumpiga Trafiki huyo tena mbele ya hadhara.

Kitendo kile kinashiria kukosekana kwa busara kwa wanajeshi wale waliovaa sare wakiwa kwenye magari yao, niwape jina gani linalostahili kwa kufanya uvunjaji wa amani, kujeruhi na kunajisi sheria za nchi ambazo Amir Jeshi Mkuu wanayemtii, Rais Jakaya Kikwete anazitii?

Sasa hawa ndio mashujaa kweli wa nchi yetu? Labda suala zima la wanajeshi kutoka kambini na kuvamia raia kwa visingizio mbalimbali, kama vile ujambazi na kunyang’anyana ‘mabibi’ na raia vimekuwa vikilaaniwa mara kwa mara na taasisi za kutetea haki za binadamu nchini.

tabia waliyoionyesha imeonyesha jinsi wasivyo na heshima kwa askari polisi na raia. Kwani nini hawataki kuthamini na kutii majukumu ya idara nyingine za serikali?

Septemba 15,2007, alipokula kiapo cha utii mbele ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete, Mkuu wa Jeshi la Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, ambapo mimi nilishuhudia tukio hilo na nikapata fursa ya kupiga naye picha ya kumbukumbu, alishutumu na kulaani vikali tabia ya wanajeshi kupiga raia na akaahidi kwamba uongozi wake utaikomesha.

Kwa kuwa chini ya uongozi Jenerali Mwamunyange tayari kumeisharipotiwa matukio kuwa baadhi ya vijana wake wanaendelea kwenda kinyume naye kwa kujichukulia sheria mkononi.

Februali mwaka jana wanajeshi walivamia ofisi za shirika la ugavi wa maji Dar es salaam (Dawasco) linalomilikiwa na serikali, na kuwapiga na kuwanyanyasa watendaji wa shirika hilo na kumpora kamera mwandishi mmoja wa habari.

walitenda tukio hilo baada ya watendaji wa Dawasco kuingia katika moja ya kambi ya JWTZ na kukata maji kwa sababu jeshi hilo lilikuwa ni miongoni mwa wadaiwa sugu.

Ili wananchi waendelee kumheshimu, kumuamini na kutolinganisha kauli yake hiyo na porojo za wanasiasa majukwaani, tunamtaka Jenerali Mwamunyange atetee heshima ya JWTZ.

Tunataka atuthibitishie kwamba wanajeshi wetu si genge la wahuni wanaochukua sheria mikononi . Ikiwa atashindwa kufanya hivyo, raia watashindwa kumuamini na kuiheshimu JWTZ.Sote tuna fahamu kuwa serikali ya awamu ya nne imetia fora kwa kuunda tume pindi jambo linapotokea, tume hizo zimekuwa zikiendeshwa kwa kodi zetu.

Uundwaji wa tume hizo ni kama vile mpango wa serikali kufuja mali za wananchi ambao hulipa kodi nyingi bila ya kuwapo kwa maendeleo waliyoyatarajia.

Kuna sababu gani ya kuunda tume kwa tukio hili la ubungo wakati kila kitu kimefanyika hadharani na watu wameshuhudia? Kwa nini tusiwakamate moja kwa moja waliohusika mpaka tuunguze fedha za wananchi?

Je tume hiyo kweli itaweza kuja na matokeo huru na ya haki ambayo hayatakuwa na chembe chembe za upendeleo kwa tukio ambalo halikuhitaji tume?.

Wananchi tuna wasiwasi mkubwa na utendaji wa hiyo tume kwa kuwa tuna uzoefu mkubwa wa makosa wanayoyafanya wanajeshi huku uraiani kama vile kupiga raia lakini mwisho wa siku hatuwaoni mahakamani, tume zilizoundwa zilifanya kazi gani?

Tabia ya wanajeshi kulindana ndiyo inasababisha baadhi ya wanajeshi wetu kuendelea kukomaa kwa tabia za utovu wa nidhamu kwa kuwapiga raia kwa kisingizio kuwa ‘mwanajeshi ndiye mwenye nchi na kwamba kazi yao ni muhimu mno kuliko kazi nyingine zote’.

Ieleweke wazi kuwa kila kazi ina umuhimu wake katika maendeleo ya taifa letu hivyo hata muuza machungwa,mfagia barabara na mzibua vyoo ni muhimu pia.Kwani bila raia hakuna jeshi cha msingi wale wote wanaojichukulia sheria mkononi wadhibitiwe.

Hata kama trafiki yule hakutoa uzito wa ombi la wanajeshi wale waliosema wanakwenda kuwahi operesheni maalum bado kutoa kipigo si uungwana hata kidogo.

Kitendo kile kilikuwa na nia ya kilidhalilisha jeshi la polisi na askari husika ili lionekana si kitu mbele ya JWTZ, si wangewasiliana na mkuu wa kazi wa trafiki yule?


Kama Wanajeshi wale walikuwa wamebeba vifaa maalum ambavyo havikuhitaji kusubiri foleni, kwa nini uongozi wa JWTZ usingewasiliana mapema na Mkuu wa Trafiki Mkoa husika kwamba watumia barabara kadhaa kusafirisha vifaa hivyo nyeti bila kupata usumbufu?

Wananchi wanaokwenda asubuhi kazini ni mashahidi wa vitendo vya uvunjaji wa sheria za barabarani vinavyofanywa na madereva wa JWTZ huku wakiwa wamewapakia ambao bila shaka nao ni vinara wa kuchochea uvunjaji wa sheria.

Wamekuwa vinara wa kukwepa foleni kwa kupita kwenye barabara za waenda kwa miguu wakiulizwa hutoa kisingizo kwamba wakati wote mwanajeshi yupo kazini.

Nategemea kama kweli jeshi linajali utu na uungwana litatoa aelezo ya kuridhisha na ikiwezekana kuomba radhi kwa tukio hilo la ‘kihuni’
Lisilopendeza machoni mwa jamii iliyostaarabika.

Kama wasipofanya hivyo basi Tanzania itakuwa imejijengea utamaduni ambao majeshi yake ni ‘miungu watu’ wanaoweza kufanya udhalimu wa aina yoyote dhidi ya haki na uhai wa raia bila kukanywa wala kudhibitiwa.

Tutakuwa tunajijengea jehenamu ya aina yake na Tanzania haitakuwa tofauti na kambi za Al Ghareb, Iraq au Guantanamo Bay, Cuba.Tukubali makosa, tukubali kusahihishwa na kama taifa tumrejee Mungu kama wimbo wetu wa taifa wa taifa unavyotuasa.

JWTZ itimize wajibu wake wa kulinda nchi na si kupiga raia wala Trafiki. Trafiki fanyeni kazi bila upendeleo na epukeni ufisadi licha miongoni mwenu mmekuwa mkituhumiwa kuomba rushwa. Hata hivyo kipigo ulichokipata Sajini Thomas Mayapila,na Trafiki wenzako kisiwakatishe tamaa, pole sana na jenga taifa lako bila woga.

Mungu ibariki Tanzania Mungu Ibariki Afrika

0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Mei 24, 2009

KORTI YAAMURU USHAHIDI KESI YA MRAMBA UANIKWE

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imeamuru upande wa mashitaka katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7, inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake, kuanika ushahidi na vielelezo watakavyovitumia.

Mbali na Mramba, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Daniel Yona, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini na Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Grey Mgonja.

Uamuzi huo ulitolewa jana na jopo la mahakimu wakazi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wanaongozwa na John Utamwa anayesaidiana na Saul Kinemela na Fatma Masengi, ambao walisema wamefikia uamuzi huo, kwani matakwa ya kisheria yanataka upande wa utetezi upate fursa ya kufahamu na kuelewa vielelezo na ushahidi utakaotumika katika kesi inayowakabili.

