MASHAHIDI WAZIDI KUMNYOSHEA VIDOLE SHEIKH PONDA


Na Happiness Katabazi
FUNDI mwashi Hamis Salum Mkangama(30), ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kuwa Oktoba  7 mwaka jana, mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya uchochezi na wizi wa malighahfi zenye thamani ya  Sh.milioni 59 inayomkabili  Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Issa Ponda Issa na wenzake 49 aliwataka wasimamishe ujenzi wa ukuta wa kutenganisha kiwanja cha Markas kilichopo Chang’ombe na Msikiti.
Mkangama ambaye ambaye ni shahidi wa sita wa upande wa jamhuri alitoa madai hayo jana mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa wakati akiongwa na wakili Mwanadamizi wa serikali Tumaini Kweka kutoa ushahidi wake.
Mkangama alieleza kuwa yeye ni fundi mwashi ambaye ambaye anatengeneza matofali na kwamba Oktoba 7 mwaka jana  yeye na wenzie 20 walikuwa katika kiwanja cha Chang’ombe Markas kinachomilikiwa na kampuni ya Agritanza Ltd akijenga ukuta unaotenganisha kiwanja cha Chang’ombe Markas na Msikiti na kwamba walikuwa katika hatua ya kuchimba msingi.
“Ghafla ilipofika saa 10 jioni alikuja Ponda na akatuuliza nani katuruhusu tujenge ukuta katika kiwanja hicho, tukamjibu ni Suleiman ambaye ni bosi wetu, Ponda akatutaka tusimamishe ujenzi haraka  kwani eneo hilo bado lina mgogoro ,sisi tukamjibu  hatuwezi kusimamisha ujenzi  hadi bosi wetu Suleiman aliyetupa kazi hiyo atukataze, sisi tutaendelea na ujenzi:
“Ponda akaamua kuachana na sisi wajenzi akaanza kupiga picha hilo eneo la kiwanja cha Markas  ambalo tulikuwa tunajenga ukuta  alipomaliza kupiga picha  akatoe mlinzi  wa eneo lile  ambaye alikuwa hamfahamu Ponda  wakanza kujibishana  na Ponda   kisha mlinzi Yule akaamua kumjulisha bosi wake kwa njia ya simu kuhusu ujio wa Ponda  na bosi yule akaja akatutaka tusieendelee na ujenzi kwani endapo tutaendelea kuna matatizo yanaweza kutokea na akatueleza kuwa yeye anaenda kuripoti ujio huo wa Ponda katika vyombo vya dola”alidai Mkangama.
Kwa upande wake Shahidi wa saba,  William Milanzi(43) ambaye  ni mlinzi wa eneo linalopakana na kiwanja cha Markas ambapo alidai amewekwa kufanya kazi hiyo na mtu mmoja aliyemtaja kwa jina la Seif  ambaye ndiye aliyempa jukumu la kulinda pia eneo la Suleiman ambalo ni la kiwanja cha Markas kwaajili ya kulinda malighafi zilizokuwa zimeifadhiwa pale ambazo ni matofali, mbao, nondo na malighafi nyingine nyingi.
Milanzi alieleza kuwa Oktoba 12 mwaka jana, alikuwa katika eneo lake la kazi lilopakana na Markas kuanzia asubuhi  na kwamba alipoajiriwa alikuwa ameukuta ukuta ambao hivi sasa haupo  na kwamba ukuta uliopo sasa ni mpya  na kwamba ukuta ule wa zamani ulivunjwa na umati ule uliovamia siku hiyo.
 “Ilipofika saa saba mchana ya Oktoba 12 mwaka jana,baada ya Sala ya  Ijumaa, niliona  umati mkubwa  sana na nikaona mbao nilizokuwa nazilinda zikichukuliwa na umati ule na na zikavushwa kupelekwa kwenye kiwancha  upande wa pili wa Markas ….baada ya muda nikaona umati huo unaingia kwenye mpaka ule uliokuwa uliokuwa ukijengwa kwaajili ya kutenganisha marks na msikiti  na kuanza kuvunja sehemu ndogo iliyokuwa imeezekwa kwa mabati;
