KESI YA WIZI BARCLAYS

Mfanyabiashara aunganishwa na
Merey Balhabou

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE serikali jana ilimuunganisha mfanyabiashara maarufu wa madini, Justice Rugaibura (36), mkazi wa Msasani Beach, jijini Dar es Salaam, katika kesi ya wizi wa dola za Kimarekani milioni 1.08 (sawa na sh bilioni 1.40) kwa njia ya mtandao wa kompyuta, mali ya Benki ya Barclays, inayomkabili Mkurugenzi Mtendaji wa Dar es Salaam Cement Muslim na mfanyabiashara maarufu wa mafuta nchini, Merey Ally Saleh (41), anayefahamika zaidi kwa jina la Merey Balhabou na wafanyakazi saba wa benki hiyo.


Wakili wa Serikali, Teophil Mutakyawa mbele Hakimu Mkazi Euphemia Mingi, alidai kesi hiyo ilikuja jana kwa ajili ya upande wa mashitaka kuweza kumuunganisha Rugaibura na washitakiwa wengine tisa, hivyo kufanya sasa kesi hiyo kuwa na washitakiwa kumi.

Akisoma hati hiyo ya mashitaka, Mutakyawa alidai kuwa ina jumla ya mashitaka 20, na kwamba Rugaibura ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea, Daudiosus Ishengoma, anakabiliwa na mashitaka kumi.

Mbali na Balhabou, washitakiwa wengine ni Meneja Mwendeshaji wa Kigamboni Oil Co. Ltd, Abdallah Said Abdallah (48), Winford Mwang’onda, Shubira Mutungi, Naima Saria, Upendo Mushi, Magreth Longway, Emmanuel Mukoni na Ramadhani Khamis.

Wakili huyo alidai kuwa, shitaka la kwanza ni la kula njama na kutenda kosa ambalo linawahusu washitakiwa wote ambapo Oktoba 29-30 mwaka jana, wanadaiwa kula njama katika eneo lisilofahamika jijini Dar es Salaam, walifanya udanganyifu na kuiibia benki hiyo dola za Kimarekani 1,081,263.00.

Shitaka la pili alidai ni la kughushi, kwamba Oktoba 27, mwaka jana, katika eneo lisilofahamika, walighushi ujumbe wa kasi wenye namba SEQ 000303, kuonyesha kwamba ni halisi na kuutuma kwenye akaunti Na. 0157001698 ya Ramadhani Mussa Hamisi, na kisha kuhamisha dola za Kimarekani 80,500, huku wakijua ujumbe huo umeghushiwa.

Shitaka la tatu linawakabili wafanyakazi wa benki hiyo ambalo ni la kusaidia kosa la wizi kwa kufungua akaunti feki Na. 0008001993 ya Kigamboni Oil Co. Ltd, iliyokuwa na dola za Kimarekani 700,767 na 299,974 bila akaunti hiyo kufunguliwa kwenye kaunta ya benki hiyo, kwa lengo la kuendelea kuiba dola za Kimarekani 1,000,741.00, mali ya benki ya Barclays.

Katika shitaka la nne, washitakiwa hao ambao ni wafanyakazi wa Barclays wanadaiwa kusaidia watu wengine kuiibia benki hiyo.

Inadaiwa kuwa, walifungua kinyemela akaunti Na. 0157001698 ya Ramadhani Mussa Khamisi iliyokuwa na akiba ya dola 80,500.00 ambapo ilimsaidia Khamisi kuendelea kuiba dola 80,500 mali ya benki hiyo.

Aliendelea kudai kuwa shitaka la tano ni la kufungua akaunti kwa njia haramu, linalomkabali Subira Mutungi pekee ambaye anadaiwa aliifungua bila mwajiri wake kujua na kisha kuingiza dola 299,974.00 kwenye akaunti Na.00080001993 ya Kigamboni Oil Co. Ltd, huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Shitaka la sita linalomkabili Mutungi ni kwamba, Oktoba 28, mwaka jana katika makao makuu ya Barclays akiwa mwajiriwa wa benki hiyo, kama muingiza kumbukumbu wa benki, kwa nia ovu aliingiza isivyo halali dola 80,000.00 kwenye akaunti Na. 0157001698 ya Ramadhani Khamisi, huku akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Shitaka la saba ambalo ni kwa ajili ya mshitakiwa wa sita (Mukono), ni la kujaribu kuiba, ambapo Novemba 3 mwaka 2008 katika makao makuu ya Barclays, bila halali yoyote, aliwasilisha hundi yenye namba 0000002 ya sh 60,000.00 na hundi yenye namba 000006 ya dola 40,000.00 kwa lengo la kutoa kiwango cha fedha kilichotajwa kutoka kwenye akaunti Na. 0222824801 ya Gralic Inter Traders Ltd.

Shitaka la nane ni la kujaribu kuiba, linalomhusu mshitakiwa wa sita, Mukono ambapo tarehe na wakati kama huo, alijaribu kuiba kiasi hicho cha fedha katika makao makuu ya Benki ya Stanbic.

Shitaka la tisa linamhusisha mshitakiwa wa saba (Khamis), ni la wizi, kwamba kati ya Oktoba 29-30 mwaka jana katika benki ya Barclays, tawi la Slipway, bila halali yoyote aliiba fedha taslimu dola za Kimarekani 80,500,000, mali ya benki hiyo.

Shitaka la kumi linalowakabili washitakiwa wa kwanza, pili, tatu, nne, tano, nane, tisa na kumi ni la kughushi, ambapo inadaiwa kwamba Oktoba 27 mwaka jana, walighushi ujumbe wa kasi wenye Na. SEQ.000305 ili kuonyesha ni halisi na kuutuma kwenye akaunti ya Kigamboni Oil Co. Ltd Na. 8001993 na kisha kuhamisha dola za Kimarekani 700,769.00.

Aliendelea kudai kuwa, shitaka la 11, pia ni la kughushi ambalo linawahusu tena washitakiwa wote hao, kwamba baada ya kughushi ujumbe huo wa kasi, walifanikiwa kuiba kwa kuhamisha dola za Kimarekani 299,974.

Shitaka la 12 ambalo linawahusisha washitakiwa wa nane, tisa na kumi (Said, Balhabou na Rugaibura), ni la wizi, kwamba wafanyabiashara hao Oktoba 30 mwaka jana katika muda tofauti katika makao makuu ya benki hiyo, bila halali yoyote waliiba fedha taslimu dola za Kimarekani 700,769.00 mali ya benki ya Barclays.

Wakili Mutakyawa alidai shitaka la 13 ni la wizi ambalo pia linawahusisha wafanyabiashara hao watatu, kwamba Oktoba 30 mwaka jana, katika makao makuu ya benki hiyo waliiba fedha taslimu dola za Kimarekani 299,974.00.

Shitaka la 14, linamhusu mshitakiwa wa kumi (Rugaibura), kwamba Oktoba 30 mwaka jana katika benki ya Stanbic tawi la May Fair bila halali yoyote kupitia akaunti Na. 0222824801 aliiba fedha taslimu dola za Kimarekani 200,000.00.

Shitaka la 15 ni la wizi ambalo linamkabili Rugaibura peke yake ambapo anadaiwa kuwa, Oktoba 31, mwaka jana katika tawi la Stanbic May Fair, alitumia akaunti Na. 012282480 na kuiba fedha taslimu sh 200,000,000 kwa kutumia hundi yenye Na. 000001, mali ya Barclays.

Shitaka la 16, Mutakyawa alidai pia linamhusu mshitakiwa wa kumi pekee (Rugaibura), la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ambapo Oktoba 30, mwaka jana, kitika makao makuu ya Barclays, alijipatia fedha taslimu dola za Kimarekani 300,000.00 kupitia hundi yenye Na. 100103 toka kwa Daudi Salehe wa Kigamboni Oil Co. Ltd.

Baada ya kuwasilisha hundi hiyo, alidai malipo hayo yametoka kwa mteja wake, ambaye ni mwekezaji kwenye mgodi wa dhahabu mkoani Mara, huku akijua kwamba si kweli.

Shitaka la 17 ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, linalomkabili pia Rugaibura, ambaye anadaiwa kuwa akiwa Mkurugenzi wa Gralic Traders Co. Ltd, Oktoba 30, mwaka jana katika benki ya Stanbic tawi la May Fair, kwa nia ovu, aliwasilisha hundi iliyoghushiwa Na.120795 na kujipatia dola za Kimarekani 345,000.00, mali ya Barclays.

Shitaka la 18 ni kwa ajili ya Rugaibura pekee la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ambapo Oktoba 30 mwaka jana, katika makao makuu ya Barclays, alijipatia fedha taslimu sh 200,000,000 kupitia hundi Na.100020 kutoka kwa Daud Saleh wa Kigamboni Oil Co. Ltd.

Baada ya kughushi hundi hiyo, alionyesha kuwa ni halisi na kwamba hayo ni malipo halali ambayo amelipwa ili aweze kuendeleza mrandi wa uwekezaji wa mgodi wa dhahabu mkoani Mara.

Aidha, wakili huyo wa serikali alidai pia shitaka la 19, linamhusu mshitakiwa huyo peke yake, ambalo ni la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kwamba akiwa ni Mkurugenzi wa Gralic Traders Co. Ltd, tarehe hizo katika benki ya Stanbic tawi la May fair aliwasilisha hundi ya kughushi yenye Na.157856 na kufanikiwa kujipatia sh 300,000,000 mali ya Barclays.

Shitaka la 20 ni la Rugaibura la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu. Kwamba akiwa mkurugenzi wa kampuni hiyo, Oktoba 30 mwaka jana, katika Benki ya Stanbic tawi la May Fair, aliwasilisha hundi yenye Na.100102 kwa lengo la kujipatia dola za Kimarekani 445,000.00, mali ya Barclays.

