KESI YA SIMU YA LIYUMBA YAKWAMA


Na Happiness Katabazi
UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kukutwa na simu ya mkononi gerezani inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu(BoT), Amatus Liyumba(63) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ulishindwa kutimiza ahadi yake kumsomea maelezo ya awali(PH) mshtakiwa huyo kwa madai kuwa wamegundua mapungufu kwenye ushahidi uliopo kwenye jalada la kesi hiyo.


Hayo yalielezwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Stewart Sanga na wakili wa serikali Ladslaus Komanya na Cecilia Mkonongo ambapo walianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya upande wa Jamhuri kumsomea mshtakiwa huyo maelezo ya awali lakini kutokana na sababu hiyo wakashindwa kuandaa maelezo ya kesi hiyo kwasababu wamegundua mapungufu kwenye ushahidi uliokuwa umekusanywa na polisi kwenye jalada la kesi hiyo.

“Kwa sababu hiyo, tunaiomba mahakama hii iiarishe kesi na tunaomba tupewe wiki mbili kuanzia leo tutakuwa tumerekebisha mapungufu hayo baada ya wiki mbili tutakuwa tayari tumeishakamilisha …kwahiyo leo tumeshindwa kumsomea maelezo ya awali Liyumba kwa sababu ya mapungufu hayo ambayo yamesababisha tushindwe kuandaa maelezo ya kesi ambayo tungekuwa tumeyaandaa ndiyo tungemsomea leo”alisema wakili Komanya.

Baada ya kumaliza kutoa sababu hiyo wakili huyo wa serikali, wakili wa utetezi Majura Magafu anayesaidiwa na Hudson Ndusyepo na Onesmo Kyauke alidai kimsingi sababu zilizotolewa na wakili huyo wa Jamhuri hazina mantiki kwani Septemba 8 mwaka huu,siku ambayo ndiyo kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo, Wakili wa Serikali Elizabeth Kaganda alimsomea mashtaka mshtakiwa na kudai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na akaomba apangiwe tarehe ya jana kwaajili ya kuja kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa huyo hivyo hiyo sababu ya eti wamegundua ushahidi uliokusanywa kwenye jalada la kesi una mapungufu,walipaswa waiseme sababu hiyo siku ile waliyojigamba kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

“Mheshimiwa hakimu kama utakumbuka hata siku ya kwanza kesi hii ilipofunguliwa ni sisi upande wa utetezi ndiyo tuliusaidia upande wa Jamhuri kuwaonyesha kuwa hati yao ina mapungufu ya kisheria hadi wewe hakimu siku hiyo hiyo ukatoa amri ya kuutaka upande wa Jamhuri uende ukaifanyie marekebisho hati yao mashitaka na wakaenda kuifanyia marekebisho na saa chache walivyorudi wakadai upelelezi umekamilika .

“Sasa sisi upande wa utetezi tunaona hizo wiki mbili walizoomba ni ndogo, tunaomba mahakama iwapatie muda wa mwezi mmoja ili kama wanaenda kumpikia kesi mpya Liyumba waende kuipika kabisa ila tunaomba Jamhuri ifahamu kuwa tayari sisi upande wa Jamhuri tumeishawasilisha kwa maandishi mahakamani hapa taarifa ya kuwasilisha pingamizi la awali na upande wa Jamhuri tumeishawapatia nakala ya pingamizi hilo na tunaiomba mahakama hii siku kesi hii itakapokuja kwaajili ya usikilizwaji wa awali basi siku hiyo hiyo ndiyo pingamizi letu nalo lisikilizwe” alidai wakili Magafu kwa sauti ya juu.

Wakili Ndusyepo alieleza pingamizi hilo la awali waliloliwasilisha kwa uongozi wa mahakama hiyo, ni wanadai kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kwamba sababu zote watazitoe siku hiyo ya pingamizi litakapokuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa.

Hakimu Mkazi Sanga alisema amesikiliza hoja za pande zote mbili amekubaliana nazo na kwamba anaiarisha kesi hiyo hadi Septemba 28 mwaka huu, ambapo siku hiyo upande wa Jamhuri itakuja kwaajili ya kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa huyo na pingamizi hilo la upande wa utetezi litasikilizwa na mahakama hiyo.

Septemba 23 mwaka huu, Liyumba alitoka gerezani la Ukonga jijini Dar es Salaam, alikokuwa akiishi baada ya kumaliza kutumikia adhabu yake ya kifungo cha miaka miwili gerezani.

Septemba 8 mwaka huu, kwa mara nyingine tena Liyumba alifikishwa mbele ya hakimu Sanga akikabiliwa na kosa la kukutwa na kitu kilichokatazwa gerezani chini ya kifungu cha 86 (1,2) cha Sheria ya Magereza kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Wakili Kaganda alidai kuwa Liyumba ambaye wakati huo alikuwa ni mfungwa mwenye Na.303/2010, Julai mwaka huu, ndani ya gereza la Ukonga, alikutwa na simu ya Nokia Na.1280 nyeusi iliyokuwa na laini yenye Na. 0653-004662 na IMEI Na. 356273/04/276170/3 ambayo alikuwa aikiitumia kufanyia mawasiliano binafsi wakati ni kinyume cha sheria. Hata hivyo alipata dhamana baada ya kujidhamini kwa bondi ya Sh 50,000.

Desemba mwaka 2010 , Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Emilian Mushi alitupilia mbali rufaa iliyokatwa na Liyumba iliyokuwa ikiiipinga hukumu ya Mahakama ya Kisutu iliyomuhukumu kwenda jela miaka miwili baada ya kumtia hatiani kwa kosa moja la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma ambapo jaji huyo alisema akubaliana na hukumu ya Kisutu kwani ilikuwa sahihi kisheria.

Mei 23 mwaka 2010, Mahakimu wawili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa walitoa hukumu ya kumtia hatiani Liyumba kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma, na hakimu mkazi mmoja Edson Mkasimongwa ambaye ndiye aliyekuwa akiliongoza jopo hilo kusikiliza kesi hiyo alitofautiana na mahakimu hao wawili na akatoa hukumu ya peke yake ambayo ilimwachiria huru mshtakiwa huyo.

Lakini hata hivyo hukumu iliyotolewa na mahakimu hao wawili ndiyo ilibaki kuwa ni hukumu ya mahakama ya Kisutu na hukumu ya Hakimu Mkasimongwa ikabaki kwenye kumbukumbu za mahakama na haikutumika kwaajili ya kumpatia adhabu Liyumba.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Septemba 30 mwaka 2011.

DOWANS YAIBWAGA TANESCO


*ZITTO:NI MATOKEO YA SIASA CHAFU
Na Happiness Katabazi

JITIHADA za wanasiasa na wanaharakati kulizuia Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO), kulipa tuzo ya mabilioni ya shilingi kwa Kampuni ya kufua umeme, Dowans Tanzania, zimegonga mwamba baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam kutoa uamuzi wa kuiruhusu Dowans kusajili tuzo hiyo ili ilipwe.


Tuzo hiyo ya dola za Marekani milioni 65 (takriban sh bilioni 94) iliyotolewa Novemba 15, mwaka jana (2010); na Januari 25, mwaka huu, Dowans iliwasilisha ombi lake la kutaka Mahakama Kuu ya Tanzania iisajili tuzo waliyopewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa migogoro ya Kibiashara (ICC).

ICC iliitia hatiani TANESCO kwa kosa la kuvunja mkataba na Dowans, na ikaiamuru iilipe tuzo hiyo na riba ya asilimia 7.5.

Lakini wanaharakati kadhaa na wanasiasa hapa nchini wamekuwa wakipinga uamuzi huo wa ICC mahakamani. Jana Jaji Emilian Mushi alisema Mahakamu Kuu ya Tanzania haina mamlaka ya kutengua hukumu ya ICC.

Hatua hiyo ya wanasiasa na wanaharakati kuchelewesha malipo ya tuzo hiyo itaifanya TANESCO kulipa kiasi kikubwa zaidi kwani riba imekuwa inaongezeka. Hadi jana Dowans ilikuwa inastahili kulipwa sh bilioni 113 badala ya sh bilioni 94 kutokana na ucheleweshwaji huo.

Katika hukumu hiyo aliyoanza kuisoma kuanzia saa 3:31 asubuhi hadi 6:53 mchana, Jaji Mushi alisema kesi hiyo ya madai Na. 8/2011 iliyofunguliwa na TANESCO dhidi Dowans Tanzania, ilikuja kwake ili atoe hukumu ya ama kuiruhusu Dowans kusajili au kutokusajili tuzo hiyo. TANESCO katika pingamizi lake iliwasilisha sababu 12 za kupinga tuzo hiyo isisajiliwe.

