RUFAA YA LIYUMBA KUSIKILIZWA AGOSTI 27

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Agosti 27 mwaka huu, inatarajiwa kuanza kusikiliza rufaa iliyokatwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba(62) ambaye Mei 24 mwaka huu, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilimuhukumu kifungo cha miaka miwili jela baada ya kumkuta na hatiani kwa kosa la matumuzi mabaya ya ofisi ya umma.


Kwa mujibu wa hati ya wito wa kuitwa mahakamani siku hiyo iliyotolewa na uongozi wa Mahakama Kuu kwa mrufani mwenyewe(Liyumba) , wakili wake Majura Magafu na upande wa Jamhuri na inaonyesha Jaji Emilian Mushi ndiye aliyepangwa kusikiliza rufaa hiyo Na 56 ya mwaka huu.

Tanzania Daima ambayo ilifanikiwa kuiona na kuisoma nakala hiyo ya wito(summons), ambayo imezitaka pande zote katika rufaa hiyo kufika mahakamani hapo saa tatu asubuhi siku hiyo ambapo rufaa hiyo itakuja kwaajili ya kutajwa kwa mara ya kwanza tangu ilipofikishwa na mrufani Mei 28 mwaka huu.

Hata hivyo taarifa za kuaminika toka Mahakama Kuu zinasema tayari mrufani(Liyumba)ameishapelekewa nakala hiyo ya wito tangu juzi katika Gereza la Ukonga anakoishi kwasasa toka alihukumiwa na kwamba jana mchana nakala nyingine ya wito inatarajiwa kupelekwa ofisini kwa wakili wa mrufani Majura Magafu.

Kwa mujibu rufaa hiyo, mrufani ametaja sababu 12 za kukata rufaa ya kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakimu wa Kazi wawili wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Lameck Mlacha na Benedict Mwingwa ambao ndiyo waliomtia hatiani mrufani Wakati aliyekuwa kiongozi wa jopo hilo la mahakimu hao wakazi Edson Mkasimongwa alitoa hukumu yake peke yake na akamwachiria huru mrufani na hukumu ya hakimu huyo imeifadhiwa na kwenye kumbukumbu za mahakama hiyo.

Liyumba anadai mahakama ya Kisutu ilishindwa kuchambua ushahidi uliotolewa mahakamani kikamilifu na matokeo yake jopo hilo la mahakimu wakazi wa tatu likajikuta linatoka na hukumu mbili tofauti,mahakimu hao wawili walifanya makosa kwa kushindwa kwake kukubali mabadiliko ya ujenzi wa mradi wa ujenzi wa Minara Pacha yalifanywa baada ya Meneja Mradi huo Deogratius Kweka kuketi kwenye kikao na timu ya wataalamu wa ujenzi na kujadili shughuli za mradi huo,kwani kwa mujibu wa ushahidi uliopo kwenye rekedi za mahakama hauonyeshi Liyumba alikuwa akiudhuria kwenye kikao hicho cha wataalamu wa masuala ya ujenzi wa mradi.

Mrufani katika sababu ya tatu anadai mahakimu hao wakazi wawili(Mlacha na Mwingwa) walifanya makosa kwa kushindwa kwao kukubali kwamba shughuli zote za uendeshaji wa mradi ule zilikuwa chini ya Meneja Mradi Deogratius Kweka ambaye alikuwa akiwajibika moja kwa moja kwa Gavana na si kwa mrufani(Liyumba), walifanya makosa kwa uamuzi wao wa kuutupilia mbali ushahidi uliotolewa na Liyumba na shahidi wake ambaye alikuwa Kaimu Katibu wa Benki Kuu, Bosco Kimela kwa maelezo kuwa mashahidi wote walikuwa wakiishi pamoja katika gereza la Keko.

“Sababu ya tano, mahakimu hao walifanya makosa kwa kusema kwamba Liyumba na Kimela ushahidi wao ulikuwa kama hadithi ya kutunga....sisi tunapinga hoja hiyo ya mahakama kwa kusema ushahidi huo haukuwa hadithi ya kutunga,mahakama ya Kisutu ilifanya makosa iliposema malipo ya mradi huo yalikuwa yakiidhinishwa na Liyumba...sisi tunapinga hoja hiyo ya mahakama kwani ni wazi kwa mujibu wa ushahidi uliopo kwenye rekodi ya mahakama hauonyeshi Liyumba alikuwa akiidhinisha malipo ya mradi huo, sasa ushahidi huo hao mahakimu wameupata wapi?alidai mrufani.

Aidha aliitaja sababu ya saba ni kwamba mahakama ya kisutu ilifanya makosa kusema Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ilipoteza mwelekeo na kwamba Liyumba na aliyekuwa Gavana marehemu Daud Balali walikuwa wakiiburuza bodi hiyo.Magafu anadai hoja hiyo ya mahakama ni ya kufikirika na hata ushahidi uliopo kwenye rekodi ya mahakama hauonyeshi mahali popote kwamba bodi hiyo ilikuwa ikiburuzwa na mrufani.

Alidai sababu ya nane ni mahakama hiyo ilifanya makosa kusema idhini za mabadiliko ya ujenzi wa mradi wa Minara Pacha zilitolewa baada ya utekelezaji kufanyika hazikubariki kisheria, wakili huyo anadai kuwa hoja hiyo ya mahakama si ya kweli kwasababu idhini zote zilizokuwa zikitolewa zinaruhusiwa na Kanuni za Fedha za Benki Kuu(BoT Financial Regulation).

“Sababu ya tisa ni kwamba mahakama ya Kisutu ilifanya makosa iliposema mrufani hakuwa na mamlaka ya kusaini zile barua ambazo zilikuwa zimeandikwa na mrufani kwaniaba ya BoT ambazo zilikuwa zikienda kwa mkandarasi ambazo ni kielelezo cha 5-12 na kwamba alifanya hivyo kinyume cha sheria....sisi mawakili wa mrufani tunasema hilo si kweli.

“Sababu ya kumi,mahakama hiyo ilifanya makosa iliposema kwamba mabadiliko ya mradi ambayo yalisababisha ongezeko la gharama katika mradi ule yalikwenda kinyume na matakwa ya bodi na kwamba bodi iliathirika”alidai mrufani.

Sababu ya 11, mrufani anadai mahakama ilikosea kusema kwamba upande wa Jamhuri katika kesi hiyo uliweza kuthibitisha kesi yake bila kuacha mashaka yoyote dhidi ya mrufani, wakili wa Liyumba anadai hilo si kweli kwani ushahidi ule wa upande wa mashtaka umeacha mashaka makubwa.Aidha sababu ya 12, mrufani anadai mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilifanya makosa kwa kushindwa kwake kufuata taratibu zilizoainishwa kisheria katika kutoa adhabu.

Januari 27, mwaka huu, Liyumba na Meneja Mradi, Deogratius Kweka walifikishwa mahakamani hapo, wakikabiliwa na makosa mawili ya matumuzi mabaya ya ofisi za umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 221.Lakini, Mei 27 mwaka jana mahakama hiyo iliifuta hati ya mashitaka baada ya kubaini ina dosari za kisheria na ikawaachia washtakiwa ingawa walikamatwa muda mfupi tu na kesho yake Mei 28 mwaka jana ,ni Liyumba peke yake ndiye alifikishwa mahakamani akikabiliwa na makosa hayo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Julai 16 mwaka 2010

MWANASHERIA MAARUFU AUAWA KINYAMA DAR


*Ni Profesa Mwaikusa wa Chuo Kikuu Dar
*Jaji Mkuu, DPP wapigwa butwaa

Na Happiness Katabazi

MHADHIRI Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Juani Timoth Mwaikusa (58) ameuawa kinyama kwa kupigwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, nyumbani kwake usiku wa kuamkia jana.


Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi (ACP), Charles Kenyela, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema watu waliohusika wanasakwa kwa udi na uvumba.

Kamanda Kenyela alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 4 usiku, Barabara ya Makonde eneo la Salasala, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Alisema Mwaikusa alifikwa na mauti baada ya kufika nyumbani kwake akiwa na gari lake aina ya Nadia, lenye namba za usajili T 876 BEX wakati akitoka kwenye shughuli zake. Alivamiwa na watu wawili wanaosadikiwa kuwa majambazi.

“Wakati Mwaikusa akijiandaa kushuka katika gari lake, majambazi hao walimgongea kioo na kumwamru kushuka, lakini Profesa Mwaikusa alisita, ndipo majambazi hayo yalipomvuta kwa nguvu kisha kummiminia risasi mwilini.

“Wakati wamemaliza kumpiga risasi, alitokea mpwae Profesa Mwaikusa, Gwamaka Daudi (25), ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Ufundi VETA kwa lengo la kumnusuru, lakini ghafla majambazi yakamgeukia na kumpiga risasi mgongoni na kufariki dunia papo hapo,” alisema Kamanda Kenyela.

Baada ya kuwaua ndugu wawili, majambazi hayo yalisogea mbele kidogo na kuona kikundi cha watu ambacho walikitilia shaka kwamba wanataka kupambana nao, ndipo walipompiga risasi mtu mwingine aliyejulikana kwa jina la John Mtui (45), ambaye ni mfanyabiashara anayeishi jirani na marehemu Profesa Mwaikusa, aliyekuwa na bastola aina ya Revolver namba 87668.

