DOWANS YAIPIGA CHENGA SERIKALI

• SASA KUIBANA SERIKALI KILA KONA MPAKA WALIPWE

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE kampuni ya kufua umeme ya Dowans Holdings SA na Dowans Tanzania Ltd zimewasilisha rasmi ombi la kuomba fidia ya sh bilioni 94 isajiliwe katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Fidia hiyo ni ile iliyoamriwa kulipwa na TANESCO kwa kampuni hiyo baada ya shirika hilo la ugavi wa umeme nchini kutiwa hatiani na mahakama ya kimataifa ya usuluhishi migogoro ya kibiashara (ICC), kwa kile kilichoelezwa kuwa ilivunja mkataba baina yake na kampuni hiyo kinyume cha taratibu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana mchana jijini Dar es Salaam, Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Salvatory Bongole, alisema ombi hilo la Dowans dhidi ya TANESCO, liliwasilishwa Januari 25 mwaka huu mahakamani hapo na wakili wa kujitegemea ambaye anaiwakilisha kampuni hiyo, Kennedy Fungamtama.

Bongele alisema ombi hilo limepewa namba 8/2011 na jaji wa kulisikiliza ameshapangwa ingawa tarehe ya kuanza kusikilizwa kwa ombi hilo bado haijapangwa.

“Kimsingi Dowans imeshawasilisha ombi la kuiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam isajili tuzo ya fidia ya sh bilioni 94 waliyoishinda TANESCO katika Mahakama ya ICC…na kweli mahakama imelipokea ombi hilo na kulipatia namba na jaji wa kuanza kuisikiliza…na tuzo hiyo iliwasilishwa hapa Mahakama Kuu na mahakama ya ICC wiki iliyopita.

“Kwa hiyo naomba Watanzania wafahamu kuwa tuzo ya hukumu iliyotolewa na ICC kwa Dowans iliwasilishwa mahakamani hapo wiki iliyopita na iliwasilishwa na mahakama ya ICC yenyewe kwa kuwa huo ndiyo utaratibu wa sheria unavyotaka.

“Na kilichofanywa na Dowans Januari 25 mwaka huu, kupitia wakili wao Fungamtama ni kuwasilisha ombi la kuiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam isajili tuzo yao hiyo …kwa hiyo ieleweke kwamba tuzo ya Dowans bado haijasajiliwa kwani taratibu za kisheria zina kwenda hatua kwa hatua, ”Alisema Bongole.

Hata hivyo, taarifa nyingine za uhakika zinasema kuwa Dowans pia imesajili ombi lao hilo katika mahakama moja nchini Uingereza na kwamba mahakama hiyo inatarajia kutoa notisi ya siku 21 kwa TANESCO kutoa utetezi wake kuhusu kuridhia au kukataa kulipa fidia hiyo.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni mbinu ya tahadhari iliyochukuliwa na kampuni hiyo ili kujihakikishia kuwa inalipwa fidia yake hata kama maamuzi ya mahakama kuu ya hapa nchini yatabatilisha fidia yao waliyotunukiwa na ICC.

“Iwapo mahakama hiyo ya Uingereza itaridhia moja kwa moja kulipwa kwa fidia hiyo na TANESCO ikikataa, basi Dowans watawatumia mawakala wa kitaifa wanaofanya kazi ya kufilisi mali za wadaiwa, ili wakamate mali za serikali ya Tanzania zitakazolingana na thamani ya fidia hiyo ya sh bilioni 94,” alithibitisha zaidi mtoa taarifa wetu.

Tuzo hiyo ya Dowans iliamriwa na ICC Novemba 15 mwaka jana baada ya kampuni hiyo kuishinda TANESCO katika kesi yake ya kudai fidia ya kuvunjiwa mkataba iliyokuwa imefunguliwa rasmi Novemba 20 mwaka 2008 na kupewa namba 15947/VRO.

Tangu ICC itoe hukumu ambayo iliipa ushindi Dowans baadhi ya wananchi, wanasiasa wakiwemo na mawaziri walijitokeza hadharani kuitaka serikali isilipe fidia hiyo kwa madai kuwa kuilipa ni sawa na kuwazawadia mafisadi waliolidanganya taifa tangu ilipoletwa kwa kampuni dada ya Richmond ambayo baadaye ilikujagundulika kuwa ni ya kitapeli.

Hata hivyo, wanasiasa wachache wamekuwa wakiitaka serikali ilipe fidia hiyo kwani kutofanya hivyo ni kukiuka misingi ya utawala wa sheria na mikataba mbalimbali ya kimataifa kuhusu haki za raia na mataifa ambayo Tanzania imeridhia kuiheshimu na kuitekeleza.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Januari 28 mwaka 2011

'NILIKUTA PINGU,MIWANI KWENYE GARI LA MURRO

Na Happiness Katabazi

MKUU wa Upelelezi wa Mkoa wa Ilala, Duani Nyanda, jana ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi alivyopekua gari la Jerry Murro, anayetuhumiwa kuomba rushwa ya sh milioni 10 ambapo alikuta pingu na miwani ya kusomea.


Nyanda ambaye ni Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, ambaye pia ni shahidi wa sita katika kesi hiyo inayomkabili Murro, Kapama na Deo Mgassa, wanaotetewa na mawakili wa kujitegemea Richard Rweyongeza na Majura Magafu, alitoa ushahidi huo akiongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, Stanslaus Boniface, mbele ya Hakimu Gabriel Mirumbe.

Alieleza kuwa Januari 31 mwaka jana saa 12 jioni akiwa ofisini aliamriwa na aliyekuwa Mkuu wake, Charles Mkumbo, kwenda kulipekua gari la Murro lenye namba za usajili T 545 BEH Toyota Cresta lililoegeshwa kwenye viunga vya Kituo Kikuu cha Polisi.

“Baada ya kupewa jukumu hilo nilimchukua Murro ambaye alikuwa ofisini kwa Mkumbo na mashahidi wengine akiwamo Koplo Lugano Mwampeta na waandishi wa habari, nikaenda nao kwenye gari lake lilipokuwa limeegeshwa.

“Baada ya Murro kulifungua nikaanza upekuzi wa gari lile, kwa sababu polisi tulipata malalamiko kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Bagamoyo, Michael Wage, kwamba kuna watu akiwamo Murro walimtishia kwa pingu, bastola na kumwomba rushwa na kwamba Wage alisahau miwani yake katika gari la Murro,” alidai SSP Nyanda.

Nyanda alieleza kuwa katika upekuzi wake alifanikiwa kupata pingu ambazo Wage alizibaini ndizo alizotishiwa nazo na Murro na miwani ya kusomea ambayo anadai ni yake aliisahau kwenye gari hilo Januari 30 mwaka jana na kuongeza kuwa alikuwa na hati ya polisi ambayo Murro na Wage walisaini kuthibitisha kushuhudia upekuzi huo na kuitoa mahakamani kama kielelezo namba tano kilichopokewa.

Pamoja na hati hiyo, pingu na miwani pia vilitolewa mahakamani kama vielelezo namba sita na saba. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 8 na 9 mwaka huu, ambapo shahidi wa saba ataanza kutoa ushahidi wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Januari 27 mwaka 2011

HUKUMU YA MARANDA NA EPA YAIVA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imesema Aprili 29 mwaka huu itatoa hukumu ya kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kwenye Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inayomkabili Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rajabu Maranda na mpwa wake, Farijala Hussein.

Jopo la mahakimu wakazi linaloongozwa na Saul Kinemela, Focus Bambikya na Elvin Mugeta, lilisema limefikia uamuzi huo baada ya wakili wa utetezi Majura Magafu kuiambia mahakama hiyo kuwa wamefunga ushahidi wao na Naibu Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, Stanslaus Boniface na Ben Lincoln kueleza kazi iliyobaki ni kwa mahakama kutoa hukumu yake.

Hakimu Kinemela alisema kesi hiyo ilifunguliwa rasmi Novemba 4 mwaka 2008, jopo hilo limeweza kusikiliza ushahidi uliotolewa na pande zote mbili na kwamba hivi sasa wanaenda kuandaa hukumu yake.

Kwamba kesi hiyo itakuja kutajwa Februari 25 na Aprili 29 mwaka huu, ndiyo jopo hilo litatoa hukumu yake.

Hiyo ndiyo kesi pekee ambayo imekaribia kufikia hatua ya hukumu kuliko kesi nyingine za EPA zilizofunguliwa mfululizo Novemba 4, mwaka 2008.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Januari 27 mwaka 2011

SHAHIDI AFICHUA ALIVYOMKAMATA JERRY MURRO

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa nne wa upande wa Jamhuri katika kesi ya kushawishi na kuomba rushwa ya Sh milioni 10, inayomkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la TBC1, Jerry Murro na wenzake, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Issa Seleman Chabu (37) ameieleza mahakama jinsi yeye na makachero wenzake walivyoweka mtego na kufanikiwa kumkamata Murro Januari 31 mwaka jana.

Chabu ambaye ndiye aliyeongoza timu ya makachero ya kumkamata Murro alitoa ushahidi huo kwa Hakimu Mkazi, Gabrile Mirumbe wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana wakati akiongozwa kutoa ushahidi na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Stanslaus Boniface.Mbali na Murro washtakiwa wengi ni Edmund Kapama na Deo Mugasa

Mpelelezi huyo kutoka ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Ilala alieleza kuwa Januari 30 mwaka jana, saa nne asubuhi akiwa kwenye kazi za nje alipigiwa simu na Station Sajenti Gervas akimwarifu kuwa amepokea taarifa toka kwa Michael Wage kuwa kuna watu wamemtishia kwa silaha na kumwomba rushwa ya sh milioni 10 akanitaka nirudi ofisini.

