MDEE AKWAA KISIKI KORTINI

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali pingamizi lilowekwa na Mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA),Halima Mdee lililokuwa likitaka hati ya madai katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu mwaka 2010 iliyofunguliwa na aliyekuwa Mgombea Ubunge kwa tiketi ya (NCCR-Mageuzi), James Mbatia ifanyiwe marekebisho kwa maelezo kuwa haina msingi wa kisheria.


Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji John Utamwa ambaye baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili alifikia uamuzi wa kukubaliana na hoja za wakili wa mlalamikaji, Mohamedi Tibanyendela aliyetaka pingamizi hilo litupwe na mahakama.

Jaji Utamwa alisema kwa mujibu wa hati ya madai, mlalamikaji ameeleza malalamiko yake yote kwa mapana dhidi ya mdaiwa na maelezo hayo yanajitosheleza kumfanya mdaiwa kujibu tuhuma hizo zilizoelekezwa kwake.

“Hivyo mahakama hii haikubaliani na pingamizi la mdaiwa anayetetewa na Wakili Edson Mbogoro anayetaka hati ya madai ifanyiwe marekebisho kwa vile hawezi kujibu baadhi ya tuhuma alizotuhumiwa nazo kwasababu zinamkera, kumtia kichefuchefu…..kwa hiyo mahakama hii leo inasema tuhuma hizo hazikeri wala kutia kichefuchefu hivyo ina muamuru mdaiwa kuzijibu na inatupilia mbali pingamizi la mdaiwa”alisema Jaji Utamwa.

Jaji Utamwa aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba Mosi mwaka huu, ambapo kesi hiyo itakuja kwa ajili ya kutajwa na kuangalia muda wa jinsi ya kuendelea nayo kwani Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010 inataka kesi za uchaguzi zimalizike ndani ya mwaka mmoja tangu zilipofunguliwa. Kesi hiyo ilifunguliwa Novemba mwaka 2010.

Uamuzi huo unatokana na pingamizi lilowasilishwa na wakili wa Mdee, Mbogoro la kuiomba mahakama hiyo imwamuru mlalamikaji aifanyie marekebisho hati yake ya madai na kuyaondoa baadhi ya madai ambayo Novemba 25 mwaka 2010 Mbatia alifungua kesi ya kupinga matokeo ya ubunge wa jimbo hilo ambayo yalimtangaza Halima Mdee(CHADEMA) kuwa mshindi.

Mbatia anadai kuwa katika mikutano ya kampeni, Mdee alimwita yeye kuwa ni fataki anayefanya mapenzi na watoto wa shule, kibaraka wa CCM na kila wiki analipwa sh milioni 80 na chama hicho, hivyo kuwataka wapiga kura wa jimbo la Kawe wasimchague Mbatia.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Oktoba 29 mwaka 2011.

KESI YA JEETU PATEL DHIDI YA MENGI YATUPWA



Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeifuta kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na mfanyabiashara Jayantkumar Chandubai ‘Jeetu Patel’ na wenzake watatu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi na Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP) kwa maelezo kuwa kesi hiyo haina mantiki ya kisheria na Kikatiba.


Uamuzi huo wa kesi hiyo Na. 30/2009 ulitolewa jana asubuhi na jopo la majaji watatu Jaji Kiongozi wa Fakihi Jundu, Semistocles Kaijage na Profesa Ibrahim Juma ambao walisema licha wanaifuta kesi hiyo kwa sababu haina mantiki ya kisheria, pia walisema madai ya Patel kuhusu tamko la Mengi alilolitoa Aprili 23 mwaka 2009 kwa vyombo vya habari kuwa yaliingilia uhuru wa Mahakama Mkazi Kisutu na kuidharau mahakama hiyo kwa kuwa hukumu walalamikaji ambao wanakabiliwa na kesi nne za EPA kupitia vyombo vya habari kuwa ni ‘Mafisadi Papa’ yalipaswa yapelekwe katika mahakama hiyo ya chini kwani mahakama za chini zimepewa nguvu za kuwaadhibu wale wote wanaotenda makosa ya kuidharau mahakama na endapo uamuzi wa mahakama hiyo ya chini asingelidhika nao ndiyo Jeetu Patel angekatia rufaa uamuzi huo wa mahakama ya Kisutu katika Mahakama Kuu.

Mdaiwa wa kwanza(AG) na wa tatu walikuwa wanatetewa na Wakili Kiongozi wa Serikali Stanslaus Boniface na mdaiwa wa pili(Mengi) alikuwa anatetewa na Michael Ngaro.
Jaji Jundu alisema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, jopo hilo lilijiuliza kwa mujibu wa Sheria ya Utekelezaji ya mwaka 2002 (Basic Rights and Eforcement Act,Cap 3; 2002) inayo mamlaka ya kutengua Ibara ya 59(B) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kuzifuta kesi nne za jinai zinazowakabili washtakiwa katika Mahakama ya Kisutu ambazo zimefunguliwa na DPP kwa kutumia Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 kwasababu kesi iliyokuwa mbele yao ni kesi ya Kikatiba.

“Jibu tulilolipata baada ya kujiuliza swali hilo ni kwamba jopo hilo lilikuwa halina mamlaka ya kutengua ibara hiyo ya 59(B) ya Katiba ambayo inataja majukumu ya DPP na haiwezi kuzifuta kesi hizo zilizopo mahakama ya Kisutu na hivyo imekubaliana na hoja ya wakili wa Mengi(Ngaro) kuwa Mengi ni mtu binafsi na hivyo hana mamlaka ya Kikatiba wa kisheria wa kuimwelekeza DPP wala mahakama kuzifuta kesi hizo zinazowakabili walalamikaji katika kesi hiyo ya Kikatiba.

“Hivyo jopo hili linakubaliana na hoja za mawakili wa utetezi kuwa Mengi ni mtu binafsi hakupaswa kuunganishwa kwenye kesi hiyo kwasababu Mengi siyo taasisi na hana nguvu za kisheria wala Katiba za kuingilia kazi za DPP wala mahakama”alisema Jaji Jundu.

Jaji Jundu alisema madai ya Jeetu Patel dhidi ya Mengi hayakupaswa kuangukia kwenye kesi hiyo ya Kikatiba bali walalamikaji kama waliona Mengi amewakosea walitakiwa kumshtaki kwa kutumia sheria ya Madai au ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 kuwa alitoa matamshi ya kuwakashfu au kuidhara mahakama kwa kutoa maneno yanayowahukumu kabla ya mahakama ya Kisutu kutolea hukumu kesi nne za EPA zinazowakabili.

Awali katika mapingamizi ya awali yaliyotolewa na mawakili wa utetezi Michael Ngaro na Stanslaus Boniface, wakili Boniface aliomba mahakama hiyo iifute kesi hiyo kwasababu viapo vilivyoapwa na walalamikaji wakati wanafungua kesi hiyo ni batili na havina hadhi ya kisheria. Huku wakili Ngaro aliomba jina la Mengi liondolewe kwenye hati ya madai au likibaki basi kesi ifutwe kwasababu Mengi hakupaswa kushtakiwa binafsi.

Aidha pingamizi la pili, mawakili hao walidai kesi hiyo ilikuwa ni kesi ya Kikatiba kwa hiyo mahakama hiyo ya Kikatiba haitakuwa na mamlaka ya kupokea,kujadili wa kutolea maamuzi mgogoro wowote unaoangukia kwenye Sheria ya madai wala jiani badala yake itabakia kuwa na mamlaka ya kujadili, kusikiliza na kutolea maamuzi mgogoro wa Kikatiba peke yake.

Aidha katika madai ya msingi ya Jeetu Patel alidai Mengi amemvunjia haki yake ya Kikatiba ya ambayo Katiba inakata mtu asichukuliwe na hatia hadi pale mahakama itakapomtia hatiani na kwamba AG na DPP wameshindwa kumchukulia hatua za kisheria Mengi kwa kitendo chake cha kuingilia uhuru wa mahakama bila kumshtaki.

Novemba 2008,Jeetu Patel na wadaiwa wenzake Davendra Vinodbhai Patel,Amit Nandy na Ketan Chohan walifikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi nne za wizi katika akaunti ya Madeni ya Nje(EPA). Kesi hizo ni kesi Na. 1153,1154,1155 na 1157 za mwaka 2008.

Julai mwaka 2009 mawakili wa Patel, Martin Matunda aliwasilisha maombi katika Mahakama ya Kisutu ya kuomba kesi zote hizo nne zisimame kusikilizwa kwasababu washtakiwa hao walifungua kesi hiyo ya Kikatiba iliyotolewa uamuzi jana itakapotolewa uamuzi. Na kwa kipindi chote hicho kesi hizo zote zilikuwa zimesimama kusikilizwa.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Oktoba 26 mwaka 2011.

HAKIMU AKWAMISHA KESI YA LIYUMBA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kukutwa na simu gerezani inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba jana ulishindwa kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa huyo kwa sababu hakimu mkazi Stewart Sanga anayesikiliza kesi yake kutokuwepo mahakamani hapo.


Wakili wa Serikali Elizabeth Kaganda alimweleza Hakimu Mkazi Aloyce Katemana kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya wao kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa huyo na mawakili wa utetezi kuwasilisha hoja za pingamizi lao lakini akaomba kesi hiyo iairishwe kwasababu hakimu anayesikiliza kesi hiyo hajafika mahakamani hapo.

Hoja hiyo ilikubaliwa na mawakili wa utetezi Hudson Ndusyepo, Onesmo Kyauke na Majura Magafu pamoja na Hakimu Katemana ambaye aliairisha kesi hiyo hadi Desemba mbili mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya Jamhuri kumsomea maelezo ya awali.

Awali Septemba 8 mwaka huu, Liyumba alifikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na kesi hiyo mpya ya kukutwa na simu akiwa katika gereza la Ukonga wakati akitumikia adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela baada ya Mei 25 mwaka jana, mahakama hiyo kumtia hatiani kwa kosa la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma.Septemba 23 mwaka huu, alitoka gerezani baada ya kumaliza kutimikia kifungo hicho.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Oktoba 29 mwaka 2011.

MAHAKAMA INA NINI NA KESI YA MRAMBA?


Na Happiness Katabazi

JANUARI 20 mwaka huu, upande wa Jamhuri katika kesi ya matumuzi mabaya na kuisababishia serikali hasara ya shilingi bilioni 11.7 inayomkabili Waziri wa Fedha wazamani, Basil Mramba na Waziri wa Nishati na Madini na Nishati wa zamani Daniel Yona na Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja,walifunga kesi yao.

Washtakiwa hao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Hurbet Nyange, Elisa Msuya ,Peter Swai na Profesa Leonard Shaidi.Wakati upande wa Jamhuri unawakilishwa na Wakili Kiongozi wa Serikali Stanslaus Boniface anayesaidiwa na Fredrick Manyanda na Ben Lincolin.

Kesi hiyo ambayo inasikilizwa kwa mtindo wa jopo.Jaji John Utamwa ndiye anaongoza jopo la Mahakimu wakazi kusikiliza kesi hiyo ambapo anasaidiwa na Sam Rumanyika na Saul Kinemela.

Binafsi mimi nimiongoni mwa waandishi wa habari wachache hapa nchini ambao nimezama katika kuripoti habari za mahakamani kikamilifu.Hivyo kuhusu kesi hii ya Mramba nadiriki kusema nimepata fursa ya kuudhulia kesi hii tangu ilipofunguliwa rasmi Novemba 25 mwaka 2008 .

Ambapo Mramba na Yona ndiyo walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa mara ya kwanza kwa pamoja kwa mbwembwe na makachero wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) zilizochagizwa na vyombo vya habari wakikabiliwa na makosa hayo lakini hata hivyo siku hiyo walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na hivyo kuamliwa kwenda gerezani hadi siku watakapotimiza masharti ya dhamana.

Kisha Desemba 15 mwaka 2008 majira ya mchana ndipo Mgonja alifikishwa peke yake hapo mahakamani na makachero wa Takukuru ambapo naye alisomewa mashtaka yale yale yanayofana na kesi ya Mramba na Yona na

Lakini ilipofika Januari 2 mwaka 2009 Jamhuri iliibadilisha hati ya mashtaka ya kesi iliyokuwa ikimkabibili Mramba na Yona kwa kumuunganisha Mgonja katika kesi hiyo hivyo kufanya kesi hiyo kuwa na jumla ya washtakiwa watatu na ile kesi iliyokuwa ikimkabili Mgonja peke yake kufutwa.