Alisema Mtui alipigwa risasi kifuani na kufariki dunia hatua chache kutoka alipouawa Profesa Mwaikusa.

Alisema majambazi hayo baada ya kumuua marehemu Profesa Mwaikusa yanadaiwa kupekua mifuko ya nguo zake alizokuwa amevaa na ndani ya gari lake, ingawa mpaka sasa haikufahamika waliondoka na nini.

Kamanda Kenyela alisema majambazi hao wa
nadaiwa kufika eneo la tukio kwa kutumia usafiri wa pikipiki na baada ya tukio yalitokomea kusikojulikana. Miili yote imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Katika hatua nyingine, kada ya wanasheria nchini wameeleza kuguswa na mauaji hayo na kusema pengo hilo kamwe halizibiki.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Agustino Ramadhan, alisema taifa limepoteza mtu hodari kwenye taaluma ya sheria.

Alisema marehemu Mwaikusa alikuwa mwenyekiti wa jopo la majaji saba waliosikiliza rufaa ya kesi ya mgombea binafsi.

Aprili 11, mwaka huu, Profesa Mwaikusa alikuwa miongoni mwa magwiji wa sheria ambao waliitwa kutoa maoni yao kama marafiki wa mahakama kuhusu hukumu ya Mahakama Kuu iliyoruhusu mgombea binafsi nchini mwaka jana.

Naye Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Eliezer Feleshi, alisema yeye na ofisi yake wameshtushwa na taarifa hiyo, kwani Mwaikusa ambaye alikuwa Mhadhiri Mwandamizi wa Shule ya Sheria Tanzania katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, enzi ya uhai wake alifanya kazi kwa uadilifu mkubwa.

“Katika kesi hizo mbili Profesa alikuwa akiudhuria kama rafiki wa mahakama,siyo wakili kwahiyo umuhimu wake haukuwa kwenye taaluma yake ya uwakili bali hata rafiki wa mahakama na aina ya mauti iliyomkuta inatufundisha kwamba uhalifu hauchagui kwahiyo tujifunze kukemea uhalifu na kifo hicho kiwe ni changamoto kwa jamii kwa kuwafichua waahalifu na kuviimarisha vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ili viweze kupambana na kuzuia uhalifu”alisema Feleshi kwa sauti ya unyonge ambaye alisema marehemu alikuiwa mwalimu wake wa sheria.

Kwa upande wake, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Fakihi Jundu, alisema mhimili wa Mahakama nchini ulimfahamu marehemu kuwa ni mchapa kazi shupavu, aliyetoa hoja zilizosaidia kupata ufumbuzi wa kesi mbalimbali.

Alisema Katiba ya nchi ipo kwa ajili ya kulinda haki za binadamu na kwa msingi huo haki za binadamu ni mama wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977; na kuongeza kuwa kama kuna kifungu kinavunja haki za binadamu basi kifungu hicho ni wazi kinakiuka haki za binadamu kwa sababu haki za binadamu zilianza, Katiba ikafuata.

“Kwa uamuzi ule wa Mahakama Kuu wa kubatilisha vifungu vya ibara 21(1) (c), 39(1) (c) (b) na 69(1) (b) za Katiba ya nchi, kama kuna ibara zinapingana, ibara inayopaswa kutumika ni ile inayolinda haki za binadamu na kuhusu hukumu ya Mahakama Kuu ilikuwa na mamlaka ya kutamka ibara hizo ni batili kwani Katiba inalinda haki za binadamu na haki hizo za binadamu zilianza Katiba ikafuata hivyo haki hizo ni sheria mama.”

Naye Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,Profesa Paramaganda Kabudi alisema kifo hicho ni pigo kwani marehemu alikuwa ni mtafiti mahiri na msomi makini kwa wanafunzi na walimu wake na alikuwa mwenye vipaji vingi kwani mbali na taaluma yake ya sheria pia marehemu alikuwa mshahiri mzuri wa mashahiri aliyoyatunga kwa lugha ya kiingereza ambayo ameyaweka kwenye kitabu cha ‘Summons Poems of Tanzania’ na kwamba mara mwisho alishirikiana naye kwenye rufaa ya mgombea binafsi ambao wote walikuwa ni marafiki wa mahakama ambao waliotoa maoni yao ya kitaaluma.

Mhadhiri Mwandamizi kutoka Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengondo Mvungi, alimwelezea marehemu kuwa alikuwa mtaalamu mzuri na mwenye msimamo wa kutetea wananchi na kwamba taarifa ya kifo hicho imewaumiza.

Naye wakili wa kujitegemea, Alex Mgongolwa, alimwelezea marehemu kuwa alikuwa miongoni mwa mawakili walioendeleza sheria kwa kiwango cha juu na kutolea mfano kuwa alikuwa wakili katika kesi ya Uchaguzi Mkuu iliyofunguliwa na Jaji Mkuu mstaafu Joseph Warioba, dhidi ya aliyekuwa mgombea mwenzake wa Chama cha NCCR –Mageuzi, Steven Wassira, mwaka 1996.

“Na hoja ya rushwa kwenye uchaguzi ambayo ilitolewa kwenye kesi hiyo na Profesa Mwaikusa kwamba mgombea akitoa vitu vidogo vidogo kwa wapiga kula ni rsuhwa na hoja yake hiyo ilisababisha bunge kutunga sheria Takrima ya mwaka 1998...kwakweli nimeupokea kwa mshtuko mkubwa taarifa ya kifo marehemu ambaye alikuwa mwalimu wangu na ninaomba polisi wafanye uchunguzi wa kina ili hatimaye washtakiwa wafikishwe mahakamani”alisema Wakili Mgongolwa.

Huyo ni wakili wa pili nchini kuuawa kikatili na watu wanaotuhumiwa kuwa majambazi. Wa kwanza alikuwa Dk. Eliuther Kapinga, mwaka 2002.
Kapinga aliuawa kikatili kwa kunyongwa shingo na kupigwa nondo kichwani nyumbani kwake, Mbezi Beach.

Majambazi waliomuua Kapinga walitiwa hatiani kwa kosa la mauaji na Jaji mstaafu wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Juston Mlay, ambaye aliwahukumu adhabu ya kunyongwa kwa kamba hadi kufa.

Katika hatua nyingine, mkazi wa Ilala, Dar es Salaam, aliyetambuliwa kwa jina la Saddam (20), aliuawa jana kwa kupigwa risasi na mmiliki wa baa ya Angel Pub iliyopo Ilala, Sharif Shamba.

Chanzo cha Saddam kupigwa risasi inadaiwa ni vurugu kubwa iliyozuka katika baa hiyo baada ya kundi lililoongozwa na marehemu huyo kuvamia baa hiyo majira ya saa 9 alasiri.

Kundi la vijana wapatao 20 walifika eneo hilo ghafla na kuanza kurusha mawe pasipo sababu zilizowekwa bayana.

Baada ya kuona hali hiyo inazidi, mmiliki wa baa hiyo alitoka nje kuzuia fujo hizo lakini hakufanikiwa.

Aliamua kuchukua bastola yake na kumpiga risasi marehemu kifuani na ambayo ilitokea mgongoni.

Kamanda wa Polisi Ilala, Faustin Shilogile, aliwataja vijana wengine wawili waliokamatwa kutokana na vurugu hizo waliotambuliwa kwa majina ya Thabit Mussa (19), ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Bariki, iliyopo Mbagala na Donald Tadei (22), wote wakazi wa Ilala, Sharif Shamba ambao walijeruhiwa kwa risasi na wamelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu.
Kaimu Kamanda Kenyela amesema chanzo cha vurugu hizo ni mteja kuibiwa mali zake chooni.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi,Julai 15 mwaka 2010

WAZIRI APINGA KULIPA MILIONI 100/=

Na Happiness Katabazi

NAIBU Waziri wa Wizara ya Sayansi na Teknolojia na Mawasiliano, Dk.Maua Daftari amewasilisha rasmi hati ya nia ya kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani nchini,akipinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,iliyotolewa mwishoni mwa wiki ambayo ilimwamuru alimpe aliyekuwa mlalalamikaji Fatma Said, Sh milioni 100.7


Hati hiyo iliwasilishwa jana chini ya hati ya kiapo kupitia wakili wa Dk.Daftari, Peter Swai ambapo amedai anakusudia kukata rufaa katika mahakama hiyo ya juu nchini na kuonyesha kasoro zilizopo kwenye hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ambayo ilisomwa kwa mara ya pili Ijumaa iliyopita na Jaji Fedrica Mgaya na kwamba endapo atakubali kutekeleza amri hiyo ataathirika mno.

“Endapo nitakubali kulipa kiasi hicho cha fedha nitaathirika sana kwani hakuna ubishi mimi nimtumishi wa umma na kiwango hicho nilichoamuriwa nikilipe nikikubwa ambacho kitaniliazimu kuuza vifaa vyangu vyote ikiwemo nyumba ninayokaa na familia yangu…na mdaiwa hatapata hasara yoyote endapo rufaa yangu sitashinda hivyo mimi ni mtumishi wa umma na anwani yangu inafahamika ila huyo mdaiwa anwani yake haifahamiki”alidai Waziri Maua Daftari.

