MAHITA AUMBUKA TENA


Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali rufaa iliyokuwa imekatwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) mstaafu, Omari Mahita, dhidi ya aliyekuwa msichana wake wa kazi anayedaiwa kuzaa naye.


Katika rufaa hiyo, Mahita alikuwa akiiomba Mahakama Kuu itengue hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni ambayo ilimuamuru kupeleka gharama za matunzo ya mtoto wake Juma Omary Mahita (14) mtoto anayedaiwa kuzaa na msichana huyo Rehema Shabani.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji Fauz Twaib ambapo alisema rufaa hiyo ya madai Na.149/2009 iliwasilishwa mahakamani hapo na mrufani (Mahita) anayetetewa na Charles Semgalawe dhidi ya mrufaniwa (Rehema) anatetewa Frederick Mkatambo toka Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC) akipinga hukumu ya kesi ya madai Na.9/2007 iliyotolewa mwaka 2009 na Hakimu Mkazi Kihawa.

Katika rufaa hiyo Mahita aliwasilisha sababu nne za rufaa ambazo ziliiomba Mahakama Kuu itengue hukumu hiyo ya mahakama ya chini.

Hata hivyo katika hukumu yake, Jaji Twaib, alisema amezisoma sababu zote nne, na hukumu ya mahakama ya wilaya ya Kinondoni na amebaini sababu zote hizo ni dhaifu na zimeshindwa kuishawishi mahakama hiyo iikubali rufaa hiyo na kuongeza kuwa kwa mantiki hiyo mahakama hiyo inakubaliana na hukumu iliyokwishatolewa na hakimu Mkazi Kihawa kuwa ilikuwa ni hukumu iliyokidhi matakwa yote ya kisheria.

Jaji Twaib alisema kwa mujibu wa hati ya madai ya rufaa hiyo, wakili wa mrufani anataja sababu ya kwanza ya kukata rufaa kuwa kesi iliyofunguliwa na Rehema dhidi ya Mahita katika mahakama ya Kinondoni ilifunguliwa nje ya muda
hivyo ilikuwa ikikinzana na kifungu cha tatu cha Sheria ya watoto Waliozaliwa nje ya ndoa (Affiliation Act: Cap 273.

Kwa mujibu wa wakili wa Mahita, alidai kifungu hicho kinataka mwanamke aliyezaa nje ya ndoa atapaswa kumfungulia kesi mzazi mwenzie ndani ya miezi 12 baada ya mtoto kuzaliwa lakini Mrufaniwa (Rehema ) alifungua kesi ile miaka tisa baada ya Juma kuzaliwa.

Katika hilo Jaji alipinga sababu hiyo akisema, “Mahakama hii inatupilia mbali sababu hiyo kwani haina ukweli wala mantiki ya kisheria kwani kifungu hicho cha Sheria ya Watoto waliozaliwa nje ya ndoa, kinasema mwanamke anaweza kuchagua kumfungulia kesi mahakamani mwanamme anayedai amemzalia mtoto na hataki kumpa matunzo ndani ya miezi 12 kuanzia mtoto alipozaliwa au muda wowote ule baadaye,” alisema Jaji Twaib.

Aidha katika sababu ya pili ya wakili huyo wa Mahita, Semgalawe alidai Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni ilikosea pale ilipoukubali ushahidi wa mrufaniwa kuwa Mahita alikataa kwenda kupimwa kipimo cha Vinasaba (DNA) kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na Mkemia Mkuu wa Serikali aliiandikia mahakama ya Kinondoni barua ya Mei 5 mwaka 2009 ambayo inasomeka hivi.

“Naijulisha mahakama yako kuwa ofisi yangu imeshindwa kutekeleza amri iliyotolewa na mahakama yako kwasababu Omar Mahita hajatokea ofisini kwangu na Rehema na mwanae Juma ndiyo wamekuwa wakifika ofisini kwangu kuanzia Aprili 24-27-30 na Mei 4 - 5 mwaka 2009 kwaajili ya kufanyiwa kipimo hicho,” inasomeka barua hiyo ya Mkemia Mkuu kwa mahakama ya wilaya ya Kinondoni.

Wakili Semgalawe alidai pia mrufaniwa katika mahakama ya chini alitoa ushahidi unaonyesha mkanganyiko wa tarehe; akisema yeye alimzaa mtoto wake Machi 1997 na kwamba mrufaniwa aliondoka nyumbani kwa mrufani Oktoba 1996 na kwamba alikuwa na ujauzito Mei 1996.

Na Mahita katika ushahidi wake alidai kuwa mwaka 1995 alikuwa Moshi wakati Rehema anadai kipindi hicho alikutana na kufanya tendo la ndoa na Mahita mwaka 1996.

Pia Mahita alihamishwa mwaka 1996 kwa hiyo haikuwezekana kwenda kitandani na mrufani Mei 1996 Moshi wakati tayari alikuwa ameishateuliwa kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini na alikuwa akiishi Dar es Salaam, na kwamba tayari mrufani alikuwa ameishapata uhamisho kutoka Moshi kwenda Arusha mwaka 1996.

Jaji Twaib alisema anakubaliana na kipisi cha ushahidi kilichotolewa na wakili Semgalawe unaoonyesha mrufaniwa alichanganya tarehe za yeye kupata ujauzito na kumzaa Juma lakini mrufani wakati akitoa ushahidi wake katika mahakama ya chini alieleza kuwa alivyoteuliwa kuwa IGP aliandaa ‘Maulid’ na mrufaniwa na mwanae walihudhuria na hakuwafukuza kwa sababu mkewe hakuwaona.

“Kama ni kweli Mahita aliteuliwa kuwa IGP mwaka 1996, sioni sababu ya kutofautiana na hilo na kwa mujibu wa mrufani alieleza aliaandza Maulid na alikwenda Arusha na mwanaye Juma siku hiyo na kwamba mtoto wao huyo alizaliwa kipindi hicho hicho cha mwaka 1996 …kwa kuwa mrufani alijichanganya kutaja tarehe hizo na alidai kupata ujauzito wakati akifanya kazi nyumbani kwa Mahita ….kwa mantiki hiyo nakubaliana na wakili wa mrufani kuwa mrufaniwa alijichanganya kutaja tarehe hizo na mahakama hii inatupilia mbali sababu hiyo ya pili kwa sababu utata huo wa tarehe unatatulika.

“Kwa maelezo hayo ya sababu ya pili na ushahidi uliotolewa na barua ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa mahakama hiyo ya chini na kwa mazingira hayo na vitendo vile vilivyokuwa vikifanywa na Mahita vya kushindwa kwenda ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali mara tano kupimwa DNA,
“Mahakama hii imefikia uamuzi wa kumuona Mahita alikataa kupimwa kipimo hicho licha ya kuwa hakusema wazi wazi kuwa hataki kupimwa kipimo hicho cha vinasaba….hivyo basi mahakama hii inaitupilia mbali sababu hii ya pili,” alisema Jaji Twaib.

Aidha alisema sababu ya tatu ilikuwa ikiiomba mahakama hiyo itengue hukumu ya mahakama ya chini iliyomtaka mrufani kila mwezi ampatie mrufaniwa sh 100,000 kwaajili ya matunzo ya mtoto kwasababu kiwango hicho cha fedha kinakwenda kinyume na Sheria ya watoto waliozaliwa nje ya ndoa (Affiliation Act) , inayomtaka mzazi atoe shilingi 100 na kwamba hata baadaye sheria hiyo ilipofanyiwa marekebisho mwaka 2002, kiwango hicho cha sh 100 hakijaondolewa kwa hiyo sheria na mahakama ya chini ilijipangia kiasi hicho cha sh 100,000 kinyume cha sheria hiyo.

Jaji Twaib katika uamuzi wake wa sababu hiyo ya tatu, alisema anaitupilia mbali kwani ni kweli sheria hiyo inataka mzazi atoe fedha ya matunzo ya shilingi mia moja lakini kutokana na kupanda kwa gharama za maisha kiasi hicho cha fedha hakiwezi kutumika kugharamia matunzo ya mtoto.

Katika hilo mahakama hiyo nayo ilikubaliana na uamuzi wa mahakama ya chini iliyomuamuru Mahita kupeleka sh laki moja kwa mzazi mwenzake kwa ajili ya matunzo ya mtoto.

Aidha jaji huyo alisema sababu ya nne, mrufani alikuwa anaomba mahakama hiyo itengue uamuzi wa mahakama ya chini ukimtaka mrufani alimpe mrufaniwa fidia kuanzia mwaka 2003 na siku ambayo hukumu ilitolewa na mahakama hiyo ya chini kwani Mahakama haikurekodi kuwa mrufani alikuwa akimtunza mtoto muda wote na kwamba mrufaniwa alikuwa alikuwa akihudumiwa tangu mwaka 1997 ambapo mtoto huyo alizaliwa.

Wakili wa Mahita alidai Hakimu wa Mahakama hiyo alikosea alipomtaka mrufani alipe gharama za matunzo kuanzia mwaka 2003 ambapo mwanamke huyo alidai Mahita alisitisha matunzo na kumuitia askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia(FFU) kumfukuza wakati alipokuwa akienda kufuata gharama za matunzo.

“Nimesoma hukumu hiyo na hakimu yule alitoa amri ya kumtaka mrufani alipe fidia kwa mrufaniwa tangu siku mtoto alipozaliwa hadi siku ya hukumu ilipotolewa mwaka 2003 ya sh 100,000, hivyo sababu hii ya nne ya mrufani kwamba hakimu alijichanganya kutoa amri hiyo haina msingi na hivyo mahakama hii leo inatamka kuwa rufaa iliyokuwa imefunguliwa mahakamani hapo na Mahita dhidi ya Rehema imetupiliwa mbali na ninamwamuru mrufani amlipe mrufaniwa gharama za uendeshaji kesi hii,” alisema jaji Twaib.

Baada ya hukumu hiyo kutolewa, dada huyo anayedai kuzaa na Mahita, Rehema, alisema amefurahishwa na uamuzi huo wa mahakama kwani umezingatia haki na kusema kwamba mwanaye Juma Omar Mahita hivi sasa ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari ya Hananasif Kinondoni jijini Dar es Salaam, na kwamba yeye binafsi kwa sasa ni mwalimu wa madrasa ya Taqwa baada ya kuachana na biashara ya kuuza karanga.

Mwaka 2009, Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni ilitoa hukumu katika kesi ya madai iliyokuwa imefunguliwa na Rehema aliyewekewa mawakili wa (LHRC) dhidi ya Mahita akiomba mahakama hiyo itoe amri itakayomlazimisha Mahita kumtunza yeye na mtoto wake kwa sababu kiongozi huyo mstaafu aligoma kutoa fedha za kumtunza mtoto huyo anayedaiwa kuwa ni wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Juni 25 mwaka 2011.

JAJI ATAKA USHAHIDI KESI YA MPENDAZOE,MAHANGA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imezitaka pande mbili katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 wa Jimbo la Segerea iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo, Fred Mpendazoe (CHADEMA) dhidi ya Mbunge wa sasa, Dk. Makongoro Mahanga (CCM) na wenzake kuwasilisha haraka iwezekavyo orodha ya nyaraka za ushahidi wanazokusudia kuzitumia katika kesi hiyo.


Mbali na Dk. Mahanga anayetetewa na wakili wa kujitegemea Jerome Msemwa, wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo ambao nao wanatetewa na wakili wa serikali, Patience Ntwina. Mpendazoe anatetewa na wakili wa kujitegemea, Peter Kibatala.

Jaji Profesa Ibrahim Juma, alitoa rai hiyo jana wakati kesi hiyo ilipokuja kwa kutajwa na kuongeza kuwa kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi ya mwaka 2010, kesi ya uchaguzi inapaswa imalizike ndani ya miezi 12 tangu ilipofunguliwa. Mpendazoe alifungua kesi hiyo Novemba mwaka jana mahakamani hapo.

