KATIBU BAKWATA AMRUKA PONDA





Na Happiness Katabazi

KATIBU Mkuu wa Baraza la Kuu la Waislamu(BAKWATA), Suleman Said Lolila(61),amekanusha madai yaliyotolewa na  Katibu wa  Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 49 wanaokabiliwa na kesi  uchochezi na wizi wa Sh milioni 59  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa Baraza Kuu la Waislamu nchini(BAKWATA), siyo chombo cha kuwakilisha waislamu wote hapa nchini.

Sambamba na waandishi wa habari  za mahakamani walipongeza hatua iliyochukuliwa na wana usalama ya jana kuzuia umati wa wafuasi wa Ponda kuingia ndani ya chumba kinachoendeshewa kesi kwani hapo awali wafuasi hao walikuwa wakifurika hali iliyosababisha waandishi wa habari,wanausalama kushindwa kufanyakazi yao kwa nafasi na kupata hewa ya kutosha kwani kesi hiyo kwanza ina washtakiwa wengi  ambao ni 50.
Suleiman ambaye ni shahidi wa kwanza wa upande wa jamhuri katika kesi hiyo, alitoa maelezo hayo jana mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa wakati akiongozwa na wakili mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka kumuongoza kutoa ushahidi ambapo jana shahidi huyo alimaliza kutoa ushahidi wake.
Itakumbukwa kuwa Novemba 15 mwaka huu, wakili Mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka aliwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao ambapo alidai Bakwata ni chombo ambacho kinawawakilisha waislamu wote, lakini Ponda na wenzake walikanusha madai yao na kusema kuwa Bakwata haipo kwaajili ya kuwawakilisha waislamu wote.
Suleiman alitoa maelezo hayo baada ya kuulizwa swali na wakili Kweka kuwa BAKWATA ni chombo gani?kipo kwaajii ya waumini wa dini gani?Mali za waislamu zinamilikiwa na nani kwa niaba yao?Na na ninani hivi sasa ni mmilikiwa wa kiwanja  kiwanja Kitalu 311/3/4 Block  T ,kilichopo eneo la Chang’ombe Markas jijini Dar es Salaam?
Akijibu maswali hayo shahidi huyo ambaye alidai yeye ndiye mtendaji mkuu wa BAKWATA alieleza kama ifuatavyo:
“BAKWATA ni chombo kilichoundwa kwa Korani  na Sunaa na imesajiliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani, na Bakwata ni chombo kilichoanzishwa kwa kwaajili ya kuwawakilisha waumini wa dini ya Kiislamu hapa nchini  na mali za waislamu zinamilikiwa kwa niaba yao na Bodi ya Wadhamini ya Bakwata ;
“Na mmiliki halali wa kiwanja hicho hivi sasa ni kampuni ya Agritanza Ltd , kwani Serikali ya Misri ilitoa wazo ya kuwasaidia waislamu wa Tanzania kielimu na ikafanya mazungumzo na viongozi wa serikali ya Tanzania ,serikali ya Tanzania ikaipatia serikali ya Misri eneo hilo la Chang’ombe Markas kiwanja hicho ili kiweze kujenga chuo kikuu cha Waislamu lakini baadaye serikali ikaja kuwagawai baadhi ya maeneo taasisi ya YCC na mfanyabashara Yusuf Manji:

“Ikabakia eneo jingine ambalo mwisho wa siku BAKWATA ikiaamua eneo hilo wabadilishane na kampuni ya Agritanza Ltd kwa mikataba halali kisheria , hivyo makubaliano yalifikishwa tena kwa maandishi BAKWATA ikaridhia kubadilisha na kampuni hiyo hivyo Agritanza hivi sasa ndiye mmiliki halali wa kiwanja hicho na si vinginevyo na alipata Baraka zote za Bakwata ambayo ni chombo kinachosimamia mali na waislamu wote’alidai shahidi huyo.