Alidai kuwa siku hiyo Gervas alikuwa zamu ofisini kwake katika ofisi za RCO-Ilala na yeye akafika ofisini hapo saa nane mchana akamkuta Wage na Gervas wakampatia taarifa za malalamiko hayo kwa kirefu na kuongeza kuwa yeye alifikia uamuzi wa kuwasiliana na Mkuu wake wa kazi-RCO wa Ilala-Duwani Nyanda na kumueleza malalamiko hayo na kwamba mlalamikaji yupo ofisini kwao na kumuomba atupe utaratibu wa kulishughulikia tatizo hilo.

“RCO-Nyanda akanielekeza kwamba nifungue jalada la malalamiko na watuhumiwa wasakwe na wafikishwe kituoni.Na Wage alikuwa akilalamika kuwa kuna watu wawili wamejitambulisha kwake kuwa ni maofisa wawili wa (TAKUKURU )hakuwataja majina na mwingine akamtaja ni Jerry Murro ambaye ni mtangazaji ...na mimi nilitekeleza maagizo kwa kufungua jalada la uchunguzi;

“ Na nikamwelekeza afande Masika achukue maelezo ya Wage na nikamwomba Wage awapigie simu watu hao waliokuwa wakimtisha na kumwomba rushwa na akampigia mmoja wao ambaye alimtaja kuwa ni Murro na simu yake aliiweka kwenye Loud Speaker’ na Wage akamtaka Murro wakutane na Murro akamtaka Wage aje ofisini kwake TBC1 au Bamaga.”alidai Mkaguzi Msaidizi Chabu.

Chabu alidai hata hivyo yeye aliairisha zoezi hilo la Murro kutaka akutane na Wage ofisi za TBC1 na akamwomba RCO-Nyanda zoezi hilo la kuwamata lifanyike kesho yake ombi ambalo lilikubaliwa na mkuu wake wa kazi nakuongeza kuwa Januari 31 mwaka jana,saa nne asubuhi yeye na Wage walitoka katika ofisi za RCO-Ilala na kabla ya kutoka alimwomba Wage awapigie watu hao ili wajue wanakutana nao katika mgahawa wa City Garden.

“Wage akampigia Murro na kumweleza aje amkute katika mhagawa huo ili ampatie mzigo ambao ni sh milioni tisa na Murro akakubali na mimi nikawachukua askari wapelelezi watatu tukafanye mtego katika mgahawa huo na wapelelezi hao ni Station Sajenti Gervas, Sajenti Omary na Koplo Masawe na na tulipofika mimi nilikuwa kiongozi wao na Gervas na Masika niliweka nje ya mgahawa huo na mimi na Gervas tuliingia tuliingia na kukaa ndani ya mgahawa huo saa tano asubuhi;

“Nilipoona Murro atokeo nikamwambia Wage ampigie tena kumwarifu kwamba ameishafika na Wage akampigia huku simu yake ikiwa kwenye Loud Speaker wote tunasikia, Murro akamjibu Wage kuwa anakuja baada ya dakika tano na ndani ya muda huo Murro akafika nje ya mgahawa huo akampigia simu Wage akimtaka atoke nje ya mgahawa ili amkabidhi mzigo huo;

“Wage kabla hajatoka nje nikamkataza asitoke kwanza asubili sisi wapelelezi wawili tuko nje tukawaongezee nguvu wapelelezi wetu wawili tuliowacha nje kwaajili ya mtego, na tulivyotoka na nikamwona Murro akiwa nje ya gari lake amesimama na mimi na wale wapelelezi wenzangu tukapeana ishara zetu za Kiintelijensia na Wage ndiyo akatoka ndani ya mgahawa huo kuja nje na akakutana na Murro ambaye alikuwa akimuita kwa mkono Wage ambaye alikuwa amebeba mkoba ambapo alifungua mlango mwingine wa gari la Murro na kuingia ndani ya gari hilo.

Chabu aliendelea kueleza kuwa baada ya Wage kuingia ndani ya gari la mshatakiwa huyo alifunga mlango haraka na kutaka kuondoka nikamweleza dereva wetu ambaye alikuwa akiendesha gari lenye namba za kiraia akaenda kulizuia gari la Murro ili lisiondoke na ndipo Murro aliposhtuka akamtaka Wage atelemke kwenye gari lake na yakazuka malumbano baina yao wawili na kutokana na hali hiyo yeye alisogea kwenye gari la mshtakiwa huyo na kumuuliza Murro kama alikuwa akimfahamu Wage, mshtakiwa huyo alikana kutomfahamu Wage.

Aidha aliieleza kuwa alimuuliza pia Wage kama alikuwa akimfahamu Murro na Wage alikiri kumfahamu mshtakiwa huyo na kusema kuwa ndiye miongoni mwa aliyemtishia kwa pisto na pingu na kumuomba rushwa y ash milioni 10 na kuongeza kuwa baada ya hapo alijitambulisha kwa Murro kuwa yeye ni ofisa wa polisi na kumweleza kuwa anakabiliwa tuhuma zinazomkabili la na kumtaka afungue gari lake ili yeye na wapelelezi wengine wapande gari lake na aliendeshe kuelekea kituo Kikuu cha Polisi Kati kwa mahojiano zaidi.

“Baada ya kumpa maelezo hayo kwanza Murro alinyamaza akasema haiwezekani kwani katika mgahawa huo yeye alifuatilia habari ya Mchina...nikapanda kiti cha mbele katika gari lake na kumtaka aendeshe gari hadi Kituo cha Kati na alitii amri hiyo na tulipofika nilimwambia afunge gari lake vizuri na anifuatwe kwenye ofisi za RCO-Ilala , tulipofika ofisini nikamuhoji kuhusu tuhuma hizo na alikana na baada ya hapo nikatoa taarifa kwa wakubwa wangu wa kazi kwamba tayari nimeishamata. Shahidi wa sita anaendelea leo kutoa ushahidi wake.

Naye shahidi wa tano wa upande wa Jamhuri, Mkaguzi wa Polisi, Antony Mwita(45) ameeleza kuwa kitabu cha kumbukumbu ya kupokea wageni cha Hoteli ya Sea Cliff kinaonyesha Januari 29 mwaka jana,Murro alifika hotelini hapo siku hiyo.

Mwita ambaye ndiye mpelelezi wa kesi inayomkabili Murro, Edmund Kapama na Deo Mgassa wanaotetewa na mawakili wa kujitegemea Richard Rweyongeza na Majura Magafu, alitoa ushahidi huo kwa Hakimu Mkazi, Gabrile Mirumbe wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana wakati akiongozwa kutoa ushahidi na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Stanslaus Boniface.

Aliieleza mahakama kuwa yeye ni mpelelezi katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZDCO), na kazi zake ni kupeleleza kesi anazokuwa ameelekezwa kuzipeleleza na (ZDCO) na kwamba Januari 31 mwaka jana kiongozi wake alimpa jukumu ya kupeleleza kesi ya kushawishi, kuomba rushwa na washtakiwa kujitambulisha kuwa wao ni maofisa wa serikali huku si kweli inayowakabili washtakiwa.

Mwita alidai Februali 2 hadi 3 mwaka jana, alianza upelelezi wa kesi hii kwa kwenda Hoteli ya Sea Cliff ambapo alipofika kwenye hoteli hiyo aliomba akutanishwe na Meneja wa Teknolojia ya Habari(IT) ili aweze kumpatia picha za kamera za CCTV kutoka kwa meneja huyo kama kweli washtakiwa hao walikutana na shahidi wa tatu(Michael Wage)katika hoteli hiyo siku hiyo ya Januari 29 mwaka jana, akiwemo Murro na wengine.

“Napia kupata maelezo ya mlinzi wa zamu wa siku hiyo Briton Babanyika wa Kampuni ya KK Security na nilichukua maelezo yake na akanipatia kitabu cha kumbukumbu ya wageni walioingia hotelini ambapo kitabu hicho kina majina na namba za magari ya wageni hao;

“Na kitabu hicho kinaonyesha mgeni wa 25 alikuwa ni Jerry Murro na alifika hotelini hapo kwa kutumia gari lake lenye namba za usajili T545 THE aina ya Cresta na mlinzi huyo aliipatia kadi Na.673 na aliingia hotelini hapo saa 7:33 na kuondoka saa 8:48 mchana. ”alidai Mkaguzi Mwita.

Aliendelea kuieleza mahakama kuwa licha ya yeye kukusanya kielelezo hicho cha kitabu pia katika upelelezi wake katika kesi hiyo alienda duka la Mizinga lililopo Upanga jijini, kujiridhisha kama ni kweli Murro alinunua pingu katika duka hilo, na upelelezi wake ulibaini kwamba ni kweli duka hilo lilimuuzia pingu hiyo Mei 26 mwaka 2009 kwa Sh 25,000 na akapewa risiti yenye kumbukumbu na. 34357410. Kwamba mahakama ilipokea risiti ya pingu hiyo kama kielelezo cha nne.Shahidi wa sita anatarajiwa kupanda leo kizimbani kutoa ushahidi wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 26 mwaka 2011.

WAGE AKIRI KUMPA RUSHWA JERRY MURRO

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa watatu upande wa Jamhuri katika kesi ya kuomba rushwa ya sh milioni 10 inayomkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la (TBC1) Jerry Murro, na wenzake Michael Wage amekiri kutoa rushwa ya sh milioni moja baada ya kutishiwa bastola na pingu.


