SERIKALI YAMNG'ANG'ANIA LIYUMBA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa jamhuri katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imuone mshitakiwa ana kesi ya kujibu.


Ombi hilo liliwasilishwa mahakamani hapo jana saa tisa alasiri kwa njia ya maandishi yaliyochukua kurasa 29 na Mkuu wa Kitengo cha Sheria cha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ben Lincoln na wakili wa serikali Prosper Mwangamila.
Kuwasilishwa kwa ombi hilo kulitokana na amri iliyotolewa Machi 15, mwaka huu, na kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi wanaosikiliza kesi hiyo, Edson Mkasimongwa ambaye alizitaka pande zote kuwasilisha maombi kwa njia ya maandishi.

Kwa mujibu wa nakala ya ombi hilo ambalo gazeti hili lina nakala yake, upande wa jamhuri umedai kwa mujibu wa vielelezo 12 walivyotoa mahakamani na mashahidi wanane waliowaleta, wameweza kutoa ushahidi thabiti dhidi ya mshitakiwa ambao utaishawishi mahakama hiyo imuone ana kesi ya kujibu na kuongeza kuwa wanaiomba mahakama hiyo itupilie mbali ombi la utetezi lililotaka mahakama imuone mshitakiwa huyo hana kesi ya kujibu kwa sababu halina msingi.

Wakichambua shitaka la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma kinyume na kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, jamhuri imejigamba kuwa imeweza kuthibitsha shitaka hilo kwa sababu mshitakiwa huyo ni kweli alikuwa mtumishi wa serikali toka mwaka 1971-2007 na kwamba alikuwa na cheo wakati wa mradi wa 10 Milambo Office Extention na alikuwa na jukumu la kuusimamia na kwamba kwa mujibu wa shahidi 1, 2, 3, 5, 6 na 8 waliithibitishia mahakama kuwa mradi huo ulikuwa ukiratibiwa na ofisi aliyokuwa akiongoza Liyumba ya Utumishi na Utawala.

Wakichambua shitaka la pili la kuisababishia serikali hasara, upande wa jamhuri umejigamba kuwa umeweza kuthibitisha shitaka hilo kwa madai kuwa hoja iliyodaiwa na upande wa utetezi kuwa haiwezekani kutambua hasara iliyopatikana bila ripoti ya mwisho ya mradi kukamilika si ya msingi kwani hata ikitolewa haiwezi kubadili makadirio ya gharama za mradi.

‘Kwahiyo hoja kwamba ripoti ya mwisho ya mradi haijatoka na kwamba hiyo ndiyo ingetuwezesha sisi kujua kuna hasara imepatikana si ya msingi..kwani hata hiyo ripoti ya mwisho ya mradi ikitolewa leo haiwezi kubadili gharama zilizokadiliwa na Mkadiliaji majengo hivyo sisi tunagemea ushahidi uliotolewa na shahidi wa saba na tunasisitiza kwamba mshitakiwa huyo ameisababishia serikali hasara kwa kufanya ongezeko la mabadiliko ya mradi na hivyo ongezeko hilo limesababisha serikali kutumia fedha nyingine za ziada kwaajili ya ujenzi huo”alidai.

Kuhusu hoja ya upande wa utetezi iliyodai upande wa mashitaka umeshindwa kuthibisha kwamba mshitakiwa huyo alitenda makosa hayo akiwa na nia ovu, umedai kuwa katika kesi za jinai hoja hiyo haina msingi.

Machi 22 mwaka huu, mawakili wa utetezi Majura Magafu, Onesmo Kyauke, Hudson Ndusyepo na Jaji Mstaafu Hillary Mkate waliwasilisha hoja zao wakitaka mahakama hiyo imuachilie huru mshitakiwa huyo kwa sababu upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha kesi yao.

Kwa sababu tayari pande zote mbili katika kesi hiyo zimekwisha wasilisha hoja zao, kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi, Mkasimongwa, Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa, April 9 mwaka huu, wanatarajiwa kutoa uamuzi wao kuhusiana na hoja hizo.

Januari 27, mwaka jana, Liyumba na Meneja Mradi wa Benki Kuu, Deogratius Kweka, walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kusomewa mashitaka hayo ya kuidhinisha mradi wa majengo ya minara pacha bila idhini ya bodi ya wakurugenzi na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Mei 27 mwaka jana, mahakama hiyo iliwafutia kesi, lakini muda mfupi baada ya kuachiliwa walikamatwa tena mahakamani hapo na Mei 28 mwaka jana, Liyumba peke yake ndiye aliyerudishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka hayo na Kweka akawa ameachiliwa huru. Tangu kipindi hicho hadi sasa Liyumba anaendelea kusota rumande, baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, ambapo mahakama ilimtaka atoe fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya sh bilioni 111

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi 30 mwaka 2010

NDEMBO:KIKWETE POKEA PICHA


Peter Ndembo akimkabidhi rais Jakaya Kikwete picha aliyoichora ambayo inasura ya rais huyo.Alimkabidhi picha hiyo kwenye hafla iliyofanyika kwenye viwanja vya Ikulu Dar es Salaam, Machi 15 mwaka huu.(Picha na Francis Dande).

PETER NDEMBO:MCHORAJI ALIYEMDUWAZA JK


MAPEMA wiki iliyopita Rais Jakaya Kikwete alijikuta akipigwa butwaa, baada ya kukabidhiwa picha yake iliyochorwa kwa ustadi wa hali ya juu na mzee Paul Peter Ndembo (64).Mwandishi Wetu Happiness Katabazi aliyefanya mahojiano na mchoraji huyo, anaelezea siri ya mafanikio yake na jinsi alivyofanikisha azima ya kuifikisha picha hiyo mikononi mwa Rais Kikwete.

“Picha yenye sura ya Rais Jakaya Kikwete na Mwalimu Julius Nyerere ambazo nilimkabidhi rais siku hiyo pale Ikulu, nilizichora mimi mwenyewe kwa mkono wangu na hazikwenda pale kwa ajili ya biashara.

“Ukweli ni kwamba picha zile nilikwenda kumkabidhi Rais Kikwete ili zikae katika jengo la Ikulu na zitumike kuipamba Ikulu. Huo ndio mchango wangu mchango wangu kwa Ikulu yetu,” anaanza kwa kusema mzee Ndembo.

Swali: Hapa Tanzania wachoraji ni wengi na wengi wamekuwa wakimchora rais na viongozi wengine wa kitaifa. Unaweza kutueleza kwanini uliamua kuzipeleka picha zako Ikulu?
Jibu: Kwanza ieleweke zile picha nilizomkabidhi rais wetu, zilinichukua muda mrefu kuziandaa na kuzikamilisha kuliko picha zote nilizowahi kuzichora maishani mwangu.
Picha ya Kikwete imenichukua takriban mwezi mmoja na kisha kuihifadhi nyumbani kwangu na hata ukiangalia fremu zake, utabaini kuwa niliziandaa kwa heshima sana kwa kujua siku moja zitaenda kupamba Ikulu yetu.
Lakini likanijia wazo la kuziweka wazi kabla ya kuzifikisha Ikulu ili jamii izione. Mtu ambaye niliona anaweza kuziangalia na kumshawishi ili azima yangu ya kuzifikisha Ikulu itimie ni Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika.
Niliamua kumpelekea picha hizo mwanzoni mwa Februari mwaka huu. Mkuchika alipoziona, aliniambia nimefanya kazi nzuri na akaniahidi kwamba lazima picha zile zipelekwe Ikulu kwa Rais Kikwete.
Basi, waziri baadaye akafanya mawasisilino na Ikulu na hatimaye nilipangiwa siku ya kwenda nazo Ikulu na kumkabidhi rais. Hakika nimefarijika sana kwani nimetimiza ndoto yangu ya kutaka kuipamba Ikulu yetu.

Swali: Kwanini unapenda kuchora picha za wanasiasa?
Jibu: Nachora picha nyingi, lakini hasa picha za viongozi wa siasa kwa sababu zinakuwa kumbukumbu kubwa ya viongozi waliopo na wastaafu.
Na katika hilo inaonyesha ni jinsi gani tunathamini michango ya viongozi hao. Ikulu yetu na ofisi nyingi za serikali kama mawizara zimejaa picha za viongozi zilizopigwa.

Nilipotembelea Ikulu ya Korea Kaskazini na Uganda miaka ya nyuma, niliona ukutani zimebandikwa picha za viongozi wa nchi zilizochorwa na wasanii wa nchi husika.
Ni picha za kuvutia na hazichoshi kuzitazama, tofauti na picha za kupigwa na kamera hata kwa kutumia kamera za kisasa.

Swali: Tangu ulipomkabidhi Rais Kikwete ile picha uliyoichora sura yake, baadhi ya wananchi wamekuwa wakipiga simu kwenye chumba chetu cha habari wakidai si picha ya kuchora. Unalisemeaje suala hilo?
Jibu: Si kweli kwamba picha ile ni ya kupigwa na kamera. Naomba kuwathibitishia wenye hofu hiyo kwamba, picha ile nimeichora mimi kwa kuigiza moja ya picha za rais zilizotumika kwenye kampeni wakati wa uchaguzi mkuu uliopita.
Hivyo nilichukua ‘pozi’ la rais kutoka kwenye picha halisi na kuibadilisha kitaalamu.

Kuna vitu vichache nilivifanya katika picha ya rais, moja ni kuongeza nywele nyingi kwenye picha ya kuchora tofauti na picha halisi.
Macho yake kwenye picha niliyoichora, nimeyafanya yamekuwa angavu, sikio lake linaonekana kukolea rangi ya blauni na koti la sasa lina rangi ya daki blue wakati katika picha halisi, linaonekana alikuwa na rangi ya kijani na nyuzi zilizotumika kutengeneza kitambaa kile cha koti zilikuwa zikionekana, lakini kwenye picha yangu hazionekani hivyo.

Kwa kifupi, picha niliyoichora na kumkabidhi rais, ukiiangalia vizuri inajionyesha kabisa kwamba ni ya kuchora ila kutokana na ustadi nilionao, inaweza kukuchukua muda kubaini hilo.
“Nawashangaa sana hao wanaopinga kwamba ile picha si ya kuchora, kwani hata kuiona kwa macho yao hawajaiona, wameishia kuona runingani,” alisema.

Swali: Unapendelea kuchora picha za aina gani?Jibu: Ninachora portraits (sura za watu), nachora picha za maharusi bila maharusi kujua na siku ya harusi kamati za harusi hizo wanawakabidhi maharusi picha kama surprise, nachora picha za wafiwa.
Kwa mfano kuna watu waliofiwa na waume au wake zao, wapo waliokuja kwangu wakitaka picha za kuchorwa za wenzi wao kama kumbukumbu, nami hufanya hivyo.
Pia nachora picha za stempu na kwa sasa ninapewa kazi ya kuchora stampu na Shirika la Posta. Shirika la Posta liliikubali kazi yangu likaamua kuingia nami mkataba hadi sasa.