Akisoma uamuzi wake jana, Hakimu Utamwa, alisema hoja ya upande wa utetezi ya kutaka kupatiwa nyaraka za vielelezo kabla ya wateja wao kusomewa maelezo ya awali si muhimu, bali upande wa mashitaka unapaswa kuanika nyaraka hizo, vielelezo vitakavyotumika katika kesi hiyo.

Akiendelea kusoma uamuzi wake alisema hoja ya upande wa utetezi iliyowasilishwa Jumatatu wiki hii na Profesa Leonard Shaidi ya kutaka kupatiwa nyaraka za vielelezo kabla ya wajeta wao kusomewa maelezo ya awali, alisema hilo siyo la muhimu.

‘Hoja ya upande wa utetezi yakutaka wapatiwe nyaraka nyaraka zitakazotumiwa na upande wa mashtaka katika kesi hii siyo muhimu, cha muhimu hapa ni upande wa mashtaka uanike nyaraka hizo,vielelezo na waakikishe upande wa utetezi unazielewa hizo nyaraka” alisema Utamwa.

Utamwa alisema anaairisha kesi hiyo hadi Juni 19 mwaka huu, ambapo itakuja kwaajili ya kutajwa na pia itaanza kusikilizwa rasmi Julai 20-24 mwaka huu, na kutaka upande wa mashtaka ulete mashahidi wake.

Hata hivyo alimruhusu Mramba kwenda kwenye shughuli za kibunge nje ya Dar es Salaam, kuanzia Mei 24-Agosti 25 mwaka huu, nakuongeza kuwa endapo Mramba ataitajika mahakamani atalazimika kusitisha shughuli za kibunge na kuja kuudhulia kesi yake mahakamani.

Jumatatu wiki hii,upande wa mashitaka katika kesi hiyo ulibadilisha hati ya mashitaka baada ya kufutwa kwa shitaka moja.

Shitaka lililofutwa, linamhusu Mramba peke yake, hivyo anabaki na mashitaka 11 badala ya 12.

Shitaka hilo la tano, awali lilikuwa likisomeka kuwa, Oktoba 10, 2003, mshitakiwa huyo (Mramba), akiwa Waziri wa Fedha, alitumia madaraka yake vibaya kwa kudharau mapendekezo ya Mamlaka ya Mapato (TRA) ambayo yalikataza Kampuni ya M/S Alex Stewart (Assayers) Government Bussiness Corporation, isipewe msamaha wa kodi.

Baada ya ombi hilo kuridhiwa na jopo hilo la mahakimu, upande wa mashitaka uliiomba mahakama iwaruhusu kuwasomea upya maelezo ya awali washitakiwa, ombi ambalo lilizua malumbano makali ya kisheria kati ya upande wa mashitaka na wakili wa upande wa utetezi, Profesa Leonard Shaidi.

Profesa Shahidi ambaye alikuwa akisaidiana na Hurbet Nyange na Joseph Tadayo, walipinga ombi hilo wakidai kuwa hawapo radhi wateja wao wasomewe maelezo ya awali bila upande wa mashitaka kuwapatia nyaraka walizopanga kuzitumia kwenye kesi hiyo.

“Waheshimiwa mahakimu, kabla ya upande wa mashitaka kuwasomea wateja wetu maelezo ya awali, tunaomba watupatie nyaraka walizopanga kuzitumia kwenye kesi hii kwa sababu sheria inataka hivyo, kwa hiyo tunaomba mahakama iwaamuru kufanya hivyo,” alidai Profesa Shaidi.

Akijibu pingamizi hilo, Boniface alidai si lazima kisheria upande wa mashitaka utoe nyaraka hizo kwa upande wa utetezi.

Malumbano hayo ambayo yalidumu kwa takribani robo saa, yalisababisha kiongozi wa jopo hilo la mahakimu wakazi, Utamwa, kuahirisha kesi hiyo hadi Alhamisi wiki hii ambapo mahakama itatoa uamuzi kuhusu pingamizi hilo.

Aprili 17, mwaka huu, Mramba ambaye ni mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, kupitia wakili wake, Nyange mbele ya Hakimu Mkazi, Henzron Mwankenja, alikiri kutoa vibali vya msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo na kwamba alifanya hivyo baada ya kuagizwa na Ikulu.

Awali, akisoma maelezo ya awali dhidi ya washitakiwa hao, mwanasheria wa Takukuru, Joseph Holle alidai kuwa washitakiwa hao wakiwa na nyadhifa hizo serikalini, walikuwa na jukumu la kuwa waaminifu na makini katika majukumu waliyokabidhiwa kisheria.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Mei 22, 2009

UAMUZI KESI YA LIYUMBA BADO

Na Happiness Katabazi

KWA mara nyingine, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilishindwa kutoa uamuzi wa kumwachilia huru mshitakiwa wa kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma, aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba na Meneja Miradi wa benki hiyo, Deogratius Kweka, au la.

Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema, alisema jana kuwa ameshindwa kutoa uamuzi huo kwa kuwa hajamaliza kuandaa uamuzi huo. ‘Sijamaliza kuandaa uamuzi, hivyo naahirisha kesi hadi Mei 27 mwaka huu,” alisema Lema.

Kabla ya kuanza kwa kesi hiyo, makachero kutoka Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) walikuwa wametanda pembe zote za mahakama hiyo, ikiwamo ndani ya chumba kilichokuwa kikiendeshwa kesi hiyo, ambao miongoni mwao walidai wamefika kwa ajili ya kuwakamata washitakiwa hao endapo wataachiliwa huru na mahakama.

Hii ni mara ya tatu kwa Hakimu Lema kushindwa kutoa uamuzi kuhusu ombi hilo.
Machi 30, mwaka huu, Lema alianza kuendesha kesi hiyo baada ya Hakimu Mkazi, Hadija Msongo, kujitoa kuendesha kesi hiyo baada ya jamii kupitia vyombo vya habari kulalamikia dhamana ya Liyumba aliyopewa Februari 17.

Awali alipanga kutoa uamuzi kuhusu ombi hilo, April 30, Mei 6 na jana lakini akashindwa kafunya hivyo kama anavyoahidi kwa maelezo kuwa ajamaliza kuandaa uamuzi huo.

April mwaka huu, wakili wa utetezi Majura Magafu anayesaidiana na Profesa Gamalieli Mgongo Fimbo, Hurbet Nyange na Hudson Ndyusepo aliomba washtakiwa waachiliwe huru kwasababu hati ya mashtaka ina kasoro, na pia itupile mbali kibali cha DPP cha kufungua kesi hiyo kwa madai kuwa nacho kina dosari za kisheria.

Hata hivyo Stanslaus aliunga mkono hoja ya Magafu ya kudai kuwa hati ya mashtaka ina kasoro licha alipinga vikali kuwa kibali cha DPP kina kasoro za kisheria.

Machi 30, mwaka huu, Lema alianza kuendesha kesi hii baada ya Hakimu Mkazi, Hadija Msongo ambaye ndiye alikuwa nayo tangu ilipofunguliwa Januari 27, mwaka huu, kujiondoa baada ya jamii kupitia vyombo vya habari kulalamikia dhamana ya Liyumba.

Februari 17, mwaka huu, hakimu Msongo alimwachia kwa dhamana iliyozua utata Liyumba.
Moja ya masharti ambayo hayakutimizwa na Liyumba, ni kuwasilisha mahakamani hati zenye thamani ya sh bilioni 55, wadhamini wawili wa serikali wakiwa na barua kutoka kwa waajiri wao na kukabidhi hati za kusafiria mahakamani hapo.

