POLISI KORTINI KWA PEMBE ZA NDOVU


Na Happiness Katabazi

ALIYEKUWA askari wa Jeshi la Polisi   mwenye namba EX G5226 PC Ramadhani Selemani (27) wa Ukonga Polisi na wenzake jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akikabiliwa na kosa la kukutwa na pembe za ndovu zenye thamani ya Sh.21 mali ya serikali.

Wakili wa Serikali Mwanaisha Kombo mbele ya Hakimu Mkazi  Nyigulila Mwaseba alimtaja mshitakiwa mwingine kuwa  ni Hamis  Mwanga(22) mkazi wa Mbadala Zakhiem.

Wakili Kombo alidai kuwa  Julai 19 mwaka huu,  washitakiwa hao walikamatwa wakiwa  Pembe nne za Ndovu, na vipande 12 za pembe za ndovu  huko eneo la Tazara Dar es Salaam, nyara zote hizo zikiwa na thamani ya Sh.Milioni 21 mali ya serikali na kwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Hata hivyo Hakimu Mwaseba aliwataka washitakiwa wasijibu chochote kwasababu  mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na hivyo akaiarisha kesi hiyo Agosti 7 mwaka huu kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya kutajwa na akaamuru washitakiwa warejeshwe rumande.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Julai 25 mwaka 2013.

WANNNE WAONGEZWA KESI YA CHE MUNDUGWAO






Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Wahudumu wa wawili wa Idara ya Uhamiaji jana walifikishwa kalifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, nakuunganishwa katika kesi ya wizi wa Paspoti 26 inayomkabili Mwanamuziki wa muziki wa Asili nchini, Chingwele Che Mundugwao na wenzake  ambapo hadi kufikia jana kesi hiyo imefanya kuwa na jumla ya washitakiwa tisa akiwemo raia mmoja wa Uingereza.

Wakili wa Serikali Lasdsalaus Komanya mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo 
alidai kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kujatwa lakini,pia upande wa jamhuri imekusudia kufanya mabadiliko ya hati ya mashitaka ambapo jana imeweza kuwaunganisha washitakiwa wawili wapya ambao ni wahudumu wa Idara ya uhamiaji Adam Athuman na Abdallah Salehe  na washitakiwa wengine wawili ambao walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Julai 18 mwaka huu ambao ni  Rajab Momba na Haji Mshamu katika kesi hiyo ya Che Mundugwao ambao inawashitakiwa watano na hivyo kufanya sasa kuwa na jumla ya washitakiwa tisa.

Washitakiwa wengine ni Che Mundugwao, Raia wa Uingereza Ahsan Iqbal au Ali Patel, Ofisa  Ugavi wa  Idara ya Uhamiaji Shemweta Kiluwasha, Injinia Keneth Pius wa Kikosi  cha Zimamoto na Uokoaji na mfanyabiashara Ally Jabir.


Hata hivyo washitakiwa hao walikanusha mashitaka hayo na kudai kuwa upelelezi bado haujakamilika na hivyo hakimu Fimbo aliarisha kesi hiyo hadi Agosti 5 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa na akaamuru washitakiwa hao warejeshwe rumande kwasababu bado Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi hajaondoa hati yake ya kuwafungia dhamana mahakamani.


Akiwasomea mashitaka wakili Komanya alidai kuwa tarehe isiyofahamika washitakiwa walikula njama ya kutenda kosa. Aidha tarehe tofauti Dar es Salaam, Momba aliiba hati ya kusafiria yenye namba AB 651926 mali ya serikali.

Alidai washitakiwa hao wa nne na wanadaiwa tarehe isiyofahamika Dar es Salaam, walighushi hati ya kusafiria yenye namba hiyo, kuonesha ni halali na imetolewa na Idara ya Uhamiaji ya Tanzania jambo ambalo si kweli.

Juni 3 mwaka huu, Chemundugwao na wenzake walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo wakikabiliwa na makosa mbalimbali yakiwemo kosa la wizi wa paspoti 26, ambapo hata hivyo DPP aliwasilisha hati ya kuwafungia dhamana ambapo hadi sasa wapo gerezani.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Julai 25 mwaka 2013.

MAHAKAMA KUENDELEA KUBORESHA MAHAKAMA ZAKE




 Na Mary Gwera, Bukoba

JAJI Mkuu  Mohamed Chande Othman  amesema mahakama  imedhamiria kuboresha miundombinu ya majengo ya Mhimili huo,ili huduma inayotolewa na mhimili huo iwe inatolewa katika mazingira mazuri na yenye hadhi.

Akizungumza na  katika uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo iliyopo katika Kijiji cha  Karabagaine, Mjini Bukoba mkoani Kagera juzi, Jaji Othman uu aliainisha kuwa moja kati ya vipaumbele vya Mahakama ni kuwafikia wananchi wa kila Mkoa katika kuhakikisha kuwa huduma za Kimahakama hususani  za Mahakama za Mwanzo  zinasogezwa karibu na wananchi.