“Baada ya kuvunja wakaingia eneo niliokuwa nalinda  na kuanza kubeba matofali  na kwenda nayo upande wa pili wa eneo la Markas  na nilipomjulisha bosi wangu Seif kuhusu hali hiyo, akanitaka niwe mtulivu  kwani anafanya mawasiliano na vyombo vya usalama na matofali yale ni mali ya Suleiman”alidai Milanzi.
Aidha alidai watu toka katika umati ule ambao hakuweza kuwatambua waliwafuata wao na kuanza tuuliza kama wao ndiyo wenye mali ya kiwanja cha Markas ,akawajibu kuwa wao ni walinzi mwenye mali ni Suleiman  na kwamba wale watu sita ambao walikuwa wamefuka vipaza sauti katike eneo hilo walijitambulisha kwao kuwa wao ni waislamu  na kwamba wamekuja pale kwaajili ya kuja kuhani  eneo lao  na waliwataka walinzi hao wakamweleze bosi wao kuwa akamtafute aliyemuuzia kiwanja hicho amrudishie fedha zake na kwamba umati ule umekuja kuchukua eneo  lao ambalo ni mali ya waislamu.
“Mheshimiwa hakimu umati ule ulichukua matofali yale  na kuyapeleka  eneo la Markas na umati ule uliendelea kudumu katika kiwanja hicho toka Oktoba 12 hadi 16 mwaka jana alfajiri ambapo polisi walikuja kuwakamata  na wakati wameweka kambi kwa siku hizo zote katika kiwanja hicho,umati huo ulikuwa umefunga vipaza sauti katika eneo hilo ambapo wakulikuwa wakitangaza  eneo lile lilokuwa limetobolewa kwaajili ya kujenga ukuta wa kutenganisha msikiti na markas lizibwe kwa matofali yale yale waliyoyakuta pale  na wakavunja na kibanda cha mabati”alidai Milanzi.
Kwa upande wake hakimu Nongwa aliairisha kesi hiyo hadi  Februali 14 itakapokuja kwaajili ya kutajwa na kusema kuwa siku hiyo aletwe Ponda na mshtakiwa wa tano tu, Mkadamu ndiyo waletwe mahakamani kwasababu wanaishi gerezani na kwamba washtakiwa waliosalia wasije mahakamani kwasababu wanadhamana na akasema kesi hiyo itakuja tena Februali 18,25,27 na 28 mwaka huu, kwaajili ya shahidi wa nane wa upande wa jamhuri kuanza kutoa ushahidi wake, na kuamuru Ponda na Mkadamu warudishwe gerezani kwasababu Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Dk.Eliezer Feleshi bado hajaondoa hati yake ya kuwafungia dhamana washtakiwa hao.
Hata hivyo jana hali ya usalama iliimalishwa kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na Januari 17 mwaka huu, kesi hiyo ilipokuja kwaajili ya kusikilizwa, kwani zaidi wafuasi wa Ponda 200 walikuwa wamefurika ndani ya viwanja vya mahakama hiyo na walijipanga katika viwanja hivyo wakisubiri basi la Jeshi la Magereza lilokuwa limembeba Ponda na Mkadamu lipite kwaajili ya kuwapeleka gereza la Segerea, ndipo umati huo ulianza kupaza sauti ya juu kwa kusema ‘Takbir   Allahwakbar,Takbir Allahwakbar’, huku wengine wakilisogelea basi alilokuwa amepanda Ponda.
“Nyie Polisi mmezidi sana, sasa kwa taarifa yenu kesho (leo) mjiandae kutuua sana kwa risasi, tunasema mjiandae kutuua kwa risasi…..serikali ya awamu ya nne ina wapendelea sana wakristo na inatugandamiza waslamu, tumechoka “walisikika wafuasi hao waliokuwa wamevalia kanzu na baraghashia wakisema.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Februali Mosi mwaka 2013. 