Lakini siku hiyo, Liyumba aliwasilisha hati yenye thamani ya sh milioni 882, hati ya kusafiria ambayo muda wake wa matumizi umekwisha, huku wadhamini wawili wakiwa hawana barua zilizosainiwa na mwajiri wao kama masharti yalivyotolewa na mahakama.


Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Mei 22, 2009

UPELELEZI KESI YA MEREY HAUJAKAMILIKA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa mashitaka katika kesi ya wizi wa dola za Marekani milioni 1.8 (sawa na sh bilioni 2.4) inayomkabili Mkurugenzi Mtendaji wa Dar es Salaam Cement Muslim na mfanyabiashara maarufu wa mafuta nchini, Merey Ally Saleh (41), jana uliomba kuahirishwa kwa kesi hiyo kwa vile upelelezi wake haujakamilika.

Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ACP) Charles Kenyela, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Euphemia Mingi, aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya kutajwa lakini anaomba iahirishwe kwa vile upelelezi bado haujakamilika.

Naye wakili wa Merey, Martin Matunda, aliomba mahakama kubadilisha wadhamini wa mshitakiwa Merey Ally, baada ya Sahau Kambi, aliyemdhamini awali kufariki. Matunda alidai kuwa mteja wake kwa sasa atadhaminiwa na Abel Mshoro, ombi ambalo lilikubaliwa na mahakama hiyo.

Mbali na Balahbou, washitakiwa wengine ni Meneja Mwendeshaji wa Kigamboni Oil Co. Ltd, Abdallah Said Abdallah (48), wafanyakazi wa Benki ya Barclays, Winford Mwang’onda, Shubira Mutungi, Naima Saria, Upendo Mushi, Magreth Longway, Emmanuel Mukoni na Ramadhani Khamis.

Washitakiwa wote wanadaiwa kuwa kati ya Oktoba 27 hadi Novemba mwaka jana, kwa nyakati tofauti, walikula njama za, kughushi ujumbe wa kasi (swift message), kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuiba dola za Marekani 1,081,263.00, sawa na sh bilioni 2.4, mali ya Benki ya Barclays.

Mapema Machi mwaka huu, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, alitahadharisha mabenki kuwapo kwa mbinu mpya ya wizi unaotumia teknolojia ya kisasa ya kompyuta, ambapo benki za CRDB na Barclays zilikwisha kukumbwa na wizi huo.

Alisema aina hiyo ya wizi ni ngeni nchini na wahusika wanaweza kuchota fedha nyingi kuliko wizi uliozoeleka wa kughushi hundi, saini au ule unaofanywa kwa kuvamia na kupora kwa nguvu kwa kutumia silaha za moto.

Wizi huo ulianza kujitokeza kuanzia mwaka jana, ambapo wezi hao wa mtandao, walifanikiwa kuwashawishi baadhi ya wafanyakazi wa benki na watu wengine kupitisha fedha hizo kwenye akaunti zao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Mei 20, 2009

MARANDA NA WENZAKE WAONGEZEWA MASHITAKA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa mashitaka katika kesi nyingine ya wizi wa sh bilioni 2.2, fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inayomkabili kada wa (CCM), Rajabu Maranda na mpwa wake, Farijara Hussein, jana ulibadilisha hati ya mashitaka, baada ya kuongezwa mashitaka mawili.

Mwanasheria wa serikali, Oswald Tibabyekoma, aliyekuwa akisaidiwa na wanasheria waandamizi wa serikali, Fredrick Manyanda, Michael Lwena na Cedrick Ephery, mbele ya mahakimu wakazi wanaoongozwa na Fatma Masengi, Benedect Mlingwa na Catherine Revocate, ulidai kuwa umefikia uamuzi huo wa kubadilisha hati ya mashitaka baada ya kuongeza shitaka moja la kula njama na kubadilisha shitaka moja.

Tibabyekoma alidai shitaka linalobadilishwa ni shitaka la tano ambalo lilikuwa ni shitaka mbadala la sita, ambapo sasa shitaka hilo litajitegemea.

Hati hiyo ya mashitaka sasa itakuwa na jumla ya mashitaka saba tofauti na awali ambapo ilikuwa na mashitaka sita.

Baada ya kubadilishwa kwa hati ya mashitaka, washitakiwa walisomewa maelezo ya awali, ambapo ilidaiwa kuwa washitakiwa wote kati ya Machi na Desemba 2005, walikula njama, kuiba, kughushi, kuwasilisha hati za uongo, kujipatia ingizo na kuibia BoT sh bilioni 2.2 kwa kuonyesha hati zinaonyesha kutolewa na ofisi ya Wakala wa Usajili wa makampuni, (BRELA) kwamba wao ni wakurugenzi wa Kampuni ya Money Planers Consultant na Kampuni ya B. Grancel ya Ujerumani imeipatia idhini kampuni yao kukusanya deni la fedha za Kijerumani 3,137,488.40 ambazo ni sawa na sh bilioni 2.2.

Washitakiwa hao wanaotetewa na wakili wa kujitegemea Majura Magafu, walikana mashitaka yote na kiongozi wa jopo la mahakimu wanaosikiliza kesi hiyo, Masengi, aliiahirisha hadi Juni 16, mwaka huu, ambapo itakuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba itaanza kusikilizwa rasmi Julai mosi mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Mei 20, 2009

KWA NINI TUSIWE WAKWELI JUU YA MAJANGA?

Na Happiness Katabazi

“UHURU kwa wengi unamaanisha uhakika wa maisha, hata kama ni kwa kutumia uchawi.Isipokuwa kama sitakutana na baadhi ya mambo ya kunitia moyo, msaada wangu utapungua na kichwa changu kitazunguka kama vile ndege anavyomfuata Kifaru.”

Maneno hayo yaliwahi kutamkwa na Baba wa Taifa letu, Julius Kambarage Nyerere alipokuwa akizungumzia umuhimu na raha ya uhuru.

Ikumbukwe kuwa April 29 mwaka huu, kwenye maghala ya silaha ya Kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) Mbagala, mabomu yalilipuka na kusababisha maafa makubwa ikiwemo watu kupoteza maisha, kujeruhiwa na makazi ya watu kuharibika jambo liliowafanya baadhi ya yao kuhifadhiwa katika kambi maalumu.

Nimelazimika kuitumia nukuu ya Hayati Nyerere katika makala yangu ya leo kwa sababu baadhi ya Watanzania waishio Mbagala na vitongoji jiji la Dar es Salaam, kwa kiasi kikubwa hivi sasa wamekumbwa na wasiwasi mkubwa usalama wao na mali wanaozimiliki.

Wananchi hao hawana uhuru kama ilivyokuwa kabla ya kutokea kwa milipuko hiyo, hawawezi kufanya shughuli zao za kuwaingizia vipato kwa ufanisi.


Kama ilivyo desturi ya serikali yetu mara kwa mara imekuwa na tabia ya kutoa kauli za kutatanisha na zenye kuwafariji wananchi pindi linapotokea tatizo lakini hujua walisemalo si hilo walitekelezalo au kulipanga.

Tabia hii hivi sasa inaonekana kuanza kuota mizizi miongoni mwa viongozi na nina hakika ipo siku watakuja kuumbuka baada ya ukweli kubainika.

Kuna mambo mengi tu ambayo kauli zao zimewaumbua lakini wameshindwa au hawataki kujifunza kutokana na makosa waliyoyafanya ama kwa kiburi au hofu waliyonayo.

Desturi hiyo ya kipuuzi pia iliendelea kutamalaki baada ya tukio hilo kutokea kwa viongozi wetu kutoa kauli za aina hiyo.

Sote tunakumbuka tamko la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, alivyowataka wakazi wa Mbagala warejee katika maeneo yao kwa kuwa uongozi wa JWTZ umemdhibitishia eneo hilo ni salama na wameshadhibiti ulipukaji wa mabomu hayo.

