LIYUMBA ATUMIA HOJA YA YESU KUTOA UTETEZI


*ASEMA SERIKALI HAIJUI ITENDALO KWA KESI YAKE
*HUKUMU YAKE KUTOLEWA MEI 24
*AMTUPIA MZIGO MAREHEMU BALLALI

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba (62), ambaye sasa anakabiliwa na shtaka moja la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma, amedai serikali haijui itendalo dhidi ya kesi iliyomfungulia.


Liyumba ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, izingatie ukweli wakati wa kutoa hukumu dhidi yake Mei 24 badala ya kuwasikiliza watu wasiojua watendalo.

Maneno hayo mawili ‘hawajui watendalo’ yanafanana na yale aliyotumia Yesu Kristo, anayeaminika kuwa ni Mwokozi wa waumini wa Kikristo wakati akieleza kitendo cha Wayahudi waliokuwa wakimsulubisha (Luka 23:34).

Mshtakiwa huyo jana alipanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kutoa utetezi wake mbele ya Kiongozi wa Jopo la Mahakimu Wakazi, Edson Mkasimongwa, aliyekuwa akisaidiwa na Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa.

Kesi hiyo ambayo imevuta hisia za watu wengi ndani na nje ya jiji la Dar es Salaam ilifikishwa mahakamani hapo Januari 26 mwaka jana ambapo Liyumba alikuwa akikabiliwa na makosa mawili ambayo ni matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia hasara serikali ya sh bilioni 221.

Hata hivyo Aprili 9 mwaka huu, mahakama hiyo ilimfutia shtaka la kuisababishia hasara serikali baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha hasara kwa namba kama ilivyokuwa ikitakiwa.

Liyumba, aliongozwa kutoa ushahidi wake na wakili mahiri wa kujitegemea Majura Magafu aliyekuwa akisaidiwa na Jaji Mstaafu Hillary Mkate, Onesmo Kyauke na Hudson Ndusyepo huku upande wa mashitaka ulikuwa ukiongozwa na mawakili waandamizi Juma Mzarau, Ben Lincoln na Tabu Mzee.

Mstahakiwa huyo, alianza kujitetea saa tano asubuhi hadi saa saba mchana mbele ya umati wa watu uliofurika ndani ya mahakama hiyo na kusababisha watu wengine kusimama nje ya ukumbi wa mahakama, alidai kuwa anaiomba mahakama kuzingatia ukweli katika kuandika hukumu yake.

Amedai kuwa ameamua kutoa tahadhari hiyo kwa sababu upande wa mashitaka umewasilisha vielelezo ambavyo baadhi yake ni barua alizozisaini zilikuwa zinatoa maelekezo kwa kampuni ya ujenzi wa mradi wa Ten Mirambo Extention “Minara Pacha” ya Design&Service wakati kuna barua nyingine zilisainiwa na wasaidizi kwa niaba yake, na barua za kampuni ya Design&Service zilizokuwa zikiandikia BoT, hazikuletwa mahakamani hapo kwa makusudi.

“Waheshimiwa naomba sana mzingatie ukweli kabla ya kufikia kutoa hukumu dhidi yangu, kwani upande wa mashitaka umeleta barua hizo tu kwa sababu zimesainiwa na Liyumba, kama upande wa mashitaka unatenda haki ni kwa nini ulishindwa kuleta barua zilizosainiwa na wasaidizi wangu kwa niaba yangu ambao nao walikuwa wakitoa maelekezo mazito tu kuhusu mradi huo?

“Na kama kweli walikuwa wanatenda haki ni kwa nini wameshindwa kuleta zile barua ambazo kampuni ya ujenzi ilikuwa ikiiandikia BoT na mimi kwa kuwa niliteuliwa na Gavana (Marehemu Balali) kushughulika na masuala ya uongozi katika mradi huo, nilikuwa nazijibu baada ya kupata idhini ya gavana.

“Kwa faida ya waendesha mashitaka mimi nilikuwa nikijibu barua za Design&Service na barua hizo nilizosaini zimeonyesha wazi nilikuwa najibu barua hizo kwa kutumia kumbukumbu mbalimbali za barua zilizokuwa zinatoka nje kuja BoT...narudia tena kama hawa waendesha mashitaka walikuwa wanatenda haki wangeleta nyaraka hizo zote nilizozitaja.

Kwa sababu wanazozijua wao walipoona tu barua hizo zinasaini yangu wakazichomoa kwenye jalada ambalo linahifadhiwa kwenye ofisi ya Meneja wa Mradi na kuzileta mahakamani,” alidai Liyumba na kusababisha watu kuangua vicheko na wakili mwandamizi wa serikali Juma Mzarau ambaye alikuwa akimhoji kujiinamia na kisha kucheka.

Liyumba ambaye ni mchumi kitaaluma, aliiambia mahakama kuwa katika kipindi cha mwaka 2001-2006 alikuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa BoT na alistaafu kwa mujibu wa sheria Desemba 2008. Majukumu yake akiwa na wadhifa huo alikuwa akishughulika na shughuli zote zinazohusu uendeshaji wa benki.

Alieleza kuwa kiongozi wake wa kazi alikuwa Naibu Gavana huku nafasi ya Gavana ilikuwa ikishikiliwa na Daudi Balali na alikuwa akiwajibika kwake lakini kama hakuwepo alikuwa akiwajibika kwa naibu wake.

Alidai anaufahamu mradi wa ujenzi wa Minara Pacha kwani wakati anahamishiwa Makao Makuu ya BoT Dar es Salaaam, akitokea mkoani Mwanza alikuta mradi huo upo kwenye mchakato na ilikuwa mwaka 2000 na ujenzi wa mradi huo ulianza rasmi mwaka 2002.

Liyumba ambaye anamiliki hoteli moja na kampuni moja ya kutoa mikopo midogo midogo , alidai kuwa kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na benki hiyo, mradi ulikuwa chini ya kurugenzi aliyokuwa akiiongoza yeye ila kulikuwa na kitengo kinachojitegemea chini ya Meneja Mradi Deogratius Kweka na meneja huyo alikuwa anapeleka taarifa za mradi huo moja kwa moja kwa gavana.

“Huyo meneja mradi hakuwa mwajiriwa wa kudumu wa BoT bali alikuwa na ajira ya mkataba ambayo aliipata kutokana na kuanzishwa kwa mradi huo. Mimi nilikuwa nahusika kiutendaji kwa sababu Kweka hakuwa mwajiriwa wa kudumu wa BoT, na kwa kuwa hakuwa na ajira ya kudumu meneja huyo hakuwa na mamlaka ya kusaini barua za BoT kwenda kwa kampuni ya Design&Service.

“Mimi ndiye niliyeteuliwa na Gavana kuwa nasaini barua mbalimbali kwa niaba ya BoT zilizokuwa zikihusu mradi huo na kama mimi sipo alikuwa akizisaini msaidizi wangu na kumbukumbu zipo...kama Kweka angekuwa amepewa dhamana ya saini barua hizo za mradi wala mimi nisingeweza kusaini,” alidai Liyumba.

Huku akionyesha kujiamini, Liyumba alieleza utaratibu wa barua zilizokuwa zikienda BoT na zile zilizokuwa zikielekezwa kwake, barua zote zilizokuwa zikihusu mradi, zilifikia kwa gavana na yeye huzipeleka kwa Meneja Mradi na meneja huyo anatoa ushauri wa kitaaluma.

“Gavana, alikuwa akitoa maelekezo kwangu ya jinsi ya kuzijibu barua hizo ambazo mimi nilikuwa naweka saini yangu, ushauri wote wa ujenzi wa mradi ule Meneja Mradi alikuwa anautoa kwa gavana kwa sababu wafanyakazi wa Benki hawakuwa mainjinia,” alieleza.

Alifafanua kwamba watu wanapoizungumzia Menejimenti ya Benki Kuu, watambue kwamba menejimenti hiyo ni Gavana; hayo yametamkwa wazi kwenye Sheria ya Benki Kuu na kuongeza kuwa Jamhuri kudai yeye aliidhinisha mabadiliko ya ujenzi wa mradi huo bila idhini ya bodi ‘haijui itendalo’.

Alidai kwamba yeye na bodi ya wakurugenzi hawafanyi kazi kama inavyodaiwa kwa sababu haimhusu na wala haikumteua kuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala huku akisisitiza kuwa yeye alihusika katika mradi huo kwa shughuli za kiutawala tu.

“Aliyekuwa na jukumu la kupeleka chochote kilichohitajika kwenye mradi ni Meneja Mradi kwani ndiye aliyekuwa anaandaa taarifa za mradi kwa gavana, ndiye alikuwa anazipeleka taarifa hizo kwenye bodi.

Mapendekezo ya ushauri mabadiliko ya mradi yalikuwa kamati ya mradi na ilijadili na kuwahusisha washauri kutoka kampuni tatu ambazo zilikuwa zinatoa ushauri wa ujenzi huku malipo ya kazi yao yalikuwa yakilipwa na BoT.

“Baada ya gavana kupelekewa ushauri huo, kama akitaka kufanya mabadiliko ya ujenzi alikuwa anamuelekeza Meneja Mradi ambayo hurudi kuiarifu kamati na hatimaye hufikisha kile kilichoamuliwa kwa gavana.

“Mwisho kabisa naiomba mahakama hii tukufu wakati inaandaa hukumu dhidi yangu izingatie ukweli na iniachilie huru kwani hilo shitaka ambalo Jamhuri inadai nimetenda ...sioni kama linanihusu mimi kwani sijatenda kosa hilo na kwa kunishitaki Jamhuri imeonyesha haijui ilitendalo,” alidai Liyumba na kusababisha watu kuangua vicheko.

Naye aliyekuwa Kaimu Katibu wa Benki Kuu na Katibu wa Bodi ya Benki hiyo ambaye ni mwanasheria kitaaluma, Bosco Kimela (52), aliieleza mahakama kuwa shitaka linalomkabili Liyumba hastahili kushtakiwa nalo kwani hajalitenda.

Kimela ambaye anakabiliwa na kesi moja ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma na mbili za EPA na anaendelea kusota rumande kwa ajili ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, aliiambia mahakama pamoja na aliyekuwa na wadhifa huo pia alikuwa na wadhifa wa kuandaa vikao mbalimbali vya benki ambavyo gavana alikuwa anaviitisha.

Alidai taarifa za kitaalamu za mradi huo zilikuwa zinaandaliwa na Meneja Mradi na kuhusu mradi huo Liyumba hakuhusika kwa namna yoyote kutoa maamuzi yake binafsi kwani gavana alikuwa akimpatia orodha ya majina kabla ya kikao kufanyika na yeye alikuwa akiiandaa barua za mialiko na ya kuwaita wajumbe.

‘Kwenye vikao Gavana alikuwa akiwasilisha taarifa mbalimbali zinazohusu benki na Meneja Mradi, Deogratius Kweka, aliyekuwa akiwasilisha taarifa zinazohusu mradi huo na tangu mwaka 1992 hadi 2008 nikiwa na nyadhifa hizo sijawahi kushuhudia Liyumba akifanya maamuzi bila idhini ya Gavana, hilo halijawahi kutokea...mimi ndiye nilikuwa naandaa taarifa za vikao, ajenda, yatokanayo na mkutano, utekelezaji wa yaliyoamuliwa na kikao na nikishaandaa napeleka kwa Gavana na si vinginevyo.”

Baada ya kutoa maelezo hayo Wakili wa serikali Juma Mzarau aliiomba mahakama ipokee maelezo ya onyo ya Bosco kama kielelezo lakini ombi hilo lilipingwa vikali na wakili wa utetezi kwa madai kwamba shahidi huyo si wa upande wa mashitaka na kama jamhuri ilimuona shahidi huyo ni muhimu kwao isingemuondoa kwenye orodha yake ya ushahidi na kwamba upande wa mashitaka haujatoa sababu za kutaka mahakama hiyo ifute ushahidi ulitolewa jana na Bosco.

Akitoa uamuzi kuhusu ombi hilo la upande wa mashtaka, Hakimu Mkazi Mwandamizi Benedict Mwingwa alisema jopo hilo linatupilia mbali kwa sababu upande huo umeshindwa kutaja sababu za kukutaka ushahidi wa Bosco mahakama hiyo ikatae na kuamuru Bosco apande tena kizimbani kwa mara nyingine ili aendelee kutoa ushahidi wake.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, wakili Magafu aliiambia mahakama kuwa walikuwa wamekusudia kuleta mashahidi wanne, lakini kutokana na mashahidi hao wawili waliomaliza kutoa ushahidi wao jana, wameona ushahidi huo unakidhi haja hivyo wamefikia uamuzi wa kufunga kesi yao.

Aidha, Hakimu Mkazi Edson Mkasimongwa alisema mahakama imekubali ombi hilo la kufunga kesi kwa upande wa utetezi, na akazitaka pande zote katika kesi hiyo kuwa Mei saba , zilete majumuisho ya mchanganuo wa ushahidi ulitolewa jana, Mei 21 kesi hiyo itakuja kwa ajili ya kutajwa na Mei 24, mahakama hiyo ndiyo itatoa hukumu ya kesi hiyo.

