MAHAKAMA YAMWEKEA 'NGUMU' MTUHUMIWA EPA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imekataa ombi la upande wa utetezi katika kesi ya wizi wa sh bilioni 3.8 za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), inayomkabili mfanyabiashara Farijala Hussein na wenzake watano, lililotaka kesi hiyo iahirishwe kwa kuwa mshitakiwa wa kwanza anasumbuliwa na figo, hivyo anahitaji matibabu zaidi.


Sambamba na uamuzi huo, mahakama hiyo jana ililazimika kumruhusu zaidi ya mara tatu Farijala aliyekuwa akiomba kupitia wakili wake, Majura Magafu, kwende maliwatoni, hali iliyosababisha wakati mwingine shahidi kusitisha kutoa ushahidi wake hadi mshitakiwa huyo aliyeonekana kuwa na maumivu, arejee kizimbani.

Uamuzi huo ulitolewa na mahakimu wakazi Samwel Karua, Elvin Mugeta na Mutungi, ambapo walisema wanakataa ombi hilo la wakili wa utetezi kwa sababu vyeti vya matibabu vilivyowasilishwa mahakamani hapo vilikuwa havionyeshi kama daktari ametoa maoni yanayotaka mshitakiwa huyo apumzike.

“Tunatupilia mbali ombi hilo na tunakubaliana na ombi la wakili wa Serikali Oswald Tibabyekomya, kupinga ombi la utetezi kwa madai kwamba cheti hicho hakikuonyesha kuwa mshitakiwa anatakiwa kupumzika.

Kwa mujibu wa kifungu cha 197 cha Sheria ya Makosa ya Jinai, kinasema kesi inaweza kuendelea kusikilizwa bila mshitakiwa kuwepo… na kwa sababu hiyo tunaagiza shahidi apande kizimbani atoe ushahidi wake,” alisema Hakimu Mkazi Karua.

Awali, Magafu aliomba kesi hiyo iahirishwe kwa kuwa Farijala hayupo katika nafasi nzuri ya kuendelea kusikiliza kesi hiyo kutokana na maumivu na kwamba yeye kama wakili hayupo tayari kuendelea na kesi hiyo kwa sababu mteja wake anaumwa.

Wakati shahidi, Rehema Kitambi ambaye ni Msajili Msaidizi wa (BRELA) alieleza mahakama kuwa Kampuni ya Mibale Farm inayotuhumiwa kuchota kiasi hicho cha fedha ilisajiliwa kwenye ofisi anayofanyia kazi isipokuwa saini iliyowekwa kwenye jina la usajili wa kampuni hiyo inafafana na yake, hivyo, imeghushiwa.

Hata hivyo, Hakimu Karua aliahirisha kesi hiyo hadi leo ambapo shahidi mwingine atakuja kutoa ushahidi wake na kukubali ombi la Farijala, la kupatiwa ruhusa ya kutofika mahakamani hapo kwa kuwa anakwenda hospitali.Hata hivyo, mahakama ilimtaka mshitakiwa huyo afike mahakamani hapo kesho.

Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa mfululizo, licha ya juzi jopo hilo kushindwa kuisikiliza kwa sababu afya ya mtuhumiwa huyo ilibadilika na kukimbizwa katika Hospitali ya Burhani.

Mbali na Farijara, washitakiwa wengine ni Rajabu Maranda, Ajay Somay na maofisa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambao ni Iman Mwakosya, Ester Komu na Sophia Kalika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Oktoba 28, 2009

MAHANGA AMDAI MSEMAKWELI BIL.3/-

Na Happiness Katabazi

IKIWA ni wiki moja tangu Mwanaharakati Kainerugaba aanike orodha ya vigogo aliyodai wamegushi sifa za kuwa shahada ya uzamivu(PhD) NAIBU Waziri wa Kazi ,Ajira na Maendeleo ya Vijana, Dk.Makongoro Mahanga, amemfungulia kesi ya kashfa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akitaka alipwe fidia ya Sh bilioni tatu kwa kumkashfu.


Dk.Mahanga ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea Kennedy Fungamtama alifungua kesi hiyo jana mchana mahakamani hapo ambapo tayari kesi hiyo imewa namba 145 ya mwaka huu.Kwa mujibu wa hati ya madai ambayo Tanzania Daima ina nakala yake inaonyesha wadaiwa wengine ni Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Nipashe Muhibu Saidi. Mkurugenzi Mtendaji wa gazeti hili na Kampuni ya The Guardian Limited.

Dk.Mahanga abnadai kuwa kwa mujibu wa mdaiwa wa kwanza (Msemakweli) kuwa Oktoba 18 mwaka huu, aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kutoa taarifa za kumkashifu na gazeti la Nipashe likachapisha habari ukurasa wa mbele kwa maneno yafuatayo:

“Dk.Mahanga amegushi sifa za kuwa ana shahahada ya uzamivu(daktari wa falsafa)wakati hajawahi kusoma shahda hiyo wakati wowote na mahali popote duniaani’: maneno ambayo alidai ni ya uongo na yalikuwa na lengo ya kupindisha ukweli.

Alidai kuwa maneno yaliyotumika kwenye nukuu hiyo yameonyesha mlalamikaji(Mahanga) alighushi vyeti hivyo, ni mtu asiyemwaminifu na ni mkosaji katika mazingira hayo na astahili kuendelea kushikilia nafasi ya kisiasa katika ofisi ya umma na bunge.

Dk.Mahanga aliendelea kudai kuwa Oktoba 19 mwaka huu, mdaiwa wa pili, tatu, na wa nne walimkashfu kwa kuchapisha taarifa iliyotolewa na mdaiwa wa kwanza, katika ukurasa wa kwanza katika gazeti la NIPASHE toleo Na.ISSN.0856-5414 Na.05443 ambalo lilibandika picha ya mlalamikaji kwa kuchapisha habari iliyotolewa na mdaiwa wa kwanza kwa malengo ya kisiasa.

“Gazeti la NIPASHE linachapishwa hapa jijini na kusambazwa hapa nchini na nchi za Afrika Mashaki, hivyo naomba mahakama hii iliamuru gazeti hilo kuniomba radhi katika ukurasa wa mbele kwa uzito ule ule wa habari waliyoichapisha awali, izuie wadaiwa kuchapisha habari inayohusu mambo binafsi kuhusu mimi ,biashara zangu,kazi zake za kisiasa bila idhini yangu”alidai Dk.Mahanga.

Wiki iliyopita Msemakweli aliitisha mkutano wake na waandishi wa habari na kudai kuwa amefanya utafiti na kubaini mawaziri sita waligushhi vyeti vya taaluma.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Oktoba 27, 2009

KESI NYINGINE YA JEETU YASIMAMISHWA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kwa mara ya tatu tena, jana imetoa amri ya kusimamisha kesi ya wizi wa sh bilionio 3.3 katika Akaunti ya Madeni ya Nje(EPA) inayomkabili mfanyabishara maarufu,Jayantkumar Chandubhai Patel, maarufu kwa jina la Jeetu Patel na wenzake wawili, hadi kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na washitakiwa hao Mahakama Kuu ya Tanzania itakapomalizika.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Mahakimu Wakazi Richard Kabate na Samwel Karua ambao walisema wamekubalina na maombi ya wakili wa utetezi Mabere Marando na Martin Matunda , yaliyotaka mahakama hiyo itoe amri ya kusimamisha usikilizwa wa kesi hiyo hadio kesi ya kikatiba inayoendelea Mahakama Kuu itakapomalizika.

Akisoma uamuzi huo Hakimu Mkazi Richard Kabate alisema mahakama hiyo inatupilia mbali pingamizi la wakili wa serikali Timon Vitalis lilotaka mahakama hiyo itupilie mbali ombi hilo la utetezi kwasababu tamko lilotolewa na Mwenyekiti wa IPP, Reginard Mengi dhini ya washitakiwa halikuwa lilikuwa haliivurugi kesi hiyo kwasababu kesi hiyo ilikuwa bado haijaanza kuendeshwa mahakamani hapo.

Hakimu Kabate ambaye alisoma uamuzi huo huku akitumia mifano ya kesi mbalimbali alisema pingamizi hilo la serikali halina msingi kwasababu kisheria kesi yoyote inapokuwa imefunguliwa mahakamani uwa inaendeshwa hatua kwa hatu hivyo siyo kweli kesi hiyo ilikuwa hainza kusilizwa.

“Kwa sababu hiyo tunatupilia mbali pingamizi la serikali lilodai kesi hiyo bado haijaanza kusikilizwa kwasababu kwasababu sheria inasema kesi ikishafunguliwa taratibu zingine ndani ya kesi hiyo zinaendelea…tunasema kesi hii imekuwa ikiendelea mahakamani hapa na ndiyo mahakama upande wa mashitaka na serikali ulikuwa ukifika mahakamani hapa na kuwasilisha maombi yao mbalimbali mbele ya jopo hili, hivyo kusema kesi hii ilikuba bado haijafikia hatua ya kuanza kusikilizwa siyo kweli”alisema Kabate.

Alisema licha washitakiwa hao wameshitakiwa kwa kesi hiyo lakini wanayo haki ya kudai haki zao za Kikatiba pindi wanapoona zinavunjwa na kuongeza kuwa mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuendelea kusikiliza kesi hiyo kwasababu tayari washitakiwa hao wameishafungua kesi ya kikatiba katika mahakama ya juu.

“Tunatoa amri ya kusimamisha kusikilizwa kwa kesi hii hadi kesi iliyofunguliwa wa shitakiwa katika mahakama ya juu itakapomalizika na tunaagiza jarada la kesi hii lipelekwe mahakama Kuu”alisema Kabate.

Juni 4 mwaka huu, Jeetu na wenzake walifungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, inayosikilizwa na jopo la majaji watu wanaongozwa na Jaji Kiongozi, Fakhi Jundu, Geofrey Shahidi na Semistocles Kaijage. inaendelea kusikilizwa ambapo upande wa walalamikaji na wadaiwa wameishawasilisha utetezi wao na imepangwa kuanza kusikilizwa Novemba 2 mwaka huu.

Katika kesi hiyo, Jeetu na wenzake wanamshitaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Reginald Mengi na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwamba kwa nafasi zao walishindwa kutimiza wajibu wao kikamilifu baada ya mdaiwa wa pili (Mengi) kuwahukumu kupitia vyombo vya habari kabla ya kesi zao nne zilizofunguliwa katika Mahakama ya Kisutu kutolewa hukumu.

Jeetu na wenzake walifungua kesi hiyo ya kikatiba Na. 30 wakiomba Mahaka ma Kuu itoe tafsiri sahihi ya ibara 13, kifungu 4, 5 na 6 (b) cha Katiba ambacho kinatamka watu wote ni sawa mbele ya sheria na pia itafsiri ibara 13 (6) (b) inayosema mtu yeyote asichukuliwe ana hatia hadi pale mahakama itakapomkuta na hatia.

Kwa mujibu wa hati ya madai, walalamikaji hao wanadai kuwa wamefikia uamuzi huo wa kuiomba mahakama itoe tafsiri ya ibara hizo za katiba kwa kuwa wanaamini zimevunjwa na Mengi ambaye Aprili 23, mwaka huu, alitumia vyombo vya habari kuwahukumu kwa kuwaita ‘Mafisadi Papa’ wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inayosikiliza kesi zao haijatoa hukumu.

Uamuzi huo ni wa watatu kutolewa katika kipindi cha Oktoba mwaka huu, mahakama hiyo ilitoa amri ya kusimamishwa kuendelea kwa kesi ya wizi wa sh bilioni 9, kesi ya wizi wa sh 3.9 zinazowakali washitakiwa hao hadi kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na washitakiwa hao itakapotolewa uamuzi.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na kesi nne za wizi wa fedha katika Akaunti ya EPA katika Mahakama ya Kisutu ambazo zilifunguliwa Novemba mwaka jana. Mbali na Jeetu, washitakiwa wengine ni Devendra Vinodbhai Patel, Amit Nady na Ketan Chohan.

Wakati huo huo, Mahakamani hapo jana mahakimu wakazi Samwel Kalua na Elvin Mgeta waliarisha usikilizwaji wa kesi wizi Fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje(EPA) Sh bilioni 3.8 inayomkabili wafanyabishara watatu Farijara Hussein, Rajabu Maranda,Ajay Somay na maofisa wa BoT, Iman Mwakosya, Ester Komu na Sophia Kalika hadi leo kwasabu mshitakiwa wa kwanza(Farijara) anasumbuliwa na ugonjwa figo.

Uamuzi huo wa kuairishwa ulitokana na ombi la wakili wa utetezi Majura Magafu ambaye aliiomba mahakama hiyo iairishe usikilizwaji huo jana kwasababu mteja wake jana asubuhi alifika katika viwanja hivyo vya mahakama ila alianza kujisikia kuugua ugonjwa huo la kulazimika kwenda hospitali ya Burhan kwaajili ya matibabu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne,Oktoba 27, 2009

SHAHIDI:BODI BOT HAIKUWAHI KUMLALAMIKIA LIYUMBA

Na Happiness Katabazi

MENEJA wa Masuala ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Justo Tongola (45), ambaye ni shahidi wa pili katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa BoT, Amatus Liyumba, ameieleza mahakama kuwa hajawahi kuona wala kusikia bodi hiyo ikilalamikia utendaji kazi wa Liyumba.

Akitoa ushahidi huo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, pia alidai hajawahi kushuhudia bodi hiyo ikikataa kuidhinisha maombi ya menejimeti ya benki hiyo wala aliyekuwa Gavana wa BoT, marehemu Daudi Balali, akilalamikia mradi wa ujenzi wa minara pacha.

Shahidi huyo alitoa maelezo hayo baada ya kuulizwa maswali na mawakili wa utetezi Majura Magafu, Hudson Ndusyepo, Jaji Mstaafu Hillary Mkate, na Onesmo Kyauke mbele ya Jopo la Mahakimu Wakazi linaloongozwa na Edson Mkasimongwa anayesaidiana na Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa.

