JERRY MURRO:POLISI WAMENIBAMBIKIZIA KESI


Na Happiness Katabazi
ALIYEKUWA mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa(TBC1), Jerry Murro(30), anayekabiliwa na kesi ya kula njama na kuomba rushwa ya Sh milioni 10, ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imuone hana hatia kwasababu kesi hiyo inayomkabili amebambikiwa na baadhi ya askari wa Jeshi la Polisi.


Murro alitoa ombi hilo jana wakati anaongozwa na wakili wake Richard Rweyongeza kutoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Mkazi Frank Moshi ambapo alidai kuwa uzalendo wake kwa jamii na uchapakazi wake katika habari za uchunguzi na kuibua ufisadi uliokuwa ukifanywa na askari wa polisi wa kikosi cha usalama barabarani ambao walikuwa wakila rushwa toka kwa madereva, na habari kuhusu ufisadi uliokuwa ukifanywa na raia mmoja wa korea katika halmashauri ya mji wa Bagamayo.

Mshtakiwa huyo kwanza alyakana mashtaka yanayomkabili ya yeye na washtakiwa wenzake Deo Muggasa na Kapama kuwa walikula njama na kisha kuomba rushwa ya sh milioni 10 kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Kaloli Wage kwa madai kuwa yeye hakuwa hakiwafahamu hao washtakiwa wala Wage na kwamba amekuja kuwafahamu kwa mara ya kwanza siku alipofikishwa mahakamani na Mahakao Mkuu ya Jeshi la Polisi.

Murro ambaye wakati akitoa utetezi wake alieleza mahakama kuwa yeye ni mwandishi wa mwanadamizi na mwenye shahada ya uandishi wa habari ya Chuo Kikuu lakini alipoulizwa swali na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Stanslaus Boniface kuwa elimu yake ya mwisho kabisa ni kiwango gani mshtakiwa huyo akajibu elimu yake ya mwisho ni ya kidato cha sita, alieleza kuwa yeye alikwenda katika Hoteli ya Sea Cliff ,Januari 28 mwaka 2010 kwaajili ya kuona na mtu ambaye hamfahamu na akafanya nae mazungumzo licha hakuweza kuieleza mahakama walifanya mazungumzo gani na mtu huyo.

Lakini hata hivyo akakanusha madai ya upande wa Jamhuri kuwa yeye alikwenda hotelini hapo Januari 29 mwaka 2010 na kukutana washtakiwa wenzake pamoja na Kaloli kama kilelezo cha picha za CCTV zinavyomuonyesha na pia akayakana maelezo aliyochukuliwa na Inspekta wa Polisi Issa Chabu na Koplo Lugano Mwansampeta aliyochukuliwa Januari 31 na Februali 2 mwaka jana licha mshtakiwa huyo akakiri saini zilizopo ndani ya maelezo hayo ni zake.

Alipohojiwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Boniface ni kwanini akubali kuweka saini yake kwenye maelezo ambayo siyo yake, Murro ambaye wakati anahojiwa na wakili huyo alionekana kuwa na jazba na kujifuta jasho, alidai siku zote polisi ni watu wa kutoa amri kwa watuhumiwa na kwamba yeye alipewa amri ya kusaini tu maelezo hayo ambayo yaliandikwa na Inspekta Issa na Koplo Mwansampeta.

“Mimi ni mtu maarufu kwenye jamii na kwasiku naweza kusalimiwa na watu zaidi ya elfu moja kutokana na kazi yangu ya kuandika habari za uchunguzi ambazo zilisababisha nipate zaidi ya tuzo tatu hapa nchini na wkaati napatwa na kesi hiyo mimi nilikuwa ndiyo Mkuu wa Dawati la Kipindi cha Usiku wa Habari TBC1, na habari zile za kulipua ufisadi wa polisi ndiyo zilizosababisha kila kukicha nipate vitisho, nijeruhiwe, gari langu ligongwe na taarifa za matukio hayo nimekuwa nikiyaripoti polisi lakini hakuna hata mtu mmoja aliyekamatwa.

“Hali iliyosababisha aliyekuwa bosi wangu kule kituo cha ITV, Reginald Mengi kuninunulia bastora yenye magazine mbili ambayo ilikuwa inaifadhi risasi 12 na bastora hiyo ilikuwa ni ya kipekee sana kwani ilikuwa ni nzito na nipia akaninunulia na pingu pale katika Duka la silaha Upanga kwaajili ya kujilinda na baada ya kununua vitu hivyo nilipewa kibali cha kumiliki naninarudia tena kutokana na umaarufu wangu kwenye jamii jeshi la polisi likanipatia maofisa wa juu wakanipeleka Makao Makuu ya FFU- Ukonga na wakanifundisha kulengaa silaha nikaweza hivyo kwenye kazi zangu zote nikawa natembea na bastora hiyo na pingu”alidai Murro ambaye hata hivyo hakutoa ushahidi kama ni kweli alikuwa akiyaripoti matukio hayo polisi na kupewa RB.

Akieleza siku ya Januari 31 mwaka 2010, ambayo ndiyo siku aliyokamatwa, kabla ya kukamatwa asubuhi alipigiwa simu na mtu asiyemhafamu akamtaka aifike katika mgahawa wa City Gargen mtaa wa Mkwepu kwani kutakuwa na mkutano na waandishi wa habari ambao utakuwa ukiwataja mafisadi hivyo mtu huyo akamtaka afike bila kukosa.

Murro aliendelea kueleza kuwa alitii mualiko huo na alipofika kwenye maegesho ya mgahawa huo akaanza kuipiga ile namba ya mtu huyo aliyemuarika huku siku hiyo ikiwa inakatwa na sekunde chache baadaye akaona mtu anamgongea kwenye kioo chake cha gari akimtaka ateremke chini huku pembeni kuwa na gaina ya aina ya Defender la Polisi likiwa na askari polisi wakiwa wamebeba silaha aina ya SMG mabegani wakalizuia gari lake kwa gari mbele na kisha askari hao wakamuonyeshea Wage na ndipo askari mmoja akaingia kwenye gari la Murro na kuanza safari ya kwenda Kituo Kikuu cha Polisi Kati kwa maelezo zaidi.

“Nilipofika kituo hicho kikuu cha polisi nilikuta waandishi wa ha bari wengi sana na polisi wakinitazama wengine wakinikebei kuwa nimekamatika nikachukuliwa maelezo nikapewa dhamana lakini siku tatu baadaye Waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo alinifuata ofisini TBC1, na kunieleza kuwa nimekwisha na akanionyesha picha za CCTV ambazo eti zinanionyesha nikiwa na hawa washtakiwa wenzangu na waziri huyo akanitaka nikaitishe mkutano na waandishi wa habari niwaeleze kuwa sikubambikiwa kesi na polisi bali nilitofautiana na polisi katika kazi, nikamweleza bosi wangu Tiddo Mhando kuhusu maelekezo hayo , Mhando akanikataza nisiitishe mkutano”alieleza Murro.

Aliendelea kueleza kuwa yeye alikuwa akifanyakazi kwa karibu na jeshi la polisi hasa Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova lakini baada ya kubambikiziwa kesi hiyo alishangazwa kumuona Kova akishiriki kumgandamiza hali iliyosababisha yeye kushikwa na hasira na kuingia ofisini kwa Kova nikisha kumsema maneno ya ukali kwani ni Kova huyo huyo ambaye alikuwa akimpatiaga fedha kidogo ili aweze kumjenga katika habari alizokuwa akizurusha kwenye TBC1 ili Kova aonekane ni mchapakazi hodari.

Yafuatayo ni mahojiano baina ya wakili wa serikali Boniface na Murro;
Swali:Wakati unatoa utetezi wako umesema unaelimu ya Chuo Kikuu, ebu tueleze vizuri elimu yako ya mwisho yaani ya mwisho kabisa ni ya kiwango gani?Jibu:Kidato cha Sita.
Swali:Pia ulieleza kuwa tangu uanze kuandika habari za uchunguzi umekuwa ukipokea vitisho na umedai umekuwa ukitoa taaarifa polisi lakini hadi unamaliza kujitetea umeshindwa kutoa ushahidi wa hata RB moja kuonyesha uliokuwa ukitoa taarifa, sasa unaizungumziaje kesi hii hii inayokukabili?

Jibu:Kesi hii ni mwendelezo wa majanga ya vitisho nilivyokuwa nikivipata kutokana na mimi kuandika habari zilizokuwa zinaibua ufusadi.

Swali:Wage siyo polisi na wala hujawai kuandika habari za ufisadi wake kwasababu ufisadi Wage alishafukuzwa kazi na waziri Mkuu Mizengo Pinda na kwamba wewe hukuona ni habari kuandika ufisadi wake, sasa ni kwanini wakati unajijetea hapa umedai Wage na polisi ndiyo wamekubambikia kesi hii?
Jibu:Kimya!

Swali:Wewe umesema hapo awali ulikuwa humfahamu Wage wala washtakiwa wenzako, sasa inakuwaje huyu Wage umekutana naye wakati ulipokamatwa halafu ashiriki kukubambikizia kesi?
Jibu:Kimya.

Swali:Ulisema vitisho vyote ulivyokuwa ukipata vilikuwa vikikutaarifu kuwa mwisho wako ni kaburi, sasa ieleze mahakama kesi hii inayokukabiri ni kaburi?

