DPP AMCHELEWESHA ZOMBE



Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, jana ilijikuta ikishindwa kuanza kusikiliza ombi la kuomba kuomba kuongezewa muda wa kukata rufaa lililowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe na wenzake kwasababu DPP halikuwa hajaupatia upande wa utetezi nakala ya ombi hilo.

Jaji Alocye Mujulisi  alisema shauri ilo lilikuja jana mbele yake kwaajili ya kuanza kusikiliza ombi hilo la DPP, lakini mahakama yake inalazimika kualisha usikilizwaji wa shauri hilo kwasababu mawakili wa upande wa utetezi wanaoongozwa na wakili wa kujitegemea Richard Rweyongeza waliomba shauri hilo lisikilizwe  kwasababu upande wa jamhuri jana  ulikuwa haujaupatia nyaraka hiyo upande wa utetezi na hivyo kusababisha mawakili wa utetezi kushindwa kujiandaa.

“Kwa sababu hiyo naairisha usikilizwa wa ombi hili la DPP hadi Septemba 5 mwaka huu, na ninaamuru upande wa jamhuri uwapatie nyaraka hiyo upande wa utetezi  na upande wa utezi ujibu  kisha tukutane hapa tarehe hiyo kwaajlili ya usikilizwaji wa ombi hili “alisema Jaji Mujulisi.

Mei 8 mwaka huu, Mahakama ya Rufani nchini iliifuta  rufaa  iliyokuwa imekatwa na DPP ya kupinga hukumu ya kesi ya mauji ya  Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,iliyomwachilia huru  Zombe na wenzake baada ya kubaini kuwepo kwa dosari katika hati ya kukatia rufaa hiyo.

Uamuzi huo ulitolewa jana na jopo la majaji wa tatu  Edward Rutakangwa,Mbarouk Mbarouk na  Bethek Mila.Uamuzi huo ulitokana  na jopo hilo Aprili 22 mwaka huu, iliposhindwa kuanza kusikiliza rufaa hiyo Na.254/2009  baada ya jopo hilo kubaini dosari katika hati hiyo   ambapo mawakili wa mwomba rufaa Timon Vitalis na Richard Rweyongeza walikiri dosari hiyo na wakaiomba mahakama iwapatie muda wa kwenda kuifanyia marekebisho hati hiyo ya kukatia rufaa.

Jaji Mbarouk siku hiyo ndiyo aliyeibaini dosari hiyo ambayo dosari yenyewe ni kwamba katika hati ya kukataa rufaa, DPP alisema anapinga hukumu ya kesi ya mauji Na. 26/2006 iliyokuwa ikimkabili Zombe na wenzake kuwa ilitolewa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa Salum Massati. Wakati DPP alipaswa kuandika Jaji Salum Massati ambaye wakati akisikiliza kesi hiyo alikuwa  ni  Jaji wa Mahakama Kuu  na wakati akiendelea kusikiliza kesi hiyo aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa , hivyo DPP katika hati yake ya kukata rufaa alipaswa amtambulishe kuwa hukumu ile ilitolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Massati na siyo jaji wa mahakama ya rufaa.

Akitoa uamuzi huo, jopo hilo lilisema kuwa ibara ya  119 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasomeka kama ifuatavyo:

