HATIMA YA PONDA MACHI 4



Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya uchochezi na wizi wa malighafi ya Sh.milioni 59 inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 49 wameiomba  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imuone Ponda na wenzake wanakesi ya kujibu kwasababu umeweza kujenga kesi yao.

Kesi hiyo ambayo jana ilikuja kwaajili ya upande wa jamhuri unaowakilishwa na wakili Mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka na Inspekta wa Polisi,  Hamisi Said na upande wa utetezi unaowakilishwa na Juma Nassor na Njama kuwasilisha majumuisho yao kwa njia yam domo ya kuomba mahakama iwaone washitakiwa wanakesi ya kujibu au la.

 Kwa upande wake wakili Kweka aliikumbusha mahakama kuwa washitakiwa wanakabiliwa na makosa matano ambayo ni kula njama kutenda kosa, kuingia kwa nguvu kwenye kiwanja cha Chang’ombe Markas ambacho ni mali ya Kampuni ya Agritanza Ltd, kujimilikisha kiwanja hicho, wizi na uchochezi.

Wakili Kweka alidai kuwa washitakiwa wote ni kweli walitenda makosa hayo na ndiyo maana walikuingia kwa jinai tangu Oktoba 12 hadi walipokuja kukamatwa usiku wa kuamkia katikaOktoba 17 mwaka jana katika kiwanja hicho na uwepo wao katika kiwanja hicho katika siku hizo zote ni ndiyo walitenda kosa la kujimilikisha kiwanja hicho isivyo halali.

Akilichambua kosa la wizi alidai kuwa wakati washitakiwa wameingia kwa jinai katika kiwanja hicho walikuta kokoto, mchanga mali ya Agritanza na kwa makusudi wakaamua kutumia malighafi hizo kwaajili ya kujenga msikiti mdomo ndani ya kiwanja hicho bila idhini ya mmiliki wa kiwanja hicho ambacho ni kampuni hiyo.

Kuhusu kosa la uchochezi wakili Kweka alidai kielelezo cha 13 kilichotolewa na Shahidi 17 ,F 8586/DC Ismail ambaye alimhoji mshitakiwa aitwaye Fiswaali ambaye ni mkazi wa Mlandizi ambaye katika maelezo yake ambayo yalipokelewa na mahakama kama kielelezo cha 13, alimweleza shahidi huyo kuwa yeye alisikia wito toka Redio Iman ambayo ilikuwa ikiwataka waislamu wote waende wakaongeze nguvu ya kujenga msikiti  katika kiwanja cha Chang’ombe Markas kwasababu kiwanja hicho mali ya waisilamu na kilikuwa kimeibwa.

“Kwa maelezo hayo ya mshitakiwa Fiswaali ambayo maelezo hayo yalipokelewa na mahakama kama ushahidi tosha kwa mshitakiwa wa kwanza(Ponda) na mshitakiwa wa tano (Mkadamu) walitenda kosa hilo la kuchochea washitakiwa waende kutenda makosa yanayowakabili katika kiwanja hicho.

Aidha Kweka ambaye alitumia dakika kumi tu kuwasilisha majumuisho alidai upande wa jamhuri umeweza kujenga kesi yake kupitia mashahidi wake 16 na vielelezo 13 walivyovileta mahakamani ambapo waamini kisheria vitawafanya washitakiwa wapande kizimbani kujitetea.

Kwa upande wake wakili wa utetezi Nassor Juma akiwasilisha majumuisho yake, aliomba mahakama iwaone washitakiwa hawa kesi ya kujibu na waachiliwe huru kwasababu kesi hiyo imefunguliwa na polisi kwa jazba na upande wa jamhuri umeshindwa kujenga kesi yao na kwamba mahakama kuwaambia washitakiwa wanakesi ya kujibu ni kuwasumbua bure washitakiwa.
Wakili Nassor alidai wanachokiona katika kesi hiyo ni kuwa kuna mgogoro wa ardhi ambao ulitakiwa ukatatuliwa kwanza na Mahakama ya Ardhi kwa mujibu wa kifungu cha 167 cha Sheria ya Ardhi Na.4 ya mwaka 1999.

