TAKUKURU NI MAAMUMA WA SHERIA?

Na Happiness Katabazi

HUENDA ule utabiri ‘bubu’ uliokuwa ukitolewa na baadhi ya wananchi kwamba zile kesi za rushwa zilizokufunguliwa ‘chapuchapu’ kwa mbwembwe na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) dhidi ya baadhi ya waliokuwa wagombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM )katika kura za maoni mwaka 2010 ni kiini macho.


Sote bado tunakumbuka kwamba miongoni mwa Wana CCM walioburuzwa mahakamani na Takukuru kwa kudaiwa kutoa rushwa ili majina yao yapitishwe kwenye uchaguzi wa ndani ya chama chao ni aliyekuwa waziri na mbunge wa muda mrefu, Joseph Mungai na Katibu Mkuu wa (TFF), mgombea ubunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Fredrick Mwakalebela.

Awali Wakili wa Takukuru, Imani Mizizi, mbele ya Hakimu Mkazi, Festo Lwiza wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa, alidai Juni 20 mwaka jana, Mwakalebela alitoa hongo ya sh 100,000 kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkoga, Hamis Luhanga, ili awagaie wajumbe 30 wa CCM, walioitwa kwenye kikao hicho cha kujipanga kupiga kura za maoni.

Mwanasheria alidai mshitakiwa huyo alitenda kosa kinyume cha Sheria ya Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007, kifungu cha 15(1),(b),kinachosomeka pamoja na sheria ya gharama za uchaguzi namba 6 ya mwaka 2010, kifungu cha 21(1),(a) na kifungu cha 24(8).

Hivi karibuni tumeisikia Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa kwa wakati tofauti ikitoa amri ya kuwafutia kesi washitakiwa kwa maelezo kwamba hati za mashitaka zimeonekana kuwa na dosari za kisheria. Hati hizo ziliandaliwa na mawakili wa taasisi hiyo.

Washitakiwa walishitakiwa kwa kutumia sheria mbili tofauti kwenye hati moja ya mashitaka, kitu ambacho ni kinyume cha sheria na kinaweza kusababisha washitakiwa washindwe kuandaa utetezi wao.

Kwa muktadha huo hapo juu, sasa tunaweza kuona ule utabiri umetimia, kwani hata wahenga walisema: “Lisemwalo lipo na kama halipo lina kuja.”

Na kwa washitakiwa hao wawili kuachiliwa na mahakama ni wazi msemo huo wa wahenga umetimia.

Takukuru ndiyo chombo chetu ambacho moja ya majukumu tuliyowakabidhi ni kuchunguza, kuzuia na kupambana na rushwa na hivi sasa kina mawakili wake ambao hufika mahakamani kuendesha kesi zinazohusiana na rushwa.

Na Watanzania ndio tumeridhia tuwe na chombo hicho kwa kuhakikisha taifa letu linamtokomeza mdudu rushwa kwasababu ni adui wa haki.

Hivyo, kitendo cha baadhi ya mawakili wa Takukuru walioshiriki kuandaa hati hizo mbili za mashitaka dhidi ya Mungai na Mwakalebela na kubainika hati hizo zimeandaliwa ovyo, ndiko kumenisukuma kuandika mtazamo huu na kuinyoshea kidole taasisi hiyo.

Kisheria upande wa Jamhuri wanaruhusiwa muda wowote kuzifanyia mabadiliko hati zao za mashitaka pindi inapobainika kisheria.

Watanzania tujiulize, hivi umakini wa wanasheria wa Takukuru katika mashauri hayo uko wapi?
Haiingii akilini kabisa, Rais Jakaya Kikwete ambaye alisaini kwa haraka Sheria ya Gharama za Uchaguzi 2010 na kuiagiza taasisi hiyo iwashughulikie bila aibu wanasiasa wote hata wa CCM wanaotoa rushwa kwenye uchaguzi, halafu hawa mawakili wa taasisi hiyo washindwe kuwa makini katika kuandaa hati za mashitaka na mwisho wa siku watuhumiwa wanaachiwa na mahakama!

Tujiulize, mawakili hao ni ‘maamuma’ na ‘mbumbumbu’ wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010?

Au taasisi hiyo iliamua kuwafungulia kesi hizo ili kumuhadaa Rais Kikwete kwamba ile sheria aliyoisaini pale Ikulu ndiyo imeanza kutumika, huku mawakili wa taasisi hiyo wakiwa wameandaa madudu katika hati hizo za mashitaka?

Kwa hiyo wananchi tumtegemee tena kumsikia Ofisa Uhusiano wa Takukuru, wiki hii kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kwamba licha mahakama kumwachia Mwakalebela, taasisi yake itamshitaki tena, kwani tungali tukikumbuka kwamba hata alipoachiwa Mungai ofisa habari huyo alisema maneno hayo ambayo kwa watu wenye akili timamu kama sisi na tunajua kinachoendelea, tunaishia kupata kichefuchefu na hasira.

Vyovyote iwavyo, ninapenda kuwaasa hasa mawakili wa serikali hususan nyie mawakili na wachunguzi wa Takukuru, tumieni taaluma zenu vizuri na kwa haki, kwa masilahi ya taifa letu na si kwa lengo la kuwafurahisha baadhi ya wanasiasa wenye hulka za kinyang’au au watu wenye nguvu ya fedha na madaraka kuwaumiza wananchi ambao wana ugomvi wao binafsi.

Kumbukeni vyeo na taaluma mlizonazo ni dhamana, kwa hiyo baadhi yenu kwa makusudi mnavyoamua kutumia vyeo au taaluma zenu kuwaumiza wananchi, ipo siku Mungu atawalipa mshahara wa dhambi.

Nasema haya kwa uchungu, kwani nina miaka 12 sasa ya kuripoti habari za mahakamani, nimeshuhudia na ninaendelea kujifunza mambo mengi, kwamba kuna baadhi ya wananchi wenzetu wanafikishwa mahakamani kwa kubambikiwa kesi, ingawa kuna wanaofikishwa kihalali.

Kwa mtazamo wangu, ni vema mawakili wa Takukuru kuwa makini katika uandaaji wa hati za mashitaka na uendeshaji wa kesi zake, kwani kubainika kwa hati hizo mbili kuwa na dosari ni wazi kunachangia kuporomosha heshima ya taasisi hiyo na ndugu wa washitakiwa wataanza kujenga chuki dhidi ya taasisi hiyo na serikali yetu. Hatutaki tufike huko.

Mungu ibariki Afrika, Mungu ibariki Tanzania.

0716- 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi Mosi mwaka 2011.

MSHTAKIWA KESI YA SAMAKI ALIDANGANYA MAHAKAMA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imesema kwamba mshtakiwa 19 Jakson Sirytoya katika kesi ya Uvuvi haramu kwenye Ukanda wa Bahari ya Hindi maarufu ‘Kesi ya Samaki wa Magufuli’ ni muongo na ameidanganya mahakama hiyo.

Hayo yalisemwa na Jaji Radhia Sheikh jana wakati akitoa uamuzi wake katika kesi ndani ya kesi(Trial within a Trial) ambapo alisema anakubaliana na hoja za Wakili wa Serikali Mwandamizi Biswalo Mganga zilizoiomba mahakama hii itupilie mbali hoja za mawakili wa mshtakiwa huyo kwasababu ni za uongo.

Jaji Sheikh alisema amefikia uamuzi huo wa kutupilia mbali pingamizi la mawakili wa mshtakiwa huyo Ibrahimu Bendera na John Mapinduzi lilotaka mahakama hiyo isipokee ungamo la mshtakiwa huyo(Sirytoya) ambaye ni raia wa Kenya kwasababu mshtakiwa huyo tangu akamatwe hakuwahi kuchukuliwa maelezo ya ungamo na kwamba maelezo hayo ya ungamo yaliyotolewa na upande wa Jamhuri na kupokelewa kama utambulisho namba moja hakuyatoa kwa ridhaa yake kwani alitishwa na Inspekta Antony Mwita.

Alisema mahakama hiyo baada ya kuendesha kesi ndani ya kesi ilipata fursa ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande mbili na kusikiliza ushahidi wa Jamhuri, Inspekta Mwita ambaye ndiye aliyeandaa ungamo la mshtakiwa na pia ilisikiliza ushahidi wa shahidi wa utetezi ambaye ni mshtakiwa mwenyewe na mahakama hii ikabaini yafuatayo:

“Shahidi wa utetezi ambaye ndiye mshtakiwa wa kwanza Sirytoya alitoa maelezo ya uongo kwani wakati akitoa ushahidi wake alisema hajawahi kuhojiwa na polisi na mara akasema maelezo hayo ya ungamo aliyatoa si kwa ridhaa yake kwani alitishwa na mara akasema kwamba Inspekta Mwita alikuwa akimhoji kirafiki, na kwamba alikuwa hafamu kusoma na kuandika hata jina lake;

‘Lakini wakati siku Jamhuri inawasomea maelezo ya awali washtakiwa hao mahakamani ambapo maelezo hayo yaliandikwa kwa lugha ya Kiingereza, mshtakiwa huyo alipewa maelezo hayo ili aweze kusaini maelezo anayoyakubali na anayoyakataa na mshtakiwa huyo aliweza kulisoma jina lake na akaweka saini ;

“Pia mahakama ilitafakari sababu hizo mbili za mshtakiwa zilizotaka tusipokee ungamo hilo kama kielelezo kwasababu eti hajawahi kuungama na ungamo hilo hakulitoa kwa ridhaa yake……Nilijiuliza kama mshtakiwa huyu anadai hakuwa kuungama polisi hii hoja yake nyingine ya kwamba ungamo hilo hakulitoa kwa ridhaa yake kwani alitishwa na polisi inatoka wapi?

“Hivyo basi kwa maelezo hayo juu mahakama hii inatamka wazi kwamba mshtakiwa huyo alitoa ushahidi wa uongo katika kesi ndani ya kesi mbele ya mahakama hii, na mahakama hii imejiridhisha kwamba mshtakiwa alipewa haki zote wakati anachukuliwa ungamo na Inspekta Mwita na kwamba ni kweli ungamo lile ni lake na wala hakutishwa hakutishwa kama anavyodai na kwamba ungamo hilo limezingatia matakwa yote ya kisheria na kwamba pingamizi hilo la mshtakiwa la kutaka ungamo hilo lisipokelewe nalitupilia mbali na ninalipokea ungamo hilo kama utambulisho namba moja katika kesi hii”alisema Jaji Sheikh.

Wakati huo huo Jaji Sheikh amesema Machi 3 mwaka huu, atatoa uamuzi wa kujitoa au kutojitoa kusikiliza kesi hiyo.

Uamuzi huo unafuatia ombi la washatkiwa 34 ambao ni raia wa kigeni katika kesi hiyo kupitia mawakili wao ,Ijumaa iliyopita kuomba Jaji huyo ajitoe kwasababu hawana imani na yeye.