“Jaji yoyote  wa Mahahakama ya Rufani hatakuwa na mamlaka  ya kusikiliza shauri lolote katika Mahakama Kuu  au katika mahakama ya hakimu  ya ngazi yoyote.:
“Isipokuwa kwamba iwapo jaji yeyote wa mahakama kuu atateuliwa  kuwa Jaji Mahakama ya rufaa, basi hata baaa ya kuteuliwa kwake kuwa jaji wa mahakama ya rufani,jaji huyo  aweza kuendelea kufanyakazi kazi zake katika mahakama kuu mpaka amalize  kutayarisha  na kutoa hukumu  au mpaka akamilishe shughuli nyingine yoyote  inayohusika na mashauri  ambayo yalikwisha anza kuyasikiliza kabla kabla  hajateuliwa  kuwa jaji  wa mahakama rufani, na kwamba ajili hivyo itakuwa  halali kwake  kutoa hukumu  au uamuzi  mwingine wowote unaohusika kwa kutumia  kutumia au  kutaja madaraka  aliyoshika kabla  ya kutueliwa  kuwa jaji wa mahakama ya rufani,  lakini endapo hatimaye hukumu hiyo au uamuzi  mwingine utapingwa kwa njia  ya rufaa itayofikishwa mbele ya  mahakama ya rufani,basi katika hali  hiyo jaji  huyo  wa mahakama ya rufani,hatakuwa  na mamlakaya kusikiliza  rufaa hiyo:inasomeka ibara hiyo.

Jaji Rutakangwa alisema kwa mujibu wa matakwa ya ibara hiyo, na kwakuwa wakili Vitalis alikiri dosari hiyo, mahakama yake imefikia uamuzi wa kuona hati ya rufaa ina dosari na kwa dosari hiyo mahakama yake imeona hakuna rufaa mbele yake na hivyo imefikia uamuzi wa kuifuta ombi hilo la rufaa iliyofunguliwa na DPP dhidi ya Zombe na wenzake.

Aidha jopo hilo lilisema  mahakama yake inatoa fursa kwa DPP kuwasilisha ombi la ukomo wa muda Mahakama Kuu wa kuomba waongezewe muda wa kukata rufaa upya kama wataona wana haja ya kufanya hivyo.
Baada ya uamuzi huo wa mahakama ya rufaa kutolewa ndio DPP aliwasilisha Mahakama Kuu ombi hilo ambalo jana lilishindwa kuanza kusikilizwa.
Agosti 17  mwaka 2009, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa hukumu ya kihistoria ya kesi ya mauji ya watu wanne iliyokuwa ikimkabili Zombe na wenzake ambapo jaji Salum Massati ambaye hivi sasa ni jaji wa mahakama ya rufani aliwaachilia huru Zombe na wenzake ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi hiyo kwa maelezo kuwa upande wa jamhuri ulishindwa kuleta ushahidi mzuri ambao ungewea kuishawishi mahakama hiyo iwaone washtakiwa hao wana hatia.


Baada ya hukumu hiyo ya mahakama kuu, DPP hakulidhishwa na hukumu hiyo Oktoba 7 mwaka 2009 akakata rufaa Mahakama ya Rufaa ,  kupinga hukumu hiyo ambayo kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya mahakama ya rufaa,rufaa hiyo ilikuwa imepangwa kuanza kusikilizwa jana lakini ikashindikana.

Mbali na Zombe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Christopher Bageni, Ahmed Makele, WP 4593 PC Jane Andrew, D 1406 Koplo Emmanuel Mabula, D 8289 DC Michael Shonza, D. 2300 Abeneth Saro, D.4656D/Koplo Rajabu Bakari na D.1317D/XP Festus Gwasabi na jana washtakiwa wote walifika mahakamani hapo.

Washitakiwa hao walidaiwa kuwa Januari 14, mwaka 2006 waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini wa wilayani Ulanga, mkoani Morogoro; Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe pamoja na dereva teski Juma Ndugu, mkazi wa Dar es Salaam kwa madai kuwa walikuwa majambazi.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Agosti 30 mwaka 2013




SIRI ZAANIKWA KESI YA JENGO LINALOKARIBIA IKULU




Na Happiness Katabazi

SHAHIDI wa  tatu katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka katika ujenzi wa jengo la ghorofa 18, lililo karibu na Ikulu, Saimon Maembe ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Manispaa ya Ilala iliwanyima kibali washtakiwa katika kesi hiyo cha kuongeza idadi ya ghorofa kwenye juu.