Nassor alidai kuwa katika hati ya mashitaka ,kosa la kwanza ni la kula njama kutenda kosa na kwamba jamhuri imeshindwa kuanisha ni kosa gani hilo la jinai au madai lililotendwa na washitakiwa na kwamba hata hilo kosa la tano la kushawishi au uchochezi upande wa jamhuri umeshindwa kuanisha wazi washitakiwa walishawishiwa kutenda kosa lipi ambalo limesababishwa kufunjwa kwa sheria.

Akichambua kosa  kosa la pili, tatu na nne la kuingia kwa jinai, kujimilikisha kiwanja hicho isivyo halali na wizi, wakili huyo alidai washitakiwa hawakuingia kwa jinai kwani hata shahidi wa jamhuri ambaye ni mlinzi  alieleza kuwa Ponda alifika katika eneo hilo  akawasalimia Asalamaleku na  Asalamaleku manaake amani iwe  na kisha mlinzi huyo akampatia simu Ponda akaongea na shahidi wa tatu ambaye ni mmiliki wa kiwanja hicho Sulemain Hilary na kuhoji kuwa kama Ponda aliwasalimia vizuri , je huko ndiko kuingia kwa jinai?

Kuhusu kosa la wizi alidai washitakiwa hao hawajatenda kosa na upande wa jamhuri umeshindwa kulithibitisha kwani Hilal alitoa ushahidi unaosema ndani ya kiwanja chake kulikuwa na kokoto, mchanga ambazo hata hazijaletwa kama kielelezo na kwamba washitakiwa walichokifanya ni kutumia malighafi hizo kujengea msikiti mdomo na kwamba huo sio wizi.

“Sisi upande wa utetezi tunaiomba mahakama hii iwaachirie huru washitakiwa wote na iwaone hawana kesi ya kujibu kwasababu kesi hii imefunguliwa kwa jazba na polisi na upande wa jamhuri umehindwa kuleta ushahidi ambao utaweza kuishawishi mahakama iwaone washitakiwa wote wana kesi ya kujibu”alidai wakili Nassor.
Kwa upande wake Hakimu Nongwa aliarisha kesi hiyo hadi Machi 4 mwaka huu, ambapo atakuja kutoa uamuzi wa ama kuwaona washitakiwa wana kesi ya kujibu au la na kuamuru Ponda na Mkadamu warudishwe rumande kwasababu bado Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk.Eliezer Feleshi hajaondoa hati yake ya kuwafungia dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Machi Mosi mwaka 2013.

JAMHURI YAFUNGA USHAHIDI KESI YA MAANDAMANO HARAMU


Na Happiness Katabazi

HATIMAYE upande wa Jamhuri katika kesi ya kula njama na kufanya maandamano haramu inayomkabili Salum Bakari Makame na wenzake 52  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana ulitangaza kufunga ushahidi wake katika kesi hiyo.

Hayo yalisemwa jana na Wakili Mwandamizi wa Serikali Bernad Kongora,Peter Ndjike,Nassor Katuga,Zuberi na Josephe Mahugo mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo ambapo alidai kuwa wamefikia uamzui huo baada ya kulizika mashahidi wote waliowaletea wanaweza kuijenga kesi yao.

“Jumla ya mashahidi 10 na vielelezo 12 tulivyovileta hapa mahakamani na vikapokelewa tunaona vinatosha kabisa upande wa jamhuri ufikie maamuzi ya kufunga  ushahidi wetu leo na tunaichia mahakama ifanye utaratibu mwingine wa kisheria’alidai Wakili Kongora.

Kwa upande wake Hakimu Fimbo alisema kuwa anaiarisha kesi hiyo hadi leo ambapo itakuja kwaajili ya upande wa jamhuri na utetezi unaowakilishwa na wakili wa kujitegemea Ibrahim Tibanyendera uje kuwasilisha kwa njia ya mdomo maombi yao ya kuwaona washitakiwa wana kesi ya kujibu au la.