Na mwisho wangu kuudhulia kesi ya washtakiwa hao ambao ni watumishi wa muda mrefu serikali na Bungeni ni Oktoba 19 mwaka huu, ambapo kesi hiyo siku hiyo ilikuja mbele ya kwa Hakimu Mkazi Sundi Fimbo kwaajili ya kutajwa na jopo la mahakimu wakazi wanaosikiliza kesi hiyo yaani Jaji Utamwa, Rumanyika na Kinemela kuwagawia mwenendo wa kesi hiyo pande mbili za kesi hiyo yaani upande wa Jamhuri na ule wa utetezi ili kila upande uende kuaandaa sababu ambazo mwisho wa siku upande wa Jamhuri utaleta sababu zake za kuiomba Jamhuri iwaone washtakiwa hao wanakesi ya kujibu na upande wa utetezi utaiomba mahakama iwaone wateja wao hawana kesi ya kujibu na baada ya pande hizo kuwasilisha mahakamani maombi hao, ndipo kisheria mahakama inabaki na jukumu ya kuyapitia kwa kina maombi hayo ya pande hizo mbili na kisha mahakama hiyo inapanga tarehe yake ya kuja kutoa uamuzi utakaowaona washtakiwa hao ama wana kesi ya kujibu au wanakesi ya kujibu.

Na endapo mahakama itafikia uamuzi wa kuwaona washtakiwa wana kesi ya kujibu, hivyo washtakiwa watalazimika kupanda kizimbani kujitetea.

Lakini katika kesi hii ya Mramba, Yona na Mgonja, upande wa Jamhuri ilijitahidi kadri ya uwezo wake kuleta jumla ya mashahidi 13 ambao walifika mahakamani hapo na kutoa ushahidi wao na kisha ilipofika Januari 20 mwaka huu, ndipo upande wa Jamhuri uliambia mahakama hiyo kuwa wamefunga kesi yao.

Nakumbuka siku hiyo baada ya wakili wa serikali Boniface kuieleza mahakama kuwa wamefunga kesi yao, Jaji Utamwa jopo lake linaueleza uongozi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu chini ya Hakimu Mkuu Mfawidhi Elvin Mugeta uuchape mwenendo mzima wa kesi hiyo(Procedings) na ukimaliza kuuchapa mwenendo huo watapewa wanajopo hili waweze kuhuhakiki na wakishamaliza kuhakiki ndipo panede hizo mbili zitapewa mwenendo huo.

Tangu Jaji Utamwa atoe ahadi hiyo ambayo kweli ilitekelezwa kwa vitendo na uongozi wa Mahakama ya Kisutu licha mahakama ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la mgao wa umeme ,ikauchapa mwenendo huo na ukaugawa mwenendo huo wa wanajopo hao na tangu kipindi hicho cha Januari 20 mwaka huu, washtakiwa na mawakili wa pande zote na waandishi wa habari za mahakamani wamekuwa wakifika mahakamani hapo kwa terehe zilizokuwa zikipangwa ambapo kesi hiyo imekuwa ikija kwaajili ya kutajwa huku mahakimu wanaoarisha kesi hizo ambazo siyo wanajopo wakihitimisha kuairisha kesi hiyo kwa kibwagizo kisemacho ‘jopo linalosikiliza kesi hiyo bado linaendelea na uhakiki wa mwenendo”.

Nakumbuka wakati mashahidi wa Jamhuri wanatoa ushahidi wao, kuna mwandishi mmoja aliripoti habari isiyosahihi kuhusu ushahidi huo hali iliyosababisha mawakili wa washtakiwa hao kugeuka mbogo na kuliomba jopo linalosikiliza kesi hiyo kulichukulia hatua gazeti hilo(siyo Tanzania Daima), lakini kiongozi wa jopo hilo Jaji Utamwa akitoleoa uamuzi ombi hilo alisema hawezi kutolea uamuzi ombi la mawakili hao kwasababu vyombo vya habari siyo sehemu ya kesi hiyo.Sehemu ya kesi hiyo ni upande wa Jamhuri na Utetezi.Nakubaliana na uamuzi huo.

Lakini sisi wanahabari tunawajibu wa ujulisha umma taarifa mbalimbali ikiwemo kesi mbalimbali zinavyoendelea mahakamani ikiwemo kesi hii ya Mramba.

Napenda ieleweke wazi kuwa kutokana na jopo hilo la mahakimu wakazi kuchukua muda mrefu bila kuzipatia pande mbili katika kes hizo ule mwenendo wa kesi hiyo, umezua minong’ono na hisia tofauti ambazo zinaendelea kusambaa chini chini kwa wananchi wenyewe, viongozi wa serikali, hata kwa mawakili wa pande hizo wamekuwa wakijiuliza nje ya mahakama kuwa kuna nini kilichojificha ambacho kinasababisha jopo hilo la mahakimu wakazi lichukue muda mrefu kuwapatia mwenendo huo?

Kwa wale tuliokuwa tukiudhulia kesi hii tunaweza kusema kesi hii ni miongoni mwa kesi chache za upande wa Jamhuri ambazo upande wa Jamhuri umejitahidi kuleta mashahidi wake kadri ya inavyoweza lakini cha kushangaza ni jopo hilo hadi kufikia leo inakaribia kumalizika mwaka mmoja inashindwa kutoa mwenendo huo wa kesi hiyo kwa pande hizo mbali hali inayosababisha kuibua maswali mengi kuliko majibu nje ya mahakama?

Ni rai yangu kwa jopo hilo linaloongozwa na Jaji Utamwa kwamba tayari kitendo cha jopo lake kuchukua muda mrefu licha jopo hilo lina haki ya kisheria kujitetea kuwa halikutoa muda kuwa kipindi fulani kitakuwa kimemaliza kuuhakiki mwenendo na kitakuwa kimeishazipatia pande pande hizo nyaraka, kimeanza kulalamikiwa chini chini na kuhusishwa na hisia mbaya na wafuatiliaji wa kesi hiyo na pia limesababisha sisi waandishi wa habari za mahakamani kuanza kujiuliza kuwa mahakama ina nini na kesi ya Mramba?.

Tunaamini jopo la mahakimu hao ni jopo la mahakimu wakazi wenye uweledi na uzoefu katika taaluma hiyo ya sheria.Na ninafahamu pia mahakama haifanyi kazi kwa hisia wala minongono ya watu waliopo nje ya mahakama lakini, ni vyema pia jopo hilo kuanzia sasa likaona ni vyema kukomesha hisia hizo mbaya ambazo hazina ushahidi zinazoelekezwa kwao na hivyo likaharakisha kuzipatia pande hizo mbili mwenendo huo ili taratibu zingine za kisheria kuhusu kesi hizo ziendelee.

Ieleweke wazi kesi hiyo inawahusu washtakiwa hao ambao walishatoa mchango mkubwa wa utumushi katika taifa letu hivyo wanamajukumu mengine yakufanya, pia nao mawakili wa serikali na mawakili wa kujitegemea nao wanamajukumu mengine, sasa kitendo cha kesi hiyo ambayo hivi sasa inakaribia kufikia mwaka mmoja , inakuja kwaajili ya kutajwa tu , ni wazi kabisa hao mawakili, washtakiwa na ndugu wawashtakiwa na sisi waandishi wa habari tunashindwa kwenda kufanya shughuli nyingine za ujenzi wa taifa tunakuja kuudhulia kesi hiyo ambayo inaairishwa kila kukicha na mbaya zaidi inaarishwa kwa mahakimu ambao hawasikilizi kesi hiyo, huku jopo hilo la mahakimu wakazi halifiki katika viwanja vya mahakama ya Kisutu kuarisha kesi hiyo.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika

0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Oktoba 27 mwaka 2011.

HAKIMU AGOMA KUJITOA KESI YA MARANDA

Na Happiness Katabazi

JOPO la Mahakimu Wakazi watatu wanaosikiliza kesi ya wizi wa Sh bilioni 3.3 katika Akaunti ya Madeni ya Nje(EPA) inayomkabili Rajabu Maranda na wenzake wanne katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,limetupilia mbali ombi la washtakiwa wawili Maranda na Farijala Hussein lilokuwa likiomba Hakimu Mkuu Mfawidhi Elvin Mugeta anayeunda jopo hilo ajitoe kwenye kesi hiyo.


Wanaounda jopo hilo ni Jaji Beatrice Mutungi, Jaji Karua na Hakimu Mkazi Mugeta.

Uamuzi huo ulitolewa jana na jopo hilo ambalo lilisema uamuzi huo unatokana na ombi lilowasilishwa juzi na wakili wa washtakiwa hao Majura Magafu ambaye ambalo lilimwomba Mugeta ajitoe kwenye kesi hiyo kwani hatatenda haki kwakuwa Mugeta ndiye aliyekuwa akiunda jopo la mahakimu wakazi Saul Kinemela na Focus Bampikya ambao Mei 25 mwaka huu, walihukumu washtakiwa hao Maranda, Farijala kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia kujipatia sh bilioni 1.8 kwa njia ya udanganyifu kutoka Benki Kuu na kwamba mashahidi waliotoa ushahidi kwenye kesi ya awali ndiyo wanaokuja kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo ya sasa.

Jaji Karua alisema wamefikia uamuzi huo kwasababu ombi hilo halina msingi wa kisheria kwani kesi hiyo inaendesha kwa mtindo wa jopo hivyo Hakimu Mugeta peke yake hawezi kulishawishi jopo hilo kutoa uamuzi anaoutaka yeye bila kukubaliana na jopo hilo na hivyo akaiarisha kesi hiyo hadi Novemba 25 itakapokuja kwaajili ya kutajwa na itakuja kwaajili Februali 13-17 mwaka 2011 kwaajili ya kuendelea kusikilizwa.

Mbali na Maranda na Farijala washtakiwa wengine ni maofisa wa BoT, Sophia Lalika na Iman Mwakosya, Ester Komu na mfanyabiashara Ajay Somani ambao wanadai wakula njama na kuibia BoT jumla ya Sh bilioni 3.3.

Chanzo:

HAKIMU AGOMA KUJITOA KESI YA MARANDA

Na Happiness Katabazi

JOPO la Mahakimu Wakazi watatu wanaosikiliza kesi ya wizi wa Sh bilioni 3.3 katika Akaunti ya Madeni ya Nje(EPA) inayomkabili Rajabu Maranda na wenzake wanne katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,limetupilia mbali ombi la washtakiwa wawili Maranda na Farijala Hussein lilokuwa likiomba Hakimu Mkuu Mfawidhi Elvin Mugeta anayeunda jopo hilo ajitoe kwenye kesi hiyo.


Wanaounda jopo hilo ni Jaji Beatrice Mutungi, Jaji Karua na Hakimu Mkazi Mugeta.

Uamuzi huo ulitolewa jana na jopo hilo ambalo lilisema uamuzi huo unatokana na ombi lilowasilishwa juzi na wakili wa washtakiwa hao Majura Magafu ambaye ambalo lilimwomba Mugeta ajitoe kwenye kesi hiyo kwani hatatenda haki kwakuwa Mugeta ndiye aliyekuwa akiunda jopo la mahakimu wakazi Saul Kinemela na Focus Bampikya ambao Mei 25 mwaka huu, walihukumu washtakiwa hao Maranda, Farijala kifungo cha miaka mitano jela baada ya kupatikana na hatia kujipatia sh bilioni 1.8 kwa njia ya udanganyifu kutoka Benki Kuu na kwamba mashahidi waliotoa ushahidi kwenye kesi ya awali ndiyo wanaokuja kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo ya sasa.

Jaji Karua alisema wamefikia uamuzi huo kwasababu ombi hilo halina msingi wa kisheria kwani kesi hiyo inaendesha kwa mtindo wa jopo hivyo Hakimu Mugeta peke yake hawezi kulishawishi jopo hilo kutoa uamuzi anaoutaka yeye bila kukubaliana na jopo hilo na hivyo akaiarisha kesi hiyo hadi Novemba 25 itakapokuja kwaajili ya kutajwa na itakuja kwaajili Februali 13-17 mwaka 2011 kwaajili ya kuendelea kusikilizwa.

Mbali na Maranda na Farijala washtakiwa wengine ni maofisa wa BoT, Sophia Lalila na Iman Mwakosya, Ester Komu na mfanyabiashara Ajay Somani ambao wanadai wakula njama na kuibia BoT jumla ya Sh bilioni 3.3.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Oktoba 26 mwaka 2011.

JERRY MURRO HANA HATIA-WAKILI

Na Happiness Katabazi

WAKILI wa aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1), Jerry Murro anayekabiliwa na kesi ya kula njama na kuomba rushwa ya sh milioni 10, Richard Rweyongeza ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,imwachilie huru mshtakiwa huyo kwasababu hana hatia katika kesi hiyo inayomkabili.


