MANJI,MWALUSAKO WAKIMBILIA MAHAKAMA YA RUFAA
Na Happiness Katabazi
MWENYEKITI wa Klabu ya Yanga Yusuph Manji na Katibu Mkuu wake, Lawrence Mwalusako, jana walifika katika Mahakama Kuu Diveshi ya Kazi Dar es Salaam lakini hawakusimama kizimbani kujieleza ni kwanini wasichukuliwe hatua za kisheria kwa kosa la kudharau amri ya mahakama.
Manji ambaye pia ni mfanyabiashara na Mwalusako walifika mbele ya Msajili wa mahakama hiyo Mohamed Gwae lakini hawakuhojiwa chochote kwasababu jalada la kesi limepelekwa Mahakama ya Rufani kwaajili ya kufanyiwa marejeo.
Katika kesi hiyo timu ya Yanga inadaiwa kukiuka umuzi uliyokwishatolewa na mahakama hiyo ambayo iliitaka timu hiyo iweke mahakamani Sh milioni 106, kwasababu ilishindwa kuwalipa walalamikaji katika kesi hiyo, ambae ni Kipa wa zamani wa timu hiyo Stephen Marashi na beki raia wa Malawi, Wisdom Ndlovu.
Jalada la kesi hiyo hiyo limeitwa Mahakama ya Rufaa baada ya mdaiwa (Timu ya Yanga), kuwasilisha ombi katika mahakama hiyo ya Rufani linaloiomba mahakama hiyo ifanye marejeo ya uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu Diveshi ya Kazi ambao uliitaka timu hiyo iweke kiasi hicho cha fedha mahakamani.
Jana Msajili Gwae
alisema kuitwa kwa Manji na Mwalusako tena mahakamani hapo, kutategemea uamuzi
utakaotolewa na Mahakama ya rufaa.
Ombi hilo la Yanga la linaloomba Mahakama ya Rufaa ifanyie marejeo uamuzi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi , waliliwasilisha Machi 25 mwaka huu, chini ya hati ya dharura likiomba mahakama hiyo ya juu kabisa nchini iitishe jalada la kesi ya msingi ili iweze kuupitia mwenendo mzima wa kesi hiyo iliione uamuzi huo ulikuwa sahihi.
Kwa mujibu wa hati ya kiapo kilichoapwa na mdaiwa wa pili ( Mwalusako) inayounga mkono ombi hilo, Oktoba 11 mwaka jana waliwasilisha ombi la marejeo pamoja na kuwasilisha ombi la kusitisha utekelezaji wa tuzo ya kuwalipa wachezaji hao.
Kwa mujibu wa hati hiyo, Februali 5 mwaka huu, Msajili Gwae ilikataa ombi la kusitisha utekelezaji wa hukumu hiyo na kuwataka Yanga kuweka fedha hizo mahakamani wakati wakisubiri uamuzi wa ombi la marejeo.
Anadai
kuwa, utekelezaji dhidi ya walalamikaji umekwenda kinyume na utaratibu
kwa kuwa msuluhishi alishindwa kuzingatia nafasi ya mlalamikaji katika suala
hilo, pia Klabu hiyo haina mali yoyote ya kuweza kutekeleza tuzo hiyo.
Katika kesi ya msingi, Marashi na mwenzake, wameiomba mahakama kumfunga jela mwenyekiti huyo na katibu wake, baada ya timu hiyo kushindwa kutekeleza amri ya mahakama, ikiamuru kiasi hicho kulipwa.
Kamisheni ya Usuluhishi na Upatanishi iliiamuru Yanga iwalipe wachezaji hao fedha hizo kutokana na kukatisha mkataba wao kinyume cha taratibu, na walitakiwa kulipwa wiki mbili kuanzia tarehe ya hukumu.