"Moja kati ya ngazi za Mahakama zinazoongoza kwa kupokea kesi kwa wingi ni ngazi ya Mahakama za Mwanzo, hivyo kuna haja kubwa ya kuboresha miundombinu pamoja na huduma za utoaji haki katika Mahakama hizi," alisema.

Katika hatua nyingine, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa uzinduzi wa jengo hilo la Mahakama ya Mwanzo ni moja ya Mahakama ambazo zitazinduliwa katika mkoa huo wiki ambapo pia jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Bukoba linatarajiwa kuzinduliwa leo asubuhi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.

"Mahakama ya Tanzania, tumedhamiria kuleta sura mpya ya Mahakama za Mwanzo, na sura hii iendane na dhamira yetu ya utoaji 'Haki sawa kwa wote na kwa wakati' hivyo basi nawasihi Viongozi na watumishi wa Mahakama hii usiishie katika muonekano mzuri wa jengo bali jengo hili liende sambasamba na kasi ya utoaji haki katika eneo hili," alilisitiza.

Kwa upande wake  Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Gad Mjemmas alisema upatikanaji wa jengo hilo la Mahakama ya Mahakama ya Mwanzo Karabagaine kutarahisisha upatikanaji wa huduma ya utoaji haki kwa wananchi waliopo katika kijiji hicho.

Jaji Mjemmas aliongeza kuwa Ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo Karabagaine umegharimu ujumla ya Sh.Milioni 138, zote zikiwa ni fedha za ndani za Mahakama ya Tanzania, na jengo hilo litahudumia wananchi wa Kijiji cha Karabagaine na vijiji vya jirani.

Mbali ya kuboresha miundombinu ya Majengo ya Mahakama, zipo hatua nyingine kadhaa zinazochukuliwa na Mahakama ikiwemo Upatikanaji wa takwimu sahihi wa kesi za muda mrefu, Utunzaji sahihi wa kumbukumbu ambao unaenda sambasamba na uboreshaji wa Masjala za Mahakama hii yote ni katika kuhakikisha kuwa huduma ya utoaji inaboreshwa.


Chanzo:Gazeti la Tanzania la Alhamisi, Julai 25 mwaka 2013.

LWAKATARE KWENDA NJE KUTIBIWA


 Na Happiness Katabazi
 
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana imempatia ruhusa  Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare anayekabiliwa na kesi ya kula njama na kutaka kumdhuru kwa sumu Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi,Denis Msacky ya kwenda nje ya nchi kutibiwa.
 
Sambamba na hilo,Hakimu Mkazi Alocye Katemana alitoa  onyo kwa mshitakiwa wa pili katika kesi hiyo Ludovick Joseph  asiendelee kuiongelea kesi hiyo nje ya mahakama kwa kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwani kesi hiyo inaendelea mahakamani hapo  na endapo atakaidi onyo hilo mahakama hiyo italazimika kumfutia dhamana.
 
Wakili wa Lwakatare,Nyaronyo Kicheere aliikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kutajwa na kwamba wanaiomba mahakama  impatie ruhusu mteja wake aende nje ya nchi kutibiwa kwani anasumbuliwa na matatizo ya mgongo na uthibitisho wa kuonyesha Lwakatare anaumwa alitoa nyaraka za matibabu zilizotolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili ambayo inaonyesha Lwakatare ni mgonjwa na ana matatizo ya mgongo.
 
Aidha wakili Kicheree  wanaulaumu upande wa jamhuri kwa kukaa kimya  bila kulalamika wakati kesi ambayo bado haijaisha mahakamani kuandikwa magazetini, akimtuhumua Ludovick kuwa yeye ndiye aliyefanya hivyo.
 
Baada ya kuwasilisha madai hayo , mahakama ilitoa kibali cha Lwakatare kwenda kutibiwa nje, ambapo leo (jana) hakuwepo mahakamani na pia ilitoa onyo kwa Ludovick.Hakimu Katemana aliarisha kesi hiyo hadi  Agosti 21 mwaka huu kitakapokuja kwaajili ya kutajwa.
.
Machi 18 mwaka huu, ilidaiwa na upande wa jamhuri kuwa Lwakatare na  Ludovick wanakabiliwa na kosa moja la kula njama ya kutaka kumdhuru kwa sumu Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Denis Msacky.

Juni 14 mwaka huu, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), aliwasilisha Mahakama Kuu ombi la kusudio la kukataa rufaa uamuzi wa mahakama ya hakimu mkazi Kisutu uliompatia dhamana Lwakatare na Ludovick na hadi sasa bado rufaa hiyo haijapangiwa tarehe wala jaji wa kuanza kuisikiliza.
 
DPP hakukubaliana na uwamuzi ulitolewa Mei mwaka huu na Jaji wa Mahakama Kuu,Lawrence Kaduri ambao ulimfutia mashitaka matatu ya ugaidi washitkiwa hao, hadi sasa bado Mahakama ya Rufaa haija panga tarehe wala jaji wa kuanza kusikiliza ombi hilo la kuomba mahakama hiyo ya juu kabisa nchini ifanyie marejeo uamuzi wa mahakama kuu ambao ulimfutia mashitaka matatu ya ugaidi Lwakatare na Ludovick..
 