Wakili Rweyongeza aliwasilisha maombi hayo mahakamani hapo kwa njia ya maandishi nakala yake (gazeti hili inayo) kufuatia amri iliyotolewa na Hakimu Mkazi Frank Moshi aliyoitoa Oktoba mwaka huu ambapo alizitaka pande zote mbili kuwasilisha majumuisho yao kuwaona washtakiwa wana hatia au la kwa njia ya maandishi ambapo upande wa Jamhuri utawasilisha majumuisho yao kesho.

Wakili Rweyongeza alidai kuwa alisikilizwa kwa makini ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa Jamhuri lakini hajasikia kitu chochote kinacho muunganisha Murro na washtakiwa wengine wasiojulikana kula njama kutenda kosa hilo kama shtaka la kwanza kwanza linavyodai kuwa Murro na washtakiwa wenzake ambao ni Deo Mugassa na Edmund Kapama na watu wengine wasiyofahamika walitenda kusa la kushawishi ili wapewe rushwa Sh milioni 10 toka kwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Michael Wage Karoli , Januari 20 mwaka 2010 ili asiwe kurusha tuhuma zake za ubadhilifu wa fedha za umma katika kipindi cha Usiku wa Habari kinachorushwa na Televisheni ya TBC1.

“Shtaka la kwanza katika hati ya mashtaka, linasomeka kuwa kosa lilitendeka Januari 28 mwaka 2010.Lakini ushahidi ulitolewa na Jamhuri ulionyesha kosa lilitendekea Januari 29 mwaka 2010…na hadi mapema Oktoba mwaka huu washtakiwa walimaliza kujitetea na hivyo kesi upande wa utetezi ikawa imefungwa , hati ya mashtaka ilikuwa ikisomeka Murro alitenda kosa hilo Januari 28 mwaka 2010 ndipo upande wa Jamhuri siku hiyo kabla ya utetezi kufunga kesi yao ukaamua kubadilisha hati ya mashtaka na mahakama ilikubali hati hiyo kubadilishwa kutokana na utofauti uliopo kati ushahidi na maelezo yaliyokuwa yameandikwa kwenye hati ya mashtaka.

“Kwa hali hiyo naona upande Jamhuri hauna maelezo ya uhakika yanayoonyesha mteja wangu alitenda makosa hayo na badala yake ikaamua kuleta ushahidi wa kuungaunga na matokeo yake ndiyo maana Murro aliyakana mashtaka yote yanayomkabili mahakamani hapa”alidai Rweyongeza.

Alidai kuwa kesi ya Jamhuri imesimama na kutegemea ushahidi wa shahidi wa tatu (Michael Wage) jambo linawapotosha kwa sisi upande wa utetezi tunamuona Wage siyo shahidi wa kuaminika na wanaoimba mahakama iupuuze ushahidi wake.

Wakili Rweyongeza alidai kuwa katika ushahidi mashahidi wa Jamhuri walidai kuwa shahidi wa tatu(Wage) kwakuanzia aliwapatia washtakiwa wote rushwa ya Sh 9,000,000 katika sehemu ya rushwa ya Sh milioni 10 aliyokuwa ameombwa na washtakiwa, na wakili huyo akadai kuwa kama hivyo ndivyo ni kwanini polisi wasingesubiri Murro apokee rushwa hiyo ndiyo wakamkamate na kuongeza ni kwanini polisi ilifanya haraka kumkamata Murro wakati bado hajapokea rushwa hiyo ya Sh milioni?

“Tunaomba mahakama hii imwachilie huru Murro kwasababu upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi yao bila kuacha mashaka yoyote hivyo namalizia kwa kuiomba mahakama hii imuone Murro hana hatia”alidai Rweyengeza.

Februali 15 mwaka 2010, ilidaiwa mahakamani na upande wa Jamhuri kuwa washtakiwa wote walitenda makosa ya kula njama, kushawishi kupewa rushwa ya Sh milioni 10 kutoka kwa Wage na kujipachika kuwa wao ni wa Maofisa ya TAKUKURU.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Oktoba 22 mwaka 2011.

SITA WAACHIWA KESI YA MAUJI NMB TEMEKE

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imewaachiria huru washtakiwa sita kati ya 15 waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya watu wawili katika Benki ya Makabwera (NMB) Tawi la Temeke Dar es Salaam.


Hatua hiyo inakuja baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Dk.Eliezer Feleshi kuwasilisha ombi la kuiomba mahakama hiyo iwafutie kesi washtakiwa hao kwasababu amebaini hana ushahidi unamshawishi kuendelea kuwashtaki washtakiwa hao kwasababu amebaini hana ushahidi wa kuendelea kuwashtaki.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya mauaji Na. 22/2011 inayosikilizwa na Jaji Dk.Fauz Twaibu ni Richard Muhanza “Leonard’, Mwanzo Bunga, Alimeshi Bibuka, Yusufu Mlete, Japo Salum, Issack Abdul ‘Swai’,Said Hamisi ‘Katikati’, Antony Solya ‘Matonya’, Richard Tawete ‘Anwari’, Shafii Abdala, Boniface Makai.

Wengine ni Fabian Mchome ‘Fabi’, Selemani Nzowa, Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ), MT.55935 Mathew Mwangunga na Deogratius Massawe ambao wanatetewa na wakili wa kujitegemea Amour Khamis.

Washtakiwa waliochiliwa huru ni mshtakiwa wa (2) Bunga, (3)Bibuka (10)Abdalah (12)Mchome(13)Nzowa na mshtakiwa wa (15)Massawe.

Jaji Twaibu alisema amefikia uamuzi wa kuwachilia huru washtakiwa hao kufuatia ombi lilowasilishwa mbele yake jana mchana na Mkurugenzi Msaidizi katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Stanslaus Boniface ambaye aliwasilisha ombi la kuwataka washtakiwa hao sita kati ya 15 waachiliwe huru chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, kwasababu DPP hana haja ya kuendelea na kesi dhidi yao kwasababu umekosekana ushahidi wa kuendelea kuwashtaki.

“Kwakuwa kesi hii imefunguliwa mahakamani hapo na upande wa Jamhuri na upande huo wa Jamhuri leo umewasilisha ombi la kuiomba mahakama iwafutie kesi, mahakama hii inakubali ombi hili na inawaachiria huru washtakiwa sita tu, washtakiwa waliosalia wataendelea kubaki kuwa washtakiwa katika kesi hii”alisema Jaji Dk.Twaibu.

Sekunde chache baada ya washtakiwa hao kuachiliwa huru na kutolewa na askari wa jeshi la Magereza nje ya kordo ya Mahakama Kuu Kitengo cha Biashara, baadhi ya washtakiwa hao walioachiliwa huru walianza kuzungumza kwa sauti ya juu hali iliyosababisha askari Magereza kutoka nje na kuwataka wakae kimya.

Baada ya Jaji Dk.Twaibu kutoa uamuzi huo, Mkurugenzi Msaidi katika ofisi ya DPP, Boniface aliambia mahakama hiyo kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao ambapo alianza kuwasomea maelezo hayo kwa kudai kuwa Julai 31 mwaka 2009 katika Benki ya NMB Tawi la Temeke, watu wawili wasiliyo na hatia mmoja akiwa ni askari wa Jeshi la Polisi, E.329 Koplo Josephat Milambo na mlinzi mwingine wa benki hiyo Seif Mkwike waliuwawa kwa kupigwa risasi na majambazi waliokuwa wamevamia benki hiyo.

Boniface ambaye pia ni Wakili Kiongozi wa Serikali, alidai tukio hilo lilitokea saa 4:30 asubuhi ambapo majambazi hao walivamia benki hiyo kwa nia ya kuiba fedha na kabla ya kufanya jambo lolote , majambazi hao walitoa silaha zao na kuwaelekezea moja kwa moja maofisa wa polisi ambao walikuwa wamekaa kwenye chumba cha walinzi.

Alidai baada ya majambazi hao kuwaelekezea polisi hao silaha, maofisa hao wa polisi nao walilazimika kuingia kwenye mapambano ya silaha dhidi ya majambazi hao na matokeo ya mapambano hayo ya silaha yalisababisha marehemu hao wawili kufariki dunia na majambazi hao wakafanikiwa kuingia ndani ya benki hiyo na kuondoka na kiasi cha fedha kisichofahamika.

“Katika eneo la tukio majambazi watatu yaani mshtakiwa aitwaye Yusufu Mlete, Issack Abdul ‘Swai” na MT 55935 Sajenti Mathew Mwangunga walitambuliwa na baadaye mashahidi walikuja kuwatambua na baada ya majambazi hao watatu kukamatwa wakitambuliwa tena na mashahidi katika gwaride la utambuzi lililokuwa limeandaliwa na Jeshi la Polisi”alidai wakili Boniface.

Aliendelea kueleza kuwa kadri majambazi wale hao waliohusika katika tukio hilo walivyokuwa wakizidi kukakamatwa na kisha wakahojiwa na polisi , majambazi katika maungamo yao walikiri kutenda makosa hayo ya mauji ya watu wawili .

Wakili Boniface aliwataja majambazi hao (washtakiwa) ambao walikiri kutenda kosa hilo katika maungamo yao ni Richard Muhanza, Mlete, Matonya, Tawete Salum, Said Hamiusi ‘Katikati’ na Makai. Na kwamba washtakiwa hao waliokiri kutenda kosa hilo walikamatwa kwa pamoja huko Mbagala Kuu wakati wakijiandaa kupanga njama za kufanya tukio jingine la uhalifu.

“Na mtukufu Jaji maungamo yao waliyoungama polisi waliungamba mbele ya ASP-Ndagile Makubi kuwa walihusika kutenda kosa la mauji ya watu wa wiwili katika NMB Tawi la Temeke, Julai 31 mwaka 2009”alidai wakili Boniface.

Aidha alidai kuwa miili ya marehemu hao ilifanyiwa uchunguzi na wataalamu na ripoti ya uchunguzi ikaonyesha marehemu Seif Athuman Mkwike aliuwa kwa shinikizo la damu na marehemu Koplo Milambo naye aliuwa kutokana na mlipuko wa bomu la mkono lililorushwa na washtakiwa hao siku ya tukio.

Hata hivyo wakili wa utetezi Amour Khamis alidai kuwa washtakiwa wote wanakanusha maelezo hayo ya awali waliyosomewa na upande wa Jamhuri na kwamba wanachokubali ni majina yao tu.

Baada ya pande hizo mbili kutoa maelezo hayo, Jaji Twaibu aliutaka upande wa Jamhuri kuleta orodha ya mashahidi na vielelezo watakavyovitumia kwenye kesi hiyo Novemba 22 mwaka huu, na kwamba anaiarisha kesi hiyo hadi Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, atakapoipanga tena.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Oktoba 25 mwaka 2011.
mwisho.

KESI YA KAKOBE YAZUA MAZITO

Na Happiness Katabazi

KESI inayomkabili Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zakaria Kakobe, imechukua sura mpya baada ya mama mzazi wa Jaji Agustine Shangwa anayesikiliza shauri hilo kumvaa mwanaye na kumtaka ajieleze kwa nini amekataliwa na walalamikaji.


Jaji Shangwa alisema kesi hiyo imemletea mzozo na mama yake mzazi anayeishi Bukoba ambaye baada ya kusoma taarifa za kukataliwa kusikiliza shauri hilo zilizochapishwa na gazeti moja la kila siku (sio Tanzania Daima), alimpigia simu na kumhoji kwa nini hawatendei haki walalamikaji.

Alidai kuwa kitendo cha walalamikaji kukimbilia katika vyombo vya habari hakikuwa cha kistaarabu kwa kuwa yeye katika kesi hiyo ni mshauri tu na sio msikilizaji.
Pamoja na kutoa siri hiyo, Jaji Sangwa amechukua uamuzi mwingine mzito wa kukataa kujitoa katika kesi hiyo kama alivyotakiwa na walalamikaji waliodai kutokuwa na imani naye kwa vile alionyesha upendeleo kwa mshtakiwa.

“Jamani mimi nilikuwa nikiwashauri tu nyie walalamikaji lakini mkaenda kwenye gazeti hilo na sijui na kwa watu gani wengine kulalamika kuwa siwatendei haki, hadi mama yangu akaniuliza, sasa nendeni mkaseme tena kuwa leo nimerudia kutowatendea haki, maana hao waandishi wana vinasa sauti vinarekodi kila kitu,” alisema Jaji Shangwa na kusababisha watu kucheka.

