Header Ads

OMBI LA MASHTAKA LATUPWA KESI YA EPA

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana ilitupilia mbali ombi la upande wa mashtaka lililoitaka mahakama hiyo iliwaruhusu wachukue kielelezo cha kesi ya wizi wa sh milioni 207 katika Benki Kuu, liende kwa matumizi mengine ya serikali, kwa kuwa halina msingi kisheria.


Uamuzi huo ulitolewa na Jopo la mahakimu wakazi, John Utamwa na Eva Nkya, ambapo walisema ombi la mashtaka, lililowasilishwa na Mwanasheria wa Serikali, Timon Vitalis, halikuzingatia matakwa ya kifungu cha 353 (3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 ambacho kinaitaka Mahakama kuondokana na kielelezo baada ya kesi kuisha.

“Kwa kuwa ombi la upande wa mashtaka halikuzingatia matakwa ya kifungu hicho na badala yake, ikaamua kuegemea kwenye ombi la kutaka mahakama iwapatie kielelezo hicho ili kitunzwe na BoT…jopo hili limeona ombi hilo halijazingatia matakwa ya kifungu ambacho kinaitaka mahakama kuondokana na kielelezo na sio utunzwaji wa kielelezo,” alisema Utamwa.

Wiki mbili zilizopita Vitalis, aliwasilisha ombi hilo la kutaka mahakama iwapatie kielelezo halisi ili wakitunze, badala yake upande wa mashtaka uwasilishe kielelezo kivuli ombi ambalo lilipingwa vikali na mawakili wa utetezi ambao ni Mabere Marando, Majura Magafu na Mpare Mpoki.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 16 mwaka huu, itakapotajwa. Washtakiwa katika kesi hiyo ni Rajabu Maranda na Farijara Hussein ambao ni wafanyabiashara na Ester Komu, Iman Mwakosya na Bosco Kimela ambao ni maofisa wa BoT.

Wakati huo huo: Hakimu Mkazi Edson Mkasimwonga jana aliahirisha kesi ya wizi wa sh bilioni sita za Akaunti ya Madeni ya Nje katika Benki Kuu, inayowakabili ndugu wawili, Johnson na Mwesiga Lukaza, kwa kuwa idadi ya jopo la mahakimu kutotimia.

Hakimu Mkasimwongo alisema kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali. kesi hiyo imeahirishwa hadi Novemba 13 mwaka huu.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Oktoba 14,2009

No comments:

Powered by Blogger.