Wakati huo huo; kesi ya wizi wa jumla ya Paspoti 26 inayomkabili mwanamuzi wa muziki wa asili, Che Mundugwao na wenzake jana ilitajwa mbele ya hakimu Sundi Fimbo na upande wa jamhuri ulidai upelelezi bado haijakamilika na akaiarisha kesi hiyo hadi kesho na kuamuru washitakiwa warudishwe rumande kwasababu bado mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi bado hajaondoa hati yake ya kuwafungia dhamana.
 
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Julai 23 mwaka 2013.

WAKO WAPI WALIOKUWA WAKIPINGA GESI ISIJE DSM?




 Na Happiness Katabazi

MEI 26 mwaka huu, niliandika makala iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “Heko JWTZ,Polisi kudhitibi vurugu Mtwara’.

Makala hiyo niliitundika kwenye ukurasa wangu wa facebook; happy  katabazi .Blogg: www.katabazihappy.blogspot.com

Baadhi ya watu waliyosoma makala hiyo na kuitafsiri wao wanavyojua wao badala ya kujadili kile nilichokuwa nimekiandika mimi, walidiriki kunitolea maneno ya kashfa na wakaitimisha kuwaita baadhi ya wakazi wa Mtwara  ambao walikuwa wakifanya vurugu kwa kisingizio cha kukataa bomba la gesi lisije Dar es Salaam, kuwa ni mashujaa na kwamba wananchi wa mikoa mingine wanastahili kuwaunga mkono.

Kwa takribani miezi mitatu sasa hatujasikia tena  wale baadhi ya Wananchi wa Mtwara na Lindi wakifanya vurugu tena kwa kisingizio cha kuzuia gesi isije Dar es Salaam, wakati wakijua hawana mamlaka ya kuzuia.

Sote tunafahamu madhara yaliyotokana na vurugu zile za kihistoria zilizofanywa na baadhi ya wakazi wa Mtwara ambao ni dhahiri sasa wamelamba matapishi yao na wameudhiirishia umma kuwa hawawezi kupambana na dola, hawana msimamo, ni waoga , wanaogopa vipigo  na kufunguliwa kesi za jinai na kushi gerezani.

Kwani kipindi kile wanaanzisha maandamano na kusambanza vipeperushi walikuwa wakijitapa kuwa hawaogopi nguvu ya dola, vipigo na wapo tayari kufa kwaajili ya kuakikisha bomba la gesi haliletwi Dar es Salaam.

Tuwaulize wananchi wale leo hii mbona hatuwasikii tena adharani wakisimamia maneno yao ya kwamba hawaliogopi dola, kufunguliwa kesi, vipigimo ,kuwekwa gerezani?

Mbona yale maandamano yao yaliyokuwa yakichagizwa  kwa matumizi ya silaha za jadi, kupambana na polisi na kusambaza vipeperushi, mbona hatuyaoni tena?Kulikoni?.Mlijiita nyie ni mashushajaa sasa iweje leo hii mmetembezewa vipigo na watu ambao mimi binafsi si wezi kudiriki kuwa ni askari wa JWTZ kwani sina ushahidi na hilo na uongozi wa JWTZ umekanusha taarifa hizo, msalimu amri?

Hivi shujaa gani anasalimu amri kwa kuogopa kipigo?Shujaa haogopi kipigo.risasi wa virungu.Shujaa anapambana hadi tone la mwisho.Sasa mimi leo nasema wale wahuni waliokuwa wanafanya vurugu Mtwara kwa kisingizio cha gesi siyo mashujaa kama walivyojiita ,minawafananisha na ‘barafu’ kwani barafu linayeyuka.Na wananchi hao wameyeyuka haraka.

Hivi karibuni kumekuwa na taarifa ambazo zimekanushwa vikali na Jeshi la Ulinzi la Wananchi(JWTZ), kuwa askari wake ndiyo wamemwagwa Mtwara na Lindi na kwamba wanajeshi hao wamekuwa wakikamata  raia wasiyo na hatia  kuwapeleka kwenye Kambi ya Naliendele na Majimaji  na kuanza  kuwapiga,kuwabaka na kuwalawiti baadhi ya wananchi hao ambao wanapinga bomba la gesi lisiunganishwe kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam.

Binafsi navieheshimu sana vyombo vyetu vya dola ikiwemo JWTZ kwani nafahamu mchango wake katika nchini yetu, hivyo kwakuwa limekanusha taarifa za wanajeshi wake kuhusika na vitendoi hivyo, name basi sina budi kuungana na jeshi hilo kupinga taarifa hizo ambazo kwanza hakuna mwananchi yoyote aliyebakwa amejitokeza  adharani au kwenda kuripoti kituo chochote cha polisi  na akalitaja jina lake na akatoa na ushahidi kuwa amebwaka au kupigwa na JWTZ.