Aidha aliomba mahakama ya rufaa itoe amri ya kusitisha utekelezwaji wa hukumu ya Mahakama Kuu kwani endapo uamuzi huo utabaki kama ulivyo, ataathirika zaidi nakuongeza kuwa anaomba apatiwe nakala ya hukumu hiyo ili aweze kuisoma na kuandaa rufaa yake ambayo ataiwasilisha mahakamani hapo ndani ya kipindi kifupi kwani anaamini hukumu ya mahakama kuu haijamtendea haki na imejaa makosa.

Ijumaa iliyopita Jaji Mgaya alisoma hukumu hiyo kwa mara ya pili, mara ya kwanza ilisomwa na Jaji Laurian Kalegeya ambapo alimwamuru Dk.Daftari amlipe Fatma Salim, kiasi hicho cha fedha baada ya kubaini alivunja mkataba na mlalamikaji huyo. Jaji Fedrica, alisema amefikia uamuzi wa kutoa amri ya kumtaka mdaiwa (Dk. Daftari), alipe kiasi hicho cha fedha mdaiwa badala ya sh milioni 410, kiasi ambacho mdaiwa aliomba amlipe, baada ya kubaini madai mengine katika hati ya madai, Dk. Daftari ameshindwa kupeleka ushahidi wa kuthibitisha madai hayo.

Jaji Mgaya, alisema dai la sh milioni 1,760 ni dai ambalo limeweza kuthibitishwa kwa vielelezo kwa sababu mdaiwa na mlalamikaji waliandikishiana kisheria na ndiyo maana ameamuru mdaiwa amlipe kiasi hicho.Matukio hayo, yalitendeka kati ya mwaka 1994-1996 na kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo mwaka 1999 na mlalamikaji dhidi ya naibu waziri huyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Julai 14 mwaka 2010

ALEX STEWART ILIANZA KAZI BILA USAJILI-SHAHIDI

Na Happiness Katabazi

MSAJILI Msaidizi wa Makampuni toka Wakala wa Usajili wa Makampuni (BRELA), Frank Kajusi (37) ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kwamba kampuni ya Alex Stewart (Assayers)Govement Bussiness Corporation ilianza kufanya biashara bila kupata hati ya usajili toka BRELA.


Kajusi ni shahidi wa 10 wa upande wa Jamhuri katika kesi ya matumizi mabaya ya ofisi ya umma na kuisababishia serikali hasara ya sh bilioni 11.7 inayomkabili aliyekuwa Waziri wa Fedha, Basil Mramba na wenzake wawili.

Kajusi alitoa maelezo hayo wakati akiongozwa kutoa ushahidi na wakili mwandamizi wa serikali, Fredrick Manyanda. alidai kisheria kampuni yoyote ya nje inapokuja nchini kabla ya kuanza kufanya biashara inatakiwa iwe imepata hati ya kufanya biashara kutoka BRELA, lakini kampuni hiyo haikuwa imetimiza sharti hilo.

Hata hivyo, wakili wa utetezi, Hurbet Nyange, alipombana kwa maswali shahidi huyo kwamba maelezo hayo ndiyo ushahidi wake ambao anaiomba mahakama iupokee shahidi huo alidai kuwa si wake, hali iliyofanya jopo la Mahakimu Wakazi linaloongozwa na John Utamwa, Sam Rumanyika na Saul Kinemela kuingilia kati na kumkumbusha shahidi huyo kuwa awali aliiambia mahakama kampuni hiyo ilianza biashara bila hati ya BRELA na wakati huo anatoa maelezo tofauti.

Hali hiyo ilimfanya shahidi huyo arudie kueleza kuwa kampuni hiyo ilianza biashara bila kupata hati ya BRELA na kuongeza kuwa haoni tatizo kwa BoT kuingia mkataba na kampuni hiyo ya Alex Stewart bila ya kampuni hiyo kuanza kufanyabiashara.

Hakimu Mkazi Saul Kinemela aliahirisha kesi hiyo hadi leo ambapo shahidi wa 11 anatarajiwa kuja kuanza kutoa ushahidi wake.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne, Julai 13 mwaka 2010

SERIKALI ISIFUNGUE KESI KWA KUKURUPUKA

Na Happiness Katabazi

JULAI 2, mwaka huu, Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Stewart Sanga alimwachia huru ofisa ugavi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Elias Mziray, na maofisa wenzake wanne waliokuwa wakikabiliwa na makosa matatu ya kula njama ya wizi wa sh milioni 119.


Mbali na Mziray, washitakiwa wengine ni Ofisa Manunuzi, David Kakoti, Gene Moshi na Mhasibu, Joseph Rweyemamu, ambao wote ni watumishi wa wizara hiyo, ambao walikuwa wakitetewa na wakili wa kujitegemea, Hudson Ndusyepo.

Uamuzi huo, ulitolewa siku hiyo na Hakimu Mkazi Sanga, bila kumung'unya maneno alisema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wa nane na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na upande wa Jamhuri, ameona washitakiwa hawana kesi ya kujibu kwasababu amebaini kwamba upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha kesi hiyo, kitendo ambacho kilimpa msukumo kuifuta kesi hiyo ya jinai namba 117 ya mwaka 2009.

Hakimu Sanga, akichambua shitaka la kwanza ambalo ni la kula njama, alisema Jamhuri ilishindwa kuthibitisha shitaka hilo kwa sababu kisheria kosa la kula njama ni lazima washitakiwa wote wakubaliane kutenda kosa ambalo limekatazwa kisheria lakini katika kesi hiyo, mashahidi wote wa Jamhuri wakati wakitoa ushahidi wao waliieleza mahakama kuwa washitakiwa walitenda kazi yao ya kutoa tangazo la zabuni na kumtafuta mzabuni, kumlipa fedha mzabuni kwa kufuata sheria hivyo mahakama hiyo haijaona kama washitakiwa walitenda kosa.

Akilichambua shitaka la pili ambalo ni wizi, alisema mashahidi wote wameshindwa kuthibitisha shitaka hilo, kwani kumbukumbu za kibenki na hundi ambazo zilitolewa kama vielelezo vinaonyesha wazi mzabuni alilipwa kwenye akaunti yake na hakuna shahidi hata mmoja aliyeieleza mahakama washitakiwa hao walinufaika binafsi na fedha hizo na kuongeza kuwa ni wazi Jamhuri, ilifahamu mapema fedha aliyelipwa ni nani kwani ni Jamhuri hiyo hiyo ndiyo iliyopeleka ‘Bank Statement’ na hundi mahakamani hapo ili zitumike kama vielelezo, ambapo vielelezo hivyo viwili vyote vinaonyesha jina la mzabuni ambaye ndiye aliyelipwa fedha hizo.

Hakimu Sanga akichambua shitaka la tatu, ambalo ni la kusababisha hasara, alisema pia Jamhuri imeshindwa kulithibitisha, kwani washitakiwa wote ni watumishi wa umma na walifanya kazi kwa nafasi zao, hivyo walifuata taratibu zilizokuwepo tena kwa kufuata utaratibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Hata hivyo ambaye ni miongoni mwa mahakimu vijana mahakamani hapo, alikemea vikali mtindo wa wizara kuwaruhusu watumishi wa umma wasio na taaluma ya kuandaa masuala ya kitaaluma, kwani kufanya hivyo ndiko kuna kosababisha wizara na serikali kwa ujumla kupata hasara na kuongeza kuwa washitakiwa hao hawakupaswa kutuhumiwa kwa kosa la wizi.

Wakati Mhasibu Mkuu wa Wizara, ambaye alikuwa shahidi wa nane, naye aliidhinisha malipo kwa mzabuni huyo bila kuusoma mkataba huo.

Alisema hao ndio walipaswa kuwajibishwa kwanza kwa sababu ndio walioiingiza wizara hiyo kwenye mkataba huo wenye utata.

Mwaka jana washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mbwembwe na upande wa Jamhuri ukidai kuwa mwaka 2005 mpaka sasa Kampuni ya Ostergad & Invest Ltd iliyoshinda zabuni ya kuiuzia wizara hiyo pikipiki 25 na kulipwa sh 119, 530,000, hazijaletwa huku wakidai mmiliki wake Yahaya Mhina alifariki dunia.

Pia wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Kyando alidai kuwa Juni 17, 2005 katika wizara hiyo, washtakiwa wakiwa ni watumishi wa umma, walishindwa kutekeleza majukumu yao na kuisababishia serikali kupata hasara ya kiasi hicho cha fedha.

Katika hatua nyingine, Fukuto la Jamii linawakumbusha wasomaji wake kuwa Juni 16 mwaka huu, mahakama hiyo ilimfutia kesi Naibu Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Dk. Ismail Kelly Alloo, baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuwasilisha mahakamani hapo hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea kumshitaki mshitakiwa huyo.

Itakumbukwa Alloo naye alifikishwa kwa mbembwe na makachero na wanasheria wa Takukuru mahakamani hapo Novemba mwaka jana, mbele ya Hakimu Mkazi Paul Kimicha na wakili wa taasisi hiyo Kasuni Nkya alidai kuwa Mei 2, mwaka 2005, mshitakiwa anadaiwa kutenda kosa la matumizi mabaya ya ofisi ya umma kwa kuruhusu mauzo ya magogo kinyume cha sheria.

