AMOS MAKALLA ATOA MSAADA WA JENERETA JIMBONI KWAKE



Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Amos Makalla ( mwenye suti) akimkabidhi Jenereta lenye thamani ya Sh: milioni 3.5 , Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Lukenge, Kata ya Mtibwa Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro , Romanus Daniel ( kushoto) juzi kwa ajili ya kufunga kwenye chanzo na kusukuma maji hadi Kijijini hapo ili kuondokana na tatizo la maji safi na salama tangu mwaka 2006 (Na Happiness Katabazi)

HAKIMU AKATALIWA

Na Happiness Katabazi

MAWAKILI wa Serikali katika kesi ya jinai Na.149/2010 ya utakatishaji fedha haramu ya zaidi ya Shilingi bilioni 3.8 inayomkabili Afisa wa Mamlaka ya Mapato(TRA), Justice Katiti na wenzake,katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana waliwasilisha ombi la kumuomba Hakimu Mkazi anayesikiliza kesi hiyo Waliarwande Lema ajitoe kwenye kesi hiyo kwasababu hawana imani naye.


Mbali na Katiti, washtakiwa wengine ni Samweli Renju , Haggay Mwatonoka na Hope Lulandala afisa wa Benki ya Taifa ya Biashara(NBC) na mfanyabiashara Erick Lugereka ambao wanaendelea kusota rumande tangu mwaka 2010 walipofikishwa mahakamani hapo kwa kosa hilo la utakatishaji fedha haramu ambalo kwa mujibu wa sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, kosa hilo halina dhamana.

Ombi hilo liliwasilishwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali Oswald Tibabyekomya kwaniaba ya mawakili wenzake Wakili Kiongozi wa Serikali Fredrick Manyanda na Shadrack Kimaro mbele ya hakimu Lema wakati kesi hiyo ilipokuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa.

Akiwasilisha ombi hilo huku akionekana kujiamini, Wakili Tibabyekomya aliikumbusha mahakama hiyo kuwa kesi hiyo ilikuja kwaajili ya kuanza kusikilizwa lakini upande wa jamhuri haupo tayari kwaajili kuanza kusikilizwa kwasababu wamekuja na ombi la kuomba hakimu Lema ajitoe na asiendelee kusikiliza kesi hiyo kwasababu hawana imani nae kwani tangu waanze kuindesha kesi hiyo wakili Manyanda na Kimaro wamekuwa wakipokea vitisho vinavyohatarisha usalama wao kwa njia ya ujumbe mfupi kutoka kwa namba moja ya simu ya kiganjani.

Wakili Tibabyekomya aliendelea kueleza kuwa kufuatia mawakili wenzake anaoendasha nao kesi hiyo kupokea vitisho mara kwa mara walifikia uamuzi wa kwenda kutoa taarifa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam, na ile namba iliyokuwa ikitumika kuwatumia vitisho waliwapatia makachero wa jeshi la polisi ambapo makachero hao walianza kuchunguza namba hiyo na bado wanaendelea na upelelezi wao na kwamba katika upelelezi wao wa awali ukabaini ujumbe huo mfupi wa vitisho ulikuwa ukitumwa kwao na mtu asiyefahamikwa na alikuwa akitumia simu ya mkononi inayosadikiwa kuwa ni Hakimu Lema.

“Na kwamba Machi 13 mwaka huu, Hakimu Lema jeshi la Polisi lilimtaka afike katika makao makuu ya Jeshi hilo, na hakimu Lema aliitii amri hiyo na alipofika na kuhojiwa na makachero hao kuhusu hilo hakimu huyo alikanusha tuhuma hizo…na kwa kuwa hali ni hiyo sisi mawakili wa serikali ili tuone haki inatendeka katika kesi hii tunakuomba wewe hakimu Lema ujitoe kwenye kesi hii ili apangwe hakimu mwingine ambaye hatutakuwa na mashaka naye ili aweze kuendelea kusikiliza kesi hii”alidai wakili Tibabyekomya.

Kwa upande wake Hakimu Lema alisema amelisikia ombi hilo na kwamba anaiarisha kesi hiyo hadi Aprili 12 mwaka huu, ambapo siku hiyo atatoa uamuzi wake kuhusu ombi hilo la mawakili wa serikali.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Machi 28 mwaka 2012.

MAWAKILI:MRAMBA HANA KESI YA KUJIBU


Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Waziri wa Fedha, Basil Mramba ameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imuone hana kesi ya kujibu na afutiwe kesi inayomkabili ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya Shilingi bilioni 11.7 kwasababu upande wa Jamhuri katika kesi hiyo umeshindwa kuthibitisha kesi yake bila kuacha mashaka.


Mbali na Mramba anayetetewa na mawakili wa kujitegemea Hurbert Nyange na Peter Swai.Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Daniel Yona na Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Gray Mgonja ambao wanatetewa na Elisa Msuya na Cuthbert Tenga ambapo kesi hiyo inasikilizwa mbele ya Jaji John Utamwa anayesaidiwa na mahakimu wakazi Saul Kinemela na Sam Rumanyika.

Ombi hilo Mramba peke yake liliwasilishwa jana kwa njia ya maandishi na mawakili wake mahakamani hapo kufuatia amri iliyotolewa Februali 17 mwaka huu, na Jaji Utamwa ambapo alisema mwenendo wa kesi hiyo umekamilika na ukautaka upande wa utetezi uwasilishe majumuisho yao ya kuwaona hawana kesi ya kujibu jana na upande wa Jamhuri uwasilishe majumuisho yake Aprili 17 mwaka huu na endapo upande wa utetezi unataka kuwasilisha majumuisho ya nyongeza uwasilishe Aprili 30 na akaiarisha hadi Mei 2 mwaka huu, jopo hilo litakuja kuangalia kama amri hizo zimetekelezwa.

Wakili Nyange anaanza kwa kuikumbusha mahakama kuwa washtakiwa wanakabiliwa na makosa mawili ya ambayo yamegawanyika katika makosa 11 na kosa kumi ni na matumuzi mabaya ya ofisi ya umma kinyume na kifungu cha 96(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 na kosa la 11 ni kusababisha serikali hasara ya kinyume na kifungu 284A(1) cha Sheria hiyo ya Kanuni ya Adhabu.

Wakili Nyange alidai mawakili wa Jamhuri wanadai mshtakiwa wa kwanza na wapili (Mramba na Yona) wanadaiwa kutenda kosa la kutumia madaraka yao vibaya kwa uamuzi wao wa kuiruhusu kampuni ya Alex Stewart (Assayers)UK na kampuni mama ya Alex Stewart Government Bussiness Corporation kufanyakazi ya ukaguzi wa dhahabu hapa nchini kinyume na Sheria ya Manunuzi ya Umma Sura ya 410 ya mwaka 2002 na Sheria ya Madini Sura ya 123.

Pia walisaini makubaliano na kampuni hizo ambapo makubaliano hayo yaliiruhusu kampuni hiyo kufanya shughuli hizo hapa nchini kwa miaka miwili kuanzia Juni 14 mwaka 2005-Juni 23 mwaka 2007 bila idhini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Nyange alidai Mramba na Mgonja wanakabiliwa na shtaka la tano, sita,saba ,nane ,tisa na kumi ambalo ni la kutoa vibali vibali sita vya msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kinyukme na ushauri wa Mamlaka ya Mapato(TRA), ambayo TRA ilitoa ushauri kwa washtakiwa isitoe msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo na kuongeza kuwa kosa la 11 ni la kusaisababishia serikali hasara ya Sh. 11,752,350,148.00 kwa uamuzi wao wa kuipatia msamaha kutolipa kodi kampuni hiyo.

“Mheshimiwa katika makosa ya jinai ili mshtakiwa atiwe hatiani kwa kosa la jinai anayodaiwa kutenda ni lazima mambo mawili yathibitishwe na upande wa Jamhuri. Mambo hayo ni lazima ithibitike kuwa mshtakiwa walitenda kosa hilo wanalokabiliwa nalo(actus reus),na wakati akitenda kosa hilo walikuwa na nia ovu(means rea).Na kwa mujibu wa kesi hii upande wa jamhuri umeshindwa kuthibitisha vitu hivyo viwili kwa mshtakiwa kwanza na kwa sababu hiyo tunaomba mahakama imuachilie huru Mramba na imuone hana kesi ya kujibu”alidai wakili Nyange.

Akilichambua shtaka la matumizi mabaya ya ofisi ya umma, upande wa Jamhuri umeshindwa kuleta shahidi wa kuthibitisha Mramba alitenda kosa hilo.Kwa sababu Tanzania ni Jamhuri na Mtendaji Mkuu wake ni rais ambaye anafanyakazi zake kwa kusaidiwa na Baraza la Mawaziri na kuongeza kuwa pia Jamhuri imeshindewa kuleta ushahidi hata wa maandishi unaonyesha Rais Mkapa hakuridhia uamuzi wa Mramba kuipatia kampuni hiyo msamaha wa kodi na kwamba shahidi nane wa upande wa Jamhuri aliyekuwa Naibu Waziri wa Fedha,Abdisalaam Issa Khatibu katika ushahidi wake alieleza mahakama kuwa hakuna shida endapo waziri yoyote akiwasiliana na rais moja kwa moja bila bila kupitia kwa Waziri Mkuu.

Wakili Nyange alieleza kuhusu Mramba kudaiwa kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo kuwa alikiuka ushauri wa TRA alidai wamejiuliza vitu vifuatavyo . “Mramba alikuwa na mamlaka ya kutoa msamaha wa kodi?Ni taratibu zipi za kutoa vibali vya serikali msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo ?Na Mramba kutoa msamaha wa kodi ametumia madaraka yake ?Mramba alikuwa jukumu la kisheria linalomlazimisha kufuata ushauri wa TRA?Je ushauri ule wa TRA kwa kukataa Mramba asitoe msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo unampana kisheria mshtakiwa huyo?

Alikafanua kuhusu maswali hayo alidai kuwa hakuna shahidi hata mmoja wa Jamhuri aliyefika mahakamani hapo na kueleza kuwa mshtakiwa huyo hakuwa na mamlaka ya kutoa msamaha wa kodi kwa Kampuni Alex Stewart na kwamba hakuna shahidi aliyekuwa kueleza mahakama kuwa taratibu zote zilizofanywa hadi kuipatia msamahama kampuni hiyo hazikufuata taratibu za kisheria na kuwa sheria ya Kodi ina mruhusu waziri wa Fedha kutoa msamaha na kwamba shahidi wa 12 alieleza mahakama kuwa Mramba hakuwa na uhusiano wa kirafiki wala hakunufaika na na uamuzi huo wa kuisamehe kodi kampuni hiyo.

Kuhusu kosa la kusababisha hasara ya sh bilioni 11.7 alidai kama serikali ya Tanzania iliipatia msamaha wa kodi kampuni hiyo kwahiyo upande wa Jamhuri hauwezi kudai msahama huo hauwezi kusababisha upotevu wa kiasi hicho cha fedha kwa maana hiyo Jamuhiri ilipaswa ithibitishe kama kampuni hiyo ilikuwa hailipi kodi kama inavyotakiwa kisheria na kuongeza kuwa kiasi hicho kinachodaiwa kuwa ni serikali imepata hasara ni cha kufikilia na kwamba siyo cha kweli.

“Naiomba mahakama hii imfutie kesi Mramba kwasababu upande wa Jamhuri imeshindwa kuthibitisha kesi yake kwasababu ushahidi na vielelezo vilivyotolewa na mashahidi wake ni dhaifu ambao hauwezi kuishawishi mahakama hii imuone mshtakiwa ana kesi ya kujibu”alidai Wakili Nyange.

Mramba na Yona walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Novemba 25 mwaka 2008 na hati ya mashtaka ilikuwa na jumla ya mashtaka 13.Lakini Januari 2 mwaka 2009 mshtakiwa wa tatu(Mgonja) alipounganishwa mashtaka yakapungua na kufikia 11.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Machi 28 mwaka 2008.

KESI YA UCHOCHEZI KIBANDA,MAKUNGA, YAPIGWA KALENDA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kuruhusu kuandikwa kwa makala ya uchochezi inayomkabili Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima,Absalom Kibanda na wenzake jana ulimsomea shtaka la kuchapisha waraka huo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd, Theophil Makunga.


Sambamba na hilo Wakili Mwandamizi wa Serikali Elizabeth Kaganda mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema alieleza kuwa mbali na kumsomea mshtakiwa huyo watatu(Makunga) shtaka lake kwasababu Machi 7 mwaka huu, alipounganishwa na hati hiyo kufanyiwa marekebisho na kisha kuwasomea mashtaka mapya washtakiwa hayo,Makunga hakuwepo mahakamani pia unaifanyia hati hiyo marekebisho ya majina ya mshtakiwa wa pili na watatu(Kibanda na Makunga) kwani yalikuwa yamekosewa hapo awali ombi ambalo lilikubaliwa na hakimu huyo.

Machi 7 mwaka huu, hati hiyo ya mashtaka majina ya Kibanda na Makunga yalikuwa yamekosewa kuandikwa.Jina la Kibanda lilikuwa likisomeka kuwa ni Kibamba na Makunga lilikuwa likisomeka Maingu.