Tunachokiona na baadhi ya vyombo vya habari kuandika taarifa hizo, ambazo kisheria haziwezi kutumika kuwafungulia kesi za ubakaji au shambulio la kudhuru mwili hao wanaodaiwa kuwa ni askari wa JWTZ  kwa majina yao binafsi na siyo jeshi kama taasisi kubaka watu.

Katika makala yangu ile ya Mei 26 mwaka huu, nilisema wazi kuwa kuna msemo usemao ‘Vita haina macho’. Nilitumia msemo huo kwasababu nilijua mwisho wa siku kuna baadhi ya watu au vyombo vya dola ipo siku vitachoshwa na uhuni ule unaofanywa na wananchi wale na wataanza kuwachukulia hatua na wakati wakichukua hatua, yeyote atakayekuwa karibu na wale wanaoshukiwa kufanya vurugu zile.

Na kweli tumesikia kupitia vyombo vya habari vikiripiti kuwa watu wanaodaiwa ni wanausalama ambao wanaendesha opareshini maalum ya kuwashikisha  adabu wale wananchi wakarofi wanaopinga gesi isije Dar es Salaam, wakiwapiga na kuwajeruhi watu wasiyokuwa na hatia.

Kama taarifa hiyo ni ya kweli, basi hapo maana msemo wa ‘Vita haina macho’ unapotimia, kwani hao wanaodai leo wamepigwa na hao wanaodai kuwa ni wanausalama bila kosa, tuwaulize wao kama Watanzania na wakazi wa mikoa hiyo, kabla na baada ya vurugu zile waliisaidie nchi kwa kuakikisha wanatoa maoni yao ya kupinga vurugu zinazofanywa na wenzao kwa kisingizo cha bomba la gesi?

Au ndiyo vyombo vya habari vilikuwa vinaminya maoni ya wale wote waliokuwa wanapinga vitendo vya kihuni vilivyokuwa vikifanywa na wananchi wenzao walikuwa wakitumia njia za kihuni kupinga bomba za gesi lisije Dar es Salaam?

Au ndiyo tuseme sasa kwa kitendo hicho ndiyo kinawafanya wanahabari wa Mtwara hivi sasa kuishi kwa mashaka kwa kuhofia kupigwa na hao wanaodaiwa kuwa ni wanausalama na hao kundi la wananchi ambalo linapingana na agizo la serikali la kutaka gesi isiletwe Dar es Salaam?

Niitimishe kwa kusema kuwa Tanzania ni yetu sote, nishati yoyote inayopatikana ndani ya ardhi hii itatumika kwaajili ya watanzania wote na kwamba nyie wananchi mliokuwa mnapinga gesi isije Dar es Salaam, mlikuwa hamna mamlaka hayo, bali mlikuwa mnafanya uhuni tu ambao mwisho wa siku mmejikuta mkiangukia kwenye mikono ya dola, kwa kupigwa, kufunguliwa kesi na kuishia kusota gerezani na makazi yenu kuaribiwa na kuishi kwa wasiwasi kama ‘mnaoga Barazani’ kwa kuhofia vigipo kutoka kwa watu mnaodai ni wanausalama wa JWTZ wakati uongozi wa JWTZ umekanusha taarifa hizo na kusema kuwa jeshi hilo halijatoa maelekezo kwa wanajeshi wake kupiga raia.

Wanasiasa uchwara  na makundi mengine yaliyokuwa yanawajaza ujinga  ujinga huo wa kutumia njia za kihuni na vurugu kupinga bomba la gesi lisiletwe  Dar es Salaam, leo hii wamewasaliti, hawapo nanyi tena, mahakamani mnakwenda peke yenu, wao wamelala majumbani kwao na wake zao na watoto zao raha mustarehe.

Ndiyo kwanza serikali ipo katika hatua za mwisho za kuakisha bomba la gesi kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam, linajengwa na nyie mkiendelea kushuhudia huku mkiwa mmefyata mkia.

Kama kweli nyie mlikuwa ni mashujaa na wapingaji wa hilo mlilokuwa mnalipinga kwa moyo safi, si hadi leo mngeendelea kusimamia kile mlichokuwa mkikiamini, na mngeakikisha bomba hilo halijengwi msingetishika na vitisho, vipigo lakini kwakuwa nyie mlikuwa ni bendera fuata upepo na mnatumika vibaya, mmesalimu amri?.

Wahenga walisema ‘akili ni nyeweli kila mtu anazake’.Hivyo wananchi tusikubali kutumiwa vibaya na wanasiasa uchwara wanaotafuta umaarufu au kukamata dola kwa njia za kuamasisha maandamano, migomo haramu na vurugu,lugha za kukashifiana na kuzuliana uongo.

Kwani  mwisho wa siku ni sisi ambo tumekubali kutekeleza upuuzi huo wa wanasiasa ndiyo tunakuja kupata madhara ya moja kwa moja ya kuangukiwa na mkono wa dola.Na wakati tunashughulikiwa na mkono wa dola wanasiasa uchwara wale waliotushawishi kufanya vitendo vya uvunjifu wa sheria, wanatuacha solemba.