Kwa upande wake wakili utetezi Nassor Mansoor akimhoji shahidi huyo alimuuliza kama  anafahamu  alikuwa akifahamu hati ya umiliki wa kwanza wa kiwanja hicho ulikuwa ukimilikiwa na nani na kwamba kabla ya kiwanja hicho kugawiwa kwa baadhi ya watu kilikuwa na ukubwa gani na kwamba kama alikuwa akiwafahamu washtakiwa .
Akijibu maswali hayo alidai yeye hafahamu awali kiwanja hicho kilikuwa kikimilikiwa na nani na kilikuwa na ukubwa gani na kuhusu kuwafahamu washtakiwa alidai anamfahamu Sheikh Ponda kwani amekuwa akimuona kupitia vyombo vya habari na kisha shahidi huyo akainuka akawasalimia washtakiwa na kusema “Asalmayek nao washtakiwa wakamjibu kwa sauti Alykmsalamu hali iliyosababisha Hakimu Mkazi Victoria Nongwa kumwaleza shahidi kuwa mahakamani hapo watu huwa hawasalimiani na kusababisha watu kuangua vicheko.

Baada ya Shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi wake, Hakimu Nongwa alisema anaiarisha kesi hiyo hadi Desemba 13 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya shahidi wa pili kuja kuanza kutoa ushahidi wake na akamuamuru mshtakiwa wa kwanza Ponda na Mukadam Abdal Swalehe(45) ambaye ni mshtakiwa wa   tano katika kesi hiyo ya jinai Na.245/2012 warudishwe gerezani kwasababu bado Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi hajaiondoa hati yake aliyoiwasilisha   ambayo  imefunga dhamana za washtakiwa hao wawili.

Baada ya hakimu Nongwa kuarisha kesi hiyo, ndugu na jamaa na washtakiwa ambao wapo nje kwa dhamana walijipanga katika viunga vya mahakama hiyo na kumpungia mkono Mukadam na Ponda ambao walikuwa wamepandishwa kwenye gazeti la Jeshi la Magereza lilokuwa likilindwa na kuongozwa na msafara wa magari ya ina ya  Defenda za jeshi la Polisi na gari mmoja lililokuwa limebebeba maji ya kuwasha ‘kikojozi’ na kuanza safari ya kumrejesha katika gereza la Segerea na wafuasi hao ambao kadri siku zinavyozidi kusonga mbele wanapungua kuja mahakamani kuudhulia kesi hiyo walisikika wakisema ‘Takbiri,Takbir’ huku wakiwapungia mkono Ponda na Mukadam ambao walikuwa wakiondoshwa kwenye eneo hilo la Mahakama kupelekwa gereza  la Segerea.

Awali Oktoba 18 mwaka huu, ilidaiwa na wakili Kweka kuwa kosa la kwanza alidai ni la kula njama ambalo linawakabili washitakiwa wote,kosa la pili ni kwaajili ya washitakiwa wote ambalo ni la  kuingia kwa nguvu  kwa nia ya kutenda kosa kinyume na kifungu cha  85 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, kuwa Oktoba 12 mwaka huu huko Chang’ombe Markas, wasipokuwa na sababu za msingi waliingia kwa jinai kwenye kiwanja kinachomilikiwa na kampuni ya Agritanza Ltd, kujimilikisha kiwanja hicho kwa njia ya iloyopelekea uvunjifu wa amani,wizi ambapo baada ya kuvamia waliiba vifaa na malighafi ikiwemo nondo, kokoto zenye jumla ya thamani ya Sh. 59,650,000 mali ya kampuni ya Agritanza na kosa la tano ni la uchochezi kinyume na kifungu cha 390 na 35 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, ambalo sasa kosa hili la uchochezi litamkabili Mukadamu na Ponda peke yao  kuwa wakiwa ni viongozi wa jumuiya hiyo , Oktoba 12 mwaka huu ,waliwashawishi wafuasi wao watende makosa hayo hata hivyo walikanusha mashtaka yote.

 Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Novemba 30 mwaka 2012

   

ATIWA HATIANI KWA MAKOSA YA KUFANYA BIASHARA HARAMU YA KUSAFIRISHA BINADAMU



Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,imemtia hatiani mfanyabiashara wa ngozi nchini, Salim Ally (61) kwa makosa ya kusafirisha binadamu na kuwatumisha na kumhukumu kwenda jela miaka 10 au kulipa fidia ya jumla ya milioni 17.