Wakili Kaganda akimsomea shtaka hilo ambalo kwa mujibu wa hati ya mashtaka ni shtaka la pili ambalo linamkabili Makunga peke yake, ambalo ni la kuchapisha waraka wa uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1) ( c) na 31 (1)(a) vya Sheria ya Magazeti Na.229 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 kwamba Novemba 30 mwaka 2011, Makunga akiwa na wadhifa huo alichapisha makala ya uchochezi iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘ Waraka Maalum kwa askari wote’ ambayo iliandikwa na gazeti la Tanzania Daima Toleo Na. 2552 la Novemba 30 mwaka 2011.

Hata hivyo mshtakiwa alikana shtaka hilo na Hakimu Lema alisema masharti ya dhamana ni kama yale yaliyoyatoa Desemba 8 mwaka 2011 ambayo yalishatekelezwa na washtakiwa wenzake, ambapo ili apate dhamana ni lazima awe na wadhamini wawili ambao watasaini bondi ya shilingi milioni tano kila mmoja, na kuwasilisha hati ya mali isiyoamishika yenye thamani hiyo ya fedha, kuripoti mara moja kwa mwezi katika Kituo Kikuu cha Polisi na kusalimisha hati ya kusafiria mahakamani, masharti ambayo yalitimizwa na Makunga na yupo nje kwa dhamana.

Wakili Kaganda pia aliikumbusha mahakama hiyo kuwa kesi hiyo jana ilikuwa imekuja kwaajili ya upande wa Jamhuri kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao lakini hawapo tayari kuwasomea kwa jana na kwamba wanaiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kuja kuwasomea maelezo hayo ya awali.

Ombi ambalo lilikubaliwa Hakimu Lema ambaye aliairisha kesi hiyo hadi Aprili 24 mwaka huu, kwaajili ya washtakiwa kuja kusomewa maelezo ya awali.

Machi 7 mwaka huu, Wakili Kaganda akiisoma hati mpya ambayo ina mashtaka mawili tu ambapo kosa la kwanza ni la uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1)(c) na 31(1)(a) cha Sheria ya Magazeti Sura ya 229 ya mwaka 2002 ambalo lina mkabili mshtakiwa wa kwanza na wa pili yaani Mwigamba na Kibanda ambao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Mabere Marando ,Isaya Matamba, Juvenalis Ngowi na John Mhozya na Frank Mwilongo.

Ambapo wakili Kaganda alidai kuwa mnamo Novemba 30 mwaka 2011 jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao wawili kwa makusudi na kwa nia kuvunja sheria za mamlaka ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitenda kosa hilo la uchochezi kwa kuruhusu makala hiyo ichapishwe kwenye gazeti la Tanzania Daima la Novemba 30 mwaka 2011 iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “ Waraka Maalum kwa askari wote’ ambapo ilikuwa ikiwachochea askari hao wasitii mamlaka za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi 27 mwaka 2012.

KAJALA ASOMEWA MASHTAKA UPYA

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE upande wa Jamhuri katika kesi ya kutakatisha fedha haramu inayomkabili msanii wa Filamu nchini Kajala Masanja na mumewe Faraja Chambo jana uliwasilisha hati mpya ya mashtaka waliyoifanyia marekebisho na kisha kuwasomea upya washtakiwa yanayowakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam.


Hatua hiyo ya kuwasilisha hati hiyo iliyofanyiwa marekebisho inatokana na amri iliyotolewa na Hakimu Mkazi Sundi Fimbo , Machi 15 mwaka huu, muda mfupi baada wakili huyo wa mashtaka kuwasomea mashtaka washtakiwa hao kwa mara ya kwanza na wakili wa utetezi Alex Mgongolwa kuomba mahakama hiyo iuamuru upande wa Jamhuri upanyie marekebisho hati hiyo kwasababu hati hiyo haijataja jina la mtu aliyeuziwa nyumba na washtakiwa hao na kwamba haikutaja nyumba hiyo iliyouziwa ipo katika Kitalu namba ngapi, ombi ambalo lilikubaliwa na hakimu huyo.

Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) Leonard Swai jana akiwasomea upya mashtaka ambayo imeletwa mahakamani hapo kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Dk.Eliezer Feleshi, licha ya mume wa kaja kutokuwepo mahakamani kwasababu yupo gerezani akikabiliwa na kesi nyingine ya utakatishaji fedha ambayo haina dhamana kwa mujibu wa sheria, alidai kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na mashataka yale yale ya awali ambayo ni matatu na kwamba jina la mtu aliyeuziwa nyumba hiyo na washtakiwa hao ni Emilian Rugalia na kwamba nyumba hiyo iliyopo

Wakili wa Takukuru, alidai washtakiwa hao wanakabiliwa na matatu, kosa la kwanza ni la kula njama kinyume na kifungu cha 34 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 ambapo washtakiwa wote kwa pamoja walitenda kosa hilo la kula njama la kuamisha umiliki wa nyumba iliyopo Kunduchi Salasala eneo ambalo halijapimwa jijini Dar es Salaam.

Shtaka la pili ni ni kwamba Aprili 14 mwaka 2010 waliamisha isivyo halali umiliki wa nyumba hiyo ambayo walikuwa wakiimiliki kwenda kwa Emilian Rugalia ambaye ndiyo walimuuzia kinyume na kifungu cha 34(2)A(3) cha Sheria ya TAKUKURU ya mwaka 2007. Na shtaka la tatu ni la kutakatisha fedha ambalo walilitenda siku hiyo ya Aprili 14 mwaka 2010 huku wakijiua ni kinyume na sheria hiyo.

Hata hivyo Kajala ambaye alikuwepo peke yake mahakamani hapo bila mshtakiwa wa kwanza (Chambo) ambaye ni mumewe kutokuwepo mahakamani hapo kwasababu yupo gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja kwasababu anakabiliwa na kesi nyingine ya utakatishaji fedha haramu iliyofunguliwa mahakamani hapo ambapo kwa mujibu wa sheria kosa hilo halina dhamana, alikana mashtaka yote matatu na akaamuriwa kurudishwa rumandwa hadi Aprili 4 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya kutajwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Machi 28 mwaka 2012.

DPP AKWAMISHA KESI YA KAJALA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kutakatisha fedha haramu inayomkabili Msanii wa Filamu nchini, Kajala Masanja na mumewe Faraja Chambo jana ulishindwa kuleta hati ya mashtaka iliyofanyiwa marekebisho kama ulivyoamliwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, wiki iliyopita kwa madai kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP),Dk.Eliezer Feleshi juzi hakuweza kupatika ofini kwake ili aweze kutoa kibali cha kuletwa kwa hati hiyo mahakamani hapo.


Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mussa Hussein aliikumbusha mahakama hiyo kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya upande wa jamhuri kuleta hati ya mashtaka iliyofanyiwa marekebisho lakini ameshindwa kufanya hivyo kwasababu juzi DDP-Dk.Feleshi hakuwepo ofisini kwake ili aweze kutoa kibali cha kuletwa hati hiyo mahakamani na kwasababu hiyo wanaomba wapewe siku moja waweze kuileta hati hiyo mahakamani.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Sundi Fimbo alikataa hati hiyo isiletwe leo na badala yake hati hiyo iletwe Machi 26 mwaka huu kwaajili wa washtakiwa kusomewa upya mashtaka hayo na akaamuru mshtakiwa arudishwe rumande , uamuzi ambao ulikubaliwa na wakili huyo wa Takukuru na wakili wa Kajala, Alex Mgongolwa.

Machi 15 mwaka huu, Kajala na mumewe ambaye hata hivyo mumewe yupo gerezani anakabiliwa na kosa la utakatishaji fedha haramu katika kesi nyingine ambapo kwa mujibu wa sheria kosa hilo halina dhamana.Wakili wa Takukury, alidai washtakiwa hao wanakabiliwa na matatu, kosa la kwanza ni la kula njama kinyume na kifungu cha 34 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 ambapo washtakiwa wote kwa pamoja walitenda kosa hilo la kula njama la kuamisha umiliki wa nyumba iliyopo Kunduchi Salasala jijini Dar es Salaam.

Shtaka la pili ni ni kwamba Aprili 14 mwaka 2010 waliamisha isivyo halali umiliki wa nyumba hiyo kinyume na kifungu cha 34(2)A(3) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007. Na shtaka la tatu ni la kutakatisha fedha ambalo walilitenda siku hiyo ya Aprili 14 mwaka 2010 huku wakijiua ni kinyume na sheria hiyo.

Hata hivyo baada wakili huyo wa Takukuru siku hiyo kumsomea mashtaka hayo, Wakili Mgongolwa alidai hati hiyo ya mashtaka ina mapungufu ya kisheria kwasababu hati hiyo ya mashhata haijasema nyumba hiyo iliuzwa kwa nani na kwamba nyumba hiyo ipo katika Kitaly gani, hoja ambayo ilikubaliwa na Hakimu Fimbo Machi 20 mwaka huu, ambapo aliuamuru upande wa Jamhuri ukaifanyie marekebisho hati hiyo na kisha jana uje na hati ya mashtaka ambayo imeishafanyiwa marekebisho.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Machi 23 mwaka 2012.

MTIKILA AMKATAA HAKIMU FIMBO

Na Happiness Katabazi

IKIWA ni siku chache baada ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Sundi Findo, atoe uamuzi wa kumuona Mwenyekiti wa chama cha Democratic(DP), Mchungaji Christopher Mtikila ana kesi ya kujibu katika kesi ya kuchapisha na kusamba waraka wa uchochezi dhidi ya Rais Jakaya Kikwete , Mtikila amewasilisha mahakamani hapo ombi la kumuomba hakimu huyo ajitoe kwenye kesi yake ya jinai Na.132/2011 kwasababu hawezi kumtendea haki.


Kwa mujibu wa barua hiyo ambayo Tanzania Daima inayo nakala yake,Mtikila anamuonmba hakimu Fimbo ajitoe kwenye kesi yake kwasababu amebaini hawezi kumtendea haki kwasababu wakati kesi hiyo ikiendelea Mtikila ambaye ni mshtakiwa katika kesi hiyo aliwasilisha ombi la kuomba usikilizwaji wa kesi hiyo usimame hadi kesi ya Kikatiba iliyopo mbele ya Jopo la Majaji wa tatu wa mahakama Kuu wanaongozwa na Jaji Fakhi Jundu na Profesa Ibrahim Juma ambapo katika kesi hiyo anaiomba mahakama hiyo izifute sheria za makosa ya uchochezi kwakuwa zinanyima haki wananachi ya kutoa maoni yao itakapotolewa uamuzi lakini huyo alilikataa ombi lake.

Mtikila alidai kuna kesi tatu za Kikatiba zilizokuwa zimefunguliwa mahakama kuu na washtakiwa wanaokabiliwa na kesi za jinai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambao ni Jayantkumar Patel ‘Jeetu Patel’, Profesa Costa Mahalu na mahakama ya Kisutu ilisitisha usikilizwaji wa kesi zinazowakabili hadio mahakama kuu ilipozitolea uamuzi kesi zao za Kikatiba.

“Na huyu Hakimu Fimbo anafahamu fika nimefungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu kuzipinga sheria za uchochezi ambao sheria hizo ndizo zimetumika kunifungulia kesi ya uchochezi iliyopo mbele yake na anafahamu fika kesi ya aina hiyo ikishafunguliwa mahakama ya juu, mahakama ya chini inatakiwa isitishe usikilizaji wa yangu hadi mahakama hiyo ya juu itakapotoa uamuzi lakini yeye amekuwa akilikataa ombi langu na kwa kitendo chake hicho minasema amevunja mwenendo wa kesi na ukiukwajili wa maadili ya sheria za nchi na haki na nimuomba ajitoe kwenye kesi yangu kwani tayari ameishaonyesha hawezi kunitendea haki ”alidai Mtikila.

Aidha Mtikila alidai sababu nyingine ya kumkataa hakimu Fimbo, ni kwamba wakati kesi hiyo ikiendeshwa aliwai kuwasilisha ombi la kutaka afutiwe kesi hiyo ya uchochezi kwasababu kesi hiyo ilifunguliwa nje ya muda kwani kesi za uchochezi zinatakiwa zifunguliwe mahakamani ndani ya miezi sita tangu mshtakiwa alituhumiwa kutenda kosa hilo na kwamba kesi hiyo inafanana na kesi ya madai ya fidia Na.166/2004 inayosikilizwa na Jaji Robert Makaramba , ambapo katika kesi hiyo anamdai Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa alikamatwa kinyume na sheria na kwamba kesi ile ambayo nayo ni ya uchochezi iliyokuwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni ilifunguliwa nje ya muda.

“Na maoni ya wananchi wengi baada ya uamuzi wako wa kuniona mimi nina kesi ya kujibu wananchi wengi wameuchukulia uamuzi huo ni wa kumfurahisha Rais Jakaya Kikwete ambaye ni mpinzani wangu kidini na kisiasa na kwamba kitendo hicho kitavuruga uhuru wa mahakama na utu wangu”alidai Mtikila.

Alipotafutwa na waandishi wa habari kuthibitisha kama mahakama imepokea barua hiyo, Kaimu Hakimu Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Frank Moshi alikiri mahakama hiyo kupokea barua hiyo na kwamba taratibu nyingine za kiutawala zitafanyika baada ya Hakimu Mkuu Mfawidhi Elvin Mugeta akirejea ofisini kwani hivi sasa yupo nje ya Dar es Salaam, kwashughuli za kikazi.