Kesi hiyo inawakabili vigogo wawili wa Wakala wa Majengo (TBA) ambao ni aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa TBA, Makumba  Togolai Kimweri na Msanifu Mkuu wa TBA, Richard John Maliyaga.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutumia madaraka yao vibaya kwa kutoa kibali cha kupanua jengo hilo kwa kuongeza ghorofa tatu zaidi kutoka 15 hadi 18, bila idhini ya mamlaka husika na bila kufuata Sheria za mipango miji.

Jengo hilo linalomilikiwa kwa ubia kati ya kampuni ya Royalle Orchard Inn na TBA, liko katikati ya Jiji la Dar es Salaam, katika mtaaa wa Chimara,  kitalu namba 45 na 46, karibu na Taasisi ya Saratani Ocean Road, katika  Manispaa ya Ilala.

Akitoa ushahidi wake jana Mchunguzi  wa kesi hiyo toka  Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), alidai wakati anafanya uchunguzi wake aligundua kuwa  Manispaa ya Ilala ilikataa maombi ya washtakiwa hao  kujenga ghorofa 15.

Maembe alidai   licha ya kuwa Wizara ya Ujenzi kutoa waraka kwa TBA ikielekeza kuwa ni lazima ishirikishwe katika mchakato wa uendelezaji wa viwanja vinavyomilikiwa na TBA kwa niaba ya Serikali, hata hivyo washtakiwa hao hawakuishirikisha wizara hiyo katika mradi huo.

Maembe aliyekuwa akiongozwa na  Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Leonard Swai, kutoa ushahidi wake alieleza kuwa alianza kufanya uchunguzi wa ujenzi wa jengo hilo   baada ya  Rais Jakaya Kikwete  na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutoa maelekezo kwa  Takukuru, na kwamba alikabidhiwa jukumu hilo na Kaimu Mkurugenzi wa Takukuru.

Alidai  wakati akifanya uchunguzi wake  alikwenda TBA ambako alipata nyaraka mbalimbali za mradi huo kama vile tangazo la zabuni ya ubia wa ujenzi wa jengo hilo, maombi ya wazabuni na taarifa ya tathmini ya zabuni hiyo.

Alizitaja nyaraka nyingine kuwa ni mihtasari ya vikao na uamuzi wa Bodi ya Zabuni ya TBA, mkataba wa ujenzi wa jengo hilo na vibali vya ujenzi, na kwamba kampuni ya Royalle Orchard Inn ndio ilishinda zabuni hiyo na kwamba  nilibaini kuwa vibali vya ujenzi vilitolewa na TBA, jambo ambalo lilimshangaza nikuona   kuwa vibali vya ujenzi vilitolewa na TBA wenyewe, kwa sababu haikuwa kawaida kwani kuna mamlaka zinazohusika na vibali vya ujenzi.

Maembe alidai kuwa katika  makubaliano ya ubia kati ya TBA na kampuni hiyo, walikuabaliana kujenga jengo kwa ajili ya makazi na biashara na kwamba jengo litakuwa ni la ghorofa 15.
Alidai kuwa kibali cha kwanza kilikuwa ni cha ujenzi wa ghorofa 15 na cha pili kikiwa ni cha upanuzi wa mradi kutoka ghorofa 15 hadi 18 na kwamba vyote vilitolewa na kusainiwa na mshtakiwa wa pili, Maliyaga.

Shahidi huyo alidai kuwa baadaye alikwenda Manispaa ya Ilala ambayo kwa mujibu wa Sheria namba  8 ya Mipango Miji ya mwaka 2007 ndio yenye mamlaka ya kutoa vibali, ili kuona kama walihusika kutoa vibali vya ujenzi huo.

“Kiongozi wa Idara ya Mipango Miji alieleza kuwa waliwahi (washtakiwa) kupeleka maombi ya kibali cha  kujenga ghorofa 15 lakini wakayakataa, kwa sababu hayakuendena na ramani ya mchoro wa eneo husika.”

