HAPPINESS KATABAZI AITIMU KOZI YA CHETI CHA SHERIA

Pichani ni Mwandishi Mbobevu wa Habari za Mahakamani nchini, Happiness Katabazi katika mahali yake ya kumaliza Kozi ya Cheti cha Sheria iliyokuwa ikitolewa na Shule ya Sheria Tanzania ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City,Novemba 27 mwaka huu.Mahafali hayo ni mahafali ya 40 ya chuo hicho.
Remove Formatting from selection
Nikiwa na mwanangu kipenzin Queen Mwaijande(Malkia) nyumbani kwetu Sinza 'C',baada ya kurejea kwenye mahafali.
Happiness Katabazi at Mliman City Shop

Baada ya kumalizika mahafali niliingia Mlimani City kupiga picha na kununua bidhaa mbalimbali ikiwemo (Wine)Mvinyo.

Nikiwa na Svea Mchome muda mfupi baada ya kuvalishwa mataji

Nikimvisha taji mhitimu mwenzangu Svea Mchome ambaye ni walikiwa ni miongoni mwa marafiki zangu wa karibu wakati tukisoma kozi hiyo ya cheti cha Sheria, UDSM,ikiwa ni muda mfupi baada ya mahafali kumalizika.
Nikiwa nimekaa chini chini na wahitimu wenzangu tukisubiri kuingia ukumbini kwaajili ya mahafali.

Tabazi na Kumbukumbu

Katabazi akiwa nyuma ya bango hilo lilokuwa linatumiwa na wapiga picha wa kujitegemea nje ya ukumbi wa Mlimani City , siku ya mahafali yake.

JAJI WARIOBA NA MAANDAMANO YA WASOMI


JAJI Joseph Warioba ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandara wakiongoza maandamano ya wanataaluma kuingia katika ukumbi wa Mlimani City, jumamosi iliyopita ambapo siku hiyo ndiyo yalikuwa mahafali ya 40 ya chuo hicho.

KATABAZI-TUMEHITIMU


Happiness Katabazi(Kulia) akifurahia jambo na wahitimu wenzake wa kozi ya cheti cha sheria iliyokuwa ikitotolewa na Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wa katikati ni Zawadi na akifuatiwa na Anna Lyamuya, nje ya ukumbi wa Mlimani City ,Dar es Salaam, Novemba 27 mwaka huu, katika mahafali ya 40 ya chuo hicho yalifanyika ukumbini hapo

ASHA BILAL:'USIMPIGE MWANAMKE PIGA MPIRA'

Mke wa Makamu wa Rais Mama Asha Bilal, akiwa na zawadi ya mpira aliokabidhiwa na waratibu wa maonyesho ya Kazi za Wake wa Mabalozi ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia watu wasiojiweza yaliyoandaliwa na Kikundi cha Wake wa Mabalozi yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Tanganyika International Masaki jijini Dar es Salaam leo Nov 20. Mpira huo ulikuwa na Ujumbe usemao ‘USIMPIGE MWANAMKE PIGA MPIRA’. Picha na Muhidin Sufiani

ASHA BILAL NA UTAMADUNI

Mke wa Makamu wa Rais Mama Asha Bilal, akivishwa beji ya kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa Vistula na mwakilishi wa ‘MABINTI Vistula’, Katia Geurts, kutoka CCBRT, wakati alipoalikwa kufungua rasmi maonyesho ya Kazi za Wake wa Mabalozi yaliyoandaliwa na Kikundi cha Wake wa Mabalozi nchini kwa ajili ya kuchangisha fedha za kuwasaidia watoto na watu wasiojiweza na NGO’s, yaliyofanyika kwenye Viwaanja vya Shule ya Tanganyika International Masaki Jijini Dar es Salaam, Nov 20 mwaka huu. Picha na Muhidin Sufiani

KAMISHNA TRA:MRAMBA HAKUITIA HASARA SERIKALI

Na Happiness Katabazi

NAIBU Kamishna wa Kodi za Ndani wa Mamlaka ya Mapato nchini(TRA), Christine Shekidele(54), katika kesi ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake,amesema kampuni ya Alex Stewart Bussiness Corporation haijailetea serikali hasara.

Mbali na Mramba, ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja.Ambao kesi yao inasikilizwa na Jaji John Utamwa anayesahidiana na Hakimu Mkazi Sam Rumanyika na Saul Kinemela na wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Hurbet Nyange, Elisa Msuya na Profesa Leonard Shahidi na upande wa Jamhuri unawakilishwa na Wakili Kiongozi, Fredrick Manyanda na Ben Lincoln.

Shekidele ambaye ni shahidi 13, alitoa maelezo hayo jana wakati akijibu swali la wakili wa upande wa utetezi, Elisa Msuya alilomtaka aieleze mahakama kwamba endapo kampuni imepewa msamaha wa kutokulipa kodi na serikali kwa kufuata kanuni na sheria za nchi ,je kiasi hicho cha kodi alichosamehewa kitahesabika kuwa ni hasara kwa taifa?

“Kwa mujibu wa sheria za Kodi, pale serikali inapotoa msamaha wa kodi kwa kampuni husika , kile kiwango cha kodi kilichosamehewa katu hakiwezi kuhesabiwa kuwa kimeletea hasara kwa serikali, hivyo kampuni hiyo ya Alex Stewart ambayo Mramba aliidhinisha ipewe msamaha wa kodi na serikali yetu kwa ujumla ikakubali kutoa vibali vya kuisamehe kodi kampuni hiyo kwa kufuata sheria, nasisitiza serikali yetu haikupata hasara kwasababu kampuni hiyo ilisamehewa isilipe kodi.”alisema Shekidele.


Aidha Shekidele akijibu swali la Jaji Utamwa lilomtaka kuieleza mahakama mahakama kwamba juzi alieleza kuwa TRA ilikuwa haina kumbukumbu za ripoti ya fedha ya kampuni hiyo na iweje jana aimbie mahakama hiyo kuwa TRA inayo taarifa za fedha za kampuni hiyo, na ninani mwenye jukumu la kuandaa ripoti ya taarifa za fedha kodi za makampuni pale TRA?

“Mhh! Nikweli Jaji unavyosema lakini …toka mwaka 2004,TRA ilikuwa haina ripoti za fedha za kampuni hiyo lakini ilipofika mwaka 2007, TRA ndiyo ikapata ripoti za fedha za kampuni hiyo na TRA na hizo ripoti za fedha za kampuni hiyo zililetwa TRA na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Dk.Edward Hosea…..lakini hata hivyo mwenye jukumu la kuandaa taarifa za fedha za kodi ni mlipa kodi na msaidizi wake” alieleza Shekidele huku akionekana kubabaika babaika.

Shahidi huyo ni shahidi wa mwisho wa upande wa Jamhuri katika kesi hiyo, ila upande wa utetezi umeiomba mahakama imuite shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri ambaye alishatoa ushahidi wake ili afike tena mahakamani hapo ili upande wa utetezi uweze kumuhoji na mahakama hiyo ilikubali ombi hilo na kuairisha kesi hiyo hadi Desemba 17 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa na Januari 19-20 mwaka 2011 itakuja kwaajili ya kumalizia kusikiliza ushahidi wa shahidi wa kwanza.

