BABU SEYA,PAPII WAKWAMA TENA



*Mahakama ya Rufaa yawatupa jela maisha
*Yawaachia huru wawili, Chichi na Mashine
*Wapunguziwa mashitaka kutoka 23 hadi 5
*Watu wahoji; nani alileta sheria duniani?

Na Happiness Katabazi

MWANAMUZI mahiri wa muziki wa dansi nchini, Nguza Viking (Babu Seya) na mwanaye Papii Kocha wameshindwa kujinasua kwenye hukumu ya kifungo cha maisha jela.

Mahakama ya Rufaa Tanzania jana ilikazia hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, lakini iliwaachia huru watoto wawili wa Babu Seya ambao ni Nguza Mbangu (Mashine) na Francis Nguza (Chichi).

Pia imeyatupilia mbali mashitaka 18 kati ya 23 yaliyokuwa yakiwakabili warufani hao kwa maelezo kuwa hayatambuliki katika sheria za nchi.

Licha ya kuwafunga wawili na kuwaachia wawili wengine, hukumu hiyo ilileta simanzi, majonzi, vilio, kwiki na huzuni miongoni mwa watu waliofurika katika maakama hiyo kusikiliza hukumu hiyo jana. Miongoni mwa makumi ya watu waliokuwa mahakamani hapo ni baadhi ya wanamuziki raia wa Kongo.

Akisoma hukumu hiyo kwa niaba ya Jaji Natalia Kimaro, Salum Massati na Mbarouk Mbarouk, Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Neema Chusi alisema kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyotumika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Mahakama Kuu kuwatia hatiani washitakiwa hao, warufani walikuwa wakikabiliwa na makosa 23 ya kubaka na kuwalawiti watoto kumi wa Shule ya Msingi Mashujaa ya jijini Dar es Salaam.

Alisema baada ya jopo hilo la majaji kusikiliza na kuchambua kwa kina ushahidi uliotolewa, walibaini kuwa mashitaka 18 ya kulawiti ambayo walitiwa nayo hatiani hayatambuliki kisheria nchini; wakayafuta.

“Jopo hili baada ya kuipitia sheria namba 4 ya makosa ya kujamiana ya mwaka 1998 imebaini sheria hiyo haiyatambui makosa ya kushirikiana kulawiti, bali sheria hiyo inatambua makosa ya ubakaji. Kwa sababu hiyo mahakama hii inafutia warufani mashitaka hayo 18.

“Hivyo warufani wanabakiwa na mashitaka matano ya kubaka, na kwa mujibu wa ushahidi uliokwishatolewa, jopo hili limeridhika nao, hivyo kuwatia hatiani Nguza Viking na Papi Kocha, na kuwahukumu kifugo cha maisha jela,” alisema.

Hata hivyo, Naibu Msajili alisema ushahidi huo umeshindwa kuthibitisha tuhuma dhidi ya Nguza Mashine na Francis Mbangu, hivyo mahakama inawaachia huru.

Baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo, Francis aliangua kilio kwa sauti ya juu kizimbani, hali iliyosababisha warufani wenzake, ndugu, jamaa na baadhi ya wananchi waliokuwa wakifuatilia kesi hiyo kukimbilia kizimbani kuungana naye kulia.

Hali hiyo ilizua simanzi kwa baadhi ya watu, huku wengine wakisikika wakijiuliza, “ni nani aliyeleta sheria duniani?”

Hata hivyo, warufani wote walichukuliwa na askari magereza na kurudishwa gerezani, ili walioachiwa wakafuate taratibu za makabidhiano na uongozi wa magereza.

Baada ya hukumu hiyo, wakili wa warufani hao, Mabere Marando, alisema mahakama hiyo ndiyo ya mwisho, hivyo fursa pekee wanayoweza kuipata ni msamaha wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa madaraka aliyopewa.

“Kwa tafsiri ya hukumu hii, tumeshinda nusu, na nusu tumeshindwa; kwani mahakama imewafutia wateja wangu mashitaka 18 kati ya 23 na iwaachia warufani wawili na kuwatia hatiani wawili.

“Kwa kweli nasema kwa niaba yao tumeipokea kwa mikono miwili hukumu hii, kwani tumeshinda nusu na nusu tumeshindwa,” alisema Marando huku akipewa mkono wa pongezi na wananchi mbalimbali.

