Header Ads

TUCTA ,KAMA MGOMO NI HALALI KWANINI MMEUSITISHA?

Na Happiness Katabazi

BABA wa Taifa mwalimu Julias Nyerere aliwahi kusema kwamba; “Ukweli unatabia moja nzuri sana ,kwani haubagui rafiki wala adui”.

Leo nimelazimika kutumia nukuu hiyo ya muhasisi wa tiafa letu kwani naamini kabisa nukuu hiyo itasaidia kuunga mkono makala yangu ambayo itajadili azimio la TUCTA liloitisha mgomo usiokuwa na kikomo kwa wafanyakazi wote nchini waliokuwa wamepanga uanze Mei 5 mwaka huu, tena kwa tambo kali, hotuba ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa wakati akizungumza na wazee wa Dar es salaam, hiv karbuni ambapo alitoa msimamo wa serikali yake kuhusu azimio hilo , na pia nitajadili uamuzi wa Tucta wa kusitisha mgomo walioutoa jumanne wiki hii ikiwa ni siku moja baada rais kikwete kutangaza msimamo wa serikali kuhusu azimio hilo.

Kwa zaidi ya kipindi cha mwezi mmoja sasa TUCTA imekua ikitaja sababu nyingi zinazosababisha wao watangaze mgomo ‘shindwa’ kwenye vyombo vya habari hivyo sioni sababu ya kuzirudia rudia katika makala hii ila sababu moja wapo walikuwa wakiishinikiza serikali iwaongezee mshahara watumishi wake hadi kufikia kiasi cha sh 315,000.

Itakumbukwa na watanzania wote waliokuwa wakifuatilia sakata hilo, TUCTA ilikuwa ikijinasbu kupitia vyombo vya habari kwamba mgomo waliouandaa una baraka zote za kisheria na kwamba hakuna kiongozi yeyote wa serikali ambaye angeweza kuwazuia kugoma.

Kwa kauli hiyo ya TUCTA ambayo hadi sasa hawajaikana, nadiriki kuwaita TUCTA walikuwa hawajajiandaa kikamilifu na mgomo , mipango yao ilikuwa ni ya kiubabaishaji na kinafiki pasipo na mfano kwani ilikuwa ikijua wazi kauli hiyo ilikuwa imefurika uongo ,yakizandiki, na ya kuwahaada wafanyakazi wasio na upeo wa kuchambua mambo na walikuwa wakijua fika walikuwa wakivunja sheria za nchi ila walichokuwa wanakifanya ni kutikisa kibiriti.

Wamekuta njiti zimejaa kwenye kibiriti.Rais Kikwete ni namba saba agawanyiki.Viongozi wa TUCTA walitaka kumgeuza Kikwete babu yao kumbe wamekuta bado wamo. Na endapo TUCTA itakana tuhuma hizo hapo juu, basi ijitokeze hadharani na iseme ni kwani imesitisha azimio lake na mgomo siku moja baada ya rais Kikwete kutoa msimamo wa serkali yake, kwani sote tuna fahamu si Rais wetu wala mwananchi yeyote yule hayupo juu ya sheria.

Sote tuliisikia TUCTA ikijitapa kuwa mgomo wao upo halali kisheria ,ni kwanini imeshindwa kuendeleza msimamo wao wa mgomo kama si unafki, uzandiki na inataka kuleta mvurugano kwenye taifa letu ambapo kwani uchumi wa taifa letu utasambaratika.?

Kwasababu hakuna mtu aliye juu ya sheria , hivyo kamwe Rais hawezi kuzuia maamuzi yao ambayo walidai ni halali mbele ya sheria,sasa TUCTA itueleze ni kwanini wamesitisha mgomo wao wakati mgomo wao walidai upo halali kisheria kama walivyokuwa wakijinasibu?