Maembe alidai   baadaye alikwenda Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambayo ndio yenye uamuzi wa mwisho ya matumizi ya ardhi, na kwamba katika Idara ya Mipango Miji alipata ramani ya eneo husika ya mwaka 2000.
“Maelekezo ya ramani yalikuwa wazi, kwanza ni kuwa matumizi ya ardhi katika eneo husika ni makazi tu na mbili  majengo katika eneo hilo ni ya ghorofa tatu hadi sita. Kwa hiyo niligundua kuwa kilichofanyika katika ujenzi huo kilikuwa kinyume cha sheria.”, alidai shahidi huyo.

Hata hivyo alidai kuwa alipowauliza wizara kama waliwahi kutoa mabadiliko ya matumizi ya ardhi katika eneo husika, walikataa kuwa hawajawahi kupata mnaombi kama hayo.

Katika ushahidi wake shahidi huyo alidai kuwa wakati akichambua nyaraka alizozikusanya, alipata waraka kutoka Wizara ya Ujenzi, ambako TBA iko chini yake, ukiielekeza TBA kuishirikisha katika mchakato wa uendelezaji wa miradi ya viwanja inavyovimiliki.

Hata hivyo shahidi huyo alidai kuwa alipokwenda Wizara ya Ujenzi kuona jinsi walivyoshirikishwa, Katibu Mkuu wa wizara hiyo alisema TBA haikuwahi kuwashirikisha katika mradi huo.
Pia shahidi huyo alidai kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma, taasisi yoyote ya umma inapotaka kuingia katika ubia na sekta binafsi katia mradi, lazima ifanye upembuzi yakinifu, ili kubaini changamoto, gharama, faida, wadau na namna ya kutatua changamoto za mradi na kwamba hata hivyo TBA haikufanya upembuzi yakinifu katika mradi huo na kwamba.

Alisisitiza licha ya ukiukwaji huo wa sheria katika ujenzi huo, washatakiwa walikuwa na ufahamu wa taratibu zilizopaswa kufuatwa kwani kulikuwa na dokezo kutoka mshatakiwa wa pili kwenda kwa mshtakiwa wa kwanza.
Katika dokezo hilo lililosomwa mahakamani hapo mshtakiwa wa pili alikuwa akieleza kuwa amefanya mawasiliano na Manispaa ya Ilala, lakini imesisitiza kuwa eneo hilo ni la makazi na linahitajika ghorofa tatu hadi sita tu.
Alidai kuwa baada ya uchunguzi huo aliwahoji washtakiwa kutokana na tuhuma hizo ambapo walikiri, katika maelezo yao ya onyo, ambayo aliomba mahakama iyapokee kama kielelezo cha ushahidi.

Hata hivyo upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Majura Magafu, ulipinga kupokewa kwa maelezo hayo na Hakimu Sundi Fimbo aliamuru kesi hiyo ya msingi isimame ili kuendesha kesi ndogo (Trial within a trial) kuona uhalali wa maelezo hayo ya onyo ya washtakiwa na hakimu huyo akaiarisha kesi hiyo hiyo hadi Septemba 5 mwaka huu, itakapokuja kwaajili ya mahakama kuanza kuisikiliza kesi hiyo ndogo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Agosti 29 mwaka 2013.

NTAGAZWA ALIPONDA JESHI LA POLISI







Na Happiness Katabazi

WAZIRI wa zamani Arcado Ntagazwa ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, analishangaa Jeshi la Polisi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka nchini kujitwishwa jukumu lisilolao la kuamua kumfungulia kesi ya jinai inayomkabili wakati  kisheria kesi hiyo ilipaswa iwe ni ya madai.

Ntagazwa ambaye hivi sasa ni Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na ni msomi wa taaluma ya sheria alieleza hilo jana mbele ya Hakimu Mkazi Gene Dudu wakati akitoa utetezi wake katika kesi ya kujipaia kofia ,fulana zenye jumla ya thamani ya Sh.milioni 74.9 kwa njia ya udanganyifu.

