MENEJA BENKI YA CRDB JELA MIAKA MITANO KWA WIZI



Na Happiness Katabazi,Mwanza

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mwanza, imemhukumu kifungo cha miaka mitano jela Meneja wa Benki ya CRDB,wa matawi ya Nyanza na Bugando mkoani Mwanza, Daniel Peter Waijaha, pamoja na mteja wa benki hiyo, Dismas Mohamed Ndaliko  baada ya kuwakuta na hatia  wa kosa la wizi wa jumla ya  Sh Milioni 140 mali ya benki hiyo.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza,  Anjelo Rumisha ambaye alikuwa akisikiliza kesi hiyo ya jinai Na.76 ya mwaka 2011.Ambapo mbali na adhabu hiyo pia hakimu huyo amemtaka meneja huyo azirejeshe fedha hizo alizoziiba katika Tawi la Nyanza.

Hakimu Rumisha alisema baada ya kumtia hatiani meneja huyo pia Meneja wa Business Banking, Stephano Harry Mboma, ambaye alikuwa mshatakiwa wa pili katika kesi hiyo amemuachia huru  baada ya kuona hana hatia katika mashitaka dhidi yake.



Kwa upande wake Ndaliko (mteja) ambaye alikuwa mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo alihukumiwa adhabu hiyo kwa kosa la kujaribu kumsaidia meneja huyo kuepukana na adhabu kwa kufuta ushahidi wa kosa hilo.
Wakati meneja huyo na mteja wakihukumiwa adhabu hiyo, Meneja wa Business Banking, Stephano Harry Mboma, ambaye alikuwa mshatakiwa wa pili katika kesi hiyo ameachiwa huru baada ya kuonekana kuwa hana hatia katika mashtaka yote yaliyokuwa yakimkabili.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, Jumatatu ya Juma hili, Anjelo Rumisha, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo.
Hata hivyo licha ya kuwatia hatiani washtakiwa hao kwa mashtaka hayo, na kuwahukumu adhabu hiyo, Hakimu Rumisha aliwaachia huru katika mashtaka mengine yote yaliyokuwa yakiwakabili.

Upande wa mashtaka  uliokuwa ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, David Kakwaya haukuridhika na uamuzi huo wa washtakiwa hao kuachiwa huru katika mashtaka mengine, na tayari umewasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa wote kwa pamoja  walikuwa wakikabiliwa na jumla ya mashtaka matano, lakini ni mashtaka mawili tu ndio yalikuwa yakiwahusu washtakiwa wote watatu, ambayo ni kula njama kutenda kosa na kughushi.

Katika shtaka la kwanza washtakiwa wote walikuwa wakidaiwa kuwa katika tarehe tofautitofauti katika miezi isiyofahamika, mwaka 2010, walikula njama kutenda kosa la kughushi nyaraka.

Shtaka la pili lilikuwa ni la wizi likiwahusu mshtakiwa wa kwanza Meneja Waijaha na mshtakiwa wa pili, Mboma. Walidaiwa kuwa katika  tarehe na miezi isiyofahamika mwaka 2010, kwa pamoja waliiba Sh 107.8 milioni katika benki hiyo tawi la Nyanza.

Shtaka la tatu ambalo pia ni wizi lilikuwa likiwahusu mshtakiwa wa  kwanza, Waijaha na wa tatu, Ndaliko (mteja). Walidaiwa kuwa Desemba 4, 2010, katika benki hiyo tawi la Bugando, waliiba Sh32.15 milioni mali ya benki hiyo.

Katika shtaka la nne la kughushi, washtakiwa wote walikuwa wakidaiwa kuwa kati ya Desemba 4, 2010, katika tawi la Bugando, kwa pamoja walitengeneza nyaraka za uwongo za kuchukulia pesa benki kwa lengo la kufanya udanganyifu.

Ilidaiwa kuwa lengo la nyaraka hizo za uwongo lilikuwa ni mteja mmoja aitwaye New Ana  Filling Station, mmiliki wa akaunti namba 01J1016800800, alichukua pesa kiasi cha Sh 140 miloni katika tawi hilo, jambo ambalo halikiuwa kweli.

Mshtakiwa wa tatu (Ndaliko) pia alikuwa pia akikabiliwa na shtaka mbadala la kusaidia kutendeka kwa kosa la wizi.
Alidaiwa kuwa kati ya  Desemba 4, 2010,  na kwa siku nyingine baadaye , akijua kuwa mshtakiwa wa kwanza aliiba pesa jumla ya Sh140 milioni mali ya CRDB, alimsaidia kufuta ushahidi ili kumwezesha kuepuka adhabu.
Shtaka la tano ni la kuwasilisha nyaraka za uwongo, lililokuwa likimkabili mshtakiwa wa kwanza peke yake (Meneja Waijaha).

Ilidaiwa kuwa Desemba 4, 2010 katika tawi la CRDB Bugando Mwanza, akijua na kwa udanganyifu, alitoa risiti ya benki ya kuchukulia pesa kwa lengo la kuonesha kuwa ilisainiwa na mteja, New Ama Filling Station na akaunti namba 01J1016800800, jambao ambalo si kweli.

Kwa mujibu wa maelezo ya awali ya kesi waliyosomewa washtakiwa hao, wizi huo ulibainika baada ya Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani kumwagiza mkaguzi wa ndani kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika tawi la Nyanza.

Uamuzi huo wa Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Ndani kuamuru kufanyika kwa ukaguzi wa kushtukiza katika tawi hilo ulitokana na taarifa zilizopatikana kuwa kulikuwa na tofauti kubwa ya ulali wa pesa katika tawi hilo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Mei 30 mwaka 2013.

MENEJA BENKI YA ACCESS KORTINI KWA WIZI

Na Happiness Katabazi
MENEJA wa Benki Access, Fadhil Muzo na maofisa wa mikopo wa benki hiyo wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam, wakikabiliwa na makosa ya wizi na uharibifu wa mali zenye thamani ya zaidi ya Sh.milioni 45,246,600.
 
Wakili wa Serikali Hilda Kato mbele ya Hakimu Mkazi Aniseth Wambura alidai kuwa mbali ya Muzo washitakiwa wengine ni  Michael Ntinga,Luka Tumbuka  ambao ni maofisa mikopo na Issack Nchembi ambaye ni dereva na kwamba wote wanakabiliwa na jumla ya makosa matatu.
 
Wakili Kato alilitaja kosa la kwanza kuwa ni la kula njama, kosa la pili ni la wizi  ambalo walilitenda Januari 29 mwaka  huu, katika eneo la Manzese jijini ambao waliiba  bidhaa mbalimbali ikiwemo  kreti za soda 31,katoni moja ya soda, katoni  53 za maji ya uhai, kreti  11 za bia aina ya Serengeti,katoni nne za bia aina ya Tusker, zenye jumla ya thamani ya Sh 45,246,600 mnali ya Rahamat Rashid Mandali.
 