LULU AREJEA URAIANI,ADAI MUNGU NDIYE ALIYEMPA DHAMANA






Na Happiness Katabazi
HATIMAYE msanii wa  filamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’ amepata dhamana baaada ya kutimiza masharti matano aliyopewa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, juzi wakati mahakama hiyo ilipokuja kusikiliza ombi lake la kuomba apatiwe dhamana katika kesi inayomkabili ya kuua bila kukusudia aliyekuwa msainii mwenzie Steven Kanumba.

Lulu alitimiza masharti hayo jana saa tisa Alasili kwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Francis Kabwe  na baada ya kutimiza masharti hayo ya dhamana aliwaeleza waandishi wa habari huku akitoka machozi kuwa anamshukuru mungu kwani yeye ndiye alifanya akapata dhamana hiyo na hivyo kumfanya atoke gerezani na kurejea kuishi uraiani.

Lulu ambaye alikuwa ameongozana na wakili wake Peter Kibatara  alisema anawashukuru wale  wote waliyokuwa nae bega kwa bega,tangu kesi yake ilipoanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

“Ninachoweza kusema ni kuwashukuru wale wote walioniangaikia na kuniombe kwa mungu hadi leo nimepata dhamana narudi kuungana na familia yangu …lakini naomba watu hao waendelee kuniombea kwani leo nimepata dhamana tu na ile kesi yangu ya msingi ya kuua bila kukusudia bado haijaanza kusikilizwa na kutolewa uamuzi hivyo naombeni sana waendelee kuniombea na wasinitupe”alisema Lulu.

Msanii huyo amedhaminiwa na Flolian Matungwa,ambaye anatoka Wizara ya Ardhi na Verus Mboneko,ambaye anatoka Wizara ya Afya.

Lulu alifikishwa eneo la Mahakama Kuu saa 7:58 mchana na gari ya Jeshi la Magereza lenye namba za usajili STK 2823.Baada ya kupatiwa dhamana  aliondoka na gari aina ya Land Cruser VX V8,lenye namba za usajili T480 CFX.
Hata hivyo wakili Kibatara, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kwaniaba ya mteja wake anakanusha uvumi  uliokuwa umeenea kuwa Lulu akiachiwa kwa dhamana jana angeenda moja kwa moja kwenye kaburi alilozikwa Kanumba lilopo eneo la Kinondoni na kuongeza kwa kumshukuru Msajili Kabwe kwa kumpatia dhamana mteja wake kwani muda wa kazi ulikuwa umepita.
Juzi  Jaji Zainabu Mruke muda mfupi baada ya mawakili wa Lulu, Peter Kibatara, Kennedy Fungamtama na Fulgence Massawe kuiomba mahakama hiyo impatie dhamana mshtakiwa huyo ambaye amesota rumande katika gereza la Segerea tangu Aprili mwaka jana  ambapo walieleza kuwa ombi la dhamana wameliwasilisha chini ya kifungu cha
148(1) ,(2) Cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 .

Jaji Mruke alisema ili mahakama impatie dhamana ni lazima asalimishe  kwa Msajili wa mahakama hiyo hati ya kusafiria,  kutotoka nje ya Dar es Salaam  bila ruhusa ya mahakama, kuripoti kwa msajili kila mwezi ,kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa serikali  ambao watasaini bondi ya Sh.milioni 20 kila mmoja.

Baada ya jaji huyo kutangaza masharti hayo Lulu na wakili wake walitoka nje ya ukumbi uliokuwa ukiendeshwa kwa shauri hilo kwa ajili ya kwenda kwa msajili kutimiza masharti hayo lakini kwa bahati mbaya Msajili hakuwepo ofisini na hivyo kufanya Lulu kurudishwa rumande na akarejeshwa jana mchana mahakamani hapo kwaajili ya kuja kutimiza masharti ya dhamana mbele ya msajili huyo Kabwe ambapo aliyatimiza jana na kupatiwa dhamana.