Mapema wiki hii, Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo alinukuliwa akiwataka wananchi kutohofia operesheni inayoendelea ya uteketezaji mabomu katika kambi ya Mbagala, aliwataka wananchi kutohofu operesheni hiyo kwa kuwa ni sehemu ya jeshi hilo kusafisha mabomu hayo baada ya mlipuko wa April 29.

Ni jambo lilo wazi kuwa kulingana na mazingira yaliyopo hivi sasa hali si shwari katika eneo hilo licha ya baadhi ya viongozi wetu sasa wamejigeuza kuwa wahudumu wa afya ambao nao miongoni mwao wamekuwa wakitoa kauli za kuwafariji wagonjwa ambao wengine wana hatua mbaya kwa kuwaambia watapona haraka lakini wakijua fika hawasemi ukweli

Hivi tunamdanganya nani katika hili kama siyo kutaka wananchi wenzetu waendelee kuumia na mwisho wa siku serikali itajikuta inatumia fedha zaidi za walipa kodi kwa ajili ya kuwatibia majeruhi wapya wa milipuko hiyo hiyo?

Au serikali yetu inaona raha wananchi wasio na hatia wanavyoanguka na kupoteza fahamu pamoja na kuvuta hewa mbaya ya mabomu pindi yanapolipuka?

Kwanini serikali isione haja ya kutafuta maeneo ya wazi mbali kabisa na maeneo ya Mbagala na kujenga kambi za muda kwa ajili ya kuwahifadhi waathirika na wale ambao bado hawajaathirika na milipuko hiyo, ili JWTZ iweze kulipua mabomu yake kwa nafasi hadi itakapomaliza kufanya kazi hiyo ndipo wananchi ambao nyumba zao hazijaathirika warejee kwenye maeneo yao?

Haingii akilini kwamba serikali yetu yenye watalaamu na wasomi lukuki kuridhia kambi za muda za kuhifadhia wahanga hao kujengwa katika eneo ambalo tayari lilikwisha athirika na milipuko hiyo.

Serikali yetu ina maeneo mengi ya wazi lakini cha kushangaza imeamua kuridhia kujengwa kwa kambi katika eneo hilo.Sote tunafahamu suala hilo ni la dharula lakini bora tuokoe afya na uhai wa watu kwani Katiba ya Nchi inasema kila mtu ana haki ya kuishi na serikali ina jukumu la kulinda mali na usalama wa raia wao.

Endapo serikali itafanyia mzaha jambo hili na mabomu yakaendelea kulipuka na wananchi wakendelea kuumia, siku za usoni, serikali isije ikahamaki pale wananchi watakapojitokeza kwa wingi katika mahakama zetu kufungua kesi dhidi ya Jeshi la Polisi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wakitaka walipwe fidia ya mabilioni kwa kile watakachokidai kuwa wamepoteza kuibiwa mali zao, wamepoteza baadhi ya viungo vyao.

Hatupendi tufike huko, naiomba serikali yetu ifikirie upya na kuwahamisha wakazi waishioo eneo hilo mpaka pale hali itakapokuwa salama kweli badala ya salama ya kauli za viongozi ambazo sasa zinaelekea kuywakwaza wananchi

Tusisigane katika hili wala kunyosheana vidole wanaoumia ni Watanzania wenzetu na wanaoteseka zaidi ni wanawake na watoto hivyo nasisitiza kufanywa kwa jitihada za haraka kuwanusuru na adha ya milipuko hiyo.

Inasikitisha mpaka sasa hakuna hata mtaalamu mmoja aliyejitokeza hadharani kutuambia kuwa vishindo na moshi ule wa mabomu vina madhara gani, lakini naamini ipo siku waliokumbwa na vitu vyote hivyo viwili watajitokeza na kuweka bayana walivyoathirika.

Mungu ibariki Tanzania,Mungu ibariki Afrika

0716 774496

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Mei 17, 2009

WASHITAKIWA WIZI OFISI YA DPP WAONGEZEKA

Na Happiness Katabazi

IDADI ya washtakiwa wa wizi wa gari na kompyuta, mali ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) inazidi kuongezeka kutokana na mshtakiwa mwingine kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Mshtakiwa huyo Abubakari Kamugisha (31) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Kinyerezi, jijini, alifikishwa mahakamani hapo mwishoni mwa wiki na kusomewa shtaka la wizi wa kutumia silaha.

Kuongezwa kwa mshtakiwa huyo katika kesi hiyo kunafanya idadi ya washtakiwa wanaokabiliwa na tuhuma hizo kufikia 12.

Akisomewa mashtaka hayo na Inspekta Emma Mkonyi alidai Machi 5, Tabata Liwiti CCM, Kamugisha aliiba gari STK 5002 Toyota Hiace modeli mpya lenye thamani ya sh 56,972,000, komyuta sita zenye thamani ya sh 4,250,000, printa zenye thamani ya sh 7,435,000, seti ya UPS, laptop na vitabu vya sheria mali ya ofisi ya DPP na vitu vyote hivyo vikiwa na jumla ya thamani ya sh 111,500,000.

Alidai kwamba kabla ya kuiba vitu hivyo alimtishia kwa bunduki Alfa Makamba, mlinzi wa gereji ambayo gari hilo lilikuwa limelazwa.

Mshtakiwa alikana tuhuma hizo mbele ya Hakimu Mkazi, Eva Nkya, na kupelekwa rumande kuwa kesi hiyo haina dhamana kisheria.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni dereva ofisi ya DPP, Ally Ramadhani Mustapha, Haji Mwanga, Bakari Makara, Deogratus Coster, Philipo Jose, Athony Mengi, Mary Lyimo, Jacob Mosha, Wilfred Maleko, Alex Kimario na Hajat Faraji Kileo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei 19, 2009

MRAMBA APUNGUZIWA SHITAKA

*Ni lile linalohusu mapendekezo ya TRA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa mashitaka katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7, inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake, umebadilisha hati ya mashitaka baada ya kufutwa kwa shitaka moja.
Shitaka lililofutwa, linamhusu Mramba peke yake, hivyo anabaki na mashitaka 11 badala ya 12.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Daniel Yona, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini na Katibu Mkuu mstaafu Wizara ya Fedha na Uchumi, Grey Mgonja.

Ombi hilo la kubadilishwa hati ya mashitaka liliwasilishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana na wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface, akisaidiana na Fredrick Manyanda na wanasheria toka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Tabu Mzee, Beni Linkoni na Joseph Holle.

Wakati Boniface akiwasilisha ombi hilo mbele ya jopo la mahakimu wakazi watatu, linaloundwa na John Utamwa, Saul Kinemela na Fatma Masengi, hakuweka wazi sababu za upande wa mashitaka kufikia uamuzi huo.

Shitaka hilo la tano, awali lilikuwa likisomeka kuwa, Oktoba 10, 2003, mshitakiwa huyo (Mramba), akiwa Waziri wa Fedha, alitumia madaraka yake vibaya kwa kudharau mapendekezo ya Mamlaka ya Mapato (TRA) ambayo yalikataza Kampuni ya M/S Alex Stewart (Assayers) Government Bussiness Corporation, isipewe msamaha wa kodi.

Baada ya ombi hilo kuridhiwa na jopo hilo la mahakimu, upande wa mashitaka uliiomba mahakama iwaruhusu kuwasomea upya maelezo ya awali washitakiwa, ombi ambalo lilizua malumbano makali ya kisheria kati ya upande wa mashitaka na wakili wa upande wa utetezi, Profesa Leonard Shaidi.