Ombi hilo la kumtaka jaji Sheikh ajitoe ulikuja saa chache baada ya jaji huyo kutoa uamuzi wa kuwanyima dhamana licha ya kifungu cha 148 (6) na (7) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, makosa yanayowakabili washtakiwa kuwa na dhamana ambapo alisema mahakama hiyo imetumia mamlaka yake kuwanyima dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi Mosi mwaka 2011.

KESI YA MPENDAZOE,MAHANGA HAKIELEWEKI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Machi 8 mwaka huu itatoa uamuzi wa kulikubali au kulikataa ombi la aliyekuwa mgombea Ubunge wa Segerea, Fred Mpendazoe (Chadema) la kutaka aruhusiwe kuweka sh milioni 15 mahakamani kama dhamana.

Dhamana hiyo ni sh milioni tano kwa kila mdaiwa ambapo wadaiwa katika kesi hiyo ni Mbunge wa Segerea na Naibu Waziri wa Kazi na Ajira Dk. Makongoro Mahanga (CCM), Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi anazotakiwa kuzitoa kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2002.

Katika kesi ya msingi Mpendazoe anapinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 jimbo la Segerea yaliyomtangaza Dk. Mahanga kuwa mbunge.

Baada ya Jaji Profesa Ibrahimu Juma kusikiliza ombi la mlalamikaji na pingazimi la mawakili wa wadaiwa lililotaka ombi hilo litupwe, amesema atatoa uamuzi wa ama kukubali au kukataa ombi la Mpendazoe Machi 8.

Awali Wakili wa mlalamikaji Peter Kibatala aliiambia Mahakama kuwa wamekuja na ombi jipya la kuomba mteja wake aruhusiwe kuweka kiasi hicho cha fedha kwani tayari mteja amepata kiasi hicho cha fedha.

Hata hivyo wakili wa wadaiwa hao Jerome Msemwa alilipinga ombi hilo na kuiomba Mahakama isimruhusu hadi pale mlalamikaji atakapopeleka ombi rasmi mahakamani la kuiomba impangie kiwango cha kuweka mahakamani hapo.

Wakili Msemwa aliongeza kuwa kifungu cha 111(3) cha Sheria ya Uchaguzi kinamtaka mwombaji anayeiomba mahakama imsamehe kulipa dhamana hiyo au kumpunguzia kiwango cha kulipa, anatakiwa awasilishe ombi hilo ndani ya siku 14 tangu alipofungua kesi ya msingi ya kupinga matokeo ya Ubunge.

Akipangua hoja hiyo wakili wa Mpendazoe, Kibatala aliambia kuwa kifungu hicho kilichotumiwa na Msemwa hakiendani na ombi lao waliloliwasilisha kwa kuwa ombi lao ni Mahakama imruhusu aweke kiasi hicho cha fedha na si vinginevyo.

Februali 15 mwaka huu, Jaji Juma alitupilia mbali ombi la Mpendazoe la kuitaka Mahakama hiyo imsamehe kulipa fedha hizo kwa sababu hana uwezo wa kupata fedha hizo na kwamba amebaini hati ya kiapo cha maombi hayo kina dosari za kisheria.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi Mosi mwaka 2011.

KUMBUKUMBU:MATTHEW DOUGLAS RAMADHANI


Mwalimu Matthew Douglas Ramadhani, leo unatimiza miaka 50 tangu ulipotuacha Machi,mosi , 1961, kwa ajali ya treni katika kituo cha Guidebridge, Ashton-under-Lyne nchini Uingereza.

Alizaliwa Septemba 11 mwaka 1915.Unakumbukwa na wanao wapendwa Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Agustino Ramadhani, Marina,Henry,Mody, Mary na Bright.


Wakati tukikumbuka kifo chako , Ibada inafanyika leo katika Kanisa Kuu la Anglikana la Watakatifu Wote, Vinghawe, Mpwapwa, ambapo kiti cha Askofu na viti vya Makanoni vitanzinduliwa kwa ukumbusho wake.

MUNGU AIWEKE ROHO YAKE PEMA PEPONI. AMINA.

KESI YA SAMAKI WA MAGUFULI:WASHTAKIWA WAMKATAA JAJI

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE raia 34 wa kigeni wanaokabiliwa na kesi ya uvuvi haramu kwenye ukanda wa Bahari ya Hindi maarufu “Kesi ya Samaki wa Magufuli’ jana waligeuka mbogo na kumuomba Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Radhia Sheikh, ajitoe kusikiliza kesi hiyo kwa sababu hawana imani naye.

Ombi hilo liliwasilishwa na mawakili wa washtakiwa hao, John Mapinduzi na Ibrahimu Bendera, mahakamani hapo ikiwa ni saa chache baada ya jaji huyo kutoa uamuzi wa kuwanyima dhamana licha ya kifungu cha 148 (6) na (7) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, makosa yanayowakabili washtakiwa kuwa na dhamana.

Sababu ya jaji huyo kuwanyima dhamana ni kwamba mazingira ya kesi hiyo washtakiwa wakipewa dhamana wanaweza wakaruka.

“Wateja wangu wamenieleza kuwa hawana kabisa imani na wewe na wanaomba ujitoe uongozi wa mahakama umpange jaji mwingine kwa sababu wanaamini dhamana ni haki yao.

“Wateja wangu wamenieleza kwamba kilichowashtua zaidi ni kwamba mapema mwaka jana jaji wa mahakama hii, Njegafibili Mwaikugile, alishatoa masharti ya dhamana kwa wateja wangu na ambapo wateja wangu walikimbilia Mahakama ya Rufani na jopo la majaji wa rufani watatu waliokuwa wakiongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Agustino Ramadhan liliamuru ombi hilo la washtakiwa la kutaka wapatiwe waliwasilishe Mahakama Kuu na mahakama hiyo isikilize ombi hilo.

“Mimi pamoja na wateja wangu tulitekeleza amri ya Mahakama ya Rufani na ndipo tukaleta upya ombi la dhamana mbele yako na Januari 17 mwaka huu, ukalisikiliza…lakini cha ajabu leo umetoa uamuzi wa kuwanyima dhamana wateja wangu wakati Jaji Mwaikugile wa mahakama hii alishatoa masharti ya dhamana …,” alidai Mapinduzi.

Alieleza kuwa sababu nyingine iliyowashangaza wateja wake na kufikia hatua ya kumkataa jaji huyo ni kwamba katika uamuzi wake huo wa maombi ya dhamana amewataja washtakiwa ni wahamiaji haramu na kwamba hawana hati za kusafiria.

Wakili Mapinduzi alidai kuwa maneno hayo ya jaji, wateja wake wamesema hayana ukweli wowote kwani kuna baadhi ya washtakiwa wana hati za kusafiria na zimegongwa mhuri wa serikali ya Tanzania na kwamba wao hawakuwa na mpango wa kuja kuishi hapa nchini isipokuwa walikuwa wakipita njia na ndipo walipokamatwa na katika Bahari ya Hindi eneo la Tanzania.

Aidha Mapinduzi alidai wateja wake wamesema katika hati ya kiapo iliyowasilishwa hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kwamba wakipewa dhamana wanaweza kuruka dhamana na kwamba kesi hiyo imechukua muda mrefu kumalizika na kwamba jaji huyo amekuwa akiichelewesha kwa makusudi.

Alisema kuchelewesha huko kwa kesi kumesababisha wateja wake kuendelea kusota rumande kwa muda mrefu tangu Machi 8, 2009.

Mapema jana asubuhi Jaji Shekhe akitoa uamuzi wake kuhusu ombi la kupatiwa dhamana washtakiwa hao ambalo liliwasilishwa mahakamani hapo na washtakiwa, alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili katika ombi hilo Januari 17 mwaka huu, alisema kwa mujibu wa sheria ya Makosa ya Jinai ,washtakiwa wana haki ya kupata dhamana ila tu kwa mazingira ya kesi hiyo mahakama hiyo imetumia mamlaka yake kuwanyima dhamana washtakiwa hao kwa sababu ilifikiria mambo yafuatayo:

Jaji Sheikhe alisema kabla ya kufikia uamuzi huo mahakama ilijiuliza kuwa washtakiwa wanakabiliwa na makosa ambayo yana adhabu kali, alisema kosa la kwanza ni la uvuvi haramu ambalo adhabu yake ni jela miaka 20 au faini ya sh bilioni tano.

Alisema kosa la pili ni uharibifu wa mazingira katika Bahari ya Hindi na endapo watapatikana na hatia watatumikia kifungo cha miaka 10 au kulipa faini ya sh bilioni tano na kosa la tatu ni kusaidia kutendeka kwa kosa ambalo kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi katika Kina kirefu cha Bahari ni miaka saba jela.

“Pia mahakama hii kabla ya kufikia kutoa uamuzi huo ilijiuliza kuwa washtakiwa wote ni wahamiaji haramu, hawana vibali vya kuishi hivyo endapo watapewa dhamana je hawawezi kuruka dhamana? Pia mahakama hii haikuona haja ya kutoa amri kwa Idara ya Uhamiaji ya hapa nchini itoe vibali kwa kuishi kwa washtakiwa hao ….kwa hiyo basi mahakama kwa kutumia mamlaka yake licha makosa yanayowakabili yanadhaminika kwa mujibu wa sheria ila kwa mazingira ya kesi mahakama inakataa kuwapatia dhamana washtakiwa,” alisema Jaji Shekhe.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi Februali 26 mwaka 2011.

SHAHIDI AELEZA ALIVYOITILIA SHAKA DECI

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA meneja wa Benki ya Afrika(BOA) Tawi la Sinza, Godliving Maro ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa benki yake ilifikia uamuzi wa kuifunga ya akaunti ya washtakiwa ambao ndiyo walikuwa viongozi wa Taasisi ya Entrepreneurship for Community Initiative(DECI), kwasababu ilipokea amri ya kufanya hivyo toka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Washitakiwa katika kesi hiyo ni Jackson Mtares, Dominic Kisendi, Timotheo ole Loitgimnye, Samuel Mtares, Arbogast Kipilimba na Samuel Mtalis, ambao wanadaiwa kuendesha na kusimamia mradi wa upatu kinyume na sheria pamoja na kupokea amana za umma bila leseni.
Maro ambaye ni shahidi wa tano wa Jamhuri alikuwa akiongozwa na Wakili wa Serikali Prosper Mwangamila na Zuberi Mkakati kutoa ushahidi wake mbele ya hakimu Mkazi Stewart Sanga ambapo alidai kuwa majukumu yake katika benki hiyo ni kuakiki nyaraka za wateja walizozitumia kufungulia akaunti zinaendana na matakwa ya benki na pia kutazama nyendo za fedha zinazoingia na kutoka kwenye akaunti za wateja wao.

Maro alidai yeye akiwa na majukumu hayo mwaka 2009 alishiriki kuihakiki akaunti DECI na kubaini nyaraka walizozitumia kufungulia akaunti aziendani na ripoti ya fedha zilizokuwemo kwenye akaunti ya washtakiwa kwasababu awali washtakiwa waliwaeleza kuwa kampuni yao ya DECI ni Saccos na kuongeza kuwa anavyofahamu yeye SACCO inapaswa kuwa inatoa mikopo tu na si vinginevyo.