Hata hivyo, washitakiwa wote walikana mashitaka yote na upelelezi wa kesi itakayotajwa tena Novemba 2, haujakamilika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Septemba 18,2009

MRAMBA,YONA WAWEWESEKA KORTINI

Na Happiness Katabazi

HALI ya mambo katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake wawili, imeanza kubadilika baada ya washitakiwa hao kukubali maelezo kuwa waliwahi kuhojiwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) na kutoa maelezo baada ya juzi kuyakana.

Washitakiwa hao walifikia uamuzi huo jana baada ya kuongozwa na mawakili wao, Hurbert Nyange, Msuya na Profesa Leonard Shahidi, Joseph Tadayo na Peter Swai, kukiri maelezo hayo yaliyotolewa na mawakili wa upande wa serikali.

Jana upande wa utetezi ulikuwa ukijibu hoja za upande wa serikali ambazo jana waliziwekea pingamizi.

Wakijibu hoja hoja, mawakili wa utetezi, walianza kwa kukubali kwamba wateja wao walitoa maelezo katika taasisi hiyo ila hawajawahi kukiri kwamba walitenda kosa hilo.

“Nakubali pia mteja wangu Mramba anakubali alipata kusailiwa na PCCB na akatoa maelezo ila ninaomba ieleweke alitoa mawelezo si kukiri kosa,”alidai wakili Nyange.

Juzi wakili Mwandamizi Fredrick Manyanda aliwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao na kudai kabla ya kufikishwa mahakamani walihojiwa na taasisi hiyo na kukiri kutenda kosa, ambapo mawakili wa utetezi walikanusha na kudai wateja wao hawajahi kuhojiwa mahala popote.

Aidha, mawakili hao wa utetezi walikubali wateja wao walikuwa ni viongozi wenye nyadhifa kubwa serikali na wanakubaliana kwamba walipaswa kuwa waadilifu, waaminifu na kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wa wakili Nyange, alieleza kuwa Mramba aliombwa na aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, marehemu Daud Balali ruhusa ya kutia saini mkataba wa kampuni Alex Stewart (Asseyers) Government Business Corporation.

Mramba pia alikubali alimwandikia barua mshitakiwa wa pili (Yona) kwamba katika makisio ya matumuzi ya fedha za serikali mwaka 2003/2004 hakukutengwa fungu la kumlipa mkaguzi wa dhahabu ambaye ni kampuni hiyo.

Kuhusu wakili wa mshitakiwa watatu, Profesa Shaidi, alidai kuwa Mgonja anakubali alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha mwaka 2002-2008 na kuyakana maeneo mengine.

Kesi hiyo imeahirishwa haod Septemba 22 mwaka huu kwa ajili ya upande wa mashitaka kuanika idadi ya mashahidi wake na vielelezo vitakavyotumika wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Septemba 18,2009

SERIKALI YAMBANA MRAMBA

*Yadai alitoa msamaha wa kodi bila kuwashirikisha mawaziri, AG
*Yaeleza Yona, Mgonja walivyoshiriki kuifutia kodi Alex Stewart
*Yatoboa siri kwamba washitakiwa waliwahi kukiri kutenda kosa

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa serikali katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi za umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7, inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake, umeieleza mahakama kuwa mshitakiwa huyo alitoa msamaha wa kodi kwa Kampuni ya Alex Stewart (Asseyers) Government Business Corporation bila baraka za Baraza la Mawaziri na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.


Maelezo hayo yalitolewa jana na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Fredrick Manyanda wakati akisoma maelezo ya awali ya kesi hiyo, mbele ya jopo la mahakimu wakazi linaloongozwa na John Utamwa, Sam Rumanyika na Saul Kinemela.

Maelezo hayo yanatofautiana na aliyowahi kuyatoa Mramba kwamba Ikulu wakati huo chini ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa pamoja na Baraza la Mawaziri, walitoa baraka za msamaha huo wa kodi.

Huku akisaidiwa na Mwanasheria wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Tabu Mzee, Manyanda alidai kuwa Mramba aliidhinisha na kuweka saini matangazo ya serikali ya kusamehe kodi kampuni hiyo namba 423/2003, 224/2003, 497/2004, 498/2004, 377/2005 na 378/2005, na kwamba matangazo hayo ya serikali, yalitolewa bila kuzingatia ushauri wa Mamlaka ya Kodi nchini (TRA).

Alidai kuwa, uchunguzi uliofanywa na TRA, umeonyesha kuwa kutokana na misamaha hiyo ya kodi iliyotolewa na Mramba bila baraka za Baraza la Mawaziri na Mwanasheria Mkuu, ilisababisha serikali kupata hasara ya sh 11,752,350,148.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo inayovuta hisia za wengi, ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja, ambao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea; Hurbet Nyange, Peter Swai, Professa Leonard Shaidi na Joseph Tadayo.

Kuhusu Yona, Manyanda alidai kuwa Mei 26, 2003, alishauriwa na Godwin Nyero kutoka Kitengo cha Sheria, kwamba haikuwa vyema kuichukua Alex Stewart (Asseyers) Government Business Corporation kwa madai kuwa ilikuwa ni kukiuka taratibu za zabuni, lakini Yona hakukubaliana na ushauri huo.

Wakili Manyanda aliendelea kudai kuwa, pamoja na ushauri huo, hatimaye hati ya makubaliano ya awali kati ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kampuni hiyo uliandaliwa, ambapo katika kipengele cha nne na tano, vilikuwa vinatoa msamaha wa kodi zote kwa kampuni hiyo.

Alidai kuwa, Mei 26, 2003, ofisa namba moja wa Menejimenti ya Fedha, Mrs Soka, aliishauri Wizara ya Fedha kwamba itafute ushauri kutoka TRA ili kujiridhisha endapo Alex Stewart (Asseyers) Government Business Corporation ilikuwa inastahili kupewa msamaha wa kodi, na kama kulikuwa na barua iliyoandikwa na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Wizara ya Fedha.

“Na katika hati ile ya makubaliano, ilikuwa na mambo mawili ndani yake. Mosi; msamaha wa kodi na alishauri kwamba ni vyema wapate ushauri kutoka TRA,” alidai Manyanda.

Huku washitakiwa hao wakifuatilia maelezo hayo kwa makini, Manyanda alidai kuwa mbali na dokezo hilo, kuna barua iliyoandikwa na Mrs. Soka ya Mei 26, 2003 kwenda kwa Kamishna Mkuu wa TRA, ambayo pia iliambatanishwa na hati ya makubaliano kati ya BoT na kampuni hiyo, ikiomba TRA itoe ushauri kuhusu kifungu cha 4.1 B-D na 5 cha hati ya makubaliano, vinavyohusiana na msamaha wa kodi.

“Wakati ushauri wa TRA unasubiriwa, hati ya makubaliano ilifanyiwa marekebisho katika vifungu hivyo na kisha ikatiwa saini na kuambatanishwa na viambatanisho vya makubaliano hayo, vyote vilitiwa saini Juni 18, 2003 na aliyekuwa Gavana wa BoT, marehemu Daudi Balali kwa niaba ya BoT na Erwin Flores ambaye ni Makamu wa Rais wa Kampuni ya Alex Stewart Government Business Corporation.

“Marekebisho hayo hayakufuata mahitaji ya msamaha wa kodi wa kampuni hiyo na makubaliano hayo yalitiwa saini Juni 18, mwaka huo kwa maelekezo ya Mramba pasipo kuthibitishwa na Baraza la Mawaziri na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, uamuzi ambao ulikiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma ya 2001,” alidai Manyanda.

Aidha, alidai Mramba aliamua kwenda kwa mshitakiwa wa tatu, Mgonja, na kukiri kwamba taratibu za utiaji saini makubaliano hayo zilikiukwa na kuomba ushauri wa namna ya kuidhinisha msamaha wa kodi.

Alidai kuwa, baada ya kutiwa saini makubaliano hayo, TRA ilitoa ushauri wake kupitia barua ya afisa wake, AAM. Temba ya Septemba 24, 2003 ambayo ilisisitiza kampuni hiyo haikustahili msamaha wa kodi.

Wakili huyo alidai kuwa, Juni 12, 2003, Mramba katika barua yake aliyomwandikia Yona, alisema kuwa zoezi la kuajiri kampuni hiyo lililetwa wakati bajeti ya mwaka 2003 hadi 2004 ilishapita, na kwamba matokeo ya kutumia makusanyo kutoka kwenye mirahaba, yangetumika katika ukaguzi wa dhahabu.

“Mramba alimshauri Yona atumie bajeti ndogo ya mwaka 2003-2004 kupeleka makadirio ya matumizi ya bajeti hiyo ili Bunge liweze kujadili kama makusanyo ya mirahaba yatatumika kusaidia zoezi hilo la ukaguzi wa dhahabu,” alidai Manyada na kuiomba mahakama ipokee barua hiyo kama kielelezo, ombi ambalo lilikubaliwa na Wakili wa Mramba, Nyange.

Manyanda alidai kuwa, lakini Mramba hakufikisha suala hilo bungeni katika bajeti ndogo ili liweze kufanyiwa maamuzi, badala yake alimtaka Mgonja amshauri jinsi gani angeweza kutoa misamaha hiyo ya kodi iliyokuwa inaombwa na kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa Manyanda, Agosti 19, 2003 barua toka Wizara ya Fedha kwenda kwa Kamishna Mkuu wa TRA, iliambatanishwa na hati ya makubaliano yaliyotiwa saini Juni 18, 2003 kwa ajili ya ushauri wa pili kama kampuni ya Alex Stewart (Asseyers) Government Business Corporation, ilistahili msamaha wa kodi.

“Kwa mara nyingine tena, TRA kupitia barua yake ya Oktoba 2003, ilithibitisha kuwa kampuni hiyo, haikustahili msamaha wa kodi,” alidai Manyanda.