Nikishachora shirika hilo hupeleka michoro hiyo nje ya nchi kwa ajili ya kuchapisha stempu tunazotumia.

Ndembo alianza kuchora picha za stempu mwaka 1978, ambazo alizichora picha za maadhimisho ya CCM kutimiza mwaka mmoja. Baada ya hapo alitumika kuchora stempu za matukio mbalimbali.

Kwa mfano amewahi kuchora stempu za sensa, stempu za uskauti, stempu za Azimio la Arusha, stempu za michezo ya Olimpiki, stempu za miaka kumi ya SADC, stempu za uwindaji wa asili, stempu za miaka 20 ya Mapinduzi ya Zanzibar, stempu za ujio wa Papa Paul John wa Pili na zingine nyingi.

“Kwa ujumla uchoraji wa stempu una umuhimu wake kwani stempu huhifadhi picha za matukio ya kihistoria, pia stempu huelimisha watu wa nje matukio mbalimbali yanayotokea hapa nchini,” anasema.

Kutokana na umuhimu huo, Ndembo anasema kuchora stempu kulihamasisha baadhi ya Watanzania kuanzisha chama cha ukusanyaji stempu ambacho yeye mwenyewe alikuwa katibu.

Lengo la kukusanya stempu za ndani na nje, lilikuwa kwa ajili ya kufanya maonyesho ya stempu na kutoa elimu inayohusiana na stempu kwa wanafunzi nchini.


Kabla ya kushughulika na sanaa ya uchoraji wa stempu alitumiwa sana na Umoja wa Vijana wa CCM kuchora picha katika matamasha mbalimbali, kazi hiyo ilimchukua hadi kwenye matamasha yaliyofanyika Libya, Urusi na Korea Kaskazini, ambako waliandaa maonyesho ya kazi za sanaa za Tanzania, ambayo yalizinduliwa na Rais wa Awamu ya Kwanza, Julius Nyerere.

Mwaka 1987, picha alizozichora katika ukumbi uliofanyika mkutano mkuu wa CCM Kizota mjini Dodoma, zilimletea sifa ya hali ya juu na kuanzia hapo alizidi kupata kazi za uchoraji.

Swali: Unaridhika na maendeleo uliyofikia katika shughuli zako za uchoraji?
Jibu: Naridhika na maendeleo niliyofikia ila hata hivyo kazi yangu pia ina matatizo yake.

Moja ya matatizo hayo ni ukosefu wa vitendea kazi vya kutosha. Kwa mfano, nina kamera moja ya kisasa lakini haitoshi.
Nataka niwe na kamera zitakazoniwezesha kutembelea mbuga za wanyama ambako nitaweza kupiga picha za sura za wanyama kwa kadiri ya matakwa yangu na kuzichora
Swali: Unavutiwa na mchoraji gani kwa sasa hapa nchini au nje?

Jibu: Navutiwa sana na mchoraji wa nje aitwaje Leonardo Da Vichi. Huyu ni msanii wa zamani aliyechora picha ya Monalisa 1503-1506.
Huyu ndiye mchora ninayempenda mimi kwani kazi zake zinavutia sana na natamani kuwa kwenye kiwango chake.

Swali: Unawashauri nini wachoraji wenzako?
Jibu: Nawashauri wasiigane katika mitindo yao ya uchoraji kwa sababu si rahisi wao kupata utambulisho wa kazi zao.
Swali: Unaiambia nini serikali?

Jibu: Naiomba serikali ituwezeshe wachoraji ili sanaa yetu ya uchoraji iweze kukubalika ndani na nje ya nchi, kwani kwa kufanya hivyo wachoraji wataweza kujiongezea kipato.

Ndembo, alizaliwa katika Kijiji cha Mumbaka, Wilaya ya Masasi. Alisoma katika Shule ya Msingi Masasi kuanzia mwaka 1962-1965.

Baadaye alipata elimu ya sekondari katika Shule ya Chidya wilayani Masasi. Alipata Diploma ya Ualimu, kisha alichukua shahada ya uchoraji katika Chuo cha Sanaa cha Margaret Trowell School of Art na mwaka 1966-1970, alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda.

Mwaka 1972-1975, aliajiriwa na Wizara ya Elimu katika Idara ya Utamaduni. Pia alifundisha katika Chuo cha Ualimu Chang’ombe.

Wapenzi wa picha zake wanaweza kuona kazi zake kupitia www.ndembo.blogspot.com

0716 774494

Chanzo:Gazeti la
Tanzania Daima la Jumatano Machi 24 mwaka 2010

Katabazi VS Ndembo



Nikihojiana na mchoraji Paul Ndembo(64) ambaye maopema wiki iliyopita alimkabidhi Rais Jakaya Kikwete picha aliyoichora yenye sura ya rais huyo ambaye baada ya kukabidhiwa picha hiyo alishikwa na butwaa kwa furaha kwa kuona mchoraji huyo amechora sura yake kwa ufasaha.(Picha na Francis Dande)

MAWAKILI WATAKA LIYUMBA AACHIWE


Na Happiness Katabazi
UPANDE wa utetezi katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumushi na Utawala wa BoT,Amatus Liyumba, umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imuone mshitakiwa hana kesi ya kujibu na imuachirie huru kwasababu upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha kesi yao(prima facie case).


Ombi hilo liliwasilishwa mahakamani hapo jana saa 6:11 mchana kwa njia ya maandishi (written submission) lenye kurasa 16 na wakili wa utetezi Majura Magafu anayesaidiwa na Jaji Mstaafu Hillary Mkate, Onesmo Kyauke na Hudson Ndusyepo ambayo aliikabidhi kwenye chumba cha makarani na ikapokelewa.Kuwasilishwa kwa ombi hilo jana kulitokana na amri iliyotolewa Machi 15 mwaka huu na Kiongozi wa Jopo la Mahakimu Wazki Edson Mkasimongwa ambaye alizitaka pande zote kuwasilisha hoja maombi hayo kwanjia ya maandishi.

Kwa mujibu wa nakala ya ombi hilo ambalo gazeti hili limefanikiwa kupatana nakala yake , Magafu anaomba mteja wao mahakama imuone hana kesi ya kujibu kwani hata mashahidi nane walioletwa na upande wa mashitaka waliambia mahakama hiyo kwamba mshitakiwa hakuwa na mamlaka ya kuidhinisha ujenzi wala mabadiliko ya ujenzi(scope of work) wa ujenzi wa 10 Mirambo office Extension na wala hawajawahi kumuona akiudhulia kwenye vikao vya bodi ya BoT kwasababu hakuwa mjumbe wa bodi hiyo na kuongeza bodi ndiyo iliyoidhinisha ujenzi huo na si Liyumba.

‘Tunaomba mahakama hii tukufu imuone mshitakiwa hana kesi ya kujibu kwani upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha kesi yake na upande wa mashitaka ushindwa kufahamu mshitakiwa alikuwa anatakiwa ashitakiwe kwa makosa gani ....Naibu gavana Juma Reli wakati anatoa ushahidi alisema wazi kwamba hadi sasa mtu hawezi kujua hasara iliyopatikana katika ujenzi huo kwasababu ripoti ya ujenzi huo haijatoka...na mashahidi wote wa Jamhuri ukiutaza ushahidi wao walimtetea Liyumba;

“Kwa nguvu zote tunarudia kuiomba mahakama imuonesha Liyumba hana kesi ya kujibu kwani pia upande wa Jamhuri umeshindwa kuleta ushahidi unaonyesha serikali imepata hasara na kwamba kwasasa hakuna mtu anayepaswa kusema hasara imepatikana kwasababu ripoti ya ujenzi huo bado haijaandaliwa,kwa mujibu wa shitaka la kusababisha hasara sheria inasema mshitakiwa lazima awe ametenda kosa hilo akiwa na nia mbaya lakini Jamhuri imeshindwa kuleta ushahidi unaounga mkono kosa hilo na kama hivyo ndivyo nia mbaya haipo.

‘Na kushindwa kwa Jamhuri kuleta vielelezo kwamba mshitakiwa alitoa maamuzi kwenye mradi huo upande huo pia umeshindwa kuleta ushahidi kuonyesha uamuzi huo kufanya mabadiliko ya mradi unaodaiwa kufanywa na Liyumba aliufanya akiwa na nia mbaya.ndiyo maana tunaimba mahakama imuone mshitakiwa hana kesi ya kujibu”alidai Magafu.

Akichambua madai ya upande wa mashitaka yaliyodai kwamba Liyumba na aliyekuwa Gavana wa BoT,marehemu Daud Balali ndiyo waliofanya mabadiliko ya ujenzi bila idhini ya bodi ya wakurugenzi ,alidai hakuna upande wa mashitaka umeshindwa kuleta ushahidi wa kuthibitisha tuhuma hiyo na pia umeshindwa kuleta nyaraka kama kielelezo ambacho kingeonyesha saini ya Liyumba kwamba ndiye aliyeidhinisha ujenzi huo.

Alidai kwa mujibu wa kumbukumbu ya ushahidi uliotolewa unaonyesha wazi Liyumba ofisi yake ilikuwa ni kiunganishi (Co-ordinator) kati ya Menejimenti ya Benki hiyo na Meneja Mradi,hivyo shughuli zote za mradi huo alikuwa akizifanya kwa niaba ya benki hiyo na sisi yeye binafsi.

“Ni dhahiri kabisa upande wa Jamhuri katika kesi hii umeshindwa kufahamu walipaswa wamfungulie mshitakiwa mashitaka ya aina gani ni wao walikiri mahakamani hapa kwamba mshitakiwa ofisi aliyokuwa akionga ilikuwa ni kiungo cha mradi huo wa ujenzi..sasa inakuwaje wakati huo huo upande wa Jamhuri udai mshitakiwa huyo alifanya maamuzi ya mabadiliko ya ujenzi na eti mshitakiwa huyo huyo akaidhinisha mabadiliko hayo ;

“Na katika hilo upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha tuhuma hiyo,na kwa akili ya kuzaliwa hivi mtu huyo Bila upande wa mashitaka kuleta ushahidi kuthibitisha tuhuma hiyo?kwa akili ya kuzailiwa mtu mmoja anaweza kuratibu kazi ile ile katika maamuzi na kuwapelekea watu huku tayari maamuzi yalishafanyika.Na licha hivyo BoT ilikuwa ina ngazi ya juu ya kufanya maamuzi ,hivyo BoT haina chumba kilichokuwa kikiitwa chumba cha kuratibu kwaajili ya kufanya maamuzi.”alidai Magafu.