Profesa Shahidi ambaye alikuwa akisaidiana na Hurbet Nyange na Joseph Tadayo, walipinga ombi hilo wakidai kuwa hawapo radhi wateja wao wasomewe maelezo ya awali bila upande wa mashitaka kuwapatia nyaraka walizopanga kuzitumia kwenye kesi hiyo.

“Waheshimiwa mahakimu, kabla ya upande wa mashitaka kuwasomea wateja wetu maelezo ya awali, tunaomba watupatie nyaraka walizopanga kuzitumia kwenye kesi hii kwa sababu sheria inataka hivyo, kwa hiyo tunaomba mahakama iwaamuru kufanya hivyo,” alidai Profesa Shaidi.

Akijibu pingamizi hilo, Boniface alidai si lazima kisheria upande wa mashitaka utoe nyaraka hizo kwa upande wa utetezi.

Malumbano hayo ambayo yalidumu kwa takribani robo saa, yalisababisha kiongozi wa jopo hilo la mahakimu wakazi, Utamwa, kuahirisha kesi hiyo hadi Alhamisi wiki hii ambapo mahakama itatoa uamuzi kuhusu pingamizi hilo.

Aprili 17, mwaka huu, Mramba ambaye ni mshitakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, kupitia wakili wake, Nyange mbele ya Hakimu Mkazi, Henzron Mwankenja, alikiri kutoa vibali vya msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo na kwamba alifanya hivyo baada ya kuagizwa na Ikulu.

Awali, akisoma maelezo ya awali dhidi ya washitakiwa hao, mwanasheria wa Takukuru, Joseph Holle alidai kuwa washitakiwa hao wakiwa na nyadhifa hizo serikalini, walikuwa na jukumu la kuwa waaminifu na makini katika majukumu waliyokabidhiwa kisheria.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei 19, 2009

MSHITAKIWA EPA AMLIPUA OFISA BOT

Na Happiness Katabazi

MSHTAKIWA wa kwanza katika kesi ya wizi wa bilioni 1.86 za Fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), Bahati Mahenge, amedai aliagizwa na ofisa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) akafungue kampuni ya mfukoni ya Changanyikeni Residential Complex kwa ajili ya wakubwa.

Madai hayo ya Mahenge ambayo aliyaandika wakati akichukuliwa maelezo ya onyo katika Ofisi za Tume ya Rais ya Kuchunguza Wizi wa EPA, Mikocheni, Machi 12 mwaka jana, ambayo yalisomwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, mpelelezi wa wizi wa kughushi nyaraka toka Makao Makuu ya Upelelezi wa Jeshi la Polisi, ASP Deustedint Mataba.

Mataba akisoma maelezo hayo, alidai Mahenge alieleza mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo ni baba yake mdogo na kwamba aliwahi kufanya kazi katika Kampuni ya Dar Air Service iliyokuwa ikimilikiwa na mshtakiwa huyo.

Alieleza wakati akifanyakazi hapo alifahamiana na ofisa huyo wa BoT aliyemtaja kwa jina moja la Berya (sasa marehemu) na kwamba alimtaka afungue Kampuni ya Changanyikeni Residential Complex.

“Siku inayofuata nikakutana na Berya na Manase (mshtakiwa wa pili) katika mgahawa wa City Garden, wakaniambia wakati nitakapofungua kampuni hiyo nisiandike jina langu la Bahati bali nitumie jina la kufikirika la Samson Mapunda ambapo kwa mujibu wa jina hilo la kufikirika nikawa mkurugenzi wa kampuni hiyo feki,” alidai Mahenge katika maelezo hayo.

Alidai baada ya kuelezwa hayo Berya hakuonyesha kushtuka kwani alikuwa akijua mpango mzima na kuongeza kuwa ofisa huyo ndiye alimpigia simu na kumtaka akafungue akaunti ya kampuni hiyo katika Benki ya CRDB Tawi la Kijitonyama ambapo alijaza fomu hizo, akabandika picha yake halisi huku akitumia jina la bandia la Samson.

Mahenge ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea Majura Magafu , alidai baada ya mchakato huo kumalizika akaunti hiyo iliingiziwa sh bilioni 1.86 toka BoT na wakati mwingine alikuwa akiletewa hundi na Manase na alikiri kutoifahamu Kampuni ya Marubeni Ltd ya Japan ambayo kwa mujibu wa hati ya kuhamisha deni inaonyesha kampuni hiyo ya nje ililiridhia kampuni ya Changanyikeni ikusanye deni lake wanaloidai.

Kesi hii ilianza kusikilizwa rasmi juzi ambapo shahidi wa kwanza ASP Mataba alianza kutoa ushahidi wake lakini hata hivyo alishindwa kumalizia baada ya Magafu kuwasilisha pingamizi kuwa kabla ya mteja wake hajachukuliwa maelezo ya onyo kwenye tume ile alifanyiwa ukatili.

Sababu hiyo ilisababisha jopo hilo kukukabili kufanyika kwa kesi ndogo ambapo upande wa mashtaka ulileta mashahidi watatu.
Leo upande wa utetezi katika kesi hiyo ndogo unatarajiwa kuleta mashahidi watatu ili kuthibitisha jinsi mshtakiwa alivyofanyiwa ukatili.

Mbali na Mahenge anayetetewa na wakili wa kujitegemea Majura Magafu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo Manase Makale, Davis Kamungu, Godfrey Mosha na Eda Makale wanatetewa na Mabere Marando, Michael Ngaro na Mafuru.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Mei 15,2009

DOWANS YABWAGWA MAHAKAMANI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Biashara, Dar es Salaam, jana ililifukuza ombi la Kampuni ya Dowans Tanzania Ltd, lililokuwa likiitaka mahakama hiyo ifute maombi ya Shirika la Umeme (TANESCO) la kutaka mitambo hiyo isiuzwe kwa sababu yalikuwa na dosari za kisheria.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Robert Makaramba, ambapo alisema amefikia uamuzi wa kutupa maombi hayo kwa sababu Dowans imeshindwa kuishawishi mahakama ni vipi Tanesco ilitumia vifungu vya sheria visivyo sahihi kuwasilisha ombi lake katika mahakama hiyo.

“Kwa kuwa Dowans imeshindwa kuishawishi mahakama hii ikubaliane na ombi lake, mahakama inalitupa ombi la Dowans na badala yake, inakubaliana na ombi la Tanesco la kutaka mitambo hiyo isiuzwe hadi nitakapotoa uamuzi wa kesi hii, Julai 2, mwaka huu,” alisema Jaji Makaramba.

Jaji Makaramba alisema kuhusu hoja ya Dowans kuwa, mamlaka hiyo haikuwa na uwezo wa kutolea maamuzi ya maombi yaliyowasilishwa na Tanesco, ni dhaifu kwa sababu tayari mahakama hiyo katika kesi hiyo hiyo, ilishawahi kutoa amri ya kuzuia kwa muda mitambo ya kampuni hiyo isiuzwe.

Mei 4, mwaka huu, Kampuni ya Dowans kupitia wakili wake, Abduel Kitururu, iliwasilisha ombi lake mahakamani hapo la kutaka mahakama hiyo itupilie mbali ombi la Tanesco la kuzuia kuuzwa kwa mitambo yake ya kufufua umeme, kwa sababu maombi hayo hayana msingi, kwamba Tanesco inayotetewa na wakili Alex Nguruma imewasilisha mahakamani maombi yake kwa kutumia kifungu kisichokubalika katika kuwasilisha maombi yao.

Katika maombi yake, Tanesco inaiomba mahakama kuzuia Kampuni ya Dowans kuuza mitambo yake kwa namna yoyote hadi shauri lililowasilishwa na Dowans kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa iliyoko Paris, Ufaransa litakapotolewa uamuzi.