Machi 13 mwaka huu, Hakimu Fimbo alimuona Mtikila ana kesi ya kujibu katika kesi ya uchochezi ambapo Hakimu Fimbo alisema baada ya kupitia ushahidi wa upande wa Jamhuri,amefikia uamuzi wa kumuona Mtikila ana kesi ya kujibu na kwamba maana hiyo Mtikila atatakiwa na mahakaa hiyo kupanda kizimbani Aprili 11 mwaka huu kwaajili ya kuanza kujitetea. Na Mtikila siku hiyo akaeleza kuwa amekusudia kuleta mashahidi 10.

Ilidaiwa kuwa kati ya Januari mwaka 2009 na Aprili 17, mwaka 2010 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya uchochezi mshitakiwa alisambaza kwa umma nyaraka zilizosema 'Kikwete kuuangamiza ukristo', 'wakristo waungane kuweka mtu Ikulu' alinukuliwa Mtikila.

Katika shitaka la pili, Aprili 16, mwaka 2010 eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam, bila kibali alikutwa akimiliki waraka wenye uchochezi kwa jamii.Na katika kesi hii Mtikila hana wakili wa kumtetea na anajitetea mwenyewe.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa,Machi 23 mwaka 2012.

LOWASSA UMEANZA MAPAMBANO NA SERIKALI?



Na Happiness Katabazi

MTUME Muhamad (SAW) katika Sura Tul munafikuna alifundisha kwamba mnafiki ana alama tatu. Alama hizo ni: ‘Mnafiki akizungumza huwa ni uongo, akiahidi jambo halitimizi na akiaminiwa hufanya hiana.’


Nimelazimika kutumia nukuu hiyo ya kiongozi wa dini ya Kiislamu kwa kuwa wengi wetu tumekuwa tukisoma, kusikiliza na kufuata maagizo ya viongozi wa kiimani ili tuweze kuwa na maisha bora hapa duniani na huko ahera.

Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa kwa nyakati tofauti katika nyumba tofauti za ibada (makanisa) amekuwa akidai kuwapo kwa tishio la bomu la ukosefu wa ajira kwa vijana ambalo likilipuka nchi itakuwa kwenye hatari.

Kiongozi huyo amekuwa akiwaomba maaskofu wa Kanisa Katoliki na mengineyo anayopata nafasi ya kushirki shughuli za kidini kusaidia kutatua tatizo hilo ambalo linaonekana kutovaliwa njuga kikamilifu na serikali.

Lowassa na wananchi wengine wana haki ya kufurahia matakwa ya Ibara ya 18(1) ya Katiba ya nchi ambayo yanatoa haki kwa kila mwananchi kutoa fikra zake pasi kuvunja sheria.

Sitaki kupora haki yake ya kutoa tamko hilo bali ninajiuliza imekuwaje analiona tatizo hilo hivi sasa ilhali yeye alikuwa Waziri Mkuu ambaye alipaswa kuonyesha mfano wa kulitegua bomu hilo?

Chama chake cha CCM ndicho kinaunda serikali ambayo kila kukicha imekuwa ikijinasibu kuzalisha ajira nyingi pamoja na kuboresha maisha ya Watanzania ambayo sasa yanazidi kudorora badala ya kuboreka.

Ni Lowassa huyu huyu wiki iliyopita alirejea nchini akitokea Ujerumani alizungumza na waandishi wa habari akisema yeye ni mzima wa afya na kwamba yupo tayari kwa ajili ya mapambano yaliyopo mbele yake.

Najiuliza, mapambano aliyoyasema ndiyo haya ya kupambana na serikali ya Rais Kikwete ambayo sasa inalazimika kutumia nguvu kubwa kujibu mashambulizi ya kada wake?

Lowassa alikuwa ni miongoni mwa viongozi wa kundi la wanamtandao waliopigana kufa na kupona mwaka 2005 kuhakikisha Rais Kikwete anaingia madarakani, alimsaidiaje rafiki yake kutegua bomu la ajira kwa vijana?

Ilani ya CCM ya mwaka 2005 na ile ya mwaka 2010 iliweka wazi kuwa iwapo chama hicho kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi kitatengeneza ajira kwa vijana, ahadi hiyo sasa imegeuka takwimu zisizo na mashiko.

Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka, Jumatano wiki hii aliamua kuyakanusha madai ya Lowassa kwa kutumia takwimu alizonazo kuwa nguvu kazi ya Tanzania ni watu milioni 20.6 kati ya watu milioni 37.5, watu milioni 18.3 sawa na asilimia 88.3 wana ajira na kwamba watu laki nane mpaka milioni moja wanaingia katika ajira mpya.

Sasa nimuulize Lowassa ni kwanini anatoa tamko la aina hiyo kila mara wakati serikali ya chama chake imefanya ‘vizuri’ kwenye kutengeneza ajira mpya, kama vigogo wa chama tawala wanakanganyana kiasi hiki mwananchi ashike la nani?

Hivi Lowassa anataka kuuambia umma kuwa zama za ajira nyingi kutolewa na serikali bado zipo? Kama ni hivyo mbona hatukumuona akisimamia utengenezaji wa ajira mpya wakati akiwa waziri mkuu?

Kila kukicha serikali ya CCM imekuwa ikiongeza nguvu na kuijengea uwezo sekta binafsi ambayo imeongeza wigo wa ajira, haya yote Lowassa hayaoni au ana lake jambo?

Kwa mujibu wa tamko hilo la Lowassa, kiongozi huyo anataka umma utafsiri kuwa yeye na serikali ya chama chake cha CCM wameshindwa kutekeleza ile ahadi ya kutoa ajira kwa vijana waliyotuahidi mwaka 2005?

Kama hivyo ndivyo ninamshanga sana Lowassa anavyoendelea kuwa mwanachama wa chama hicho ambacho serikali yake imeshindwa kutekeleza ahadi hadi leo. Katika hili nikisema Lowassa ‘anauhadaa umma’ nitakuwa nimekosea?

Lowassa nilimshuhudia Oktoba mwaka 2010 wakati akinadiwa jukwaani jimboni kwake na aliyekuwa mgombea mwenza wa CCM, Dk. Mohamed Gharib Bilal ambapo mara baada ya Dk. Bilal kumaliza ngwe yake alipanda Lowassa kunadi sera za CCM na alisema serikali yake imeweza kufanya mengi ikiwemo kuwapatia ajira vijana.

Sasa anapoibukia makanisani na kutoa tamko hilo ambalo limeishapingwa na serikali, kwa kweli nilimshangaa sana, sijui ni kiongozi wa aina gani asiyekumbuka kile alichokiahidi miaka miwili iliyopita au ndiyo mikakati yake ya kuelekea 2015?

Nimalizie kwa kumshauri mzee wangu Lowassa, fikiri kwa kina kila unaloambiwa au unalotaka kusema ili usije ukajijengea mazingira ya ‘kuumbuka’ kama ilivyo hivi sasa.

Inawezekana ziara zako hizo za kila kukicha makanisani ndiyo miongoni mwa mbinu ulizopewa na kikosi kazi chako ambacho kinadhani unaweza ukapenya kwenye chekeche la kuwania urais mwaka 2015, lakini ni vema akili za kuambiwa ukachanganya na zako.

Huku mitaani baadhi ya marafiki zako wamekuwa wakihusisha kauli zako na kuwania urais. Hata hivyo sijakusikia ukitamka kuwania nafasi hiyo.

Nakuomba uwaangalie watu wanaokusaidia kwenye mikakati ya kuwania uongozi wa nchi wasije wakakuangusha kabla hujaangushwa na wananchi au makada wenzako ambao wanajua kinaga ubaga unachokifanya.

Binafsi siamini kama kuna jipya ulilotuonyesha ili utushawishi wewe ni mtu mpya na unaweza kulikabili tatizo la ukosefu wa ajira, tofauti na njia zinazotumiwa na serikali ya chama chako.

Mimi nilikuwa miongoni mwa waandishi wa habari wachache tulioalikwa katika mkutano wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Jakaya Kikwete, mwaka 2005 uliofanyika nje ya ofisi ya Makao Makuu ya CCM Mkoa wa Pwani.

Katika mkutano huo Rais Kikwete alitangaza rasmi nia yake ya kuomba apitishwe na chama chake ili awanie kugombea urais, kiongozi huyo alisema ukosefu wa ajira ni bomu linalosubiri kulipuka.

Kwa hiyo kimsingi tukubaliane tamko hilo si jipya katika masikio ya watu ambao tunafuatilia kwa karibu matamshi na mienendo ya viongozi wetu siku hadi siku.

Kikwete alipitishwa na CCM kuwa mgombea urais, wakati wa kampeni za mwaka 2005 alituhakikishia Watanzania kuwa akiingia Ikulu atahakikisha nyumba za serikali ambazo ziliuzwa kwa watumishi wa umma atazirejesha serikalini, ahadi ambayo hadi sasa ameshindwa kuitekeleza kwa vitendo.

Wakati akitoa ahadi hii alikuwa ni mjumbe wa baraza la mawaziri enzi za utawala wa Rais Benjamin Mkapa na uuzwaji nyumba hizo ulibarikiwa na baraza hilo, ikimaanisha na yeye alibariki ila kwa sababu alikuwa akizihitaji kura za wananchi na wananchi wengi ni watu tunaopenda kudanganywa na kutotaka kuchanganua mambo tulifurahia mno ahadi hiyo.

Kwa mifano hiyo hai, ambayo binafsi nimeishuhudia kwa macho, nataka nitoe rai kwa wananchi wenzangu wasilipe uzito tamko la Lowassa, kwani alikuwa mtumishi wa muda mrefu serikalini, CCM na muda wote umma umekuwa ukipigia kelele matatizo mbalimbali, lakini yeye na viongozi wenzake walikuwa wakitubeza.

Ila kwa kuwa hivi sasa hana yale madaraka ya juu yaliyokuwa yanampa upofu wa kutoona wananchi tunakabiliwa na hali mbaya ya ugumu wa maisha na ukosefu wa ajira, ndiyo leo hii anaanza kuuaminisha umma yupo pamoja nao!

Tusidanganyike, kwani nimejifunza kitu kimoja, watu wengi waliowinda madaraka wanajifanya ni wakosoaji wa uendeshaji wa serikali kila kukicha na wachapakazi, lakini siku wakipewa madaraka watu wa aina hiyo hugeuka mabubu na kuacha kupigania haki za wanyonge ambapo awali wakati wakisaka madaraka walituahidi wangetupigania.

Mifano ni mingi, wala si ya kutafuta. Aliyekuwa Rais wa Chama cha Walimu (CWT), Margaret Sitta, enzi zile za waziri wa Elimu akiwa, Joseph Mungai, aliwapigania sana walimu, lakini Rais Kikwete alipoingia madarakani na kumteua kuwa waziri, hatukumsikia tena mwanamama huyo akiendeleza harakati zake za kumkomboa mwalimu hapa nchini.

Kwa hiyo ni wazi kabisa hata Lowassa akiukwaa tena uongozi hatutamsikia tena akilalamikia bomu la ukosefu wa ajira kwa vijana, bali atakuwa akikerwa na kauli za aina hiyo zitakazokuwa zikitolewa na wengine.

Mbinu anayoitumia kiongozi huyo ya kwenda kwenye nyumba za ibada ‘kujisafishia njia’ imepitwa na wakati, haitakusaidia kukufikisha unakotaka kufika.

Mbinu za aina hiyo zilishatumiwa na Rais Kikwete katika hatua zake za mwisho, katika kampeni zake na kweli akafanikiwa na utambue kuwa mbinu iliyotumiwa na Kikwete kuingia madarakani ni nadra mbinu hiyo hiyo kuitumia wewe ili ufanikiwe pia.

Unaweza kubuni mbinu nyingine, haujachelewa.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Machi 25 mwaka 2012.

KESI YA NG'UMBI,MNYIKA KUANZA KUUNGURUMA LEO



Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA mgombea Ubunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM), Hawa Ng’umbi leo anatarajia kupanda kizimbani katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kutoa ushahidi wake katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa jimbo hilo wa mwaka 2010 ambayo yalimtangaza John Mnyika(CHADEMA) kuwa mshindi.


Ng’umbi ambaye amewahi kuwa mkuu wawilaya ya Mvomero, Makete na Bukombe ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea Issa Maige ataanza kujitetea mbele ya Jaji Upendo Msuya ambapo kesi hii in aanza kusikilizwa mfululizo kuanzia leo.

Novemba mwaka 2010, Ng’umbi alimfungulia kesi hiyo Na.107/2010 Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mnyika na Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo, akiiomba mahakama hiyo itangaze kuwa matokeo yaliyompa ushindi Mnyika ni batili kwasababu yalikiuka taratibu za Sheria ya Uchaguzi na kanuni zake ya mwaka 2010 na kwamba mdaiwa wa kwanza na wa tatu walishindwa kutimiza wajibu wao kikamilifu.

Kwa upande wake Mnyika ambaye anatetewa na wakili Edson Mbogoro alipinga madai hayo na kwamba taratibu za uchaguzi hazikukiukwa wakati wa zoezi zima la kuhesabu kura hadi Tume ya uchaguzi ilipomtangaza yeye kuwa ndiye mbunge wa jimbo hilo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatatu, Machi 19 mwaka 2012.