Akieleza sababu za kugoma kujitoa, Jaji Shangwa alisema walalamikaji wameshindwa kutoa hoja za maana ambazo zingeweza kumfanya ajiondoe kwenye kesi hiyo.

Jaji Shangwa alitoa uamuzi huo mwishoni mwa wiki akisema amefikia uamuzi huo wa kukataa kujiondoa kwenye kesi hiyo kwa kuwa yeye si msikilizaji bali ni msuluhishi.

“Msisononeshwe na uamuzi huo, mimi ni Jaji Msuluhishi tu katika kesi hii na si Jaji Msikilizaji. Hivyo kama usuluhishi wa kesi hii ukishindikana jalada litarudishwa kwa Jaji Mfawidhi ili ampange jaji mwingine wa kuisikiliza kesi hii,” alisema Jaji Shangwa.

Walalamikaji katika kesi hiyo ya tuhuma za ubadhirifu wa mali na pesa zaidi ya shilingi bilioni 14 pamoja na ukiukwaji wa katiba ya kanisa hilo, Dezedelius Patrick, Angelo Mutasingwa na Benedict Kaduma walimtaka Jaji Shangwa ajiondoe mwenyewe katika kesi hiyo kwa madai kuwa hawana imani naye.

Walalamikaji hao walimwandikia barua Msajili wa Mahakama Kuu Dar es Salaam, Agosti 26, mwaka huu, wakimtaka Jaji Shangwa ajiondoe mwenyewe katika kesi hiyo wakidai kuwa amekiuka maadili ya kitaaluma, taratibu na heshima ya mahakama na ameonyesha upendeleo kwa mlalamikiwa.

Wanadai kuwa mlalamikiwa hakuwasilisha maelezo yake ya maandishi (WSD) ndani ya siku 21 na kwamba siku ya kutajwa kwa kesi hiyo wakili wake Miriam Majamba alitoa sababu za uongo lakini jaji hakutilia maanani na badala yake Agosti 2, 2011 yeye alitoa hukumu dhidi yao wakati kesi hiyo haijafikia hatua hiyo.

Walalamikaji hao wanadai maneno ya jaji huyo yalikuwa na upendeleo wa waziwazi kwa Kakobe. Katika ushauri wake katika kesi hiyo, jaji huyo alisema, “Nyie walalamikaji nasema bila kumung’unya maneno kuwa madai yenu yote ni majungu… Kakobe ni mungu wa kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, kanisa ni mali yake… kwa hiyo kama anakula fedha za kanisa anakula fedha zake, hakuna wa kumhoji kwani lile ni kanisa lake na ni mali yake,” alisema.

Walalamikaji hao wananukuu maneno ya jaji huyo aliyedai: “Kakobe atawashinda kesi hii na kuwadai pesa nyingi, kwa hiyo futeni kesi, kama na ninyi mnataka kaanzisheni makanisa yenu, uaskofu wake alijipa mwenyewe sio kama makanisa mengine wanaosomea.”
Kwa mujibu wa hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani, walalamikaji hao wanamtuhumu Kakobe kuwa amekuwa akikusanya fedha kutoka kwa waumini wake kwa madai ya kufanyia shughuli na miradi mbalimbali ya kanisa na kuzitumia isivyo halali.

Mbali na kufuja fedha hizo kama vile kugharamia kampeni za kisiasa, pia wanadai kuwa amekuwa hatoi taarifa ya mapato na matumizi ya fedha anazozikusanya.
Miongoni mwa madai hayo ni makusanyo ya shilingi milioni 800 kwa ajili ya kununulia vifaa vya kuanzisha televisheni.

Hata hivyo wanadai kuwa badala yake Kakobe anadai kuwa vifaa hiyo amevirudisha Marekani alikovinunua kwa kuwa eneo la mradi huo limeathiriwa na mradi wa umeme wa msongo mkubwa na kwamba kwa sasa anataka kuhamia jijini Boston Marekani.

Kuhusu ukiukwaji wa katiba ya kanisa hilo, walalamikaji hao wanadai kuwa katiba inataka kuitishwa kwa mkutano mkuu kila baada ya miaka mitano ambacho ndicho chombo cha juu cha maamuzi lakini Kakobe hajawahi kuitisha mkutano huo tangu mwaka 1989.

Pia wanadai kuwa katiba hiyo inataka kanisa liwe na Katibu Mkuu na Mweka Hazina ambao ndio watakaolinda mali za kanisa lakini Kakobe amekuwa akifanya maamuzi na shughuli zote peke yake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Oktoba 24 mwaka 2011.

WATUHUMIWA WA MAUAJI WAACHIWA HURU

Na Happiness Katabazi

MWEKEZAJI wa Hoteli ya South Beach ya Kigamboni, Salim Nathoo ‘Chipata’ (53), na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kijana Lila Hussein (25), wameachiwa huru kufuatia Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) Eliezer Feleshi kuwasilisha hati ya kuiondoa kesi hiyo mahakamani.


Nathoo aliyeshtakiwa pamoja na Meneja wake Bhushan Mathkar na John Mkwanjiombi (32) waliachiwa wiki hii na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Kassim Mkwawa.

Mwendesha mashtaka katika kesi hiyo, Dunstun Kombe, aliliambia Tanzania Daima kwamba amri ya kuachiwa huru kwa watuhumiwa hao ilitolewa Oktoba 10 na DPP kwa kutumia kifungu 91 (1) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2002, inayompa madaraka ya kuondoa kesi mahakamani ikiwa ataona ushahidi wa kesi husika hautoshelezi bila kuhojiwa na mtu wala taasisi yoyote.

Ndugu wachachamaa, wataka maelezo

Hata hivyo, kuachiwa kwa mwekezaji huyo kumezua utata mkubwa kwa baadhi ya ndugu wa marehemu na wakazi wa jiji la Dar es Salaam waliokuwa wakifuatilia kwa makini kesi hiyo tangu kutokea kwa mkasa huo, usiku wa April 9, mwaka huu.

Akizungumza kwa niaba ya ndugu wa marehemu, Abdullah Saiwaad, alisema wamesikitishwa na hatua ya serikali ya kuwaachia huru watuhumiwa wa mauaji ya ndugu yao, bila kujali madhara makubwa yaliyopatikana.

Alisema kitendo cha kuachiwa kwa mwekezaji huyo tena kwa muda mfupi tu tangu kukamatwa na kufikishwa mahakamani, bila kujali athari waliyopata ndugu wa marehemu, kimewafanya waamini kwamba mwenye pesa yuko juu ya sheria.

“Ndugu yetu ameuawa kinyama kwa kuchomwa moto kama kuku, alafu leo hii watu hawa wanaachiwa huru katika mazingira yenye utata namna hii..inasikitisha sana,” alisema Saiwaad.

Aliiomba serikali kurudia upya uchunguzi huo na kufungua mashtaka mapya dhidi ya watuhumiwa hao na kwa kuzingatia zaidi ushahidi wa marehemu alioutoa kabla hajafariki.

Mkasa mzima wa kifo

Lila anadaiwa kukumbwa na mkasa huo Aprili 11 mwaka huu majira ya kati ya saa 5:00 na 6:00 usiku akidaiwa kuingia katika ukumbi wa muziki hotelini hapo bila kulipa kiingilio.

Inadaiwa kwamba marehemu alikamatwa na kupigwa vibaya na askari wanaolinda usalama kwa amri ya meneja na mwekezaji huyo, kabla ya kufikia uamuzi wa kumvua nguo na kummwagia mafuta ya petroli na kumchoma moto.

Habari zinaongeza kuwa wafanyakazi wawili walioshuhudia ukatili huo, walilazimika kupeleka taarifa za tukio hilo kwa ndugu zake, kijiji cha Mjimwema waliofika na kumkimbiza hospitalini.

Lila aliyelazwa wodi namba 7 katika Hospitali ya Temeke akiwa hajitambui akiwa amejeruhiwa vibaya kuanzia magotini hadi shingoni, alifariki dunia Aprili 17 mwaka huu, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Watuhumiwa hao walikamatwa na kufunguliwa kesi ya kujeruhi ambayo iliunguruma katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke, kabla ya kubadilishiwa mashtaka na kuwa ya mauaji kufuatia kifo cha kijana huyo.

Sababu za kuondolewa kwa kesi

Nayo Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini, imetoa ufafanuzi wa kina wa kile kilichosababisha kufutwa kwa kesi hiyo.

Akizungumza na Tanzania Daima katika mahojiano maalum, Mkurugenzi Msaidizi katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Stanslaus Boniface, ofisi hiyo iliifuta kesi hiyo baada ya kubaini upungufu mkubwa ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa ushahidi kwa washtakiwa.

Bonifasi aliongeza kuwa ofisi yake ilifikia uamuzi wa kulikagua jalada hilo, baada ya kupokea malalamiko mengi toka ndugu wa washtakiwa waliodai kubambikiziwa kesi ya mauaji.

Katika barua ya maamuzi kwenda kwa mwanasheria wa Kanda ya Dar es Salaam, Mkurugenzi Msaidizi huyo alisema ushahidi uliokuwa ukitarajiwa kuijenga kesi hiyo ulikuwa ni wa aina mbili: ushahidi wa kwanza ni tamko linalodaiwa kutolewa na marehemu kabla hajakata roho na ushahidi wa mazingira.

Barua hiyo (nakala tunayo) inasema ushahidi uliomo katika jalada la kesi hiyo ulikuwa na mapungufu mawili. “Kama ni kweli marehemu aliwaeleza maneno hayo hao mashahidi wawili Aprili 10 mwaka huu saa 6:30 usiku, kwa nini mashahidi hao hawakutoa maelezo hayo polisi siku ya kwanza kabisa walivyokuwa wakichukuliwa maelezo yao na polisi Aprili 10 mwaka huu saa 5:30?

“Kitendo cha miezi miwili kupita bila ya polisi kuarifiwa na mashahidi hao kile walichoelezwa na marehemu, pia kimesababisha ushahidi uliopo kwenye jalada hilo kuwa na mapungufu makubwa na sababu hiyo ya kwanza pia ndiyo imenisukuma kuifuta kesi hiyo kwani ofisi ya DPP haiwezi kuendelea kuwashtaki watu pindi inapobaini ushahidi uliopo ndani ya jalada hautoshelezi kuendelea kuwashtaki,” alisema Boniface.

Boniface alichambua ushahidi ambao ni tamko lililotolewa na marehemu kabla ya kifo na ulidhibitishwa na Salum Ally, Saidi Kau Sahan, marehemu mwenyewe na G.5975 PC Saidi.

Salum Ally na Said Kau Sahani ndiyo walikuwa watu wa kwanza kukutana na marehemu katika hoteli ya Sunrise baada ya kuchomwa moto.

Na katika maelezo ya nyongeza waliyoyatoa polisi Juni 7, 2011, Salum Ally kwa mara ya kwanza walisema:

“Niliambiwa naye (marehemu) wakati tulipokutana naye kuwa amechomwa moto huko South Beach.”

Sababu ya pili, hata kama wataamua kuhisi kuwa ni hicho ndicho marehemu alichowaeleza mashahidi hao, ni wazi maelezo hayo hayasababishi mshtakiwa yeyote kushtakiwa kwa kesi ya mauji kwa kuwa maelezo ya mashahidi hao yanatofautiana na ushahidi wa Saidi Kau Sahani ambaye ana uhusiano katika kesi hiyo.

Katika ushahidi wake, Sahani alisema, “Kuhusiana na mtu aliyemchoma moto mimi sifahamu ila nilisikia toka kwa Lila (marehemu) kuwa ni Mkurugenzi wa Hoteli aitwaye Chipata na Wahindi wa hapo Hoteli ya South Beach.”

Wakati Salum Ally, Sahani katika maelezo yao walienda mbali na kulitaja jina la mshtakiwa wa kwanza “Chipata” kuwa ni miongoni mwa watu waliomchoma moto marehemu, maelezo hayo yalileta mkanganyiko na sheria katika hali hiyo inasema kama kuna mashahidi wawili wanatoa ushahidi wa kusikia mtu akiwaelezea migogoro miwili tofauti kuwa hicho ndicho alichoelezwa na mtu huyo, basi ushahidi utakaotolewa na mashahidi wa aina hiyo hautakubaliwa na utakuwa hauna thamani.