Shitaka la pili, ni kuwa Machi 17 mwaka 2005 katika ofisi za makao makuu ya Takukuru jijini Dar es Salaam, wakati wa uchunguzi wa matumizi mabaya ya rushwa, mshitakiwa alitoa taarifa za uongo kuhusu tangazo la mazao ya misitu mali ya Kampuni ya Aqeel Traders Ltd. Pamoja na kwamba upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo ulikuwa umekamilika, kesi hiyo ilikuwa ikitajwa mahakamani hapo hadi mshitakiwa alipofutiwa kesi hiyo na DPP.

Fukuto la Jamii linapenda kumpongeza Hakimu Mkazi Stewart Sanga kwa ujasiri wake wa kuweza kufuata sheria na haki kama ambavyo taaluma yake inavyomtaka katika kuifuta kesi hiyo ambayo ni miongoni mwa kesi zilizopewa jina la ‘kesi za ufisadi’, ambazo kwa sisi waandishi wa habari za mahakamani tumeshuhudia kesi hizo zikifunguliwa mahakamani hapo kwa mbwembwe nyingi na kufuatiliwa kwa karibu na mashushushu ambao walikuwa wakihudhuria kesi hizo kwa mitindo mbalimbali, hali ambayo baadhi ya mahakimu wengine wamekuwa wakijikuta wakiogopa kutoa haki katika baadhi ya aina hiyo ya kesi kwa kigezo kuwa kesi hizo zinafuatiliwa na ‘manusanusa’.

Fukuto la Jamii linampongeza Hakimu Sanga kwani yote hayo hakuyajali, alichozingatia ni sheria na maadili ya kazi yake na si kisingizo cha maslahi ya taifa, kisingizio cha sasa hivi taifa lipo kwenye mapambano dhidi ya wabadhirifu wa fedha za umma.

Alichozingatia ni matakwa ya sheria na hivyo ndivyo tunataka mahakimu na majaji wetu wazingatie hilo kama taaluma yao inavyowataka na si vinginevyo.

Tunaamini kabisa wachunguzi wa TAKUKURU waliopeleleza kesi hiyo walitumia rasilimali na muda wa walipa kodi kupeleleza kesi hiyo, hivyo nasisitiza wananchi tuna haki ya kuwalaumu na kuhoji ni kwanini wameshindwa kufanya vizuri katika kesi hii licha ya kwa mujibu wa dhana ya sheria, kesi inapofunguliwa mahakamani kuna kushinda kesi au kushindwa.

Kwa muktadha huo hapo juu, Fukuto la Jamii linahoji umakini na weledi wa wachunguzi toka TAKUKURU ambao walipeleleza kesi Na. 117/2010 uko wapi?

Hivi hawa wapelelezi wa kesi na mawakili wa serikali wanafahamu kwamba ukosefu wao wa umakini katika kupeleleza kesi au kuendesha kesi ambapo mwisho wa siku wanamfungulia kesi mtu ambaye hakustahili kufunguliwa kesi.

Wananchi tujiulize hivi mchunguzi aliyefundwa chuoni, anaweza kufanya upelelezi wa kesi kama hiyo ambayo matokeo yake tumeona wachunguzi hao walikusanya vielelezo ambavyo ni hundi na bank statements ambazo hazioani na sheria waliyoitumia kuwashitaki washitakiwa hao?

Kwa mujibu wa kesi hiyo, upande wa Jamhuri ulileta bank Stament na hundi kama vielelezo ili viweze kusaidia kesi yao kushinda, wakati vielelezo hivyo vimeonyesha wazi wizara hiyo ilimlipa kiasi hicho cha fedha mzabuni na wakati huo hati ya mashitaka inadai washitakiwa walikula njama, waliiba na kusababisha hasara ya sh milioni119.

Hivi tuiulize Takukuru na ofisi ya DPP iliamua kuifungua kesi hiyo mahakamani kwa sababu gani?

Je, walifungua kweli kwakutaka kuona haki inatendeka au waliamua kuwafungulia kesi hiyo kwa ajili ya mashinikizo ya wanasiasa?

Au taasisi hizo zilihakikishiwa na wazandiki na wambeya kwamba wafungue kesi hiyo haraka, mbele ya safari wazandiki hao wangezipelekea taasisi hizo ushahidi mzito ambao ungeweza kuwabana washtakiwa hao?

Au Watanzania tuziulize taasisi hizo mbili, shitaka la kusababisha hasara linawababaisha hawa wapelelezi wetu na waendesha mashitaka wetu au shitaka hilo limekuwa ni fasheni sasa ya kuwaumiza watu ambao hawana hatia ila tu taasisi hizo zinaamua kuwafungulia kesi wananchi wenzetu kwa ajili ya majungu au kujipatia umaarufu wa kipuuzi? Fukuto la Jamii linapata wakati mgumu kuelewa hilo.

Watanzania huu ni mzaha mbaya katika matumizi ya rasilimali za walipa kodi na muda wa mahakama kusikiliza kesi zisizokuwa na kichwa wala miguu kama hiyo iliyoandaliwa ovyo ovyo na upande wa Jamhuri ambapo mwisho wa siku Rais Jakaya Kikwete akiwa nyumbani kwa Baba wa Taifa-Butiama mwaka jana, aliwahutubia wana CCM na wananchi kwa ujumla akiwaeleza wananchi hao kwamba mtu akiwauliza wananchi serikali ya awamu ya nne imefanya nini tangu iingine madarakani, wamjibu serikali yake imeweza kufungua kesi za ufisadi mahakamani.

Sasa kama rais wa nchi anatamba kwamba uongozi wake umeweza kuimarisha utawala wa sheria ikiwa ni pamoja na kufungua kesi za ufisadi mahakamani zinazowahusu vigogo na matokeo yake baadhi ya kesi hizo kumbe zimeandaliwa ovyo ovyo na wapelelezi na waendesha mashitaka, ina leta picha gani kwa umma?

Aiingii akilini mchunguzi na mwanasheria makini na anayethamini utu wake na utu wa binadamu mwenzake kukubali kupeleleza na kufungua kesi hiyo kwa kigezo cha kuwa na vielelezo kama hivyo ambayo mwisho wa siku serikali yetu imejikuta imepoteza fedha za walipa kodi kwa ajili ya kuwawezesha wachunguzi.

Na mahakama imepoteza muda wa kusikiliza kesi kama hiyo na mwisho wa serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete imeendelea kusukumiwa kwa chini chini zigo la tuhuma kuwa ni serikali ya kionevu, kwani imekuwa ikiwabambikia kesi baadhi ya maofisa wa serikali kwa uonevu na visasi ili serikali ijipatie umaarufu wa kwamba inapambana na ufisadi.

Na siyo siri tuhuma hiyo kila kukicha imekuwa ikiwahusisha baadhi ya viongozi wakuu wa nchi kwamba kuna baadhi ya washtakiwa wanafikishwa mahakamani kwa kukomolewa kwa sababu wakati wapo serikalini walikuwa mabingwa wa kupora mahawala wa vigogo wenzao.
Tuhuma hizi zinazoelekezwa kwa serikali ya awamu ya nne ziwe na ukweli ndani yake au la, Fukuto la Jamii linasema tuhuma hiyo inaipaka matope, kwani si nzuri na inaamsha chuki baina ya ndugu, jamaa wa washitakiwa waliofunguliwa kesi na wale walioshinda kesi hizo dhidi ya serikali ya awamu ya nne.

Sasa ili serikali kujiondoa katika tuhuma hiyo, ione wakati umefika wa kupeleka muswada bungeni utakaoweza kuwabana wapelelezi wanaopeleleza kesi za jinai bila umakini na ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ambayo ndiyo yenye dhamana ya kutoa kibali cha kesi za jinai kufunguliwa mahakamani ambapo mwisho wa siku serikali inashindwa vibaya kesi hizo.

Naamini hilo likifanikiwa hawa wapelelezi na ofisi ya DPP ambao wamepewa dhamana hizo watakuwa makini na kamwe hawatakubali kufungua kesi mahakamani kwa mashinikizo ya wanasiasa ili wakubwa wao wazione taasisi hizo zinafanya kazi kwa kupeleka baadhi mahakamani kumbe ni upuuzi mtupu wanaoupeleka mahakamani ambao haulisaidii taifa badala yake unaliumiza taifa letu na washitakiwa na ndugu zao.

Hakuna ubishi kwamba kila kukicha wananchi mbalimbali akiwemo Mkurugenzi wa Takukuru, Dk. Edward Hosea ambaye kwa zaidi ya mara mbili amenukuliwa kwenye vyombo vya habari akiilalamikia mahakama kwamba inachelewesha kumalizika na wala mahakama hiyo haitoi kipaumbele kwa kushughulikia haraka kesi kubwa ambazo ni za kifisadi na kwamba DPP - Eliezer Feleshi, amekalia kesi zaidi ya 60 za ufisadi ambazo taasisi yake ilishakamilisha upelelezi na kuzikabidhi ofisini kwa DPP.