Jaji Mushi alianza kwa kusema maneno yafuatayo:

“Kwanza, naishukuru TANESCO na zile taasisi nne za wanaharakati waliokuwa wakiongozwa na LHRC; walijitokeza mahakamani hapa kupinga tuzo ya Dowans isisajiliwe na kutumia muda wao kuchambua kesi mbalimbali na kuandaa mapingamizi yao, ambayo hata hivyo niliyatupilia mbali.

“Pili, nafahamu fika kuwa kesi hii ya Dowans ina sayansi nyingi sana za kisiasa, hivyo napenda niwafahamishe mapema kabisa kabla ya kuendelea kuwa hukumu yangu nitakayotoa leo haijatoa nafasi kwa sayansi hizo za kisiasa, kwa sababu imezingatia misingi ya sheria na haki.”

Jaji Mushi alisema miongoni mwa sababu zilizowasilishwa na mlalamikaji (TANESCO) za kutaka tuzo ya Dowans isisajiliwe ni pamoja na majaji wa Mahakama ya ICC kuipendelea Dowans, hukumu yake kuwa na upungufu wa kisheria, hukumu kutofuata sera na maslahi ya taifa na Mahakama Kuu ya Tanzania kutokuwa na mamlaka ya kuisajili tuzo hiyo. Dowans ilikuwa inatetewa na Wakili Kennedy Fungamtama, huku TANESCO ikitetewa na Kampuni ya uwakili ya Rex Attorney. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliwakilishwa na Naibu Mwanasheria Mkuu, George Masaju na Dk. Hawa Senare.

Jaji Mushi alisema baada ya kuipitia hukumu ya ICC amebaini kuwa haina makosa ya kisheria kama anavyodai mlalamikaji, na ndani ya hukumu hiyo alikuta kiambatanisho ambacho ni mkataba kati ya TANESCO na Dowans uliosainiwa Juni 23, mwaka 2006; na kufafanua kwamba pande zote mbili katika mkataba huo zilikubaliana kwamba uamuzi wa ICC ndiyo utakuwa wa mwisho, na utazibana pande zote mbili na hautaweza kukatiwa rufaa.

Jaji huyo alisema kifungu cha 14 (f) cha mkataba huo kinasomeka hivi: “The parties waive any right to challenge or contest the validity or enforceability of this arbitration agreement or any arbitration proceeding or award brought in conformity with this section.” Kwa tafsiri nyepesi, Fungamtama alisema kifungu hicho kinasema, TANESCO na Dowans katika mkataba wao walikubaliana kwa maandishi kuweka kando haki za kupinga au kuhoji mwenendo na tuzo zitakazotolewa na baraza la usuluhishi.

Jaji akasema: “Sasa kwa mujibu wa mkataba huo ni wazi kuwa TANESCO na Dowans walikubaliana kuwa endapo utatokea mgogoro baina yao utapaswa upelekwe ICC tu na ICC itakapotoa hukumu ya mgogoro baina yao, pande hizo mbili hazitakuwa na mamlaka ya kuikatia rufaa hukumu hiyo ya ICC.

“Kwa makubaliano hayo ya pande hizo mbili ndani ya mkataba huo wa POA ambao TANESCO hadi wanakwenda kujitetea ICC hawakuwa wameuvunja huo mkataba wa POA na kupitia mkataba huo ICC pia iliutumia kutolea uamuzi wake…ni wazi kabisa mahakama hii inakubaliana na hukumu ya ICC kuwa ilikuwa ni hukumu ya haki na iliyofuata sheria na ilizingatia pia masilahi ya sera za Tanzania na kwakuwa pande hizo zilikubaliana hukumu ya ICC hawataweza kuikatia rufaa basi ndivyo hivyo hivyo mahakama hii ya Tanzania haiwezi kutoa uamuzi wa kutengua hukumu hiyo iliyotolewa na ICC.”

Alisema anakubaliana na hoja ya wakili wa Dowans, Fungamtama, kuwa kifungu cha 3 cha jedwali la 3 katika Sheria ya Usuluhishi ya Tanzania, Sura ya 15 ya mwaka 2002 ambacho kinasomeka hivi: Kwa tafsiri rahisi, kifungu hicho utaona tayari nchi imejifunga mikono na utekelezaji wa hukumu zinazotolewa na mahakama za kimataifa kwa sababu ni nchi yetu yenyewe imeridhia sheria na mikataba ya kimataifa.

Jaji Mushi alisema kitendo cha TANESCO kuwasilisha ombi mbele yake likidai kuwa Mahakama Kuu haina mamlaka ya kusajili tuzo hiyo, halina ukweli na kwamba mwanasheria aliyefahamu vema Sheria ya Usuluhishi ya Tanzania ya mwaka 2002 Sura ya 15, Mikataba ya Kimataifa na Sheria ya Makosa ya Madai ya mwaka 2002 ataona wazi kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania imepewa mamlaka ya kusajili tuzo hapa nchini zinazotolewa na Mahakama za Kimataifa.

Jaji alisema hoja ya TANESCO kuwa mwenendo wa hukumu ya ICC ulikuwa na mapungufu ya kisheria, haikupaswa kupelekwa mbele yake kwani Tanasco walikuwa ni wadaiwa katika kesi iliyofunguliwa ICC na walipaswa kuiwasilisha hoja hiyo ICC kabla ya mahakama hiyo ya kimataifa kutoa hukumu yake na kuikumbusha TANESCO kuwa ni yenyewe iliyoingia mkataba wa POA na Dowans ambao kwa ridhaa yao waliridhia kuwa hukumu itakayotolewa na ICC haitakatiwa rufaa.

Kutokana na makubaliano ya pande hizo mbili, Jaji Mushi aliishangaa TANESCO kwa hatua yake ya kuwasilisha hoja hiyo ambayo ni wazi ilipaswa iwasilishwe kwenye mashauri ambayo yamekatiwa rufaa na kwamba shauri lilokuwa mbele yake halikuwa shauri la rufaa.

Hata hivyo Jaji Mushi alisema anatupilia mbali hoja ya TANESCO iliyodai kuwa hukumu ya ICC haikuzingatia sera za Tanzania kwa maelezo kuwa haina msingi na baada ya kuisoma hukumu ya ICC amebaini kuwa hukumu ya majaji wa ICC ilizingatia sera za Tanzania na kuitaka TANESCO itambue kuwa nchi yetu imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa na mahakama zote kote duniani zinatoa maamuzi yake kwa kufuata ushahidi uliowasilishwa mbele yake, sheria na haki na siyo vinginevyo.

Jaji Mushi alitupilia mbali hoja nyingine ya TANESCO iliyokuwa ikidai kuwa aliyekuwa mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, ndiye aliyekuwa akimiliki Dowans iliyokiuka taratibu za kupata tenda ya kuzalisha umeme kwa madai kuwa kesi iliyokuwa imefunguliwa ICC na Dowans dhidi ya TANESCO ilikuwa haihusiani kabisa na nani mmiliki wake, na akakubaliana na hukumu hiyo kuwa Rostam Aziz hausiki kwa namna yoyote ile kwenye kesi hiyo.

Jaji Mushi alikubali ombi la Dowans la kusajili tuzo waliyopewa na ICC isajiliwe na mahakama ya Tanzania. aidha, jaji aliiamuru TANESCO kulipa gharama zote za uendeshaji wa kesi hiyo, na Dowans ianze taratibu za kukazia hukumu ya Mahakama ya ICC.

Septemba 6 mwaka huu, Jaji Emilian Mushi alitoa uamuzi wa kuyatupilia mbali maombi ya wanaharakati waliokuwa wakiongozwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ambao waliiomba mahakama hiyo ikatae kusajili tuzo iliyotolewa na Mahakama ya ICC kwa kampuni ya Dowans Holdings SA(Costa Rica) na Dowans Tanzania kwa sababu wanaharakati hao hawana haki wala mamlaka ya kupinga hilo.

Katika uamuzi wake huo, Jaji Mushi alisema anakubaliana na pingamizi la wakili wa Dowans, Fungamtama kwamba walalamikaji hao hawakuwa wahusika kwenye kesi ya Dowans dhidi ya TANESCO iliyomalizika ICC, hivyo ni wazi hawakuwa na mamlaka ya kufungua kesi ya kupinga utekelezaji wa hukumu hiyo katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

“Katiba na sheria za maamuzi mbalimbali ya mahakama yapo wazi na yametamka wazi kuwa mashauri ya madai yanayohusu nchi mwenye dhamana ya ulinzi na kufungua kesi za aina hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hivyo natupilia mbali ombi la wanaharakati hao ambao walidai kuwa wao ni watanzania wenye haki na wajibu wa kulinda mali za watanzania ndiyo maana wakafungua kesi hii ya kutaka Tuzo ya Dowans isisajiliwe. Kwa msingi huo, nalitupilia mbali ombi lao,” alisema Jaji Mushi.