Magafu alidai kwamujibu wa kumbukumbu ya ushahidi,unaonyesha Bodi ya BoT iliiruhusu Menejimenti ya benki hiyo kutoa fedha kwaajili ya ujenzi wa mradi huo na hivyo hakuna ushahidi ulioletwa mahakamani unaonyesha vidole vya mshitakiwa vilitumika kuidhinisha fedha za BoT zitolewe kwaajili ya ujenzi huo.

Upande wa Jamhuri nao utawasilisha hoja zake zitakazomuona mshitakiwa anakesi ya kujibu Machi 29 na mahakama itatoa uamuzi wa mshitakiwa ana kesi ya kujibu au la April 9 mwaka huu.

Januari 27, mwaka jana, Liyumba na Meneja Mradi wa Benki Kuu, Deogratius Kweka, walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kusomewa mashitaka hayo ya kuidhinisha mradi wa majengo ya minara pacha bila idhini ya bodi ya wakurugenzi na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Mei 27 mwaka jana, mahakama hiyo iliwafutia kesi, lakini muda mfupi baada ya kuachiliwa walikamatwa tena mahakamani hapo na Mei 28 mwaka jana Liyumba peke yake ndiye aliyerudishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka hayo na Kweka akawa ameachiliwa huru.

Tangu kipindi hicho hadi sasa Liyumba anaendelea kusota rumande, baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, ambapo mahakama ilimtaka atoe fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya sh bilioni 111.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi 23 mwaka 2010

RITES IWE MWANZO,TUMULIKE NA KWINGINE

Na Happiness Katabazi

MACHI 12 mwaka huu, Baraza la Mawaziri chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete lilifikia uamuzi wa kujadiliana na Kampuni ya RITES ambao ndio waendeshaji Shirika la Reli Tanzania (TRL) ili iweze kununua hisa zinazomilikiwa na mwekezaji huyo.

RITES ni wawekezaji kutoka India, wenye hisa 51 ndani ya TRL huku serikali ikiwa na hisa 49, kutokana na wingi wa hisa mwekezaji huyo amekuwa na sauti kubwa zaidi kuliko serikali.

Pamoja na nguvu hizo bado mwekezaji huyo ameshindwa kuboresha huduma za TRL na kadiri siku zinavyosonga ndivyo mambo yanavyozidi kuwa mabaya kiasi cha kulifanya baraza la mawaziri kuamua kununua hisa za mwekezaji ili TRL irudi mikononi mwa serikali.

Ujio wa RITES umekuwa chanzo kikubwa cha kuzuka kwa migomo ya mara kwa mara kati ya wafanyakazi na menejimenti yao, ugomvi wa abiria na wafanyakazi na vitendo mbalimbali vyenye kushusha hadhi ya kampuni husika.

Hivi sasa si jambo la ajabu kusikia uahirishwaji wa safari, ubovu wa mabehewa na kero nyinginezo ambazo zimezorotesha usafiri pamoja na kukwamisha mizigo ya wateja.
Tathmini ya kiasi cha fedha kilichopotea kutokana na kulega lega kwa huduma za TRL ikifanyika, nina hakika tutapata mshtuko wa kile tutakachoelezwa hasa katika kipindi hiki ambacho nchi yetu imekuwa ikipambana na kuondoka katika shimo la umaskini.

Kimsingi tukubaliane migomo iliyokuwa ikifanywa na wafanyakazi wa TRL imekuwa ikiipaka matope serikali yetu mbele ya wananchi walioiweka madarakani.

Binafsi nilikuwa miongoni mwa wananchi tuliokuwa tukiilalamikia serikali kwa kitendo chake cha kuendelea kuikumbatia RITES, ambapo wakati mwingine ililazimika kuttoa fedha kuwalipa mishahara wafanyakazi wa TRL.

Makala za kila aina kuilalalmikia serikali juuu ya kuibeba kampuni hiyo ziliandikwa, miongoni mwa makala za kuilalamikia serikali kuhusu mwekezaji huyo ni ile iliyochapishwa katika gazeti hili Aprili 27, mwaka 2008 iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Serikali isikumbatie wawekezaji wababaishaji’.

Binafsi nimefarijia na kusudio hilo la baraza la mawaziri lakini nimekaa na kutafakari kwa kina juu ya mtiririko mzima wa malalamiko ya wananchi dhidi ya mwekezaji huyo na ninajiuliza maswali yafuatayo:

Uamuzi huo wa baraza la mawaziri si janja ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutaka kupata kura za wafanyakazi wa TRL kiulaini kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba?

Je, uamuzi huo si wa kuwapaka mafuta Watanzania kwa mgongo wa chupa? Hivi serikali inataka kununua hisa 51 hewa? Hawa RITES hata mishahara ya kuwalipa wafanyakazi walishindwa kuitoa sasa wana kipi hasa?

Nimefurahia mawaziri kugutuka dhidi ya wawekezaji ‘uchwara’ na wanafanya taratibu za kisheria kutaka kununua hisa za RITES ambazo kwa maneno mengine naweza kuita kuwa serikali itavunja mkataba wa mwekezaji huyo.

Mara kadhaa tumeshuhudia maamuzi ya jazba yenye kukinzana na sheria yakitumika kuvunja mikataba mbalimbali ambayo mwisho wake huitokea puani serikali ambapo fedha za wavuja jasho hutumika kulipa fidia kwa wakezaji ambao mara wasikiapo maamuzi hayo huenda katika mahakama kudai haki zao kwa kuvunjwa kwa mikataba.

Itakumbukwa mara kadhaa sera ya ubinafsishaji wa mali za umma ilikuwa ikilalamikiwa kuwa ni mbovu lakini viongozi walionekana kuweka pamba masikioni.

Sera hii imejikita kwenye msingi wa kuwanyenyekea na kuwaona miungu watu wawekezaji wajao hapa nchini huku ikiwasahau wananchi ambao kwa muda mrefu ndio waliokuwa wakiuhudumia mradi, kiwanda au kampuni husika.

Kundi kubwa la wananchi limesahaulika, halitazamwi kuwa nalo linaweza kuwa wawekezaji wazuri zaidi kama litajengewa mazingira mazuri ambayo yatawafanya waungane kwa lengo la kupata mtaji mkubwa ili kununua mali inayobinafsishwa.

Inawezekana kabisa mali tulizokuwa nazo zingeweza kuwa mikononi mwetu kama tungejenga uwazi na mazingira mazuri ya kuwabinafsishia wazawa mali zao badala ya kuwafikiria wageni ambao kila kukicha wamekuwa na ghiliba mpya za kuchuma na si kuendeleza nchi.

Shirika la Reli limebinafsishwa kwa Kampuni ya RITES ambayo uwezo wake umeonekana mdogo, licha ya kuwa wakati likipewa zabuni ya ushindi kulikuwa na mbwembwe za kuuaminisha umma kuwa nguo imepata mvaaji.

Zipo nchi nyingi ambazo zinasifika kwa kuwa na teknolojia ya kuendesha reli kuliko India ambao ndiyo tumewapa TRL ili wagange njaa badala ya kuiboresha kwa viwango vinavyokubalika kwa watumiaji.

Ujerumani, Japan, China na Ufaransa ni miongoni mwa nchi zilizo mstari wa mbele katika teknolojia hiyo, inashangaza kwamba Watanzania tulijiingiza kwa mwekezaji asiye na uwezo mkubwa tena kwa miaka 25 ijayo.

Nyimbo zilizokuwa zikiimbwa tangu awali ni kuwa mwekezaji ataleta vichwa vipya, injini mpya na mabehewa mapya lakini matokeo yake wote tumeyaona, kwani hata kile tulichokuwa nacho awali sasa hakiwezi kutusaidia au kimepotea katika mazingira ya kutatanisha.

Tunapaswa kujiuliza, ni nani katuroga au tumekosa nini kwa Mungu? Kwa nini tunaendelea kujidhalilisha kwa rasilimali tulizonazo wenyewe?

Mara kadhaa serikali ilikuwa ikichota fedha za kuwalipa mishahara wafanyakazi wa TRL ambapo Waziri Mkuu Mizengo Pinda ndiye alikuwa mstari wa mbele kutuliza hasira za wafanyakazi, je, fedha za wavuja jasho zitarudije baada ya RITES kuondoka?

Ni vema tukajulishwa kama fedha zetu zimekwenda na maji au tutalipwa kupitia ununuzi wa hisa hizo 51, la sivyo tutaendelea kuilaumu serikali yetu na watendaji wake kwa kuingia ubia na wawekezaji ‘wachovu’.

Kama mwekezaji anashindwa kutekeleza wajibu wake, kisha serikali inambebea mzigo wake, kuna sababu gani ya kuwapamba kwa jina zuri la mwekezaji wakati tukifahamu fika hana uwezo wala sifa hiyo?

Nimalizie kwa kuwaasa viongozi wetu kwamba hakuna sababu ya serikali yetu kuendelea kulea baadhi ya wanasheria na watendaji wake wanaoshiriki katika mchakato wa kuzichagua kampuni za uwekezaji zinazotaka kuwekeza hapa nchini.
Kuna faida gani ya kuendelea kuwalipa mamilioni ya fedha watendaji wanaoliingiza taifa katika hasara kubwa kwa kuingia mikataba mibovu na kampuni hewa ambazo mwisho wake mzigo unaliangukia taifa?
Serikali ni lazima ibadilike na iache tabia ya kuwalinda watendaji wake wanaoweka mbele masilahi binafsi kwa kukubali zawadi na kauli za kuwarubuni kutoka kwa wawekezaji uchwara wenye nia ya kutafuna rasilimali za nchi.
Watendaji wengine wamejikuta wakiingiza nchi matatizoni kwa sababu ya kutoisoma kwa makini mikataba wanayotaka kuingia na wawekezaji, tuna sababu gani ya kuendelea kuwa na watu wa aina hii?
Kuingiza nchi kwenye mikataba ya kinyonyaji ni uhujumu uchumi na uuaji, watu wanaofanya vitendo vya aina hiyo washughulikiwe kwa kuwa wanataka kuwaua wananchi kwa njaa.
Naamini hilo litakuwa funzo kwa wanasheria wa serikali ambao wamesomeshwa kwa kodi za wananchi na wanaendelea kulipwa mishahara na kupewa posho nono pindi wanaposafiri au wanapohudhuria vikao vya kuandaa mikataba hiyo halafu mwisho wa siku shukurani yao kwa serikali ni kuingiza nchi kwenye mikataba isiyo na masilahi ya taifa hili.
Baraza la mawaziri limeonyesha njia, sasa tupige hatua kwa kuanza kuwawajibisha mabingwa wa kuitumbukiza nchi kwenye mikataba mibovu kwa sababu tunawajua na tunaishi nao kwenye jamii yetu.
Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema ‘inawezekana, timiza wajibu wako’, kauli hii kwa bahati mbaya haijapata mashiko kwa sababu watu hawatimizi wajibu wao lakini ndiyo hao wanaokuwa mstari wa mbele kulalamikia masilahi duni wanayopata katika kazi zao.