MATTAKA AONGEZEWA MASHITAKA




Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya matumuzi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia hasara Kampuni ya serikali ya Air Tanzania Limited(ATCL) ya dola za Kimarekani 143,442.75 inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo David Mattaka na wenzake umebadilisha mashtaka na kuwaongezea mashtaka washtakiwa hao.

Mbali na Mattaka anayetetewa na wakili Peter Swai,washtakiwa wengine ni Kaimu Ofisa Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Elisaph Mathew Ikomba na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Ndani, William Haji anayetetewa na wakili Alex Mgongolwa.

Mbele ya Hakimu Ritta Tarimo wakili wa serikali Shadrack Kimaro, Oswald Tibabyekomya na wakili wa Mwandamizi toka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU), Ben Lincoln waliikumbusha mahakama hiyo kuwa jana kesi hiyo ilikuja kwaajili ya upande wa jamhuri kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao ili hawataanza kuwasomea maelezo ya awali kwanza kwasababu wamebadilisha hati ya mashataka kwa mujibu wa kifungu cha 234 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, na hivyo wataanza kuisoma hati hiyo ya mpya ya mashtaka yenye jumla ya makosa sita ukilinganisha na hati ya awali iliyokuwa na jumla ya makosa matatu tu.

Wakili Kimaro alidai kuwa shtaka la kwanza linawakabili washtakiwa wote watatu ni la kula njama kinyume na kifungu cha 32 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya mwaka 2007 ambapo Mattaka na wenzake katika tarehe tofauti Machi –Julai 2007 jijini Dar es Salaam, walikula njama na watu wengine wasiojulikana kutenda kosa la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma .

Wakili Kimaro alidai shtaka la pili ambalo pia linawahusu washtakiwa wote ni la matumizi mabaya ya ofisi ya umma kinyume na kifungu ch 31 Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 ambapo washtakiwa hao wakiwa ni watumishi wa umma wa kampuni hiyo ya ATCL kwa nyadhifa zao wakati wakitekeleza majukumu yao kwania ovu walitumia madaraka yao vibaya kwa kuidhinisha ununuzi magari yaliyokwishatumika 26 kitendo ambacho ni kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Manunuzi ya Umma Na.21 ya mwaka 2008 pamoja na kanuni zake zilizotengenezwa na sheria hiyo.

Alidai shtaka la tatu pia ni kwa washtakiwa wote ambalo ni matumuzi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Takukuru ambapo mshtakiwa wa kwanza na wapili (Mattaka na Komba) wakiwa waajili wa ATCL wakati wakitekeleza majukumu yao na kwania ovu,walitumia madaraka yao vibaya na kisha waliagiza magari hayo ya mitumba bila kutangaza tenda ya ushindani na wakayanunua magari hayo kwa thamani ya dola za kimarekani 809,000 kutoka kampuni ya 3 IN DALIMOUK MOTORS ya Dubai katika Jamhuri ya Emireti, kinyume na kifungu cha 59 cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2008 na kanuni zake.

Wakili Kimaro alidai shataka la nne ni matumizi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha sheria ya Takukuru, na kwamba Agosti 2007 washtakiwa hao wakiwa ni waajiliwa wa Kampuni ya Ndege ya Taifa( ATCL) wakati wakitekeleza majukumu yao na kwania ovu walinunua magari hayo 26 ya mitumba kwaniaba ya ATCL inayomilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na kifungu cha 58(3) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2008.

Wakili Kimaro alidai shtaka la tano ni la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma kinyume na kifungu cha 31 cha Sheria ya Takukuru na kwamba kati ya Julai 2 na Agosti 23 mwaka 2007 katika wilaya ya Ilala, washtakiwa wote kwa pamoja wakati wakitekeleza majukumu yao kwa nia ovu waliruhusu kununuliwa kwa magari hayo toka kwa kampuni ya 3 IN DALIMOUK MOTORS ya Dubai bila kuwepo kwa mkataba baina ya kampuni hiyo na ATCL ambapo kwa upande wa ATCL Mkataba huo ulipaswa usainiwe na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kinyume na kifungu cha 55 Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2008 na kanuni ya 15 ya sheria hiyo.

Katika shitaka la sita alidai ni la kusababisha hasara kampuni hiyo ya ndege ya taifa kinyume na kifungu cha 284(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 ,katika tofauti Julai 2007-Desemba 2001 jijini Dar es Salaam.Washtakiwa wote wakiwa waajiliwa wa ATCL ,walishindwa kuchukua taadhali na wakanunua magari hayo ya mitumba 26 toka kwa kampuni hiyo bila kuwepo kwa bajeti iliyotengwa na serikali kwaajili ya kununulia magari hayo.

Baada ya kumaliza kuwasomea mashtaka hayo mapya ,wakili Kimaro akaiomba mahakama iwasomea maelezo ya awali washtakiwa, ombi ambalo lilipingwa vikali na mawakili wa utetezi Alex Mgongolwa na Peter Swai ambao waliomba maelezo hayo ya awali yasisomwe jana ili wapate waende wakayasome ili siku ya kuja kusomwa kwa maelezo hayo ya awali wawe wameelewa nini wanakikataa na nini wanakikubali hata hivyo wakili mwandamizi wa serikali Tibabyekomya alipinga hoja hiyo kwasabababu haina sababu za msingi na kuiomba mahakama ikubali wawasomee washtakiwa hao maelezo ya awali.

Malumbano hayo yalisababisha Hakimu Tarimo saa nne asubuhi aiarishe kesi hiyo hadi saa 6:40 ili aje kutolea uamuzi wa ama maelezo ya awali yasome au yasisomwe jana ambapo alilikataa ombi la upande wa Jamhuri lilotaka kuwasomea maelezo hayo ya awali washtakiwa jana kwamaelezo kuwa ili haki ionekane imetendeka ni lazima upande wa wadaiwa nao upewe nafasi ya kujiandaa kwaajili ya washtakiwa kusomea maelezo .

Akitoa masharti ya dhamana kwa washtakiwa hao, Hakimu Tarimo alisema ili mshtakiwa apate dhamana kwa mujibu wa hati hiyo mpya ya mashtaka ni lazima kila mshtakiwa atoe fedha taslimu au kuwasilisha mahakamani hati ya mali isiyoamishika yenye thamani ya Sh milioni 38 na washtakiwa hao walitimiza masharti hayo ya dhamana kwa kuwasilisha hati za mali isiyoamishika na kesi imearishwa hadi Machi 20 mwaka huu, ambapo kesi hiyo nitakuja kwaajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Novemba 22 mwaka 2011,washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza wakikabiliwa na makosa matatu,kosa la kwanza lilikuwa ni la kushindwa kutunza kumbukumbu za mawasiliano ya manununuzi ya magari hayo waliyokuwa wamefanya na kampuni hiyo na kosa la tatu ni la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma ambalo lilikuwa likimkabili Mattaka peke yake.

Itakumbukwa kuwa Rais Jakaya Kikwete alipochaguliwa kuwa rais wa Tanzania Desemba 21 mwaka 2005 muda mchache baadaye alimteua Mattaka kuwa mkurugenzi wa shirika hilo la ATCL na kisha baadaye kumteua Mattaka kuwa Mjumbe wa Tume ya Rais ya Kikosi Kazi cha Kurekebisha Shirika la Bima la Taifa.

Wakati Rais Kikwete akimteua Mattaka kushika nyadhifa hizo katika kipindi cha Serikali ya awamu ya nne, wananchi mbalimbali walilaani uteuzi huo bila mafanikio.

Na kabla ya Rais Kikwete kumteua Mattaka kushika nyadhifa hizo,Rais wa serikali ya awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alikuwa amemstaafisha Mattaka kwa manufaa ya umma.Na wakati Mkapa anamstaafisha mshtakiwa huyo kwa manufa ya umma alikuwa akishikilia cheo cha Ukurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pesheni wa Mashirika ya Umma(PPF).

CHANZO;GAZETI LA TANZANIA DAIMA LA JUMAMOSI, MACHI 17 MWAKA 2012.

MASHAHIDI 10 KUMVAA LIYUMBA



Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kukutwa na simu gerezani inayomkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania, Amatus Liyumba umeiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa unatarajia kuleta jumla ya mashahidi 10 na vielelezo 10 katika kesi hiyo siku itakapoanza kusikilizwa.


Wakili wa Serikali Hamphrey Marick mbele ya Hakimu Mkazi Stewart Sanga alitoa maelezo hayo jana mahakamani hapo ambapo kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya upande wa jamhuri kumsomea maelezo ya awali ambapo alimsomea maelezo ya awali mshtakiwa huyo ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea Majura Magafu.

Wakili Marick akimsomea maelezo ya awali, alidai kuwa Julai 27 mwaka 2011 , Liyumba alikuwa ni mfungwa mwenye Namba 303/2010 ambaye alikuwa amefungwa katika gereza la Ukonga baada ya mahakama hiyo mwaka 2010 kumhukumu kifungo cha miaka miwili jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma.

Wakili Marick alidai mshtakiwa huyo akiwa gerezani alikutwa na kifaa kilichozuiwa na Sheria ya Magereza ambacho ni simu ya mkononi aina ya Nokia 1280 yenye rangi nyeusi ambayo ilikuwa na line yenye namba 0653 0004662 na IMEI namba 356273/04/276170/3.

Aliendelea kudai siku hiyo ya tukio mshtakiwa huyo alikuwa katika chumba binafsi namba tisa gerezani humo ambapo ndiyo alikuwa akiishi. Na kwamba mfungwa mwenye namba MF 891/169 Hamidu Henji “Tiba” ambaye ni Nyapara, alikuwa akitembea akitembea katika gereza hilo na alimuona Liyumba akiwa ameshika mfuko wa kuifadhia miwani akiwa ameugesha masikioni mwake.

“Mara baada ya Liyumba kumuona Nyapara huyo aliuweka chini ule mfuko wa miwani na kubakia akiongea na simu na hata hivyo Nyapara huyo tayari alikuwa ameishaiona ile simu na ule mfuko na haraka sana Nyapara huyo akaenda kutoa taarifa kwa maofisa wa Magereza waliokuwa kwenye doria siku hiyo gerezani humo”alidai wakili Marick.

Alidai kuwa maofisa hao waliopewa taarifa za tukio hilo na Nyapara huoni ni askari Magereza mwenye namba mwenye namba B 4948 WDR, Patrick na B 4885 WDR Iman Kyejo na askari hao walipokwenda kukagua chumba alichokuwa akiishi Liyumba,walifanikiwa kumkuta Liyumba akiitumia simu hiyo huku akiwa anatuma ujumbe mfupi(SMS) na kwamba kabla ya kutenda kosa hilo, hapo awali akiwa gerezani aliwahi kuonywa aache kutumia simu akiwa gerezani.

“Liyumba alipokutwa na maofisa hao akiitumia simu hiyo chumbani kwake aliamaki na akaomba kwanza wampatie dawa za ugonjwa shinikizo la Damu ili ameze na maji ya kunywa na maofisa hao walimpatia vitu hivyo alivyowaomba na baadaye wakampeleka Liyumba kwa Ofisa Msimamizi Mkuu wa Gereza:

“Akiwa katika ofisi ya Msimamizi Mkuu wa gereza hilo kwaajili ya kuanza kuchukuliwa maelezo,Liyumba akawaeleza maofisa hao kuwa hawezi kutoa maelezo yake kwanjia ya mdomo bali atatoa maelezo yake kwa njia ya maandishi na katika maelezo yake aliyoyatoa kwa njia ya maandishi ,mshtakiwa huyo alikiri kukutwa na simu gerezani’alidai wakili huyo wa serikali.

Wakili Marick alidai kuwa katika maelezo hayo Liyumba alieleza pia kuwa aliichukua simu hiyo kwenye Simintenki la kuifadhia maji ambalo lilikuwa karibu na Pampu ya maji ndani ya gereza hilo na kwamba hakuwai kukabidhi simu kwa hiyo kwa ofisa yoyote wa magereza kwasababu alikuwa anaiitaji kuitumia kwa kufuatilia hoja za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU).

Hata hivyo Liyumba alikanusha maelezo hayo na Hakimu Sanga akaiarisha kesi hiyo hadi Aprili 13 mwaka huu, ambapo kesi hiyo itakuja kwaajili ya mashahidi wa upande wa Jamhuri kuanza kutoa ushahidi wao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Machi 16 mwaka 2012.

KAJALA KUSOTA RUMANDE


Na Happiness Katabazi

MSANII wa Filamu nchini, Kajala Masanja na mumewe Faraja Chambo jana walijikuta wakiifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabili na makosa matatu likiwemo kosa la kutakatisha fedha haramu.


Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKUKURU), Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo alidai kuwa washtakiwa hao ambao ni wanandoa na wanatetewa na wakili wa kujitegemea Alex Mgongolwa wanakabiliwa na makosa matatu.

Wakili Swai alidai kuwa kosa la kwanza ni la kula njama kinyume na kifungu cha 34 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 ambapo washtakiwa wote kwa pamoja walitenda kosa hilo la kula njama la kuamisha umiliki wa nyumba iliyopo Kunduchi Salasala jijini Dar es Salaam.

Shtaka la pili ni ni kwamba Aprili 14 mwaka 2010 waliamisha isivyo halali umiliki wa nyumba hiyo kinyume na kifungu cha 34(2)A(3) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.