“Na hasa kilichoitufanya tuitilie shaka akaunti hiyo ni kuona dola 200,000 kuingizwa kwenye akaunti ya DECI ikabidi BOA iende kutembelea ofisi za taasisi hiyo ilipo Mabibo na tulipofika ofisini kwao kutaka kujua chanzo cha fedha hizo lakini washtakiwa hao hawakutueleza na benki haikuridhika ikabidi benki iwasilishe taarifa kwa Kitengo cha Usalama wa Fedha(FIU) ndani ya Wizara ya Fedha na Uchumi. ”alidai Maro.

Alieleza kuwa baada ya (FIU) kupokea taarifa hizo toka BOA, Wakurugenzi wa DECI, washatakiwa hao walifika katika benki yao kutaka wapatiwe fedha taslimu Sh bilioni moja na kwamba uongozi wa benki hiyo ulikataa kuwapatia licha fedha hizo zilikuwa ni mali ya washtakiwa.

Aidha baada ya muda siku chache kupitia benki ilipokea barua toka kwa kampuni ya uwakili ya Azania Law Chamber ambayo iliitaka benki hiyo iwapatie washtakiwa kiasi hicho cha fedha na kwamba benki ilikataa tena kutoa fedha taslimu na kuwataka washtakiwa iwapatie namba ya akaunti ili waweze kuwatumia fedha hizo.

“Washtakiwa hao hatimaye wakaleta namba ya akaunti inayomilikiwa na kanisa la Jesus Christ Delivers la Magomeni iliyopo kwenye Benki ya Dar es Salaam, na BOA ikawatumia zaidi ya Sh bilioni moja na zaidi ya Sh.milioni mia moja zilizokuwa zimesalia kwenye akaunti washtakiwa ,benki hiyo ilizipeleka kwenye akaunti inayoshukiwa na nia ya kufanya hivyo ni BOA kutaka kuifunga hiyo akaunti kwenye yetu na kusubiri maelekezo toka serikalini;

“Aprili 2009 nikiwa ofisini ilikuja barua toka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa BOA na kuitaka benki yetu iifunge akaunti ya DECI ambayo ilikuwa na salio la zaidi ya sh.milioni 100” .alidai Maro.

Aidha alieleza mahakama kuwa anamfahamu mshtakiwa Tomotheo ole Olitiginye na Samwel Mtares kwasababu washtakiwa hao walifungua akaunti ya pamoja kwenye benki hiyo na katika upekuzi wake alibaini nayo ilikuwa na shaka katika nyaraka walizozitumia kufungulia akaunti na mtiriko wa fedha unaoingia kwenye akaunti hiyo na hivyo akalamizika kutoa taarifa kwenye Kitengo cha Usalama wa Fedha na mwisho wa siku Mwanasheria Mkuu pia alitoa amri kwa benki yao kuifunga pia akaunti hiyo.

Kuhusu mshtakiwa wa kwanza na wa pili Jackson Mtares na Domic Kigendi nao alidai kuwa aliwafahamu pia kwasababu walifungua akaunti ya pamoja katika benki hiyo na kwamba upekuzi wake ulibaini akaunti na nyaraka zilizotumiwa na washtakiwa kufungulia akaunti hiyo hazikuwa na matatizo yoyote ila kwasababu washtakiwa hao wote walikuwa wakihusika kwenye akaunti ya DECI ambayo ilishafungwa kwa maelekezo ya AG , Benki yao ikaamua kusitisha biashara na washtakiwa haoi na pia akaunti ikafungwa kwa amri ya mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Shahidi huyo akijibu swali aliloulizwa na mawakili wa utetezi Onesmo Kyauke na Hudson Ndusyepo kwamba ni kwanini shahidi alivyokwenda kuikagua ofisi ya DECI na kukuta umati mkubwa nje ya ofisi ya DECI asitambue kuwa watu wale ndiyo waliokuwa chanzo cha fedha cha taasisi hiyo, Maro alijibu kuwa uwingi wa watu siyo kigezo cha fedha na kwamba wateja walipaswa wafungue mioyo yao na kuwaeleza kwa mapana chanzo cha fedha zao kuwa nyingi kwenye akaunti ile ya DECI.Shahidi wa sita anatarajiwa kupanda kizimbani leo kuanza kutoa ushahidi wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Februali 25 mwaka 2011.

JAMHURI YAKWAMISHA KESI YA JAMHURI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, jana ilishindwa kuanza rasmi kusikiliza ushahidi wa upande wa Jamhuri katika kesi ya tuhuma za kughushi na kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa serikali inayomkabili Naeem Adam Gile kwasababu upande wa jamhuri ulishindwa kuleta mashahidi wake.

Gile anadaiwa kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa umma na kwamba Julai 20, 2004 eneo la Ubungo Umeme Park, alitoa taarifa ya uongo kwa wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Shirika la Umeme (TANESCO). Kwamba Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 100 kwa Tanzania ili wajumbe wa bodi hiyo waweze kumpendekeza kupewa tenda ya kutoa huduma hiyo.

Mbele ya Hakimu Mkazi Walirwande Lema, Wakili Serikali Fredrick Manyanda aliikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa ila kwa bahati mbaya hawakuwa wameleta mashahidi na hivyo kuomba iarishwe.

Kwa upande wake wakili wa mshtakiwa, Alex Mgongolwa aliiomba mahakama iuamuru upande wa Jamhuri ile mashahidi kama inavyokuwa imeamuriwa na mahakama kwani kesi hiyo ni ya muda mrefu.Hakimu Lema aliairisha kesi hiyo hadi Machi 24 mwaka huu, na itakuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa.

Wakati huo huo Kesi ya Uhujumu ya Euro milioni mbili inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia na Grace Martin jana walishindwa kuanza kujitetea kwasababu Jaji Sivangilwa Mwangesi anayesikiliza kesi hiyo kutotokea mahakamani lipa upande wa Jamhuri na Utetezi kuwa tayari kuendelea na kesi hiyop , hali iliyosababisha Hakimu Mkazi Mustapher Siyani kuiarisha hadi Machi 25 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kuanza washtakiwa kuanza kujitetea.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Februali 25 mwaka 2011.

WANAHABARI TUHESHIMU TAALUMA

Na Happiness Katabazi

BABA wa taifa Mwalimu Julias Nyerere aliwahi kusema kuwa “Ukweli una tabia moja nzuri sana ,achagui adui wala rafiki”.

Hivyo basi leo nimelazimika kutumia nukuu hiyo kwasababu mtazamo wangu utawahusu sana wanahabari wenzangu ambao naweza kusema ni familia moja na mimi na hivyo ni marafiki.
Februali 16 mwaka huu, Kambi ya 511 KJ ya Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam na kusababisha baadhi ya wananchi wenzetu kupoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya na makazi yao kuharibika vibaya.

Binafsi natoa pole kwa wahanga waliokumbwa na janga hilo likiwemo Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi waTanzania (JWTZ), ambalo nalo nimiongoni mwa wahanga kwani wanapiganaji wetu wanne walijeruhiwa na nyumba mbili ziliabiwa.

Lakini kama ilivyoada kwa sisi watanzania wengi hasa baadhi ya wanahabari kupitia kalamu kila litokeapo jambo huwa hatukosi kuingiza hisia zetu badala ya kusubiri taarifa za wanataaluma husika wa matukio hayo.

Na hii ndiyo imeanza kuwa mila na desturi ya sisi wanahabari na baadhi ya wanasiasa wa hapa nchini kupenda kuhararisha vitu na kuwaaminisha wananchi baadhi ya taarifa huku tukijua wazi huku wakijua wazi hawana ushahidi wa jambo husika.

Ifike mahala sasa jamii ya watanzania tuje utamaduni wa kuheshimu taaluma za wanataaluma wengine naamini tukifanya hivyo tutakuwa tunaliondoa taifa kweny ugonjwa huu ambao uanaanza kulitafuna taifa la wananchi na wanahabari la kutoheshimu taarifa na kazi za wanataluma wengine.

Ijumaa iliyopita mimi nilikuwa ni miongoni mwa wanahabari tulioudhuria mkutano wa JWTZ ambao ndiyo ulikuwa mkutano wa kwanza wa jeshi hilo tangu milipuko hiyo .

Kwanza nikiri kwamba tangu nianze kazi hii ya uandishi wa habari kwa takribani miaka 12 sasa, sikuwahi kuudhulia mikutano inayohusisha wahariri na wakurugenzi wa vyombo vya habari lakini siku hiyo Mhariri wangu Mtendaji Absalom Kibanda alinituma nimwakirishe kwenye mkutano huo kwaniaba yake.

Kwanza napenda kumshukuru kwakunikabidhi majukumu hayo kwani ama kwa hakika fursa hiyo ilipa fursa ya kuthibitisha pasipo shaka kwamba kuna baadhi ya wahariri wanaotuongoza kwenye vyumba vya habari, uelewa wao wa kujua mambo ni mdogo wakati mwingine ukilinganisha na sisi waandishi wa habari wadogo.

Kwani kupitia baadhi ya maswali yaliyokuwa yakiulizwa na mabosi wetu hao kuhusu tukio hilo yalikuwa yakidhiirisha wazi uwezo wetu wa kutanyambua na kufahamu majukumu yanayofanywa jeshi letu ni mdogo mno.Inasikitisha sana.

Kwani wakati mabosi wetu hao wakiuliza maswali hayo ambayo yalikuwa yakipanguliwa vyema kwa hoja za kutaaluma na Mkuu wa Usalama na Utambuzi Jeshi, Brigedia Jenerali Paul Meela na Mkuu wa Milipuko Jeshini,Brigedia Jenerali Leonard Mdeme hali iliyosababisha baadhi ya wanajeshi na wanausalama wa jeshi waliokuwa wamevalia nguo za kirai na mimi tukiwa tukiangua vicheko mara kwa mara.

Mfano mhariri anahoji ni kwanini JWTZ inapomaliza kufanya uchunguzi wake ni kwanini haitoi ripoti nzima kwa waandishi wa habari?Hivi katika akili ya kawaida tu na haitaji uwe ni mwanajeshi au wazazi wako ni wanajeshi, jeshi linaweza kutoa kutoa ripoti yake ya uchunguzi kwa ikaitapanya kwenye vyombo vya habari.

Ndiyo JWTZ yenye inasema uchunguzi ukikamilika utatoa taarifa.Sisi wanahabari tunaitaka hiyo ripoti ya uchunguzi tuipeleke wapi,Je kwa maadui wa nchi yetu kesho na kesho kutwa waje kutudhuru?