Januari 3 mwaka huu, jopo hilo la majaji watatu likiongozwa na Natalia Kimaro lilisikiliza rufaa hiyo kwa siku moja, na mawakili wa rufani waliomba mahakama iwaachilie huru warufani hao, wakisema hukumu hiyo imejaa dosari nyingi za kisheria.

Mawakili hao, Marando na Hamidu Mbwezeleni, walidai kesi hiyo ilikuwa ni ya kupangwa na kwamba hawajawahi kuona hukumu ya hovyo ya aina hiyo tangu waanze kufanya kazi ya uwakili kwa zaidi ya miaka 30.

Januari 27 mwaka 2005, aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Thomas Mihayo ambaye kwa sasa amestaafu, alitupilia mbali rufaa yao iliyokuwa ikipinga hukumu iliyotolewa na aliyekuwa Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Addy Lyamuya aliyewatia hatiani kwa makosa 23, Juni 25 mwaka 2004.

Waomba rufani hao walikuwa wakikabiliwa na makosa 10 ya kubaka watoto wa kike wenye umri kati ya miaka sita na minane na mengine 11 ya kulawiti watoto wa kike wenye umri kama huo. Walidaiwa kutenda makosa hayo kati ya Aprili na Oktoba mwaka 2003, eneo la Sinza kwa Remmy, Dar es Salaam.

Katika kesi hiyo, Mwalimu wa Shule ya Msingi Mashujaa, Sigirinda Ligomboka, ambaye alishitakiwa kwa makosa mawili ya kumsaidia Babu Seya kutenda makosa hayo kwa kuwaruhusu baadhi ya watoto hao kutoka madarasani, aliachiwa huru na Mahakama ya Kisutu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Februali 12 mwaka 2010

TUNASUBIRI HIVI HUKUMU YA BABU SEYA-MAPAPARAZI




Happiness Katabazi nikiwa na waandishi wenzangu wa Habari za Mahakama nchini, (kulia)ni Rose Mirondo wa Gazeti la The Guardian na Faustine Kapama wa Daily News, jana asubuhi ndani ya ukumbi wa Mahakama ya Rufani Tanzania Dar es Salaam, tukisubiri kuanzwa kusomwa kwa hukumu ya rufaa ya mwanamuziki mahiri nchini Nguza Viking(Babu Seya na wanaye watatu).Hata hivyo mahakama hiyo iliwahukumu kifungu cha maisha jela Babu Seya, Papii Kocha na kuwaachiria huru Francis Mbangu(Chichi)na Nguza Mashine.
Picha imepigwa Februali 11 mwaka 2010.

KESI YA RICHMOND HAINA MLALAMIKAJI-WAKILI

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa utetezi katika kesi ya kashfa ya Kampuni ya kuzalisha umeme ya Richmond, inayomkabili Naeema Adam Gile katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, umecharuka na kudai kuwa kitendo cha upande wa mashitaka kutokuwa na jalada la uchunguzi wa kesi hiyo kwa takriban mwaka mmoja sasa ni sawa na kesi hiyo haina mlalamikaji.


Dai hilo lilitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Waliawande Lema na wakili wa utetezi, Zakhe Katto, muda mfupi baada ya wakili wa serikali, Beatrice Mpangala kuiambia tena mahakama kwamba upande wa mashitaka hauna jalada hilo, kwani bado lipo Jeshi la Polisi.

“Mheshimiwa hakimu mara kwa mara kesi hii inakuja kutajwa na upande wa mashitaka unakuwa ukidai upelelezi haujakamilika na leo umedai hauna jalada la uchunguzi …kama upande wa mashitaka ulivyoiambia mahakama hii kwamba hauna jarada hilo, basi ni wazi kesi inayomkabili mteja wangu haina mlalamikaji,” alidai wakili Katto.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Lema, aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 21 mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na kuamuru upande wa mashitaka siku hiyo uje kuieleza mahakama hatua ya upelelezi umefikia wapi na pia waje na jalada hilo.

Gile ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea, Alex Mgongolwa na Zakhe Katto, alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Januari 14, mwaka jana, na tangu wakati huo kesi hiyo imekuwa ikiahirishwa kwa kile kinachodaiwa kutokamamilika kwa upelelezi.

Januari 14, mwaka jana , ilidaiwa mahakamani hapo na Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface kuwa mshitakiwa huyo anakabiliwa na mashitaka matano ambayo aliyatenda kwa nyakati tofauti.