Tutambue sheria za nchi zipo na zinawashughulikia wale wote wanaozivunja, na kuna watu ambao wamepewa madaraka ya kuruhusu au kutoruhusu jambo fulani lifanyike au lisifanyike kwa niaba yetu.

Nawapongeza askari wanaodaiwa na baadhi ya wakazi wa Mtwara kuwa ni wa JWTZ kuwa wamekuwa wakiwapiga na kuwatesa wananchi wale kwa lengo la kuakikisha wananchi hao wanaachana na habari ya kupinga gesi isiletwe Dar es Salaam.

Kwani askari hao ambao mimi sijawaona na ninarudia kuwa sina uhakika kuwa ni wa JWTZ , wameweza kusaidia kutokomeza vitendo vya uvunjifu wa sheria vilivyokuwa vikifanywa na baadhi ya wananchi wa Mtwara.

Kwani uenda bila kundi hilo la askari wanaodaiwa kuwa ni wa JWTZ  wasingeingia mitaani na kuwaadhibu wananchi hao, uenda wananchi wale wangeendelea na kelele na na vitendo vyao vya uvunjifu wa sheria kwa kisingizio cha gesi hali ambayo ingesababisha hali ya uchumi, usalama huko Mtwara kudorora.

Mwisho napongeza vyombo vyote vya ulinzi na usalama kwa kuweza kudhibiti vurugu za wahuni wale waliokuwa na kisingizio cha kukaidi gesi isiletwe Dar es Salaam, kwani zilikuwa zinalitia doa taifa letu kwenye sura ya dunia.

Kwani ni wazi sasa nilichojifunza mimi hapa nchini hasa katika utawala wa serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete, wananchi wengi wanapenda sana kuongea, kuhukumu, bila kwanza kuwa na ushahidi na maelezo ya kutosha kuhusu jambo wanalolijadili na matokeo yake sehemu kubwa ya jamii yetu imekuwa ikiamini habari na taarifa hizo hata kama habari hizo zilitangazwa na vyombo vya habari kwa nia ovu ya ama kumchafua mtu, kundi au chama fulani kwa makusudi na kwa uongo na pindi dola linapoamua kutumia mamlaka yake wananchi wanafyata mkia.

Sasa tunapenda sana kuvunja sheria za nchi lakini pindi tunaposhughulikiwa na dola ndipo akili zinatukaa sawa, na tunakuwa na adabu. Sasa wale wakazi wa Mtwara waliokuwa wanafanya vurugu walikuwa hawajatiwa adabu, sasa wametiwa adabu kwa kufikishwa mahakamani.

Na hilo kundi linalodaiwa ni la askari wa JWTZ kutembezea kipigo ndiyo limesaidia sana kuwatia dabu wahuni wale na ndiyo maana hadi leo huko  Mtwara tunaelezwa hakuna watu kukaa vikundi vikundi, wala kuzungumzia masuala ya gesi inatoka au haitoki,watu wanafanyakazi za kujenga uchumi wanchi.

Na mkumbuke kuwa kifungu cha 21(2) cha  Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002, kinawapatia mamlaka polisi  kutumia nguvu kuwakamata wale wote wanavunja kwa makusudi sheria za nchi.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Facebook; happy katabazi ;
0716 -774494
Julai 19 mwaka 2013.




KESI YA CHE MUNDUGWAO YAZIDI KUSOMBA WASHITKIWA



Na Happiness Katabazi

WAKAZI wawili wa Dar es Salaam,jana walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  kwaajili  ya hapo baadae kuja kuunganishwa katika kesi ya wizi wa Paspoti 26 inayomkabili Msainii wa Muziki wa asili, Chingwele Che Mundugwao na wenzake wanne.

Wakili wa serikali  Aidah Kisumo mbele Hakimu Mkazi Sundi Fimbo aliwataja washitakiwa hao walifikishwa jana kwa mara ya kwanza mahakamani hapo wakikabiliwa na makosa yanayofanana ambayo yanamkabili Chemundugwao na wenzake ni  Rajab Momba na Haji Mshamu.

Akiwasomea mashitaka Momba na Mshamu, Wakili Kisumo alidai kuwa tarehe isiyofahamika washitakiwa walikula njama ya kutenda kosa. Aidha tarehe tofauti Dar es Salaam, Momba aliiba hati ya kusafiria yenye namba AB 651926 mali ya serikali.

Alidai Momba, Mshamu na Iqbal wanadaiwa tarehe isiyofahamika Dar es Salaam, walighushi hati ya kusafiria yenye namba hiyo, kuonesha ni halali na imetolewa na Idara ya Uhamiaji ya Tanzania jambo ambalo si kweli.

Mbali na Che mundugwao washitakiwa hao wataunganishwa na Raia wa Uingereza Ahsan Iqbal au Ali Patel, Ofisa  Ugavi wa  Idara ya Uhamiaji Shemweta Kiluwasha, Injinia Keneth Pius wa Kikosi  cha Zimamoto na Uokoaji na mfanyabiashara Ally Jabir.