Jibu:Ndiyo ni kaburi, maana naweza kupelekwa gerezani nikazibwa mdomo nikauwawa,kesi hii imesababisha nifukuzwe kazi, sina mshahara, Dola za Kimarekani nilizopata baada ya kushinda Tuzo ya Mwandishi Bora wa mwaka 2009, Katibu Mkuu wa Baraza wa Habari Kajubi Mkajanga ameniandikia barua ya kuniarifu kuwa hawataweza kunipatia fedha hizo hadi kesi itakapomalizika na kwamba hela hiyo ina kikomo cha mimi kuichukua ambayo ni Desemba mwaka huu, pia ile nyumba niliyopanga Kunduchi watu wameenda kwa mwenye nyumba wakamjaza maneno baba mwenye nyumba akasitisha mkataba na mimi akanitaka niondoke na hivi sasa nimerudi kuishi kwenye Mabibo.

Swali:Kama kesi hii ni kaburi kwahiyo wewe unayezungumza hapa mahakama ni mzimu maana kaburi analala marehemu ambaye hawezi kuzungumza?
Jibu:Kimya!watu wakacheka.

Swali:Taja kwa majina hao polisi unaodai wamekubambikizia kesi na wanaendelea kukuangamizia!
Jibu:Kimya! Mimi sio msemaji wa jeshi la polisi.

Mshtakiwa huyo alimaliza jana kutoa utetezi wake na Hakimu Moshi iliairishwa hadi Septemba 27 mwaka huu,ambapo shahidi mmoja wa Murro anapanda kizimbani kumtetea Murro.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Agosti 19 mwaka 2011.

SERIKALI ISIFANYE PUPA KUWASHTAKIWA VIGOGO WA BP

Na Happiness Katabazi

KWA takribani wiki mbili sasa taifa lilijikuta likikabiliwa na uhaba wa mafuta kwasababu ya wafanyabiashara wa nishati hiyo kugoma kuuza nishati hiyo kwa bei elekezi iliyopangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji(EWURA) ambayo iliwataka wafanyabiashra hao kushusha bei.


Lakini wakati sekeseke hilo likitulia, Jumapili ya wiki hii EWURA ilijitokeza adharani na kusema kuwa wamepandisha bei ya mafuta ambayo bei hiyo mpya ilianza kutumikia tangu jumatatu wiki hii.

Wakati EWURA ambayo ipo chini ya Wizara ya Nishati na Madini ikitangaza bei mpya,Jumatatu wiki hii naye waziri wa wizara hiyo William Ngeleja alizungumza bungeni akisema bei hiyo haipaswi kuanza kutumika sasa.Kauli hizo mbili siyo tu zimewakera wananchi bali pia zimewafanya wananchi kuendelea kuwadharau baadhi ya viongozi wa serikali ambao hivi sasa wamekuwa na utamaduni wa kutoa matamko yanayokinzana ilihali wapo kwenye serikali moja.

Ukiachulia mbali hayo pia vyombo vya vimekuwa vikiripoti Mwenyekiti wa Bodi ya BP, Philemon Felix amekuwa akihojiwa na jeshi la polisi ni kwanini BP ambayo Tanzania inahisa 50 nayo ilishiriki kugoma kuuza mafuta na wakati Felix akiendelea kuhojiwa gazeti hili lilifanikiwa kunasa barua waliyokuwa wamewaandikiwa wamiliki wa BP Tanzania ambaye ni Kaimu Msajili wa Hazina na PB Africa ya Afrika Kusini kueleza kuwa endapo BP itatekeleza agizo la EWURA kuuza mafuta kwa bei iliyopunguzwa ni wazi kampuni hiyo ingepata hasara zaidi ya sh bilioni 3.1.

Napenda ieleweke kuwa lengo la mtazamo huu si kutaka kuingilia kazi za wapelelezi wetu wala waendesha mashtaka bali lengo la mtazamo huu ni kutaka kutoa taadhari kwa wapelelezi wetu na waendesha mashtaka na serikali kwa ujumla kwamba wakati wanaendelea na mchakato huo wa kipelelezi wa kutaka kubaini ni kwanini nayo kampuni ya BP haikuuza mafuta, wasiwe na papara wala pupa ya kukukusanya vielelezo na kuandaa hati za mashtaka.

Nimelazimika kutoa taadhari hiyo kwasababu nina ushahidi wa baadhi ya kesi ambazo zilifunguliwa kwa papara, mashinikizo ya kisiasa na kelele za wananchi na matokeo yake upande wa Jamhuri katika kesi hiyo mara kadhaa ikajikuta inapigwa mweleka mahakamani.

Na mifano michache ya kesi zilizofunguliwa matokeo yake serikali ya awamu ya nne ikajikuta inakumbwa na aibu,kudaiwa ni serikali ya visasi ni kesi ya mauji ya wafanyabiashara wa nne iliyokuwa ikimkabili Kamishna Msaidizi wa Polisi, Abdallah Zombe na wenzake, kesi ya kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa serikali kuhusu kampuni ya kufua umeme ya Richmond LLC, iliyokuwa ikimkabili Naeem Gile, kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika benki ya NBC Ubungo, kesi mbili za kutoa rushwa katika wa CCM mwaka jana mkoani Iringa zilizokuwa zikimkabili aliyekuwa mgombea Ubunge wa jimbo la Iringa mjini, Fredrick Mwakalebela na mkewe na kesi nyingine ya kutoa rushwa iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa waziri wa zamani, Joseph Mungai.

Katika kesi hizo zote wapelelezi wa Takukuru na Jeshi la Polisi walivurunda vibaya katika kukukusanya vielelezo na kwakuwa wapelelezi walishavurunda nao mawakili wa serikali waliokuwa wakiendesha kesi hizo walikuwa wakishindwa kutamba mahakamani na mwisho wa siku mahakama ilikuja kuwaachiria huru washtakiwa wote.

Na ikumbukwe kesi hizo zote zilifunguliwa kwa mbwembwe na mikogo ya hali ya juu na mawakili wetu wa serikali na Takukuru katika serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete katika mahakama kadhaa hapa nchini.

Ni ukweli usiopingika kuwa katika awamu hii ya awamu ya nne, kesi za jinai ambazo zinawahusu waliokuwa viongozi serikalini ndani ya CCM, wafanyabiashara na watu wenye majina makubwa zimefunguliwa kwa kishindo na zinaendelea licha nyingine zinaendelea kwa kusuasua na kesi nyingine zimemalizika na serikali iliweza kushinda kesi hizo kwasababu ilikuwa imeandaa ushahidi mzuri na hatimaye mahakama ikawatia hatiani washtakiwa.

Kwa muktadha huo hapo juu ni wazi kabisa kama ni kweli serikali imedhamiria kumburuza mahakamani Mwenyekiti wa BP, Tanzania Limited, Philemon Felix na watendaji wengine wa bodi hiyo, sina pingamizi na hilo ila ushauri wangu kwa mamlaka za kipelelezi kwanza wasiwe na papara, waakikishe wanafanya upelelezi wao kikamilifu kwa kukusanya nyaraka vielelezo mbalimbali ambavyo vitakuja kuisaidia Jamhuri katika kesi hiyo kwani tayari kuna taarifa zinadai kuwa katika hilo la sakata la BP, BP walijaribu kuchukua hatua fulani fulani kutaka kupata ridhaa ya ushauri wa serikali bila mafanikio.

Nimelazimika kueleza wasiwasiwa wangu huo kwasababu hivi sasa kumezuka tabia chafu sana ambayo haina tija kwa taifa letu inayofanywa na baadhi ya viongozi wa baadhi ya taasisi zetu za serikali kwa kila mmoja wao kutaka kujifanya yeye ni mchapakazi hodari kwenye jamii kuliko kiongozi wa taasisi nyingine hali inayosababisha viongozi hao ambao wapo kwenye serikali moja kutoa matamko yanayokinza hali inayosababisha wananchi kuanza kuidharau serikali yao.

Na wananchi hao kuishia kuitolea matusi ya nguoni na kumtusi kiongozi wa nchi Rais Kikwete kuwa anaipeleka nchi kuzimu , pindi wananchi hao wawapo kwenye vijiwe vyao mitaani.Matusi ambayo hatuwezi kuyaandika kwenye vyombo vya habari.

Hakuna ubishi kuwa tangu aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba, Gray Mgonja na Daniel Yona , aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na aliyekuwa Mkurugezi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba ambaye Mei 23 mwaka jana alihukumiwa na mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kifungo cha miaka miwili jela kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma.Na vigogo hao wengine ambao wanakabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi, kusababisha hasara na matumuzi mabaya ya ofisi ya umma.

Ni wazi kabisa mashtaka hayo kwa asilimia kubwa yamechangia viongozi wengi wengi wa serikali ya awamu ya nne kuogopa kuchukua maamuzi ya mambo fulani fulani kwa maelezo kuwa mwisho wa siku nao wanaweza wakajikuta wanafikishwa mahakamani kwa makosa kama hayo.Na hali hiyo imekuwa ikielezwa na baadhi ya viongozi tunaokutanaga nao faragha kubadilishana nao mawazo.

Umefika wakati sasa wa serikali ya Kikwete kuwa ni ya viongozi wanajiheshimu,wanaojitambua, wenye kutoa matamko yasiyokinzana kwa maslahi ya taifa letu na wafanyekazi kwa mtindo wa uwajibikaji wa pamoja siyo kusalitiana,kugeukana,kuchimbana, kuzuliana majungu.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania la Ijumaa, Agosti 19 mwaka 2011.

TAO 'AKWAA KISIKI' KORTI KUU

Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali ombi la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha (TLP) Hamad Tao dhidi ya Mbunge wa Ilala(CCM), Mussa Hassan ‘Zungu’lilokuwa linataka mahakama hiyo imsamehe asilipe dhamana ya kesi hiyo ya uchaguzi kwa maelezo ombi hilo liliwasilishwa kabla ya wakati wake.