Ifuatayo ni mahojiano kati ya mawakili wa utetezi na shahidi huyo:
Wakili:Nani alitoa kibali cha Kurugenzi ya Utumishi na Utawala iliyokuwa ikiongozwa na Liyumba, iratibu mradi huo?
Shahidi:Sina hakika sana ila miradi yote inayoangukia kwenye eneo la Capital Expenditure zote zina ratibiwa na ofisi hiyo.
Wakili:Umesema ofisi iliyokuwa ikiongozwa na mshitakiwa ilikuwa ikiratibu mradi huo ,ilikuwa ikifanyakazi hiyo ya uratibu kwa niaba ya Benki Kuu?
Shahidi:Ndiyo.
Wakili:Taarifa za uaandaaji wa taarifa ya mabadiliko ya upanuzi wa ujenzi zilikuwa zinaratibiwa na ofisi ya mshitakiwa na nani?
Shahidi:Ofisi ya Liyumba na Meneja Mradi Deogratius Kweka ambaye aliajiriwa na Benki Kuu kwa mkataba.
Wakili:Ninani mweingine alihusika katika uaandaji wa hiyo taarifa ya mabadiliko ya ujenzi,ukiacha Kweka?
Shahidi:Hilo sina taarifa.
Wakili:Taarifa ikishaandaliwa zinapelekwa kwenye bodi?
Shahidi:Ndiyo.
Wakili:Ulisema mradi ulikuwa kwenye Capital Expenditure katika kipindi chochote bodi ilikuwa hailidhiki na mabadiliko?
Shahidi:Kuna kipindi bodi baada ya kupokea maombi kadhaa ilikuwa hairidhiki na ilikuwa inarudisha baadhi ya maombi kwa Menejimenti ili zifanyiwe marekibisho kisha zinarejeshwa tena kwenye bodi na bodi inatoa idhini.
Wakili:Kuna kipindi chochote wewe ulivyokuwa kwenye vikao vya bodi kama bodi iliwahi kumlalamikia Liyumba kama Liyumba?
Shahidi:Hilo sijawahi kusikia wala kuliona kwenye vikao ila kuna wakati Menejiment ilikuwa inaondolewa kwenye vikao.
Wakili:Ina maana Gavana na Naibu Gavana waliondolewa kwenye vikao vya Menejimenti?
Shahidi:Hapana, kwani hao ni kwa vyeo vyao ni sehemu ya bodi ila baadhi ya wafanyakazi waliondolewa
Wakili:Kuna sehemu uliona gavana aliwahi kulalamika kuhusu mradi huo?
Shahidi:Mibinafsi sijawahi kuona hilo.
Wakili:Ni kweli kwamba hakuna hata siku moja kikao cha Menejimenti hakijawahi kujadili mradi huo hata mara moja?
Shahidi:Kumbukumbu zangu vikao vya bodi na menejimenti vilivyouzulia mwaka 2000-2007,kwakweli sikumbuki kama menejimenti iliwahi kuzungumzia mradi huo.
Wakili:Ina wezekana kurugenzi ya utawala ipewe jukumu la kuratibu mradi halafu isiujadili?
Shahidi:Menejimenti ipo katika sehemu mbili.Mosi, Gavana ndiye mwenye mamlaka ya kusimamia menejimenti na gavana halazimiki kupeleka kila jambo kwenye menejimenti.
Wakili:Nitakiwa sijakosoe, mambo yanayofayofanywa na utawala lazima gavana awe na taarifa?
Shahidi:I presume so.
Wakili:Na lazima gavana hayabariki?
Shahidi:Ndiyo.
Wakili:Utakubaliana na mimi jukumu la bodi ni kulinda maslahi ya BoT na serikali kwa ujumla yasihujumiwe?
Shahidi:Ni kweli na hilo ni jukumu la kisheria.
Wakili:Kuna kipindi chochote kuna maombi yalipelekwa na Menejimenti kwenye Bodi na bodi ikakataa kuidhinisha?
Shahidi:Sikuwai kushuhudia hiyo la bodi kukataa kuidhinisha.
Awali kabla ya mahojiano hayo Wakili wa serikali Juma Mzarau, Ben Lincoln.Thadeo Mwenepazi na Prospa Mwangamila walimuongoza shahidi huyo kutoa ushahidi wake.Ifuatayo ni mahojiano kati ya wakili Mzarau na shahidi:
Wakili:Kazi zako kubwa pale BoT ninini?
Shahidi:Tangu 1994 nilianza kujishughulikia maswala ya bodi kwa kumsaidia Katibu wa Benki.
Wakili:Katibu wa benki anaitwaje kwenye Bodi?
Shahidi:Katibu wa Bodi.
Wakili:Majukumu yake ninini?
Shahidi:Kuratibu maandalizi ya mikutano ya bodi na menejimenti na kuakikisha wajumbe wanapata madokezi yote na maadhimio yote yanawekwe kwenye maandishi.
Wakili:Unapoingalia Menejimenti ya BoT inasura ngapi?
Shahidi:Kisheria Menejimenti ipo chini ya Gavana kwa hiyo Menejimenti inapotoa maamuzi inamaanisha gavana katoa maamuzi.Menejimenti nyingine ipo chini ya gavana na Naibu Gavana na Wakurugenzi wa Benki hiyo.
Wakili:Je Gavana anapotoa maelekezo uwa anayatoa kwa njia hipi?
Shahidi:Kwa njia ya dokezo.
Wakili:Umekuwa msaidizi wa Katibu wa Bodi wa vikao vyote hivyo,ieleze mahakama approval structure ya bodi iko je?
Shahidi:Bodi ndiyo yenye mamlaka ya kuunda sera na kuzitekeleza na kusheria imepewa jukumu la kupitisha bajeti inapotokea kazi za Benki za kila siku gavana ndiyo mwenye mamlaka ya mwisho ya kutoa maamuzi mbalimbali.
Wakili:Katika BoT kuna matumizi ya fedha ya aina ngapi?
Shahidi:Aina mbili.Aina ya kwanza ni Capital Expenditure(matumizi ya mradi unaotekelezwa na pili ni Current Expenditure) yaani yale ya matumizi ya kawaida kimsingi yanahusu mambo mbalimbali yanayotokea kila siku yanahusu Benki hiyo.
Wakili:Tukianzia matumizi ya Capital Expenditure,sura yake ikoje?
Shahidi:Ni sera iliyopitishwa na bodi na Capital Expenditure inatakiwa ipate kibali cha bodi.
Wakili: Current Expenditure ikoje?
Shahidi:Inapitishwa na bodi na baada ya hapo matumizi yanapitishwa na menejimenti na kuna mengine yanaitaji kibali cha gavana.Kwa hiyo b inapokuja Capital Expenditure gavana hana mamlaka hadi bodi.
Wakili:Jukumu la Menejimenti ni nini?
Shahidi:Kisera ambayo inapitishwa na bodi ,Menejimenti inapaswa kuwasilisha maombi kwenye bodi na baada kupata kibari ndipo inaweza kwenda kuendelea na matumizi.
Wakili:Katika kipindi cha 2000-2008 ulikuwa unaudhiria vikao vya bodi?
Shahidi:Nilikuwa naingia ila kuna baadhi nilikuwa siingii.
Wakili:Kuna vikao vingapi vya bodi?
Shahidi:Vipo vikao vya aina mbili.Kuna kikao cha kinachofanyika kila baada ya miezi miwili na kingine kinafanyika kwa dharula.Vikao vya dharula uitishwa pale tu kuna jambo la dharula linatokea ili bodi ije iidhinishe.
Wakili:Uliwahi kuufahamu mradi mradi wa ujenzi wa minara pacha?
Shahidi:Niliufahamu kwa kuona ukiendelea pia kupitia vikao mbalimbali vilikuwa vikiujadili.
Wakili:Mradi huo ulikuwa ukijadiliwa kwenye vikao vya bodi?
Shahidi:Ndiyo ulijadiliwa.
Wakili:Nini kilichojadiliwa kwenye bodi kuhusu mradi huo?
Shahidi:Menejimenti ilkikuwa inawasilisha taarifa za utekelezaji wa mradi huo na taarifa za mabadiliko ya upanuzi na kuomba bodi itoe idhini.
Wakili:Kibali cha bodi kiliombwa wakati gani?
Shahidi:Wakati mabadiliko ya mradi na matumuzi yalikuwa yameishatekelezwa kwa maana hiyo kibari kilikuwa kinaombwa kwenye bodi ili kubaliki mabadiliko hayo.

Kiongozi wa jopo Edson Mkasimogwa aliarisha kesi hiyo Oktoba 28 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya kutajwa ambapo siku hiyo watapanga tarehe ya kuendelea kusikiliza kesi hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Oktoba 24, 2009

MAWAKILI WA LIYUMBA WAMKABA KOO SHAHIDI

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa kwanza katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, inayomkabili Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala mstaafu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, Seif Kasanga Mohamed (49), ameiambia mahakama kuwa mabadiliko ya upanuzi wa ujenzi wa Minara Pacha (Twin Tower), yaliidhinishwa na Bodi ya Wakurugenzi wa BoT.

Kasanga ambaye ni mchunguzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambambana na Rushwa (TAKUKURU), alitoa madai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, mbele ya kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi Edson Mkasimongwa, anayesaidiana na Lameck Mlacha na Benedict Mwinga wakati akitoa ushahidi wake.

Shahidi huyo ambaye pia ni mhandisi wa ujenzi kitaaluma, alifafanua kuwa Bodi ya BoT iliidhinisha baada ya Liyumba kuwa ameishatoa maagizo ya utekelezaji wa upanuzi wa mradi kwa mkandarasi.

“Ni kweli bodi ilitoa idhini ya upanuzi wa Twin Tower, lakini ilitoa idhini hiyo wakati Liyumba tayari alikuwa ameishatoa maagizo ya upanuzi wa ujenzi na malipo kwa Kampuni ya Lead Consultant (Design and Services Ltd), kwa hiyo utaona bodi ni kama vile ilikuwa ni mhuri,” alidai Kasanga.