Wakili Boniface alidai kuwa, Machi 13, 2006, Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa na dhamira ya kutenda kosa, alighushi hati ya nguvu ya kisheria (power of attorney) inayoonyesha imetolewa na Hamed Gile, ambaye ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, kwamba amemruhusu kufanya shughuli za kampuni hiyo hapa nchini.

Alidai kwamba, shitaka la pili ni kutoa taarifa za uongo, kuwa Machi 20 mwaka 2006, katika eneo la Ubungo, Umeme Park, Barabara ya Morogoro, mshitakiwa alitoa hati hiyo ya nguvu ya kisheria inayomuidhinisha yeye kwamba ameruhusiwa kufanya kazi ya kampuni hiyo ya Marekani hapa nchini.

Aliendelea kudai kuwa, shitaka la tatu linalomkabili mtuhumiwa huyo ni kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa umma na kwamba Julai 20, 2004 eneo la Ubungo, Umeme Park, alitoa taarifa ya uongo kwa wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Shirika la Umeme (TANESCO), kwamba Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 100 kwa Tanzania ili wajumbe wa bodi hiyo waweze kumpendekeza kupewa tenda ya kutoa huduma hiyo.

Katika shitaka la nne, Boniface alidai Juni, 2006 jijini Dar es Salaam, mshitakiwa alitoa taarifa za uongo kwa wajumbe wa timu ya majadiliano ya serikali, kuwa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme kwa kiwango hicho ili apewe tenda hiyo.

Wakili Boniface alidai shitaka la tano ni kwamba Julai, 2006, ambapo mshitakiwa akifahamu na kwa ulaghai, alitoa hati ya nguvu ya kisheria iliyotolewa Machi 3, mwaka huo iliyokuwa ikimuonyesha kuwa ameruhusiwa na Mwenyekiti wa Kampuni ya Richmond, Hemed Gile, kufanya kazi za kampuni hiyo hapa nchini.

Gile amefikishwa mahakamani ikiwa ni takriban mwaka mmoja sasa baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kuachia ngazi baada ya Tume Teule ya Bunge kubaini kuwa alihusika katika mchakato wa utoaji zabuni kwa Richmond.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi,Februali 11 mwaka 2010

MGOMBEA BINAFSI YAIVURUGA SERIKALI

•JAJI MKUU ASEMA HUKUMU YA MAHAKAMA IKO PALE PALE

Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Rufani Tanzania imesema hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliyoruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi nchini, itaendelea kuwepo hadi pale mahakama hiyo itakapotoa uamuzi mwingine.


Kiongozi wa jopo la majaji saba, Jaji Mkuu Agustino Ramadhani, alisema hayo jana alipokuwa akiahirisha kusikiliza rufaa ya kupinga mgombea binafsi iliyofunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Mchungaji Christopher Mtikila.

“Rufaa iliyokatwa katika Mahakama ya Rufani nchini ya kupinga mgombea binafsi, haitengui uamuzi wa Mahakama Kuu ulioruhusu kuwepo mgombea binafsi.

“Hivyo taratibu za uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, zitafuata hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu na hivyo ndivyo sheria inavyosema....kwa hiyo mgombea binafsi anaendelea kuwepo hadi Mahakama ya Rufani itakapoamua vinginevyo,” alisema Jaji Mkuu Ramadhani.

Majaji wengine wanaosikiliza rufani hiyo ni Eusebio Munuo, Nataria Kimaro, Januari Msofe, Mbarouk Mbarouk, Sauda Mjasiri na Bernad Ruhanda.

Jaji Ramadhani ambaye ni Jaji Mkuu wa Tanzania, alisema wamesikiliza hoja ya upande wa mkata rufani (Mwanasheria Mkuu wa Serikali) ambaye katika rufaa hiyo aliwakilishwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, aliyekuwa akisaidiwa na Methew Mwaimu na Edson Milungwi ambao waliomba usikilizwaji wa kesi hiyo uahirishwe kwa kuwa hawajafanya utafiti wa kutosha kuhusu rufaa hiyo.

Jaji Ramadhani aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 8 itakapokuja kusikilizwa.

Awali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Masaju, alidai rufaa hiyo inaenda kuweka historia katika Katiba na sheria za nchi, hivyo kuomba mwongozo wa mahakama ni kwa nini rufaa hiyo inasikilizwa na jopo la majaji saba badala ya watano au watatu kama ibara ya 118(1) na 122(1) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inavyotaka.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Jaji Mkuu na Naibu Mwanasheria Mkuu
Jaji Mkuu:
Nikuulize katika uelewa wako jopo la majaji watano wa mahakama ya rufani linakaa wakati gani?