Uamuzi wa kesi hiyo ya uchaguzi Na.104/2010 iliyofunguliwa na Tao ambaye hivi karibu alifukuzwa uanachama wa chama hicho, ulitolewa jana na Jaji Dk.Fauz Twaibu ambaye alisema amefikia uamuzi baada ya kubaini ombi hilo la Tao lakutaka asamehewe kulipa dhamana ya kesi hiyo kwasababu ombi hilo pia halikukidhi matakwa ya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010.

Jaji Dk.Fauz alisema sheria ya uchaguzi imeweka kiwango cha juu cha shilingi milioni tano ambacho mlalamikaji anapaswa kuweka mahakamani kama dhamana kwa kila mlalamikiwa, lakini sheria hiyo inamtaka mlalamikaji afike mahakamani na kuieleza mahakama kuwa yeye anauwezo wa kulipa kiasi gani sasa baada ya mahakama kuamuru mdaiwa alipe kiwango gani cha dhamana bado sheria hiyo inamruhusu mlalamikaji kuwalisha ombi la kuiomba mahakama imsamehe kabisa kulipa fedha yoyote kama dhamana na mahakama inaweza kurithia kama inajiridhisha mlalamikaji huyo ni kweli hana huwezo wa kulipa dhamana.

“Sasa kwa mtiririko huo wa sheria ya uchaguzi ya mwaka 2010, ombi hilo la Tao halikufuata mtiririko huo matokeo yake Tao amewasilisha moja kwa moja ombi la kutaka asamehewe badala ya kwanza kuwasilisha ombi la kuomba apunguziwe dhamana ya sh milioni tano kwa kila mdaiwa ….kwahiyo mahakama hii inatupilia mbali ombi la Tao kwasababu liliwasilishwa kabla ya wakati wake na kwa sababu hiyo kesi ya msingi haitaweza kuendelea”alisema Jaji Fauz.

Katika kesi ya msingi ambayo Tao anamshtaki Zungu, Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo la Ilala na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mlalamikaji huyo anadai kuwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa Jimbo la Ilala, mwaka 2010 yaliyomtangaza Zungu kuwa mshindi yafutwe kwasababu yeye alizuiliwa kuingia kwenye kinyang’anyiro na Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo hilo .

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Agosti 18 mwaka 2011.

BP YAFICHUA SIRI YA MGOMO

Na Happiness Katabazi

KAMPUNI ya BP Tanzania Limited imefichua siri kwamba ingeendelea kuuza mafuta yake kwa bei elekezi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji(EWURA), ingeingia hasara ya sh. bilioni 3.1.


Mbali na hasara hiyo, BP Tanzania Limited ilieleza kuwa Benki isingewaruhusu kukopa zaidi ya dola milioni 30 (zaidi ya shilingi bilioni 40) kuingiza nishati hiyo, itashindwa pia kulipa mkopo wake benki na kushindwa kulipia gharama za mzigo wa mafuta waliouingiza nchini.

Kwa mujibu wa barua ya BP Tanzania limited ya Agosti 10 (Tanzania Daima inayo) iliyosainiwa na Mwenyekiti wa bodi ya kampuni hiyo Philemon Felix kwenda kwa wnaahisa ambao ni serikali ya Tanzania iliyowakilishwa na Kaimu Msajili wa Hazina, Geoffrey Msella na mwana hisa mwingine Sipho Maseko/Richard King wa BP Afrika Pty wa Johannsburg, Afrika Kusini, mwenyekiti huyo aliwaeleezea wanahisa hao juu ya tatizo hilo.

Felix katika barua hiyo alisema kuwa kikao cha bodi ya BP kilichokutana siku hiyo kilitoa maamuzi kuwa kuna umuhimu wa haraka wa wanahisa hao kukutana kujadili mustakabali na hatma ya kampuni hiyo endapo watatekeleza agizo la Ewura la kupunguza bei ya mafuta.

Alisema kwa kipindi hicho kampuni ilikuwa na akiba ya mafuta ya petroli lita milioni mbili ambazo zingetumika kwa siku 10 na dizeli lita milioni 11 ambazo zingetumika kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Mwenyekiti huyo wa bodi alieleza kuwa pia waliiandikia barua Ewura kuelezea mazingira hayo yanayoikabili kampuni.

Nakala ya barua hiyo ilipelekwa kwa Waziri wa Nishati na Madini, Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo na Kamishina msaidizi wa Nishati (petroli na gesi) wa wizara hiyo.

Uchunguzi umebaini kuwa Hazina iliipokea barua hiyo Agosti 11, mwaka huu wakati mwanahisa mwingine wa Afrika Kusini aliipokea barua hiyo siku hiyo hiyo aliyoandikiwa na kumwandikia mwanahisa mwenzake ambaye ni serikali ya Tanzania kupitia msajili wa hazina.

Katika barua hiyo ya mwanahisa wa Afrika Kusini, alimtaka mwanahisa mwenzake (Tanzania) kufanya jitihada za kukutana ili kujadili mazingira magumu yanayoikabili kampuni hiyo kwa Tanzania.

Katika barua hiyo, mwanahisa huyo aliitaka serikali ya Tanzania itakapofika kwenye mkutano huo kwanza iwe inafahamu kwa kina agizo la Ewura, athari zinazoweza kuikumba kampuni hiyo na nini hatma ya kampuni hiyo nchini Tanzania kwa wanahisa hao.

Uchunguzi zaidi unaonyesha kuwa serikali ilishindwa kujibu barua hiyo ya bodi na hata ile ya mwanahisa mwenzake juu ya kuandaa mkutano huo.

Habari kutoka ndani ya bodi ya BP Tanzania Limited zinaeleza kwamba vikao vya bodi viliendelea kujadili hali hiyo huku ikisubiri maelekezo kutoka serikalini, lakini serikali iliendelea kukaa kimya hadi Ewura ilipoamua kuiffungia BP kutofanya biashara hiyo kw akipindi cha miezi mitatu.

Chanzo chetu kutoka ndani ya bodi hiyo kiliwataka Watanzania kwanza kuelewa muundo wa bodi ya BP Afrika uko vipi ikiwa ni pamoja na mwenyekiti kutokuwa na kura ya veto.

“Hapa nataka Watanzania waelewe muundo wa kampuni ya BP ukoje. BP Afrika ina hisa 50 na Serikali ya Tanzania ina hisa 50 na Tanzania mwenye mali hiyo ni Msajili wa Hazina. Kwa mtiririko huo ndiyo tunapata BP Tanzania na katika BP Tanzania ndiyo tunaipata Bodi ya BP Tanzania.

“Kwa hiyo Tanzania inatoa Mwenyekiti wa Bodi na wajumbe wanne na upande wa BP Afrika nayo kwenye bodi inakuwa Katibu wa bodi na wajumbe wa nne na kwamba shughuli zote za utawala za wanahisa zinatawaliwa na BP Afrika na Mwenyekiti wa Bodi ambaye anatoka Tanzania anakuwa hana kura ya Veto ya kuamua jambo hata kama mwanahisa mwenzake halitaki.

“Sasa kwa mtindo huo mlitaka bodi ya BP ifanye nini? Ieleweke wazi kwamba sisi wajumbe tulichaguliwa kuwa wajumbe ili kwenda kuiendeleza BP kwa faida na siyo kuiletea hasara ambayo sisi wanataaluma wa mahesabu tulishapiga mahesabu kuwa endapo tutakubali kuuza mafuta kwa bei iliyokuwa imetangazwa na EWURA Agosti 2, mwaka huu, ni wazi BP Tanzania ingepata hasara ya Sh. bilioni 3.1.

“…sasa sisi kama bodi tulivyolitambua hilo ndiyo maana mapema kabisa tukawaandikia wamiliki ili wakae kwenye vikao na watupatie ufumbuzi lakini cha kushangaza hadi sasa mwenye mali mmoja ambaye ni Tanzania hajajibu barua ya bodi yetu,” kilieleza chanzo hicho.

Akizungumza na Tanzania Daima, mwenyekiti wa bodi hiyo, Felix alithibitisha kuwa bodi yake ilimuandikia barua Kaimu Msajili wa Hazina na BP Africa Limeted ili waweze kukutana na kulipatia ufumbuzi jambo hilo, lakini alisema hazina hawakuijibu hali iliyosababisha kuiweka bodi yake katika wakati mgumu.

Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa Hazina Msella, alithibitisha kupokea barua hiyo Agosti 11 kutoka Bodi ya BP.

“BP wameniletea barua yao ya kuomba ushauri kwa serikali baada ya BP ambayo Tanzania nayo ina hisa 50 kugoma kuuza mafuta…sasa kama BP ilishajichukulia uamuzi wake ikaungana na kampuni nyingine za mafuta kugoma, sasa mimi nifanyeje?

“BP ilitaka mimi kwa niaba ya serikali niwashauri nini, wakati tayari ilikuwa imeshajichukulia maamuzi yake ya kugoma,” alisema Msella.

Habari za uhakika ambazo gazeti hili imezipata kutoka ndani ya jeshi la polisi, Mwenyekiti wa Bodi amekuwa akiripoti Makao Makuu ya Jeshi la Polisi tangu Ijumaa wiki iliyopita kila siku hadi jana mchana.

Hata hivyo chanzo chetu cha habari kutoka Jeshi la Polisi kilisema jeshi hilo linasubiri maelekezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) kuhusu sheria gani itumike na kwa mashitaka gani yatakayo mkabili mwenyekiti huyo wa bodi.