Mahakama ya ICC ilitoa hukumu ya kesi ya Dowans dhidi ya TANESCO, Novemba 15 mwaka jana baada ya kampuni hiyo kuishinda TANESCO katika kesi yake ya kudai fidia ya kuvunjiwa mkataba iliyokuwa imefunguliwa rasmi Novemba 20 mwaka 2008 na kupewa Na. 15947/VRO ambapo Mahakama ya ICC iliitia hatiani TANESCO kwa kosa la kuvunja mkataba na Dowans na ikaiamuru iilipe fidia ya dola za Marekani milioni 65 na riba ya asilimia 7.5.

Hukumu hiyo ya ICC, muda mfupi baada ya kutolewa ilizusha malumbano makali baina ya wananchi, wanaisiasa, mawaziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa kauli zinazopishana huku wachache wakitaka serikali iilipe Dowans na wengine wakisema kulipwa fidia kampuni hiyo ni ufisadi.

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, ndiye aliyekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari kuhamasisha umma na serikali isiilipe Dowans. Kwa upande mwingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Fredrick Werema na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, walitaka Dowans ilipwe, hali iliyosababisha baadhi ya wananchi kuwashambulia kwa maneno makali wale wote waliokuwa wakitaka Dowans isajiliwe kisha ilipwe tuzo yao.

Malumbano hayo nje ya mahakama yalisababisha pia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuunda Kamati ya Wabunge kujadili hukumu hiyo na kisha wabunge watatu wa chama hicho, George Simbachawe (Kibakwe), Mbunge wa Karagwe, Gosbert Blandes, Mbunge wa Viti Maalumu, Angellah Kairuki na raia wengine wanne kufungua kesi ya Kikatiba Na. 5/2011 dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na TANESCO ambayo imeanza kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Njegafibili Mwaikugile, Agustine Shangwa na Projest Rugazia.

Kwa mujibu wa hati ya madai, walalamikaji hao wanaiomba mahakama itoe amri ya kuizuia serikali isiilipe Kampuni ya Dowans na endapo malipo hayo yatafanywa kwa kampuni hiyo ni wazi wadaiwa hao ambao wanaiwakilisha serikali kwa ujumla watakuwa wamevunja ibara 26(2),27(1) na 27 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambazo mahakama hiyo ina wajibu wa kuilinda ibara hizo zisivunjwe.

ZITTO KABWE ATOA MAONI:
Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe, ameupongeza uamuzi huo wa Mahakama Kuu akidai kuwa ni malipo ya maamuzi yanayotokana na siasa za kipuuzi na uzalendo pofu.

Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu Kabwe alisema tumeliingiza taifa hasara kubwa kwa sababu ya uongozi dhaifu na siasa za makundi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alisema TANESCO hawataweza kulipa fidia hiyo kwani walilazimishwa kuingia mkataba na kisha kuuvunja.

Kabwe alisema Kamati ya Mashirika ya Umma imeishaagiza kwamba deni hilo lisitokee katika hesabu za Shirika la TANESCO bali Serikali Kuu na kwamba hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amegoma kusaini hesabu za TANESCO za mwaka 2010 mpaka serikali ikubali kubeba mzigo huo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Septemba 29 mwaka 2011.

MNYIKA AMTOA JASHO NG'UMBI KORTINI

Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeyakataa maombi ya aliyekuwa mgombea Ubunge Jimbo la Ubungo(CCM), Hawa Ng’umbi yaliyokuwa yanaiomba mahakama itamke kuwa mbunge wa sasa wa jimbo hilo John Mnyika(Chadema) alijihusisha na vitendo vya uvunjifu wa sheria za uchaguzi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.


Sambamba na uamuzi huo, Jaji Msuya alisema anamshangaa mlalamikaji(Ng’umbi) kwa kushindwa kwake kuyaondoa mapungufu hayo mapema hadi muda mrefu umepita sasa ndiyo mahakama inakuja kuyabaini mapungufu hayo jana.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Upendo Msuya wakati akitoa uamuzi wa kesi hiyo ya uchaguzi ambapo pia alisema anatupilia mbali ombi la mlalamikaji lilokuwa likiomba mahakama hiyo itamke kuwa matokeo yaliyomtangaza Mnyika ambaye jana alikuwepo mahakamani hapo kuwa mbunge hayakuwa halali.

Pia Jaji Msuya alitupilia mbali pingamizi la Ng’umbi liloomba mahakama itoe amri ya kumzuia Mnyika kushiriki uchaguzi wowote na lile liloomba mahakama hiyo itoe amri ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa huru na haki katika jimbo la Ubungo kwasababu amebaini maombi hayo hayanamsingi.

Jaji Msuya alisema amefikia uamuzi huo baada ya kukubaliana na hoja za wakili wa Mnyika (Edson Mbogoro) kuwa hati ya madai iliyofanyiwa marekebisho ina makosa kwani kuna baadhi ya haya hazifafanui tuhuma anazotuhumiwa na mdaiwa hali inayosababisha yeye kushindwa kuaanda utetezi wake.

“Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, nakubaliana na hoja za wakili wa mdaiwa(Mbogoro) kuwa hati ya madai haifafanui kwa uwazi tuhuma zinazomkabili mdaiwa hali ambayo imesababisha mahakama hii ione hati hiyo ina mapufungu na inaamuru hati hiyo iondolewe na ikafanyiwe marekebisho na kisha irejeshwe mahakamani hapa ndani ya siku 14 kuanzia leo”alisema Jaji Msuya.

Aidha Jaji Msuya alimtaka Ng’umbi aakikishe hati mpya atakayokuwa ameifanyia marekebisho aakishe anaifafanua kwa mapana tuhuma anayodai kuwa Tume ya Uchaguzi(NEC) ilishindwa kutimiza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kuwa akikishe analeta ufafanuzi kuhusu tuhuma alizomtuhumu Mnyika kuwa alitumia mikutano yake ya kampeni kumchafua kuwa yeye ni fisadi kwani aliuza nyumba za Jumuiya ya Umoja wa Wanawake(UWT).

Hata hivyo Jaji Msuya alimwamuru Ng’umbi awasilishe hati mpya iliyofanyiwa marekebisho mahakamani hapo Oktoba 11 , na wadaiwa wajibu Oktoba 25 na kesi hiyo itakuja kwaajili ya kutajwa Novemba mosi mwaka huu.
Agosti mwaka huu, wakili wa Mbogoro aliwasilisha mapingamizi yake yanayotaka mahakama hiyo iifute hati hiyo kwasababu katika marekebisho ya hati hiyo, mlalamikaji ameendelea kujitoa malalamiko ya jumla yenye utata, yasiyojibika na yenye mkanganyiko kisheria hali inayofanya mdaiwa hawezi kujitetea dhidi ya madai yanayomkabili.

Miongoni mwa madai katika kesi ya msingi ,Ng’umbi aliyoifungua Novemba mwaka jana,anadai Mnyika na au wasaidizi na mashabiki wake walifanya vitendo ambavyo ni ukiukwaji wa sheria kwa makusudi kwa madhumuni ya kushinda uchaguzi na kwamba kaisis wa Kanisa Katoliki Saranga Oktoba 3 mwaka jana aliwashawishi wahumini kupigia kura Mnyika na kuwataka wasipigie kura CCM kwa kuwa ni chama cha Mafisadi na Jaji Msuya alifuta dai hilo kwasababu haliwataji kwa majina viongozi wa makanisa hayo.

Na kwamba Mnyika mara kadhaa alitumia barua ya TANROADS, ya Machi 30 mwaka 2010 iliyotumwa kwa CCM kuwadanganya wakazi wa Kimara kwamba nyumba zao zitabolewa kama watamchagua Ng’umbi na kwamba Mnyika aliwanunulia pombe na kuwalipa sh 20,000 wananchi wa Kimara Saranga hili wampigie kura.

Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Septemba 28 mwaka 2011.

AMATUS LIYUMBA ATOKA GEREZANI

Na Happiness Katabazi
HATIMAYE aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba (63) ametoka jela katika gereza la Ukonga jijini Dar es Salaam , alikokuwa akiishi baada ya kumaliza kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka miwili gerezani.


Kwa mujibu wa taarifa za kuaminika toka ndani ya familia ya Liyumba, zililiambia Tanzania Daima jana kuwa Liyumba alitoka gerezani hapo jana saa 3:30 asubuhi bila ya kuwepo kwa vikwazo vyovyote.