Yanga iliingia kwenye mgogoro na wachezaji hao, baada ya kuvunja nao mikataba mwaka 2010 kutokana na sheria mpya ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuzitaka klabu kuwa na nyota watano tu kutoka nje, hivyo kuwaacha Ndlovu, Mkenya John Njoroge na Mtanzania Marashi. Njoroge alilipwa milioni 17.
Walalamikaji hao
wanadai kuwa, walisajiliwa na Yanga kwa mkataba wa miaka miwili kuanzia Machi
18, 2010, wanadai Julai 17, 2010, wakiwa wanajiandaa na kipindi kingine kipya
cha msimu wa ligi, Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic aliwaambia kwa mdomo
kwamba wao si wachezaji wa Yanga.
Walidai kwa
mujibu wa mkataba, Yanga walitakiwa kuwasiliana nao kuhusu kukatisha mikataba
yao ndani ya siku saba kabla ya tarehe iliyokuwa imewekwa na TFF, kwa timu za
ligi kuu kuwasilisha majina ya wachezaji watakaoachwa jambo hilo liliwakosesha
nafasi ya kucheza katika timu nyingine.
Kamisheni
iliamuru, Ndlovu alipwe sh. milioni 57 kama mshahara wa miaka miwili, sh.
milioni 1.8 kama gharama za usafiri wa kumrejesha Malawi na sh. milioni 20 kama
fidia ya kumkosesha nafasi ya kucheza.
Kwa upande wa
Marashi, Yanga iliamriwa imlipe sh. milioni 18 kama gharama za kutia saini
mkataba na mshahara kwa miaka miwili, sh. milioni 10 kwa kupoteza nafasi ya
kucheza na sh. 500,000 kama malipo aliyopaswa kulipwa wakati anatia saini
mkataba wa 2009 hadi 2010.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Machi 28 mwaka 2013.
ANAYEDAIWA KUUMUA TRAFIKI KORTINI
Na Happiness Katabazi
ANAYEDAIWA kumuua askari wa kikosi cha Usalama Barabarani
wiki iliyopita, Elikiza Nnko, Jakson Stephen Fimbo jana alifikishwa katika
Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni akikabiliwa na makosa ya matatu likiwemo kosa
la kuingilia msafara wa kiongozi.
Mbele ya Hakimu Mkazi Kwey Lusema wakili mwandamizi wa
serikali Lasdilaus Komanya alilitaja kosa la kwanza ni la kusababisha kifo cha trafiki huyo kupitia kwendesha gari kwa hatari na kwamba Machi 18 mwaka huu, katika barabara ya Bagamoyo katika mataa ya
Bamaga jijini Dar es Salaam, mshitakiwa
akiwa ni dereva kiongozi wa gari lenye
namba za usajili T328 BML aina ya Land
Lover Discovery.
Wakili Komanya alidai mshitakiwa huyo aliendesha gari hilo ka mwendo wa hatari katika barabara hiyo ambayo ni ya umma Mshitakiwa
huyo jambo ambalo lina hatarisha usalama wa raia na kutokana na mshitakiwa huyo kuendesha gari
hilo kwa mwendo huo wa hatari alimgonga askari huyo ambaye amezikwa alhamisi
iliyopita.
Alidai kosa la pili ni
kuingilia msafara wa kiongozi,kuwa
siyo ya Machi 18 mwaka huu, katika eneo hilo la mataa ya Bamaga,mshitakiwa huyo
hakutii maelekezo yaliyokuwa yakitolewa
kwa ishara ya askari huyo Elikiza,ambaye alikuwa na wajibu wa kuyasimamisha magari
kwa njia ya ishara.
Wakili Komanya alidai shitaka la tatu ni la kushitwa kutoa taarifa za kusababisha ajali katika barabara
hiyo ya umma na kwamba alishindwa kutoa tarifa za kusababisha ajali hiyo katika
kituo chochote cha jirani.
Hata hivyo mshitakiwa huyo alikanusha mashitaka hayo na
wakili Komanya alidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na anaomba tarahe ya
kuja kumsomea maelezo ya awali mshitakiwa.