AG:
Majaji watano wanakaa baada ya majaji watatu kukaa na jopo hilo la majaji watano linafanyia marejeo uamuzi wa majaji watatu kama kulikuwa na malalamiko ya uamuzi uliotolewa na majaji watatu.

Jaji Mkuu: Kesi ikishafunguliwa Mahakama ya Rufani haikatiwi tena kitakachofanyika ni kufanyiwa mapitio ya uamuzi sasa sijui tatizo hapa linatoka wapi! Na Mgombea binafsi ni suala kubwa nchini na ndiyo maana mahakama yetu imepanga idadi kubwa ya majaji na Mahakama ya Rufani ina mamlaka hayo...sasa sijui tatizo linatoka wapi.

AG: Basi Jaji Mkuu nimekuelewa naondoa hoja.

Masaju alidai Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ndiyo iliyokata rufaa na waliwapatia hoja kwa vielelezo upande wa wadaiwa Ijumaa iliyopita na wao wakaturudishia majibu Jumamosi na aliyepewa ni Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali, Mwaimu, ambaye anauguliwa.

Kwa upande wake, wakili wa utetezi, Richard Rweyongeza, anayesaidiana na Mpale Mpoki alikiri kupatiwa vielelezo kwa maandishi na upande wa mkata rufani na kwamba wao waliitumia siku ya Jumamosi na Jumapili iliyopita kujiaandaa na wako tayari kuendelea kusikilizwa kwa rufaa hiyo.

Jaji Mkuu: Hivi course list (ratiba ya kikao cha Mahakama ya Rufani) ilitoka lini?

AG: Januari 28 mwaka huu.

Jaji Mkuu: Sasa kilichoifanya ofisi ya AG, muwa-‘save’ wadaiwa hivyo vielelezo vyenu Ijumaa iliyopita ni kitu gani? Na suala la Mwaimu kuuguliwa na baba yake tafadhari naomba liwekwe kando sasa.

AG: Mh! Mheshimiwa Jaji Mkuu hata jopo lako limekubali rufaa hii ni nzito....hivyo bado tunafanyia utafiti hoja zetu tutakazoziwasilisha katika rufani hii.

Jaji Mkuu: Hivi si ni serikali ndiyo iliyokata rufaa, ina maana siku zote hizo hamkufanya utafiti na kama leo hii (jana) mnadai bado hamjafanya utafiti na zile sababu sita mlizoziwasilisha kwenye rufaa yenu nazo ina maana pia hamkuzifanyia utafiti? Na mnakataje rufaa bila kufanya utafiti?

AG: Mhh (kimya).

Jaji Mkuu: Swali langu linabaki palepale inakuaje ofisi ya AG iu-‘save’ vielelezo upande wa mdaiwa Ijumaa iliyopita?

AG: Mhh! Tunaepuka malalamiko kwamba wanasheria wa serikali tumekuwa tukifungua kesi bila kufanya utafiti wa kutosha. Na tunaomba msajili wa Mahakama ya Rufani aipange rufaa hii katika kikao kijacho.

Jaji Mkuu: Kwani Msajili wa Mahakama ya Rufani atajuaje kama mmeishamaliza kufanya utafiti wenu? Kwani Msajili wa Mahakama ya Rufaa akiwa anapanga course list huwa anaihusisha ofisi ya AG?

AG: Hapana.

Jaji Mkuu:
Inasikitisha sana kuona kauli hiyo inatolewa na Naibu Mwanasheria Mkuu anayetokea ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, yaani nyie ndiyo mmekata rufaa halafu mnasema hamjajiandaa! Wenzenu wa utetezi mmewapatia vielelezo vyenu na wamejiandaa ndani ya siku mbili...halafu nyie wanasheria wa serikali ndiyo mnaoingoza bar (meza ya mawakili wa pande zote mbili) sasa sijui mnaongoza nini (watu wakaangua vicheko).

AG: Mi’ najitetea, mi’ niliteuliwa hivi karibuni kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Jaji Mkuu: Hakuna cha kujitetea hapa. Jopo liko tayari kuahirisha usikilizaji wa rufaa hii sasa nyie semeni tuiahirishe hadi lini?

AG: Tunaomba miezi minne ijayo kuanzia leo.

Jaji Mkuu: Tunaiarisha rufaa hii hadi April 8.