Januari 26, mwaka jana, Liyumba na Meneja Mradi wa Benki Kuu, Deogratius Kweka, walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kusomewa mashitaka hayo ya kuidhinisha mradi wa majengo ya minara pacha bila idhini ya bodi ya wakurugenzi na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Mei 27 mwaka jana, mahakama hiyo iliwafutia kesi, lakini muda mfupi baada ya kuachiliwa walikamatwa tena mahakamani hapo na Mei 28 mwaka jana, Liyumba peke yake ndiye aliyerudishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka hayo na Kweka akawa ameachiliwa huru. Tangu kipindi hicho hadi sasa Liyumba anaendelea kusota rumande, baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, ambapo mahakama ilimtaka atoe fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya sh bilioni 110.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Aprili 23 mwaka 2010


BRELA:TULIISAJILI KENERL LTD

Na Happiness Katabazi

MSAJILI Msaidizi Mwandamizi wa BRELA, Maria Kiwia(52) ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kwamba kampuni ya Kenerl Ltd iliyodaiwa ni kampuni hewa na ilichota sh bilioni sita katika Benki Kuu ya Tanzania, ni kampuni halili kwani imesajiliwa na BRELA kwa mujibu wa taratibu zote za kisheria.


Kiwia ambaye ni mwanasheria kitaaluma alieleza alieleza hayo jana wakati akihojiwa na wakili wa utetezi Alex Mgongolwa na wakili wa serikali Timon Vitalis mbele ya jopo mahakimu wakazi, Prophil Lyimo, Edson Mkasimongwa na Salome Mwandu, alipokuwa akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo.

Shahidi huyo ambaye mwaka 2000 alikuwa akifanyakazi katika Kitengo cha Msajili wa Makampuni akiwa na wadhifa huo,shughuli zake zilikuwa ni kusimamia usajili wa makampuni na kutoa ushauri na alama za biashara na kuongeza kuwa anaifahamu vyema kampuni hiyo ya Kenerl Ltd kwani ilisajiliwa na Msajili wa Makampuni na kwamba yeye ndiye aliyeuska na ubadilishwaji wa jina la biashara ya kampuni hiyo ambayo awali ilikuwa ikiitwa Kenerl Mills Holdings Ltd kwenda Kenerl Ltd.

“Naitambua kampuni hiyo kwani ilisajiliwa na BRELA na mimi ndiye niliyeshughulikia na ombi lao kubadilisha jina la biashara na kuisajili hivyo si sahihi kusema kampuni hii ni hewa....kampuni hii ipo hai na ilitimiza matakwa yote ndiyo maana ikasajiliwa na hata siku moja BRELA haijawahi kulalamika kwamba kampuni hiyo ilikiuka taratibu za usajili”alidai Kiwia ambaye kwasasa ni wakili katika Benki ya Dimond Trust.

Kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi aliarisha usikilizaji wa kesi hiyo Mei 21-25 mwaka huu, na akauamuru upande wa mashitaka uakikishe siku hiyo unaleta mashahidi bila kukosa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Aprili 23 mwaka 2010

TUNAMSUBIRI UTETEZI WA LIYUMBA HIVI!


Katikati ni mimi Happiness Katabazi (Tanzania Daima),kulia ni Furaha Omar(Uhuru na Mzalendo),kushoto ni Neema Mgonja(Jambo Leo) na nyuma ni Regina Kumba (Habari Leo).Sisi sote pichani waandishi wa habari za mahakama nchini,tukiwa ndani ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, leo tukisubiri Aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba(62) aanze kujitetea.(Picha na Fancis Dande)

'UTOAJI FEDHA EPA ULIKUWA SAHIHI'

Na Happiness Katabazi

MENEJA wa Akaunti ya Fedha za Nje katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Steven Mwakalukwa (55) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kuwa benki hiyo iliidhinisha Kampuni ya Kenerl Ltd inayomilikiwa na Johnson Lukaza na nduguye Mweisigwa Lukaza ilipwe deni la sh bilioni sita kwa kuwa ombi lake lilikidhi matakwa ya kisheria na lilipita kwenye mlolongo sahihi.


Mwakalukwa alieleza hayo jana wakati akihojiwa na wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa, mbele ya jopo la mahakimu wakazi, Prophil Lyimo, Edson Mkasimongwa na Salome Mwandu, alipokuwa akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo.

Meneja huyo ambaye ni shahidi wa pili wa upande wa Jamhuri, alidai mwaka 2005 alikuwa akifanya kazi katika Idara ya Fedha za Nje BoT na majukumu yake yalikuwa ni kupokea majalada yanayoingia katika Idara ya Malipo na kwamba ombi la Kenneld Ltd alihusika na malipo yake kwa njia ya ujumbe wa kibenki.

Alidai kampuni hiyo ilikuwa ikitaka ilipwe deni la Kampuni ya Marubeni ya Japan na kuongeza kuwa Desemba mosi mwaka 2005 aliyekuwa Gavana marehemu Daudi Balali aliidhinisha deni hilo lilipwe na Desemba 8 mwaka huo, BoT iliandikia barua kampuni hiyo kuijulisha kwamba tayari imeishawaingizia kiasi hicho cha fedha kwenye akaunti ya kampuni hiyo yenye Na. 0220031004 iliyopo kwenye Benki ya Euro Africa, ambayo kwa sasa inatambulika kama Bank of Africa (BOA).

“BoT hailipi deni kiholela, hivyo ombi la kulipwa deni liliwasilishwa ofisini kwetu na kampuni ya washitakiwa, lilipita kweye idara ya madeni kisha likafikishwa kwa gavana na gavana akaidhinisha,” alieleza. Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa leo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Aprili 22 mwaka 2010

MENEJA BOA BANK ATETEA FEDHA ZA EPA

Na Happiness Katabazi

MENEJA Mkuu Msaidizi anayeshughulika na wateja wadogo wa Benki ya Afrika (BOA), Jerome Kimario (39), ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa ingizo la shillingi bilioni sita toka Benki Kuu kwenda akaunti ya Kampuni ya Kennely Ltd inayomilikiwa na Jonhson na ndugu yake Mwesigwa Lukaza halikuwa na kasoro yoyote.


Kimaro ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri katika kesi ya wizi wa sh bilioni 6, katika akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), inayowakabili washtakiwa hao wanaotetewa na mawakili wa kujitegemea Richard Rweyongeza na Alex Mgongolwa alitoa maelezo hayo jana wakati akihojiwa na wakili wa utetezi Alex Mgongolwa mbele ya jopo la mahakimu wakazi, Prophil Lyimo, Edson Mkasimongwa na Salome Mwandu, ambapo jana kesi hiyo ilianza kusikilizwa rasmi.

Kimario alidai washtakiwa hao ambao waliwasilisha nyaraka sahihi mwaka 2004, wakiomba kufungua akaunti ya kampuni hiyo kwa kianzio cha shilingi milioni 15, ambapo BOA, haikuwa na shaka kuhusiana na akaunti hiyo kutokana na kwamba kampuni ni mteja wa kuaminika.

“Kennely Ltd inamilikiwa na Johnson na Mwesigwa ni wateja wazuri wa benki yetu kwani walifuata taratibu zote za ufunguaji akaunti ambapo waliweka kianzio cha sh milioni 15, na Desemba 7, 2005, BoT iliingizia akaunti ya kampuni hiyo dola za Kimarekani milioni 6 na kwa kweli benki yetu ililipokea vyema ingizo hilo na kulifanyia kazi kitaalamu kwani tulibaini halikuwa na kasoro zozote,” alieleza Kimario.

Awali akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili wa Serikali Timon Vitalis aliithibitishia mahakama kuwa ni kweli mshtakiwa wa kwanza (Johnson), ndiye aliyefungua akaunti hiyo kwa kuwasilisha nyaraka halali, na kudai mshtakiwa wa pili hakuhusika katika ufunguaji wala uchukuaji wa fedha katika akaunti hiyo.

Kiongozi wa Jopo la Mahakimu Wakazi, Profil Lyimo, aliahirisha usikilizaji wa kesi hiyo hadi leo na kuamuru upande wa serikali umlete shahidi wa pili.

Wakati huo huo mfanyakazi wa Benki ya International Commercial, Dorine Chonjo, anayetetewa na wakili wa kujitegemea, Furgence Massawe, alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Stewart Sanga, akikabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama, kughushi na wizi wa sh bilioni moja kwa njia ya mtandao, mali ya benki hiyo.

Wakili wa Serikali Tofil Mtakyawa alidai makosa hayo yalitendeka Desemba 21 mwaka jana. Mshtakiwa alikana mashtaka yote.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Aprili 21 mwaka 2010

SHAHIDI KESI YA EPA AUGUA GHAFLA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana ilishindwa kuanza kusilikiza ushahidi katika kesi ya wizi wa sh bilioni 6 katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu, inayomkabili Johnson Lukaza na nduguye Mwesigwa Lukaza kutokana na shahidi kuugua ghafla.


Wakili Mwandamizi wa Serikali, Fredrick Manyanda, alidai mbele ya jopo la mahakimu wakazi, Phofily Lyimo, Edson Mkasimongwa na Salome Mwandu, kuwa wasingeweza kuendelea na kesi hiyo kwa kuwa shahidi, Mary Kiwia, waliyekuwa wamemuandaa ameugua ghafla.

“Tunaomba kesi iahirishwe kusikilizwa kwa sababu leo shahidi tuliyekuwa tumemuandaa ameugua ghafla na tulikuwa hatujaandaa shahidi mwingine” alidai Wakili Manyanda.

Hakimu Mkazi Lyimo alikubaliana na ombi hilo na akaiahirisha kesi iyo hadi leo ambapo shahidi wa upande wa mashitaka anatarajiwa kutoa ushahidi wake.

Hii ni mara ya pili kwa shahidi huyo kuugua pindi inapofika wakati wa kutakiwa kupanda kizimbani kutoa ushahidi wake.

Mara ya kwanza ilikuwa Juni 8 mwaka jana, alipofika mahakamani hapo wakati akisubiri kupanda kizimbani kutoa ushahidi wake aliugua ghafla na hivyo kufanya mahakama kuahirisha usikilizwaji wa shauri hilo.

Mbali na Johnson, mshitakiwa mwingine ni Mwesigwa Lukaza ambapo wote kwa pamoja wanatetewa na wakili wa kujitegemea Alex Mgongolwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne Aprili 20 mwaka 2010

LIYUMBA KUANZA KUJITETEA

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba ambaye anakabiliwa na tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi ya umma, kwa kuidhinisha ujenzi wa mradi wa majengo ya minara pacha ‘Twin Towers’ bila idhini ya bodi ya wakurugenzi, ataanza kujitetea wiki ijayo.


Kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Edson Mkasimangwa, alisema jana kuwa Liyumba ataanza kujitetea Aprili 22 na 23.

Awali, wakili wa mshitakiwa huyo, Majura Magafu, alidai mteja wake anatarajia kuwa na mashahidi watatu katika utetezi wake.

Aliwataja mashahidi hao kuwa ni Mkurugenzi wa Mahesebu wa BoT, Rashid Mwanga, Kaimu Katibu wa Kitengo cha Sheria BoT, aliyekuwa Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi wa BoT, anakabiliwa na kesi mbili za Akaunti ya Maeni ya Nje (EPA) ambaye mpaka sasa anasota rumande kwa kushindwa kutumiza masharti ya dhamana, Bosco Kimela, Mkurugenzi wa Fedha Mstaafu wa BoT, Elisa Isangya.

Kimela na Isanya, awali walikuwa mashahdi wa upande wa mashitaka, lakini baadaye waliondolewa kwenye orodha ya mashahidi wa upande huo.

Wakili Magafu baada ya kutaja shahidi hao aliiomba mahakama kutoa hati za kuitwa mahakamani kwa mashahidi hao.

Wakili huyo aliwasilisha orodha hiyo ya mashahidi kutokana na amri iliyotolewa na kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi wakiongozwa na Mkasimangwa Aprili 9 mwaka huu.

Aprili 9, Mahakama ya Kisutu ilimfutia Liyumba shitaka moja la kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221, hivyo kubakiwa na shitaka moja la matumizi mabaya ya ofisi ya umma.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Aprili 17 mwaka 2010

MARANDA AANZA KUJITETEA KESI YA EPA

Na Happiness Katabazi

MWEKA HAZINA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma, Rajabu Maranda, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kuwa alichokizingatia katika mchakato wa kudai deni katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu ya Tanzania ni kupata fedha na si kutazama nyaraka.


Maranda alitoa maelezo hayo mbele ya jopo la mahakimu wakazi, Saul Kinemela, aliyekuwa akisaidiana na Elvin Mgeta na Focus Bambikya ambapo jana ilikuwa ni mara yake ya kwanza kupanda kizimbani kujitetea katika kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 katika akaunti ya EPA, inayomkabili yeye na binamu yake Farijala Hussein.

Akiongozwa na wakili wake, Majura Magafu, kutoa ushahidi wake ambapo ushahidi aliokuwa akiutoa ulikuwa ukitofautiana na vielelezo vya upande wa mashtaka na maelezo aliyoyatoa wakati alipohojiwa kwenye Tume ya Rais ya Kuchunguza Wizi wa EPA, alidai kwamba yeye aliweka umuhimu katika kupata fedha toka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwanza na si kutazama nyaraka ambazo ni hati ya idhini ya kudai deni la kampuni ya BC /Cars Export ya Mumbai India na hati za usajili wa kampuni yao ya Kiloloma&Brothers iliyotolewa na BRELA kwa sababu nyaraka hizo zilikuwa zimeshapokelewa na Farijala.