“Kesi hii ni ya uchaguzi na imefunguliwa chini ya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010 ambayo inataka kesi imalizike kusikilizwa ndani ya miezi 12 tangu ilipofunguliwa …sasa ili twende na muda huo, mahakama inazitaka pande zote kuwasilisha orodha ya nyaraka za ushahidi haraka iwezekanavyo,” alisema Jaji Profesa Juma.

Kabla ya Jaji Juma kutoa rai hiyo, wakili wa serikali, Patience Ntwina, alisema kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa, hivyo kuomba mahakama iwapatie siku 14 kuanzia jana, ili waweze kuwasilisha majibu ya hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho ambayo yaliwasilishwa mahakamani hapo Juni 20 mwaka huu.

Kuwasilishwa mahakamani kwa hati hiyo iliyofanyiwa marekebisho, kulitokana na utekelezaji wa amri iliyotolewa na Jaji Juma, Juni 6 mwaka huu, ambapo aliamuru hati ya madai ikafanyiwe marekebisho kwa kuviondoa vituo 10 vya kupigia kura ambavyo mlalamikaji hakuvitaja kwa majina.

Baada ya kufanyiwa marekebisho, Wakili Kibatala alisema hivi sasa hati hiyo inasomeka kuwa wamebakiwa na vituo vya kupigia kura 249 ambapo vituo 120 ni vya Kata ya Kiwalani na vituo 129 ni vya Kata ya Vingunguti.

Jaji Juma aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 12 mwaka huu ambapo kesi hiyo itatajwa na kupanga tarehe ya kuanza kusikilizwa.

Novemba mwaka 2010 Mpendazoe alifungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo ambayo yalimtangaza mbunge wa sasa Dk. Mahanga kuwa ndiye mshindi kwa sababu uchaguzi huo ulikiuka matakwa ya sheria ya uchaguzi ya mwaka 2010.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Juni 23 mwaka 2011.

AG,WAZIRI WATAKA KESI YA KIKATIBA IFUTWE


Na Happiness Katabazi
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali , waziri wa Nishati na Madini na Shirika la Umeme (TANESCO), wameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iifukuze kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na wabunge watatu wa Chama cha Mapinduzi(CCM) na raia wengine wa nne dhidi yao kwa madai kuwa kesi hiyo imefunguliwa hayana mantiki ya kisheria.

Mwanasheria Mkuu,waziri wa Nishati na Madini na Tanesco ni wadaiwa katika kesi hiyo ya Kikatiba Na.5/2011 iliyofunguliwa mapema mwaka huu na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe (CCM), George Simbachawene, Mbunge wa Karagwe (CCM), Gosbert Blandes na Mbunge wa Viti Maalumu, Angellah Kairuki chini Ibara ya 27(1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Wengine katika orodha ya waliofungua kesi hiyo ni raia wa kawaida, Hassan Ngoma, Senkoro Izoka, Salum Kambi na Salma Shomari Mohamed, ambao wanatetewa na wakili wa kujitegemea Mpare Mpoki na Kampuni ya Uwakili ya Lukwaro, wakiliomba Jopo la Majaji watatu Jaji Njegafibili Mwaikugile, Agustine Shangwa na Projestus Lugazia kutoa amri ya kuizuia serikali isilipe fidia ya sh bilioni 94 kwa Kampuni ya Dowans Holdings SA na Dowans Tanzania Ltd.

Kesi hiyo ambayo jana ilikuja kwaajili ya kutajwa na iliarishwa hadi Julai 4 mwaka huu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wenzake waliwasilisha pingamizi hilo lenye sababu sita la kutaka kesi hiyo ifutwe kwasababu maombi yaliyopo ndani ya hati hiyo ya madai hayana msingi, yameletwa mahakamani kinyume cha sheria na kwamba ubovu huo wa hati hiyo ya madai ya walalamikaji ni matumuzi mabaya ya sheria za nchi.

Kwa mujibu wa pingamizi hilo la wadaiwa ambalo Tanzania Daima inayo nakala yake walalamikaji wanaomba kesi kesi hiyo itupwe kwa gharama kwa sababu hati ya madai imekiuka taratibu na kanuni za uletaji madai ya Kikatiba kama Sheria ya Utekelezaji haki za binadamu na wajibu (Basic Rights and Duties Enforcement Act Cap 3 R.E 2000)

Sababu nyingine, wadaiwa wanaomba kesi hiyo itupwe kwasababu walalamikaji wametumia vifungu vya sheria visivyo sahihi kuwasilisha madai yao na kwamba na kwamba wadaiwa hao wameshindwa kutaja ibara zilizovunjwa na wadaiwa kwasababu kifungu cha 6 cha Sheria ya ya Utekelezaji haki za binadamu na Wajibu ambacho kinamlazimisha mlalamikaji katika kesi husika kutaja kwenye hati yake ya madai Ibara ambazo anadai mdaiwa amezivunja.

Aidha walidai hati hiyo madai ilishindishwa kumuunganisha mdaiwa mwingine muhimu ambapo hata hivyo Mwanasheria Mkuu wa serikali hakumtaja kwa jina mtu huyo.

“Kwa mapungufu hayo yaliyokuwepo kwenye hati ya madai ya walalamikaji, ndiyo maana sisi wadaiwa tumewasilisha pingamizi hilo lenye sababu sita mahakamani na tunaomba kesi hiyo itupiliwe mbali kwa gharama kwasababu hati hiyo ya madai ya Kikatiba ina udhahifu mwingi wa kisheria” alidai Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mapema mwaka huu, wabunge wa tatu wa CCM na wananchi wa kawaida wa nne walifungua kesi ya Kikatiba mahakamani hapo chini ya Ibara ya 26(2) inasema: “Kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na sheria za nchi.”

Ibara ya 27(1) inasema: “Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya mamlaka ya nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.”

Ibara ya 27(2) inasema: “Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.”

Walalamikaji hao kwa mujibu hati yao ya madai wanaiomba mahakama itoe amri ya kuizuia serikali isiilipe kampuni ya Dowans na endapo malipo hayo yatafanywa kwa kampuni hiyo ni wazi wadaiwa hao ambao wanaiwakilisha serikali kwa ujumla watakiwa wamevunja ibara hizo za Katiba ya nchi ambayo mahakama hiyo ina wajibu wa kuilinda ibara hizo zisivunjwe.


Simbachawene anadai kuwa tuzo iliyotolewa na ICC kwa Dowans Novemba 30 mwaka 2010, inakwenda kinyume cha Katiba ya nchi na inajaribu kufuja fedha za umma.Na tuzo hiyo ipo kinyume cha sheria kwa madai kuwa inakinzana na maazimio ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambalo kupitia mjadala juu ya ripoti ya kamati teule ya Bunge kuhusu mkataba tata wa TANESCO na Richmond, liliwahi kuweka wazi kwamba mkataba huo ulikuwa ni batili.

Aidha, alidai kuwa tuzo hiyo Dowans ikilipwa itakuwa ni kwenda kinyume cha sera za nchi na kwamba haiwezi kutekelezwa na mahakama za Tanzania.

“Kwa sababu hizo hapo juu tunaomba mahakama hii itoe amri ya kuwazuia wadaiwa wasijaribu kulipa fidia hiyo kwa Kampuni ya Dowans kwa sababu tuzo hiyo ni batili kisheria, inakinzana na maazimio ya Bunge na haiwezi kusajiliwa na mahakama za hapa nchini na inakwenda kinyume cha sera za nchi na kitendo cha kuilipa fidia kampuni hiyo basi ni wazi serikali itakuwa imevunja Katiba ya nchi”, alidai Simbachawene.

Simbachawene na wenzake wanaeleza kuwa mdaiwa wa kwanza ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ni mshauri wa sheria wa serikali na mdaiwa wa pili ni waziri wa Wizara ya Nishati na Madini, ambaye ndiye mwenye jukumu la mdaiwa wa pili la masuala ya umeme.

Kwamba Juni 21 mwaka 2006 mdaiwa wa tatu (Tanesco) chini ya maelekezo ya mdaiwa wa pili (waziri) waliingia mkataba na Kampuni ya Richmond Develepment Company LLC ya Texas Marekani kwa makubaliano yaliyojulikana kama “Power Off Take Agreement” wa kusambaza umeme wa megawati 100.

Lakini Kampuni ya Richmond ilidanganya na haikuweza kuzalisha umeme huo kwa wakati na wakati wanaingia mkataba huo hakukuwa na mwanasheria wa Serikali ya Tanzania wala wa Marekani.

Hati hiyo ya madai inasema, kwa kitendo hicho mdaiwa wa pili ambaye ni Waziri wa Nishati na Madini alikuwa amevunja kifungu cha 38,31(1)(a) na 31(1)(b) na 31(2) ,42(a) na 59(1) vya Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004.

Kwa maana hiyo utaratibu wote wa kuipatia tenda kampuni hiyo ulikuwa batili na ulikiuka vifungu hivyo vya sheria ya manunuzi ya umma.

Akiendelea kuchambua makubaliano yaliyoingiwa, alidai kuwa Kampuni ya Richmond ilipaswa kuanza kusambaza umeme ndani ya siku 150 kuanzia siku ambapo mkataba baina ya Tanesco na kampuni hiyo ulisainiwa, ambayo ni Juni 23 mwaka 2006 na muda wa kuanza kazi hiyo kwa mujibu wa makubaliano ulikuwa ni Februari 2 mwaka 2007.

Walalamikaji hao walidai tangu hapo hadi Desemba mwaka 2006 Kampuni ya Richmond ilishindwa kutekeleza kwa vitendo makubaliano hayo hali iliyosababisha mdaiwa wa tatu (Tanesco) kuandika barua kwa mdaiwa wa pili (waziri) ya kumwomba avunje mkataba huo kwa sababu Richmond imeshindwa kutimiza makubaliano waliyokubaliana na kwamba uthibitisho wa barua hiyo wanao.

Pia walidai kuwa Spika wa Bunge aliyepita, Samuel Sitta, Novemba 2007 aliunda Kamati ya Bunge kuchunguza tuhuma kuhusu mkataba huo, ambapo kamati hiyo ilibaini kampuni hiyo haikuwa na uwezo wa kuzalisha kiwango hicho cha umeme, na taratibu za upatikanaji wa tenda zilikiukwa, hivyo kusababisha aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, mawaziri waliowahi kuongoza Wizara ya Nishati na Madini Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi kujiuzulu nafasi zao za uwaziri.

Januari 25 mwaka huu, Dowans iliwasilisha ombi lake la kutaka Mahakama Kuu ya Tanzania ambalo limepewa Na. 8/2011 iisajili tuzo waliyopewa na Mahakama ya ICC na siku chache baadaye Tanesco, LHCR na Timothy Kahoho wakawasilisha hati ya nia ya kupinga ombi hilo la kutaka tuzo hiyo isajiliwe. Kesi hiyo ambayo imekwisha kuanza kusikilizwa mbele ya Jaji Emilian Mushi, itakuja tena kwa ajili ya kutajwa Julai 28, mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Juni 22 mwaka 2011.

MHINDI ALIYEUA MTANZANIA KUNYONGWA


Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemhukumu kunyongwa kwa kamba hadi kufa raia wa India Vinoth Praveen kwa kosa la kumchoma visu hadi kufa Mtanzania, Abdul Basit.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji Dk. Fauz Twaibu aliyesema kwamba mahakama imeridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri.


Katika kesi hiyo ya jinai namba 83/2009 upande wa Jamhuri uliwakilishwa na Wakili wa Serikali Shadrack Kimaro, wakati upande wa utetezi uliwakilishwa na Wakili wa kujitegemea Majura Magafu.

Jaji Dk.Twaibu alisema kwa mujibu wa shahidi wa upande wa Jamhuri Inspekta Mapunda, aliyeieleza mahakama hiyo kwamba aliandaa maelezo ya onyo yaliyotolewa na mshtakiwa ambaye alikiri kufanya mauaji hayo.