Hata hivyo washitakiwa  hao walikana mashitaka na kurudishwa rumande kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),Dk.Eliezer Feleshi  aliwasilisha hati ya kuwafungia dhamana washitakiwa hao wawili kama alivyofanya kwa kina Chemunduwao na wenzake na kwamba  upelelezi bado haujakamilika na kesi itatajwa tena Julai 22, mwaka huu, ili waunganishwe na Chemundugwao ambapo kesi yao nayo imepangwa kuja kutajwa Julai 22 mwaka huu.

Juni 3 mwaka huu, Chemundugwao na wenzake walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo wakikabiliwa na makosa mbalimbali yakiwemo kosa la wizi wa paspoti 26, ambapo hata hivyo DPP aliwasilisha hati ya kuwafungia dhamana ambapo hadi sasa wapo gerezani.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Julai 19 mwaka 2013.

OFISA JKT KORTINI TENA KWA PEMBE ZA NDOVU

 
Na Happiness Katabazi
 
OFISA uvuvi  wa Jeshi la Kujenga Taifa(JKT) Suleiman Isanzu Chesana na anayekabiliwa na kesi ya kukutwa na meno ya Tembo yenye thamani ya Sh.bilioni nne, jana tena kwa mara nyingine amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam akikabiliwa na kesi nyingine  ya kukutwa na meno ya teambo Kg.781 yenye thamani ya Sh.bilioni 9.3.
 
Mbele ya Hakimu Sundi Fimbo, wakili Mwandamizi wa Serikali  Tumaini Kweka alidai kosa la kwanza ni la kujishughulisha na  nyara hizo za serikali bila kibali kinyume na sheria ya uhujumu uchumi na kwamba Mei 23 mwaka huu,  katika mpaka wa Malawi  na Tanzania   alikamatwa akisafirisha isivyo halali nyara hizo za serikali   zenye thamani ya Sh.bilioni 9.3 zikiwa zimefichwa  katika mifuko  ya sementi  wakidai wanasafirisha cementi na kwamba upelelezi bado haujakamilika.
 
Hata hivyo Hakimu Fimbo alimtaka mshitkiwa asijibu chochote kwasababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na kwamba ni Mahakama Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza na akaiarisha kesi hiyo hadi  Julai 20 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa na kuamuru mshitakiwa arejeshwe gerezani.
Julai 9 mwaka huu, mshitakiwa huyo, alifikishwa mahakamani hapo kwa hakimu mkazi Nyigulile Mwaseba  akikabiliwa na kesi ya kukutwa na meno ya tembo yenye thamani ya  Sh.bilioni  nne, ambapo pia hakimu Mwaseba siku hiyo alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na akaamuru apelekwe gerezani.
 
Wakati huo huo , Ramadhan Shabani na Pendo Msaki waliokamatwa na askari wa kikosi cha Kupambana na kuzuia dawa za kulevya katika Uwanja wa Mwalimu Julias Nyerere  mwishoni mwa wiki, jana walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na  makosa ya kula njama na kusafirisha dawa za kuleya zenye  uzito wa gramu  833.51 zenye thamani ya Sh 82,732,950 .
 
Katika kosa la pili linalomkabili  Pendo peke yake ni  la kusafirisha dawa za kulevya  nakwamba Julai 6 mwaka huu, katika uwanja wa mwalimu Nyerere alikamatwa  gramu 500.08  aina ya Heroine zenye thamani ya sh67,536,000. Upelelezi bado na hakimu akaamuru waende gerezani hadi  Julai 24 mwaka huu, kwaajili ya kutajwa na akasema mahakama yake haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
 
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Julai 12 mwaka 2013.

MRAMBA KWENDA KUTIBIWA NJE YA NCHI




Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imempatia ruhusa ya kwenda kutibiwa nje ya nchi aliyekuwa Waziri wa Fedha Basil Mramba anayekabiliwa na kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali harasa ya Sh.bilioni 11.7.
 
Mbali na Mramba washitakiwa wengine ni aliyekuwa Waziri wa  Nishati na Madini Daniel Yona na Katibu Mkuu Mstaafu wizara ya fedha, Gray Mgonja wanaotetewa na mawakili wa kujitegemea Hurbet Nyange, Peter Swai, Profesa Leonard Shahidi na Elisa Msuya.
 
Ruhusa hiyo ilitolewa jana na jaji Sam Rumanyika  ambapo alisema anakubaliana na ombi la wakili wa Mramba, Elisa Msuya  ambaye aliomba mahakama impatie ruhusa Mramba ya kwenda kutibiwa nje ya nchi kwasababu daktari anayemtibia Mramba amependekeza Mramba akatibiwe nje ya nchi.
 
Jaji Rumanyika alisema anakubaliana na ombi hilo na kwamba anamruhusu Mramba aende kutibiwa nje ya nchi na kwamba wakati Mramba atakapokuwa amekwenda nje ya nje kwaajili ya matibabu kesi yake haitaweza kuendelea kwasababu Mramba  hajatoa idhini kesi hiyo iendelee bila ya yeye kuwepo.
 