Habari zaidi zinaeleza kuwa polisi walilazimika kumpa dhamana mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Fedha wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) ambapo ameacha hati yake ya kusafiria polisi kama dhamana.

Wiki iliyopita, taifa lilijikuta na wakati mgumu na vurugu za hapa na pale kufuatia wafanyabiashara wa mafuta kugoma kuuza mafuta kwa madai ya kukaidi agizo la EWURA lilowataka wafanyabiashara hao kupunguza bei.

Lakini hata hivyo juzi Meneja wa Biashara wa EWURA , Godwin Samuel aliibuka na kuzungumza na waandishi wa habari kuwa mamlaka hiyo inatangaza kupanda kwa bei za mafuta zote nchini ambazo zinaanza kutumika rasmi jana na kuongeza kuwa hali hiyo inatokana na kupanda kwa bei ya nishati hiyo katika soko la dunia sambamba na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya Marekani.

Akitangaza bei mpya, Samwel alisema petroli imepanda kwa sh 100.34 sawa na asilimia 5.51, dizeli sh 120.47 sawa na asilimia 6.30 huku mafuta ya taa yakipanda kwa sh 100.87 sawa na asilimia 5.30.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Agosti 17 mwaka 2011.





MALUMBANO HAYA HAYANA TIJA

Na Happiness Katabazi
KIFUNGU cha 7(1)(a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002; kinasema ni wajibu wa kila mwananchi anayefahamu taarifa za kutendeka au kuna mtu anania ya kutenda uhalifu au mauji,anapaswa atoe taarifa hizo kwenye mamlaka husika za dola.


Na endapo mtu huyo atashindwa kutimiza waibu huo anaweza kushtakiwa kwa kosa la kusaidia kutendeka kwa kosa kwa mujibu wa Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code R:E;2002).

Nacho kifungu cha 99(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002,kina mruhusu hakimu kutoa kibali kwa mwananchi aliyeomba mahakama impatie kibali cha kuendesha kesi binafsi bila kuhusisha waendesha mashtaka wa serikali.

Na kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili Sanifu Toleo la Pili iliyochapishwa na Oxford Universty Press, inatoa maana ya neno Fisadi .Ina sema Fisadi maana yake ni “Mtu mbaya ,mtongozaji,mharibifu,mpotevu,mwasherati;-guberi”.

Nimelazimika kunukuu vifungu hivyo vya sheria na maana ya neno Fisadi ambalo limefafanuliwa kwenye kamusi hiyo kwasababu kwa takribani wiki mbili sasa kumeibuka malumbano ya hoja ndani na nje ya bunge ambayo yanaendeshwa na wazi wazi na wabunge wengi wa Dar es Salaam, dhidi ya Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk.Didas Masaburi ambayo malumbano hayo yamekuwa yakibebwa kwa mbeleko ya hali ya juu na baadhi ya vyombo vya habari hali inayoleta kichefuchefu kwa jamii ya watu wanaofikiri sawa sawa na wazalendo wa kweli wa taifa hili.

Malumbano hayo ni kwamba mbunge wa Ilala, Zungu, Mbunge wa Temeke, Abasi Mtemvu, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Jimbo la Ubungo John Mnyika ambayo wakiwa ndani ya Bunge walitoa kile wao wanachodai ni ufisadi uliofanyika ndani ya Shirika la Uda na kutaka Dk.Masaburi awajibishwe naye hawakutosheka wabunge hao wakasafiri hadi jijini Dar es Salaam, na kuja na nyaraka mbalimbali wakionyesha kuwa wao hawausiki na kile kilichodaiwa na Dk.Masaburi kuwa wamefanya ufisadi katika jengo la Machinga Complex.

Kwa watu wanaofikiri sawa sawa na tunaofahamu vyema hulka na tabia chafu walizonazo wanasiasa wa nchi hii tunapoendelea kusikiliza malumbano hayo uwa tunakereka na kusikia kichefuchefu kabisa.

Kwani tunaamini kabisa hao wabunge ndiyo watunga sheria wetu wameendelea kujigamba kuwa wanaushahidi wa Dk.Masaburi amefanya ufisadi UDA na Zungu amefanya ufisadi Machinga Complex kwanini wasitekeleze matakwa ya vifungu hivyo vya sheria kwa kupeleka huo ushahidi walionao mfukoni kwenye vyombo vya dola ambavyo ndivyo vyenye thamana ya kufanyia uchunguzi tuhuma hizo wanazitumia hivi sasa kupakana matope mbele ya wapiga kura wao na umma?

Na kama hilo litawashinda kwasababu miongoni mwa wabunge hao walishawahi kutamka kuwa hawana imani na TAKUKURU, kwanini wasiende mahakamani kuomba kibali cha kuendesha kesi binafsi kuliko hivi sasa wanavyoendelea kupakana matope na kushushiana heshima mbele ya wapiga kura na jamii kwa ujumla?

Nadiriki kusema kuwa mimi nikiwa ni miongoni mwa waandishi wachache makini ambao wakati malumbano hayo yakitokea nilichukua hatua ya kuwataadharisha wanahabari wenzangu kuwa wawe makini na malumbano hayo yanayoendelea kwani tayari kuna taarifa za Kiichunguzi zimeanza kuusisha malumbano hayo na ubaguzi wa kidini, uasama na kisasi ya kampuni mmoja ambayo nyuma yake yupo mtu ambaye kwa hasira ya kampuni hiyo ambayo inadaiwa kuwa ana mahusiano nayo ndiyo amekuwa akiendesha chini chini malumbano hayo.

Na kwakuwa watanzania huwa atunyimani maneno tunanyimana matonge ya ugali.Muda si mrefu itakuja kubainika wazi kwamba chanzo na nyuma ya mgogoro huo ambayo minasema hauleti tija kwa taifa letu ni wakina nani wapo nyuma ya mgogoro huyo, na ni kwanini wapo nyuma ya malumbano hayo?

Mbaya zaidi wote wanaolumbana kuhusu kutuhumiana ni viongozi waliochaguliwa na wanachi.Sasa sisi wapiga kula umefika wakati tujiulize ni kwanini hawa viongozi wetu ambao wanatuhumia kupitia vyombo vya habari ni kwanini wanashindwa kuomba viongozi wao wajuu wawaite pamoja na kuweza kutatuliwa kero zao kwenye vikao vya ndani?

Malumbano hayo wanayoyaendeleza kupitia vyombo vya habari, yanatupa picha gani sisi wapiga kura wao?Je malumbano hayo yanatumalizia kero za maji, uhaba wa madawa, barabara mbovu kwenye majimbo yetu?

Na sisi waandishi wa habari ifike mahala tuamke na tutafute kilichopo nyuma ya pazia kwani somo zuru kuhusu ushetani wa wanasiasa wetu wa kupenda kuzuliana majungu na kashfa zisizona ukweli na kutaka waungwe mkono na jamii,wakishafanikiwa azma yao hiyo ya kumchafua mwanasiasa mwenzao wanasiasa hao uwaacha solemba wananchi na vyombo vya habari ambavyo vilikuwa vikiwaunga mkono katika usheni huo pasipo kujua na mfano mzuri ni kashfa ya mkataba wa kufua umeme wa Richmond.

Kwahiyo katika malumbano hayo ya UDA ni vyema waandishi wa habari wakaingia msituni kafanya utafiti wa kweli UDA imeuzwa au inataka kuingia ubia na kampuni binafsi?Maana kuuza shirika la umma ama kuuza ni vitu viwili tofauti. Au je utendaji kazi thabiti wa Dk.Masaburi wa kuanza kufumua uozo ndani jiji hili ndiyo umeanza kuwatia matumbo joto wabunge hao?

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Agosti 13 mwaka 2011.




UAMUZI KESI YA DOWANS WANUKIA

Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imesema itatoa tarehe ya kutolea uamuzi wa ama tuzo ya fidia y ash bilioni 94 ya kampuni ya Dowans isajiliwe au isisajiliwe na mahakama hiyo kwa njia ya maandishi.


Hayo yalisemwa jana na Msajili wa Wilaya ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Projestus Kahyoza wakati akiarisha kesi hiyo ambayo ilifunguliwa na wakili wa Dowans, Kennedy Fungamtama kwaajili ya kuiomba mahakama hiyo iiweze kuisajili tuzo waliyoipewa Novemba 15 mwaka jana na Mahakama ya Kimataifa na Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara(ICC) ambapo kesi hiyo ilikuja jana kwaajili ya kutajwa na kupangiwa tarehe ya kuja kutolewa uamuzi wa mapingamizi hayo.

Kahyoza alisema kesi hiyo jana anaiarisha yeye kwasababu Jaji Emilian Mushi anayeisikiliza kesi hiyo hayupo hivyo akasema tarehe ya uamuzi pande zote katika kesi hiyo ambazo ni Dowans yenye dhidi ya Tanesco, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kituo cha Kutetea Haki za Binadamu (LHRC) na Timoth Kahoho kwa njia ya maandishi.

Wadai ambao ni Tanesco na wenzake katika kesi hiyo nao waliwasilisha mapingamizi wakiomba mahakama hiyo isiisajili tuzo hiyo ya Dowans.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Agosti 12 mwaka 2011.

MSOMI WA UDSM AJITOSA KUMRITHI ROSTAM


Na Happiness Katabazi
KADA kijana wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Ngassa Nichoulaus (26) jana alijitokeza kuchukua fomu za kuwania ubunge katika Jimbo la Igunga mkoani Tabora na kusema kuwa amefikia uamuzi huo kwasababu anataka kujenga misingi ya umoja na ushirikiano baina ya watendaji wa serikali na wananchi wake.


Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana mchana muda mfupi baada ya kuchukua fomu , Ngassa ambaye mwenye Shahada ya Siasa na Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akabidhiwa fomu hizo jana na Katibu wa CCM, Wilayani Igunga Neema Adamu ambapo alisema amefikia uamuzi huo wa kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya CCM, ili aweze kuendelea kusukuma gurumu la maendeleo katika jimbo hilo na kuendeleza yote aliyoaanzisha Rostam Aziz ambaye alijiudhuru kiti hicho Julai 13 mwaka huu.

“Naomba chama changu CCM kinipe ridhaa ya kupeperusha bendera yake ili niweze kujenga uongozi wenye misingi yenye uwajibikaji wa kweli kwa wananchi wa jimbo la Igunga na taifa kwa ujumla ili kuakikisha wananchi wanapata fursa ya kutimiziwa mategemeo na matumaini yao yaliyojengwa kwa msingi wa imani kubwa ya juu ya serikali ya CCM chini ya Rais Jakaya Kiwkete”alisema Nichoulaus.

Aidha alisema endapo atapata ridhaa ya chama chake ataendelea kuwasemea kuwasemea wananchi wa jimbo hilo ndani ya Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania kwa kujenga hoja na ushawishi katika kutekeleza ahadi za chama,ahadi za serikali na ahadi za rais kwa wananchi wa jimbo la Igunga.

Hata hivyo anawaomba wananchi wa jimbo hilo waiunge mkono kwa moyo mmoja na imani kubwa juu yake katika kuendelea kujenga Igunga yao yenye watu wachapakazi na rasilimali zenye umuhimu mkubwa katika kujenga uchumi wao katika kutimiza hilo atashirikiana nao katika kuimalisha sekta za kiuchumi,kijamii na kisiasa,kufukia malengo yao yanayoongozwa na dhamira ya kweli itakayojengwa katika misingi ya Dira ya maendeleo ya Taifa 2025,Mpango wa Maendeleo ya Taifa 2011/2012-2015/2016 na Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2010-2015.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Agosti 12 mwaka 2011.

KESI YA MTIKILA YAPIGWA KALENDA

Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mare nyingine tena jana ilijikuta ikishindwa kuendelea kusikiliza kesi ya uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila kwasababu shahidi wa upande wa jamhuri kushindwa kufika mahakamani kwasababu ni mgonjwa.


Wakili wa Serikali Zuberi Mkakatu mbele ya Hakimu Mkazi Ritha Tarimo alidai kuwa shahidi waliyekuwa wakitarajia kumleta leo kutoa ushahidi wake anaugua hivyo wanaiomba mahakama iairishe usikilizwaji wa kesi hiyo.

Hakimu Tarimo alikubaliana na ombi hilo na akaiarisha hadi Septemba 7 mwaka huu, na akaamuru hati za wito wa wakuitwa mahakamani zitolewe kwa mashahidi na mashahidi wafike mahakamani bila kukosa.

Kesi hiyo ya uchochezi Na. 132/ 2010 , Mtikila anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi dhidi ya Rais Jakaya Kikwete kuwa kiongozi huyo anaangamiza ukristo kwasababu amekuwa akiukumbatia uislamu hivyo kuwataka waskristo wote waungane haraka na waakikishe wanamuingiza rais mkristo Ikulu ili kuweza kuunusuru ukristo hapa nchini.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Agosti 11 mwaka 2011.

MAHALU AANZA KUJITETEA

Na Happiness Katabazi
ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu ameileza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa alipofika katika ubalozi huo alikuta ofisi hizo zikiwa na hali mbaya hali iliyosababisha kutoa fedha zake mfukoni na kunua thamani zenye hadhi ya ofisi ya ubalozi.


Sambamba na hilo Balozi Mahalu mawasiliano kati ya rais wanchi, balozi,waziri wa Mambo ya Nje na Katibu uwa ya aina tatu.Aina ya kwanza ni mawasiliano ya maandishi yaani barua za kawaida, maandishi ya mafumbo na mawasiliano ya mdomo.Rais anamamlaka ya kumpigia simu balozi kokote alipo na kumpa maelekezo au kumwita balozi aje hapa nchini na kisha kumpa maelekezo ya ana kwa ana bila maandishi.

Profesa Dk.Mahalu alitoa maelezo hayo jana wakati akiongozwa kutoa utetezi wake na wakili wake Mabere Marando, Alex Mgongolwa kwa mara ya kwanza tangu alipofunguliwa kesi ya uhujumu uchumi mwaka 2007, mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Ilvin Mugeta ambapo alidai kutokana na kuikuta ofisi hiyo ikiwa na hali hiyo mbaya alilazimika kutoa fedha zake mfukoni kwaajili ya kununulia thamani za ofisini.

Mahalu alidai kuwa Aprili 1 mwaka 2000 ndiyo siku aliyofika rasmi mjini Rome nchini Italia ikiwa ni siku chache baada ya aliyekuwa rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa kumteua kuwa Balozi wa Tanzania nchini humo, ambapo alieleza majukumu yake yalikuwa ni kulinda na kuyatetea maslahi ya Tanzania na wakati akiwa Balozi wa Italia pia wakati huo huo alikuwa pia ni balozi wa nchi tisa ambazo ni Griss, Turkey, Sebia,Slovenia,Croation, Mesedonia, Mountentenegro.

Alieeleza pia jukumu jingine ni kupokea maelekezo toka hapa nchini kuhusu kukuza mahusiano baina ya nchini na nchi na kwamba yeye ndiye aliyekuwa mkuu wa masuala yote ya utawala wa ofisi ya ubalozi na kwamba masuala yote ya utawala yalikuwa yakiletwa kwake na maofisa wa ubalozi na serikali kwa ujumla.

“Nilipofika Italia nilikuta hali ni mbaya inasikitisha kwani ubalozi wa wetu nchini Italia ulikuwa umefungwa tangu mwaka 1994 na nilipoteuliwa mimi kwenda huko ndiyo nikawa nimeenda kuufungua ubalozi huo uanze kufanyakazi.Na wakati nafika hapo kila kitu cha ubalozi kilikuwa kimeondolewa na kurudishwa nchini kikabaki kiofisi kidogo tu kwaajili ya kushughulikia masuala ya kilimo na mwaka 1997 ndiyo serikali ilimpeleka msimamizi wa ofisi hiyo.

“Nilipofika hapo Rome nilianzia kazi kwenye hicho kiofisi kidogo chenye ukubwa wa skwea mita kati ya 88 na 100, nikakuta ofisi hiyo ikiwa na meza ya miguu mitatu ,kiti kimoja ambacho kilikuwa kinaaribika mara kwa mara ambacho niliogopa kukitumia na kochi lililochoka na simu moja vitu vyote hivyo vikiwa vimechakaa, maofisa wake watatu ofisi zao zilikuwa ni vyumba vitatu vidogo vya kulala,huduma ya maliwato ilikuwa mbovu, jiko ndiyo tukaifanya ofisi ya kupokelea wageni ambapo dereva ,katibu mhutasi na wahudumu ndiyo walikuwa wakishinda humo wakati wa saa za kazi.

“…ikanilazimu kutoa fedha zangu mfukoni zikaenda kununua thamani za kisasa ambazo ni meza, seti ya makochi kwaajili ya matumuzi ya ofisi lakini kutokana na udogo wa ofisi hiyo ni makochi mawili tu ndiyo yaliyoingia makochi mengine yakakosa nafasi”alidai Profesa Dk.Mahalu.

Alidai kuwa baada ya kukuta hali hiyo alichukua hatua ya kumweleza aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa wakati huo, Balozi Kibeloh na kwamba aliyekuwa waziri wa wizara hiyo kwa kipindi hicho alikuwa Jakaya Kikwete ambaye kwa sasa ndiyo rais wanchi ambaye naye alifika katika ofisi za ubalozi huo na kushuhudia hali hiyo mbaya na kwamba Kikwete aliunga mkono hoja yake kwamba ofisi hiyo ni mbovu na akashauri ipatikane ofisi yenye hadhi ya ubalozi.

Aliendelea kueleza mbali na Kikwete, pia aliyekuwa Makamu wa Rais wa Serikali Dk.Ally Mohamed Shein naye alitembelea ofisi hizo za ubalozi na kushuhudia ubovu ule na akamuahidi mshtakiwa huyo kuwa akirudi nchini atafikisha tatizo hilo ili taratibu zifanywe za kupatikana jengo kubwa la ubalozi.

Profesa Dk. Mahalu alieleza kuwa baada ya kumueleza matatizo hayo ya ubalozi Katibu Mkuu, Balozi Kibeloh ,alikubaliana naye akasema ni muhumi kwa serikali kutafuta jengo jipya na kwamba Mei 2001, alitaarifa na balozi huyo kuwa Rais Mkapa atakwenda Brussels kwa ziara ya kikazi na kwamba yeye mshtakiwa akamuomba tena katibu mkuu huyo amruhusu akamweleza Mkapa matatizo hayo pindi atakapofika Brussels na katibu mkuu huyo alimruhusu.