Kwa upande wake hakimu Lusema alisema ili apate dhamana ni
lazima awe na wadhamini wawili ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh.milioni
mbili ,hata hivyo mshitakiwa huyo alitimiza masharti hayo ya dhamana na akapata
dhamana na hakimu huyo akaiarisha kesi hiyo
Aprili 15 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya upande wa jamhuri kumsomea
maelezo ya awali.
Katika hatua hutua nyinge, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
Dar es Salaam, imeshindwa kuendelea kusikiliza kesi ya kuchapisha makala ya
uchochezi inayomkabili aliyekuwa Mharii Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima na
wenzake,kwasababu Kibanda bado amelazwa katika hospitali moja nchini Afrika
Kusini kwaajili ya matibabu na hivyo ameiarisha hadi Aprili 29 mwaka huu.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Machi 26 mwaka 2013.
KAJALA ATIWA HATIANI,WEMA SEPETU AMLIPITIA FAINI YA SH.MIL 13
Na Happiness
Katabazi
HATIMAYE
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imewahukumu kwenda jela miaka
nane au kulipa faini ya Sh.milioni 13 msainii wa Filamu nchini, baada ya kumtia
hatiani katika makosa ya kula njama kuamisha umiliki wa nyumba, na kuamisha
umiliki wa nyumba iliyokuwa iliyokuwa imezuiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
isiuzwe.
Hukumu hiyo
iliyolewa jana na Hakimu Mkazi Sundi Fimbo ambapo alianza kwa kuikumbusha
mahakama hiyo kuwa Kajala na Faraja Chambo walikuwa wakikabiliwa na makosa
matatu yaliyofunguliwa mapema mwaka jana mahakamani hapo..
Makosa hayo
ni kosa la kwanza ni la kula njama kinyume na kifungu cha 34 cha
Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007, ambako washitakiwa wote
kwa pamoja, walitenda kosa hilo la kula njama la kuhamisha umiliki wa nyumba
iliyopo Kunduchi, Salasala eneo ambalo halijapimwa jijini Dar es Salaam.
Shitaka la pili ni kwamba, Aprili 14 mwaka 2010 walihamisha isivyo halali umiliki wa nyumba hiyo, ambayo walikuwa wakiimiliki kwenda kwa Emilian Rugalia, ambaye ndiye walimuuzia kinyume na kifungu cha 34(2)A(3), cha Sheria ya TAKUKURU ya mwaka 2007, na shitaka la tatu ni la kutakatisha fedha, ambalo walilitenda siku hiyo ya Aprili 14 mwaka 2010, huku wakijiua ni kinyume cha sheria hiyo.
Hakimu Fimbo
alisema baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, alisema upande wa
Jamhuri umeweza kuithibitisha kesi hiyo na hivyo mahakama hiyo imemtia hatiani
Kajala katika kosa la kwanza na la pili tu wakati Chambo amepatikana na hatia
katika makosa yote matatu.
Alisema
katika kosa la kwanza Kajala na Chambo watatakiwa walipe faini ya Sh.milioni
tano kila mmoja au kwenda jela miaka mitatu. Kosa la pili watatakiwa walipe
faini ya Sh.milioni nane aukwenda jela
miaka mitano kwa kila mmoja.
Aidha katika
kosa la tatu ambayo ni Chambo ndiyo amekutwa na hatia atatakiwa alipe faini ya Sh.milioni 200 au
kwenda jela miaka mitano na kwamba adhabu hizo hazitakwenda pamoja.Hivyo Kajala
peke yake amehukumiwa kwenda jela jumla
ya miaka nane au kulipa jumla ya
Sh.milioni 13 .
“Mahakama
imewakutana na hatia washitakiwa wote katika kosa la pili kwasababu ushahidi umethibitisha
kuwa washitakiwa wote walikuwa
wakifahamu kuwa kuwaliwa na hati ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliyokuwa
imezuia nyumba yao waziize kwasababu Taasisi ya Kuzia na Kupambana na Rushwa
ilikuwa ikidai kuwa nyumba hiyo imepatikana kwa njia ya utakatishaji fedha,lakini
wao wakakaidi amri hiyo wakaamua kuiuza”alisema Hakimu Fimbo.