Maranda alidai licha ya kutokuwa makini kuzikagua nyaraka hizo pia alikana madai ya kuibia BoT na kusisitiza fedha hizo aliingiziwa kihalali kwenye akaunti yake na akakana kuitambua kampuni ya Kiloloma & Brose Enterprises ila akakiri anaitambua kampuni ya Kiloloma &Brothers ambayo yeye ni miongoni mwa wamiliki wake.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati Magafu na Maranda:

Wakili: Unadaiwa ulijipatia ingizo la sh bilioni 1.8 kwenye akanti yako mkijidai mmepewa idhini na kampuni hiyo ya India. Ieleze mahakama ukweli ni upi?

Maranda:Nakumbuka mwaka 2005 Farijala alikuja na mtu aitwaye Charles Issac Kissa, akamtambulisha kwangu na Kissa akanieleza ana shida anaomba nimkopeshe sh milioni 500, kwani alikuwa amepewa kazi na BC/Cars ya kudai deni lake ambalo walikuwa wakiidai BoT kwa miaka 20.

Nilimuuliza dhamana yake nini akasema hana, hivyo nikamshauri aende benki akaonyeshe nyaraka zinazoonyesha amepewa kazi hiyo.

Wakili:Baada ya Kissa kushindwa kupata kitu cha kuweka dhamana, alifanyaje?

Maranda:Nilimshauri aende nyumbani akatafakari na atuuzie ile kazi yake ili sisi tudai lile deni zima na atukabidhi sisi kwa yule anayedai ili mimi na Farijala tudai na yeye akataka atuuzie kampuni yake ya Kiloloma&Brother, lakini sisi tulikataa kwani hatukujua mbeleni kungetokea nini.

Ninakumbuka siku hiyo hatukfikia mwafaka aliporudi kesho yake akasema alikuwa tayari kukubaliana na sisi kwa utaratibu kwamba amana yake atupatie nusu na tukafungue akaunti pamoja ili siku deni likilipwa atupatie fedha zetu na tulikubaliana naye kwani tuliona hilo ni la msingi.

Wakili:Hii kampuni ya Kiloloma &Brothers nani alikuwa mmiliki wake?

Maranda:Charles Issack Kissa. Na tulikubaliana naye na tukamwambia Kisssa aende BRELA akaingize jina langu na la Farijala kama wamiliki pia wa kampuni hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa,Aprili 16 mwaka 2010

WAZEE EAC WAITEKA MAHAKAMA KUU DAR

Na Happiness Katabazi

WAZEE wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jana walizusha tafrani katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, muda mfupi baada ya Jaji Njengafibili Mwaikugile kutoa maelekezo ya kuwataka waende wakatafakari upya na kumletea taarifa sahihi zitakazomwezesha kufikia uamuzi wa kutoa haki katika shauri lao.


Wazee hao ambao wanakadiriwa kufikia zaidi ya 100, walizingira viwanja vya Mahakama Kuu kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa sita mchana, hali iliyosababisha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), wakiwa kwenye gari aina ya Defender, yenye namba za usajili T220 AMV kuwasili katika viwanja hivyo na kuwatawanya wazee hao.

Tanzania Daima Jumatano, ilishuhudia askari hao wakiwa wamebeba silaha nzito na kuvalia mabomu ya machozi kiunoni, tayari kuwakabili wazee hao ambao walikuwa wakali mithili ya mbogo.

“Leo hatuondoki hapa, tunalala hata kama ni mwezi mzima. Tumechoka kupigwa tarehe, leo tuliambiwa ni siku ya hukumu, lakini tumejikuta tunapangiwa tarehe nyingine kuja kuchukua mafao yetu. Kibaya zaidi jaji anatuambia mambo mengine tusiyoyataka. Leo hatuondoki hapa,” alisikika akisema mzee mmoja wa makamo ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja kutokana na purukushani iliyokuwepo.

Hata hivyo Polisi na FFU walipofika, hawakutumia nguvu kuwatawanya badala yake iliwachukua wawakilishi wao saba na kuondoka nao hadi katika ofisi ya Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa mahojiano.

Wakati wawakilishi wao saba wakichukuliwa na polisi hadi Ofisi ya Kanda Maalum ya Dar es Salaam, wazee wengine zaidi ya 100 waliandamana kujua hatma ya wenzao ambao hata hivyo waliachiwa baada ya kuhojiwa kwa muda.

Awali Jaji Mwaikugile anayesikiliza kesi hiyo, alikataa ombi la wazee hao kutaka mahakama iwatambue wawakilishi wapya katika kukazia hukumu ya kesi ya madai Na.95/2010 na badala yake aliwataka mawakili wao wa zamani, Adronicus Byamungu na Rukwalo na wakili wao mpya, Pius Chabruma, kukaa pamoja ili waondoe hati ya kusudio la kukata rufaa na kuwataka kurudi mahakamani hapo Aprili 30.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na vurugu hizo, Msajili wa Mahakama Kuu Wilaya ya Dar es Salaam, Lameck Mlacha, alikiri kutokea kwa vurugu hizo za wazee.

“Kama mlivyoshuhudia, tafrani iliyokuwa ikiendelea katika viwanja vya mahakama yetu. Hao wazee wameleta rabsha na walitaka kuingia ndani ya mahakama ili wawashambulie wenzao saba kwa madai kwamba wamewasiliti; lakini polisi wamefanikiwa kuwadhiti na tunapenda kuutangazia umma kwamba rabsha hizo hazijaleta uharibifu katika ofisi za mahakama,” alisema Mlacha.

Kwa upande wake, Kamanda Kova, naye alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kuongeza kwamba wamezungumza na wazee hao na kufikia uamuzi wa kusitisha tafrani hiyo na kutekeleza maagizo ya mahakama.

“Kinachoonekana katika tafrani hiyo ni wazee hao kugawanyika katika makundi mawili ambayo hayaaminiani na kundi jingine lilifahamu jana kesi yao ilikuja kwa ajili ya kutolewa hukumu wakati si kweli kesi hiyo ilikuja kwa ajili kusikiliza hoja,” alisema Kova.

Baada ya kuzungumza na waandishi wa habari, Kova alilazimika kutoka ndani ya ofisi yake na kusimama katika uwanja wa ofisi na kuanza kuwahutubia wazee hao kilichotokea mahakamani hapo jana.

Wazee hao walimwelewa na ilipofika majira ya saa 9:21 alasiri, walitawanyika huku wengine wakimpongeza Kova kwa kuwapa ufafanuzi bila kutumia nguvu.

Awali katika kesi ya madai 95/2003 iliyofunguliwa na wazee 31,831 hao dhidi ya serikali, Mahakama Kuu ilitoa hukumu ya maridhiano na ikaamuru wazee hao walipwe sh bilioni 117 lakini baadaye waliwasilisha ombi la mapitio ya hukumu hiyo na Jaji Katherine Oriyo alilitupa ombi hilo.

Baada ya ombi hilo kutupwa, wazee hao waliwasilisha hati ya kutaka kukata rufaa, lakini waligawanyika baada ya wengine kutaka kukazia hukumu ya awali.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano Aprili 14 mwaka 2010

RAUNDI YA PILI LIYUMBA KIDEDEA,DOLA IMEJIFUNZA NINI?


Na Happiness Katabazi

MEI, 31 mwaka jana niliandika makala katika gazeti hili iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho: “Raundi ya kwanza Liyumba kidedea,dola limejifunza nini?.” Paragrafu ya kwanza ilikuwa na maneno yasemayo, ‘Vita dhidi ya ufisadi vilianza kwa kishindo. Kwa kishindo hichohicho itamalizika bila ya wananchi kujua imemalizika kwa namna gani.”


Nilifikia uamuzi wa kuandika makala hiyo baada ya Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema, Mei 27 kuifuta kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221 iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba, na meneja mradi majengo ya minara pacha katika benki hiyo, Deogratius Kweka.

Hakimu huyo aliifuta kesi hiyo baada ya upande wa mashtaka uliokuwa ukiongozwa na Wakili Kiongozi Justus Mulokozi kukiri mbele ya mahakama hiyo kuwa hati ya mashtaka ilikuwa imekosewa lakini muda mfupi baada ya washtakiwa kuachiliwa walikamatwa tena.

Mei 28 mwaka jana, Liyumba anayetetewa na mawakili wa kujitegemea Jaji Mstaafu Hillary Mkate, Majura Magafu, Onesmo Kyauke na Hudson Ndusyepo peke yake ndiye aliyerudishwa mahakamani hapo na kufunguliwa kesi mpya ya jinai Na.105/2009 ambapo mashitaka yalikuwa ni yale yale ya matumuzi mabaya na kusababisha hasara ya sh bilioni 221, huku Kweka akiachwa huru.

Tangu kipindi hicho hadi sasa Liyumba ameendelea kusota rumande kwa sababu ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka atoe fedha taslimu au kuwasilisha hati ya mali yenye thamini ya sh bilioni 110.

Aidha, Septemba 20 mwaka jana, katika gazeti hili niliandika makala iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho, “Watanzania wategemee nini kwenye ‘PH’ ya Liyumba?”
Ndani ya makala hiyo nilimweleza DPP kwamba kama mkoba wake katika kesi hiyo haukuwa na ushahidi madhubuti ni vizuri angeiondoa mapema mahakamani ili wasipoteze muda wa mahakama na fedha za walipa kodi.

Baada kuandika makala hizo baadhi ya wanasheria wa serikali waandamizi walinipongeza kwa makala hizo kwani zina ukweli mtupu na wakaniuma sikio na kunieleza mwisho wa siku serikali itashindwa kufurukuta katika kesi hiyo na walidiriki kuifananisha kesi hiyo na ‘sinema’.

Nimewahi kuandika kuwa Sheria ya Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ya mwaka 2006 ilitungwa kwa shinikizo la wafadhili, serikali iliburuzwa miguu kwa miaka kadhaa lakini hatimaye ilisalimu amri pale wafadhili walipotishia kuwa wasingetoa mikopo, misaada katika nchi ambazo zisingeonyesha nia ya kupambana na rushwa (ufisadi sasa), dawa za kulevya na ugaidi.

Tanzania ilisalimu amri haraka na ikatunga sheria ya ugaidi ambayo ni kinyume kabisa na haki za binadamu na ikatunga sheria ya rushwa iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2006 ambayo inatumika hivi sasa. Kwa hiyo tunaona serikali yetu haikuwa na nia ya dhati ya kupambana na majanga hayo, ila sheria hizo zilitungwa kishabiki, kishikaji na kisanii.

Nimelazimika kutumia kumbukumbu hizo sahihi hapo juu ili ziweze kuunga mkono mada yangu ya leo ambayo nitajadili uamuzi uliotolewa April 9 mwaka huu na Kiongozi wa Mahakimu Wakazi (Edson Mkasimongwa), Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa wa kumfutia shitaka moja kati ya mashitaka mawili yaliyokuwa yakimkabili Liyumba.

Kwa maelezo kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha kupeleka ushahidi wa kuthibitisha shitaka la pili ambalo ni la kuisababishia serikali hasara. Aidha imemuona Liyumba ana kesi ya kujibu katika shitaka la kwanza la matumizi mabaya ya ofisi ya umma.

“Mahakama inaamini alichokizungumza Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Juma Reli, katika ushahidi wake ni ukweli mtupu na ndiyo maana alivyomaliza kutoa ushahidi wake alitoka ndani ya mahakama hii kwa amani na mawakili wa serikali hawakulalamika kwamba shahidi wao ametoa ushahidi wa uongo…kwa hiyo mahakama hii inatamka kiasi cha fedha kilichoongezeka katika ujenzi wa mradi ule kilitumika kwa utaratibu wa fedha za serikali zinavyotakiwa zitumike.

“Kwa heshima na taadhima jopo hili halikubaliani na hoja ya upande wa mashitaka iliyotaka mahakama hiyo isikubaliane na hoja ya upande wa utetezi iliyosema huwezi kuthibitisha hasara katika mradi huo hadi uwe na ripoti ya mwisho ya fedha zilizotumika kwenye mradi ule kwa sababu hata ripoti hiyo ingekuwepo isingeweza kuondoa makadirio ya gharama zilizokadiriwa na mkadiriaji wa majengo wa mradi huo.

“Mahakama inasisitiza haikubaliani na hoja hiyo ya upande wa mashitaka kwa sababu katika kesi hiyo hasara iliyodaiwa amepata mwajiri wa mshitakiwa ni lazima ithibitishwe kwa namba na ripoti…sasa katika kesi hii hasara iliyopatikana haiwezi kuwa sawa na namba ya ripoti ya Mkadiriaji wa Majengo kwani majengo ya nyongeza yamejengwa …labda ingekuwa majengo hayo mengine yanayodaiwa kujengwa nje ya mkataba wa awali na fedha hazionekana hilo lingekuwa ni jambo jingine.

