Header Ads

KIKWETE MGENI RASMI YA SHERIA LEO

Na Happiness Katabazi

JAJI Mkuu wa Tanzania Mohamed Chande Othman amesema rais Jakaya Kikwete leo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika siku ya sheria nchini ambapo wadau mbalimbali watapa fursa ya kujadili kauli mbiu ya sherehe hiyo isemayo “Adhabu mbadala katika kesi za jinai: Faida zake katika Jamii”.

Jaji Chande aliyasema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika katika Mahakama ya Rufani Tanzania jijini Dar es Salaam, wakati akitangaza rasmi kuwa leo ni siku ya Sheria nchini ambapo leo ni miaka 12 tangu ilipoanza kuazimishwa hapa nchini mwaka 1999 chini ya Jaji Mkuu Mstaafu, Francis Nyalali.

Jaji Chande ambaye alikuwa ameambatana na Msajili wa Mahakama ya Rufani Francis Mutungi mbaye jana ilikuwa ni mara ya kufanya mkutano na waandishi wa habari hapa nchini tangu alipoteuliwa na Rais Kikwete kushika wadhifa huo, alisema wadau mbalimbali akiwemo yeye wataijadili kauli mbiu hiyo kupitia hotuba zao ambapo aliwataka wananchi wengi kujitokeza katika sherehe hiyo ambayo ukutanisha viongozi wa mihimili mitatu ya nchini, wanachi wa kada tofauti na kwamba vituo vya mahakama kote nchini zinaadhimisha sherehe hiyo.

Katika hatua nyingine Jaji Chande alisema ili majaji na mahakimu waende na wakati katika kuendesha mashauri mbalimbali mahakama hiyo tayari imeanzisha utaratibu wa kuwapeleka majaji na mahakimu katika kozi fupi na endelevu katika Chuo cha Uongozi wilayani Lushoto. Na kwamba kila jaji atakayeteuliwa atalazimika kuudhulia kwanza mafunzo mafupi yatayomsaidia kuweza kutenda kazi yake ya kijaji.

“Hakuna mahakama isiyokosea ila kuna makosa mengine majaji na mahakimu wanaweza kuyaepuka hivyo ndiyo maana uongozi wa Mahakama hivi sasa umefikia uamuzi huo wa kuwapeleka kwa awamu majaji na mahakimu wake katika Chuo cha Uongozi Lushoto ili waweze kupata mafunzo na utaratibu huo umeishakamilika na mwaka huu, unaanza kutekelezwa kwa vitendo.

Alipoulizwa swali na mwandishi wa habari hizi ni kwanini kila mwaka sherehe ya siku ya sheria imekuwa ikifanyika kitaifa jijini Dar es Salaam, alisema hakuna sababu maalum inayoulazimisha mhimili kufanya sherehe hiyo hapa jijini ila mahakama italifanyiakazi jambo hilo kwa siku zijazo.

ChanzoGazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Februali 3 mwaka 2012.

No comments:

Powered by Blogger.