Mwanahabari anauliza swali kwamba ana taarifa kwamba wananchi tayari wamepoteza imani na jeshi lao kutokana na milipuko hiyo? Na wakati mwanahabari huyo anauliza swali hiyo mkononi hana hata ushahidi wa majina hata walau matano ya wananchi ambao wamekosa imani na jeshi hilo.
Na ndiyo maana nimeshindwa kuficha hisia zangu kwani makamanda wale wa JWTZ,Meela na Mdeme waliweza kuyapangua maswali ya wanahabari napia mara kwa mara Brigedia Mdeme alilazimika kuwaingiza katika darasa la milipuko na Meela kulazimika kuwaingiza kwenye darasa la sheria wahariri hao ambao aliwaambia JWZT huwa hawajiudhuru na kuwataka wakaisome Sheria ya Usalama na Ulinzi ya mwaka 1964.

Tumekuwa wepesi mno kutaka kupatiwa ripoti hiyo ya uchunguzi lakini mbona sisi wananchi tunakuwa wagumu sana kudai tupatie maamuzi yanayifikiwa kwenye baraza la mawaziri ambazo kwa mujibu wa Sheria ya Usalama wa Taifa ni siri?Na huko ndiko wakati mwingine yanapitishwa maamuzi ambayo yametekelezwa mwisho wa siku yamekuja kuligharimu taifa.

Inawezekana hili linasababishwa na sisi wanahabari kutotaka kubobea kwenye eneo Fulani la kuandika habari za aina fulani(specialization),makusudi, kutotaka kujifunza, ujinga,kununuliwa au ni umaamua wetu?

Na tatizo hilo la kukosekana kwa specialization ndiyo kunakosababisha sasa baadhi ya wahariri ambao hata mlango wa mahakama haujui au kesi zinaendeshwaje kuishia kuzipotosha habari za mahakama pindi wanapozihariri,hujikuta wanaweza hisia zao ambazo habari za mahakama ni mwiko kuweka hisia zao, kinachitakiwa kuandika kile kilichosemwa mahakamani.

Nafahamu kuwa ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inatoa huru kwa wananchi wa kutoa maoni yao. Lakini Hata mwalimu Nyerere alishawahi kusema ‘uhuru bila mipaka ni sawa na wendawazimu”.Na msemo huu rafiki yangu kipenzi aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam,(ACP), Abdallah Zombe ninpokutana naye katika mazungumzo yetu amekekuwa akinukuu nukuu hiyo ya Nyerere akisema kuwa hivi sasa huu uhuru wa kutoa maoni hivi sasa ambao inaonekana hauna mipaka sasa kwani unaingilia hadi taaluma za watu ni hatari kwa mustakabali kwa taifa.

Sote ni mashahidi kwa jinsi ya baadhi ya vyombo vya habari vilivyokuwa vikiripoti kesi ya Zombe na kabla ya kufikishwa mahakamani kwa hisia zao badala ya kuripoti kile kilichokuwa kikisemwa mahakamani.Na matokeo yake akaja kushinda kesi na yeye akafikia uamuzi wa kuyashtaki magazeti hayo ikiwemo gazeti letu.

Wanahabari hivi sasa ndiyo kimbilio kubwa la wananchi na hivi sasa wanahabari ndiyo wamekuwa wakipata habari nyingi sana tena kwa haraka ukilinganisha na miaka iliyopita.Kwahiyo nasisi wanahabari tubadilike.

Hivyo basi nimalizie kwa kuwaasa wanaandishi wenzangu,wanasiasa na wananchi wa kada nyingine tuheshimu taaluma za watu pamoja na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwani leo hii tunaenda maofisi na kurudi nyumbani salama na kukaa kwenye mabaa na kulewa pombe ni kwasababu kuna baadhi ya wanajeshi JWTZ, Idara ya USalama wa Taifa,Polisi wanakesha kwa kutumia mbinu walizofunzwa mafunzoni kuakikisha taifa letu na wananchi wake wanaishi salama.

Na ieleweke kwamba kulinda usalama wa taifa na mali zake ni taaluma za watu, serikali ilipeleka askari wetu JWTZ chini ya Jenerali Mwamunyange huko Mafinga ,Mafinga nayo Idara ya Usalama wa Taifa chini ya Rashid Othman inapeleka askari wake kuhenya kwenye chuo chake Mbweni na Jeshi la Polisi chini ya IGP-Said Mwema linapeleka askari wake kuhenya Kule CCP-Moshi.

Hivyo tunapaswa tuheshimu kazi zao na pindi wanapolitaka taifa liwe nasubira kwani bado wanafanyia uchunguzi jambo Fulani ,tusiwaharikishe kwani wengine ni maamuma katika fani hiyo ya uskari.

Ikumbukwe kwamba taifa la wananchi na viongozi wanaishi na kuaminishwa umbeya, chuki, na uongo ambao umekuwa ukiandikwa kwenye vyombo vyetu vya habari na baadhi ya waandishi wasiyo na maadili ,kamwe hilo siyo taifa thabiti.

Nalisema hili kwa uchungu sana kwani hivi sasa taifa letu ndiyo linaelekea huko kwani wananchi wengi huko mitaani na maofisini wamekuwa wakiamini sana habari ambazo tumekuwa tukiziandika kumbe wakati mwingine sisi waandishi tumekuwa tukiandika habari hizo bila kuwa na ushahidi wa kutosha, hisia zetu kuliko uhalisia wa jambo husika na mwisho wa siku aliyeandikwa hivyo kwa kupakaziwa uenekana ni mtu mchafu kwa jamii kumbe si kweli.

Sisi wanahabari tusilifikishe taifa huko,kwani mwisho wa siku hata watoto wetu watakuwa ni waathirika wa dhambi hiyo ya uzushi na umbeya.Tanzania ni nchi yetu na JWTZ itabaki kuwa ni chombo chetu ambaItaliccho kimeanzishwa kwamujibu wa Sheria Na. 24 ya Ulinzi na Usalama ya mwaka 1964.Tumekikabidhi jukumu la kulinda mipaka ya nchi yetu na ndiyo Jeshi la Tanzania.

Hivyo katika hili la milipuko ya mabomu ya Gongo la Mboto ni vyema na haki tukalipa nafasi ya kufanyakazi yake chini ya Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na Mkuu wa Jeshi hilo Jenerali Davis Mwamunyange.

Tuache hisia (speculation) katika jambo hili na katika masuala mengine ya taaluma za watu ambazo sisi hatujazisomea kama walivyotutaka Mabrigedia Jenerali Paul Meela na Leonard Mdeme kwani kufanya hivyo ni wazi tutapandikiza chuki mbaya kwa wananchi na jeshi lao pamoja serikali.Na sisitiza kwamba tuheshimuwa taaluma watu wengine na tuachane na maneno ya kusikia, tusimame kwenye maadili ya taaluma yetu ya uandishi naamini tutakuwa tulijenga taifa letu.

Mungu ibariki Tanzania,Mungu ibariki Afrika.
0716-774494.


Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Februali 22 mwaka 2011.

DAWA ZA KULEVYA ZA SH.BIL 6.2/-ZAWAFIKISHA KORTINI

Na Happiness Katabazi

WATU wanne wakiwamo rai wawili wa Pakstan wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kula njama na kusafirisha kilo 179 za dawa za kulevya aina ya heroin zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 6.2.


Wakili wa Serikali Mwandamizi, Biswalo Mganga, mbele ya Hakimu Mkazi, Agustina Mmbando, aliwataja washitakiwa hao kuwa ni Freddy Chonde na Kambi Zubery ambao ni Watanzania na Abdul Ghan Peer Bux na Shahbaz Malik ambao ni raia wa Pakstan.

Wakili Mganga alidai kuwa kwa wakati tofauti kati ya Januari mosi na Februari 21 mwaka huu, katika maeneo tofauti hapa Tanzania na nchini Pakistan, washitakiwa kwa pamoja walikula njama kutenda kosa la kuleta na kusafirisha dawa za kulevya nchini Tanzania.

Mganga alidai kuwa Februari 21, mwaka huu, maeneo ya Mtaa wa Jogoo, Mbezi Beach kwa pamoja washitakiwa wote waliingiza nchini dawa za kulevya zenye uzito wa gramu 179,000 sawa na kilo 179 aina ya heroin zenye thamani hiyo.

Hakimu Augustina alisema kuwa washitakiwa hao hawapaswi kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Mganga alidai upelelezi wa shauri hilo haujakamilika. Hata hivyo, mawakili wanaowatetea washitakiwa hao wakiongozwa na Yassin Member, uliomba upande wa mashitaka kukamilisha upelelezi haraka kwa kuwa watuhumiwa wamekamatwa hapa nchini.

Akijibu hoja hiyo, Mganga alidai kwamba watuhumiwa hao wamekamatwa juzi na kwamba shauri hilo linawahusisha raia wa kigeni, hivyo inawapasa wafanye upelelezi wa kina na kwa nafasi.

Hata hivyo, Hakimu Mmbando aliutaka upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi haraka na akaliahirisha shauri hilo hadi Machi 9, mwaka huu na siku hiyo litakuja kwa ajili ya kutajwa na akaamuru washitakiwa wote warudishwe rumande.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Februali 24 mwaka 2011.

MPENDAZOE AKWAMA KORTI KUU

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali ombi la aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea(CHADEMA), Fred Mpendazoe lililokuwa linaiomba mahakama hiyo imsamehee kulipa shilingi milioni 15 za kesi yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambayo yalimtangaza Naibu wa Kazi na Ajira, Dk.Makongoro Mahanga (CCM) kuwa ndiye mbunge wa jimbo hilo kwasababu lina dosari za kisheria.

Katika kesi ya msingi ya kupinga ubunge wa jimbo hilo iliyofunguliwa mahakamani hapo mwishoni mwa mwaka jana na Mpendazoe na ambayo bado haijaanza kusikilizwa wadaiwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk.Mahanga na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo.Na Mdaiwa anaomba mahakama hiyo itengue ubunge wa mdaiwa wa pili (Dk.Mahanga) anayetetewa na wakili wa kujitegemea Jerome Msemwa.

Uamuzi wa ombi hilo la kuomba mahakama imsamehe kulipa gharama za kesi ya uchaguzi ulitolewa jana na Jaji Profesa Juma Othman ambaye alisema baada ya kupitia kwa kina ombi hilo amebaini hati ya kiapo iliyoambatanishwa na ombi hilo lina dosari za kisheria na kwasababu hiyo analitupilia ombi hilo.

Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 inamtaka mlalamikaji katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge aliweke Mahakama Kuu shilingi milioni tano kwa kila mtu anayemlalamikia.Na Kwenye Kesi hiyo Mpendazoe anapaswa aweke mahakamani jumla ya Sh milioni 15 kwababu anawalalamikia wadaiwa watatu ambao ni Mwanasheria Mkuu wa Seriakali, Dk.Mahanga na Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Segerea.

Aidha Jaji Othman aliairisha kesi hiyo Februali 23 mwaka 2011 kesi ya msingi itakapokuja kwaajili ya kutajwa na kuangalia mlalamikaji kama tayari ameishaweka weka kiasi hicho cha fedha mahakamani ili mahakama hiyo iweze kupanga tarehe ya kuanza kusikiliza kesi hiyo ya msingi iliyofunguliwa na Mpendazoe.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Februali 16 mwaka 2011.