Litakuwa jambo la busara kwa serikali kama itaanza kuweka wazi mchakato wa kumpata mwekezaji pamoja na mikataba yao ili wananchi waweze kujua wanafaidika vipi na mwekezaji husika.

Zama za kuburuzana na kutumia fedha za walipa kodi zimepitwa na wakati, inapaswa kila mtu atimize wajibu wake kulingana na taratibu za kazi.

Uamuzi huu wa baraza la mawaziri usiishie kwa TRL pekee bali uangalie na miradi mingine ya uwekezaji ambayo mpaka sasa imekuwa ikisuasua kwenye uzalishaji kwa sababu ya mmiliki wake kutokuwa na uwezo wa kutosha.

Wananchi wanawajua wawekezaji uchwara na mikataba tata, kila kukicha wamekuwa wakipaza sauti zao hivyo ni vema serikali ikayafanyia kazi malalamiko haya badala ya kuonekana ni walalamishi na wasiowataka wawekezaji.

Halitakuwa jambo jema kama uamuzi huu wa baraza la mawaziri umefanywa kwa kukitafutia chama tawala sifa za kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu, nchi hii ni yetu sote, tunapaswa kuchukia aina zote za unyonyaji.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili,Machi 21 mwaka 2010

USHAHIDI KESI YA MRAMBA UTATA MTUPU

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa utetezi wa kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.9 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba, na wenzake, jana uliushutumu vikali upande wa jamhuri katika kesi hiyo kuwa umepeleka mahakamani vielelezo vya kughushi.


Mbali na Mramba, washtakiwa wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona, na Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja.

Shutuma hizo zilitolewa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam mbele ya jopo la Mahakimu Wakazi John Utamwa, Sam Rumanyika na Saul Kinemela na mawakili wa utetezi, Hurbet Nyange, Peter Swain a Elisa Msuya, wakati wakipinga kielelezo ambacho ni barua iliyoandikwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) kwenda kwa Mramba ambapo kwa mujibu wa barua hiyo, TRA ilikataa kampuni ya Alex Stewart Government Bussiness Corporation kupewa msamaha wa kodi.

Wakili Nyange kwa niaba ya mawakili wengine wa utetezi alitoa shutuma hizo muda mfupi baada ya Wakili Mwandamizi wa Serikali Fredrick Manyanda ambaye alikuwa akimuongoza shahidi wake wa sita, Ludovick Kandege, kutoa ushahidi wake alipoiomba mahakama ipokee barua kama hiyo ambayo iliandikwa na shahidi huyo mwaka 2003 kama kielelezo.

“Kwa ujumla tunapinga kielelezo hicho (orginal) kisipokelewe kwa sababu ni cha kughushi na kimetofautiana kabisa na nakala ya kielelezo walichonacho upande wa utetezi ambacho walipewa na upande huo wa mashtaka…kwani zinatofauti kubwa sana; nakala tuliyopewa sisi haina ‘indosement’ lakini kielelezo hiki kinachotaka kutolewa na shahidi huyu kina indosement. Kielelezo tulichopewa sisi kinaonyesha barua hiyo iliandikwa Oktoba 7 mwaka 2003 lakini kielelezo kinachotaka kutolewa sasa kinaonyesha barua hiyo iliandikwa Septemba 7 mwaka 2003.


“Kielelezo tulichopewa sisi kinaonyesha namba ya Faksi ya TRA ni tofauti na namba ya Faksi ya TRA kwenye kielelezo kinachotaka kutolewa leo(jana),na hata saini za mwandishi wa barua hiyo zinapishana herufu…licha maudhui ya vielelezo hivyo halisi na nakala yanafanana,kwenye kielelezo walichopewa wao chini TRA inanukta lakini kwenye kielelezo halisi kwenye neno TRA hakuna nukta…kwa sababu hizo sisi tunataka kielezo hicho kisipokelewe kwani hakifanani na nakala ya kielezo tulichopewa na upande wa mashitaka na tunachokiona upande wa Jamhuri umenza kuleta vielelezo vya kughushi.

“Na tunapinga kwamba TRA haijawahi kumwandikia mshitakiwa wa kwanza hiyo hiyo barua ya iliyokuwa ikimshauri asitoe msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo….na ninarudia tena kwa tofauti hizo nilizozianisha nadiriki kutamka kwamba kuna namna fulani ya kughushi katika kuleta kielelezo hiki mahakamani.

“Upande wa mashitaka wenyewe hapo mahakamani umekiri kwamba ni wao ndiyo umetupa nakala ya barua hiyo …swali la kujiuliza hivi mtu anapoenda kutoa fotokopi siinatoka nakala ile ile sasa kwani upande wa mashitaka katika kesi hii unaleta barua halisi ambayo inatofautiana na nakala halisi?alidai Nyange na kusababisha watu kuangua vicheko mahakamani

Akijibu shutuma hizo, Wakili Manyanda alidai kielelezo hicho kinafanana na nakala waliyowapatia upande wa utetezi na kuamua kueleza kweli ila mchapishaji wa barua hiyo alikosea kuandika mwezi na usahihi ni kwamba barua hiyo iliandikwa Septemba 7 mwaka 2003 na siyo Oktoba 7 mwaka huo kama inavyosomeka kwenye nakala ya barua hiyo ambayo upande wa Jamhuri ndiyo uliwapatia upande wa utetezi.

Hata hivyo jopo la mahakimu hao, lilisema uamuzi wa barua hiyo ipokelewe kama kielezo au la itautoa Aprili 15 mwaka huu kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutajwa na akautaka upande wa utetezi usimuulize maswali shahidi huyo ambayo yatatokana na barua hiyo hadi hapo jopo hilo litakapotoa uamuzi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Machi 20 mwaka 2010

MWAKALUKWA:NILIHISI KIASI KILICHOTOZWA NI KIKUBWA

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Kamishna wa Madini katika Wizara ya Nishati na Madini, Gray Mwakalukwa (58), ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa alihisi kiasi cha ada asilimia 1.9 kilichotozwa na Kampuni ya Alex Stewart Government Business Corporation kwa serikali ni kikubwa.


Mwakalukwa ambaye ni shahidi wa tano alieleza hayo jana baada ya kubanwa maswali na mawakili wa utetezi, Hurbet Nyange, Peter Swai, Profesa Leonard Shahidi na Elisa Elia, ambao wanamtetea aliyekuwa Waziri wa Fedha wa zamani, Basil Mramba, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja, mbele ya jopo la mahakimu wakazi, John Utamwa, Sam Rumanyika na Saul Kinemela.

Mwakalukwa ambaye sasa ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) baada ya kusema hayo, wakili wa utetezi Peter Swai, alimtaka shahidi huyo atoe vielelezo vya kiasi cha gharama zinazotozwa na makampuni ya ukaguzi wa dhahabu katika nchini nyingine, lakini hata hivyo shahidi huyo aliiambia mahakama kuwa hana ulinganisho wa nchi nyingine, hali iliyosababisha watu waliohudhuria kesi hiyo kuangua vicheko.

“Wakati huo mimi nilikuwa kamishna wa madini pale wizarani, kiasi hicho kweli nilihisi ni kikubwa, licha ya kuwa sikuwa nimefanya utafiti katika nchi nyingine, lakini kiasi hicho kiliwekwa kwenye mkataba na mimi sikuhusika kuandaa mkataba, hivyo sijui chochote kuhusu mkataba huo ila baada ya BoT kwa niaba ya serikali kuingia kwenye mkataba na kampuni hiyo na kusainiwa Julai 2003, uliletwa kwangu kama sheria ya madini inavyotaka.

“Baada ya kuona, niliteua mtu akafanye ukaguzi kwenye migodi kwa niaba yangu (Kamishna wa Madini) na kampuni hiyo ya ukaguzi wa madini ilikwenda kufanya kazi hiyo na sijahusika kuandaa kipengele cha ada ya ukaguzi wa dhahabu kilichowekwa kwenye mkataba huo wala kuandika barua ya kuiombea msamaha wa kodi kampuni hiyo, kwakuwa yeye alikuwa akishughulika na utoaji wa msamaha wa mirahaba wa makampuni ya madini,” alidai Mwakalukwa.

Alisema yeye akiwa kamishna wa madini, alitoa ushauri mapema kwa Yona kabla ya mkataba huo kusainiwa na alitoa ushauri huo kwa maandishi, aliangalia maeneo matatu, ambapo aliangalia kampuni hiyo baada ya kuingia mkataba na serikali itaingiaje kwenye migodi au serikali itatumia sheria ya madini au ya ukaguzi kutoa mapendekezo ya tozo kwa kampuni hiyo na alishauri hayo malipo yalipwe na kampuni ya madini au serikali.

Kiongozi wa Jopo la mahakimu wakazi, John Utamwa, aliahirisha kesi hiyo hadi kesho ambapo shahidi wa sita ataanza kutoa ushahidi wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Machi 18 mwaka 2010

HATIMA YA LIYUMBA APRILI 9

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imesema kuwa Aprili 9, mwaka huu, itatoa uamuzi wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), anayekabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, iwapo ana kesi ya kujibu au la.
Sambamba na hilo, hatimaye jana upande wa Jamhuri ulitangaza rasmi kuifunga kesi hiyo.

Kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi, Edson Mkasimongwa, anayesaidiana na Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa, alitoa amri hiyo baada ya kusikiliza malumbano ya kisheria yaliyotolewa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Juma Mzarau na Ben Lincoln na wakili wa utetezi, Majura Magafu, aliyekuwa akisaidiwa na Jaji Hillary Mkate, Hudson Ndusyepo na Onesmo Kyauke.

Hakimu Mkazi Mkasimongwa alisema kuwa anakubaliana na maombi ya pande zote yaliyohusu mahakama kuwapatia fursa ya kuwasilisha majumuisho yao ya kumuona mshitakiwa ana kesi ya kujibu na kuongeza kuwa jopo lake limefikia uamuzi wa kuzitaka pande zote mbili kuwasilisha majumuisho hayo kwa njia ya maandishi.

“Hivyo natoa amri kwamba upande wa utetezi uwasilishe majumuisho yake kwa njia ya maandishi mahakamani Machi 22 na upande wa mashitaka uwasilishe majumuisho yake mahakamani Machi 29 na kwamba kesi hii itakuja kutajwa Machi 26 na mahakama hii itatoa uamuzi wa mshitakiwa kama ana kesi ya kujibu au la Aprili 9, mwaka huu,” alisema Mkasimongwa.

