HEKO IDARA YA USALAMA WA TAIFA

Na Happiness Katabazi

KATIKA mchakato wa mageuzi ambayo yamefanyika kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, mfumo wa sheria na siasa za nchi, taasisi za dola zimejikuta zikiwa nyuma wakati vuguvugu la mageuzi likienda mbele.


Moja ya tasisisi zilizokumbwa na fukuto hilo ni Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), ambayo hapo awali, yaani chini ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Kwanza na ya Pili, ilikuwa ni taasisi ambayo haikutambulika kisheria kutokana na muundo wake kuwa wa siri na wa gizani mno.

Matokeo ya utendaji wa idara hiyo uliiletea sifa ya kuogopwa sana na kuonekana ni chombo cha majungu, chuki na wauaji wa wananchi wenye misimamo tofauti na watawala wa serikali hizo mbili zilizopita zilizoongozwa na hayati Rais Julius Kambarage Nyerere na Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.

Maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa wakiwa katika umbile la kiraia ni wanajeshi na; idara hiyo ni chombo nyeti katika uhai wa dola letu.

Ni kweli kiasili, chombo hiki hufanya kazi kwa taratibu za idara zote za usalama wa taifa na kamwe mwanasiasa hawezi kukitumia; hata hivyo mwanasiasa anaweza kumtumia ofisa wa idara hiyo kwa siri kitendo ambacho ni cha ukiukwaji wa maadili.

Nchi inapoingia kwenye matatizo, migogoro ya kisiasa, lawama kubwa huelekezwa kwa taasisi hii kwani ndiyo inayotambua, kubashiri na kutoa ushauri wa nchi inavyoweza kukabiliana na hatari zozote zile za kiusalama na kiulinzi.

Hapa Tanzania, mageuzi ya mwaka 1992 yaliyoanzisha mfumo wa vyama vingi na mabadiliko mengine ya kisheria na Katiba, yalisababisha kuundwa kisheria kwa Idara ya Usalama wa Taifa.

Kutambulika rasmi kisheria hapa nchini kulianza mwaka 1996, baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha Sheria ya Idara ya Usalama wa Taifa Na.5 ya mwaka 1996 na kutambulika rasmi kwa jina la Tanzania Intelligence and Security Services (TISS), ambapo kwa sasa idara hiyo inaongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Rashid Othman.

Cheo hicho cha Mkurugenzi Mkuu ni sawa na Mkuu wa Jeshi la Ulinzi na Kujenga Taifa (CDF), David Mwamunyange, na Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema.
Kwa mujibu wa sehemu ya nne ya sheria hiyo inayounda (TISS), kazi na mamlaka iliyonayo ni kukusanya habari, kuchunguza na kutathmini habari zote zinazohatarisha usalama wa taifa na hatimaye kuishauri serikali hatua muafaka za kuchukua kwa maslahi ya taifa.

Ni wazi kwamba idara hii imechangia kwa kiasi kukubwa kudhibiti na kuzuia matendo mengi ya kihalifu ambayo yametendeka au yanayotarajia kutendeka kwa kutoa taarifa mapema kwa Jeshi la Polisi na taasisi nyingine husika ambazo mwisho wa siku ndizo zimeshiriki na kufanikisha kushindwa kwa matukio ya kihalifu.

Hivyo hatuna budi kuipongeza TISS kwa kazi nzuri wanayoifanya; haiwezi kuonekana moja kwa moja na wananchi kwa sababu moja ya miiko ya kazi zinazofanywa na idara hii ni siri.

Na idara hii imenyang’anywa mamlaka ya kukamata wahalifu kwani enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere idara hii ilikuwa na mamlaka hayo chini ya ‘Detention Order’ yaani sheria ya kumuweka mtu kizuizini.

Kwa muktadha wa majukumu hayo, idara hiyo ilitakiwa ijiunde upya kutoka kwenye giza na usiri ili ifanye kazi kama chombo cha dola chenye majukumu ya kulinda amani, usalama na demokrasia. Kwa vyovyote vile idara hiyo haiwezi kufuta mfumo wa utaratibu wake wa kufanya kazi zake kwa siri kwa kuwa hiyo ndiyo namna pekee inayowezesha kupata taarifa na habari za kiusalama.

Lakini pia katika dola ya kidemokrasia lazima chombo hiki kivae umbile la uwazi katika utendaji kazi wake ili wananchi wakijue, wajue majukumu yake na waweze kushirikiana nacho pale inapobidi.

Kwa vyovyote vile usalama wa taifa unalindwa na kusalitiwa na wananchi ambao ndiyo wenye nchi; hivyo ni bora wakajua masuala mbalimbali yanayowazunguka.

Idara hiyo isipojijengea haiba ya kupendwa na wananchi, na hasa wazalendo, mwisho wa siku itajikuta inashindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kwa urahisi zaidi.

Hivi sasa lawama nyingi zinahusu kuibwa au kuporwa kwa rasilimali za nchi kunakodaiwa kufanywa na matapeli kwa kushirikiana na baadhi ya wawekezaji. Idara hii inaelekezewa lawama hizo, kuhujumiwa kwa uchumi wa nchi, kuuzwa kwa mashirika ya umma kwa bei chee na sasa mikataba mibovu mbalimbali ambayo dola imeingia na wawekezaji lazima ielekezwe kwenye idara hii. Kwa vyovyote vile kashfa ya ufisadi wa BoT, EPA na ombwe la viongozi bora lazima shutuma zielekezwe kwenye idara hii.

Kumbe basi wajibu wake si kama ilivyosadikiwa hapo zamani; yaani kuwa kazi kubwa ya maofisa wa idara hii ni kubeba mikoba ya viongozi, kuwatayarishia malazi salama viongozi pindi wanaposafiri, kuwakuwadia mabibi viongozi, kuhesabu vizibo kwenye mabaa, majungu, chuki dhidi ya wananchi na viongozi wao.

Kwa hiyo tunapojikuta leo tuna mgogoro wa kisiasa katika vyama vya siasa vya ushindani vikiwa vimehujumiwa visifanye kazi, makundi yanayohasimiana kuibuka ndani ya CCM, ufisadi wa kupindukia mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika, ni mambo yanayowaelemea maofisa wetu wa idara yetu ya usalama.

Kwa vyovyote vile mbeba lawama wa mwisho ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Yeye ndiye anamteua Mkurugenzi Mkuu wa idara hiyo. Idara hiyo nyeti isipofanya kazi vizuri rais atayumba, ataboronga na dola kwa ujumla itaonekana ni ya hovyo ndani na nje ya nchi.

Wananchi wanailalamikia dola kwamba inawanyanyasa na kuminya haki zao bila fidia ya kutosha. Hii inatoa tahadhari kwamba malalamiko hayo yanatokana na utendaji usioridhisha wa idara hiyo.

Natoa wito kwa viongozi wa idara hii kuamka na kushika nafasi kikamilifu kwenye kazi hiyo nyeti ya usalama kwa maslahi ya taifa letu bila kuyumbishwa na wanasiasa manyang’au na wachumia tumbo.

Hatujasikia idara hii kukosa uwezo au vitendea kazi; kwa hiyo haya mambo madogo madogo yanayotishia usalama wa nchi, hayawezi kutolewa visingizio kwamba haijawezeshwa.

Hivi sasa nchi yetu imekuwa na uhuru mkubwa zaidi wa kutoa maoni ambapo wananchi wamekuwa wakijadili kashfa mbalimbali hadharani kila zinapoibuka pasi mtu kukamatwa, kuwekwa mbaroni na kuteswa; tunaamini Idara ya Usalama wa Taifa inafanya kazi yake kwa maadili yanayostahili. Kwa hili tunaipa heko.

Nchi nyingine maofisa wa idara kama hii hawajaenda shule vizuri na wala hawajui maadili ya kazi zao.

Watanzania wengi wangeishia kuumia na kuteswa kwenye majumba ya siri yenye giza, nge na kila aina ya mateso.

Tunasema haya kwa sababu tunajua yanayoendelea kufanywa na idara kama hii katika nchi nyingi za Afrika.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Januari 24 mwaka 2010

KORTI YAWANG'ANG'ANIA MAOFISA WA BoT

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imetupilia mbali ombi la upande wa utetezi katika kesi ya wizi wa sh milioni 207 katika Benki Kuu(BoT) lilokuwa likitaka washitakiwa watatu katika kesi hiyo ambao ni maofisa wa benki hiyo wafutiwe mashitaka kwa sababu wanakinga ya kutoshitakiwa wakati wakitetekeleza majukumu yao ya kikazi.


Washitakiwa katika kesi hiyo ni Kada wa CCM,Rajab Maranda, Farijara Hussein na maofisa watatu wa BoT, ambao ni Ester Komu, Iman Mwakosya na Bosco Kimela wanaotetewa na mawakili wa kujitegemea Mabere Marando,Majura Magafu na Mpare Mpoki.

Uamuzi huo ulitolewa jana na kiongozi wa jopo la Mahakimu Wakazi Ignas Kitusi anayesaidiana na Eva Nkya na John Utamwa kufuatia juzi wakili wa utetezi Mpare Mpoki kuwasilisha ombi hilo ambapo alisema kwa mujibu wa kifungu cha 65 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 inakata mfanyakazi au mjumbe wa bodi wa benki hiyo asishitakiwe kwa makosa aliyoyatenda wakati akitimiza majukumu ya kikazi na hivyo DPP kabla ya kuwashitaki alipaswa awaondolee kinga , hoja ambayo ilipingwa vikali na Wakili Kiongozi wa Serikali Stanslaus Boniface.

Akisoma uamuzi huo Kitusi alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, jopo hilo limebaini tatizo lipo kwenye tafsiri ya kifungu hicho cha sheria ambapo alisema ni kweli kifungu hicho kinatoa kinga kwa wafanyakazi na wajumbe wa bodi ila kwasababu washitakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya wizi,kula njama,kughushi makosa ambayo si moja ya majukumu yakazi ya washitakiwa hao.

“Baada ya kusema hayo tunakubalina na wakili Mkuu wa Serikali Boniface kwamba ni kweli wafanyakazi na wajumbe wa bodi ya BoT wanakinga lakini makosa yanayowakabili siyo moja ya majukumu yao yakazi…hivyo tunatupilia mbali pingamizi ombi la utetezi na washitakiwa ambao ni maofisa wa BoT wataendelea kubaki kwenye kesi hii kama ilivyokuwa awali”alisema Ignas Kitusi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamis, Januari 21 mwaka 2010

KORTI YAWANG'ANG'ANIA MAOFISA WA BoT

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imetupilia mbali ombi la upande wa utetezi katika kesi ya wizi wa sh milioni 207 katika Benki Kuu(BoT) lilokuwa likitaka washitakiwa watatu katika kesi hiyo ambao ni maofisa wa benki hiyo wafutiwe mashitaka kwa sababu wanakinga ya kutoshitakiwa wakati wakitetekeleza majukumu yao ya kikazi.