“Kwa hiyo maoni yetu kutokana na ushahidi tuliouchambua kwenye jalada la kesi hii umesababisha ofisi ya DPP kuamini kuwa marehemu hakuwaeleza mashahidi hao yaani Ally na Sahani jambo lolote lilompata yeye na hivyo tunakubaliana na na ushahidi wa shahidi Fatuma Hussein ambaye ni dada wa marehemu ambaye alitoa maelezo yafuatayo polisi:
“Nilijaribu kumuuliza huyo mtu aliyemleta (yaani Saidi Kau Hassan) ilikuwaje naye akanijibu naye hajui lolote kwani naye alifuatwa na kijana aitwaye MBAVU (Salum Ally,) wakati huo huyo marehemu hakuweza kuniambia lolote zaidi ya kupiga kelele akiomba maji.”

Wakili Boniface alisema kabla ya marehemu kufariki alichukuliwa maelezo na G.5975 Pc Saidi ambapo marehemu katika tamko lake alisema alikwenda kucheza muziki South Beach Resort na kwamba mmiliki wa hoteli hiyo alimwita mwizi na akampiga kwa kutumia fimbo na kisha akamvalisha tairi na kumchoma moto.

Marehemu anadai kwamba ili kuiokoa ngozi yake alikimbia katika Bahari ya Hindi na katika tamko lake hilo alihitimisha kwa kusema hamfahamu ni nani aliyempeleka nyumbani kwao.

“Ofisi ilijiuliza kama kweli marehemu aliacha tamko ambalo linaungwa mkono na ushahidi wa PC Saidi ambaye ndiye aliyemchukua maelezo Lila kabla hajafa Aprili 10 mwaka huu saa 7:15 mchana kwa mtindo wa maswali na majibu ….. na PC Saidi wakati akimchukua maelezo Lila hospitalini alisema ‘…nilijaribu kumhoji kama anaweza kunieleza mkasa mzima uliompata alitoa maelezo yake kwa taabu sana…”

Wakili Boniface alisema pia baadhi ya mashahidi waliendelea kusema, “Ukweli maneno yake hayo aliyatoa kwa taabu sana huku akipoteza kumbukumbu sahihi ya alichokuwa anakieleza.”

“Sasa kwa mazingira yanayotatanisha namna hiyo ofisi ya DPP inaamini kulikuwa na uchelewaji wa kuchukuliwa tamko la marehemu hivyo kufanya tamko hilo kutokuwa na thamani kwa sababu halionyeshi ukweli wowote katika umakini hivyo kufanya tamko hilo kuonekana siyo la kweli …hivyo katika kesi hii hilo tamko la marehemu halina maana yoyote na tunakihesabu ni kipande kidogo sana cha ushahidi ambacho hakiifikishi mahali popote upande wa Jamhuri na hata ushahidi wa nyongeza haupo ndani ya jalada hilo na hivyo kufanya kesi hiyo kubakiwa na ushahidi wa mazingira tu ambao nao pia ni dhahifu,” inasema sehemu ya barua hiyo.

Aidha, alisema Ofisi ya Mwanasheria wa Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa maoni yake kuwa kuna haja ya kuendelea kwa kesi hiyo mahakamani kwa sababu mbili ambapo sababu ya kwanza ushahidi uliopo kwenye jalada hilo unatosheleza na sababu ya pili , kesi hiyo ilikuwa na maslahi kwa umma.

‘Ni kweli ofisi ya DPP inakubaliana na ofisi ya mwanasheria wa kanda , lakini ieleweke kwamba hicho mnachokiita maslahi ya umma peke yake bila ya kuwepo kwa ushahidi wa kutosha katika kesi hiyo kamwe haiwezi kuchukuliwa kuwa ni kigezo ambacho kitailazimisha ofisi ya DPP isiondoe kesi hiyo mahakamani,” alisema Wakili Boniface.

Hata hivyo, kufutwa kwa mashtaka hayo, hakuzuii kufunguliwa upya kwa kesi hiyo, iwapo utapatikana ushahidi mwingine makini unaoweza kuishawishi Jamhuri kufungua upya shauri hilo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Oktoba 21 mwaka 2011.

SERIKALI YAJICHANGANYA KESI YA MAHALU

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi wa zaidi ya euro milioni mbili, inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Prof. Dk. Costa Mahalu na Grace Martin, jana umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kuwa imepata nyaraka halisi za mawasiliano yaliyokuwa yakifanywa kati ya mshitakiwa huyo na serikali licha ya awali ulidai kutokuwa na nyaraka hizo.


Kesi hiyo ambayo jana ilikuwa imekuja kwaajili ya kuendelea kusikilizwa huku Wakili Mwandamizi wa Serikali, Ponsia Lukosi, akitarajiwa kuieleza mahakama amebaini nini kwenye zile nyaraka 11 zilizotolewa juzi na Prof. Mahalu ambaye aliomba zipokewe kama vielelezo, adala yake wakili huyo aliomba mahakama kabla ya kuvipokea, kesi hiyo iahishwe hadi jana ili upande wa Jamhuri uweze kupata nafasi ya kuzipitia nyaraka hizo.

Mbele ya Hakimu Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Elvin Mugeta , wakili Ponsian jana alishindwa kueleza amebaini nini baada ya kuvipitia vielelezo hivyo na matokeo yake akaomba kesi hiyo ihairishwe.

Sababu ya kuomba kuahrishwa kwa kesi hiyo ni kwamba, juzi wakati kesi hiyo inaendelea, aliletewa bahasha kubwa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambayo ndani yake kulikuwa na nyaraka kadhaa zikiwemo zile ambazo Prof. Mahalu alizitoa juzi mahakamani hapo kama vielelezo.

Kwamba vile vile ndani ya bahasha hiyo kulikuwa na barua iliyokuwa ikimjulisha kuwa serikali imeshapata nyaraka za mawasiliano yaliyokuwa yakifanywa kati ya Mahalu na Serikali ya Jamhuri ya Tanzania kuhusu ununuzi wa jengo la ualozi mjini Rome,Italia.

“Baada ya kupata ujumbe huo toka wizara ya Mambo ya Nje, nilifanya jitihada za kwenda wizarani hapo na kuendelea kukusanya nyaraka nyingine kwa jili ya kuja kuzilinganisha na nyaraka vivuli ambazo zinatolewa na Mahalu mahakamani kama vielelezo na kwa kuwa bado tunaendelea kukusanya nyaraka hizo na kesi hii imepangwa leo na kesho kwaajili ya mshtakiwa kuendelea kujitetea tunaona si busara kesi hii ikaendelea kusikilizwa,” alisema.

Wakili Lukosi aliongeza kuwa kwa sababu upande wa Jamhuri unaendelea kukusanya nyaraka hizo ambazo zimepatikana, wanaomba kesi iahrishwe kwa siku chache ili waweze kuzikusanya nyaraka zote.

Baada ya wakili Ponsian kutoa ombi hilo, wakili wa utetezi, Beatus Malima,alieleza mahakama kuwa hana pingamizi na ombi hilo.

Naye Hakimu Mugeta, alisema kwa kuwa hakuna uhakika hadi kufikia jana upande wa Jamhuri utakuwa umeishamaliza kukusanya nyaraka hizo na vile vile ilikuwa imepangwa kusikilizwa mfululizo kuanzia juzi, ana na leo, kwa sababu hiyo anaiahisha hadi Novemba 15,16,17 na 18 mwaka huu, kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa mfululizo.

Mapema mwaka huu, mawakili wa Mahalu na Martin;Mabere Marando, Alex Mgongolwa na Beatus Malima waliuandikia barua upande wa Jamhuri kuomba uwapatie nyaraka halisi ambazo wateja wao walikuwa wakikusudia kuzitumia kwa ajili ya kujitetea, lakini wakili wa serikali Lukosi kwa kujiamini mbele ya Hakimu Mugeta aliwajibu kuwa serikali haina nyaraka hizo na haiwezi kuwapatia.

Hatua hiyo ilimfanya Prof. Mahalu kupanda kizimbani kujitetea kwa kukutumia nyaraka vivuli na mahakama kulazimika kuzipokea kama vielelezo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Oktoba 20 mwaka 2011.

MAHALU AFICHUA BEI UNUNUZI JENGO LA UBALOZI ,ROME ITALIA


Na Happiness Katabazi
ALIYEKUWA balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa ripoti ya bei ya ununuzi wa jengo la Ubalozi wa Tanzania mjini Roma aliyokuwa ameipendekeza yeye ilikuwa ni ya bei ya chini ukilinganisha na ripoti ya ununuzi wa jengo hilo iliyokuwa imependekezwa na serikali kupitia Wizara ya Ujenzi.


Profesa Mahalu alitoa maelezo hayo jana mbele ya Hakimu Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Elvin Mugeta wakati mshtakiwa huyo anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi wa zaidi ya Euro milioni mbili akiongozwa na Wakili wake Mabere Marando, Alex Mgongolwa, Beatus Malima na Cuthebert Tenga kutoa utetezi wake.

Profesa Mahalu alidai kuwa mujibu wa kielelezo cha saba kilichotolewa na shahidi wa Jamhuri ambaye ni Mchunguzi toka TAKUKURU, hakijakamilika alidai kuwa kielelezo kile ni barua ya Februalia 2 mwaka 2002 ambayo akiwa Balozi aliandika yeye kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Kimataifa na nakala ya barua hiyo ilikwenda kwa Waziri wa wizara hiyo Jakaya Kikwete ambaye ni rais wa nchi kwa sasa, Waziri wa Fedha, Basil Mramba, Katibu Mkuu Kiongozi, Kamishna wa Bajeti Wizara hiyo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo akiwaarifu viongozi hao wa serikali kuhusu shughuli za ununuzi wa jengo la ofisi za Ubalozi mjini Roma,Italia hatua aliyofikia sasa ni ya kulipia jengo lenyewe ili liweze kuwa letu na hatimaye kuhamia na kwamba malipo ya jengo hilo kwa ujumla ni dola za Kimarekani 2,788,862.24 au Euro 3,098,741.38 sawa na Shilingi 2,534,770,448.80.

“Ni kweli barua hiyo iliyotolewa na shahidi huyo wa Jamhuri ilikishwapokelewa na mahakama hii kama kielelezo cha saba kweli kielelezo hicho ni barua ambayo niliandika mimi kwenda kwa mkuu wangu wa kazi lakini barua nilikuwa nimeambatanisha na viambatanisho kumi na moja vikiwemo ripoti tatu za uthamini wa majengo ambapo ripoti A ni ropiti iliyoandaliwa na Kaimu Mkurugenzi-Idara ya Majengo wa Wizara ya Ujenzi M.T.Kimweri, Ripoti B, ilikuwa ni ripoti ambayo ambayo nilikuwa nimeiandika kama balozi ambapo nilipendekeza jengo hilo linunuliwe kwa gharama ya dola za Kimarekani milioni 2.7 sawa na Sh bilioni 2.5 ambayo mwisho wa siku ndiyo ilikuja kutumiwa na serikali kununulia jengo jipya la Ubalozi na ripoti C, ilikuwa ni ya mwenye jengo F.Morelli, viambatanisho hivyo havimo kwenye barua hiyo”alidai Profesa Mahalu.

Alieleza kwa mujibu wa safari ya Roma nchini Italia ya Julai 15-26 mwaka 2001 iliyoandaliwa na Kimweri toka Wizara ya Ujenzi baada ya kuyachunguza majengo matatu la Via Colli della, Via Continad ‘ Appezo 185-Rome ambapo kila jengo lilikuwa likiuzwa kwa dola za kimarekani milioni tatu wakati jengo la Via San Marno 25 Rome ambalo lilikuwa likiuzwa kwa dola za Kimarekani milioni 2.25 ambapo katika ripoti yake baada ya uchunguzi huo , Kimweli alitoa mapendekezo yake akiitaka serikali ikubali kununua jengo la Via Continad’ Apezzo 185-Roma kama itashindikana kulinunua hilo jengo la Via Colli della 128-Roma kwa kuwa majengo hayo yapo maeneo mazuri.

Hata hivyo kwa mujibu wa barua hiyo ya Mahalu kwenda kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, yeye alipendekeza jengo hilo la Via Continad Appezzo 185 –Rome ninunuliwe kwa bei ya chini ya jumla ya dola za kimarekani 2,788,862.24 sawa na Shilingi 2,534,770,448.80 ambazo serikali ilizilipa kwa awamu kwa mmiliki wa jengo hilo F.Morelli.

“Kwa kuwa mimi ndiyo mwandishi wa barua hiyo ,ndiyo ninayefahamu wakati naituma barua kwa viongozi wangu wa serikali nilikuwa nimeambatanisha na viambatanisho vyote hivyo ambapo nashangaa shahidi ametoa barua hii pekee yake bila viambatanisho hivyo na kushindwa kwake kuleta viambatanisho hivyo hapa mahakamani ambapo mimi ninazo nakala ya hivyo viambatanisho na ninaiomba nivitoe hivyo viambatanisho kama vilelezo mahakamani”alidai Profesa Mahalu.