Mbali na Mramba washtakiwa wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mipango na Uchumi, Gray Mgonja ambao wanatetewa na mawakili wakujitegemea , Hurtbet Nyange, Elisa Msuya na Professa Leonard Shahidi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Novemba 25 mwaka 2010

KESI YA MRAMBA YASHIKA KASI

Na Happiness Katabazi

NAIBU Kamishna wa Kodi za Ndani wa Mamlaka ya Mapato nchini(TRA), Christine Shekidele(54), katika kesi ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake, ameimbia mahakama kuwa Kampuni ya Alex Stewart Bussiness Corporation ilikuwa haifuati sheria za kodi.

Mbali na Mramba, ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja.

Shekidele ambaye ni shahidi wa 13 wa upande wa jamhuri katika kesi , alitoa madai hayo mbele ya Jaji John Utamwa aliyekuwa akisaidiwa na Mahakimu Wakazi Sam Rumanyika na Saul Kinemela katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,jana wakati akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili Kiongozi wa Serikali Fredrick Manyanda.

Shekidele aliambia mahakama kuwa mwaka 2007 wakati akiwa na wadhifa huo pia alikuwa ni Kaimu Kamishna wa Kodi za ndani, na majukumu yake yalikuwa ni kuangalia utendaji wa makusanyo ya kodi za ndani na kujijbu mawasiliano na barua zitokazo nje ya Idara yake na kwamba kampuni hiyo ilikuwa haileti ripoti za mahesabu yake.

Hata hivyo Shekidele alianza kubabaika baada ya kubanwa maswali na wakili wa Mramba, Hurbert Nyange kwamba ana ushahidi gani kama zile ripoti za mahesabu za mwaka za kampuni hiyo ambazo zilitolewa na TAKUKURU kwa TRA kama kweli ni za kampuni hiyo.

“Mh! sikuziona hizo ripoti ya mahesabu ya kampuni hiyo.....aah waheshimiwa mahakimu naomba nibadili jibu langu la awali, nimekumbuka niliziona hizo ripoti ila sijui ni nani alizisaini...na sifahamu kama wakati TRA inaandaa ripoti hizo za mahesabu za kampuni hiyo sifahamu kama kampuni hiyo ilituma mwakilishi wake kushiriki kushirikiana na TRA kuandaa mahesabu hayo”alidai Shekidele.Kesi hiyo inaendelea kusikiklizwa tena leo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Novemba 24 mwaka 2010

KESI YA MARANDA NA EPA YASHIKA KASI

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya wizi ya sh bilioni 2.2 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) Benki Kuu ya Tanzania, (BoT), inayomkabili Mweka Hazina wa CCM, Mkoa wa Kigoma, Rajabu Maranda, na ndugu yake, Farijala Hussein, umefunga kesi yake rasmi.


Mbele ya Jaji, Fatma Masengi, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Wakili Kiongozi wa Serikali, Fredrick Manyanda, aliiambia mahakama hiyo kuwa upande wa Jamhuri umefunga rasmi kesi hiyo baada ya mashahidi wake sita kumaliza kutoa ushahidi wake jana.

“Sisi upande wa Jamhuri leo tunatangaza rasmi kuifunga kesi yetu baada ya kuleta idadi hiyo ya mashahidi,” alidai Wakili Kiongozi Manyanda.

Kwa upande wake wakili wa utetezi, Majura Magafu aliomba mahakama iuamuru upande wa Jamhuri umpatie mwenendo mzima wa kesi hiyo ili aweze kwenda kuupitia na kuweza kumsaidia kujenga hoja itakayoweza kuishawishi mahakama iwaone wateja wake hawana kesi ya kujibu na Jaji Masengi alikubaliana na ombi hilo.
Jaji huyo aliiahirisha kesi hiyo hadi Desemba 13 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa na kuona kama tayari upande wa Jamhuri umeishawapatia mwenendo huo upande wa utetezi.

Awali shahidi wa sita wa upande wa Jamhuri, ambaye ni Msajili Msaidizi (BRELA), Noel Shani, akiongozwa kutoa ushahidi wake na Manyanda aliambia mahakama kuwa yeye ndiye aliyelisajili jina la Kampuni ya Money Planner ambayo ilitumiwa na washitakiwa kuchota fedha za EPA.

Alisema anachokifahamu yeye ni kwamba alisajili jina hilo la kampuni ambayo wamiliki wake ni Paul Nyingo na Fundi Ayeshi Kitunga na si Maranda na Farijala kama washitakiwa wanavyodai kuwa kampuni hiyo ni yao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Novemba 17 mwaka 2010

DK.SLAA AUKACHA USULUHISHI KORTINI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ilishindwa kuanza kuendesha usuluhushi katika kesi ya madai ya kupora mke wa mtu inayomkabili aliyekuwa mgombea urais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kupitia chama (CHADEMA), Dk.Willbroad Slaa baada ya mdaiwa na wakili wake kutotokea mahakamani.

Kesi hiyo ambayo jana ilikuja kwaajili ya usuluhishi lakini katika hali isiyotarajiwa mdaiwa huyo wala wakili wake Mabere Marando walishindwa kufika mahakamani hapo wala kutoa taarifa za udhuru.

Hali hiyo iliyomsababisha msuluhishi wa kesi hiyo(Jaji )Zainabu Muruke kusema kuwa kitendo hicho kimetafsiriwa na mahakama kuwa mdaiwa Dk.Slaa hayuko tayari kwaajili ya usulushi kwahiyo ataandika taarifa kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Semistocles Kaijage ili aweze kupanga jaji mwingine wa kuanza kuisikiliza kesi hiyo.
“Kutokana na mdaiwa (Dk.Slaa) na wakili wake Marando kutokufika leo(jana) mahakamani hapa kwaajili ya usuluhishi kama walivyokuwa wamekubali awali kushiriki katika meza ya usuluhishi tena bila hata kutoa taarifa ya udhuru , mahakama hii imetafsiri kitendo hicho kuwa mdaiwa hayupo tayari kwaajili ya usuluhishi na hivyo nitaandika taarifa kwa Jaji Mfawidhi ili aweze kupanga jaji mwingine kwaajili ya hatua zitakazofuata ili ianze kusikilizwa..”alisema Jaji Muruke.
Awali pande zote mbili katika kesi hiyo zilikubalina kushiriki katika meza usulushi na kwamba kama usuluhishi huo ukishindika , kila upande utaleta mashahidi wa nne pindi kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa.
Kisheria kesi za madai kabla haijaanza kusikilizwa kunakuwa na usuluhishi ambapo jaji ndie anakuwa msuluhishi na endapo mdaiwa akikubali madai anayolalamikiwa,kesi humalizikia hapo na endapo mdaiwa atakwepa kushiriki kwenye usuluhishi au akashiri kwenye meza ya usulushi lakini wakashindwa kufikia mwafaka kesi hiyo uendelea kusikilizwa mahakamani.