Lakini cha kushangaza hadi sasa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshatolea uamuzi kesi tatu ambazo aliziita kesi kubwa ambazo zimepelelezwa na ofisi yake lakini hadi sasa hatujamsikia kiongozi huyo akijitokeza hadharani kuupongeza mhimili wa mahakama kwa kuweza kuzimaliza kesi hizo ndani ya kipindi kifupi ukilinganisha na kesi nyingine za walalahoi ambazo zinachukua zaidi ya miaka minne na kuendelea mahakamani.

Mfano, kesi ya matumizi mabaya ya ofisi za umma iliyokuwa ikimkabili aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu, Amatus Liyumba, ambayo ilifunguliwa mahakamani hapo Januari 27 mwaka jana na ikamalizika Mei 24 mwaka huu.

Kesi nyingine ni Na. 117/2009 iliyomalizika Julai 2 mwaka huu, kesi iliyokuwa ikimkabili Naibu Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, Dk. Ismail Kelly Alloo ambayo ilifunguliwa Novemba mwaka jana na ikamalizika Juni mwaka huu.

Siku mbili baadaye baada ya Liyumba aliyefungwa miaka miwili jela, tulimsikia Dk. Hosea kupitia vyombo vya habari akishangilia hukumu hiyo na kujigamba kwamba hukumu hiyo ni matunda ya kazi nzuri ya upelelezi iliyofanywa na taasisi yake.

Lakini chakushangaza, Dk. Hosea hatujamsikia tena akichomoza kwenye vyombo vya habari akiwaeleza wananchi kuhusu uamuzi wa Hakimu Sanga uliowaachiria huru maofisa wanne wa Wizara ya Maliasili wala uamuzi wa DPP wa kumfutia kesi Dk. Alloo.

Tumuulize Dk. Hosea ameamua kukaa kimya kwa sababu upelelezi uliofanywa na taasisi yake umeshindwa kufurukuta kwenye kesi hizo mbili ambayo moja imefutwa na mahakama baada ya kubaini ushahidi ulioletwa na upande wa mashitaka ni dhahifu na kesi nyingine ilifutwa na mahakama hiyo baada ya DPP-Feleshi kuwasilisha hati ya kuondoa kesi hiyo kwasababu hana haja kuendelea na kesi hiyo?

Namshauri Dk. Hosea asijitokeze kwenye vyombo vya habari kushangilia kesi wanazoshinda tu , awe mwepesi pia kujitokeza na kueleza umma pindi baadhi ya kesi zake zinaposhindwa kufurukuta mahakamani ili umma ujue ni kwanini ushahidi uliokusanywa na vijana wake ulikuwa ni dhahifu, kwasababu binafsi naamini kiongozi huyo ameishajiwekea utamaduni wa kwenda kwenye vyombo vya habari kutoa malalamiko yake dhidi ya taasisi nyingine ambazo anaamini zinamkwaza kiutendaji.Naamini huo ndio uwajibikaji wa kweli wa kukubali kushindwa, kushinda na kukosolewa.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili,Julai 11 mwaka 2010

WAZIRI MAUA AAMULIWA KULIPA SH MIL.100

Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemwamuru Naibu Waziri wa Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, Dk. Maua Daftari, kumlipa mfanyabiashara Fatma Salim, sh milioni 100.7 baada ya kubaini alivunja mkataba na mdaiwa huyo.


Hukumu hiyo, jana ilikuwa ni mara ya pili ikiwa chini ya Jaji Fedrica Mgaya, ambapo mwaka juzi hukumu hiyo, ilisomwa na jaji Laurian Kalegeya ambaye kwa sasa ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.

Jaji Fedrica, alisema amefikia uamuzi wa kutoa amri ya kumtaka mdaiwa (Dk. Daftari), alipe kiasi hicho cha fedha mdaiwa badala ya sh milioni 410, kiasi ambacho mdaiwa aliomba amlipe, baada ya kubaini madai mengine katika hati ya madai, Dk. Daftari ameshindwa kupeka ushahidi wa kuthibitisha madai hayo.

Jaji Mgaya, alisema dai la sh milioni 1,760 ni dai ambalo limeweza kuthibitishwa kwa vielelezo kwa sababu mdaiwa na mlalamikaji waliandikishiana kisheria na ndiyo maana ameamuru mdaiwa amlipe kiasi hicho.

Matukio hayo, yalitendeka kati ya mwaka 1994-1996 na kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo mwaka 1999 na wakili wa Dk. Daftari Peter Swai.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi,Julai 10 mwaka 2010

MTAMBALIKE KUMVAA ROSTAM IGUNGA

Na Happiness Katabazi

MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Deusdedit Mtambalike, ametangaza rasmi nia ya kuwania ubunge katika Jimbo la Igunga ambalo kwa sasa linaongozwa na Rostam Aziz.


Akizungumza na Tanzania Daima juzi jijini Dar es Salaam, Mtambalike alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuona jimbo hilo halipigi hatua za kimaendeleo.

Mtambalike ambaye ameishawahi kuwa mkuu wa wilaya katika Wilaya ya Muleba, Igunga, Ngara, Tunduru na Ludewa, alisema nia yake ni kutaka kuleta maendeleo katika jimbo hilo kwani Wilaya ya Igunga anaifahamu vema.

“Nia yangu ni njema nataka kuleta maendeleo kwenye Jimbo la Igunga kwani si siri wakulima wa pamba, tumbaku, na wafugaji hawana mtu wa kuwasemea wala kuwapigania haki zao,” alisema

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Julai 8 mwaka 2010

UPELELEZI KESI YA WARAKA WA UCHOCHEZI WAKAMILIKA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi kusamba na kimiliki waraka wa uchochezi dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa Democratic Party(DP) jana ulieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kwamba upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.


Mbele ya Hakimu Mkazi Michael Mteite, Mwendesha mashtaka Inspenkta wa Polisi, Francis Mboya alieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na anaiomba mahakama hiyo ipange tarehe ya upande wa mashtaka kuja kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa.
Hakimu Mkazi Mteite alikubaliana na maelezo hayo na akaairisha kesi hiyo hadi Julai 27 mwaka, kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali ya upande wa Jamhuri.

Kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo Juni 21 mwaka huu, na wakili wa Serikali Angel Chacha aliyekuwa akisaidiwa na Inspekta Mboya alidai kuwa Mtikila alifanya makosa hayo ya uchochezi ambayo ni kinyume cha kifungu cha 32(1)(c) cha Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.

Chacha alidai kuwa shtaka la kwanza ni kuwa mnamo Novemba mosi mwaka 2009-Aprili 17 mwaka huu, ndani ya jiji akiwa na nia ya uchochezi Mtikila alisambaza kwa umma waraka uliochapishwa ambao una kichwa cha habari kisemacho: ‘Kikwete kuangamiza ukristo, Wakristo waungane upesi wamuweke Mkristo Ikulu’ huku akijua maneno hayo ni ya kichochezi.

Alidai shtaka la pili ni kwamba Aprili 16, mwaka huu, huko nyumbani kwake Mikocheni bila kibali alikuwa akimiliki waraka huo wa kichochezi ambao ulikuwa na maneno hayo.
Kwa upande wake, Mtikila alikana mashtaka yote na wakili huyo wa serikali aliiambia mahakama kuwa hawana pingamizi na dhamana na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hiyo ni mara ya 41 sasa serikali inamfungulia kesi ya kutoa maneno ya uchochezi na kesi nyingi ameshinda isipokuwa kesi moja ya uchochezi iliyokuwa imefunguliwa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni mbele ya Hakimu Gabriel Mirumbe mwishoni mwa miaka ya 1990, ambapo Mtikila alidaiwa kutoa maneno ya uchochezi alipodai CCM ilimuua aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Horace Kolimba, na ndipo mahakama hiyo ya wilaya ilipomfunga jela mwaka mmoja na alitumikia kifungo hicho katika gereza la Ukonga.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Julai 7 mwaka 2010

MAWAKILI ZINGATIENI USHAURI WA JAJI JUNDU


Na Happiness Katabazi

JUNI 24 mwaka huu, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Fakihi Jundu, alisema hadi kufikia siku hiyo Tanzania ina jumla ya mawakili wa kujitegemea 1,322 idadi ambayo alisema ni ndogo ukilinganisha na nchi jirani za Jumuiya ya Afrika Mashariki.


Jaji Jundu, aliyasema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika ofisini kwake, ikiwa ni muda mfupi tu baada ya Jaji Mkuu Agustino Ramadhani kufunga sherehe za kuwakubali na kuwasajili mawakili wapya 128.

Alisema mahitaji ya huduma ya mawakili, inazidi kuongezeka lakini idadi ya mawakili wa kujitegemea hapa nchini bado haikidhi mahitaji ukilinganisha na nchi kama ya Kenya ambayo ina zaidi ya mawakili 3,000.

”Nchi yetu ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na siku chache zijazo, itafungua milango ya soko la ajira kwa ajili ya raia wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo , chini ya Itifaki ya Soko la Pamoja.

Kutokana na hali hiyo, mawakili kutoka nchi hizo watakuwa wakiruhusiwa kutoa huduma za kisheria katika mahakama za nchi jirani, hivyo idadi ya mawakili isipoongezeka, ni wazi Tanzania tutashindwa kufurukuta,”anasema Jaji Jandu.