Kwa mujibu wa rufaa hiyo namba 45 ya mwaka jana, inaonyesha serikali iliwasilisha rufaa hiyo, mwishoni mwa Juni mwaka jana, mahakamani hapo ikipinga hukumu iliyotolewa na waliokuwa majaji wa Mahakama Kuu, ambao ni Jaji Mstaafu Amir Manento, Salum Massati (Jaji wa Mahakama ya Rufani) na Thomas Mihayo (Mstaafu), ambao walikubaliana na ombi na Mtikila na kuruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi nchini.

Katika rufaa hiyo, serikali imetoa sababu sita za kukata rufaa hiyo zikiwemo: Mahakama Kuu ilikosea kujipa mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo; ilikosea kutengua vifungu vya Katiba ya nchi; na ilikosea kisheria kwa kupunguza matakwa ya lazima ya Ibara 30(5) na 13(2) ya Katiba ya nchi.

Sababu nyingine ni kujipachika mamlaka ya kibunge ya kutunga sheria, kukosea kisheria kwa kuiweka Katiba ya nchi katika vyombo vya kimataifa na pia ilikosea kuitolea maamuzi kesi hiyo bila kuweka suala hilo bayana.

Mara ya kwanza, serikali ilikata rufaa dhidi ya hukumu ya Mahakama Kuu, katika mahakama hiyo ya rufaa mwaka 2007, ambapo ilidai mahakama hiyo ya chini ilikosea kisheria kutafsiri Ibara ya 21(1)(c), 39(1)(c) (b) na 69(1)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977.

Hata hivyo, rufaa hiyo ilitupwa na Mahakama ya Rufaa baada ya mahakama hiyo kukubaliana na ombi la wakili wa Mtikila, Richard Rweyongeza, kwamba rufaa hiyo haina msingi na kwamba imejaa dosari za kisheria.

Awali katika hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa Mei 2006, iliruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi katika uchaguzi, kwa sababu Katiba ya nchi inatoa haki hiyo.

Mahakama Kuu ilibainisha kuwa Katiba inatamka wazi kuwa kila mwananchi ana haki ya kuchagua au kuchaguliwa kuwa kiongozi na haiweki masharti kuwa hilo lifanyike kwa mtu kujiunga na chama fulani.

Mwaka 1993, Mtikila alishinda kesi kama hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, lakini licha ya uamuzi huo wa mahakama, Bunge lilishindwa kutunga sheria ya kuruhusu mgombea binafsi hivyo alifungua kesi hiyo ya Kikatiba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kushinda tena.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Februali 9 mwaka 2010

BABU KURUDI URAIANI KESHO?

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE mahakama ya Rufani nchini kesho inatarajia kutoa hukumu ya mrufani ambaye ni mwanamuziki mahiri wa muziki wa dansi nchini, Nguza Viking maarufu kwa jila la ‘Babu Seya’ na wanaye watatu.


Mbali na Babu Seya, warufani wengine ni Papii Kocha Nguza,Nguza Mbangu na Francis Nguza ambao wanatatewa wakili wa kujitegemea Mabere Marando na Hamidu Mbwezeleni toka Zanzibar.

Kwa mujibu wa hati za wito(summon) zilizotolewa na Msajili wa Mahakama ya Rufani, Francis Mutungi kwa Wakili wa wa wa kuitwa mahakamani kesho kwaajili ya kusikiliza hukumu itakayotolewa na mahakama hiyo, kwa Wakili wa warufani Mabere Marando na uongozi wa Gereza la Ukonga ambapo katika gereza hilo ili siku huyo uongozi wa gereza hilo uweze kuwaruhusu warufani hao kufika mahakamani kusikiliza hukumu yao.

Akilithibithitishia gazeti hili wakili Marando alisema:”Ni kweli leo (jana)nimepokea hati ya wito(summons)toka mahakama ya Rufani ikiniarifu mimi na wateja wangu tufike asubuhi katika mahakama hiyo ili tuweze kusikiliza hukumu itakayotolewa na majaji watatu ambao ndiyo walikuwa wakiliza rufaa yetu:

“Na ninakuhakikishia kwamba tayari wateja wangu(warufani)wameshapelekewa hati hiyo ya wito kule gerezani Ukonga na tumejiandaa kwenda kusikiliza na kuipokea kwa mikono miwili hukumu hiyo ambayo inavuta hisia za watu wengi”alisema Wakili Marando ambaye ni wakili maarufu nchini.