Washitakiwa katika kesi hiyo ni Kada wa CCM,Rajab Maranda, Farijara Hussein na maofisa watatu wa BoT, ambao ni Ester Komu, Iman Mwakosya na Bosco Kimela wanaotetewa na mawakili wa kujitegemea Mabere Marando,Majura Magafu na Mpare Mpoki.

Uamuzi huo ulitolewa jana na kiongozi wa jopo la Mahakimu Wakazi Ignas Kitusi anayesaidiana na Eva Nkya na John Utamwa kufuatia juzi wakili wa utetezi Mpare Mpoki kuwasilisha ombi hilo ambapo alisema kwa mujibu wa kifungu cha 65 cha Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 inakata mfanyakazi au mjumbe wa bodi wa benki hiyo asishitakiwe kwa makosa aliyoyatenda wakati akitimiza majukumu ya kikazi na hivyo DPP kabla ya kuwashitaki alipaswa awaondolee kinga , hoja ambayo ilipingwa vikali na Wakili Kiongozi wa Serikali Stanslaus Boniface.

Akisoma uamuzi huo Kitusi alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, jopo hilo limebaini tatizo lipo kwenye tafsiri ya kifungu hicho cha sheria ambapo alisema ni kweli kifungu hicho kinatoa kinga kwa wafanyakazi na wajumbe wa bodi ila kwasababu washitakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya wizi,kula njama,kughushi makosa ambayo si moja ya majukumu yakazi ya washitakiwa hao.

“Baada ya kusema hayo tunakubalina na wakili Mkuu wa Serikali Boniface kwamba ni kweli wafanyakazi na wajumbe wa bodi ya BoT wanakinga lakini makosa yanayowakabili siyo moja ya majukumu yao yakazi…hivyo tunatupilia mbali pingamizi ombi la utetezi na washitakiwa ambao ni maofisa wa BoT wataendelea kubaki kwenye kesi hii kama ilivyokuwa awali”alisema Ignas Kitusi.

Kesi hiyo imeairishwa hadi leo ambapo mashahidi wengine wataendelea kutoa ushahidi wao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi Januari 21 mwaka 2010

JEETU PATEL ARUHUSIWA KUTOKA NJE YA DSM

Na Happiness Katabazi

IKIWA ni siku sita tangu Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, itengue uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kusimamisha usikilizaji wa kesi ya wizi wa Sh bilioni 7.9 katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu (BoT), inayomkabili Mfanyabiashara maarufu Jayantkumar Chandubhai Patel maarufu ‘Jeetu Patel na wenzake wawili, upande wa utetezi umedai unapinga uamuzi huo.


Sambamba na hilo mahakama hiyo imewaruhusu washitakiwa hao kwenda nje ya Dar es Salaam na kukuwataka waakikishe siku ya kesi yao wanafika mahakamani bila kukosa ila mahakama hiyo ikakataa ombi la washitakiwa la kutaka ruhusa ya jumla ya kutoka nje ya mkoa na badala yake imewataka washitakiwa pindi wanapotaka kusafiri wafike mahakamani na kuomba ruhusa kwa mujibu wa sheria.

Mbele ya jopo la mahakimu wakazi Rwaichi Meela, John Kayoza na Grace Mwakipesile,wakili wa utetezi Mabere Marando, Martin Matunda waliikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili kutajwa na kutolewa uamuzi lakini upande wa utetezi unawasilisha ombi la kutaka mahakama hiyo itoe amri ya kusitisha usikilizwaji wa kesi hiyo.

Marando alisema wamefikia kuiomba mahakama itoe amri hiyo kwasababu juzi waliwasilisha notisi ya kupinga maelekezo yaliyotolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ,Semistocles Kaijage kwa Mahakama ya Kisutu Ijumaa iliyopita, katika Mahakama ya Rufani nchini ili mahakama hiyo iweze kuyapitia maelekezo ya jaji huyo na kuyatolea uamuzi.


Marando alieleza kuwa tayari notisi hiyo imeishapokelewa katika Mahakama ya Rufani na imeishapewa na Na.3 ya mwaka huu,ambapo warufani ni washitakiwa Ketan Chohan ,Devendra Vinodbhai Patel, Amit Nady

“Sisi tunapinga hayo maelekezo ya mahakama kuu kwa mahakama hii na ndiyo maana tumewasilisha ombi katika Mahakama ya Rufani ya kutaka mahakama juu kabisa ifanye mapitio ya maelekezo hayo …hivyo ndiyo maana tunaiomba mahakama hii ya Kisutu itoe amri ya kusitisha usikilizwaji wa kesi hii hadi mahakama ya rufani itakapotolea uamuzi ombi letu”alidai Marando.

Alisema kwenye kesi za masuala ya Kikatiba yanayofikishwa Mahakama Kuu,yanasikilizwa na kutolewa maamuzi na jopo la majaji wa tatu lakini chakushangaza jaji Kaijage ametoa maelekezo hayo peke yake.

Aidha kwa upande wa wakili kiongozi wa serikali Stanslaus Boniface,Fredrick Manyanda walidai kuwa hawana pingamizi na ombi hilo na Hakimu Mkazi Rwaichi Meela aliairisha kesi hiyo Februali 12 mwaka huu, ndipo watakapokuja kutoa uamuzi kuhusu ombi hilo la upande wa utetezi.

Hii ni mara ya pili kwa upande wa utetezi kuwasilisha ombi la kutaka kesi usikilizwaji wa kesi hiyo usitishwe, mara ya kwanza ilikuwa Oktoba 26 mwaka jana , mahakama hiyo ilikubali ombi hilo la kusitisha usikilizwaji wa kesi hiyo kwasababu washitakiwa hao walikuwa wamefungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu.

Hata hivyo Ijumaa iliyopita Mahakama Kuu ilitengua uamuzi huo wa Mahakama ya Kisutu uliokuwa umekubali kesi hiyo isitishwe kwasababu ilibaini maombi waliyowayoyatoa mahakama ya kisutu na kuyaleta Mahakama Kuu na maombi yao katika kesi ya Kikatiba iliyopo mahakama kuu yanafanana.

Novemba 4 mwaka 2008 , ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kati ya Agosti na Desemba 2005 ndani ya jijini la Dar es Salaam, washitakiwa hao waligushi nyaraka mbalimbali na zilizoonyesha kampuni yao ya Bencon International Limited imepewa idhini ya kurithi deni la kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan na kufanikiwa kuiba sh 7,962,978,372.48 mali ya Benki Kuu ya Tanzania.

Juni 4 mwaka jana, Jeetu na wenzake walifungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, inayosikilizwa na jopo la majaji watu wanaongozwa na Jaji Kiongozi, Fakhi Jundu, Geofrey Shahidi na Semistocles Kaijage. inaendelea kusikilizwa ambapo upande wa walalamikaji na wadaiwa wameishawasilisha utetezi wao na imepangwa kuanza kusikilizwa Novemba 2 mwaka huu.

Katika kesi hiyo ya Kikatiba , Jeetu na wenzake wanamshitaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Reginald Mengi na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwamba kwa nafasi zao walishindwa kutimiza wajibu wao kikamilifu baada ya mdaiwa wa pili (Mengi) kuwahukumu kupitia vyombo vya habari kabla ya kesi zao nne zilizofunguliwa katika Mahakama ya Kisutu kutolewa hukumu.

Jeetu na wenzake walifungua kesi hiyo ya kikatiba Na. 30 wakiomba Mahaka ma Kuu itoe tafsiri sahihi ya ibara 13, kifungu 4, 5 na 6 (b) cha Katiba ambacho kinatamka watu wote ni sawa mbele ya sheria na pia itafsiri ibara 13 (6) (b) inayosema mtu yeyote asichukuliwe ana hatia hadi pale mahakama itakapomkuta na hatia.

Kwa mujibu wa hati ya madai, walalamikaji hao wanadai kuwa wamefikia uamuzi huo wa kuiomba mahakama itoe tafsiri ya ibara hizo za katiba kwa kuwa wanaamini zimevunjwa na Mengi ambaye Aprili 23, mwaka huu, alitumia vyombo vya habari kuwahukumu kwa kuwaita ‘Mafisadi Papa’ wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inayosikiliza kesi zao haijatoa hukumu.

Uamuzi wa kusimamaishwa kwa kesi hii iliyofunguliwa katika Mahakama ya Kisutu , ulikuwa ni uamuzi wa tatu kutolewa katika kipindi cha Oktoba mwaka jana, mahakama hiyo ilitoa amri ya kusimamishwa kuendelea kwa kesi ya wizi wa sh bilioni 9, kesi ya wizi wa sh 3.9 zinazowakabili washitakiwa hao hadi kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na washitakiwa hao itakapotolewa uamuzi.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na kesi nne za wizi wa fedha katika Akaunti ya EPA katika Mahakama ya Kisutu ambazo zilifunguliwa Novemba mwaka juzi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania daima la Alhamisi, Januari 21 mwaka 2009

JOHN VICENT MATTAKA



Abuni njia rahisi ya kufahamu hisabati
*Agundua tatizo ni njia za ufundishaji
*Aja na njia yake mpya, aiita ni mkombozi

Na Happiness Katabazi

KILIO cha wanafunzi wengi hapa nchini hususan katika shule za msingi na sekondari ni kutolipenda somo la hisabati. Na hili limekuwa ni tatizo kubwa kwa wanafunzi walio wengi kwa miaka mingi hapa nchini.


Ufaulu wa masomo ya lazima katika matokeo ya kidato cha nne kwa mwaka uliopita unaonyesha kuwa somo la Kiswahili linaongoza likiwa na asilimia 81.59 ya ufaulu, likifuatiwa na Kiingereza (63.23). Somo la siasa likishika nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 62.09, likifuatiwa na jiografia (58.97) na la mwisho ni hisabati ambapo ufaulu ni asilimia 24.

Si sekondari pekee, adha hii ya matokeo mabaya katika somo la hisabati imekuwa ikiwakumba pia wahitimu wa shule za msingi kila mwaka.

Sababu zinazotolewa na wanafunzi hao ni kwamba somo hilo ni gumu na hawawezi kulimudu, hali iliyosababisha wanafunzi wengi kukimbia na kukimbilia kuchukua masomo ya michepuo mingine ambayo wamekuwa wakidai ni nafuu kwao.

Jambo ambalo serikali na wadau wa sekta ya elimu wasipolitafutia umbuzi wa tatizo hilo, mwisho wa siku taifa litajikuta lina wataalamu wachache wa hisabati na biashara.