”Hivyo, sisi kama mhimili wa mahakama nchini tumejipanga kuhakikisha tunaendelea kuapisha mawakili wengi zaidi ili taifa liwe na mawakili wengi ambao wataenda kutoa huduma hii kwa wananchi,” anasema Jaji Jandu.

Jaji Jundu, alisema idadi ya mawakili wapya 128 imegawanyika katika mafungu mawili, kundi la kwanza ni waombaji 53 waliohitimu shahada ya sheria na baadaye kuhitimu katika chuo cha Wanasheria kwa Vitendo.

Anasema kundi hilo ni la kihistoria kwa vile hii ni mara ya kwanza kwa wanasheria wanaohitimu kutoka chuo hicho kukubaliwa kuwa mawakili kwa mujibu wa kifungu cha 12(3) cha Sheria ya Chuo hicho ya mwaka 2007.

Anasema kundi la pili, lina waombaji 75 ambao walipitia usaili wa Baraza la Elimu ya Sheria.

Alisema hapa nchini, mawakili wa kujitegemea wengi ofisi zao zina mawakili wasiozidi watatu au wakili mmoja hali inayosababisha baadhi ya wateja kusita kuwapatia kazi za kuwawakilisha mahakamani.

Hata hivyo, aliwashauri waombaji wa usajili wa uwakili ambao bado majina yao hayajapitishwa kuwa mawakili, wawasiliane na Baraza la Elimu la Sheria ambalo yeye ni mwenyekiti wake.

Kutokana maelezo hayo, Fukuto la Jamii linapenda kuunga mkono ushauri huo, uliotolewa na Jaji Kiongozi kwani safu hii inaona ushauri huo umejaa uzalendo endapo utafuatwa na wadau husika.

Itakumbukwa kwamba, Alhamisi wiki hii Tanzania ilifungua milango ya soko la ajira kwa ajili ya raia wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), chini ya Itifaki ya Soko la Pamoja iliyoanza kutekelezwa rasmi. Pia Fukuto la Jamii linapongeza utekelezaji huo.

Kwa sisi waandishi wa habari za mahakama nchini, tumeshuhudi kesi mbalimbali zikiahirishwa, wananchi wakikosa mawakili wa kuwawakilisha mahakamani kwa madai kuwa mawakili wao wana kesi katika mahakama zingine, wanaumwa au wamesafiri, hivyo inakuwa sababu moja wapo mahakama kuahirisha kesi kwa sababu ambayo nayo naweza kusema inachangia kesi kuchukua muda mrefu mahakamani bila kumalizika.

Kwa muda mrefu, wananchi wengi na baadhi ya viongozi wa serikali, wamekuwa hawaoni uhaba wa mawakili kama unachangia kesi kuchelewa mahakamani na badala yake wamekuwa wakiitupia lawama kila kukicha ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), ambayo kwa sasa inaongozwa na Eliezer Feleshi.

Ni rai yangu kuwa mawakili wa kujitegemea nchini, waanze kujitazama upya na kuufanyia kazi ushauri huu uliotolewa na Jaji Jundu kwani tutake tusitake viongozi wa mataifa ya nchi za EAC ndiyo wameisharidhia.

Hakuna ubishi kwamba idadi ya mawakili hapa nchini ni ndogo, lakini licha ya idadi hiyo, kuwa ndogo bado mawakili wengi wamejenga kasumba ya kufungua ofisi mijini zaidi kulikoa mikoani ambako kuna wananchi wenzetu wanateseka kwa kukosa huduma hiyo muhimu.

Hivyo, wananchi wengi wanapoteza haki zao au wanakubali kwa shingo upande haki zao, zipotee kwa sababu ya kukosa mawakili wa kuwawakilisha mahakamani au mawakili wa kuwapatia msaada wa kisheria.

Ikumbukwe mawakili walipokuwa vyuoni kusomea fani ya sheria walifundishwa na walimu hawa waende wakatende haki na kulisaidia taifa kupitia taaluma yao hivyo tutaona si burasa kwa mawakili wetu kuamua kufungua ofisi mijini tu eti kwa kigezo kwamba mijini ndipo kuna biashara zaidi kuliko kwenda kufungua maofisi katika wilaya ambayo mikoa yake bado haijapiga hatua za kimaendeleo au kupandishwa hadhi ya kuwa jiji.

Inasikitisha kuona vyuo vikuu vyetu kila mwaka wahitimu wa fani ya sheria idadi yake inazidi kuongezeka lakini kila siku tunasikia baadhi ya viongozi wa mhimili wa mahakama wakitoa taarifa kwa umma kwamba mawakili wengi hawataki kwenda kufanya kazi mikoani.

Na pia inasikitisha kama siyo kukatisha tamaa kuona idadi kubwa ya waombaji wa kusajiliwa kuwa mawakili kwenye Baraza la Elimu la Sheria ,maombi yao yanashughulikiwa kwa idadi ndogo.

Pia inastaajabisha kusikia malalamiko kutoka kwa baadhi ya waombaji wa usaili wa uwakili kwamba wamewasilisha maombi yao muda mrefu lakini cha kushangaza kuna baadhi ya waombaji wanaowasilisha maombi yao kwenye Baraza la Elimu la Sheria wakiwa wamechelewa lakini mwisho wa siku waombaji hao waliochelewa ndiyo wanakuwa wakanza kupewa leseni za uwakili.

Ama kwa hakika malalamiko hayo hayaleti picha nzuri kwenye baraza hilo na mhimili wa mahakama na kama yana ukweli wowote tunamuomba Jaji Jundu ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza hilo, ayafanyie kazi ili mwisho wa siku haki ipatikane kwa wote na kwa wakati.

Fukuto la Jamii, linamaliza kwa kuwashauri mawakili wa hapa nchini kuacha ubinafsi wa kufungua ofisi zinazokuwa na mawakili wa wiwili au mmoja, badala yake watanue ofisi zao ambazo zitakuwa namawakili wengi zaidi(Partners) , ili wakili mmoja siku hayupo wakili mwingine wa kampuni hiyo hiyo anashika kesi ya mteja husika na kuendelea nayo mahakamani, naamini wakifanya hayo wanaweza kushindana katika Itifaki ya Soko la Pamoja.

Kwani wananchi wa nchi za EAC wataweza kuja kuwakodi kuendesha kesi zao katika mahakama toka nchi za jumuiya zao bila ofisi zao kuteteleka kwani wakili mmoja akienda kuhudhuria kesi ya mteja mmoja, mfano nchini Kenya, ofisi yake ya uwakili hapa nchini kesi nyingine alizokuwa akizishikilia wakili huyo, zitaweza kuendeshwa na wakili mwingine katika ofisi hiyo ambayo itakuwa na mawakili wengi, hivyo kipato katika kampuni hiyo kitaongezeka.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.


Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili la Julai 4 mwaka 2010

KESI KUBWA YA UFISADI YAFUTWA

•HAKIMU AITAKA SERIKALI KUWA MAKINI NA MIKATABA

Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana iliwaachia huru ofisa ugavi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Elias Mziray, na maofisa wenzake wanne waliokuwa wakikabiliwa na makosa matatu ya kula njama ya wizi wa sh milioni 119.


Mahakama hiyo, ilifikia uwamuzi huo baada ya kuwaona washtakiwa wote kwa pamoja hawana kesi ya kujibu.

Mbali na Mziray, washtakiwa wengine ni Ofisa Manunuzi, David Kakoti, Gene Moshi na Mhasibu Joseph Rweyemamu ambao wote ni watumishi wa wizara hiyo, ambao walikuwa wakitetewa na wakili wa kujitegemea Hudson Ndusyepo.

Uamuzi huo, ulitolewa jana na Hakimu Mkazi, Stewart Sanga, ambaye bila kumung'unya maneno alisema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi nane na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka, amebaini kwamba upande wa Jamhuri umeshindwa kuthibitisha kesi hiyo, kitendo ambacho kinampa msukumo kuifuta kesi hiyo.

Hakimu Sanga, akichambua shtaka la kwanza ambalo ni la kula njama, alisema Jamhuri umeshindwa kuthibitisha shtaka hilo kwa sababu kisheria kosa la kula njama ni lazima washtakiwa wote wakubaliane kutenda, kosa ambalo limekatazwa kisheria lakini katika kesi hiyo, mashahidi wote wa Jamhuri wakati wakitoa ushahidi wao waliambia mahakama kuwa washtakiwa walitenda kazi yao ya kutoa tangazo la zabuni na kumtafuta zabuni, kumlipa fedha mzabuni kwa kufuata sheria hivyo mahakama hiyo haijaona kama washtakiwa walitenda kosa.

Akilichambua shtaka la pili ambalo ni wizi, alisema mashahidi wote wameshindwa kuthibitisha shtaka hilo, kwani kumbukubu za kibenki na hundi ambazo zilitolewa kama vielelezo vinaonyesha wazi mzabuni alilipwa kwenye akaunti yake na hakuna shahidi hata mmoja aliyeieleza mahakama washtakiwa hao walinufaika binafsi na fedha hizo na kuongeza kuwa ni wazi Jamhuri, ilifahamu mapema fedha aliyelipwa ni nani kwani ni Jamhuri hiyo hiyo ndiyo iliyopeleka ‘Bank Statement’ na hundi kama vielelezo ambavyo vyote vinaonyesha jina la mzabuni aliyelipwa fedha hizo.