MPENDAZOE AKWAMA KORTI KUU

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali ombi la aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Segerea(CHADEMA), Fred Mpendazoe lililokuwa linaiomba mahakama hiyo imsamehee kulipa shilingi milioni 15 za kesi yake ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ambayo yalimtangaza Naibu wa Kazi na Ajira, Dk.Makongoro Mahanga (CCM) kuwa ndiye mbunge wa jimbo hilo kwasababu lina dosari za kisheria.

Katika kesi ya msingi ya kupinga ubunge wa jimbo hilo iliyofunguliwa mahakamani hapo mwishoni mwa mwaka jana na Mpendazoe na ambayo bado haijaanza kusikilizwa wadaiwa ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk.Mahanga na aliyekuwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo hilo.Na Mdaiwa anaomba mahakama hiyo itengue ubunge wa mdaiwa wa pili (Dk.Mahanga) anayetetewa na wakili wa kujitegemea Jerome Msemwa.

Uamuzi wa ombi hilo la kuomba mahakama imsamehe kulipa gharama za kesi ya uchaguzi ulitolewa jana na Jaji Profesa Juma Othman ambaye alisema baada ya kupitia kwa kina ombi hilo amebaini hati ya kiapo iliyoambatanishwa na ombi hilo lina dosari za kisheria na kwasababu hiyo analitupilia ombi hilo.

Kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 inamtaka mlalamikaji katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa ubunge aliweke Mahakama Kuu shilingi milioni tano kwa kila mtu anayemlalamikia.Na Kwenye Kesi hiyo Mpendazoe anapaswa aweke mahakamani jumla ya Sh milioni 15 kwababu anawalalamikia wadaiwa watatu ambao ni Mwanasheria Mkuu wa Seriakali, Dk.Mahanga na Msimamizi wa Uchaguzi jimbo la Segerea.

Aidha Jaji Othman aliairisha kesi hiyo Februali 23 mwaka 2011 kesi ya msingi itakapokuja kwaajili ya kutajwa na kuangalia mlalamikaji kama tayari ameishaweka weka kiasi hicho cha fedha mahakamani ili mahakama hiyo iweze kupanga tarehe ya kuanza kusikiliza kesi hiyo ya msingi iliyofunguliwa na Mpendazoe.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Februali 16 mwaka 2011.

NYARAKA ZA MENGI KUHUSU EPA,KAGODA ZAKATARIWA TENA KORTINI

Na Happiness Katabazi

KWA mara ya pili Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imetupilia mbali ombi la Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Ltd, Reginald Mengi, lililotaka mahakama hiyo iwapatie nakala ya uamuzi iliyoutoa Ijumaa iliyopita ili aweze kwenda Mahakama Kuu kuomba ufanyiwe mapitio.

Mengi kupitia wakili wake Michael Ngaro, wanapinga kutupwa kwa nyaraka zinazohusu wizi wa fedha kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), inayoihusisha kampuni ya Kagoda ambazo Mengi anadai ina uhusiano na Manji.

Uamuzi wa kulitupa ombi hilo, ulitolewa jana na Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana, ambaye alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili anakubaliana na hoja ya mawakili wa mlalamikaji (Manji), Mabere Marando, Dk. Ringo Tenga, Richard Rweyongeza na Beatus Malima, ambao walidai ombi lililowasilishwa na wakili wa mdaiwa Michael Ngaro na Deo Ringia, halina msingi wa kisheria.

Muda mfupi baada ya hakimu huyo kutoa uamuzi wa kukataa nyaraka za Mengi, zinazohusu EPA na Kagoda mawakili wake walieleza kutoridhishwa na uamuzi huo na kuomba wapatiwe nakala ya uamuzi ili waende kuiomba Mahakama Kuu iufanyie mapitio.

“Nataka ieleweke kwamba mahakama inaongozwa na kutenda kazi zake kwa mujibu wa sheria na hivyo basi mahakama hii inatupilia mbali ombi la mdaiwa (Mengi) lililotaka apatiwe nakala ya uamuzi wangu ili aweze kuomba upitiwe na Mahakama Kuu kwa sababu Sheria ya Mabadiliko ya Sheria ambazo zimeandikwa Na. 25 ya mwaka 2002, inakataza upande wowote katika kesi yoyote kwenda mahakama ya juu kupinga amri za muda zinazotolewa na mahakama ya chini hadi kesi ya msingi itakapomalizika na kutolewa hukumu.

“Sababu hiyo ya kimsingi na kisheria niliyoitoa hapo juu ndiyo imenisukuma kulitupilia mbali ombi hilo la mdaiwa (Mengi) la kutaka kwenda kuiomba Mahakama Kuu iupitie uamuzi wangu nilioutoa Ijumaa iliyopita na kwa maana hiyo kesi hii itaendelea kusikilizwa katika mahakama hii ya Kisutu na hata sasa niko tayari kwa ajili ya kuanza kuisikiliza na imeamriwa hivyo na mahakama hii,” alisema Hakimu Mkazi Katemana kwa kujiamini.

Baada ya kumaliza kusoma uamuzi huo, Hakimu Katemana aliziuliza pande zote mbili kama ziko tayari kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa shauri hilo jana, lakini wakili wa Manji, Marando, alidai kuwa kwa jana hawakuwa tayari kwani mteja wao hakuwa amefika mahakamani na pia walikuwa wanafahamu kesi hiyo jana ingelikuja kwa ajili ya mahakama kutoa uamuzi huo, hivyo waliiomba ipangiwe tarehe nyingine.

Hakimu huyo aliahirisha usikilizwaji wa kesi hiyo hadi Machi 14 na 15 mwaka huu.

Ijumaa iliyopita Hakimu Katemana alitoa uamuzi wa kuzikataa nyaraka 14 zikiwemo zinazoihusu kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd.

Mapema mwaka juzi, Manji alimfungulia kesi ya madai ya kashfa Mengi na kituo cha televisheni cha ITV akitaka amlipe fidia ya shilingi moja kwa madai kuwa Mengi alitumia televisheni yake kumkashfu kwa kumuita ‘Fisadi Papa’ na kwamba mmoja wa watu wanaopora rasilimali za Tanzania.

Ili kuthibitisha madai ya kumuita Manji Fisadi Papa, Mengi alitaka kuzitumia nyaraka za EPA na Kagoda, lakini mahakama ilikataa kuzitumia nyaraka hizo kutokana na madai yaliyotolewa na wakili Marando anayemtetea Manji.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Februali 16 mwaka 2011.

KESI YA MANJI Vs MENGI:KORTI YATUPA NYARAKA ZA MENGI

Na Happiness Katabazi


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imevikataa vielelezo vya utetezi vilivyowasilishwa na Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Ltd, Reginald Mengi, katika kesi aliyofunguliwa na mfanyabiashara Yusuf Manji.

Uamuzi wa kuvikataa vielelezo hivyo vinavyojumuisha nyaraka 14 zikiwamo zinazoihusu kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd ulitolewa mahakamani hapo jana na Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana.

Katika kesi hiyo, Manji anamlalamikia Mengi kwa madai ya kumkashfu akimdai fidia ya shilingi moja kwa kumuita fisadi papa.

Hakimu Katemana alisema amefikia uamuzi huo baada ya kusikiliza hoja za kisheria zilizowasilishwa mbele yake na pande zote mbili kwa siku mbili tofauti.

Akisoma uamuzi wake huo, alisema anakubaliana na hoja za kisheria zilizowasilishwa awali na jopo la mawakili wa mlalamikaji ambao wanaongozwa na Mabere Marando, Richard Rweyongeza, Dk. Ringo Tenga na Beatus Malima kwamba mahakama hiyo itupilie mbali maombi ya mdaiwa (Mengi) ya kutaka nyaraka hizo zikiwemo nyaraka vivuli ambazo zinaonyesha ni mali ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mkataba baina kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd na Quality Finance Corporation Ltd.

“Kwa kauli moja mahakama hii inatupilia mbali ombi la mdaiwa (Mengi) kwa sababu nyaraka hizo anazotaka kuzitumia kutolea ushahidi hazihusiani na kesi hii kabisa, na pia nyaraka hizo ni vivuli.”

Baada ya Hakimu Katemana kumaliza kusoma uamuzi wake, Wakili wa mdaiwa Michael Ngaro anayesaidiwa na Deo Lingia aliinuka kwenye kiti alichokuwa ameketi na kuieleza mahakama kuwa uamuzi wa hakimu huyo haukuwa wa kushtukiza.

Wakili Ngaro alidai kuwa kitendo cha hakimu huyo kuzikataa nyaraka hizo ni wazi sasa kimesababisha mteja wake asizitumie nyaraka hizo kama ushahidi wakati siku atakapoitwa na mahakama hiyo kujitetea na kwamba wanaomba nakala ya uamuzi huo na ili kwenda kuupinga Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Hata hivyo hoja hiyo ya wakili Ngaro ya kutaka kwenda Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu, ulipingwa vikali na mawakili wa mlalamikaji ambao walimwomba Ngaro asiipotezee muda mahakama hiyo kwani katika mabadiliko ya sheria yaliyofanywa na Bunge mwaka 2002 yanakataza kuyakatia rufaa maamuzi madogo (ruling) yanayotolewa na mahakama za chini kabla kesi ya msingi haijamalizika.

Hata hivyo hoja hiyo ya mawakili wa Manji, ilimfanya wakili wa Mengi kuwasilisha ombi jipya la kuiomba mahakama itumie busara zake kwani siku itakapofika mteja wake kuja kujitetea atakosa nyaraka.

Baada ya ombi hilo, Katemana aliahirisha shauri hilo hadi Februari 15 mwaka huu ambapo atatoa uamuzi.

Mapema asubuhi jana wakili wa Mengi, alianza kujibu hoja za mawakili wa mlalamikaji zilizowasilishwa mahakamani hapo Februali 4, mwaka huu, aliomba nyaraka za mteja wake zipokelewe na pingamizi la Manji kutaka nyaraka hizo zisipokelewe litupwe.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi,Februali 12 mwaka 2011.

MAWAKILI WA MINTANGA WAGEUKA MBOGO

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa utetezi katika kesi ya kula njama na kusafirisha dawa za kulevya inayomkabili aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Alhaji Shabani Mintanga, umeiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kuifuta kesi hiyo kwasababu upande wa Jamhuri umeshindwa kuleta mashahidi.

Mawakili wa utetezi Majura Magafu, Jerome Msemwa na Yasin Memba mbele ya Jaji Agustino Mwarija jana waligeuka kuwa mbogo mahakamani hapo na kuomba kesi hiyo ifutwe kwani licha ya upande wa Jamhuri kushindwa kuleta mashahidi hao katika kesi hiyo ilianza rasmi kusikilizwa jana juzi pia imeonyesha aitilii umuhimu kesi hiyo.