Januari 3 mwaka huu, jopo la majaji wa tatu wa mahakama ya rufani wanaongozwa na Jaji Nataria Kimaro, Salum Massati na Mbarouk Mbarouk walisikiliza kesi kwa siku moja rufaa hiyo ambapo mawakili wa rufani waliomba mahakama hiyo iwaachirie huru warufani hao kwani hukumu zilizowatia hatiani zilikuwa zimejaa dosari nyingi za kisheria.

Mawakili hao walidai kuwa kesi hiyo ilikuwa ni yakupangwa na kwamba hawajawahi kuona hukumu ya ovyo ya ina hiyo tangu waanze kufanyakazi ya uwakili kwa zaidi ya miaka 30 sasa.

Mawakili hao waliwasilisha sababu nne za kupinga rufaa ya Mahakama Kuu iliyotolewa na Jaji mstaafu, Thomas Mihayo na hukumu ilioyotolewa na aliyekuwa Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Addy Lyamuya, ambao wote waliwatia hatiani washitakiwa kwa makosa ya kujamiana na hivyo kuwafunga kifungo cha maisha jela.


aji na hakimu huyo kwakusema hayo hakitaka hukumu zao walikosea kisheria kwani sheria inaitaka mahakama kabla haijaanza kuchukua ushahidi wa mtoto ni lazima ijiridhishe mtoto huyo anaakili timamu na anaelewa maana ya kiapo na kisha irekodi hayo kwenye jarada la kesi lakini Hakimu Lyamuya hakufanya hivyo wala kuandika rekodi ya hayo”alida Marando.

Marando akiwalisha sababu hizo kwa kujiamini alidai kuwa kwa makosa hayo ya kisheria yaliyofanywa na hakimu na Lyamuya huyo hadi wakafikia uamuzi wa kufunga kifungo cha maisha warufani, ni wazi kabisa walikuwa wanapinga na sheria za nchi na maamuzi yaliyotolewa na majaji wa mahakama za hapa nchini kwenye kesi mbalimbali , ambazo alizitumia kusapoti hoja zake.

“Lakini majaji katika rufaa ya Mahakama Kuu hakuna ushahidi ulitolewa unaonyesha warufani walibaka...hayo yalikuwa ni mawazo ya hakimu kwamba lazima Babu Seya na watoto wake waende gerezani....narudia tena sijawahi kuona hakimu wa aina hii na hukumu ya aina hii ambayo hakimu aliamua kuweka maoni yake binafsi kwani kinachowatia hatiani washitakiwa katika kesi zote ni ushahidi nasiyo maoni ya hakimu”

“Ni wajibu wa mahakama kutafakari ushahidi wa utetezi hata kama hauana uzito sasa huyu Lyamuya katika hukumu yake amewataja mashahidi wa utetezi waliokuja kutoa ushahidi bila kueleza mashahidi kwa mapana walieleza nini”

“Kwa mkanganyiko huu uliofanywa na Hakimu Mkazi Mwandamizi Lyamuya siyo tu alikosea kisheria nasema alifanya makusudi na alikuwa ameshaamua kuwapeleka jela warufani” alidai Marando kwa hisia kali.

Alihoji ni kilichofanya upande wa mashitaka kuficha ripoti ya daktari aliyewafanyia uchunguzi watoto hao wanaodaiwa walibakwa na warufani na kushindwa kuleta mashahidi ambao ni wanamuziki wa Bendi ya Achigo, mama wa Babu Seya na Mke wa Babu seya kwasababu waliona mashahidi hao wangewaumbua.

“Kesi hii ni ngumu kweyu sote na kama mahakama na sisitunaona warufani walifanya haya makosa tuwalaani ila mimi Marando nasema nimejiridhisha hawajafanya hayo makosa:

“Hivi tujiulize Kibaiolojia kweli inawezekana mtoto wa miaka sita apakwe na wanaume hawa(warufani)nyuma na mbele halafu mtoto wa umri huo aweze kutembea?Aiingii akilini hata kidogo nasema kesi hii ni ya kutunga kwani hata mwanamke mwenye umri wa utu uzima akifanyiwa unyama huo hawezi kutembea.”alidai Marando na kusababisha umati uliofurika kuendelea kuacha vinywa wazi kwa mshangao.