Yafuatayo ni mahojiano kati ya mawakili wa utetezi; Majura Magafu, Hillary Mkate, Onesmo Kyauke na Hudson Ndusyepo dhidi ya shahidi:Wakili: Ndugu shahidi uliwahi kuchunguza ramani ya majengo?
Shahidi: Nilipata fursa ya kuchunguza ramani.
Wakili: Nani alileta mabadiliko ya upanuzi wa Minara Pacha?
Shahidi: Liyumba.
Wakili: Liyumba siyo injinia, aliwezaje kufanya hayo mabadiliko wakati yeye alikuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala?
Shahidi: (Kimya) Uchunguzi unaonyesha Liyumba alikuwa akitoa maagizo ya kuidhinisha ongezeko la ujenzi.
Wakili: Je, ukiambiwa ongezeko hilo liliidhinishwa na bodi utakubali?
Shahidi: Watakuja wajumbe wa bodi wenyewe waeleze na katika uchunguzi wangu sikubaini hili.
Wakili: Tukikuambia kulikuwa na idhini ya bodi utakubali?
Shahidi: Katika uchunguzi wangu, Aproval ya bodi inayozungumzwa hapa ni ile Approval baada ya Liyumba kufanya mabadiliko ya upanuzi wa ujenzi.
Wakili: Huo mkataba wa ujenzi ulikuwa ni kati ya Liyumba na kampuni ya ujenzi?
Shahidi: Hapana, ulikuwa ni kati ya BoT na Kampuni ya Lead Consultant. Lakini baadaye Kurugenzi ya Utumishi na Utawala iliyokuwa ikiongozwa na Liyumba ndiyo ilikuwa ikiratibu mradi huo (Cordinator).
Wakili: Huyo Liyumba alikuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala ndiyo apewe mzigo wa kushughulikia ujenzi wa mradi huo, je inaingia akilini?
Shahidi: (Kimya) Nimesema ofisi ya Liyumba ilikuwa inaratibu na ilikuwa kiungo.
Wakili: Mshitakiwa kwa cheo chake ndiye aliyeidhinisha mabadiliko hayo wakati yeye siyo mhandisi?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Wewe ni mhandisi wa ujenzi hilo swali siyo la kufikiria… jibu hilo swali upesi.
Shahidi: Kimya.
Wakili: Mabadiliko yote hayo yanatakiwa yaidhinishwe na bodi?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Kwa hiyo mabadiliko yote hayo hayakuidhinishwa na bodi ya BoT?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Je, Gavana marehemu Daud Balali hakuusika na mabadiliko hayo?
Shahidi: Gavana hakuhusika kabisa.
Wakili: Mbona upande wa mashitaka wakati unamsomea maelezo ya awali mshitakiwa hivi karibuni, ulidai kuwa ni Liyumba na Ballali ndiyo walifanya mabadiliko hayo bila idhini ya bodi ya wakuregenzi?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Ulisema Liyumba alikuwa akiandika barua za maagizo ya mabadiliko hayo ya upanuzi wa ujenzi kama mtu binafsi au mtumishi wa BoT?
Shahidi: Mahakama itajua.
Wakili: Ballali alikuwa Gavana na kwa mujibu wa sheria ya benki, ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi, sasa unasemaje mabadiliko alifanya Liyumba bila idhini ya Bodi?
Shahidi: Kwa sababu Ballali ameishakufa, siwezi kumzungumzia hapa.
Wakili: Hapa, jibu swali kwani wakati Ballali alipokuwa hai, ndiye alikuwa na madaraka yote na maagizo aliyokuwa akiyatoa Liyumba angeweza kuyakataa?
Shahidi: Mshitakiwa asingeweza kuyakataa.
Wakili: Kwa sababu angeyakataa angeonekana ni mtovu wa nidhamu na hivyo basi Liyumba alikuwa ni mtiifu na alikuwa katika ofisi hiyo ya umma?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Katika uchunguzi wako ulibaini mshitakiwa kafanya kosa la rushwa?
Shahidi: Nimebaini kafanya kosa linaloendana na rushwa.
Wakili: Kwa hiyo unataka kuiambia mahakama hata bodi ya BoT ilikumbwa na rushwa?
Shahidi: Sina jibu.
Wakili: Shitaka linalomkabili mshitakiwa ni kuisababishia serikali hasara kwa sababu aliongeza upanuzi wa majengo, hivi Liyumba hayo majengo aliyachukua na kuyapeleka nyumbani kwake?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Hivi upanuzi wa ujenzi wa minara pacha ulitokea usiku wa manane, au uliota kama uyoga?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Hivi bodi ilikuwa haina akili hadi isikataze hayo mabadiliko ya upanuzi wa ujenzi unayodai yalifanywa na Liyumba?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Katika uchunguzi wako, Liyumba alikuwa ni mjumbe wa bodi?
Shahidi: Hapana.
Wakili: Tunakubalina kwamba yale majengo ya ghorofa 18 yapo na je, yana thamani nzuri?
Shahidi: Yapo
Wakili: Thamani ya majengo yale imeteremka?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Ebu iambie mahakama sasa, serikali inapata hasara ipi?
Shahidi: Kwa kuwa hakukuwa na idhini ya bodi, ndiyo hasara yenyewe na wajumbe wa bodi watakuja kueleza (kicheko).
Shahidi: Liyumba alikuwa ni mtu mdogo kwenye bodi na mabadiliko hayo angefanya bila idhini si bodi ingemtimua kazi?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Utakubaliana na mimi wewe huwezi kuwa mchunguzi?
Shahidi: Sikubaliani na wewe, mimi ni mchunguzi.
Wakili: Unajua kazi za Takukuru zilizoainishwa kwenye Sheria ya Takukuru kifungu cha 7?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Utakubaliana kimsingi kazi ya taasisi yenu ni kuchunguza kesi zinazohusiana na rushwa na si vinginevyo?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Kwa hiyo utakubaliana na mimi makosa yanayomkabili mteja wangu hayahusiani na rushwa na ndiyo maana yanaangukia kwenye Sheria ya Kanuni ya Adhabu?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Kwa hiyo kazi hii ya uchunguzi katika kesi hii haikupaswa kufanywa na Takukuru ilipaswa kufanywa na jeshi la Polisi?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Ni nani mwenye mamlaka ya mwisho ya kuamua nini kifanyike na kipi kisifanyike BoT?
Shahidi: Bodi ya BoT.
Wakili: Uliwahi kuwahoji wajumbe wa bodi kwanini waliidhinisha mabadiliko ya upanuzi wakati mabadiliko hayo yalishatekelezwa?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Uliwauliza wajumbe hao ni kwanini wasikatae mabadiliko hayo kwa sababu wao walikuwa pale kwa ajili ya kulinda maslahi ya benki hiyo na serikali?
Shahidi: Walisema walikataa bila mafanikio.
Wakili: Uliwahi kuzisoma hizo minute za vikao vya bodi ilikuona?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Kwanini hukuzileta hapa mahakamani?
Shahidi: Zitaletwa na mchunguzi mwenzangu.
Wakili: Uliwahi kuusoma mkataba wote wa ujenzi wa mradi huo?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Kwenye huo mkataba kuna kipengele kinaruhusu kampuni ya ukandarasi wa mradi na BoT kufanya marekebisho kutokana na thamani ya shilingi kushuka?
Shahidi: Ndiyo.
Wakili: Timu yenu ya uchunguzi iliwahi kumhoji Ballali?
Shahidi: Haikuwahi kumhoji ila nilimhoji Liyumba.
Wakili: Ulivyomhoji Liyumba ulimuuliza hizo barua za marekebisho ya mkataba ya kupanua ujenzi wa majengo aliandika kwa maelekezo ya nani?
Shahidi: Sikumbuki.
Wakili: Ulimuuliza Liyumba ni kwanini Bodi ya BoT ilikubali ongezeko la ghorofa nne, nne badala ya 14 zilizoainishwa kwenye mkataba?
Shahidi: Ndiyo na alinijibu ilikubali kwa sababu kulikuwa na ongezeko kubwa la wafanyakazi BoT kwa hiyo kulikuwa na uhaba wa ofisi.
Wakili: Bodi ilikubali kuidhinisha baada ya kuridhika kwamba yale marekebisho ya upanuzi yalikuwa ni ya msingi na yasingeweza kuisababishia serikali hasara?
Shahidi: Hapa.
Wakili: Kama hapana, bodi nayo ilifanya makosa kuidhinisha marekebisho huku ikijua itaingiza serikali hasara?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Bodi ilikuambia hiyo na haikuwa na haja ya kukataa?
Shahidi: Bodi haikukataa, ila wajumbe wa bodi walikemea.
Wakili: Hayo mahesabu ya mteja wetu kusababishia hasara ya kiasi hicho cha fedha haliyafanya nani?
Shahidi: Mimi
Wakili: Haya tupe huo mchanganuo wa mahesabu uliyoyafanya hadi ukapata hiyo hasara?
Shahidi: Sina.
Wakili: Katika hayo maagizo ya upanuzi wa ujenzi yaliyokuwa yakitolewa na Liyumba yalikuwa yakitaja kiasi chochote cha fedha?
Shahidi: Hapana.
Wakili: Hicho kiasi cha gharama umekipata wapi wakati hujui hata vifaa vya ujenzi hujui vilinunuliwa kiasi gani?
Shahidi: Kimya.
Wakili: Nani alikuwa na jukumu la kutunza miniti za vikaa vya bodi licha uliieleza mahakama miniti nyingine hukuzipata na baadhi ulizozipata hazina saini?
Shahidi: Katibu ambaye ni Mwanasheria wa BoT, Bosco Kimela.
Wakili: Hivi miniti zisizokuwa na saini ya Mwenyekiti na Katibu ninakuwa miniti kweli?
Shahidi: Miniti ili ziwe miniti ni lazima ziwe na saini ya watu hao.
Kesi hiyo inayovuta hisia za wengi nchini imeahirishwa hadi leo ambapo shahidi wa pili ataanza kutoa ushahidi wake.
Ifuatayo ni mahojiano kati ya jopo la Mahakimu wakazi na shahidi huyo?
Jopo:Majengo yamejengwa hayajajengwa?Liyumba alifaidika binafsi na mabadiliko ya upanuzi wa ujenzi huo?Je kulikuwa na udanganyifu katika kiasi cha fedha kilichotumika katika ujenzi huo?Sasa hasara inapatikanaje?
Shahidi:Kimya(watu wakaangua kicheko).
Awali kabla ya shahidi huyo kuhojiwa na upande wa utetezi, wakili wa serikali Juma Mzarau, Ben Lincoln,Thadeo Mwenepazi na Prospa Mwangamila,alimuongoza shahidi huo kutoa ushahidi wake:Yafuatayo ni mahojiano kati ya Mzarau na shahidi huyo:
Wakili:Je lini ulikabidhiwa jukumu la kuchunguza shauri hili?
Shahidi:Februali 2008.
Wakili:Baada ya kukabidhiwa jukumu hilo uligundua nini?
Shahidi:Niligundua shauri lilipokelewa April 2006 ofisi kwetu Takukuru.
Wakili:Baada ya kukabidhiwa shauri hilo ulifanya nini?
Shahidi:Kufanya uchunguzi wa wazi kwa kukusanya vielelezo na kukusanya vielelezo na kuhoji mashahidi pamoja na Liyumba na kutembelea mradi wa minara pacha na nilibaini Bot ilisaini mkataba na kampuni ya Group Five East(PTY) Ltd ya Afrika Kusini.
Wakili:Ulishawahi kuona mkataba huo?
Shahidi:Ndiyo naniaomba kuotoa mahakama kama kielezo(jopo limepokea kama kielezo Na.moja).
Wakili:Kwa mujibu wa mkataba huo gharama za ujenzi zilikuwa kiasi gani?
Shahidi:USD milioni 73.6
Wakili:Unakumbuka gharama za kazi zilizoainishwa kwenye mkataba huo?
Shahidi:Ni za ujenzi wa jengo la South Tower ghoroga 14,North Tower ghorofa 14,ukumbi wa mikutano,sehemu ya kuegesha magari ghorofa nne na kazi za nje.
Wakili:Je katika uchunguzi wako uliwahi kutembeleza ujenzi wa mradi wa Minara Pacha?
Shahidi:Ndiyo na niligundua jengo la South Tower,Noth zilijengwa ghorofa 18 badala ya 14 zilizoainishwa kwenye mkataba, vile vile kwenye ninara hiyo majengo hayo vilijengwa viwanja vya kutua Helkopta na kwenye kuta za majengo hayo kuliwekwa(glass curtain)badala ya rangi ya kawaida ambayo iliainishwa kwenye mkataba.
Wakili; Je kulikuwa na jengo lilojengwa nje ya mkataba?
Shahidi:Ndiyo.jengo la North block lilijengwa nje ya mkataba.
,Basement mbili badala ya basement moja.
Wakili:Nani alikuwa Meneja mradi wa Minara Pacha?
Shahidi:Deogratius Kweka.
Wakili:Kielelezo gani kingine unakumbuka ulikipata kwenye uchunguzi wako?
Shahidi:Cost Alasisy report toka 2002-2008 na ninaomba niitoe mahakamani kama kielelezo.
Ghafla aliinuka wakili wa utetezi Majura Magafu na kuiomba mahakama isipokea kielelezo hicho kwani kinaonyesha wazi kiliandaliwa kwani mbaya na hakikuandaliwa kitalaamu kwani ina saini,jina la mwandishi wala mhuri wa kampuni, tarehe na kwa kifupi hiko kielelezo ni cha kuokoteza barabarani na wala haijaandikwa na shahidi huyo.

“Tunapinga kupokelewa kwa kielezo hicho kwani ni cha kuokoteza barabarani na wala hakikuandikwa na shahidi huyu tunataka aliyoandika hiyo ripoti afike hapa tumuulize maswali ..shahidi huyu atakuwa bubu tukianza kumuuliza maswali na sisi atutaki awe bubu”alidai Magafu kwa sauti ya ukali .

Hata hivyo baada ya wakili Magafu kupinga kilelezo hicho kisipokelee wakili wa serikali Mzarau aliinuka na kudai hawataki kupoteza muda wa mahakama na hivyo upande wa mashitaka wanakiondoa kielelezo hicho na kisipokelewe na mahakama na kusababisha watu kuangua vicheko.

Kiongozi wa Jopo Mkasimongwa,aliarisha kesi hiyo hadi leo ambapo shahidi wa pili ataanza kutoa ushahidi wake katika kesi hiyo ambayo umati wa wananchi wengi wanafika mahakamani hapo kwaajili ya kusikiliza kesi hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Oktoba 23, 2009

WALIOGUSHI KUDHAMINI KIGOGO BOT KORTINI

Na Happiness Katabazi

BAADA ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuamuru wafanyabiashara wawili wakamatwe kwa kuwasilisha ripoti za uthamini wa majengo za kughushi, jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka saba.


Mbele ya Hakimu Mkazi Liad Shamshana, Wakili wa Serikali Frola Massawe, aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Teligon Rutaihwambyemo “David Majebele” (46), na mwenzake Koli Syikiliwe Sanga “Felix Mussa Nyuki” (53), wakazi wa Mwanyamala, Mchangani jijini Dar es Salaam.

Wakili Massawe alidai kuwa, shitaka la kwanza kwa washitakiwa hao ni la kula njama kwa nia ya kutenda kosa, ambapo kwa pamoja, wanadaiwa kuwa Oktoba 20, mwaka huu, katika sehemu isiyofahamika jijini Dar es Salaam, walikula njama na kutenda kosa la kughushi.

Alidai shitaka la pili na la tatu linamhusu kila mshitakiwa peke yake. Mshitakiwa wa kwanza anadaiwa kuwa siku hiyo alijitambulisha kwa Msajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu, Lameck Mlacha kwa jina la David Majebele, wakati mshitakiwa wa pili alijitambulisha kwa msajili huyo kama Felix Nyuki, huku wakijua si kweli.

Wakili huyo wa serikali alidai kuwa, shitaka la tano ni kwa ajili ya mshitakiwa wa kwanza, Rutaihwambyemo, ambaye anadaiwa kuwa Septemba 14, mwaka huu, katika eneo lisilofahamika katika Manispaa ya Kinondoni, alitengeneza taarifa ya tathimini ya kughushi inayoonyesha kitalu E, namba 247 cha Mbezi, kina thamani ya sh bilioni tatu huku akiwa na lengo la kuonyesha kuwa taarifa hiyo ni halali na imetolewa na Mthamini Mkuu wa Serikali.

Aidha, alidai shitaka la tano ni kwa ajili ya mshitakiwa wa pili (Sanga), ambaye anadaiwa kuwa Septemba 29, mwaka huu, ndani ya Manispaa ya Kinondoni, aliandaa ripoti ya tathimini inayoonyesha kuwa jengo lililopo katika Kitalu 74, eneo la Gerezani, lina thamani ya sh bilioni 5.8 na kuonyesha taarifa hiyo ilitolewa na Mthamini Mkuu wa Serikali, huku akijua si kweli.

Alidai shitaka la sita na saba linamhusu mshitakiwa mmoja mmoja ambapo Oktoba 20, mwaka huu, wanadaiwa waliwasilisha taarifa hizo za uthamini, huku wakijua zimeghushiwa kwa Msajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu, Lameck Mlacha.

Hata hivyo, washitakiwa walikana mashitaka yote na kurejeshwa rumande hadi Novemba 4 mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena.

Wiki iliyopita, Hakimu Mlacha aliamuru washitakiwa hao waliokuja kumdhamini mshitakiwa wa nne ambaye ni Mkurugenzi Mstaafu wa Benki Kuu (BoT), Ally Bakari, katika kesi ya kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 104.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Oktoba 23, 2009

MAHAKAMA YADANGANYWA

*Wadhamini wawasilisha hati bandia
*Walitaka kuwadhamini vigogo BoT
*Washtukiwa na kusekwa mahabusu

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, jana iliamuru wadhamini watatu waliojitokeza kumdhamini mshtakiwa wa nne katika kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 104 inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Ally Bakari wakamatwe baada ya kupatikana kwa taarifa kuwa hati walizotumia kumdhamini mshtakiwa ni za kughushi.


Amri hiyo ilitolewa jana mchana na Msajili namba mbili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Lameck Mlacha, baada ya kukubaliana na maombi ya Wakili wa Serikali, Ephery Fredrick na Proper Mwangamila, waliotoa taarifa za kutolewa kwa hati hizo bandia na wadhamini.

Mawakili hao katika madai yao, waliitaka mahakama isikubali taarifa hizo za udhamini na zisitumike kumdhamini mshitakiwa huyo.

Wadhamini walioamuriwa kukamatwa ambao waliwasilisha hati hizo za dhamana, ni David Majedele, Felix Musa Nyuki na Hamad Juma. Hata hivyo mdhamini wa tatu alitoweka katika mazingira ya kutatanisha hivyo kufanya walioshikiliwa na polisi kubaki wawili.

Hakimu Mlacha alisema, anakubaliana na ombi hilo kwa sababu hati hiyo ya udhamini inaonyesha ilipitia kwa Mthamini Mkuu wa Serikali, kitu kilichodaiwa na mawakili wa upande wa mashitaka kuwa si kweli.

Walieleza kuwa, wanazo taarifa kuwa Mthamini Mkuu wa Serikali hajawahi kutoa hati hizo jambo linaloonyesha kuwa zimeghushiwa.

Tukio hilo lilitokea wakati kesi hiyo ilipokuwa mahakamani jana kwa ajili ya kutimiza masharti ya dhamana.

Majedele aliwasilisha hati na mali namba 105046 kitalu 247 block E Mbezi na taarifa ya uthamini ilikuwa inaonyesha kuwa ina thamani ya sh 369,679,950 wakati upande wa mashitaka ulibaini hati hiyo ilishawahi kupotea na kuripotiwa polisi ambapo ilitangazwa katika gazeti la Daily News la Oktoba 30 na ikatangazwa pia katika gazeti la serikali la Oktoba 24 mwaka jana.

Baada ya kupotea, Majedele alidaiwa kuomba hati mpya ambayo ilionyesha kutolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani, Desemba 10, mwaka jana.
Ilidaiwa mahakamani hapo, hati aliyowasilisha haitambuliwi na serikali na badala yake inayotambuliwa ni hati mpya aliyoomba.

Kwa upande wa Nyuki, aliwasilisha hati ya mali namba 76918 kitalu 74 Gerezani ikionyesha kuwa na thamani ya sh 587,820,000.

Mdhamini wa tatu (Juma) yeye aliwasilisha hati namba 107622 kitalu 40 eneo la Gerezani na jengo lenye thamani ya sh 549,600,000.

Hati zote ziliambatanishwa na taarifa ya Mthamini Mkuu wa Serikali.Lakini baada ya upande wa mashitaka kwenda kuzihakiki katika ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali ilibainika kuwa hazijawahi kutolewa na serikali.

Vyanzo vya kuaminika kutoka serikalini vilidai kuwa, wadhamini hao wanatarajiwa kufikishwa kizimbani leo kwa makosa ya kughushi.