Hukumu hiyo ya kesi hiyo ya ki historia na ya kwanza kutolewa katika Mahakama hiyo tangu Sheria ya Usafirishaji haramu binadamu ya mwaka 2008 ilipotungwa na bunge, ilitolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo Ilvin Mugeta.

Akitoa hukumu hiyo hakimu Mugeta alisema  upande wa jamhuri ambao ulikuwa ukiwakilishwa na wakili mwandamizi wa serikali Arafa Msafiri, Prosper Mwangamila na Hamid Mwanga katika kujenga kesi yao walileta jumla ya mashahidi watano wakati mshtakiwa aliyekuwa akitetewa na wakili wa kujitegemea Majura Magafu alijitetea yeye mwenyewe bila kuleta shahidi yoyote.

Hakimu Mugeta alianza kwa kuikumbusha mahakama hiyo kuwa ilidaiwa mahakamni hapo na upande wa jamhuri kuwa Agosti 8 mwaka 2010 alimsafirisha Abduswamad na wenzake kwenda nchini Yemen na kwenda kuwatumisha kwa nguvu na bila ya kuwalipa ujira wao kinyume na kifungu cha 4(1)a,6(2)c, cha Sheria ya Usafirishaji haramu wa binadamu ya mwaka 2008.

Alisema baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili na vielelezo ,mahakama yake imefikia uamuzi wa kuona upande wa jamhuri umeweza kuthibitisha kesi yake na kwamba baadhi ya ushahidi uliotolewa na mshtikakiwa na wakili wa Magafu ulikuwa unatofautiana kwani Magafu katika majumuisho yake alidai Abduswamad  alijisafirisha mwenyewe kwenda Yemen akusafirishwa na mshtakiwa lakini Mshtakiwa katika utetezi wake alidai yeye aliwasaidia fedha washtakiwa kwenda Yemen kwasababu washtakiwa hao walikuwa wakiitaji fedha za kwenda Yemen kufanyakazi kwa mtu mwingine na yeye akaamua kuwapatia kwa makubaliano kuwa wakimaliza kufanyakazi kwa mtu huyo wataenda kufanyakazi kwenye nyumba yake iliyopo Yemen na kwamba fedha hizo alizowaazima watakuwa wakimlipwa katika fedha watakazokuwa wanalipwa kutoka kwa mtu waliyokuwa wamekwenda kumjengea nyumba.

“Mahakama hii inasema upande wa jamhuri umeweza kuthibitisha kesi yake kwani ushahidi ulitolewa ambao upande wa utetezi umeshindwa kuupinga umetosha kuifanya mahakama hii iamini kuwa ni mshtakiwa ndiye aliyewasafirisha watu hao kutoka Tanzania kwenda Yemen kuwatumisha bila kuwa ujira na kwasababu hiyo mahakama hii inamtia hatiani kwa makosa hayo”alisema hakimu Mugeta.
Baada ya kumtia hatiani wakili Msafiri alidai mahakama haina rekodi ya mshtakiwa ambayo inaonyesha ni mhalifu mzoefu na kwasababu hiyo hii ni kesi yake ya kwanza kutiwa hatiani na kwamba anaomba mahakama imwamuru mshtakiwa amlipe  faini waathirika(waliosafirishwa) na itoe adhabu stahili.
Kwa upande wake wakili mshtakiwa, Magafu aliomba mahakama isimpe adhabu ya kwenda kutumikia kifungo gerezani kwani mshtakiwa ni mtu mzima sana,ana matatizo ya kiafya na kwamba akifungwa jela ,watanzania watapata hasara kwasababu kodi zao zitatumika kumtunza wakati mshtakiwa huyo hawezi kufanya kazi ngumu.

Aidha Hakimu Mugeta alisema amesikiliza maombi ya mawakili hao na kwamba ana mwamuru Ally kwenda jela miaka 10 au kulipa faini ya Sh.milioni saba pamoja kumlipa fidia Abduswamad na mwenzake sh milioni 10.