Wage alitoa maelezo hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Gabriel Mirumbe wakati akiongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Boniface Stanslaus.

Alidai kuwa alilazimika kutoa rushwa hiyo kwa sababu alitishwa na Murro na mshtakiwa wa pili Kapama aliyejitambulisha kuwa ni Kaimu Mkurugenzi wa PCCB na mshtakiwa wa tatu Deo Mgassa alijitambulisha kuwa ni msaidizi wa mkurugenzi huyo.

Shahidi huyo ambaye alikuwa mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kabla ya hajasimamishwa kazi na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Januari mwaka jana, alidai kuwa washtakiwa hao wote watatu Januari 31 mwaka jana, katika Hoteli ya Sea Cliff walimtaka awapatie sh milioni 10 ama sivyo wangembambikia kesi kama alivyobambikiwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba, kwa kumwambukiza maradhi mpenzi wa rafiki wa Kapama ndiyo maana akabambikiziwa kesi iliyomfanya ahukumiwe kwenda jela miaka miwili.

Wage aliieleza Mahakama kuwa Januari 28 mwaka jana akiwa nyumbani kwake Bagamoyo alipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa mtangazaji wa TBC1 na hakuwa hakimfahamu, akimtaka kesho yake aje Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano kwani amepata taarifa kuwa anakabiliwa na tuhuma za ufisadi katika Halmashauri ya Bagamoyo.

Katika hilo Wage alieleza kuwa alikubaliana na ombi hilo na Januari 29 mwaka jana, saa tano asubuhi alifikia katika mgahawa wa Califonia ulioko jijini hapa akiwa na dereva wake.

Alisema akiwa njiani alimpigia simu Murro ili aje aungane naye na baada ya dakika chache Murro aliwasili katika mgahawa huo akiwa na gari ndogo na akamweleza watafute meza nyingine ili wakae mbali na dereva wake na walipohamia kwenye meza nyingine ndipo Murro alipoanza kumueleza tuhuma za ufisadi zinazomkabili na kwamba anataka kuzitangaza kwenye kipindi cha Usiku wa Habari kinachorushwa na TBC1.

“Baada ya Murro kunieleza tuhuma hizo akaniambia mahojiano kamili yangefanyika katika Hoteli ya Sea Cliff kwani huko ndiko walikokuwa mabosi wake na kunitaka nimwache dereva wangu kwenye mgahawa huo nikapande gari lake twende nae Sea Cliff na nilifanya kama alivyonielekeza nikapanda na tulipokuwa njiani akampigia simu mtu akawa anazungumza naye na akanitaja jina langu… alivyokata simu nikamuuliza ni kwa nini alikuwa akitaja jina langu akasema alikuwa akizungumza na Kaimu Mkurugenzi wa PCCB (Kapama) naye pia atanihoji.

“Kitu kingine wakati nilipokuwa ndani ya gari hilo tukielekea Sea Cliff, Murro aliniambia yeye ni ofisa wa jeshi na ana nyota tatu na amechukua mafunzo nchini Marekani na Afrika Kusini na ana madaraka ya kunikamata… na baada ya hapo alifungua dashibodi ya gari lake akatoa pingu akaniambia nikimletea vurugu atanifunga na pingu na kisha akanionyeshea bastola pia akaniambia nikifanya vurugu atanifyatulia risasi ili kunidhibiti,” alieleza.

Wage aliendelea kueleza kuwa walipofika tu Hoteli ya Sea Cliff walipokelewa na mtu aliyejitambulisha kuwa ni Kaimu Mkurugenzi wa PCCB, anaitwa Mussa ambapo hata hivyo Wage alimtambua mtu huyo mahakamani kuwa ni Mugassa na akaongeza mtu mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Dokta ambaye Wage jana alimtambua mahakamani kuwa ni Kapama na kuongeza kuwa baada ya hapo mahojiano yakaanza na Dokta akaanza kumueleza kuwa yeye ni fisadi mkubwa na kwamba kama alihitaji msaada wao angesema mapema ili mahojiano yao yasiweze kurushwa kwenye kipindi cha Usiku wa Habari cha TBC1.

“Niliwajibu mimi siyo fisadi; ndipo yule Dokta (mshtakiwa wa pili) akaniambia kuwa hata Liyumba alifungwa jela kwa kuonewa kwani ile kesi ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma, alibambikiziwa kwa kuwa alikuwa akitembea na mpenzi wa rafiki yake anayefanya kazi BoT akamwambukiza maradhi… nilipokea taarifa hiyo kwa mshtuko mkubwa na nikaona wanaweza kunibambika kesi watu hao na siku hiyo nilikuwa na sh milioni moja mfukoni ikabidi nimpatie kiasi hicho cha fedha Kaimu Mkurugenzi wa PCCB (Kapama), mshtakiwa wa pili, ndani ya gari na Murro alikuwa nje ya gari na kuwaahidi kesho yake Januari 31 mwaka jana ningewaletea sh milioni tisa zilizokuwa zimebaki.

“Baada ya kumaliza kuwapatia sh milioni moja, niliingia kwenye gari la Murro akaenda kunishusha mgahawa wa Best Bite na tutakubaliana kesho yake tukutane kwenye mgahawa wa City Garden ulioko mtaa wa Mkwepu… Nikapanda kwenye gari langu nikaenda nyumbani kwangu Bagamoyo nikawaeleza ndugu zangu kuhusu tukio la mimi kutishiwa bastora na kuombwa rushwa; wakaniambia nikatoe taarifa polisi….na kweli Januari 31 mwaka jana, nilivyokuja Dar es Salaam nilifikia moja kwa moja kituo kikuu cha Polisi Kati huku mfukoni nikiwa na sh milioni tisa,” alidai Wage.

Alisema mara baada ya kutoa taarifa hizo polisi wakamtaka ampigie simu Murro na amweleze kuwa tayari ameishafika kwenye mgahawa wa City Garden.

Wage alieleza kuwa alifanya hivyo na baada ya dakika chache Murro aliwasili kwenye mgahawa huo lakini alivyomuona Wage ameambatana na watu wengine watatu alishtuka na polisi waliwahi kuzuia gari lake lisitoke katika viwanja vya mgahawa huo na askari kanzu hao walimwamuru aendeshe gari lake na kulipeleka kituo cha polisi Kati na Murro alitii amri hiyo na wote walifika kituoni hapo.

Alisema Murro alipoulizwa kama alikuwa akimfahamu Wage alikana kumfahamu na polisi hao walipopekuwa gari la Murro walikuta bastola, pingu na miwani ya kusomea ambayo Wage alidai ni yake na aliisahau jana yake wakati alipopanda katika gari hilo wakati anapelekwa Sea Cliff.
Vitu hivyo vyote pingu, bastola na miwani ilipokelewa mahakamani hapo kama utambulisho.

Kwa upande wake wakili wa Murro, Richard Rweyongeza, na Majura Magafu, anayemtetea Kapama na Muggasa akimhoji shahidi huyo alidai kuwa shahidi huyo haoni kwamba Murro alikuwa akitangaza habari za hatari hatari za kuligusa jeshi la polisi na alikuwa akitaka kurusha tuhuma za ufisadi zinazomkabili Wage ndiyo maana alishirikiana na polisi kumbambikizia kesi mteja wake, hoja hiyo ilipingwa vikali na shahidi huyo. Leo shahidi wa nne ataanza kutoa ushahidi wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Januari 25 mwaka 2011

WANYAMBO WAMPIGIA MAGOTI NCHIMBI

Na Happiness Katabazi

WASANII wa vikundi vya ngoma za asili za kabila la Wanyambo wenyeji wa wilaya ya Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera wamemuomba Waziri wa Habari Utamaduni, Vijana na Michezo Emmanuel Nchimbi, kuwatafutia wafadhili ili waweze kuingia studio kurekodi nyimbo zao.


Hayo yalisemwa kwa nyakati tofauti na mkuu wa kikundi cha Makondelee Rwanyango, Salvatory Byarufu, kikundi cha Kihanga Isingiro, Sabinus Leopord, na mkuu wa kikundi cha ngoma sanaa cha Rumanyika Rwantale, Seta Mathias, wakati wakizungumza na waandishi wa habari katika kijiji cha Makumbusho Dar es Salaam, ambapo jana tamasha hilo lilihitimishwa ambalo lilidumu kwa siku tatu.


Mathias alisema wanaamini Nchimbi kwa niaba ya serikali ya awamu nne, wizara yake imebeba jukumu la kuulinda na kuusimamia utamaduni wa makabila ya Tanzania hivyo wanaamini kilio chao atakisikia na kukifanyia kazi kwa karibu.


Alisema Wanyambo kila kukicha wamekuwa wakilalamika kuwa wanabaguliwa na kunyanyaswa na maofisa uhamiaji kwa sababu kabila hilo limekuwa halitambuliwi na watu wengi na kuongeza kuwa makabila mengine yamekuwa yakitambuliwa kwa urahisi kutokana na makabila hayo kuuinua utamaduni wa makabila yao ikiwemo vikundi vya ngoma.


Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Wanyambo, Danile Rutasyamuka, aliishukuru serikali kupitia Idara ya Makumbusho ya Taifa kuwaruhusu kufanya tamasha hilo pia aliwashukuru Wanyambo wote waishio jijini Dar es Salaam na wananchi wa makabila mbalimbali na raia wa kigeni waliojitokeza kuhudhuria tamasha hilo.