Ntagazwa ambaye anatetewa na wakili wa kujitegemea Alex Mshumbusi alitoa maelezo hayo wakati akipangua maswali aliyokuwa akihojiwa na wakili wa serikali Charles Anindo  ambapo alidai kuwa kesi hiyo ilipaswa iwe nay a madai na aliyekuwa  na haki ya kuifungua ni mkwe wa Edward Lowassa, Noel Severe ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Visual Storm na siyo Polisi ,DPP kwani Polisi ,DPP wanajukumu la kufungua kesi ya jinai tu na siyo kesi za madai.

Akiongozwa na wakili Mshumbushi kutoa utetezi wake, Ntagazwa alieleza kuwa  yeye ni miongozi wa wadhamini wa Asasi isiyo ya kiserikali ya FORD na kwamba  mwaka 2010 taasisi hiyo ilikuwa inataka kumuenzi Baba wa Taifa Julias Nyerere ambaye Oktoba 14 mwaka 2010 alikuwa anatimiza miaka 10 tangu afariki dunia na kwamba FORD ilikuwa imeandaa mradi ukiwemo wa kutengeneza fulana, kofia zilizokuwa zinapinga vitendo vya kifisadi kwaajili ya kumuenzi Nyerere na kwamba FORD kwakuwa haikuwa haina fedha, iliamua kuandika mradi na kuupeleka kwa wafadhili mbalimbali ili ziweze kuwapatia fedha za kuweza kufanikisha mradi huo  uliokuwa umebeba dhima ya kumuenzi Nyerere kwa kupinga ufisadi.

“Baada ya kupeleka maombi yetu hayo kwa wafadhili, wafadhili walikubali ombi letu na wakatuambia tuendelee na taratibu nyingine na kwamba watatupatia fedha…na sisi FORD kwa kuanzia tulienda kuona na kampuni ya Visual Storm ambayo mmoja wa wakurugenzi wake ni Mkwe wa Lowassa , Severe na kumwomba atutengenezee fulana na kofia  zenye thamani ya Sh.milioni 74.9  na tulimweleza mapema kuwa wafadhili wakitupatia fedha tutamlipa na Severe alitukubalia akatutengenezea hizo fulana na FORD na Visual Storm haikuwa imeandikishia mkataba wa maandishi kwaajili ya kazi hiyo;

“Lakini ilipofika  Januari 23 mwaka 2010 gazeti la Mtanzania lilichapisha habari iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘ Vigogo walioisaliti CCM wahanikwa’. Na ndani ya habari hiyo zilipigwa picha fulana zetu ambazo zilitengenezwa na Visual Storm na hiyo habari kumbe ilisomwa vizuri na wale wafadhili waliokuwa wametuahidi kutupatia fedha, wale wafadhili wakashtushwa na habari ile wakatuita viongozi wa FORD na kueleza kuwa hawatawafadhili tena fedha kama walivyowaadi kwasababu kutokana na habari hiyo wameona kumbe FORD siyo asasi ya kirai ni chama cha siasa cha upinzani” alidai Ntagazwa.

Ntagazwa ambaye alikuwa akitumia lugha ya Kiingereza  na kisheria kujitetea alieleza kuwa baada ya wafadhili wale kujitoa, FORD wakaamua kwenda polisi kutoa taarifa kuhusu habari hiyo iliyochapishwa na gazeti la Mtanzania lakini baada ya muda mfupi baadaye alishangaa polisi wanakuja kumkamata nyumbani kwake akiwa bafuni na hadi leo polisi hawajawai kumchukua maelezo ya onyo  na jeshi la polisi na akashtukia anafunguliwa kesi hiyo ambayo alilisitiza ni kesi ya madai siyo ya jinai na polisi imekuwa ni jadi yao sasa kudandia mambo hata yasiyowahusu mke na mume wanadaiana polisi wanaingilia kati.