Aidha, mshtakiwa alimueleza shahidi huyo kwamba hawezi kumruhusu mtu wake wa karibu kusikiliza anachomueleza shahidi huyo kwa sababu wakati anafanya mauaji hayo alikuwa peke yake na kwamba alifanya hivyo kwa kuwa shahidi huyo alionyesha kumjali.

“Pia kwa mujibu wa ungamo la mshtakiwa alilotoa mbele ya mlinzi wa amani (hakimu) alikiri kutenda kosa hilo kwa sababu mshtakiwa huyo alikuwa akimdai marehemu dola 20,000 za Marekani ambazo walikubaliana zirejeshwe kwa mshtakiwa katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja lakini marehemu alishindwa kumfanya hivyo ndipo mshtakiwa akaamua kumuua.

“…Kwa ungamo hilo la mshtakiwa mbele ya mlinzi wa amani, maelezo ya onyo aliyochukuliwa na polisi ambayo amekiri kutenda kosa hilo na yalipokelewa na mahakama hii kama vielelezo na ushahidi wa mazingira wa kesi hii umethibitisha mshtakiwa alikuwa na dhamira ya kutenda kosa hilo.

“Mahakama hii inatamka wazi kuwa inakubaliana na vilelezo hivyo kuwa ni kweli mshtakiwa huyo alimuua kwa kukusudia mshtakiwa huyo na kwamba adhabu ya mtu anayepatikana na kosa la mauaji hapa nchini ni moja tu, kunyongwa kwa kamba hadi kufa… hivyo mahakama hii inakuhukumu wewe Plaveen adhabu ya kunyongwa hadi kufa,” alisema Jaji Dk.Twaibu.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Februali 6 mwaka 2009 eneo la Kipata Kata ya Kariakoo jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alimuua marehemu kwa kumchoma visu na mshale mgongoni, tumboni, shingoni na mdomoni kisha kuuweka mwili wake kwenye begi na kuutelekeza kwenye jengo la Harbours View ambayo awali liliitwa JM ALL jijini Dar es Salaam.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Juni 21 mwaka 2011.

'WASHTAKIWA SAMAKI WA MAGUFULI WANA KESI YA KUJIBU'

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya uvuvi haramu kwenye kina kirefu cha Bahari ya Hindi upande wa Tanzania, umeiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iwaone washtakiwa wana kesi ya kujibu.


Ombi hilo liliwasilishwa jana na Wakili Mwandamizi wa Serikali Biswalo Mganga mbele ya Jaji Augustine Mwarija ambapo aliikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya upande wa Jamhuri kuwasilisha majumuisho ya kesi hiyo, kuwaona washtakiwa wote 36 kuwa wana kesi ya kujibu.

Wakili Mganga aliomba mahakama hiyo izitupe hoja za upande wa utetezi zilizowasilishwa mwishoni mwa wiki zikiiomba mahakama hiyo iwaone washtakiwa wote hawana kesi ya kujibu kwa sababu vielelezo na ushahidi uliotolewa na mashahidi wote 13 wa Jamhuri ni thabiti utaishawishi mahakama iweze kuwaona washtakiwa wana kesi ya kujibu.

Mganga aliyetumia saa nne kuwasilisha hoja zake, alidai kuwa shahidi wa tatu, Kapteni Ernest Bubamba, kutoka Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi aliieleza mahakama kwamba siku ambayo meli ya Tawariq 1 ilikamatwa, aliyeingia melini na kuikaguzi ambapo rada ‘GPS’ ilimwonyesha kuwa meli hiyo ilikamatwa eneo la Tanzania.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, alipomhoji nahodha wa meli hiyo ambaye ni mshtakiwa wa kwanza alikiri kuvua katika eneo hilo na kwamba walikuwa na kibali cha kufanya hivyo.

“Mheshimiwa Jaji, Bubamba katika ushahidi wake alidai kuwa alipotaka kibali hicho, mshtakiwa alimpa kibali kinachoonyesha kilitolewa na Serikali ya Zanzibar Januari 2, 2008 na kinamalizika Aprili 4 mwaka huohuo… kilitolewa kwa meli ya Tawariq 2 siyo Tawariq 1 iliyokuwa ikitumiwa na washtakiwa. Meli hiyo ni kielelezo pia,” alidai wakili Mganga.

Wakili huyo alidai kwamba shahidi huyo aliiambia mahakama kuwa wakati akiikagua meli hiyo alikuta baadhi ya samaki wakivuja damu, wengine wamehifadhiwa kwenye majokofu.

“Upande wa Jamhuri tunadiriki kusema tumeweza kuthibitisha kesi yetu kikamilifu kwani washtakiwa wanakabiliwa na kosa la kuvua bila leseni, ni kweli leseni aliyokutwa nayo mshtakiwa wa kwanza inaonyesha ilitolewa kwa meli ya Tawariq 2 na siyo Tawariq 1 na leseni hiyo ilikwisha muda wake na wewe jaji umeipokea kama kielelezo.

“Pia rada ya meli hiyo GPS ilisoma meli hiyo kati ya Januari 10 na Machi 8 mwaka 2008 meli hiyo ilikuwa ikivua katika eneo hilo, ni kwa nini samaki hao wawe wanavuja damu katika kipindi hicho walichokamatwa?” aliuliza Mganga.

Jaji Mwarija aliahirisha kesi hiyo hadi leo ambapo upande wa Jamhuri utaendelea kuwasilisha hoja zake za kuishawishi mahakama iwaone washtakiwa hao ambao hadi sasa wanasota rumande baada ya kunyimwa dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Juni 21 mwaka 2011.

DIWANI CCM JELA MIAKA 10 KWA RUSHWA

Na Happiness Katabazi, Tunduru

MAHAKAMA ya Wilaya ya Tunduru, imemhukumu kifungo cha mika 10 jela na faini ya sh milioni 6.7 Diwani wa Viti Maalum (CCM) Kata ya Mlingoti, Atindanga Mohammed kwa makosa 11 ya rushwa.


Hukumu hiyo ya aina yake ilitolewa jana na Hakimu Shemuli Cyprian baada ya mahakama hiyo kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka ambapo diwani huyo aligawa vitenge na kanga kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.

Katika kesi hiyo upande wa mashtaka uliwakilishwa na wakili wa serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Christa Kadekenga.

Hakimu Cyprian alisema mshtakiwa huyo alikuwa akikabiliwa na makosa 15 ya kushawishi na kutoa rushwa kwa wapiga kura 15 ili wampigie kura za ndiyo ashinde udiwani huo ambapo alitoa doti 12 za kanga na doti tatu za vitenge kwa wapiga kura hao.

“Mahakama hii imeridhika na ushahidi na vielelezo vilivyotolewa na upande wa Jamhuri…inakutia hatiani kwa makosa 11 na kukufutia makosa mengine manne kwa sababu upande wa Jamhuri katika kesi hii umeshindwa kuthibitisha makosa hayo,” alisema hakimu Cyprian.

Baada ya hukumu hiyo diwani Atindanga, aliangua kilio ndani ya mahakama kisha kupakizwa kwenye karandika kwa ajili ya kupelekwa gerezani kuanza kutumikia kifungo hicho.

Katika uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani uliofanyika nchini kote mwaka jana, madai ya kuwepo kwa rushwa yalitawala licha ya Rais Jakaya Kikwete kutia saini Sheria ya Matumizi ya Fedha za Uchaguzi.

Hata hivyo ushindi wa baadhi ya madiwani na wabunge umepingwa mahakamani, mengi ni madai ya rushwa kwenye uchaguzi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Juni 21 mwaka 2011.

WASHTAKIWA SAMAKI WA MAFUGULI HAWANA HATIA-MAWAKILI

Na Happiness Katabazi
UPANDE wa utetezi katika kesi ya uvuvi haramu katika kina kirefu cha Bahari ya Hindi maarufu kama kesi ya ‘Samaki wa Magufuri’inayowakabili raia 36 wa kigeni, umeiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, uwaone washtakiwa wote hawana kesi ya kujibu kwasababu upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi yao.

Maombi hayo yalitolewa Juni 16-17 mwaka huu na mawakili wa washtakiwa Ibrahim Bendera na John Mapinduzi mbele ya Jaji Agustine Mwarija wakati kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya upande wa utetezi kuwasilisha majumuisho ya kesi hiyo yanayowaona washtakiwa hao hawana kesi yakujibu kwa njia ya mdomo ambapo upande wa jamhuri nao utawasilisha majumuisho yao Juni 20 mwaka huu.

Wakili Bendera alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa Sheria mama ya Uvuvi katika kina kirefu(The Deep Sea Fishing Authority) Act Cap 388 ilitakiwa ianze kazi kwa tango la Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi wakati huyo alikuwa John Magufuri ambalo waziri huyo alilitangaza kwenye gazeti la serikali Na.138 , Agosti 15 mwaka 2009 na akaisaini tangazo hilo Julai 21 mwaka 2009 na waziri huyo ndani ya tangazo hilo akasema sheria hiyo mama itaanza kufanyakazi Julai 1 mwaka 2008.

Bendera alidai kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Tanzania ya Kutafsiri Sheria (Interpretation of Laws Act Cap 1) kifungu cha 17 kinatoa mamlaka kwa waziri yoyote katika tangazo lake la kutaka sheria mama anayoitunga ianze kazi kabla ya tarehe aliyoisaini tofauti na sheria ndogo ndogo ambazo zinaweza kuanza kutumika kabla ya waziri kusaini sheria hiyo.

“Kwa maelezo hayo hai niliyoyatoa hapo juu kwamba sheria hiyo iliyotumika kuwafungulia mashtaka washtakiwa ilitungwa kabla ya washtakiwa kukamatwa na kwa maana hiyo wakati washtakiwa hao wanakamatwa Machi 7 mwaka 2009 Tanzania ilikuwa haina sheria hiyo.Waziri Magufuri alisaini tangazo Julai 21 mwaka 2009 na kusema sheria hiyo itaanza kufanyakazi Julai 1 mwaka 2008….kwa hiyo mheshimiwa Jaji sisi tunasema waziri alikosea kufanya hayo aliyoyafanya kwani duniani kote siku sheria inapo saini ndiyo siku hiyo inapoanza kufanyakazi sasa huyu waziri kasaini sheria hiyo mwaka 2009 halafu tena kwa maandishi anasema sheria hiyo itaanza kutumika kuanzia mwaka 2008”alidai wakili Bendera.

Aidha alidai kifungu cha 3 cha Sheria ya Uvuvi katika kina kirefu, inasema mtu mwenye mamlaka ya mwisho kwenye shughuli zote za meli ya uvuvi ni keptaini lakini cha kushanga upande wa Jamhuri umewakamata na kuwafungulia kesi hata wapishi na wafagizi wa meli ya Tawariq 1 ambao ni miongoni wa washtakiwa katika kesi hiyo.

Aliendelea kudai kuwa sababu nyingine ya kutaka mahakama hii iwaone hawana kesi ya kujibu ni kwamba mashahidi wote 13 wa upande wa Jamhuri walieleza mahakama kuwa meli hiyo haikuwa na usajili, bendera ya taifa lililotokea,ambapo alidai kuwa mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao ni uvuvi kwenye kina kirefu cha bahari ya hindi hila leseni na kuchafua mazingira katika eneo hilo na kwamba jamhuri hawakuwashtaki washtakiwa hao kwamba walikuwa wakiendesha meli hiyo ikiwa haina bendera wala kuwa na usajili na kwamba washtakiwa ambao ni wapishi na wafagizi hawawezi kufahamu hati ya usajili ipo wapi na wala meli hiyo kama ina bendera.