Mbali na Mkonga katika kesi hiyo inayowakabili vigogo hao wa BoT, washitakiwa wengine ni Simon Jengo na Naibu Mkurugenzi Fedha za Nje, Kisima Mkango, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Bosco Kimela pamoja na Mkurugenzi wa masuala ya kibenki, Ally Bakari.

Katika kesi hiyo, washitakiwa wanadaiwa kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2004 na 2007, kuisababishia serikali hasara hiyo kwa kudanganya miongozo kwa kuongeza gharama za uchapishaji wa fedha za noti ikilinganishwa na gharama halisi.
Kesi hiyo ya msingi inasikilizwa katika mahakama ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Oktoba 21, 2009

MWALIMU NYERERE NATAMANI UONE TUNAVYOKUENZI-(3)


Na Happiness Katabazi

BABA wa Taifa letu la Tanzania, Julius Nyerere, kwa mara nyingine nachukua kalamu kuandika kumbukizi yako. Oktoba 14 mwaka huu, ulitimiza miaka 10 tangu Mwenyezi Mungu alipokuita nawe ukaitika.


Tunazidi kukukumbuka baba japo mwili wako umelala mavumbini kule Mwintongo-Butiama, mkoani Mara.

Ni ajabu na kweli kwamba mawazo yako, falsafa na fikra zako zinaendelea kuishi miongoni mwetu.

Baba wanao tulio hai hadi sasa tunaamini kabisa hautasaulika kamwe.
Tunakukukumbuka baba kila tunaposikiliza na au kuzisoma hotuba zako. Bado zina utamu ule ule na uzito ule ule usiochuja siku hadi siku.

Wosia wako uliukita katika mtindo wako wa maisha binafsi, uongozi wako uliotukuka, matamshi na matendo yako. Miongoni mwa mambo uliyotuusia yanahusu elimu.
Ulipenda watu wote wapate elimu na ukatuambia kila apataye elimu afanye nini.

Baba, uliwahi kutuambia kwamba; aliyepata bahati ya kusoma na akapata elimu ni kama mtu ambaye kijiji kimempa chakula chote kilichopo ili ale ashibe, avuke ng’ambo akakiletee kijiji chote chakula , na asipofanya hivyo akajenga kiburi ni sawa na msaliti, tunakuenzi kwa hilo.

Tunakuenzi kuanzia katika suala la elimu, ambalo ulibobea katika hilo ukiwa mwalimu na mwanafalsafa.

Ulitufundisha falsafa ya elimu ya kujitegemea, uliyoiasisi mwenyewe; ulituusia kwamba elimu itujengee akili za udadisi.
Leo tunakuenzi baba kwa kupuuza kuwa wadadisi na wabunifu.

Shuleni tunasoma kwa kukariri ili tufaulu mitihani. Baba, hata udadisi wa kisiasa umepigwa marufuku katika taasisi za elimu ya juu, ili tuwe mbumbumbu, mazumbukuku, mzungu wa reli, wasioweza kuhoji lolote.

Usiwe na wasiwasi baba, viranja wanaimudu kazi hiyo vizuri sana, hii ni katika kuhakikisha tunaienzi vyema taaluma yako ya ualimu kwa kuifanya si taaluma tena, bali kichwa cha mwenda wazimu ambacho hata asiyejua kushika wembe anaweza kukinyoa, kwani baba, lazima mtu ajue kusoma ndiyo awe mwalimu?

Tunakuenzi baba kwa kuendelea kusoma tukiwa watu wazima na katika siku zote za maisha yetu. Chungulia baba uone jinsi wengi wetu walivyofanikiwa kusoma ukubwani na kujipatia shahada za juu kabisa.

Tangu uondoke baba idadi ya wanao wenye shahada za falsafa (PhD) imeongezeka kwa kasi. Usishangae baba tumewezaje hilo, siku hizi kuna shahada tunazipata kiurahisi kwenye mtandao. Wenyewe baba wanaziita za ‘on line’.

Kwahiyo tunakuenzi kwa kurahisisha mambo, tunatafuta wenzetu wenye uwezo kichwani tunawapa visenti kidogo wanatufanyia ‘assignments’ na kutuandikia thesis, tunawasilisha kwenye vyuo vya ughaibuni, kisha kufumba na kufumbua tunaitwa ‘madokta’. Hicho cheo tunakitumia vilivyo kukuenzi katika siasa, maana kitaaluma hatuwezi kukitumia, samahani baba hatuna ujuzi wowote katika nyanja za shahada tunazotunukiwa.

Kukuenzi kwetu hakuishii hapo baba. Si unakumbuka ulituachia vyuo vikuu. Tumekuenzi si tu kwa kuviboresha bali tumeongeza na vingine vingi. Kwa sasa tunavyo visivyopungua thelathini (30). Zaidi tumekuenzi kwa kuongeza kwa kiasi kikubwa udahili katika vyuo hivyo.

Tunaendelea, maana kupata mwongozo wa mambo mbalimbali kutoka katika wosia wako.

Utakumbuka baba kwamba kila baada ya miaka mitano kwa mujibu wa utaratibu ulioshiriki kuasisi, kunakuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa hatimaye rais,wabunge na madiwani.

Tunakuenzi baba kwa kuzingatia sifa uliotuhusia za viongozi wanaofaa.
Ulituasa baba tuepuke kuchagua viongozi kwa kigezo cha fedha.

Tupo tunaolizingatia hilo, lakini wapo wanao watukutu walioamua kukuenzi kwa kufanya kinyume kwa kuzidisha matumizi ya fedha chafu nyakati za chaguzi hizo.

Baba tunaadhimisha miaka 10 ya kuondoka kwako kwa taarifa kutoka kwa wanao wanaojihusisha na utafiti kwamba kwa sasa hivi gharama za kugombea na kufanya kampeni za urais ni mabilioni ya fedha.

Ilhali za kufanya kampeni za ubunge na udiwani wenyeviti wa serikali za mitaa ni mamilioni ya fedha.

Ni wazi baba tumeamua kukuenzi kwa kuzifanya nafasi zote za uongozi wa siasa kuwa mali ya kudumu kwa wenye fedha na jamaa zao.

Utusamehe baba kwakuwa tumepuuza wosia wako kwamba Ikulu ni mahala patakatifu na uongozi ni kazi takatifu na haipaswi kukimbiliwa kwa kutumia fedha, maana hakuna biashara huko.

Uliuliza anaye tumia fedha kupata uongozi kazipata wapi? kama kakopa atazilipaje. Baba tumeishaanza kujua vyanzo vya fedha za hawa wanao watukutu ambao hivi sasa tunawaita ‘mafisadi’.

Tunakukumbuka ulivyotunusuru kwa kukata mirija ya wanyonyaji ‘weupe’waliowahi kuivamia nchi yetu hivi sasa tunao wanyonyaji ‘weusi’ wanaojitahidi kunyonya kila palipokuwa na rasilimali ya nchi hii, kila palipo na hazina ya taifa na kila palipo na chenye thamani na wanafanya hivyo bila haya na wanalindwa na sheria za dola.

Tunakusihi uzidi kutuombea kama ulivyotuaidi ili kwa kudra za Mwenyezi Mungu tunusurike kwenye mirija hii ya watu weusi ambao wamekubuhu kwa ufisadi.

Utuombee tufunuliwe na kuwatambua mafisadi ili kwenye uchaguzi tuweze kuwanyima kura kwa lengo la kuwazuia kakalia uongozi.

Vile vile baba tunaendelea kukuenzi kwa urithi wa aina pekee uliyotuachia ambao si mwingine ila Muungano uliozaa Tanzania.

Baba tunasema ni urithi wa kipekee kwa sababu mataifa mengi duniani yamejaribu kuungana lakini yalishindwa.

Yale yaliyoungana tunashuhudia yakisambaratika lakini sisi wanao tunakuenzi kwa kuudumisha muungano hadi leo.

Baba ulituasa tuudumishe muungano huu kwa kuziona nyufa kila zinapojitokeza na kuziziba, bahati mbaya wapo wanao wamemua kukuenzi kwa kuuchokonoa nyufa kwenye ukuta wa muungano mara kwa mara.

Katika siku za karibuni baba kumekuwa na chokochoko zinazohusiana na suala la kupatikana mafuta katika upande mmoja wa Muungano.

Ni ajabu kwamba wapo wanaokuenzi kwa kuleta chokochoko ati suala la mafuta ni la upande mmoja tu.

Utuombee ili wanao wote wenye mawazo ya kutumia rasilimali za nchi hii kuvunja Muungano, washindwe na walegee.

Siku za nyuma kidogo wapo wengine waliuchokonoa Muungano kwa kuzua hoja ya Zanzibar ni nchi, wengine wakasema si nchi na wengine walifikia hatua ya kumuambia mwano mmoja ambaye amerithi cheo chako cha kwanza cha uongozi cha (uwaziri mkuu), Mizengo Pinda, akapimwe akili. Eti kosa lake ni kukuenzi wewe kwakusema Tanzania ni nchi moja. Tunashukuru hilo lilipita salama bila madhara makubwa zaidi.

Baba mwaka huu, tunakuenzi katika kukumbuka miaka 30 tangu kumalizika kwa Vita ya Kagera.

Tumekuenzi kwa kukumbuka ushindi tulioupata dhidi ya majeshi ya nduli Idd Amin.
Tunakuenzi baba kwa kutambua kwamba kimsingi kuzuka kwa vita hiyo hakukuwa na maana ya uadui kati ya Watanzania na Waganda.

Tunazidi kupendana na majirani zetu hawa, zaidi ya hayo, baba hata mtoto wa marehemu Idd Amin, amekuenzi kwa kuzuru kaburi lako na kuzungumza kindugu na familia yako iliyopo Butiama.

Tunaendelea kukuenzi kwa kukidumisha chama cha siasa ulichokiasisi, chama ulichokijengea misingi ya kipekee iliyotukuka, cha ajabu wapo wanaokuenzi kwa kuimomonyoa vilivyo misingi ya chama hicho.

Hivi karibuni baadhi ya wanachama waandamizi waliwaziba midomo wanachama wenzao wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) kilichofanyika Dodoma.

Baba walizibwa midomo wasikemee maovu na wanazibwa midomo wasiwasakame wanaoliibia taifa, wanaopotoka kimaadili, wamezibwa midomo wasihoji wala kutoa ukali dhidi ya wanaopindisha miiko na kanuni za chama hicho! Hakika baba huku ni kukuenzi kwa aina yake.Hakika baba taifa lina kuenzi kwa staili za aina mbalimbali.

Stahili ya kupotoka kimaadili nayo imetia fora. Usishangae baba kusikia hayo, kwani hata sisi hatukutarajia kwamba tutafika mahali tukuenzi kwa kuwatandika vibao, warithi wa nafasi yako kuu ya uongozi.

Eti kwa sababu wako mstari wa mbele kupambana na gonjwa la ukimwi katika misingi inayozingatia uhalisia. Baba wanao wanakuenzi kwa vitendo vilivyo kithiri vya kujichukulia sheria mkononi ikiambatana na utovu wa nidhamu.

Hatukutarajia baba kukuenzi kwa kupopoa kwa mawe msafara wa mrithi wako mwingine, Rais Jakaya Kikwete, ati kwasababu msafara wake ulichelewa kufika na kuongea na wananchi wa mkoa wa Mbeya.

Tunakuenzi baba kwa kuimarisha ulinzi wa nchi kiasi kwamba hata baadhi ya silaha ulizotuachia bado zipo kwenye maghala yetu.

Sitalaumu baba sisi si wazembe sana, japo Aprili 29 mwaka huu, zililipuka na kuyakatisha maisha ya baadhi ya watu huku wengine wakiharibiwa mali zao.

Kadhalika Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), nalo mwaka huu, limekuenzi kwa kuadhimisha miaka 45 tangu kuanzishwa kwake, kwa namna ya kipekee kabisa, maadhimisho yaliyoambatana na maonyesho ya zana mbalimbali za kivita.

Utuombee tuweze kukuenzi kuzingatia falsafa yako ya kujitegemea kupitia uzalishaji wa wingi wa magari ya kizalendo aina ya ‘Nyumbu’. Baba utuombee ili siku moja tukuenzi kwa kutumia magari hayo hata kwa viongozi wetu ambao wanakuenzi kwa njia iliyopotoka, kwa kutumia magari ya kifahari huku wananchi wanaowaongoza ni maskini.

Baba nikudokeze kwamba mwanao mmoja mwaka huu, amekuenzi kwa kubadili magari Ikulu, hautumii tena Benz au Land Rover kama wewe, kanunua mabima (BMW) ya kifahari kutumika katika shughuli mbalimbali, ikiwamo Ikulu, mahali ulipotuambia ni patakatifu.

Baba tumekuenzi kwa kukodisha lililokuwa Shirika la Reli (TRC). Samahani mwekezaji tuliyemkodishia hana fedha kiasi kwamba kila siku anakwenda serikalini kulialia asaidiwe kuwalipa mishahara wafanyakazi.

Baba, nitakuwa natenda dhambi kama sitakueleza hili kwamba uendelee kumuombea mkuu wetu wa Kaya, Rais Jakaya Kikwete, aendelee na moyo wake wa uongozi, aendelee kuruhusu uhuru wa watu kutoa maoni, kwani katika hili binafsi nampongeza.

Huko uliko baba, uendelee kumuombea kwa Mungu ili asibadilishe msimamo wake wa kuturuhusu sisi wananchi wake kutoa maoni.

Katika hili, baba nampongeza Kikwete kwani hivi sasa baba ni ruksa kuikosoa serikali na viongozi wake, licha ya kwamba kuna baadhi ya watendaji wake wanakosa uvumilivu.
Tunakuenzi baba kwa kudumisha demokrasia ya vyama vingi.

Na utakumbuka ulishauri vyama vingi viwepo lakini visiwe utitiri kiasi cha kukosa maana kwa jamii.

Utuwie radhi baba, kwani kadiri muda unavyozidi kwenda, vyama vingi vilivyoanzishwa nchini vinazidi kuwa dhaifu.

Sababu za udhaifu ni nyingi, ikiwamo kuhama hama kwa vijana wako walioamua kukuenzi kwa kuendekeza uchu wa madaraka na ubinafsi.

Leo hii wakikosa madaraka hapa, kesho wakikosa ruzuku pale, wanaamua kukimbilia kwingine.

Kwa upande mwingine baba, wapo wanaandishi wa habari wenzetu wasomi, tena ni wasomi sana, ambao kwa makusudi wameamua kujigeuza ‘matambala ya deki’ ya wanasiasa manyang’au, ambao wanabaka uchumi wa taifa kwa kuwaandikia habari na makala za kuwasafisha ili jamii iwaone ni wanasiasa wema.

Aidha, baba tunakuenzi kwa mifumuko ya migomo na maandamano ya kila kukicha. Hata Oktoba 14 mwaka jana, pale Diamond Jubilee walimu walifanya vurugu na kumpiga rais wa chama chao kwa meza, viti, mawe na siku iliyofuata wakagoma kufundisha karibu nchi nzima kuishinikiza serikali iwalipe haki zao.