Katika hatua nyingine Wanyambo wamemwagia sifa Mkuu wa Wilaya yao, Kanali mstaafu, Fabian Masawe, kwamba ni kiongozi wa kuigwa ambaye anafuatilia kwa karibu matatizo ya wananchi wake.


Walipendekeza kwamba Masawe aendelee kuwa mkuu wao wa wilaya, asihame kwa sababu amekuwa na umuhimu mkubwa kwao, tamasha hilo lilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mohamed Babu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Januari 24 mwaka 2011

NYUMBA YA ASILI KABILA LA WANYAMBO


Hii ni nyumba ya kiasili ya Kabila la Wanyambo ambao ni wenyeji wa Wilaya ya Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera.Nyumba hii imejengwa kwa michango ya Wanyambo waishio jijini Dar es Salaam, ndani ya Kijiji cha Makumbusho,Kijitonyama kwaajili ya matumuzi ya kudumisha mila na desturi la Kabila hilo ambalo Ijumaa ya Januari 21 mwaka 2011, inafanya tamasha la kabila letu la Wanyambo(Picha na Happiness Katabazi)

MSHIKEMSHIKE WA WANYAMBO KIJIJI CHA MAKUMBUSHO LEO

Na Happiness Katabazi

WENYEJI wa Wilaya ya Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera ambao ni Wanyambo,leo wanatarajiwa kuanza tamasha la siku tatu la kuenzi utamaduni wao ikiwa ni katika kunadi mila na desturi zao.

Asili ya jina la kabila hilo limetokana na maana kuwa Mnyambo ni mtu mwenye asili ya eneo la Maziwa Makuu.Pia asili ya jina la kabila hilo limetokana na aina moja wapo ya ndizi inayofahamika kwa jina la Enyambo.

Aidha neno nyambo linamaanisha mtu au kitu au mmea asilia pia yupo ng’ombe wa asili wilayani Karagwe ambaye anajulikana kwa jina la Enyambo linalofahamika katika nchi za Uganda na Rwanda.

Maneno hayo yanatamkwa na Mwenyekiti wa Tamasha la Wanyambo, Revelians Tuluhungwa alipofanya mahojiano na Tanzania Daima mapema wiki hii, kuhusu uzinduzi wa tamasha la Wanyambo litakalo zinduliwa leo na kumalizika Jumapili wiki hii na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.Mohamed Ghalib Bilal katika kijiji cha Makumbusho,Kijitonyama jijini Dar es Salaam.

Anasema jumla ya wanyambo 200 kutoka Karagwe wamekuja kuungana na wanyambo waishio hapa jijini kusherehekea tamasha hilo la kuenzi utamaduni wao.

Anasema Wanyambo wamejiandaa kuonyesha na kueleza mila na desturi za kabila hilo hasa nyumba ya asili, makazi ya Mnyambo iliyojengwa kijijini hapo hivi karibuni ambayo imegharimu zaidi ya Sh. milioni nne, vyakula na vinywaji vyao vya asili, mavazi, nyimbo ,ngoma,kazi za mikono, misemo, majigambo na malezi ya watoto.

Katika makala hii Tuluhungwa anaelezea mazingira ya himaya ya Karagwe na wanyambo kutukuka na kufahamika duniani miaka katika kipindi cha miaka 150 iliyopita na kutofahamika katika Tanzania ya leo sambamba na kupanda na kushuka kwa umaarufu wa kabila hilo.

Tuluhungwa anaeleza historia ya Karagwe kwa kusema himaya ya mfalme wa Karagwe ilikuwa ndiyo utawala mkubwa katika maeneo ya maziwa makuu kwa miaka kama 500 na Bweranyange Mji Mkuu wa Mfalme wa Karagwe ndipo alikaa mfalme Ruhinda wa kwanza, mwanzilishi wa himaya za Kihinda.

Anasema Ruhinda alitawala eneo lote la Karagwe, Ankole, Kihanja, Ihangiro Biharamulo Bushubi na Bugufi Kaskazini ,Akipakana na Bunyoro na mto Mwiruzi Kusini ya Biharamulo na Mkoa wa Kigoma.

Tulungwa ambaye ni mtumishi wa miaka mingi wa Shirila Umoja wa Mataifa la UNICEF, anasema maeneo yote aliyoyataja hapo juu yalitawaliwa na watoto wa Mukama wa Karagwe ambao muda ulipopita walijitenga na kuanzisha tawala huru.Himaya ya mfalme wa Karagwe hiyo ilitukuka na kuandikwa kwenye magazeti ya ulimwengu wakati wa wavumbuzi hususani Uingereza zaidi ya miaka 160.

“Karagwe ilikuwa ndiyo njia pekee ya kufikia utawala wa Buganda kwa wageni wote toka Pwani na Zanzibar .Kati ya Novemba 1861 na Februari 1862 John Hannington Speke na James Grant walikaa miezi mitatu Kafuro jirani na Bweranyange na wakaandika kwa kirefu juu ya mila na desturi za Karagwe chini ya mfalme Rumanyika Orugundu Rzinga Mchuchu wa Nkwanzi ambalo ni jina la utani lenye maana ya shujaa mfuga nywele ndefu mwana wa Nkwanzi. Na kwamba kwa hivi sasa kuna hifadhi ya wanyama ya rumanyika Orugundu kuenzi mtawala huyo ambayo kwa mashariki yake katika kijiji cha Ibamba kunapatikana mto wenye maji moto ya Mutagata”anasema Tuluhungwa.

Kupungua umaarufu wa Karagwe
Tuluhuhungwa anasema kufikia miaka ya 1880 na 1890 wakati wababe duniani wakishindwa kugawana Afrika huko Berlin 1884 na baadaye wakati Zanzibar na Buganda zilikuwa tawala zinazolindwa na mfamle wa Uingereza , Karagwe iliangukiwa na nuksi ambazo zilifika tawala nyingine zote kubwa katika historia kama za Alexander mkubwa utawala wa Kirumi.Ilipungua umaarufu mpaka wakoloni wa kijerumani hawakuitamani na Wamisionari pia waliipita kando na kuongeza kuwa visa vya kuipunguza Karagwe umaarufu vimeandikwa kwa kirefu na marehemu Profesa Katoke katika kitabu chake cha ‘The Making of The karagwe Kingdom’

Anasema awali ilikuwa ni vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vilikuwa vimeanza wakati Speke na Grant wakiwa Karagwe Novemba 1861 mpaka Desemba 1862 Matokeo yake ilikuwa kupungua kwa amani na kuihama Karagwe upande ulioshindwa na kupunguza wingi wa watu.

Pili ugunduzi wa njia fupi toka Mombasa kwenda Uganda kulitoa Karagwe kwenye njia Kuu ya biashara ya kimataifa na kupunguza umaarufu wake.

Magonjwa ya mifugo kama ng’ombe sotoka ilishambulia mifugo ya wakazi wa karagwe katika kipindi hiki na kupunguza utajiri wa Karagwe.Wakoloni walikuwa hawavutiwi na nchi maskini.

Sababu za kisiasa na utawala; Karagwe ilipita kipindi ambacho wafalme walikufa wakiwa wadogo bila kuacha warithi walioishafikia umri wa kutawala ,ikalazimu kutawala kwa kutumia viongozi wa muda kama vile Kakoko waliotawala kwa ukatili na kuharibu himaya.

Matokeo ya kupungua umaarufu
Ni kutopewa kipaumbele katika mipango ya wakoloni wa Kijerumani kulifanya Wamisionari kutovutiwa kuweka vituo vyao Karagwe.

Kwahiyo wamisionari wa Kikatoliki wao walianzisha vituo vyao Kashozi 1892, Bunena 1905, Kagondo na Rubya 1904,Katoke Biharamulo na kuanzisha shule sehemu zote hizo.Misheni ya kwanza Karagwe ilianzishwa 1934 baada ya miaka 40 baada ya kumpata Padri wa kwanza mwafrika wa kwanza Oscar aliyepadrishwa Bukoba 1917.Wa kwanza Karagwe Padri Rwakiboine alipandrishwa 1943 miaka 26 baadaye na shule na hospitali zilifata misheni.

Kupoteza umaarufu
Kama watu wote waliotawaliwa na wageni na kunyanyaswa, kutawaliwa na wageni wa Kihanja chini ya Wajerumani kuliwaathiri kujiheshimu, nakujitambua kama wanyambo.
Kujifunza elimu na dini kwa njia ya kuhemea katika lugha zaidi ya Kinyambo kiliathiri sana Kinyambo,Waumini na wanafunzi walizoea kusikia makatekista na walimu wakifundisha kinyambo kibovu kilichoathiriwa na lafudhi na misemo ya kabila la wahaya.

Bila kutaka wasomi walijikuta wakiathiri matumizi ya lugha yao ya kinyambo kwa jeuri kutokana na wingi wa mashule ya dini, serikali.Jumla ya yote ni kwamba kuanguka umaarufu wa Karagwe ghafla wakati wa kuja kwa ukoloni, kulitekeleza mazingira ya kuathiri kinyambo mpaka wanyambo wenyewe wakawa kama wamemezwa na Wahaya ,kabila ambalo hakukuwepo kabla ya ukoloni.
Leo hii tunapoaadhimisha tamasha la wanyambo, tunasimama kwa ujasiri wao kufanya tamasha hili la siku tatu kuanzia leo na kurudisha mchango wa wanyambo wanaojiamini katika kujenga taifa la Tanzania.