Awali kabla ya uamuzi huo kutolewa, wakili Mzarau aliikumbusha mahakama kuwa shauri hilo lilikuwa limepangwa jana kuendelea na mashahidi wa upande wa mashitaka, lakini baada ya wao kupitia kwa kina nakala ya mwenendo wa kesi hiyo ulionyesha ni mashahidi wanane waliotoa ushahidi na vielelezo 13 vilitolewa mahakamani hapo na wamefikia hatua muafaka ya kuifunga kesi yao kwa mujibu wa kifungu cha 231 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.

Baada ya Mzarau kutoa maelezo hayo, wakili wa utetezi Magafu aliinuka na kuomba mahakama iwaruhusu jana hiyo hiyo waweze kuwasilisha majumuisho yao kwa njia ya mdomo, ya kwamba mteja wake (Liyumba) hana kesi ya kujibu.

Hata hivyo, ombi hilo lilipingwa na wakili Mzarau, kwa madai kuwa wanahitaji wapate muda wa kujiandaa na kwamba wanaiomba mahakama majumuisho hayo ya mshitakiwa kama ana kesi ya kujibu au la, wao na upande wa utetezi wawasilishe majumuisho hayo kwa njia ya maandishi ili waweze kuisaidia mahakama kufikia maamuzi sahihi.

Kabla ya uamuzi huo wa jana wa upande wa mashitaka kuifunga kesi hiyo, wakati wakimsomea maelezo ya awali Liyumba, waliiambia mahakama kuwa wanakusudia kuleta mashahidi kumi na ilipofika hatua ya mshitakiwa wa tatu wakati anatoa ushahidi wake, upande wa mashitaka uliongeza idadi ya mashahidi na kufikia mashahidi 15.
Kwa idadi hiyo, hadi kufikia jana upande wa mashitaka umeweza kuleta jumla ya mashahidi wanane tu.

Januari 27, mwaka jana, Liyumba na Meneja Mradi wa Benki Kuu, Deogratius Kweka, walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kusomewa mashitaka hayo ya kuidhinisha mradi wa majengp ya minara pacha bila idhini ya bodi ya wakurugenzi na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Mei 27 mwaka jana, mahakama hiyo iliwafutia kesi, lakini muda mfupi baada ya kuachiliwa walikamatwa tena mahakamani hapo na Mei 28 mwaka jana Liyumba peke yake ndiye aliyerudishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka hayo na Kweka akawa ameachiliwa huru.

Tangu kipindi hicho hadi sasa Liyumba anaendelea kusota rumande, baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, ambapo mahakama ilimtaka atoe fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya sh bilioni 111.


Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne,Machi 16 mwaka 2010

WANAWAKE WAPO WAPI KWENYE SHERIA?

Happiness Katabazi

MACHI 8 kila mwaka huwa ni kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani. Kwa Tanzania maadhimisho hayo yalifanyika mkoani Tabora na Rais Jakaya Kikwete alikuwa mgeni rasmi.


Maadhimisho hayo yanazidi umaarufu na kujulikana kwa watu mbalimbali kwa sababu vyombo vya habari vimekuwa vikiyatangaza kwa muda mrefu sambamba na kufanya mahojiano na watu mbalimbali kuelezea umuhimu wa mwanamke katika jamii pamoja na changamoto zinazomkabili.

Lengo hasa la vyombo vya habari na wanaharakati ni kuhakikisha jamii inaachana na mfumo dume, ambao kwa muda mrefu umekuwa ukimuweka kando mwanamke katika nyanja za utawala na shughuli za kiuchumi.

Mfumo dume huu ndio ule unaomuona mwanamke kuwa ni pambo la nyumbani pamoja na mlezi wa familia, ambaye hata mumewe anapofariki dunia hapaswi kurithi mali alizochuma naye.

Sekta ya sheria nayo imeathirika na mfumo huo ambapo bado kuna idadi ndogo ya mawakili wanawake ndani ya serikali na wale wanaojitegemea kiasi cha kuwafanya hata waliopo wakose kujiamini katika utendaji wao.

Kutokujiamini huko kunawafanya mawakili wanawake wa serikali wasipangwe kuwa mawakili viongozi katika kuendesha kesi kadhaa za jinai ambazo zinavuta hisia za wananchi.

Kesi ambazo zimekuwa zikivuta hisia za wananchi wengi ni kesi za wizi wa Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara, kulawiti na mauaji, ambazo nyingi zimefunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mahakama ya Wilaya ya Ilala na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Binafsi naamini mawakili wanawake hawana woga ila wengi wa washitakiwa au wadaiwa ni wanaume na pindi wafikiriapo kumtafuta wakili wa kuwatetea hujikuta wakifikia uamuzi wa kuwapa kazi mawakili wa kujitegemea wanaume ili wawatete mahakamani.

Wanaume wengi nao wamejenga dhana kwamba mawakili wanawake ni waoga, jambo linalowawia vigumu kuwapa kazi ya kuwawakilisha mahakamani.

Kwa mfano huo tunaona kwamba mfumo dume bado upo na unaendelea hadi kwa wananchi wanaohitaji huduma ya kisheria kutoka kwa mawakili wa kujitegemea, kwani wanaoshitakiwa wengi kila kukicha hapa nchini ni wanaume.

Pamoja na hilo, wanasheria wanawake nchini bado ni wachache ukilinganisha na wanaume.

Na inapotokea kesi zinazogusa hisia za wananchi unakuta Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi au Mwanasheria wa Kanda ya Dar es Salaam, Stanslaus Boniface au Mkuu wa Kitengo cha Sheria katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Ben Lincoln, wanawapanga mawakili wanaume kuongoza jopo la mawakili wa serikali na TAKUKURU kuendesha kesi hizo na mawakili wanawake kutoka taasisi hizo wanaishia kuwa wasaidizi wa mawakili hao wanaume.

Na hili si siri, kwani tunalishuhudia kila kukicha pale Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi za EPA na matumizi mabaya ya ofisi za umma tangu zilipoanza kufunguliwa Novemba 4, mwaka 2008 hadi leo, ni mawakili wa serikali wanaume ndio wanaongoza kuendesha kesi hizo na mawakili hao ni Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface, Fredrick Manyanda, Oswald Tibabyekoma, Michael Lwena, Timon Vitalis, Ben Lincoln, Prosper Mwangamila, Justus Mulokozi na Biswalo Mganga.

Na mahakama huishia kuambiwa na mawakili hao wa serikali wanaume kabla ya kuanza kwa kesi hizo kwamba watasaidiwa na mawakili ambao wana jinsia ya kike, Tabu Mzee kutoka TAKUKURU na Arafa Msafiri, kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuendesha kesi hizo.

Lakini wakati washitakiwa wa kesi hizo wanasomewa hati za mashitaka na maelezo ya awali (PH), tulishuhudia mawakili wanawake ndio walisoma hati hizo.

Kesi zinapofikia wakati wa mashahidi kuanza kutoa ushahidi, utaona mawakili wa serikali wanaume ndio wanaongoza jopo la mawakili wa serikali kuendesha kesi hizo.

Swali, je, kama mawakili wanawake wa serikali waliweza kuwasomea hati za mashitaka washitakiwa na kuwasomea maelezo ya awali (PH) ni kwanini inapofika wakati wa mashahidi kutoa ushahidi mawakili wanawake wa serikali hawapewi fursa na badala yake tunawaona mawakili wa serikali wanaume ndio wanawahoji mashahidi wa kesi hizo husika?

Ni kweli kwamba wanasheria wana kanuni moja isemayo katika kuendesha kesi mahakamani anapokuwepo Mwanasheria Kiongozi au Mwanasheria Mwandamizi, basi mwanasheria mchanga ambaye hajafikia ngazi hizo atabakia kuwa msaidizi katika uendeshaji wa kesi.

Si lengo langu kupingana na kanuni hiyo, ila kama mtindo huo utaendelea wa kesi zinazovuta hisia kwa jamii kuendelea kuongozwa na majopo ya mawakili wanaume wa serikali kwa kigezo kwamba wao ndio wana uzoefu na kazi hiyo si haki.

Je, hao mawakili wanawake kutoka TAKUKURU na wale wanaotoka Ofisi ya DPP ni lini watapata uzoefu wa kuongoza jopo la mawakili wa serikali katika kesi za aina hiyo ambazo zinavuta hisia katika jamii?

Ikumbukwe kuwa hapo kale hata kwenye ulingo wa siasa wanawake walionekana hawawezi na kwamba saizi yao ilikuwa ni kuwapigia kampeni wagombea wanaume tu. Lakini leo hii katika ulingo huo wanawake wamepewa nafasi za uongozi, wachache wao wameweza kuvunja dhana hiyo na kuthibitisha uwezo wao.

Kumekuwa na fikra za kimageuzi katika sekta ya elimu ambazo zinatambua wanawake wanahitaji mazingira tofauti na wavulana ili wanawake waweze kufanya vizuri. Hayo mabadiliko bado hayajawakomboa wanawake wengi kwani wanawake bado ni wachache sana.

Zamani ilionekana kazi ya uendesha mashitaka ni kazi ya wanaume lakini kutokana na mabadiliko ya kifikra,wanawake sasa wamekuwa wakifanya kazi hiyo ya uendeshaji mashitaka katika mahakama zetu.

Hili jambo ni la kulipa muda lakini hatua za makusudi zichukuliwe kuwajengea uwezo wanawake, kwa sababu hivi sasa wanawake ndio wanaanza kujitokeza kwa wingi kusomea fani ya sheria na wanapohitimu wanajikuta wanapata kazi sehemu zenye mvuto zaidi wa kifedha kuliko kushughulikia kesi za jinai mahakamani.

Ndiyo maana hatuwaoni kwa wingi mahakamani ila wanavyozidi kuhitimu wataonekana wengi mahakamani.

Kama wanawake wengi walivyoanza kujitokeza kusoma sheria, tunawahamasisha wale waliohitimu sheria wajiunge katika maeneo ambayo yamekuwa yakihodhiwa na mawakili wanaume kama vile uendeshaji mashitaka na uandikaji sheria. Hasa haya ndiyo maeneo nyeti mno.

Nitoe rai kwa DPP Feleshi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Fredrick Werema, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk. Hosea wawapokee wanasheria wanawake na wawape mafunzo na kipaumbele, tunaamini watafanya kazi vizuri.

Wanasheria wanawake waliopo kwenye taasisi zinazoongozwa na viongozi hao, tunaomba wapewe fursa sawa na wanaume ili mwisho wa siku serikali yetu iwe na mawakili wa serikali wanawake wengi mahiri, watakaoweza kuhakikisha wanakabana kisheria kikamilifu na mawakili wa kujitegemea.