“Hivyo natupilia mbali ombi la wakili wa Jamhuri Oswald Tibabyekomya lilokuwa linataka kesi hiyo iendelee kusikilizwa hata kama Mramba hayupo….na kwamba nakubali ombi la wakili wa Mramba hivyo mahakama hii inamruhusu Mramba aende kutibiwa nje ya nchi na ninairisha kesi hii hadi Septemba 16 hadi 20 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya Mramba kuendelea  kuhojiwa na mawakili wa upande wa jamhuri’alisema Jaji Rumanyika.
 
Awali wakili Tibabyekomya aliikumbusha mahakama kuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili Mramba kuendelea kuhojiwa lakini ikashindikina kwasababu Mramba anaumwa lakini hata hivyo jana Mramba aliweza kufika mahakamani hapo.
 
Wakati huo huo; mahakama hiyo ilishindwa kutoa uamuzi wa kumuona Johnson Lukaza na Mwesigwa Lukaza kama wanakesi ya kujibu au la kwasabu miongoni mwa wanajopo wanaosikiliza kesi hiyo ni mgonjwa na hivyo hakimu Nyigulile Mwaseba aliarisha kesi hiyo ya wizi wa sh.bilioni sita hadi Julai 15 mwaka huu,  ambapo jopo hilo litakuja kutoa uamuzi wake  wakuona washitakiwa hao ama wanakesi ya kujibu au la.
 
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima Ijumaa, Julai 12 mwaka 2013.

RAIA WA UINGEREZA AUNGANISHWA KESI YA CHE MUNDUGWAO

 
Na Happiness Katabazi
 
RAIA wa Uingereza Ahassan jana aliunganishwa kwenye kesi  ya wizi wa Paspoti  26 inayomkabili  Msanii wa Muziki wa Asili nchini, Chigwele Che Mundugwao na wenzake ambao wanaoendelea kusota gerezani  tangu Mei 3 mwaka huu, kufuatia Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP),Dk.Eliezer Feleshi awafungie dhamana.
 
Wakili Mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka mbele ya Hakimu Sundi Fimbo alieleza mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kwaajili ya kutajwa ambao inajumla ya washitakiwa wanne lakini ,upande wa jamhuri unaomba kubadilisha hati ya mashitaka kwasababu inamuunganisha mshitakiwa mwingine ambaye ni raia wa Uingereza na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
 
Wakili Kweka pia aliomba mahakama isitoe masharti ya dhamana kwa mshitakiwa huyo kwani upande wa jamhuri utaleta hati ya DPP ya kumfungia pia mshitakiwa huyo dhamana kama washitakiwa wengine walivyofungiwa kwa mujibu wa kifungu cha  148(4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.
 


 Hakimu Fimbo alikubali ombi hilo na kusema sasa hati ya mashitaka itasomeka kuwa ina jumla ya washitakiwa wa tano na akautaka upande wa jamhuri ulete kwa maandishi hati hiyo  ya DPP ya kumfungia dhamana mshitakiwa huyo wa tano na akaiarisha kesi hiyo hadi Julai 22 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa na akaamuru washitakiwa wote warejeshwe rumande.

Mbali na Che Mundugwao ,washitakiwa wengine ni ofisa  Manunuzi  wa Idara ya Uhamiaji, Shemweta Kilwasha (31), Mhandisi wa Idara ya Zimamoto na Ukoaji, Keneth Pius (37) na mfanyabiashara, Ally  Jabir  (34) wanaotetewa na wakili Peter Kibatara.

 Mei 3 mwaka huu, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Ladslaus Komanya  mbele ya Hakimu Mkazi  Aloyce Katemana aliwasomea mashitaka washitakiwa hao na kudai kuwa wanakabiliwa na kosa la kula njama kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha  384 cha Sheria ya Kanuni ya adhabu ya mwaka 2002.

Wakili Komanya alieleza kuwa kati ya Aprili 16 na Mei 10, mwaka huu , Shimweta akiwa ni mtumishi wa umma,  katika Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji aliiba paspoti 26, mali ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Komanya alidai kuwa washitakiwa  Chigwele, Keneth na Ally, Mei 30, mwaka huu, huko Yombo Makangarawe jijini Dar es Salaam ,walikamatwa wakiwa na pasipoti hizo 26 za wizi.

Kuhusu  Che Mundugwao,wakili Komanya alidai kuwa mshitakiwa huyo kuwa Aprili 22, mwaka huu alikamatwa akimiliki  paspoti 12  za watu wengine bila ya kuwa na sababu yoyote ya msingi .

Wakili huyo wa Serikali, aliendelea kudai kuwa Mei , mwaka huu  Che Mundugwao pia alikamatwa na maofisa wanausalama akimiliki pasipoti nyingine mbili  zenye majina ya watu wengine sababu yoyote ya msingi. 
Komanya aliendelea kuwa Aprili 24 mwaka huu, mshitakiwa Ally , alighushi paspoti yenye namba AB 65196 akionyesha kuwa ilikuwa ni halali na kwamba ilitolewa na Idara ya Uhamiaji wakati akijua kuwa si kweli.