Awali kabla ya Hakimu Fimbo kuanza kusikiliza kesi hiyo alianza kwa kumuachilia huru mshitakiwa wa 21 baada ya wakili wa serikali Kongora kuwasilisha hati iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk.Eliezer Feleshi chini ya kifungu cha 91(1) ya Sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 ,ambapo DPP ameona hataki kuendelea kumshitaki mshitakiwa huyo ambaye wakili Tibanyendera alieleza kuwa mtu huyo ana maradhi ya akili na Mkazi wa Mkuranga na siku hiyo ya maandamano Februali 15 mwaka huu, alikamatwa wakati akiwa na mjomba wake ambaye ni mshitakiwa wa 16 wakati wakitokea katika Hospitali ya Taifa ya Mhimbili kuchukua dawa za  mshitakiwa huyo aliyeachiliwa huru jana.

Aidha jana  Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam(ZDCO), Hemed Msangi ambaye ni shahidi wa kwanza katika kesi hiyo aliitwa tena kwa ajili ya kuhojiwa na wakili wa utetezi ambapo alieleza  kuwa kati ya Februali 11-17 mwaka huu, yeye alikuwa ndiye Kamanda wa Polisi Kanda Maalum  ya Dar es Salaam, na kwamba  Februali 11 alipokea barua toka Shura ya Maimamu iliyokuwa imesainiwa na  Sheikh Juma Idd  ikimuomba kibari cha kufanya maandamano ya kwenda ofisi kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kumhoji ni kwanini hampatii dhamana  Ponda na kwamba maandamano hayo walikuwa wakitaka yafanyike Februali 15 baada ya swala ya Ijumaa na wandamanaji watakuwa wakitokea misikiti mbalimbali.

ACP- Msangi alidai  yeye na maofisa wenzake walitafakari hiyo barua  ambayo ilikuwa na saini ya Sheikh  Juma  Idd ambaye ni Amir wa Shura ya Maimamu  Temeke na walijiuliza uzito wa maandamano hayo na kwamba jeshi hilo walibaini kuwa hawakuwa na askari wa kutosha wakuwapeleka kila msikiti kwaajili ya kuyalinda waandamanaji hao na hivyo uhaba huo wa askari ungeweza kuleta usalama mdomo na pia walifikia uamuzi wa kuyakaza maandamano yake kwasababu waliona ofisi ya DPP ipo katikati ya jiji na ina sehemu finyu hivyo maandamano hayo yangeruhusiwa yangweza kuathiri haki za watu wengine wanaotumia jengo hilo la ofisi ya DPP ambalo linatumiwa na maofisi mengi na watembea kwa mguu.

“Pia jeshi la polisi lilitazama kuwa kesi ya Ponda ipo mahakamani hivyo ingewaruhusu waandamanaji hao kwenda mahakamani ni kama kuingia huru wa mahakama  na kwamba jeshi lilipata taarifa toka kwa DPP kuwa DDP alikuwa amepokea barua toka kwa Baraza la Wanazuoni iliyokuwa ikimuomba wakazungumze naye na kwamba tayari DPP alishalikubalia baraza hilo kuwa angekutana nao Februali 28 mwaka huu, ....kwasababu hiyo mimi niliwandikia barua ya kuzuia kufanyika kwa maandamano kwa sababu hizo zilizozitaja hapo juu kwani pia jeshi lilikuwa limepata taarifa za watu walikuwa wamepanga kufanya vurugu katika maandamano hayo”alidai ZDCO-Msangi.

Aliendelea kueleza kuwa licha ya kuwapelekea zuio hilo la maandamano kwa maandishi waombaji hao wa maandamano, pia yeye aliutangazia umma kupitia vyombo vya habari kuwa jeshi la polisi limezuia maandamano hayo lakini ilipofika Februali 15 washitakiwa hao walikaidi amri hiyo ya jeshi polisi waliandamana wakiwa na mabango, mawe,na silaha za jadi na yeye alitoa amri kwa askari wake wawatawanye na kuwakamata  na kuwafikisha polisi na kisha wafiksihwe mahakamani.

Itakumbukwa kuwa kesi hii ilifunguliwa rasmi Februali 18, na Februali 19 mwaka huu itakaanza kusikilizwa mfululizo hadi jana upande wa jamhuru ilipofunga ushahidi wao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Februali 27 mwaka 2013.