Aidha aliendelea kuchambua kuwa Sheria ya Kimataifa ya Mambo ya Bahari ,inaitaka nchi yoyote inayotoa kutoa uhuru kwa vyombo vinavyopita baharini kama meli kupata haki stahili na pindi nchi moja inapobadili au kutungusha sheria kuhusu mambo ya bahari nchi hiyo italazimika kutoa taarifa na kuisambaza sheria hiyo kwa nchi wanachama ili waielewe sheria hiyo inasemaje na kuongeza kuwa kwa muktadha huo hadi washtakiwa hao wanakamatwa serikali ya Tanzania haikuwa imesambaza sheria hiyo kwa nchi wanachama.

Hata hivyo alidai kwa mujibu wa vielelezo na mashahidi wote 13 wa Jamhuri waliotoa ushahidi, hakuna shahidi hata mmoja aliyetoa ushahidi unaothibitisha kuwa aliwaona washtakiwa hao na meli ya Tawariq 1 walikuwa wakivua samaki na kuaribu mazingira katika kina kirefu cha Bahari ya Hindi katika Ukanda wa Tanzania na kuongeza kuwa anaomba mahakama hiyo iwaaone washtakiwa wote hawana kesi ya kujibu na hivyo iwaachilie huru.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Juni 20 mwaka 2011.

MFUNGWA MSOMI ASHINDA RUFAA

Na Happiness Katabazi
HATIMAYE Mahakama ya Rufani nchini imemfutia adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela yule mfungwa aliyepata Shahada ya kwanza ya Sheria katika Chuo Kikuu Huria(OUT) akiwa gerezani,askari mpelelezi wa Jeshi la Polisi E.6937 D/C Haruna Pembe Gombela baada ya kubaini huku zote zilizotolewa na mahakama za chini zilimtia hatiani kimakosa.


Uamuzi huo wa Mahakama ya Rufani nchini unatokana na rufaa Na.44/2006 iliyokatwa mahakamani hapo na mrufani Gombela ambaye alikuwa akiishi katika Gereza Ukonga dhidi ya Jamhuri aliyoomba mahakama hiyo ya juu nchini itengue hukumu ya ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam iliyotolewa na Jaji Katherine Orioyo Oktoba 31 mwaka 2005, ambayo pia nayo ilikubaliana na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Ilala katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha Na.1426/1990 ambazo hukumu zote hizo zilimtia hatiani kwa kosa hilo na kumhukumu kwenda jela miaka 20.

Jopo la majaji watatu wa mahakama ya rufani waliokuwa wakisiliza rufaa ya Gombale ambalo lilikuwa likiongozwa na jaji Eusebio Mnuo,Steven Bwana na Sauda Mjasiri walisema hawana sababu ya kutofautiana na upande wa Jamhuri kwasababu jopo hilo limeridhika kuwa gwaride la utambulisho lilofanywa kumtambua mrufani halikuacha mashaka.

Jaji Mnuo alisema mahakama za chini zilimtia hatiani mrufani huyo kwa kuegemea ushahidi maelezo ya onyo yaliyotolewa kama ushahidi dhidi ya mrufani na ambapo mshtakiwa huyo wa tatu alishachiwa huru na mahakama za chini, ambapo jaji huyo alisema kwa mujibu wa kifungu cha 33(2) cha Sheria ya Ushahidi ya Tanzania ya mwaka 2002, vinasema ushahidi utakaotolewa na mshtakiwa mmoja dhidi ya mshtakiwa mwenzake ambao wanakabiliwa katika kesi mmoja, haupaswi kutumiwa na mahakama kumtia hatiani mshtakiwa mwingine ambao ushahidi huo ulimtaja.

“Kwa hiyo jopo hili linatamka wazi kuwa linatengua hukumu ya Mahakama Kuu iliyomtia hatiani Gombale kwasababu mahakama hiyo ya chini ilimtia hatiani kimakosa kwani mahakama hiyo ilimtia hatiani mrufani huyo kwa kuegemea ushahidi wa maelezo ya onyo ya mshtakiwa mwenzake na mrufani kwasababu kifungu cha 33(2) cha Sheria ya Ushahidi, kinakataza mshtakiwa mmoja kutiwa hatiani kwa ushahidi wa maelezo ya onyo ya mshtakiwa mwenzake ambaye anashtakiwa naye kwenye kesi moja na tuna amuru mshtakiwa huyo aachiriwe huru. ”alisema Jaji Mnuo.

Gombela na wenzake ambao siyo wahusika katika rufaa hiyo, walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala na kufunguliwa kesi unyang’anyi wa kutumia silaha Na.1426/1990 ambapo yeye alitiwa hatiani na wenzake kuachiliwa huru. Lakini Mkurugenzi wa Mashtaka nchini alidai adhabu hiyo ni ndogo na hivyo DPP alikata rufaa katika Mahakama Kuu ambayo ilipewa Na.155/1992 kwamba kosa walilotiwa nalo hatiani kisheria inapaswa wafungwe jela miaka 30 lakini akadai anashangwa na mahakama hiyo kuwafunga miaka 20 jela.

Wakati Mkurugenzi wa Mashtaka akiwasilisha rufaa hiyo Mahakama Kuu, pia Gombale alikata rufaa dhidi ya hukumu hiyo ambayo ilipewa Na. 84/1992 ambayo hata hivyo mahakama Kuu iliitupilia mbali ili kuruhusu warufani waudhulie katika rufaa Na.155/1992 ambayo nayo pia haikufanikiwa.

Ndipo Gombela alifikia uamuzi tena wa kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa ambao alitoa sababu nane za kukata rufaa ambapo alidai hukumu zilizotolewa dhidi yake na mahakama za chini ambazo zote zilimhukumu kwa kutumia ushahudi wa mshtakiwa mwenzake, mahakama ya wilaya ya Ilala haikufanya usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo (PH) jambo ambalo ni kinyume na cha kifungu cha 192 cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.

Itakumbukwa kuwa miaka ya hivi karibuni Gombale aliandika historia mpya ya kuwa mfungwa aliyefungwa gerezani lakini wakati akitumia adhabu yake katika gereza la Ukonga alipata fursa ya kujiendeleza kielimu ambapo alikuwa akijisomea Shahada ya Sheria katika Chuo Kikuu Huria (OUT) jijini Dar es Salaam, na kutunikiwa shahada hiyo, hali iliyofungua ukurasa mpya katika Magereza ya Tanzania, kuwa mtu kuwa mfungwa siyo kigezo cha kushindwa kujiendeleza kielimu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi,Juni 18 mwaka 2011.

HAPPY BIRTHDAY QUEEN MWAIJANDE (3)


Mwandishi Mwandamizi wa gazeti hili Happiness Katabazi akiwa na mwanae Queen Mwaijande(3) wenye nyuso za furaha katika hafla fupi ya mtoto huyo kutimiza miaka mitatu iliyofanyika nyumbani kwao Sinza C, Dar es Salaam.Queen akiwa mkubwa anasema anataka awe Askari Mpelelezi ‘chatu,nusanusa’ wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS)

HAPPY BIRTHDAY QUEEN MWAIJANDE (3)


Queen Kissa Mwaijande(3) pichani katika hafla fupi ya mtoto huyo kutimiza miaka mitatu iliyofanyika nyumbani kwao Sinza C, Dar es Salaam.Queen akiwa mkubwa anasema anataka awe Askari Mpelelezi ‘chatu,nusanusa’ wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS)

Happiness Katabazi akifurahia jambo na mwanae Queen Juni 8 mwaka huu, siku ambayo mtoto huyo alikuwa akitimiza miaka mitatu.

Happiness Katabazi nikimlisha mwanangu Queen ,keki Juni 8 mwaka 2011 katika hafla fupi ya kukumbuka kwake kuzaliwa ambapo siku hiyo alikuwa akitimiza miaka mitatu.

WASHTAKIWA WASITISHA MGOMO WA KUTOFIKA MAHAKAMANI

Na Happiness Katabazi

WASHITAKIWA nane wa kesi ya uporaji wa sh mil. 150 katika benki ya Standard Chartered jijini Dar es Salaam, ambao wiki hii waliweka mgomo wa kutokwenda mahakamani wameamua kusitisha mgomo huo.

Mgomo huo umesitishwa juzi baada ya kufanyika kwa mazungumzo baina ya uongozi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu na watuhumiwa hao.

Kwa mujibu wa watuhumiwa hao, uongozi huo wa mahakama uliowatembelea gerezani, uliwahidi kuwa
kesi zao zitasikilizwa na katika kipindi cha miezi miwili zitakuwa zimemalizika.

Mei 7, mwaka huu, washtakiwa watano wa kesi nyingine ya uporaji wa zaidi ya sh milioni 233.8 uliofanyika katika duka la kubadilishia fedha za Kigeni la Maksons waligoma kula na kufika mahakamani kutokana na madai ya kutotendewa haki na mahakama.

Mahakama ya Kisutu imeshindwa kuwaleta mashahidi mahakamani tangu kesi hiyo ifunguliwe miaka mitano iliyopita.

Washtakiwa hao ni Martin Mndasha, Eric Mfinanga, Mashaka Mahengi, John Mndasha, Philip Mushi, Rashid Eliakim, Lucas Aloyce, na Jafar Mkenda.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Juni 10 mwaka 2011.

HAKIMU KORTINI KWA RUSHWA DAR

Na Happiness Katabazi

HAKIMU wa Mahakama ya Mwanzo Ukonga jijini Dar es Salaam, Ndevera Kihangu na wenzake wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na makosa ya kushawishi na kupokea rushwa ya sh 100,000.


Mbali na Hakimu Kihangu, washitakiwa wengine ni karani wa hakimu huyo, Eveline Mowo na mhasibu wa mahakama hiyo, Victoria Mtasiwa.

Wakili wa Serikali, Salha Abdallah, mbele ya Hakimu Mkazi, Ritha Tarimo, alidai washitakiwa wanakabiliwa na makosa matatu ya kushawishi na kuomba rushwa ya kiasi hicho cha fedha.

Alidai kosa la kwanza ambalo linamkabili mshitakiwa wa kwanza na wa pili ni kuwa Aprili 24 mwaka huu, katika Mahakama ya Mwanzo Ukonga washitakiwa hao walimshawishi Joyce Msaki awapatie kiasi hicho cha fedha ili wampatie dhamana katika kesi inayomkabili iliyopo katika mahakama hiyo.

Wakili Abdallah alidai kuwa kosa la pili ni la kupokea rushwa ya sh 40,000, ambalo linamkabili mshitakiwa wa kwanza na wa pili. Siku hiyo walipokea kiasi hicho cha fedha kama kianzio cha kumpatia dhamana.

Alidai kosa la tatu ambalo linawakabili washitakiwa wote ni kuwa Mei 27 mwaka huu katika mahakama hiyo, washitakiwa hao walipokea tena sh 60,000 kutoka kwa Msaki.

Washitakiwa wote walikana mashitaka na washitakiwa wawili ambao ni Hakimu Kihengu na Mhasibu Victoria walipata dhamana baada ya kutimiza masharti huku mshitakiwa Mowo alipelekwa mahabusu kwa kushindwa kutimiza masharti na kesi hiyo imeharishwa hadi Juni 22, mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Juni 9 mwaka 2011.

WALIONDAMANA DAR WAPATA DHAMANA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imewapa dhamana wafuasi watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu wanaokabiliwa na kesi ya kufanya maandamano bila kibali.

Wafuasi hao ni Julian Daniel (24) mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), General Kaduma (25) ambaye ni Mwanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na Joseph Mseti (50) ambaye ni mkulima.

Watuhumiwa hao wanatetewa na wakili wa kujitegemea Mabere Marando wakati upande wa jamhuri uliwakilishwa na mwanasheria wa serikali Elizabert Kaganda.

Hakimu Mkazi Sundi Fimbo alisema ameamua kuwapatia dhamana washtakiwa hao ambao walifikishwa kwa mara ya kwanza juzi baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambayo yaliwataka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya sh milioni nne.