Majura Magafu ni miongoni mwa mawikili wa kujitegemea ambao hivi sasa amejizolea sifa kemkemu nchini kutokana na umahiri wake wakati akiwa mahakamani, akiwatetea wateja wake (washitakiwa) na mwisho wa siku serikali inajikuta ikishindwa kesi nyingi za jinai, ambazo zilikuwa zikiwakabili washitakiwa waliokuwa wakitetewa na wakili huyo.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili Machi 14 mwaka 2010

ASKARI JKT AONGEZWA KESI YA MAUJI YA FUNDIKIRA

Na Happiness Katabazi

ASKARI wa Jeshi la Kujenga Taifa wa kikosi cha JKT Mbweni, MT 8567 Mohamed Ally Rashid ameunganishwa kwenye kesi ya mauaji ya Sechu Fundikira na kufanya idadi ya askari wa jeshi wanaokabiliwa na kesi hiyo kufikia watatu sasa.


Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Genevetus Dudu, Wakili wa Serikali, Ester Kyala, akisoma mashitaka alidai Januari 23 mwaka huu, saa saba mchana maeneo ya Kinondoni Mwinjuma, mshitakiwa huyo na mwenzake walimuua Swetu Fundikira.

Mshitakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina uwezo kisheria na kusikiliza kesi ya mauaji.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni ambao walishafikishwa mahakamani ni Sajenti Roda Robert (42) wa kikosi cha JKT Mbweni na Koplo Ally Ngumbe wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kikosi cha Kunduchi.

Kesi imeahirishwa hadi Machi 24 mwaka huu, itakapotajwa tena.

Chanzo;Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi,Machi 11 mwaka 2010

JINA LA NYERERE LISITUMIKE VIBAYA

Happiness Katabazi

HAKUNA ubishi kwamba jina la mhasisi wa taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na picha yake, tangu atutoke Oktoba 14 mwaka 1999, hadi sasa baadhi ya wananchi wamekuwa wakivitumia kwa ajili ya kukidhi matakwa yao.


Wengi miongoni mwa wanaotumia jina la Nyerere na picha yake kwenye taasisi zao wamekuwa wakifanya hivyo kwa ajili ya kujiongezea kipato.

Kwa makusudi kabisa, wameamua kutumia jina la Mwalimu kwenye shughuli zao kibiashara kama shule, bahati nasibu, mihadhara mbalimbali kwa kigezo cha kumuenzi.

Ieleweke wazi kuwa wananchi wengi wamekuwa wakiiga sera, mavazi misimamo na matendo yaliyokuwa yakitendwa na kuvaliwa njuga na viongozi wa kisiasa wa mataifa mbalimbali duniani na pia wamekuwa wakisimama katika matendo sahihi yaliyokuwa yakifanywa na viongozi hao ambao wengi ni waasisi wa mataifa yao.

Lakini leo hii hapa nchini kwetu mambo yamekuwa ndivyo sivyo, wengi wetu tumekuwa tukiwaenzi viongozi hao kwa maneno badala ya vitendo, hukariri yaliyofanywa na waasisi hao kwa ajili ya kujibia mitihani na tukishamaliza, yanahama kwenye vichwa vyetu.

Tunaimba sera walizoziasisi siku za kumbukumbu za vifo vyao na pindi tunapotaka kuomba fedha kwa wafadhili. Baadhi ya wanasiasa wakati wa kampeni husimama majukwaani wakiomba kura wananchi na kutamba kuwa wanamuenzi Nyerere kwa vitendo wakati kwenye uchaguzi ndio vinara wa kutoa rushwa.

Tukubaliane kimsingi kwamba hadi sasa nchi yetu bado haijatunga sheria ya kudhibiti matumizi holela ya picha ya Nyerere na jina lake, hivyo hata hawa wenzetu wanaotumia jina na picha hiyo kwa ajili ya kuchumia matumbo yao, wanakuwa hawajavunja sheria zozote za nchi yetu kwa hiyo wanaendelea kupeta.

Licha serikali yetu kipindi cha nyuma kuahidi kwamba inakusudia kuanzisha mchakato wa kutunga sheria ya kuthibiti matumizi yasiyo sahihi ya jina na picha ya Mwalimu, lakini hadi leo serikali haijatueleza mchakato huo umefikia wapi.

Na matokeo yake hivi karibuni tumeshuhudia chama kipya cha siasa, CCJ kilichopewa usajili wa muda mapema wiki iliyopita, nyuma ya kadi za chama hicho kuna picha ya Mwalimu Nyerere.

Katika mazingira kama haya ya taifa kutokuwa na sheria ya kuthibiti matumizi holela ya picha ya mhasisi wa taifa hili, kadiri siku zinavyosonga mbele vyama vya siasa vipya vitasajiliwa na kutumia picha ya Mwalimu Nyerere kiholela. leo ni CCJ kadi yake inapicha ya Nyerere, kesho watatokea Watanzania wengine wataanzisha vyama vya siasa ambavyo kadi zao pia zitakuwa na picha ya mhasisi huyo au marais wengine wastaafu au wataweka picha za waasisi wa vuguvugu la vyama vingi nchini.

Aidha kadri miaka inavyozidi kusonga mbele, ndiyo watanzania wanavyozidi kuvumbua mbinu mpya za kujiingizia kipato. Wataibuka watu waanzishe madanguro, nyumba za kulala wageni na biashara nyingine haramu kisha wazibatize jina la Mwalimu Nyerere au majina ya marais wastaafu.

Na hili linawezakana, ni suala la muda tu, tusubiri tuone. Kwani hata hao wanaoongoza vyama vya siasa na wanaojigamba wanamuenzi Nyerere kwa vitendo hawastahili kabisa kujinasibu kuwa wanamuenzi kwani miongoni mwao wanakabiliwa na tuhuma za ukosefu wa maadili, ikiwemo rushwa.

Na tukiruhusu tufikie huko, tukae tukijua wazi heshima na hadhi ya viongozi wetu hao wa nchi itaporomoka.

Nihitimishe kwa kutoa rai kwa serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete kwamba wakati umefika sasa wa Bunge lake kutunga sheria ya kudhibiti matumizi holela ya picha ya mhasisi wa taifa hili, na iainishe picha na jina linatakiwa litumikeje au wanaotaka kulitumia jina hilo kwa ajili ya shughuli zao za kibiashara ni vyema wakaomba ridhaa kwa familia yake na wale wanatakaobainika kulitumia vibaya wakumbane na mkono wa dola.

Naomba kutoa hoja.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano la Machi 10 mwaka 2010

VIONGOZI WA DINI AMKENI MUIKOE JAMII

Happiness Katabazi
KWA takriban miaka miwili sasa viongozi wa madhehebu ya dini mbalimbali hapa nchini wamekuwa wakiitumia kikamilifu ibara ya 18(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.


Ibara hiyo inasema ‘kila mtu anao uhuru wa kutoa maoni na kueleza fikra zake’.

Viongozi hao wa dini wamekuwa wakiitumia vyema ibara hiyo kwa kupaza sauti kwa kukemea wakidai ufisadi umeshamiri nchini hasa katika utawala wa Rais Jakaya Kikwete, hadi kufikia hatua ya viongozi hao kutofautiana kimsimamo na wanasiasa wakongwe akiwemo Kingunge Ngombare Mwiru.

Kingunge aliwataka viongozi wa dini kuacha kujiingiza kwenye ulingo wa siasa kwani endapo wataendelea kufanya hivyo wanaweza kuvuruga amani ya taifa letu. Hata hivyo viongozi hao wa dini waliweka pamba masikioni; waliendelea na msimamo wao kupinga ufisadi kwa matamshi yao na maovu mengine ambayo walipaswa wawafundishe waumini wao wasiyatende, wala hawakuyapigia kelele kama walivyopogia kelele ufisadi.

Leo katika makala hii nitazungumzia aina mpya ya mahusiano yaliyozuka kwenye jamii yetu ambayo yameanza kutishia amani, mila na desturi zenu: ushoga na usagaji.

Kwa mujibu wa kifungu cha 138A na kifungu cha 157 CAP 15, Offence Against Morality of Tanzania Penal Code, 2002, vinakataza vitendo hivyo vya kibazazi.

Lakini kuna aina mpya ya mahusiano ya kubadilisha jinsia imezuka; mwanaume anabadili jinsia, anaweka ya kike!

Hili ni tatizo na halijatungiwa sheria, linatishia usalama wa jamii na mila zetu kwani haiwezekani watoto katika familia ambayo baba au mama wanamuona mtoto wao akibadilisha jinsia.

Hakika hii ni dhambi na itatupeleka motoni; na tukae tukijua watoto wetu pindi washuhudiapo ufedhuli huu ni wazi wataathirika kisaikolojia.

Hapa viongozi wetu wa dini wanatakiwa kutusaidia kukomesha mambo haya ili maadili yasiteketee.

Viongozi wa dini wanatakiwa wajue wajibu wao kwa jamii, watumie muda mwingi kufikiri mbinu sahihi za kuifundisha jamii ili iweze kuelewa kwa urahisi.

Leo inawezekana tutaliona ni tatizo dogo lakini tutakapogundua kua si dogo litakuwa limetuzidi nguvu.

Aidha, kumekuwepo na madai kwamba baadhi ya viongozi wa dini nao wamekumbwa na mmomonyoko wa maadili kwa kujihusisha na dhambi ya uzinzi ambayo imekemewa vikali kabisa katika vitabu vitakatifu vya Mungu hususan ndani ya Biblia katika kitabu cha Mithali 6:36 inayosema ‘Yeyote aziniye hana akili kabisa tena afanya jambo litakaloangamiza nafsi yake’.

Kufanya ngono zembe na waumini wao au wake za waumini wao, wanatumia nguvu za giza kuendesha nyumba za ibada, wanatumiwa na wanasiasa, wanaishi maisha ya hali ya juu kuliko waumini wao, kwa wale viongozi wadini waliokatazwa kuoa au kuolewa wamekuwa na mahusiano ya kimapenzi hadi kufikia kuzaa watoto kinyemela na kuwatunza kwa siri kubwa.

Lakini pamoja na kujifanya wanaficha dhambi za uzinifu wao, jamii imeshawang’amua na ile heshima waliyokuwa wakipewa zamani imepungua au kumalizika na wanaonekana ni viongozi wa dini wanaotumia dini kuficha maovu wanayoyafanya.

Tukubaliane kuwa kuna mmonyoko wa maadili kwa baadhi ya viongozi wetu wa dini, ni vizuri wakatambua nafasi yao kwa waumini wao na ikiwezekana waache mambo yanayowashushia heshima mbele ya umma kwa kuwa wao ni kioo.