Kufuatia mahakama hiyo juzi  kumpatia masharti ya dhamana Lulu kutoka na ombi lake Na.125/2012 la kuomba mahakama hiyo impatie dhamana, lakini bado kesi ya msingi inayomkabili Lulu ambayo ni ya kuua bila kukusudia bado haijapangiwa jaji wala tarehe ya kuanza kusikilizwa.

Wasanii waliyokuwepo kumuunga mkono Lulu mbali na mama yake mzazi mahakamani hapo alikuwepo Mahsein Awadh maarufu Dk.Cheni, Muna na msanii mwingine mmoja.

Desemba 21 mwaka jana , Hakimu Mkazi Christine Mbando wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu aliifunga kesi ya kuua bila kukusudia Lulu na kuiamishia rasmi kesi hiyo katika Mahakama Kuu, na uamuzi huo wa mahakama ulitokana na upande wa Jamhuri kumsomea maelezo ya kesi yake kwa kina mshtakiwa huyo na kuieleza mahakama kuwa wanakusudia kuleta jumla ya mashahidi tisa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 30 mwaka 2013.







KESI YA KUPINGA WABUNGE WA EAC KUANZA KUSIKILIZWA LEO


Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Afrika Mashariki inayoketi mkoani Arusha, leo inatarajia kuanza kusikiliza usikilizwaji wa awali wa kesi ya kupinga mchakato uliofanywa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwapata wabunge tisa wa Bunge la Afrika Mashariki kwasababu ulikiuka Ibara ya 50 ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kesi hiyo Na.7/2012 ilifunguliwa mahakamani hapo na aliyekuwa mgombea Ubunge wa bunge la Afrika Mashariki kwa tiketi ya Chadema, Antony Komu ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea Edson Mbogoro dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kesi hiyo ambayo itasikilizwa na jopo la majaji wa tano wa mahakama hiyo litaongozwa na jaji Johnston Busingye, Merry Tella, Arack Amoco, John Mkwawa,Isaac Leneoli.
Akizungumza na gazeti hili kutokea mkoani Arusha wakili wa Komu, Mbogoro alisema tayari ameishafika Arusha kwaajili ya leo kuudhulia kesi hiyo ya kihistoria  na kwamba madai ya msingi ya mteja wake ni kwamba anapinga mchakato mzima ulioendeshwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kuwapata wabunge  wa Bunge la Afrika Mashariki  kwasababu mchakato wote ulikiuka matakwa ya Ibara ya 50 ya Mkataba wa Uanzishwa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Komu ambaye naye alikuwa ni mgombewa nafasi ya bunge wa Bunge la Afrika Mashariki kwa tiketi ya Chadema, hakuweza kushinda nafasi hiyo na hivyo kufanya chama cha Chadema kukosa mbunge wa bunge la Afrika Mashariki, na Komu hakulidhishwa na mchakato huo muda mfupi baadaye aliamua kufungua kesi hii katika Mahakama hiyo ya Afrika Mashariki.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 30 mwaka 2013.

MASHAHIDI WAKWAMISHA KESI YA VIGOGO SUMA JKT


Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA  ya Hakimu  Mkazi Kisutu Dar es Salaam,jana ilishindwa kuanza kusikiliza kesi ya  inashindwa kuanza kusikiliza KESI ya matumizi mabaya ya madaraka inayomkabili Mkurugenzi wa Shirika la Kujenga Taifa (SUMA JKT), Kanali Ayoub Mwakang’ata na maofisa wengine wa jeshi hilo kwasababu shahidi wa upande wa jamhuri aliyetarajiwa kuja jana kutoa ushahidi ameshindwa kufika mahakamani hapo kwasababu amesafiri.

Hakimu Mkazi Alocye Katemana alisema kesi hiyo ilikuwa imekuja kwaajili ya mashahidi wa upande wa jamhuri kuanza kutoa ushahidi wao ,lakini wakili wa upande wa Jamhuri ameiomba mahakama hiyo iarishe hadi tarehe nyingine kwasababu shahidi waliyekuwa wamemuanda ajae kutoa ushahidi amesafiri.