Hakimu Fimbo aliahirisha kesi hiyo hadi Juni 21 mwaka huu, itakapopelekwa kwa kwaajili washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Washtakiwa hao walikamatwa Juni 5, mwaka huu jijini Dar es salaam walipokuwa wakiandamana bila kibali kushinikiza kuachiwa huru kwa Mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe aliyekuwa akishikiliwa na polisi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Juni 8 mwaka 2011.

WASHTAKIWA WA UNYANG'ANYI WAGOMA KWENDA KORTINI

Na Happiness Katabazi

MAHABUSU watano kati ya tisa wanaokabiliwa na kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kuiba ya milioni 233 katika duka la kubadilishia fedha za kigeni la Maxson Bureau Change jana waligoma kwenda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam.

Watuhumiwa hao waliamua kutohudhuria kesi yao hiyo wakishinikiza kuonana na uongozi wa juu wa mahakama nchini kwa lengo la kuwaeleza matatizo yanayowakabili.

Mahabusu hao kuanzia juzi walianza mgomo wa kutokula chakula na jana kuendeleza mgomo huo kwa kukataa kwenda mahakamani kushinikiza kutekelezwa kwa takwa lao.

Waliogoma kufika mahakamani hapo ni Martin Mndesha, John Mndesha, Mashaka Pastor, Erick Mfinanga na Lucas Nyamaira watuhumiwa wote tisa wanatetewa na wakili wa kujitegemea Majura Magafu.

Mbele ya Hakimu Mkazi Frank Moshi, wakili Magafu alidai kuwa kesi hiyo ilikwenda mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa lakini wateja wake wamemweleza kuwa washtakiwa wengine watano wamegoma kwenda mahakamani kwa madai wanahitaji kuonana na uongozi wa mahakama.

Watuhumiwa waliofika mahakamani hapo jana ni Jafari Mkenda, Philip Mushi, Hussein Masoud na Rashid Eliakimu.

Magafu alidai wateja wake wanahitaji kuonana na Jaji Kiongozi Fakhi Jundu au Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kwasababu upande wa jamhuri katika kesi hiyo umekuwa ukiwatendea mambo yanayokiuka haki ikiwemo kutopeleka mashahidi mahakamani.

“Kesi hii ina miaka mitano sasa tangu ifunguliwe hapa mahakamani na bado haijamalizika na ni mashahidi wawili tu wanaoishi Arusha ndiyo wametoa ushahidi, mashahidi wengine tena wanaishi hapa hapa jijini hawaji mahakamani kutoa ushahidi wakati washtakiwa wanaendelea kusota gerezani.” Hakimu Mkazi Frank Mosha, alisema amesikia malalamiko hayo ila yeye siyo hakimu anayesikiliza kesi hiyo hivyo hawezi kutolea maamuzi maombi hayo na kwamba ataakikisha anayafikisha mkwa hakimu Katemana.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Juni 15 mwaka huu, itakapopelekwa mahakamani hapo kwaajili ya kutajwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Juni 8 mwaka 2011.

KAMPENI AFYA YA UZAZI WA MAMA,MTOTO IWE ENDELEVU


Na Happiness Katabazi

JANA Tanzania ilizindua Kampeni ya kitaifa la Afya ya uzazi wa mama na mtoto katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam na kudhuriwa na mamia ya watu.

Kampeni hiyo ambayo ni ya kwanza kuzinduliwa hapa nchini chini na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk.Haji Mponda tayari imeshazinduliwa katika baadhi ya nchi za Jumuiya ya Afrika Masharki.Na kuzinduliwa kwa kampeni hizo ni utekelezaji wa azimio la nchi wanachama wa umoja wa Afrika ambao waliazimia kila nchi mwanachama wa umoja huo kuakikisha inaongeza kasi ya kupunguza kasi ya vifo vya uzazi na watoto.

Kauli mbiu ya uzinduzi huo ni “Kuongeza kasi ya kupunguza vifo vinavyotokana na matatizo ya uzazi na vifo vya watoto”:Kampeni hiyo ambayo imefadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu(UNFPA).

Fukuto la Jamii kwanza linaanza kwa kutoa pongezi kwa uongozi wa nchi hii kuzindua kampeni hiyo kwani hakuna ubishi ni ukweli ulio wazi vifo vinavyotokana na matatizo ya uzazi na vile vya watoto wadogo chini ya miaka miatano vinatokea sana hapa nchini.

Na ukitaka kuthibitisha matukio hayo ni kupitia takwimu mbalimbali za kitaifa na ukilazwa katika wodi ya wazazi au wodi ya watoto, vifo vya aina hiyo utokeo.

Kwakuwa mwandishi wa safu hii ni mama wa mtoto wa mmoja aitwaye Queen Kissa Mwaijande ‘Malkia’ ambaye kesho Juni 8 anatimiza umri wa miaka mitatu,ni shuhuda wa vifo vya aina hiyo kwani kama mtoto wa kike mwaka 2008 nilibeba ujauzito na likuwa nikiudhulia kwenye kliniki ya wajawazikama mama niliwahi kubeba ujauzito na nilipokuwa nikiudhuria kliniki ya Mwenge inayomilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ) na kisha kwenda kujifungulia katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo kikosi cha 521 kinachoongozwa na Meja Jenerali, Salim Salim.

Na katika kuudhulia kliniki hapo ambapo wanawake wajawazito upata fursa ya kufundishwa jinsi ya kuweza kuulea ujauzito kwa kufuata kanuni ya kitabibu na kuchukua taadhali mapema pindi tunapojigundua tuna dalili mbaya kuwahi hospitalini.

Na ikumbukwe tayari taifa letu lina sera inayotamka bayana kuwa mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano anapaswa kutibiwa bure.

Na baada ya kujifungua mwanangu Queen salama, niliendelea kumlea vizuri kwa kuzingatia maelekezo ya madaktari na manesi wa Hospitali ya Lugalo.Lakini Juni mwaka jana, mwanangu Queen alilazwa hospitalini hapo kwa takribani wiki tatu akisumbuliwa na ugonjwa Rimonia.Kwa kweli nilichanganyikiwa sana lakini kwa nguvu za mungu na jitihada za madaktari wa Lugalo ziliweza kumwokoa uhai wake.

Kwa kipindi hicho cha wiki mbili nilicholazwa pale katika Wodi ya Watoto Hospitali ya Jeshi Lugalo, niliweza kushuhudia watoto wadogo waliokuwa wakiumwa sana majumbani kwao wakifikishwa hospitalini hapo hata usiku wa manane wakiwa wamecheleweshwa kuletwa hospitali hapo kupatiwa matibabu wakifika moja kwa moja wodini na kabla ya kuanza kupatiwa matibabu walikuwa wakikata roho kabla ya kuanza kupatiwa matibabu.

Na wengine watoto wadogo ambapo walikuwa wakiletwa wodi hapo wakiwa katika hali mbaya ambapo baadhi ya madaktari na manesi walipokuwa wakiowaona tu watoto hao, manesi na madaktari hao walikuwa wakiwaeleza wazazi watoto hao kuwa hospitali hiyo haina uwezo wa kuwatibia na badala yake walikuwa wakiwapatia msaada wa nesi mmoja na gari la kubebea wagonjwa(Ambulance) ili wawakimbize kwenye Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili kwa matibabu.

Pia kuna baadhi ya wanawake wajawazito ambao hadi wanaujauzito wenye umri wa miezi saba wanakwepa kwenda kuanza kliniki kwa kisingizio eti cha hofu ya kutakiwa kupimwa ukimwi.Wakati huo huo wataalamu wa afya wanashauri mama mwenye ujauzito anapaswa aanze kwenda kliniki tangu mimba ikiwa na umri wa kuanzia miezi minne.

Aidha pia kumekuwepo na tuhuma zinazoelekezwa moja kwa moja kwa baadhi ya wakunga katika baadhi ya hospitali za serikali kuwa wamekuwa wakichangia wajawazito kupoteza maisha yao kwaajili ya uzembe au kudai rushwa.

Lakini kuna wakina mama ambao watoto wao kweli walikuwa wakiumwa sana lakini waliwawahisha kuwafikisha hospitalini hapo na waliweza kupokelewa na kupatiwa matibabu ama wengine ulazwa au wengine utibiwa na kurudi majumbani kwao.

Kama ilivyohada ya manesi na madaktari kila siku nasema kazi yao ni wito,pindi wanapobaini wazazi wamewachelewesha watoto kuwaleta hospitali hawasiti kuwasema waziwazi na kuwataka waachache na tabia hiyo kwani wao wanaamini vifo vingi vinavyotokana na uzazi na watoto wadogo huweza kudhuirika kama kila mmoja wetu atafuata ushauri unatolewa wahudumu ya sekta ya afya.

Kwahiyo basi utaona basi licha ya serikali yetu kuwa na sera hiyo inayoruhusu watoto wote chini ya miaka mitano kutibiwa bure lakini kuna watoto wa umri huo wanaugulia majumbani na wazazi wao wapuuzia kuwapeleka hospitalini hadi mwisho wa siku watoto hao wasiyo na hatia wanajikuta wakikatishwa uhai wao kwaajili ya uzembe wa wazazi.Sisi kama wazazi tuache hii tabia.

Kwani miongoni mwa vigezo vinachokulia kuipima nchi fulani ni maskini, ni pamoja na vifo vingi ikiwemo vifo vya watoto.Kwahiyo kama taifa letu limeridhia kuzindua kampeni dhidi ya afya ya uzazi na mtoto ni wazi sasa kuanzia sasa tukaongeza kasi kwa pamoja kuakikisha kutokomeza vifo vya aina hiyo ambavyo kwa mujibu wa wanataaluma ya afya wanasema vifo hivyo vinaepukika.

Fukuto la Jamii linatoa dira ya kuona jinsi gani ya kampeni hiyo inaweza kufanikiwa na mwisho wa siku taifa letu likajikuta likudhiti vifo hivyo kwa kiwango cha juu. Mosi; ni kupitia vyombo vya habari ambapo kama wahusika wa kampeni toka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambao miongoni mwao ni Mkurugenzi Msaidizi Afya na Elimum Dk.Godfrey Kiangi, Meneja Programu ya Afya ya Mtoto Dk.Georgina Msemo na Dk.E.Mapella na wafadhili wa kampeni hiyo UNFP kuakikisha wanashirikiana kitaaluma kupitia vyombo vya habari naamini mwisho wa siku jamii itafahamu umuhimu wa kampeni hiyo.

Na sisi vyombo vya habari kama wanazalendo wa taifa hili na ambao tunapenda kuona taifa letu likiondokana na tatizo hilo mbalo linakatisha uhai wa mama na mtoto ni jukumu letu sasa kuakikisha tunazipa umuhimu pia habari na makala zinazoelimisha kuhusu afya ya uzazi wa mama na mtoto ili jamii ibadilike na kuona haja ya kukabiliana na tatizo hilo.

Kama sisi vyombo vya habari tutabadilika kwa dhati na kuanza kuona haja ya kuzipa uzito na umuhimu habari zinazohusu jamii yetu moja kwa moja kama tunazipaka umuhimu kila kukicha habari za kisiasa na burudani, ni wazi kabisa mashirika mbalimbali na wananchi wenye fedha watajitokeza kutoa michango yao ya hali na mali itakayowezesha majengo ya wodi za watoto wa changa wa chini ya umri wa miezi mitatu katika hospitali nyingi za wilaya na mikoa.

Kwani hali ilivyo hivi sasa karibu hospitali nyingi ziwe za serikali na zile binafsi hazina wodi maalum ya kuwalaza watoto wa changa wenye umri wa miezi mitatu kushuka chini.Na matokeo yake watoto hao wachanga hao ta waliozaliwa siku nne zilizozipita wakiugua na kufikia hatua ya kulazwa ,ulazwa katika wodi ya watoto wenye umri wa chini ya miaka 10 kushuka chini.