Alidai kuwa, Septemba 5, 2003, Wizara ya Nishati na Madini, iliiandikia barua Wizara ya Fedha ikiomba msamaha wa kodi kwa niaba ya kampuni hiyo iliyoandikwa na G. L. Mwakalukwa, ambaye ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, ikiomba msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.

Aidha, wakili huyo wa serikali alidai baada ya barua hiyo, Mgonja alimshauri Mramba atoe matangazo ya serikali yaliyokuwa yanatoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.
Kwa kuzingatia ushauri huo, alidai kuwa Mramba aliidhinisha na kuweka saini matangazo ya serikali ya kusamehe kodi kampuni hiyo na yalitolewa bila kuzingatia ushauri wa TRA.

“Tunayo barua toka TRA kwenda kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU ya Septemba 6, 2002, iliyoandikwa na Christine Shekidele, ikieleza matangazo hayo na hasara iliyopatikana, na tunaomba ipokelewe kama kielelezo kama upande wa mashitaka hauna pingamizi,” alidai.

Manyanda alidai kuwa, kati ya Novemba 2003 hadi 2007, Mgonja alikuwa anafanya malipo ya gharama kwenda kwa kampuni hiyo yaliyofikia sh 56,426,913,932.60 ambapo kiasi hicho kilicholipwa, ndicho kampuni hiyo ilipaswa kulipia kodi, na kuongeza kwamba kuna rundo la barua 44, zinazoonyesha malipo hayo na kuomba zipokelewe kama kielelezo.

Aidha, alidai Mramba, Yona na Mgonja walitoa maelezo ya ungamo, na walikiri kila mmoja kwa nafasi yake kwamba walishiriki kutenda makosa wanayoshitakiwa nayo na kuiomba mahakama hiyo ipokee maungamo ya washitakiwa hao.

Hata hivyo, mawakili wote walipinga mahakama isipokee maungamo hayo kwa madai kuwa wateja wao hawajawahi kuungama sehemu yoyote.

Hali hiyo ilisababisha kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi, Utamwa, kutaka vielelezo vyote vilivyobishaniwa na upande wa mashitaka, visipokelewe na jopo lake hadi hapo upande wa mashitaka utakapoanza kuleta mashahidi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi,Septemba 17,2009

MED MPAKANJIA AFARIKI DUNIA

Maelfu wafurika nyumbani kwake Sinza
Msiba wake waibua simanzi ya kifo cha Amina

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA mume wa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), marehemu Amina Chifupa, Mohamed Mpakanjia, amefariki dunia.


Mpakanjia, ambaye alikuwa mfanyabiashara maarufu, amefariki dunia jana majira ya saa nane mchana katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo, kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya hospitali hiyo aliyofia mkewe Amina miaka mitatu iliyopita, vilisema kuwa Mpakanjia, maarufu kwa jina la Med, alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini hapo kwa matibabu.

Kwa mujibu wa habari hizo, mara baada ya kufikishwa katika hospitali hiyo, Mpakanjia aliingizwa kwenye wodi ya watu mashuhuri (VIP), ambako amekuwa akilazwa mara kwa mara na kupatiwa matibabu.

“Ni kweli Mpakanjia amefariki dunia na alifikishwa hapa mchana huu na ndugu zake, lakini alionekana kuzidiwa na ugonjwa, kwani hata baada ya kupokewa na kuanza kutibiwa, aliendelea kuzidiwa na baada ya muda mfupi, alifariki dunia,” alisema mmoja wa wauguzi hospitalini hapo na kuongeza kuwa mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Ndugu wa karibu wa Mpakanjia, waliiambia Tanzania Daima kuwa Mpakanjia amekuwa akifika hospitalini hapo na kutibiwa na wakati mwingine kulazwa kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua tangu alipofariki dunia mkewe na hali hiyo ilidaiwa kutokana na msongo wa mawazo, hasa ikizingatiwa kuwa mkewe alifariki siku chache tu baada ya wanandoa hao kutalikiana.

Akizungumzia kifo hicho, baba wa marehemu Amina, mzee Gabriel Chifupa, alithibitisha kutokea kwa kifo cha mkwewe na kuongeza kuwa msiba utakuwa nyumbani kwa marehemu Mpakanjia, Sinza Mori, Dar es Salaam.

Mpakanjia amekuwa maarufu, lakini umaarufu wake ulizidi hasa baada ya kumwoa Amina, na ndoa ya wawili hao kutawala kwenye vyombo vya habari.

Amina alifariki dunia Juni 27, mwaka 2007, siku ya kilele cha maadhimisho ya Kupambana na Madawa ya Kulevya Duniani.

Enzi za uhai wa wanandoa hao, walibahatika kupata mtoto mmoja wa kiume aitwaye Rahman.

Marehemu Amina Chifupa, ambaye alikuwa mbunge kijana, kitaaluma alikuwa mtangazaji na mwandishi wa habari na alifanikiwa kuingia bungeni kwa mara ya kwanza katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 kupitia UVCCM.

Katika kipindi kifupi alichokaa bungeni, Amina alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na hoja zake nzito, katika kutetea masilahi ya vijana na kukemea rushwa na kuvalia njuga mapambano dhidi ya dawa za kulevya

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Septemba 15,2009

KESI YA KIKATIBA YA LIYUMBA YATAJWA LEO

Na Happiness Katabazi

KESI ya Kikatiba iliyofunguliwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania,Amatus Joachim Liyumba , akiomba mahakama hiyo itamke kwamba kifungu 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya 2002, kinapingana na Katiba ya Nchi,jana ilitajwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo.


Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Kaijage, Zainabu na Projest Rugazia, hata hivyo jana iliweza kutajwa mbele ya jaji mmoja Rugazia, ambaye hata hivyo aliwaeleza mawakili wa mlalamikaji, Hudson Ndusyepo na Majura Magafu kwamba anaairisha kesi hiyo hadi Oktoba 9 mwaka huu kwaajili ya kuona siku hiyo kama upande wa mlalamikaji utakuwa umepewa majibu na upande wa mdaiwa.

Hata hivyo wakati Jaji Rugazia akiairisha kesi hiyo upande wa mdaiwa ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hakuwa umetuma mwakilikishi katika kesi hiyo hali iliyosababisha mahakamani kuwepo na mawakili wa mdaiwa na jaji Rugazia tu.

Liyumba ambaye hadi hivi sasa anaendelea kusota rumande kwaajili ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, alifungua kesi hiyo mapema Julai mwaka huu, na kwa mujibu wa hati yake ya madai katika kesi hii ya Kikatiba, anafafanua kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya 2002, kina mtaka mtuhumiwa anayedaiwa kuiba zaidi ya sh milioni kumi,atoe fedha taslimu au hati ya nusu ya mali anayotuhumiwa kuiba mahakamani ,ndipo apate dhamana.

Kwa mujibu wa hati , Liyumba anaiomba mahakama hiyo itamke kifungu hicho kuwa kinapingana na Ibara ya 13(6)(b) ya Katiba ya nchi ya mwaka 1977, inayotamka bayana kwamba mtu asichukuliwe kuwa ana hatia hadi pale mahakama itakapomkuta na hatia.

Aidha hati hiyo ya madai inadai kuwa kifungu hicho cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, pia kinapingana na Ibara 17(1) ya Katiba ya Nchi, ambapo ibara hii inatamka bayana kuwa kila mtu ana haki ya kuwa huru.

Liyumba anadai hatua ya mtuhumiwa kutakiwa kutoa fedha taslimu au nusu ya mali wakati bado hajatiwa hatiani na kesi inayomkabili, ni wazi mshitakiwa anakuwa ameishahukumiwa jambo alilodai linakwenda kinyume na Ibara ya 13(6)(b) ya Katiba ya Tanzania.

“Kwa sababu hizo tunaiomba mahakama hii,itamke kifungu hicho kuwa ni batili kwani kinakwenda kinyume na haki za msingi zilizoainishwa kwenye ibara hizo za Katiba ya nchi ambayo ndiyo sheria mama” ilisomeka hati hiyo.

Aidha Liyumba aliendelea kudai kuwa yeye kama Mtanzania ana haki ya kuwa huru kwa mujibu wa ibara hiyo, lakini hivi sasa ameshindwa kupata haki hiyo ya uhuru kwasababu kushindwa kuwasilisha fedha au hati ya nusu ya mali ya bilioni 110, mahakamani ili apate dhamana.

“Hivyo haki zangu kwa mujibu wa ibara hizo za Katiba zimenyang’anywa na kifungu hicho cha Sheria ya Mwenendo wa Janai, hivyo naiomba mahakama iliangalie na hilo wakati ikisikiliza kesi hii ya Kikatiba niliyofungua”.alidai Liyumba.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Septemba 15,2009

MAFISADI WANAOMWAGA FEDHA MAJIMBONI WATAJWE

Na Happiness Katabazi

NITAKUWA ni mchawi ambaye ninakula nyama za watu kama ningeshindwa kuandika makala ya kuwapongeza baadhi ya wabuge wa ccm ambao wameendelea kuonyesha ushujaa mbele ya umma kwakupinga wanachoma wenzao ambao wanatuhuma za ufisadi.

Wabuge CCM waliojipambanua kupiga ufisadi ulioota mizizi kwa baadhi ya wanachama wenzao ni Spika wa bunge, Samuel ,Sitta,Dk.Harrison Mkwakyembe(Kyela),Christopher Sendeka(simanjiro),Fred mpendazoe(kishapu),Beatrice Shelukindo(Kilindi),Lucas selelii,John Shibuda(Maswa),James Lembei na mjumbe wa NEC, Nape Nnauye.

Makamanda hao wameka wazi msimamo wao kwamba bila kujificha wataendelea kupambanana ufisadi kwa sababu ni kikwazo cha maendeleo la taifa letu.