Katika makala hii mwandishi wa gazeti hili amefanya mahojiano na mgunduzi wa njia rahisi za kufahamu na kulielewa somo la hisabati kupitia ugunduzi wa utafiti unaojulikana kama PEACEFUL START, Mtanzania John Vincent Mattaka (43) ambaye anaanza kwa kusema:

“Falsafa ya Peaceful Start inafanana sana na falsafa ya taasisi za tiba. Ubora wa taasisi ya tiba unadhihirika pale unapomsaidia yule ambaye ni mgonjwa zaidi kupata ahueni, au kupona kabisa. “Vivyo hivyo kwa Peaceful Start ina wigo mpana wa ubora wa kitaaluma unaochochea fikra za ubunifu, usiowaacha kando hata wale wanaodaiwa kuwa na uelewa mdogo, wale wanaosuasua darasani na kuonekana mzigo kwa wanaowafundisha.

“Hawa wakinolewa kifikra na vionjo vya Modeli-bunifu ya Peaceful Start, wanabadilika haraka na pengine hata kuwazidi wale ambao kabla ya hapo walikuwa wanawapita kwa uelewa.”

Mattaka anabainisha kuwa mwaka 1989 Chama cha Hisabati (CHAHITA) kilimteua kuwa miongoni mwa watu waliokwenda kushiriki katika Olimpiki ya Hisabati iliyoandaliwa na Muungano wa Vyama vya Hisabati vya nchi za Afrika (The African Mathematical Union ) huko Ibadan - Nigeria.

Anasema akiwa Ibadan alipata changamoto iliyomsukuma kujikita katika utafiti ulioleta ugunduzi huo. Changamoto hiyo iliyomgusa ilikuwa ya kuambiwa kuwa Bara la Afrika halimo kabisa katika ramani ya ulimwengu wa hisabati.

Anasema alipohitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1993, aliamua kutoajiriwa. Badala yake alijikita katika utafiti wa hisabati kwa lengo mahususi la kujibu ile changamoto kwa kupata ujuzi mpya utakaolistahilisha Bara la Afrika katika ramani ya wachangiaji mahiri wa somo la hisabati duniani.

Alitaka kuwafunulia Watanzania, Waafrika na wengineo kuhusu fikra za uoni wa ndani wa sifuri hadi tisa ambao yeye anauona kuwa ni wa msingi sana katika kulielewa somo la hisabati kwa wanaofundisha na wanaojifunza.

Hata hivyo, baada ya kuukamilisha utafiti kwa kupata njia bunifu, rahisi na mbadala ya kufundisha na kujifunza hisabati, bado aliona wanafunzi wengi hawaelewi hisabati haraka na kwa kiwango alichotarajia. Akagundua kuwa lugha nayo ilikuwa ni kikwazo kinachochangia ugumu wa somo hilo.

Hivyo aliamua kuzama na kujikita tena katika utafiti kwa nia ya kupata njia bunifu, rahisi na mbadala za kufundisha na kujifunza Kiingereza na Kiswahili na akafanikiwa kupata njia inayojulikana kama ‘SuVerbA ya kujifunza Kiingereza na ya ‘Abadafaga’ kwa somo la Kiswahili.

“Kutokana na ugunduzi huo tunawatangazia kwamba tatizo linaloonekana kuwa ni sugu la ugumu wa hisabati na Kiingereza limeshapata ufumbuzi kupitia ugunduzi huu wa Peaceful Start. Hivyo wanafunzi wanaodaiwa kuwa na uelewa mdogo katika kujifunza, wakiwekwa chini ya mfumo wa Modeli-bunifu ya Peaceful Start wanabadilika haraka,” anasema.
Anasema walengwa wao wakuu ni wanafunzi wa ngazi ya shule ya msingi. kujijengea upekee wa kueleweka kama wataalamu waliobobea katika ujenzi wa misingi imara ya usomaji na ufundishaji. Hivyo wanafunzi wa shule za msingi ndio walengwa wetu wa kwanza na kuongeza kuwa kulegalega kwa ubora wa elimu kwa ngazi za sekondari na vyuo kunaashiria makosa yalilofanyika kwenye ngazi ya elimu ya msingi.

Anahoji kwani Kiingereza ni kigumu kiasi gani hadi mtu afike chuo kikuu hajakijua, nako huko wahangaike kumfundisha? Hata hisabati si ngumu kiasi hicho kinachovumishwa.
Walengwa wao wakuu kama alivyotangulia kusema ni wanafunzi wa ngazi ya shule ya msingi. Kama jina lao lilivyo PEACEFUL START ina azima ya kujijengea upekee wa kueleweka kama wataalamu waliobobea katika ujenzi wa misingi imara ya usomaji na ufundishaji wa somo la hisabati.

Anasema licha ya yeye kuwa mtafiti wa taasisi hiyo pia taasisi hiyo ina Katibu Mkuu wake ambaye ni Brigedia Jenerali Mstaafu Gerald Kiswaga, ambaye ndiye anajishughulisha na shughuli za utendaji wa taasisi hiyo.

Taasisi hiyo ya kiraia ilisajiliwa kisheria mwaka (2005), ili kuwezesha matokeo ya utafiti uliofanywa kwa njia bunifu, rahisi na mbadala za kufundisha na kujifunza hisabati, Kiingereza na Kiswahili kutumiwa na walengwa waliomo katika sekta ya elimu na mafunzo na utafiti aliufanya kwa miaka 15.

Anasema katika dunia ya leo ushiriki wa wananchi wake kwenye biashara ya mtandao wa kompyuta (e-commerce) ni miongoni mwa vigezo muhimu vinaovyoonyesha kukomaa kwa uchumi wa nchi husika.

Katika hilo, mtafiti huyo anasema kuwa hatuwezi kuingia kwenye ushiriki wa namna hii ya biashara ya kisasa iwapo bado tuko nyuma kwenye umahiri wa masomo ya sayansi na tekonolojia ambayo moja kwa moja yanahusisha somo la hisabati.

“Kwa hiyo sayansi na tekonolojia haiwezekani iwapo umahiri wetu wa kujifunza na kufundisha hisabati na lugha utazidi kuwa ni huu usioridhisha hata kidogo.
Anasema yawapasa wajizatiti vilivyo, vinavyogunduliwa hapa kwetu tuvilinde kwa hatimiliki husika na tuvitangaze kwa nguvu zote na hatimaye tuviuze ili nasi tupate fedha za kigeni kupitia hivyo.

“Tumefikia wakati somo la hisabati limekuwa kama janga la taifa. Hivyo ni vema tukampa nafasi yeyote atakayedai kuwa na ufumbuzi juu ya suala hili, akasikilizwa.
“Kwa hali ilivyo sasa ki-hisabati, kesho yetu, haina matumaini hata kidogo. Hivi tutawapataje wataalamu wa fani mbalimbali kama vile za ualimu, udaktari, uhasibu, urubani, kilimo, ulinzi na usalama, kompyuta, biashara, uchumi, na wengineo?” anasema.
Kwa mantiki hiyo, anasema taasisi hiyo ni hazina yenye rasilimali kubwa na muhimu , lakini baya zaidi ipo tu bila kujua hatima ya itakavyotumika na kutusaidia.
Anasema iwapo watapata ushirikiano wanaotarajia kutoka kwa wadau mbalimbali wataweza kuusimika mfumo wa utoaji elimu bora na endelevu.

Ni matumaini yao kuwa katika muda mfupi wataweza kuboresha maendeleo ya sekta ya elimu na mafunzo hapa nchini, Afrika na hata dunia nzima.

Mtafiti huyo anasema kuwa, ugunduzi na utaalamu huu ukianza kutumika na kusambaa nje ya nchi utachangia kwa kiwango kikubwa suala zima la ajira na pato la fedha za kigeni.
Mattaka ni baba wa watoto watatu. Mwaka 1975-1981 alisoma Shule ya Msingi Mwongozo, wilayani Newala. Mwaka 1986-1988 akajiunga na Shule ya Sekondari ya Tosamaganga, Iringa na mwaka 1982-1985 alisoma Shule ya wavulana ya Songea.

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Januari 21 mwaka 2010

MIAKA MITANO YA SERIKALI YA AWAMU YA NNE:


*TUMFUNDE NINI RAIS JAKAYA KIKWETE?

Na Happiness Katabazi

UONGOZI wa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, umebakisha takriban miezi tisa kabla haujamaliza kipindi chake cha miaka mitano ambacho kimeainishwa katika Katiba ya nchi.


Moja kati ya mambo aliyokuwa ameahidi Kikwete pamoja na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye kampeni za kuwania kiti cha urais ni kuwaletea Watanzania maisha bora pasi na kuainisha njia za kutekelezea ahadi hiyo ambayo sasa inaonekana ni kitendawili kikubwa kilichokosa mteguaji.

Ni ukweli usiopingika kuwa ahadi hiyo na kauli mbiu ya Ari Mpya, Nguvu Mpya na Kasi Mpya vilivyochangia kumpa ushindi wa kishindo alioupata mwaka 2005 na kuwabwaga washindani wake kutoka vyama vya upinzani.

Ushindi huo haukupatikana kwa uraisi kutokana na kukabiliwa na upinzani mkali ndani na nje ya CCM, kundi la wanamtandao lililokuwa likiratibiwa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, na Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, ambao wanasemekana kuwa ‘maswahiba’ wa Rais Kikwete ambao ndio waliokuwa na jukumu kubwa la kuhakikisha mtandao wao unamuingiza mgombea wao Ikulu iwe kwa mbinu chafu au safi.

Rais mstaafu Benjamin Mkapa, ambaye kwa wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa CCM, alilazimika kumpigia kampeni Rais Kikwete hata kama alikuwa hajui ni mbinu gani zingetumika kutimiza ahadi ya maisha bora kwa kila Mtanzania; ahadi hizi za kwenye kampeni hizo ziligubikwa na mizengwe ya kila aina.

Baada ya Kikwete kuingia madarakani wanamtandao waliofanikisha safari yake ya kuingia Ikulu walijikuta kila mmoja wao akizawadiwa kulingana na nafasi yake kwenye mtandao. Waliochangia fedha nyingi nafasi zao zilikuwa kubwa (uwaziri), waliouunganisha mtandao na kuufanya ufanikiwe wakaambulia vyeo serikalini, kuanzia ukatibu mkuu hadi ukuu wa wilaya.

Waliokuwa kwenye jamii wakatupiwa mfupa wa kutafuna ulioitwa ‘mabilioni ya JK’.

Hayo ndiyo yaliyokuwa matokeo ya maisha bora kwa kila Mtanzania. Aliyepata alipata na aliyekosa alikosa. Sandakalawe…amina!

Leo CCM imeparaganyika siyo tena chama kile kilichomteua Kikwete akitetee kipate ushindi wa Tsunami, kuna makundi yanayowania nafasi ya urais wa nchi kwa udi na uvumba tena kwa kauli za kushtua na za kuulaumu utawala wa sasa kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo pamoja na kuwalea baadhi ya wanachama wenzao wanaodaiwa kuwa ni mafisadi.

Si jambo la ajabu kwa makundi hayo kuibuka kwa kasi kipindi hiki na kudai nchi imekosa uongozi imara kwa kuwa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, Kikwete katika kipindi hiki cha miaka mitano kashindwa kuvunja makundi na kukiunganisha chama kwani bado kuna CCM mtandao ile ya wasio wanamtandao.

