Header Ads

MTOTO WA KINGUNGE KORTINI KWA UTAPELI WA MIL.424/-

Na Happiness Katabazi

MTOTO wa mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Kombale - Mwiru, Tony Mwiru (36), jana alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na makosa ya kula njama, kuwasilisha nyaraka za uongo, kughushi na kujipatia sh milioni 424 kwa njia ya udanganyifu.


Mbele ya Hakimu Mkazi, Gabriel Milumbe, Mwendesha Mashitaka, Inspekta wa Polisi, Emma Mkonyi, alidai kuwa mshitakiwa huyo anakabiliwa na mashitaka manne.

Shitaka la kwanza ni la kula njama ambapo yeye na wenzake ambao hawakuwepo mahakamani jana, waliwasilisha nyaraka za uongo katika Kampuni ya SCI (TZ) Ltd na kujipatia sh 424,488,799.29.

Inspekta Mkonyi alidai shitaka la pili ni la kughushi. Katika shitaka hilo, Mwiru anadaiwa kughushi maombi ya ujumbe kasi wa kuamishia fedha wenye namba 17 wa Agosti 27 mwaka 2008, kwa nia ya kuonyesha ujumbe huo ni halali na ulitolewa na Savishankar Resman ambaye ni Mkurugenzi wa SCI (TZ), Ltd wakati si kweli.

Aidha, alidai shitaka la tatu ni la kuwasilisha nyaraka za uongo. Inadaiwa kuwa Agosti 29, mwaka 2008 katika Benki ya Barclays (TZ), iliyopo Mtaa wa Ohio jijini, mshitakiwa aliwasilisha nyaraka za uongo ambazo ni fomu ya maombi ya ujumbe kasi yenye namba E7 kwa mfanyakazi wa benki hiyo, Bitun Chiza.

Shitaka la nne ni la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ambapo inadaiwa kuwa Oktoba 9, mwaka 2008, katika Benki ya CRDB, Tawi la Kijitonyoma, alijipatia kiasi hicho kupitia akaunti namba 01j014293000, akionyesha Kampuni ya SCI (TZ), Ltd imeidhinisha ilipe kiasi hicho cha fedha kwa kampuni ya Temm Power Ltd.

Hata hivyo mshitakiwa alikana mashitaka yote na Inspekta Mkonyi alidai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika na kuomba tarehe ya kutajwa.

Baada ya kumaliza kusikiliza mashitaka hayo, Hakimu Milumbe alimuuliza mshitakiwa kama mzee Kingunge Ngombale - Mwiru ni baba yake, naye alijibu kuwa ndiyo.

“Ujue baba yako tunamheshimu sana, sasa kwanini wewe mtoto wake unajihusisha na mambo kama haya?” alihoji Hakimu Milumbe.

Mshitakiwa huyo amerejeshwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Agosti 18 mwaka 2010

No comments:

Powered by Blogger.