“Jopo la mawakili wa utetezi kwa kauli moja tunaomba kesi hii ifutwe kwani upande wa Jamhuri haileti mashahidi licha ya mahakama hii imekuwa ikiwataka ifanye hivyo na miongoni mwa mashahidi wa Jamhuri ni Katibu Mkuu wa Kamati ya Olmpiki(TOC), Filbert Bayi na Mkurugenzi wa Michezo nchini, Leonard Thadeo wanaishi hapa jijini na tunawaona kila siku lakini cha ajabu upande wa Jamhuri unashindwa kuwaleta mashahidi hao kuja kutoa ushahidi mahakamani na matokeo yake mteja wetu anaendelea kusota rumande;

“Jumanne wiki hii kesi hii ilikuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa rasmi lakini upande wa Jamhuri ukasema haujaja na shahidi na ukaomba upewe siku moja yaani Juzi ili waweze kuitumia siku hiyo kumpata shahidi ili waweze kumleta shahidi huyo leo(jana) aanza kutoa ushahidi lakini pia wanadai wameshindwa kumleta shahidi na hivyo mahakama hii haina budi kuairisha usikilizaji wa kesi hii na mteja wetu anarudi rumande kuendelea kusota…kwa sababu hizi sisi tunaomba kesi hii ifutwe” alidai wakili Jerome Msemwa.

Awali Wakili wa Serikali Zuberi Mkakati aliikumbusha mahakma kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya shahidi wa upande wao kuanza kutoa ushahidi lakini hilo halitaweza kufanyika kwasababu pia jana wameshindwa kuwapata mashahidi na kwamba hawana uhakika hati za wito wa mahakama wanazozitoa kama zinawafikia mashahidi hao na kuomba kesi hiyo iairishwe tena.

Kwa upande wake Jaji Mwarija alisema anatoa nafasi ya mwisho kwa upande wa Jamhuri kuleta mashahidi wao na akaiairisha kesi hiyo hadi kikao kijacho.

Mintanga alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, mwaka 2008 akikabiliwa na mashitaka ya kula njama na kusafirisha dawa za kulevya zenye thamani ya shilingi milioni 120 nchini Mauritius kupitia mabondia Emmilian Patrick, Petro Mtagwa na kocha Nasoro Michael na wengine watatu walipokwenda kushiriki mashindano ya ngumu ya pili ya Afrika nchini humo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Februali 11 mwaka 2011.

KESI YA RICHMOND SASA KUUNGURUMA FEBRUALI 24

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam,Februali 24 mwaka huu, itaanza rasmi kusikiliza kesi ya tuhuma za kughushi na kutoa taarifa za uongo kwa watumushi wa serikali inayomkabili Naeem Adam Gile.

Wakili wa Serikali Shadrack Kimaro mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema alieleza kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kutajwa na kwamba upande wa Jamhuri upo tayari kwaajili kuanza kusikilizwa.

Hakimu Mkazi Lema alisema anakubaliana na ombi hilo na anaiarisha kesi hiyo hadi Februali 24 mwaka huu, kesi hiyo ambapo itakuja kwaajili ya mashahidi wa upande wa Jamhuri kuanza kutoa ushahidi wao.

Awali Janurai 13 mwaka 2009, ilidaiwa mahakamani hapo na Wakili Mkuu wa Serikali, Stanslaus Boniface kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka matano ambayo aliyatenda kwa nyakati tofauti.

Wakili Boniface alidai kuwa, Machi 13, 2006, jijini Dar es Salaam, mshitakiwa akiwa na dhamira ya kutenda kosa, alighushi hati ya nguvu ya kisheria (power of attorney) inayoonyesha imetolewa na Hamed Gile, ambaye ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, kwamba amemruhusu kufanya shughuli za kampuni hiyo hapa nchini.

Wakili Boniface alidai kwamba, shitaka la pili ni kutoa taarifa za uongo, kuwa Machi 20 mwaka 2006, katika eneo la Ubungo, Umeme Park, Barabara ya Morogoro, mshitakiwa alitoa hati hiyo ya nguvu ya kisheria inayomuidhinisha yeye kwamba ameruhusiwa kufanya kazi ya kampuni hiyo ya Marekani hapa nchini.

Aliendelea kudai kuwa, shitaka la tatu linalomkabiri mtuhumiwa huyo ni kutoa taarifa za uongo kwa watumishi wa umma na kwamba Julai 20, 2004 eneo la Ubungo Umeme Park, alitoa taarifa ya uongo kwa wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Shirika la Umeme (TANESCO). Kwamba Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 100 kwa Tanzania ili wajumbe wa bodi hiyo waweze kumpendekeza kupewa tenda ya kutoa huduma hiyo.
Katika shitaka la nne, alidai Juni, 2006 jijini Dar es Salaam, mshitakiwa alitoa taarifa za uongo kwa wajumbe wa timu ya majadiliano ya serikali, kuwa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas, Marekani, ina uwezo wa kuzalisha umeme kwa kiwango hicho ili apewe tenda hiyo.

Aidha alidai shitaka la tano alinadaiwa kulitenda Julai, 2006, ambapo mshitakiwa akifahamu na kwa ulaghai, alitoa hati ya nguvu ya kisheria iliyotolewa Machi 3, mwaka huo iliyokuwa ikimuonyesha kuwa ameruhusiwa na Mwenyekiti wa Kampuni, Hemed Gile, kufanya kazi za kampuni hiyo hapa nchini.

Gile alifikishwa mahakamani hapo ikiwa ikiwa ni siku chache baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na mwenzake aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha, walilazimika kujiuzuru nyadhifa zao kwa kashfa hiyo ya Kampuni ya Richmond.

Chanzo:Gazeti la Tanzania la Jumapili, Februali 10 mwaka 2011.

MANJI,MENGI WAVUTANA MAHAKAMANI

• Kisa ni nyaraka za Kagoda
Na Happiness Katabazi

JOPO la mawakili wa kujitegemea wanaomtetea mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji (35), jana walipambana kwa kutumia hoja za kisheria ili kuishawishi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, ikubaliane na pingamizi lao la kutaka nyaraka zilizowasilishwa na mdaiwa Reginald Mengi zisitumike katika kesi hiyo.

Jopo hilo lililosheheni mawakili wa kujitegemea maarufu linaloongozwa na Mabere Marando, Dk. Ringo Tenga, Sam Mapande, Richard Rweyongeza na Beatus Malima mbele ya Hakimu Mkazi Aloyce Katema waliiambia mahakama kuwa juzi mawakili wa mdaiwa Mengi ambao ni Michael Ngaro na Deo Ringia, waliwapatia nyaraka hizo ambazo walidai Mengi atazitumia kujitetea wakati ukifika.

Sababu zilizotolewa na Marando kutaka nyaraka hizo zisitumike ni kwamba hazihusiani na kesi hiyo ambayo mteja wake Manji anataka Mengi amlipe fidia ya shilingi moja. Kwa mara nyingine tena jana Manji alifika mahakamani hapo.

Marando alisema sababu nyingine ambayo wanataka nyaraka hizo zilizoletwa na mawakili wa Mengi zitupwe na mahakama ni kwa sababu nyaraka hizo ni kivuli.

Kadhalika zinaonyesha ni mali ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na ofisi ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (takukuru) na kwamba nyaraka hizo licha ya kuwa ni vivuli lakini pia hazionyeshi kama zimethibitishwa kisheria (certified copy).

“Sheria ya ushahidi ya mwaka 2002, inamtaka mtu alete nyaraka halisi mahakamani kama ushahidi na kama hana nyaraka halisi mdai au mdaiwa anaruhusiwa kuomba upande wa pili wa kesi hiyo umpatie nyaraka halisi ili aweze kuzitoa mahakamani kama ushahidi.
“Lakini hawa mawakili wa Mengi hawajatuomba nyaraka halisi hadi sasa na pia walitakiwa hizo nyaraka wazilete mapema mahakamani kabla ya kesi haijaanza kusikilizwa.

Marando pia alishangazwa na nyaraka hizo zinazoonyesha zimetolewa na ofisi ya AG na TAKUKURU kufikishwa mahakamani bila kibali cha mamlaka hizo wala kuonyesha kama alilipia ada ya kupata nyaraka hizo.

Akisoma moja ya nyaraka hizo ambayo ni mkataba ulioingiwa baina ya Kagoda Agriculture Ltd na Quality Group Finance Ltd, Marando alieleza kuwa mkataba huo uliiingiwa na makampuni hayo na si mteja wao (Manji) na kwamba wao ni mawakili wanaomtetea mlalamikaji binafsi na wala si mawakili wa makampuni yanayomilikiwa na mteja wao.

Katika hilo, wakili huyo wa Manji alimshauri Mengi kama anataka kutumia nyaraka ni vyema akafungua kesi nyingine dhidi ya makampuni ya Manji.

Hata hivyo ilipofika upande wa wakili wa Mengi, Ngaro, kujibu hoja hizo aliieleza mahakama kuwa hayuko kwenye nafasi nzuri ya kujibu hizo hoja hivyo kuomba muda wa kwenda kuwasiliana kwanza na mteja wake (Mengi) ambaye yuko safarini mkoani Arusha.

Ombi hilo la Ngaro lilikubaliwa na Hakimu Mkazi Katemana ambaye aliahirisha usikilizaji wa kesi hiyo inayovuta hisia za watu wengu hadi Februali 11 mwaka huu.

Mapema mwaka juzi, Manji alimfungulia kesi ya madai ya kashfa Mengi na kituo cha televisheni cha ITV akitaka amlipe fidia ya shilingi moja kwa madai kuwa Mengi alitumia televisheni yake kumkashifu kwa kumuita ‘Fisadi Papa’ na kwamba mmoja wa watu wanaopora rasilimali za Tanzania.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Februali 5 mwaka 2011.

MHASIBU MAHAKAMA KUU KORTINI KWA WIZI

Na Happiness Katabazi

MHASIBU Msaidizi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kitengo cha Ardhi, Raymond Mazale, amefikishwa mahakamani akikabiliwa na kosa la wizi wa sh milioni 22 mali ya mwajiri wake.

Wakili wa Serikali Beatrice Mpangala mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu Dar es Salaam, Aloyce Katemana, alieleza mahakama kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka manne ya wizi.

Alisema mshtakiwa anatuhumiwa kufanya udanganyifu wa stakabadhi za serikali na kujipatia kiasi hicho cha fedha kwa nyakati tofauti.

Mpangala alidai kuwa kati ya Machi 4, 2009 katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi Upanga jijini Dar es Salaam, mshtakiwa akiwa ni mhasibu msaidizi wa mahakama hiyo kwa njia ya udanganyifu alitumia stakabadhi za malipo ya serikali Na.3359401 hadi 33659600.
Hata hivyo Mpangala alisema kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Mshtakiwa huyo alikana mashtaka hayo na Hakimu Mkazi Katemana alisema makosa hayo kwa mujibu wa sheria yana dhaminika na kusema ili mshtakiwa apate dhamana atoe fedha taslimu au hati ya mali yenye thamani ya sh milioni 11.08, wadhamini wawili ambao kila mmoja atatoa hati ya mali yenye thamani ya sh milioni tano.