Jambo jingine ni kushindwa kukiondoa chama na watu walio karibu naye katika kashfa mbalimbali za ubadhirifu wa fedha (ufisadi) unaoonekana kuwa wa kitaasisi zaidi kuliko ilivyofikiriwa mwanzoni kuwa ni utashi wa baadhi ya watu wenye tamaa za kuchuma mali kwa njia zisizo halali.

Chama hivi sasa kinaonekana kukumbatiwa na baadhi ya watu wanaodaiwa kuwa ni matajiri ambao kila wanachokisema ndicho kinachofuatwa hali ambayo imekifanya kipoteze sifa ile kilichojizolea siku nyingi kuwa ni chama cha wakulima na wafanyakazi ambao walihenya kukiimarisha chini ya utawala wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Lakini kubwa zaidi ambalo watu wamekuwa wakililalamikia ni kuwa serikali yao imegeuka kuwa ya kidhalimu; isiyojali wananchi wake hasa kwa kutekeleza sera ya ubinafsishaji, kubomoa bomoa nyumba, unyang’anyaji wa mali za watu bila fidia inayostahili.

Cha kusikitisha zaidi hata zile ahadi tamu tamu walizokuwa wakipewa huku wakigaiwa fulana, kofia na khanga za kuisifu CCM, karibu zote zote hazijatekelezwa ipasavyo ikiwemo elimu bure kwa vijana hadi chuo kikuu, nyumba za serikali zilizouzwa kurejeshwa mikononi mwa serikali pamoja na maboresho makubwa ya sekta ya afya.

Leo hii wale waliokuwa mstari wa mbele kusema kuwa ahadi hizo zingetekelezwa wamekuwa wakitembea vichwa chini kwa aibu kila wanapopita na kushuhudia umaskini unavyozidi kushamiri kadiri siku zinavyosonga mbele, elimu inavyozidi kushuka, nchi inavyozidi kutegemea misaada kutoka nje na mambo mengi ambayo kimsingi yanaondoa dhana nzima ya taifa kuwa huru.

Utawala wa sasa unaweza kujivunia mafanikio ya kujenga na kuanzisha mahusiano mazuri na nchi nyingi duniani, baadhi ya sekta angalau naweza kusema zimeweza kupiga hatua za kimaendeleo, uhuru wa kutoa maoni kwa wananchi ambao umeainishwa kwenye Ibara ya 18(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, umepanuka kwa kiasi kikubwa chini ya uongozi wa Rais Kikwete kulinganisha na awamu zilizopita.

Rais Kikwete, bado amezingirwa na kundi kubwa la wapambe wanaodai wanampenda na wanamshauri vizuri. Hawa baadhi yao leo nalazimika kuwaita ni ‘mbwa mwitu’ waliovaa ngozi ya kondoo, kwa sababu wakati mwingine Rais anashindwa kuona uborongaji wa mambo unaofanywa na watendaji walio chini yake lakini wapambe hawa wanashindwa kumueleza ukweli badala yake wanabaki wakimsifia kwa kuteua watendaji wachapa kazi na makini ilhali wajua wanampaka mafuta kwa mgongo wa chupa.

Aina hii ya wapambe haijaanza kwa Rais Kikwete pekee kwani ilianza katika Awamu ya Mwalimu Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.

Viongozi ama kwa kujua au kutokujua wamejikuta wakikubaliana na maelezo wanayopewa kila mara na wapambe hao ambapo wamekuwa wakijitahidi kujenga ukuta mkubwa kati ya viongozi na wananchi kwa hofu kuwa fursa hiyo ikipatikana wananchi wataeleza kila kitu kuhusu matatizo yao pamoja na utendaji usioridhisha.

Nina hakika wapambe hawa hawataishia hapa hata kura zako (Kikwete) zitakapotosha katika kipindi chako cha pili cha kuliongoza taifa kwa miaka mitano mingine (2010-2015), ndipo utaanza kuona rangi halisi za wapambe na wale uliowapa madarakani kwa kuwa wanajua huwezi tena kuwania kiti hicho kulingana na matakwa ya Katiba.

Wengi wao watajitenga nawe, licha ya baadhi yao hivi sasa kutokubaliana nawe; bali wanafanya hivyo kwa woga na unafiki hasa kutokana na nguvu uliyonayo katika kiti cha ukuu wa nchi, hawa watakusaliti na watakupaka matope na kila aina ya uchafu kiasi cha kufanya uchukiwe na jamii kama anavyoonekana Rais mstaafu, Benjami Mkapa.

Najua wakati huo hutakuwa na nguvu ya kuwadhibiti kama ilivyo hivi sasa. Leo wanakuchekea na kukupamba kwa kuwa uko madarakani, lakini kesho watakukimbia na kukucheka huku wakikuzomea kwa yale waliyokushauri vibaya na ukayafuata.

Ni vyema Kikwete ungesikia wosia huu ukabadilika kwa kuamua kuwa rais wa Watanzania wote . Kumbuka Watanzania walikuchagua uwaongoze siyo ugeuze urais kuwa ni kikundi cha watu wachache.

Ni vyema pia rais wetu na serikali unayoingoza mngesikia wosia huu na kuamua kuwa watenda haki mkasimamia haki za wanyonge wa nchi hii badala ya hao mafisadi na matajiri wanaodaiwa kuwa na ushawishi mkubwa kwako. Hivi kweli utakapoondoka Ikulu hizo kampuni za madini ambazo serikali inaonekana kuzitetea na kuzilinda kwa gharama kubwa zitayaenzi yale yote uliyozifanyia?

Ni vyema Kikwete ukayatafakari yanayoendelea kumpata mtangulizi wako Rais mstaafu Benjamin Mkapa, ambaye wakati anakaribia kustaafu na alivyostaafu alijikuta anakabiliwa na wimbi kubwa la kashfa dhidi ya serikali yake na familia yake ambazo ziliibuliwa na kuenezwa na kukuzwa na vyombo vya habari na wale waliokuwa baadhi ya wapambe wake wa karibu ambao aliwaamini na kuwapenda.

Wapambe hao wengine walikuwa ni wataalamu wa fani mbalimbali; walimshauri baadhi ya sera ikiwemo ile ya uuzwaji wa nyumba za serikali, ubinafsishaji; Rais Mkapa bila kujua alikuwa akitegwa na mbwa mwitu hao aliidhinisha sera hizo zitumike lakini mwisho wa siku walimgeuka na kuanza kumcheka na kumpakazia kwamba ameuza nchi na nyumba za serikali.

Na hata wewe Rais Kikwete ambaye wakati Mkapa akiwa madarakani, ulikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, sera hizo wakati zinapitishwa ulikuwa ni mjumbe wa Baraza la Mawaziri, ulizikubali. Na bado ningali nikikumbuka mwaka 2005 ulivyokuwa ukiomba kura uliwaahadi wananchi kuwa wakikuchagua utazirejesha nyumba hizo serikalini lakini hadi sasa bado ahadi hiyo inaonekana mwiba kwako na kwa watendaji wako.

Na kwa tafsiri ya ahadi hiyo, wewe ulikuwa ukiikosoa kinyumenyume sera hiyo ya uuzwaji wa nyumba za serikali kwa watumishi wake iliyoasisiwa na serikali ya Mkapa hali iliyopelekea wananchi wakuone wewe ni shujaa na Mkapa akaonekana ni kiongozi asiye mzalendo kwa taifa lake na fisadi wa kupindukia.

Baadhi ya wananchi wasiotaka kutafuta ukweli na kuchambua mambo kwa kina wanaendelea kumchukia Mkapa, utafikiri hakuwahi kufanya jema hata moja katika utawala wake.

Jambo hilo ni hatari kwa usalama wa taifa letu siku za usoni kwani mtindo huu wa wanasiasa uchwara wasiotaka kutumia nguvu ya hoja kupinga maamuzi yaliyochukuliwa na wanasiasa wenzao matokeo yake wanaamua kutumia uzushi na majungu kwa kushirikiana na baadhi ya waandishi ‘wachumia tumbo’ na kuanza kuchapisha baadhi ya habari za uongo dhidi ya viongozi tena wakubwa wa nchi hii, tukae tukijua ipo siku hao wanaochafuliwa kwa uzushi uvumilivu utawashinda kwani nao ni binadamu hawajatolewa nyongo, nao watajitokeza hadharani kuanika wanachokijua, ni wazi nchi haitakalika.Tusifike huko.

Mwisho ni vyema Rais Kikwete ujue kwamba Tanzania haina uongozi wa kichifu au usultani inapotokea watoto wa rais kwa kipindi kifupi tu wanatumia jina la rais kupewa madaraka kwenye chama kinachoongozwa na baba yao, tabia kama hiyo ni chanzo cha udhaifu mkubwa kwa rais mwenyewe na ishara ya kutokuwa makini.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Januari 17 mwaka 2010

MAHAKAMA KUU YATENGUA UAMUZI KESI YA JEETU PATEL

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mahama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetengua uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wa kusimamisha usikilizaji wa kesi ya wizi wa Sh bilioni 7.9 katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu, inayomkabili Mfanyabiashara maarufu Jayantkumar Chandubhai Patel maarufu ‘Jeetu Patel na wenzake wawili.


Uamuzi huo ulisomwa jana Katika Mahakama ya Hakimu MKazi Kisutu na Kiongozi wa Jopo la Mahakimu Wakazi Rwaichi Meela anayesaidiana na John Khayoza na Grace Mwakipesile ambapo kabla ya kuusoma uamuzi huo alisema uamuzi huo ni maelekezo yaliyopewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Semistocles Kaijage.

Rwaichi alisema maelekezo hayo ya Mahakama Kuu kwa jopo lake,alisema yamefikiwa baada ya mahakama kuu kupitia maombi ya washitakiwa yalitoka Kisutu na kufikishwa hapo na Kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa mahakamani hapo na washitakiwa hao na akabaini kuwa maombi yote yanafanana.

Jeetu na wenzake mwishoni mwa mwaka jana waliwasilisha katika Mahakama ya Kisutu ombi la kutaka usikilizwaji wa kesi yao katika Mahakama ya Kisutu usimamishwe na jarada la kesi hiyo lipelekwe Mahakama Kuu kwaajili ya kutumika katika kesi ya Kikatiba waliyoifungua dhidi ya serikali, ombi ambalo Oktoba 26 mwaka jana, lilikubaliwa na jopo la mahakimu wakazi hao ambao walisimamisha usikilizwaji kesi hiyo hadi kesi ya Kikatiba itakapotolewa uamuzi.

“Natengua uamuzi wa Mahakama ya Kisutu uliosimamisha usikilizaji wa washutakia kwasababu korti kuu imebaini kwamba maombi hayo yanafanana na yale waliyoyawasilisha kwenye kesi yao ya Kikatiba ambayo yapo katika Mahakama Kuu”alisema Rwaichi kwaniaba ya Jaji Kaijage.