Akijibu hoja za mrufani, wakili Mkuu wa Serikali Justus Mulokozi ambaye alitumia nusu saa kujibu hoja hizo alidai kuwa kitendo cha shahidi kushindwa kumtambua mshitakiwa mahakamani siyo sababu inayopeleka ushahidi wa shahidi huyo kuonekana hauna thamani, jibu lilosababisha umati wa watu kuangua vicheko.

Mulokozi alidai pia mahakama ikiamini upande mmoja, halazimiki kuangalia upande mwingine lakini hata hivyo hoja hiyo ilipingwa vikali na Marando ambaye alidai kuwa hoja hiyo haikupaswa kutolewa na wakili mwandamizi kama Mulokozi kwani hoja hiyo inatofautiana na sheria za nchi na kauli hiyo ya wakili wa serikali imedhiirisha sasa ni kweli Lyamuya aliegemea uegemea ushahidi wa upande wa mashitaka tu.

Januari 27 mwaka 2005, aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Thomas Mihayo ambaye kwa sasa amestaafu alitupilia mbali rufaa yao iliyokuwa ikipinga hukumu iliyotolewa na aliyekuwa Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,Addy Lyamuya ambaye aliwatia hatiani kwa makosa yote waliyokuwa wameshitakiwa nayo Juni 25 mwaka 2004.

Waomba rufani hao wanakabiliwa na makosa kumi ya kubaka watoto wa kike wenye umri kati ya miaka sita na nane na makosa mengine 11 ya kulawiti watoto wa kike wenye umri kama huo na kwamba wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya April na Oktoba 2003 eneo la Sinza kwa Remmy, jijini.

Aidha katika kesi hiyo mwalimu wa shule ya Msingi Mashujaa, Sigirinda Ligomboka, alishitakiwa kwa makosa mawili ya kumsaidia Babu Seya kutenda makosa ya kubaka na kulawiti kwa kuwaruhusu baadhi ya watoto hao kutoka madarasani.

Upande wa mashitaka ulileta mashahidi 24, ambao upande wa utetezi ulipinga vikali kutenda makosa hayo na uliita mashahidi nane.Katika hukumu yake Hakimu Lyamuya alitupilia mbali na utetezi wa Babu Seya na wanawe na akawatia hatiani kwa makosa hayo na hivyo kuwafunga kifungo cha maisha jela.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Februali 10 mwaka 2010

KESI YA LIYUMBA:NAIBU GAVANA AIBUA MAMBO MAZITO

Na Happiness Katabazi

NAIBU Gavana wa Benki Kuu (BoT), Juma Reli (54), ameshindwa kuithibitishia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuhusu hasara iliyopatikana katika mradi wa ujenzi wa minara pacha kwa sababu hadi sasa ripoti ya mwisho ya matumuzi ya fedha za mradi huo haijakamilika.

Sambamba na hilo, katika hali isiyotarajiwa, upande wa mashitaka katika kesi hiyo umesema unakusudia kupunguza idadi ya mashahidi wake kutoka 15.

Naibu Gavana huyo ambaye ni shahidi wa nane wa upande wa mashitaka katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, alitoa maelezo hayo jana mbele ya kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi, Edson Mkasimongwa, Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa baada ya wakili wa utetezi, Majura Magafu na Hudson Ndusyepo kutaka ufafanuzi.

Kesi hiyo ya matumizi mabaya katika ofisi ya umma inamkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa benki hiyo, Amatus Liyumba,.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano baina ya mawakili wa utetezi na shahidi huyo:

Wakili: Lini umeajiriwa BoT?

Shahidi: Niliteuliwa kuwa Naibu Gavana Februari 2005 na ndipo nilipoanza rasmi kufanya kazi katika BoT.

Wakili: Unajua mradi huu wa ujenzi wa minara pacha ulianza lini?

Shahidi: Sikumbuki sawa sawa.

Wakili: Utakubaliana nami kimsingi wakati unaanza kufanya kazi hapo, mradi huo ulikuwa umefikia hatua za mwisho?

Shahidi: Ni kweli mradi niliukuta katikati.

Wakili: Utakubaliana na mimi hayo mabadiliko ya nyongeza yanazolalamikiwa na upande wa mashitaka, hilo zoezi lilikuwa limeishapita?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Ni mabadiliko ya nyongeza katika mradi huo yalifanyika wakati wewe upo BoT, unayajua?

Shahidi: Mradi huo ni mkubwa, siwezi kukumbuka.

Wakili: Ni nani alikuwa na maamuzi ya mwisho ya hili lifanyike au hili lisifanyike?

Shahidi: Gavana.