“Kwanza nikuulize wewe wakili wa serikali Charles hivi hata kama kweli kesi hii ilikuwa inatakiwa iwe ya jinai ,minikifungwa jela ndiyo huyo Severe atazipata hizo fedha?,Umesikia wewe kijana nenda kamwambie huyo Severe kuwa  polisi wamemdanga sana kwa kumshauri anifungulie kesi ya jinai….narudia tena hata nikifungwa ndiyo hizo hela atalipwa na polisi? Hizo fulana hadi leo zipo nyumbani kwa mjumbe wa wadhamini wa FORD ,Wakili Steven Thonya  ambaye naye ni wakili na atakuja kutoa ushahidi wake na hata leo hii mahakama ikitaka kuthibitisha hilo iamie nyumbani kwa Thonya na itazikuta hizo fulana” alidai Ntagazwa na kusababisha watu kuangua vicheko.

Baada ya Ntagazwa kumaliza kutoa utetezi wake hakimu Dudu aliarisha kesi hiyo hadi Septemba  17 mwaka huu, itakapokuja kwaajili mshitakiwa wa tatu ambaye ni mtoto wa Ntagazwa, Dk. Webhale Ntagazwa na mshitakiwa wa kwanza Senetor Mirelya (60) alishamaliza kutoa utetezi wake.

Aprili 23 mwaka 2012, ilidaiwa mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Ladslaus Komanya  kuwa Oktoba 22 mwaka 2009 huko Msasani Mikoroshini washtakiwa hao kwania ovu walijipatia fulana 5000 na kofia 5000 zenye jumla ya thamani ya Shilingi milioni 74.9 toka kwa Noel Sevele kwa makubaliano kuwa wangemlipa Sevele kiasi hicho cha fedha katika kipindi cha mwezi mmoja tangu walipochukua vifaa hivyo lakini hata hivyo walishindwa kumlipa na washtakiwa walikana shtaka na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. 

Ntagazwa ambaye kwa sasa ni Kada wa Chadema , kabla ya kujiunga na chama hicho miaka minne iliyopita, akitokea chama cha Mapinduzi (CCM).Akiwa mwanachama wa CCM, aliwahi kuteuliwa na rais wa Serikali ya awamu ya pili na ya tatu, Ally Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa kushika nyadhifa za uwaziri katika wizara mbalimbali hadi ilipofika mwanzoni mwa mwaka 2006, Rais Jakaya Kikwete alipounda baraza lake jipya la mawaziri na kuamuacha nje ya baraza hilo. 

Ntagazwa ambaye aliwahi kuwa mbunge wa muda mrefu wa Jimbo la Mhambwe kwa tiketi ya CCM, hadi sasa nakumbukwa kwa msemo wake mmoja maarufu aliowahi kuutoa bungeni akiwa Waziri Nchi ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Mazingira alisema ‘Ipo siku wajukuu zetu watafukua makaburi yetu wachunguze ubongo wetu kama tulikuwa na akili timamu’. Ntagazwa alitoa msemo huo kutokana na kutoridhishwa na baadhi ya maamuzi yaliyokuwa yakifanywa na baadhi ya watendaji waliopewa dhamana.
  
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Agosti 28 mwaka 2013.