Wakili Kato alilitaja kosa la tatu kuwa ni la uharibu wa mali ambalo walilitenda Januarui 29 mwaka huu, huko Manzese ambapo waliaribu Mlango wa ‘Gril’ wenye thamani y ash 250,000, mlango wa mbao wenye thamani ya Sh.90,000 na vishikizo vya kushikia mlango huo vitu vyote hivyo vina thamani ya Sh. 420,500 mali ya Wilbert  Makishe.
 
Na wakili Kato alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba wanaomba mahakama iwapangie tarehe ya kuja kuwasomea maelezo ya awali.
 
Hata hivyo washitakiwa hao walikana mashitaka na walitimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka kila mshitakiwa asaini bondi ya Sh.milioni nne.
 
Kwa upande wake Hakimu Wambura aliairisha kesi hiyo Juni 24 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya upande wa jamhuri kuwasomea maelezo ya awali washitakiwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Mei 29 mwaka 2013. 
 

FANYENI KAZI KWA MASILAHI YA TAIFA NA SI VINGINEVYO

HAPPINESS KATABAZI NIKIWA NYUMBANI KWETU SINZA LEO ASUBUHI KABLA YA KWENDA KAZINI. (MEI 28/2013)

LWAKATARE AKWAMISHWA TENA


*Korti yuaamuru  Makunga akamatwe

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana iliarisha tena kesi ya kula njama na kutaka kumuua kwa sumu mhariri mtendaji wa Gazeti la Mwananchi Denis Msacky inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph.

Hakimu Mkazi Sundi Fimbo alisema anaiarisha kesi hiyo hadi Juni 10 mwaka huu, kwa ajili ya kuja kutajwa na kusema kuwa hawezi kupanga tarehe za mwanzo  kwasababu hata hakimu anayesikiliza kesi hiyo Alocye Katemana ambaye hivi sasa hayupo kazini, akirejea kwanza atatakiwa apate muda wa kuzipitia hoja kuomba dhamana na kupinga dhamana ya washitakiwa hao ambazo ziliwasilishwa mawakili wa pande zote mbele ya Hakimu Fimbo Mei 13 mwaka huu na akaamuru washitakiwa hao warejeshwe gerezani.

Awali jana kabla   ya Hakimu Fimbo kuairisha kesi hiyo wakili Mwandamizi wa Serikali Prudence Rweyongeza alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo  jana ilikuja kwaajili ya kutajwa.

Hata hivyo kwa upande wake wakili wa washitakiwa Peter Kibatara, Profesa Safari  na Nyaronyo Kichere walieleza kuwa wanafahamu kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kutajwa na kwamba wanaiomba mahakama iwapangie tarehe za karibu.

“Kwa mujibu wa rekodi za mahakama zinaonyesha kesi hii  leo ilikuja kwaajili ya kutajwa na kwamba amesikia ombi la wakili wa utetezi lakini mahakama yake haiwezi kupanga tarehe za karibuni kwasababu hata hakimu Katemana akirejea kazini ,atatakiwa kupata muda wa kuyapitia maombi kuomba dhamana na kupinga dhamana  hivyo anaiarisha hadi Juni 10 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya kutajwa na ninaamuru mshitakiwa arejeshwe gerezani”alisema Hakimu Fimbo.

Baada ya washitakiwa kutolewa ndani ya chumba cha mahakama na kupitishwa katika korido za mahakama chini ya ulinzi mkali wa askari Magereza, baadhi ya wafuasi wa Chadema waliokuwa wamevalia sare za chama hicho hicho walikuwa wakisikika wakisema maneno yafuatayo;

“Hii aikubaliki …huu ni mchezo mchafu  unaofanywa na CCM na mahakama kupiga chenga kumpatia dhamana Lwakatare….Kamanda wetu amesota gerezani muda mrefu sana na leo ni mara ya pili tunakuja hapa mahakamani kesi inaarishwa anashindwa kupewa dhamana eti kwa kisingizo cha hakimu anayesikiliza kesi hiyo hayupo…kwani uongozi wa mahakama hauwezi kumpangia hakimu mwingine akampatia dhamana….na hatutaki Televisheni ya TBC imrekodi wakili wa Lwakatare kwasababu TBC inapendelea Serikali;

‘….Mahakama aitendi haki kabisa na tumemsikia Mwigulu Nchemba akimpigia simu Hakimu Katemana akimwelekeza leo hakimu asije mahakamani kumpatia dhamana Kamanda wetu Lwakatare na hata gazeti la Tanzania Daima la leo (jana), limeandika hilo ebu oneni ….”walisikika wafuasi hao wakisema hayo huku wakionyesha watu wengine gazeti hilo la Tanzania Daima la jana.

Hata hivyo Lwakatare aliwapungia mkono wafuasi hao na kuwaeleza neno moja tu ‘Msichoke kupambana’.

 Machi 20 mwaka huu, Lwakatare na wenzake walifunguliwa rasmi kesi Na.6/2013  ya tuhuma za ugaidi ambapo kosa la pili, tatu, na la nne yalikuwa hayana dhamana na hivyo Mei 8 mwaka huu, Jaji Kaduri aliyafuta makosa hayo kwa maelezo kuwa hajaona kama kuna maelezo ya kutosha ya kuwafungulia mashitaka ya aina hiyo washitakiwa hao. Na hivyo kuwabakizia shitaka moja la kula njama ambalo lina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Wakati huo huo  Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Kisutu Waliarwande Lema ametoa hati ya kukamatwa kwa mshitakiwa wa tatu katika kesi ya kuchapisha makala ya uchochezi,aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendai wa Kampuni ya Mwananchi, Theophil Makunga.

Kesi hiyo inayomkabili aliyekuwa Mahariri mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima, Absalom Kibanda na mwandishi wa makala hiyo ya uchochezi Samson Mwigamba jana ilikuja kwaajili ya kutajwa na Kibanda hakuwepo mahakamani kwasababu yupo nchini Afrika Kusini kwaajili ya matibabu na Mwigamba alikuwepo ila Makunga hakuwepo na hakuwa ametoa taarifa za udhuru mahakamani hapo.

Hali iliyosababisha wakili wa serikali Lilian Itemba kuomba mahakama itoe amri ya kukamatwa kwa Makunga, ambapo Hakimu Lema alitoa amri ya kukamatwa kwa Makunga kwasababu ameshindwa kutokea mahakamani jana bila kutoa taarifa na akaiarisha kesi hiyo hadi Juni 20 mwaka huu,itakapokuja kwaajili ya kutajwa.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Mei 28 mwaka 2013.