Sote tunafahamu kuwa watoto wachanga ni wepesi sana kushambuliwa na magonjwa yoyote sasa inapotokea mtoto mchanga analazwa kwenye wodi ya watoto wenye maradhi mengine ambayo hatutarajii mtoto huyo mchanga ayapate kwa umri wake huo, ujikuta anaweza kuambukizwa magonjwa hayo haraka iwezekanavyo.

Hivyo basi sisi vyombo vya habari hasa wahariri katika vyumba vyetu vya habari kuakikisha vinatoa kipaumbele kwa habari za aina hiyo za kuwaelimisha umma kuhusu kampeni hiyo ili mwisho wa siku nchi yetu iweze kuondokana na tatizo hilo.Nanina imani kabisa kama habari kuhusu kampeni hii zitapewa umuhimu, pia wanasiasa wetu nao wataona haja ya kuanza kulipigia chapua tatizo hilo ili mwisho wa siku serikali iongeze bajeti katika kukabiliana na janga hili.

Hakuna ubishi kwamba wanasiasa wetu tena kuanzia ngazi ya taifa hadi wilayani wamekuwa vinara sana wakuongoza harambee za kuchangia matamasha ya Injili,harambee za kuchangia kampeni za vyama vyao,ujenzi wa mashule na mambo mengine lakini siwaoni wanasiasa hasa wanasiasa wanawake wakielekeza nguvu zaidi katika kukabiliana na tatizo hilo na hivyo basi wakati umefika kwa wanasiasa kuelekeza nguvu katika afya ya uzazi wa mama na mtoto.

Ikumbukwe sote tulikuwa watoto tukalelewa vizuri na kwa umakini wa hali ya juu na ndiyo maana leo hii tumekuwa wakubwa tunaweza kujitegemea na kujieleza mbele ya madaktari kwamba tunaumwa nini.Sasa inakuwaje baadhi ya wazazi wanasahau wazazi wao waliwaangalia vyema walipokuwa watoto wadogo na kushindwa kuwafikishwa kwa wakati hospitalini watoto wao wadogo wanapougua?

Sisi watu wazima wa leo ifike mahali tujiulize kuwa Je tusingeangalia vyema na kufikishwa mahospitalini kupata tiba kwa wakati, tungefika hapa tulipo? Kwa hiyo tulitendewa haki na kuangaliwa vizuri na walezi na wazizi wetu hadi leo tumefikia hapa tulipofikia, inakuwaje miongoni mwetu tushindwe kuwatendea haki watoto wetu kwa kuwapeleka mahospitalini kwa wakati?

Nyie manesi ambao mnalalamikiwa kukiuka miiko yenu ya taaluma hadi wakati mwingine mnasababisha vifo vya wajawazito, Je na nyie kipindi kile mama zenu wakati wamebeba ujauzito wenu tumboni wangefika hospitalini na wauguzi waliokuwa wakiwahudumia wangekiuka miiko ya taaluma yao kwaajili ya kudai rushwa,mngekuwepo duniani nyie kama si nyie na mama zenu mngekuwa mmekufa na uzazi?

Ikumbukwe kuwa Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inatamka bayana kuwa. “Kila mtu anayo Haki ya Kuishi na kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria.”.

Kwa hiyo kimsingi tukubaliane haki ya kuishi imetamkwa kwenye Katiba yetu na hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kwa nafasi yake kuakikisha anailinda haki hiyo bila kuivunja.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Juni 7 mwaka 2011.

KESI YA MPENDAZOE YAONDOLEWA KORTINI

Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetoa amri ya kuondolewa kwa hati ya madai ya kesi ya kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 wa Jimbo la Segerea iliyokuwa imefunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya (CHADEMA), Fred Mpendazoe dhidi ya mbunge wa sasa (CCM), Dk.Makongoro Mahanga na wenzake mahakamani hapo baada ya kubaini hati hiyo ina mapungufu yanayosababisha wadaiwa kushindwa kuaandaa utetezi wao.


Mbali na Mahanga ambaye ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Segerea ambapo mdaiwa wa kwanza na wa pili wanatetewa na mawakili wa serikali David Kakwaya na Patience Ntwina na Mahanga anatetewa na wakili wa kujitegemea Jerome Msemwa.

Uamuzi huo ulitolewa jana mchana na Jaji Profesa Ibrahim Juma ambapo alisema kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya yeye kutolea uamuzi mapingamizi matatu yaliyowasilishwa mbele yake na upande wa utetezi Mei 25 mwaka huu, ambayo yaliomba mahakama hii itoe amri ya ama ya kuifuta kesi hii au kuamuru hati ya madai ifanyiwe marekebisho kwasababu baadhi ya aya zilizopo ndani ya hati hiyo zina mapungufu yanayonyima haki wadaiwa kuandaa utetezi wao.

Jaji Profesa Juma alisema amefikia uamuzi wa kukubaliana na mawakili wa serikali wa kwasababu mapingamizi yao ya msingi wa kisheria kwani baadhi ya baadhi ya Aya katika hati hiyo ya madai inasomeka kuwa wasimamizi wa uchaguzi katika vituo vinne vya kupigia kura toka Kata ya Buguruni, vituo viwili toka Kata ya Tabata, Vituo vinne toka Kata ya Kipawa walikubali matokeo bila ya kura zote zilizopigwa kuhesabiwa.

“Kwa kuwa hati hiyo ya madai katika aya yake ya 7:4 mlalamikaji ameishia kutaja idadi hiyo ya vituo toka katika Kata hizo za Buguruni, Tabata na Kipawa na akashindwa kutaja majina yenyewe ya vituo hivyo, jumla ya idadi za kura zilizopigwa na jumla ya idadi ya kura zilizopigwa kwa kila mgombea …mahakama hii inakubaliana na hoja za upande wa utetezi kuwa kwa mdaiwa huyo kushindwa kuweka wazi majina ya vituo na idadi ya kura kutasababisha upande wa utetezi kukosa haki ya kuandaa utetezi wao katika kesi hiyo.

“Kuhusu aya 7:5 katika hati hiyo Mpendazoe anadai kuwa majina yote ya Wasimamizi wa vituo vya kupigia kura toka Kiwalani,Vingunguti na baadhi toka Buguruni,Tabata na Kipawa kuwa walijumlisha matokeo katika fomu Na.21B ambazo siyo fomu rasmi za Tume ya Uchaguzi….pia mahakama hii inakubaliana na upande wa utetezi kuwa aya hiyo pia ina mapungufu na mahakama hii inaamuru hati ya madai iondolewe mahakamani ili ikafanyiwe marekebisho”alisema Jaji Juma.

Akiendelea kuchambua mapungufu hayo yaliyokuwemo kwenye hati hiyo huku akitumia baadhi ya mifano mbalimbali ya kesi, Jaji Juma alisema pia anakubaliana na hoja ya utetezi kuwa aya ya 7:6 ya hati hiyo ya madai ambayo mlalamikaji anadai kuwa jumla ya majina ya vituo 53 vya kupigia kura matokeo yake hayakujumlishwa na kusema kuwa haya hiyo pia ina mapungufu kwasababu mlalamikaji alipaswa ataje majina ya

Aidha alisema pia anakubaliana na upande wa utetezi kuwa Aya ya 7.7 nayo ilikuwa na mapungufu kwasababu mlalamikaji ameshindwa kutaja majina ya maofisa wa vituo vya kupigia kura katika vituo vya Kiwalani, Vingunguti na baadhi ya maeneo ya Buguruni,Tabata na Kipawa ambayo Mpendazoe anadai kuwa maofisa hao walishindwa kuwasilisha matokeo ya kura zilizopigwa kama walivyotakiwa Oktoba 30 mwaka 2010 na matokeo yake maofisa hao waliwasilisha matokeo hayo Novemba 1, mwaka 2010.

‘Kwa mchanganuo hapo juu mahakama hii inakubaliana na mapingamizi ya upande wa utetezi kuwa baadhi ya aya za hati ya madai zina mapungufu ambayo yanasababisha wadaiwa kushindwa kuandaa utetezi wao na kwa sababu hiyo mahakama hii itatoa amri ya kuondolewa kwa hati ya madai ya kesi hii iende ikafanyiwe marekebisho na mdaiwa na kisha irejeshwe mahakamani hapa ndani ya siku 14 kuanzia leo na kesi hii itakuja kwaajili ya kutajwa Juni 22 mwaka huu”alisema Jaji Profesa Ibrahim Juma.

Hata hivyo Jaji huyo alitupilia mbali ombi la Dk.Mahanga lililotaka kesi hiyo ifutwe kwasababu mdaiwa aliifungua kwa mbele ya Jaji badaya Msajili wa mahakama hiyo kwa maelezo huo amelikataa ombi hilo kwasababu halina ukweli wowote kwani mlalamikaji alifungua kesi hiyo kwa kufuata misingi yote ya sheria.

Chanzo:Gazeti la Tanzania la Jumanne, Juni 7 mwaka 2011.

SERIKALI YASHINDA KESI TANO MAUJI YA ALBINO


Na Happiness Katabazi

MKURUGENZI wa Mashtaka nchini (DPP),Eliezer Feleshi ameeleza kuwa hadi sasa ofisi yake imeshinda jumla ya kesi tano za mauji ya watu wenye ulemavu wa ngozi(Albino) walizokuwa wamezifungua katika Kanda mbalimbali za Mahakama Kuu hapa nchini na Mahakama Kuu nchini.


Sambamba na kushinda kesi hizo tano za mauji ya albino, pia imeweza kushinda kesi moja ya biashara haramu ya kusafirisha binadamu ( Human Traffick and Abduction) iliyomhusisha Robison Mukwena ambaye ni mlemavu wa ngozi.

Akizungumza na Tanzania Daima katika mahojiano maalum ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Feleshi alianza kwa kutoa takwimu ambapo alisema kuanzia mwaka 2007 hadi Januari 2011 jumla ya matukio 54 yanayowahusu watu wenye ulemavu wa ngozi yaliripotiwa kwa Jeshi la Polisi kote nchini nzima na jumla ya matukio manne ndiyo yaliyotokea mwaka 2010 katika wilaya za Kibondo,Kahama,Mwanza na Morogoro.

Feleshi alisema hadi sa jumla ya kesi tano za mauji ya Albino zimeshasikilizwa na kutolewa hukumu na Mahakama Kuu Kanda mbalimbali. Alizitaja kesi hizo za mauji ni kesi ya jinai Na.24/2009 ya Jamhuri dhidi ya Masumbuko Matata ‘Matata’ na wenzake wawili.Ambapo washtakiwa wote walitiwa hatiani na mahakama kwa kosa la mauji na washtakiwa hao wakakata rufaa katika Mahakama ya Rufaa lakini mahakama hiyo ya rufaa iliitupilia mbali rufaa hiyo.

Mkurugenzi huyo wa Mashtaka aliitaja kesi ambayo ni Na.26/2009 Jamhuri dhidi ya Joseph Lugata ambapo mahakama ilimtia hatiani mshtakiwa huyo na mshtakiwa huyo alikata rufaa mahakama ya rufaa na mahakama ya rufaa hadi sasa bado haijatoa hukumu ya rufaa hiyo.

Akiizungumzia kesi tatu ambayo Jamhuri ilishinda ni kesi Na.25/2009 iliyokuwa ikimkabili Mboje Mawe na wenzake watatu ambao walitiwa hatiani na Mahakama Kuu kwa kosa la mauji na wamekata rufaa mahakama ya Rufaa na hadi sasa mahakama hiyo ya juu kabisa nchini bado haijaanza kusikiliza rufaa hiyo.

Feleshi alisema kesi ya nne waliyoshinda ni kesi Na.42/2009 iliyokuwa ikimkabili Kazimili Mashauri na mwenzake ambapo Mashauri alitiwa hatiani na mwenzake akaachiliwa huru na aliyetiwa hatiani alikata rufaa Mahakama ya Rufaa na rufaa yake bado haijaanza kusikilizwa.