  



SERIKALI YAFUNGA USHAHIDI KESI YA PONDA


Na Happiness Katabazi

HATIMAYE upande wa jamhuri katika kesi ya uchochezi na kuiba malighafi zenye thamani ya Sh.milioni 59 inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Pnda Issa Ponda na wenzake 48 , umetangaza rasmi kuifunga kesi yake.

Hayo yalisemwa jana na Wakili Mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, muda mfupi baada ya shahidi wa 17 wa upande wa Jamhuru D/C F8586 Ismail wa kituo cha Polisi Chang’ombe kumaliza kutoa ushahidi wake ambapo jana jumla ya mashahidi watatu kwa mpigo walitoa ushahidi wao.

Wakili Kweka alieleza kuwa hadi kufikia jana upande wa jamhuri ulikuwa umeleta mashahidi 17 na vielelezo 13 ambavyo vilipokelewa mahakamani kama vielelezo vimetosheleza upande wa jamhuri kufikia uamuzi huo wa kuifunga kesi yao.

Baada ya wakili Kweka kutoa maelezo hayo wakili wa Ponda, Juma Nassor aliomba mahakama iwapatie muda hadi Machi 4 ili waweze kwenda kujiandaa na kufanya utafiti utakaowawezesha kuwasilisha maombi ya kuwaona wateja wao wote 49 hawana kesi ya kujibu.

Hata hivyo Hakimu Nongwa alisema jukumu la kupanga tarehe ya kuja kufanya majumuisho ya mawakili wa pande hizo mbili katika kesi hiyo ya kuwaona washitakiwa wanakesi ya kujibu au la ni vyema ikaachiwa mahakama na hakimu huyo akatoa amri kuwa majumuisho hayo yatafanyika kesho (Februali 27 mwaka huu),saa mbili asubuhi  na kwamba na akautaka upande wa utetezi ndiyo utakuwa wa kwanza kuwasilisha majumuisho yao kwa njia ya mdomo.

Kabla ya Hakimu Nongwa jana saa nane mchana ya kukubali ombi la upande wa jamhuri la kuifunga kesi yake, alisikiliza ushahidi wa mashahidi watatu wa waliokuwa wameletwa na upande wa jamhuri ambao ni shahidi wa 15 ambaye ni F3929 D/C ,Constebo Eliaeli (35) ,shahidi wa 16 ambaye ni Stationi Sajenti  Amos wa kituo cha Polisi Kati na Shahidi wa 17 ambaye askari mpelelezi Na. F8586 D/C Ismail.

Kwa upande wake shahidi wa 17, D/C Ismail aeleza mahakama kuwa Oktoba 17 mwaka jana, alipewa kazi na Mkuu wake wa kazi  na saa 2-9 alasiri alikuwa katika kituo cha Polisi Kijinyoma alipewa jukumu la kuwahoji washitakiwa ambao walikamatwa katika kiwanja cha Chang’ombe Marskas  wakikabiliwa na makosa ya kuingia kwa jinai katika kiwanja hicho .

Ismail alidai kuwa yeye alimhoji mshitakiwa aitwaye  Fiswaa ambaye alimweleza kuwa kati ya tarehe ,mwezi na saa isiyofahamika akiwa nyumbani kwake Mlandazi Mkoani Pwani, akiwa anasikiliza Redio Iman, alisikia tangazo lilokuwa likiwataka waumini wa dini ya Kiislamu kwenda kuongeza nguvu ya kujenga msikiti katika kiwanja cha Chang’ombe Markas ambacho ni mali ya waislamu na si Bakwata lakini kilikuwa kimevamiwa.

Shahidi huyo alidai kuwa , mshitakiwa huyo alimweleza kuwa  aliitikia wito huo na kufunga safari toka nyumbani kwake Mlandizi na kwenda kuja hadi kwenye kiwanja hicho kilichopo Dar es Salaam, na kuungana na wenzake ambapo kiongozi wao aliyekuwa akiwaongoza walipokuwa kwenye kiwanja hicho ni mshitakiwa wa kwanza ambaye ni  Ponda.