“Rais Mkapa nilipokutana naye pale Brussels nikamueleza umuhimu wa kununua jengo jipya la ofisi ya ubalozi mjini Rome na kwasababu majadiliano ya kuaandaa bajeti ya serikali yalikuwa yameanza inawezekana rais mkapa akalieleza jambo hilo kwa mawaziri wake ili watenge bajeti ya kununua jengo la ubalozi huo…rais alinielewa na alikuwa akifahamu ubalozi huo ulikuwa umefungwa tangu mwaka 1994 na akaniakikishia serikali yake itajitahidi ipate fedha za kujenga au kununua jengo la ofisi hizo lenye hadhi na sifa za ubalozi.

“Niliporudi mjini Rome Italia, nilimjulisha kwa barua Katibu Mkuu Balozi Kibeloh mazungumzo yangu na rais Mkapa na balozi huyo naye akanijibu kuwa atazidi kulifuatilia jambo hilo na kuliweka kwenye bajeti ya wizara ya mambo ya nje na kwasababu hiyo ilikuwa ni sera ya wizara yake ya kutaka ofisi za ubalozi wetu nje ya nchi zinunuliwe majengo yao hivyo hoja hiyo itapelekwa bungeni na haitapingwa ”alidai Profesa Dk.Mahalu.

Mshtakiwa huyo aliendelea kueleza kuwa wakati akisubiri ahadi hiyo ya Katibu Mkuu huyo, mwanzoni mwa Juni 2001, Katibu Mkuu huyo alimpigia simu akimpongeza kwamba maombi ya wizara yao katika bajeti ya kutaka kila ofisi ya ubalozi inunue jengo lake itapitishwa na bunge na kuongeza kuwa Katibu mkuu alimtaka mshtakiwa huyo na maofisi wengine wa ubalozi kuanza kutafuta majengo na kwamba yeye mshtakiwa aliwaagiza maofisa wake kwenda kutafuta majengo ndani na nje ya mji wa Rome kwaajili ya kulinunua ili kulifanya ofisi ya ubalozi.

Alidai kuwa baada ya kupokea habari hiyo njema toka kwa Katibu Mkuu, yeye mshtakiwa alimuandikia barua katibu mkuu huyo ya kumshukuru ambayo ni barua ya Mei 4 mwaka 2009 ambayo ninakala na kwamba aliomba mahakama iipokee kama kielelezo na hakimu mkazi Mgeta aliipokea kama kielelezo cha kwanza.

Hakimu Mgeta aliairisha kesi hiyo Agosti 26 mwaka huu, ambapo mshtakiwa huyo wa kwanza Mahalu ambaye bado hajamaliza kutoa utetezi wake ataendelea kutoa utetezi wake.Mbali na Mahalu mshtakiwa mwingine wa kesi hiyo ya uhujumu uchumi wa Euro milioni mbili ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima, Agosti 5 mwaka 2011.

HAKIMU KESI YA JERRY MURRO ACHARUKA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imesema inachukizwa na tabia ya mawakili wa utetezi katika kesi ya kushawishi na kuomba rushwa ya sh milioni 10 inayomkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa(TBC1), Jerry Murro na wenzake ya kutofika mahakama siku ya kesi hiyo kwa maelezo kuwa wapo Mahakama Kuu kwaajili ya kuudhuria kesi nyingine.


Hayo yalisemwa jana na Hakimu Mkazi Frank Moshi muda mfupi baada ya Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, Stanslaus Boniface kuieleza mahakama kuwa kesi hiyo imekuja jana kwaajili ya washtakiwa kuanza kujitetea lakini mawakili wa utetezi Richard Rweyongeza na Majura Magafu wamemwarifu kuwa hawatakuwepo kwasababu wamekwenda Mahakama Kuu kuudhuria kesi mbalimbali na kwamba upande wa jamhuri upo tayari kwaajili ya kuendelea na kesi.

“Kwa zaidi ya mara nne sasa washtakiwa wanashindwa kupanda kizimbani kuanza kutoa utetezi wao kwasababu mawakili wao wamekuwa wakitoa udhuru kuwa hawatafika katika Mahakama ya Kisutu kwasababu wapo Mahakama Kuu kuudhuria kesi nyingine…sasa nasema sitaki tena kuona kesi hii inaarishwa kwasababu kama hizo,sote tumekuwa tukipanga tarehe za kuanza kusikilizwa na tunakubaliana lakini siku kesi inapokuja kesi haiendelei kwasababu eti mawakili wa utetezi wanakuwa mahakama za juu kwaajili ya kesi nyingine.

“ Hivyo leo nataka mjitambue nyie wote hapa ni mawakili na kila wakili ana dayari yake inayoonyesha ni lini atakuwa na kesi fulani katika mahakama hipi ….sasa leo pangeni tarehe ambayo nyie mnafahamu siyo mtafika hapa mahakamani bila kukosa ili mahakama hii ianze kupokea utetezi wa washtakiwa narudia tena hii tabia ya kutoa udhuru siku ya kesi hii inapokuja eti mawakili wa utetezi wapo mahakama kuu inakera sana” alisema Hakimu Moshi.

Hakimu Moshi aliarisha kesi hiyo hadi Agosti 18 mwaka huu, kwa kuendelea kusisitiza kwa kuwataka mawakili wa washtakiwa kufika siku hiyo bila kukosa ili washtakiwa waanze kupanda kizimbani kujitetea.

Mbali na Murro, washitakiwa wengine ni Edmund Kapama na Deogratius Mugasa ambao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 15 mwaka 2010.
Washitakiwa haop wanadaiwa kula njama, kushawishi na kuomba rushwa ya sh milioni 10 kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Karoli Wage. Kati ya mashitaka matatu yaliyofunguliwa dhidi yao, Murro anakabiliwa na mashitaka mawili.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Agosti 4 mwaka 2011.

MAHAKAMA YAOMBWA KUFANYIA MAREJEO AMRI UTETEZI WA KAKOBE

Na Happiness Katabazi
WALIOKUWA wachungaji watatu wa Kanisa Full Gospel Bible Fellowship wameiomba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ifanye marejeo ya amri yake iliyoitoa Julai 11 mwaka huu, ambayo ilimtaka mdaiwa ambaye ni askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Zakaria Kakobe awasilishe utetezi lakini akashindwa kutekeleza amri hiyo.


Wachungaji hao ambao ni walalamikaji katika kesi ya madai Na. 79/2011 ni mchungaji Dezidelius Patrick, Angelo Mutasingwa na Benedict Kaduma ambao katika kesi ya msingi iliyopo mbele ya Jaji Agustine Shangwa, wanamlalamikia Kakobe kuwa amekuwa akiliendesha kanisa hilo kinyume na taratibu.

Wadaiwa hao wamewasilisha ombi hilo la kuoiomba mahakama hiyo iifanye mapitio ya amri yake ikiwa ni siku chache tu baada ya mdaiwa (Kakobe) kuwasilisha utetezi wake ndani ya siku 21 ambapo siku hizo 21 zilianza kuhesabiwa Juni 29 mwaka huu, siku ambayo mdaiwa huyo alipokea hati ya wito wa mahakama(Summons) toka katika kampuni ya udalali ya Majembe Auction Mart na siku hizo 21 zilikuwa zikimalizika Julai 21 mwaka huu.

“Tunaiomba mahakama hii ichukulie uzito hili ombi letu kwamba mdaiwa(Kakobe) alikataa kukubali hati ya wito wa mahakama kaunzia Juni 23,25 na 27 mwaka huu wakati mwakilishi wa kampuni hiyo ya udalali ilipomlekea hati hiyo na mwakili huyo alirudi kwa kwa wakili wetu Miriam Majamba na kumweleza ameshindwa kumpatia Kakobe hati hiyo kwasababu hakuwepo wakati ukweli ni kwmaba alikuwepo Juni 29 mwaka huu.

“Siku hiyo hiyo ya Juni 29 mwaka huu, hati hiyo ya wito ilipokelwa na mtu mmoja aitwaye Mpokela kwaniaba ya mdaiwa na kwamba mdaiwa siku zote hizo alikuwepo hapa jijini Dar es Salaam, isipokuwa Julai 6 na 7 ambapo mdaiwa alikuwa safari mkoani Dodoma.

Aidha wadaiwa hao walidai kuwa kwakuwa mdaiwa alishindwa kuwasilisha utetezi wake ndani ya 21 alizopewa na mahakama na badala yake akawasilisha utetezi wake Julai 29 mwaka huu, alipaswa aiombe mahakama imuongee muda wa kuweza kuleta utetezi wake na kwakuwa ameshindwa kafanya hivyo ni kinyume na cha sheria ya madai na katiba ya nchi.

Katika utetezi wake huo Kakobe ameieleza mahakama kuwa walalamikaji wote waliwai kubainika kutenda vitendo viovu na kwamba uongozi wa kanisa hilo ulishawavua madaraka yao ya uchungaji hivyo na kuongeza kwa kuiomba mahakama hiyo itupilie mbali kesi hiyo kwani haina msingi wowote.

Aidha Jaji Shangwa aliairisha kesi hiyo hadi Septemba 5 mwaka huu, ambapo siku atasikiliza pingamizi lilowasilishwa na Kakobe.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Agosti 3 mwaka 2011.

ZOMBE:GODBLESS LEMA NI MBUMBUMBU WA SHERIA

Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi,(ACP), Abdallah Zombe amesema Mbunge wa Arusha Mjini(CHADEMA) Godbles Lema ni mbumbumbu wa Sheria na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.


Sambamba na hilo Zombe amemtaka Lema kufuata yale yote aliyotumwa na wapiga kura wake bungeni na siyo kumjadili yeye na kwamba wakati mbunge huyo alipokula kiapo cha utii wa kuitii Katiba na leo hii anatenda matendo yanakwenda kinyume na kanuni za bunge na katiba hiyo, hivyo mbunge huyo ni hatari kwa nchi na wapiga kura wake.