Hata hivyo mshtakiwa huyo alishindwa kutimiza masharti hayo na kupelekwa rumande hadi kesi hiyo itakapotajwa tena Februari 12.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Februali 5 mwaka 2011.

MANJI AMVAA MENGI KORTINI

Na Happiness Katabazi
MFANYABIASHARA maarufu nchini, Yusuf Manji(35) jana ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa kashfa zilizotolewa na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Ltd,Reginald Mengi kuwa yeye ni Fisadi Papa zimemvunjia heshima na kusababisha asiaminiwe tena wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Manji ambaye jana ilikuwa ni mara yake ya kwanza kupanda kizimbani hapo , alitoa maelezo hayo wakati akiongozwa kutoa ushahidi wake na mawakili maarufu wa kujitegemea nchini, Mabere Marando, Dk.Ringo Tenga, Richard Rweyongeza, Sam Mapande na Beatus Malima mbele ya Hakimu Mkazi Aloyce Katemana.

Wakati kesi hiyo ya kashfa ya madai ya Shilingi moja iliyofunguliwa na Manji dhidi ya Mengi na Televisheni ya ITV ilipoanza kusikilizwa rasmi mahakamani hapo jana ambapo Manji ndiyo shahidi wa kwanza wa upande wa mlalamikaji kutoa ushahidi wake na msafara wa Manji uliambatana na magari mbalimbali likiwemo gari aina ya Fuso lilokuwa limebeba lundo la magazeti ambayo yalichapisha habari iliyomnukuu mdaiwa akimkashfu mdaiwa ili yatumike mahakamani hapo kama vielelezo.

Manji alieleza mahakama kuwa kupitia Kipindi Maalum kilichorushwa na ITV, April 23-27 mwaka 2009 ambacho kilimuonyesha Mengi akimtaja yeye na wafanyabiashara wengine wanne kuwa ni mafisadi papa, wanaamisha rasilimali za taifa kupeleka nje ya nchi na kwamba wameshiriki kikamilifu katika ufisadi wa ununuzi wa magari ya JWTZ, Rada,Mradi wa makaa ya mawe wa Mchuchuma,mifuko ya hifadhi ya jamii ya PSPF na NSSF, Dowans na Richmond ,kutoa rushwa kwa maofisa wa serikali ili waweze kupata tenda za serikali na kwamba fedha walizonazo zimetokana na ufisadia kwaajili ya ufisadi na kipindi hicho cha jana kilionyeshwa kama ushahidi mahakamani hapo na mahakama kupokea DVD ya kipindi hicho kama kielelezo cha tisa.

“Mheshimiwa hakimu kupitia matamshi hayo ya mdaiwa (Mengi) kwenye Kipindi hicho maalum…kwakweli kimenifunjia heshima ndani ya familia yangu, kwa zaidi ya wafabnyakazi 4,000 niliyowaajili kwenye makampuni yangu, kwa wafanyabiashara wenzangu wa ndani na nje ya nchi, jamii inaniona mimi ni mtu mchafu sana na wabunge wamepoteza imani na mimi kwaajili ya matamshi hayo;

“Na kuthibitisha kuwa wabunge hawana imani na mimi hasa wabunge waliokuwa wabunge wa bunge lilopita….kama uchumi ya bunge iliniarika kwenye mmoja ya kikao chao nikatoe hotuba lakini cha ajabu nilivyofika kwenye kikao hicho kuna baadhi ya wabunge wa kamati hiyo walinikataza nisitoe hotuba yangu kwasababu ni mtu mchafu kwenye jamii na Mengi alikwishanitaja adharani kuwa mimi ni fisadi papa na mimi ikaniradhimu niondoke kwenye mkutano huo na kurejea nyumbani.

“Na ninaomba kashfa hizo zilizoelekezwa na mdaiwa kwangu mimi si za kweli kabisa kwani misijawahi kujihusisha na biashara za Rada,Dowans, Richmond, ununuzi wa magari ya jeshi, kuamisha fedha hapa nchini kuzipeleka nje ya nchi na wala sijawahi,kushtakiwa kwa kutoa rushwa ili nipate tenda za serikali na hadi nina umri huu sijawahi kutoa fedha zangu mfukoni kujenga nyumba hata moja hapa nchini wala nje ya nchi…hapa jijini naishi kwenye nyumba ya familia pale Upanga na Marekani kuna nyumba ya familia aliyoiacha marehemu baba yangu Meibou Manji.”alidai Manji.

Wakili Marando alipomhoji Manji anatafsri vipi neno fisadi papa aliloitwa na Mengi; Manji alijibu kuwa analitafsiri kwamba yeye ni mtu anayekabiliwa na maskendo na kwamba Papa ni aina ya samaki mkubwa aishie baharini na kukana kwamba yeye siyo samaki aina ya papa yeye ni binadamu nakuongezwa kuwa hiyo nayo ilichangia kusababisha afikie uamuzi wa kumfungulie kesi hiyo Mengi kwani amemdhalilisha na kumshushia heshima yake vya kutosha waki yeye ni mtu safi na anayeheshimika katika ndani na nje ya nchi.

Manji ambaye aliwasili mahakamani saa 6;07 baadhi ya mawakili na wananchi waliokuwa wamefika mahakamani hapo kwaajili ya kufuatilia kesi zao na za jamaa zao kulazimika kuingia kwenye ukumbi namba mbili wa mahakama hiyo kwaajili ya kuwahi nafasi ya viti ili waweze kusikiliza kesi hiyo ambayo imeonekana kuvuta hisia za watu wengi na mjadala, wakati akitoa ushahidi wake alitoa nyaraka nane halisi ambazo ni mialiko ya shughuli za kiserikali,ya ndani na nje ya nchi iliyokuwa ikimtaka awe mgeni rasmi katika shughuli hizo na kutoa hotuba mbalimbali za masuala ya kiuchumi,magazeti ya This Day na Kulikoni pamoja na DVD vyote hivyo vilipokelewa na mahakama na kufanya jumla ya vielelezo vilivyopokelewa kuwa tisa.

Nakwamba aliudhulia shughuli hizo na watu walimpokea vizuri na kumpa heshima zote na kwamba kwa kashfa hiyo ya Mengi dhidi yake imefanya wahitimu wa shule mbalimbali alizokwenda kwenye mahafali yao waliyomwalika kama mgeni rasmi hivi sasa wanamtazama kama ni mtu mchafu na mtoa rushwa hali aliyosisiza kuwa imemvunjia heshima na kumpatia wakati mgumu wa katika majukumu yake ya kila siku.

Hakimu Katemana aliairisha usikilizaji wa kesi hiyo hadi leo asubuhi ambayo shahidi huyo Manji atakapoendelea kutoa ushahidi wake na kuhojiwa na mawakili wa Mengi.

Mapema mwaka juzi, Yusuf Manji alimfungulia kesi ya madai ya kashfa Mengi na kituo cha televisheni cha ITV akitaka amlipe fidia ya shilingi moja kwa madai kuwa Mengi alitumia televisheni yake kumkashifu kwa kumuita ‘Fisadi Papa’ na kwamba mmoja wa watu wanaopora rasilimali za Tanzania.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Februali 4 mwaka 2011.

KIKWETE AITAKA MAHAKAMA IJISAFISHE

Na Happiness Katabazi

RAIS Jakaya Kikwete ameomba uongozi wa Mhimili wa Mahakama nchini kuondoa hisia za ukosefu wa uhadilifu zinazowakabili baadhi ya watendaji wa mahakama nchini.

Rais Kikwete aliyasema hayo jana katika sherehe ya siku ya Sheria nchini iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ambapo maudhui ya siku ya sheria mwaka huu ni “ Umuhimu wa elimu kuhusu mahakama kama hatua ya msingi ya utatuzi wa migogoro katika jamii”.

“Leo katika kusherekea siku hii ya sheria minauomba mhimili wa mahakama mambo mawili .Mosi; uadilifu katika utoaji haki…bado kuna hisia ya ukosefu wa uhadilifu kwa watoaji haki ambao ni mahakama kwamba wenye fedha ndiyo wanapata haki na wasiyo na fedha hawapati haki:

“….Uwezo wa kuondoa hisia hizo mbaya upo mikononi mwenu na ninatambua sifa za uadilifu mlizokuwa nazo majaji na mahakimu licha miongoni mwenu wamekuwa na sifa za ukosefu wa uhadilifu na kwa taarifa nilizonazo uongozi umekuwa ukiwashughulikia kiutawala”alisema Rais Kikwete.

Aidha Rais Kikwete alisema ombi lake la pili kwa mhimili wa mahakama linahusu maboresho katika sekta ya sheria, kwamba anaomba maboresho yafanywe kwa kasi kwani kasi ya sasa ya ufanywaji wa maboresho ya sheria ni ndogo na kwamba wabia wa nchi katika sekta hiyo wameishaanza kulalamikia utendaji wa programu hiyo ya maboresho kwamba inasuasua hali inayosababisha wabia wetu kurudisha fedha ambazo awali zilitengwa kwaajili ya maboresho ya sheria na kuongeza kuwa changamoto nyingine zinazoikabili mahakama hivi sasa kwa asilimia fulani zinachangiwa na kasi hiyo ya kusuasua ya sekta ya maboresho ya sheria.

Hata hivyo Rais Kikwete aliutaka mhimili wa mahakama kushirikiana na vyombo vya habari kutoa elimu kwa umma kuhusu tendaji kazi, na muundo wa mahakama ukoje kwani kwakufanya hivyo pia kutamuondolea adha anayoipata hivi sasa kwani baadhi ya wananchi ambao kesi zao mahakamani zimekwisha amriwa na wakashindwa katika kesi hizo ,kila kukicha wamekuwa wakifika ofisini kwake Ikulu wakimuomba atengue hukumu hizo kwakuwa yeye ni rais wa nchi na kwamba ana mamlaka ya kutengua.

“Ndiyo maana leo hii nasisitiza mahakama ione umuhimu wa kushirikiana na vyombo vya habari kikamilifu kutoa elimu kwa umma kuhusu utendaji na muundo wa mahakama kwani kuna wananchi wamekuwa wakijazana pale ofisini wakitaka nitengue hukumu zilizokwishatolewa na mahakama na mimi nimekuwa nikiwaambia sina mamlaka ya kufanya hivyo… wananchi hao wamekuwa wakinijibu kama siwezi kufanya hivyo watamchagua rais anayeweza kufanya hivyo na kwamba ndiyo maana wanataka Katiba mpya…lakini yote hii inasababishwa na umma kuwa na uelewa finyu wa sheria na muundo wa mahakama.’alisema Kikwete nakusababisha watu kuangua vicheko.

Aidha kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman alisema bado mahakama inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa fedha, majengo na rasilimali watu na hivyo kumuomba rais aongezee bajeti mhimili huo.

