Header Ads

SILAHA ZA JADI ZAPOKELEWA KAMA KIELEZO KESI YA SHEIKH PONDA



Na Happiness Katabazi
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam ,jana ilipokea mapanga, Jambia, mabango,vipaza sauti,masufulia ,majenereta  kama kielelezo cha nane cha upande wa jamhuri katika kesi ya uchochezi na wizi wa malighafi zenye thamani y a sh.milioni 59 inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu ,Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake 49.
Uamuzi wa kuvipokea vielelezo hivyo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Victoria Nongwa baada kukubali ombi la wakili mwandamizi wa serikali Tumaini Kweka na Zuberi Mkakatu lilokuwa linaomba mahakama hiyo ipokee hati inayoonyesha idadi ya vitu hivyo iliyotolewa na shahidi wa kumi wa upande wa jamhuri Inspekta Thobias Walelo (34) ,ipokelewe kama kielelezo ambacho kinaonyesha vifaa hivyo vilivyokuwa vikitumiwa na washitakiwa hao wakati walipokamatwa wakiwa wamevamia na kuishi isivyo halali katika kiwanja cha Chang’ombe Markas ambacho ni mali ya kampuni ya Agritanza Ltd na siyo mali ya waislamu kama wanavyodai washitakiwa na kutupilia mbali pingamizi la wakili wa utetezi Juma Nassor lilokuwa linaomba hati hiyo isipokelewe.
Akitoa ushahidi wake Inspekta Walelo ambaye ni Mpelelezi mkuu wa kesi hiyo, alieleza kuwa alipokea jalada la kesi hiyo ilianze kulifanyiakazi ya upelelezi ambapo lilikuwa likihusiana na kosa la kuingia kwa jinai katika kiwanja hicho Oktoba 13 mwaka jana aliindikia barua  ofisi ya ardhi katika Manispaa ya Temeke ilikutaka kufahamu nani hasa ni mmiliki halali wa kiwanja cha Chang’mbe Markas na nilizipeleke mwenyewe.
Inspekta Walelo alidai kuwa Oktoba 14 mwaka jana ,kwa kuwa yeye ndiye mpelelezi mkuu wa kesi hiyo alienda hadi kwenye kiwanja hicho kupata uhakika na nilikuta umati wa watu ambao ni washitakiwa na niliueleza umati ule kuwa sikuwa na nia mbaya kwani nataka kupata ukweli wa nani hasa ni mmiliki wa kiwanja kile na ndipo umati ule ukamteua mwenzao mmoja ambaye ni Sheikh Hussein Ismail ili aweze kunipa majibu sahihi ambapo umati ule ulinijibu upo pale kwaajili ya kulikomboa eneo lao wanaolimiliki kihalali na kwamba nyaraka za kuthibitisha hilo wanazo na akamweleza Sheikh Hussein kuwa kuna mtu alifika kituo cha Polisi Chang’ombe kulalamika kuwa hicho ni kiwanja chake na kwamba wao wamevamia na kwamba akamtaka sheikh Hussein kesho yake afike kituoni waje kumpatia ukweli wa mmiliki halali wa eneo hilo ni nani.
“Ilipofika Oktoba 15 mwaka jana  kweli Sheikh Ismail na wenzake ambao Hamza Kambi, Sheikh Said Nyoni, Mkadamu Adhallah ambaye  ni mshitakiwa wa tano na Mbaraka Daluweshi na  kweli walifika asubuhi  na nilipowataka nianze kuwachukua maelezo yao ,masheikh hao wakasema hawapo tayari kuchukuliwa maelezo bila ya kuwepo wakili wao na wakaniomba niwaruhusu waende kumleta wakili wao kisha watarudi naye mchana ili ndiyo nianze kuwachukua maelezo:
“Niliizingatia kauli mbinu ya Jeshi la Polisi inayosema Utii wa sheria bila shuruti,niliwaruhusu waende kumleta wakili wao lakini cha kushangaza ilipofika huo mchana hawakurudi tena nikaamua kuwapigia simu zao na kuwakumbusha kuwa wanatakiwa warudi polisi wachukuliwe maelezo lakini walinijibu hawatarudi ng’o na wakanitaka eti mimi nirekodi yale niliyoongea nao asubuhi”alidai Inspekta Walelo na kusababisha watu kuangua vicheko.
Aidha Inspekta Walelo alieleza kuwa Oktoba 15 mwaka jana, alipota majibu ya barua yake yaliyokuwa yanayaka kufahamu nani ni mmiliki na manispaa ikamdhibitishia mmiliki wa kiwanja kile ni kampuni ya Agritanza na ndipo akaamua kutoa taarifa kwa viongozi wake wa juu ambao waliunda kikosi kazi ambapo usiku wa kuamkia Oktoba 17 mwaka jana, kikosi hicho ambapo yeye alikuwa miongoni mwao walifika eneo hilo ambalo washitakiwa hao walikuwa wameingia kwa jinai na kuwakamata washitakiwa wale ambao jumla yao walikuwa ni 50.
Aidha alieleza kuwa baada ya kuwakamata washitakiwa hao wakiwa na majambia, visu, vipaza sauti, viloba viwili vya unga wa sembe, mikeka,mabango, visu,sufulia ,ndoo za plastiki waliamua kuwabeba washtakiwa hao kwenye magari ya polisi kwa awamu mbili na kisha kuwapeleka katika kituo cha polisi Kijitonya ambapo waliwafikisha saa 12 asubuhi na kuanza kuwahoji ambapo waliwahoji hadi Oktoba 18 mwaka jana , washitakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo wakikabiliwa na kesi hiyo.
Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa mfululizo kuanzia Jumatatu wiki hii, inaendelea tena leo.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Februali 21 mwaka 2013.

  

No comments:

Powered by Blogger.