Lakini baba pia tunakuenzi kwani taifa lako uliloliasisi limeweza kupiga hatua za kimaendeleo katika sekta ya afya, miundombinu, teknolojia, afya na jitihada zaidi za kuliletea maendeleo taifa zinaendelea licha ya watoto wako baadhi ambao ni watukutu wanajaribu kurudisha nyuma jitihada hizo kwa kuendekeza kutafuna rasilimali za umma.

Tuombee baba, ili mfumo wa elimu yetu ukuenzi, mfumo wa uchumi wetu nao ukuenzi na mfumo wa siasa ukuenzi pia.Kadhalika viongozi wetu wakuenzi kwa maneno yao, mawazo yao na matendo yao.

Baba, viongozi wetu inabidi wakumbuke maneno ya Yesu Kristo aliyowaambia watu wa taifa la Uyahudi, kwamba “Hamjui kuwa mnaye baba mwingine, ninyi si watoto wa Ibrahim, ninyi ni watoto wa ibilisi, kwa kuwa ibilisi amekuwa mwongo na mnafiki tangu mwanzo, nanyi mnayatenda hayo hayo kama baba yenu”.

Sasa baba , wanao tunapojivunia ubaba wako, baadhi yetu wanaye baba mwingine ambaye si wewe!

Baba yao ni ibilisi ‘fisadi’, ndiye wanayempenda, kumsikiliza, kumuenzi na kumtumikia.Hata leo hii,angali akinyonya kwakutumia utandawazi, ubinafsishaji na kuendekeza masilahi binafsi.

Viongozi wetu wa leo mnamuenzi baba yupi? Baba Mungu alikuumba na ukiisha kuifanya kazi yake hapa kwetu, akakutwaa. Jina la Bwana lihimidiwe na aipumzishe roho yako mahali pema peponi. Amina.

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Oktoba 18,2009

MGAO WA UMEME SASA WAIVURUGA KESI YA SAMAKI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi katika kesi ya uvuvi haramu, inayowakabili raia 37 wa kigeni waliokamatwa kwenye meli ya Tawariq 1.


Ombi hilo lilitaka mahakama isipokee ombi la upande wa mashitaka la kutaka ifanye mapitio ya amri yake ya awali ya kutaka uuze samaki hao haraka kwa kuzingatia sheria ya manunuzi ya kimataifa kwa madai kuwa taifa linakabiliwa na mgawo wa umeme, hivyo wanaweza kuharibika.

Akitoa uamuzi huo, Jaji Radhia Sheikh alisema anapokea ombi hilo la upande wa mashitika la kutaka kufanyia mapitio kwa amri aliyoitoa Oktoba mosi mwaka huu, kwamba uuzaji wa samaki hao, ufuate sheria ya manunuzi ya kimataifa.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Jumatatu ambapo itakuja kwa ajili ya kusikilizwa maombi ya msingi ya upande wa mashitaka, yanayotaka masharti ya uuzwaji wa samaki hao yapitiwe upya kuhofia kuharibika kutokana na kuwapo mgawo wa umeme.

Kwa mujibu wa hati ombi hilo, inaonyesha Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP)Eliezer Feleshi alimwandikia barua Katibu Mkuu wa Wiraza ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi,C.Nyamrunda ambayo alikuwa akimwalifu Katibu huyo amri iliyotolewa na Jaji Sheikh, Oktoba mosi mwaka huu, ya kuuza tani 296.3 za samaki baada baada ya kukubali ombi la upande wa mashitaka ambalo halikupingwa na upande wa utetezi.Na katika utekelezaji wa amri hiyo mahakama hiyo imeelekeza samaki wauzwe haraka.

Aidha Oktoba 6,mwaka huu, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo aliandika barua kwa Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,nakala kwa DDP na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, inasomeka hivi :Wizara ya Mifugo na Uvuvi iko tayari kutekeleza agizo la mahakama kwa haraka na kwa umakini kadri itakavyowezekana kwa manufaa ya taifa.Hata hivyo inaona kuna ugumu wa utekelezaji wa agizo linaposema samaki hao wauzwe kwa zabuni ya kimataifa.

“Ugumu huo unatokana na ukweli kwamba sheria ya Manunuzi Na.21 ya 2004 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2005 zinaelekeza ununuzi na uuzwaji wa mali za umma ufanyike kwa kuzingatia jedwali Na.3 ambalo linasema utangazaji ufanywe kwa siku 45 kwa zabuni ya kimataifa na kwa zabuni ya taifa hili ni siki 30.Tunaona muda wa kutangaza ni mrefu sana kwani bidhaa hii ina asili ya kuharibika mapema na pia samaki husika baada ya kupakuliwa kwenye meli wamekwisha hifadhiwa kwenye majokofu kwa takribani siki 207 hadi hivyo wapo ukingoni wa kuisha thamani yake.

“Baadhi ya matatizo makubwa yanoyotukabili hadi sasa kuhusu samaki hao ni gharama kubwa ya kuifadhi ambapo zinalipwa takribani sh milioni 103-104 kwa mwezi .Pia tunakabiliwa na tatizo la kuendelea kupungua kwa thamani na kuzimika kwa umeme mara kwa mara na sasa hivi jambo ambalo linapelekea athari ya kudorora zaidi kwa thamani ya samaki hao au hata kuaribika kabisa.

“Kwa maelezo haya tunashauri utaratibu wa uuzaji samaki hao ubadilishwe ili waezwe kwa njia iliyo rahisi zaidi kwa kutumia muda mfupi bila kuvunja taratibu na sheria ya ununuzi.”ilisomea barua hiyo.

Washitakiwa hao, wanakabiliwa na mashitaka mawili la kuvua samaki bila leseni na kuvua kwenye kina kirefu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume na sheria ya uvuvi wa samaki ya mwaka 2009.

Ilidaiwa kuwa, Machi 8, mwaka huu, washitakiwa wote kwa pamoja, majira ya saa sita usiku katika ukanda wa Bahari ya Hindi, ndani ya eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walikamatwa wakivua samaki bila leseni.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Oktoba 17, 2009

MBARONI KWA KUKUTWA NA NOTI BANDIA

Na Happiness Katabazi

WATU wawili akiwemo mwanamke jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakikabiliwa na tuhuma za kukutwa na noti bandia za mataifa mbalimbali kinyume na taratibu.


Mbele ya Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana,Wakili wa Serikali, Mutalemwa Kishenyi, aliwataja washtakiwa hao kuwa ni Maina John (40), raia wa Kenya na Nuru Swalehe (31) ambao ni wafanyabiashara.

Akiwasomea mashtaka hayo, alidai kuwa Oktoba 9, mwaka huu, saa 9.00 alasiri, eneo la Kinondoni, walikamatwa na ofisa wa polisi Lugano, wakiwa na noti bandia za mataifa mbalimbali.

Kishenyi alidai walikutwa na euro mia 11300; euro miatano 41000; euro hamsini 3900; dola mia 1,408; na pauni hamsini 252.

Washtakiwa hao walikana tuhuma hizo na upande wa mashtaka ulipinga dhamana kwa washtakiwa hao kwa maelezo kuwa John ni raia wa kigeni na kwamba alipokamatwa alikutwa na hati mbili za kusafiria, hivyo akiachiwa kwa dhamana anaweza kutoroka.

Pia, waliiomba mahakama hiyo, iwapo itatoa dhamana kwa washtakiwa itumie kifungu cha 148(5)(e) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, ambapo kinataka mshtakiwa kutoa nusu ya fedha anayodaiwa kuiba, kama dhamana.

Hata hivyo, wakili wa utetezi, Frank Malongo, aliiomba mahakama hiyo kuwapatia wateja wake dhamana, na kupinga sababu za upande wa mashtaka. Kesi hiyo itatajwa Jumatatu, kwa uamuzi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Oktoba 17, 2009

HAPPINESS VS MAPAPARAZI WENZAKE



Kulia ni mimi na kushoto ni mwandishi mwenzangu wa habari za mahakamani nchini toka Televisheni ya ITV, Salum Makambara, tukimsikiliza kwa makini Jaji Mkuu Agustino Ramadhani, hayupo pichani, leo mchana wakati akizungumza na watumishi wa mahakama mkoa wa Dar es Salaam, katika ukumbi namba moja wa Mahakama Kuu.(Picha imepigwa Oktoba 13, 2009)

JAJI MKUU 'AWATULIZA' WATUMISHI WA MAHAKAMA

Na Happiness Katabazi

JAJI Mkuu wa Tanzania, Agustino Ramadhani amewataka watumishi wa Mahakama kumpa ushirikiano katika kipindi hiki anacho hakikisha watumishi wote wa mhimili huo, wanaboreshwa maslahi yao kwa kufuata msingi wa sheria.


Jaji Ramadhani alitoa wito huo alipozungumza na watumishi wa Mahakama za Mkoa wa Dar es Salaam, uliofanyika katika moja ya kumbi za Mahakama Kuu na kusema amelazimika kufanya hivyo kutokana na habari za mgomo unaokusudiwa kufanywa na watumishi wa mahakama za Iringa.

Katika habari hizo, imedaiwa kwamba, watumishi hao wameipa serikali siku 60 ili kuboreshea maslahi zao vinginevyo watagoma na kutaka ongezeko la bajeti ya mahakama.

“Kwanza ni kweli mishahara ya majaji na mahakimu imeongezeka tena kwa kiasi kikubwa…alhamdulah ila makarani, madereva na watumishi wengine wa mhimili huu, wamepandishiwa kidogo kuanzia Julai mwaka huu.

…Uongozi wa mahakama unaendelea na jitihada za kudai maslahi kwa ajili ya kndi hilo la watumishi nalo liangukiwe na rehema hiyo.

Nitakwenda Iringa muda wowote kuanzia sasa kwani huko ndipo kwenye chimbuko la habari hiyo ili nikajiridhishe kama ni kweli wale watumishi 60 waliweka saini kwenye ule waraka wao. Kama ni kweli ni watumishi wetu na ninaahidi sijawachukulia hatua kwani binafsi naifahamu fika njaa iliyopo kwenye mhimili huu wa mahakama,” alisema Jaji Mkuu Ramadhani.

Jaji Ramadhani ambaye aliongozana na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Francis Mutungi, alisema chanzo cha majaji na mahakimu kupandishwa mishahara kimetokana na mapendekezo yaliyowasilishwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kuwa chombo hicho kinashughulikia ajira, upandishwaji vyeo na maslahi ya mahakimu na majaji pekee.

“Kiongozi wa chombo hicho ni Jaji Mkuu na ndicho chombo kilichopeleka mapendekezo ya ongezeko la mishahara kwa majaji na mahakimu na mishahara ikapandishwa na ninawataka mfahamu chombo hicho kimeundwa na Katiba ya nchi na kazi zake zimeainishwa katika Katiba.

Sasa ili chombo hiki kiweze kushughulikia mishahara na kupandisha vyeo watumishi wengine wa mahakama, ni lazima Katiba ya nchi ibadilishwe na ikibadilishwa ndiyo itaweza kuwahusisha watumishi wote wa Mahakama.

…Hivyo naomba tuvute subira mabadiliko yatatokea. Mimi ni miaka miwili tangu niteuliwe kuwa Jaji Mkuu na hayo mabadiliko ya mishahara kwa mahakimu na majaji ni makubwa katika kipindi kifupi tu tangu nishike wadhifa huu. Naitaji nguvu toka kwenu ili niweze kusikilizwa katika sehemu husika,” alisema Jaji Mkuu kwa unyenyekevu.

“Nipeni muda ili tuweze kufanikisha madai yenu kwani majaji na mahakimu peke yao hawawezi kutoa huduma katika mahakama…siwafichi, nawaambia ukweli kwamba nafanya kile kiloiho ndani ya uwezo wangu kwani mimi sio Bunge la kubadilisha Katiba. Tume ya Utumishi wa Mahakama nimeikuta, sijaiunda mimi,” alisema.

Akizungumzia kuhusu bajeti ya mahakama alisema bado ni ndogo ukilinganisha na mihimili mingine na kwamba uongozi wa mahakama unaendelea kupambana ili uweze kupata bajeti itakayotosheleza mahakama ambazo katika mikoa yote 21 ya nchi.

Wiki mbili zilizopita moja ya gazeti la kila siku (Sio Tanzania Daima), lilishapisha habari iliyosema watumishi wa mahakama ambao si majaji wala mahakimu, mkoani Iringa wametoa siku 60 kwa serikali kuboreshewa maslahi na mishahara yao vinginevyo wangegoma kushinikiza maboresho hayo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Oktoba 14,2009

OMBI LA MASHTAKA LATUPWA KESI YA EPA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana ilitupilia mbali ombi la upande wa mashtaka lililoitaka mahakama hiyo iliwaruhusu wachukue kielelezo cha kesi ya wizi wa sh milioni 207 katika Benki Kuu, liende kwa matumizi mengine ya serikali, kwa kuwa halina msingi kisheria.


Uamuzi huo ulitolewa na Jopo la mahakimu wakazi, John Utamwa na Eva Nkya, ambapo walisema ombi la mashtaka, lililowasilishwa na Mwanasheria wa Serikali, Timon Vitalis, halikuzingatia matakwa ya kifungu cha 353 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 ambacho kinaitaka Mahakama kuondokana na kielelezo baada ya kesi kuisha.

“Kwa kuwa ombi la upande wa mashtaka halikuzingatia matakwa ya kifungu hicho na badala yake, ikaamua kuegemea kwenye ombi la kutaka mahakama iwapatie kielelezo hicho ili kitunzwe na BoT…jopo hili limeona ombi hilo halijazingatia matakwa ya kifungu ambacho kinaitaka mahakama kuondokana na kielelezo na sio utunzwaji wa kielelezo,” alisema Utamwa.

Wiki mbili zilizopita Vitalis, aliwasilisha ombi hilo la kutaka mahakama iwapatie kielelezo halisi ili wakitunze, badala yake upande wa mashtaka uwasilishe kielelezo kivuli ombi ambalo lilipingwa vikali na mawakili wa utetezi ambao ni Mabere Marando, Majura Magafu na Mpare Mpoki.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 16 mwaka huu, itakapotajwa. Washtakiwa katika kesi hiyo ni Rajabu Maranda na Farijara Hussein ambao ni wafanyabiashara na Ester Komu, Iman Mwakosya na Bosco Kimela ambao ni maofisa wa BoT.

Wakati huo huo: Hakimu Mkazi Edson Mkasimwonga jana aliahirisha kesi ya wizi wa sh bilioni sita za Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu, inayowakabili ndugu wawili, Johnson na Mwesiga Lukaza, kwa kuwa idadi ya jopo la mahakimu kutotimia.