Alidai shtaka la tatu ni la kutakatisha fedha ambalo walilitenda siku hiyo ya Aprili 14 mwaka 2010 huku wakijiua ni kinyume na sheria hiyo.

Hata hivyo mshtakiwa wa pili (Chambo) wakati wanasomewa mashtajka hayo jana hakuwepo mahakamani kwasababu yupo gerezani kwakuwa anakabiliwa kesi nyingine ya utakatishaji fedha ambayo ipo katika mahakama hiyo na kwa mujibu wa sheria kosa la kutakatisha fedha halina dhamana.

Kajula alikanusha mashtaka hayo na wakili Swai alidai upelelezi bado haujakamilika.Hakimu Fimbo aliarisha kesi hiyo Aprili 20 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa na akaamuru Kajala arudishwe rumande kwa sababu kosa la kutakatisha fedha linamkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Machi 16 mwaka 2012.

MTIKILA ANASWA KESI YA KUMWITA JK GAIDI


Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imesema Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Part(DP), Mchungaji Christopher Mtikila ana kesi ya kujibu katika kesi ya kuchapisha na kuusambaza waraka wa uchochezi dhidi ya Rais Jakaya Kikwete.


Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Mkazi Sundi Fimbo ikiwa ni siku chache baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wake baada ya kuwaleta mashahidi watano kutoa ushahidi wao.

Hakimu Fimbo alisema baada ya kupitia ushahidi wa upande wa Jamhuri,amefikia uamuzi wa kumuona Mtikila ana kesi ya kujibu na kwamba maana hiyo Mtikila atatakiwa na mahakaa hiyo kupanda kizimbani Aprili 11 mwaka huu kwaajili ya kuanza kujitetea.


Baada ya Hakimu Fimbo kutoa uamuzi huo, Mtikila alidai kuwa anatarajia kuleta mashahidi 10.

Februali mwaka huu, Mtikila alikiri maelezo aliyochukuliwa na afisa wa polisi ni yake na kwamba hana pingamizi nayo na hivyo mahakama iliyapokea kama kielezo cha upande wa jamhuri.Mtikila katika maelezo hayo ya onyo alikiri kuwa ni kweli aliuandaa waraka huo na kuusambaza ila akakanusha waraka huo si wa uchochezi ila unahusu maneno ya mungu.

Mtikila alikiri maelezo hayo yaliyosomwa na kutolewa mahakamani kama kielelezo baada ya shahidi wa Jamhuri, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Ibeleze Mrema (54) kudai kwamba Aprili 15, mwaka 2010 akiwa kituo cha polisi kikuu jijini Dar es Salaam, aliitwa na mkuu wake wa kazi na kumpa kazi ya kumhoji Mtikila kuhusu tuhuma za kukutwa na waraka wa uchochezi.

Alidai kuwa wakati akimhoji mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na nyaraka hizo na kwamba alikuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya kuokoa wakristo na alisaini yeye waraka huo.

“Mtikila alikiri kuhusika kuandaa waraka huo kama mwenyekiti alisaini kwa niaba ya wengine … nilipomhji walichapisha wapi mtikila hakupenda kusema bali alidai kuwa zilikuwa nyaraka 100,000 ambazo zilisema kwamba Rais Kikwete anaangamiza ukristo na amekuwa jasiri kuingiza uislamu katika katiba ya Jamhuri” alidai Mrema kupitia maelezo hayo yaliyotolewa na Mtikila.


Mrema aliendelea kudai kupitia maelezo hayo kwamba, Mtikila alikuwa anahamasisha wakristo wajitoe mhanga kukomesha ugaidi na wamuweke rais mkristo Ikulu.

Ilidaiwa kuwa kati ya Januari mwaka 2009 na Aprili 17, mwaka 2010 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya uchochezi mshitakiwa alisambaza kwa umma nyaraka zilizosema 'Kikwete kuuangamiza ukristo', 'wakristo waungane kuweka mtu Ikulu' alinukuliwa Mtikila.

Katika shitaka la pili, Aprili 16, mwaka 2010 eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam, bila kibali alikutwa akimiliki waraka wenye uchochezi kwa jamii.Na katika kesi hii Mtikila hana wakili wa kumtetea na anajitetea mwenyewe.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumatano, Machi 14 mwaka 2012.

MTEJA AIBURUZA AIRTEL KORTINI

Na Happiness Katabazi

MTEJA wa kampuni ya simu ya mkononi ya Airtel Tanzania,Bernard Samson Thobias ameifungulia kesi ya madai ya ya fidia ya shilingi milioni 60 kampuni hiyo katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam, akitaka imlipe kiasi hicho cha fedha kwasababu ilimtangaza yeye kuwa ndiye mshindi wa Promosheni ya Kwanjuka sms Promotion lakini ikashindwa kumlipa shilingi 50,000,000 alizoshinda.

Thobias ambaye ni mlemavu wa masikio asiyesikia vizuri na anatetewa na wakili wa Kituo cha kutetea Haki za Binadamu, Fulgence Masawe amefungua kesi hiyo ya madai namba 12/2012 ambayo tayari imeishapangwa kwa Hakimu Rusema kwaajili ya kusikiliza.

Kwa mujibu wa hati ya madai ambayo gazeti hili inalo, inaeleza kuwa Thobias ni mteja wa kampuni ya airtel na ni mmiliki aliyeandikishwa na namba yake ni 0686-163144. Na bahati nasibu hiyo ilianza kuchezeshwa na kampuni hiyo kuanzia Aprili hadi mwanzo mwa Agosti 2011.Na kwamba Thobias alianza kushiriki kwenye bahati nasibu hiyo Mei ,2011 na mshindi alikuwa akitakiwa apewe Shlingi milioni 50.

Wakili Masawe anadai kuwa mteja wake huyo alianza kushiriki mchezo huo kuanzia Agosti 2011 na akajikusanyia zaidi ya pointi milioni 20 katika mchezo huo ambao mshindi alitakiwa apewe shilingi milioni 50, na kwamba Agosti 4 mwaka jana, na tangazo la yeye kuwa ndiye ameibuka mshindi lilitangazwa na mfanyakazi wa kampuni hiyo ambae alikuwa akitumia namba 0784 100778.

Wakili huyo anadai, baada ya mdaiwa kumpigia simu hiyo mteja wake, mteja wake aliamua kutoa kijijini alikokuwa akiishi na kuja katika ofisi za airtel kwaajili ya kufuatilia hiyo zawadi yake lakini alipofika katika ofisi za mdaiwa na kujitambulisha aliaelezwa na ofisa mmoja wa kampuni hiyo yeye siyo mshindi ila ameshindwa shilingi milioni moja za kitanzania na kwamba kwa ajabau hata hiyo shilingi milioni moja aliyoelezwa ameshinda hakupewa na kampuni hiyo hadi sasa.

“Mteja wangu kupitia wakili wake kabla ya kufungua kesi hii tulifanya juhudi za kuwasiliana uongozi wa juu wa kampuni hiyo kujua ni kwanini wanakataa kumlipan fedha hiyo aliyoshijnda, mdaiwa katika majibu yake alikiri kampuni yake kumpigia simu ya kumualifu kuwa ameshinda lakini kampuni hiyo ilishangaa wakati lipompigia simu mwanzo alipokela mlalamikaji lakini baada ya muda simu hiyo ikapokelewa na mkewe….na kwamba Thobias ni mlemavu wa masikio na asikii vizuri na kwamba uthibitisho wa kuwa yeye ni mgonjwa wa masikio umeandikwa katika ripoti ya uchunguzi uliofanywa na madaktari wa hospitali ya Taifa ya Muhimbili’alidai wakili Masawe.

Aidha alidai kuwa kwa sababu kampuni hiyo ndiyo iliyompigia simu mteja wake kuwa ameshinda na anastahili kupokea zawadi hiyo hajapewa eti kwasababu simu aliyopigiwa ilipokelewa na mkewe na hivyo kampuni hiyo kuchanganyikiwa na kwakuwa mteja wake amekuwa mara kwa mara akifika katika ofisi za kampuni hiyo kudai zawadi yake bila mafanikio, anaiomba mahakama iiamuru kampuni hiyo imlipe sh milioni 60 kama fidia ya usumbufu alioupata.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi 13 mwaka 2012

MADAKTARI,WAUNGWANA HAWASIFIWI USHENZI



Na Happiness Katabazi

HII ni mara ya pili narudia kuandika makala hii ambayo ninaendelea kusisitiza mgomo wa madaktari uliofanyika Februali mwaka huu na mgomo mwingine ulioanza Machi 7 mwaka huu ,huenda una ajenda mbaya nyuma yake na tusipokuwa macho ipo siku tutajikuta unatufikisha baya kama taifa.


Na kwamba mgomo huu haramu wa Februalia mwaka huu , ulilelewa na serikali yetu na ndiyo maana leo hii madaktari hao wameanza kuwa na kiburi cha kutoa amri kwa rais Jakaya Kikwete kutaka aridhie mawaziri hao wajiuzuru ama sivyo watagoma tena.
Madaktari hao wanaposhinikiza Waziri wa Afya Dk.Haji Mponda na Naibu wake Dk.Lucy Nkya wajiuzuru hadi kufikia jana,ni wazi wanamshikiniza rais wa nchi awawajibishe hao wateule wake na aridhie kujiuzuru kwao hata kama yeye haoni haja kwa wateule wake wajiuzuru.

Ibara ya 37(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasomeka hivi “Mbali na kuzingatia masharti yaliyomo katika Katiba hii, na sheria za Jamhuri ya Muungano katika utendaji wa kazi na shughuli zake, Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote , isipokuwa tu pale anapotakiwa na Katiba hii au na sheria nyingine yoyote kufanya jambo lolote kulingana na ushauri anaopewa na mtu au mamlaka yoyote”.
Kwa hiyo ibara hiyo inampa uhuru rais katika utendaji kazi na shughuli zake hatalazimika kufuata ushauri atakaopewa na mtu yeyote isipokuwa pale anapotakiwa na Katiba na Sheria. Kwahiyo kumbe mashinikizo hayo ya madaktari na wanaharakati kumshinikiza rais awawajibishe mawaziri, rais halazimiki kisheria kufuata ushauri huo wa madaktari.

Nalazimika kuamini hivyo kwani mwishoni mwa wiki iliyopita Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania(MAT), Dk.Namala Mkopi alizungumza baada ya kumalizika kwa mkutano wa madaktari uliofanyika Dar es Salaam, ambapo alisema yeye na chama chake wameazimia kugoma kuanzia jana ikiwa Waziri wa Afya, Dk.Haji Mponda na Naibu wake Dk.Lucy Nkya hawatajiuzuru nyadhifa zao kwani mgomo wa awali ulisababisha vifo vya wananchi wengi na kwamba mawaziri hao ni kikwazo katika majadiliano yao na serikali.

Dk.Mkopi alikwenda mbali zaidi na kujinasibu kuwa mgomo huo utakuwa ni mgomo mkubwa na wa aina yake.Tamko hilo linasikitisha na kukera.

Wakati Dk.Mpoki na hao madakatri wenzake wakifikia uamuzi huo serikali kupitia Waziri Mkuu Mizengo Pinda Jumatatu wiki hii, amenukuliwa na gazeti moja akisema anasikitishwa na uamuzi huo wa wanataaluma kwasababu serikali ingali ikiyafanyia kazi madai yao.

Na Juzi jioni Pinda amezungumza na waandishi wa habari kuhusu tishio hilo la mgomo na akawataka madaktari hao wasigome na kwamba sheria za nchi zinakataza baadhi ya wanataaluma wa aina fulani kugoma na kwamba serikali imejipanga kukabiliana na hali mgomo huo endapo utatokea.

Mapema kabisa naomba nieleweke kuwa madai yao ya kuboreshewa maslahi yao na kuboreshewa vitendea kazi kwa wanataaluma hao siyapingi.

Ninachopingana na chama hicho ni hali yake ya hivi sasa kutaka kuiweka serikali mifukoni mwao na wao ndiyo wawe wenye sauti ya mwisho na amri ya kuiamrisha serikali ifanye wanachokitaka wao na kwa muda wanaoutaka wao wakati kada nyingine kama walimu ambao ndiyo wamewatoa hao madaktari umbumbumbu ambao wana maisha mabaya sana kuliko wao lakini wanatumiaga busara sana katika kudai maslahi yao.

Ebu watanzania wenye akili timamu na tunaofikiri sawa sawa ,tuamke usingizini na tuanze kujiuliza huu ni mgomo kweli wa madaktari au kuna manyang’au ya kisiasa yenye uchu wa madaraka yanayotaka nchi hii isitawalike yameamua kuwatumia baadhi ya madaktari kuanzisha migomo kila kukicha ili serikali iliyopo madarakani ionekane ni dhahifu na imeshindwa kufanya kazi na wananchi wenzetu wapoteze maisha kwa kukosa huduma za kitabibu?

Aiingii akilini kabisa kwa madaktari ambao ni wasomi kwa ridhaa yao walianza kukaa meza moja ya majadiliano na serikali ili waweze kuyapatia ufumbuzi matatizo yao tena ndani ya kipindi kifupi tu serikali inasema ndiyo inaanza kuyafanyia kazi matatizo yao wanaibuka tena na kutaka mawaziri hao wajiuzuru mara moja na kwamba hivyo ndivyo walivyokubaliana na serikali kupitia Pinda na madaktari walitiliana saini Februali 9 mwaka huu.