Hata hivyo ndugu wa mshtakiwa walilipa kiasi hicho cha fedha na hivyo kumfanya mshtakiwa huyo aliyesota gerezani kwa zaidi ya miezi nane sasa kuwa huru.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Novemba 29 mwaka 2012.

MAHAKAMA YAMBWAGA HAMAD RASHID


Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetupilia mbali ombi lilotaka mahakama hiyo itoe amri ya kuliita Baraza la Wadhamini wa Chama cha Wananchi(CUF) na wenzake waje wajieleze ni kwanini walikaidi amri ya mahakama na ni kwanini wasitiwe hatiani kwa kosa la kudharau amari ya mahakama ambalo liliwasilishwa mahakamani hapo na Mbunge wa Wawi(CUF), Hamad Rashid na wenzake 10.


Rashid na wenzake waliwasilisha maombi mahakamani hapo  Januari 10, 2012,na walikuwa wakiiomba mahakama  iwaite Wadhamini wa Cuf wajieleze ni kwa nini wasitiwe hatiani kwa kukiuka amri ya mahakama hiyo kutokana na uamuzi wa Baraza la Taifa la Uongozi la Cuf kumfukuza uanachama Hamad na wenzake.

Katika ombi hilo walalamikaji hao walidai kuwa licha ya Baraza hilo kupata taarifa za kuwepo kwa amri hiyo ya mahakama ilitolewa saa tatu ya Januari 4 mwaka huu, kabla ya kikao cha cha Baraza la CUF kuanza, baraza hilo liliendelea na kikao chake na kufikia maamuzi ya kuwavua uanachama walalamikaji hao.

Mbali na wadhamini wa CUF, wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni wajumbe wa Baraza Taifa la Uongozi la CUF.

Kwa hiyo walalamikaji waliomba  mahakama iwatie hatiani na kuwafunga jela wadhamini hao wa pamoja na wajumbe wa Baraza la Taifa la Uongozi la chama hicho akiwemo Makamu wa kwanza wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Katika maombi hayo, Rashid na wenzake walikuwa wakidai kuwa Baraza la Taifa la Uongozi la Cuf lilipuuza amri ya mahakama hiyo iliyolizuia kuwajadili wala kuwachukulia hatua zozote wakati wa mkutano wake wa Januari 4, 2012, mjini Zanzibar.

Hata hivyo Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Agustine Shangwa,alisema kuwa hakuna ushahidi wowote unaonyesha kuwa baraza wadaiwa walipata amri hiyo.

Jaji Shangwa alisema kwamba ingawa kumbukumbu zinaonesha kuwa wadaiwa walipewa amri hiyo, lakini alisema kuwa hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa wadaiwa waliipata amri hiyo wakati likiendelea na mkutano wake kabla ya kutoa uamuzi wa kuwavua uanachama walalamikaji.

“Kwa sababu hiyo mahakama hii imeshindwa kuwaita wadaiwa hapa mahakamani waje wajieleze ni kwanini walikaidi amri ile ya mahakamana…hivyo basi natupilia mbali ombi la walalamijaji”alisema Jaji Shangwa.

Amri hiyo ya Mahakama kulizuia baraza hilo kuwachukuliwa hatua yoyote Rashid na wenzake ilitolewa na Jaji Agustine Shangwa Januari, 2012 kufuatia maombi waliyoyawasilisha mahakamani hapo na kina Rashid, Januari 3, 2012, chini ya hati ya dharura.


Hata hivyo kwa mujibu wa mawakili hao, hata kama amri hiyo ingekuwa ni halali na hata kama ingekuwa na ushahidi kuwa iliwafikia wadaiwa kabla ya kutoa uamuzi wa kuwavua uanachama walalamikaji bado Mahakama Kuu haiwezi kuwachukuliwa hatua.

Mbali na Hamad Rashid wengine waliofukuzwa uanachama CUF ni Doyo Hassan Doyo, Shoka Khamis Juma na Juma Saanane, wote wakiwa wajumbe wa Baraza Kuu la chama hicho.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Novemba 29 mwaka 2012.