TASWIRA YA MKUTANO MKUU WA SACCOS YA POLISI MOROGORO

 
Mwenyekiti wa Bodi  URA SACCOS, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP),  Jonas N. S. Mugendi, aliyesimama, akitoa mada mbele ya wajumbe na wanachama wa Bodi hiyo walipokutana katika mkutano wa tano wa mwaka unaofanyika mkoani Morogoro, Kutoka kushoto Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu Wizara ya Mambo ya Ndani,  Bi. Lilian Lamek, akifuatiwa na Mkuu wa Utawala Wa Jeshi la Polisi,SACP Thobias Andengenye, na wengine kutoka kushoto ni Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, Awadhi Chicco, ambaye sasa amestaafu  na Kamishina  Msadizi (ACP), Alli Omar All.(Picha na Demetrius Njimbwi wa Jeshi la Polisi Morogoro. 






  1. Mkurugenzi wa Rasilimali watu Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi, Bi. Lilian Lamek, akizungumza na Wajumbe na Wanachama  wa Bodi ya URA SACCOS, ambao hawapo pichani wakati akifungua mkutano wa tano wa mwaka unaofanyika mkoani Morogoro.(Picha na Demetrius Njimbwi wa Jeshi la Polisi Morogoro)


     

NAENDELEA KUMLILIA WAKILI STANSLAUS BONIFACE 'JEMBE'






Na Happiness Katabazi
Leo  Mei 27 mwaka  2013, mpendwa wetu  aliyekuwa Wakili Kiongozi wa Serikali mwenye  cheo cha Mkurugenzi  Msaidizi wa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini, Stanslaus Boniface Makulilo (44) ‘Jembe’ afariki ghafla  tarehe kama ya leo katika  Hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam.

Binafsi mimi na wengine wote tunaoheshimu mchango wako wa Taaluma ya sheria uliyokuwa ukiiutoa kwenye mashauri mbalimbali yaliyokuwa yakiendeshwa katika mahakama mbalimbali hapa nchini, na wale mawakili wa serikali uliokuwa ukiwafundisha kazi tunaendelea kukumbuka na kukuenzi.

Na ndiyo maana leo hii mimi binafsi nikiwa Mwandishi wa Habari za Mahakamani na mwanafunzi wa  mwaka wa pili wa fani ya Sheria,ndiyo maana nimechukua muda wangu na  na ndiyo maana hata leo hii nimeweza kuchukua muda wangu na kuketi kitako na kuandika makala hii ya kumbukumbu ya mwaka mmoja ya kifo chako, na kukusimulia ni kesi gani za jinai kubwa zilifunguliwa na Mkurugenzi wa Mashitaka nchini DPP-Dk.Eliezer Feleshi na vijana wako uliowafundisha kazi waliweza kuziendesha kikamilifu na wakafanikiwa kushinda na nyingine wakashindwa na kesi nyingine ulizoziacha nyingine zimeishatolewa hukumu na nyingine bado.

Nianze kwa kukusimulia kesi kubwa kufunguliwa baada yaw ewe kufariki ni kesi ya uhujumu uchumi na madai ya kupokea rushwa inayomkabili Waziri wazamani Idd Simba na wenzake.Kesi hii ilifunguliwa rasmi  siku ambayo wewe Boniface ulikuwa unazikwa pale katika Makaburi ya Kinondoni  na ilikuwa ni Mei 29 mwaka jana, na hadi sasa bado haijaanza kusikilizwa.

Lakini pia Oktoba 18 mwaka jana, Dpp alimfungulia kesi wizi wa malighafi za Sh.milioni 59 na uchochezi Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Shaikh Ponda Issa Ponda na wenzake 49. Na DPP aliwasilisha hati ya kumfungia dhamana Ponda na Mkadamu Abdalah na kweli walisota gerezani hadi kesi hiyo ilipotolewa hukumu Mei 9 mwaka huu, ambapo Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Victoria Nongwa alimpotia hatiani Ponda peke yake kwa kosa moja la kuingia kwa jiani katika kiwanja cha Markazi Chang’ombe na kuwaachiria washitakiwa wengine 49 kwa maelezo kuwa jamhuri imeshindwa kuthibitisha kesi dhidi yao na hivyo Hakimu Nongwa akaamuru Ponda kutumikia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja nje.

Kwa upande wa jamhuri katika kesi hii ulikuwa ukiwakilishwa na wakili mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka ambaye kwasasa ni wazi amekuwa akitajwa tajwa na watu wanaomshuhudia wakati akiendesha mashauri mbalimbali ya jinai, kuwa anafuata nyayo za marehemu Boniface.

Kesi nyingine ni kesi ya wafusi 53 wa Sheikh Ponda ambayo ilikuwa ikiendeshwa kwa Hakimu Mkazi Sundi Fimbo, ambapo  Machi 21 mwaka huu, alitoa hukumu ya kuwafunga mwaka mmoja jela baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya kufanya mkusanyiko haramu na kukaidi amri ya jeshi la polisi iliyowataka watawanyike na wasiandamane kwenda ofisi ya DPP, kumshinika ampatie Ponda dhamana.

 Lakini pia Machi 20 mwaka huu, Jamhuri ilimfungulia kesi ya tuhama za ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph  lakini hata hivyo Lwakatare alikimbilia Mahakama Kuu kuomba mahakama hiyo iitishe jalada la kesi hiyo na ilipitie kuona kama DPP alikuwa sahihi kumfungulia mashitaka Lwakatare ya ugaidi Machi 18 na kisha Machi 20 asubuhi kuyafuta na kisha Machi 20 mchana kumfungulia tena kesi yenye makosa hay ohayo  ambapo Jaji Lawrence Kaduri katika uamuzi wake aliotuoa Mei 8 mwaka huu, alimfutia mashitaka matatu ya ugaidi Lwakatare na kumbakizia kosa moja la kula njama kutaka kumuua kwa sumu Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi Denis Msacky.

Lakini hata hivyo Mei 8 mwaka huu, Jaji Kaduri alitoa uamuzi wa maombi hayo ya Lwakatare ambapo alisema DPP alikuwa sahihi kufuta na kumfulia mashitaka hayo, ila jaji huyo pia akatoa uamuzi wa kumfutia jumla ya makosa matatu ya ugaidi.

Hata hivyo Mei 21 mwaka huu, DPP aliwasilisha ombi lake Mahakama ya Rufani nchini akiomba mahakama hiyo itengue uamuzi huo wa mahakama kuu wa kumfutia Lwakatare  mashitaka ya ugaidi na hadi sasa bado uongozi wa mahakama ya rufaa haujapanga tarehe wala majaji wa kuanza kusikiliza rufaa hiyo.Na kesi ya msingi ya Lwakatare inakuja leo katika mahakama ya Kisutu kwaajili ya kutajwa mbele ya hakimu Mkazi Alocye Katemana.Na tangu Machi 18 mwaka huu hadi leo Lwakatare bado wapo katika gereza la Segerea kwasababu kesi inayowakabili haina dhamana.