Baada ya kusomwa kwa maelekezo hayo, wakili wa utetezi Gabriel Mnyere aliomba kesi hiyo ije kwaajili ya kutajwa ili wapate nafasi ya kutafakari maelekezo hayo na pia akaiomba mahakama hiyo iwaruhusu washitakiwa waweze kutembelea ofisi zao katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Pwani, Morogoro,Tabora,Arusha,Mtwara na Zanzibar kwaajili ya kuzungukia kampuni zao kwani bila ya hivyo kampuni hizo zitakufa na zikifa Watanzania walioajiriwa katika kampuni hizo wanazoziongoza watapoteza ajira na kwamba wapo tayari kuripoti kwa Wakuu wa Upelelezi kila watakapokuwa wakifika katika mikoa hiyo.

Hata hivyo Wakili Mwandamizi wa Serikali,Fredrick Manyanda na Oswald Tibabyekoma walipinga vikali hoja ya upande wa utetezi yakutaka kesi hiyo ije kwaajili ya kutajwa tu kwa kile alichodai kuwa ombi hilo si la msingi na kuongeza kuwa kesi hiyo ni ya muda mrefu kwani ilifunguliwa tangu Novemba 4 mwaka 2008 na upelelezi ulishakamika na upande wa mashitaka upo tayari kwaajili ya kuwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao.

Aidha wakili wa serikali Tibabyekoma alipinga tena ombi la washitakiwa wasipewe ruhusa ya kusafiri nje ya Dar es Salaam,kwasababu ombi hilo limeletwa kwa kiapo na siyo ombi kama inavyopaswa iwe kisheria na kufafanua kuwa hati ya kiapo kisheria ni ushahidi wa kwamba ombi husika limeletwa au linatarajiwa kuletwa mahakamani.
Hata hivyo Hakimu Mkazi Rwaichi alisema amesikiliza maombi ya pande zote mbili na akaairisha kesi hiyo Januari 20 mwaka huu, ambapo siku hiyo ndiyo jopo hilo litakuja kwaajili ya kutoa uamuzi wa maombi hayo.

Mbali na Jeetu washitakiwa wengine ni Devendra Patel na Amin Nandy wanaotetewa na Mabere Marando.

Novemba 4 mwaka 2008 , ilidaiwa mahakamani hapo kuwa kati ya Agosti na Desemba 2005 ndani ya jijini la Dar es Salaam, washitakiwa hao waligushi nyaraka mbalimbali na zilizoonyesha kampuni yao ya Bencon International Limited imepewa idhini ya kurithi deni la kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan na kufanikiwa kuiba sh 7,962,978,372.48 mali ya Benki Kuu ya Tanzania.

Juni 4 mwaka jana, Jeetu na wenzake walifungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, inayosikilizwa na jopo la majaji watu wanaongozwa na Jaji Kiongozi, Fakhi Jundu, Geofrey Shahidi na Semistocles Kaijage. inaendelea kusikilizwa ambapo upande wa walalamikaji na wadaiwa wameishawasilisha utetezi wao na imepangwa kuanza kusikilizwa Novemba 2 mwaka huu.

Katika kesi hiyo, Jeetu na wenzake wanamshitaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Reginald Mengi na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwamba kwa nafasi zao walishindwa kutimiza wajibu wao kikamilifu baada ya mdaiwa wa pili (Mengi) kuwahukumu kupitia vyombo vya habari kabla ya kesi zao nne zilizofunguliwa katika Mahakama ya Kisutu kutolewa hukumu.

Jeetu na wenzake walifungua kesi hiyo ya kikatiba Na. 30 wakiomba Mahaka ma Kuu itoe tafsiri sahihi ya ibara 13, kifungu 4, 5 na 6 (b) cha Katiba ambacho kinatamka watu wote ni sawa mbele ya sheria na pia itafsiri ibara 13 (6) (b) inayosema mtu yeyote asichukuliwe ana hatia hadi pale mahakama itakapomkuta na hatia.

Kwa mujibu wa hati ya madai, walalamikaji hao wanadai kuwa wamefikia uamuzi huo wa kuiomba mahakama itoe tafsiri ya ibara hizo za katiba kwa kuwa wanaamini zimevunjwa na Mengi ambaye Aprili 23, mwaka huu, alitumia vyombo vya habari kuwahukumu kwa kuwaita ‘Mafisadi Papa’ wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu inayosikiliza kesi zao haijatoa hukumu.

Uamuzi wa kusimamaishwa kwa kesi hii iliyofunguliwa katika Mahakama ya Kisutu , ulikuwa ni uamuzi wa tatu kutolewa katika kipindi cha Oktoba mwaka jana, mahakama hiyo ilitoa amri ya kusimamishwa kuendelea kwa kesi ya wizi wa sh bilioni 9, kesi ya wizi wa sh 3.9 zinazowakabili washitakiwa hao hadi kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na washitakiwa hao itakapotolewa uamuzi.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na kesi nne za wizi wa fedha katika Akaunti ya EPA katika Mahakama ya Kisutu ambazo zilifunguliwa Novemba mwaka juzi. Mbali na Jeetu, washitakiwa wengine ni Devendra Vinodbhai Patel, Amit Nady na Ketan Chohan

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Januari 16 mwaka 2010

WASHITAKIWA WIZI NBC UBUNGO HURU

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam imewaachiria huru washitakiwa tisa kati ya kumi waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya wizi wa sh milioni 168 kwa kutumia silaha mali ya Benki ya Taifa ya Biashara(NBC)Tawi la Ubungo maarufu kama ‘kesi ya mtandao’baada ya kuwaona hawana hati.


Sambamba na washitakiwa hao kuwaachia huru pia imemkuta na hatia ya katika makosa hayo mshitakiwa watano Rashid Eliakimu ambaye amehumiwa kwenda jela miaka 30. Na walioshinda kesi hiyo ni Ramadhan Dodo na mkewe Rahma Galos,Mashaka Mahengwa, Philipo Mpolea,John Mdesha,Martin Dashi,Jackson Isangu,Lucas Aloyce na Hussein Masoud ambao walikuwa wakitetewa na mawakili wa kujitegemea Majura Magafu,Shambwee Shitambala,Juvin.

Hukumu hiyo ambayo ilikuwa ikisubiriwa kwa hamu ilitolewa jana na Jaji Pelagia Khadai ambaye alianza kuisoma saa 6:08-7:50 huku akitumia lugha ya Kiswahili kusoma hukumu hiyo alianza kwa kusema ataisoma taratibu hukumu hiyo na kuitafsiri kwa lugha ya Kiswahili na mwananchi atakayechoka andoke mahakamani hapo taratibu ,siongee.

Jaji Khadai alianza kuuchambua ushahidi wa mashahidi 20 , na vilelezo vilivyoletwa na upande wa mashitaka alisema baada ya kuchambua ushaudi wa upande wa mashitaka , anakubaliana na hoja ua upande wa mawakili wa utetezi kwamba katika kesi hiyo upande wa Jamhuri umeshindwa kuleta kuleta ushahidi wa wa moja kwa moja au mazingira na pia ushahidi wa maungamo waliyoyatoa mashahidi haukufuta taratibu za kisheria na kuongeza kuwa hata utaratibu wa kufanyika kwa gwaride la utambuzi ulikiukwa.

Alisema shahidi wa kwanza na pili wa upande wa mashitaka ulimtaja mahakamani mshitakiwa wa 11(Masoud) lakini aliyekuja kumtambua Masoud kizimbani ni mtu ambaye hakuitwa kwenye kwenye gwaride la utambuzi , hivyo mahakama hii imeuona ushahidi wa mashahidi hao hauna sifa za kutosha kuishawishi mahakama hii imuone mshitakiwa huyo ana hatia.

“Pia hakuna kielelezo kilicholetwa mbele ya mahakama hii kinaonyesha mshitakiwa wa kwanza (Dodo) alitambuliwa kwenye gwaride la utambuzi lilofanyika Februali 18 mwaka 2006 lakini kielelezo ambacho ni rejista inaonyesha gwaride lilifanyika Februali 17 mwaka huo, sasa kwa mkanganyiko huu mahakama imeshindwa kuuamini ushahidi huo .... na mashahidi wote waliofika kutoa ushahidi waliambia mahakama hii kuwa siku hiyo wanatoa ushahidi ilikuwa ndiyo mara yao ya kwanza kuwaona washitakiwa hao”alisema Jaji Khadai.

Jaji Khadi ambaye muda mwingi wakati akisoma hukumu hiyo alionekana mwenye kutoka jasho usoni na kila mara alilazimika kutoa kitambaa chake cha mkononi kujifuta jasho alisema ,kwa mujibu wa shahidi wa pili, tatu walimtambua mshitakiwa wa kwanza lakini hawakupelekwa kwenye gwaride la utambuzi lilofanyika polisi na kisheria ndiyo unaotambulika na kutumika mahakamani.

“Mahakama hii imejiuliza je ushahidi dhidi ya mshitakiwa kwanza, na wanne unatosha?mahakama hii imeona ushahidi huo hautoshi kuwatia hatiani. Na ninakubaliana na upande wa utetetezi ,ushahidi wa mazingira uliomzingira mshitakiwa wa kwanza Ramadhan Dodo hautoshi kuishawishi mahakama hii imuone ana hatia kwani imeonyesha wazi kabisa gwaride la utambuzi lilifanyika miezi mitatu kabla ya mshitakiwa huyo kukamatwa”alisema Jaji Khadai.

Kuhusu washitakiwa wengine, hakuna gwaride la utambuzi lililofanywa na hakina shahidi aliyeeleza mahakama kuwa siku ya tukio Februali 2 mwaka 2006 aliwaona washitakiwa hao wakitenda kosa hilo la wizi wa kutumia silaha NBC Tawi la Ubungo.Na kuongeza kuwa mahakama inakataa utetezi ulitolewa na baadhi ya washitakiwa kwamba walichukuliwa maelezo polisi chini ya mateso makali kwani hakuna ushahidi ulioletwa unaonyesha washitakiwa walitoa maelezo chini ya mateso makali ya askari polisi.

Aidha alisema kisheria mshitakiwa anapofikishwa polisi anatakiwa achukuliwe maelezo ndani ya saa 48 lakini cha kushangaza washitakiwa walichukuliwa maelezo yao baada ya siku nne toka walipokamatwa na polisi na polisi walishindwa kuleta sababu za msingi au kifungu kilichowaruhusu kuwachukua maelezo washintakiwa nje ya sheria za nchi.

“Ni kweli askari polisi iliwakamata watuhumiwa kwa lengo la kutokomeza ujambazi hapa nchini lakini cha kushangaza baadhi ya askari waliowakamata baadhi ya washitakiwa hao walikuja kusema historia ya nyuma kwamba washitakiwa hao waliwahi kufanya uhalifu katika maeneo mbalimbali wakati katika kesi hii kilichokuwa kinatakiwa wathibitishe tukio la ujambazi lilotokea Februali 2 mwaka 2006 na si vinginevyo...na katika mashahidi wote wa upande wa Jamhuri wameshindwa kuieleza mahakama kuwa waliowaona washitakiwa hao wakitenda kosa hilo siku hiyo”alisema Jaji Khadai.