Hata hivyo, Tanesco katika kesi hiyo, inaiomba mahakama iiamuru Dowans iweke mahakamani asilimia kumi ya dola za Kimarekani 109,857,686 kama dhamana kufuatia gharama zitakazotumika katika kesi iliyopo Paris.

Katika hoja zake zilizowasilishwa mahakamni hapo kupinga maombi hayo, Wakili Kitururu amedai Tanesco imeleta maombi hayo kwa kutumia kifungu 95 cha sheria ya mwenendo wa kesi za madai (Civil Procedure Code) na kifungu cha 23 (2) cha Sheria inayojulikana kama International Chamber of Commerce Rules.

Kupitia hoja hizo, kifungu hicho hakiwezi kuipa mamlaka mahakama ya Tanzania kushughulikia maombi kama yaliyowasilishwa na Tanesco hapa nchini, bali kipengele hicho cha sheria kinaweza kutumiwa na upande husika katika shauri hilo katika mahakama ya kimataifa kutafuta amri ya zuio kabla kesi ya msingi haijamalizika kusikilizwa.

Inadaiwa kuwa, Juni 23, 2006 Tanesco iliingia makubaliano ya usambazaji wa umeme wa dharura na Kampuni ya Richmond, ambayo ilielekeza majukumu yake kwa Dowans Holding SA.

Baadaye, Dowans Holdings ilielekeza majukumu yake kwa kampuni yake dada ya Dowans Tanzania Limited. Baada ya mapitio ya makubaliamo hayo na mapungufu yaliyojitokeza Juni 30, mwaka jana, Tanesco iliiandikia Dowans ikieleza kuwa, uhamishaji huo wa majukumu ya kiutendaji hayakuwa halali.

Novemba 2, mwaka jana, Dowans ilifungua kesi katika mahakama hiyo ya kimataifa ikidai kiasi cha dola za Kimarekani 109,857,686 kama gharama za huduma za umeme ambazo zilikuwa hazijalipwa.

Aidha, Desemba 11, mwaka jana, Tanesco iliwasilisha maombi ya kuomba iongezewe muda wa kuwasilisha utetezi wake katika mahakama hiyo, lakini kabla kesi hiyo haijafikia mwisho, Dowans ilitangaza kuiuza mitambo yake.

Kitendo hicho kilikuwa na lengo la kuvuruga namna ya ukazaji wa hukumu itakayotolewa na mahakama hiyo ya kimataifa juu ya gharama za kuendesha kesi hiyo kwa upande wa Tanesco.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamis, Mei 14,2009

MAHAKAMA:MwanaHALISI LIMEMKASHIFU ROSTAM AZIZ

*Latakiwa kumlipa fidia ya shilingi bilioni tatu
*Ni kwa kumhusisha na umiliki wa Richmond
*Latakiwa kumuomba radhi ukurasa wa kwanza
*MwanaHALISI kukata rufaa kupinga hukumu

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, imeliamuru gazeti la kila wiki la MwanaHALISI na washitakiwa wengine kumlipa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz fidia ya shilingi bilioni tatu kwa kuandika habari za kumkashifu na za uongo zilizomhusisha na umiliki wa kampuni ya Richmond.

Mbali na hilo, Mahakama Kuu katika hukumu yake ambayo inaweza kuibua mjadala mkubwa katika taaluma ya uandishi wa habari kwa siku zijazo, imeliamuru gazeti hilo, kuandika habari yenye uzito ule ule katika ukurasa wa kwanza kukanusha habari hiyo dhidi ya Rostam.

Uamuzi huo wa Mahakama Kuu umechukuliwa baada ya Rostam kupitia kwa wakili wake, Kennedy Fungamtama kufungua kesi dhidi ya MwanaHALISI akilalamikia habari iliyochapishwa ukurasa wa kwanza Februari 13, mwaka jana iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho Richmond ya Rostam Aziz-Ikulu.

Mbali ya MwanaHALISI (Mhariri na mchapishaji), wadaiwa wengine katika kesi hiyo ya madai namba 53/2008 iliyofunguliwa na Rostam ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu wa CCM ni kampuni za uchapishaji za Printech Ltd na Standard Printers.

Taarifa ambazo Tanzania Daima Jumatano imezithibitisha kutoka Mahakama Kuu na kwa mawakili wa pande zote mbili zinaeleza kuwa, Jaji Makaramba alitoa hukumu Aprili 30 mwaka huu baada ya kusikiliza malalamiko ya upande wa mashitaka, baada ya walalamikaji, ambao ni gazeti la MwanaHALISI kutowasilisha utetezi wake katika muda uliotakiwa.

Jaji Makaramba ambaye kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo, alikuwa Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Mhadhiri wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema kwa sababu hiyo aliamua kusikiliza ombi la wakili wa mlalamikaji la kutaka mahakama hiyo itumie Order 8 Rule 14 ya Sheria ya Kesi za Madai ya mwaka 2002.

Sheria hiyo ambayo kwa mujibu wa Jaji Makaramba ilitumika pia kuamua kesi kati ya Kilindu dhidi ya CRDB mwaka 1994 inaipa mahakama mamlaka ya kutoa hukumu baada ya kusikiliza hoja za upande wa mmoja pale tu upande mwingine unaposhindwa kuwasilisha utetezi wake kwa wakati.

“Baada ya kusikiliza ombi la Fungamtama kwa makini na kwa kuwa hakuna ubishi kwamba upande wa utetezi umeshindwa kuwasilisha utetezi katika waliopewa na mahakama, natoa hukumu kwa wadaiwa wote na nawaamuru wadaiwa wote kulimpa fidia mlalamikaji sh bilioni tatu,” alisema Jaji Makaramba.

Sambamba na wadaiwa kuamriwa kulipa kiasi hicho cha fidia, Jaji Makaramba amewazuia wadaiwa kuchapisha na habari kama ya awali ambazo zilisababisha mlalamikaji kufungua kesi hiyo kwa sababu habari hiyo ni ya uongo na yenye lengo la kumkashifu mlalamikaji.

Kutokana na hukumu hiyo, tayari Fungamtama ambaye ni wakili wa ameshaliandikia gazeti la MwanaHALISI na kiwanda kilicholichapa gazeti hilo, barua Mei 8 mwaka huu, akilipa siku 14 tangu siku ya hukumu kuwa limeshatekeleza hukumu hiyo ya mahakama. Amri hiyo inafikia mwisho wake kesho Alhamisi.

Fungamtama katika barua yake hiyo, ameieleza MwanaHALISI kwamba, iwapo watashindwa kutekeleza amri hiyo ya katika kipindi hicho, basi watachukua hatua kutekeleza hukumu ya mahakama iliyowapa ushindi.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano kwa simu, Wakili wa MwanaHALISI, Mabere Marando alikiri kuitambua hukumu hiyo na akasema tayari walikuwa wamewasilisha mahakamani kusudio lao kwa kukata rufaa kupinga uamuzi wa Jaji Makaramba.

Mbali ya hilo, Marando alikiri kuchelewa kwao kuwasilisha utetezi kwa wakati uliopangwa na kwamba walipoomba kuongezewa muda Jaji aliwakatalia.

“Ni kweli kwamba tulichelewa ku- file (kuwasilisha) utetezi tukaomba kuongezewa muda, Mheshimiwa Jaji akakataa. Mwenzetu (Rostam) akaomba apewe hukumu moja kwa moja. Jaji akakubali na Aprili 30, hukumu ikatoka.