Katika kesi hiyo ya madai inayomkabili Dk.Slaa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa (CHADEMA). Aminiel Mahimbo amemshitaki Dk. Slaa akidai kuwa amempora mke wake Josephine Mushumbusi na kuwa anamnadi katika majukwaa ya kisiasa katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, kuwa ni mchumba wake, hoja ambazo Dk .Slaa alizipinga katika majibu yake na kudai kuwa hakufahamu kuwa mwanamke huyo ni mke wa mtu.

Mahimbo anaomba mahakama imwamuru Dk.Slaa amlipe Sh.bilioni moja ikiwa ni fidia ya kudhalilishwa kiongozi huyo wa kisiasa. Mahimbo katika madai yake anadai kuwa Septemba 7, 2002 alifunga ndoa na mwanamke huyo katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ushirika wa Kijitonyama na wala ndoa yao haijawahi kuvunjwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Novemba 17 mwaka 2010

WAKILI KESI YA ZOMBE AFARIKI DUNIA

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Mwanasheria Mwandamizi wa Serikali, Jasson Kaishozi katika kesi ya mauji ya wafanyabiashara wa nne iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelele Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP),Abdallah Zombe na wenzake nane amefariki dunia jana.

Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Elizer Feleshi alisema ofisi yake ilipata taarifa za kifo hicho jana mchana kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mbeya na kwamba alikwenda hospitalini hapo kwa ajili ya kumuona daktari, alipomaliza aliishiwa nguvu na kufariki dunia wakati akipatiwa matibabu.

“Nikiwa kama DPP wa Tanzania na timu yangu wa waendesha mashtaka nchini, tumepokea kwa masikitiko na mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha Kaishozi kwani alikuwa ni miongoni mwa mawakili mahiri wa serikali hasa kwa upande wa uendeshaji wa mashauri ya jinai,” alisema Feleshi kwa masikitiko.

Alisema taratibu za mazishi zinafanywa na mwili wa marehemu utasafirishwa kupelekwa nyumbani kwao Bukoba Vijijini kwa mazishi. Hadi kifo chake Kaishozi alikuwa Wakili wa Serikali Mfawidhi wa Kanda ya Mbeya.

Mbali na Zombe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Christopher Bageni, Ahmed Makele, WP 4593 PC Jane Andrew, D 1406 Koplo Emmanuel Mabula, D 8289 DC Michael Shonza, D. 2300 Abeneth Saro, D.4656D/Koplo Rajabu Bakari na D.1317D/XP Festus Gwasabi.

Washitakiwa hao walidaiwa kuwa Januari 14, mwaka 2006 waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini wa wilayani Ulanga, mkoani Morogoro; Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe pamoja na dereva teski Juma Ndugu, mkazi wa Dar es Salaam kwa madai kuwa walikuwa majambazi
Agosti 17 mwaka jana, Jaji wa Salum Massati aliwaachilia huru washtakiwa wote kwa maelezo kuwa upande wa Jamhuri ambao ulikuwa ukiwakilishwa na marehemu Kaishozi, Mwipopo, Mgaya Mtaki, Mzikila umeshindwa kuthibitisha kesi hiyo ambayo ilikuwa ikivuta hisia za watu wengi hapa nchini.

Kaishozi ambaye katika kesi ya Zombe alikuwa akisaidiana na mawakili wenzake wa serikali, Angaza Mwipopo, Mgaya Mtaki na Alexanda Mzikila ni wakili wa pili kufariki dunia katika kesi hiyo wa kwanza alikuwa wakili aliyekuwa akimtetea Zombe, Moses Maira.

Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Novemba 16 mwaka 2010

GIRE AIKANA RICHMOND KORTINI

Na Happiness Katabazi

MSHITAKIWA, Naeem Adam Gire, anayekabiliwa na mashitaka ya kughushi hati ya nguvu ya kisheria na kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa serikali kuhusu Kampuni ya kuzalisha umeme ya Richmond LLC ya Texas, Marekani amekana kuwa miongoni mwa wakurugenzi wa kampuni hiyo na kwamba wala hakutoa taarifa za uongo.


Gire alikanusha tuhuma hizo zilizoelekezwa kwake na upande wa Jamhuri katika kesi hiyo jana mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Walirwande Lema, muda mfupi baada ya Wakili Mkuu wa Serikali, Fredrick Manyanda, kumaliza kumsomea maelezo ya awali mshitakiwa huyo ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea, Richard Rweyongeza.

“Nakanusha mbele ya mahakama hii kuwa mimi si mkurugenzi wa kampuni hiyo ila nakubali kwamba mfanyabiashara anayeishi Marekani, Mohamed Gire, ambaye ni Mwenyekiti wa Richmond Development Company Limited, Liabilities Company (LLC), ni kaka yangu na mimi pia ni mfanyabishara ninayemiliki Richmond Internet CafĂ© iliyopo Mtaa wa Kipata nyumba Na.66 Dar es Salaam,” alidai Naeem Gire.

Manyanda aliendelea kueleza kuwa Machi 13, 2006, jijini Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa na dhamira ya kutenda kosa, alighushi hati ya nguvu ya kisheria (power of attorney) inayoonyesha imetolewa na Mohamed Gire, ambaye ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, kwamba amemruhusu kufanya shughuli za kampuni hiyo hapa nchini.

Aliendelea kuieleza mahakama kuwa mshitakiwa huyo Machi 20 mwaka 2006, katika eneo la Ubungo, Umeme Park, Barabara ya Morogoro, alitoa hati hiyo ya nguvu ya kisheria inayomuidhinisha yeye kwamba ameruhusiwa kufanya kazi ya kampuni hiyo ya Marekani hapa nchini.

Manyanda aliendelea kuieleza mahakama kuwa Juni 2006 hapa jijini, mshitakiwa huyo pia alitoa taarifa za uongo kwa wajumbe wa timu ya majadiliano ya serikali, kuwa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme kwa kiwango hicho ili apewe tenda hiyo.

Wakili Mkuu huyo wa serikali Manyanda, aliendelea kuieleza mahakama kuwa Julai, 2006, ambapo mshitakiwa akifahamu na kwa ulaghai, alitoa hati ya nguvu ya kisheria iliyotolewa Machi 3, mwaka huo iliyokuwa ikimuonyesha kuwa ameruhusiwa na Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, Mohamed Gire, kufanya kazi za kampuni hiyo hapa nchini.

Aidha, wakili Manyanda alisema baada ya mshitakiwa huyo kukamatwa na kuhojiwa na vyombo vya dola Oktoba 13 mwaka 2008, alikiri kutenda makosa hayo aliyoshitakiwa nayo mahakamani.
Hakimu Lema baada ya kusikiliza maelezo hayo ya awali aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 8 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Kwa mara ya kwanza mshitakiwa huyo alikamatwa na kufikishwa mahakamani Januari 13 mwaka jana na Gire amefikishwa mahakamani ikiwa ni mwaka mmoja baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na mwenzake aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha, walilazimika kujiuzulu nyadhifa zao kwa kashfa hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Novemba 16 mwaka 2010

UBAGUZI KATIKA CHAGUZI USILIVURUGE TAIFA

Na Happiness Katabazi

KWA takribani miezi miwili mwandishi wa safu hii nilishindwa kuwaletea makala kama ilivyoada kwasababu ya kuwa kwenye kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 31 mwaka huu, hapa nchini.