Nimelazimika kuandika makala hii kwasababu mimi nimiongoni mwa wananchi ambao tumekuwa tukikemea ufisadi unonywa na baadhi ya wananchi wenzetu walioshika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM na serikalini,lakini wakati tukikemea uovu huo kwa njia mbalimbali baadhi ya viongoi wa chama tawala walitupinga moja kwa moja.

Hivyo leo hii tunaposhuhudia wabunge wa CCM wakisimama majukwaani na kukiri kwamba ndani ya chama chao kweli kuna manyang’au napata faraja sana na kuanza kuamini lile somo letu la kupinga ufisadi wa mali za umma limenza kueleka hata kwa wabunge wa ccm.

Hivi karibuni makamanda hao wa ccm wameukuliwa wakisema kuna mafisadi wamemwaga fedha kwenye majimbo yao ili waangushwe kwenye uchaguzi ujao, binafsi nawataka makambana hao wawataje kwa majina hao mafisadi hao kwasababu wasipofanya hivyo wakae wakijua watakuwa wakiwajengea nguvu mafisadi ambazo hivi sasa hawana.

Kwasababu vyama vya upinzani walikwisha wakata miguu mafisadi kwahiyo makamanda hao wasitake kuwavalisha miguu ya bandia mafisadi.

Binafsi nilikuwa miongoni mwa wananchi tulioudhuria mkutano wa kihistoria ulioandiliwa na vyama vya upinzani pale uwanja wa mwembeyanga temeke mwaka juzi,ambapo Dk.Willbroad Slaa alianika orodha mafisadi na wala hakuficha jina la watuhumiwa hapo ambao miongoni mwa aliyowataja hivi sasa wameishaburuzwa mahakamani.

Kwahiyo kama wakina Dk.Mwakyembe wameamua kwa dhati kujiunga katika vita ya ufisadi ,basi waingie kwa gia ile ile vyama vya upinzani kwa kuwataja kwa majina hao mafisadi wanaotapanya fedha kwa malengo ya kuwang’oa wao ili wawekwe wagombea watakaokidhi matakwa ya mafisadi ili tuwajue na siwachague.

Ninachokiona kinachofanywa na wakina Mwakyembe ni kizuri kwasababu hapo nyuma tulisema ccm inanuka ufisadi,inakabiliwa na makundi,wanachama hawapiki chungu kimoja lakini Katibu Mkuu wa chama hicho,Yusuf Makamba alipinga wazi wazi,sasa leo hii wabunge wachama chake na mwenyekiti wa chama hicho rais Jakaya Kikwete wiki hii amekiri hayo na akaeleza wazi matatizo hayo yamebua chuki mbaya miongoni mwa wanachama hadi kufikia hatua ya kuhofiaa kutiliana sumu kwenye vinywaji.

Ipo haja ya kuwapa moyo wabunge hao wa ccm lakini wapinzani walivyoeleza ufisadi na kusem ccm ni chama cha mafisadi ,walieleza kwamba ufisadi upo ndani ya Itikadi na sera za chama hicho.Kwa hiyo wabunge hata mwenyekiti wao wakiamua kupambana na hilo wabadilishe Itikadi na sera za chama chao na kama hawawezi watoke huko wakajiuge na vyama vya upinzani ama waanzishe chama chao kwasababu huko siyo kwao.

Mimi ninachokiona kwa makanda hao,ile nyumba ya ccm siyo yao,watoke huko na kama hawataki kutoka ama watauwawa ama nao mwisho wa siku nao watageuka kuwa mafisadi na hili ni rais kufanyika kwani kila mmoja wao atatupiwa mfupa atafune.

Na ndicho ambacho tunaweza kusema walichokubaliana kwenye kikao cha Halmashauri kuu(NEC)hivi karibuni wakaunda kamati itakayosimamiwa na rais mstaafu Ally Hassan Mwinyi,Spika wa Bunge la Afrika mashariki mstaafu,Abdullahman Kinana na Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Pius Msekwa,ni kamati ya kuwatafutia mifupa wabunge ‘vizabizabina’ili wapoe.

Kama rais kikwete amekiri kuwepo kwa chuki miongoni mwa wanachama wake na baadhi ya wanachama wake wakabilia na tuhuma za ufisadi na mambo hayo yameibua chuki kali anaunda kamati hiyo ya nini?

Nikweli kampeni zisizo rasmi zimeanza kuelekea uchaguzi mkuu wa mwakani, hilo aitushangazi hivyo hoja kama makamanda hao wanajitautia umaarufu kwenye majimbo yao na jamii na kwamba vita wanayopigana ni yakutaka kupigania majimbo yao ni ya kweli tupu.

Hivyo hatuwezi kuwalaumu wabunge hao kwamba wanajitafutia umaarufu ,hapana kwani kila mwasiasa anataka umaarufu.Kahiyo hoja ya kwamba makamanda hao wanajitafutia umaarufu haina msingi kwani hata viongozi wa vyama vya upinzani nao pia wanataka umaarufu.

Wanasema siku za mwizi ni arobaini ,kwani ni ccm hii iliwakejeli wapinzani kuwa inawapakazia sifa mbaya na kwamba chama hicho hakina mafisadi lakini leo hii wabunge wa ccm wanasema wapishana majukwaani kuthibitisha madai ya wapinzani kwamba ndani ya chama hicho kuna mafisadi.

Kwahiyo hata hizo kesi zilizofunguliwa mahakama za ufisadi wa fedha za umma na kesi tatu kubwa zinazotorajiwa kufunguliwa wakati wowote,zote ziliibuliwa na wapinzani kwahiyo ccm kamwe hawana la kutambia hapo kwani huwezi ukafanya ufisadi badala ya kuumbuliwa,tuisifu kwasababu imekiri uwepo w ufisdi.

Kwahiyo ccm aina hoja juu ya vita ya ufisadi kwakuwa kila wakalofanya kuhusu ufisadi wakae wakitambua waanzilishi wa vita hiyo ni vyama vya upinzani na makundi mengine ya kijamii vikiwemo vyombo vya habari.

Ikumbukwe tunaelekea uchaguzi mkuu mwakani,ccm wasijaribu kujitapatia sifa kupiti kupinga vita ufisadi.

Mungu ibariki Tanzania,mungu Ibariki afrika

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Septemba 13, 2009
0716 774494

MAHITA AUMBUKA

*Mahakama yasema mtoto aliyemkana ni wake
*Yaamuru atoe 100,000/- za matunzo kila mwezi

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, imemwamuru aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Omar Mahita kulipa malimbikizo ya gharama za matunzo ya kumhudumia mtoto Juma Omar Mahita (12) baada ya mahakama hiyo kujiridhisha kuwa mtoto huyo ni wake.


Hukumu hiyo ilitolewa jana majira ya saa mbili asubuhi na Hakimu Suzan Kihawa katika mahakama ya siri (chamber), ambapo siku zote wanaoruhusiwa kuudhuria kesi hiyo ni mlalamikaji, Rehema Shabani na wakili wake toka Kituo cha Haki za Binadamu, Fredrick Mkatambo na wakili wa mdaiwa, Charles Semgalawa na mdaiwa Omar Mahita kutokana na mazingira ya kesi hiyo kumhusisha mtoto.

Kwa mujibu wa Mwanasheria wa Kituo cha Haki za Binadamu cha Kinondoni, Mkilya Daudi, muda mfupi baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mahakama hiyo imeutazama ushahidi wa mazingira na maneno, uliotolewa na mlalamikaji na ushahidi uliotolewa na Mahita na kuridhika kuwa mtoto huyo ni wa mkuu huyo wa zamani wa Jeshi la Polisi.

Katika ushahidi wake, mlalamikaji Rehema ambaye ni mama wa mtoto Juma, aliithibitishia mahakama kuwa, alianza uhusiano wa kimapenzi na Mahita mwaka 1996 mjini Moshi akiwa mfanyakazi wa ndani katika nyumba yake wakati huo akiwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa ushahidi wa Rehema, wakati wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi na IGP huyo mstaafu, alipata ujauzito na mwaka 1997 alijifungua mtoto ambaye Mahita alimkana kwa madai kuwa si wake na hajapata kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mlalamikaji.

Rehema katika ushahidi wake, alidai kuwa wakati akiwa na ujauzito, Mahita alikuwa akimhudumia kwa kumpa sh 40,000 kila mwezi na siku chache baadaye alimpatia nauli ili aende nyumbani kwao Kondoa kwa ajili ya kujifungua.

Alidai kuwa, tangu aliporejea nyumbani kwao Kondoa kwa ajili ya kujifungua, Mahita alisitisha kutoa gharama za matunzo, hali iliyosababisha mama huyo kuishi katika mazingira magumu na hatimaye kuanza kutafuta haki yake kwenye vyombo vya sheria.

“Hakimu Kihawa ameridhika kwamba Juma Omar Mahita ni mtoto wa nje ya ndoa wa Omar Mahita na mahakama imemtaka mdaiwa kwa sababu tangu mtoto huyo azaliwe alikuwa anaishi na mama yake, ataendelea kuishi na mama yake ambaye awali alikuwa mfanyakazi wa ndani wa mdaiwa,” alisema Daudi.

Alisema pia mahakama imemwamuru Mahita amlipe sh 100,000 kila mwezi kama gharama za matunzo ya mtoto huyo, kulipa malimbikizo ya gharama za matunzo toka mwaka 2003 hadi sasa kwa kiwango cha sh 100,000, na alipie gharama za masomo ya mtoto huyo hadi atakapoanza kujitegemea.

“Pia mahakama imeona kwamba mlalamikaji hajawahi kulipa gharama za uendeshaji wa kesi hiyo, hivyo imetoa amri kwamba asilipe gharama za kesi na kumtaka Mahita kukata rufaa katika mahakama za juu kama ataona inafaa,” alisema Daudi ambaye aliwaonyesha waandishi wa habari amri hizo zilizotolewa na mahakama hiyo.