Hivi nyie madaktari wa kisasa mmeona mgomo ndio dili sana? Hivi aliyeajiriwa katika hospitali kutoa huduma za kitabibu ni madaktari au waziri Mponda na Dk.Nkya?
Aliyegoma kutoa huduma za kitabibu kwa wagonjwa Februali mwaka huu, kwa zaidi ya wiki tatu na kusababisha baadhi ya wananchi kukosa huduma na wengine kufa kwa kukosa huduma ya kitabibu ni madaktari au mawaziri hao?

Sasa kwani huyu Dk.Mkopi anataka kujiepusha na hilo kuwa hata wao madaktari kama ni hivyo nao wanapaswa kuwajibika kwanza kwani ni wao waliutangazia umma kuwa wamegoma na wataalamu wa sheria wanatueleza mgomo wao wa awali ni batili kisheria?
Sawa mawaziri wanaweza kuwajibika baada ya kubainika kuwa walishindwa kusimamia vyema ofisi wanazoziongoza na mwisho wa siku uzembe huo ukasababisha madhara kwa wananchi.

Lakini vipi kuhusu nyie madaktari ambao mnaviapo vyenu ambacho vinawazuia msigome lakini miongoni mwenu mlisaliti viapo vyenu na mkagoma mbona na nyie hatuwasikii mkijisema kuwa katika hilo mlikiuka maadili ya kazi yenu?

Lakini hao wanaharakati na hao madaktari waache unafki wa kushinikiza waziri na naibu wake wajiudhulu peke yao bila kushinikiza na madaktari nao wachukuliwe hatua ya kukiuka viapo vyao kwa kugoma na kusababisha baadhi ya wananchi wenzetu kukosa huduma za kitabibu.

Serikali na wananchi kwa ujumla tuwe macho na madaktari wa aina hii kwani hawana msimamo na siku zote mtu au kiongozi yoyote asiye na msimamo mwisho wake anawaweza kutufikisha pabaya.

Ningali nikikumbuka katika mgomo wa awali, ni hawa hawa madaktari walijinasibu mfululizo kwenye vyombo vya habari kuwa kama hawataongezewa mishahara na kuboreshewa mazingira ya kufanyia kazi hawatasitisha mgomo, lakini Februali 9 mwaka huu, Pinda alipokwenda kuzungumza nao pale Hospitali ya Muhimbili akatangaza kuwa serikali imewaongezea posho na akaridhia kumsimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Brandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali Deogratius Mtasiwa kupisha uchunguzi , madaktari hawa walichekelea na wakarejea kazini.

Zilienea taarifa ambazo hadi sasa hazijathibishwa kuwa katika ule mgomo wa awali ni Brandina Nyoni ndiye haswa alikuwa anatakiwa aondolewe madarakani.Na uamuzi wa Pinda wa kumsimamisha kazi mama huyo ambaye baadhi ya madaktari wanamtambulisha kuwa ni mwanamke mbabe ni hatua ya mafanikio ya ajenda ya baadhi ya madaktari hao iliyokuwa imejificha.

Kuna baadhi ya watumishi wa Wizara ya Afya wanaeleza kuwa Nyoni alikuwa ni mwiba mkali na aliziba mirija ya fedha zisitumike ovyo na alipenda mambo yote yafanyike kwa kufuata utaratibu na siyo kienyeji na wengine walimtuhumu mama huyo si msafi.Vyovyote iwavyo minaamini ipo siku ukweli wa mambo utakuja kufahamika.

Kwa mtazamo wangu nasisitiza kuwa huenda kuna ajenda ya siri iliyojificha katika sakata hili la madaktari kwani aingii akilini kuwa madaktari hawa wamekubaliana na serikali matatizo yao yafanyiwe kazi na majadiliano baina yao yanaendelea ,wakati matatizo yao yanaanza kufanyiwa kazi wanatangaza kuibua balaa jingine la mgomo.

Huu ni uhuni na ufedhuli wa aina yake na serikali yoyote imara kokote duniani isingeweza kuuvumilia kwani mwisho wa siku tunaokuja kupata madhara makali ya mgomo huu ni sisi wananchi ambao hatuna uwezo wa kifedha wa kwenda kutibiwa hospitali binafsi za zile za nje ya nchi.

Niwaulize maswali wewe Dk.Steven Ulimboka na Dk.Namala Mkopi kama mnadini na kama dini zenu zinaruhusu kupata mshahara mnono kupitia vifo vya wagonjwa vilivyotokana na mgomo wa awali na mliohuamasisha?

Wewe Dk.Ulimboka,DK.Mkopi itokee kipindi cha mgomo mliouamasisha baba zenu,mama zenu waliowazaa,watoto wenu,wake zenu wanaitaji huduma ya upasuaji ya haraka ,mtakuwa tayari kutowapatia huduma kwasababu mpo kwenye mgomo? Bila shaka hamtakuwa tayari kwasababu wahenga walisema ‘damu nzito kuliko maji.

Sasa kama hivi ndivyo muwe na roho za utu,msipende maisha manono au kujipatia umaarufu kupitia migomo ambao mwisho wa siku sisi wananchi ambao kodi zetu ndiyo zimewasomesha na leo ndiyo zinawalipa mishahara ndiyo tunaoathirika.

Endapo rais Jakaya Kikwete ataridhia hao mawaziri wake Dk.Mponda na Dk.Nkya wajiuzuru kwaajili ya shinikizo la madaktari hao ambao hivi sasa wanajiona taaluma yao ni bora kuliko taaluma zingine hapa nchini , basi siku si nyingine yeye Kikwete na waziri mkuu Pinda nao watajikuta wakijiuzuru nyadhifa zao kwa mashinikizo ya aina hiyo.

Na mwisho wa serikali ya awamu ya nne itaweka rekodi ya viongozi wake kujiuzuru mara kwa mara, na kodi za wananchi zitakuwa zikitumika kuwalipa mafao na kuwatunza wastaafu hao.

Ikumbukwe kuwa hata kipindi kile cha mwaka 2008, wakati Waziri mkuu alikuwa Edward Lowassa, kuna watu waliokuwa hawataki Lowassa aendelee kuwa waziri mkuu kwa sababu anaandamwa na tuhuma mbalimbali za ufisadi, na watu hao walifanikiwa kupenyeza ajenda yao kwenye vyombo vya habari, mitaani na kwingineko na hatimaye waasisi wa ajenda hiyo walifanikiwa kumjaza jazba Lowassa na hatimaye mwisho wa siku bungeni badala ya kujibu hoja zilizowasilishwa na Kamati ya Bunge kuchunguza mkataba wa kampuni ya kufua umeme ya Richmond LLC, akaishia kusema kusema ‘nimesikitishwa sana, nimeuzunishwa sana na nimekasilishwa sana….’ Akatangaza kujiuzuru wadhifa wake na kisha Pinda akatangazwa kumrithi.

Kwa maana hiyo basi mgomo huu wa madaktari vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa vifanye kazi yake kikamilifu na kubaini mgomo huo ni wa madaktari kweli au kuna watu wanaotaka madaraka ya urais na kuonyesha serikali hii imeshindwa kuongoza.

Natoa rai kwa madaktari wote wawe makini na vinara wa migomo hiyo ya madaktari kwani tayari kuna taarifa za chini chini kuwa vinara wa migomo hiyo ya madaktari wanatarajia kuingia kwenye ulingo wa siasa kwenye baadhi ya majimbo na kwamba wanatumia migomo hiyo kujijengea umaarufu miongoni mwa wa Tanzania kuwa wao ni viongozi shupavu na wanastahili kupewa nyadhifa za uongozi kupitia damu za watanzania maskini na migongo ya madaktari wasiyojua siri iliyojificha katika migomo hiyo.

Naomba serikali iwachukulie hatua viongozi wa mgomo huo kwasababu wanachokifanya hakina tofauti na maofisa wenye nyadhifa za juu serikali ambao walifikishwa pale Mahakama ya Kisutu kwa makosa mbalimbali ya jinai kama matumuzi mabaya ya ofisi ya umma, uhujumu uchumi na wizi.lakini hawa vinara wa migomo ya madaktari kwa mtazamo wangu naona wanafanya makosa ya wazi ya mauaji ya kukusudia kwani daktari au nesi anapokataa kumtibia mgonjwa ni wazi anataka mgonjwa huyo afe.

Kwanza vinara hawa wa mgomo mnapotembea mkae mkijua mnanuka damu za watanzania maskini waliokufa katika mgomo wa awali.Na kana kwamba hiyo mmeona haiwatoshi mnataka damu nyingine kwa kuitisha mgomo wa pili ambao mmepanga uanze jana.
Ushauri wangu kwenu nyie madaktari kama mnaoa fani ya udaktari hailipi,ingieni kwenye ulingo wa siasa rasmi kama walivyofanya madaktari wenzenu na baadhi ya wasomi wa ngazi juu wenye shahada mbili na tatu.

Ikumbukwe kuwa baadhi ya marais waliowahi kushika nyadhiza za urais katika baadhi ya nchi walikuwa wakitumia vyama vya wafanyakazi kuhamasisha migomo na tafrani kila kukicha kwa serikali iliyopo madarakani na kwa kuwa vyama hivyo vilikuwa na nguvu mwisho wa siku vilifanikiwa kuwang’oa marais waliokuwa madarakani na kisha marais waliokuwa wakivitumia vyama hivyo vya wafanyakazi wakafanikiwa kushika nyadhifa za urais.

Na mfano wa marais waliojijenga kupitia migomo na kufanikiwa kupata madaraka ya nchi ni rais wa Zambia, marehemu Fredrick Chiluba, Waziri Mkuu wa sasa wa Zimbambwe Morgan Shivangilai na wengine wengi.

Sisi kama Tanzania tusijidanganye kwamba hilo halitaweza kutokea hapa nchini kwakuwa hatujampa mungu rushwa, kwani akili, tabia, na roho za Watanzania wengi hivi sasa zimebadilika wengi wetu tumekuwa na tamaa ya kupata madaraka, mali kwa njia isiyompendeza mungu na tumekuwa na roho za kikatili kama hawa visokorokwinyo wanaoongoza mgomo wa madaktari na hatupendani,tumekuwa mabingwa wafitina na wanafki kama ilivyokuwa miaka nyuma,tumeanza kukumbwa na tabia ya ubinafsi na umimi.

Nimalizie kwa kuwakumbusha vinara wa mgomo wa madaktari usemi wa wahenga usemao ‘muungwana asifiwi ushenzi, bali usifiwa kwa matendo yake yaliyomema’.

Mungu ibariki Tanzania,Mungu Ibariki Afrika
0716 774494

Chanzo:www.katabazihappy.blogspot.com
. Machi 9 mwaka 2012

KIBANDA ABADILISHWA HATI YA MASHTAKA




Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kuchapisha makala ya uchochezi inayomkabili Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima, Absalom Kibanda na mwandishi Samson Mwigamba jana ulishindwa kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao na badala yake umeibadilisha hati ya mashtaka na pia kumuongeza mshtakiwa mmoja.


Katika hatua nyingine kwa mujibu wa hati hiyo ambayo gazeti hili lina nakala yake inayoonyesha imeletwa mahakamani hapo kwa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DDP), Dk.Eliezer Feleshi ambaye aliisaini Machi 6 mwaka huu, majina ya washtakiwa yanasomeka kimakosa kama ifuatavyo Samson Maingu Mwigamba, Absalom Norman Kibamba na Theophil Christian au Maingu.

Wakati majina sahihi ya washtakiwa hao yalipaswa yasomeke kwa usahihi kama ifuatavyo Mangu Samson Mwigamba ,Absalom Norman Kibanda na Theophil Christian Makunga. Lakini mwisho wa siku ni mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kutamka vinginevyo kuhusu hati hiyo.

Wakili wa Serikali Elizabeth Kanda mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema, alianza kwa kuikumbusha mahakama hiyo kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya upande wa Jamhuri kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao lakini imeshindwa kufanya hivyo kwasababu inabadilisha hati ya mashtaka na kumwongeza mshtakiwa mwingine ambaye alikuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd, Theophil Makunga na hivyo kufanya kesi hiyo jinai Na.289 ya mwaka 2011.

Wakili Kaganda akiisoma hati mpya ambayo ina mashtaka mawili tu ambapo kosa la kwanza ni la uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1)(c) na 31(1)(a) cha Sheria ya Magazeti Sura ya 229 ya mwaka 2002 ambalo lina mkabili mshtakiwa wa kwanza na wa pili yaani Mwigamba na Kibanda ambao wanatetewa na mawakili wa kujitegemea Isaya Matamba, Juvenalis Ngowi na John Mhozya.

Ambapo wakili Kaganda alidai kuwa mnamo Novemba 30 mwaka 2011 jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao wawili kwa makusudi na kwa nia kuvunja sheria za mamlaka ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walitenda kosa hilo la uchochezi kwa kuruhusu makala hiyo ichapishwe kwenye gazeti la Tanzania Daima la Novemba 30 mwaka 2011 iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “ Waraka Maalum kwa askari wote’ ambapo ilikuwa ikiwachochea askari hao wasitii mamlaka za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika shtaka la pili ambalo linamkabili Makunga peke yake ni la kuchapisha makala hiyo ya uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1)(c) na 31(1)(a) cha Sheria ya Magazeti Na.229 ya mwaka 2002 , ambapo alidai kuwa Novemba 30 mwaka jana Makunga akiwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Ltd, ilichapisha makala hiyo ya uchochezi iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “ Waraka Maalum kwa Askari wote’ ambayo ilichapishwa kwenye gazeti la Tanzania Daima.