Vyanzo hivyo ambavyo havikutaka kutaja majina yao gazetini kwa madai kuwa wao siyo wasemaji wa familia Liyumba, vilisema kuwa ndugu zake wachache walifika saa mbili asubuhi katika gereza la Ukonga kwaajili ya kumchukua ndugu yao na ilipofika saa 3:30 asubuhi, uongozi wa Gereza la Ukonga ulimruhusu Liyumba kutoka gerezani hapo baada ya mfungwa huyo na uongozi huo wa gereza kukamilisha taratibu zote za kumuachilia huru mfungwa anayekuwa amemaliza muda wake wa kutumikia kifungo na wakafanikiwa kuondoka naye.

“Tunamshukuru mungu ndugu yetu Liyumba leo katoka gerezani baada ya kumaliza kutumikia kifungo cha miaka miwili jela na hivi tunayofuraha kwani amerudi uraiani kurejea na familia yake…kwakweli tunafuraha na yote yaliyompata ndugu yetu tunamwachia mungu”kilisema chanzo hicho.

Hata hivyo juhudi za gazeti hili za kumpata Liyumba ili azungumzie kumalizika kwa adhabu yake, zilishindikana kufuatia ndugu zake wa karibu kueleza kuwa hivi sasa ndugu yao hayupo tayari kuzungumza na vyombo vya habari kwani anaitaji kupumzika pamoja na familia yake.

Septemba 8 mwaka huu, Liyumba anayetetewa na mawakili wa kujitegemea Hudson Ndusyepo na Onesmo Kyauke alifikishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Stewart Sanga akikabiliwa na kesi mpya ya kukutwa simu gerezani hata hivyo alipata dhamana baada ya kujidhamini kwa bondi ya Sh 50,000. Na wakili wa Serikali Elizabeth Kaganda alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo mpya umekamilika na kwamba Septemba 29 mwaka huu, watakuja kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa huyo.

Desemba mwaka jana , Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Emilian Mushi alitupilia mbali rufaa iliyokatwa na Liyumba iliyokuwa ikiiipinga hukumu ya Mahakama ya Kisutu iliyomuhukumu kwenda jela miaka miwili baada ya kumtia hatiani kwa kosa moja la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma ambapo jaji huyo alisema akubaliana na hukumu ya Kisutu kwani ilikuwa sahihi kisheria.

Mei 23 mwaka 2010, Mahakimu wawili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa walitoa hukumu ya kumtia hatiani Liyumba kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma, na hakimu mkazi mmoja Edson Mkasimongwa ambaye ndiye aliyekuwa akiliongoza jopo hilo kusikiliza kesi hiyo alitofautiana na mahakimu hao wawili na akatoa hukumu ya peke yake ambayo ilimwachiria huru mshtakiwa huyo.

Lakini hata hivyo hukumu iliyotolewa na mahakimu hao wawili ndiyo ilibaki kuwa ni hukumu ya mahakama ya Kisutu na hukumu ya Hakimu Mkasimongwa ikabaki kwenye kumbukumbu za mahakama na haikutumika kwaajili ya kumpatia adhabu Liyumba

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Septemba 24 mwaka 2011.

JAJI AKWAMISHA UAMUZI KESI YA MBATI VS MDEE

Na Happiness Katabazi
JAJI wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam John Utamwa , jana ilishindwa kutoa uamuzi wa ama hati ya madai katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 iliyofunguliwa na aliyekuwa Mgombea Ubunge(NCCR-Mageuzi) dhidi ya mbunge Jimbo hilo Halima Mdee(Chadema) ifanyiwe marekebisho au la kwa maelezo kuwa bado hajakamilisha kuandaa uamuzi huo.


Wakili wa Mbatia, Mohamed Tibanyendera aliikumbusha mahakama hiyo kuwa jana kesi hiyo ilikuja kwaajili ya mahakama kutoa uamuzi huo na kwamba pande zote mbili zipo tayari kwaajili ya kupokea uamuzi huo.

Hata hivyo kwa upande wake Jaji Utamwa alisema hataweza kutoa uamuzi huo jana kwasababu bado hajamaliza kuandaa uamuzi huo hivyo akaiarisha kesi hiyo ya uchaguzi hadi Septemba 29 mwaka huu, ambapo atakuja kuitolea uamuzi.

Hatua hiyo ya mahakama kutaka kutoa uamuzi kuhusu hati hiyo ya madai, kunafuatia pingamizi lilowasilishwa na wakili wa Mdee, Edson Mbogoro la kuiomba mahakama hiyo imwamuru mlalamikaji aifanyie marekebisho hati yake ya madai na kuyaondoa baadhi ya madai ambayo Mbatia anadai kuwa katika mikutano ya kampeni Mdee alimwita yeye kuwa ni Fataki anayefanya mapenzi na watoto wa shule, kibaraka wa CCM na kila wiki analipwa sh milioni 80 na CCM hivyo kuwataka wapiga kura wa jimbo la Kawe wasimchague Mbatia.

Mdee anadai tuhuma hizo zilizoelekezwa kwake na Mbatia ndani ya hati hiyo ya madai zinamletea kinamkera na hataweza kuziandalia utetetezi na kusisitiza kwa kuomba mahakama hiyo imwamuru Mbatia aondee hizo tuhuma kwenye hiyo hati ya madai.

Novemba 25 mwaka 2010 Mbatia alifungua kesi ya kupinga matokeo ya ubunge wa jimbo hilo ambayo yalimtangaza Halima Mdee(CHADEMA) kuwa ndiye aliyeshinda na ataliongoza jimbo hilo kwa kipindi cha miaka mitano.

Chanzo:Chazeti la Tanzania Daima la Septemba 22 mwaka 2011.

HATI YA KESI YA NG'UMBI INA MAKOSA

Na Happiness Katabazi
ALIYEKUWA mgombea ubunge wa Jimbo la Ubunge(CCM), Hawa Ng’umbi ambaye ni ndiye mlalamikaji katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 yaliyomtangaza John Mnyika kuwa mbunge wa jimbo hilo, amekiri kuwa hati yake ya madai aliyoifanyia marekebisho ina makosa ya kisheria na anaiomba mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imruhusu aende kuifanyia marekebisho.


Ng’umbi aliyasema hayo kupitia majimbu yake yaliyowasilishwa kwaniaba yake na wakili wake Issa Maige kwa Jaji Upendo Msuya ambapo alidai anakubaliana na baadhi ya mapingamizi aliyowekewa na Mnyika yanayotaka hati hiyo ifutwe kwasababu ina makosa ya kisheria yanayosababisha wadaiwa ambao ni Mnyika, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo washindwe kuandaa utetezi wao.

Hati hiyo ya madai iliyofanyiwa marekebisho na Ng’umbi iliwasilishwa mahakamani hapo kufuatia amri ya Jaji Msuya aliyoitoa Julai 18 mwaka huu, ya kuleta mabadiliko hayo baada ya lalamiko la mlalamikaji la awali kupingwa na Mnyika.

Baada ya kuwasilishwa kwa hati hiyo iliyofanyiwa marekebisho, Mnyika anayetetewa na wakili Edson Mbogoro naye aliwasilishwa mapingamizi yake yanayotaka mahakama hiyo iifute hati hiyo kwasababu katika marekebisho ya hati hiyo, mlalamikaji ameendelea kujitoa malalamiko ya jumla yenye utata, yasiyojibika na yenye mkanganyiko kisheria hali inayofanya mdaiwa hawezi kujitetea dhidi ya madai yanayomkabili.

“Katika hati yake ya madai, mlalamikiaji anadai hukiukukwaji wa sheria, Kanuni na taratibu za uchaguzi ulifanywa na mimi wakati wa kampeni za uchaguzi ,pamoja na mambo mengine …kwa makosa hayo makubwa ya kisheria ambayo ni mdaiwa mwenyewe amekiri kuwa hati yake inadosari tunaomba mahakama hii itoea amri ya kuifuta hati hiyo ili mahakama iendelee na taratibu nyingine”alidai Mnyika.

Miongoni mwa madai katika kesi ya msingi ,Ng’umbi aliyoifungua Novemba mwaka jana,anadai Mnyika na au wasaidizi na mashabiki wake walifanya vitendo ambavyo ni ukiukwaji wa sheria kwa makusudi kwa madhumuni ya kushinda uchaguzi na kwamba kaisis wa Kanisa Katoliki Saranga Oktoba 3 mwaka jana aliwashawishi wahumini kupigia kura Mnyikka na kuwataka wasipigie kura CCM kwa kuwa ni chama cha Mafisadi.