Hakimu Sanga, akichambua shtaka la tatu ambalo ni la kusababisha hasara, alisema pia Jamhuri imeshindwa kuthibitisha, kwani washtakiwa wote ni watumishi wa umma na walifanya kazi kwa nafasi zao, hivyo walifuata taratibu zilizokuwepo tena kwa kufuata utaratibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Hata hivyo, alikemea mtindo wa wizara kuwaruhusu watumishi wa umma wasio na taaluma ya kuandaa vitu vya kitaaluma, kama mikataba kufanya hivyo ndiko kunakosababisha wizara na serikali kwa ujumla kupata hasara.

Wakati Mhasibu Mkuu wa Wizara, ambaye alikuwa shahidi wa nane, naye aliidhinisha malipo kwa mzabuni huyo bila kuusoma mkataba huo.

Alidai hao, ndiyo walipaswa kuwajibishwa kwanza kwa sababu ndiyo waliyoingiza wizara hiyo kwenye mkataba wenye utata.

“Mtu wa kwanza kulaumiwa kwa kuisababishia wizara hiyo hasara ni Katibu Mkuu ambaye kwa uzembe wake alisaini mkataba bila kuusoma na kujua kuna nini ndani yake, matokeo yake akaidhinisha mzabuni alipwe na mwingine ni Mhasibu Mkuu wa wizara hiyo kwa kupitisha malipo hayo hivyo washtakiwa hao hawawezi kuitwa wezi kwa sababu fedha zinaonekana zilikwenda sehemu husika,” alisema Hakimu Sanga.

Mwaka jana, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo kwa mbwembwe na upande wa Jamhuri ukidai kuwa mwaka 2005 mpaka sasa Kampuni ya Ostergaad & Invest Ltd iliyoshinda zabuni ya kuiuzia wizara hiyo pikipiki 25 na kulipwa sh 119, 530,000, hazijaleta huku wakidai mmiliki wake Yahaya Mhina alifariki dunia.

Pia Jamhuri ilidai kuwa Juni 17, 2005 katika wizara hiyo,washtakiwa wakiwa ni watumishi wa umma, walishindwa kutekeleza majukumu yao na kuisababishia serikali kupata ya hasara ya kiasi hicho cha fedha.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Julai 3 mwaka 2010

ASASI ZATAKIWA KUJIKOSOA

Na Happiness Katabazi aliyekuwa Dodoma

WANAHARAKATI kutoka asasi zisizo za kiserikali nchini,wametakiwa wajikosoe wenyewe kwanza katika matumuzi ya fedha na rasilimali wanazopewa na wafadhali.


Rai hiyo imetolewa na Mchumi toka Idara ya Bajeti Wizara ya Fedha na Uchumi, Oswald Kyamani wakati akichangia mada ya mkutano mkuu wa asasi hizo ulioandaliwa na Pact Tanzania ambao uliofanyika kwa siku mbili New Dodoma Hoteli mjini humo.

Kyamani alisema kimsingi asasi hizo zimekuwa zikifanyakazi nzuri hali ambayo imesababisha hivi sasa baadhi ya watendaji serikalini wamekuwa na nidhamu ya matumuzi ya fedha na rasilimali ya mali ya umma na wameongeza uwajibikaji nakuongeza kuwa serikali itaendelea kuthamini mchango wa asasi hizo kwa lengo la kuliletea taifa maendeleo.

“Serikali hasa wizara yetu inautambua mchango wetu ila asasi hizi zimekuwa zikifichua mabaya tu yanayofanywa na baadhi ya watendaji na mazuri yanayofanywa na watendaji hao wamekuwa hawayasemi katika ripoti zao….kwahiyo sisi serikali tupo tayari asasi zenu zifichue ubadhilifu unaofanywa na watendaji wetu lakini na nyie asasi za kirai mmekuwa mkituhumiwa kwa ubadhilifu wa fedha mnazopewa na wafadhili sasa wakati umefika nanyie asasi za kiraia mjisafishe na mnyosheane vidole.

“Kwasababu huwezi kuinyoshea kidole serikali kwamba baadhi ya watendaji wa wilaya zake zimefanya ubadhilifu wakati katika hizo asasi zenu miongoni mwenu mnafuja fedha mlizopewa na wafadhili kwaajili ya kufanya shughuli za maendeleo katika tauifa hili”alisema Mchumi Kyamani.

Aidha alizishauri asasi hizo pindi zimalizapo kuandika ripoti zao za matokeo ya ufutiliaji wa matumuzi ya fedha za serikali waakikishe wanatengeza mtandao ambao utawawezesha kuzifikisha ripoti hizo katika idara yake ili ziweze kufanyiwa kazi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumamosi, Julai 3 mwaka 2010

HAPPINESS Vs Dk.GHARIB BILALI


Nikifurahia jambo na Waziri Kiongozi Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) ambaye pia ni mgombea kiti cha urais visiwani Zanzibar, Dk. Mohamed Gharib Bilal,nyumbani kwake Mazizini Juni 26 mwaka huu, ikiwa ni saa chache baada yake kiongozi huyo kurejesha fomu katika Makao Makuu ya CCM-Kisiwandu na kisha kwenda kuwashukuru mamia ya wafuasi na mashabiki wake katika viwanja vya Mwembekisonge wilaya ya mjini Magharibi.(Picha na Mhidini Sufiani)

TAYARI WAMEKWISHA ANZAA


Kushoto ni (Katabazi) na kulia Hellen Mwango tukiwa kwenye picha ya pamoja tuliyopiga kwenye bwawa la kuogelea katika hoteli ya New Dodoma Hoteli mapema wiki hii, ikiwa ni muda mchache baada ya mkutano mkuu wa asasi zisizo za kiserikali ulikuwa umeandaliwa na Pact Tanzania kumalizika.

TUNAWASIKILIZA PACT TANZANIA


Kulia ni mwandishi mwenzangu wa Habari za Mahakamani, Hellen Mwango toka gazeti la Nipashe,katikati ni mimi(Happiness Katabazi),Amina Juma (Daily news) tukifuatili kwa makini mada zilizokuwa zikiwasilishwa na wadau wa asasi zisizo za kiserikali katika Mkutano Mkuu wa mwaka, uliofanyika Juni 28-29 mwaka huu, New Dodoma Hoteli mkoani Dodoma, ambao uliandaliwa na Pact Tanzania.

VIONGOZI WA DINI MSITUFIKISHWE HUKO

Happiness Katabazi

NI kweli kwamba Ijumaa ni siku ya ibada ya waumini wa dini ya Kiislamu. Kwa mujibu wa dini yao, ibada yao wanasali saa saba mchana.

Wao hawachukui siku nzima ya Ijumaa kufanya ibada, wanasali mchana wakimaliza wanaendelea na kazi zao na waajiri wao wanawaruhusu kwenda misikitini kushiriki ibada.


Waislamu hawajaomba siku nzima ya Ijumaa iwe siku ya ibada, kwa hiyo ili mradi wanapata na kupewa fursa ya kwenda kusali misikitini siku hiyo haijazua jambo.

Siku ya Jumamosi ni siku ya ibada pia kwa Wasabato. Na kwa mujibu wa kanuni za Wasabato, siku nzima ya Jumamosi ni siku ya ibada kwa hiyo hawafanyi kazi kabisa, ikiwa ni pamoja na kutopika chakula kwa sababu wanaamini kupika chakula siku hiyo ni kazi.

Hawa Wasabato siku hiyo wanakula chakula kilichopikwa jana yake au wananunua vyakula hotelini.

Suala la Wasabato kutofanya kazi siku hiyo bado lina utata kwa sababu waajiri wengi katika sekta binafsi uitumia siku hiyo kama siku ya kazi. Na mara nyingi siku hiyo imekuwa ikitumiwa kwa ajili ya masomo na kufanya mitihani shuleni na vyuoni.

Nayo siku ya Jumapili imekuwa siku ya mapumziko duniani kote toka zamani hadi leo hii, pia siku hiyo ni siku ya ibada kwa madhehebu kadhaa ya dini ya Kikristo, ikiwa ni pamoja na Wakatoliki, Walutheri, Wapentekosti, Waanglikana na madhehebu mengine.

Kwa mujibu wa maelezo hayo, waumini wa makanisa hayo wanasali Jumapili. Siku hiyo si ya kazi kwa sababu waumini wa madhehebu hayo wanaamini Jumapili ni siku ya saba ambayo Mungu aliitumia kupumzika baada ya kazi ngumu ya kuumba ulimwengu kwa siku sita za juma.

Hata hivyo Wakristo wanafanya kazi siku hiyo ya Jumapili pamoja na ibada kuwepo. Haijawahi kutokea viongozi wa madhebu ya Kikristo hapa nchini kupiga marufuku waumini wao wasifanye kazi siku hiyo.

Sasa pendekezo lililotolewa hivi karibuni na baadhi ya viongozi wa dini za Kikristo wakiwamo baadhi ya maaskofu kwamba Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu, usifanyike siku ya Jumapili kwa sababu eti siku hiyo ni siku ya Wakristo kwenda makanisani kumuabudu Mungu wao, linajadilika na si lazima pendekezo hilo likubaliwe na serikali yetu.