Aidha kesi ya tano ni kesi Na.672/2010 iliyofunguliwa na Jamhuri dhidi Nathan Mutei Mwasha iliyofunguliwa na kusikilizwa na Mahakama ya Wilaya ya Nyagamana mkoani Mwanza na mshtakiwa alitiwa hatiani kwa kosa la biashara haramu ya kusafirisha binadamu (Human Traffick and Abduction) iliyomhusisha Robison Mukwena ambaye ni mlemavu wa ngozi kutoka Kenya aliyesafirishwa kwa lengo la kuuzwa ambapo Feleshi alisema kesi hiyo ilisikilizwa ndani ya 20 na mahakama na kisha kutolewa hukumu.

Hata hivyo alisema kesi moja ya mauaji ya albino Na.22/2009 iliyofunguliwa na Jamhuri dhidi ya Mwigulu Madata na wenzake imeishaanza kusikilizwa na katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora. Na kuongeza kuwa bado kesi nyingine za mauji ya aina hiyo zinaendelea kusikilizwa na mahakama.

“Ushindi wa kesi hizo ambazo zilifunguliwa mahakamani na ofisi yangu na kuendeshwa timu ya waendesha mashtaka wangu ambao wamebobea kwenye tasnia ya kuendesha mashtka nadiriki kusema kuwa umechangia kwa kiasi kikubwa mauji ya albino kupungua kwani kabla ya watuhumiwa kukamatwa na kufikishwa mahakamani walifikiri serikali imelala lakini baada ya baadhi ya watuhumiwa kutiwa hatiani na makosa hayo ya mauji vitendo hivyo vya kikatili ambavyo vilikuwa vinailetea sifa mbaya nchini yetu kwenye uso wa dunia”alisema Feleshi.

Akizungumzia ushindi mwingine ambao ofisi yake imeupata Mei 23 mwaka huu, katika kesi ya jinai Na.1161/2008 Jamhuri dhidi ya Mweka Hazina wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoani Kigoma, Rajabu Maranda na Binadamu yake Farijala Hussein ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi ya wizi wa Sh bilioni 1.8 katika Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu ya Tanzania, ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilihukumu kwenda jela miaka mitano jela alisema , siri ya ushindi huo ni jeshi la polisi liliipatia ofisi yake ushahidi mathubutu na waendesha mashtaka wake walitumia vyema taaluma yao kisheria na ushahidi huo katika kuendesha kesi hiyo na mwisho wa siku upande wa Jamhuri ukaibuka mshindi.

Aidha alisema ofisi yake inafanyakazi kwa misingi ya taaluma ya sheria na ushahidi uliokusanywa na vyombo vya upelelezi na kamwe hatakubali ofisi yake ifungue kesi mahakamani kwaajili maneno yanayosemwa barabarani ambayo hayana msingi wowote wa kisheria na wala hayana ushahidi mathubutu ambao hauwezi kuishawishi ofisi yake kufungua kesi yoyote dhidi ya mtu yoyote mahakamani na kuongeza kuwa ofisi yake kote mikoani imejipanga kikamilifu kuakikisha inaendelea kufanya kazi zake kwa misingi ya kisheria.

Itakumbukwa kuwa miaka mitatu nyuma wimbi la mauji ya watu wenye ulemavu wa ngozi lilishamiri hapa nchini hali iliyosababisha albino kuishi kwa hofu na serikali kutangaza vita dhidi ya watu wote wanajiusisha na mauji hayo kwa ambayo yaliusishwa na imani za kishirikina na mwisho wa siku Jaji Mkuu Mstaafu Agustino Ramadhani alitenga bajeti ya fedha kwaajili ya kuzishughulikia kesi za mauji hayo ambazo ziliendeshwa na kutolewa maamuzi haraka zaidi lengo likiwa ni jitihada za serikali za kutokomeza mauji hayo ambayo yalikuwa yanaipa sifa mbaya Tanzania.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Juni 6 mwaka 2011.

JK KUZINDUA KAMPENI YA AFYA UZAZI,MTOTO

Na Happiness Katabazi

RAIS Jakaya Kikwete anatarajia kuwaongoza Watanzania kuzindua kampeni ya kitaifa ya afya uzazi na mtoto katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa mafunzo kuhusu namna ya kuripoti habari za afya ya uzazi na mtoto, Mkurugenzi Msaidizi wa Afya na Elimu Dk. Godfrey Kiangi alisema kampeni hiyo inafanyika kitaifa.

Alisema tayari kampeni hizo zimezinduliwa kwenye baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Masharki na kuongeza kuwa kampeni hiyo itaendelea kuzinduliwa kwa nchi nyingine barani Afrika kwa kuwa tafiti zimebaini kwamba tatizo la afya ya uzazi na mtoto ni kubwa kwa nchi zinazoendelea.

Dk.Kiangi alisema ujumbe wa kampeni hiyo ni ‘Kampeni ya kuongeza kasi ya kupunguza vifo vinavyotokana na matatizo ya uzazi na vifo vya watoto’ baada ya uzinduzi huo wizara itaendelea kufanya uzinduzi kwa ngazi ya mikoa na wilaya zote.

Kwa upande wake Meneja Mpango wa Afya ya Mtoto kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Georgina Msemo alisema siku ya uzinduzi wizara itaweka mabanda yatakayotoa huduma ya afya ya uzazi, uchangiaji damu kwa hiari na watu kupima ukimwi kwa hiari.

Aidha Dk. Msemo aliviomba vyombo vya habari kuwa mstari wa mbele kuandika habari za afya ya uzazi na mtoto ili jamii ibadilike na kuanza kuchangia katika kuboresha afya ya uzazi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Juni 3 mwaka 2011.

WABUNGE CCM WAIBURUZA SERIKALI YAO MAHAKAMANI


*WAFUNGUA KESI YA KIKATIBA KUZUIA ISIILIPE DOWANS

Na Happiness Katabazi

WABUNGE watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na raia wengine wanne wamefungua kesi ya kikatiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam Tanzania dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wenzake wakiiomba serikali izuiwe kulipa fidia ya sh bilioni 94 kwa Kampuni ya Dowans Holdings SA na Dowans Tanzania Ltd.


Kwa mujibu wa hati ya madai, wabunge hao wanataka serikali izuiwe kuilipa Dowans kwa sababu serikali ikilipa tuzo hiyo itakuwa imekiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Hati hiyo ya madai ya kesi Na. 5 ya mwaka huu, inawataja wabunge waliofungua kesi hiyo kuwa ni Mbunge wa Jimbo la Kibakwe (CCM), George Simbachawene, Mbunge wa Karagwe (CCM), Gosbert Blandes na Mbunge wa Viti Maalumu, Angellah Kairuki.

Wengine katika orodha ya waliofungua kesi hiyo ni raia wa kawaida, Hassan Ngoma, Senkoro Izoka, Salum Kambi na Salma Shomari Mohamed, ambao wanatetewa na wakili wa kujitegemea Mpare Mpoki na Kampuni ya Uwakili ya Lukwaro.
Mbali na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wadaiwa wengine ni Waziri wa Nishati na Madini na Shirika la Umeme (TANESCO).
Kwa mujibu wa hati ya madai ambayo Tanzania Daima inayo nakala yake, waombaji hao wanaeleza kuwa endapo malipo hayo yatafanywa kwa Dowans ni wazi wadaiwa hao ambao wanaiwakilisha serikali kwa ujumla watakuwa wamevunja Ibara ya 26(2),27(1),(2) ya Katiba ya nchi ambayo mahakama hiyo ina wajibu wa kulinda ibara hizo zisivunjwe.

Ibara ya 26(2) inasema: “Kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na sheria za nchi.”
Ibara ya 27(1) inasema: “Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya mamlaka ya nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.”

Ibara ya 27(2) inasema: “Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.”

“Sisi walalamikaji katika kesi hii tunao wajibu wa kulinda na kuhifadhi mali za umma wa Watanzania na wadaiwa wanao wajibu wa kikatiba wa kuhakikisha sheria za nchi yetu hazivunjwi;
“Kulipa au kusudio la wadaiwa kutaka kuilipa Dowans Holdings SA (Costa Rica) na Dowans Tanzania Limited, vitakuwa vinavunja Ibara ya 27(1) na (2) ya Katiba ya nchi na tunaomba itolewe amri na mahakama hii ya kuwazuia wadaiwa katika kesi hii kuilipa Dowans tuzo waliyoshinda katika Mahakama ya Kimataifa ya Kusuluhisha Migogoro ya Uwekezaji (ICC),” alidai Simbachawene.

Simbachawene anadai kuwa tuzo iliyotolewa na ICC kwa Dowans Novemba 30 mwaka 2010, inakwenda kinyume cha Katiba ya nchi na inajaribu kufuja fedha za umma.

Alidai tuzo hiyo ipo kinyume cha sheria kwa madai kuwa inakinzana na maazimio ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambalo kupitia mjadala juu ya ripoti ya kamati teule ya Bunge kuhusu mkataba tata wa TANESCO na Richmond, liliwahi kuweka wazi kwamba mkataba huo ulikuwa ni batili.

Aidha, alidai kuwa tuzo hiyo Dowans ikilipwa itakuwa ni kwenda kinyume cha sera za nchi na kwamba haiwezi kutekelezwa na mahakama za Tanzania.

“Kwa sababu hizo hapo juu tunaomba mahakama hii itoe amri ya kuwazuia wadaiwa wasijaribu kulipa fidia hiyo kwa Kampuni ya Dowans kwa sababu tuzo hiyo ni batili kisheria, inakinzana na maazimio ya Bunge na haiwezi kusajiliwa na mahakama za hapa nchini na inakwenda kinyume cha sera za nchi na kitendo cha kuilipa fidia kampuni hiyo basi ni wazi serikali itakuwa imevunja Katiba ya nchi”, alidai Simbachawene.

Simbachawene na wenzake wanaeleza kuwa mdaiwa wa kwanza ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ni mshauri wa sheria wa serikali na mdaiwa wa pili ni waziri wa Wizara ya Nishati na Madini, ambaye ndiye mwenye jukumu la mdaiwa wa pili la masuala ya umeme.

Kwamba Juni 21 mwaka 2006 mdaiwa wa tatu (Tanesco) chini ya maelekezo ya mdaiwa wa pili (waziri) waliingia mkataba na Kampuni ya Richmond Develepment Company LLC ya Texas Marekani kwa makubaliano yaliyojulikana kama “Power Off Take Agreement” wa kusambaza umeme wa megawati 100.

Lakini Kampuni ya Richmond ilidanganya na haikuweza kuzalisha umeme huo kwa wakati na wakati wanaingia mkataba huo hakukuwa na mwanasheria wa Serikali ya Tanzania wala wa Marekani.

Hati hiyo ya madai inasema, kwa kitendo hicho mdaiwa wa pili ambaye ni Waziri wa Nishati na Madini alikuwa amevunja kifungu cha 38,31(1)(a) na 31(1)(b) na 31(2) ,42(a) na 59(1) vya Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004.

Kwa maana hiyo utaratibu wote wa kuipatia tenda kampuni hiyo ulikuwa batili na ulikiuka vifungu hivyo vya sheria ya manunuzi ya umma.

Akiendelea kuchambua makubaliano yaliyoingiwa, alidai kuwa Kampuni ya Richmond ilipaswa kuanza kusambaza umeme ndani ya siku 150 kuanzia siku ambapo mkataba baina ya Tanesco na kampuni hiyo ulisainiwa, ambayo ni Juni 23 mwaka 2006 na muda wa kuanza kazi hiyo kwa mujibu wa makubaliano ulikuwa ni Februari 2 mwaka 2007.

Walalamikaji hao walidai tangu hapo hadi Desemba mwaka 2006 Kampuni ya Richmond ilishindwa kutekeleza kwa vitendo makubaliano hayo hali iliyosababisha mdaiwa wa tatu (Tanesco) kuandika barua kwa mdaiwa wa pili (waziri) ya kumwomba avunje mkataba huo kwa sababu Richmond imeshindwa kutimiza makubaliano waliyokubaliana na kwamba uthibitisho wa barua hiyo wanao.