Katika kipindi chote hicho nilikuwa nikizunguka nchini nzima na aliyekuwa mgombea mwenza wa Chama cha Mapinduzi(CCM), ambaye kwa sasa ndiye Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Mohamed Ghalib Bilal ,nikiwa miongoni mwa waandishi wa habari wachache tuliochaguliwa kuunda timu ‘Press Team Bilal 2010 Campaign’.

Namshukurumu mungu tumeweza kumaliza kazi hiyo salama na kurejea ofisini kwangu tayari kabisa kwaajili ya kuendelea kulitumikia taifa hili kupitia kalamu yangu.Hivyo nawaomba radhi wasomaji wangu kwa kushindwa kuwaletea makala kwa kipindi chote hicho.

Mbali na maelezo hayo leo katika safu hii, nitajadili kwakina mchakato mzima wa uchaguzi mkuu uliopita pamoja na makandokando yake.
Watanzania tumeuona uchaguzi mkuu wa 2010 ukimalizika kwa taswira ambayo ni ya mchanganyiko.Wapo waliofurahi kwa kuwa ama wameshinda ama wagombea wao wameshinda.

Lipo kundi jingine la walioshindwa ambao wao wameshindwa ama wagombea wao wameshindwa .Lakini hivyo ndivyo ilivyotazamiwa iwe katika mazingira ya kinyang’anyiro ambacho kinapelekea kupatikana kwa mshindi mmoja tu kati ya wengi.Kura moja ni ushindi na hiyo ndiyo falsafa ya ushindi .

Sasa uchaguzi mkuu ulimalizika hivi karibuni ni wa tatu kufanyika tangu vyama vingi vianzishwe hapa nchini Julai 1992.

Je, tukiondoa mazingira tuliyoyataja hapo juu, Watanzania tumejifunza nini cha kuweza kujivunia kuwa sasa tunaelekea kwenye demokrasia bora iliyokomaa?

Mosi; nililoliona ni kukosekana kwa mazingira bora ya kisheria ya uchaguzi huru na wa haki.Jambo hili ni kubwa kwasababu chanzo chake ni Katiba ya nchi ,ambacho ni kilio cha wananchi wengi tangu mwaka 1992.
Hatujapa Katiba mpya inayopiganiwa na wana mageuzi na wala hatujapata Katiba nzuri kutokana na viraka vinavyobandikwa mara kwa mara na watawala waliopo madarakani.

Hivyo hatuna Tume huru ya Uchaguzi , hatuna sheria inayoweka mazingira sawa ya ushindani wa vyama vya siasa na hatuna uwezeshwaji wa washiriki wa uchaguzi ili kuakikiasha kila raia ana faidi haki yake ya binadamu na Katiba ya kuchagua au kuchaguliwa.

Pili;uchaguzi wa mwaka 2010,umeonyesha udhaifu mkubwa wa misingi kitaifa tuliokuwa tunajivunia kuwa tunayo na tunaheshimu sana.Msingi wa kwanza ambao ufa wake umeshindikana kuzibwa katika uchaguzi huu ni udini.Ghafla baadhi ya wagombea wakuu na wafuasi wa vyama vya siasa hasa wa CCM na CHADEMA walijikuta wakirushiana makombora ya udini .Kila mmoja akimlaumu mwenzake akitumia udini kujipatia udini kujipatia ushindi.

Ni kweli kwamba katika nchi yetu wengi wetu tuna dini kwa hiyo ni vigumu kumpata mgombea asiye na dini.Lakini ni hatari dini inapotumika kama mbinu halali ya kusaka uongozi.

Hilo halina mjadala kuwa ni baya ,la kukemewa vikali na ni la aibu na lina hatarisha usala wa taifa.Ila wasiwasi wangu ni viongozi wanapaswa wawe mstari wa mbele kukemea pepo huyo wa udini ,baadhi yao walitumia mbinu hiyo ya ubaguzi wa udini katika kampeni zao na kufanikiwa kupata madaraka na kwakuwa wanasiasa hao wenye hulka za kinyang’au wamefanikiwa kisiasa kwa kutumia mbinu hiyo ambayo ina hatarisha usalama wa taifa letu.

Sasa tujiulize katika chaguzi nyingine za kiasa wanasiasa hawa wataacha kutumia mbinu hiyo hatari ya udini katika chaguzi nyingine za kisiasa ili waweze kutwaa tena madaraka ya kisiasa?

Tayari hivi sasa watu wanangojea kuona serikali itakayoundwa na Rais Jakaya Kikwete itakuwa na sura kutokana na balaa hilo la udini?.

Kila mara mteuaji atakapoweka usawa au uwiano wa kidini ,haina maana kwamba hatumii kigezo cha udini.
Tatu; ukabila,ukanda,sehemu anakotoka mgombeaji. Tanzania ni nchi mmoja na Watanzania ni taifa moja linalojitambua kuwa ni ndugu moja.

Pamezuka hatari kubwa ya watu kuulizana asili,koo,kabila zao,ukanda anakotoka au sehemu anapotokea mgombeaji.

Kwa hiyo imefika mahali sasa imekuwa nongwa mfano mgombea atokee Karagwe mkoani Kagera aje kugombea udiwani au ubunge jijini Dar es Salaam, au atoke mkoa wa Mbeya aende akagombee katika moja ya jimbo au Kata mkoani Tanga.Mgombea atakayeenda kugombea Tarime ataulizwa kabila na anatokea ukoo gani?
Kwa hiyo mgombea ubunge wa mfano jimbo la Ubungo,Kawe na majimbo mengi atapata ushindi kwasababu watu wengi wanaoishi katika majimbo wa kabila lake.

Hivi tangu lini tumeulizana makabila?Hata unapoenda kununua kiwanja ujenge nyumba ,kweli ni nani anauliza kwanza ni eneo gani watu wa kabila lake wanaishi wengi?

Huu ni puuzi na umaamuma.Na kama utamaduni wa aina hii utapewa nafasi uote mizizi ,kwa sababu tayari umeishaanza kuchipua, ni wazi hatuwezi kuamisha vijiji vyetu tulikozaliwa huko mikoani tukaviamishia Dar es Salaam.

Nne; jinsia , baada ya miaka 15 ya vyama vingi bado taifa letu halijaweza kuimarisha uwiano wa kijinsia katika siasa za nchi. Kwa hiyo wanawake hawajapewa nafasi katika fikra za kisiasa kwa wa wananchi kuwa ni watu wanaostahili kuongoza kwa hiyo tumezidi kuimarisha mfumo wa Viti Maalum badala ya kuimarisha mafunzo ya kiungozi kwa wanawake ili waweze kuwa na ushindani uliobora katika Nyanja ya siasa.

Kwa hiyo japo kuwa wanawake wenzangu wamekuwa wakidai kwamba Viti Maalum viongezwe hadi kufikia asilimia 50; uwiano huo hautuakikishii sisi wanawake uwezo endelevu wa kiungozi.