Wakili Komanya alidai kuwa kati ya mwaka 2007 na 2011 Dar es Salaam,   Shemweta alighushi nyaraka ya serikali ambayo ni muhuri akijaribu kuonyesha kuwa nyaraka hizo zilikuwa ni halali na kwamba zimetolewa na Idara ya Uhamiaji wakati si kweli.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Julai 10 mwaka 2013.

UPELELEZI KESI YA LWAKATARE BADO


Na Happiness Katabazi
 
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,imearisha kesi ya kula njama na kutaka kuumua kwa sumu Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Mwananchi, Denis Msacky inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema),Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph.
Hakimu MKazi Alocye alisema kwakuwa kesi hiyo jana ilikuja kwaajili ya kutajwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Ponsia Lukosi amedai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, mahakama yake inaiarisha kesi hiyo hadi Julai 22 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya kutajwa.

Wakili wa Lwakatare, Nyaronyo Kichere ambaye alifika mahakamani hapo  na Lwakatare ambaye yupo nje kwa dhamana, Ludovick yeye bado yupo gerezani kwasababu ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyotolewa na mahakama hiyo Juni 11 mwaka huu, ambapo Hakimu Katema alisema ili washitakiwa wapate dhamana ni lazima kila mshitakiwa awe na wadhamini wawili wanaotoka taasisi zinazotambulika kisheria  ambapo kila  mdhamini atatakiwa asaini bondi y a sh.milioni 10 pamoja na washitakiwa wenyewe,washtakiwa hao kusalimisha  hati zao za kusafiria mahakamani na kutotoka  nje ya jiji la Dar  es Salaam bila ya kuwa na kibali cha mahakama. Lakini hadi jana Ludovick ameshindwa kutimiza masharti hayo nab ado anaendelea kusota gerezani.

Machi 18 mwaka huu, ilidaiwa na wakili wa serikali Mkuu Lukosi kuwa washitakiwa walitenda kosa hilo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Julai 9 mwaka 2013.

HAPPINESS KATABAZI Vs BALOZI COSTA MAHALU

Happiness Katabazi nikiwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu chetu cha Bagamoyo(UB), Profesa Costa Mahalu,nilipomtembelea ofisini kwake Mikocheni na kuzungumza nae mambo mbalimbali.Mungu ampe maisha marefu Balozi Mahalu kwa wale tunaomtambua vilivyo tutaendelea kumheshimu yeye binafsi na taaluma yake. Julai Mosi mwaka 2013. (Picha na Dk.MTARO)

KADATTA .K.KADATTA AOMBA FEDHA ZA MATIBABU




Na Happiness Katabazi

MWANAMICHEZO maarufu nchini, Kadatta .K.Kadatta ameiomba serikali na umma umsaidie kumlipia gharama za matibabu ambazo zinazidi kuongezeka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimimbili Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kwa taabu huku akidai ana maumivu makali kichwani na kifuani,Kadatta ambaye aliwai kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Kinondo(KIFA), alisema amefikia uamuzi wa huo wa kuomba msaada huo baada ya kuona hana huwezo wa kugharamia gharama za matibabu ambazo zinazidi kuongezeka kila siku.

Kadatta alisema Jumamosi mchana wakati anatoka kumuangalia mjukuu wake Magomeni Mtaa wa Dosi Dar es Salaam, akiwa amesimama ilitokea pikipiki iliyokuwa inaendeshwa kwa mwendokasi na kisha ikamgonga na kukimbia ambapo wasamalia mwema walimbeba kwenye gari na kisha kumkimbiza katika Taasisi ya Mifupa Mosi, na kisha juzi kufanyiwa upasuaji wa mguu kulia ambapo imebainika amefunjika mfupa katika mguu wa wa kulia.

“Hivi jana juzi jioni ndiyo nimetolewa Moi na kisha kuletwa katika Wodi ya Sewaaji Na. 18 ambapo nimelazwa na nimewekewa vifaa maalum katika mguu wangu wa kulia siwezi kutembea na pia ninamaumivu makali sana kichwani na kifuani, na daktari ameshauri nikapigwe X-Ray kifuani na kichwani lijulikane tatizo ni nini:

“Kwa kweli ninamaumivu makali sana, na mbaya zaidi sina fedha za kujitibia, hivyo naomba wewe mwandishi wa habari ukautangazie umma kuwa mimi naomba umma wa watanzania wananisaidie kunichangia fedha ili niweze kuendelea kutibiwa hapa hospitalini…ila nashukuru uongozi wa hospitali unanipatia huduma”alisema Kadatta ambaye pia aliwai kuwa mwandishi wa makala za habari za michezo wa gazeti la Tanzania Daima.

Anayetaka kumsaidia Kaddata, atume mchango wake kupitia simu ya mkononi ya Kaddata ambayo ni 0787 777199.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano,Julai 4 mwaka 2013.