Endapo itajitetea kuwa wameamua kuairisha mgomo kwasababu hawataki kubishana na rais au wanamstahi rais la nchi.Swali je wakati wote iivyokuwa ikiandaa mgomo ilikuwa ikifikiri kiongozi huyo wa nchi na wasaidizi wake watanyamaza kimya?

Na ikiwa endapo sababu iliyosababisha TUCTA kusitisha mgomo wao ghafla ni kuogopa msimamo wa serikali uliotolewa na rais kikwete mapema wiki hii, kwamba hawezi kuongeza mshahara kwa kiasi hicho na asiyetaka kazi aache na atakayegoma atakutana na mkono wa dola,basi kuanzia sasa nadiriki kuita TUCTA ni chui wa karatasi.

Ni TUCTA hii kwa nguvu zote wamejitahidi kuuaminisha umma wa wafanyakazi wa serikali kwamba ifikapo Mei 5 mwaka huu,watagoma na baadhi ya wafanyakazi ambao ni bendera fuata upepo wasiyofahamu kuwa viongozi wa jumuiya hiyo hawana ujasiri wa kupambana na dola mwisho ,waliwaamini msimamo huo wa viongozi wao.

Tuwaulize hawa viongozi wa taifa wa TUCTA ,Kaimu Katibu Mkuu, Nicholas Mgaya na Rais wa TUCTA, Omary Ayoub,ambao ndiyo walikuwa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha mgomo ‘shindwa’unafanikiwa , hawaoni kwamba kwa ubabaishaji wao katika uandaaji wa suala nyeti kama mgomo wafanyakazi na mgomo huo ukashindwa kufanyika kwa maelezo ambayo hayana kichwa wa miguu,na kuudanganya kwao umma kwamba vikao vya vya serikali vimeshindwa kuafikiana huku wakati ikijua Mei 8 mwaka huu, TUCTA ilikuwa imekubali kuudhulia mkutano wa majadiliano na serikali ambayo wameiituhumu haijali maslahi ya wafanyakazi na kwakuwa tucta walimeishaituhumu hivyo serikali ni kwanini inakubali tena kwenda kufanya mazungumzo na serikali isiyowajali?

Kama hili la kuandaa mgomo usiokoma limewashinda TUCTA , watanzania na vyombo vya ulinzi na usalama kwani tusiwe na hofu na shirikisho hilo kwamba kwa ubabaishaji wake wa kuandaa mambo mbalimbali yanayohusu wafanyakazi wa umma ,hatuoni ipo siku wanaweza kulipeleka taifa kuzimu?

Na wakilishalipeka taifa kuzimu, mwisho wa siku watakaoathirika moja kwa moja na haraka zaidi ni watoto,wanawake, wazee na wagonjwa ambao wamelazwa tayari mahospitalini na wagonjwa watarajiwa kwani ni wazi wasingepata huduma ya matibabu kwasababu wauguzi wangedai wapo kwenye mgomo,wanafunzi mashuleni na vyuoni wangekosa kufundishwa na walimwa na taifa kwa ujumla lingepata hasara.

Wanajeshi wa wapo vitani mkuu wa Majeshi huwa aendi vitani bali uteua mabrigedia jenerali kuongoza brigedi tofauti vitani.Hivyo inapobainika kiongozi wa brigedi vitani hana msimamo katika kupiganisha vita, mara moja kiongozi huyo hurudishwa nyuma na nafasi yake inachukuliwa na mmoja wa wafuasi wake na unyanganywa silaha na hurudisha nyuma na na nafasi yake uchukuliwa na mwanajeshi mwingine na kisha kiongozi huyo ambaye alionesha kutokuwa na msimamo uchukuliwa hatua na yule aliyepewa jukumu la kushika nafasi ya kiongozi huyo, huendelea na jukumu la kupiganisha vita.