Sawa, kama baadhi ya Waislamu wanavyodai Mahakama ya Kadhi ili nalo linatuelekeza huko huko kwenye kuanza kuiingiza dola katika kuendesha mambo yake kwa misingi ya kidini.

Natahadharisha kuwa mapendekezo kama haya yenye mwelekeo wa udini ni simema kwa taifa letu kwani yanaweza yakachochea hisia tofauti za kutoelewana kwa wananchi.

Ni vizuri sote, yaani viongozi wa dini na waumini wa dini zote tujielekeze kwenye kutafakari na kutoa mapendekezo yanayolenga kuleta maendeleo kwa taifa letu badala ya yale yanayolenga kutenganisha na kujenga uhasama miongoni mwetu.

Hivi sasa taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu, wananchi wanatamani viongozi wao wa dini wawe mbele katika kutoa elimu ya uraia na kupambana na unyang’au na wagombea wa nafasi za uongozi wenye hulka za unyang’au hasa rushwa katika uchaguzi.

Viongozi wetu wa dini wakielekeza nguvu zao kwenye hoja zinazo changanya na kuwagawanya wananchi kidini, wanalikosea taifa haki.

Tunategemea nguvu zao za ushawishi zitumike kuwanyoshea vidole viongozi wabovu na pia zitumike kifichua uovu unaowanyima wananchi maendeleo.

Kinyume cha hapo tutaamini kuwa viongozi wa dini wamekengeuka na kugeuka kuwa wapambe wa mafisadi.

Fukuto la Jamii linatoa rai kwa viongozi wa dini waende kuisoma vyema Ibara ya 19(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasema: “Kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.”

Sasa kwa wale viongozi wa dini waliotoa pendekezo la kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi ibadilishe kalenda yake kuhusu kufanyika kwa uchaguzi mkuu ambapo tayari Tume hiyo ya Uchaguzi imeishaipanga siku ya Jumapili ya Oktoba 31 mwaka huu, ndiyo siku Tanzania itafanya uchaguzi mkuu, watakuwa wanaikwaza serikali kutenda kazi zake kwani serikali yetu haina dini na kwa mujibu wa ibara hiyo inatamka wazi shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.

Kwa hiyo tunaona kupitia ibara hiyo, ombi hilo la baadhi ya viongozi wa dini ya Kikristo la kuomba uchaguzi usifanyike Jumapili kama ilivyozoeleka kwa namna moja au nyingine linaikwaza serikali, kwani ibara hiyo inaeleza wazi, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Juni 27 mwaka 2010

DK.BILAL:NITAPAMBANA



• AWAAMBIA WANZANZIBARI WAKIMTUMA,ATATUMIKA
Na Happiness Katabazi,Zanzibar

MGOMBEA anayewania uteuzi wa kiti cha urais visiwani Zanzibar, Dk. Mohamed Gharib Bilal, amekuwa wa kwanza kurejesha fomu yake huku akisema kwamba safari hii atapambana hadi dakika ya mwisho.


Dk. Bilal ambaye ni mara yake ya tatu kuwania uteuzi wa kiti hicho kinachoshikiliwa na Rais Aman Abeid Karume, alirejesha fomu jana majira ya saa nne katika ofisi ya Makao Makuu ya CCM Kisiwandui kwa mbwembwe, huku akisindikizwa na umati mkubwa wa mashabiki wake.

Wakati akirejesha fomu, Dk. Bilal ambaye ni Waziri Kiongozi Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), aliongozana na wake zake wawili.

Alisindikizwa pia na baadhi ya wazee wenye ushawishi wa siasa za Zanzibar, huku wengine wakimsubiri kandokando ya barabara kutoka katika ofisi hizo za Makao Makuu ya CCM, hadi katika tawi la wakereketwa la Kisonge, eneo la Michenzani.

Pia alisindikizwa na vijana waliokuwa kwenye msafara wa pikipiki zilizopambwa kwa bendera za CCM pamoja na vikundi mbalimbali vya burudani.

Akizungumza na wafuasi hao wa CCM waliokuwa wamevalia sare za chama chao, Dk. Bilal alisema kuwa kazi waliyomtuma ya kuchukua fomu na kurejesha, ameimaliza na kuwataka mashabiki wake kuwa na subira.

“Ndugu zangu, nawashukuru kwa michango yenu ya fedha za kuchukulia fomu, kazi mliyonipa nimefanya vizuri, tusubiri taratibu zingine zitakazoendelea ndani ya chama Inshallaah Mwenyezi Mungu atatusaidia, Amen,” alisema Dk. Bila huku akishangiliwa na mashabiki wake.

“Napenda kuwaeleza kwamba sikupata shida ya kutafuta wadhamini na nawaomba wote mnaoniunga mkono, mzidi kuomba Mungu mchakato umalizike salama na tukibahatika tutakwenda NEC. Mmenisubiri kwa muda wa miaka kumi, tumebakiza siku chache, nawasihi muwe wavumilivu,” alisisitiza Dk. Bilal.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika nyumbani kwake Mazizini, alipoulizwa atachukua hatua gani endapo CCM haitamteua kuwania kiti hicho, Dk. Bilal alisema safari hii atahakikisha anapambana hadi dakika ya mwisho kwa kuwa ridhaa ya kugombea nafasi hiyo kwa mara ya tatu imetoka kwa wananchi.

Akijibu swali kwamba atakubali matokeo kama atashindwa kwa haki, Dk. Bilal alisema yuko tayari kukubaliana na matokeo ya aina yoyote ile kama atashindwa kwenye kura za maoni.

Alipoulizwa kama kuna ahadi yoyote alipewa wakati alipowania kiti hicho mwaka 2005 na baadaye kushinikizwa kuondoa jina lake ili kumpisha Rais Aman Abeid Karume, Dk. Bilal alisema hakuna ahadi iliyotolewa pamoja na kwamba alijitoa kwa maandishi.

Alisema mwaka 2005 alipogombea urais wa Zanzibar, baadhi ya wanachama wenzake walimwona kana kwamba amefanya dhambi kubwa wakati alikuwa sahihi.

“Sikutenda dhambi na hata jina langu lilivyopelekwa kwenye vikao vya juu vya chama, walinisihi sana niondoe jina, nami nilifanya hivyo kwa maandishi lakini hadi leo sijajibiwa hiyo barua yangu, madai kwamba chama kiliniahidi cheo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, hizo ni hisia tu za watu,” alisema Dk. Bilal.

Hata hivyo alipoulizwa ni mambo gani atayafanya endapo atapatiwa ridhaa ya kuwaongoza Wazanzibari, Dk. Bilal alisema anategemea kufanya mabadiliko makubwa na kutekeleza yatakayoachwa na kiongozi aliyetangulia kwa mujibu wa ilani ya chama chake.

Alisema Zanzibar haina msisimko katika masuala ya maendeleo na kukuza uchumi, endapo ataingia madarakani, alisema, atahakikisha anavibadilisha visiwa hivyo ili viweze kwenda sambamba na nchi nyingine ambazo zimo katika Jumuia ya Afrika Mashariki.

Baadhi ya wazee wa Zanzibar ambao wamepata kushika nyadhifa serikalini, Abdul Razak Mussa (Kwacha), Hamidi Amiri Ally na Ibrahim Aman Ibrahimu, walisema kwa nyakati tofauti kuwa ndiyo waliomtuma Dk. Bilal kuchukua fomu kwani safari hii, ndiyo chaguo lao.

Wazee hao walitaka viongozi wa juu wa CCM, kusikiliza matakwa na si kufanya maamuzi yao kama walivyozoea katika miaka mingine ya kipindi cha kumtafuta mgombea urais kwa tiketi hiyo.

“Vikao vya NEC vinatakiwa kujua kwamba mchujo wa kwanza tunao sisi wazee wa mkoa huu na si vinginevyo,” alisema Abdurazak Musa Simai maarufu kwa jina la Mzee Kwacha.

Mzee Kwacha ambaye aliwahi kushika nyadhifa tofauti za juu katika kipindi cha rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, alisema kwa kuwa walishawahi kumpigia kura mara mbili na kushinda katika nafasi hiyo, wanaviomba vikao vya juu vya CCM, safari hii vimpitishe kwani hawataki kuongozwa na mtu mwingine.

“Sijatumwa kuzungumza maneno haya na mtu yeyote…hii ni mara yangu ya kwanza kuzungumza maneno haya, hata nikiwa katika shughuli za chama na serikali…nasema Dk. Bilal sasa apewe nafasi ya kuongoza kwani wananchi ndiyo waliomchangia fedha za fomu,” alisema Mzee Kwacha.

Mbali ya Dk. Bilal, wengine waliochukua fomu kuwania kiti hicho Zanzibar ni pamoja na Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha, Balozi Ali Karume na Naibu Waziri Kiongozi, Ali Juma Shamhuna.

Wengine ni Makamu wa Rais wa Serikali ya Muungano, Dk. Ali Mohammed Shein, Hamad Bakari Mshindo na Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mohamed Aboud Mohamed, Mfanyabiashara Mohamed Darammushi Raza, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amari, Harouna Ali Suleiman na Mohamed Yusuf Mshamba.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Juni 27 mwaka 2010