Mtu anapokuwa kioo ni lazima atende matendo ya kuigwa badala ya kufanya mambo yanayodhalilisha cheo chake pamoja na taasisi anayoiongoza.

Napenda kutoa rai kwa viongozi wa dini kwamba nguvu zile walizozitumia kupaza sauti kuhusu ufisadi nchini, basi wazitumie kupaza sauti kukemea ushoga, usagaji, uzinzi, mauaji dhidi ya binadamu wenzetu, nguvu za giza, pepo wa tamaa ya mali na madaraka.

Huko nyuma tulipokuwa tukihudhuria nyumba za ibada, viongozi wa dini hususan sisi waumini wa Kanisa la Kiinjili ya Kilutheri tulikuwa tukihamasishwa mno kuheshimu amri za Mungu zisemazo usitamani mwanamke wa mwenzio, usimshuhudie jirani yako uongo, usitamani mali ya jirani yako wala ng’ombe, punda, au mjakazi wake, usilitaje bure jina la bwana Mungu wako.

Leo hii ukihudhuria kwenye nyumba za ibada au ukiwa na mazungumzo na viongozi wa dini, ni nadra mno kuwasikia viongozi hao wa dini wakizitaja amri hizo…utawasikia wakitaja ufisadi umeshamiri.

Hakuna asiyefahamu kwamba nchi yetu nayo inakabiliwa na maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi ambao kwa asilimia kubwa chanzo chake ni ngono zembe.

Umefika wakati kwa viongozi wa dini kuelekeza nguvu zao kwa kupiga vita maovu hayo na kuwakumbusha mara kwa mara waumini wa dini husika amri hizo za Mungu naamini mioyo ya watu na akili zao zitabadilika na kuwa na hofu ya Mungu na kuachana na madhambi hayo.

Naomba kutoa hoja.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili la Machi 7 mwaka 2010

UTEUZI WA WABUNGE CUF NDIYO MWISHO WA SAFARI?

Happiness Katabazi

KWA zaidi ya miongo miwili sasa Tanzania imekuwa na siasa za vyama vingi.
Vyama hivi vimegawanyika katika chama tawala na kwa upande wa pili vyama vya ushindani.


Lengo la kuwa na vyama vingi ni kuwapa wananchi demokrasia pana ya kushiriki katika uongozi wa nchi yao. Kila chama kina sera zake, maono, itikadi na utamaduni wake wa kisiasa.

Kwa mfano kipo Chama NCCR-Mageuzi ambacho kinajitambulisha kuwa na itikadi ya demokrasia ya kijamii, sera zake katika maeneo mengi zinalenga kuleta mageuzi katika mifumo ya utawala, katiba, sheria na jinsi ya kutoa huduma ya ustawi wa jamii.

Viko vyama ambavyo vipo kambi ya ushindani ama vina sera za utajirisho ama mapesa. Vyama hivyo ni kama Chama cha Wananchi (CUF), Chama Cha Mapinduzi (CCM), United Democratic (UDP na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Mchanganuo huu unatuonyesha kwamba ukiondoa zana ya chama tawala kwa upande mmoja na vyama vya ushindani kwa upande wa shilingi. Siasa za kweli za vyama ziko katika itikadi, sera na utamaduni wake kisiasa.

Ndiyo maana mijadala ya kitaifa kuhusu masuala nyeti ya kitaifa inabidi itazamwe katika muktadha huu wa sera, itikadi na utamaduni wa kisiasa.

Ni vyama gani vipo kwenye kundi moja, jukwaa moja na vinaweza kuendesha serikali pamoja? Maridhiano ya Zanzibar kati ya CCM na CUF yanaonyesha kuwa tofauti kuu kati ya vyama hivi haipo katika itikadi, sera, wala utamaduni wa kisiasa bali katika ubinafsi uliojengeka katika maudhui ya falsafa za kihafidhina za ubepari. Ambao wengine wanauita utajirisho au mapesa.

Hakuna jipya linaloweza kuletwa kimageuzi na CUF, UDP au CHADEMA ambalo haliwezi kuletwa na CCM kwani hawa ni ndugu moja. Hawa wanaweza kutawala pamoja. Wakigombana kwa uroho na ubinafsi uliojengeka ndani ya familia moja.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, chama cha ushindani kilichokataa kuweka saini makubaliano ya ushirikiano wa pamoja wa vyama vya ushindani kilikuwa ni CUF. Kilirejea kwenye kambi ya ushirikiano baada ya kushindwa.

Kila mara CUF inakubali ushirikiano na chama kingine, mfano wa CHADEMA, katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, ilijihakikishia ushindi si wa pamoja bali wake binafsi.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, kila chama cha upinzani kiligombea kivyake kwa vile si CUF wala CHADEMA walikuwa tayari kushirikiana na chama kingine.

Walikuwa tayari kununua wagombea wa vyama vingine na kuwafanya wagombea wa vyama vyao.

Mfano, marehemu Chacha Wangwe kutoka NCCR-Mageuzi akiwa diwani na mgombea wa chama hicho, ghafla alikihama akiwa na nyadhifa hizo.

Ilidaiwa alinunuliwa na kwenda kugombea ubunge Tarime kupitia CHADEMA katika Jimbo la Tarime.

Lakini si huyo tu, hata aliyekuwa Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi wakati huo Mosena Nyambambe, alijitosa kugombea ubunge katika Jimbo la Serengeti kupitia CUF.

NCCR -Mageuzi haikulalamika wala kuwawekea pingamizi wagombea hao, japo ikumbukwe uchaguzi wa mwaka 2000, Naila Jiddawi, alipoondoka CUF na kujiunga na NCCR kisha kugombea urais wa Zanzibar aliwekewa pingamizi na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad.

Uchaguzi Mkuu ujao, unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, unatupa hisia kali kuhusu mustakabali wa siasa za mageuzi nchini.

Tayari vyama vinavyojiita vigogo wa upinzani vikirubuniwa na CCM. Sasa CUF ni CCM. Waliojifanya wana ‘ngangari’ sasa hawafui dafu kufukuza kuku mbele ya CCM.

Hatujui mambo yatakwenda vipi kwa vyama kama CHADEMA, UDP, kwani vyama hivyo vina wabunge kwenye Bunge la sasa, vilijiita wao ndio vigogo.

Kama siasa za maridhiano za kwenda kutembeleana, kula biriani na CCM zitatawala siasa za mageuzi, je, wananchi wategemee nini sasa kama mustakabali wa nchi yao?

Msemaji wa Ikulu, Salva Rweyemamu alishataadharisha kwamba utabiri wa Sheikh Yahya Hussein uheshimiwe. Hatujui matamshi ya Rweyemamu ndiyo msimamo rasmi wa rais wetu kuhusu jambo hilo au la.

Lakini kwa kuwa rais hajalikanusha hilo, tunapata sababu ya kuwa na mashaka kuwa rais wetu ni mshabiki au mfuasi wa utabiri wa mnajimu huyo.

Wapinzani kula matapishi yao: mjadala huu kuhusu mastakabali wa mageuzi hautanoga kama tusipojikumbusha yaliyowahi kusemwa kuhusu Serikali ya Awamu ya Nne.

Tunachokiona hapa katika matukio ya hivi karibuni, ni pamoja na maridhiano ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar na kuteuliwa viongozi wawili wa CUF kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Rais Amani Abeid Karume.

Lakini pia Rais Kikwete naye alimteua Ismail Jussa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Haya yote yametosha kuziba midomo, kelele na kebehi nyingi kutoka CUF dhidi ya utawala wa Rais Kikwete.

Ghafla Kikwete na Rais Karume wamegeuka waungwana, wasikivu, malaika, viongozi bora, hawakumbatii mafisadi, si wezi wa kura.

Nadhani tatizo lilikuwa ni njaa ya wenzetu, wala wasitudanganye kitu, sasa tumeelewa wazi kwamba kelele tulizozisikia miaka nenda rudi, kejeli na majigambo vimezikwa.

Lakini CUF kukubali kupewa vyeo hivi dakika za majeruhi wakati taifa likielekea kwenye uchaguzi mkuu zitawapeleka pabaya.

Ikitokea hivyo, CUF isigeuke nyuma kuomba huruma ya wana mageuzi wengine kwani wamepiga jaramba huku wakijiona. Hongera CCM kwa ‘usanii’ na ufundi mkubwa kwa kufunga bao dakika za majeruhi.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Machi 21 mwaka 2010

RAIS KIKWETE FUTA MACHOZI YA MAHAKAMA

Happiness Katabazi

“NAKUMBUKA Rais Jakaya Kikwete Mei, 2008 ulipokutana na majaji wote Bagamoyo, ulikubali kuutengea mhimili wa Mahakama mfuko wake lakini hadi leo hilo halijafanyika, tunajua kuwa nia yako bado ipo pale pale.

Lakini nakumbuka jeshini niliambiwa mjue kamanda wako, nami nathubutu kusema kuwa ninamjua kamanda wangu, hana kauli mbili, alisemalo ni sahihi atalitenda tu ni suala la muda.”
Maneno haya yalitamkwa na Jaji Mkuu Agustino Ramadhani, Februari 4 mwaka huu, katika sherehe ya Siku ya Sheria nchini ambayo huadhimishwa hapa nchini na mahakama zote, kuashiria mwanzo wa mwaka wa mahakama.

Kaulimbiu ya mwaka huu ilikuwa “Mahakama ikiwa mdau muhimu wa maendeleo katika taifa na umuhimu wa kuboresha mazingira yake ya kazi ili iweze kutoa huduma bora zaidi.”

Jaji Mkuu anasema kama kuna tatizo basi itungwe sheria au kama ipo sheria basi ifanyiwe marekebisho. Lakini hii miaka miwili na nusu ya kuwa Jaji Mkuu ameng’amua kuwa mafanikio yote ni lazima yakubiliwe na watendaji husika wa chombo hicho.

‘Wahenga wanasema penye udhia, penyeza rupia,’ hiyo ni rushwa, lakini nimetambua ili ufanikiwe lazima uelewane na watendaji ambao ndio mashine muhimu ya kutekeleza mipango yote iliyokusudiwa.

Anasema mahakama kuwa na mfuko wake ndio njia ya uhakika ya kung’oa mzizi wa fitina wa sababu zinazochelewesha utoaji wa haki kwa wakati na kuongeza kuwa suala muhimu linatakiwa kutekelezwa kwa haraka ni ujazwaji wa huo mfuko.

Anaeleza kuwa kifungu cha 16 cha Sheria ya Vyama vya Siasa, yaani The Political Parties Act, Mlango wa 258 wa sheria za Tanzania,kinasema: The Government shall...disburse up to not more than two per centum of annual recurrent budget. Na kwamba kwa mwaka huu wa fedha mahakama imepata asilimia 056 tu ya bajeti ya serikali . Lakini vyama vya siasa vimewekewa kisheria kiwango cha juu cha asilimia mbili.