Na kwamba Mnyika mara kadhaa alitumia barua ya TANROADS, ya Machi 30 mwaka 2010 iliyotumwa kwa CCM kuwadanganya wakazi wa KImara kwamba nyumba zao zitabolewa kama watamchagua Ng’umbi na kwamba Mnyika aliwanunulia pombe na kuwalipa sh 20,000 wananchi wa Kimara Saranga hili wampigie kura.
Hata hivyo Jaji Msuya alisema uamuzi wa maombi hayo atautoa Septemba 27 mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Septemba 21 mwaka 2011.

KESI YA 'HASSANOO' YAPIGWA KALENDA

Na Happiness Katabazi
KESI ya kula njama na kuiba tani 26 za Shaba zenye thamani ya Sh milioni 400 mali ya kampuni ya Liberty Express Ltd ya Dar es Salaam inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha soka Mkoa wa Pwani (COREFA) Hassan Othman ‘Hassanoo’ na wenzake watatu,jana ilitajwa na kuairishwa mahakamani hapo.


Wakili wa Serikali Komanya mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa alieleza mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kwamba wanaomba iairishwe hadi tarehe nyingine ili siku hiyo waje kuona kama upelelezi umekamilika.

Ombi hilo lilikubaliwa na Hakimu Nongwa ambaye aliairisha hadi Oktoba 12 mwaka huu,ambapo mahakama itakuja kuona kama upelelezi wa shauri hilo kama umekamilika.

Septemba 2 mwaka huu, mawakili wa serikali Andrew Rugarabamu na Aneth Kaganda,walidai mbele mahakamani hapo kuwa Agosti 26, mwaka huu ,maeneo ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam, washitakiwa walikula njama na kuiba mali hiyo kwenye gari namba T 821 BCL iliyokuwa inasafirishwa kwenda Zambia.

Wakili Rugarabamu alidai katika kosa la nne, washitakiwa hao wanadaiwa kupokea tani hizo za shaba kinyume cha sheria huku wakijua wazi mali hiyo iliibwa
Mbali na Hassanor washtakiwa wengine ni Wambura Kisiroti (32), Najim Msenga (50) na Salim Shekibula (29) ambao wanatetewa na wakili wa kujitegemea Majura Magafu.

Chanz:Gazeti la Tanzania Daima la Septemba 21 mwaka 2011.

TANESCO MSIKATE UMEME MAHOSPITALINI


Na Happiness Katabazi
KWA TAKRIBANI miaka mitano sasa Watanzania waliobahatika kupata nishati ya umeme wamekuwa wakikabiliwa na ukosefu wa umeme wa uhakika.


Hali hiyo imekuwa ikisababisha baadhi ya watu kukosa ajira, uzalishaji viwandani kupungua, wagonjwa kupoteza maisha mahospitalini kwaajili ya ukosefu wa uhakika wa nishati hiyo na hata uchumi wa nchi yetu kusuasua kutokana nauzalishaji viwandani kupungua kutokana na ukosefu wa umeme.

Ijumaa iliyopita mwanangu Queen ‘Malkia’ (3) alilazwa kwa siku moja katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam, ambapo alililazwa kwa siku moja baada ya Daktari wa watoto Dk. Zubeda Kange na Dk. Saumu Mweli kumgundua anasumbuliwa na ugonjwa Tonsilite.

Kwanza nawashukuru madaktari na wauguzi wote wa wodi ya watoto katika Hospitali hiyo ya Jeshi Lugalo kwani walijitahidi kadri ya uwezo wao kuakikisha wanampatia huduma bora mwanangu na watoto wengine ambao walikuwa wamelazwa katika wodi hiyo.

Tangu asubuhi siku hiyo ndani ya hospitali hiyo kulikuwa na umeme lakini ilipofika saa 10-moja jioni umeme ulikatika hali iliyosababisha baadhi ya wananchi waliokuwa wakifika hospitalini hapo na kuonana na madaktari ambapo waliandikiwa vipo mbalimbali ili waende mahabahari kwaajili ya kupimwa na kugundulika na maradhi gani, lakini wagonjwa hao walipokuwa wakifika kwenye mahabara hiyo muda huo kwaajili ya kuchukuliwa vipimo.

Wataalamu wa mahabara walishindwa kuwachukua vipimo kwasababu ya umeme kukatika ndani ya hospitali hiyo.Kutokana na joto lilokuwa ndani ya wodi ya watato mimi na mwanangu tulitoka ndani ya wodi hiyo na kuketi kwenye viti ambavyo vimetazamana na mahabara hiyo na niliweza kuwashuhudia zaidi wananchi zaidi ya sita katika kipindi hicho wakifika katika mahabara hiyo kwaajili ya kuchukuliwa vipimo wakati umeme umekatika waliamua kwenda hospitali nyingine kupima na wengine waliamua kupima vipimo hapo na kuviacha mahabara ili umeme ukirudi muda usiofahamika warudi kuvichukua vipimo hivyo.

Hali hiyo ilinisikitisha sana licha halikuwa limeniathiri mimi binafsi.Kwani miongoni mwa watu hao waliokuwa wamefika katika kuchukuliwa vipimo walikuwa wanamaumivu makali katika mihili yao na walikuwa wakiitaji wapatiwe matibabu haraka lakini ndiyo ilikuwa haiwezekani kumpatia mgonjwa matibabu bila kujua amegunduliwa na vipimo vya mahabara kuwa anasumbuliwa na maradhi gani.

Niliishia kujiuuliza hivi kweli Shirika la Umeme(TANESCO) limeshindwa kabisa kuketi chini na kuorodhesha hospitali zote nchini kuwawekea ‘line’maalum ambazo zitafanya umeme katika hospitali hizo usikatike?

Kama ni Tanesco hii hii imeweza kutenganisha ‘line’ katika baadhi ya makazi watumishi wa Idara nyeti hayakatwi umeme, ni kwanini Tanesco hii inashindwa kuunganisha line maalum katika mahospitali yetu ili yasiwe yanakatiwa umeme?

Hivi Tanesco inajipendekeza nini kwa makazi hayo ya wafanyakazi wa idara nyeti za serikali kutowakatia umeme, halafu inaona fahari kukata umeme katika mahospitali ambayo wananchi wengine maskini tunaosumbuliwa na maradhi tunakwenda mahospitalini kwaajili ya kupata tiba halafu kisha tunajikuta tunakosa tiba kwa wakati eti kwasababu ya mgao wa umeme hadi mahospitalini?

Ikiwa ni mahospitali haya haya ya serikali kila kukicha yamekuwa yakikabiliwa na upungufu wa madawa, ufinyu wa vitanda vya kulazia wagonjwa, leo hii serikali hii kupitia Tanesco inaendelea kuzitumbukiza kwenye shimo hospitali hizo ambazo zinatumiwa na wananchi, kuziingiza kwenye mgao wa umeme ambao unasababisha hospitali hizo kuingia gharama ya kununua mafuta kila wakati kwaajili kuweka kwenye majenereta?

Mfano mzuri ni pale wodi ya wazazi ya Hospitali ya Mwananyamala, wanawake wanaosubiri kwenda chumba maalum kwaajili ya kujifungua wengine ujikuta wakilala chini kutokana na uhaba wa vitanda.Sasa katika hali kama hiyo ya msongamano ya wanawake wajawazito kulala chini, ongezea ukosefu wa umeme iwe mchana au usiku, hivi katika hali ya kawaida huyo mama mjazito anakuwa na hali gani ya kiafya?

Na mbaya zaidi Tanesco wakatapo umeme wala hawatoi taarifa kwamba dakika chache zijazo wanakata umeme, wanajikatia tu umeme wanavyojisikia wao na wakati wanakata kwa mtindo huo wa kutotoa taarifa mapema, kuna wananchi wenzetu wengine wanakuwa ndani ya vyumba vya upasuaji kwaajili ya kufanyiwa upasuaji na madaktari na wakati huo uenda majenereta ya baadhi ya mahospitali yanakuwa hayana mafuta, au yanahitilafu za ghafla hivyo uwezekano wa wananchi wenzetu kupoteza maisha wakiwa kwenye vyumba vya upasuaji kutokana na ukatikaji wa ovyo wa umeme ni mkubwa.

Imebidi tukubali kwamba Tanesco ndiyo mungu wa nishati ya umeme hapa Tanzania,kwani hadi sasa hajapatikana kiongozi mwenye maono na mwenye maamuzi ya kuweza kutupatia mbadala wa Tanesco ndiyo maana Tanesco inajiona ni mungu wa nishati ya Umeme.

