Happiness Katabazi
NI kweli kwamba Ijumaa ni siku ya ibada ya waumini wa dini ya Kiislamu. Kwa mujibu wa dini yao, ibada yao wanasali saa saba mchana.
Wao hawachukui siku nzima ya Ijumaa kufanya ibada, wanasali mchana wakimaliza wanaendelea na kazi zao na waajiri wao wanawaruhusu kwenda misikitini kushiriki ibada.
Waislamu hawajaomba siku nzima ya Ijumaa iwe siku ya ibada, kwa hiyo ili mradi wanapata na kupewa fursa ya kwenda kusali misikitini siku hiyo haijazua jambo.
Siku ya Jumamosi ni siku ya ibada pia kwa Wasabato. Na kwa mujibu wa kanuni za Wasabato, siku nzima ya Jumamosi ni siku ya ibada kwa hiyo hawafanyi kazi kabisa, ikiwa ni pamoja na kutopika chakula kwa sababu wanaamini kupika chakula siku hiyo ni kazi.
Hawa Wasabato siku hiyo wanakula chakula kilichopikwa jana yake au wananunua vyakula hotelini.
Suala la Wasabato kutofanya kazi siku hiyo bado lina utata kwa sababu waajiri wengi katika sekta binafsi uitumia siku hiyo kama siku ya kazi. Na mara nyingi siku hiyo imekuwa ikitumiwa kwa ajili ya masomo na kufanya mitihani shuleni na vyuoni.
Nayo siku ya Jumapili imekuwa siku ya mapumziko duniani kote toka zamani hadi leo hii, pia siku hiyo ni siku ya ibada kwa madhehebu kadhaa ya dini ya Kikristo, ikiwa ni pamoja na Wakatoliki, Walutheri, Wapentekosti, Waanglikana na madhehebu mengine.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, waumini wa makanisa hayo wanasali Jumapili. Siku hiyo si ya kazi kwa sababu waumini wa madhehebu hayo wanaamini Jumapili ni siku ya saba ambayo Mungu aliitumia kupumzika baada ya kazi ngumu ya kuumba ulimwengu kwa siku sita za juma.
Hata hivyo Wakristo wanafanya kazi siku hiyo ya Jumapili pamoja na ibada kuwepo. Haijawahi kutokea viongozi wa madhebu ya Kikristo hapa nchini kupiga marufuku waumini wao wasifanye kazi siku hiyo.
Sasa pendekezo lililotolewa hivi karibuni na baadhi ya viongozi wa dini za Kikristo wakiwamo baadhi ya maaskofu kwamba Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba mwaka huu, usifanyike siku ya Jumapili kwa sababu eti siku hiyo ni siku ya Wakristo kwenda makanisani kumuabudu Mungu wao, linajadilika na si lazima pendekezo hilo likubaliwe na serikali yetu.
Sawa, kama baadhi ya Waislamu wanavyodai Mahakama ya Kadhi ili nalo linatuelekeza huko huko kwenye kuanza kuiingiza dola katika kuendesha mambo yake kwa misingi ya kidini.
Natahadharisha kuwa mapendekezo kama haya yenye mwelekeo wa udini ni simema kwa taifa letu kwani yanaweza yakachochea hisia tofauti za kutoelewana kwa wananchi.
Ni vizuri sote, yaani viongozi wa dini na waumini wa dini zote tujielekeze kwenye kutafakari na kutoa mapendekezo yanayolenga kuleta maendeleo kwa taifa letu badala ya yale yanayolenga kutenganisha na kujenga uhasama miongoni mwetu.
Hivi sasa taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu, wananchi wanatamani viongozi wao wa dini wawe mbele katika kutoa elimu ya uraia na kupambana na unyang’au na wagombea wa nafasi za uongozi wenye hulka za unyang’au hasa rushwa katika uchaguzi.
Viongozi wetu wa dini wakielekeza nguvu zao kwenye hoja zinazo changanya na kuwagawanya wananchi kidini, wanalikosea taifa haki.
Tunategemea nguvu zao za ushawishi zitumike kuwanyoshea vidole viongozi wabovu na pia zitumike kifichua uovu unaowanyima wananchi maendeleo.
Kinyume cha hapo tutaamini kuwa viongozi wa dini wamekengeuka na kugeuka kuwa wapambe wa mafisadi.
Fukuto la Jamii linatoa rai kwa viongozi wa dini waende kuisoma vyema Ibara ya 19(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasema: “Kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.”
Sasa kwa wale viongozi wa dini waliotoa pendekezo la kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi ibadilishe kalenda yake kuhusu kufanyika kwa uchaguzi mkuu ambapo tayari Tume hiyo ya Uchaguzi imeishaipanga siku ya Jumapili ya Oktoba 31 mwaka huu, ndiyo siku Tanzania itafanya uchaguzi mkuu, watakuwa wanaikwaza serikali kutenda kazi zake kwani serikali yetu haina dini na kwa mujibu wa ibara hiyo inatamka wazi shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi.
Kwa hiyo tunaona kupitia ibara hiyo, ombi hilo la baadhi ya viongozi wa dini ya Kikristo la kuomba uchaguzi usifanyike Jumapili kama ilivyozoeleka kwa namna moja au nyingine linaikwaza serikali, kwani ibara hiyo inaeleza wazi, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la hiari la mtu binafsi.
Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Juni 27 mwaka 2010
No comments:
Post a Comment