Sasa kwa mtindo huo unaotumiwa na wanajeshi wote duniani wakati wa wapo vita, ni wazi kabisa mtindo huo leo hii ungetumiwa na wanachama wa TUCTA ni wazi wange wanyang’anya madaraka viongozi wao kwasababu wameonekana hawana msimamo katika kupiganisha vita ‘harakati’ya kudai kuboreshewa maslahi ya wafanyakazi wa umma.

Kwa sababu viongozi wa TUCTA wamekuwa ni chui wa karatasi , kwani kwa kipindi chote hicho wametumia muda wa serikali kuketi katika vikao vyao vya kujadili masuala ambayo hatimaye wameshindwa kuyatekeleza kama walivyoadi, na katika kuketi katika vikao hivyo lazima walilipana posho ambazo ni uenda ni michango ya wanachama, walijaza mafuta kwenye magari kwaajili ya usafili wa kuudhulia vikao hivyo ambapo,sasa wanayakazi wa umma ni kwanini wasianze kuhoji matumuzi hayo ya vikao hivyo ambavyo maazimio yake viongozi hao wameshinmdwa kutekeleza ni kwanini wasiwalazimishe viongozi hao walipe gharama zote walizotumia kuendesha vikao hivyo ambavyo havijazaa matunda waliyohahidiwa?

TUCTA imekuwa ikivuma wakati inapofika wakati wa kudai kuboreshewa maslahi yao, lakini TUCTA hatuisiki kabisa ikitoa ripoti kwa umma kwamba imeweza kushirikiana kikamilifu na waajiri kuwachukulia hatua wafanyakazi wazembe, watoro na wakosefu wa nidhamu makazi au kutoa matamko ya kuwaasa wafanyakazi wake wafanyakazi kwa bidii ili ili kuongeza tija kwa taifa.

Hivi si ni wafanyakazi hawa hawa wa umma ndiyo nao waliochangia kwa kiasi kikubwa kwa marais wetu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete kukubali kuruhusu sera ya uwekezaji nchini, kwasababu viongozi hao walishabaini wazi kwamba baadhi ya wafanyakazi wa umma wamechangia kuyaua mashirika ya umma kama KAMATA, UDA na ATC kwa kushindwa kuzalisha kikamilifu na wakati makampuni hayo ya umma yalikuwepo, hakukuwa na makampuni mengine shindani lakini wafanyakazi hao walishindwa kuyaendeleza na matokeo yake yakafa kifo cha mende.

Leo hii tunawashuhudia watanzania wakijitumbukiza kwenye biashara ya huduma za usafirishaji (daladala) na wamekuwa wakipata faida na kila kukicha wamekuwa wakiagiza daladala nyingi mitaani kwaaji ya kuuendelea kutoa huduma hiyo ambayo inatumiwa na wananchi wengi.

Na wamikili wa magari hayo wamekuwa wakiwalipa ujira mdogo makonda na madereva wa magari hayo.Itakumbukwa enzi mashirika ya umma ya UDA,wafanyakazi waliokuwa wakifanyakazi kwenye mashirika hayo walikuwa wakilipwa mishahana usalama wa ajira zao na mishahara ya uhakika lakini walishindwa kuliendesha shirika hilo .

Kwahiyo wafanyakazi wa umma mnapodai kuboreshewa maslahi yenu haraka lazima mjiulize mara mbili kwenye nafsi zenu kama nyie wenyewe kwanza mnatimiza wajibu wenu ipasavyo na utendaji wenu huo unaliletea taifa tija ipasavyo?Maana msiwe mstari wa mbele kulalamikia kuboreshewa maslahi yenu wakati miongoni mwenu hamtimizi wajibu wenu kikamilifu.