“Na upande wa mashitaka wenyewe kupitia mawakili wake ukiri mbele yetu kwamba makadirio ya awali yaliyapaswa kujengwa magorofa 14 lakini baada ya mabadiliko ya ongezeko la ujenzi ziliongezeka ghorofa tatu nyingine juu hivyo kufanya kuwa na majengo mawili na kila jengo lina ghorofa 17 kwenda juu na kweli majengo yamejengwa:

“Kwa maelezo hayo mahakama hii inamfutia mshitakiwa shitaka la pili kwa mujibu wa kifungu cha 230 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 an na akaueleza upande wa mashitaka upo huru kukata rufaa kama haujalidhika na uamuzi huo,” alisema Mkasimongwa na kusababisha ndugu na jamaa wa mshitakiwa wakisikika kwa sauti wakisema, ‘Asante Yesu.’

Kutokana na uamuzi huo wa Hakimu Mkazi Mkasimongwa na wanajopo wenzake, umedhihirisha pasipo shaka kwamba wachunguzi wa TAKUKURU ambao ndiyo walipeleleza kesi hii, na waendesha mashitaka walikuwa hawajui walichokuwa wanakifanya katika kuthibitisha shitaka hilo lililofutwa au walikuwa wakijua ila waliamua kumuandalia shitaka hilo Liyumba.

Kwa makusudi mazima ili wamkomeshe kwasababu walijua hawezi kutimiza masharti na hivyo ni lazima angesota jela kwa sababu kisheria mahakama inapotoa masharti ya dhamana kwa mshitakiwa wa kesi yoyote ile ni lazima masharti hayo yatimizwe na si vinginevyo na endapo mshitakiwa anashindwa kutumiza anatakiwa aende rumande hadi atakapoyatimiza masharti husika.

Kama mawakili wa serikali ambao tunawashuhudia wakija pale mahakamani kwa mikogo huku wakiwa wanayaburuza masanduku kama wamehifadhi nyoka kwenye masanduku hayo na kuvalia suti utadhani ni wachungaji waliokimbiwa na waumini’ kama hawana taaluma ya kutosha kwa nini wasiombe ushirikiano wa kitaalum toka kwa mawakili wengine wenye ujuzi ambao mawakili wengine binafsi walikuwa walimu wenu vyuoni?

Serikali sasa iache uchoyo na ukiritimba katika mambo ya kitaaluma, ipende kushirika wanataluuma wenye uwezo kwenye maeno yao. Naomba kutoa hoja.

Nayasema haya kwa uchungu kwasababu ni kodi za wanachi ndizo zilizowasomesha mawakili wengi wa serikali na ndizo zinazotumika kuwalipa mishahara na fedha hizo za wavuja jasho zinazotumika kuwaweka hotelini baadhi ya mawakili wanakwenda kujichimbia katika hoteli hizo kuandika hoja mbalimbali katika kesi zilizofunguliwa na jamhuri.

Kama hawa mawakili wa serikali wanapokea mishahara inayotokana na kodi zetu, wananchi tuna haki ya kuhoji mambo wanayoyafanya ambayo hayaturidhishi.

Baadhi ya mawakili wetu wa serikali wanaonekana kuwa dhaifu na wababaishaji katika kesi wanazozisimamia na wakati mwingine nimekuwa kijiuliza akilini mwangu ubabaishaji huo unatokana ama wakati wapo vyuoni walikuwa wakiangalizia majibu kutoka kwa wenzao au walikuwa wakiiba mitihani.

Sasa kubabaikababaika kwa mawakili wa serikali waliokuwa wakiongozwa na Juma Mzarau aliyekuwa akisaidiwa na Prosper Mwangamila na Ben Lincolin katika kesi ya Liyumba hadi kusababisha mahakama hiyo awali kumfutia kesi mshitakiwa kwa sababu hati ya mashitaka ilikuwa imekosewa na juzi Hakimu Mkazi Mkasimongwa kumfutia shitaka moja mshitakiwa kwasababu upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha shitaka hilo la kusababisha hasara ni dhahiri ni ishara mbaya kwa shitaka lilobaki.

La matumizi mabaya, Watanzania sasa tujiulize kama jamhuri imeshindwa kuthibitisha shitaka la kusababisha hasara ambapo shitaka hilo linakuja baada ya mtu kutumia ofisi yake vibaya. Je upande wa mashitaka wanauakikishiaje umma kwamba mwisho wa siku wataweza kuthibitisha shitaka la matumuzi mabaya? Hilo tuliachie mahakama kwani mwisho wa siku itatoa hukumu yake kutokana shitaka hilo, ni suala la muda, tusubiri tuone.

Je, itakapotekea watuhumiwa wa kuachiwa huru si kesi zitakuwa zimekwisha kwa kishindo kile kile kama zilivyofunguliwa kwa kishindo? Tuseme nini sasa.usanii mtupu au ufisadi mtupu unaofanywa na mawakili wetu wa serikali?

Kushindwa kufurukuta kwa serikali katika shitaka hilo, nawaomba wananchi wenzangu wawe pamoja na sisi waandishi wa habari za mahakama kufuatilia kesi kama hizi zilizosalia mahakamani mfano kesi ya matumuzi mabaya na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba,Gray Mgonja na Daniel Yona; kesi nyingine ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia Profesa Costa Mahalu na Mkurugenzi Fedha na Utawala wa ubalozi huo Grace Martin ili hatimaye tukoleze kiu ya Watanzania katika harakati za kupambana na ufisadi.

Mwisho kabisa naupongeza Mhimili wa Mahakama nchini kwa kujipambanua kama chombo cha kutoa haki bila upendeleo, kushinikizwa na bila kuogopa. Jopo la mahakimu wakazi linalosikiliza kesi hiyo, Mkasimongwa, Mlacha na Mwingwa kutokana na uamuzi wake juzi nadiriki kusema kuwa limefanya kazi ya kishujaa na iliyoendelea kuuletea heshima mhimili wa mahakama wa nchi yetu.

Sisi tuliokuwa tunahudhuria kesi hii tangu ilipofunguliwa mahakamani hapo Januari 26 mwaka jana hadi juzi, tumeshuhudia vituko, shinikizo, ubabe uliojidhihirisha kwa wingi wa makachero waliokuwa wanaipamba mahakama ya Kisutu kwa staili tofauti kila kukicha.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Aprili 11 mwaka 2010

LIYUMBA APANGUA SHITAKA KUU


Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana ilimfutia shitaka moja kati ya mashitaka mawili yaliyokuwa yakimkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, kwa maelezo kuwa upande wa mashitaka umeshindwa kupeleka ushahidi wa kuthibitisha shitaka mojawapo.


Katika kesi hiyo ya jiani Na.105/2009 inayomkabili mshitakiwa huyo, Liyumba alikuwa akikabiliwa na shitaka la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma pale alipoidhinisha ujenzi wa mradi wa majengo ya minara pacha “Twin Tower” bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi. Shitaka la pili ni kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Uamuzi huo ulitolewa jana na kiongozi wa Jopo la Mahakimu Wakazi, Edson Mkasimongwa, aliyekuwa akisaidiana na Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa. Jana kesi hiyo jana ambayo iliudhuriwa na umati wa watu wakiwemo ndugu na jamaa wa mshitakiwa kwaajili ya mahakama hiyo kutoa uamuzi wa kwamba mshitakiwa huyo ana kesi ya kujibu au la.

Akisoma uamuzi huo uliochukua dakika 50 na huku akionyesha kujiamini Mkasimogwa alisema jopo hilo limepitia kwa kina ushahidi uliotolewa na mashahidi nane wa upande wa Jamhuri na vielelezo 12 na kupitia majumuisho ya kesi hiyo yaliyowasilisha na mawakili wa pande zote mbili, jopo hilo limeona Liyumba ana kesi ya kujibu katika shitaka la kwanza la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma. Amefutiwa shitaka la pili la kusababisha hasara.

Mkasomongwa ambaye alikuwa akisoma uamuzi huo huku akionyesha umakini alisema kwa mujibu wa ushahidi uliotelewa umedhibitisha kwamba ofisi ya Kurugenzi ya Utumishi na Utawala ilikuwa ikiongozwa na Liyumba na ndiyo ofisi iliyokuwa imepewa jukumu la kuradi mradi huo wa ujenzi licha hakuna ushahidi uliotolewa mahakamani kwamba mshitakiwa huyo alikuwa na mamlaka ya kuidhinisha mabadiliko ya ujenzi wa mradi wa majengo hayo isipokuwa.

“Na kwamba mujibu wa ushahidi huo umeonyesha Meneja Mradi sisi tunamkewa Meneja mradi chini ya Liyumba kwani alikuwa akiripoti kwa mshitakiwa na mshitakiwa alikuwa akiripoti kwenye Menejimenti na Menejimenti ilikuwa ikiripoti kwenye bodi kuhusu taarifa ya maendeleo ya mradi …sasa kwa mtiririko huo tunaungana na upande wa mashitaka mabadiliko ya ongezeko la mradi kabla ya kufanyika yalipaswa yapewe idhini na bodi na si kama ilivyodaiwa kufanywa na Menejimenti kufanyamabadiliko ya mradi na kisha kupeleka taarifa kwa bodi ili ipewe idhini.

“Kwa mujibu wa kielelezo cha kwanza ambacho kilikuwa ni mkataba, hakukuwa na mkataba mwingine mradi ule ulikuwa na thamani ya dola za Kimarekani milioni 73,600 lakini katika utekelezaji ambapo Liyumba alikuwa akisimamia gharama zilipanda na kufikia dola 357,675 na zilitumika na ushahidi unaonyesha mradi huu menejimenti ilipitisha ongezeko hilo awali kabla idhini ya bodi.

“Pia kuna ushahidi kwamba masula hayo ya mabadiliko ya mradi hayakujadiliwa na Menejimenti ya Benki isipokuwa Bodi ndiyo iliyoyajadili, na inaonekana ni matumuzi ya bodi; hivyo mahakama inamuona mshitakiwa anapaswa ajitetee au ajieleze kuhusu shitaka la kwanza,” alisema Mkasimongwa.

Kuhusu shitaka la pili la kusababisha hasara, alisema mahakama ilipaswa ielezwe na upande wa mashitaka kuwa mshitakiwa alisababisha hasara kwa makusudi, au bahati mbaya na kuendelea kuchambua kuwa kuhusu hoja ya serikali kupata hasara, mwajiri wa mshitakiwa alipaswa aonyeshe mradi uligharimu kiasi ghani na hasara iliyopatikana ni kiasi gani.

Akichambua ushahidi wa shahidi wa nane ambaye ni Naibu Gavana wa Benki Kuu, Juma Reli, ambaye aliieleza mahakama hiyo kuwa anashindwa kuthibitishia mahakama hasara iliyopatikana kwasababu hadi sasa ripoti ya mwisho ya fedha za matumuzi ya ujenzi wa mradi huo haijatoka, alisema kutokana na ushahidi huo umesababishia mahakama ifikie uamuzi wa kujiridhisha kwamba ushahidi ushahidi wa upande wa mashitaka una mkanganyiko.

“Mahakama inaamini alichokizungumza Juma Reli ni ukweli mtu na ndiyo maana alivyomaliza kutoa ushahidi wake alitoka ndani ya mahakama hii kwa amani na mawakili wa serikali hakulalamika kwamba shahidi wao hametoa ushahidi wa uongo…kwahiyo mahakama hii inatamka kiasi cha fedha kilichoongezeka katika ujenzi wa mradi ule kilitumika kwa utaratibu wa fedha za serikali zinavyotakiwa zitumike.

“Kwa heshima na taadhima jopo hili halikubaliani na hoja ya upande wa mashitaka iliyotaka mahakama hiyo isikubaliane na hoja ya upande wa utetezi iliyosema huwezi kuthibitisha hasara katika mradi huo hadi uwe na ripoti ya mwisho ya fedha zilizotumika kwenye mradi ule kwasababu hata ripoti hiyo ingekuwepo isingeweza kuondoa makadirio ya gharama zilizokadiwa na mkadiriaji wa majengo wa mradi huo.

“Mahakama inasisitiza haikubaliani na hoja hiyo ya upande wa mashitaka kwasababu katika kesi hiyo hasara iliyodaiwa amepata mwajiri wa mshitakiwa ni lazima ithibitishwe kwa namba na ripoti…sasa katika kesi hii hasara iliyopatikana haiwezi kuwa sawa na namba ya ripoti ya Mkadiriaji wa Majengo kwani majengo ya nyongeza yamejengwa …labda ingekuwa majengo hayo mengine yanayodaiwa kujengwa nje ya mkataba wa awali na fedha hazionekana hilo lingekuwa ni jambo jingine.

“Na upande wa mashitaka wenywe kupitia mawakili wake ukiri mbele yetu kwamba makadirio ya awali yaliyapaswa kujengwa magorofa 14 lakini baada ya mabadiliko ya ongezeko la ujenzi ziliongezeka ghorofa tatu nyingine juu hivyo kufanya kuwa na majengo mawili na kila jingo lina ghorofa 17 kwenda juu na kweli majengo yamejengwa …na kwa maelezo hayo mahakama hii inamfutia mshitakiwa shitaka la pili kwa mujibu wa kifungu cha 230 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 an na akaueleza upande wa mashitaka upo huru kukata rufaa kama haujalidhika na uamuzi huo.‘alisema Mkasimongwa na kusababisha ndugu na jamaa wa mshitakiwa wakisika kwa sauti wakisema, ‘Asante Yesu.’”

Baada ya hakimu huyo kumaliza hukumu hiyo wakili wa utetezi Majura Magafu, Onesmo Kyauke, Hudson Ndusyepo na Jaji Mstaafu Hillary Mkate pamoja na wakili wa serikali Prosper Mwangamila na Ben Lincoln na Tabu Mzee walisema hawana pingamizi na uamuzi huo.