Hivyo inabidi turejee suala hili kwa kudai mafunzo ya kiuongozi kwa wanawake yatolewe katika shule za msingi , sekondari na vyuoni ili kuwaandaa wawe washindani bora katika mfumo wa sasa wa siasa za ndani na nje ya nchi.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
0716-774494


Chanzo:Gazeti la Tanzania la Jumapili, Novemba 15, mwaka 2010

MAHAKAMA YA KISUTU YALITUPA PINGAMIZI MURRO

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, ilitupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi katika kesi ya kuomba rushwa ya sh mil. 10 inayomkabili aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC1), Jerry Murro na wafanyabiashara wawili.


Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Gabriel Mirumbe, ambapo alisema baada ya kusikiliza malumbano ya kisheria yaliyoibuliwa na pande zote mbili juzi, amefikia uamuzi wa kutupilia mbali pingamizi za mawakili wa utetezi, Richard Rweyongeza, Majura Magafu na Pascal Kamala, waliotaka mahakama hiyo ikatae kupokea kielelezo cha pili cha upande wa Jamhuri, kwa sabababu pingamizi hilo halina hoja za msingi.

Juzi Wakili wa Rweyongeza aliwasilisha pingamizi la kutaka kielelezo hicho ambacho ni picha za CCTV zinazomuonyesha mshitakiwa wa kwanza, Murro, Deogratius Mugassa na aliyekuwa Mweka hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Wage, wakiwa wanaingia na kutoka ndani ya Hoteli ya Sea Cliff, siku ya Januari 31 mwaka huu, saa 7:31 wakiingia katika hoteli hiyo na picha nyingine inaonyesha walitoka hotelini hapo saa 8:27 ya siku hiyo, kilichotolewa na shahidi wa pili wa upande wa mashitaka ambaye ni Meneja wa Teknolojia ya Mawasiliano wa Hoteli ya Sea Cliff, Pounama Kumar, kwa madai kwamba picha hizo ni kivuli na si halisi.

Hakimu Mirumbe, alisema amefikia uamuzi wa kukubalina na hoja za Wakili Kiongozi wa Serikali, Boniface aliyeiomba mahakama hiyo ipuuze pingamizi la utetezi, kwa madai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 40A cha Sheria ya Ushahidi ya mwaka 2002, kinairuhusu mahakama kupokea ushahidi wa kielektroniki, video na redio unaomhusu mshitakiwa na wala kifungu hicho hakiizuii mahakama kupokea ushahidi wa aina hiyo ambao ni kivuli au halisi.

“Mahakama hii inatupilia mbali pingamizi la upande wa utetezi na linakubaliana na hoja za upande wa jamhuri, kwa sababu ni za msingi na ni za kisheria, hivyo mahakama hii inapokea picha hizo za CCTV kama kielelezo cha pili kilichotolewa na upande wa Jamhuri na inaahirisha usikilizaji wa kesi hii hadi Januari 17,18 na 19 mwaka kesho,” alisema Hakimu Mkazi Mirumbe.

Katika shitaka la kwanza, watuhumiwa hao wanadaiwa kula njama kwa mujibu wa kifungu cha 32 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Novemba 13 mwaka 2010

MAHAKAMA KISUTU KUPOKEA VIELELEZO KESI YA MURRO

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, mjini Dar es Salaam, imesema leo itatoa uamuzi wa kupokea au kutopokea kielelezo cha pili kilichotolewa na upande wa Jamhuri jana katika kesi ya kuomba rushwa ya sh mil. 10 inayomkabili aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1), Jerry Murro na wafanyabiashara wawili.


Hakimu Mkazi, Gabriel Mirumbe, alifikia uamuzi huo baada ya kuibuka malumbano makali ya kisheria baina ya pande hizo katika kesi hiyo. Upande wa utetezi unaowakilishwa na wakili wa kujitegemea, Richard Rweyongeza, Majura Magafu na Pascal Kamala na kuiomba mahakama isipokee picha za CCTV zilizotolewa mahakamani hapo, kama kielelezo na shahidi wa pili wa Jamhuri ambaye ni Meneja Teknolojia ya Mawasiliano wa Hoteli ya Sea Cliff, Apaumr, kwa madai picha hizo ni kivuli na si halisi .

Kwa upande wake Wakili Kiongozi wa Serikali, Stanslaus Boniface, aliomba mahakama ipuuze pingamizi hilo la utetezi, kwa madai kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 40A cha Sheria ya ushahidi ya mwaka 2002, kinairuhusu mahakama kupokea ushahidi wa kielektroniki, video, redio unaomhusu mshitakiwa na wala kifungu hicho hakiizuii mahakama kupokea ushahidi wa aina hiyo ambao ni kivuli au halisi.

Awali shahidi huyo wa pili kabla ya kutoa kielelezo hicho cha picha ya CCTV ambazo zinawaonyesha washitakiwa hao wakiwa kwenye Hoteli ya Sea Cliff, Januari 29, mwaka huu, kipokewe mahakamani kama kielelezo.

Akiongozwa kutoa ushahidi wake na wakili Kiongozi wa Serikali, Boniface, shahidi huyo alieleza kuwa Februali 2, mwaka huu, meneja mkuu ambaye ni bosi wake alimuita ofisini kwake akimtaka aongozane na maofisa watatu wa polisi waliokuwa wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda ya Dar es Salaam (ZDCO), Charles Mkumbo, awapeleke kwenye chumba maalumu cha kurekodi (CCTV) ili waweze kuangalia wageni waliofika kwenye hoteli hiyo siku ya Januari 28-31 mwaka huu.

Mbali na Murro, washitakiwa wengine ni Edmund Kapama na Deogratius Mugasa, ambao Februari 15 mwaka huu, walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza wakikabiliwa na mashitaka matatu ya kula njama za kutaka kupokea rushwa kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Karoli Wage. Kati ya mashitaka matatu yaliyofunguliwa dhidi yao, Murro anakabiliwa na mashitaka mawili.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Novemba 12 mwaka 2010

HEKO MAHALU,HEKO KORTI KUU

Happiness Katabazi

JUMATATU ya wiki hii, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, iliandika historia mpya katika tasnia ya sheria nchini, baada ya kutoa hukumu iliyotamka bayana kuwa kifungu cha 36(4)(e) sura ya 200 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi ya mwaka 2002, ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.


Sambamba na hiyo, mahakama hiyo ilitoa maelekezo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndani ya mwaka mmoja kuanzia siku hiyo awe amefanyia marekebisho kifungu hicho ama sivyo mahakama hiyo itakitamka kifungu hicho ni batili.

Kifungu hicho kilikuwa kinatamka kila mwenye kushitakiwa au kutuhumiwa kwa kosa la uhujumu uchumi ili apate dhamana ni lazima adhaminiwe kwa nusu ya kiwango anachotuhumiwa nacho.

Mfano, mtu mwenye kutuhumiwa kuiingiza hasara serikali ya sh bilioni 12 atatakiwa apatiwe au atoe dhamana ya sh bilioni sita, kinyume na hapo ataendelea kusota rumande.

Hukumu hiyo ya kesi ya kikatiba ya mwaka 2008, iliyofunguliwa mahakamani hapo na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ilitolewa Oktoba 5, mwaka huu, saa nane mchana na jopo la majaji watatu.