Lakini hata hivyo Boniface Mei mwaka huu, Jaji wa Mahakama Kuu, Dk.Faudhi Twaibu alitoa amri ya kutupilia mbali hoja za mawakili wa jamhuri uliokuwa ukiwakilishwa na Oswald Tibabyekomya katika ile rufaa yetu ya kupinga hukumu ya kesi ya madai ya kuomba rushwa iliyokuwa ikimkabili Jerry Murro ambapo upande wa jamhuri ulikuwa ukiomba mahakama hiyo itoe amri ya kesi hiyo ilirudishwe mahakama ya Kisutu ianze upya kwasababu mwenendo wa kesi hiyo hausomeki vizuri, lakini Jaji Twaib alisema anatupilia mbali ombi hilo na kwamba sababu za kufikia uamuzi huo ameziifadhi.
 Pia wakili Boniface Aprili mwaka huu, Jaji Kaduri wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, alikubali rufaa iliyokuwa imekatwa na DPP katika kesi ya kupinga uamuzi wa Hakimu MKazi wa Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu,Waliarwande Lema ambapo ulimuona Kigogo wa Kampuni ya Richmond Naeem Gire hana kesi ya kujibu.

Jaji Kaduri katika hukumu yake hiyo alisema kulikuwa na ushahidi wa kutosha ambao unamfanya Gire apande kizimbani ajitetea na hivyo hakimu Lema alikosea na hivyo jaji huyo akaamuru Gire apande katika mahakama ya Kisutu naanze kujitetea na tayari uongozi wa mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu umeishampangia hakimu Emilius 

Mchauru kuanza kusikiliza utetezi wa Gire Juni 6 mwaka huu.
Lakini hata hivyo tayari Gire ameishawasilisha hati ya kusudio la kukata rufaa katika Mahakama Kuu na kwamba anachosubiri ni uogozi wa mahakama kuu umpatie nakala ya hukumu hiyo ili aweze kuandaa hoja zake na kuziwasilisha katika mahakama ya rufaa ni nchini kupinga hukumu hiyo.

Kuhusu zile jumla ya kesi 11 za wizi katika akaunti za EPA katika Benki Kuu, ambazo wewe na mawakili wenzako mlikuwa mkiziendesha na hadi unakutwa na mauti uliweza kufanikiwa kushuhudia kesi moja ya EPA ya wizi wa sh.bilioni 1.3 iliyokuwa ikimkabili Rajabu Maranda na Farijala Hussein wakihukumiwa kwenda jela miaka mitano, na ulivyofariki pia tayari kuna hukumu za kesi mbili za EPA ambazo zinamhusisha Maranda ,Farijala na maofisa wa BOT watatu zilitolewa hukumu. Hivyo kesi nyingine za EPA zilizosalia bado haizajatolewa hukumu .

Ila zile kesi nne za EPA zinazomkabili mfanyabiashara maarufu Jeetu Patel  zilizofunguliwa Novemba 2008 bado hata shahidi mmoja wa upande wa jamhuri hawajaanza kupanda kizimbani kuanza kutosha ushahidi wake.

Hizo ni simulizi chache za baadhi ya kesi zilizovuta hisia katika jamii na sisi waandishi wa habari kwa kipindi hiki cha mwaka mmoja ambacho wewe haupo nasi duniani.Ila napenda nikuakikishie tu kuwa mawakili wa serikali bado wanatupatia ushirikiano wa kutosha sisi waandishi wa habari za mahakamani kama zamani.

Unakumbukwa na waandishi wa habari za mahakamani wenzangu Furaha Omary, Regina Kumba, Magai James, Tausi Ally, Faustine Kapama, Kulwa Mzee,Grace Gurisha, Frola Mwakasala ,Karama ,Hellen Mwango.

Lakini bado unakumbukwa na mawakili wenzako wa Serikali, Dk.Eliezer Feleshi, Biswalo Mganga, Malangwe Mchungahela, Sedekia Emphere,Fredrick Manyanda,Oswald Tibabyekomya, Lasdslaus Komanya, Tumaini Kweka, Ponsian Lukosi,Ben Lincoln,Arafa Msafiri, Timon Vitalis,Michael Lwena na wengine wengi.Ambao kwa kadri ya uwezo wao wafanya vizuri katika majukumu yao ya ueneshaji wa mashitaka, na wengi niliozungumza nao wanakushukuru kwa mchango wako wa kitaaluma kwani hukuwa mchoyo wa kuwafundisha kazi pale walipoitaji msaada huo.

Miongoni mwa kesi kubwa ambazo mimi binafsi nilimshuhudia  Marehemu Boniface  akiziendesha kwa zaidi ya miaka mitano katika mahakama mbalimbali hapa nchini sasa ni kesi ya wizi wa shilingi bilioni 1.8 katika EPA, iliyokuwa ikimkabili Kada wa CCM, Rajabu Maranda na Farijala Hussein ambapo mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mei 23 mwaka juzi, iliwahukumu kwenda jela miaka mitano, kesi ya kula njama na kuomba rushwa ya shilingi milioni 10 iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la TBC, Jerry Murro na wenzake ambapo Murro alishinda kesi hiyo mwaka juzi.

Kesi  ya Kikatiba iliyofunguliwa na mfanyabishara Jayankumar Patel “Jeetu Patel’ na wenzake dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, DPP na Reginal Mengi iliyokuwa akitaka afutiwe kesi zake nne za EPA zilizopo katika mahakama ya Kisutu kwasababu Mengi alimuhukumu kabla ya hajahukumiwa na mahakama kwa sababu alimuita ni Fisadi Papa, ambapo Boniface alimwakilisha AG na DPP na aliibuka mshindi katika kesi hiyo.

