Header Ads

MARANDA AMTUPIA MZIGO MSHITAKIWA MWENZAKE

Na Happiness Katabazi

MSHITAKIWA wa pili katika kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Rajabu Maranda, amedai mshitakiwa mwenzake, Farijara Hussein ndiye alikuwa akijua fedha hizo zilitoka wapi.


Maneno hayo yamo kwenye maelezo ya onyo ya Maranda ambayo aliyatoa kwenye timu ya rais ya kuchunguza wizi wa fedha hizo, ambayo yalisomwa jana na shahidi wa sita, SSP-Salum Kisai, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.

Kisai alidai Oktoba 5, mwaka jana, alimpigia simu Maranda na kumtaka afike kwenye ofisi ya tume hiyo iliyopo Mikocheni, kwa ajili ya kuandika maelezo ya onyo, lakini alisema anaumwa figo.

Alidai kesho yake alikwenda na kusema hali yake si mbaya na kwamba alikuwa tayari kuendelea na maelezo na akaanza kuandika maelezo yake baada ya kumtahadharisha kuwa anatakiwa atoe maelezo yake kwa hiari.

“Tukasitisha kuandika maelezo kwa kuwa ilikuwa ni jioni, kesho yake aliomba aje mchana kwa kuwa alikuwa anaumwa, akaja saa 8:45 mchana.
“Tukaendelea saa 9:00 -11 jioni na akawa amemaliza kutoa maelezo yake na nilimtaka asome maelezo hayo na kisha asubuhi aliweka saini yake,” alidai SSP-Kisai.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, Maranda alieleza yeye alifika kwa mara ya kwanza Dar es Salaam, 1994, akaanza kufanya biashara ya kuuza mitumba hadi hivi sasa anamiliki kituo cha Mafuta New BP Petrol kilichopo Mbezi Tanki Bovu.

Alieleza kuwa anaifahamu Kampuni ya Kiloloma & Brothers kwamba ni kampuni ya Charles Kiza, ambaye alimuomba sh milioni 150.

Alidai hawakuandikishana wakati anampatia hizo fedha, kwani Kiza alimweleza kuwa ni mjomba wa aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu, Daud Ballali.

“Tulifungua akaunti katika Benki ya United Bank of Africa (UBA) na nikamtuma Farijala ndiye aende kufungua hiyo akaunti Agosti 31, mwaka 2005,” alidai.

Aidha, Maranda alidai hamtambui mmiliki wa kampuni hiyo ila alisema Farijara anajua alizitoa wapi hizo fedha na baada ya akaunti kufunguliwa Charles Kiza alikuja kuchukua na kunitaarifu ameishapewa fedha BoT na baada ya hapo alichukua fedha zake sh milioni 150 na Kiza aliendelea kuchukua fedha zake.

“Hata deed of assignment niliziona kutoka kwa Kiza kwa B.C Cars Export ya Mumbai ya India na kwamba sh milioni 308 zilitumwa kwenda Uingereza na kuongeza fedha zote kwenye akaunti zilikuwa zikichukuliwa na Farijala na kwamba kuna baadhi ya fedha nilielekezwa na Kiza nichukue na nimlipe Jay Somani ambaye naye ni mtuhumuwa kwenye kesi nyingine ya EPA,” alisema.

Wiki iliyopita shahidi Kisai alisoma maelezo ya onyo ya Farijala, ambapo katika maelezo hayo Farijala alidai kuwa fedha zote zilikuwa zikichukuliwa na Maranda. Kesi hiyo inaendelea leo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Machi 3 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.