Lakini katika hili la Tanesco kukata umeme katika mahospitali tunaomba likome mara moja, tunaamini wataalamu wale wale wa Tanesco waliweza kutenganisha line zinazokwenda kwenye makazi ya wafanyakazi wa idara nyeti za serikali ambazo hazikatwi umeme, pia ni wataalamu hao hao wanaweza sasa kutumia taaluma yao kutenganisha line zinazokwenda kwenye mahospitali ili umeme usiwe unakatika mahospitalini.

Kama Tanesco ipo kwaajili ya kulitumikia taifa hili bila ubagudhi wa makundi fulani, naamini wanaweza kuweka mpango mkakati wa kuakisha mahospitali yote hayakatiwi umeme, na hili linawezekana isipokuwa tu bado hatujapata viongozi wenye uchungu wa kwale wananchi wa taifa hili hasa wale wenye hali ya chini.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika
0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Septemba 16 mwaka 2011.

MASAWE,BENDERA WAPONGEZWA NA WADAU WA MICHEZO

Na Happiness Katabazi
CLUB ya Tanzania Youth Athletics yenye maskani yake Holili Mkoani Kilimanjaro imempongeza Mkuu mkoa wa Kagera Mteule, Kanali Mstaafu, Fabiani Masawe kwa kuteuliwa na Rais Jakaya Kikwete juzi kushika wadhifa huo.


Akizungumza na gazeti hilo kwa njia ya simu jana Mwenyekiti wa Club hiyo, Dominic Rwezaula na Nahodha wa timu Nelson Brighton alisema kwaniaba ya klabu yake ambayo imeanzishwa kwaajili ya kuinua vipaji vya riadha mkoa wa Kagera anampongeza Masawe ambaye awali alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Karagwe kwa kuteuliwa kwake juzi na Rais Kikwete kuwa mkuu wa Mkoa wa Kagera.

“Pongezi hizi zinatokana na Masawe mwenye kuwa ni mdau sana wa michezo na kuamini club ya riadha iliyoanzishwa itaendelezwa na kuibua vipaji vyavya riadha mkoa wa Kagera na tunaimani chini ya wadhifa wake mpya wa ukuu wa mkoa huo ,ataiendeleza michezo sambamba na kuwaunganisha wakazi wa mkoa huo kwaajili ya kujiletea maendeleo”alisema Rwezaula.

Wakati huo huo wadau mbalimbali wamepongeza hatua ya Rais Kikwete kumteua Joel Bendera kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwasababu Bendera naye ni mdau wa sekta ya michezo hapa nchini na waimani kuwa atakapokuwa Morogoro pia ataweza kukukuza michezo katika mikoa hiyo na kwamba wamefurahishwa kwa hatua hiyo ya rais Kikwete kuwateua wakuu wa mikoa ambao ni wadau wakubwa wa michezo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Septemba 16 mwaka 2011.

JAJI LYIMO AAGWA

Na Happiness Katabazi
JAJI Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Fakihi Jundu amesema kuwa mchango wa kitalaamu uliotolewa na Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Vicent Lyimo utabaki kuwa alama na kumbumbuku katika mhimili wa mahakama nchini.


Jundu aliyasema hayo jana wakati akiongoza sherehe za kitaaluma za kumuaga jaji Lyimo ambaye amestaafu kazi ya ujaji kwa mujibu wa Katiba Septemba 12 mwaka huu ambapo alisema mchango wake katika kuamua kesi mbalimbali alizoziamua na shughuli za kiutawala alizozifanya ,mhimili huo utaendelea kuziheshimu na kuzithamini.

“Jaji Lyimo leo mahakama kuu inakufanyia sherehe ya kitaaluma ya kukuaga baada ya wewe kutimiza umri wa kustaafu kwa mujibu wa Katiba ya nchini, hivyo kwaniaba ya Mahakama Kuu ya Tanzania napenda kuchukua fursa hii kukutakia afya na maisha mema wewe na familia yako katika maisha yako mapya ya kustaafu …na tunakukuakikishia kuwa yale yote mazuri uliyoyatenda katika ukiwa mtumishi wa umma tuyaenzi”alisema Jaji Kiongozi Jundu.

Kwa upande wake Jaji mstaafu Lyimo akisoma hotuba yake alianza kwakumshukuru Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mussa Kipenga ambapo alisema alipoteuliwa kuwa jaji alipangiwa kituo cha kazi cha Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba ambapo huko alikutana na Jaji Mussa Kipenga ambaye ndiye alikuwa Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo ambapo alisema ushirikiano mkubwa wa kikao na Jaji Mussa.

Jaji Lyimo alisema hadi amefikia muda wa kustaafu, ataendelea kumheshimu na kumshukuru Jaji Kipenka ambaye kwa sasa ndiye Jaji Mfawidhi Kanda ya Tanga na kuongeza kuwa utendaji kazi wake mzuri ulichangiwa kwa kiasi kikubwa na ushirikiano wa kikazi alioupata awali alipoteliwa kuwa jaji toka kwa Jaji Kipenda na familia yake.

Aidha alisema bado mhimili wa mahakama unakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo zinatakiwa zitatuliwe licha ya Tume ya Kurekebisha Sheria imekuwa ikifanyakazi nzuri ya kutoa misaada ya vitendea kazi, mafunzo kwa mahakama.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Septemba 15 mwaka 2011.

LIYUMBA ASHITAKIWA TENA


Na Happiness Katabazi
ALIEYUKUWA Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania, Amatus Liyumba (63), ambaye Septemba 23 mwaka huu anamaliza kutumikia adhabu ya kifungu cha miaka miwili jela, jana alijikuta akipandishwa tena katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kwa kesi mpya ya kukutwa na simu gerezani.


Hata hivyo baada ya kuingizwa mahakamani saa 7:20 na wakili wa serikali, Elizabeth Kaganda, kumsomea shtaka moja linalomkabili, mawakili wake, Majura Magafu na Hudson Ndusyepo, waliibuka na hoja ya kutaka mteja wao asijibu chochote baada ya kusomewa shtaka hilo kwa hati yenye dosari.

Hali hiyo, ilisababisha Hakimu Mkazi, Stewart Sanga, anayesikiliza kesi hiyo kukubaliana na mawakili wa utetezi na akalazimika kutoa amri ya kuutaka upande wa Jamhuri uende ukaifanyie marekebisho hati hiyo na kisha muda kidogo baadaye urudi mahakamani hapo ikiwa na hati mpya ambayo imefanyiwa marekebisho.

Wakili wa serikali, Kaganda, akimsomea shtaka Liyumba kwa kutumia hati yenye dosari, alidai anakabiliwa na kosa la kukutwa na kitu kilichokatazwa gerezani chini ya kifungu cha 86 cha Sheria ya Magereza kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Alidai kuwa Liyumba ambaye ni mfungwa mwenye namba 303/2010, Julai, mwaka huu, ndani ya gereza la Ukonga, alikamatwa na simu aina ya Nokia Na.1280 nyeusi iliyokuwa na laini yenye namba 0653- 004662 na IMEI Na. 356273/04/276170/3 ambayo alikuwa akiitumia kwa ajili ya kufanya mawasiliano binafsi wakati ni kinyume cha sheria.

Baada ya Kaganda kumaliza kusoma shtaka hilo, wakili Magafu aliinuka na kudai kuwa hawaoni sababu ya mteja wao kukana au kukubali shtaka hilo kwa sababu tayari hati ya mashtaka ina makosa.

Magafu alidai kwa mujibu wa kifungu cha 86 cha Sheria ya Magereza, kifungu hicho kina vifungu vidogo vitatu yaani kifungu cha 86 (1, 2, 3) na kwamba hawaelewi Jamhuri inamshtaki mteja wao kwa kifungu cha 86 (1, 2, 3) au kipi na kuongeza kuwa ili mshtakiwa aweze kujibu mashtaka yanayomkabili ni lazima mashtaka yaliyo kwenye hati ya mashtaka yaeleweke yamefunguliwa chini ya kifungu kipi na si kama hivi ilivyofanya Jamhuri kwenye kesi hii.

Hivyo aliiomba Jamhuri ikaifanyie marekebisho hati hiyo ili mteja wake aweze kujibu kuhusu shtaka analoshtakiwa.

Akijibu hoja hiyo wakili wa serikali, Kaganda, alikiri kuwa ni kweli hati ya mashtaka inamshtaki kwa kifungu cha 86 cha Sheria ya Magereza lakini wanamaanisha kuwa anashtakiwa kwa kifungu cha 86 (1, 2, 3) cha Sheria ya Magereza na kuiomba hati hiyo ya mashtaka isomeke kuwa anashtakiwa chini ya kifungu hicho na vifungu vyote vidogo vilivyopo ndani ya kifungu hicho.