Jaji Khadai alisema baada ya kuuchambua ushahidi huo alisema pia hukumu yake iliangalia ushahidi wa mazingira ambapo alisema kwa mujibu wa hati ya ushahidi wa upande wa Jamhuri, ulidai kuwa Dodo alikamatwa Kibaha Kontena akifanya njama za kufanya uhalifu na mshitakiwa wa pili ambaye ni mke wake na wala hakuna ushahidi ulionyesha mkewe alimshawishi afanye tukio hilo na hakuna ushahidi unaonyesha walifanya ujambazi.

Akiendelea kuchambua ushahidi wa upande wa Jamhuri ulisema mshitakiwa wa nne alikamatwa Kariakoo,wa tano alikamatwa Arusha, wa sita alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere inagawa mshitakiwa huyo alikataa alisema yeye alikamatwa nyumbani kwake.Mshitakiwa saba walidai walimkamata Kariakoo na mshitakiwa huyo alikana akasema yeye alikamatiwa Bukoba Mkoani Kagera na mshitakiwa nane walidai walimkamata Mbezi na wala hakubisha kwamba alikamatiwa eneo hilo na mshitakiwa wa tisa polisi walidai hawajui sehemu waliyomkamata haijulikani na mshitakiwa wa kumi walidai amekamatiwa Moshi.

“Katika ukamataji huu wa washitakiwa mahakama inaona nini kinafuata baada ya ukamataji huo .Mshitakiwa tano alikamatwa na akawapeleka polisi kwenye gari ambalo lilipopekuliwa lilikutwa na silaha hivyo bila mshitakiwa wa tano kuwapeleka kwenye gari hilo mshitakiwa wa kumi ambaye tayari alikuwa ameishakamatwa na polisi asingetajwa,hakuna ushahidi:

“Kwa maana hiyo basi mahakama inamuona mshitakiwa wa tani anajua jinsi gani silaha hizo zilitumika kwenye ujambazi hatakama hakutambuliwa na mashahidi na hizo silaha alizitumia kufanya uhalifu na watu wengine tusiwatambua na ambao hawapo hapa mahakamani..hivyo katika kuangalia uzito wa kesi hii mahakama imeangalia ushadi wa pande zote mbili na unamtia hatiani mshitakiwa wa tano kwenda jela miaka 30 kwa makosa mawili kati ya sita, kosa la kula njama na kuibia benki hiyo kwa kutumia silaha.

Baada ya kulimaliza kusoma hukumu hiyo aliwataka waendesha mashitaka Inspekta Emma Mkonyi na wakili wa seriklai Edger Luoga kuangalia washitakiwa hao kama wanakabiliwa na kesi nyingine waendelee kubaki gerezani na wasiokabiliwa na kesi nyingine waruhusiwe waende nyumbani.Pia hukumu hiyo ilipokewa kwa shangwe na washitakiwa na ndugu zao huku wengine wakitaja jina Yesu,Mtume Mhamad na mama wa mshitakiwa wa tano ambaye hakuweza kutambuliwa jina lake mara moja, alianza kulia na kusababisha ndugu zake kumsaidia kushuka ngazi na kumuingiza kwenye gari.

Hii ni kesi ya tatu kati ya kesi saba za wizi wa kutumia silaha katika taasisi mabenki na maduka ya kubadilishia fedha za kigeni, na zile za mauji ,washitakiwa hao wanashinda.Kesi ya kwanza ni ile ya ya mauji katika duka la kubadilisha fedha za kigeni la Namanga Bureud Change, Mkunguni na hii ya Nbc Ubungo.Kesi nyingine ambazo bado zinawakabili ni ile ya mauji ya Ubungo mataa wakati wakidaiwa kuiba fedha za benki ya NMB Tawi la Wami-Morogoro, Msimbazi, Maxson Berued Change na Standard Charted ambazo bado zinaendelea kuunguruma katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Mahakama ya Kisutu.

Tukio hili la wizi ya ubungo lilitikisa jijini la Dar es Salaam na vitongoji vyake kwani watu wanaodaiwa kuwa ni majambazi wanadaiwa walitumia silaha nzito kufanya uhalifu huo.Nilikuwa ni muendelezo wa matukuo ya ujambazi yaliyokuwa yakitokea ndani ya muda mfupi tu tangu Rais Jakaya Kikwete apishwe kuongoza taifa hili Desemba 21 mwaka 2005.

Mapema 2006 ilidaiwa mahakamani hapo washiatakiwa wote wanakabiliwa na makosa sita ya kula njama na wizi wa kutimia silaha kwamba Februali 2 mwaka 2006 saa tatu asubuhi katika tawi la NBC Ubungo waliiba Sh 168,377,275 na dola za kimarekani 1680 mali ya benki hiyo na hivyo kusababishwa kusota rumande toka wakati huo kwasababu kesi hiliyokuwa ikiwakabili haina dhamana kisheria.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Januari 15 mwaka 2010

KIKWETE AZULIWA JAMBO

• ADAIWA KUMTAKA MTIKILA KWENYE MTANDAO WAKE

Na Happiness Katabazi

MWENYEKITI wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila ambaye ametupwa lupango baada ya kufutiwa dhamana kwa kosa la kushindwa kujiheshimu, amedai hatua hiyo imetokana na msimamo wake wa kukataa kuingizwa kwenye mtandao wa kumsaidia Rais Jakaya Kikwete ashinde.


Tayari hivi sasa kuna madai ya kuwapo kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani ambao wako katika mtandao unaojulikana kama ‘Saidia Jakaya Kikwete Ashinde’.

Baadhi ya viongozi wanaotajwa na ambao siku za hivi karibuni wamekuwa wakitoa kauli za kuwashambulia wanaompinga Rais Kikwete, ni pamoja na Rais wa Chama cha TADEA, Lifa Chipaka, Mwenyekiti wa UPDP, Fahmir Dovutwa na Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema.

Mtikila alitoa madai hayo mazito ya kukataa kuingizwa kwenye mtandao huo wa Rais Kikwete juzi, muda mfupi kabla ya kuwekwa mahabusu kwa kosa la kutojiheshimu na kuruka dhamana.

Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano kwa njia simu, Mchungaji Mtikila ambaye ana historia ya kukabiliana na kesi za kashfa dhidi ya viongozi wa juu serikalini, alisema Jumatano ya wiki iliyopita, aliitwa na Katibu wa Rais Kikwete, Kassim Mtawa katika Hoteli ya Kempinski ya jijini Dar es Salaam na kuwa na mazungumzo ya faragha.

Mtikila ambaye amepata kuhukumiwa kwenda jela mwaka mmoja kwa kosa la kumkashifu Mwalimu Nyerere, alidai kuwa alipofika hotelini hapo alikutana na Mtawa na kuelezwa kuwa lengo la kikao chao ni kutaka ajiunge kwenye mtandao wa Saidia Kikwete Ashinde katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba.

“Mtawa alinipa majukumu matatu; moja ni la kuitisha mkutano na vyombo vya habari na kutoa kauli ya kuwalaani wote waliomshambulia Rais Kikwete kwenye mdahalo ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere, pili alinitaka niitishe mkutano na wanahabari ili niweze kuunga mkono utabiri wa Sheikh Yahya Hussein na tatu, niwachafue wote wanaotaka kujitokeza kumpinga Rais Kikwete ndani ya CCM.

“Mimi nilikataa katakata kufanya kazi hiyo kwani kwangu mimi huo ni udhalimu kwa sababu ninamuogopa Mungu na kuheshimu katiba ya nchi na suala la kugombea nafasi yoyote ni haki ya kila mtu kikatiba,” alisema Mtikila kwa sauti ya upole.

Aliendelea kudai kuwa katika mazungumzo yao, Mtawa alimuahidi kuwa endapo angekubali kufanya mambo hayo matatu, angepewa fedha nyingi za kuendeleza familia yake.

Hata hivyo Mtikila alipoulizwa kama katika mazungumzo hayo hakuchukua kiasi chochote cha fedha, alisema alizikataa kwani alikataa kuingizwa kwenye mtandao huo.

Akizungumzia madai hayo dhidi ya Rais Kikwete kwa njia ya simu, Katibu wa Rais, Mtawa alikanusha na kuyaita ni ya uongo na uzushi wa hali ya juu.

“Jamani huo ni uongo wa hali ya juu. Mimi sijakutana na Mtikila kama anavyodai. Kwanza mimi si niliyemshitaki. Mtu anapofutiwa dhamana maana yake amevunja masharti ya dhamana, ameyakiuka mwenyewe, ndiyo maana mahakama imemfutia dhamana.

“Tena mimi si Msajili wa Mahakama, sasa nashangaa anavyotaka kuniingiza kwenye mambo yasiyo na msingi… Huyo Mtikila ni muungo, tena nashukuru sana umenipa nafasi ya kujieleza,” alisema Mtawa.

Juzi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, ilimfutia dhamana Mtikila kwa madai ya kushindwa kujiheshimu.

Amri hiyo ya kumfutia dhamana ilitolewa na Hakimu Mkazi Waliarwande Lema baada ya kusikiliza utetezi wa mshitakiwa ambaye alifika katika viwanja vya mahakama hiyo saa tano asubuhi akiwa amechelewa na ghafla alijikuta akikamatwa na askari polisi wa mahakamani hapo.

Kwa mujibu wa habari hizo, Mtikila alipaswa kufika mahakamani hapo majira ya saa tatu asubuhi wakati kesi hiyo ilipotajwa, lakini hakuwepo, ndipo Wakili wa Serikali, Beatrice Mpangala aliomba hati ya kukamatwa kwa mshitakiwa.

Kabla ya Mtikila kukamatwa, aliiambia mahakama kwamba alidamka mapema na kumtafuta daktari wake aliyemtaja kwa jina moja la Katembo, ambaye alimfanyia upasuaji baada ya kugongwa na nyoka aina ya kobra wakati alipokuwa katika shughuli za kidini nchini Zimbabwe mwaka jana.

Alisema alijitahidi kuwatafuta wadhamini wake ili wafike mahakamani kwa niaba yake, lakini hakuweza kuwapata, ndiyo maana alikuja mwenyewe mahakamani hapo akiwa na maumivu makali mwilini mwake.

Hata hivyo hakimu Lema alieleza kutoridhishwa na utetezi huo na kuamuru Mtikila atupwe rumande hadi Januari 25 kesi yake itakapotajwa tena.

Hii ni mara ya pili kwa Mchungaji Mtikila kushindwa kufika mahakamani wala wadhamini wake. Mara ya kwanza ilikuwa Oktoba 22, mwaka jana.