Wanyambo kabila lisilojulikana
Tuluhungwa anasema athari za kutotambulika wanyambo ni nyingi na zinazeondelea kuathiri watanzania wa kinyambo wengi.Taarifa zinajitokeza kila siku wanyambo kubughudhiwa Idara ya Uhamiaji kwa sababu baadhi ya Maofisa wake hawajui kwamba kabila hilo lipo.Ni maombi ya wanyambo kupitia tamasha hili kwamba kubughudhiwa wanyambo kwa kutowajua au kudhihaki wao kama kwamba kabila la wanyambo suyo raia halali nchini ni unyanyasaji usiokubalika na ukomeshwe mara moja.

Kabila la wanyambo ni miongoni mwa makabila makubwa Mkoani Kagera mengine ni Wanyambo wenyewe, wasubi, washubi,wahangaza,wazinga na wahaya.

Wanyambo wengi hawajitambui
Anasema inatia hofu kwamba hata wanyambo wenyewe hasa waishio nje ya Karagwe hawana ufahamu kama wao ni wanyambo au ni wahaya kwa sababu baadhi yao hujitambulisha kama ni wahaya na wanajaribu hata kuigiza lugha yao.

Historia ya Wanyambo haijatafitiwa kwa kina na hivyo hakuna machapisho ya kutosha yanayoelezea historia ya Wanyambo.Yapo machapisho machache sana hasa ya Profesa Katoke na hadithi za wapelelezi kana Hans Mayer ambayo hayako sokoni tena na yaliyopo hayatoshelezi mahitaji.

Anasema mila na desturi za Wanyambo zilizo nje ziko hatarini kutoweka ikiwa ni pamoja na ngoma za asili, nyimbo ,misemo ,majigambo,hadithi na taratibu za maisha nyingi zimetoweka na zilizobaki ziko hatarini kupotea kabisa.

Mfano mzuri ni ngoma ya Amakondere ambayo imebaki ikichezwa na kundi moja tu la wazee waishio Rwanyango ambazo hazijarekodiwa ambapo itakuwa vigumu kuruthishwa kizazi kimoja hadi kingine.

Aidha uwepo wa ngoma ile unategemea sana uhai wa wazee hao hata ala za muziki wa ngoma hizo (Amakondere) hazilimwi tena na huenda mmea huu umeshatoweka kabisa.Kwa upande wa lugha ya wanyambo (Orunyambo) imeanza kupoteza uhalisia wake kutokana na mwingiliano na kutozungumzwa mara kwa mara hivyo huenda ikapotea kabisa.

“Kwa ujumla wanyambwa wanapata usumbufu katika kujitambulisha hasa wanapohitaji baadhi ya huduma katika Wizara ya Mambo ya Ndani kwa sababu hudhaniwa jamii ya wanyambo ni wakimbizi kutoka nchi jirani za Burundi na Rwanda”.

Historia ya Wanyambo
Wanyambo ni kabila lilokuwa miongoni mwa makabila makubwa na yenye nguvu za kivita na kiuchumi.Watu wa kabila hili la wanyambo walikuwa na ufalme ulioongozwa na wafalme Abakama 14 kwa nyakati tofauti.Watu wake ni wakulima na wafugaji.

Historia ya kabila hili ilifahamika ukanda wote wa Ziwa Magharibi Victoria pamoja na nchi za Rwanda na Burundi.Kutokana na uhunzi wa mapambo mengi ya kifalme yalitengenezwa na kuhifadhiwa kwenye ngome ya mfalme.Mapambo hayo yalipendwa na mengine yalichukuliwa na Wajerumani ,walipewa zawadi na Omukama Rumanyika. Kwa ujumla ni kabila lililoheshimika hivyo wanyambo walijivunia Unyambo wao hali iliyoibua misemo kama, Ndyu Munyambo akala nakalenje, Omunyambo agamba echabweine.

Aidha anasema siku ya utamaduni wa Mtanzania ni utaratibu uliobuniwa na Bodi ya Makumbusho ya Taifa chini ya Wizara ya Elimu na Utamaduni mwaka 1994 kabla Makumbusho ya taifa haijahamishwa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kama ilivyo sasa ili kutoa fursa kwa jamii mbalimbali hapa nchini kuonyesha tamaduni zao katika Kijiji cha Makumbusho ,Kijitonyama,Dar es Salaam.

Malengo ya kuwa na siku ya Utamaduni wa Mtanzania
Ni kutoa nafasi kwa jamii moja baada ya nyingine kati ya jamii nyingine tulizonazo kuonyesha mila, desturi na mienendo yao mbalimbali ya jadi ili jamii nyingine ziweze kuelewa na kuthamini utamaduni wa watanzania wenzao.

Kujifunza na kufahamu aina mbali mbali za mila na desturi zinazofaa kudumishwa, kuboreshwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kama utamaduni wa Taifa.

Kufanya Kijiji cha Makumbusho kuwa kielelezo halisi cha maisha ya Watanzania.

Malengo ya kufanya Tamasha la Wanyambo
Kuonyesha mila, desturi na mienendo yao mbalimbali ili Wanyambo wenyewe na jamii nyingine ziweze kuelewa ,kuheshimu na kuthamini Utamaduni wa wanyambo hivyo kukuza uelewano wa kitaifa.
Wanyambo na jamii nyingine zitaweza kujifunza aina mbalimbali za mila na desturi za Wanyambo zinazofaa kudumishwa, kuboreshwa na kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Hali hii itaondoa utata na kupunguza usumbufu pale wanapokuwa wanahitaji huduma muhimu kama vyeti vya kuzaliwa , hati za kusafiria,viza, vitambulisho vya kupiga kura pamoja na nyaraka nyingine muhimu kwani wamekuwa wakipata shida kwa sababu ya kutojulikana kwa kabila lao.

Kuweka mikakati ya kufanya utafiti ili kubaini mila, desturi na tamaduni za Wanyambo zilizo njema na kuzihifadhi kwa njia ya maandishi ili ziweze kurithishwa kizazi hadi kizazi na zitumike kwa manufaa ya jamii nzima.Kila la Kheri Wanyambo.

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Januari 21 mwaka 2011

ZOMBE AIDAI SERIKALI BIL.5/

*Sasa kuishitaki rasmi mahakamani

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Mohamed Zombe, ametangaza rasmi nia yake ya kuishitaki serikali kwa hoja kuwa ilikiuka sheria na Katiba ya nchi wakati ilipomkamata na kumfungulia kesi ya mauaji.
Zombe alikamatwa mwaka 2006 na kufunguliwa kesi ya mauaji ya watu wanne lakini aliishinda serikali katika kesi hiyo.

Uamuzi huo ameutangaza baada ya siku 90 alizotoa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Said Mwema na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kumwomba radhi na kumlipa fidia ya sh bilioni tano kumalizika.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima yaliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, kamishina huyo wa zamani kupitia kwa wakili wake, Richard Rweyongeza, alikabidhi notisi hiyo ya siku 90 kwa IGP Mwema Septemba 27 mwaka jana, akisisitiza atakwenda mahakamani iwapo masharti hayo ya kuombwa radhi na kulipwa fidia hayatatekelezwa.

Alisema siku tisini hizo zilimalizika rasmi Desemba 25 mwaka jana huku IGP Mwema na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiwa hawajamjibu chochote mpaka sasa.

Kwa mujibu wa hati hiyo ambayo gazeti hili linayo nakala yake, Jeshi la Polisi lilikiuka sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 inayotaka kabla ya mtu kukamatwa ni lazima aelezwe anakamatwa kwa sababu gani na akifikishwa kituo cha polisi ni lazima ahojiwe na kuchukuliwa maelezo yake ambayo baadaye hutumika mahakamani kama kielelezo.

Mbali na hilo, Jeshi la Polisi lilikiuka pia haki za msingi za binadamu na Ibara ya 15(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inayosomeka kama ifuatavyo:

“Kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu kuwa huru na kuishi kwa uhuru, itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kukamatwa, kufungwa, kufungiwa, kuwekwa kizuizini, kuhamishwa kwa nguvu au kunyang’anywa uhuru wake vinginevyo, isipokuwa tu-
“(a) Katika hali na kwakufuata utaratibu uliowekwa na sheria.”

Akiongea kwa kujiamini huku akilionyesha gazeti hili hukumu mbalimbali ambazo Mahakama ya Rufaa ilitupilia mbali rufaa zilizokuwa zimekatwa na serikali dhidi ya wananchi walioshinda kesi za mauaji katika mazingira kama aliyoshinda yeye, Zombe alisema serikali kama serikali ni nzuri ila kuna baadhi ya watendaji wana hulka za kinyang’au na hawatimizi wajibu wao kama inavyotakiwa.

“Nafahamu kwamba DPP amekata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Salum Massati, ambayo ilituachilia huru mimi na wenzangu tisa….hilo halinitishi.

“Nimewasilisha hati hiyo ya nia ya kutaka kuwashitaki na hawajanijibu, hivyo imeonyesha wazi wapo tayari kwenda mahakamani, na mimi na wakili tupo tayari na muda wowote kuanzia leo tunakwenda Mahakama Kuu kufungua kesi ya kudai sh bilioni tano ikiwa ni fidia ya usumbufu na kunyanyaswa kipindi kile nilipokuwa nakabiliwa na kesi ile ya mauaji.

“Sasa kitendo cha Jeshi la Polisi kunikamata na kunifikisha mahakamani na kwenda kuishi gerezani kwa miaka minne bila kuhojiwa na polisi, je, si ndiyo lilikiuka sheria na Katiba zilizotungwa na Bunge, ambapo na huyu huyu IGP aliapa kuilinda Katiba hiyo?” alihoji huku akionyesha kukerwa na jambo hilo.