Hata hivyo washtakiwa hao wawili yaani Mwigamba na Kibanda ndiyo waliokuwepo mahakamani walikanusha kosa hilo, lakini Makunga hakuwepo mahakamani na wakili Kaganda akaiomba mahakama itoe hati ya wito ya kumuita Makunga mahakamani ili aje asomewe shtaka linalomkabili katika kesi hiyo na kwamba wanaiomba mahakama hiyo iwapangie tarehe ya kujakuwasomea maelezo ya awali washtakiwa wote hao wa tatu.

Kwa upande wake Hakimu Mkazi Lema alikubaliana na maombi hayo ambayo alitoa amri ya kutoa wito wa kuitwa mshtakiwa wa tatu(Makunga) kuitwa mahakamani na kwamba Machi 26 mwaka huu, kesi hiyo itakuja kwa upande wa jamhuri kuwasomea maelezo ya washtakiwa hao.

Kubadilishwa kwa hati hiyo ya mashtaka jana kumefanya sasa washtakiwa hao kushitakiwa kwa kosa hilo la uchochezi na kuchapisha makala hiyo ya uchochezi kwa kinyume na Sheria ya ya Magazeti ya mwaka 2002 na siyo kama ilivyokuwa hapo awali ambao washtakiwa hao yaani Mwigamba na Kibanda walikuwa wakishtakiwa kwa makosa ya kuchapisha makala iliyokuwa inachochea uasi kwa askari na maofisa wa Jeshi la Ulinzi(JWTZ), Jeshi la Polisi na Magereza kinyume na Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 , kwamba askari hao wasitii amri zinatolewa na makamanda wao.
Desemba 21 mwaka jana, upande wa Jamhuri ulibadilisha hati yake mashtaka kwa kumuongeza mshtakiwa wa pili(Kibanda) na hivyo kufanya jumla ya washtakiwa kuwa wawili yaani Mwigamba na Kibanda.

Ambapo wakili Kaganda alidai washtakiwa alidai wanakabiliwa na kosa moja la kuwashawishi askari na maofisa wa jeshi la polisi, magereza na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) kutoendelea kuitii serikali iliyopo madarakani kwa sasa ambayo inaongozwa na Rais Jakaya Kikwete kinyume na kifungu cha 46(b),55(10(a) na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Desemba 8 mwaka jana, Mshtakiwa wa kwanza Mwigamba ambaye ndiye aliyeandika makala hiyo inayodaiwa na upande wa Jamhuri kuwa ni uchochezi alifikishwa mahakamani hapo peke yake kwa kosa hilo ambapo mwisho ilipofika Desemba 21 mwaka jana ndipo Jamhuri ilibadilisha hati ya mashtaka kwa kumuongeza Kibanda.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Machi 8 mwaka 2012

UGONJWA WA DK.MWAKYEMBE USITUGAWE



Na Happiness Katabazi

ITAKUMBUKWA kuwa tangu Oktoba 2 mwaka jana, Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi Dk.Harrison Mwakyembe aliondoka hapa nchini na kupelekwa India kwaajili ya matibu, maneno maneno na hisia mbalimbali zimekuwa zikibuliwa kupitia vyombo vya habari na huko mitaani.


Kuna watu wamediriki kujitokeza adharani na kwanjia ya mitandao ya kijamii akiwemo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Samwel Sitta zaidi ya mara moja amenukuliwa na vyombo vya habari akisisitiza Dk.Mwakyembe amelishwa sumu na mafisadi bila kuyataja majina hayo ya mafisadi.

Na wengine wamekuwa wakienda mbali zaidi kupitia hiyo mitandao ya kijaami wakijinasibu kuwa wamefanya uchunguzi wao binafsi kuhusu chanzo cha ugonjwa anaosumbuliwa nao naibu waziri huyo na Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya na wakaitimisha kwa kusema serikali kupitia Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) ambayo kwasasa inaongozwa na Mkurugenzi Mkuu Rashid Othman.

Kwa wale wanaotembelea mitandao hiyo ya kijaami karibu kila siku watakubaliana na mimi kuna taarifa moja zinawekwa humo ambazo waandishi walioandika taarifa hizo wanadai kuwa wamefanya utafiti na kubaini kuwa ni maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa ndiyo wameshiriki kikamilifu kumdhuru Dk.Mwakyembe na Profesa Mwandosya.

Na siyo waraka huo tu pia kuna waraka mwingine ambao unadaiwa kuandikwa na Mwakyembe mwenyewe ambapo gazeti hili iliandika habari hiyo na kudai kuwa inayo nakala yake ambayo ndani ya wakala huo eti Dk.Mwakyembe amewataja kwa majina wabaya wake waliomtenda.

Na waraka huo ambao unadaiwa kuwa umeandikwa na Dk.Mwakyembe mwenyewe kwa ndugu na jamaa zake ambao hadi sasa hatujamsikia Dk.Mwakyembe akiukanusha, unaeleza kuwa kuna sabuni na kitaulo ambacho aliwekewa ofisini kwake na mhudumu na alipotumia ndiyo alianza kuwashwa na baada ya muda mfupi akasikia mhudumu alifariki na akaenda kuzikwa kijijini kwao Ipinda –Kyela mkoani Mbeya hali ambayo naibu waziri huyo anasema katika waraka huo kuwa kifo hicho cha ghafla cha mhudumu huyo kilimshtua.

Awali ya yote naomba nieleweke kuwa mtazamo huu hauna lengo la kupora matakwa ya Ibara ya 18 ya Katiba ya nchi ambayo yanampa haki mwanachi kueleza fikra zake kuhusu afya kiongozi huyo la hasha mtazamo huu una lengo la kuvitaka vyombo vya dora hususani kuamka usingizini na kuanza kuwashughulikia wale wote ambao wanaojitokeza adharani kwa majina yao halisi au bandia kueneza taarifa dhidi ya mgonjwa huyo kuwa amelishwa sumu bila kuambia ni watu gani wamemlisha sumu, na ni kwanini Dk.Mwakyembe alishwe sumu?Na alilishiwa wapi na lini?

Inawezekana madai hayo yana ukweli ndani yake kuwa lakini ikumbukwe kuwa kifungu cha 7(1) Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, kinasema mtu yoyote ambaye anafahamu kutendeka kwa kosa, mtu huyo ana wajibu wa kupeleka taarifa hizo katika vyombo husika ana akishindwa kufanya hivyo atashtakiwa kwa kosa la kusaidia kutenda kosa kinyume na Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Sasa hawa wanasambamba za taarifa kuwa Mwakyembe kapewa sumu kwenye mitandao na kwenye vyombo vya habari wanapaswa wapeleke taarifa hizo kwenye mamlaka husika na wakishindwa kufanya hivyo wanatakiwa waadhibiwe.

Ikumbukwe kuwa minong’ono na hisia kama hizo uliwahi kuibuka pia katika kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi(CCM), Horace Kolimba alizidiwa ghafla wakati yupo kwenye kikako cha Kamati Kuu kilichokuwa kikifanyika mjini Dodoma.

Baada ya kifo hicho kutokea Mwenyekiti wa Chama cha Democraty(DP), Mchungaji Chsristopher Mtikila alijitokeza adharani na kusema kuwa Kamati Kuu ya CCM, ndiyo iliyomua Kolimba kwani masaa manne kabla ya Kolimba kuingia kwenye mkutano ule alikuwa ni mzima wa afya.

Kufuatia matamshi hayo ambayo yalianza kujenga hisia mbaya kwa wana jamii, Jeshi la Polisi lilimkamata Mtikila na kumfungulia kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni na kisha Hakimu Gabriel Mirumbe ambaye ndiye aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo na mwaka 1999 alimhukumu Mtikila kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa hilo ambalo Mtikila alishindwa kuleta ushahidi ambao ungethibitisha maelezo yake kuwa ni kweli Kamati Kuu CCm ndiyo iliyomuua Kolimba.

Na Mtikila alitumikia adhabu hiyo katika gereza la Keko na alikata rufaa katika Mahakama ya Kuu na Mahakama ya Rufaa lakini rufaa zake zote mbili zilitupwa na mahakama hizo za juu nchini kwasababu waliona rufaa ya mwanasiasa huyo haina msingi wowote.

Kwa hiyo basi tunaweza kuona vyombo vyetu vya dola vikiamka usingizini na kuona hayo maneno na waraka mbalimbali unaondelea kusambazwa kupitia mitandao, vinaweza kuwachukulia hatua wale wote wanaosema Mwakyembe kalishwa sumu na serikali ,mafisadi kama alivyochukuliwa hatua Mtikila.Nimejiuliza hivi huyu Sitta na Mwakyembe wote si ni viongozi na hivyo ni sehemu ya serikali? Kwa hiyo nao basi wanawafahamu hao watu waliomtenda hivyo sasa kama wanawafahamu kwanini wasiwaje kwa majina kuliko kuishia kusema amelishwa sumu na mafisadi hivi hao mafisadi hawana majina mbona majina hamyataji?

Waraka mwingine unaodaiwa kuandikwa na Mwakyembe ambao eti amewaandikia ndugu na jamaa zake unasema anahisi matatizo yaliyompata uenda chanzo chake kinatokana na sabuni na taulo aliyokuwa amewekea ofisini kwake na mhudumu kwani baada ya kutumia vitu hivyo alianza kuwashwa.

Na kauli hizo za Sitta na Mwakyembe zimeanza kutufanya tuamini kuwa uwenda hawa wamejitenga na serikali yao na walichoamua sasa nikuanza kuipaka matope serikali yao kuwa inawakumbatia wauaji kwamba serikali tena haiwalindi viongozi wake.

Na kushindwa kwa vyombo vya dola kuwachukulia hatua watu wa aina hiyo ni wazi kabisa vyombo hivyo hivyo vya dola vitakuwa vimeshiriki kikamilifu kujenga taifa la baadhi ya wananchi waropokaji, wenye chuki na hasira dhidi ya serikali yao kupitia TISS kuwa idara hiyo ndiyo ilimsababishia maradhi hayo Mwakyembe wakati idara hiyo ilikuwa na jukumu la kumlinda kiongozi na viongozi wengine.

Na tukiruhusu tufike huko ipo siku nchi hii itajikuta inaingia kwenye vita ya makabila au wenyewe kwa wenyewe .

Kila mmoja kwa nafasi yake alijuilize mfano ndiyo unamuuguza mzazi wako au ndugu yako halafu wanajitokeza watu kwenye vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii wanasema wazi kuwa maradhi yanayomsumbua mzazi wako au ndugu yako yamesababishwa na kikundi cha watu fulani au serikali kumlisha sumu?.

Ni wazi kabisa utaanza kujenga chuki na serikali na kikundi hicho na mwisho wa siku mtu yoyote ambaye alishapandikizwa chuki moyoni na akilini anaweza kulipiza kisasi kwa njia yoyote dhidi ya watu alielezwa kuwa ndiyo waliomdhuru mzazi wake hata kama hana ushahidi.

Ieleweke wazi Mwakyembe ni mtu aliwahi kuwa mwalimu pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,mbunge, pia ana watu wengi ambao anafahamiana nao nawao anawafahamu na aliowasaidia na waliomsaidia katika maisha.

Sasa inapotokea taarifa za yeye kulishwa sumu bila ya hao wanaozisambaza kutoa ushahidi kukutolea ushahidi amelishwa sumu na nani,lini na ni kwasababu gani hao watu wamlishe yeye ?

Ni wazi watu hao wanaofahamiana na Mwakyembe kama hawana roho nguvu na siyo waelewa wa mambo ni wazi kabisa wataanza kujenga hisia mbaya na chuki dhidi ya wale wanaodaiwa ni maadui wa naibu waziri huyo na serikali.

Nampa pole Mwakyembe kwa maradhi yanayomsumbua ila msimamo wangu ni kwamba siwezi kukubaliana moja kwa moja na wale wote wanaosema kiongozi huyo kalishwa sumu au kugusishwa kwani wameshindwa kuanika ushahidi ni nani aliyemlisha sumu, kwanini yeye alishwe sumu na alilishiwa wapi na hata yeye Mwakyembe hakuna sehemu yoyote ambayo ametamka amelishwa sumu?

Kwani hadi sasa ripoti ya madaktari waliomtibia tumeelezwa kuwa wamebaini kuna kitu kipo kwenye Bon Marro ndiyo kinamsumbua na kwamba wanaendelea na uchunguzi zaidi ya kitabibu .Sasa huko kulishwa kunakodaiwa na baadhi ya watu kunatoka wapi?

Nimalizie kwa kumshauri Dk.Mwakyembe kuwa hivi sasa anatakiwa azingatie ushauri anaopewa na madakatri wake wanaomtibia,amrejee mungu wake ,atulize akili yake na awakataze hao baadhi ya ndugu zake na yeye kueneza taarifa za hisia hasi kuhusu maradhi yayomkabili kwani minaona akiruhusu jamii iendelee kujadili anachoumwa ni wazi hali hiyo pia itakuwa inamsumbua kisaikolojia ata yeye pia pamoja na familia yake na kumshushia hata yeye heshima hasa ukizingatia yeye ni msomi wa sheria kwani wanasheria wanamsemo usemo usemao hoja kwa vielelezo.