Wakili Magafu alidai kuwa mahakama hiyo imefuta shtaka hilo ambali linaangukia kifungu cha 148(5)(e)cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambayo ndiyo iliyotumika kumpatia dhamana awali mshitakiwa na ilimtaka atoe fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya sh bilioni 110 na mshitakiwa alishindwa kutimiza masharti hayo, hivyo akaomba mahakama itoe masharti mapya ya dhamana yanayoendana na shitaka la kwanza ambalo ni la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma ambalo aliangukii kwenye matakwa ya kifungu hicho.

Alipotakiwa na mahakama hiyo aseme chochote kuhusu ombi hilo lilowasilisha na utetezi, wakili wa seriakali Mwangamila alisema hawana pingamizi na ombi hilo ila aliomba mahakama itoe masharti ya dhamana yatakayofanya mshitakiwa aweze kufika mahakamani.

Akisoma uamuzi uamuzi wa ombi hilo la kutaka jopo hilo litoe masharti mapya ya dhamana kwa mashitakiwa huyo Hakimu Mkazi Lameck Mlacha kwaniaba ya jopo alisema wamepata wasaa wakupitia uamuzi dhamana uliotolewa na Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ,Geofrey Shahidi mwaka jana, alisema jopo limejikuta halipo tayari kukubaliana maombi ya pande hizo hizo mbili kwasababu mahakama ya Hakimu Mkazi haina mamlaka ya kutengua uamuzi huo wa mahakama kuu ambao ulimpatia masharti ya dhamana mshitakiwa huyo chini ya kifungu cha 148(5)(e) cha Sheria ya Makosa ya Jinai, ila kama mshitakiwa anataka kupewa dhamana basi aende kuomba Mahakama Kuu.

“Jopo hili limeona busara kesi hiyo imefikia uamuzi wa juu sana kwa hiyo si vyema leo tuendelee kuzungumzia maombi ya dhamana ya mshitakiwa hivyo tunaona ni vyema kesi hii ikaendelea kusikilizwa,” alisema Hakimu Mkazi Mlacha na kusababisha ndugu wa mshitakiwa na kuyeyusha matumaini ya ndugu yao angepata dhamana.

Aidha Magafu aliomba amri zilizokwisha tolewa na mahakama zibaki kama zilivyo na akasema ni mapema wao kueleza kwamba wataka rufaa mahakama kuu na kuongeza kuwa mshitakiwa wake atatoa ushahidi wake kwa kiapo na anakusudia kuleta mashahidi sita na vilelezo ila kwana hakuwa katika nafasi nzuri ya kuweza kutaja orodha ya mashahidi hao na kuomba apewe wiki moja ili aweze kuleta orodha hiyo ya mashahidi.

Hakimu Mkazi Edson Mkasimongwa aliamuru upande wa utetezi April 16 mwaka huu, upande wa utetezi ulete orodha ya mashahidi wake mahakamani na iwapatie orodha hiyo upande wa mashitaka na kisha anairisha kesi hiyo hadi April 22 na 23 mwaka huu, ambapo Liyumba atajitetea na mashahidi wake watatoa ushahidi.

Hata hivyo saa tisa Alasiri jana wakili wa Liyumba, Onesmo Kyauke aliwasilisha barua katika uongozi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ili iweze kuwapatia nakala ya mwenendo wa uamuzi ulitolewa na jopo hilo jana ili waweze kupitia kwa kina uamuzi huo na kisha wajue nini cha kufanya.

Januari 27, mwaka jana, Liyumba na Meneja Mradi wa Benki Kuu, Deogratius Kweka, walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza na kusomewa mashitaka hayo ya kuidhinisha mradi wa majengo ya minara pacha bila idhini ya bodi ya wakurugenzi na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.

Mei 27 mwaka jana, mahakama hiyo iliwafutia kesi, lakini muda mfupi baada ya kuachiliwa walikamatwa tena mahakamani hapo na Mei 28 mwaka jana, Liyumba peke yake ndiye aliyerudishwa mahakamani hapo na kusomewa mashitaka hayo na Kweka akawa ameachiliwa huru. Tangu kipindi hicho hadi sasa Liyumba anaendelea kusota rumande, baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana, ambapo mahakama ilimtaka atoe fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya sh bilioni 11.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, April 10 mwaka 2010

MGOMBEA BADO ALITESA TAIFA

*MJADALA WAKE WATAWALA NEC YA CCM,MAHAKAMA YA RUFAA

Na Happiness Katabazi

SUALA la mgombea binafsi limeendelea kuwa tete, na juzi lilizua mjadala mkali katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM); na jana lilizua ubishi wa kisheria katika Mahakama ya Rufaa kwa siku ya pili mfululizo.


Habari kutoka ndani ya kikao cha NEC, zinasema juzi suala la mgombea binafsi lilileta ubishi mkubwa, huku wajumbe wengi wakisisitiza kwamba serikali lazima ifanye lolote inaloweza kulizima kabisa, ili mgombea binafsi asiruhusiwe, kwa maelezo kuwa akiruhusiwa atakuwa mwiba mkali kwa chama.

Hata hivyo, wajumbe wawili vigogo, John Malecela na Samuel Sitta waliwasihi wajumbe walegeze msimamo kwa maelezo kuwa nyakati zimebadilika, na kwamba hata wakikataa, mahakama inaweza kutoa uamuzi wasioupenda.

Kwa mujibu wa habari hizo, hatimaye wajumbe walikubaliana kwamba hatima ya suala hili ibaki mahakamani, na kwamba mahakama ikishatoa uamuzi, uheshimiwe.

Jana, mvutano wa kisheria uliendelea katika Mahakama ya Rufaa, miongoni mwa magwiji wa sheria, ambao waliitwa kutoa maoni yao kama marafiki wa mahakama kuhusu hukumu ya Mahakama Kuu iliyoruhusu mgombea binafsi nchini, mwaka jana. Magwiji hao ni wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Palamagamba Kabudi na Profesa Jwani Mwaikusa, wakishirikiana na Mkurugenzi wa Mashitaka wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (DDP), Othman Masoud.

Walikuwa wanaishauri Mahakama ya Rufaa kabla haijatoa hukumu ya rufaa iliyofunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka jana kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyoruhusu mgombea binafsi, katika kesi ya msingi iliyofunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila.

Profesa Mwaikusa alieleza jopo la majaji saba wanaosikiliza kesi hiyo kwamba lile ni suala la haki za binadamu, na kwamba mahakama, kwa mamlaka yake, haina kikomo cha kujadili haki hiyo.

Alisema Katiba ya nchi ipo kwa ajili ya kulinda haki za binadamu na kwa msingi huo haki za binadamu ni mama wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977; na kuongeza kuwa kama kuna kifungu kinavunja haki za binadamu basi kifungu hicho ni wazi kinakiuka haki za binadamu kwa sababu haki za binadamu zilianza, Katiba ikafuata.
“Kwa uamuzi ule wa Mahakama Kuu wa kubatilisha vifungu vya ibara 21(1) (c), 39(1) (c) (b) na 69(1) (b) za Katiba ya nchi, kama kuna ibara zinapingana, ibara inayopaswa kutumika ni ile inayolinda haki za binadamu.”

Kuhusu Mahakama Kuu kama ilikuwa na uwezo au la, alisema:

“Mimi nasema ilikuwa na uwezo wa kutamka ibara hizo ni batili kwani Katiba inalinda haki za binadamu na haki hizo za binadamu zilianza Katiba ikafuata hivyo haki hizo ni sheria mama.”

Jopo la majaji hao wa Mahakama ya Rufaa linaongozwa na Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani, likiwashirikisha pia Jaji Januari Msofe na Eusebio Munuo, Natalia Kimaro, Mbarouk Mbarouk, Sauda Mjasiri na Bernard Ruhanda.

Kwa upande wake, Profesa Kabudi alisema mahakama haikumuita mahakamani hapo aseme mgombea binafsi awepo au asiwepo.

“Ila iliniita niwasaidie kujibu kisheria na kikatiba kama ndani ya Katiba kuna ibara inapingana na ibara nyingine mahakama ina inauwezo wa kutamka ibara hizo ni batili.…Jibu langu ni rahisi sana mahakama za Tanzania hairuhusiwi kutamka ibara au kifungu cha sheria kinavunja kifungu kingine isipokuwa pale tu Katiba yenyewe iruhusu mahakama ama wazi wazi au kimkandomkando,” alisema Profesa Kabudi.

Alitoa mifano ya maamuzi yaliyotolewa kwenye kesi mbalimbali katika nchi ya Afrika Kusini, alisema katika nchini nyingine, katiba zinazipa mamlaka mahakama zao uwezo wa kutamka kifungu au ibara moja inavunja ibara nyingine, kwahiyo panapotokea mgongano wa ibara kama ilivyotokea katika kesi ya mgombea binafsi iliyofunguliwa na Mtikila ni kazi ya mahakama kusoma vifungu vya sheria na ibara za katiba kwa pamoja, na kisha kutafuta uwiano, na si kutengua au kuzivunja ibara hizo.
“Ni haki ya kila mwananchi kwenda mahakamani kudai haki, akinyimwa au kupewa ni uamuzi wa mahakama. Hivyo, Mtikila alikuwa sahihi kwenda mahakamani kufungua kesi hiyo, na jukumu la kusema haki yake ilivunjwa au la ni la mahakama,” alisema Profesa Kabudi.
Naye DPP wa Zanzibar, Othuman Masoud, alisema kuruhusu mgombea binafsi kutaondoa haki nyingine, mfano za haki ya wanawake kuruhusiwa kushiriki kwenye ngazi za maamuzi kama ilivyotamkwa kwenye ibara 66(b) ya Katiba na kuongeza kuwa Katiba imeweka utaratibu wa jinsi vyama vya siasa vitakavyofanya kazi yake, lakini haijasema kama endapo mgombea binafsi ataruhusiwa atafuata utaratibu upi.

Jaji Mkuu Ramadhani baada ya kusikiliza ushauri wa wanataaluma hao wa sheria, alisema anaahirisha usikilizaji wa rufaa hiyo, na kwamba mahakama itatoa tarehe ya siku ya kutoa hukumu hiyo. Rufaa hiyo ilianza kusikilizwa jana na kuhudhuriwa na umati mkubwa watu wa kada mbalimbali.

Juzi Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, wakati akiwasilisha hoja zake, alidai kwamba hapa nchini hakuna mahakama yenye mamlaka ya kutengua ibara za katiba, akaiomba mahakama hiyo itengue hukumu ya Mahakama Kuu. Mawakili wa Mjibu Rufaa, Richard Rweyongeza na Mpare Mpoki, walisisitiza kwamba hukumu ya mahakama kuu ilikuwa sahihi, wakaiomba Mahakama ya Rufaa itupilie mbali rufaa hiyo .

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Aprili 10 mwaka 2010

KARATA YA MWISHO BABU SEYA

Na Happiness Katabazi

MWANAMUZIKI mahiri wa muziki wa dansi nchini Nguza Vikings “Babu Seya na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha” jana walirusha karata yao ya mwisho katika Mahakama ya Rufaa Tanzania wakiomba mahakama hiyo ipitie upya hukumu iliyotolewa mahakama hiyo ambayo ilisisitiza kwamba warufani hao waendelee kutumikia kifungo cha maisha jela.


Ombi hilo liliwasilishwa jana na mawakili wa warufani hao Mabere Marando na Gabiel Mnyere na kwa mujibu wa nakala ya ombi hilo warufani wanaomba mahakama hiyo ya rufaa ipitie upya hukumu iliyotolewa Februali mwaka huu na majaji wa tatu wa mahakama hiyo kwani walipitiwa kisheria kutoa hukumu ile.

“Wanaamini mahakama hii ikipitia upya hukumu iliyotolewa na majaji wa mahakama hiyo watabaini mapungufu yaliyofanywa na majaji wale watatu na kisha watafutia adhabu ya kifungo cha maisha washitakiwa hao”alisema Marando.

Babu Seya na mwanawake wanatumikia kifungo cha maisha jela baada ya mahakama ya Hakimu MKazi Kisutu, Mahakama Kuu na Mahakama hiyo ya rufaa kuwakuta na hatia ya kubaka watoto wa shule.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi,Aprili 10 mwaka 2010

MAJAJI WAITOA JASHO SERIKALI KORTINI DAR

.RUFAA YA MGOMBEA BINAFSI

Na Happiness Katabazi

NAIBU Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, amedai kuwa hakuna mahakama yoyote nchini ambayo inaweza kusikiliza kesi ya kutaka kuwepo kwa mgombea binafsi.


Masaju ambaye anasimama kwa niaba ya serikali, alitoa dai hilo jana mbele ya jopo la majaji saba wa Mahakama ya Rufaa nchini lililokuwa likiongozwa na Jaji Mkuu, Augustino Ramadhani, aliyekuwa akisaidiwa na majaji Januari Msofe na Eusebio Munuo.

Majaji wengine wanaosikiliza rufaa hiyo ambayo kesi ya msingi ilifunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila ni Nataria Kimaro, Mbarouk Mbarouk, Sauda Mjasiri na Bernad Ruhanda waliokuwapo wakati mwanasheria huyo akiwasilisha hoja zake za kupinga hukumu ya Mahakama Kuu.