Zombe ambaye kwa sasa anafanya shughuli zake zinazomuingizia kipato huko mkoani Morogoro, alisema anataka hilo liwe fundisho kwa Jeshi la Polisi ambalo baadhi ya askari wake wamekuwa wakikiuka taratibu kwa makusudi na kuonea wananchi wasio na hatia.
Agosti 17, mwaka 2009, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitoa hukumu ya kushtusha baada ya kumwachilia huru Zombe na wenzake wanane waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja.

Serikali ilikata rufaa Oktoba 7 mwaka 2009 katika Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwachilia Zombe na wenzake.

Akisoma hukumu, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati, alisema baada ya kupitia ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo, alibaini kuwa serikali ilishindwa kuthibitisha mashitaka na kuwa kamwe mahakama haiwezi kumhukumu mshitakiwa kwa ushahidi dhaifu na wa kusikia kama uliowasilishwa mahakamani hapo, kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria.

Kwamba washitakiwa hao si wauaji na aliliagiza Jeshi la Polisi liwatafute wauaji halisi wa marehemu wale.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Januari 20 mwaka 2011

WANYAMBO WAWASILI DAR

Na Happiness Katabazi

UJUMBE wa watu 74 wa kabila la Wanyambo kutoka wilaya za Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera jana waliwasili jijini Dar es Salaam kwa ajili kushiriki tamasha la kitaifa la Wanyambo linaloanza Ijumaa wiki hii.


Katibu wa tamasha la Wanyambo taifa, Annamerry Bagenyi, alisema Wanyambo hao waliwasili jana saa 5:00 asubuhi katika Kijiji cha Makumbusho Kijitonyama na basi la RS Investment wakitokea Karagwe na walipokelewa na Wanyambo waishio hapa jijini, ambao pia walitoa burudani ya ngoma kwa waandishi wa habari.

Bagenyi alisema, ujumbe huo umejumuisha madiwani, maofisa wa serikali wa wilaya na mkoa wa Kagera, vikundi vya ngoma za Kinyambo na kuongeza kuwa ujumbe mwingine wa watu 60 unatarajiwa kuwasili leo ukitokea wilaya hizo ambazo ndiko wanakoishi watu wa asili ya kabila hilo hapa nchini.

Aidha alisema ujumbe huo umekuja na vitu vinavyotambulisha uasilia wa Mnyambo ambavyo vitatumika kwenye maonyesho ya tamasha hilo linaloanza Ijumaa na kumalizika Jumapili, ikiwa ni pamoja na mavazi, ngoma na vyakula.

Kila mwaka hapa nchini, Wizara ya Maliasili na Utalii huteua kabila mmoja, kufanya tamasha la kuonyesha utamadani wake kwa niaba ya makabila mengine na kwa mwaka huu, Wanyambo wameteuliwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 19 mwaka 2011

KESI YA MENGI YAPIGWA KALENDA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana ilishindwa kuanza kusikiliza kesi ya kashfa ya madai ya shilingi moja iliyomkabili Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Ltd, Reginald Mengi kutokana na mawakili wa mlalamikaji, Yusuf Manji kutojiandaa.

Hakimu Aloyce Katemana alisema anakubaliana na hoja ya kuarishwa usikilizwaji wa kesi hiyo ambayo ilipangwa kuanza kusikilizwa jana. katika kesi hiyo Manji anawakilishwa na mawakili Mabere Marando, Beatus Malima, Dk. Ringo Tenga na Richard Rweyongeza.

“Nakubaliana na hoja ya mawakili wa mlalamikaji kwamba leo tusianze kusikiliza kesi hii hivyo naihairisha hadi Februali 3-4 mwaka huu, kwani licha ya mawakili hao kutojiandaa pia mimi ni mgeni na kesi hii na jalada lake bado sijalipitia,” alisema Hakimu Mkazi Katemana.

Awali akijibu hoja ya Wakili Marando ya kutaka kesi hiyo isianze kusikilizwa jana kwa madai upande wa madai haukuwa haujajiandaa, wakili wa Mengi, Michael Ngaro alielezwa kushangazwa na ombi hilo kwa sababu mawakili wa mlalamikaji ndiyo waliifungua kesi hiyo Na.85/2009 na kuhoji ni kwanini hawakuwa wamejiandaa.

“Sisi tunashangazwa na ombi la hawa wenzetu wa upande wa mlalamikaji la kutaka usikilizwaji usiendelee…sisi upande wa mdaiwa tupo tayari kuendelea na usikilizwaji wa kesi hii,”alisema Wakili Ngaro.

Mapema mwaka juzi, Yusuf Manji alimfungulia kesi ya madai ya kashfa Mengi na kituo cha televisheni cha ITV akitaka amlipe fidia ya shilingi moja kwa madai kuwa Mengi alitumia televisheni yake kumkashifu kwa kumuita ‘Fisadi Papa’ na kwamba mmoja wa watu wanaopora rasilimali za Tanzania.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 19 mwaka 2011

MABAHARIA KESI YA SAMAKI WA MAGUFULI "HAKIELEWEKI"

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ilisikiliza ombi la dhamana lililowasilishwa mahakamani hapo na upande wa utetezi katika kesi ya uvuvi haramu kwenye ukanda wa Bahari ya Hindi inayowakabili raia 36 wa kigeni.

Ombi hilo liliwasilishwa na mawakili wa utetezi Ibrahim Bendera na John Mapinduzi mbele ya Jaji Radhia Shekhe ambapo waliomba mahakama hiyo iwapatie dhamana wateja wao kwa kuwa mashtaka yanayowakabili yanadhaminika kwa mujibu wa kifungu cha 148 (6) na (7) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.

“Tunaomba mahakama hii iwapatie wateja wetu dhamana hasa ukizingatia wamekaa rumande muda mrefu na makosa yanayowakabili yanadhaminika kwa mujibu wa kifungu hicho ila ni kweli nakili wateja wangu hawana mahali pa kuishi hapa nchini licha kwa sasa wanaishi gerezani,” alidai wakili Mapinduzi.

Kwa upande wake Wakili Mwandamizi wa Serikali Biswalo Mganga alidai kuwa upande wa Jamhuri hauna pingamizi na ombi hilo ingawa wanaiomba mahakama kabla haijakubali ombi hilo izingatie kwamba watuhumiwa hao si raia, hawana vibali vya kuishi nchini na kuendelea kwao kuwa mahabusu ni kwa usalama wa maisha yao pia.

“Tunaomba mahakama hii iwapatie wateja wetu dhamana hasa ukizingatia wamekaa rumande muda mrefu na makosa yanayowakabili yanadhaminika kwa mujibu wa kifungu hicho ila ni kweli nakili wateja wangu hawana mahali pa kuishi hapa nchini licha kwa sasa wanaishi gerezani. ”alidai wakili John Mapinduzi.

Hata hivyo Jaji Shekhe alisikiliza hoja za pande zote mbili na kuahidi kutoa uamuzi wa mahakama hiyo kwa maandishi.

Wakati huo huo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, ililazimika kuairisha usikilizaji wa kesi ya kuomba rushwa ya sh milioni 10 inayomkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji nchini(TBC1), Jerry Murro, na wenzake baada ya wakili wa utetezi Majura Magafu kushindwa kufika mahakamani.

Hakimu Mkazi Gabriel Mirumbe alisema kwa sababu hiyo ameahirisha usikilizwaji wa kesi hiyo hadi Januari 24, 25 na 26 mwaka huu kwa kuwataka wahusika wa pande zote kufika mahakamani.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Januari 18 mwaka 2011

WAKILI:DOWANS ITADHOHOFISHA NCHI


*Afichua mashahidi walioitetea Tanesco Tanesco ICC
*Atoa tahadhari kuhusu msimamo wa Sitta

Na Happiness Katabazi

MMOJA wa mawakili mahiri wa kujitegemea nchini, Kennedy Fungamtama, ameiomba serikali na umma upuuze ushauri wa aliyekuwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta, wa kutaka serikali kukataa kuilipa fidia ya sh bilioni 94 Kampuni ya kuzalisha umeme ya Dowans, kwani ushauri huo unaweza kulidhohofisha taifa kwa kuliingiza katika matatizo makubwa.


Fungamtama aliyasema hayo juzi katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima yaliyofanyika ofisini kwake jijini Dar es Salaam, ikiwa ni muda mfupi baada ya gazeti hili kupata taarifa kuwa wakili huyo ni miongoni mwa wanasheria walioisoma hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Kusuluhisha Migogoro ya Uwekezaji (ICC).


Mwanasheria huyo ambaye alimuelezea Sitta kuwa mtu anayejaribu kucheza na akili za Watanzania, kwa sababu ya kutojua kwao undani wa hukumu ya ICC, alisema endapo serikali itakaidi kulipa fidia hiyo ni wazi taifa linaweza kukabiliwa na madhara makubwa mawili.
Alisema moja ya madhara hayo ni kwa wafadhili kuiweka nchi kwenye orodha ya kunyimwa misaada, kwa sababu ya kutoheshimu sheria na mikataba ya kimataifa ambayo imeridhia.


Wakili huyo alisema madhara mengini ni pamoja na wawekezaji kuingiwa na hofu ya kuja kuwekeza hapa nchini na kuongeza kuwa hilo likitokea taifa ndilo litakalopata hasara na si Waziri Sitta binafsi.