Baada ya kumaliza kuzungumzia hukumu hiyo, mwanasheria huyo wa kituo cha haki za binadamu, aliwaeleza waandishi kwamba Februari 26 mwaka 2007, Rehema alikwenda kituoni kwao kuomba msaada wa kisheria, akidai kuwa mzazi mwenzake Mahita, amemtelekeza mtoto wake na amekataa kutoa gharama za matunzo ya mtoto.

“Baada ya kupokea malalamiko hayo, tulifikia uamuzi wa kupeleka suala hilo mahakamani, lakini kabla ya Rehema kufika katika kituo chetu Agosti 10 mwaka 2006, alishapeleka lalamiko lake kwenye ofisi za Ustawi wa Jamii na hata maofisa wa Ustawi wa Jamii walivyojitahidi kumwita Mahita, alikataa kuitikia wito huo, na ndiyo ofisi hiyo ilipoamua kuiandikia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikiiarifu mahakama hiyo isuluhishe.

“Lakini sisi kituo chetu tuliona Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya aina hiyo ya madai ya matunzo ya mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa kutokana na Sheria ya Watoto waliozaliwa nje ya Ndoa Na. 278 ya 1949, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

“Februari 26 mwaka 2007, kituo chetu kilimsaidia mama huyo kwa kupeleka kesi Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni na Mahita akaweka wakili wake na wakati kesi ikiendelea, mdaiwa alitaka kesi hiyo ifutwe kwa sababu imefunguliwa nje ya muda na mahakama ikatupilia mbali ombi hilo na badala yake mahakama hiyo Aprili 24 mwaka huu, ilitoa amri mlalamikaji na mdaiwa na mtoto, wakapime kipimo cha DNA na gharama za kipimo hicho zitolewe na pande zote mbili,” alisema Daudi.

Alisema jumla ya sh 300,000 zilitakiwa kwa ajili ya kufanyia kipimo hicho, lakini Mahita alikaidi amri hiyo ya mahakama ya kuchangia sh 100,000, ndipo kituo hicho kikaamua kubeba jukumu hilo kwa kutoa fedha taslimu sh 300,000 ili watu wote watatu wakapime kipimo hicho, lakini pia Mahita aligoma tena kwenda kufanyiwa kipimo hicho.

Daudi alisema baada ya Mahita kugoma kwenda kupima kipimo hicho, mahakama hiyo iliendelea kusikiliza kesi hiyo na kupokea ushahidi wa pande zote mbili hadi jana ilipotoa hukumu.

Akizungumzia jinsi kituo chake kilivyopokea hukumu hiyo, alisema kesi hiyo imeangukia katika utekelezwaji wa sheria mbovu ya Sheria ya Watoto Wanaozaliwa Nje ya Ndoa ya 1949, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 ambayo inasema mtoto wa nje ya ndoa, baba atapaswa atoe sh 100 kwa mwezi kwa ajili ya matunzo.

“Sisi tunatumia mahakama zetu kuanza kutamka kiasi cha sh 100 hakitoshi kulingana na mazingira ya sasa, kwa hiyo kiasi hicho cha sh 100,000 kilichotamkwa na mahakama hiyo jana, ni kiasi kikubwa na angalau kinaendana na gharama za maisha ya sasa.

“Hivyo tunaamini hukumu ya kesi hii italeta mabadiliko ya kitabia kwa wanaume wenye tabia kama Mahita, za kuwapachika mimba wanawake nje ya ndoa zao na kisha kuwatelekeza, na pia kituo hiki kinatoa pongezi kwa mlalamikaji Rehema, kwani ni mwanamke jasiri ambaye ameweza kutetea haki yake bila woga kwani hasingekuwa jasiri, hivi sasa mtoto wake Juma hasingekuwa na baba na angekosa haki zake za msingi kama mtoto, na tunawahamasisha wanawake wasio na uwezo wanaohitaji msaada wa kisheria, wajitokeze kwenye vituo vyetu, tuwapatie msaada wa kisheria,” alisema.

Chanzo:Gazeti la Tanzania la Ijumaam,Septemba 11,2009

JAJI KATEKA AULA

Na Happiness Katabazi

JAJI wa Mahakama ya Kimataifa ya Sheria ya Bahari (ITLOS) yenye makao yake nchini Ujerumani, James Kateka, ambaye ni Mtanzania pekee katika mahakama hiyo, amechaguliwa kuwa mjumbe wa Taasisi ya Wanasheria wa Kimataifa.

Taarifa iliyowekwa kwenye tovuti ya taasisi hiyo inaeleza Jaji Kateka anakuwa mjumbe wa kwanza kutoka nchi za Afrika Mashariki kuchaguliwa kujiunga na taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 1873 nchini Ubeligiji.

Taarifa hiyo ambayo imethibitishwa na Jaji Kateka, ilisema wajumbe wengine katika taasisi hiyo ni pamoja na majaji wa mahakama za kimataifa, maprofesa wa vyuo maarufu duniani na wakuu wa vyombo vya utafiti wa sheria za kimataifa.

Aidha, ilisema Waafrika wengine waliochaguliwa kuwa wajumbe ni pamoja na Jaji Abdul Koroma wa Mahakama ya Dunia kutoka Sierra Leone, Jaji Thomas Mensah kutoka Ghana ambaye alikuwa Rais wa kwanza wa ITLOS, Jaji Abdi Yusuf wa Mahakama ya Dunia kutoka Somalia na Profesa John Dugard kutoka Afrika Kusini.

“Jaji Kateka alichaguliwa katika raundi ya kwanza kwa kupata kura nyingi kuliko wajumbe wote waliochaguliwa, katika kikao kilichofanyika Naples, nchini Italia. Walikuwapo wagombea 28 na waliochaguliwa ni 11. Baadhi ya walioshindwa katika uchaguzi huu ni pamoja na Jaji wa Mahakama ya Dunia,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo inasema wajumbe wengine waliochaguliwa katika taasisi hiyo ni pamoja na majaji wa mahakama za kimataifa, maprofesa wa vyuo maarufu duniani na wakuu wa vyombo vya utafiti wa sheria za kimataifa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima, Septemba 11, 2009

WIZI WA NMB TEMEKE

Watuhumiwa wengine sita wakamatwa

*Wakutwa na SMG moja, bastola mbili na risasi 52
*Yumo mwanajeshi mstaafu raia wa nchini Burundi
*Wawili wafikishwa kortini wakiwa hoi kwa kipigo

Na Happiness Katabazi

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia watuhumiwa wengine sita, akiwemo raia wa Burundi, wakiwa na silaha tatu, zinazodaiwa kutumika katika tukio la ujambazi, lililotokea katika Benki ya Microfinance (NMB), tawi la Temeke, Julai 31, mwaka huu.
Kati ya watuhumiwa sita waliokamatwa hivi karibuni, wawili kati yao, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana, wakikabiliwa na tuhuma za wizi wa zaidi ya sh milioni 60 na kusababisha vifo vya askari wawili waliokuwa lindoni siku ya tukio.

Kukamatwa kwa watuhumiwa hao, kunafanya idadi ya waliokwishakamatwa kuhusina na tukio hilo la ujambazi wa kutumia silaha nzito za kivita lililotikisa nchi, kufikia 17.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema watuhuniwa hao walikamatwa katika maeneo tofauti, ikiwemo jijini Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Pwani.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Richard Muhonza (29), raia wa Burundi aliyewahi kuwa mwanajeshi wa nchi hiyo, Willibert Ugini (22), mkazi wa Arusha, Selemani Nzowa (33), na Halima Mvungi (49), wote wakazi wa jijini Dar es Salaam. Wengine wawili majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi.

“Msako huu ni mkali na wa aina yake, ambao unaendelea nchi nzima ili kuwabaini wote waliohusika kwa njia moja au nyingine katika ujambazi uliofanyika NMB Temeke,” alisema Kamanda Kova.

Aidha, alizitaja silaha zilizokamatwa kuwa ni SMG namba AB 2763836, ikiwa na risasi 40, magazini moja yenye risasi 30 na nyingine risasi 10, bastola mbili, moja ikiwa imetengenezwa China, yenye namba 073095 na risasi mbili na nyingine ni aina ya Maknov, iliyokuwa na risasi sita kwenye magazini na risasi nyingine 10 zilizokutwa kwenye paketi ya sigara iliyofichwa kwenye soksi.

“Majambazi wote wamekamatwa katika operesheni ya pamoja iliyofanyika kwa ushirikiano wa askari wa Mkoa wa Pwani, vikosi maalum vya kudhibiti uhalifu, wananchi na Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam,” alisema Kova.

Tayari watuhumiwa wawili kati ya sita waliotangazwa jana, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuungana na wenzao wanane, kujibu mashitaka yanayowakabili.

Mbele ya Hakimu Mkazi Binge Mashabala, Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Richard Lucas Mahuza maarufu Leonard ambaye ni raia Burundi na Selemani Omar Nzowa.

Kimaro alidai washitakiwa wote wanakabiliwa na makosa mawili ya mauaji ambapo kwa pamoja na wenzao wanane waliofikishwa mahakamani hapo hivi karibuni, wanadaiwa kuwa Julai 31, mwaka huu, katika benki ya NMB, tawi laa Temeke, walimuua Seif Abdallah.
Katika shitaka la pili, Kimaro alidai kuwa mnamo tarehe na muda kama huo, washitakiwa hao na wengine ambao walishafikishwa mahakamani hapo hivi karibuni, katika tawi la NMB Temeke, walimuua askari polisi mwenye namba E329, Koplo Joseph.

Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu kwani mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji.

Hata hivyo, watuhumiwa hao waliingia mahakamani hapo wakiwa hoi kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kipigo, kwani walishindwa kutembea na kulazimika kutembea kwa msaada wa askari polisi.