Hakimu Mkasimwongo alisema kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali. kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 13 mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Oktoba 14,2009

HAPPINESS NA ZOMBE



Nikifanya mahojiano na aliyekuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe(55),kwa mara ya kwanza tangu yeye na washitakiwa wenzake nane washinde kesi ya mauji ya wafanyabiashara wa tatu na dereva teksi mmoja iliyokuwa ikiendeshwa katika Mahakama Kuu Kanda.Hapo ni nyumbani kwa Zombe, Mtoni Kijichi.(Picha hii ilipigwa Jumamosi Oktoba 3,2009)

HAPPINESS NA JAJI WARIOBA




Nikiwa na Jaji Joseph Warioba,ofisini kwake Masaki Jijini Dar es Salaam,ambapo siku hiyo alizungumza na waandishi wa habari kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu mustakabali wa tiafa.(Picha ilipigwa Jumanne,Septemba 23,2009)

MRAMBA AITEGA SERIKALI

*Sasa agoma kutaja orodha ya mashahidi wake
*Mjadala mzito waibuka, Mahakama kuamua leo


Na Happiness Katabazi

UPANDE wa utetezi katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi za umma na kuisababishia hasara serikali ya sh bilioni 11.9, inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake wawili, umekataa kutaja orodha ya mashahidi wake.


Msimamo huo mkali ulitolewa jana na jopo la mawakili wa upande huo, linaloongozwa na Hurbet Nyange, Peter Swai, Profesa Leonard Shahidi pamoja na Cuthbert Tenga, mbele ya jopo la Mahakimu Wakazi wanaosikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, John Utamwa, Sam Rumanyika na Saul Kinemela.

Awali kabla ya mawakili hao kuanza kuwasilisha pingamizi hilo, Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface akiwa na Fredrick Manyanda, waliikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kuona upande wa utetezi umebaini nini katika Waraka Na. 2, wa Jaji Mkuu wa mwaka 1999, ya Sheria za Mwenendo wa Makosa ya Jinai na Sheria ya Mahakama za Mahakimu Wakazi ili kujibu ombi la upande wa mashitaka lililowataka wataje orodha ya mashahidi wao.

Akijibu hoja hiyo wakili wa Mramba, Nyange aliieleza mahakama kuwa kwa niaba ya mteja wake, msimamo alioutoa juzi bado haujabadilika wa kukataa kutaja orodha ya mashahidi.

“Vile vile leo (jana) napenda kuongezea nguvu msimamo wangu kwa vifungu vya sheria na kwa ufasaha kabisa tunaheshimu nafasi ya Jaji Mkuu kutoa miongozo ya kisheria kuhusiana na miendeno ya kesi mahakamani.

“Pamoja na hayo kwa niaba na kwa nafasi niliyonayo kama wakili, pia ofisa wa mahakama nipo hapa kuisaidia mahakama kufikia maamuzi sahihi ya kisheria na si vinginevyo, hivyo napinga ombi la upande wa mashitaka la kutaja orodha ya mashahidi,” alidai Nyange.

Nyange ambaye alikuwa akiwasilisha hoja hizo kwa tahadhari kubwa, alieleza kuwa kutokana na barua yenye kumbukumbu namba JWC/C40/8/135 ya Mei tano mwaka 1996 na Waraka namba mbili wa Jaji Mkuu wa mwaka huo, na kupitia kwa makini ukurasa wa mwisho, aligundua mapungufu yakiwemo ya sahihi ya Jaji Mkuu, marehemu Francis Nyalali na kuongeza kuwa ana shaka kama barua hiyo iliandikwa na Jaji huyo.

Wakili huyo aliendelea kudai kuwa mahakama itakuwa imekiuka sheria endapo itatumia taratibu nyingine ambazo hazijaainishwa kwenye kifungu cha sita cha Judicatural Application of Law, sura ya 128(JALA), ambapo kifungu hiki kinaeleza Mahakama Kuu inapaswa kufuata sheria zilizoandikwa na kutangazwa kwenye gazeti la serikali, nguvu zilizowekwa katika mahakama, vitabu mbalimbali vya sheria hivyo mahakama ya hakimu Mkazi inapaswa kufuata kifungu hicho.

Nyange aliendelea kuchambua sheria kwamba kifungu cha 192(6), cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, inampa Waziri wa Sheria kutunga sheria kwa kushirikiana na Jaji Mkuu, kisha itangazwe kwenye gazeti la serikali, pia hana pingamizi juu ya kifungu cha 71(1), cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu Wakazi, kinachoeleza Jaji Mkuu ana uwezo wa kutengeza utaratibu na kutoa maelekezo ya jinsi mahakama wakati zitakavyoendesha kesi.

“Kwa hiyo kwa heshima na taadhima tunatamka kuwa waraka wa Jaji Mkuu sio sheria na endapo mahakama hii itauona kuwa ni sheria basi waraka huo ulitengenezwa kinyume na kifungu cha 192(6), na auendani kabisa na matakwa ya kifungu chenyewe,” alidai Nyange.

Aidha alidai, muda ambao mshitakiwa anatakiwa kutaja mashahidi wake ni baada ya upande wa mashitaka kufunga kesi yake na mahakama ikamwona mshitakiwa ana kesi ya kujibu, hapo ndipo mahakama inawajibu wa kumuuliza mshitakiwa kama ana mashahidi, endapo atakuwa nao atatakiwa kujata orodha ya mashahidi wake.

“Maelekezo ya Jaji Mkuu na waraka wake huo unapingana na kifungu cha 231 (4), cha Sheria ya Makosa ya Jinai, ambayo ndiyo sheria mama ya makosa hayo, kwani kifungu hicho kinataja wazi muda wa mshitakiwa kutaja orodha ya mashahidi wake,” alidai Nyange na kusababisha watu wanaoudhuria kesi hiyo kuangua vicheko mara kwa mara.

Wakili huyo alidai kesi inayomkabili mteja wake (Mramba) ni mpya nchini ambapo kwa lugha ya Kiswahili inaitwa (kesi za ufisadi) na kama mteja wake atalazimishwa na mahakama kutaja orodha ya mashahidi hadharani, atakuwa hajatendewa haki,”

Katika kuiunga mkono hoja hiyo wakili wa mshitakiwa wa pili (Yona), Cuthbert Tenga, alikubali hoja hiyo iliwasilishwa na wakili mwezake Nyage, ambapo pia aliupinga vikali Waraka wa Jaji Mkuu kwa kufafanua kuwa, ulitolewa kwa shughuli za kiutalawa katika mahakama na posho za mashahidi hivyo waraka huo hauna kitu kipya.

“Nasema waraka wa Jaji Mkuu ulitolewa kwa ajili ya utawala na posho za mashahidi wanaofika mahakamani kutoa ushahidi, hata ulipotengenezwa alipewa IGP na Mwendesha Mashitaka wa Serikali kutokana na taasisi hizi mbili kuhusika kikamilifu katika kesi za jinai mahakamani, hivyo ieleweke wazi waraka wa Jaji Mkuu upo kwa ajili ya posho za mashahidi. ”alidai Tenga na kusababisha watu kuangua vicheko.

Wakili wa tatu kujibu hoja alikuwa wakili wa mshitakiwa wa tatu (Mgonja), Profesa Shahidi ambapo pia aliupinga waraka kutumiwa na upande wa mashitaka katika kesi hiyo, kwa lengo la kuwalazimisha watoe orodha ya mashahidi.

Alidai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 192(6) cha Sheria ya Jinai, kinampa uwezo Waziri wa Sheria kutunga sheria kwa kushirikiana na Jaji Mkuu na ikishatungwa, lazima itangazwe kwenye gazeti la serikali.

“Taarifa ya umma kutangazwa kwenye gazeti la seriakali ni kitu muhimu, wananchi wataisoma na kuifahamu na ndiyo maana jana (juzi) mawakili wote wa utetezi tulisema hatuujui huo Waraka Na.2 wa Jaji Mkuu wa mwaka 1999, kwa sababu haujawahi kutangazwa kwenye gazeti la seriakali, hivyo naungana na mawakili wenzangu kukataa ombi la upande wa mashitaka la kuutaka upande wa utetezi kujata orodha ya mashahidi sasa kwani huu siyo wakati wake kisheria,” alidai Profesa Shahidi.

Akipangua hoja za mawakili wa utetezi kwa mwembwe, wakili Kiongozi wa Serikali, Boniface alidai ukiangalia waraka wa Jaji mkuu wakati huo Francis Nyalali una majina yake na kuongeza kuwa, upande wa utetezi umeonyesha wasiwasi kuhusu waraka huo.

Alidai kuwa ni jukumu la upande huo kuleta ushahidi utakaoishawishi mahakama kuwa waraka huo sio wa Jaji Mkuu kwani wao wanafahamu kwamba waraka huo ni wa jaji Mkuu.

Bonicafe, alidai upande wa mashitaka unakataa hoja ya kuwa Waraka huo haukinzani na Sheria ya Makosa ya Jinai kwa sababu tayari wakili Tenga alishaiambia mahakama hiyo kuwa waraka huo hauna kitu kipya na kuhoji kuwa kama haina kitu kipya ni kwanini upande huo unadai waraka huo unapingana na Sheria ya Makosa ya Jinai na kuhoji kuwa kama hauna kitu kipya mgongano unatoka wapi?.

“Tunaona upande wa utetezi umejichanganya, sisi tumewambia wataje orodha ya mashahidi siyo wawaite mashahidi mahakamani, sasa sioni kama kunakubisha katika hili, sisi tulitaka mtaje orodha ya mashahidi siyo kuwaita, ugumu uko wapi. Nafikiri upande wa utetezi hawakutuelewa,” alidai Boniface nakusababisha watu kuangua vicheko.

Hata hivyo Utamwa umeutaka upande wa utetezi leo kuzijibu hoja hizo mahakamani ambapo usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo inayovuta hisia za wengi, unaendelea.

Juzi Wakili wa serikali Boniface baada ya kumaliza kutaja idadi ya mashahidi 17 kuwa ndiyo wanatarajiwa kutoa ushahidi kwa upande wa mashitaka, aliutaka upande wa utetezi nao utaje na orodha ya mashahidi wao watakaowaletwa kutoa ushahidi katika kesi hiyo.

Mbali na Mramba, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Septemba 24, 2009

SIASA KATIKA UTENDAJI HADI LINI?

Na Happiness Katabazi

UTAWALA wa awamu ya nne umefikia pahala unatisha.Raia wanyonge wananyang’anywa kile kidogo walichonacho kwa kutumia sheria za dola.
Hilo tumeliona kwa wingi wa matukio ya bomoa bomoa ,uchukuaji wa ardhi za kutolipwa fidia zinazostahili kwa waathirika wa matukio hayo.

Rasilimali za nchi zinaporwa na wageni wakishirikiana na kikundi kidogo cha mafisadi wenyeji kwa kisingizio cha uwekezaji.Hilo nalo limetungiwa sheria na kufadhiliwa na dola.

Watendaji wa serikali walio wengi wamekumbwa na utendaji utokanao na sheria zenye kulinda ufisadi na hivyo ama kwa kutodhamiria wanajikuta wamekuwa sehemu ya ukandamizaji wa uhujumu wa maslahi ya nchi.

Utawala wa kisiasa umejivisha joho la ‘siasa pendwa’ zisizozingatia haki ,hila zinajali majungu,fitna,kujikomba ,wivu,uonevu,ubaguzi,mifarakano na ushirikina.Vyombo vya utendani wa haki vimekaliwa na baadhi ya watendaji ambao wengi wao ni dhahifu kitaaluma na baadhi yao ni makuwadi wa wanasiasa na wengine ni mafisadi.Haki imewekwa njia ya panda, inanunulika ukiwa na fedha na nguvu kwenye mamlaka ya nchi katika awamu hii.

Raia wanapopiga mayowe kwa hamaki na uchungu kuusiana na haya yote , wanapewa lugha kwamba mamlaka ya nchi ipo vitani dhidi ya ufisadi na wataona matokeo yake kwa kesi nyingi zilizofunguliwa na zitakazofunguliwa mahakamani zinazohusu vigogo.

Wapo baadhi wanalolishangilia hili wakizani ni ufumbuzi kumbe wasijue kiini macho au usanii uliojengeka katika mfumo wa ‘siasa pendwa’ .Kesi hata zingekuwa elfu moja haziwezi kuwa ufumbuzi wa ufisadi kama Katiba na Sheria zetu hazikuumbwa kupambana na ufisadi.

Hao watuhumiwa watabezwa,kukashifiwa,kunyanyaswa lakini wanaweza kuachiwa na Mahakama mwisho wa siku.Hata kama kweli ni mafisadi tatizo ni ubora wa Katiba na sheria tulizonazo.

Lakini watuhumiwa waliopo mahakamani na watakaofikishwa wanaweza kuwa ni wahanga wa usanii wa ‘siasa pendwa’,wamekamatwa na kupelekwa mahakamani ili kutuliza hasira za umma wakati ukweli ni kwamba hawausiki wala hakuna ushahidi kwamba kweli walifanya ufisadi wanashitakiwa nazo.

Sasa hili ni jambo kubwa ambalo wananchi wengi hawajaliona na Idara ya Usalama wa Taifa chini ya Mkurugenzi shupavu,Rashid Othman walitupie macho na kulifanyia kazi haraka na kikamilifu.Kwani ni hatari watu wasiyo na hatia kutuhumiwa ,kunyanyaswa,kukashfiwa na hata kufunguliwa kesi za ufisadi au kesi zozote bila ushahidi.

Jambo kama hilo uzaa chuki binafsi ndani ya familia za watuhumiwa na kuligawa taifa katika makundi kwani tukumbuke kila binadamu ni mwanajamii ana ndugu,marafiki na ana jamii inayomzunguka ambayo inaweza kuungana naye na kumtetea kwa namna yoyote pale inapoonekana hakutendewa haki.

Taifa linaweza likajikuta linaingia kwenye machafuko na mauaji ya koo,makabila,dini na hata Kiitikadi kama itaadhiirika kwamba mtu fulani alituhumiwa na kufikishwa mahakamani bila ushahidi ili kumchafulia jina, chuki binafsi,kutokana na kunyang’anyana mabibi ,kutokana na magomvi ya kushindana kwenye zabuni,vyeo,kumkomesha mtu fulani kwasababu unadhani hakuheshimu au alikuwa akuungi mkono katika harakati zako za kupata cheo fulani.

Sote tunajua hao baadhi ya watuhumiwa wa kesi mbalimbali wengine wanaangukia katika makundi hayo niliyoyataja hapo juu.

Tutaona mmoja baada ya mwingine akiachiwa na mahakama na hilo lisijekutushangaza wala isije ikafikirika kwamba mahakama imenunuliwa kwa kuwa tunachokijua katika baadhi ya kesi hizo ni kwamba upelelezi ulifanyika harakara na ovyo ovyo kwa mashinikizo ya kisiasa yaliyogubikwa taaluma za kipelelezi na kisheria na chuki za wazi zimejidhiirisha na kuashiria maslahi binafsi katika kesi hizo badala ya maslahi ya taifa.

Watanzania na hayo ninayoyasema tumekuwa tukielezwa kwa siri na wahusika wa kuu wa kesi hizo wanaofanyakazi serikali na ndiyo sababu inayonisukuma kuandika makala hii kutoa taadhari hizo.Licha wananchi wengine ambao nao wamekuwa wakipata taarifa hizo toka kwa serikali wamekuwa wakizungumza katika mitaani.