Zombe aliyasema hayo jana kwenye mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika nje ya viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ambapo alisema uamuzi huo baada ya Julai 28 mwaka huu, wakati Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha kuwasilisha bajeti yake na mbunge huyo ambaye ni waziri kivuli wa wizara hiyo kuhoji ni kwanini Zombe na wenzake waliachiliwa huru wakati nimiongoni mwa askari polisi walioua raia bila hatia.

“Mwalimu Julias Nyerere aliwahi kusema kuwa huru bila nidhamu ni sawa na wendawazi na nidhamu bila uhuru ni sawa na utumwa…sasa kwanukuu hiyo na ukiioanisha na vitendo vya utovu wa nidhamu vinavyofanywa na baadhi ya wabunge akiwemo Lema nasema kabisa wabunge hao wanaofanya vitendo hivyo ni wendawazimu na hawastahili kuendelea kuwepo bungeni kwani wanaporomosha heshima ya bunge letu tukufu”alisema Zombe.

Alisema tangu mwaka 1992 vyama vingi viliporuhusiwa hapa nchini, vyama vya upinzani viliweza kushinda katika majimbo mbalimbali na kufanya wabunge wao kuingia ndani ya bunge ambao siku zote wabunge hao wa upinzani kama Freeman Mbowe Said Arif,Wilbroad Slaa, Habib Mnyaa wamekuwa wakiheshimu kanuni za bunge lakini cha kushangaza Lema na wenzake wamekuwa mstari kufanya vitendo vya kiwendawazimu bungeni hali inayopelekea kuidhalilisha CHADEMA.

Zombe alimtaka Lema akaisome Ibara ya 107A ya Katiba, ambayo inasema wazi mamlaka ya mwisho ya utoaji haki ni mahakama lakini anashangazwa na mbunge huyo kwenda kuhoji kesi ilikwishatolewa uamuzi na Mahakama Kuu na rufaa yake tayari imeshafunguliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka katika Mahakama ya Rufaa na kuongeza kuwa kitendo kilichofanywa na mbunge huyo dhidi yake ni dhahiri mbunge huyo hafamu kuwa majukumu yanayofanywa na mihili mitatu ya nchi ya Serikali,Bunge na Mahakama.

“Lema anasimama katika ya bunge ananizungumzia mimi wakati anajua wazi ananizungumzia mimi ambaye sinafursa ya kwenda kujieleza bungeni?Ninavyomfahamu mimi huyu Lema ni miongoni mwa watu wanaotuhumiwa kuwa mwanamtandao wa wezi wa magari Arusha na taarifa hizo za Kiintelijensia zilinifikia ofisini kwangu wakati nipo RCO hapa jijini na wakati zikifanyiwa kazi ndiyo nikapatwa na matatizo ya kubambikiwa kesi na sina hakika kama amaeacha hiyo tabia ….na ninasisitiza naungana na kauli ya mbunge wa (CCM), Deo Filikunjombe utovu wa nidhamu unaoendelewa kufanywa na baadhi ya wabunge ni utoto”alisema Zombe.

Aidha alisema anashangazwa na Lema kuwa na jeuri ya kuhusu kesi mauji iliyokuwa ikimkabili yeye na wenzake lakini mbunge huyo anashindwa kutumia bunge hilo hilo kuhoji kesi ya maandamano haramu inayomkabili yeye na wanachama wengine wa CHADEMA katika Mahakama ya Mkoa wa Arusha imefikia wapi na kuongeza kwa kuwataka wabunge wafuate kilichowapeleka bungeni na siyo kumaliza muda mwingi kuwajadili wananchi ambao siyo wabunge.

Wakati huo huo, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam, Upendo Msuya aliairisha kesi ya madai y ash bilioni 5.2 iliyofunguliwa na Zombe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambapo alisema kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kutajwa na kwamba anaiarisha hadi Septemba 8 mwaka huu, kwaajili ya kuanza kusikilizwa.

Agosti 17, 2009, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa hukumu ya kushtusha baada ya kumwachilia huru Zombe na wenzake wanane waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja.

Serikali ilikata rufaa Oktoba 7, 2009 katika Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwachilia Zombe na wenzake.

Akisoma hukumu, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati, alisema baada ya kupitia ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo, alibaini kuwa serikali ilishindwa kuthibitisha mashtaka na kuwa kamwe mahakama haiwezi kumtia hatiani mshtakiwa kwa ushahidi dhaifu na wa kusikia kama uliowasilishwa mahakamani hapo.

Jaji huyo alihitimisha hukumu yake kwa kusema kuwa washtakiwa hao si wauaji na aliliagiza Jeshi la Polisi liwatafute wauaji halisi wa wafanyabiashara waliouawa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Agosti 2 mwaka 2011.

BOSI WA RICHMOND AIBWAGA SERIKALI


*SERIKALI YADHAMIRIA KUKATA RUFAA KUPINGA
Na Happiness Katabazi
HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es salaam, imemwachiria huru mfanyabiashara Naeem Adam Gire aliyekuwa akikabiliwa na makosa ya kughushi, kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa serikali kuhusu kampuni ya Richmond LLC ya Texas ya Marekani kwasababu ushahidi ulitolewa na upande wa Jamhuri ni dhahifu.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Waliarwande Lema ambaye alisema kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya mahakama hiyo kutoa uamuzi wa ama mshtakiwa huyo Gire aliyekuwa akitetewa na wakili wa kujitegemea Alex Mgongolwa na Richard Rweyongeza ambapo Jamhuri ilikuwa ikiwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali Fredrick Manyanda na Shadrack Kimaro ana kesi ya kujibu au la.

Lema alisema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wote tisa na vilelelezo vilivyotolewa na upande wa Jamhuri, amebaini ushahidi na vielelezo hivyo ni dhahifu na una mapungufu ambao umeacha mashaka na maswali mengi na hivyo mahakama yake imefikia uamuzi wa kutumia kifungu cha 330 cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, ambacho kinaipa mamlaka mahakama ya kumwona mshtakiwa hana kesi ya kujibu na kumwachiria huru.

“Hii kesi ambayo leo(jana) naitolea uamuzi ni wazi kabisa imejaa mapungufu mengi ya kisheria tena yapo wazi kabisa na simung’unyi maneno nasema wazi kabisa hii kesi ni miongoni mwa baadhi ya kesi za jinai zinazofunguliwa na Jamhuri ambazo mwisho wa siku mahakama inajikuta ikitupiwa lawama…na sheria za nchi zipo wazi zinaipa mamlaka mahakama kumuona mshtakiwa hana kesi ya kujibu pindi itakapobaini ushahidi ulioletwa na Jamhuri dhidi yake ni dhahidi na usio na mashiko”alisema Hakimu Lema.

Hakimu Lema alisoma uamuzi huo(ruling) uliokuwa ukisubiliwa kwa hamu na wananchi wengi kwa mtindo wa kuyaweka mashtaka yaliyokuwa yakimkabili mshtakiwa.Alisema Gile alikuwa akikabiliwa na makosa ya kugushi, kutoa hati ya uwakilishi iliyogushiwa(Power of Attorney), kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa serikali ambao ni wajumbe wa Bodi ya Tenda ya Shirika la Umeme la Tanesco na Timu ya Tathimini.

Kwamba Januari 13 mwaka 2009 mahakamani hapo Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Stanslaus Boniface, alidai kuwa Machi 13 mwaka 2006 jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu , mshtakiwa huyo aligushi hati ya uwakilishi(Power of Attorney) ya Machi 13 mwaka 2006 iliyokuwa imeguhishiwa na kuonyesha Mwenyekiti wa Kampuni ya Richmond LLC ya Texas ya Marekani, Mohamed Gile ambaye ni kaka wa mshtakiwa anaishi Marekani alikuwa amemuidhinisha mshtakiwa kuiwakilisha hapa Tanzania.

Hakimu Lema alisema kuwa kwa mujibu wa hati hiyo ya mashtaka, Jamhuri inadai kuwa Machi 20 mwaka 2006 katika eneo la Umeme Park Bara bara ya Morogoro jijini Dar es Salaam, kwa nia ovu mshtakiwa huyo alitoa hati hiyo ya uwakilishi kwa maofisa hao wa serikali iliyokuwa ikionyesha imesainiwa na Mohamed Gile kuonyesha kuwa Mohamed amemteua mshtakiwa kuiwakilisha kampuni hiyo hapa nchini kinyume na kifungu cha 333, 335(e)(3),337,342 na 122(a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Akitoa uamuzi wake kwa kuanza kulichambua kosa la kugushi ambalo ni kinyume cha kifungu cha 333 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, Hakimu Lema hati iliyogushiwa ni lazima iwe na udanganyifu ndani yake na katika kesi hiyo hati inayodaiwa kugushiwa na upande wa jamhuri ni Power of Attorney.

“Hivyo basi katika kutatua mgogoro huo wa hati hiyo ya uwakilishi , Jamhuri ilileta mashahidi watatu kwaajili ya kuutatua mgogoro huo miongoni mwa mashahidi hao ni mawakili wawili ambao ndiyo waliyoiandaa hati hiyo na shahidi sita ambaye ni mtaalamu wa maandishi toka Jeshi la Polisi, Hamis Hamad.