 Kesi nyingine kubwa ambayo marehemu alikuwa akiziendesha ambazo bado hadi umauti unamkuta hazijatolewa hukumu ni ile ya mauji ya Ubungo Mataa ambayo inaendelewa kusikilizwa na Jaji Projestus Rugazia, rufaa ya kupinga hukumu ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyomwona mfanyabiashara Naeem Gile ambayo inasikilizwa mbele ya Jaji Laurence Kaduri ambaye alikuwa akikabiliwa na makosa ya kutoa taarifa za uongo kuhusu kampuni ya kufua umeme ya Richmond LCC, kuwa hana kesi ya kujibu, rufaa ya kupinga hukumu ya mahakama ya Kisutu iliyomuona Jerry Murro hana hatia na kesi ya matumizi mabaya na kuisababishia serikali hasara ya shilingi bilioni 11.7 inayomkabili waliokuwa mawaziri wa Fedha na Nishati, Basil Mramba, Daniel Yona na Gray Mgonja ambapo kesi hii hivi sasa imefikia hatua ya Mramba kuendelea kujitetea

Boniface alizaliwa Februali 21 mwaka 1968 ameacha mke na watoto watatu, aliitimu shahaha ya kwanza ya Sheria mwaka 1995 na shahada ya pili ya sheria alimaliza mwaka 2008 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Julai Mosi mwaka 1995 aliajiriwa rasmi katika ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa serikali kama Wakili wa Serikali, ilipofika Oktoba Mosi mwaka 2006 alipandishwa cheo na kuwa Wakili wa Serikali Mwandamizi.Oktoba Mosi mwaka 2007 alipandishwa cheo tena na kuwa Wakili Kiongozi wa Serikali. 

Nyadhifa ambazo Boniface aliwahi kuzishika enzi za uhai wake ni kati ya mwaka 2003-2007 alikuwa ni Wakili wa Serikali Mfawidhi Mkoa wa Mbeya.Kati ya Mei 2007 na Oktoba 2010 alikuwa Wakili wa Serikali Mfawidhi Kanda ya Mwanza.Novemba 2009 hadi Novemba 2010 alikuwa Mwanasheria Mfawidhi wa Serikali mkoani Dar es Salaam. Kutokana na utendaji kazi wake mzuri ilipofika Desemba 2010 hadi mauti yanamkuta aliteuliwa kushika wadhifa wa Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha uendesha mashitaka na pia awaka Msimamizi wa uendeshaji kesi zenye maslahi kwa umma. Bwana alitoa na bwana ametwaa jina lake liimidiwe.

Leo umetimiza mwaka mmoja tangu Boniface ufariki dunia, naendelea kukulia.

Chanzo:www.katabazihappy.blogspot.com
Facebook:happy katabazi  ; Jumatatu,  Mei 27 mwaka 2013
0716 774494

HEKO JWTZ,POLISI KUDHIBITI VURUGU MTWARA





Na Happiness Katabazi

BILA woga wala kumung’unya maneno  napenda kutoa  pongezi  zangu za dhati kwa vyombo vya ulinzi na usalama yaani Jeshi la Ulinzi la Watanzania (JWTZ), chini ya  Jenerali Davis Mwamunyange, Jeshi la Polisi na chini ya Inspekta Jenerali(IGP), Said Mwema na serikali kwa ujumla wake kwa kuweza kuwadhibiti wale wahuni  ambao ni baadhi ya wakazi wa Mtwara ambapo kwa makusudi wiki hii waliamua kuanzisha vurugu kubwa mkoani hapo kwa kisingizio kuwa hawataki bomba la gesi lisije Dar es Salaam.

Maana bila vyombo hivyo kuingia kazini ni wazi machafuko makubwa yangeendelea kutokea na kusababisha  madhara makubwa mkoani hapo.Tena napenda kuvitia moyo vyombo hivyo kuwa viendelee kutimiza wajibu wake bila kuwaonea haya wahuni ambao wana kila dalili za kutumiwa na watu wenye hulka za kinyang’au kwa maslahi yao binafsi ili mwisho wa siku waone Taifa letu nalo likitumbukia katika vita, jambo ambalo wahuni hao ambao wamekamatwa na hao manyang’au wanaowatuma kufanya hivyo hawatafanikiwa.

Hivyo basi vyombo hivyo vya dola vilikuwa sahihi kabisa katika kufanya oparesheni yake kule Mtwara  hadi vimefanikiwa kumaliza ghasia hizo na washiriki wa ghasia hizo wameweza kukamatwa na hivi kinachosubiriwa ni ofisi ya Mkurugunzi wa Mshitaka(DPP),Dk.Eliezer Feleshi na waendesha mashitaka wake kuwafungulia kesi wale wote waliokamatwa wakishiriki uhalifu huo.  

Tanzania itaendelea kuwa ni nchi ya mshikamano na amani yake ni mfano wa kuigwa ulimwenguni licha ya hivi sasa kumeanza kuibuka baadhi ya matukio yasiyopendeza yanayoashiria uvunjifu wa amani lakini,kwakuwa vyombo vya unzi na usalama vipo imara wahusika wanakamatwa na kisha kufikishwa mahakamani na kwa wale wafuasi 53 wa Sheikh Issa Ponda , Machi 21 mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi iliwafunga jela mwaka mmoja baada ya kuwakuta na hatia ya kufanya mkusanyiko haramu, kukaidi amri ya jeshi la polisi.

Na Mei 9 mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu pia ilimhukumu kifungo cha mwaka mmoja nje ,Sheikh Ponda baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kuingia kwa jinai katika kiwanja cha Chang’ombe Markas.

Sasa na nyie wahuni wa Mtwara mnaofanya vurugu mjifunze katika hukumu hizo mbili wale vihelehele waliokuwa wakiandamana wakitaka kwenda kwa ofisini kwa DPP-Dk.Feleshi ili wamshinikize aondoe hati yake ya kumfungia dhamana Ponda, walikamatwa na kufikishwa mahakamani na wakafungwa gerezani mwaka mmoja na hivi sasa wamesambazwa katika magereza kadhaa hapa nchini, na huyo Ponda waliyokuwa wakimpigania yeye kafungwa kifungo cha nje.

Sasa na nyie wahalifu mliofanya uhalifu Mtwara nawasii sana mjifunze kutokana na hukumu hizo, kuwa kama kuna mtu anawatuma kufanya uhalifu huo basi mkae mkijua mtu huyo anawatoa kafara nyie kwani mtaoshughulikiwa moja kwa moja ni nyie na mtakaopata madhara makubwa ya kisheria ni nyie.

Na vurugu za madai ya kidini katika mkoa wa Dar es Salaam, baada wahusika kukamatwa na kufikishwa mahakamani, zimetulia, Dar es Salaam, hivi sasa ipo shwari na  nchi inazidi kusonga mbele.Hivyo kule Mtwara napo mamlaka husika inatakiwa itumie sheria kuwashikisha adabu wavunjivu wote wa sheria.

Wiki hii Tanzania ilijikuta ikiandika historia mbaya katika sura ya dunia kwasababu ya ghasia kubwa zilizotokea mkoani Mtwara na kusababisha mtu mmoja kupoteza maisha na wengine,kujeruhiwa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo makazi yao na sehemu zao za kufanyia biashara kuaribiwa.