Kwani siyo siri kuna wafanyakazi wa umma wanaenda ofisini siku wanazojisikia wao na ndiyo wamekuwa mabingwa kughushi ruhusa fupi za mapuziko ya ugonjwa(ED) zinazoonyesha zimetolewa na madaktari wa hospitali,au wakiingia ofisini basi hawakai ofisini hadi muda wa mwisho wa serikali unamtaka mfanyakazi wa umma atoke ofisini, au akiwahi ofisini basi muda mwingi atautumia kufanya mambo yake binafsi tena kwa kutumia rasilimali za serikali kama simu, nukushi, internate, printer au wakati mwingine wanaamua kupiga soga,na wengine wanajibu wagonjwa kuwa dawa hazipo katika hospitali na baada ya kumtolea kauli hiyo umvuta pembeni mgonjwa huyo na kumwambia kama atampa fedha ya chai anaweza kumpatia dawa hiyo ambayo ataitoa hapo hospitalini.

Na ninapenda kuishauri TUCTA ikipata wasaa ikaisome vyema ibara ya 37(1) ya Katiba ya Nchi , inasema “Mbali na kuzingatia masharti yaliyomo katika Katiba hii, na sheria za Jamhuri ya Muungano katika utendaji wa kazi na shughuli zake, Rais atakuwa huru na hatalazimika kufuata ushauri atakapewa na mtu yeyote, isipokuwa tu pale anapotakiwa na Katiba hii au na sheria nyingine yoyote kufanya jambo lolote kulingana na ushahuri anaopewa na mtu au mamlaka yoyote’.

Na hapo ndipo nipomweleza rais Kikwete kwamba uzi ni ule ule uliouonyesha Jumatatu wiki hii wakati akizungumza na wazee hapa jijini.Na ninamtaka atambue kuwa kushindwa kwake kutoa kukemea na kuwachukulia hatua katika matukio mbalimbali ambayo yanalihusu taifa hili toka alipoingia madarakani naweza kusema ndiko hasa kulikosababisha miongoni mwetu tuanze kuamini Tanzania ina ombwe la uongozi kwasababu ya rais aliyepo maradakani uenda ameshindwa kutumia vyema madaraka yake yaliyopewa katika Sura ya pili ya Ibara ya 33-46 B za Katiba ya Jamhuru ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Hisia kali ulizozionyesha siku hiyo zimedhiirisha kwamba kaya ya Tanzania ina mwanamme(rais) na hivyo ndivyo mwanamme ndani ya nyumba anavyopaswa aonyeshe kuwa mwanamme ambaye ndiyo kichwa cha familia.Kwani hapa nchini hivi sasa ilifika mahali hajulikani rais ni nani kwani kila mtu anaropoka anachoweza kuropoka hata kama anazungumza uongo hakuna wakumchukulia hatua.

Kwa sisi tunaotamani nchi yetu izidi kupiga hatua za kimaendeleo tungependa kumuona kiongozi wa nchi akiwa mkali kuwachukulia hatua kwa wafanyakazi au mwananchi yeyote anayetaka kurudisha nyuma jitihada za kuliletea tiafa letu maendeleo.

Ieleweke kuwa huu si wakati wa rais wetu kuendelea kuwaonea haya watendaji wa serikalini ,wabunge wake na mawaziri ambao miongoni mwao wana hulka za kinyang’au,wababaishaji,ambao siku za hivi karibuni wamekuwa vinara wa kuvujisha kwenye vyombo vya habari siri za vikao vya chama tawala na baraza la mawaziri, na kumgeuza rais kama ‘ mwanasesere’ katika masuala mbalimbali mfano Sheria ya Gharama za Uchaguzi, kumkabidhi hundi zilizokosewa tarakimu, kumpatia taarifa za uongo ambazo mwisho wa siku mzigo wa fedhea una muungukia kiongozi huyo wa nchi.

Mwisho na waasa wafanyakazi wa umma wasiwe kama vifurushi vinavyobebwa kwenye mifuko laini (Rambo)maana vifurushi hivyo huwa havijui vinapelekwa wapi.

Mungu Ibariki Tanzania ,Mungu ibariki Afrika

0716 774494

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne Mei 11 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.