Jopo hilo lilikuwa likiongozwa na Jaji Kiongozi, Fakhi Jundu, aliyekuwa akisaidiwa na Jaji Agustine Mwarija na Projest Rugazia, ambaye hakuwepo mahakamani hapo wakati hukumu hiyo ikisomwa.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Jundu alisema kimsingi Mahakama Kuu inakubaliana na hoja za mawakili wa mlalamikaji (Mahalu), aliyekuwa akitetewa na mawakili mahiri wa kujitegemea, Alex Mgongolwa na Cuthbert Tenga kwamba kifungu hicho cha 36 (4)(e) sura ya 200 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi kinakwenda kinyume na Katiba ya nchi na kinaleta ubaguzi.

Alisema wanakubaliana na hoja za mawakili wa Mahalu, kwamba uwepo wa kifungu hicho unafanya mshitakiwa mwenye fedha ndiye apate dhamana na mshitakiwa ambaye hana fedha kutoweza kutimiza masharti hayo ya dhamana, hivyo kuishia kusota gerezani.

Hata hivyo, Jaji Jundu alisema kwa mujibu wa Ibara ya 30 (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahakama Kuu inapoona kifungu chochote cha sheria kinakiuka ibara za Katiba, ina mamlaka ya kutoa maelekezo kwa Mwanasheria Mkuu kukifanyia marekebisho.

Hii ni kesi ya pili ya kikatiba kufunguliwa na wananchi katika mahakama hiyo hiyo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mwisho wa siku, wanashinda tangu serikali ya awamu ya nne iingie madarakani.

Kesi ya kikatiba ilifunguliwa na kituo cha Haki za Binadamu, ambapo pia kituo hicho kilikuwa kikitetewa na wakili Alex Mgongolwa waliomba mahakama hiyo itamke takrima katika uchaguzi ni rushwa.

Mwaka 2006 Mahakama Kuu ilikubaliana na hoja za wakili Mgongolwa ambapo ilitamka Takrima ni rushwa na ikamwagiza Mwanasheria Mkuu akafanyie marekebisho katika kifungu hicho kinachoruhusu takrima katika Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985.

Mahalu, alilazimika kufungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu, ikiwa ni muda mfupi baada ya mwaka 2006, kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ya sh bilioni tatu, ambapo hata hivyo kesi hiyo usikilizwaji wake unashindwa kuendelea katika mahakama hiyo kwa sababu jalada la msingi la kesi hiyo lipo katika Mahakama ya Rufani nchini.

Mahalu aliwasilisha ombi la kuiomba mahakama hiyo ya juu nchini ifanye mapitio ya uamuzi uliotolewa na aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu (mstaafu), Juxon Mlai, ambaye alitupilia mbali ombi la Mahalu lililokuwa likiomba mahakama hiyo imuache huru kwasababu utaratibu wa kisheria haukufuatwa kabla ya yeye kufunguliwa kesi hiyo ya uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa maelezo hayo hapo juu, napenda kutoa pongezi zangu za dhati Profesa Mahalu kwa moyo wake wa ujasiri wa kufungua kesi hiyo tena kwa kutumia gharama zake kwa kuwaweka mawakili mahiri.

Nawapongeza mawakili hao kwa kazi nzuri ambayo iliweza kuwashawishi Jaji Kiongozi Fakhi Jundu na wenzake kukubaliana na hoja zao na mwisho wa siku wakatoa hukumu ambayo nalazimika kusema itawasaidia wananchi wengi ambao watapatwa na mabalaa ya kufunguliwa kesi za uhujumu uchumi .

Kwa wale wananchi ambao si waumini wa tasnia ya sheria au hawajawahi kufika mahakamani na kuona baadhi ya watu wanaokabiliwa na kesi za uhujumu uchumi na mahakama inapowatamkia washtakiwa wa kesi za aina hiyo kwamba ili wapate dhamana ni lazima watoe nusu ya kiasi cha fedha wanachotuhumiwa kuiba au kusababisha hasara, naamini itawawia vigumu kuona uzito, maana na faida ya hukumu hii.

Vyombo vingi vya habari havijaipa uzito wa kipekee hukumu hii, kama vyombo hivyo vilivyokuwa vizipata uzito wa kipekee hukumu ya rufaa ya mgombea binafsi au kesi ya mauaji ya watu wafanyabiashara wa nne iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa mkuu wa upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi, Abdallah Zombe na wenzake na kesi za wizi wa akaunti ya madeni ya nje katika Benki Kuu (EPA). Na si vyombo vya habari peke yake pia jamii kwa ujumla na hizo taasisi zinazojinasibu kila kukicha kwamba ni taasisi za kiharakati za kutetea wanyonge na maskini.

Hili ni jambo la kusikitisha kama si la kushangaza kwani ndani ya jamii yetu hasa kwa sisi tunaotokea kwenye familia za kimaskini, kama si leo, basi kesho, mimi, wewe au mwingine tunaweza kujikuta mikononi mwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Eliezer Feleshi.

Tunaweza kuangukia katika mikono hiyo na baadaye kufikishwa mahakamani kwa kesi za uhujumu uchumi iwe tumetenda kweli kosa hilo au tumebambikiziwa kesi na mahakama italazimika kutumia kifungu hicho cha sheria ya uhujumu uchumi kwa ajili ya sisi maskini ndiyo tupate dhamana.

Nayaandika haya kwa hisia kali kwani kwa takriban miaka 11 sasa nimekuwa mwandishi wa habari za mahakamani hapa nchini, nimekuwa nikishuhudia wananchi wenzetu wakishindwa kumudu na kutimiza masharti ya dhamana kwa makosa ya uhujumu uchumi.

Watu hawa wamejikuta wanaozea magerezani miaka nenda miaka rudi wakati kesi zikiendelea kuunguruma, tena kwa kasi ya mwendo wa kinyonga kiasi kwamba zinachukua mpaka miaka minne hadi kutolewa uamuzi.

Msingi mmoja wapo wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, unapiga marufuku mtu yeyote kuchukuliwa kuwa na hatia mpaka pale mahakama itakapothibitisha kuwa mtu huyo ana hatia. Sasa kwa msingi huo wa Katiba ni dhahiri kifungu hicho cha 36(4) cha Sheria ya uhujumu uchumi ya mwaka 2002, kinapingana na msingi huo wa Katiba ambayo ndiyo sheria mama.

Wakati mwingine hukumu za washitakiwa hao zinapotoka mahakama inawaachilia huru washitakiwa hao kwasababu mahakama hiyo haijaletewa ushahidi unaojitosheleza.

Lakini vyovyote iwavyo, nadiriki kusema kuwa uwepo wa rushwa unatokana na mfumo wetu dhahifu katika masuala ya utoaji haki.Tuna matatizo makubwa kwa wale tuliowakabidhi majukumu ya kupambana na rushwa kwani baadhi yao watendaji wake wanakubali kutumiwa vibaya na wanasiasa wenye hulka za kinyang’au, kula rushwa na kisha kubambikia kesi watu wasio na hatia.

Watu hao wasio na hatia wakishaburuzwa mahakamani hujikuta wanabanwa na masharti ya kifungu hicho kilichotamkwa na Jaji Jundu na wenzake kuwa kinakwenda kinyume na Katiba ya nchini.