“Licha ya kuletwa kwa mashahidi hao watatu kwaajili ya kuutatua mgogoro huo, mahakama hii imebaini hakuna ushahidi walioutoa unaonyesha hati hiyo ya uwakilishi ilighushiwa, pia hakuna ushahidi uliotolewa unaonyesha mshtakiwa huyo kweli alighushi hati hiyo kwakuwa hata huyo shahidi wa sita ambaye ni mtaalamu wa maandishi toka Polisi, Hamad, hakuweza kutoa mapungufu yaliyokuwepo kwenye ile hati ya uwakilishi ambayo Jamhuri inadaiwa hati hiyo inasaini ambayo imegushiwa.

“Na mtaalamu huyo wa maandishi aliangalia saini zilizokuwa kwenye hati hiyo na hakuna sehemu shahidi huyo aliyoangalia saini ya mshtakiwa na ile saini iliyokuwa kwenye hati ile na mahakama hii inasema katika uchunguzi wake shahidi huyo wa sita (Hamad) alitakiwa achukue saini ya mshtakiwa ailinganishe na saini iliyosainiwa kwenye ile hati ya uwakilishi na kwakuwa shahidi huyo ameshindwa kufanyakazi yake yake hiyo ya kikamilifu, mahakama hii inasema jamhuri imeshindwa kuthibitisha kosa hilo kwasababu mtaalamu wa maandishi ameshindwa kuyaainisha mapungufu yaliyopo kwenye hati hiyo halisi na hati iliyogushiwa ”alisema Hakimu Lema.

Kuhusu shtaka la pili na tano ambalo ni la kuwasilisha hati iliyogushiwa kwa maofisa wa serikali, hakimu Lema alisema kwa kuwa kosa la kwanza la kughushi hati hiyo ya wakilishi Jamhuri imeshindwa kulithibitisha, ni wazi kabisa hati hiyo ya uwakilishi iliyowasilishwa kwa maofisa wa Tanesco haikuwa imegushiwa kwasababu Jamhuri imeshindwa kuleta mashahidi ambao wangeweza kuonyesha hati halisi ya uwakilishi ni na hati iliyogushiwa ni hipo hivyo basi katika kosa la pili na tano, jamhuri imeshindwa kuyathibitisha.

Aidha Hakimu Lema ambaye alikuwaa akiusoma uamuzi wake huo huku akionyesha umakini, akitolea uamuzi kuhusu kosa la tatu na la nne, ambayo ni kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa serikali kuwa kampuni ya Richmond inauwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 100 huku akijua si kweli, alisema kwakuwa mashahidi wa tatu wa jamhuri walifika mahakamani hapo na kuieleza mahakama kuwa jumla ya makampuni nane yaliomba kupatiwa tenda ya kuzalisha umeme hapa nchini.

Lakini mashahidi hao wakaieleza mahakama kuwa katika kikao cha kwanza cha ufunguzi wa tenda hiyo kilichofanyika Machi 2 mwaka 2006, makampuni yote yalifanyiwa usaili na bodi na timu hiyo ikabaini hakuna kampuni hata moja iliyokidhi vigezo na ikaamuru usahili ufanyike upya kwa mara ya pili na hata ulipofanyika bado makampuni yote yalishindwa kukizi vigezo ndipo shahidi wa tatu Injinia wa Tanesco, Simon Jilima mwaka 2006 akateuliwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati huo Dk.Ibrahim Msabaha aende kusimamia ufungwaji wa mitambo ya Richmond.

“Kwa ujumla mahakama hii inasema jamhuri imeleta ushahidi dhahifu ambao umeshindwa kuishawishi mahakama imuone mshtakiwa ana kesi ya kujibu hakuna kabisa ushahidi unaonyesha nyaraka za kampuni ya Richmond zilizowasilishwa kwa Bodi ya Tanesco ziliwasilishwa na mshtakiwa ila kwa mujibu wa shahidi wa nne aliambia mahakama nyaraka hizo ziliwasilishwa kwenye bodi hiyo na mwenyekiti wa Richmond, Mohamed na siku hiyo Mohamed aliwatambulisha wajumbe wa bodi kuwa mshtakiwa ni mdogo yake na kwamba ndiye amempa jukumu la kuiwakilisha kampuni yake hiyo hapa Tanzania.

“Na kwakuwa Jamhuri ilidai mshtakiwa alighushi saini Mohamed Gile katika ile hati ya uwakilishi, Jamhuri ilipaswa imlete Mohamed hapa mahakama aje atoe ushahidi kwamba hakumpa mshtakiwa mamlaka ya kuiwakilisha kampuni yake hapa nchini kwasababu hilo Jamhuri imeshindwa kutekeleza jukumu lake ili mwisho wa siku mahakama ilaumiwe, mahakama hii inamwachiria huru mshtakiwa na inamfutia kesi hiyo”alisema Lema.

Baada ya kutoa uamuzi huo wakili wa serikali Shadrack Kimaro alisema Jamhuri haijaridhishwa na uamuzi huo hivyo inaomba ipatiwe mwenendo wa kesi hiyo ili iende Mahakama Kuu kukata rufaa.

Kwa upande wake Naeem Gire aliwaeleza waandishi wa habari nje ya viwanja vya mahakama, hiyo alisema amefurahishwa na uamuzi huo na kwamba mahakama imetenda haki.
Gile amefikishwa mahakamani Januari 13 mwaka 2009 ikiwa ni mwaka mmoja upite tangu aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na mwenzake aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha, mapema Februali mwaka 2008 viongozi hao walipolazimika kujiuzulu nyadhifa zao kwa kashfa hiyo ya Kampuni hiyo ya kufua umeme ya Richmond.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Julai 29 mwaka 2011.

PINGAMIZI LA AG KESI YA MPENDAZOE KUSIKILIZWA KWA MAANDISHI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam,jana ilijikuta ikishindwa kuanza kusikiliza pingamizi la Mwanasheria Mkuu wa Serikali lililotaka kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa Jimbo la Segerea iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo, Fred Mpendazoe(Chadema) ifutwe kwasababu hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho imekiuka amri ya mahakama hiyo, badala yake imezitaka pande zote kuwasilisha hoja zake kwa maandishi.


Wadaiwa katika kesi hiyo ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 wa Jimbo la Segerea ni Mwansheria Mkuu wa Serikali(AG), Mbunge wa jimbo hilo, Dk.Makongoro Mahanga (CCM) anayetetewa na wakili wa kujitegemea Jerome Msemwa na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo.Mahanga anayapinga matokeo yaliyomtangaza mshindi Mahanga kwasababu kanuni na sheria ya Uchaguzi zilikiukwa.

Mawakili wa Serikali Patience Ntinwa na David Kakwaya mbele ya Jaji Profesa Ibrahim Juma waliikumbusha mahakama hiyo kuwa kesi hiyo ya madai ilikuja jana kwaajili ya mahakama hiyo kuanza kusikiliza pingamizi hilo la mdaiwa ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya mlalamikaji Mpendazoe.

Jaji Profesa Juma alisema muda alikuwa na muda mchache ambao usingeweza kusikiliza pingamizi hilo na kwasababu hiyo anatoa amri ya pingamizi hilo kusikilizwa kwa njia ya maandishi hivyo akamtaka mwanasheria mkuu wa serikali kuwasilisha sababu za pingamizi lake kwa maandishi Agosti 10 na mlalamikaji (Mpendazoe) awasilishe majibu ya pingamizi hilo Agosti 24 na mdaiwa ajibu kama analakujibu kutokana na hoja zitakazokuwa zimewasilishwa na mlalamikaji Agosti 30 na kwamba uamuzi wa pingamizi hilo atautoa Septemba 15 mwaka huu.

Julai 5 mwaka huu, wadaiwa wawili AG, na Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Segerea waliwasilishwa kwa maandishi mahakamani hapo mapingamizi mawili ambapo pingamizi la kwanza wanadai kuwa hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho na kuwasilishwa na mlalamikaji mahakamani ni batili kwasababu imekiuka amri ya mahakama iliyomtaka mlalamikaji huyo akaifanyie marekebisho tu hati hiyo ya madai lakini cha kustaajabisha mlalamikaji huyo amewasilisha hati hiyo iliyofanyiwa marekebisho huku akiwa ameongeza dai jipya ambalo halikupaswa kuwekwa kwenye hati hiyo iliyofanyiwa marekebisho akiwa ameongeza dai jipya ambalo halikupaswa kuwekwa kwenye hati hayo hivyo wakaomba hati hiyo iliyofanyiwa marekebisho nayo itupwe.

Kuwasilishwa majibu hayo ya hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho pamoja na pingamizi hilo kulitokana na amri iliyotolewa na Jaji Juma, Juni 22 mwaka huu kwa wadai hao.

Kuwasilishwa mahakamani kwa hati hiyo iliyofanyiwa marekebisho na Mpendazoe, kulitokana na utekelezaji wa amri iliyotolewa na Jaji Profesa Juma, Juni 6 mwaka huu, ambapo aliamuru hati ya madai ya awali ikafanyiwe marekebisho kwa kuviondoa vituo 10 vya kupigia kura ambavyo mlalamikaji hakuvitaja kwa majina.

Baada ya kufanyiwa marekebisho, Wakili wa mlalamikaji Peter Kibatala alieleza hivi sasa hati hiyo inasomeka kuwa wamebakiwa na vituo vya kupigia kura 249 ambapo vituo 120 ni vya Kata ya Kiwalani na vituo 129 ni vya Kata ya Vingunguti.

Novemba mwaka 2010 Mpendazoe alifungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo ambayo yalimtangaza mbunge wa sasa Dk. Mahanga kuwa ndiye mshindi kwa sababu uchaguzi huo ulikiuka matakwa ya sheria ya uchaguzi ya mwaka 2010.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamis, Julai 28 mwaka 2011.