Wakili: Nani alikuwa na maamuzi ya mwisho ya kuidhinisha mabadiliko ya mradi na fedha?

Shahidi: Ni bodi ya wakurugenzi ambayo mwenyekiti wake ni gavana.

Wakili: Je, mkurugenzi wa idara zozote pale BoT anaweza kutoa maamuzi bila gavana na bodi kujua?

Shahidi: Hapana.

Wakili: Kuna kipindi chochote wakati mradi huu unaendelea Liyumba aliwahi kuandika maombi ambayo hayaendani na matakwa ya menejimeti?

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili: Kuna kipindi chochote wakati wewe ukiwa Naibu Gavana, wewe binafsi na gavana mliwahi kupeleka maombi kwenye bodi yakakataliwa?

Shahidi: Hatujawahi kupeleka.

Wakili: Kwa hiyo Liyumba alikuwa anapata maelekezo ya ujenzi kutoka kwa Meneja Mradi Deogratius Kweka?

Shahidi: Ndiyo.

Wakili: Kuna siku Mkurugenzi wa Fedha wa benki hiyo aliwahi kulalamikia matumizi mabaya ya fedha katika huo mradi?

Shahidi: Sikumbuki (watu wakaangua vicheko).

Wakili: Nyie kama BoT, huu mradi umeleta madhara kwenu?

Shahidi: Haujaleta madhara kabisa.

Wakili: Hadi hapa tulipofikia kuna hasara yoyote imepatikana kutokana na ujenzi wa mradi huo?

Shahidi: Siwezi kusema wala kuthibitisha hasara eti imetokea katika mradi huo kwa sababu hadi hivi sasa ninapotoa ushahidi ripoti ya mwisho ya matumizi ya fedha za ujenzi wa mradi huo ‘Finacial Account’ haijakamilika. (watu wakaangua vicheko).

Mahojiano kati ya Hakimu Mkazi na shahidi huyo yalikuwa kama ifuatavyo:

Hakimu: Shahidi kumbuka mshitakiwa (Liyumba) ameshitakiwa kwa kesi ya kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, sasa mahakama hii tunatafuta uthibitisho wa kiasi hicho kutoka pande zote mbili za kesi hii?

Shahidi: Sipendi kudanganya ila ukweli ni kwamba hatuwezi kuthibitisha hasara kwa sababu Financial Account haijakamilika.

Hakimu: Ulisema mradi huu haukupitia kwenye menejimenti, ulipitia moja kwa moja kwenye bodi ya wakurugenzi, ieleze mahakama ulifikajefikaje kwenye bodi na ni Liyumba yeye kama yeye ndiye aliupeleka?

Shahidi: Kama nilivyokwishaeleza, gavana ana nguvu za kisheria. Jambo linaweza kutoka idara fulani akalipitisha bila ya kuwepo kwa wajumbe wengine wa bodi au menejimenti na kisheria anaruhusiwa.

Baada ya shahidi kumaliza kutoa ushahidi wake, Wakili wa Serikali, Juma Mzarau, aliiomba mahakama hiyo iahirishe kesi hiyo hadi Februari 4-5 mwaka huu, kwani wanatarajia kupunguza idadi ya mashahidi kutoka mashahidi 15.

Aliieleza mahakama kwamba kuna shahidi wanayemtegemea kutoka nchini Singapore na waliihakikishia mahakama kuwa katika siku hizo wataleta mashahidi watu wa mwisho.

Hata hivyo wakili wa utetezi, Magafu alidai upande wa mashitaka haupo makini na kazi yao na kuongeza kuwa kama watakubaliana na kesi hiyo ikiahirishwa hadi tarehe hiyo, basi uhakikishe unawaleta mashahidi hao bila kukosa, la sivyo siku hiyo wafunge kesi yao.

Aidha, Kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi, Edson Mkasimongwa, alikubaliana na ombi hilo na kwa mujibu wa ratiba ilipangwa itaanza kusikilizwa mfululizo kuanzia jana hadi Februari 5, mwaka huu.

Aidha, aliamuru upande wa utetezi upewe nakala ya mwenendo mzima wa kesi ili waweze kujiandaa kwa ajili ya kujibu hoja kama mshitakiwa ana kesi ya kujibu au la.

Liyumba alifikishwa mahakamani hapo Januari 26, mwaka jana akikabiliwa na makosa mawili ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Hadi sasa Liyumba yupo rumande kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 27 mwaka 2010