Akiwasilisha hoja zake mbele ya jopo hilo, ambalo jana lilianza kusikiliza rufaa ya kupinga kuwepo mgombea binafsi nchini na huku akitumia kesi mbalimbali zilizotolewa na Mahakama Kuu ya India, Kenya na Malawi na huku akikabwa na maswali ya mara kwa mara toka kwa jopo hilo yaliyokuwa yakimlazimisha atoe hoja zake kwa vielelezo na si vinginevyo. Masaju alidai, Mahakama Kuu ilikosea katika hukumu yake kwa sababu hapa nchini hakuna mamlaka yenye uwezo wa kusikiliza kesi hiyo isipokuwa majukwaa mbalimbali (forums).

Masaju alidai sababu nyingine ya wao kupinga hukumu hiyo, ni kwamba Mahakama Kuu ilijipachika mamlaka ya kibunge ya kutunga sheria.

Mbali ya hilo, Masaju alidai pia kuwa katika hukumu yake Mahakama Kuu ilikosea kisheria kwa kuiweka Katiba ya nchi katika vyombo vya kimataifa na pia ilikosea kuitolea maamuzi kesi hiyo bila kuweka suala hilo bayana, hivyo akaiomba mahakama hiyo ya rufani kutengua hukumu hiyo kwa gharama.

Hata hivyo, majaji hao kwa nyakati tofauti walimkatisha Masaju kuwasilisha hoja zake na kumkumbusha kwamba madai yake kuwa Mahakama Kuu ilikosea kutumia sheria za kimataifa zinazohusu haki za binadamu yalikuwa yakiacha maswali.

“Lakini mbona wewe wakati unawasilisha hoja zako na ulikuwa unatumia kesi za India, Malawi ili zikusaidie kuunga mkono hoja zako na kwa maana hiyo nawe unapofanya hivyo unakosea?

“… Hizo hukumu zilizotolewa na Mahakama ya India na Malawi uliyoitumia na unaomba mahakama iitumie kufikia maamuzi yake umeisoma yote na tumekusikiliza sana ukisema hapa nchini hakuna mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hii ikiwemo hata Mahakama ya Rufaa ambayo miongoni mwa majaji wake ni sisi ambao ndiyo tunaisikiliza rufaa hiyo lakini umeshindwa kabisa kutueleza ni mahakama ipi inastahili kusikiliza kesi hii na kama unasema hakuna mahakama ya kusikiliza kesi hii mbona Mwanasheria Mkuu amekata rufaa katika Mahakama ya Rufaa?” walihoji majaji hao.

Maswali hayo yalisababisha umati wa watu waliohudhuria katika Ukumbi Namba Moja wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kuangua vicheko na Naibu Mwanasheria Mkuu huyo kukaa kimya na kuishia kujifuta jasho mara kwa mara tangu alipoanza kuwasilisha hoja zake saa 3:00 asubuhi hadi saa 6:30.

“Umedai huridhiki na hukumu ya Mahakama Kuu kwa sababu ilitumia sheria za vyombo vya kimataifa, sasa sisi tunakutaka uisome Ibara 9 (f), 30 (3) (5) 108 (1) za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, usome kwa sauti zinasemaje;

“Ibara ya 9(f) inasema kwamba ‘heshima ya binadamu inahifadhiwa na kudumishwa kwa kufuata Kanuni za Tangazo la Dunia kuhusu haki za Binadamu. Ibara 30 (3) inasema; “mtu yeyote anayedai kuwa sharti lolote katika Sehemu hii ya Sura hii au katika sheria yoyote inayohusu haki yake au wajibu kwake, limevunjwa, linavunjwa au inaelekea litavunjwa na mtu yeyote popote katika Jamhuri ya Muungano, anaweza kufungua shauri katika Mahakama Kuu.

“Na ibara 30 (5) inasema; ‘Endapo katika shauri lolote inadaiwa kwamba sheria yoyote iliyotungwa au hatua iliyochukuliwa na serikali au mamlaka nyingine inafuta au inakatiza haki, uhuru na wajibu muhimu zitokanazo na ibara ya 12 hadi 29 za Katiba ya Nchi hii, na Mahakama Kuu inaridhika kwamba sheria au hatua inayohusika, kwa kiwango inachopingana na Katiba ni batili au kinyume cha Katiba basi Mahakama Kuu ikiona kuwa yafaa au hali au masilahi ya jamii yahitaji hivyo, badala ya kutamka kuwa sheria au hatua hiyo ni batili, itakuwa na uwezo wa kuamua kutoa fursa kwa ajili ya serikali....” Masaju alinukuu ibara hizo.

Baada ya kumaliza kuzisoma, majaji hao walimuuliza kama bado anaendelea kusimamia hoja zake zinazodai Mahakama Kuu haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi ile na ilikosea kutumia sheria za nje katika hukumu ile wakati Ibara ya 9(f) ya Katiba ya nchini inatamka wazi kwamba Tanzania imeridhia utekelezaji wa Tangazo la Dunia kuhusu haki za Binadamu na kwamba ibara ya 30(3)(5) zinaainisha wazi Mahakama Kuu ina mamlaka hayo ya kusikiliza kesi hiyo na kutamka sheria ni batili kwa mujibu wa Kanuni na Tamko la Haki za Binadamu?

“Mmmh! Mbona nimeishasema sana hapa kwamba Mahakama Kuu na hata hiyo Mahakama Rufaa haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, Tanzania ni taifa hivyo lina sheria zake kwa hiyo kitendo cha Mahakama Kuu kutumia sheria za nje katika hukumu ile ni kuvunja Katiba ya nchi na walikiuka viapo vyao walivyoapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo wakati wanaapa waliahidi kuhifadhi Katiba ya nchi,” aliendelea kudai Masaju na kusababisha watu kuangua vicheko vya chinichini.

Majibu hayo ya Masaju yalisababisha Jaji Mkuu amtake aendelee kurudia matamshi yake kwa kusema wao ni wagumu kuelewa hivyo aendelee kurudiarudia ili wamuelewe, hatua ambayo ilisababisha vicheko tena ndani ya chumba cha mahakama.

Masaju aliendelea kudai kwamba majaji watatu wa Mahakama Kuu ambao walitoa hukumu ile Salum Massati (sasa Jaji wa Mahakama ya Rufani), Jaji mstaafu Amir Manento na Thomas Mihayo (mstaafu) walivunja Katiba na kuongeza kuwa anashangazwa na kuhumu ile na akaifananisha na hukumu zinazotolewa na mahakimu.

Hakuishia hapo alikwenda mbele zaidi na kudai kuwa hukumu ya majaji hao watatu ni yao na si ya Watanzania wote kwani miaka ya nyuma yalishakusanywa maoni ya kutaka uwepo wa mgombea binafsi lakini asimilia 92 ya wananchi walikataa.

Maelezo hayo ya Masaju yalisababisha Jaji Mkuu Ramadhani alazimike kutumia mfano wa maoni ya asilimia 80 ya wananchi waliotaka mfumo wa chama kimoja uendelee mbele ya Tume ya Jaji Francis Nyalali, jambo ambalo hata hivyo lilipingwa na serikali na kusababisha kuanza kutumika kwa mfumo wa vyama vingi.

Kutokana na maelezo hayo, Jaji Mkuu alisema hoja ya Masaju kuhusu maoni ya wananchi walio wengi kukataa mgombea binafsi haina msingi katika rufaa hiyo.

Wakipangua hoja za Masaju, mawakili wa mjibu rufaa, Richard Rweyongeza na Mpare Mpoki, walianza kwa kuiomba Mahakama ya Rufani itupiliwe mbali rufaa hiyo kwa gharama.

Wakifafanua walidai, hoja kwamba, Mahakama Kuu ilitumia sheria za nje siyo ya msingi kwa sababu Ibara ya 9(f) ya Katiba ya nchi inaitaka itumie sheria hizo hivyo ibara hiyo haikuwekwa kwenye Katiba kama pambo bali iliwekwa ili itumike kikamilifu na kwamba Mahakama Kuu ilitoa hukumu sahihi.

Akiichambua hoja kwamba Mahakama Kuu ilijipachika jukumu la kibunge la kutunga sheria, Rweyongeza na Mpoki ambao walikuwa wakiwasilisha hoja zao kwa vielelezo, walisema hoja hiyo haina msingi kwani Mahakama Kuu imepewa mamlaka chini ya Ibara 30 (5) ya Katiba na katika hukumu ile Mahakama Kuu haikutunga sheria, ila ilielekeza hitilafu iliyoiona katika Ibara 21 (1) (c), 39 (1) (c) (b) na 69 (1) (b) ya Katiba ya nchi na ilitoa muda ibara hizo zirekebishwe.

“Hivyo dai kwamba Mahakama Kuu ilijipachika jukumu la kibunge na kutunga sheria si la msingi ...ila tunakubali Bunge lina mamlaka ya kutunga sheria zinazofaa kama ilivyoainishwa kwenye Ibara ya 28 (2) ya Katiba, lakini Bunge halina mamlaka ya kubadilisha misingi ya Katiba lakini kitendo cha Bunge kuweka ibara ya 21 (1) (c), 39 (1) (C) katika Katiba ya nchi limevunja misingi ya Katiba hivyo Bunge ndilo lilivunja Katiba na siyo Mahakama Kuu.

“Ni rai yetu kwa hayo niliyoyaeleza hapo juu kumbe Mahakama Kuu ina mamlaka pindi inapoona kifungu fulani cha sheria kinapingana na Katiba kifanye nini? Kumbe uamuzi uliofikiwa na Mahakama Kuu ulikuwa ni kitu kizuri kwani ilifikia hukumu ile ya kuwepo kwa mgombea binafsi kwa sababu ilichokifanya kipo ndani ya ibara ya 30 (5) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alidai Rweyongeza.

Baada ya pande zote mbili kumaliza kuwalisha hoja hizo, Jaji Mkuu aliahirisha kesi hiyo hadi leo ambapo marafiki wa mahakama akiwemo Mkuu wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Paramagamba Kabudi na Profesa Jwani Mwaikusa, watatoa maoni ya kuishauri mahakama kuhusu rufaa hiyo.

Mara ya kwanza, serikali ilikata rufaa dhidi ya hukumu ya Mahakama Kuu, katika mahakama hiyo ya rufaa mwaka 2007, ambapo ilidai mahakama hiyo ya chini ilikosea kisheria kutafsiri Ibara ya 21(1)(c), 39(1)(c) (b) na 69(1)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977.

Hata hivyo, rufaa hiyo ilitupwa na Mahakama ya Rufaa baada ya mahakama hiyo kukubaliana na ombi la wakili wa Mtikila, Richard Rweyongeza, kwamba rufaa hiyo haina msingi na kwamba imejaa dosari za kisheria.

Awali katika hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa Mei 2006, iliruhusu kuwepo kwa mgombea binafsi katika uchaguzi, kwa sababu Katiba ya nchi inatoa haki hiyo.

Mwaka 1993, Mtikila alishinda kesi kama hiyo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma iliyokuwa ikisikilizwa na Jaji Kahwa Lugakingira, lakini licha ya uamuzi huo, serikali ilipeleka bungeni muswada wa kupinga hukumu hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Aprili 9 mwaka 2010

KWA HERI KAMANDA KONGA,TUTAKUKUMBUKA DAIMA


Na Happiness Katabazi

APRILI 5 mwaka huu, saa 10:12 jioni nikiwa ofisi nilipokuwa katika chumba chetu cha habari nilipokea simu toka kwa mama yangu mzazi Oliva Katabazi ikiniarifu kwamba kaka yangu Aristariko Konga (49) amefariki dunia.

Na akaniambia hanitanii kwamba taarifa hizo ni za kweli na yeye amepigiwa simu na mke wa marehemu, Aniwiye Konga ambaye ndiye alikuwa akimuuguza katika Hospitali Kuu ya Jeshi la Wananchi Lugalo Dar es Salaam kwa takribani wiki tatu sasa.

Baada ya kupokea taarifa hizo za kusikitisha,nilijikuta nikipaza sauti kwa uchungu ndani ya chumba chetu habari cha gazeti hili kwamba ‘Konga amefariki’ na waandishi wenzangu waliokuwepo ofisi Kulwa Karedia, Betty Kangonga,Martin Malela na Meneja Uhusiano wa Benki ya NMB Shy-Rose Banji ambaye siku hiyo ya Jumatatu ya Pasaka, alifika ofisini kwetu kikazi walinizunguka kwa simanzi na mkuu wangu wa kazi Kulwa Karedia aliniambia pamoja na kupokea simu hiyo alinitaka niandike habari ya kifo cha mwandishi huyo mkongwe.

Nami nilifanya hivyo nilikaa kwenye Kompyuta nakuanza kuandika habari huku nikilengwa na machozi ila kwasababu nisizozifahamu habari hiyo iliyotakiwa itoke kwenye gazeti Tanzania Daima la jana, haikutoka.

Mara ya mwisho mimi kuzungumza kwa simu na Konga ilikuwa ni siku ya Sikuu ya Pasaka April 4 mwaka huu, ambapo niliipiga simu yake akapokea mke wake nikasalimiana nae akaniambia kaka yangu Konga hali yake imebadilika hata kuzungumza sauti haitoki vizuri lakini akaniambia ngoja ajaribu kumpa simu ndipo nikazungumza naye huku sauti yake nikiisikia kwa taabu akaniambia kwamba hajisikii vizuri hata kuzungumza anazungumza kwa tabu namini nikamtakia Pasaka njema na kumuadi kesho yake ambayo ndiyo siku aliyokufa ningeenda tena kumuona.Uzuni Konga amekwenda.