Mchungaji Mtikila anakabiliwa na kesi ya uchochezi namba 1767/2007.

Ilidaiwa kuwa alitoa maneno ya uchochezi na kashfa dhidi ya Rais Kikwete kwa kumuita gaidi kwa madai kuwa serikali anayoiongoza inataka kuanzisha Mahakama ya Kadhi, jambo ambalo ni kinyume na katiba ya nchi.

Chanzo:Gazeti la Jumatano ,Januari 13 mwaka 2010

MTIKILA ATUPWA RUMANDE

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imemtupa rumande Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila baada ya kumfutia dhamana kwa kukiuka masharti.


Amri ya kumfutia dhamana na kutupwa rumande ilitolewa jana na Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema, baada ya kusikiliza utetezi wa Mtikila aliyechelewa kuhudhuria kesi ya uchochezi inayomkabili mahakamani hapo.

Mtikila alipofika mahakamani hapo majira ya mchana alikamatwa na askari polisi waliokuwa na hati ya kukamatwa kwake baada ya kutoonekana mahakamani hapo jana asubuhi wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Hati ya kukamatwa kwa Mtikila ilitolewa baada ya ombi la Wakili wa Serikali, Beatrice Mpangala aliyekuwa tayari kusikiliza kesi hiyo, lakini mshitakiwa huyo kutoonekana mahakamani bila kuwapo kwa sababu za msingi.

“Sababu ulizotoa za kushindwa kufika mahakamani leo asubuhi zimeshindwa kuishawishi mahakama na hii ni mara ya pili kwa wewe kushindwa kufika mahakamani wala wadhamini wako.

“Mara ya kwanza ilikuwa Oktoba 22 mwaka jana, ulichelewa pia kuja mahakamani. Ili tabia hii ikome mahakama inakufutia dhamana yako kwa sababu umeshindwa kujiheshimu,” alisema Hakimu Lema.

Alisema Mtikila atakaa rumande hadi Januari 25, kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya upande wa mashitaka kumsomea maelezo ya awali.

Kabla ya kutoa amri hiyo, hakimu huyo alimhoji Mtikila alikuwa wapi wakati kesi yake inatajwa mahakamani, naye kujibu kwamba alikwenda kwa daktari wake aliyemfanyia upasuaji alipogongwa na nyoka nchini Zimbabwe.

Mtikila aliendelea kujitetea kuwa asubuhi alijitahidi kuwatafuta wadhamini wake ili wamuwakilishe mahakamani lakini hakuwapata.

“Mheshimiwa Hakimu asubuhi nilijitahidi kuwasiliana na wadhamini wangu, lakini sijafanikiwa, ndiyo maana mimi nimekuja mchana,” alidai Mtikila.

Hata hivyo, hakimu Lema alisema kuwa sababu hizo si za msingi, hivyo ameshindwa kuishawishi mahakama isimfutie dhamana.

Katika kesi hiyo ya uchochezi Mtikila anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi ya kumkashfu Rais Jakaya Kikwete kwa kumuita gaidi kwa sababu serikali anayoingoza inataka kuanzisha Mahakama ya Kadhi, jambo ambalo linapingana na katiba ya nchi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Januari 12 mwaka 2010

JWTZ KIWE CHOMBO CHA ULINZI NA MAENDELEO YA WANANCHI


Happiness Katabazi

KUNA msemo usemao ‘Wanajeshi/askari ni mbwa wa Mfalme’.

Kama msemo huu ni kweli au sikweli si hoja ya makala hii. Makala hii inalenga Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ), ni chombo chenye nidhamu na kikitumika vizuri kinaweza kuliletea taifa letu neema kubwa.


Jukumu mojawapo la msingi la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakati wa amani, ni kusaidia mamlaka za kiraia kulinda usalama wa wananchi na mali zao,mipaka ya nchi na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kutoa misaada ya uokoaji wakati wa majanga na kukarabati miundombinu inapoharibika.

Katika kusaidia shughuli za kijamii, JWTZ kwa muda wote wa uhai wake, imeweza kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi mkubwa na kujipatia sifa kemkem kutokana na mchango wake, hasa katika uokoaji na urejeshaji miundombinu ya barabara na madaraja wakati wa mafuriko.

Jukumu hilo limekuwa likifanywa na wanajeshi wote, wakiongozwa na wahandisi wa medani wa JWTZ wenye makao makuu yao eneo la Sangasanga mkoani Morogoro, ambao wamebobea katika fani hiyo.

Wahandisi wa medani ndio watalaamu ambao wakati wa vita huwezesha vikosi kusonga mbele kwa kuonyesha njia, kwa kufanya doria na kuchagua sehemu nzuri ya kupitisha vikosi, zana na vifaa. Wao pia husafisha njia kwa kutegua mabomu, kujenga barabara, madaraja na viwanja vya ndege.

Kwa misingi hiyo basi, naona kuna umuhimu kwa taifa letu kuanzisha utaratibu wa kuwatumia wahandisi,mabwana shamba wa JWTZ wakati wa amani ili taifa liweze kupiga hatua ya maendeleo katika sekta ya miundombinu, kilimo na ujenzi.
Jeshi letu hivi sasa lina hazina ya wataalam wa kila fani, lakini baadhi yao taaluma zao hawazitumii ipasavyo kutokana na serikali yetu kutowapa fursa ya kutumia ujuzi wao wakati wa amani.

Sote ni mashaidi kwamba inapotekea maafa na mfano mzuri ni yale yaliyotokea Kilosa,Same na kwingineko wahandisi wa JWTZ wamekuwa wakisukumizwa kutengeneza barabara, kuokoa majeruhi nk., lakini hali hiyo ya pilikapilika hawaipati wakati wa amani.

Pamoja na kuwa na fani ya uhandisi, lakini wanajeshi wote wamefundishwa ukakamavu na kazi zao huzifanya ndani ya muda unaotakiwa.

Ni barabara, madaraja mengi tunayashuhudia yamejengwa na raia wa kawaida, tena kwa gharama kubwa, lakini yamekuwa yakichukua muda mrefu kukamilika,au yakikamilika yanaaribika ndani ya kipindi kifupi na mara nyingine tunaambiwa serikali ndiyo imekuwa ikichelewesha fedha za kuwalipa makandarasi na wakati mwingine tunaambiwa makandarasi hao ni wazembe.

Hakika habari kama hizi hazipendezi kusikiwa maskioni mwa mwananchi yeyote mpenda maendeleo, kwani sote tunafahamu taifa lisilo na miundombinu ya uhakika ni wazi litakuwa linajirudisha nyuma kimaendeleo kwani shughuli za uzalishaji zitakwama kwa kuwa mazao au mawasiliano hayasafirishwi kwa wakati muafaka, hivyo kufanya pato la wananchi na taifa kwa ujumla kukosekana na bidhaa kukosekana sokoni.

JWTZ litumike wakati wa amani katika kudhibiti mipaka na katika udhibitio huo ni pamoja na kuweka uzio wa kiulinzi katika maeneo ambayo yanapenyeka kwa urahisi na maadui wanaoweza kuja kuhuju nchi yetu mfano mzuri wezi wa ng’ombe kule Tarime kwani mpaka huo umekuwa na matatizo kila mara kwa mara.Na hiyo ni kazi ya Jeshi wakati wa amani na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kila mwaka ionyeshe jinsi ambavyo wameimalisha ulinzi.

Serikali iwaijengee uwezo JWTZ iweze kufanyakazi za ujenzi katika maeneo ya vijijini ambayo yanatakiwa yafikike.Maeneo hayo yanaitaji barabara,visima.JWTZ watakapopewa miradi hiyo watatengeneza hizo barabara,watachimba visima kisha watawafundisha wanakijiji hao jinsi ya kutumia miundombinu hiyo na jinsi ya kuzifanyia ukarabati pindi zitakapoaribika kisha wanawakabidhi wanakijiji mradi huo.

Pia wanajeshi wetu waweze kupewa miradi mikubwa ya kilimo , waende huko vijijini kuwasaidia wananchi wenzetu kuwajengea miundombinu ya mashamba makubwa ya kilimo .Kisha wanawakabidhi miradi hiyo wananchi.Na Hapo ndipo tunaweza kusema Kilimo Kwanza kitafanikiwa kwasababu ikumbukwe kinaitaji ujezni wa miundombinu ya umwagiliaji kabla ya kilimo chenyewe.

Katika maeneo mengine wahandishi wa JWTZ wanaweza kwenda vijijini kuwafundisha wananchi jinsi ya kujenga nyumba za kisasa.Hii ni teknolojia ambayo wananchi wanatakiwa wafundishwe,Jeshi likishamaliza kuwafundisha ,idadi kubwa ya wanakijiji itakuwa ikijua kwa vitendo ujenzi wa kisasa.Haya ndiyo mambo ambayo serikali makini kote duniani inafanya kama kweli inataka wananchi wake wapate maendeleo.

JWTZ isitumike tu kwenye kupendezesha magwaride katika sherehe za kitaifa ,mazishi ya viongozi,maafa na kuswagwa kwenda kuimarisha ulinzi kule Pemba nyakati za uchaguzi mkuu.

Huu ni wakati wa zama za maendeleo ya sayansi na teknolojia na hivyo vinapaswa kulikumba jeshi pia na njia mojawapo ya kulifanya liende sambamba na maendeleo hayo, ni kupanua wigo wa utendaji wake na ninafikiri njia mojawapo ni kwa kujishughulisha katika ujenzi wa taifa kwa kutumia rasilimali watu iliyonayo.

Hizi si zama za wanajeshi wetu kutembea na silaha wakati wote, au kulewa pombe muda mrefu pale Upanga Messi,Sabasaba Messi,Muungano Messi-Tabora, kunyang’anyana mabibi mitaani na raia bali kubadilika ili liwe jeshi la ujenzi wa taifa, huku likihakikisha amani na usalama wa mipaka ya nchi yetu.

Tujiulize kipi bora, kuendelea kuwatumia makandarasi toka nje ya nchi kwa gharama kubwa ambao wakimaliza kazi wanaondoka na vifaa vyao au taifa lijinyime na kununua vifaa vyake na kutumia wahandisi wake katika ujenzi wa miundombinu ya taifa letu?

Lengo langu si kupiga vita makandarasi wa nje ili wasipewe tenda, la hasha! Ila kwa kuwa serikali kila kukicha imekuwa ikilia kuwa haina fedha za kutosha kutokana na bajeti ya taifa kuwa tegemezi kwa wafadhili, sasa kwanini hicho kidogo tulichonacho kisizunguke humu ndani ili wananchi na taasisi nyingine za serikali ziweze kufaidika nacho?Tunachokiona fedha nyingi zimeelekezwa kwenye siasa.