HASANOO SASA AKIMBILIA KORTI KUU KUSAKA DHAMANA



 

Na Happiness Katabazi

MWENYEKITI wa Chama cha Soka mkoa wa Pwani (Corefa), Hassani Othman maarufu kama Hasanoo (43)  na wenzake watano ambao wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo kosa la uhujumu uchumi  na kusafirisha Pembe za ndovu zenye thamani ya Sh.bilioni 1.1 kwenda Hong Kong nchini China, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jana aliwasilisha ombi la kuomba apatiwe dhamana na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.


Hassanoo ambaye anatetewa na wakili wa kujitemea Richard Rweyongeza ndiye aliyewasilisha maombi hayo jana kwanjia ya maandishi kwa niaba ya mshtakiwa hayo ambaye anasota gerezani tangu alipofikishwa katika mahakama ya Kisutu Ijumaa iliyopita akikabiliwa na kesi hiyo mpya ya kusafirisha pembe za ndovu.

Wakili Rweyongeza alifikia hatua ya kuwasilisha ombi hilo jana kwasababu mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na pia Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Dk.Eliezer Feleshi hakutoa kibali cha kuruhusu kesi hii isikilizwe katika Mahakama ya Kisutu.

Novemba 23 mwaka huu, siku ambayo kesi hii ilifunguliwa Wakili Mwandamizi wa  Serikali, Shedrack Kimaro mbele ya Hakimu Mkazi Augustina Mbando alidai kuwa mbali na Hassanoo washtakiwa wengine ni  Ally Kimwaga, Dastan Mwanga, Godfrey Mwanga, John Mlai na Khalid Fazaldin.

Kimaro alidai shtaka la kwanza ni la kula njama na kujihusisha na biashara haramu ya kusafirisha nyara za serikali bila leseni ambalo walilitenda  kati ya Septemba Mosi na Novemba 20, mwaka huu, Dar es Salaam na Hong Kong kinyume na kifungu cha 384  cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Katika shtaka la pili,ni kwamba washtakiwa hao  kwa nia ovu walipanga,wakatekeleza,wakasimamia  na kuwezesha  kifedha  kufanyika kwa biashara hiyo haramu ya kutorosha vipande 569 vya Pembe za ndovu, vyenye uzito wa kilogramu 1330 na thamani ya Sh 1,185,030,000 kwenda Hong Kong, kosa ambalo walilitenda walilitenda kati ya Septemba Mosi na Novemba 20 mwaka huu, kusafirisha nyaraka hizo toka Dar es Salaam , kwenda Hong Kong.

Aidha alidai shtaka la tatu kuwa siku hiyo ya tukio ,washtakiwa walijihusisha  na biashara hiyo ya nyara za serikali  kinyume na kifungu cha 80 na 34 ya uhifadhi wa Wanyama Pori namba 5.

Aliongeza kwa kudai kuwa, washtakiwa hao kwa nia ovu waliendesha biashara hiyo ya nyara za serikali bila ya kuwa na kibali halali kinachowaruhusu kufanya biashara hiyo.

Baada ya wakili Kimaro kumaliza kuwasomea mashtaka hayo , Hakimu Mmbando aliwaambia washtakiwa hao kuwa, kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi, Ritha Tarimo ambaye hayupo na kwa sababu hiyo, na kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hivyo washtakiwa hawatatakiwa kujibu chochote.

Wakili Kimaro alidai kuwa upelelezi wa kesi bado haujakamilika na kuomba ipangiwe tarehe nyingine ya kutajwa ambapo kesi hiyo inakuja leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwaajili ya kutajwa.

Mbali na kesi hiyo, Hasanoo aliyewahi kuwa kiongozi wa Simba pia anakabiliwa na kesi nyingine ya wizi wa tani 26.475 za madini aina ya Shaba zenye thamani ya Sh333, 467,848.13 kutoka Zambia kinyume na kifungu cha 258, 265 na 269 (c) vya kanuni ya adhabu mali ya Kampuni ya Liberty Express Tanzania Ltd ambayo ilifunguliwa mahakamani hapo na DPP, mwaka jana na imefikia hatua ya kuanza kusikilizwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Novemba 28 mwaka 2012.