Chanzo cha vurugu hizo zinaelezwa kuwa baadhi ya wakazi wa eneo hilo la Kigoma Mjini kumaliza kusikiliza hotuba ya Wizara ya Nishati na Madini iliyowasilishwa na waziri wa wizara hiyo Profesa Sospitha Muhongo.

Na baadhi ya wakazi wa Mtwara wamekuwa wakikataa gesi iliyogundulika Mtwara, isiletwe Dar es Salaam.
Itakumbukwa kuwa Januari mwaka huu, wananchi wa Mtwara walipozusha ghasia ,niliandika makala na niliiweka kwenye ukurasa wangu wa facebook ambayo dhima ya makala yangu ilikuwa ikimshauri Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP),Dk.Eliezer Feleshi awafikishe mahakamani wale wote walioshiriki kwenye vurugu za Januari mwaka huu huko Mtwara kwa kisingizo wanazuia bomba la Gesi lisijengwe kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam.

Kuna usemi usemao ‘Vita haina macho’.Sasa vurugu zile zilizotokea wiki hii Mtwara naweza kuzifananisha na vita baaida ya wananchi hao ambao kwa makusudi waliamua kujichukulia sheria mkononi na kuanza kufanya uhalifu na kujibishana jeshi la polisi kwa kisingizio kuwa bomba la gesi lisijengwe kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam.
Na matokeo ya kitendo hicho cha kujichukulia sheria mkono kilichofanywa na baadhi ya wananchi wa Mtwara ndicho mwisho wa siku kilichopelekea Jeshi la Polisi kuingia kazini kama  kifungu cha 20, 21(2) vya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 inavyoanisha wazi majukumu ya jeshi hilo.

Ambapo kifungu cha 20 kinampa polisi mamlaka wakati akifanya jukumu lake la ukamataji wa mwarifu/waharifu kuvunja eneo lolote na kuingia kumkamata mwarifu huyo kwa lengo la ku.Wakati kifungu cha 21(1) kinamruhusu ofisa wa polisi kutumia nguvu wakati akikamata waharifu.

Kwa mtiririko huo ndiyo maana nimelazimika kutumia msemo huo kuwa ‘Vita haina macho’ kwani vurugu za Mtwara zilipoanza kufanywa na baadhi ya wakazi wa Mtwara  ambao nao wahuni hao walikuwa na silaha za jadi mkononi zilisababisha Jeshi la Polisi kuingia kazini na kuanza kuwashughulikia wale wote waliokuwa wakifanya vurugu  hizo na mwisho wa siku hata wale ambao hakushiriki katika vurugu hizo kwa njia moja ama nyingine wameathiriwa na vurugu hizo na wengine wakijikuta wamepoteza mahali pa kuishi.

Lakini Binafsi nimekuwa nijikijiuliza kuwa mbona kila kukicha tunasikia kwenye vyombo vya habari vikitoa nafasi kubwa ya kusikika habari za wale wahuni wanaofanya vurugu Mtwara lakini hatuoni vyombo hivyo vya habari vikitoa nafasi kwa wakazi wengine wa Mtwara ambao hawawaungi mkono wahuni hao?

Je ina maana ni wakazi wote wa Mtwara wanataka bomba la gesi lisijengwe kuja Dar es Salaam kwa niia ya vurugu kama zile? Kule Mtwara kuna waandishi wenzetu lakini mbona hatusikii waandishi wenzetu hao wakienda kuwahoji wakazi wa Mtwara ambao wanapingana na wenzao kwa kuwasilisha madai yao kwa njia ya vurugu?

Wakati umefika sasa kwa waandishi wenzetu wa Mtwara kutuletea habari toka kwa wananchi wengine ambao hawaungi mkono kudai dai hilo kwa njia ya vurugu.Kwani kwa kushindwa kufanya hivyo,jamii italazimika kuamini wakazi wote wa Mtwara nao wanaunga mkono wahalifu hao.

Maana binafsi sikubaliani kuwa ni wakazi wote wa Mtwara wanawaunga mkono wenzao wale wanaodai kiwanda cha gesi kijengwe Mtwara kwa njia ya vurugu.  

Sote tunafahamu kuwa Tanzania ni nchi inayoongozwa kwa kufuata utawala wa sheria, na inamruhusu mtu yoyote yule ambaye anaona haki yake imeporwa au kuvunjwa aende mahakamani kuidai.

Sasa hawa waliofanya vurugu Mtwara walikuwa wanapaswa kwenda kudai dai hilo kwa njia ya amani na kama wangeshindwa wangechangisha fedha wakamweka wakili ,akafungua kesi ya madai ya kupinga bomba hilo lisijengwe kuja Dar es Salaam, kwaniaba yao,kuliko uhuni walioufanya.

Licha kuna watu wamekuwa wakidai kuwa wananchi hao hawajapewa elimu ya kutosha, mi binafsi sikubaliani na hilo kwani elimu imetolewa ila tu hawa waliofanya vurugu tayari wana ajenda yao mbaya mioyoni na akili mwao.

Kwani hata kama hoja ni kwamba hawajapewa elimu ya kutosha, ni kwanini siku Waziri wa Nishati Profesa Mhongo alipomaliza kusoma bajeti yake,wakaanzisha vurugu?Tena kama ya bajeti kusomwa siku mbili nyuma walisambaza vipeperushi vya kufanya vurugu siku hiyo.

Tuwaulize wahalifu wale hivi siku hiyo Waziri Mhongo aliingia mkataba na wahalifu wale wa kuwapatia elimu ya gesi akiwa bungeni wahalifu wale ?

Tunachokifahamu sisi waziri huyo alikuwa akienda kusoma bajeti ya wizara inayohusu nchi nzima siyo wakazi wa Mtwara.Kwahiyo nasisitiza kuwa wale waliofanya vurugu Mtwara ni wahuni na ni wahalifu kama walivyowahalifu wengine, na sheria za nchi zipo ,na ziwashughulikie kikamilifu ili wasiweze kurudia kufanya uhalifu huo ambao umesababisha watu kupoteza maisha, makazi ya watu kuaribiwa.

Nafahamu watu watailamu jeshi la polisi ,lakini tunapaswa tujiulize kwanza hivi kama wale wahalifu wasingezusha vurugu siku ile, jeshi la polisi na JWTZ lingeingia mtaani kukabiliana na wahalifu wale?Jibu ni jepesi tu ,JWTZ na Polisi wasingepoteza muda na nguvu zao kuingia mtaani mjini Mtwara na kupambana na wahalifu wale ambao tayari wameishaipaka matope nchi.

Kwa kitendo kile walivyokifanya ,hata kama walichokuwa wakikidai ni sahihi, wakae wakijua wamevunja sheria za nchi, na watafikishwa mahakamani kwa makosa ambayo yatakuwa yameandaliwa na waendesha mashitaka wetu na hapo ndipo itakapokuwa imeanza safari yao ya utumwa baina ya wahalifu hao  na Mahakama na mahabusu.