“Mahakama itaendelea na mikakati maalum ya kuongeza kasi ya usikilizaji na umalizikaji wa kesi, tutakumbushana, tutawajibishana,tutarekebisha kanuni zenye mafumbo, tutarahisha taratibu,tutabadilisha zile za kale,tutawaelimisha zaidi na kuwasimamia mahakimu.Tutawaandika majaji wastaafu”alisema Jaji Mkuu Othman.

Awali mshereheshaji wa sherehe hiyo ambaye ni Msajili wa Mahakama ya Rufani, Francis Mutungi alisema sherehe hizo ni kiashiria cha kuanza kwa mwaka mpya wa mahakama na kwamba sherehe hiyo kwa mwaka huu itakuwa ni tofauti na miaka iliyopita kwani itaendeshwa kwa lugha ya Kiswahili na siyo Kiingereza nakwamba huko ni kukukuza lugha ya Kiswahili na hotuba zote jana ziliandika na kusomwa kwa lugha ya Kiswahili hali iliyopokelewa kwa furaha na waudhuliaji wengi ambao katika sherehe za miaka iliyopita walikuwa wakipata wakati mgumu kuelewa baadhi ya maneno ya kisheria yaliyokuwa yakisomwa kwenye hotuba za wanasheria.

Wakati huo huo katika hali isiyotarajiwa Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), Freeman Mbowe aligeuka kivutio wakati akiinuka kwenye kiti alichokaa kuelekea kwenye ngazi za mahakama kuu kwaajili ya kushiriki na viongozi mbalimbali wa serikali na mahakama kupiga picha, ambao watumishi wa mahakama, mawakili na wananchi mbalimbali walioudhulia sherehe hiyo walioanza kumshangilia kwa sauti ya juu ‘Mbowe Mbowe,Mbowe’ na kiongozi huyo kulazimika kuwapungia mkono na kutabasamu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Februali 3 mwaka 2011

JWTZ WATOA BOTI KIGAMBONI

Na Happiness Katabazi

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limetoa boti zake mbili kwa ajili ya kusaidia usafiri katika kivuko cha Kigamboni.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya Jeshi hilo iliyosambazwa jana mchana kwa vyombo vya habari, ilieleza kuwa boti hizo za Kamandi ya Wanamaji-Kigamboni zinatoa msaada huo wa kuvusha abiria kutokana na kusitishwa kwa kivuko kikubwa (pantoni) kiitwacho MV Magogoni baada ya kupata hitilafu ambayo isingewezekana kuendelea na shughuli zake.

“Boti hizo mbili za JWTZ zimekuwa zikivusha abiria tangu Januari mosi mwaka huu kati ya Kigamboni na Magogoni na kutoka Magogoni kuelekea Kigamboni hadi pantoni ya mv Magogoni itakapokuwa tayari kwa kazi hiyo,” ilieleza taarifa hiyo.

Aidha, ilisema kitendo cha JWTZ kutoa huduma au msaada kwa wananchi ni sehemu ya majukumu yake ya msingi ya kusaidia wananchi na mamlaka za kiraia pale yanapotokea matatizo au majanga yanayohusu jamii moja kwa moja.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa huduma hiyo ni moja ya huduma nyingi ambazo JWTZ lilishatoa na litaendelea kufanya hivyo wakati wote panapohitajika msaada wa dharura.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Februali 3 mwaka 2011

WAFANYAKAZI WA KAMPUNI YA FREE MEDIA LTD ,WAKIUKARIBISHWA MWAKA 2011 KWA KISHINDO

Happiness Katabazi ambaye ni mwandishi wa habari mwandamizi akigonganisha glasi na mgeni rasmi katika sherehe hiyo, Freeman Mbowe.

****************************************************
Mbowe aiongezea mtaji Free media Saccos
Mwenyekiti wa makampuni ya Bilicanas Co.Group na Freemedia Ltd, Freeman Mbowe, ameahidi kutoa mtaji wa kutosha kwa kila mfanyakazi kwa ajili ya uanzishwaji wa “Freemedia Saccos” inayolenga kutoa fursa zaidi za mikopo kwa wafanyakazi wa kampuni hizo.
Mbowe aliyasema hayo usiku wa kuamkia jana wakati wa sherehe maalum ya kuukaribisha mwaka 2011 na kupongezana ambazo ziliandaliwa kwa pamoja na viongozi wa kampuni hizo wakiwemo wale wa Freemedia Ltd inayochapisha magazeti ya Tanzania Daima na Sayari.
Katika shughuli hiyo, Mbowe aliwaomba wafanyakazi kuendelea kujituma pamoja na kukabiliana na ushindani wa kibiashara sambamba na kuhakikisha wanafanikiwa kuendesha maisha yao kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya kujipatia kipato.
“Kilio chenu nimekisikia, ni hakika wakuu wenu wa idara wanakamilisha taratibu zote ili kuondoa matatizo yaliyopo, na jambo la msingi ni uwepo wa SACCOS, nimelipokea na nawaahidi nitawasaidia kwa hali na mali,” alisema Mbowe.
Alisisitiza kuwa atatoa wataalam wa kushughulikia suala hilo na mtaji wa kutosha kwa SACCOS hiyo.
Katika shughuli hiyo wafanyakazi kutoka idara zote za makampuni hayo matatu walikutana kwa pamoja na familia zao na kuweza kubadilishana mawazo pamoja na kusherehekea.


Nuru Yanga,Hadija Kalili, Dina Ismail na Iren Mark wakifurahia
Nikienda kugonganisha glasi ya mvinyo na wenzangu
Jinsi Happiness Katabazi nilivyoupamba mkono wangu kwa nakshi ya swaga.
Mhariri Mkuu Mtendaji wa Magazeti ya Tanzania Daima na Sayari Absalom Kibanda wakwanza kushoto, Mwenyekiti wa Makampuni ya Free Media na Bilicanas Group Freeman Mbowe na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hizo Dk. Lilian Mtei Mbowe hawpa wakiiinua glass zao juu kuashiria ufunguzi wa sherehe ya kuuona salama 2011 katika hafla iliyofanyika Jumatatu usiku kwenye ukumbi wa Cassa Complex Mikocheni Jijini Dar es Salaam.Mbowe aiongezea mtaji Free media

Katabazi na Hadija Kalili

Katabazi na Hadija Kalili


Jinsi ninavyopenda nakshi nakshi Happiness Katabazi nilivyopagawisha swaga hili mkononi.

Dk.Lilian Mbowe ambaye ni Mmiliki wa Freemedia Ltd akikata ndafu katika sherehe hiyo.
Hadija Kalili na Makuburi Ally wakisakata rumba.

Katabazi akicheza kisanora na stage show.

Mhariri Mtendaji Absalom Kibanda akitoa akisoma risala katika sherehe hizo

Katabazi akimpatia taarifa Said Michael (WAKUDATA)kwamba mke wake amejifungua mtoto wa kike katika hospitali ya Jeshi Lugalo saa tatu usiku wa siku hiyo ya sherehe ambapo siku hiyo Wakudata ndiye aliyekuwa Mshereheshaji wa sherehe hiyo.

















Katabazi katika pozi


Happiness Katabazi, kabla ya kuanza kwa sherehe ya kufunga na kuukaribishwa mwaka mpya wa 2011 iliyoandaliwa na mmilikiwa kampuni ya Freemedia Ltd, Freeman Mbowe iliyofanyika kwenye ukumbi wa KasaClub iliyopo Mikocheni Dra es Salaam, Januari 31 mwaka huu.

UVCCM KUANDAMANA BODI YA MIKOPO IVUNJWE

• Kuwashirikisha wanafunzi wa sekondari

Na Happiness Katabazi

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umetishia kuitisha maandamano nchi nzima iwapo serikali haitoivunja bodi ya mikopo ya elimu ya juu na kuiunda upya.


Umesema kuwa bodi hiyo hivi sasa imekuwa ikiwanyanysa wanafunzi na kuwa chanzo cha migomo kwa wasomi wa vyuo vikuu hapa nchini.

Tishio hilo limetolewa jana jijini Dar es salaam na Makamu Mwenyekiti wa UVCCM, Taifa, Beno Malisa muda mfupi baada ya kukubaliana na ombi la Shirikisho la wanafunzi wa vyuo vikuu (CCM) mkoa wa Dar es Salaam lililotaka kufanyika kwa maandamano hayo .

Shirikisho hilo lilisema kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kuona kila kukicha migomo ya wanafunzi imekuwa ikitokea na sababu kubwa ni watendaji wa bodi hiyo kutowajibika.
Malisa pamoja na Katibu Mkuu wa umoja huo, Martin Shigela waliishutumu vikali bodi ya mikopo kwamba imeshindwa kazi, na kuwataka viongozi wa bodi hiyo watumie busara zao kuziacha ofisi hizo kabla ya kufukuzwa.

Alibainisha kuwa bodi hiyo imekuwa ikiwanyanyasa wanafunzi na kuichonganisha serikali ya CCM na wasomi hapa nchini.

Alisema kama serikali haitokisikia kilio chao hicho watafanya maandamano ya nchi nzima wakiwashirikisha wanafunzi wa shule za sekondari kwa sababu wao ni wahanga watarajiwa wa bodi hiyo inayofanya ubaguzi na unyanyasaji wakati wa kutoa mikopo.

“Kimsingi tumekubaliana na tamko lenu lililoutaka uongozi wa UVCCM tukaiambie serikali iivunje bodi…sisi tumewaelewa na tunawaahidi kuanzia sasa UVCCM itaandaa maandamano makubwa nchini nzima kuishinikiza serikali iivunje bodi hiyo kwani imekuwa ikiropokaropoka hovyo na kuwanyanyasa wanafunzi.

“Serikali imekuwa ikiipatia fedha bodi ya mkopo kwa wakati, lakini kwa sababu inazozijua imekuwa ikiwacheleweshea wanafunzi hadi wamejikuta wakiishi maisha ya taabu na kuanza kuichukia serikali yao.

“Kila kukicha wanafunzi wamekuwa wakiilalamikia bodi na migomo haiishi…hivi bodi ni dudu gani hadi tuliruhusu liwanyanyase Watanzania wenzetu…tunasema hatukubali lazima tuandae maandamano ya kushinikiza bodi hii ivunjwe,” alisema.

Kwa upande wake, Katibu wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Salum Ally, alisema lengo la mkutano huo ni kutoa tamko la kuipongeza UVCCM la hivi karibuni lililotaka bodi ivunjwe na kuiomba UVCCM iandae maandamano nchi nzima kushinikiza bodi hiyo kuvunjwa na kwamba tamko hilo wamelitoa kwa niaba ya vyuo vikuu vyote nchini.

Ally alisema katika tamko hilo wameainisha matatizo yanayoikabili bodi hiyo likiwamo la kiutendaji kwamba bodi imekuwa na uwezo mdogo wa kuhakiki taarifa zinazotolewa na waombaji wa mikopo.

Pia alisema tatizo lingine ni la utunzaji mbovu wa kumbukumbu za waombaji, hali inayochangia usumbufu kwa wanafunzi.
Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Januari 31 mwaka 2011