Header Ads

MAHAKAMA YA RUFAA YAKWAMISHA RUFAA YA ZOMBE





Na Happiness Katabazi

MAHAKAMA ya Rufaa nchini jana ilishindwa kuanza kusikiliza rufaa iliyokatwa na Mkurugenzi wa Mashtaka(DPP), Dk.Eliezer Feleshi dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam (ACP), Abdallah Zombe na wenzake kwa sababu jaji mmoja Semistockles Kaijage anayeunda jopo la majaji watatu anaumwa.

Rufaa hiyo ambayo ilikuja kwa ajili ya kuanza kusikilizwa chini ya jopo la majaji wa tatu wanaongozwa na Jaji Natalia Kimaro anayesaidiwa na Catherine Oriyo Semistocles Kaijage .

Upande wa mwomba rufaa(DPP), unawakilishwa na jopo la mawakili waandamizi wa serikali saba ambao ni Mgaya Mtaki, Timon Vitalis,Edward Kakolaki, Angaza Mwipopo, Prudence  Rwenyongeza ,Alexanda Mzikila na Peter Njike .

Wakati mawakili wajibu rufaa ambapo Zombe anatetewa na wakili maarufu nchini Richard Rweyongeza na washtakiwa wengine wanatetewa na mawakili Majura Magafu, Denis Msafiri, Deodoras Ishengoma ambao walisema wapo tayari kwaajili ya usikilizwaji wa rufaa hiyo.

Jaji Kimaro akiarisha rufaa hiyo alisema mwana jopo mmoja (Kaijage) ni mgonjwa hivyo rufaa hiyo haitaweza kusikilizwa jana na kwamba anaiarisha hadi pale pande hizo mbili zitakapojulishwa kwa maandishi na uongozi wa mahakama tarehe nyingine ya kuja kuisikiliza.

Agosti 17  mwaka 2008, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ilitoa hukumu ya kihistoria ya kesi ya mauji ya watu wanne iliyokuwa ikimkabili Zombe na wenzake ambapo jaji Salum Massati ambaye hivi sasa ni jaji wa mahakama ya rufani aliwaachilia huru Zombe na wenzake ambao walikuwa wakikabiliwa na kesi hiyo kwa maelezo kuwa upande wa jamhuri ulishindwa kuleta ushahidi mzuri ambao ungewea kuishawishi mahakama hiyo iwaone washtakiwa hao wana hatia.

Baada ya hukumu hiyo ya mahakama kuu, DPP hakulidhishwa na hukumu hiyo akaamua kukata rufaa mahakama ya rufaa kupinga hukumu hiyo Septemba mwaka 2008 kupinga hukumu hiyo ambayo kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya mahakama ya rufaa,rufaa hiyo ilikuwa imepangwa kuanza kusikilizwa jana lakini ikashindikana.

Mbali na Zombe, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Christopher Bageni, Ahmed Makele, WP 4593 PC Jane Andrew, D 1406 Koplo Emmanuel Mabula, D 8289 DC Michael Shonza, D. 2300 Abeneth Saro, D.4656D/Koplo Rajabu Bakari na D.1317D/XP Festus Gwasabi na jana washtakiwa wote walifika mahakamani hapo.

Washitakiwa hao walidaiwa kuwa Januari 14, mwaka 2006 waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini wa wilayani Ulanga, mkoani Morogoro; Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe pamoja na dereva teski Juma Ndugu, mkazi wa Dar es Salaam kwa madai kuwa walikuwa majambazi.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Desemba 12 mwaka 2012

No comments:

Powered by Blogger.