Hata walipoingizwa ndani ya mahakama hiyo, watuhumiwa hao walishindwa kukaa na kulazimika kulala kwenye viti.

Walipopandishwa kizimbani na kuanza kusomewa mashitaka, watuhumiwa hao walimwomba hakimu awape kibali cha kwenda kutibiwa kwa madai kuwa wana maumivu makali mwilini, yaliyotokana na kipigo walichokipata.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi keshokutwa na hakimu aliagiza washitakiwa wakapatiwe matibabu wakiwa gerezani.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Septemba 8,2009

WIZI WA NMB TEMEKE

Watuhumiwa wengine sita wakamatwa

*Wakutwa na SMG moja, bastola mbili na risasi 52
*Yumo mwanajeshi mstaafu raia wa nchini Burundi
*Wawili wafikishwa kortini wakiwa hoi kwa kipigo

Na Happiness Katabazi

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia watuhumiwa wengine sita, akiwemo raia wa Burundi, wakiwa na silaha tatu, zinazodaiwa kutumika katika tukio la ujambazi, lililotokea katika Benki ya Microfinance (NMB), tawi la Temeke, Julai 31, mwaka huu.
Kati ya watuhumiwa sita waliokamatwa hivi karibuni, wawili kati yao, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana, wakikabiliwa na tuhuma za wizi wa zaidi ya sh milioni 60 na kusababisha vifo vya askari wawili waliokuwa lindoni siku ya tukio.

Kukamatwa kwa watuhumiwa hao, kunafanya idadi ya waliokwishakamatwa kuhusina na tukio hilo la ujambazi wa kutumia silaha nzito za kivita lililotikisa nchi, kufikia 17.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema watuhuniwa hao walikamatwa katika maeneo tofauti, ikiwemo jijini Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Pwani.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Richard Muhonza (29), raia wa Burundi aliyewahi kuwa mwanajeshi wa nchi hiyo, Willibert Ugini (22), mkazi wa Arusha, Selemani Nzowa (33), na Halima Mvungi (49), wote wakazi wa jijini Dar es Salaam. Wengine wawili majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi.

“Msako huu ni mkali na wa aina yake, ambao unaendelea nchi nzima ili kuwabaini wote waliohusika kwa njia moja au nyingine katika ujambazi uliofanyika NMB Temeke,” alisema Kamanda Kova.

Aidha, alizitaja silaha zilizokamatwa kuwa ni SMG namba AB 2763836, ikiwa na risasi 40, magazini moja yenye risasi 30 na nyingine risasi 10, bastola mbili, moja ikiwa imetengenezwa China, yenye namba 073095 na risasi mbili na nyingine ni aina ya Maknov, iliyokuwa na risasi sita kwenye magazini na risasi nyingine 10 zilizokutwa kwenye paketi ya sigara iliyofichwa kwenye soksi.

“Majambazi wote wamekamatwa katika operesheni ya pamoja iliyofanyika kwa ushirikiano wa askari wa Mkoa wa Pwani, vikosi maalum vya kudhibiti uhalifu, wananchi na Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam,” alisema Kova.

Tayari watuhumiwa wawili kati ya sita waliotangazwa jana, walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuungana na wenzao wanane, kujibu mashitaka yanayowakabili.

Mbele ya Hakimu Mkazi Binge Mashabala, Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Richard Lucas Mahuza maarufu Leonard ambaye ni raia Burundi na Selemani Omar Nzowa.

Kimaro alidai washitakiwa wote wanakabiliwa na makosa mawili ya mauaji ambapo kwa pamoja na wenzao wanane waliofikishwa mahakamani hapo hivi karibuni, wanadaiwa kuwa Julai 31, mwaka huu, katika benki ya NMB, tawi laa Temeke, walimuua Seif Abdallah.
Katika shitaka la pili, Kimaro alidai kuwa mnamo tarehe na muda kama huo, washitakiwa hao na wengine ambao walishafikishwa mahakamani hapo hivi karibuni, katika tawi la NMB Temeke, walimuua askari polisi mwenye namba E329, Koplo Joseph.

Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu kwani mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji.

Hata hivyo, watuhumiwa hao waliingia mahakamani hapo wakiwa hoi kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kipigo, kwani walishindwa kutembea na kulazimika kutembea kwa msaada wa askari polisi.

Hata walipoingizwa ndani ya mahakama hiyo, watuhumiwa hao walishindwa kukaa na kulazimika kulala kwenye viti.

Walipopandishwa kizimbani na kuanza kusomewa mashitaka, watuhumiwa hao walimwomba hakimu awape kibali cha kwenda kutibiwa kwa madai kuwa wana maumivu makali mwilini, yaliyotokana na kipigo walichokipata.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi keshokutwa na hakimu aliagiza washitakiwa wakapatiwe matibabu wakiwa gerezani.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Septemba 8,2009

'HAPPY BIRTHDAY' JWTZ

Na Happiness Katabazi

‘HAPPY birthday to you, happy birthday to you.
‘Happy birthday Tanzania People’s Defence Forces (TPDF), happy birthday to you’.


Naamini Watanzania wote tunakumbuka Septemba mosi mwaka huu, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilitimiza miaka 45 baada ya kuundwa mwaka 1964, baada ya kuchukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na jeshi la kikoloni la King’s African Rifles (KAR) lililovunjwa baada ya machafuko ya Januari 1964.

Tarehe hiyo wakati jeshi letu lilikuwa likitimiza miaka hiyo, pia ndiyo ilikuwa ni siku ya hitimisho la maadhimisho yaliyoanza takriban wiki moja iliyopita katika viwanja vya Jeshi la Anga, Ukonga Dar es Salaam.

JWTZ ilihitimisha kwa kuweka wazi silaha zake mbalimbali za kivita pamoja na kuonyesha mbinu na shughuli zinazofanywa na jeshi hilo ambalo katika kipindi hicho , nadiriki kusema pasipo shaka kwamba jeshi letu limepata mafanikio makubwa.

Wakati jeshi letu linatimiza umri huo, wanajeshi wamefanya mengi licha ya kushiriki kwenye ukombozi wa nchi nyingi za kusini mwa Afrika ili kuhakikisha zinakuwa huru kama ilivyo kwa Tanzania,JWTZ, imekuwa ni tanuri la kuyapika baadhi ya majeshi mengine ya nchi za Afrika.

Wananchi wenzangu waliopata fursa ya kutembelea maonyesho hayo watakubaliana nami kwamba jeshi letu sasa limekubali kubadilika na sasa limeanza kufanya kazi kisayansi na kiteknolojia na kwamba limekataa kuendelea kufanya kazi zake gizani na wasiwasi mithili ya mtu anayeoga barazani.

Kwa moyo mkunjufu napenda kutoa pongezi kwa wafanyakazi wote wa JWTZ na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kwanza kwa kutimiza umri huo, pili, kwa uamuzi wao kukataa kuendelea kuficha dhana zetu za kivita ambazo zimenunuliwa kwa kodi ya wananchi, kwani umri huo ni mkubwa ukilinganisha.

Sote ni mashahidi kila kukicha tumekuwa tukisia au kuona majeshi ya nchi nyingine za Afrika yamekosa mshikamano wake kweli na hivyo kufikia uamuzi wa baadhi ya wanajeshi wake kuasi na kuanzisha vikundi vyao haramu vinavyokuwa na maskani misituni na lengo la vikundi hivyo vya waasi limekuwa ni kupambana na jeshi linaloshika hatamu.

Huwa vimedhamiria kupindua serikali kisha watwae madaraka, jambo limeleta machafuko katika nchini nyingi lakini kwa kuwa Mungu bado anaipenda nchi yetu, JWTZ bado haijafikia hatua hiyo kwani wanajeshi wake wana mshikamano wa dhati kweli kweli.

Mapema wiki iliyopita niliposikia JWTZ imeanika silaha zake katika maonyesho hayo, iliniwia vigumu kuamini taarifa hizo.

Kwa sababu tangu nianze kufuatilia shughuli zinazofanywa na jeshi letu na binafsi nimezaliwa na kulelewa katika kambi ya jeshi, sikuwahi kusikia jeshi letu likithubutu kufanya maonyesho ya namna hii hadharani.

Kwa wale tunaopenda kutembelea vikosi, makambi ya JWTZ tumekuwa tukiona zana mbalimbali zikiwamo maghala ya silaha, ndege za kivita n.k, lakini pindi umuulizapo mwanajeshi hata kama ni rafiki yako kwamba ile ni silaha aina gani au komandoo naye anafamilia? Mwanajeshi ataishia kukujibu kwa mkato “fuata kilicho kuleta, hizo ni siri za jeshi hutakiwi kujua, umekuja kutupeleleza na utaruka kichurachura sasa hivi.”

Si siri majibu ya aina hiyo ambayo nilianza kuyapata tangu nikiwa mtoto hadi leo hii, ndiyo yalifanya wiki iliyopita niwe mgumu kukubali kwamba JWTZ imeanika silaha zake na wananchi wakajitokeza kwa wingi kushuhudia na wakapewa fursa ya kuuliza maswali na kujibiwa na wanajeshi wetu. Kweli Mungu mkubwa.

Wakati nikitoa pongezi kwa maadhimisho hayo, nitoe angalizo kwa jeshi letu kwamba bado wananchi wana imani nalo licha ya kuwapo kwa baadhi ya vitendo vya utovu wa nidhamu unaofanywa na baadhi ya askari wa chache, hivyo ambayo wakati mwingine vitendo hivyo vinalipaka matope jeshi.

Hata hivyo, hivi sasa jeshi letu limekuwa likitoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi pindi wanapokamatwa wanajeshi kwenye matukio ya ujambazi na hatimaye wanafikishwa mahakamani.