Hukumu ya kesi ya mauji ya watu wanne iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi(ACP)Abdallah Zombe na wenzake iliyotolewa na Jaji Salum Massati Agosti 17 mwaka huu, iwe mfano endelevu wa haya tunayoyasema.Tunachokiona kesi hizi za ufisadi zinaweza zenyewe kuzaa ufisadi kwa maana mabilioni ya fedha yanaendelea kutumika kuzishughulikia wakati mavuno yatakuwa kiduchu.

Atakayebeba msalaba huu ni mlipa kodi hivyo tuna haki ten asana ya kutoa taadhari kwamba ofisi ya Mwendesha Mashitaka ,ofisi ya TAKUKURU zivunjwe na kuundwa upya kwa kuzingatia vigezo vya kitaaluma zaidi kuliko siasa.Kwani hivi sasa zinafanyakazi kama Idara ya Chama cha Mapinduzi(CCM).Hatuoni jinsi gani ofisi hizi ni za kitaaluma kwani sheria bado inaziweka mikononi mwa rais ambaye Mwenyekiti wa CCM.

Kwa hiyo ofisi hizo kupokea mashinikizo na maelekezo ya kisiasa sijambo la kubuni.Na ndiyo maana rais Jakaya Kikwete hivi karibuni, alikuwa na jeuri ya kuwaeleza wananchi kwamba kuna kesi tatu kubwa zitafunguliwa hivi karibuni.Sasa Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP) ni rais Kikwete au Eliezer Mbuki Feleshi?

Katiba na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, inasema mwenye mamlaka ya kushitaki au kutoshitaki ni DPP ,sasa inakuwaje rais wa nchi kuingilia mamlaka ya DPP?.Na katika kutoa tamko hilo rais alitumia kofia ipi ya urais au mwenyekiti wa CCM?

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Oktoba 11,2009

KESI YA EPA:JEETU AITIKISA SERIKALI

• Mahakama yazuia kesi yake kuendelea

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kwa mara nyingine imetoa amri ya kusimamisha kesi ya wizi wa sh bilioni 3.9 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) inayomkabili mfanyabiashara maarufu, Jayantkumar Chandubhai Patel, maarufu kwa jina la Jeetu Patel na wenzake watatu, hadi kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na washitakiwa hao Mahakama Kuu itakapomalizika.


Uamuzi huo ulitolewa jana na mahakimu wakazi John Mgeta na Fussi ambao walisema wamekubaliana na ombi la mawakili wa utetezi, Martin Matunda na Mabere Marando lililotaka mahakama hiyo itoe amri ya kusimamishwa usikilizaji wa kesi hiyo hadi kesi ya kikatiba inayoendelea Mahakama Kuu itakapomalizika.

“Tunakubaliana na ombi la utetezi la kutaka kesi hii isimamishwe kwa sababu kuna kesi ya kikatiba inaendelea Mahakama Kuu, na kwa sababu hiyo jopo hili limetupilia mbali pingamzi la upande wa mashitaka lililotaka kesi hiyo isisimamishwe kwa sababu tamko lililotolewa na mdaiwa wa pili, Reginald Mengi dhidi ya washitakiwa halihusiani na kesi hiyo.

“Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, tumebaini maombi ya upande wa utetezi ni ya msingi, kwani yameegemea kwenye haki za msingi zilizoainishwa kwenye katiba ya nchi, hivyo natoa amri ya kusimamishwa kwa kesi hii na ninaamuru jalada la kesi hii lipelekwe Mahakama Kuu ili liweze kutumika kwenye kesi hiyo ya kikatiba,” alisema Hakimu Mgeta.

Kesi hiyo ya kikatiba ambayo inasikilizwa na majaji watatu wanaoongozwa na Jaji Kiongozi, Fakhi Jundu, inaendelea kusikilizwa ambapo upande wa walalamikaji na wadaiwa wameishawasilisha utetezi wao na imepangwa kuanza kusikilizwa Novemba 2 mwaka huu. Majaji wengine ni Geofrey Shahidi na Semistocles Kaijage.

Katika kesi hiyo, Jeetu na wenzake wanamshitaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mengi na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwamba kwa nafasi zao walishindwa kutimiza wajibu wao kikamilifu baada ya mdaiwa wa pili (Mengi) kuwahukumu kupitia vyombo vya habari.

Juni 4, mwaka huu, Jeetu na wenzake walifungua kesi hiyo ya kikatiba Na. 30 wakiomba mahakama hiyo itoe tafsiri sahihi ya ibara 13, kifungu 4, 5 na 6 (b) cha katiba ambacho kinatamka watu wote ni sawa mbele ya sheria na pia itafsiri ibara 13 (6) (b) inayosema mtu yeyote asichukuliwe ana hatia hadi pale mahakama itakapomkuta na hatia.

Kwa mujibu wa hati ya madai, walalamikaji hao wanadai kuwa wamefikia uamuzi huo wa kuiomba mahakama itoe tafsiri ya ibara hizo za katiba kwa kuwa wanaamini zimevunjwa na Mengi ambaye Aprili 23, mwaka huu, alitumia vyombo vya habari kuwahukumu kwa kuwaita ‘Mafisadi Papa’ wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inayosikiliza kesi zao haijatoa hukumu.

Uamuzi huo ni wa pili kwani juzi mahakama hiyo ilitoa amri ya kusimamishwa kuendelea kwa kesi ya wizi wa sh bilioni 9 inayowakabili washitakiwa hao hadi kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na washitakiwa hao itakapotolewa uamuzi.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na kesi nne za wizi wa fedha katika Akaunti ya EPA katika Mahakama ya Kisutu ambazo zilifunguliwa Novemba mwaka jana.

Mbali na Jeetu, washitakiwa wengine ni Devendra Vinodbhai Patel, Amit Nady na Ketan Chohan.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Oktoba 9,2009

KORTI KUU YATOA DHAMANA KWA VIGOGO WA BOT

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ilitoa masharti ya dhamana kwa kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara y ash bilioni 104,inayomkabili Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT), Simon Mkonga na wenzake watatu.


Uamuzi huo ombi la dhamana lilowasilish mwishoni mwa mwezi Septemba mwaka huu, mahakamani hapo,ulitolewa na Jaji Emil Mushi ambaye alisema amekubaliana na ombi la mawakili wa washitakiwa Mpare Mpoki na Richard Rweyongeza kwasababu kwasababu kisheria mahakama hiyo ndiye yenye mamlaka ya kutoa dhamana kwa washitakiwa wa kesi ya uhujumu uchumi.

Jaji Mushi alisema ili mshitakiwa apate dhamana ni lazima kila mmoja asaini bondi ya bilioni 13, kutoa hati au fedha taslimu sh bilioni 13 na kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya kiasi hicho cha fedha, kusalimisha hati ya kusafiria, kutotoka nje ya Dar es Salaam hadi kwa kibari cha mahakama na kila Jumatatu kabla ya saa sita mchana kuripoti kwa Mkuu wa Polisi Mkoa Ilala na kwamba hati hizo zipelekwe kwa Msajili wa Mahakama Kuu ili asikague.

Septemba 18 mwaka huu, Hakimu Samwel Maweda ambaye ndiye anasikiliza kesi ya msingi iliyofunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala dhidi ya washitakiwa hao, alitupia mbali hoja ya utetezi iliyokuwa ikidai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Hakimu Maweda alisema hoja hiyo iliyowasilishwa na wakili wa utetezi, Mpare Mpoki, imeshangaza na kusema kwamba hakubaliani nayo kwani ina nia ya kupotosha kwa makusudi kifungu cha 29 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, na kifungu cha 245(1,2,3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Alisema kifungu hicho cha sheria kinatamka wazi kwamba, mtuhumiwa wa kesi ya aina hiyo anapokamatwa anapaswa kupelekwa katika mahakama za chini kwa ajili ya hatua za awali.

“Kwa sababu hiyo ya kisheria, natupilia mbali hoja hiyo ya upande wa utetezi kwa sababu ina lengo la kupotosha kifungu hicho cha sheria kwani kesi hiyo imefunguliwa kihalali na washitakiwa walisomewa mashitaka yao na hawakupaswa kujibu chochote kwa sababu mahakama hii haina mamlaka ya kusikiliza,” alisema Hakimu Maweda.

Pia alisema anatupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi lililotaka mahakama hiyo iwaachilie huru washitakiwa kwa sababu hawakupaswa kushitakiwa kwa kuwa wana kinga ya kutokushitakiwa kama ilivyoainishwa kwenye kifungu cha 65(1)(c) cha Sheria ya BoT.

“Nakubaliana na hoja ya upande wa mashitaka kwamba washitakiwa hao wakati wanatenda makosa hayo walikuwa na nia mbaya, na ikumbukwe sheria hiyo ya BoT inaweka kinga ya kutoshitakiwa kwa wafanyakazi wanaotenda makosa wakiwa na nia njema...hivyo natupilia mbali pingamizi hilo,” alisema.

Mbali na Mkango, washitakiwa wengine ni Simon Jengo na Naibu Mkurugenzi Fedha za Nje, Kisima Mkango, Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Bosco Kimela pamoja na Mkurugenzi wa masuala ya kibenki, Ally Bakari.

Katika kesi hiyo, washitakiwa hao wanadaiwa kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2004 na 2007, waliisababishia serikali hasara hiyo kwa kudanganya miongozo kwa kuongeza gharama za uchapishaji wa fedha za noti ikilinganishwa na gharama halisi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Oktoba 10,2009

RUFAA YA ZOMBE YATINGA KORTINI

*DPP atoa sababu 11 kupinga hukumu yake

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Eliezer Feleshi, amewasilisha rufaa yake kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu na kuwaachilia huru aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Abdallah Zombe na wenzake wanane waliotuhumiwa kwa mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi.


Rufaa hiyo iliwasilishwa katika Mahakama ya Rufani, jana saa 9:00 alasiri na kupewa namba 254/09 ambapo ilitiwa saini na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Francis Mutungi.
Katika rufaa hiyo ambayo Tanzania Daima inayo nakala yake, DPP ametoa sababu 11 za kukata rufaa.

Kwa mujibu wa rufaa hiyo, sababu ya kwanza, DPP anadai kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati aliyewaachilia huru Zombe na wenzake, alikosea kisheria na alijichanganya katika kuumba na kutafsiri misingi ya shitaka la mauaji lililokuwa likiwakabili washitakiwa.

Sababu ya pili, anadai kuwa, kwa mujibu wa mazingira ya kesi hiyo, Jaji Massati alichanganya katika kutafsiri misingi ya dhamira ya pamoja kwa washitakiwa kutenda kosa hilo na kwamba anadaiwa kukosea kutoa tafsiri ya ungamo.

Mrufani anadai kuwa Jaji Massati, alikosea kumwachia huru mshitakiwa wa kwanza, Zombe, kwa sababu kulikuwa na ushahidi wa mazingira unaombana.

Pia alikosoa kumwachilia huru mshitakiwa wa pili, Mrakibu wa Polisi, Christopher Bageni, kwa sababu upande wa mashitaka uliwasilisha ushahidi uliomgusa katika kutenda kosa hilo.

Aidha, alishindwa kutoa sababu za muda wa kisheria za kutomtia hatiani mshitakiwa wa tatu, ASP- Ahmed Makelle, kwa kosa la mauaji.

“Jaji pia alikosea kumwachilia huru mshitakiwa wa nne (Jane Andrew) na saba (Koplo Abineth Sarro) kwa sababu wao ni waathirika wa kimazingira bila kufafanua na kuonyesha mazingira hayo ni yapi.

“Sababu ya nane, Jaji alikosea kumwachilia huru mshitakiwa wa tano, Koplo Emmanuel Mabula na wa sita, Michael Shonza, kwa kuukubali ushahidi wao usioaminika uliotolewa na washitakiwa wakati wakijitetea,” inaeleza sehemu ya rufaa hiyo.

Mrufani alidai sababu ya tisa ni kwamba, Jaji Massati alikosea kumwachilia huru mshitakiwa wa nane, Koplo Rajabu Bakari, kwa sababu kulikuwa na ushahidi mzito dhidi yake.

Sababu ya 10 iliyotolewa na mrufani ni kwamba, katika mazingira ya kesi hiyo, jaji alishindwa kumtia hatiani mshitakiwa wa kwanza (Zombe) na wa tisa (Koplo Festus Gwabisabi), kwa mujibu wa kifungu cha 300 (2) cha Sheria ya Makosa ya Jinai kama ilivyofanyiwa mapitio mwaka 2002; ambacho kinasema mshitakiwa anaweza kutiwa hatiani kwa kosa dogo.

Alidai sababu ya 11 anadai kuwa jaji huyo alikosea kisheria kuchambua ushahidi katika kumbukumbu na kusababisha kupoteza mwelekeo wa kesi na kujichanganya alipotoa hukumu hiyo.

Rufaa hiyo ya DPP imekuja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuwaachilia huru washitakiwa hao Agosti 17, mwaka huu, pale Jaji Massati aliposema amebaini kuwa washitakiwa hao sio waliowaua marehemu na akaliagiza Jeshi la Polisi kuwatafuta waliofanya mauaji hayo.

Jana, gazeti hili lilichapisha habari kubwa ambayo ilikuwa ikimnukuu Zombe ambaye alisema atishiki na rufaa itakayokatwa dhidi yake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Oktoba 7,2009

ZOMBE:SITISHIKI


*Atamba rufaa inayokatwa dhidi yake haimtishi
*Aitaka serikali kuacha kubambikia watu kesi

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Kamanda wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe (55). ambaye hivi karibuni alishinda kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja, ameibuka na kusema hatishwi na rufaa inayokusudiwa kukatwa dhidi ya hukumu yake.


Zombe alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, katika mahojiano maalum na Tanzania Daima, yakiwa ya kwanza kwake tangu aachiwe huru na Mahakama Kuu ya Tanzania, Agosti 17 mwaka huu.

Katika mahojiano hayo, Zombe alisema hatua hiyo ya serikali kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), ni ya kutaka kujikosha kwa umma kuwa inafanya kazi vizuri wakati inajua kuwa wapelelezi wake walikiuka taratibu na sheria, na kwamba rufaa hiyo ni mwendelezo wa kufuja fedha za walipa kodi.

Zombe alisema uamuzi wa ofisi ya DPP kukata rufaa dhidi yake, anaufananisha na mcheza mpira anayemfanyia faulo mchezaji mwenzake na kisha adhabu ya penati inapigwa kwenye lango la mchezaji aliyefanyiwa faulo na kufafanua kuwa, Jeshi la Polisi na DPP walimchezea mchezo mchafu wa kisheria, hivyo hawawezi kupiga penati kwake.

“Nasubiri kwa hamu kuona huo mtindo wa msuko (wa rufaa) unaousukwa na ofisi ya DPP, kama ni ‘Twende kilioni’, ‘Kilimanjaro’ au ‘Jicho la kuku’ dhidi yangu… Ofisi ya DPP ina wataalamu wengi wa sheria, kwanini inashindwa kukubali ukweli kwamba kesi dhidi yangu ina upungufu mkubwa wa kisheria ambao hata mtoto wa shule ya chekechea anauona?