“Sululu,mapanga vilitumika kama vifaa vya kujengea msikiti wa muda  katika kiwanja hicho  na ndipo usiku wa kuamkia Oktoba 17 mwaka jana, tukiwa tumekaa kwenye kiwanja hicho nikasikia sauti ikisema kuwa panda kwenye gari ,panga kwenye gari na sikuwa na kumbukumbuku yoyote’alidai Ismail kuelezwa na Fiswaa na maelezo ya mshitakiwa huyo yalipokelewa kama kilelezo cha 13 na hakikupingwa na mawakili wa utetezi.

Kwa upande wake shahidi wake Shahidi wa 16, Station Sajenti Amos, alidai kuwa Oktoba 17 mwaka jana alipewa jukumu la kumhoji mshtakiwa Hussein Ally  ambaye mshitakiwa huyo alimweleza kuwa alipokea maelekezo kutoka kwa msheikh wake wa msikiti wa Kinyerezi yakimtaka afike katika kiwanja cha Markas na alienda akakutana na wenzake ambapo walianza kufanya usafi  ili waweze kujenga msikiti na walikuwa wakiongozwa na Ponda kufanya ujenzi na usafi katika kiwanja hicho ambacho tayari mashahidi wengine toka Bakwata walishasema kiwanja hicho ni mali ya kampuni ya Agritanza Ltd siyo Bakwata tena na maelezo ya mshitakiwa hayo yalipokelewa kama kielelezo cha 12.

Aidha kwa upande wake shahidi wa 15 , D/C Constebo Elieli  alidai kuwa Oktoba 17 mwaka jana , alipewa jukumu na mkubwa wake wa kazi la kuandika maelezo ya mshitakiwa Mohamed Ramadhan ambaye alimweleza kuwa siku hiyo yeye alikwenda kusali katika eneo la kiwanja hicho akitoa Oysterbay Dar es Salaam.

Elieli alieleza kuwa mshitakiwa huyo alimweleza kuwa alifikia uamuzi wa kwenda kusali swala ya alfajiri hapo Chang’ombe markas kwasababu alikuwa anauguliwa na ndugu yake anayeishi Keko ambapo yeye mshitakiwa hakutaka kwenda kusali misikito ya Keko kwasababu hali ya usalama ili ni mbaya na hivyo akaamua kwenda kusali katika eneo hilo la Markas.

“Mshitakiwa huyo akanieleza eti baada ya kusali hapo alfajiri ya Oktoba 17 mwaka jana, ndiyo ghafla alishitukia anakamatwa na mapolisi na kwamba yeye hakuwa.Na kwamba nilipomhoji kama analifahamu vuguvugu la waislamu kudai haki zao, mshitakiwa huyo alikubali kulifahamu vuguvugu hilo na kwamba yeye pale kwenye lile eneo alipokamatiwa alikuwa katika kutetea  na kudai haki yao ya kurejeshewa kiwanja kile ambacho ni mali ya waislamu na si Bakwata”alidai Elieli lakini hata hivyo mahakama ilikataa kuyapokea maelezo hayo kama kielelezo kwasababu yana dosari nyingi za kisheria.

Awali Oktoba 18 mwaka jana, ilidaiwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo na wakili Kweka mbele ya Hakimu Nongwa kuwa washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa matano likiwemo kosa la kula njama,wizi wa malighafi zenye thamani y ash.milioni 59 na uchochezi ambalo linamkabili Ponda na mshitakiwa wa tano Mkadamu Swalehe ambao wanaendelea kusota gerezani kwasababu Mkurugenzi wa Mashitaka,Dk.Eliezer Feleshi bado hawajaondolea hati ya kuwafungia dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Februali 26 mwaka 2013.

SHAHIDI ADAI PONDA ALIAMASISHA WAISLAMU WAFANYE UVAMIZI




Na Happiness Katabazi


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu  Dar es Salaam imeelezwa kuwa Katibu  wa Jumuiya na Taasisi za kiislamu Shekhe Ponda Issa Ponda  ndiye aliwapatia taarifa masheikh  wa misikiti  pamoja na kuwaamasisha  waumini wa dini ya kiislamu waende wakaiokombee mali ya waislamu ambacho ni kiwanja Chan’ombe Markas ambacho walidai kimeporwa wakati kiwanja hicho si mali ya waislamu ni mali ya kampuni ya Agritanza Ltd.