Hoja hiyo ilimlazimu tena wakili Magafu kudai kuwa wanasikitishwa na hoja hiyo ya Jamhuri kwani kifungu cha 86 (2) cha sheria kinatoa maana ya vitu vinavyokatazwa gerezani lakini hakiundi kosa.

Na pia kifungu cha 86 (3) kinataja vitu vilivyokatazwa gerezani na kinatoa mamlaka kwa Jeshi la Magereza kutaifisha kitu walichokikamata ndani ya gereza ambacho kimekatazwa na sheria hiyo.

“Tulitegemea tuusaidie upande wa Jamhuri kuweka vizuri hati yao ya mashtaka lakini ndiyo kwanza wanaenda njia potofu…sasa sisi tunasema haya mashtaka yameletwa kimakosa hapa mahakamani na mteja wetu hapaswi kujibu chochote hivyo tunaomba hati hiyo itupwe ili Jamhuri iende ikaifanyie marekebisho; mahakama hii ina mamlaka ya kuifuta hati hiyo au kuiamuru Jamhuri iende ikaifanyie marekebisho,” alidai Magafu.

Kufuatia malumbano hayo, Hakimu Sanga alisoma kifungu cha 86 cha Sheria ya Magereza, mstari kwa mstari, hivyo kukubaliana na hoja za wakili wa utetezi Magafu kuwa hati hiyo ina makosa na hivyo akauamuru upande wa Jamhuri uiondoe hati hiyo na iende ikaifanyiwe marekebisho na baada ya muda mfupi iletwe hati iliyofanyiwa marekebisho mahakamani hapo na kumsomea upya mashtaka mshtakiwa huyo.

Upande wa Jamhuri ulitii amri hiyo na ilipofika saa 8:22 mchana, Wakili Kaganda alirejea na kuiambia mahakama kuwa tayari ameishaifanyia marekebisho hati hiyo na kwamba hivi sasa itasomeka kuwa Liyumba anashtakiwa chini ya Kifungu cha 86 (1,2) cha sheria hiyo, ambapo mshtakiwa alikana shtaka huku wakili wa serikali akidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Wakili Magafu alidai kuwa kifungu cha 148 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 hakiikatazi mahakama kutoa dhamana kwa mfungwa anayekabiliwa na kesi mpya.

Aliongeza kuwa kwa vile Septemba 23, mteja wao anamaliza kutumikia adhabu yake gerezani na kwamba kosa linalomkabili hivi sasa lina dhamana, wanaiomba mahakama impatie dhamana, ombi ambalo halikupingwa na wakili wa serikali.

Hakimu Sanga alikubaliana na ombi hilo ambapo alisema ili mshtakiwa huyo apate dhamana, atatakiwa asaini bondi ya sh 50,000 na awe na mdhamini mmoja wa kuaminika.

Liyumba alitimiza mashtari hayo na kupatiwa dhamana kwa kesi hiyo lakini hata hivyo alirudi gerezani kwa ajili ya kutumia adhabu ya kesi ya matumuzi mabaya ya madaraka aliyohukumiwa nayo.

Hakimu aliahirisha kesi hiyo mpya hadi Septemba 29, mwaka huu, ambapo itakuja kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Mei 24 mwaka jana, Mahakama ya Hakimu Mkazi ilimtia hatiani kwa kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kumhukumu kwenda jela miaka miwili lakini hata hivyo, Liyumba hakuridhika na hukumu hiyo akakata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Mbele ya Jaji Mushi, Desemba mwaka jana alitupilia mbali rufaa ya Liyumba kwa maelezo kuwa hukumu ya Mahakama ya Kisutu ilikuwa sahihi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Septemba 9 mwaka 2011.

DOWANS HAIKAMATIKI

*Mahakama yatupa maombi yawanaharakati

Na Happiness Katabazi
HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeyafukuza maombi ya wanaharakati waliokuwa wakiongozwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu(LHRC) ambao yaliyokuwa yakiomba mahakama hiyo ikatee kusajili tuzo iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa migogoro ya Kibiashara(ICC) kwa kampuni ya Dowans Holdings SA(Costa Rica) na na wenzake kwasababu wanaharakati hao hawana haki wala mamlaka ya kupinga hilo.


Sambamba na hilo, Jaji Emilian Mushi ambaye ndiye ametoa uamuzi huo wa kesi hiyo ya madai Na.8/2011iliyofunguliwa na LHRC, Chama cha Wanasheria wa Mazingira(LEAT),Kampuni ya Sikika Limited(SCL), na mwandishi wa habari Timothy Kahoho wanaotetewa na Dk.Sengondo Mvungi dhidi ya Dowans Tanzania,Dowans Holdings SA(costa rica) na Tanesco alisema uamuzi wa kusajiliwa au kutosajiliwa kwa tuzo ya Dowans ataitoa baadaye.

Jaji Mushi alianza kwa kuimbusha mahakama na kuwataka waandishi wa habari ufahamu kuwa uamuzi alioutoa jana ni mapingamizi ya awali yaliyowasilishwa na wakili wa wadaiwa Kennedy Fungamtama dhidi ya walalamikaji(Wanaharakati) na kwamba mahakama hiyo imefikia uamuzi wa kukubalina na mapingamizi ya wakili huyo kuwa walalamikaji hawana haki ya kisheria ya kufungua kesi ya kupinga tuzo hizo isisajiliwe kwa niaba ya Watanzania na kwamba wanaharakati hao wameshindwa kuonyesha ushahidi kuwa wao wanahaki,maslahi kwaniaba ya umma ya kufungua kesi kupinga tuzo hiyo isisajiliwe.

Jaji Mushi alisema pia anakubaliana na pingamizi la pili la wakili wa Dowans, Fungamtama kwamba walalamikaji hao hawakuwa wahusika kwenye kesi ya Dowans dhidi ya Tanesco iliyomalizika kwenye mahakama ya kimatiafa ya ICC hivyo kwakuwa hawakuwa wahusika katika kesi hiyo ni wazi hakuwa na mamlaka ya kufungua kesi ya kupinga utekelezaji wa hukumu ya ICC katika Mahakama Kuu ya Tanzania.

“Katiba na Sheria za maamuzi mbalimbali ya mahakama yapo wazi nayametamka wazi kuwa mashauri ya madai yanayohusu nchi mwenye dhamana ya ulinzi na kufungua kesi za aina hiyo ni ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hivyo natupilia mbali ombi la wanaharakati hao ambao walidai kuwa wao ni watanzania wanahaki na wajibu wa kulinda mali za watanzania ndiyo maana wakafungua kesi hii ya kutaka Tuzo ya dowans isisajili, nalitupilia mbali ombi lao;

“Pia natupilia mbali maombi ya waombaji ‘wanaharakati’ kwasababu hayo maombi ya uwakilishi yakufungua kesi hiyo yameambatanishwa na mwenendo wa kesi iliyotolewa hukumu na mahakama ya kimataifa (ICC) na kwakushindwa kwao kafanya hivyo wakati Amri 1 Kanuni ya (8) ya Sheria ya Madai ya mwaka 2002 inawalazimisha wafanye hivyo, mahakama hii kwa mara nyingine inakubalina na pingamizi la wakili wa Dowans kuwa maombi hayo ya wanaharakati yanadosari ya kisheria na hivyo nayafukuza katika mahakama hii kwa gharama”alisema Jaji Mushi.

Sekunde chache baada ya Jaji Mushi kumaliza kusoma uamuzi wake mwombaji wa nne, Kahoho aliamka kwenye kiti alichoketi na kusema kuwa hajaridhishwa na uamuzi huo na kwamba atakarufaa katika Mahakama ya Rufaa na alipomaliza kusema maneno hayo jaji Mushi naye alimjibu maneno yafuatayo;

“Eeeh! Kahoho ni haki yako kusema hayo uliyoyasema naniaamini ukienda Mahakama ya Rufaa huko kuna wazee wazee ‘majaji’ watakusikiliza…lakini nataka utambue kuwa hata ukienda kukata rufaa hata sasa katika mahakama hiyo ya juu nchini, uamuzi wako huo hautanizuia mimi kutoa hukumu ya kesi ya Dowans dhidi ya Tanesco ambayo Dowans iliwasilishwa ombi lake hapa Mahakama Kuu lakuomba mahakama hii iisajili tuzo waliyopewa na mahakama ya ICC ”alisema Jaji Mushi na kusababisha watu kuangua vicheko mahakamani hapo.

Januari 25 mwaka huu, Dowans iliwasilisha ombi lake lakutaka Mahakama Kuu ya Tanzania iisajili tuzo waliyopewa na Mahakama ya ICC na siku chache baadaye wanaharakati hao wakawasilisha maombi ya kutaka tuzo hiyo isajiliwe kwasababu ni batili na ikisajiliwa Tanesco ambalo ni shirika la umma litajikuta likipoteza fedha nyingi kuilipa fidia ya bilioni 94 kampuni hiyo ya Dowans.