Hata hivyo baada ya Mahalu kuomba viambatanisho hivyo mahakama hiyo ivipokee kama vielelezo , Wakili Mwandamizi wa Serikali Lukosi ,ghafla aliomba mahakama iarishe kesi hiyo hadi leo ili waweze kupata nafasi ya kulinganisha viambatanisho vivuli hali iliyosababisha hakimu Mgeta kumhoji wakili huyo wa serikali kuwa anaenda kulinganisha viambatanisho hivyo na nyaraka zipi kwasababu hapo awali Jamhuri ilishasema haina nyaraka halisi za nyaraka hizo anazozitumia Mahalu katika utetezi wake kwasababu serikali siyo mwandishi wa barua hiyo hali iliyosababisha wakili huyo kujibu kuwa wanaomba muda ili waweze kwenda kuzipitia nyaraka hizo na siyo kwenda kuzilinganisha(cross check).

Hakimu Mgeta alikubali ombi hilo la kuarishwa kwa kesi hiyo akaiarisha kesi hiyo hadi leo saa tatu asubuhi.

Chanzo; Chanzo Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Oktoba 19 mwaka 2011.

TAHADHARI YA BABU WA LOLIONDO


Na Happiness Katabazi
JUMATATU wiki hii gazeti moja siyo Tanzania Daima, lilimnukuu aliyekuwa Mchungaji wa Kanisa la Kiinjiili la Kilutheli nchini(KKKT), Ambilikile Mwasapile akisema kuwa wananchi wajiandae kupokea muujuzi mpya kutoka kwake.


Mwasapile kwa jina maarufu ‘Babu wa Loliondo’ pamoja na kutoa ahadi hiyo pia aliwashutumu baadhi ya viongozi wa makanisa na waganga wa kienyeji ambao wamekuwa wakikimbiwa na wateja wao kuwa ndiyo wamekuwa wakimchafulia jina lake.

Sote tungali tukikumbuka kuwa mapema mwaka huu maelfu ya watanzania na raia wa kigeni waliliminika katika makazi ya babu huyo kule Kijijini Samunge mkoani Arusha kwaajili ya kupatiwa tiba ya magonjwa sugu iliyokuwa ikitolewa kwa gharama ya Sh 500/- na babu huyo ambapo babu huyo aliwaaminisha wagonjwa hao kuwa dawa yake inawaponya wagonjwa waliokuwa na imani na haitawaponya wagonjwa ambao hawatakuwa na imani.

Binafsi sina taaluma ya kitabib, mahabara wala siyo mtumishi wa dini hivyo ndiyo maana sitaki kukubali kwamba dawa ya babu huyo kuwa haikuwaponya au imewaponya wagonjwa waliokunywa dawa yake ‘Kikombe cha Babu’ kwasababu kati ya watu watano ambao ninawafahamu na waliniaga wakati wanakwenda kunywa dawa kwa babu huyo, hadi leo wameshindwa kunieleza wamerudi mahabara na kupimwa na kukutwa maradhi yaliyokuwa yakiwasumbua yametoweka.

Vyovyote iwavyo, Mtazamo wangu wa leo si kutaka kupingana na ahadi ya babu aliyoitoa mapema wiki hii kuwa wananchi wajiandae kupata muujiza mpya kutoka kwake, la hasha mibinafsi baada ya kusikia ahadi hiyo ya Babu wa Loliondo nimebaki kujiuliza je muujiza huo unaotarajiwa kutolewa na babu huyo, Je muujiza huo utolewa kwa njia ya dawa ya mitishamba ambayo itawalazimu wahusika kuitumia kwanjia ya kuinywa?
Basi kama muujiza unaotarajiwa kutolewa na Babu wa Mwasapile atautoa kwa njia hiyo ya dawa, tafadhali sana kabla ujaanza kutoa dawa hiyo nakuomba uwaite faragha watafiti watatifi wa madawa toka taasisi za serikali ili uwaeleze ili waweze kuifanyia utatifi kwanza kabla ya wewe kuanza kutoa huduma hiyo kwa wananchi.

Kwani tungali tukikumbuka kuwa dawa yako ya awali”kikombe cha babu’ ulianza kuwapatia wagonjwa na wakanywa kabla haijafanyiwa utaifiti na wataalamu wa Taasisi ya Utafiti NIMR na Taasisi cha ya Chakulia na Dawa, wagonjwa walipojitokeza kwa wingi ndipo serikali kupitia taasisi hizo nazo zikafunga safari na kwenda kuchukua sampo za dawa ya babu huyo na kwenda kuifanyia utafiti kama inafaha kwa matumuzi ya binadamu.

Itakumbukwa kuwa mengi yamesemwa kuhusu dawa hiyo ya babu kuwa dawa hiyo haitibu na imesababisha wagonjwa wengi kupoteza maisha yao, binafsi sina ushahidi na hilo.

Ila angalizo langu kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuwa nayo imeshamsikia babu wa Loliondo akijinasbu kuwa anatarajia kutoa muujiza mwingine, ni vyema basi ikawatuma kimya kimya maofisa wake kwenda kuzungumza na babu huyo ili awaeleze mapema ni muujiza wa aina gani anatarajia kuutoa na utawalenga wananchi wa makundi gani.

Ili serikali iweze kujipanga sasa kuweza kutoa msaada wake pindi itakapoitajika kutoa msaada pindi muujiza huo utakapoanza kutolewa kwani ikumbukwe kuwa muujiza huo unahusu maisha ya watanzania na Kikatiba kila Mtanzania ana haki ya kuishi na kila mwananchi ana haki ya kulindwa.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika
0716 774494
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Oktoba 18 mwaka 2011.

KORTI YAAMURU RAMA AKAPIMWE AKILI

MAHAKAMA Kuu Dar es Slaam imeamuru mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya mauaji ya kukusudia, Ramadhani Selemani, aliyekutwa akitafuna kichwa cha mtoto eneo la Hospitali ya Taifa Muhimbili, akapimwe akili.

Ramadhani na mama yake mzazi Hadija Ally wanashtakiwa kwa kosa la mauaji ya kukusudia ya mtoto Salome Yohana (3) eneo la Tabata jijini Dar es Salaam.
Kesi hiyo ilitarajiwa kuanza kusikilizwa kwa washtakiwa kusomewa maelezo ya awali ya mashtaka yao (PH) lakini ilishindikana baada ya wakili wa washtakiwa hao Yusufu Shehe kuiomba mahakama iamuru mshtakiwa huyo akapimwe akili.

Mheshimiwa Jaji, kulingana na ushahidi wa kesi hii, chini ya kifungu cha 219 (1) Sura ya 20 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), inaiomba mahakama yako iruhusu mshtakiwa wa kwanza akapimwe akili zake kwanza.

Alisema ameamua kutoa ombi hilo ili kujiridhisha na utimamu wa akili za mshtakiwa kwanza kabla ya kuanza usikilizwaji wa kesi hiyo kulingana na kumbukumbu za maelezo ya ushahidi ulioko.

Hata Hivyo Wakili Shehe alibainisha kuwa anakusudia mshtakiwa huyo apimwe akili kwa wakati ule tu aliotenda kosa analoshtakiwa kwalo na si kwa wakati mwingine wowote.
Wakili wa upande Jamhuri (mashtaka) Dionisia Saiga akisaidia na Wakili wa Serikali Nassoro Katuga, alisema kuwa kulingana na ushahidi wa kesi hiyo hata wao hawana pinagmizi dhidi ya ombi la wakili wa utetezi kwa mshtakiwa huyo kupimwa akili.

Baada ya kusikiliza pande zote Jaji Karua alikubaliana na ombi hilo la wakili wa utetezi na kutoa amrim rasmi mshtakiwa huyo akapimwe akili kabla ya kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo.

Hivyo Jaji Karua aliahirisha kesi hiyo hadi itakapopangwa tarehe nyingine ya kuendelea nayo katika awamu nyingine ya vikao vya mahakama vya kesi za jinai.
Kabla ya kutoa ombi la mshtakiwa kupimwa akili, Wakili Shehe aliomba mahakama iliamuru atafutwe wakili mwingine kwa ajili ya kumtetea mmoja wa washtakiwa katika kesi hiyo.
Wakili Shehe ambaye alikuwa akiwatete washtakiwa wote wawili katika kesi hiyo alisema kwa mazingira ya kesi hiyo na ushahidi yakiwemo maelezo ya washtakiwa asingeweza kuendelea kuwatetea wote.
Moja ya maelezo ambayo yalimsukuma Wakili Shehe aombe atafutwe wakili mwingine kwa ajili ya kumtetea mmoja wa watuhumiwa hao, ni yale ya mshtakiwa wa kwanza, Ramadhani kumsukumia mama yake mzigo kuwa ndiye aliyefanya mauaji hayo.

Hata hivyo mama yake Ramadhani naye anakana tuhuma hizo akidai kuwa siyo yeye aliyemuua mtoto huyo, maelezo ambayo pia yanaashiria kuwa anamwachia mzigo huo mwanaye Ramadhani, aliyekutwa na kicha cha mtoto huyo.

Mahakama ilikubaliana na ombi hilo la wakili wa utetezi na kuamuru atafutwe wakili mwingine kwa ajili ya kumtetea mshtakiwa mwingine, kabla ya kesi hiyo haijapangiwa tarehe nyingine ya kuanza kusikilizwa.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo
Ramadhan alikamatwa na mlinzi wa Hospiltali ya Muhimbili Furgence Michael akiwa na kichwa cha mtoto huyo kikiwa kimesukwa nywele, April 26, 2008, akidai kuwa alikuwa anampelekea zawadi muuguzi mmoja wa hospitali hiyo.Kichwa hicho kilikuwa ndani ya mfuko wa nailoni aina ya Rambo huku akikitafuna hadharani huku akidai kuwa alikuwa amezoea kula nyama za watu yeye na bibi yake.

Tukio hilo liliwafanya wafanyakazi wa hospitali hiyo na watu wengine waliofika hospilatini hapo kwa sababu mbalimbali kuacha shughuli zao na kwenda kumshuhudia kijana huyo akitafuna kichwa hicho

Hata hivyo walimweka chini ya ulinzi mkali, na kutoa taarifa polisi ambapo baada ya polisi kufika walimuhoji akadai kuwa alikuja na bibi yake anayeishi makaburi ya Jeti Lumo na kwa bahati mbaya wamemuacha na wao wamepaa na ungo.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala Kanda Maalum Dar es Salaam, Faustine Shilogile alisema kuwa Ramadhan amekuwa akipatikana kwenye matukio tofauti ya ajabu na wanaendelea kumchunguza kutokana na matukio hayo.
Kabla ya mwili na kichwa chake kupatikana mahali tofautotofauti mtoto Salome alipotea muda wa saa 2 usiku April 25 akiwa nyumbani kwa shangazi yake Furaha Majani (28), anayeishi Segerea kwa Bibi.

Mtoto huyo alifika kwa shangazi yake hapo akiwa na wazazi wake, baba yake Yohana Majani na mama yake Upendo Datsun, wakazi wa Kimara, kwa ajili ya kumtembelea shangazi yake huyo.Baada ya kubaini kuwa mtoto huyo alikuwa amepotea katika mazingira ya kutatanisha walitoa taarifa kituo cha polisi baada ya kumtafuta kwa ndugu na jamaa bila mafanikio.Baadaye kiwiliwili cha mtoto huyo kiliokotwa ndani ya shimo la choo kikiwa kimekatwa kichwa na wazazi walitambua kuwa ni kiwiliwili cha mtoto wao.Baada yakupata taarifa za Ramadhani kukamatwa Muhimbili akiwa na kichwa cha mtoto, wazazi hao walifika hospitalini hapo na walikitambua kichwa hicho kuwa ni cha mtoto wao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Daima, Oktoba 5 mwaka 2011.

TANESCO IMEVUNA ILICHOPANDA DOWANS

Na Happiness Katabazi
SEPTEMBA 28 mwaka huu,Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, Emilian Mushi alitoa hukumu ya kihistoria ambayo ilikata ngebe ya vizabinazabina ambao ni baadhi ya wanasiasa na wanaharakati waliokuwa wakifanya harakati za kulizuia Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO), kulipa tuzo ya mabilioni ya shilingi kwa Kampuni ya kufua umeme, Dowans Tanzania.


Tuzo hiyo ya dola za Marekani milioni 65 (takriban sh bilioni 94) iliyotolewa Novemba 15, mwaka jana (2010); na Januari 25, mwaka huu, Dowans iliwasilisha ombi lake la kutaka Mahakama Kuu ya Tanzania iisajili tuzo waliyopewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa migogoro ya Kibiashara (ICC).