Kwani hivi sasa serikali inatumia fedha nyingi kuleta makandarasi toka nje ya nchi kwa ajili ya ujenzi wa barabara wakati jeshi lina wahandisi wengi tu wasiotumiwa ipasavyo.Matokeo yake wanajeshi endapo serikali itakubali kuwatumia wahandisi medani, ni wazi kwamba serikali itatumia fedha kidogo kwa ajili ya kulipa gharama za huduma hiyo.

Nitoe pia changamoto kwa JWTZ kwamba, kama kweli nayo ina nia njema na taifa hili na inapenda kuona miundombinu ya taifa lao ikiimarika, pia nayo ina jukumu la kuikomaria serikali iiwezeshe na kisha iwaruhusu kufanya kazi za kuboresha miundombinu wakati wa amani.

Naamini fedha za kununulia vifaa vya ujenzi wa miundombinu kote nchini tukiwa na nia ya dhati tunaweza kuzipata, kwani nchi yetu ina utajiri mwingi wa rasilimali, ambao tukiutumia vizuri, unaweza kutupatia haraka fedha hizo.

Yawezekana wakawapo watakaosema kuwa jeshi halina vifaa vya kutosha vya kuweza kufanya shughuli hiyo, sawa, lakini hatuoni sababu ya JWTZ kutowezeshwa ili waweze kununua vifaa hivyo ambavyo vitakuwa ni mali yetu ya kudumu na tutakuwa tukivitumia muda wowote tunapovihitaji kuliko hali ilivyo hivi sasa ambako tunatoa tenda kwa wahandisi wa nje ambao huongeza gharama kwa kuingiza vifaa vya ujenzi na bado hujinufaisha kwa kuviuza mara wanapomaliza kazi zao.

Naona wakati umefika kwa serikali ya awamu ya nne ambayo kwa bahati nzuri inaongozwa na Rais Jakaya Kikwete ambaye kabla ya kuingia kwenye ulingo wa siasa alikuwa ni ofisa wa jeshi hili, na wakati akiomba kura kwa wapiga kura aliahidi kuwa atayatupa majeshi yote, aketi kitako kwa kushirikiana na Wizara ya Miundombinu ione jinsi ya kuwashirikisha wahandishi wa jeshi kwenye ujenzi wa miundombinu ya taifa hata wakati wa amani.

Na endapo hilo litafanyika basi litakuwa limesaidia sana wanajeshi wetu kuondokana na ile dhana ya utani wanayaoitumia wawapo mafunzoni au kwenye messi zao wakipata ‘moja moto moja baridi’ ya “3WWWs’.Tafrsi yake ni War,Women and Wine’,yaani mwanajeshi lazima atekeleze kwa vitendo vitu hivyo vitatu ,yaani vita, wanawake na mvinyo.

Ikumbukwe endapo wanajeshi wetu akiwamua kuitekeleza kikamilifu utani huo kwa vitendo ni wazi kabisa wanajeshi wetu wengi watateketea kwa gonjwa la ukimwi.

Rais Kikwete haitoshi kuona ukiteua baadhi ya maofisa wa JWTZ kuwa wakuu wa mikoa na wilaya. Kama ulivyoweza kuteua maofisa hao kuja uraiani kufanya kazi, vivyo hivyo tunataka kuona wahandisi medani wa jeshi hilo wakitumiwa na serikali yako katika shughuli za ujenzi ,ukarabati na ujenzi wa miundombinu ili taifa lipate maendeleo kwa kukimbia kama sote tunavyotamani.

Wanajeshi madaktari na fani nyingine ndani ya jeshi hilo, tunaona hivi sasa wamekuwa wakitumia fani zao vizuri kwa sababu kuna hospitali zinazoeleweka ndani ya jeshi hilo ambazo zimekuwa zikitoa huduma bora za matibabu tena kwa nidhamu hata kwa raia. Na mfano halisi ni kile kikosi cha 521KJ cha Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo Dar es Salaam, kinachoongozwa na Meja Jenerali Salim Salim.

Ni vyema tukumbuke kuwa, mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe, hivyo basi Tanzania itajengwa na Watanzania wenyewe na si wageni. Sote kwa pamoja tujifunge mkanda bila kubaguana katika kushiriki kwenye shughuli za ujenzi wa taifa na naamini tutafanikiwa.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Januari 10 mwaka 2010

CHONDE CHONDE JAJI MKUU

Happiness Katabazi

DESEMBA 15, mwaka jana, Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani, alisema anakusudia kuzungumza na baadhi ya waliokuwa majaji wa Mahakama Kuu (wastaafu) ili wasaidie kupunguza wingi wa kesi zilizoko mahakamani hivi sasa.


Endapo hilo litakubalika, majaji hao wastaafu hawatalipwa mshahara bali watapata malipo kwa kadiri ya idadi ya kesi watakazoziamua. Jaji Mkuu alitoa kauli hiyo siku hiyo wakati wa hafla ya kuwapokea na kuwasajili mawakili wapya wa kujitegemea 20, hafla iliyofanyika katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

“Ninakusudia kuongea na baadhi ya ya majaji wa Mahakama Kuu waliostaafu tukubaliane malipo kwa kesi inayomalizwa. Kama inawezekana nitafikiri kuongea na rais ili ateue mahakimu wakazi waandamizi waliostaafu wawe makaimu jaji ambao hawatalipwa mishahara bali kwa kesi watakazoamua,” alisema Jaji Mkuu Ramadhan.

Alisema kutokana na wingi wa kesi Mahakama Kuu, kuanzia Desemba mosi mwaka jana, aliwateua Majaji wa Mahakama Kuu wote kuwa majaji katika Kitengo cha Ardhi kwa lengo la kuondoa ukiritimba kwa eneo hilo kusikiliza kesi zote.

Akizungumza hilo, Jaji Ramadhani alisema kwamba yanayosubiriwa kwa sasa ni marekebisho ya Sheria ya Ardhi katika sura ile ya 216 kama ilivyofanyiwa mapitio mwaka 2002 ili utekelezaji huo uanze.

Jaji Mkuu huyo ambaye ni Brigedia Jenerali Mstaafu wa JWTZ pamoja na kuwataka mawakili hao kufuata miiko ya kazi yao kwa kuwajali wananchi maskini na mikoani, alizungumzia suala la mlundikano wa kesi na kuahidi kupitia kanuni mpya ya Mahakama ya Rufaa (Court of Appeal Rules, 2009) itakayotumika mwaka huu ili kupunguza tatizo hilo.

Kwanza kabisa napenda nipongeze uamuzi wa Jaji Mkuu wa kuwateua majaji wote wa Mahakama Kuu kuwa Majaji wa Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kwani hakuna ubishi kwamba wananchi wengi waliofungua au waliofunguliwa mashauri katika kitengo hicho wamekuwa wakilalamika ucheleweshwaji wa kutolewa maamuzi kwa mashauri na sababu moja wapo ni uhaba wa majaji wa kuzisikiliza kesi hizo.

Ndiyo maana nikaanza kwa kupongeza hatua hiyo kwani inatasaidia kwa kiasi fulani mrundikano wa kesi.

Lakini pia naomba nitofautiane na kusudio la Jaji Ramadhani la kuzungumza na baadhi ya waliokuwa majaji wa Mahakama Kuu (wastaafu) ili wasaidie kupunguza wingi wa kesi zilizoko mahakamani hivi sasa.

Tujiulize ni majaji na mahakimu wakazi wa aina gani anaotaka kuwarejesha? Na atatumia chujio lipi kuwachuja majaji na mahakimu wasafi na wazalendo kuwarejesha? Kwani si miongoni mwao mahakimu na majaji ndiyo walishindwa kuzimaliza baadhi ya hizo kesi ambazo leo tunazilalamikia kuwa kuna mlundikanao wa kesi mahakamani?

Kuna baadhi ya mahakimu walivyostaafu, baadhi ya wananchi na watumishi wa mahakama walishukuru na kufanya sherehe na kugonganisha bilauri kwani mahakimu hao walikuwa hawazingatii maadili ya taaluma. Ila kwa sababu tu mhimili wetu wa Mahakama hapa nchini haupendi kuwafukuza kazi watumishi wake licha ya kuwa baadhi yao ni wachafu.

Sisi Watanzania tuna haki ya kuletewa watendaji wenye damu inayochemka, wachapakazi na wanaoweza kukabiliana na mikikimikiki. Kuna vijana wengi wamesoma diploma na shahada za sheria wanaweza kuwa mahakimu wazuri tu.

Kwa nini Jaji Mkuu anatafuta njia ya mkato ya kuwatumia wastaafu badala ya mpango endelevu ambao akiutumia ipasavyo mlundikano wa kesi mahakamani utakuwa ni historia?

Kwa nini asione haja ya kuiomba serikali iongeze fedha kwenye mhimili anaouongoza ili kwa kipindi cha masomo cha mwaka ujao, mahakama iweze kupeleka wanafunzi wengi katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), mkoani Tanga, ili waweze kuhudhuria kozi ya uhakimu na wakitoka hapo wapewe ajira ya uhakimu kwenye mahakama zetu?

Jaji Mkuu na watendaji wake hawana njia, bali kuikaba koo serikali iweze kuwaongezea fungu ili mwaka ujao wa fedha , mahakama iweze kuongeza idadi kubwa zaidi ya mahakimu wakazi wengi ukilinganisha na miaka iliyopita.

Binafsi naona itakuwa ni vyema kama uongozi wa mahakama ungetumia mkakati wa muda mrefu ambao utakuwa ni endelevu kwa kufuata njia hizo mbili ambazo naamini mwisho wa siku msongamano wa kesi mahakamani utapungua kwa kiasi kikubwa.

Kwani ni uongozi huu wa mahakama kila kukicha umekuwa ukilia kwamba vyumba vya kuendeshea kesi ni vichache na wakati mwingine unakuta mahakimu wakazi wawili wanatumia ofisi moja na hali siyo tu ipo mikoani, hata pale Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu tunaishuhudia kila kukicha.

Sasa tumuulize Jaji Mkuu, hao wastaafu anaokusudia kuwakodisha ili waje kumaliza mlundikano wa kesi, watakuwa wanakaa kwenye vyumba vipi? Au wataandaliwa vyumba maalumu vya kuendeshea kesi hizo?

Ni kweli baadhi ya majaji na mahakimu wastaafu wamekuwa wakiujua muundo wa mhimili wa mahakama vizuri na ni wazalendo, lakini hatuoni kwamba wakati umefika sasa wa kuwaacha wazee wetu hao wapumzike na badala yake wabaki kuwa washauri wa mahakimu na majaji wa sasa ?

Nchi ni yetu sote mambo yatakapoharibika ni wote tunaharibikiwa, hivyo ni vyema tukawa na mipango ya muda mrefu ili mwisho wa siku iwe endelevu na suluhisho la matatizo fulani fulani. Naelewa wazi Jaji amefikia uamuzi huo kwa moyo wa uzalendo kwa taifa lake lakini nimalizie kwa kumweleza kwamba Watanzania tunahitaji mipango endelevu na itakayomaliza matatizo hayo.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Januari 3 mwaka 2010