Kwa watu wanaofikiri sawa sawa ,inawawia vigumu kuamini hawa wananchi ni wao wenyewe ndiyo wanaojituma kufanya uhalifu huo ule kwa kisingizio cha dai hilo.

Kwani hawa wananchi kwa muda mrefu walikuwa wakilalamika kucheleweshea malipo yao ya mauzo ya Korosho lakini hata siku moja hatujawahi kuwaona wakifanya uhalifu wa haina ile.

Na kama kweli dai lao ni hilo ni la kukataa bomba la gesi lisije Dar es Salaam, dai ambalo na fahamu haliwezi kutekelezekwa kwasababu ni dai lisilo na tija ,ni kwanini wahalifu hao wakimbilie kuchoma nyumba za viongozi ,mahakama, ofisi za CCM,na nyumba ya Mwandishi wa Habari ?

Naviomba vyombo vya dola ikiwemo Polisi, JWTZ na Idara ya Usalama wa Taifa, ifanye kazi yake ya uchunguzi ili kujua kama kweli wahalifu hao wanadai hilo kweli? Nani anawapa jeuri na morali wahalifu  hao kufanya uhalifu ule bila woga tena kwa njia haramu?

Huenda kuna kikundi cha wadhalimu kipo nyuma ya hawa wahalifu kina watuhumia wahalifu hawa kufanya uhalifu huo kwa kisingizio cha kukataa bomba hilo lisije Dar es Salaam,wakati wakifahamu wazi hao wahalifu wanachokikataza hawana mamlaka nacho.

Naamini dola likiamua kufanyakazi yake kikamilifu huko Mtwara,inauwezo wa kubaini kilichopo nyuma ya pazia ya chanzo cha vurugu hizo na itawadhibiti na dai hilo litakuwa ndoto kwa wahalifu hao.

Kwani mifano ya dola kusambaratisha vikundi vya wahalifu hao hao ni mingi sana na wala si yakutafuta.Mfano vyombo vya ulinzi na usalama vilivyofanikiwa kuwasambaratisha wale baadhi ya waumini wa dini ya Kiislamu Mkoani Dar es Salaam, mwaka jana na Machi mwaka huu ,waliokuwa wakiendesha maandamano haramu kwa kisingizio cha kutetea uislamu, kutokomeza ujambazi katika mikoa ya Kigoma, Kagera na Arusha, vurugu za Msikiti wa  Mwembe Chai, ujambazi wa kutisha katikati ya jiji la Dar es Salaam, kati ya miaka ya 2006 muda mfupi tu tangu Rais Jakaya Kikwete Desemba 21 mwaka 2005, alipoapishwa kushika madaraka ya urais.

Narudia tena bado ninaimani kubwa na vyombo vya ulinzi na usalama kuwa vikiamua kufanya kazi vinafanyakazi yake kikamilifu na ndiyo maana hata leo hii nimejitokeza kuvipongeza kwa kuweza kurejesha amani mkoani Mtwara ambayo ilitoweka kwa siku mbili kwaajili ya vurugu baina ya wahalifu wale na vyombo vya dola.

Niitimishe makala yangu kwa kuvipongeza vyombo kwa kufanya oparesheni hiyo ambayo imezaa matunda na kukata ngebe za hao wahalifu ambao ambao kama ya kupata mkong’oto wa wana usalama walijitapa kuwa wapo tayari kufa kwaajili ya kuipigania gesi.

Lakini cha kushangaza wahalifu hao waliokuwa wakijitapa kuwa hawaogopi dola, leo hii wamefya mkia kwa kuhofia oparesheni hiyo.

Nimejiuliza kuwa hivi mpiganaji gani ambaye ameapa kufa kwaaiili ya kuipigania gesi asalimu amri baada ya polisi kuwatembezea mkong’oto?

Shujaa au mpiganaji yoyote huwa aogopi polisi wala bunduki.Sasa iweje hawa waliojitapa kutoliogopa dola na kuamua kujichukulia sheria mkononi leo hii wameona JWTZ na Polisi wamekalia kooni wameshusha silaha chini? Ni wazi hawa ni watu waoga kwani kama siyo waoga wangejitokeza kupambana na askari hao ili tuwajue kuwa nao ni mahodari na wapo tayari kwa lolote.

Tanzania ni nchi inayooendelea hivyo binafsi sioni kama ni muda mwafaka kwa sisi wananchi hususasini wakazi wa Mtwara kuanza kujiingiza kwenye vurugu badala ya kushiriki kwenye shughuli za kujiletea maendeleo na taifa letu.

Wanahabari na wananchi wengine wote wapenda amani na tunaoheshimu utawala wa tuukatae uhuni unaofanywa na wahalifu wale wanaofanya vitendo vya uvunjifu wa amani kwa kisingizio cha kuzuia bomba la gesi lisijengwe kuja Dar es Salaam,kwani una hatarisha amani na wanaoteseka ni watoto na wanawake na miundombinu yetu inaaribika ambayo imejengwa kwa kodi zetu.

Pia napenda kutoa raia kwa wale wananchi wote ambao wamechoka kuishi hapa Tanzania katika nchi yenye amani, basi ni wakati mwafaka kwa watu hao wapenda vurugu kwenye kuamia katika nchi zenye vita ili wakaishi huko kwenye nchi zenye vita wafurahi zaidi ,kuliko kuishi hapa nchi na kuanza kutuletea vurugu ambazo zinahatarisha amani yetu ambazo sisi wengine hatutaki vita jamani.

Mwisho nimalizie kwa kuvipongeza vyombo ya dola yaani Polisi na JWTZ kwa kuweza kuwadhibiti wahalifu wale walioleta vurugu kule Mtwara.Na itafute chanzo cha vurugu hizo kwani hii ni mara ya pili sasa wahuni wale wanazusha vuru hizo kwa kisingizo hicho na mara ya kwanza vurugu ambazo zilisababisha pia watu kupoteza maisha ni Januari mwaka huu.

Mungu ibariki Tanzania,Mungu Ibariki Afrika
Chanzo: www.katabazihappy.blogspot.com
Facebook:happy katabazi  , Mei 26 mwaka 2013.
  
0716 774494



RAMA 'MLA KICHWA' HURU




Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemwachiria huru mtoto  Ramadhamani Selemani Mussa, maarufu kama ‘Rama mla kichwa’,na mama yake mzazi Hadija Ally waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauji.

Rama na mama yake walikuwa wakikabiliwa na kosa la kuua kwa kukusudia mtoto Salome Yohana (3), kinyume na kifungu cha 196 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ya mwaka 2002.