“Sisi tunavyojua mlalamikaji alipaswa kupewa muda wa kuwasilisha ushahidi wake dhidi yetu hata kama kesi hiyo iliamriwa isikilizwe kwa upande mmoja. Lakini haikuwa hivyo Jaji kampa bilioni tatu. Ameshatoa hukumu. Tunaamini Mheshimiwa Jaji alikosea ndiyo maana tunapinga hukumu yake,” alisema Marando.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano ofisa mmoja wa juu wa Printech ambao ni washitakiwa wa tatu katika kesi hiyo baada ya Mhariri na Mchapishaji wa MwanaHALISI, alisema kampuni yao ina makubaliano ya kisheria na gazeti hilo la kutohusika kwa namna yoyote na shauri lolote litakalotokana na habari wanazoziandika.

Kwa upande wake, Mhariri Mtendaji wa magazeti ya Serikali ambao ndiyo wamiliki wa kampuni ya kuchapisha magazeti ta Standard Printers Ltd, Isaac Mruma alilieleza gazeti hili kwamba, waliingizwa kwa makosa katika kesi hiyo kwani wao hawachapisha toleo la gazeti ambalo lililalamikiwa.

Mruma ambaye alikiri kupata kulichapa gazeti hilo katika mitambo yao, alisema jambo hilo lilitokea muda mrefu kabla ya habari hizo kuandikwa.

Hata hivyo Mruma alisema alikuwa akikusudia kuwasiliana na mwanasheria wao ili kuiangalia hukumu hiyo ambayo wametajwa wakiwa si wahusika.

Wakati Mruma akitoa kauli hiyo, katika barua ya wakili wa Rostam kwenda kwa washitakiwa, hakuiorodhesha Standard Printers Ltd katika barua yake ya Aprili 8, ambayo iliwapa walalamikiwa siku 14 za kutekeleza hukumu ya Mahakama Kuu.

Katika hati yake ya madai ya kesi hiyo ambayo ilifunguliwa Aprili 22, 2008, Rostam anadai kuwa, gazeti la MwanaHalisi la Februali 13-19 la mwaka jana, lenye namba 084, liliandika liliandika na kuchapisha ya habari ukurasa wa mbele habari iliyokuwa na kichwa cha habari- “Richmond ya Rostam Aziz-Ikulu. Ndiye aliyeileta nchini. Lowassa alimuingiza”

Kwa mujibu wa hati hiyo, Rostam anadai kuwa katika matoleo mengine ya gazeti hilo hilo la MwanaHALISI lilikuwa likiandika habari zilizokuwa na lengo la kumkashifu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumatano, Mei 13, 2009

WAKILI AHAHA KUMWOKOA ZOMBE

*Watumia zaidi ya saa sita kutoa hoja mahakamani
*Waomba washitakiwa waachiwe ushahidi ni dhaifu

Na Happiness Katabazi

MAWAKILI wa utetezi katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja, inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (ACP), Abdallah Zombe na wenzake, jana walikuwa na kibarua kibarua kizito cha kuhakikisha wanawanasua wateja wao katika kesi hiyo.

Walikuwa wakiwasilisha majumuisho ya ushahidi katika kesi hiyo baada ya washitakiwa kumaliza kutoa ushahidi wao na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuufunga.

Mbele ya Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Salum Massati, mawakili hao kwa nyakati tofauti walianza kuwasilisha hoja zao saa 4:20 asubuhi na kumaliza kazi hiyo saa 11:19 jioni.
Waliiomba mahakama hiyo kuwaachia huru wateja wao kwa kuwa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo umejaa mkanganyiko mkubwa na pia ni wa kuungaunga.

Pia walisema mashahidi katika kesi hiyo wameshindwa kuthibitisha kama washitakiwa hao walihusika kufanya tukio hilo la mauaji, Januari 14, mwaka 2006.

“Tunaomba wateja wetu waachiliwe huru kwa kuwa hati ya mashitaka inasema mauaji yalifanyika msitu wa Pande, lakini kuna baadhi ya mashahidi walieleza yalifanyika Sinza Ukuta wa Posta. Kwa sababu hiyo, upande wa mashitaka umeshindwa kupeleleza kesi hii kwa umakini na matokeo yake ikaamua kutumia mtego wa panya wa kukamata hata wasiohusika,” alidai wakili Majura Magafu.

Wakili Jarome Msemwa ambaye anamwakilisha Zombe, alidai kitendo cha mteja wake kutoa taarifa za mauaji ya watu hao kwenye vyombo vya habari, si kosa, kwani alifanya hivyo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa askari wake wa chini.

“Hivyo, Zombe alikuwa akiripoti tukio hilo tu, hakuwa mpelelezi na wala hakuwa na mamlaka ya kuwakamata wale marehemu na ndiyo maana alipofika ndugu wa marehemu pale ofisini kwake, aliamuru apelekwe kituo cha polisi Oysterbay kwa sababu askari wa kituo hicho ndio walikuwa wakishughulika na marehemu,” alidai Msemwa.

Kuhusu hoja ya mteja wake kufika Kituo cha Urafiki Januari 15, Msemwa alidai alifanya hivyo baada ya kuitwa na SSP Mantage na kuelezwa tukio zima, na kwamba kama Zombe alikuwa na nia mbaya angechukua sh milioni tano zilizopatikana katika tukio hilo.

Alidai kuhusu maelezo ya aliyekuwa mshitakiwa wa 11, marehemu Rashid Lema, kuwa walipokuwa barabara ya Sam Nujoma alimsikia Bageni akizungumza na simu akiitikia ndiyo afande, wakili huyo alieleza ushahidi huo ni wa kusikia na kamwe hauthibitishi kwamba siku hiyo alikuwa akizungumza na Zombe.

Pia alidai kuhusu Zombe kutoa mkono wa pongezi kwa askari hao, ni kitendo cha kawaida kama ofisa anaridhika na taarifa za askari wake na kuongeza kuwa Zombe hakufanya hivyo kwa ridhaa yake bali kwa mujibu wa utartibu wa Jeshi la Polisi.

“Unaposema mtu kaua ni lazima uonyeshe ushahidi na si vinginevyo, sasa hakuna hata shahidi aliyeweza kuithibitishia mahakama hii kama Zombe aliua watu hao…kilichofanyika Zombe aingizwe kwenye kesi hii ni hatua yake ya kutoa mkono wa pongezi kwa askari na kwenda Urafiki tu,” alidai.

Wakili Msemwa alidai kuhusu baadhi ya washitakiwa kuwa na vikaratasi vilivyoandikwa maelekezo na mteja wake ili wakatoe maelezo ya uongo mbele ya Tume ya Jaji Musa Kipenka, alidai hakuna mshitakiwa aliyeweza kuthibitisha suala hilo kwa vielelezo.

Alieeleza kuwa kesi hiyo imepikwa na magezeti, hali iliyoifanya jamii kumuona mteja wake kuwa ni muuaji na kwamba ni lazima atahukumiwa kunyongwa.

“Lakini hata Yesu alisulubiwa na kudhihakiwa kwamba si mwana wa Mungu, lakini baada ya mateso makali ndipo watesi wake waliamini Yesu ni mwana wa Mungu, hivyo mfano huo naufananisha na mteja wangu ambaye anasulubiwa bila hatia,” alidai Msemwa. Kwa upande wake, wakili wa mshitakiwa wa pili (Christopher Bageni), Ishengoma, alidai kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa, mteja wake hana hatia, kwani kesi hiyo imejengeka katika ushahidi wa mazingira na hakuna ubishi kwamba marehemu walikamatwa Sinza A.

Wakili huyo alidai kuwa, ushahidi uliotolewa na mshitakiwa wa 12, Rajabu Bakari, kwamba siku ya tukio Bageni alipata taarifa za tukio hilo kupitia ‘radio call’, ni uongo na kueleza kuwa anachokifanya mshitakiwa huyo ni kujinasua katika kesi hiyo.

“Rajabu ni muongo na anachokifanya ni kutaka kujinasua aonekane hakushiriki kwenye tukio hilo, kwa kifupi naomba mahakama hii imuone mteja wangu kuwa hana hatia, kwani hata ushahidi uliotolewa ni wa kusikia na wala hauonyeshi kama Bageni alikuwepo kwenye tukio,” alidai.