Pia walidai kuwa Spika wa Bunge aliyepita, Samuel Sitta, Novemba 2007 aliunda Kamati ya Bunge kuchunguza tuhuma kuhusu mkataba huo, ambapo kamati hiyo ilibaini kampuni hiyo haikuwa na uwezo wa kuzalisha kiwango hicho cha umeme, na taratibu za upatikanaji wa tenda zilikiukwa, hivyo kusababisha aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, mawaziri waliowahi kuongoza Wizara ya Nishati na Madini Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi kujiuzulu nafasi zao za uwaziri.

Januari 25 mwaka huu, Dowans iliwasilisha ombi lake la kutaka Mahakama Kuu ya Tanzania ambalo limepewa Na. 8/2011 iisajili tuzo waliyopewa na Mahakama ya ICC na siku chache baadaye Tanesco, LHCR na Timothy Kahoho wakawasilisha hati ya nia ya kupinga ombi hilo la kutaka tuzo hiyo isajiliwe.

Kesi hiyo ambayo imekwisha kuanza kusikilizwa mbele ya Jaji Emilian Mushi, itakuja tena kwa ajili ya kutajwa Julai 28, mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Juni 2 mwaka 2011.

KESI YA MAHALU: USHAHIDI WA MKAPA TISHIO


*MAWAKILI WAVUTANA CHANZO CHA KUVUJA KWAKE

Na Happiness Katabazi

WAKATI Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imeahirisha kuanza kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi wa zaidi ya euro milioni 2, sawa na sh bilioni 3 inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, na Grace Martin, ushahidi wa Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, umeivuruga serikali ya Rais Kikwete.


Mvurugano huo ulijionyesha jana mahakamani baada ya wakili mkuu wa serikali, Ponsian Lukosi, anayesaidiwa na wakili mwandamizi toka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Ben Lincoln, kuwasilisha ombi la kuitaka mahakama itoe mwongozo wa kesi hiyo kwa madai kuwa mawakili wa Mahalu, Mabere Marando na Alex Mgongolwa, wamekuwa wakitoa mwenendo wa kesi hiyo kwenye vyombo vya habari kabla ya kusikilizwa na mahakama hiyo.

Akitolea mfano wa ushahidi wa kiapo wa Mkapa, wakili huyo wa serikali alidai kuwa ulitolewa kwenye vyombo vya habari kabla haujawasilishwa mahakamani.

Aliyataja gazeti la Mwanahalisi la Aprili 27 mwaka huu, Toleo Na.239, Tanzania Daima, Mwananchi, The Citzen na Mtanzania la Mei 6 mwaka huu kwamba yaliandika habari kuhusu ushahidi wa Mkapa kabla ya kufikishwa mahakamani.

“Tunavyoona sisi ni kwamba kama kesi inakuja mahakamani, kuna haja gani sisi maofisa wa mahakama kwenda kuzungumza kesi hiyo na vyombo vya habari halafu ndipo tuje mahakamani kuendelea na kesi? Upande wa jamhuri kwa namna moja ama nyingine tunaona huko ni kuingilia uhuru wa mahakama,” alidai Lukosi.

Wakili Lukosi alilibana gazeti la Mwanahalisi kwamba ndilo lililochapisha hati ya kiapo cha Rais Mkapa kabla hakijawasilishwa mahakamani na mwisho wa habari hiyo, likatoa hukumu kabla ya mahakama kufanya hivyo.

Alinukuu sehemu ya gazeti hilo ambayo ilisomeka hivi ‘Jamhuri kwa hati hiyo ya kiapo cha Mkapa akiwa Mtendaji Mkuu wa serikali ya Tanzania, alikuwa akielewa kila kitu kilichokuwa kikitendeka chini ya uongozi wake. Upande wa Jamhuri katika kesi ya Mahalu, ujiandae kufungasha jamvi la mashtaka’.

Aliendelea kulalamika kuwa “Wakati gazeti hilo likichapisha habari hiyo, kiapo cha Mkapa kilikuwa hakijawalishwa mahakamani na tumekuwa tukijiuliza kwa nini mawakili wa utetezi, wenye hati hiyo hawajajitokeza kulalamika kwamba ushahidi wao umevuja kwenye vyombo vya habari wakati bado hawajauwasilisha mahakamani?!” alihoji Lukosi.

Akijibu kombora hilo mahakamani hapo, wakili Marando alidai kuwa yeye ndiye aliyeandaa hati hiyo ya kiapo cha Mkapa na kabla ya kuiwasilisha mahakamani, aliiwasilisha kwa baadhi ya maofisa wa serikali kwa sababu ya unyeti wa hati hiyo kabla ya Aprili 27 mwaka huu na ndiyo siku gazeti la Mwanahalisi lilichapisha taarifa ya kiapo hicho.

Marando aliiambia mahakama kuwa yeye na wakili mwenzake, walishtushwa kuiona taarifa hiyo gazetini na alifanya mawasiliano na mhariri kujua walikozipata nyaraka hizo bila mafanikio.

‘Mheshimiwa hakimu na mahakama yako tukufu, katika hili wa kulaumiwa ni serikali. Wao ndio waliovujisha nyaraka za kiapo hicho kwenye vyombo vya habari kwa sababu mimi ndiye niliyeiandaa na kabla ya kuiwasilisha mahakamani, nilipeleka kwa siri kubwa kwa maofisa wa serikali na wakati ipo mikononi mwa maofisa wa serikali, haijarudi kwangu kwa ajili ya kuendelea kuiandaa, ndipo nyaraka hizo zilipovuja kwenye vyombo vya habari,” alisema Marando.

Wakili huyo maarufu nchini, alidai kuwa kutokana na umaarufu wa kesi hiyo ya Mahalu, hakuna mwandishi wa habari makini ambaye angekubali kuacha kuichapisha kabla haijafikishwa mahakamani.

Marando alidai kuwa kama ni onyo, ionywe serikali kwa kuvujisha nyaraka hizo na aliiomba mahakama isikubali ombi hilo kwa madai kuwa lina lengo la kunyamazisha vyombo vya habari visiendelee kuripoti kesi hiyo.

Akitoa uamuzi wa hoja hiyo iliyovuta hisia za wengi mahakamani hapo, Hakimu Mugeta alisema kwa mamlaka aliyonayo hawezi kutoa mwongozo wala onyo kwa vyombo vya habari na kuamua kuiahirisha kesi hiyo hadi Juni 24. Washtakiwa hao sasa wataanza kujitetea Julai 8 hadi 11.

Awali kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya washtakiwa kuanza kujitetea, lakini walishindwa kufanya hivyo kwa kuwa mawakili wa Mahalu walikusudia kuwasilisha maombi mawili.

Akiwasilisha maombi hayo mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Elvin Mugeta, Marando kwanza aliiomba mahakama iuingize kwenye jalada la kesi hiyo utetezi wa maandishi wa Rais mstaafu Mkapa ambao umeandaliwa kwa njia ya kiapo kumtetea Mahalu.

Katika ombi la pili, Marando aliiomba mahakama iwape mwenendo mzima wa kesi ili wakaandae utetezi wa wateja wake kwani mwenendo wa awali, una makosa ya kimaandishi.
Akitolea uamuzi wa maombi hayo, Halimu Mugeta alisema si muda muafaka kwa mahakama na pande zote mbili kuanza kuzungumzia ushahidi wa Mkapa kwa sababu hata washtakiwa wenyewe hawajaanza kujitetea.

“Kuhusu ombi la pili, mahakama hii imekubaliana na ombi hilo na kuahidi ifikapo hadi Juni 4, mahakama itakuwa imeshawapatia mwenendo sahihi wa kesi hiyo tangu ilipoanza hadi pale mahakama ilipowaona washtakiwa wana kesi ya kujibu,” alisema Hakimu Mugeta.

Hivi karibuni Mkapa alitoa utetezi wake mahakamani kwa njia ya maandishi ambao unaweza kuandika historia mpya katika mwenendo wa kesi nchini.

Katika hati ya kiapo chake cha Machi 31, mwaka huu, ambayo imeandaliwa kwa mujibu wa Sheria ya Usajili wa Nyaraka (The Registration of Documents Act, Cap. 117 of 2002), Mkapa anaeleza kuwa kila kilichofanywa na Mahalu kilikuwa sahihi na kilikuwa na baraka ya serikali aliyokuwa akiingoza toka mwaka 1995-2005.

Ushahidi huo wa Rais Mkapa umeorodhesha maelezo yake yaliyoainishwa katika vipengele 13.
Mkapa katika utetezi wake huo anadai kuwa mchakato mzima wa ununuzi wa jengo hilo la ubalozi lililoko katika mtaa wa Vialle Cortina d’Ampezzo 185 mjini Rome ulizingatia sera ya serikali ya upatikanaji au ujenzi wa majengo ya kudumu ya ofisi na makazi na kwamba ulizingatia maslahi ya taifa.

Hati hiyo ya kiapo ambayo tayari wakili Marando amesema ameishaiwasilisha pia Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi, inaanza kwa kusema, “Mimi Benjamin Mkapa, mtu mzima, Mkristo, mkazi wa Dar es Salaam, ninaapa kama ifuatavyo, ’nilikuwa Rais mtendaji wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa vipindi viliwili mwaka 1995-2005 na nina uhakika wa yote haya nitakayosema ndani ya kiapo hiki.’”

Katika kiapo hicho Mkapa anadai pia kuwa alifahamishwa na watendaji wa serikali aliyokuwa akiiongoza jinsi mchakato ulivyofanyika na ripoti ya uthamini wa serikali iliyotumika katika kufikia hatua ya kununua jengo hilo la ubalozi.

Anadai kuwa tathmini ya jengo hilo ambalo Mahalu anadaiwa kufanya udanganyifu na wizi kwa kulipa fedha kinyume na ilivyotajwa katika mkataba ambao ulifanywa na serikali ya awamu ya tatu kupitia wizara mbili tofauti, Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Ardhi na Maendeleo Mijini.

Anaendelea kudai anatambua kuwa ripoti ya serikali ya uthamini wa jengo hilo iliandaliwa na Wizara ya Ujenzi kwa kiwango cha dola za Marekani milioni 3 na Wizara ya Ardhi kwa thamani ya euro milioni 5.5.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo kupitia mchakato wa ununuzi wa jengo hilo ulikuwa wa aina mbili, mmoja ni rasmi na mwingine wa kibiashara na kuongeza kuwa kwa mujibu wa taratibu ya serikali ya Italia na kuwa hilo lilifanyika kwa baraka za serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Shahidi huyo wa Mahalu anadai pia kuwa kwa mujibu wa kiapo chake anakumbuka vyema taarifa ya serikali iliyotolewa bungeni Agosti 3, 2004 iliyosema na kuthibitisha kuwa taratibu zote zinazohusiana na manunuzi ya jengo kwa mujibu wa maelekezo ya serikali, zilifuatwa na kwamba muuzaji wa jengo hilo alilipwa fedha zote.

Akimwelezea Mahalu katika utetezi wake, Mkapa alidai katika kipindi chote alichokuwa Rais wa nchi alifanya kazi na mshtakiwa huyo katika nyadhifa mbalimbali za utumishi wa umma na kwamba mshtakiwa huyo ni mtu wa tabia njema, mkweli, mwaminifu na mchapaji kazi.

Katika kesi hiyo namba 1/2007, Mahalu na Martin wanatuhumiwa kwa wizi wa sh bilioni 3 katika ununuzi wa jengo la ubalozi mjini Rome.

Mbali na Mkapa, mashahidi wengi wanaotarajiwa kumtetea Mahalu na mwenzake ni Rais Kikwete, kwani wakati akinunua jengo hilo ndiye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Mashahidi wengine ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba, ambaye pia anakabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bil. 11.7.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Juni 1 mwaka 2011.