“Mahakama ni mhimili ambao vyama vya siasa vyenyewe vinautegemea sana, fomu za uteuzi wa kugombea urais, ubunge na udiwani lazima zipitie mahakamani, baada ya uchaguzi mkuu kunakuwepo na kesi za kupinga matokeo.

“Nina hakika alichotuambia Bagamoyo Mei mwaka 2008, kuhusu mfumo wa Mahakama, atatupa bajeti hii, tena tunaomba ututilie walau asimilia mbili tu ya bajeti ya serikali, kwa hesabu za mwaka huu wa fedha itatakiwa kiasi cha sh bilioni 133.7 kiasi ambacho bado ni kidogo kuliko walichopewa Mkoa wa Mwanza cha sh 135,019,803,000,” anasema.

Jaji Ramadhani anaendelea kueleza kuwa hicho ndio kilio chake cha mwisho kwa rais na kwamba siku hiyo ya sheria ilikuwa siku yake ya mwisho kwani Desemba mwaka huu anang’atuka na kuongeza kuwa hilo ni hitaji la kikatiba na lazima alitii kwani Rais Amani Karume ametoa somo muhimu pamoja na kutakiwa na chama cha upinzani aendelee.

Aidha, anasema Katiba ya nchi inaiagiza Mahakama itoe haki kwa haraka lakini pia inawaruhusu kuchelewa kutoa haki kama zipo sababu za msingi.

Moja ya sababu ni ufinyu wa bajeti,kwa mwaka wa fedha wa 2009-2010 mahakama imepewa sh 37,854,397,000 (recurrent), kwa wilaya 123 za Tanzania Bara, mhimili huo upo mikoa yote 21 lakini bajeti inayopewa mikoa ni kubwa ukilinganisha na ile inayopewa mahakama na kutolea mfano kwa kipindi cha mwaka huu wa fedha na kwa current budgets, amechukua mikoa mitatu ambayo ni midogo kieneo, Mkoa wa Mtwara umepewa sh 51,691,383,000, Mkoa wa Mwanza sh 135,019,803,000 na Mkoa wa Mara umepewa sh 74,617,161,000.

“Bajeti ya Mtwara imezidi ile ya Mahakama kwa takriban sh bilioni 13, Mwanza ni kubwa zaidi ya mara tatu wakati bajeti ya Mara ni kubwa mara dufu.

“Narejea tena kusema Rais Kikwete mahakama tupo katika kila wilaya lakini tunayo bajeti ndogo kuliko mikoa yote hata ule mdogo kabisa,” anasema kwa masikitiko.

Hata hivyo anasema Mahakama inachukua hatua kadhaa kujaribu kukabiliana na upungufu huo, kwa mfano kwa upande wa Mahakama Kuu kuna mrundikano mkubwa wa kesi za jinai ambazo zinaleta kero kubwa na kufanya mahabusu katika magereza kadhaa kugoma kula.

Mradi wa Kurekebisha Sekta ya Sheria umekubali ombi lao na kuipatia Mahakama sh 831,640,000 ili kukabiliana na mrundikano wa kesi unaoendelea kukua siku hadi siku na kuzusha malalamiko yasiyoisha.

Jaji Ramadhani ambaye ni Brigedia Jenerali mstaafu, anaeleza kuwa Desemba 30 mwaka jana, alikutana na majaji wafawidhi wote 13, Naibu Mwanasheria Mkuu, Inspekta Jenerali wa Polisi, Mkurugenzi wa Mashitaka na mwakilishi wa Kamishna Mkuu wa Magereza kupanga mkakati wa kuzishughulikia kesi za jinai na namna ya kuzishughulikia hizo fedha katika hiyo miezi mitano iliyobaki kabla ya mwaka wa fedha kumalizika.

Katika kikao hicho anasema lilizuka suala la msingi, mahakama ndiyo waliopewa hizo fedha lakini wadau wengine muhimu hawakuambulia kitu, alikubali kugawana kiasi hicho ili wote wafanye kiwezekanacho badala ya kuzirejesha hizo fedha.

Kuhusu upande wa kesi za madai zinazohusiana na uchumi, anasema amekwishazungumza na Chama cha wenye mabenki nchini, zipo jumla ya kesi 261 katika kundi hilo zinazosubiri kumalizwa kusikilizwa zenye thamani ya trilioni za fedha za Kitanzania na za kigeni, chama cha wenye mabenki wamekubali kimsingi kuchangia fedha ili waweke mbinu za kuzimaliza hizo kesi haraka iwezekanavyo.

“Nimetumia unconventional ways, au kama wasemavyo kule nilipokuwa nikifanyakazi zamani, nimetumia madaraka kutafuta njia za kujikwamua, mashauri haya yanaathiri mno uchumi na maendeleo, trilioni za shilingi zimegandishwa kusubiri maamuzi ya hizi kesi, katu hatuwezi kuwa na maendeleo bila kutatua kesi hizi,” anasema Jaji Mkuu huku akionyesha kukerwa na hali hiyo.

Akiitaja sababu nyingine ni ile ya vitendea kazi hasusan zana za kitekinolojia za kisasa ambavyo vina gharama kubwa na kulipia mafunzo yake. Hata hivyo Aprili ,2008 mahakama iliingia mkataba na Investment Climate Facility for Africa ambayo Rais Mstaafu Benjamin Mkapa ni Mwenyekiti Mwenza wa mfuko huo na Omari Issa ni Afisa Mtendaji Mkuu kwenye makao makuu yao hapa jijini.

Anasema ICF imeipatia Mahakama dola za Marekani 2,000,000 na kupitia fedha hizo majaji wote wa Mahakama ya Rufaa, majaji wa Mahakama Kuu wote waliopo Dar es Salaam pamoja na makatibu wamepatiwa mafunzo ya hali ya juu ya kompyuta huko ESAMI, Arusha.

Anaendelea kueleza kuwa si hivyo tu bali zimenunuliwa kompyuta za mezani 164, laptop 126, printer heavy duty 4, photocopy kubwa 6, scanner 9, server kubwa 10 na vifaa vingine na kuongeza kuwa mwaka huu wanatarajia kutiliana saini mapatano mengine ya kiasi hicho.

Jaji Ramadhani anasema wakati mwingine sheria zenyewe zinawafanya wasuesue, kwa mfano uanzishwaji wa Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi kunawafanya majaji watano kushughulikia kesi zote za ardhi za nchi nzima.

Ardhi ndiyo msingi wa maendeleo ya nchi yoyote duniani, kuanzia Desemba mosi mwaka jana, alitoa agizo kuwa majaji wote wa Mahakama Kuu kote nchini ni majaji wa Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi.

Anasema agizo hilo lilipokewa vyema hata na Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi, John Chiligati, kwani sheria imefanyiwa marekebisho kuhusu hilo. Lakini bado watakuja na mapendekezo ya kufuta hata mabaraza ya ardhi ya wilaya (District Land Tribunals) watumie mfumo wa kawaida wa mahakama.

Aliongeza kuwa kuna uhaba wa majaji, kuwa anamshukuru Rais Kikwete kwa kuteua majaji wa Mahakama Kuu wengi zaidi, katika kipindi kifupi cha miaka minne ya uongozi wake ameweza kuteua majaji 41 na anajua kuwa hivi karibuni atampatia majaji wengine kumi na atateua majaji saba wa rufaa.

Katika kipindi cha miaka minne wapo waliostaafu au kumaliza mikataba yao, jumla ya majaji wa Mahakama Kuu 14 na 11 rais aliwateua kuwa majaji wa rufaa kujazia pengo la majaji 25 waliopungua Mahakama Kuu.

Hivyo majaji 41 walioteuliwa wameziba mapengo hayo 25 na ni majaji 16 tu ndiyo wamekuwa wa ziada na kukuza idadi ya majaji, kwa upande wa mahakama ya rufaa, majaji watatu wamestaafu na mmoja amefariki, Rais Kikwete alipoingia madarakani Mahakama ya Rufaa ilikuwa na majaji 8 sasa wapo 16, ongezeko la mara mbili, hilo ni jambo la kumpongeza rais.

Aidha, anaeleza katika kukabiliana na tatizo hilo la uchache wa majaji, majaji wa rufaa kumi waliamua kukatisha likizo yao ya mwaka na wakarudi kazini ambapo Januari 11 mwaka huu, walianza kusikiliza jumla ya rufaa na maombi 83, katika hizo walimaliza kabisa mashauri 61, mashauri manane yanasubiri kutolewa maamuzi na mashauri 13 yameahirishwa kwa sababu mbalimbali.

Kwa maelezo hayo ya kina yaliyotolewa na Jaji Mkuu, binafsi napongeza hatua zote za kimaendeleo zilizochukuliwa na uongozi wa Mahakama pia nawahamasisha wananchi wa kada zote wakiwemo wanasiasa tuungane na uongozi wa Mahakama kwa hatua yake ya kuanzisha mfuko wa Mahakama, kwa kumkaba koo Rais Kikwete na serikali yake kwa ujumla ili kuhakikisha anatimiza ahadi yake ya kuuchangia fedha mfuko huo.

Ieleweke kwamba wananchi wote ni wadau wa Mahakama kwa namna moja au nyingine hivyo tutambue huo msongamano wa viporo vya kesi mahakamani unasababisha wananchi wenzetu wanaokabiliwa na kesi za jinai ambao wameshindwa kutimiza masharti ya dhamana, au dhamana zao zimefungwa, au kesi zinazowakabili hazina dhamana kwa mujibu wa sheria ni wazi wataendelea kusota rumande.

Na siyo hivyo tu, pia tukae tukijua mahakama zinaposhindwa kutoa uamuzi wa kesi hizo ni wazi wanaokabiliwa na kesi hizo wawe washitakiwa au walalamikaji kwa nafasi zao watashindwa kushiriki shughuli za uzalishaji mali kwa ajili ya kesi hizo.

Hivyo rai yangu kwa Rais Kikwete, kama wewe mwenyewe kwa kinywa chako bila shinikizo la mtu yeyote ulilidhia uanzishe mfuko wa mahakama, basi uwe mwepesi kuagiza serikali yako ichangie fedha mfuko huo, uamuzi wa kuwateua majaji wengi bila kuuwezesha mhimili wa Mahakama ili uwe na bajeti imara kwani mwisho wa siku uamuzi huo usipotekelezwa utazidisha kilio.

Wakati umefika kwa serikali yetu kuongeza fedha kwenye sekta nyingine zinazoshirikiana na mahakama ambazo zinapata fedha kidogo kwani hakuna ubishi, serikali yetu imeelekeza fedha nyingi kwenye shughuli za kisiasa.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Februali 14 mwaka 2010