“Kwa sababu hiyo mahakama hii inaairisha kesi hii hadi  Machi 4 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya mashahidi wa jamhuri kuanza kutoa ushahidi wao”alisema Hakimu Katemana.
Mbali na Kanali Mwakang’ata washitakiwa wengine ambao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na TAKUKURU, Julai 2 mwaka jana , ni Luteni Kanali Mkohi Kichogo,Luteni Kanali Paul Mayavi,Meja Peter Lushika,Sajenti John lazier,Meja Yohana Nyichi na Mkurugenzi wa Miradi ya Matrekta wa SUMA JKT-Luteni Kanali Felex Samillan wanaotetewa na wakili wa kujitegemea Majura Magafu.

Wanakabiliwa na makosa ya kula njama na matumuzi mabaya ya madaraka kuwa washitakiwa wakiwa ni wajumbe Ilidai kuwa Machi 5 mwaka 2009 katika chumba cha mikutano cha ofisi ya SUMA JKT Dar es salaam,wakiwa ni wajumbe wa bodi na Bodi ya Tenda ya SUMA JKT kwa makusudi walitumia madaraka yao vibaya kwa kutoa maamuzi ya bodi hiyo ambayo yaliyoonyesha yametolewa na TAKOPA kwa madhumuni ya kununua magari na vifaa vya ujenzi bila kupata idhini ya kutoka Bodi ya ya Wakurugenzi ya TAKOPA. 

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Januari 30 mwaka 2013.

MSAJILI WA MAHAKAMA KUU AMKWAMISHA LULU




Na Happiness Katabazi
HATIMAYE Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ilimpatia masharti matano ya kupata dhamana kwa msanii wa Filamu nchini Elizabeth Michael ‘Lulu’,  anayekabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia aliyekuwa msanii mwenzake marehemu Steven Kanumba.

Masharti hayo yaliyolewa jana na Jaji Zainabu Mruke muda mfupi baada ya mawakili wa Lulu, Peter Kibatara, Kennedy Fungamtama na Fulgence Massawe kuiomba mahakama hiyo impatie dhamana mshtakiwa huyo ambaye anasota rumande tangu April mwaka jana ambapo walieleza kuwa ombi la dhamana wameliwasilisha chini ya kifungu cha
148(1) ,(2) Cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 .

Jaji Mruke alisema ili mahakama impatie dhamana ni lazima asalimishe  kwa Msajili wa mahakama hiyo hati ya kusafiria,  kutotoka nje ya Dar es Salaam  bila ruhusa ya mahakama, kuripoti kwa msajili kila mwezi ,kuwa na wadhamini wawili ambao ni watumishi wa serikali  ambao watasaini bondi ya Sh.milioni 20 kila mmoja.

Baada ya jaji huyo kutangaza masharti hayo Lulu na wakili wake walitoka nje ya ukumbi uliokuwa ukiendeshwa kwa shauri hilo kwa ajili ya kwenda kwa msajili kutimiza masharti hayo lakini kwa bahati mbaya Msajili hakuwepo ofisini na hivyo kufanya Lulu kurudishwa rumande hadi leo atakapoletwa kwaajili ya kujatimiza masharti hayo mbele ya Msajili wa mahakama hiyo.

Kufuatia mahakama hiyo jana kumpatia masharti ya dhamana Lulu kutoka na ombi lake Na.125/2012 la kuomba mahakama hiyo impatie dhamana, lakini bado kesi ya msingi inayomkabili Lulu ambayo ni ya kuua bila kukusudia bado haijapangiwa jaji wala tarehe ya kuanza kusikilizwa.

Desemba 21 mwaka jana , Hakimu Mkazi Christine Mbando wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu aliifunga kesi ya kuua bila kukusudia Lulu na kuiamishia rasmi kesi hiyo katika Mahakama Kuu, na uamuzi huo wa mahakama ulitokana na upande wa Jamhuri kumsomea maelezo ya kesi yake kwa kina mshtakiwa huyo na kuieleza mahakama kuwa wanakusudia kuleta jumla ya mashahidi tisa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Januari 29 mwaka 2013