Hivyo ni rai yangu kwa watanzania wote kuwa maradhi yanayomkabili kiongozi wetu huyo yasiwe chanzo cha kuusambaratisha ummoja wetu,ugonjwa wa kiongozi huo usigeuzwe ajenda ya kuanza kuwapandikiza chuki wananchi dhidi ya wananchi wenzao na serikali yao kuwa ndiyo waliomlisha sumu wakati tumeishaelezwa kuwa madaktari bado wanatafuta chanzo cha maradhi hayo yanayomsumbua .

Kwa kuwa ni dhahiri baadhi ya wananchi huko mitaani wameishaanza kuamini taarifa hizo kuwa ni kweli kalishwa sumu wakati hiyo ripoti ya daktari haijasema hivyo.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Jumapili, Machi 4 mwaka 2012
www.katabazihappy.blogspot.com

JK ALINIPA IDHINI YA KUNUNUA JENGO LA UBALOZI-MAHALU




Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete ndiye aliyempatia mamlaka ya kisheria (Special Power of Attoney) ya kununua jengo la Ubalozi wa Tanzania nchi Italia kwa kutimia njia ya mikataba miwili kwa thamani ya Euro 3,098,034
.


Sambamba na hilo Hakimu Mkuu Mfawidhi Elvin Mugeta ametupilia mbali pingamizi la wakili wa serikali Ponsian Lukosi,Ben Lincol lilotaka mahakama hiyo isipokee barua ya Machi 21 mwaka 2001 iliyoandikwa na Mahalu kwenda kwa Kikwete ambaye wakati huyo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akimwarifu kuhusu jengo hilo litauzwa na mwenye jengo kwa mikataba miwili.

Wakili Lukosi alidai kuwa barua hiyo ilikuwa ni ya siri na binafsi na siyo ya kiserikali, hoja mbayo hakimu huyo aliitupilia mbali kwa maelezo kuwa barua hiyo ni ya kiserikali kwani ina nembo ya serikali na inatunzwa na ofisi za serikali na kwamba nakala ya barua hiyo ya Mahali aliituma pia kwa viongozi wengine wa serikali na akasema anaipokea barua hiyo kama kielelezo cha upande wa utetezi.

Profesa Mahalu alitoa maelezo hayo kwa maandishi jana wakati akiongozwa kutoa utetezi wake na wakili wake Mabere Marando mbele ya Hakimu Mkazi Elvin Mugeta.Ambapo jana mshtakiwa huyo alimaliza kujitetea.

Profesa Mahalu ambaye tangu aanze kujitetea amekuwa akitumia nyaraka mbalimbali za serikali ambayo ni mawasiliano baina yake na viongozi wengine wa serikali kuhusu ununuzi wa jengo hilo lilivyonunuliwa kwa kutumia mikataba miwili ambapo alidai kuwa akiwa Balozi mjini Rome,Kikwete ambaye wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa alimpatia nguvu maalum ya kisheria ya (Special Power of Attoney) ya kununua jengo hilo kwa thamani ya Euro Milioni tatu ambapo nguvu hiyo ya kisheria inaonyesha kutolewa na rais huyo Septemba 2002 na kwamba aliipokea na kuifanyia kazi kwa vitendo na ilikuwa na saini ya rais Kikwete.

Aliendelea kueleza kuwa Machi 24 mwaka 2004 , alimwandia barua waziri wake Kikwete na kwamba ndani ya barua hiyo alikuwa ameambatanisha nyaraka zote za ununuzi wa jengo hilo la ubalozi ikiwemo mikataba miwili ya ununuzi wa jengo hilo na kipindi hicho tayari jengo hilo lilikuwa limeishanunuliwa na serikali na kwamba nakala ya barua hiyo nilimtumia Katibu Mkuu Kiongozi, Waziri wa Ujenzi John Magufuli, Mhasibu Mkuu wa Serikali wa wakati huo Brandina Nyoni na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje Na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo na akaomba atoe barua hiyo kama kielelezo ambapo pia mahakama ilikipokea barua hiyo kama kielezo.

“Mheshimiwa hakimu Aprili 23 mwaka 2008 shahidi wa tatu wa upande wa Jamhuri ambaye alikuwa ni mhasibu wa ubalozi huo Steward Migwano alipotoa ushahidi wake alileta nyaraka mikataba hiyo miwili na nyaraka za kibenki za kibalozi zilizokuwa zikionyesha jinsi ofisi ya ubalozi ilivyopokea fedha toka serikali ya Tanzania na jinsi ubalozi wetu ulivyokuwa ukizitoa fedha hizo kwa awamu na kwenda kumlipa mmiliki wa jengo hilo kwa awamu na itoshe kusema kuwa ushahidi wa shahidi huyo wa tatu wa jamhuri unaunga mkono utetezi wangu;

“Na Oktoba 24 mwaka 2008 shahidi wa tano ambaye ni Mchunguzi toka TAKUKURU, Isidori Kyando alitoa ushahidi unaotofautiana na ushahidi wangu na hotuba ya Kikwete aliyoitoa Bungeni Agosti 3 mwaka 2004 , ambapo shahidi huyo alidai yeye anautambua mkataba mmoja tu wa (Official price) ambao unaonyesha jengo hilo lilinuliwa kwa Euro Milioni 1,032,913.80 “ alidai Profesa Mahalu.

Profesa Mahalu alidai ushahidi wa Kyando unatofautiana na ushahidi wake na hotuba iliyotolewa na Rais Kikwete katika mkutano wa 16 Kikao cha 39 cha Bunge, Agosti 3 mwaka 2004, ambapo wao wawili yaani (Mahalu) na Kikwete kwa maandishi walieleza kutambua kuwa jengo hilo lilinuliwa kwa mikataba miwili ambapo mkataba wa kwanza ni ule wa (book value ) ambao unaonyesha jengo lilinuliwa kwa Euro milioni 1.032,913.80 na kisha jengo hilo katika tarehe tofauti likaja kununuliwa katika mkataba wa pili uotambulika kwa bei ya kibiashara(Commercial price) ambapo katika mkataba huo wa pili unaonyesha jumla jengo hilo lilinuliwa kwa thamani ya Euro 3,098,034.

Aidha aliendelea kueleza kuwa Rais Kikwete katika hotuba yake bungeni kuhusu sakata la ununuzi wa jengo hilo kwa mikataba miwili, alilieleza bunge kupitia Hansard ya bunge ukurasa wa 166, Rais Kikwete alisema “Naibu Spika mwaka 2001-2002 Wizara ya Mambo ya Nje ilinunua jengo hilo la ubalozi kwa thamani ya Euro 3,098,034 ili serikali iweze kuondokana na mzigo wa kupanga ofisi na kwamba ununuzi wa jengo hilo ulifuata taratibu sote za serikali na na kwamba tayaribu hizo zilipata baraka za wizara ya yake ,wizara ya ujenzi Fedha na kwamba Machi 6 mwaka 2002 serikali ilituma fedha za awali kwaajili ya manunuzi hayo katika ofisi za ubalozi wa Tanzania nchini Italia, na akaomba kumbukumbu hiyo ya bunge ipokelewa kama kielelezo ambapo Hakimu Mugeta alikipokea.

“Kwa hiyo mheshimiwa hakimu utaona bei ya manunuzi ya jengo hilo iliyotajwa na Rais Kikwete Bungeni na bei ya jengo hilo niliyoitaja mimi na yule shahidi wa upande wa Jamhuri Migwano zinafanana “alidai Mahalu.

Hata hivyo alidai kuwa anashangazwa na upande wa jamhuri kumfungulia kesi hiyo ya uhujumu uchumi kuhusu ununuzi wa jengo hilo kwasababu hadi upande mashtaka unaifunga kesi yake mwaka juzi, haujaleta ushahidi unaonyesha aliyekuwa akiuza jengo hilo alikuwa hajapa fedha hizo ambazo zilitumwa na serikali katika ubalozi wa Tanzania nchini Italia ili wamlipe muuzaji wa jengo lile na pia upande wa mashtaka haujaleta ushahidi wowote wa maneno au nyaraka unaonyesha serikali iliwahi kukataza au kulalamikia utaratibu wa ununuzi wa jengo hilo kwa njia ya mikataba miwili:

“Na ili kuithibitishia mahakama hii kuwa nchini Italia, kununua ardhi, jengo au kupangisha jengo mikataba miwili haizuwi kisheria naomba nitoe kitabu kilichoandikwa na mwandishi aitwaye Tobias Jones ambacho kina kichwa cha habari kisemacho “ The Dark Hearty Italy’ kama kielelezo.

“Ukurasa wa 139-140 wa kitabu hicho,Mheshimiwa hakimu, mwandishi huyo raia wa Italia, anaeleza wazi kuwa suala la mikataba miwili nchini ni la kawaida na wananchi wa Italia wamekuwa wakiifuata utaratibu huo ambao hauzuiwi kisheria na akafafanua kuwa mkataba wa kwanza ambao unaitwa (book value) ndiyo mwisho wa siku unakuwa hati ya mali liwe jengo au ardhi na kwamba katika ununuzi wa kupitia mikataba miwili risiti ya ununuzi inakuwa ni moja tu”alidai Profesa Mahalu.

Hata hivyo wakili Marando alipomuuliza Mahalu kuwa amewahi kupata rekodi yoyote ya ubadhirifu wa mali ya umma, Mahalu alikanusha hilo na kuonyesha yeye ana rekodi nzuri tena ya kimataifa zinazoonyesha yeye ni mhadilifu na akatoa zaidi ya medani tano mahakamani hapo alizotunukiwa na Raia wa Italia, na marais wengine dunia na mashirika mengine ya Kimataifa kwa ajili ya uhadilifu, uchapakazi wake na jitihada zake za kukuza ushirikiano wa kiuchumi baina ya Serikali ya Italia na Tanzania.

Wakili Marando alidai kuwa huo ndiyo mwisho wa utetezi wa Mahalu na Wakili wa Jamhuri Lukosi akadai kuwa hayupo tayari jana kuanza kumhoji mshtakiwa huyo na kwamba anaomba kesi hiyo iarishwe ili aweze kwenda kujiandaa ombi ambalo lilikubaliwa na Hakimu Mugeta ambaye aliarisha kesi hiyo hadi Machi 21 mwaka huu, ambapo siku hiyo upande wa Jamhuri utaanza kumhoji mshtakiwa huyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Machi Mosi mwaka 2012

MAWAKILI WA UTETEZI WAKWAMISHA YA RICHMOND

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ilijikuta ikishindwa kuanza kusikiliza rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) dhidi ya aliyekuwa kigogo wa Kampuni ya Kufua umeme ya Richmond LLC , Naeem Gile kupinga uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mwaka jana ulimuona mshtakiwa huyo hana kesi ya kujibu.


Rufaa hiyo Na.126 ya mwaka jana , ambayo inasikilizwa na Jaji Lawrence Kaduli jana ilikuja kwaajili ya kuanza kusikiliza sababu za mrufani(DPP), ambaye anawakilishwa na Mawakili Wakuu wa Serikali Stanslaus Boniface na Fredrick Manyanda ambapo jaji huyo alisema anakubaliana na sababu za mawakili wa utetezi zilizoomba rufaa hiyo isisikilizwe jana na hivyo akaiarisha kesi hiyo hadi Aprili 18 itakapokuja kusikilizwa.

Awali Mawakili wa Gile, Alex Mgongolwa jana aliomba mahakama iairishe usikilizwaji wa rufaa hiyo kwasababu juzi ndiyo mshtakiwa huyo ameingia nae mkataba wa kuanza kumtetea katika rufaa hiyo kwani kipindi kile mshtakiwa anashtakiwa katika Mahakama ya Kisutu alikuwa akimtetea na mkataba wao ulimalizika pale mahakama ile ya chini ilipotoa uamuzi wa kumuona ana kesi ya kijibu hivyo anaomba apewe muda akapitie hoja za mawakili wa serikali katika rufaa hiyo.

Aidha Mgongolwa alieleza sababu nyingine ya kuomba usikilizwaji wa rufaa hiyo uairishwe ni kwamba wakili wa Gile, Richard Rweyongeza yupo katika kesi kusafirisha kilo 92.2 za dawa ya kulevya aina ya Heroine yenye thamani ya sh bilioni mbili inayomkabili Assad Azizi Abdulasul ambaye ni mdogo wake aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz ambayo imeanza kusikilizwa mfululizo kuanzia Jumatatu ya wikik hii na Jaji Kipenka Mussa katika Mahakama Kuu Kanda ya Tanga.

Katika rufaa hiyo DPP anaomba Mahakama Kuu itengue uamuzi wa mahakama hiyo ya chini iliomuona Gile hana kesi ya kuiibu kwasababu mahakama hiyo ilikosea kisheria kutoa uamuzi huo.

Julai 27 mwaka 2011 , Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Waliarwande Lema alitoa uamuzi wa kumuona Gile aliyekuwa akikabiliwa na makosa ya kughushi, kutoa taarifa za uongo kwa maofisa wa serikali kuhusu kampuni ya Richmond LLC ya Texas ya Marekani kuwa hana kesi ya kujibu kwasababu ushahidi ulitolewa na upande wa Jamhuri ni dhahifu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima na Alhamsi, Machi Mosi mwaka 2012