Mahakama ya ICC, ilitoa hukumu ya kesi ya Dowans dhidi ya Tanesco, Novemba 15 mwaka jana, ambapo mahakama ilitia hatiani Tanesco kwa kosa la kuvunja mkataba na Dowans na ikaimuru iilipe fidia ya shilingi bilioni 94.

Hukumu hiyo ya ICC, muda mfupi baada ya kutolewa ilizusha malumbano makali baina ya wananchi, wanaisiasa na kusababisha baadhi ya mawaziri na mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa kauli zinazopisha huku wachache wakitaka serikali iilipe Dowans huku wengine wakisema kulipwa fidia kampuni hiyo ni ufisadi.

Malumbano hayo ya nje ya mahakama yalisababisha pia Chama cha Mapinduzi(CCM), kuunda Kamati ya Wabunge kujadili hukumu hiyo na kisha wabunge watatu wa chama hicho Mbunge wa Kibakwe(CCM)George Simbachawe na Mbunge wa Karagwe(CCM), Gosbert Blandes na mbunge wa Viti Maalum,Angellah Kairuki na raia wengine wa nne kufungua kesi ya Kikatiba Na.5/2011 dhidi ya Waziri wa Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tanasco ambayo imeanza kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Njegafibili Mwaikugile, Agustine Shangwa na Projest Rugazia

Kwa mujibu wa hati ya madai ya walalamikaji hao wanaiomba mahakama itoe amri ya kuizuia serikali isiilipe kampuni ya Dowans na endapo malipo hayo yatafanywa kwa kampuni hiyo ni wazi wadaiwa hao ambao wanaiwakilisha serikali kwa ujumla watakiwa wamevunja ibara 26(2),27(1) na 27 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambazo mahakama hiyo ina wajibu wa kuilinda ibara hizo zisivunjwe.\

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Septemba 7 mwaka 2011.

MTIKILA AFUNGUA KESI KUZUIA MAHAKAMA YA RUFAA ISIUZWE

Na Happiness Katabazi

MWENYEKITI wa Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, amefungua kesi ya Kikatiba katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam jana, akiitaka izuie kuuzwa kwa jengo la Mahakama ya Rufaa lililopo eneo la Kivukoni Front, kwa mmiliki wa Hoteli ya Kempinski.


Kwa mujibu wa hati ya madai ambayo tayari imeshapewa namba 23 ya mwaka huu, Mtikila anamshtaki Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Katiba na Sheria na Jaji Mkuu wa Tanzania kwa kuruhusu jengo hilo la mahakama ya juu nchini liuzwe.

Mtikila amefungua kesi hiyo chini ya ibara ya 27(1) ya Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inayosomeka: “Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.”

Anadai kuwa amefikia uamuzi wa kuwashtaki walalamikaji hao kwa sababu wadaiwa hao wana dhamana ya kulinda mali za umma zisifujwe lakini cha kushangaza ndiyo wamekuwa mstari wa mbele kwa kushindwa kulinda jengo hilo ambalo ni mali ya umma na matokeo yake wameshiriki kuharibu mali hiyo ambayo ni jengo la kihistoria.

Hatua hiyo ya Mtikila kufungua kesi, imekuja ikiwa ni siku chache toka Waziri wa Katika na Sheria, Celina Kombani, kuueleza umma kuwa taratibu za kisheria zimefuatwa za kuliuza jengo hilo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Septemba 9 mwaka 2011.

SHAHIDI KESI YA MTIKILA AISHANGAZA MAHAKAMA

Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa pili wa upande wa Jamhuri katika kesi ya kumkashfu Rais Jakaya Kikwete kuwa anakumbatia waislamu inayomkabili Mchungaji Christopher Mtikila, Daniel Kikunile(34) ameshindwa kumtambua mshtakiwa huyo ambaye alikuwepo mahakamani hapo wakati kesi hiyo inayomkabili ikiendelea jana.


Kikunile ambaye ni Mchungaji wa Kanisa Groly Of Christ Tanzania mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo alikuwa akiongozwa na wakili wa serikali Elizabeth Kaganda kutoa ushahidi wake ambapo alieleza kuwa Mwishoni mwa Machi 2010 asubuhi alikuwepo ndani ya kanisa hilo na alikuja mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Mchungaji Mtikila(mshtakiwa) na kumuulizia Mchungaji Kiongozi wa kanisa hilo Joseph Gwajima kama yupo.

Yafuatayo ni mahojiano kati ya Wakili wa Serikali Kaganda na shahidi:
Swali:Huyo mtu aitwaye Mtikila aliyekuja siku hiyo kanisani kwako na kukukuta unaweza kumtambua hapa mahakamani?
Jibu: Mtu huyo aitwaye Mtikila hayupo hapa mahakamani.(Watu wakaangua kicheko kwasababu Mtikila alikuwepo mahakamani.
Swali:Huyo mtu alikupatia ujumbe gani siku hiyo kanisani?
Jibu:Alinipatia barua ambayo alinitaka nimpatie Gwajima pindi atakaporudi na Gwajima aliporudi kanisani hapo nilimpatia barua hiyo na wala sikuwa nafahamu kilichokuwa kimeandikwa kwenye ile barua kisha nikaondoka kwenda kuendelea na kazi zangu.Na baada ya siku chache walikuja wageni wawili kanisani hapo na wakakutana na Gwajima na Gwajima akaniita na kunitambulisha kwa wale wageni kuwa mapolisi na kwamba wamefika pale kwasababu ya ile barua ya niliyokadhiwa na Mtikila ambayo Gwajima alikuja kunieleza kuwa ule ulikuwa ni Waraka wa kumkashfu Rais Kikwete kuwa anakumbatia waislamu hivyo wakristo waungane wamuweke mkristo Ikulu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Kwa upande wake Mtikila ambaye hana wakili aliambia mahakama kuwa hawezi kumhoji zaidi shahidi kwasababu tayari shahidi huyo wa Jamhuri ameshindwa kumtambua. Hakimu Fimbo akaiarisha kesi hiyo hadi Oktoba 3 mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Septemba 8 mwaka 2011.

MWENENDO KESI YA MRAMBA WAKAMILIKA

Na Happiness Katabazi
HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imesema kuwa mwenendo wa kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilinioni 11.7 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake umeishachapwa na hivi sasa unafanyiwa uhakiki na jopo la mahakimu wanaoisikiliza.


Hayo yalisemwa jana na Hakimu Mkazi Frank Moshi wakati kesi hiyo ilipokuja jana kwaajili ya kutajwa na kuangalia kama mwenendo huo wa kesi umeishakamilika ili pande zote katika kesi hizo uwe kupatiwa kwaajili ya kwenda kujiaanda na majumuisho ya kuwaona washtakiwa wanakesi ya kujibu au la.

Hakimu Moshi alisema taarifa alizopewa ni kwamba tayari mwenendo huo umeishachapwa na kwamba kinachofanywa na mahakimu wanaosikiliza kesi hiyo ni kuuhakiki mwenendo huo na kusema kuwa anaairisha kesi hiyo hadi Oktoba 5 mwaka huu, ambapo siku hiyo uhakiki utakuwa umeishakamilika nakala za mwenendo huo wa kesi utatolewa kwa pande zote.

Mbali na Mramba washtakiwa wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona na Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonjwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania la Jumanne, Septemba 6 mwaka 2011.

KESI YA MAHALU YAPIGWA KALENDA

Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilishindwa kuendelea kusikiliza kesi ya uhujumu wa uchumi wa Euro zaidi ya milioni mbili inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na Grace Martin kwasababu wakili wa washtakiwa hao Mabere Marando amefiwa na ndugu yake.


Kesi hiyo ambayo ilikuja jana kwaajili ya Profesa Mahalu kuendelea kujitetea lakini Kiongozi wa jopo la mawakili wa Mahalu, Marando mbele ya Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi Elvin Mugeta aliomba mahakama hiyo jana iairishe usikilizwaji wa kesi hiyo kwasababu amefiwa na ndugu yake na kwamba yeye ndiyo kiongozi wa msiba huyo.

Ombi hilo lilikubaliwa na Hakimu Mugeta na wakili wa serikali Ponsian Lukosi ambapo hakimu huyo aliairisha kesi hiyo hadi Septemba 26 ambapo kesi hiyo itakuja kwaajili ya kutajwa na Oktoba 18,19 na 20 mwaka huu, kesi hiyo itakuja kwaajili ya kuendelea kusikilizwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Agosti 27 mwaka 2011.