Kisha nikatuma ujumbe mfupi kwa ofisa mwandamizi mmoja toka ofisi moja nyeti serikalini na kumueleza hali ya Konga siyo nzuri naye akasema kesho yake angeenda kumuuona na kweli ofisa huyo wa serikali Jumatatu ya Pasaka majira ya saa sita mchana alikwenda kumuona Konga wodini na alipomaliza kumuona aliniarifu Konga hazungumzi tena na hali yake ni mbaya kilichobaki tumuombee kwa mungu.Nilisikitika sana.

Huyu mtumishi wa serikali (jina na mhifadhi) ndiye alikuwa mtu wa kwanza kabisa mwanzoni mwa Februali mwaka huu, kunitumia ujumbe mfupi kuniarifu kwamba alikuwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,kikazi akamkuta mwandishi mmoja wa gazeti la Mwanahalisi yaani Konga anaumwa vibaya na akanitaka nipeleleze afya yake inaendeleaje.

Mimi nilimjibu Konga namfahamu ni kaka yangu kiumri na amenitangulia kwenye fani hii ya Uandishi wa Habari,nilichokifanya Februali mwaka huu, nikawa nampigia mara kwa mara simu mhariri wa Michezo wa Gazeti la Mwanahalisi Alfred Lucas kumuuliza kama Konga anaumwa na alinijibu ni kweli anaumwa na kwamba yeye amekuwa akiagizwa mara kwa mara na uongozi wa ofisi yake kwenda kumjulia hali nyumbani kwa Konga na kumjulia hali pamoja na kutoa msaada uliokuwa ukiitajika.

Nakumbuka Lucas alieleza kwamba Konga ni mgonjwa na nikamtaka Alfred anipatie namba ya simu ya Konga, alifanya hivyo alinipatia nami kwa zaidi ya wiki tatu nikiipiga namba ile ya mtandao wa Tigo, simu ile ikawa haipatikani mwisho nikamweleza Alfred mbona ile simu uliyonipatia haipatikani, akanieleza amesikia kwamba Konga amebadili simu amekuwa na mtandao wa Vodacome ila namba hiyo anayo Mhariri Mtendaji wa Magazeti ya Mseto na Mwanahalisi Saed Kubenea akaniaidi kumwomba anipatie.

Nilisubiri bila mafanikio, nikaamua kumpatia maendeleo ya nilipofikia yule ofisa mwandamizi wa serikali na kumweleza kwamba namba ya Konga nimeshindwa kuipata akanijibu kupitia ujumbe mfupi, ‘sawa’.

Kesho yake yaani Machi 18 mwaka huu, ofisa yule wa serikali aliangaika na akaakikisha anaipata namba hiyo ya Konga na akanitumia na akasema anachokitaka kwangu ni kuakisha Konga anatibiwa na anatolewa ndani ya nyumba kwa nguvu na anaopelekewa Hospitali akatibiwe kwani kwa uchunguzi alioufanya na amejiridhisha kwamba Konga halikuwa haendi hospitali kupata matibabu.

Baada ya hapo nilimpigia simu Konga akapokea nikajitambulisha kwake akafurahi sana nikamueleza kwamba nimesikia kwamba anaumwa, akanijibu ni kweli nikamuuliza anatibiwa hopsitali gani akaniambia anatibiwa hospitali ya Mikocheni kwa Dk.Kairuki ,kwakuwa nilikuwa najua ananidanganya hatibiwi kokote, nikamweleza kwanini asiende kutibiwa katika hospitali ya Lugalo, akanijibu hana mtu anayefahamu pale nikamweleza kwamba hospitali ya Lugalo haina urasimu na wananchi wa kada zote wanaruhusiwa kutibiwa pale na kama yupo tayari aseme kesho mke wake ampeleke pale hospitali.

Konga ambaye ni mwandishi wa habari mkongwe na mchambuzi wa masuala ya siasa ,jamii na utawala, alinijibu kwa unyenyekevu, atashukuru sana kama nitafanya hivyo na nikamwambia kesho yake saa kumi usiku ya siku ya Ijumaa Machi 19 mwaka huu,nilimpigia simu Konga ili kuakikisha je ni kweli atakwenda Lugalo siku hiyo kutibiwa, lakini simu ilipokelewa na mkewe namini nikajitambulisha akasema mumewe alikuwa amemweleza jana yake na mkewe akasema ndiyo anaenda kutafuta gari la kukodi ili ampeleke Lugalo na kunieleza kwamba usiku kucha hawakulala kwasababu alizidiwa sana.

Baada ya mkewe kuniakikishia kwamba wangekwenda Lugalo, saa kumi mbili kasorobo asubuhi ya siku hiyo nilimpigia Kubenea na Alfred kwa bahati mbaya simu zao zilikuwa zimezimwa.Ndipo muda huo nikaamua kumpigia simu Mshauri wa habari wa gazeti la Mwanahalisi ambaye pia ni mwandishi wa habari mkongwe nchini Ndimara Tigambwage kuwaeleza nilivyofanya jitihada zangu hizo.

Ndimara akaniunga mkono na kusema hilo ni la msingi ni vyema Konga akafie hospitali na siyo nyumbani ila akasema yeye hana mamlaka ya utawala katika Mwanahalisi ila akanisii sana nisubiri kupambazuke uenda simu ya Alfed na Kubenea zitakuwa zimewashwa na atawaeleza yote ili uongozi wa kampuni huo une unaweza kusaidia nini.

Lakini ilipofika saa mbili asubuhi ya siku hiyo mkewe alinipigia simu akinieleza kwamba Konga amekataa kutoka ndani na amesema hataki kupelekwa hospitali nikamweleza mke wake akaa atulie pale nyumbani kwake, nitampa jibu baada ya muda mchache.Ndipo Ndimara alinipigia simu akinieleza kwamba ameishazungumza na Kubenea na kwamba Kubenea ametoa maelekezo kwa Mhariri wake Alfred Lucas kuhusu kumsaidia .Uzuni Konga amekwenda.

Na nikamweleza Ndimara licha amenieleza hayo lakini mkewe amenipigia simu akiniambia kwamba mumewe hataki kwenda hospitali na ndipo nilipomueleza tena Ndimara kwamba amueleze Alfred Lucas akifika nyumbani kwa Konga pale Ubungo Kibo asifanye majadiliano naye ambambe amtumbukize kwenye gari na kisha ampeleke Lugalo akatibiwe.Uzuni Konga amekwenda.

Ilipofika majira ya saa tatu asubuhi ya siku hiyo tena , Alfred alinipigia na kuniambia tayari wameishamwingiza kwa nguvu Konga kwenye gari na wapo njiani wanaelekea kuelekea Lugalo ila hali ya Konga ni mbaya sana.

Siku hiyo walipofika Lugalo pale mapokezi baahati nzuri walipokelewa na ofisa wa JWTZ mwenye cheo cha Kepteni ambaye Dk.Hashim Thabit ambaye alimpatia matibabu ya awali na kumuandikia alazwe na alienda kulazwa wodi Na.11 na baadaye akaamishiwa wodi 11C ambapo alilazwa hapo hadi umauti ulipomkuta juzi.

Kufikia kwa hatua hiyo tena nilitumua ujumbe mfupi kwa yule ofisa wa serikali na kumweleza kwamba hatimaye Konga ameishafikishwa Lugalo na amelazwa. Na yule ofisa nakumbuka alinijibu kupitia ujumbe mfupi akiniambia yafuatayo:

“Nashukuru sana.Wapo watu wanaogopa sana hospitali hata kuwatizama wagonjwa wanaogopa.Wewe kweli nimeamini ni mpiganaji .Unaweza uongozi”

Kwa wale tuliopata fursa ya kumtembelea mara kadhaa Konga akiwa wodi, ndani ya siku mbili tangu afikishwe hopitalini pale ambapo alifikishwa akiwa hajifahamu wala hamtambui mtu, alianza kupata nafuu na kuzinduka na kuanza kufahamu watu na kujua kwamba yupo hospitali.

Lakini wakati harakati zote zinafanyika hadi anafishwa hopitalini hapo alikuwa hazitambui na baada ya siku ya tatu kupata fahamu yaani siku ya tatu kupata fahamu Machi 17 mwaka huu, nilikwenda pale wodini na kumwelezea mkanda mzima mbele ya mke wake aliinuka na kunishukuru na kushukuru wote waliofanya jitihada za kumfikisha pale na kusema atatuombea kwa mungu.

Minilimweleza yeye ni binadamu mwenzetu hivyo hakukuwa na maana yoyote kumuacha aendelee kutaabika bila kumpatia msaada uliopo ndani ya uwezo wetu na kwamba yote ni mipango ya mungu.

Kutoka kutojifahamu alipata nafuu anakaanza kula chakula, na kutoka wodi kwenda kukaa kwenye baraza za hospitalini hapo na kuzungumza na watu lakini hali yake ya kiafya ilianza kudorola Ijumaa Kuu ya wiki iliyopita ambapo hata chakula alikuwa hataki kula na ndipo juzi asubuhi ndugu zake walipoamua kumuandaa kiroho na kumletea mchungaji ambaye alimuongoza kusali sara ya toba na hatimaye juzi saa tisa alivyopelekwa bafuni na mkewe kuoga ndipo alipofariki bafuni wakati amekaa kwenye kiti hospitalini hapo.Uzuni Konga amekwenda jamani.

Konga amefariki ameacha watoto wawili na mke mmoja.Amekufa wakati uhuru wa wananchi wa kujieleza na kutoa maoni yao bila kubudhiwa na vyombo vya dola unazidi kukuwa chini ya serikali ya awamu ya nne.

Konga umetutoka wakati bado taifa lilikuwa likitaji mchango wako wa kwa njia ya kalamu katika kuliletea maendeleo taifa letu.Konga umekufa kindi hiki wakati taaluma ya habari imeingiliwa na mdudu rushwa na miongoni mwetu tumegeuka kuwa manyang’au wa kuwa na tamaa ya fedha na mali, tumekuwa na makundi na tumekubali kutumiwa vibaya na wanasiasa,baadhi ya wanabahari wamepakatwa na wanasiasa na matokeo yake wamekuwa wakiandika habari na makala za uchonganishi baina ya wanasiasa ambazo hazileti tija kwa taifa letu.

Konga umekufa wakati nchi yetu Oktoba mwaka huu, inaingia kwenye uchaguzi mkuu ,mchango wako wa makala za siasa ulikuwa ukiitajika sana.Mwili wa marehemu ilitorowa heshima za mwisho jana katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Ubungo-Gide na kuudhuriwa na waandishi wa habari wa kongwe na chipukizi nchini na jioni mwili wake ulisafirishwa kwenda nyumbani kwao wilayani Makete mkoani Iringa kwaajili ya mazishi.Uzuni Konga amekwenda.

Mazuri yaliyofanywa na Konga enzi za uhai wake naahidi nitayaenzi na mabaya yaliyofanywa nae kama binadamu hatutayaenzi.Shukurani za pekee ziwaendee madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Jeshi Ulinzi la Wananchi Lugalo, kwa jitihada zao za kitabu walizozitoa kwa mpendwa wetu Konga ili kuokoa maisha yake hadi siku alipikumbwa na umauti.

Konga ana historia pana kwenye tasnia ya habari hapa nchini lakini hadi umauti ulikuwa mwandishi wa habari wa mwandamizi wa gazeti la Mwanahalisi, lakini amepata mwandishi na Mhariri Mwandamizi wa kampuni zinzozochapisha magazeti ya Mwananchi, Raia Mwema,The Guradian na iliyokuwa Habari Corporation ambayo kwasasa ina tambulika kwa jina la New Habari.

Konga atakumbukwa kwa ujasiri wake katika kusimamia mambo ya msingi kwani wakarti fulani mwanzo mwa mwaka 2000 aliunguliwa nyumba katika mazingira yaliyoacha utata mwingi suala ambalo lilidhaniwa kuwa uunguaji huo ulikuwa ni shambulio la kulipiza kisasi dhidi ya msimamo wa habari na makala alizokuwa akiandika katika masuala kadhaa ya kitaifa.

Sisi tulimpenda Konga lakini Mungu amempenda zaidi.Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.Uzuni Konga amekwenda.

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, April 8 mwaka 2010

KWANINI TUANDALIWE KUHONGA NA KUHONGWA?

Na Happiness Katabazi

SHERIA ya gharama za uchaguzi ya mwaka 2010 iliyosainiwa na Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni si suluhisho la rushwa katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba na chaguzi za miaka mingine ijayo.


Kwanza sheria hiyo imekuja ghafla na kushtukiza. Leo hii ni Aprili ikiwa ni miezi takriban sita kabla taifa halijaingia katika uchaguzi.

Wanachama wa CCM wanaotaka urais, ubunge na udiwani walishaanza kampeni miaka mitatu iliyopita, sheria hii inasaidia nini kudhibiti mamilioni ya fedha yaliyokwishatumika katika kipindi hicho?