Akilichambua
kosa la kwanza, alisema pia upande wa jamhuri umeweza kulithibitisha kwasababu kosa la pili limeweza kuthibitishwa
.
Kuhusu
shitaka la tatu, hakimu huyo alisema amemwachilia huru Kajala kwasababu upande
wa jamhuri umeshindwa kuthitisha Kajala alishiriki vipi katika upatikanaji wa
fedha haramu kwasababu ilidaiwa kuwa
Chambo alizipata fedha haramu katika maelezo ya onyo kuwa alizipata fedha za kujengea nyumba hiyo wakati
akiwa mfanyakazi wa Benki ya NBC.
‘Na kwa
mujibu wa maelezo ya onyo ya Chambo ambaye ni mume wa Kajala, alikiri kuwa wakati akiwa mfanyakazi wa benki ya NBC
alikuwa akichukua fedha na kuzituma kwa baadhi ya watu wa ofisi ya TTCL ,watu
ambao hawakuwa wakistahili kulipwa na baada ya vyombo vya dola kuanza
kumfuatulia akaamua kuizua nyumba yake hiyo”alisema hakimu Fimbo.
Hata hivyo
baada ya hukumu kutolewa wasanii wa filamu nchini walikuwa wamefika mahakamani
hapo kufuatilia hukumu ya kesi hiyo, walikusanyika katika viunga vya mahakama
hiyo na kuanza kujadiliana ili wachangishane fedha lakini msanii Wema Sepetu
aliwataka wenzake wasichanganishane fedha ,badala yake yeye analipa Sh.milioni
13 na akaondoka katika eneo hilo na kisha kurejea mahakamani hapo saa saba
mchana na kulipa faini hiyo na kisha kuondika na Kajala ,wakati Chambo
akirudishwa gerezani kwani alishindwa kulipa fidia hiyo na pia anakabiliwa na
kesi nyingine ya utakatishaji fedha mahakamani hapo.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi 26 mwaka 2013.
LWAKATARE SASA AKIMBILIA MAHAKAMA KUU
Na Happiness
Katabazi
MAWAKILI
wanaomtetea Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo(Chadema), jana wamewasilisha Mahakama Kuu Dar es Salaam, ombi la
kuomba mahakama hiyo iitije majadala ya kesi tuhuma za ugaidi zilizofunguliwa
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwaajili ya kuzifanyia marejeo.
Maombi hayo
ambayo tayari yameishapewa namba 14 ya mwaka huu, na yameapwa na wakili
wake wa washitakiwa hao Peter
Kibatara yaliwasilishwa jana mchana na
karani wa wakili huyo mahakamani hapo.
Kwa mujibu wa
kiapo kilichoapwa na wakili Kibatara, mawakili hao wanaomba mahakama hiyo
ifanyie marejeo wa majadala ya kesi ya ugaidi Na.37/2013 iliyofunguliwa wa
Machi 18 mwaka huu na Mkurugenzi wa Mashitaka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu dhidi ya Lwakatare na Ludovick Joseph mbele ya hakimu Emilius
Mchauru ambapo siku hiyo alisikiliza
maombi ya pande mbili.
Maombi ya
mawakili wa utetezi yaliomba washitakiwa wapewe dhamana wakati mawakili wakuu
wa serikali Ponsian Lukosi, Prudence Rweyongeza na Peter Mahugo waliomba
mahakama isitoe dhamana kwasababu kesi makosa yanaoyoangukia katika sheria za
ugaidi ya mwaka 2002 hayana dhamana.