ALEX MASSAWE AFUNGULIA KESI YA KUGHUSHI









*Mahakama yaamuru arejeshwe Tanzania

Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam,imetoa hati ya kukamatwa na kurejeshwa nchini  mfanyabiashara maarufu nchini Alex Siliyamala Massawe ili aje kukabiliana na kesi yake mpya ya kughushi nyaraka za umiliki wa ardhi na kutoa taarifa za uongo.
Amri hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Gene Dudu muda mfupi baada ya wakili Mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka kuwasilisha ombi hilo mahakamani na kuiarifu mahakama kuwa upande wa jamhuri umemfungulia   kesi Massawe na.150/2013 ya kughushi hati za umiliki wa ardhi na kutoa nyaraka za uongo mahakamani hapo na kumsomea mashashitaka Massawe ambaye anashikiliwa na Askari wa Interpol Dubai bila ya Massawe kuwepo mahakamani hapo .
Hakimu Dudu alisema anakubaliana na ombi hilo la wakili Kweka na kwamba mahakama yake imetoa amri ya kukamatwa kwa Masawe kokote alipo na arejeshwe nchini ili aje akabiliane na kesi yake hiyo mpya iliyofunguliwa mahakamani hapo.
Aidha Hakimu Dudu alisema pia anakubaliana na ombi la wakili Kweka lilokuwa linaiomba mahakama hiyo itamke majina sahihi yanayotumiwa na Massawe  hata kama  kule Dubai anakoshikiliwa na  askari wa Interpol anatumia majina mengi, ambapo hakimu Dudu alisema majina halali ya Massawe ni Alex Siliyamala Massawe ambayo ndiyo yaliyoandikwa kwenye hati ya mashitaka ya kesi hiyo Na.150 ya mwaka huu.
Hivi karibuni vyombo vya habari na Mkuu wa Kitengo cha Interpol cha Jeshi la Polisi hapa nchini , Babile alithibitishia vyombo vya habari kuwa Massawe amekamatwa na askari wa Interol huko Dubai kwa tuhuma mbalimbali.


Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Agosti 24 mwaka 2013

ALIYEGUSHI SAINI YA MIZENGO PINDA KIZIMBANI




Na Happiness Katabazi

MFANYABIASHARA  Amadi Ally Popi(35), jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, akikakabiliwa na makosa mawili likiwemo la kughushi barua inayoonyesha imeandikwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Inspekta wa Polisi Hamis Said mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema alilitaja kosa la kwanza linalomkabili Popi ni  la kughushi kinyume na kifungu cha  333,335(a) na 337 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Inspekta  Said alidai  kuwa tarehe na siku isiyofahamika ndani ya jiji la Dar es Salaam,  kwa nia ya kudanganya  Popi alighushi  barua  yenye kumbukumbu Na,DA21/3078/01A/142 ya Desemba 3 mwaka 2012 akijaribu kuonyesha  kuwa barua hiyo ni halali na ilikuwa imeandikwa na kusainiwa na  Waziri Mkuu  Pinda.

Said alilitaja kosa la pili kuwa  ni la kutengeneza nyaraka  ya serikali bila ya kuwa na mamlaka ya kufanya hivyo kosa ambalo ni kinyume cha kifungu cha  346(a) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, ambapo tarehe na siku isiyofahamika ndani ya jiji la Dar es Salaam, Popi  bila ya kuwa na mamlaka yoyote  alitengeneza barua hiyo na kuisani na kisha alimpatia barua hiyo  Islamu Mohammed Mtila  akijaribu kuonyesha barua hiyo  imetoka katika ofisi ya waziri Mkuu na imesainiwa na waziri Mkuu Pinda.

Hata hivyo mshitakiwa huyo alikanusha mashitaka yote na Hakimu Lema alisema ili mshitakiwa apate dhamana ni lazima  awe na wadhamini wawili wanaofanyakazi serikali au kwenye taasisi zinazofahamika  ambapo watasaini bondi ya Sh.milioni 10 na mmoja katika wadhamini hapo atawasilisha mahakamani hati ya mali isiyoamishika  yenye thamani hiyo, masharti ambayo yalishindwa kutekelezwa na mshitakiwa huyo na hivyo hakimu Lema aliamuru mshitakiwa apelekwe rumande hadi Septemba 5 mwaka huu, kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya kutajwa na upepelezi wa shauri hiyo haujakamilika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la  Jumamosi Agosti 24 mwaka 2013.