ICC iliitia hatiani TANESCO kwa kosa la kuvunja mkataba na Dowans iliyokuwa ikitetewa na wakili wa kimataifa Kennedy Fungamtama, na ikaiamuru iilipe tuzo hiyo na riba ya asilimia 7.5.

Lakini wanaharakati kadhaa na wanasiasa hapa nchini wamekuwa wakipinga uamuzi huo wa ICC mahakamani.Jaji Mushi alisema Mahakamu Kuu ya Tanzania haina mamlaka ya kutengua hukumu ya ICC.

Hatua hiyo ya wanasiasa na wanaharakati kuchelewesha malipo ya tuzo hiyo itaifanya TANESCO kulipa kiasi kikubwa zaidi kwani riba imekuwa inaongezeka. Hadi siku hukumu inatolewa na Jaji Mushi Dowans ilikuwa inastahili kulipwa na Tanesco Sh bilioni 113 badala ya sh bilioni 94 kutokana na ucheleweshwaji huo.

Jaji Mushi alianza kwa kusema maneno yafuatayo:

“Kwanza, naishukuru TANESCO na zile taasisi nne za wanaharakati waliokuwa wakiongozwa na LHRC; walijitokeza mahakamani hapa kupinga tuzo ya Dowans isisajiliwe na kutumia muda wao kuchambua kesi mbalimbali na kuandaa mapingamizi yao, ambayo hata hivyo niliyatupilia mbali.

“Pili, nafahamu fika kuwa kesi hii ya Dowans ina sayansi nyingi sana za kisiasa, hivyo napenda niwafahamishe mapema kabisa kabla ya kuendelea kuwa hukumu yangu nitakayotoa leo haijatoa nafasi kwa sayansi hizo za kisiasa, kwa sababu imezingatia misingi ya sheria na haki.”
Jaji Mushi alisema baada ya kuipitia hukumu ya ICC amebaini kuwa haina makosa ya kisheria kama anavyodai mlalamikaji, na ndani ya hukumu hiyo alikuta kiambatanisho ambacho ni mkataba kati ya TANESCO na Dowans uliosainiwa Juni 23, mwaka 2006; na kufafanua kwamba pande zote mbili katika mkataba huo zilikubaliana kwamba uamuzi wa ICC ndiyo utakuwa wa mwisho, na utazibana pande zote mbili na hautaweza kukatiwa rufaa.

Jaji huyo alisema kifungu cha 14 (f) cha mkataba huo kinasomeka hivi: “The parties waive any right to challenge or contest the validity or enforceability of this arbitration agreement or any arbitration proceeding or award brought in conformity with this section.” Kwa tafsiri nyepesi, Fungamtama alisema kifungu hicho kinasema, TANESCO na Dowans katika mkataba wao walikubaliana kwa maandishi kuweka kando haki za kupinga au kuhoji mwenendo na tuzo zitakazotolewa na baraza la usuluhishi.

Jaji akasema: “Sasa kwa mujibu wa mkataba huo ni wazi kuwa TANESCO na Dowans walikubaliana kuwa endapo utatokea mgogoro baina yao utapaswa upelekwe ICC tu na ICC itakapotoa hukumu ya mgogoro baina yao, pande hizo mbili hazitakuwa na mamlaka ya kuikatia rufaa hukumu hiyo ya ICC.

“Kwa makubaliano hayo ya pande hizo mbili ndani ya mkataba huo wa POA ambao TANESCO hadi wanakwenda kujitetea ICC hawakuwa wameuvunja huo mkataba wa POA na kupitia mkataba huo ICC pia iliutumia kutolea uamuzi wake…ni wazi kabisa mahakama hii inakubaliana na hukumu ya ICC kuwa ilikuwa ni hukumu ya haki na iliyofuata sheria na ilizingatia pia masilahi ya sera za Tanzania na kwakuwa pande hizo zilikubaliana hukumu ya ICC hawataweza kuikatia rufaa basi ndivyo hivyo hivyo mahakama hii ya Tanzania haiwezi kutoa uamuzi wa kutengua hukumu hiyo iliyotolewa na ICC.”alisema Jaji Mushi.

Alisema anakubaliana na hoja ya wakili wa Dowans, Fungamtama, kuwa kifungu cha 3 cha jedwali la 3 katika Sheria ya Usuluhishi ya Tanzania, Sura ya 15 ya mwaka 2002 ambacho kinasomeka hivi: Kwa tafsiri rahisi, kifungu hicho utaona tayari nchi imejifunga mikono na utekelezaji wa hukumu zinazotolewa na mahakama za kimataifa kwa sababu ni nchi yetu yenyewe imeridhia sheria na mikataba ya kimataifa.

Jaji Mushi alisema kitendo cha TANESCO kuwasilisha ombi mbele yake likidai kuwa Mahakama Kuu haina mamlaka ya kusajili tuzo hiyo, halina ukweli na kwamba mwanasheria aliyefahamu vema Sheria ya Usuluhishi ya Tanzania ya mwaka 2002 Sura ya 15, Mikataba ya Kimataifa na Sheria ya Makosa ya Madai ya mwaka 2002 ataona wazi kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania imepewa mamlaka ya kusajili tuzo hapa nchini zinazotolewa na Mahakama za Kimataifa.

Jaji alisema hoja ya TANESCO kuwa mwenendo wa hukumu ya ICC ulikuwa na mapungufu ya kisheria, haikupaswa kupelekwa mbele yake kwani Tanasco walikuwa ni wadaiwa katika kesi iliyofunguliwa ICC na walipaswa kuiwasilisha hoja hiyo ICC kabla ya mahakama hiyo ya kimataifa kutoa hukumu yake na kuikumbusha TANESCO kuwa ni yenyewe iliyoingia mkataba wa POA na Dowans ambao kwa ridhaa yao waliridhia kuwa hukumu itakayotolewa na ICC haitakatiwa rufaa.

Kutokana na makubaliano ya pande hizo mbili, Jaji Mushi aliishangaa TANESCO kwa hatua yake ya kuwasilisha hoja hiyo ambayo ni wazi ilipaswa iwasilishwe kwenye mashauri ambayo yamekatiwa rufaa na kwamba shauri lilokuwa mbele yake halikuwa shauri la rufaa.

Aidha Jaji Mushi alihitimisha kwa kusema kuwa anakubali ombi la Dowans la kusajili tuzo waliyopewa na ICC isajiliwe na mahakama ya Tanzania. Pia aliiamuru TANESCO kulipa gharama zote za uendeshaji wa kesi hiyo, na Dowans ianze taratibu za kukazia hukumu ya Mahakama ya ICC.

Awali ya yote napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa Mahakama Kuu ya Tanzania kupitia Jaji Mushi, kwani kupitia hukumu ya kesi hiyo kudhiirisha wazi bado tuna majaji majasiri ambao hawayumbishwi na makelele ya wanasiasa wahuni ambao walikuwa wakifikiri kupitia nyadhifa zao wangeweza kuiweka mfukoni mhimili huo wa mahakama ili uweze kutoa uamuzi wanaotuka wao katika kesi hiyo ya Dowans dhidi ya Tanesco.Hongera sana Jaji Mushi.

Napenda wasomaji wa makala hii wafahamu kuwa mimi nilikuwa ni miongoni mwa waandishi wa habari wa chache hapa nchini tuliyoifuatilia kwa karibu kesi hiyo kabla haijafunguliwa, ilipofunguliwa, ilipokuwa ikiendeshwa na hadi hukumu ilipotolewa Alhamisi wiki hii.

Nakumbuka baada ya kufikishwa kwa hukumu ya ICC katika Mahakakama Kuu ya Tanzania, waandishi wa habari za mahakama tulikuwa tunapata wakati mgumu wa kupata ufafanuzi wa jinsi ya ombi hilo la kusajiliwa kwa tuzo lakini mwisho wa siku kwa busara ya uongozi wa mahakama ulitenga utaratibu uliotuwezesha sisi kuwa tunapata habari kuhusu kesi hiyo.Tunashukuru kwa hilo.

Sasa basi kwa muktadha huo hapo juu wa baadhi ya maneno yaliyopo kwenye hukumu hiyo, sote tutakubaliana na Jaji Mushi kuwa kesi hiyo ilikuwa imegubikwa na siasa zilizokuwa zikiendeshwa na baadhi ya wanasiasa manyang’au, wakorofi ambao wanafahamu fika nchi yetu inafuata sheria lakini kwa makusudi wakaamua kutumia nyadhifa zao kuamasisha umma ushiriki katika mzozo huo wa Tuzo ya Dowans isisajiliwe eti kusajiliwa kwa Dowans ni ufisadi mkubwa.

Kwa maneno machache hayo hapo juu ambayo yanapatikana kwenye hukumu ya Jaji Mushi, binafsi nampongeza Jaji Mushi kwa ujasiri wake wa kutoa hukumu hiyo ambayo nyuma ya kesi hiyo ilikuwa imegukibwa na magomvi ya siasa chafu hasa za wanasiasa wa CCM na baadhi ya taasisi za wanaharakati ambao hata nakala ya ICC na mkataba wa POA naimani hawakuzisoma kwa makini na kujua ziliandikwa nini kwani wangekuwa wamesoma, katu wasingekuwa wanabwatuka na kwenda kuipinga Tuzo ya Dowans mahakamani.

Hivyo basi utekelezwaji wa hukumu hiyo itatekelezwa kwa kuchukuliwa kodi za wananchi wa Tanzania na kisha kuilipa Dowans. Lakini chanzo cha uwendawazimu wote ni makundi yanayohasimiana ndani ya CCM ambayo yalifanikiwa kuuteka umma wa Tanzania uwange mkono katika harakati zao za kuikashfu kampuni Richmond na Dowans na kweli harakati zao zilifanikiwa kwani taifa likajikuta linaingia kwenye malumbano makali kuhusu kulipwa kwa kampuni hiyo.

Kumbe nyuma ya pazia ya wanasiasa hao wa CCM ilikuwa ni chuki zao za kibiashara na siasa ambazo pia zinadaiwa ndizo zilizoisukuma Tanesco kuyumba kitaaluma na kimaamuzi na matokeo yake ikajikuta inavunja mkataba na Dowans kwaajili ya kelele hizo za wanasiasa manyang’au.

Kwahiyo hapa hoja ya Tanesco haiwezi kulipa kiasi hicho cha fedha haina msingi wowote ,kwani kushindwa kwao kusimamia maslahi ya taifa matokeo yake ikajikuta inafanya kazi na kutoa maamuzi kwaajili ya kuwafurahisha wanasiasa manyang’au ndiko kulikosababisha leo hii fedha za walipa kodi zitumike kuilipa dowans?

Inakuwaje ni Tanesco ndiyo ilikuwa ya kwanza kuvunja mkataba halafu ikashtakiwa na hukumu ilivyotolewa ndiyo ikurupuke kutoa maneno matamu ya kuhadaa umma kuwa kulipwa kwa fedha hizo kutaifanya Tanesco ifilisike?Tuiulize Tanesco wakati ikitenda kosa hilo la kuvunja ule mkataba kwa mashiniko ya kisiasa mwisho wa siku ilitegemea Dowans iwafanye nini kama siyo kuwashtaki?

Ieleweke wazi Tanzania ni nchi inayoendeshwa kwa misingi ya sheria na kila siku Jaji Mkuu Mstaafu Agustino Ramadhani amekuwa akisema haki ni gharama.Kwahiyo katika hili Tanzania hatuna budi kugharimika kwa kuilipa Dowans kiasi hicho mabilioni ya shilingi.

Na nipende kutoa taadhari kwa Tanesco ule mkataba waliousaini wa POA na Dowans na kitendo chao cha kuvunja mkataba na Dowans kabla ya muda, kuendesha mambo hayo kwa matakwa ya kelele za wanasiasa manyang’au ndiko kuliko tukifisha leo hii.

Lakini Tanesco wanawafanya Watanzania wote ni mazuzu wasioshindwa kung’amua kuwa matendo hayo waliyoyatenda hapo na hatua yake ya kuwakodi mawakili wa kujitegemea toka kampuni ya FK Chamber, Rex Attoney kulitetea shirika katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro(ICC), Mahakama Kuu ya Tanzania, kunaendelea kuteketeza fedha za walipa kodi kwa kisingizo cha kutoa fedha za umma kuwalipa mawakili hao wa kujitegemea wakati mawakili wa serikali tena wazuri tu wapo.