Aidha, Wakili Magafu ambaye anawawakilisha washitakiwa wa 3, 5, 7, 9 na 10, alidai katika kesi hiyo kuna mkanganyiko mkubwa uliosababishwa na upande wa mashitaka kwa sababu ulikosa umakini na kwamba wapelelezi wa kesi hiyo hawakufanya kazi yao kwa uadilifu.

Magafu akizungumza huku akipaza sauti, alidai ushahidi unaonyesha wazi kuwa marehemu walikamatwa eneo la Sinza, ila mkanganyiko umekuja na umefanya upande wa utetezi ujiulize maswali kuwa mauaji yalifanyika sehemu gani, kwani mashahidi wa upande wa mashitaka walidai kulikuwa na mapambano ya risasi eneo la Sinza, Ukuta wa Posta.

Magafu alidai mkanganyiko wa pili, ni wapi waliuawa marehemu hao, kwani upande wa mashitaka kwenye hati ya mashitaka unaeleza waliuawa msitu wa Pande, lakini mashahidi wanaeleza mapambano ya risasi yalifanyika Sinza.

“Ni mkanganyiko ulioletwa na upande wa mashitaka na swali linabaki, hawa watu waliwaulia wapi? Na mahakama haitakiwi kubebeshwa mzigo wa kujibu swali hilo.

Wanaotakiwa kuthibitisha ni wapi waliuliwa ni upande wa mashitaka na hadi sasa wameshindwa kuonyesha hilo,” alidai Magafu na kuomba mahakama kuwaachia huru wateja wake.

Kwa upande wao mawakili wa mshitakiwa wa 13 na 12, Myovela na Denis Msafiri nao pia waliomba wateja wao waachiliwe huru, kwani hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa walitenda kosa.

Baada ya mawakili wa utetezi kumaliza kuwasilisha hoja zao, Jaji Massati aliwataka mawakili wa upande wa mashitaka nao kuwasilisha hoja zao, lakini walimuomba jaji kuahirisha kesi hiyo hadi leo.

Hata hivyo, Jaji Massati alisema kwa mujibu wa ratiba ya kikao cha kesi hiyo, inaonyesha kuwa imemalizika jana, hivyo kuiahirisha mpaka itakapopangwa tena.

Mbali ya Zombe na Bageni, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni SP Ahmed Makelle, Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Koplo Abeneth Saro, Rajabu Bakari na Festus Gwasabi.

Wahsitakiwa hao wanadaiwa Januari 14 mwaka 2006, eneo la Mbezi Luis, katika msitu wa Pande, waliwaua Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe, ambao ni wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, Ulanga na Juma Ndugu, ambaye ni dereva teksi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Mei 8,2009

MAREHEMU DITOPILE MZUZURI, NAENDELEA KUKULILIA


Pichani ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, marehemu Ditopile Ukiwaona Mzuzuri, ambaye April 20 mwaka huu, ametimiza mwaka mmoja, tangu afariki dunia mwaka jana mkoani Morogoro.Binafsi nitaendelea kukulia na kukuombea kwa mungu aiweke roho yako mahala pema peponi.Sisi tulikupenda lakini mungu amekupenda zaidi.

LALA SALAMA KESI YA ZOMBE

* Korti yafunga ushahidi wa washitakiwa
* Aliyekuwa mshitakiwa amtetea mwenzake

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imefunga ushahidi wa utetezi katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja, inayomkabili aliyekuwa Kamanda wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (ACP), Abdallah Zombe na wenzake.

Mahakama hiyo imefunga ushahidi huo, baada ya mashahidi wawili wa washitakiwa wa pili na 13 kumaliza kutoa ushahidi wao jana.

Baada ya mashahidi hao kutoa ushahidi wao, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati, alisema hatua inayofuata katika kesi hiyo leo ni kwa pande zote mbili kuwasilisha hoja za majumuisho ya ushahidi.

“Kwa sababu upande wa utetezi nao umefunga ushahidi, naahirisha kesi hii hadi kesho (leo), ambapo pande zote zitakuja kutoa hoja za majumuisho ya ushahidi uliotolewa na upande wa utetezi,” alisema Jaji Massati.

Aidha, katika hali isiyotarajiwa, jana Zombe mara kwa mara alionekana akijifuta machozi wakati shahidi wa mshitakiwa 13, Koplo Morris Nyangelela alipokuwa akitoa ushahidi wake.

Nyangelela ambaye awali alikuwa mshitakiwa katika kesi hiyo na baadaye kuachiwa huru, alidai Januari 15, mwaka 2006 waliitwa ofisini kwa Zombe na kupewa mkono wa pongezi kwa kazi nzuri ya kuwaua majambazi.

Alidai askari kupewa mkono wa pongezi ni jambo la kawaida kwa kuwa taarifa za matukio ya uhalifu huanzia kwa askari wa chini na kisha kupelekwa kwa askari wa vyeo vya juu.

Alidai Januari 15, mwaka 2006, akiwa askari polisi wa kituo cha Chuo Kikuu, walipokea taarifa ya kuwapo kwa tukio la uhalifu Barabara ya Sam Nujoma, hivyo yeye na askari wenzake walikwenda eneo la tukio na kukuta lori la Bidco.

Alieleza walipowahoji walielezwa kwamba wameporwa sh milioni tano na kabla ya kuporwa walitishiwa kwa bastola na majambazi waliokuwa wakitumia gari aina ya saloon nyeupe.

Kwa upande wake, shahidi wa mshitakiwa wa pili, DE4595 Koplo Jumanne Mussa (42) kutoka Kituo cha Polisi Oysterbay, jana alijikanyaga alipokuwa akitoa utetezi wake, hali iliyowafanya mawakili wa serikali kumuuliza maswali ya kumtilia shaka kwamba alikuwa amekwenda mahakamani hapo kutoa ushahidi wa uongo.

Mussa akitoa ushahidi wake alidai kuwa, Januari 14, 2006 alimpeleka mshitakiwa wa pili, Christopher Bageni kwenye grocery iliyopo Kijitonyama ambayo ilikuwa imevamiwa na majambazi na kwamba waliwachukua majeruhi na kuwapeleka Hospitali ya Mwananyamala.

Kauli hiyo ilimfanya Wakili wa Serikali, Angaza Mwipopo kuuliza maswali kadhaa ambayo alionekana kushindwa kuyajibu na hata alipopewa kumbukumbu za Jeshi la Polisi azisome alikataa kufanya hivyo.

Hata hivyo, Wakili Mwipopo alidai kwa mujibu wa kumbukumbu za Jeshi la Polisi, siku hiyo ulinzi 122 ambayo ni Bageni, hakufika eneo hilo na aliyefika alikuwa ulinzi 121 (Mkuu wa Kituo cha Polisi Oysterbay).

Bageni wakati akijitetea aliiambia mahakama siku hiyo alikuwa shambani kwake Pugu na kwamba simu na redio call zilikuwa hazipatikani kwani mawasiliano yalikuwa mabovu na kwamba tukio hilo la uhalifu wa Sinza alilipata kupitia redio call.

Mbali ya Zombe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni SP Christopher Bageni, SP Ahmed Makelle, Jane Andrew, Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Koplo Abeneth Saro, Rajabu Bakari na Festus Gwasabi.

Zombe na wenzake, wanadaiwa kufanya mauaji hayo Januari 14 mwaka 2006, eneo la Mbezi Luis, katika msitu wa Pande, ambapo waliwaua, Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe, ambao ni wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, Ulanga na Juma Ndugu, ambaye ni dereva teksi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi,Mei 7,2009