Amri ya kuachiliwa huru kwa Mussa na mama yake ilitolewa jana na jaji Rose Temba ,ambaye alisema mahakama yake imefikia uamuzi huo baada ya kuridhishwa na  ripoti ya jopo la madaktari waliomfanyia uchunguzi wa Akili zake Mussa, iliyoeleza kuwa wakati wa tukio hilo hakuwa na akili timamu.

“Kwa sababu hiyo mahakama hii inamuachiria huru Mussa kwasababu ripoti ya madaktari imethibitisha kuwa wakati Mussa anatenda kosa hilo la kukutwa na kichwa cha binadamu hakuwa na akili timamu.Na pia mahakama hiyo inamuachiria huru mama yake Rama kwasababu Mkurugenzi wa Mashitaka amewasilisha taarifa yake ya kuwa hana nia tena ya kuendelea kumshitakiwa mama huyo chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai”alisema Jaji Temba.



Baada ya jaji huyo kutoa uamuzi huo wa kuwaachilia huru washitakiwa hao, ghafla uamuzi huo ulisababisha mama wa mtoto aliyeuwawa na kichwa cha marehemu kukutwa anacho Mussa, Upendo Dustani na shangazi wa mtoto huyo, Furaha Mussa, aliyekuwa akiishi na mtoto huyo nyumbani kwake Tabata kuangua kilio.

Septemba 29, 2011, Mahakama Kuu iliamuru Rama apelekwe katika hospitali ya magonjwa ya akili ili apimwe akili kama alikuwa na akili timamu au la, wakati wa tukio hilo.

Amri hiyo ya Mahakama iliyotolewa na Jaji Samuel Karua, ilitokana na maombi yaliyotolewa na Wakili Yusuph Shehe aliyekuwa akiwatetea

Wakili Shehe alidai amefikia uamuzi wa kuwasilisha mahakani hapo ombi hilo kwasababu anataka mahakama ijiridhishe kuwa Mussa alikuwa ana akili timamu kabla ya kuanza usikilizwaji wa kesi hiyo ya mauji Na.26/2010 kulingana na kumbukumbu za maelezo ya ushahidi ulioko mahakamani.

Jana, kabla ya washtakiwa hao kuachiwa, Wakili wa Serikali, Secy Mkonongo aliyekuwa akisaidiana na Clara Charles, alidai kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya usikilizwaji wa awali, kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao.
Hata hivyo Wakili Shehe alidai kuwa mara ya mwisho Mahakama hiyo iliamuru mshtakiwa wa kwanza, Rama, apelekwe katika hopsitali ya magonjwa ya akili kwa ajili ya uchunguzi wa akili zake.
Wakili Shehe alidai kuwa  ripoti hiyo tayari imeshawasilishwa mahakamani hapo kutoka Taasisi ya Magonjwa ya Akili ya  Isanga tangu Juni 20, 2012, ikiwa imesainiwa na Dk Mndeme Eramus na kwamba inaeleza kwa mshtakiwa wakati akitenda kosa hilo hakuwa na akili timamu.
Kutokana na ripoti hiyo, Wakili Shehe aliiomba mahakama hiyo  ijielekeze katika vifungu cha 220 (4) na 219 (2) vya CPA na kumfutia mashtaka mshtakiwa huyo

Kwa upande wake wakili wa  Serikali Mkonongo alidai kuwa upande wa jamhuri hauna pingamizi na hoja hiyo ya wakili wa washitakiwa.


Jaji Temba alisema kuwa kwa mujibu wa ushahidi ulitolewa mahakamani hapo,mahakama yake inaamini mshitakiwa wa kwanza alitenda kosa la mauji  licha mahakama yake inamuachiria huru mshitakiwa huyo kwasababu ripoti ya daktari imethibitisha kuwa Mussa wakati akitenda kosa hilo alikuwa hana akili timamu.

Jaji Temba alisema kutokana na ripoti ya daktari ambayo imesema wazi Mussa wakati akitenda kosa hilo hakuwa na akili timamu , chini ya kifungu cha 219 (2) CPA, Sura ya 20 kama kilivyorekebishwa mwaka 2002,  mahakama haiwezi kumtia hatiani kwa kosa hilo na badala yake ina muachiria huru.

“Licha mahakama hii inamuachiria huru Mussa kwa kigezo hicho cha ripoti ya daktari ,mahakama hii inatoa amri ya Mussa aendelee kubakia  chini ya uchunguzi wa Watalamu wa magonjwa ya akili na hospitali itakuwa ikitoa taarifa kwa Waziri wa Sheria na Katiba.”, alisema Jaji Temba.

Ramadhan alikamatwa na mlinzi wa Hospiltali ya Muhimbili Furgence Michael akiwa na kichwa cha mtoto huyo kikiwa kimesukwa nywele, April 26, 2008, akidai kuwa alikuwa anampelekea zawadi muuguzi mmoja wa hospitali hiyo.

Kichwa hicho kilikuwa ndani ya mfuko wa nailoni aina ya Rambo huku akikitafuna hadharani huku akidai kuwa alikuwa amezoea kula nyama za watu yeye na bibi yake.
Hata hivyo walimweka chini ya ulinzi mkali, na kutoa taarifa polisi ambapo baada ya polisi kufika walimuhoji akadai kuwa alikuja na bibi yake anayeishi makaburi ya Jeti Lumo na kwa bahati mbaya wamemuacha na wao wamepaa na ungo.
Kabla ya mwili na kichwa chake kupatikana mahali tofautotofauti mtoto Salome alipotea muda wa saa 2 usiku April 25 akiwa nyumbani kwa shangazi yake Furaha Majani (28), anayeishi Segerea kwa Bibi.
Mtoto huyo alifika kwa shangazi yake hapo akiwa na wazazi wake, baba yake Yohana Majani na mama yake Upendo Datsun, wakazi wa Kimara, kwa ajili ya kumtembelea shangazi yake huyo.
Baada ya kubaini kuwa mtoto huyo alikuwa amepotea katika mazingira ya kutatanisha walitoa taarifa kituo cha polisi baada ya kumtafuta kwa ndugu na jamaa bila mafanikio.
Baadaye kiwiliwili cha mtoto huyo kiliokotwa ndani ya shimo la choo cha washtakiwa kikiwa kimekatwa kichwa na wazazi walitambua kuwa ni kiwiliwili cha mtoto wao.
Alidai kuwa baadaye walipata taarifa za Ramadhani kukamatwa Muhimbili akiwa na kichwa cha mtoto, wazazi hao walifika hospitalini hapo  na walikitambua kichwa hicho kuwa ni cha mtoto wao.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Mei 25 mwaka 2013.