“Wananing’ang’ania tu, huku ni kufuja fedha za umma… mbona wale askari waliopeleka maiti za watu wanne katika Hospitali ya Muhimbili siku ile ya Januari 14 mwaka 2006, hawajashitakiwa? Hadi sasa wanaendelea na kazi na serikali inawafahamu fika, lakini ajabu wananishupalia mimi nisiyehusika na mauaji hayo.

“DPP na polisi waende mochwari pale Muhimbili, waombe kitabu cha mapokezi, waangalie Januari 14 mwaka 2006 ni askari gani walipeleka zile maiti za watu wanne, wakiwapata majina yao ndiyo wawakamate na kuwahoji maiti zile walizipata wapi, siyo kunifuatafuata mimi,” alisema Zombe.

Aliutaka umma wa Watanzania na wanasheria uamke na uiulize ofisi ya DPP na Jeshi la Polisi maswali matatu, kwamba ni nani aliyeandika maelezo yake ya onyo katika kesi aliyoshitakiwa? Je, maelezo ya ushahidi yanaweza kutumiwa kumpeleka na kumshitaki mtu yeyote mahakamani? Na je, kwa kutumia hati ya mashitaka pekee bila maelezo ya onyo, inawezekana kumshitaki mtu yeyote mahakamani kwa jinai?

Zombe alisema anachokiona sasa ni fedha za walipa kodi kuteketea kwa kufungulia watu kesi kwa ajili ya visasi, chuki binafsi, na kutaka kujionyesha ofisi hizo zipo imara, na kwamba polisi na ofisi ya DPP zikijibu maswali hayo ndipo uimara wao utakamilika, vinginevyo zitakuwa zikipoteza muda juu yake.

“Nasikitika sana serikali imenipotezea muda mwingi gerezani, ila hivi sasa namuachia Mungu, naamini kwa wakati wake atashughulika na wale wote walioshiriki kuniangamiza, kwa sababu fitna hizo za kunibambikia kesi ya mauaji zilikuwa kubwa mno.

“Serikali iache mchezo wa kubambika watu kesi kwa visasi na kutaka umaarufu wa kijinga, kwani mwisho wa ubaya ni aibu,” alisema Zombe kwa hisia, huku akilionyesha nyaraka mbalimbali gazeti hili.

Alihoji ikiwa yeye ana mwanga wa sheria na amefanya kazi ya upelelezi kwa muda mrefu amebambikiziwa kesi, je, wale wananchi waliobambikiwa kesi na wanaosubiri kesi zao wakiwa mahabusu ni nani atawaokoa?

“Kule gerezani nimekaa, watu wanateseka kwa kubambikiwa kesi, nashauri serikali ikaangalie watu wale na kwa mtindo huu wa kubambikia watu kesi, tukae tukijua mrundikano magerezani hautaisha hadi ofisi ya DPP na polisi wanaopeleka watu mahakamani waache mtindo wa kubambika watu kesi.

“Kwani hao waliobambikwa kesi ambao wanaendelea kusota mahabusu, siku wakiamka usingizini wakajua haki zao kwa undani, serikali itakuwa ikisumbuliwa kila siku kuwalipa fidia, na hii ni hatari kwani waliobambikizwa kesi wataanza kuichukia serikali yao, huku waliowafanyia unyama huo ni watumishi wachache tu,” alisema.

Zombe alisema kuwa, wakati akibambikwa kesi, umma wa Watanzania ukapumbazwa na propaganda zilizokuwa zikienezwa na baadhi ya vyombo vya habari, ambavyo vilimchafua na kuamini kuwa yeye ni katili, muuaji na hafai kuwepo katika jamii.

“Dhana hiyo ya propaganda ya baadhi ya vyombo vya habari ni ya kisiasa, ambayo inatumika kummaliza adui ili jamii ijenge chuki dhidi yake, na mfano mzuri ni Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, baadhi ya vyombo vya habari vilitumika kuwachafua wagombea wengine na waliochafuliwa walionekana ovyo mbele ya jamii.

“Naomba ieleweke kesi zangu nilizoyafungulia baadhi ya magazeti sitazifuta hadi pale mahakama itakapozitolea maamuzi,” alisema Zombe huku akionyesha kujiamini.

Akizungumzia maisha aliyokuwa akiishi gerezani kwa miaka minne, alisema yalikuwa mazuri kwake kwa sababu alikubali matokeo na akamwachia Mwenyezi Mungu, kwamba alipelekwa gerezani kwa dhuluma kama alivyopelekwa Nabii Yusufu, na kuwa aliamini siku moja ukweli utajulikana na Jaji Salum Massati ndiye aliyeanika ukweli wa kesi dhidi yake.

Alisema kuhusu mahitaji yake katika kipindi chote alichosota gerezani, familia yake iligharamia kila kitu, ikiwa pamoja na chakula alichokuwa akiletewa na mke wake kila siku, na alikuwa pia akifanya mazoezi ili kuuweka fiti mwili wake na kulinda afya yake.

“Nilikuwa nakula chakula cha nyumbani kwangu ambacho nilikuwa naletewa na mke wangu Fatma. Familia yangu iliingia gharama kubwa ya usafiri wa kuniletea chakula na mahitaji mengine wakati nipo gereza la Ukonga na Keko, na nilipokuwa huko nilikuwa nafanya mazoezi na mpaka sasa nafanya mazoezi ya viungo… ila nasema huo ulikuwa ni mtihani na ninasisitiza kuwa yote namwachia Mwenyezi Mungu,” alisema Zombe huku akionekana kulengwa na machozi.

Kuhusu ajira yake serikalini, Zombe alisema tayari amewasilisha notisi ya kuacha kazi Agosti 18, mwaka huu ikiwa ni siku moja tangu ashinde kesi, kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, kupitia kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) ambayo gazeti hili lina nakala yake.

“Nilipokuwa nikiishi gerezani, nilikuwa nikiwaza mambo mengi, likiwemo hilo la kuacha kufanya kazi serikalini, nimeamua kuchukua hatua hiyo nikihofia kuwa kama nikiendelea kufanya kazi serikalini nitaweza kubambikiziwa kesi nyingine,” alisema Zombe.

Notisi hiyo ambayo ina kichwa cha habari kisemacho; ‘Ombi la kustaafu kwa hiari baada ya kutimiza miaka 55 katika utumishi Jeshi la Polisi jalada Na. PF 12599 Check Na. 48812558’ inaonyesha kuwa ilipokelewa na ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI).

“Ifikapo Septemba 21, mwaka huu, nitakuwa natimiza umri wa miaka 55 ambapo kwa hiari yangu mwenyewe pasipo kushawishiwa na mtu yeyote, nimeamua nistaafu kwa hiari, hasa nikizingatia matatizo ambayo nimeyapata kwa kubambikiziwa kesi ya mauaji na huku taratibu za kisheria zikikiukwa wazi wazi kwa hila na kunikomoa.

“Napenda kufahamisha ofisi yako kuwa, ifikapo Septemba 21, mwaka huu, mimi naomba nistaafu kwa hiari na nilipwe mafao yangu yote kama sheria inavyoelekeza katika kifungu Na.58(4) cha “Police Force and Auxilliary Service Act, R.E 2002’, baada ya kuonekana sina hatia ya kosa hilo la mauaji na nilipoachiliwa na Mahakama Kuu Agosti 17 mwaka huu, na vifaa vya serikali ikiwemo sare za jeshi nitazirudisha pasipo shaka,” inasema sehemu ya notisi hiyo.

Aidha, kwa mujibu wa barua yake kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), aliyoiandika Septemba 22, mwaka huu, ambayo ilipokelewa na ofisi ya IGP, alimwarifu mkuu huyo kuwa anakabidhi kitambulisho cha kazi Na. 8051 kilichotolewa Machi 8, mwaka 1999 kwa cheo cha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Abdallah Zombe.

“Katika barua hii ya pili kwako IGP, napenda kurudia tena nimeamua kustaafu kwa hiari katika Jeshi la Polisi Tanzania baada ya kubambikiziwa kesi ya mauaji kwa makusudi yaliyo wazi, huku vifungu vya sheria ya nchi hii vikikiukwa wazi wazi kwa lengo la kunikomoa.

“Ibara ya 15(2)(a) ya katiba ya nchi inaeleza wazi nanukuu: ‘Ni marufuku kwa mtu yeyote kukamatwa, kufungwa, kufungiwa, kuwekwa kizuizini, kuhamishwa kwa nguvu au kunyang’anywa uhuru wake, vinginevyo isipokuwa tu kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria

“Kifungu cha 131 cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, kinaeleza wazi kwamba mtuhumiwa yeyote wa kesi ya jinai ni lazima ahojiwe na maelezo yake yaandikwe kwa njia ya onyo ‘All accused person to be cautioned’.

“Kanuni ya Sheria ya Polisi (Police General Order Na.236 haya ya 18 ) inaeleza wazi utaratibu maalum unaowataka maofisa wa polisi waufuate kwa kumhoji mtuhumiwa wa kesi ya jinai, na utaratibu huo umeainishwa kwenye ‘Jugdes Rules’ katika kiambatanisho A cha PGO 236 ambapo ukisoma na kiambatanisho A cha Sheria Na. 2 na 5 ya ‘Jugdes Rules’ ambavyo vinasema mara tu ofisa wa polisi anapofikiria kwamba anataka kumshitaki mtuhumiwa wa kesi ya jinai, lazima kwanza achukue maelezo ya onyo ya mshitakiwa na utaratibu huo wa kuchukua maelezo ya onyo unatakiwa ufuatwe na Jeshi la Polisi na umeainishwa katika haya ya 8(b) ya PGO 236.

“Na Sheria ya Jeshi la Polisi ambapo zamani ikiitwa Police Force Ordinance sura ya 322 ambayo hivi sasa inaitwa The Police Force and Auxilliary Services Act Cap 322 ya mwaka 2002, kifungu cha 32(4) kinaeleza umuhimu wa askari polisi kuchukua maelezo ya onyo kwa mtuhumiwa anayekabiliwa na kesi ya jinai,” anasema Zombe kwenye barua hiyo.

“Kama sheria hizo tatu nilizozitaja hapo juu, polisi walizikiuka dhidi yangu, sheria hizo sikuzitunga mimi, zilitungwa na Bunge ila kwa makusudi walizikiuka na kunibambikizia kesi ya mauaji… sasa nimeona nikiendelea tena kufanya kazi serikalini, watanibambikizia kesi nyingine, hata kesi ya kubaka, na kwa sababu hiyo nimeona watu hawa sio wazuri tena kwangu,” anasema Zombe.

“Je nani aliyeandika maelezo yangu ya onyo katika kesi mliyonishitaki nayo? Je maelezo ya ushahidi unaweza kuyatumia kumpeleka na kumshitaki mtu yeyote mahakamani? Je, kwa kutumia hati ya mashitaka pekee bila maelezo ya onyo, unaweza kumshitaki mtu yeyote mahakamani kwa jinai?

“Maelezo yaliyotumika mahakamani na upande wa mashitaka yaliandikwa chini ya kifungu 34(B)2(C) cha Sheria ya Ushahidi ya mwaka 2002, ndiyo yaliyotumika ‘is this not a fatal illegality? Huu ni ukiukwaji wa hali ya juu wa sheria za nchi, hivyo nimeona ni heri nipumzike nyumbani na familia yangu kuliko kuendelea kufanya kazi serikalini.

“Nilichoeleza hapa ni mfano mmoja tu kati ya sheria zilizokiukwa dhidi yangu wazi wazi, hivyo leo hii ninakabidhi kitambulisho cha kazi nilichokuwa nacho, chenye cheo cha Mrakibu wa Polisi. Nawatakia mafanikio mema katika ujenzi wa taifa, lakini kumbuka usemi wa Kiingereza usemao ‘If you want to go equity you must go with clean hands’ - yaani unapotaka kwenda mbinguni lazima uwe na mikono misafi,” ilisomeka barua hiyo ambayo pia gazeti hili inayo nakala yake.

Aidha, alisema katika utumishi ndani ya jeshi hilo, kuna mengi mazuri aliyafanya na kuna mabaya aliyafanya kama binadamu, lakini baadhi ya watumishi wenzake wameamua kumlipa maovu kwa hila na fitina zao, na huku wakijua wanakiuka taratibu za sheria.

“Nimetolea mfano huo mmoja, lakini ninayo mingi, kwani kwenye tukio la mauaji ya marehemu wale sikuwepo na upande wa mashitaka ulikiri wenyewe katika mambo yasiyobishaniwa kisheria pale Mahakama Kuu kesi ilivyoanza, kwamba mimi sikwenda eneo la tukio… sasa kama sikwenda eneo la tukio, wale watu wanne niliwauaje hadi serikali iniunganishe kwenye kesi ya mauaji?” alihoji.

Pamoja na hatua hiyo ya Zombe, wakili wake Jerome Msemwa, Septemba mosi, mwaka huu, aliwasilisha barua kwa IGP na nakala kwa Waziri wa Mambo ya Ndani yenye kumbukumbu Na. JM/ADV/047/2009 ambayo analiomba jeshi hilo limlipe malimbikizo ya makato ya nusu mshahara waliyokuwa wakimkata mteja wake tangu Juni mwaka 2006 hadi sasa, na kwamba amekuwa akikatwa makato hayo bila ya Wizara ya Mambo ya Ndani kumharifu kwa maandishi.

“Baada ya kuwasilisha barua hizo, nikaenda kufuatilia majibu yangu, nikaonana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Nyambibo, akaniambia jalada langu la kuomba kustaafu kwa hiari limepelekwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Nikashangaa kuona ofisi ya AG ndiyo ilipindisha sheria na kunifikisha mahakamani, sasa huyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali anataka kutoa maamuzi gani?

“Namuonya Mwanasheria Mkuu wa Serikali asije akathubutu kutoa maamuzi yasiyozingatia misingi ya sheria ambayo mwisho wa siku yataligharimu taifa, na mfano mzuri namkumbusha arejee kesi iliyoamuliwa Mahakama Kuu Dar es Salaam na Jaji Kyando, iliyomhusu Kamisha wa Polisi, Hilary Hemed Rashid na wenzake, ambapo serikali iliwalipa mamilioni ya fedha kwa ajili ya uzembe wa watumishi wachache wasiozingatia sheria za nchi,” alisema Zombe.

Agosti 17, mwaka huu, Zombe na wenzake tisa ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja, walishinda kesi hiyo baada ya Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati kutoa hukumu yake ambapo alisema anawaachilia huru kwa sababu hawakuhusika na mauaji hayo na akaagiza Jeshi la Polisi likawatafute walioua.

Siku mbili baadaye baada ya hukumu hiyo kutolewa, ofisi ya DPP iliwasilisha hati ya nia ya kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani, kupinga uamuzi huo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Oktoba 6,2009.Hii story ilishtua jamii, kwani nilikuwa mwandishi peke yangu ambaye niliweza kumhoji Zombe, nilipongezwan ofisi na jamii kwa ujumla.Story hii sitaisahau kwani iliendelea kuniletea heshima katika jamii.