Header Ads

UPELELEZI KESI YA WARAKA WA UCHOCHEZI WAKAMILIKA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi kusamba na kimiliki waraka wa uchochezi dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Mwenyekiti wa Democratic Party(DP) jana ulieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kwamba upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.


Mbele ya Hakimu Mkazi Michael Mteite, Mwendesha mashtaka Inspenkta wa Polisi, Francis Mboya alieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na anaiomba mahakama hiyo ipange tarehe ya upande wa mashtaka kuja kumsomea maelezo ya awali mshtakiwa.
Hakimu Mkazi Mteite alikubaliana na maelezo hayo na akaairisha kesi hiyo hadi Julai 27 mwaka, kesi hiyo itakapokuja kwaajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali ya upande wa Jamhuri.

Kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo Juni 21 mwaka huu, na wakili wa Serikali Angel Chacha aliyekuwa akisaidiwa na Inspekta Mboya alidai kuwa Mtikila alifanya makosa hayo ya uchochezi ambayo ni kinyume cha kifungu cha 32(1)(c) cha Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976.

Chacha alidai kuwa shtaka la kwanza ni kuwa mnamo Novemba mosi mwaka 2009-Aprili 17 mwaka huu, ndani ya jiji akiwa na nia ya uchochezi Mtikila alisambaza kwa umma waraka uliochapishwa ambao una kichwa cha habari kisemacho: ‘Kikwete kuangamiza ukristo, Wakristo waungane upesi wamuweke Mkristo Ikulu’ huku akijua maneno hayo ni ya kichochezi.

Alidai shtaka la pili ni kwamba Aprili 16, mwaka huu, huko nyumbani kwake Mikocheni bila kibali alikuwa akimiliki waraka huo wa kichochezi ambao ulikuwa na maneno hayo.
Kwa upande wake, Mtikila alikana mashtaka yote na wakili huyo wa serikali aliiambia mahakama kuwa hawana pingamizi na dhamana na kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hiyo ni mara ya 41 sasa serikali inamfungulia kesi ya kutoa maneno ya uchochezi na kesi nyingi ameshinda isipokuwa kesi moja ya uchochezi iliyokuwa imefunguliwa Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni mbele ya Hakimu Gabriel Mirumbe mwishoni mwa miaka ya 1990, ambapo Mtikila alidaiwa kutoa maneno ya uchochezi alipodai CCM ilimuua aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Horace Kolimba, na ndipo mahakama hiyo ya wilaya ilipomfunga jela mwaka mmoja na alitumikia kifungo hicho katika gereza la Ukonga.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Julai 7 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.