Ambapo siku
hiyo hakimu Mchauru aliairisha kesi hiyo hadi Machi 20 kwaajili ya kuja kutolea uamuzi wa maombi
hayo pamoja na maombi mengine lakini
hakimu huyo alijkuta akishindwa kutoa uamuzi wake kwasababu Mkurugenzi
wa Mashitaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi amewasilisha hati ya kuwafutia kesi washitakiwa hao chini
ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002
kwasababu hana haja ya kuendelea
kuwashitaki.
Lakini
dakika chache baada ya hakimu Mchauru kuwafutia kesi hiyo, wanausalama
waliwakamata tena washitakiwa hao na kisha kuwapandisha mahakamani mbele ya
Hakimu mwingine Alocye Katemana na wakili wa serikali Rweyongeza alianza kuwasomea mashitaka manne
mapya katika kesi mpya iliyopewa Na.6/2013 ambayo mashitaka ni yale yale yaliyokuwa kwenye hati ya mashitaka ya
awali iliyofutwa na DPP,ambapo Katemana
aliwataka washitakiwa wasijibu chochote na akaamuru waende gerezani hadi Aprili
tatu.
Kwa mujibu
wa madai yao mawakili wa Lwakatare wanaomba Mahakama Kuu ipitie uamuzi wa DPP wa kuifuta hati ya awali ya mashitaka na
kisha kuwafungulia kesi upya washitakiwa hao wakati kesi hiyo ilikuwa imekuja
kwaajili ya mahakama kuitolea uamuzi lakini mahakama ikashindwa kutoa uamuzi
wake kwasababu DPP aliwasilisha hati ya kuifuta kesi hiyo.
Kwa mujibu
wa habari za kuaminika toka ndani ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,
zimelieleza gazeti hili kuwa tayari uongozi wa mahakama imeishatoa amri ya
kuyaitisha majalada hayo mawili ya kesi yanayomkabili Lwakatare na mwenzake
yatoke mahakama ya Kisutu yaletwe mahakama kuu kwaajili ya kuyafanyia marejeo.
Kosa la kwanza
ambalo linawakabili washitakiwa wote kuwa ni la kula njama kutenda kosa la
jinai kinyume na kifungu cha 284 cha
Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 , na kwamba mnamo Desemba 28 mwaka
jana, huko Kimara King’ong’o Stopover,
wote kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa kutaka kutumia sumu kwa lengo la kumdhuru Denis Msaki
ambaye ni Mhariri wa habari wa Gazeti la Mwananchi ambalo ni kinyume na
kifungu cha 227 cha sheria hiyo.
Wakili
Rweyongeza alilitaja kosa la pili kuwa
ni la kula njama ambalo pia ni kwaajili
ya washitakiwa wote ambalo ni kinyume na
kifungu cha 24(2) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi Na.21 ya mwaka 2002, ambapo
washitakiwa hao walitenda kosa la ugaidi la
kutaka kumteka Msaki kinyume na
kifungu cha 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya
Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.
Shitaka
la tatu ni la washitakiwa wote ambapo wanashitakiwa kwa kosa la kupanga kufanya makosa ya ugaidi kinyume na kifungu cha 59(a) cha Sheria ya
Kuzuia ugaidi kwamba Desemba 28 mwaka jana,walishiriki katika mkutano wa kupanga
kufanya vitendo vya kumteka nyaraka Msaki
kinyume na kifungu 4(2)(c) (iii) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi.
Shitaka
la nne, Rweyongeza alidai linamkabili Lwakatare peke yake ni aliwezesha kutendeka kwa kosa la ugaidi
kinyume na kifungu cha 23(a) cha sheria ya kuzuia ugaidi , kwamba Desemba 28
mwaka jana, Lwakatale akiwa ni mmiliki nyumba hiyo ilipo Kimaraka
King’ong’o kwa makusudi aliliruhusu
kufanyika kwa kikao hicho baina yake na Ludovick cha kutenda kosa la ugaidi la kutaka kumteka
nyara Msaki hata hivyo walikanusha mashitaka hayo.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Machi 23 mwaka 2013.