Sheria hiyo inataka fedha zipitie kwenye chama cha siasa husika lakini ni ukweli usiopingika kuwa fedha nyingi zimeshapitia au zinapitia katika mikono ya watu binafsi kwa ajili ya kampeni, hizi zitadhibitiwa vipi?

Tatu; sheria hiyo ya gharama za uchaguzi inatamka kiasi cha fedha atakachotumia mgombe urais, ubunge na diwani, vyanzo halali vya fedha hizo viko wapi? Mbona sheria hiyo haitambui wawezaje kupata hizo fedha kutokana na vyanzo halali?

Inataka mgombea udiwani atumie kiasi cha fedha kisichozidi milioni saba lakini haiangalii uwezo wa vyama husika ambavyo kila kukicha vimekuwa vikigalagala kwa njaa isipokuwa CCM.

Vyama visivyokuwa na uwezo vitawezaje kuwapa wagombea ubunge kiasi kisichozidi milioni 50 ili kuwania ubunge? Hapa si tunaendelea kuwaneemesha wabunge wanaolipwa kiinua mgongo kila unapokaribia uchaguzi?

Bila shaka wenye kunufaika zaidi ni wana CCM ambao wana wabunge wengi pamoja na vitega uchumi mbalimbali vilivyojengwa kwa nguvu ya wananchi lakini sasa vinatumika kwa manufaa ya chama.

Kwa mujibu wa sheria hiyo mgombea urais anatakiwa asitumie zaidi ya sh bilioni tano, hapa ni lazima tuweke mazingira mazuri ya kujua usafi na uhalali wa fedha zinazotolewa na mgombea au chama chake ili kufanikisha azma waliyojiwekea.

Je, rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania analipwa kiasi gani? Anao uwezo wa kudunduliza fedha zitakazomsaidia katika kampeni hizo au chama chake kitakuwa tayari kutoa fedha zote hizo?

Ikiwa mgombea hana uwezo au marafiki wa kumchangia fedha za kampeni, je, chama chake kina vyanzo halali vya fedha?

Chama tawala kimekuwa kikihusishwa mara kwa na ukwapuaji wa fedha kwenye mashirika ya umma au zile wanazopewa na wafanyabiashara ambao inadaiwa kuwa hupatiwa misamaha ya kodi kwa biashara wanazozifanya.

Kwa hali ilivyo si kila chama kina mwanya wa kutoa misamaha ya kodi kwa wafanyabaishara au kukatiwa ‘mishiko’ na baadhi ya wawekezaji wanaopora rasilimali za nchi ambao wamekuwa wakipewa kipaumbele kikubwa zaidi kuliko wazawa.

Kumbe hili la chama kuwa chanzo cha fedha za uchaguzi ni mwanya wa rushwa na ufisadi uliovishwa joho la kisheria. Serikali haijakubali kwamba itachangia kwa vyovyote vile gharama za uchaguzi .Hilo ndilo tulilolitazamia liwe lengo kuu la sheria hii.

Kila mgombea akigharamia kwa kiwango fulani na kodi ya wananchi ni halali kumbana asizidishe kiwango fulani kilichowekwa na sheria ya gharama za uchaguzi anapochangisha fedha.

Lengo la sheria kama hii ni kupambana na fedha chafu kuingizwa kwenye mfumo wa uchaguzi wa nchi yetu, jingine ni kuzuia matumuzi mabaya ya kifisadi, kuhonga wapiga kura jambo ambalo litapelekea kuwa na serikali iliyoletwa madarakani kwa rushwa.

Kwa kuwa hayo yote hayakuzingatiwa na sheria, tunaona sasa wagombea wengi wa CCM hususan wa Jimbo la Ubungo ambako mimi ni mkazi wake tunawashuhudia kwa miaka miaka mitatu sasa makada wa chama hicho wakiendelea kuvinjari mitaani na maburungutu ya fedha ambayo hatuyajui wameyapata wapi.

Na mbaya zaidi wala hatuoni Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ikiwashughulikia. Kwa hiyo tuna haki ya kuamini kwamba sheria hii ni danganya toto na kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu utakuwa mchafu, wenye rushwa ya kupindukia kupita uchaguzi wowote uliokwishafanyika hapa nchini. Nawatakia Pasaka Njema.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Aprili 4 mwaka 2010

MKURUGENZI WA EASY FINANCE KORTINI

Na Happiness Katabazi

MMOJA wa wakurugenzi wa Kampuni ya kutoa mikopo nchini ya Easy Finance, Aloycious Gonzaga (43) na mkewe, Magreth Gonzaga (38), jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka manne ya kula njama na kuwasilisha hati ya kiwanja ya kughushi na kisha kujipatia isivyo halali sh milioni 50.


Mbali ya washitakiwa hao ambao ni mke na mume, mshitakiwa mwingine ni Anthony Patrick (25), ambaye ni mshitakiwa wa kwanza.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Salome Mwandu, Mwendesha Mashitaka, Inspekta Emma Nkonya, alidai kuwa washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka manne.

Alidai shitaka la pili ni kughushi, ambapo Desemba 31 mwaka jana katika Kampuni ya uwakili ya Solanus Mhenga hapa jijini walitenda kosa la kula njama kughushi hati ya kibali cha kugawa kiwanja Na. 27005, kitalu 201, Mbezi Beach na kujaribu kuonyesha hati hiyo ni halisi na imetolewa na Msajili wa Ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Inspekta Nkonya alidai shitaka la tatu ni la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ambapo shitaka hili linamhusu mshitakiwa wa kwanza Patrick, kwamba mnamo tarehe na mwaka huo katika Skyline General Business International Ltd kwa makusudi alijipatia sh milioni 50 kutoka kwa Jackson Swai kwa kumuuzia kiwanja hicho kilichopo kitalu Na. 27005 Mbezi Beach, huku akijua hati hiyo ya kiwanja ni ya kughushi.

Alidai shitaka la nne ni la kuwasilisha nyaraka za kughushi, kwamba Patrick akiwa katika ofisi za Skyline General Business International Ltd zilizopo Mtaa wa Livingstone hapa jijini aliwasilisha nyaraka hizo za kughushi kwa lengo la kuonyesha hati hiyo ya kibali cha kugawa kiwanja ni halisi.

Hata hivyo washitakiwa wote walikana mashitaka yote na Hakimu Mkazi Mwandu akitoa masharti ya dhamana, alisema ili mshitakiwa apate dhamana ni lazima awe na wadhamini wawili wa kuaminika na mmoja kati yao awe ni mfanyakazi wa serikali, ambao watasaini bondi ya sh milioni 40 kwa kila mshitakiwa mmoja na walitimiza masharti ya dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 14 mwaka huu.

Wakati huo huo, wafanyakazi watatu wa Benki ya Stanbic, Grace Mushi, Gerald Msegeya na Robi Nyamhanga na mfanyabiashara, Nyakaliro Mauma, walifikishwa mbele ya hakimu huyo wakikabiliwa na mashitaka manne ya kula njama, kughushi na kuibia benki hiyo sh milioni 32.

Inspekta Nkonyi alidai kuwa Juni 2009 katika Benki ya CRDB katika Tawi la Morogoro, mkoani Morogoro walijitambulisha kuwa ni Issa Singano na Michael Sarungi na walifungua akaunti Na. 01J1078287500 kwa jina la Uduzungwa Heritage Ltd huku wakijua wanadanganya.

Alidai shitaka la tatu ni la kughushi Tanzania Interbank Settlement System (TISS) yenye Kumbukumbu Na. IND/TISS/565/09 ya Juni 30, mwaka jana, kuonyesha kwamba TISS ni halisi na imetolewa na Diesel Auto Electric Services Ltd yenye akaunti Na. 01400503589 kwa ajili ya kuipatia fedha Kampuni ya Uduzungwa Heritage Ltd kupitia akaunti Na. 01J1078287500 katika Benki ya CRDB Tawi la Morogoro kwa kuhamisha sh milioni 32 kwenye akaunti hiyo.

Aidha, alidai shitaka la nne ni kwa ajili ya mshitakiwa wa pili, wa tatu na wa nne ambalo ni la kusaidia kutendeka kwa kosa hilo, Juni 2009 katika Benki ya Stanibic Ltd Industrial, wakijua hati TISS ni ya kughushi na wakashindwa kuchukua hatua ya kujiridhisha kwenye mtandao wa kibenki kwamba Kampuni ya Uduzungwa ilikuwa ikiiba fedha za Benki ya Stanbic kupitia akaunti hiyo ya Udizungwa.

Aidha, washitakiwa hao walikana mashitaka yote na hakimu huyo alisema ili mshitakiwa apate dhamana ni lazima wawe na wadhamini wawili, mmoja awe ni mtumishi wa serikali, ambapo wadhamini hao watasaini bondi ya sh milioni 20 kwa kila mshitakiwa na washitakiwa wote walipata dhamana baada ya kutimiza masharti na kesi hiyo itatajwa Aprili 14, mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi,April 1 mwaka 2010

MTUHUMIWA EPA ASHINDWA KUFIKISHWA MAHAKAMANI KWA MARA NYINGINE

Na Happiness Katabazi

KWA mara ya pili sasa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana imejikuta ikishindwa kuendelea kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya wizi wa sh milioni 207 katika Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu kwa sababu mshtakiwa wa tano katika kesi hiyo, Bosco Kimela, ameshindwa kuletwa mahakamani hapo na Jeshi la Magereza kwa sababu zisizojulikana.


Kiongozi wa jopo la mahakimu wakazi, Ignas Kitusi, anayesaidiwa na Eva Nkya na John Utamwa juzi na jana walilazimika kuahirisha kusikilizaji kesi hiyo kwa sababu mshtakiwa huyo ambaye yuko mahabusu ameshindwa kuletwa mahakamani hapo na Jeshi la Magereza licha ya jopo hilo kuandika hati ya kutaka aletwe mahakamani.

Hakimu Mkazi Kitusi alimsikiliza kwa makini Wakili Mwandamizi wa Serikali, Fredrick Manuyanda, aliyesema wao walikuwa tayari kuendelea na kesi hiyo licha ya mshtakiwa huyo kwa mara nyingine kushindwa kuletwa mahakamani hapo.

Katika hilo, hakimu huyo alilazimika kumuita askari mmoja wa Jeshi la Magereza na kumhoji ni kwa nini mshtakiwa huyo hajaletwa mahakamani.

Askari huyo alimjibu kuwa hafahamu ni kwa nini; na wala hati iliyotolewa na mahakama juzi ya kulitaka jeshi hilo limlete mshtakiwa jana hakukabidhiwa yeye.

“Hili tatizo liko juu ya uwezo wetu, yaani mahakama na upande wa mashtaka na utetezi, hivyo kwa mara nyingine naiahirisha kesi hii ambayo ilipangwa kusikilizwa kwa siku nne mfululizo kuanzia juzi hadi Aprili mosi, na ninauamrisha upande wa mashtaka ulete mashahidi wake siku hiyo ya Aprili Mosi,” alisema Utamwa.

Mbali na Bosco ambaye alikuwa katibu wa BoT wengine ni Rajabu Maranda na Farijala Hussein ambao ni wafanyabiashara; maofisa wa BoT ni Iman Mwakosya na Ester Komu ambao wanatetewa na Majura Magafu, Ademba Agomba na Gabrile Mnyele.

Wakati huo huo, upande wa utetezi katika kesi ya wizi wa sh bilioni 3.9 katika akaunti ya EPA inayomkabili mfanyabiashara maarufu nchini Jayantkumar Patel na wenzake watatu jana uliwasilisha ombi la kutaka mahakama hiyo itoe amri ya kusimamisha usikilizaji wa kesi hiyo hadi ombi Na.3/2010 la mapitio ya uamuzi uliotolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Semistocles Kaijage, litakapotolewa uamuzi na Mahakama ya Rufani nchini.

Ombi hilo liliwasilishwa jana na wakili wa utetezi Martin Matunda ambaye alidai upande wa utetezi haujaridhishwa na uamuzi wa Jaji Kaijage ambao alitoa amri ya kurudishwa majarada ya kesi nne zinazowakabili washtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kesi hizo ziendelee kama kawaida kwa sababu amebaini kwamba maombi ya utetezi yanafanana na kesi ya Kikatiba waliyofungua washtakiwa hao dhidi ya Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginard Mengi, DPP na AG.

“Kwa sababu hatujaridhishwa na uamuzi huo wa Jaji Kaijage ndiyo maana tayari tumeishawasilisha ombi katika Mahakama ya Rufani nchini la kutaka mahakama hiyo ipitie upya uamuzi wa Mahakama Kuu na wakati mchakato huo ukiendelea tunaiomba mahakama hii itoe amri ya usikilizwaji wa kesi ya msingi iliyopo mahakamani hapa hadi Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi wake,” alidai Matunda.

Hata hivyo kwa upande wake wakili wa serikali, Manyanda, alidai hakuwa amejiandaa kujibu hoja hizo na akaomba apewe muda lakini hata hivyo wakili Matunda alisema kuwa hoja hiyo haina nia njema kwani Septemba 21 na Septemba 25 mwaka jana, waliwasilisha maombi ya aina hiyo mbele ya mahakimu hao hao na mawakili hao hao wa serikali hivyo haoni sababu ya wakili huyo kutaka apewe muda wa kwenda kutafuta hoja.

Hata hivyo Hakimu Kitusi aliutaka upande wa mashtaka ulete hoja zake Aprili mosi mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Machi 31 mwaka 2010