Fungamtama alisema amefikia uamuzi wa kuzungumzia jambo hilo baada ya kuisoma na kujiridhisha kwamba hukumu hiyo yenye kurasa 150 ya kesi namba 15947/VRO kati ya Kampuni ya Dowans na Tanesco ilipokewa na ICC Novemba 20, mwaka 2008 na ikatolewa hukumu Novemba 15 mwaka jana.


Alisema mkataba kati ya Tanesco na Dowans ulisainiwa Juni 23, mwaka 2006 na mkataba huo unajulikana kama ‘Power Off - Take Aggreement (POA)” chini ya kifungu cha 14 (e) cha POA, na kufafanua kwamba pande zote mbili katika mkataba huo zilikubaliana kwamba uamuzi wa Mahakama ya ICC ndio utakuwa wa mwisho na utazibana pande zote mbili na hautaweza kukatiwa rufaa.


Fungamtama alisema kifungu cha 14 (f) cha POA, kinasomeka: “The parties waive any right to challenge or contest the validity or enforceability of this arbitration agreement or any arbitration proceeding or award brought in conformity with this section.”


Kwa tafsiri nyepesi, Fungamtama alisema kifungu hicho kinasema, Tanesco na Dowans katika mkataba wao walikubaliana kwa maandishi kuweka kando haki za kupinga au kuhoji mwenendo na tuzo zitakazotolewa na baraza la usuluhishi.


Alisema Waziri Sitta amenukuliwa na vyombo vya habari akitaka serikali itumie kifungu cha 16 cha Sheria ya Tanzania ya Usuluhishi Sura ya 15 kama ilivyofanyiwa marekebisho ya mwaka 2002, kwamba serikali inaweza kutumia kifungu hicho kutengua hukumu ya mahakama ile ya kimataifa.


“Ni kweli Mahakama Kuu ya Tanzania imepewa mamlaka ya kutengua maamuzi yanayotolewa na mahakama za kimataifa endapo tu itadhihirika kuwapo kwa mambo mawili yafuatayo:


Moja; msuluhishi wakati akiendesha kesi alikuwa akiegemea na kupendelea upande mmoja (arbitrator has miss - conducted himself. Pili: Mazingira ya kufikia uamuzi ule yalitawaliwa na rushwa au shauri lilifikishwa mahakamani bila kufuata taratibu za kisheria (an arbitration or award has been improperly procured).


“Hayo ndiyo mambo mawili peke yake yanayoweza kusababisha Mahakama Kuu ya hapa nchini kutengua hukumu zilizokwisha kutolewa na mahakama za kimataifa za usuluhishi na si kwa jambo jingine lolote.


“Sasa kama Sitta ana ushahidi, vigezo hivyo viwili vya kisheria katika lililokuwa shauri baina ya Dowans na Tanesco kwamba wasuluhishi wale ambao ni majaji waliipendelea Dawans, au walikura rushwa, ingekuwa ni vyema haraka apeleke ushahidi huo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili aweze kuwatuma wanasheria wake wakafungue kesi Mahakama Kuu ili iweze kutengua hukumu hiyo kupitia huo ushahidi wake kama anao na si kama anavyofanya hivi sasa kupayukapayuka kwenye vyombo vya habari,” alisema wakili huyo.


Aidha, alisema kwa mujibu wa kifungu cha 3 cha jedwali la 3 katika Sheria ya Usuluhishi ya Tanzania, Sura ya 15 ya mwaka 2002 kinasomeka hivi:


“Each contract state undertakes to ensure the execution by its authorities and in accordance with the provisions of its national laws of arbitrarily awards made in its own territory under the preceding articles”.


“Kwa tafsiri rahisi, kifungu hicho utaona tayari nchi imejifunga mikono na utekelezaji wa hukumu zinazotolewa na mahakama za kimataifa kwa sababu ni nchi yetu yenyewe imeridhia sheria na mikataba ya kimataifa.”


Alisema kwa hiyo maelezo ya Waziri Sitta ya kutaka Dowans isilipwe, ni kutaka kuishawishi serikali na umma kukaidi kutekeleza maamuzi halali chini ya sheria na mikataba ambayo serikali iliiridhia kuitii na kuitekeleza.


Aidha, alisema jambo jingine lililojitokeza wakati kesi hiyo ikiendelea baina ya Dowans na Tanesco ni Tanesco walitaka kujua wamiliki wa Dowans ni kina nani na Mahakama ya ICC iliona hoja hiyo ya Tanesco ya kutaka kumjua mmiliki haina umuhimu wowote katika mgogoro uliokuwa mbele yao na ikatupilia mbali, kwa sababu iliona hoja hiyo haina maana yoyote mbele yao.


“Kwa hiyo kwa kitendo cha Waziri Sitta kulianzisha suala hilo la kutaka kujua wamiliki wa Dowans wakati hoja hiyo tayari ilikwishatolewa uamuzi na ICC, kisheria hawezi kulianzisha tena jambo hilo la kutaka kujua wamiliki kwa njia anayoitumia ya vyombo vya habari.


“Kwa hiyo maelezo yote yanayoendelea kutolewa kuhusu hukumu hiyo ni kutaka kujinasua katika lawama wakati yeye na baadhi ya maswahiba zake enzi zile akiwa Spika wa Bunge ndio waliokuwa chanzo cha Tanesco kuvunja mkataba na Dowans, hivyo mwisho wa siku shirika hilo la umeme kujikuta likiburuzwa katika korti ya ICC.


“Na ifike mahala wananchi na vyombo vya habari na serikali itoke usingizini na ijiulize maswali yafuatayo kwamba Sitta hakuwepo kwenye usikilizwaji wa shauri hilo? Sitta hakuwa akijua kwamba Tanesco imefunguliwa kesi na Dowans katika Mahakama ya ICC?


“Kwa kuwa Sitta alikuwa mstari wa mbele kuzipiga vita Dowans na Richmond, ni wazi alikuwa akifahamu kwamba Tanesco imeburuzwa mahakamani na kama kweli Sitta ni mzalendo wa kweli na hana chuki binafsi katika hili ni kwanini hayo madai anayoyasema asingeiomba serikali imuweke kama shahidi wa upande wa Tanesco ili akatoe ushahidi anaousema kila kukicha kwenye vyombo vya habari?


“Amesubiri tayari shirika letu la umeme ambalo ndilo lilikuwa mdaiwa katika shauri hili limeshindwa kufurukuta kwenye kesi hiyo na tumetakiwa tulipe kiasi hicho kikubwa cha fidia ndiyo kila kukicha anazungumza kwenye vyombo vya habari kuhusu hukumu hiyo, tena ukitazama maoni anayoyatoa utafikiri si mtu aliyesomea sheria kabisa….naomba sana hasa serikali ipuuze ushauri wa Sitta kwani ni wazi kabisa anataka kuliingiza taifa kwenye matatizo mengine makubwa.


“Watanzania na huyo Waziri Sitta ambao hawajaisoma hukumu ile naomba niwaeleze wazi mimi nimeisoma hukumu hiyo kwa zaidi ya mara saba, kama taifa kupitia hukumu hiyo tumeshikwa pabaya, hivyo hatuwezi kukata rufaa, isipokuwa tu kama tutathibitisha sababu zile mbili nilizozitaja,” alisema wakili Fungamtama.


Aidha, Fungamtama aliviasa baadhi ya vikundi mbalimbali vya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari kuacha kuzungumzia hukumu hiyo ambayo hata wengine hawajawahi kuisoma wala kuiona, kwani tayari kuna baadhi ya waandishi wa habari wamekuwa wakiandika makala kwamba wakati kesi hiyo ikiendeshwa Tanesco haijawahi kuleta shahidi hata mmoja kutoa ushahidi.


Jambo ambalo Fungamtama alisema si kweli na linalenga kuhadaa umma, kwani majibu na nakala ya hukumu hiyo ambayo anayo inaonyesha Tanesco ilipeleka mashahidi watano na walitoa ushahidi wao.


Wakili huyo aliwataja mashahidi hao kuwa ni Subira Wandiba, ambaye ni Mwanasheria wa Tanesco, ambaye pia ni mjumbe wa Bodi ya Zabuni iliyotoa tenda kwa Dowans, Balozi Fulgence Kazaura, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo, aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Dk. Idrisa Rashid, Mhasibu Mkuu wa shirika hilo, Jamhuri Ngeline na Boniface Njombe.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Januari 13 mwaka 2011

TUJENGE KIWANDA CHA KUCHAPA VYETI

Happiness Katabazi

NASHUKURU Mungu kwa kuweza kunipa afya njema hadi siku ya Sikukuu ya Krismasi mwaka huu, nilikuwa nikitimiza umri wa miaka 32. Na pia namshukuru Mungu kwa kunipa uzima hadi nimeweza kuona Mwaka Mpya wa 2011.


Fukuto la Jamii linawapongeza wasomaji wake walioweza kumaliza sikukuu zote salama na kufanikiwa kuuona mwaka mpya na kwamba linawahidi kuwa kwa kipindi cha mwaka huu litaendelea kuwaletea makala moto moto kupitia safu hii.

Leo katika safu hii nitajadili kile kinachodaiwa kuwa ni kero na kinachowarudisha nyuma kitaaluma wanafunzi kwenye baadhi ya vyuo vikuu nchini hasa wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Ardhi na baadhi ya vyuo vingine vya serikali, kuwa ni kero na kinawarudisha nyuma kimaendeleo.

Kero hiyo ni ucheleweshaji wa kutolewa vyeti kwa wahitimu na sababu inayotolewa ni kuwa vyeti hivyo vinatengenezwa nje ya nchi na mara nyingine wahusika wa kuandaa maelezo ya vyeti hivyo hudaiwa kutotimiza wajibu wao kwa wakati.