Ni hatari kwa sheria kumkabidhi binadamu yeyote mamlaka makubwa kiasi hicho. Leo na kesho itakapotokea kwamba mtu alifikishwa kortini na kuswekwa gerezani kwa kunyimwa dhamana kwasababu ya masharti ya kifungu hicho cha sheria ya uhujumu uchumi, na baadaye kubainika hana hatia, ana kuwa amedhalilishwa na kutopetezwa muda wake mwingi.

Kwa bahati mbaya, wengi wetu bado hatujajifunza thamani ya uhuru wa binadamu wenzetu.

Ni vyema sheria zetu zibadilishwe ili wale wanaoonekana mapema upande wa Jamhuri hauna sababu ya kuwafungulia mashtaka walipwe fidia kwa sababu thamani ya uhuru na heshima ya binadamu ni kubwa kuliko kiasi cha fedha chochote kinachohusika kwenye hizo kesi za uhujumu uchumi.

Kwenye tasnia ya sheria tunasema hivi ‘ni afadhali wahalifu tisa waachiliwe huru kuliko mtu mmoja asiye na hatia kuwekwa hatiani’.

Aidha, nimalizie kwa kumpongeza Profesa Costa Mahalu kwa uzalendo wake wa kufungua kesi hiyo na kisha kushinda, matunda ya hukumu hiyo si yake pekee, ni ya Watanzania wote watakaopatwa na matatizo ya kufunguliwa kesi za uhujumu uchumi.

Nina matumaini kuwa hukumu hii itawasaidia wanafunzi wa fani ya sheria vyuoni kwani watatumia hukumu hiyo kujibu maswali kweye mitihani, pia ni faida pia kwa majaji, mahakimu na mawakili ambao sasa watalazimika kutumia hukumu kama kielelezo cha kuunga mkono hoja zao za kisheria na kuitumia kutolea maamuzi katika kesi mbalimbali.

Hukumu hii iwe ni changamoto kwetu sisi waandishi wa habari hapa nchini kwani tumekuwa na kasumba ya kuinung’unikia sheria ya magazeti kuwa ni moja ya sheria mbaya lakini tunashindwa kupiga hatua moja mbele ya kutafuta mawakili watusaidie kufungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu, kutaka sheria hiyo ifanyiwe marekebisho.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Oktoba 10 mwaka 2010

MAHALU AIBWAGA SERIKALI KORTINI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, imetamka kuwa kifungu cha 36(4)(e) sura ya 200 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.


Sambamba na hiyo, mahakama hiyo, imetoa maelekezo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndani ya mwaka mmoja kuanzia jana, awe amefanyia marekebisho kifungu hicho.

Hukumu hiyo ya Kesi ya Kikatiba ya mwaka 2008, iliyofunguliwa mahakamani hapo na aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ilitolewa jana na jopo la majaji watatu lililokuwa likiongozwa na Jaji Kiongozi, Fakhi Jundu, aliyekuwa akisaidiwa na Jaji Agustine Mwarija na Projest Rugazia ambaye hakuwepo mahakamani hapo wakati hukumu hiyo ikisomwa.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Jundu alisema kimsingi Mahakama Kuu inakubalina na hoja za mawakili wa mlalamikaji (Mahalu), aliyekuwa akitetewa na mawakili wa kujitegema, Alex Mgongolwa na Cuthbert Tenga kwamba kifungu hicho cha 36 (4)(e) sura ya 200 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi, kinakwenda kinyume na Katiba ya nchi na kinaleta ubaguzi.

Alisema wanakubaliana na hoja za mawakili wa Mahalu, kwamba uwepo wa kifungu hicho unafanya mshtakiwa mwenye fedha ndiye apate dhamana na mshtakiwa ambaye hana fedha hawezi kutimiza masharti hayo ya dhamana hivyo kuishia kusota gerezani.

Hata hivyo, Jaji Jundu alisema kwa mujibu wa Ibara ya 30 (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mahakama Kuu inapoona kifungu chochote cha sheria kinakiuka ibara za Katiba , ina mamlaka ya kutoa maelekezo kwa Mwanasheria Mkuu kukifanyia marekebisho kifungu hicho.

Hii ni kesi ya pili ya Kikatiba kufunguliwa na wananchi katika mahakama hiyo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mwisho wa siku, wanashinda tangu serikali ya awamu ya nne iingie madarakani.

Mahalu alilazimika kufungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu, ikiwa ni muda mfupi baada ya mwaka 2006, kufikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ya sh bil. 3.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Oktoba 5 mwaka 2010

MEMBE AMDUWAZA DK.BILAL

Na Happiness Katabazi, Lindi

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe, juzi alimduwaza mgombea mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Mohammed Gharib Bilal, baada ya kukamata kipaza sauti jukwaani na kuanza kuimba na kucheza wimbo wa kabila lake la Wamwela.


Tukio hilo la aina yake, ambalo lilivutia umati mkubwa wa wananchi waliojitokeza kumlaki Dk. Bilal kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Mtama, Wilaya ya Lindi Vijijini, ambako mgombea mwenza huyo alitumia fursa ya kumnadi Membe, anayewania ubunge wa Mtama.

Kabla ya Dk. Bilal kupanda jukwaani kumnadi, Membe alitangulia na kushika kipaza sauti na kusema kuwa, yeye atamkaribisha jukwaani mgombea mwenza kwa kumuimbia wimbo wa kabila lao la Wamwela, uliokuwa na maneno yasemayo: “Pano Pano Palipanda, Pano Pano Palipanda,”. Membe alisema, wimbo huo una maana kwamba, hapo hapo ndipo alipotoka yeye.

Wakati Membe akiimba wimbo huo, huku akionekana kupandisha mzuka, vikundi vya ngoma vilikuwa vikimchagiza kwa midundo sambamba na alivyokuwa akiimba jukwaani kwa zaidi ya dakika tano, huku umati wa wananchi akiwamo Dk. Bilal na mkewe Asha Bilal wakiangua vicheko meza kuu, wasiamini alichokuwa akikifanya Membe.

Baada ya Membe kumaliza kuuimba wimbo huo huku akitokwa jasho, alisema ulikuwa una maana ya kumweleza Dk. Bilal kwamba, yeye ametokea Mtama si Dar es Salaam.

Kwa upande wake Dk. Bilal alivyopanda jukwaani, alianza kwa kubainisha kwamba inamuwia vigumu kuamini Membe yule anayemuona Dar es Salaam, ndiye aliyemuona Mtama akiwa jukwaani akiimba wimbo wa kwao bila kujivunga na kumpongeza kwa kumwimbia wimbo huo, kwani alipata burudani.

Aidha, Dk. Bilal akimnadi mgombea huyo ambaye amepita bila kupingwa jimboni humo, aliwaomba wananchi wa Mtama wampatie kura nyingi mbunge huyo, kwani katika uongozi wake ameweza kusimamia ujenzi wa zahanati kadhaa, ambazo hivi sasa zimeletewa magari ya kubebea wagonjwa, shule, maji safi na salama yanapatikana kwa uhakika jimboni humo.