Madai hayo yaliyolewa jana na shahidi wa 14 wa upande wa Jamhuri D/C Koplo Zakayo  katika kesi ya uchochezi na wizi wa malighafi zenye thamani ya Sh.milioni 59 inayomkabili Ponda na wenzake 48  wakati akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili Mwandamizi wa Serikali Tumaini Kweka mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa ambapo alidai kuwa  alidai kuwa mshitakiwa Ayubu Juma alimueleza hayo wakati akimuhoji katika kituo cha polisi Kijitonyama.

Koplo Zakayo alidai, Juma alimueleza kuwa Oktoba 12 mwaka jana ,saa mbili usiku  baada ya swala ya Insha kumalizika  katika msikiti Mwanamtoti, Shekhe Amri  Said ambaye ni kiongozi wa msikiti huo, aliwatangazia waumini waliokuwa wameudhulia ibada hiyo  kuwa amepata taarifa kutoka kwa  mshitakiwa wa kwanza  Ponda kuwa eneo la Markas ambao wao walidai ni mali ya waislamu wakati Bakatwa inadai eneo hilo si mali ya waislamu kuwa limevamiwa.

Zakayo alidai kuwa Juma alimweleza kuwa Sheikh Said akaendelea kuwatangazia kuwa Ponda amewataka  waislamu waungane kwenda kulikomboa eneo hilo  lakini yeye alishindwa kwenda hadi usiku wa Oktoba 16 mwaka jana  alipowasisitizia, wakaenda watu 14 walipofika katika eneo la Chang’ombe   wakaambiwa wajenge msikiti wa muda.

Aliendelea kueleza kuwa , Juma katika maelezo yake alimueleza kuwa Baraza la Waislamu (BAKWATA) waliuza eneo hilo kwa manufaa yao binafsi  na pia hawakuwa wamefuata taratibu  za kisheria kwasababu  kiwanja kile ni mali ya waislamu.
Kwa upande wake shahidi wa 13, Koplo Masiku ambaye ni ASkari kituo cha polisi Chang’ombe alidai kuwa, wakati akimuhoji mshitakiwa Khalid Issa alimueleza kuwa, walikwenda katika eneo la Chang’ombe Markazi kwaajili yakufanya harambee ya kujenga msikiti.

Koplo Masiku alidai kuwa wakati akimhoji mshitakiwa Abdalah Senza , mshitakiwa huyo alimweleza  kuwa aliteuliwa na viongozi wa msikiti wa Vingunguti kwa ajili ya kwenda kulinda eneo hilo linalomilikiwa na waislamu ili lisiuzwe.

Katika maelezo yake alidai, eneo hilo lilikuwa linamilikiwa na Wamisri na walijenga shule ili waislamu wasome bure pamoja na hospitali ambayo bado haijaanza kutoa huduma. Aidha mashahidi hao wawili walitoa maelezo waliyokuwa wamewachukua washitakiwa hao wakati wakiwahoji  na waliomba mahakama ipokee kama vielelezo na mawakili wa upande wa utetezi hawakupinga .

Hakimu  Nongwa alipokea nakala ya maelezo hayo kama vielelezo na kisha akaiarisha kesi hiyo hadi Jumatatu ijayo ambayo shahidi wa 15 ataanza kutoa ushahidi wake katika kesi hiyo ambayo ambayo imeanza kusikilizwa mfululizo tangu Jumatatu wiki hii chini ya ulinzi mkali wa vyombo vya ulinzi na usalama na akaamuru Ponda na mshitakiwa wa tano Mkadamu Abdallah warudishwe rumande kwasababu Mkurugenzi wa Mashitaka,Dk.Eliezer Feleshi bado hajaondoa hati yake iliyowangia dhamana na akaamuru washitakiwa dhamana zao zinaendelea.


Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Februali 23 mwaka 2013.