Kilio hicho kadri siku zinavyozidi kwenda kimekuwa kikizidi kushika kasi na wahitimu wamekuwa wakikichukulia kama ni sehemu ya hujuma na inayokwamisha kupata kazi ndani na nje ya nchi

Fukuto la Jamii kwa takriban miezi miwili sasa, imekuwa ikifanya mawasiliano na baadhi ya wahitimu ambao wamekuwa wakishangazwa na watendaji wa ofisi za umma wanaoshindwa kuwajibika ipasavyo lakini wanaendelea kukalia nyadhifa mbalimbali.

Hoja kubwa wanayoijenga wahitimu hao ni kuwa mbali na kukwazwa katika ajira lakini pia wanashindwa kupata usajili wa kujiunga na vyuo vikuu vingine kwa muda mwafaka wanapotaka kuongeza maarifa zaidi.

Wanaweka wazi kuwa ofisi nyingi wanazopeleka maombi ya kazi na vyuo wanavyoomba kujiunga navyo huhitaji nakala halisi za vyeti na siyo taarifa ya matokeo ya mitihani jambo ambalo limekuwa likikwamisha kutimia kwa ndoto zao za kupata ajira mapema au kujiunga na vyuo husika.

Nimekuwa nikijuliza kuwa inawezekanaje serikali iliyosheheni watalaamu wengi ambao wametumia fedha nyingi kusomea fani za uchapaji na uandaaji wa nyaraka mbalimbali kushindwa kuchapa vyeti hivyo hapa nchini.

Kama serikali imekuwa ikiwasomesha wataalamu wa fani hiyo na nyingine, iweje sasa serikali hiyo hiyo inakubali kuidhinisha fedha nyingine za kutaka vyeti vya wahitimu wao vikatengenezwe nje ya nchi?

Inawezakana nia ya uongozi wa vyuo hivyo ni nzuri ya kufikia uamuzi huo wa kutengenezea vyeti nje ya nje kwa sababu ya kutaka kuwadhibiti wale wanaovighushi ambao binafsi nawaita Manyang'au.

Kwa muda mrefu imekuwa ikiaminika kuwa kutengeneza vyeti nje ya nchi kutadhibiti kughushiwa pamoja na kuwa na ubora mkubwa kuliko vikitengenezwa hapa nchini, jambo hilo sina uhakika nalo ila tunapaswa kuangalia sababu za kuendelea kufanya hivyo.

Nasema tunapaswa kuangalia utaratibu wa kufanya hivyo kwa sababu katika mazingira ya sasa ya maendeleo ya teknolojia vyeti hivyo vinaweza kuchapishwa hapa nchini kwa ubora mkubwa lakini pia kwa gharama nafuu.

Viongozi wa vyuo husika na serikali wanapaswa kujiuliza maswali yafuatayo kwamba; hatuoni wakati umefika kwa sisi kaka nchi kuwa na kiwanda chetu cha kutengenezea vyeti vya wahitimu wetu na vipatikane kwa wakati?

Je, uongozi wa vyuo hivyo vikuu hasa vile vya serikali, havioni ni wakati muafaka kwao kuandika michanganuo na maombi kwa serikali ya kuomba fedha za kununulia vifaa vya uchapaji, mishahara ya watendaji na kujengewa kiwanda?

Nina amini wakati mwingine serikali yetu ni sikivu hasa yanapokuja masuala kama haya kitaaluma. Kama ni serikali yeti imediriki kutoa mikopo kwa wanafunzi wasome japo haikidhi viwango vinavyohitajika, ikakubali kujenga ofisi ya Bodi ya Mikopo na hadi sasa inatoa mishahara kwa watendaji wote wa bodi hiyo, itashindwaje kujenga kiwanda.

Fukuto la Jamii, halitaielewa serikali kama itakatupilia mbali ombi la kujengwa kwa kiwanda cha uchapaji wa vyeti kwa wahitimu wake hapa nchini, endapo uongozi wa vyuo vikuu ikipeleka ombihilo kwa kufuata taratibu zote.

Nalazimika kuamini kwamba serikali haiwezi kukataa ombi hilo na kuidhinisha fedha za uanzishwa wa kiwanda hicho kwa sababu kitasaidia kuongeza ajira kwa Watanzania lakini pia kupunguza gharama za kusafirishia vyeti hivyo.

Kwani ni nyaraka ngapi za siria za serikali yetu zimekuwa zikichapwa na Ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali? Mbona nyaraka hizi bado zimeendelea kuwa ni siri na hazivuji wala wala kughushiwa na Manyang'au?

Ni lazima tukubali kuwa mambo mengi tunayoyaoana hivi sasa ndani ya nchi yetu yamesababishwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa maadili pamoja na utoaji wa ajili usiozingatia umakini mkubwa.

Katika ofisi za umma na kule mitaani tumekuwa na mabingwa wa kughushi saini, vyeti, hundi, hati na vinginevyo ambao wanajulikana lakini kwa sababu ya kuporomoka kwa maadili au kulindana watu hao hatuwafikishi kwenye vyombo vya sheria.

Ninamini serikali yetu ina macho na mkono mrefu wa kuwatambua wanaofanywa uovu huo, natarajia inaweza kuwatumia watendaji wake kuwakamata na kuwachukulia hatua waharibifu wa sekta yetu ya elimu.

Katika mazingira ya kawaida watu wanaoghushi vyeti mbali na kuporomosha kiwango cha elimu lakini pia ni hatari kwani wanapoajiriwa hushindwa kutimiza matakwa husika kwa sababu wao si wabobea kwenye sekta husika.

Ila kama hao wataalamu wetu walivyokuwa vyuoni hawakuwa wakisoma vizuri na wakawa wanatazamia na kuiba mitihani kipindi cha mitihani, ni wazi kabisa hawatakuwa na mbinu ya kitaaluma ya kudhibiti vyeti hivyo vikichapwa hapa visigushiwe na matapeli wa mjini ambao hawa ni wataalamu wa kughushi saini za mtu yoyote walichoshindwa kughushi ni saini Mungu kwasababu bado hawajaona mfano wa saini ya Mungu.

Ikumbukwe kuwa moja ya kauli mbiu ya serikali ya awamu ya nne ilivyokuwa ikiingia madarakani mwaka 2005 chini ya Rais Jakaya Kikwete, ilisema itatoa ajira kwa wananchi wake, sasa inapotokea baadhi ya wahitimu wa vyuo vinavyomilikuwa na serikali hiyo hiyo vinachelewa kutoa vyeti na matokeo yake wahitimu wanakosa ajira kwa sababu ya maofisa walioomba ajira hizo wanasema ili wawape ajira ni lazima wawe na vyeti halisi.

Je tukisema uchelewaji wa kupatikana kwa vyeti hivyo vya wahitimu, kuna kwaza utekelezaji wa sera ya ajira kwa wasomi wetu tutakuwa tunakosea?

Aidha nataka nikumbushe uongozi wa vyuo vikuu vyetu kuwa kule ughaibuni mnakokimbilia kupeleka majina ya wahitimu wetu kuwatengenezea vyeti vyao, kwamba serikali za nchi hizo zilijifunga vibwebwe kuwasomesha wananchi wake hadi wakapata utaalamu huo na pia walikaa chini wakafikiri sana ndiyo maana wakaibuka na mitambo na vifaa vya kutengenezea vyeti hivyo vyenye ubora.

Sasa kila kukicha tunaambiwa nchi yetu imepiga hatua za kimaendeleo na wasomi wengi ukilinganisha na kipindi kile taifa limetoka kupata uhuru, sasa hao wasomi wanashindwa kufanya mkakati wa kuikaba koo serikali ili iweze kujenga kiwanda cha kuchapa vyeti hapa nchini?
Au wasomi wetu wanachojua hivi sasa ni kuandika tafiti mbalimbali (reseach)kwenye mashirika ya kimataifa yanashughulikia ugonjwa ukimwi, mazingira n.k. ili wajipatie fedha binafsi chap chap?

Wasomi wetu sasa wamegeuza faida ya elimu waliyonayo ni yao binafsi badala ya elimu yao iwe faida kwa taifa?

Kwani haiingii akilini kabisa kama Katiba ya Nchi, sheria za nchi mbalimbali na nyaraka nyingine za serikali zinachapwa hapa nchini halafu linapofika suala la kuchapa vyeti vya vyuo vikuu au mitihani ndiyo ikachapwe nje ya nchi.

Hata hii mantiki kwamba huenda vyeti hivyo kuchapwa nje ya nchi ni kudhibiti vyeti kughushiwa, hainiingii akilini kwani dunia ya sasa ni kijiji na hao waliopewa jukumu la kuitengeza vyeti huko nje ya nchi ni binadamu wenzetu na kama siyo waamini wanaweza kula njama na wananchi wa Tanzania na wakajikuta wanaingia kwenye 'dili' chafu ya kutengeneza vyeti feki.

Au wakati vyeti hivyo vinasafirishwa kuletwa nchini vinaweza kuporwa na majambazi pale uwanja wa ndege kama fedha zinazodaiwa kuwa ni Benki Kuu, zilivyoripotiwa kuibwa na jambazi pale uwanja wa ndege Dar es Salaam.

Lakini yote hayo hatuyaombei yatokee ila Fukuto la Jamii linatoa angalizo kwamba wakati umefika wa Taifa letu kuwa na kiwanda cha kuchapa vyeti vya wasomi wake.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Januari 2 mwaka 2011