Kwa sisi tunaowafahamu hulka na tabia za mawakili wengi wa kujitegemea ,cha kwanza wanapenda fedha toka kwa mteja wao na uwa wanatabia za kama za matapeli za kuwahada wateja wao kuwa nilazima watashinda kesi inayomkabili mteja wake huku akijua wazi na akikaa pembeni ya watu wa mbali na mteja huyo anasema kesi inayomkabili mteja wake ni ngumu na watashindwa ila anachokifanya ni kuchukua fedha na kumfariji mteja wake kuwa atashinda.

Kwa hiyo Idara ya Usalama wa Taifa(TISS), iamke usingizi na kuwatumia hata wanasheria wake kuzisoma hizo nakala za hukumu za ICC na mahakama kuu ya Tanzania na ule mkataba wa POA na pia iwachunguze hao mawakili wakujitegemea waliopewa tenda ya kuitetea Tanesco tangu ICC, Mahakama Kuu na aliyewapa tenda hiyo, wanatumia taaluma zao kikweli kweli au wapo hapo kwaajili ya kutafuna tu fedha za walipa kodi na kuwaada wananchi huku wakijua moyoni kesi hiyo hatutaweza kushinda?

TISS ikishabaini ukweli pia ikachunguze katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni kweli kabisa hatukuwa na wanasheria wa serikali ambao nao wangepewa fursa ya kuendesha kesi hiyo tangu ICC na Mahakama Kuu? Na endapo itabaini ni ngumu Tanesco kushinda rufaa katika Mahakama ya Rufaa, ni vyema iikataze Tanesco kukata rufaa mahakama ya rufaa kwani fedha zetu zitaendelea kutafunwa bure na mawakili na gharama za liba ya kuilipa Dowans zitakuwa zimeongezeka maradaufu.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Fredrick Werema, Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja hakuwa wapumbavu walivyojitokeza adharani siku za nyuma kusema ni lazima Dowans ilipwe licha baadhi ya wanasiasa na waandishi wa habari ambao ni mambumbu wa sheria waliwakejeli.

Werema na Ngeleja na wengineo walikuwa wakijua wanachokisema kwasababu ni wanasheria wazuri waliobobea katika fani hiyo.Na walichokisema ndicho kilichokuja kuamuliwa na mahakama kuwa tuzo ya Dowans isajiliwe.

Na cha kustajaabisha kabisa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta na aliyekuwa Spika na kundi lake ambalo ndilo lilikuwa mstari wa mbele kutoa kauli za kuamasisha umma tuamini kuwa kampuni ya Richmond, Dowans ni kampuni za mafisadi na mikataba iliyoingiwa na Tanesco ivunjwe na leo hii wamekaa kimya utafikiri hawaishi Tanzania.Zile taasisi za wanaharakati ambazo ziliandaa maandamano ya kupinga Dowans isilipwe nazo leo hii baada ya hukumu kutolewa, hawasikikiti tena utafikiri wameaga dunia.

Hakuna ubishi yale malumbano ya visasi na kusingiziana kuhusu kampuni ya Richmond,Dowans na baina ya baadhi ya viongozi wa kisiasa hususasi wale wa CCM kuhusu mikataba ya makampuni hayo, kama serikali yetu isingekuwa imara, ni wazi leo hii taifa hili lingekuwa limeingizwa mtoni na malumbano hayo ambayo yalikuwa yanachagizwa kwa kiasi kikubwa na sisi vyombo vya habari bila kujua kilichopo nyuma ya ajenda hiyo ya malumbano.

Ieleweke wezi kuwa Tanzania itabaki kuwa nchi yetu na hao wanasiasa manyang’au ambao wamekuwa wakitumia ushawishi wao wa kisiasa kuutumia umma usifahamu kilichopo nyuma ya pazia ya ajenda chafu zao , watapita na kusaulika.

Hivyo nitoe rai kwa viongozi wetu wa siasa, taasisi za wanaharakati, vyombo vya habari na wananchi kuwa hukumu ile ya ICC na ile ya Mahakama Kuu ya Tanzania iwe funzo kwetu kuanzia sasa tukatae kugeuzwa makasuku wa ajenda chafu za wanasiasa hasa wa CCM na wale vyama vya upinzani kwani tukikubali kuwa makasuku wa ajenda za manyang’au mwisho wa siku tukubali matokeo kama haya ya kutakiwa na mahakama kuilipa fidia Dowans ya zaidi ya dola za kimarekani bilioni 111. Na tutakapotakiwa na mahakama kufanya hivyo tusikasilike, tufurahi kwani tuliyataka wenyewe.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika
0716 774494
Chanzo:Gaazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Oktoba 2 mwaka 2011.

RAIS KIKWETE TANGAZA VITA DHIDI YA UGONJWA HUU


Na Happiness Katabazi

JUMATATU ya wiki hii mimi na mwandishi mwenzangu wa habari za mahakamani Regina Kumba(Habari Leo), tulikwenda Wodi ya watoto wenye maradhi ya vichwa vikubwa vilivyojaa maji kitaalamu unajulikana kama Hydrocethalus katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwaajili ya kumjulia hali mwanataaluma mwenzetu(jina naliifadhi) ambaye mtoto wake mchanga amelazwa katika wodi hiyo akisumbuliwa na maradhi hayo.


Tulipofika hapo tulimkuta mwanataaluma mwenzetu akiwa na mama yake mzazi na mtoto wake ambaye tayari ameishafanyiwa upasuaji wakiendelea kumuuguza kichanga hicho. Tuliwajulia hali na kuwafariji na kwakweli walishukuru madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo wanajitahidi kadri ya uwezo wao kutoa matibabu mazuri kwa watoto waliolazwa wodi hapo kwaajili ya matibabu.Nifarijika sana na kauli hiyo.

Pia nilishuhudia nje ya wodi hiyo ndugu na jamaa hasa wanawake wakiwa wamekaa chini ya miti na watoto wao wenye maradhi yao wakipunga upepo na kubadilishana mawazo na ndugu na jamaa zao waliofika hapo kwaajili ya kuwajulia hali.

Pia kwa macho yangu niliwashuhudia watoto zaidi ya saba ambao wanasumbuliwa na maradhi hayo wakiwa wamepakatwa na wazazi wao na watoto wengine wakiwa wamekarishwa kwenye baiskeli za walemavu wakipunga upepo na kunywa vinywaji baridi.

Niwe muwazi baada ya kuishuhudia hali hiyo kwa macho, nilijisikia uchungu, mwili ulisisimka, nikakosa raha na nikajiuliza swali moja moyoni , hivi wale watoto wamekosa nini kwa mungu?Lakini nikaishia kwakumaliza kwa kujibu mwenyewe kimoyo moyo kuwa yote hayo yanayowapata watoto hao ni mipango ya mungu.

Tatizo hilo lilinilazimu kuwasiliana na baadhi ya madaktari kuwauliza chanzo hasa cha tatizo hilo ni nini lakini ili kama wazazi wakiwa wajawazito au watoto waliozaliwa wakiwa wazima lakini baada ya muda wakaja kupata tatizo hilo, wachukua hatua gani za taadhari ili waweze kujiepusha na janga hilo, kwa kweli madaktari hao wanne walishindwa kunipatia jibu.

Hivyo basi kutokana na kushuhudia hali hiyo nikiwa kama mama, mwanahabari nimelazimika kuandika mtazamo huu kuiamasisha serikali, sekta binafsi na sisi waandishi wa habari na wanajamii wengine kila mmoja kwa nafasi yake kuona wakati umefika sasa kwa taifa letu kuanza vita ya kuutokomeza ugonjwa huo ambao unawasumbua watoto wengi wasiyokuwa na hatia.

Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii walifanikiwa kusaka fedha za miradi waliyoibuni ya kutokomeza ugonjwa wa ukimwi na wakaupa kauli mbiu isemayo ‘Tanzania bila ukimwi inawezekana’, mradi wa kutokomeza maralia ambapo kaya nyingi zilipewa vyandarua kwaajili ya kuzuia mbu wasiwaambukie maralia, mradi wa afya ya uzazi salama kati ya mama na mtoto na miradi mingine mingi tu ambayo ilipata mwitikio mkubwa na jamii.

Tena kupitia mradi wa kampeni ya afya ya uzazi salama kutoka kwa mama na mtoto imesababisha taasisi mbili za nchini Marekani wiki iliyopita kumtunukia tuzo mbili kwa mpigo rais Jakaya Kikwete tuzo kwa kazi nzuri ya kusimamia kampeni hiyo.

Na situ serikali imekuwa ikiendesha kampeni kama hizo za kutokomeza magonjwa kadhaa, pia taasisi nyingine za kiraia nazo zimekuwa zikipambanua kuyapiga vita baadhi ya maradhi kama Saratani ya matiti kwa wakina mama na kweli kampeni hizo zimekuwa zikifanikiwa kwasababu ya wasamalia wema kujitokeza kuchangia fedha katika miradi hiyo na hatimaye waathirika wa maradhi hao wanafuatwa walipo na kupatiwa tiba.Napongeza katika hili.

Lakini kuhusu ugonjwa huo wa watoto kujaa vichwa maji,kimsingi tukubaliane kuwa jamii yetu ya Tanzania, bado hatutaki kutambua ugonjwa huu kadri siku zinavyozidi kwenda idadi ya watoto wanaopata tatizo hilo wanaongeza, na si viongozi wa kitaifa, dini, kijamii wala sisi vyombo vya habari hatujajitokeza adharani kupaza sauti au kutoa misaada ya kuwezeshwa kupanuliwa kwa wodi au kujengwa hospitali maalum kwaajili ya watoto wenye matatizo hayo au Taifa kuamua kufanya kampeni ya ama ya kuutokomeza au kuuzuia ugonjwa huu usiwapate watoto wetu.

Ndiyo maana nasema ushawishi ule ule uliotumiwa na serikali ya Kikwete kuomba fedha kwa wafadhili au kuchukua fedha kwenye bajeti ya serikali na fedha hizo wakaziingiza kwenye kampeni zile na kwa kiasi Fulani zikafanikiwa, basi tunataka kuona sasa ushawishi huo huo wa kiongozi wetu wanchi pamoja na serikali yake wakiutumia kwaajili kuamasisha jamii kuukataa ugonjwa huo kwamba kwa kila mzazi anapona mtoto wake anaanza kunyemelewa na maradhi hayo ya kujaa maji amkimbize haraka hospitali, pia madaktari waliobobea katika ugonjwa huo wawezeshwe ili waweze kupewa fursa ya kutoa elimu kwa umma kuhusu ugonjwa huo kupitia vyombo vya habari.

Nimemuomba rais Kikwete na serikali yake atumie ushawishi wake wa kuanza mikakati ya kuupiga vita ugonjwa huo kwasababu naamimi akifika katika ile wodi ya wototo wanaosumbuliwa na maradhi hayo na akafanikiwa kuwaona watoto wale naamini kabla ya kuondoka madarakani mwaka 2015, atatumia fursa alizonazo kuakikisha nguvu za kitaalamu, madawa, ujenzi wa wodi katika za watoto wenye maradhi kama hayo katika hospitali zenye hadhi ya mikoa hapa nchini zitajengwa.

Kama serikali yetu imeweza kuelekeza nguvu zake na kuomba misaada kwenye taasisi za kimataifa kwaajili ya waathirika wa ukimwi na ikafanikiwa kupata misaada ya ujenzi wa wodi maalum za wagonjwa hao na matabibu wakapelekwa kuudhulia kozi mbalimbali kwaajili ya kuwahudumia wagonjwa wa ukimwi, basi ni wazi serikali yetu ikiamua kulivalia njuga ugonjwa huo wa watoto wenye vichwa vikubwa vinavyojaa maji ambao mtaani wanauita ‘mabichwa maji’haishindwi.

Ili nisianze kuamini kwamba katika miradi ile ya maralia, ukimwi, Kifua Kikuu, Saratani ambazo bado mnaendeleza kampeni zake kuwa mnafaidika binafsi, naomba uzalendo na shauku ile iliyowasukuma kuanzisha miradi hiyo, sasa muielekeze kwakuanza kusaka fedha kwaajili ya kuanzisha kampeni ya kuupunguza au kuutokomeza ugonjwa huo wa Hydrocethalus.

Napenda kuitimia moyo serikali yetu sasa ione haja ya kuanzisha kampeni ya kutoa elimu kuhusu ugonjwa huo ili kama unaepukika watu wauepuke, kuutokomeza ugonjwa huo ambao ni wazi kabisa kwanjia moja au nyingine nao unachangia umaskini ndani ya familia ya watu ambao wanamtoto anayesumbuliwa na tatizo hilo.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0716 -774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Oktoba mosi mwaka 2011.