Naunga mkono ombi la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, katika maadhimisho hayo la kutaka raia wawe na uhusiano mwema na jeshi hilo. Lakini napenda kutoa angalizo kwamba uhusiano mwema kati ya pande hizo mbili uwe na mipaka na masilahi ya kwa nchi.

Uhusiano mwema huo usiwe ni ule wa baadhi ya wanajeshi wetu kutumia mafunzo ya kivita waliyoyapata kwenye vyuo vyao vya kijeshi, wakaanza kutoa mafunzo hayo kinyemela kwa baadhi ya wananchi watukutu ili mwisho wa siku waunde magenge ya kihalifu kwa maana ya mwanajeshi anatoa mafunzo kwa raia, silaha na kumcholea michoro ya kwenda kufanya ujambazi.

Naweza kusema kilichofanywa na JWTZ sasa, kinataka kulandana na kinachoendelea kufanywa na Jeshi la Polisi chini ya Inspekta Jenerali Said Mwema, kwani tangu kamanda huyo ateuliwe kushika wadhifa huo kwa kushirikiana na askari wake wameweza kuanzisha mfumo mpya wa ‘Ulinzi Shirikishi’ na kwa hakika mfumo huo nadiriki kusema umeleta mafanikio ya kiutendaji katika jeshi hilo, kwakuwa wananchi ndio wanaoishi na wahalifu mitaani na maofisini.

Ni kazi ya Jeshi la Polisi kupitia makachero wake na kikosi chake cha kupambana na ujambazi ‘scopion’ ndiyo kinatakiwa kuwasaka majambazi, lakini Jeshi la Polisi kwa kutambua kwamba bila kushikirikisha raia haliwezi kufanikiwa, wakaamua kushirikisha raia na kweli leo hii tunalisikia Jeshi la Polisi likijitokeza hadharani kupongeza raia kwa kuwapa ushirikiano.

Lakini nimng’ate sikio Jenerali Mwamunyange, kwamba licha ya yeye kutoa wito kuendelezwa kwa mahusiano mema kwa raia vijana wake, namtaka aigeukie Kurugenzi ya Habari ya jeshi hilo, kwani baadhi ya waandishi wa habari nikiwemo mimi, tumekuwa tukiwasilisha maombi kwa njia ya maandishi katika kurugenzi hiyo ya kuomba turuhusiwe kufanya mahojiano na baadhi ya viongozi ukiwamo wewe, lakini katika hali ya kushangaza, kurugenzi yako imekuwa ikishindwa kutupatia majibu kwamba kiongozi tunayetaka kumhoji masuala mbalimbali yahusuyo jeshi ambayo yakijibiwa yatakuwa yanaelimisha taifa, tumekuwa hatujibiwi chochote.

Kitendo hiki kimekuwa kikitukera kwani waandishi wa jeshi pindi wanapokuja kwenye vyombo vya habari vya uraiani huwa wanapewa ushirikiano wa kutosha.

Na baadhi ya vijana wako ambao nimekuwa nikiwadadisi kuhusu hali hiyo kila mmoja wao kwa nafasi yake wamekuwa wakinijibu kwamba Kurugenzi ya Habari ya jeshi haipo huru hivyo na wao imekuwa ikiwawia vigumu kuwasilisha maombi yetu kwa maafande wao.

Ni rai yangu kwa Jenerali Mwamunyange na makamanda wako mlitazame hili, kwa mtazamo mpana, kwani wananchi wanahitaji kupata taarifa za jeshi lao ambapo taarifa hizo jeshi litahakikisha linatoa taarifa ambazo hazimnufaishi adui wa taifa letu.

Hii aipendezi na kwa namna nyingine hali hiyo ni aina fulani ya kukandamiza uhuru wa wananchi kupata habari za jeshi letu.

Watanzania hawawezi kuamini, kwa wiki moja sasa gazeti hili limeanza kuandika makala za habari za maadhimisho ya JWTZ, wananchi mbalimbali waliokuwa wakizisoma makala hizo wamekuwa wakipiga simu katika chumba chetu cha habari wakisema makala hizo zimewafunza mengi na wengine wakadiriki kuuliza taratibu za kujiunga na jeshi ni zipi lakini tukawaelewesha nafasi za jeshi huwa zinatangazwa kwenye vyombo vya habari.

Sasa kwa hali hiyo, tunaona kwamba kuna wananchi wanaopenda kupata taarifa mbalimbali za jeshi letu, wengine wanapenda kujiunga na jeshi hilo, kutembelea makumbusho ya jeshi lakini kwa sababu ya jeshi hili ama kwa kushindwa kuwa karibu na wananchi ama kwa kuandaa vipindi maalumu katika televisheni au redio au kuweka taarifa mpya mara kwa mara katika tovuti ya jeshi hilo ambalo lilizinduliwa na Luteni Jenerali Abdulahman Shimbo, pale Upanga Mess, ambapo nami nilikuwa miongoni mwa waandishi wa habari tuliohudhuria uzinduzi wa tovuti hiyo, kama wanavyofanya Jeshi la Polisi hivi sasa ndiyo kuna sababisha wananchi wengi kubaki gizani kuhusu utendaji wa jeshi letu.

Lakini cha kushangaza kama si cha kustaajabisha, licha ya JWTZ kuwa na wasomi wa taaluma ya teknolojia ya habari lakini tovuti ya jeshi hilo imekuwa haina vitu vingi, ama kuweka taarifa mpya mara kwa mara.

Natoa rai kwa Jeshi la Magereza nalo liige mfano huo ulioonyeshwa na majeshi mengine ili wananchi wafahamu majukumu yao kwani wananchi wengi wanaelewa jukumu lao ni kutunza mahabusu na wafungwa.Happy Birthday JWTZ.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Septemba 6, 2009

MAWAKILI WAMBANA SHAHIDI WA EPA

Na Happiness Katabazi
SHAHIDI wa pili katika kesi ya wizi wa sh milioni 207 fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), inayomkabili Rajab Maranda na wenzake wanne, Emmauel Boaz, ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwamba alikuwa ni miongoni mwa waliousika kutoa maelekezo ya kampuni ya Rashaz inayodaiwa kuiba fedha Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilipwe fedha hizo.


Boaz ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Fedha za Kigeni(BoT) aliyasema hayo jana wakati alipobanwa na maswali kwa nyakati tofauti na jopo la mawakili wa utetezi Majura Magafu, Mpare Mpoki, Mabere Marando na Ademba Agomba kwani jana ilikuwa ni upande wa utetezi kumhoji shahidi huyo,mbele ya jopo la mahakimu wakazi Ignas Kitusi, John Utamwa na Eva Nkya.