Mkutano huo wa kampeni kufanyika jimboni hapo, ndiyo ulikuwa wa mwisho kwa Dk. Bilal mkoani Lindi, leo ameanza kampeni mkoani Mtwara.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Agosti 29 mwaka 2010

CCM HAITAAHIDI UONGO-DK.BILAL

Na Happiness Katabazi, Mtwara

MGOMBEA mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Gharib Bilal, amesema chama chake hakipo tayari kutoa ahadi za uongo kwa wananchi katika kampeni zake zinazoendelea hivi sasa ili kipate kura.


Dk. Bilal alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akiwahutubia maelfu ya wananchi katika Uwanja wa Umoja mjini Mtwara ambapo alisema chama chake kitatoa ahadi na kutekeleza yale yaliyo ndani ya uwezo wake na si vinginevyo.

Akihutubia mkutano huo , alisema wapinzani wamekuwa wakijinasibu kwamba wakiingia Ikulu wataleta maendeleo zaidi ya CCM , huku wakibeza maendeleo kiliyoyafanya chama hicho.

“Hivi wana Mtwara, Mtwara ya mwaka 1960 ndiyo Mtwara ya sasa? CCM haiwezi kuahidi jambo isilo na uwezo nalo,” alisema Dk. Bilal.

Mgombea mwenza huyo aliwataka wananchi wa Mtwara wawasikilize viongozi wa CCM kwa umakini mkubwa huku akiwasisitiza kuwa wawasikilize wapinzani kwa nusu sikio na ikiwezekana wasiwasikilize kabisa.

Aliwataka wafuasi wa chama hicho kufanya kampeni za kistaarabu na kuwa watulivu katika kipindi hiki cha kampeni kwani taifa lisipokuwa makini katika Uchaguzi Mkuu nchi inaweza kuingia kwenye machafuko yasiyo ya lazima.

Alibainisha kuwa mifano hai ya madhara ya vurugu za uchaguzi imeonekana kutoka nchi jirani, hivyo ni vema wananchi wakachukua tahadhari mapema.

“Nawaombeni mkimaliza kupiga kura rudini majumbani msubiri matokeo yatangazwe, ni lazima CCM itashinda, nchi yetu inasifika kwa amani na utulivu, tusikubali uchaguzi uwe mwanzo wa mfarakano.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Agosti 29 mwaka 2010

JK,BILAL WAENDELEA KUTOA AHADI

Na Happiness Katabazi

MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete na mgombea mwenza wake, Dk. Mohamed Gharib, wameendelea kutoa ahadi mbalimbali katika mikutano yao ya kampeni.

Akimalizia ziara yake katika Mkoa wa Kagera, Kikwete amewaahidi umeme wa uhakika wakazi wa Ngara na maeneo jirani, kupitia mradi mkubwa unaoshirikisha nchi tatu utakaozalisha megawati 63 kutoka kwenye maporomoko ya Mto Rusumo yaliyopo wilayani humo.

Akizungumza na wakazi wa Ngara mjini, mgombea huyo alisema mradi huo unatarajia kuanza mapema mwakani baada ya taratibu za mwisho za kumpata mkandarasi kukamilika.

Alisema, kupitia mradi huo, tatizo la umeme litamalizika na kuzitaja nchi zitakazonufaika kupitia mradi huo kuwa ni Burundi, Rwanda na Tanzania ambapo kila moja itapata megawati 21 huku akifafanua kwamba umeme huo utaingizwa kwenye gridi ya taifa.

“Huu ni mradi mkubwa ambapo megawati 63 zitakazozalishwa hapo tutagawana… sisi tutapata megawati 21 na wenzetu kila mmoja atapata kama hizo. Napenda kuwa hakikishia ndugu zangu tatizo la umeme litakuwa limemalizika kabisa. Tuchagueni tuendelee kuwaletea maendele.

“Penye umeme maendeleo yapo. Nawaomba msiniangushe, juhudi zetu mmeziona,” alisema Kikwete aliyekuwa akiwahutubia mamia ya wakazi wa Ngara kwenye uwanja wa posta mjini hapa ikiwa ni siku ya tatu na ya mwisho ya mikutano ya kampeni zake mkoani Kagera.

Akizungumzia changamoto za maendeleo zinazoikabili serikali yake kwa upande wa elimu, mgombea huyo alisema mikakati ya kuhakikisha kuwepo kwa walimu wa kutosha inafanyika, ikiwa ni pamoja na kuwapatia ajira wahitimu wote wa fani ya ualimu ngazi ya shahada, wanaomaliza kwenye vyuo binafsi.

Rais Kikwete leo ataanza mikutano ya aina hiyo kwa siku mbili kwenye wilaya mbalimbali za Mkoa wa Kigoma kabla ya kwenda Rukwa.

Kwa upande wake, mgombea mwenza, Dk.Mohamed Gharibu Bilal akiwahutubia mamia ya wananchi wa Manispaa ya Lindi, Halmashauri ya Ruangwa na Liwale, aliwataka wasomi kote nchini kuanzisha utamaduni wa kujenga makazi yaliyo bora ili taifa liweze kupiga hatua katika sekta ya makazi.

“Tunao mpango madhubuti wa kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata makazi bora. Mpango huu upo katika ilani ya ccm na ni imani yangu kuwa wananchi wakimchagua Rais Kikwete katika uchaguzi ujao, basi itakuwa kazi rahisi kwetu kufanikisha azima hii muhimu katika maendeleo ya wananchi wetu,” alisema.

Katika kampeni hizo, Dk. Bilal pia alisisitiza umuhimu wa wananchi kutambua kuwa serikali ya CCM imejipanga vema na kwamba ina kila sababu za kutaka kuwapa maendeleo zaidi ya hapo walipo. Mgombea mwenza huyo bado anaendelea na kampeni katika Mkoa wa Lindi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Agosti 27 mwaka 2010

DK.BILAL AMPOZA MUDHIHIR

Na Happiness Katabazi, Lindi

MGOMBEA mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Garib Mohamed Bilal, amempoza machungu aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Mchinga aliyeangushwa katika kura za maoni, Mudhihir Mudhihir.


Akihutubia mkutano wa kampeni katika Kijiji cha Kilangala mkoani hapa jana, Dk. Bilal hakusita kummwagia sifa mbunge huyo wa zamani kwa ushujaa wake wa kujitokeza na kumuunga mkono mpinzani wake.

Mudhihir amekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa vipindi vitatu, ambapo awali ilidaiwa kudondoshwa kwake kulitokana na kutoelewana kwake na Mbunge wa Mtama, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe.

“Sisi katika CCM hatuna tabu, hata kama kuna vita ndani yetu tunaimaliza baada ya uchaguzi…na kwasababu hiyo makundi yamekwisha, kwahiyo natangaza rasmi kwa moyo mmoja, nitamuunga mkono mgombea ubunge wa sasa na nitahakikisha anapata ushindi wa kishindo,” alisema Mudhihir huku akimalizia hotuba yake kwa kuimba wimbo.

Dk. Bilal alisisitiza kwa kuwataka wanachama wa chama hicho kumaliza makundi haraka iwezekanavyo, alisema siku zote panapokuwepo makundi yanayohasimiana ndani ya chama, ni wazi chama hicho kinaweza mara kwa mara kujikuta kinaingia kwenye migogoro isiyo na tija.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamis, Agosti 26 mwaka 2010