Yafuatayo ni mahojioano kati ya mawakili hao na shahidi huyo kwa nyakati tofauti:
Swali:Pale Benki Kuu nani alikuwa anakaa na data base ya madeni?
Jibu:Sijui.
Swali:Kwa wewe ujui kama deni hilo lilikuwepo au la?
Jibu:Sijui.
Swali:Sasa ni kwanini ulikuwa miongoni mwa viongozi wa BoT mlioidhinisha malipo kwa kampuni hiyo wakati hata kuona data base?
Jibu:Mimi niliegemea katika idhini ya Gavana Daud Balali ambaye ndiye aliyeidhinisha kampuni hiyo iliopwe.
Swali:Wewe , Peter Noni, Isangya ,na Mkurugenzi wa uchumi na sera Benki Kuu, Kilato,kabla ya kesi za EPA kufunguliwa mliohijiwa je mlitoa maelezo kama haya unayotoa leo mahakamani ?
Jibu:Ndiyo.
Swali:Boaz kwa cheo chako hukuwai kupata nafasi kuwa na data base ya malipo ya EPA?
Jibu:Ndiyo sijawahi kupata nafasi ya kuiona.
Swali:Wewe ni mtaalamu wa masuala ya fedha kwa taaluma yako hiyo ,huwezi kuizinisha malipo bila kuwa na data base sasa ieleze mahakama ni kwanini uliidhinisha malipo bila ya kuona data base?
Jibu:Kimya.
Swali:Wewe ni msomi mwenye CPA na shahada mbili ni kwanini ulitoa maelekezo ya malipo na ukashindwa kumshauri kitaalamu gavana asilipe deni hilo?
Jibu:Naweza kumshauri Gavana siyo kumkataza.
Swali:Wewe ,Peter Noni ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Benki ya TIB , Isanga mliohojiwa lakini hamjashitakiwa,ni kweli?
Jibu:Kimya.
Swali:Shahidi pamoja na usomi wako huo ,kabla ya kuelekeza deni lilipwe ulishindwa kubaini kasoro za kimaandishi katika fomu za maombi ya kulipwa deni?
Jibu:Sikuona.
Swali:Uliwahi kuona deed of assignment(hati ya kuamisha deni)?
Jibu:Sikuwahi kuona.
Swali:Ebu iambie mahakama hiyo shahada yako ya pili ulimaliza lini maana sikuelewi ?
Jibu:2005
Swali:Wewe na mshitakiwa wa nne(Esta Komu)wote ni kaimu wakurugenzi wa vitengo mkipewa maelekezo na Gavana mlikuwa mkiyapinga?
Jibu:Hapana,tuna tekeleza.
Swali;Sasa ni kwanini Komu, Mwakosya na Kimela ndiyo wameshitakiwa na siyo wewe na Peter Noni?
Jibu:Kimya.
Swali:Kwanini Gavana aliidhinisha deni la fedha za India milioni 8 zilipwe kwa dola za kimarekani milioni 1.2 wakati alikuwa akijua sh moja ya India ni sawa n ash 30 ya Tanzania na dola moja ya marekani ni sh 110 ya hapa nchini?
Jibu:Sijui.
Swali:Ieleze mahakama ni watu wangapi Benki Kuu walihusika kuidhinisha malipo hayo kwenda Rashaz (T)Ltd?
Jibu:Gavana.
Swali:Wengine ni wakinanani?
Jibu:Kimya.
Swali:Wewe ulihusika?
Jibu:Ndiyo.
Swali:mshitakiwa wa tano Bosco Kimela alihusika?
Jibu:Ndiyo.
Swali:Kaimu Mkurugenzi wa Fedha za Kigeni wakati huo(Peter Noni) alihusika?
Jibu:Ndiyo.
Swali:Yupo kizimbani?
Jibu:Hayupo kizimbani na wala hajashtakiwa.
Swali: Taja upesi mwingine nani alihusika?
Jibu:mshitakiwa wa tatu na wa nne Iman Mkwakosya, Ester Komu,Mkurugenzi wa Uchumi na Sera Issack Kilato na Gavana.
Swali:Kwa mujibu hilo jarada la maombi ya malipo, kuna utata wowote ulijitokeza kabla ya malipo kuidhinishwa?
Jibu:Sikuona tatizo la malipo hayo.
Swali:Nani alikuwa na mamlaka ya mwisho ya malipo yafanyike au yasifanyike?
Jibu:Gavana.
Swali:Na Gavana aliamua au alikuwa analidhika baada ya watu wote maofisa wake ukiwamo wewe ndiyo anaidhinisha malipo yafanyike kweli si kweli?
Jibu:Gavana, alikuwa anategemea ushahuri wa watalaam.
Swali:Wewe unavyojua kuna mtaalamu alimshauri vibaya katika hayo malipo?
Jibu:Siwezi kujua kwasababu lilikuwa linahusu idara nyingine.
Swali:Ni kwanini kabla ya nyie kuidhinisha malipo mlikuwa mkiitaji deed of asigment?
Jibu:Sijui.
Swali:Ni kitu gani kilikufanya uizinishe malipo ya Rashaz (T) Ltd bila kufuata taratibu hizo?
Jibu;Kimya.
Swali:Ulilidhika na maombi ya mwambaji kulipwa deni hilo, naomba ujibu swali hili kwani ni swali jepesi mno?
Jibu:Nililidhika baada ya mchakato wa kulipwa deni hilo kukamilika.
Swali:Wewe kama mtaalamu hata kama gavana angeizinisha na kuona malipo yanakasoro wewe ungekubali?
Jibu:Nisingekubali kuidhinisha.
Swali:Deed of assignment ya Rashaz T Ltd na Rashaz Tanzania ,sasa ni kwanini mlitoa malipo kwenye nyaraka hizo zenye dosari za kimaandishi na je wewe uliwai kubaini dosari hizo?
Jibu: Sijawai kubaini.
Swali:Utakubaliana na mimi watu wote mlioshughulikia malipo ya kampuni hiyo mlikuwa makini?
Jibu:Siwezi kujua wengine ila mimi nilikuwa makini.
Lifuatalo ni swali aliloulizwa shahidi na hakimu mkazi Ignus Kitusi:
Swali:Shahidi, ulikuwa na wajibu wa kujiridhisha taratibu za malipo zinafuatwa kabla ya kulipa kampuni hiyo?
Jibu:Ndiyo.
Baada ya mahojiano hayo kumalizika wakili wa serikali Vitalis Timon aliyekuwa akisaidiana na Fredrick Manyanda na Oswald Tibabyekomya waliwasilisha ombi la kuonyesha ushahidi kwamba jarada halisi la maombi ya malipo ya kampuni hiyo bado linaitajiwa Benki Kuu, na wakaiomba mahakama hiyo isikilize jana ombi hilo bila hata upande wa utetezi kupewa nakala la ombi hilo na kulipitia.

Akitoa uamuzi hukusu ombi hilo la upande wa serikali, hakimu Mkazi Kitusi alisema kwa mujibu wa sheria za kesi za jinai ni lazim a upande wa pili nao upewe nafasi ya kujibu ombi hilo hivyo akatupilia mbali ombi la upande wa mashtaka la kutaka ombi hilo lisikilize na kuutaka upande wa utetezi kuwasilisha majibu ya ombi hilo Jumatatu ijayo na kwamba Septemba 8 mwaka huu, ombi hilo litasikilizwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Septemba 5,2009

DPP APINGA DHAMANA YA WAVUVI HARAMU

Na Happiness Katabazi

MKURUGENZI wa Mashitaka nchini (DPP)Eliezer Feleshi amekata rufaa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, kupinga masharti ya dhamana yaliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, katika kesi ya uvuvi haramu inayowakabili raia 32 wa kigeni waliokamatwa kwenye meli ya Tawariq 1.

Kwa mujibu wa vyanzo kuaminika toka ndani ya Mahakama Kuu, zimelieleza gazeti hili kuwa ofisi ya DPP iliwasilisha ombi la rufaa mahakamani hapo hivi karibuni na imeishapewa Na.78 ya mwaka huu.

‘Nakukuakikisha DPP amefungua ombi hilo la rufaa na Jaji Njegafibile Mwaikugile ndiye amepangwa kusikiliza rufaa na ombi hilo litaanza kusikilizwa rasmi Septemba 3 mwaka huu’kilisema chanzo chetu kwa masharti ya kutotajwa jina.

Katika ombi hilo, DPP anapinga masharti ya dhamana yaliyotolewa na Mahakama ya Kisutu ambayo moja ya sharti la dhamana lilisema ili mshitakiwa adhaminiwe ni lazima awe na wadhamini wawili wanaotambulika na ofisi za ubalozi,sharti ambalo linapingwa na DPP kwa madai kwamba ofisi ya ubalozi siyo sehemu ya Tanzania.

Julai 22 mwaka huu, Hakimu Mkazi Waliarwande Lema alitupilia mbali ombi la upande wa mashitaka katika kesi hiyo lilokuwa likiomba mahakama isipokee ripoti ya tathimini ya meli hiyo kwasababu ripoti hiyo ni ya uongo na kamwe haiwezi kuisaidia mahakama.

Lema alisema mahakama hiyo ilichokuwa ikikitaka katika ripoti ni tathimini na si dosari za uandaaji wa ripoti kama inavyodaiwa na upande wa mashitaka na kuongeza kuwa ripoti hiyo imewezesha mahaka a hiyo kufikia uamuzi wa kutoa dhamana kwa washitakiwa ambao ambao wamesota rumande kwa miezi saba sasa.

Akitoa masharti ya dhamana siku hiyo alisema meli hiyo na samaki ambao wanathamani ya sh bilioni 2.7, vitadhaminiwa kwa bondi ya dola za kimarekani 250,000, kila mshitakiwa anadhaminiwa na wadhamini wawili wanaotambulika na ofisi za balozi ambapo wadhamini hao wawili watasaini bondi ya dola 25,000 hata hivyo washitakiwa walishindwa kutimiza masharti ya dhamana hadi sasa.

Machi 10 mwaka huu, ilidaiwa mahakamani hapo kuwa washtakiwa wote wanakabiliwa na mashtaka mawili, shitaka la kwanza ni kuvua samaki bila leseni kinyume na sheria ya Uvuvi wa Samaki katika kina kirefu ya mwaka 2009.

Alidai Machi 8 mwaka huu, washtakiwa wote kwa pamoja, saa sita usiku katika ukanda wa bahari ya Hindi ndani ya eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walikamatwa wakiwa wakivua samaki bila leseni.Na washtakiwa wote walikana mashtaka na wapo rumande kwaajili ya wameshindwa kutimiza masharti dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Septemba 1,2009

WALIOKAIDI AGIZO LA EWURA WATOZWA FAINI MIL.10/-

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es salaam, imewahukumu kifungo cha miezi sita nje na kulipa faini ya sh milioni 10 wafanyabiashara wawili wa vituo vya mafuta baada ya kupatikana na hatia ya kukaidi amri ya Mamlaka ya Uthibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ya kufunga vituo vyao vilivyokuwa vikiuza mafuta yaliyochachuka.

Wafanyabiashara hao ni Mohamed Twalib Nahdi na ndugu yake Abdulatif Twalib Nahdi ambao wote ni wakazi wa Morogoro.

Akitoa hukumu hiyo mwishoni mwa wiki, Jaji Thomas Mihayo, alisema amekubaliana na hoja zilizowasilishwa na Wakili wa Ewura, James Kabakama, kwamba amri iliyotolewa na mamlaka hiyo Septemba 19, 2008 inapaswa kuheshimiwa.

Jaji Mihayo alisema yeyote atakayekiuka amri ya mamlaka hiyo atachukuliwa hatua kali za kisheria na kwamba ametoa adhabu nafuu kwa wafanyabiashara hao, ili waweze kujirekebisha.

Kufuatia uamuzi huo, Jaji Mihayo amewataka wafanyabiashara hao kutotenda kosa kama hilo ndani ya miezi sita na akawapa wiki mbili wawe wameshalipa faini ya sh milioni tano kila mmoja. Vituo vya mafuta anavyomiliki Abdulatif Twalib Nahdi ambavyo vimefungiwa ni Kobil Msamvu Petrol Station na Abdulatif Petrol Station.

Aidha, Mohamed Twalib Nahdi naye anamiliki vituo vya Mohamed Twalib Petrol Station, Oilciom Kihenda Petrol Station na Mohamed Twalib Oilcom Petrol Station.

Ilidaiwa kuwa EWURA walifanya ukaguzi wa vituo vyote vya mafuta mkoani Morogoro kati ya Septemba 13 na 14 mwaka jana na kubaini vituo vya wafanyabiashara hao kuwa vilikuwa vinauza mafuta yaliyochakachuliwa.

Kutoka na hali hiyo, EWURA, iliwataka wafanyabiashara hao kufunga vituo vyao na kujieleza kwa nini wasichuliwe hatua kwa kuuza mafuta yaliyochakachuliwa. Hata hivyo, wafanyabiashara hao walikiuka amri hiyo na kuendelea na shughuli zao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Agosti 31, 2009