Header Ads

WAFUASI 53 WA SHEIKH PONDA WAFUNGWA JELA MWAKA MMOJA


Na Happiness Katabazi

HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es  Salaam, imewahukumu kwenda jela mwaka mmoja wafuasi 53 wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Sheikh Issa Ponda waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kula njama  na kufanya maandamano haramu.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Sundi Fimbo ambapo alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa  mshitakiwa Salum  Bakari Makame na wenzake 52 wanaotetewa na wakili wa kujitegemea Mohamed Tibanyendera walikuwa wakikabiliwa na jumla ya makosa manne ya kuandamana kwenda ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP),Dk.Eliezer Feleshi kumshinikiza ampatie dhamana Ponda kwani DPP ndiye ameifunga dhamana ya Ponda.

Hakimu Fimbo alilitaja kosa la kwanza ni la kula njama kutenda kosa kinyume na kifungu 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, kosa la pili ni la kufanya mkusanyiko haramu kinyume na kifungu cha 74 na 75 cha sheria hiyo  ambavyo vinasomwa pamoja na kifungu cha 43(2)(4) na 46 cha Sheria ya Jeshi la Polisi ya mwaka 2002.

Kosa la tatu ni la kukaidi amri ya jeshi la polisi iliyowataka watawanyike ambalo ni kinyume na kifungu 79 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu na kinachosomwa pamoja na kifungu cha 44 cha Sheria ya Jeshi la Polisi  ya mwaka 2002 na kosa la nne  ni la uchochezi ambalo lilikuwa likiwakabili washitakiwa watatu tu ambao ni Makame, Said Idd, Ally Nurdin Nandumbi  ambao wote hawa Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP), aliwafungia dhamana tangu walipofikishwa kwa mara ya kwanza mahakama ni hapo Februali 18 mwaka huu.



Hakimu Fimbo alisema ili kuthibitisha kesi yao upande wa jamhuri uliokuwa ukiwakilishwa na mawakili  waandamizi wa serikali  Serikali Bernad Kongora,Peter Ndjike,Zuberi Mkakatu na Joseph Mahugo na Nassor Katuga walileta jumla ya mashahidi 10  na upande wa utetezi walileta jumla ya mashahidi 54.

Hakimu Fimbo alisema mahakama yake kabla ya kutoa hukumu yake mahakama ilijiuliza maswali manne kuwa je washitakiwa walikula njama kutenda kosa?,walifanya mkusanyiko haramu?,walikaidi amri ya jeshi la polisi iliyowataka wasiandamane?na je walifanya uchochezi?

“Baada ya kujiuliza maswali hayo mahakama hii imefikia uamuzi wa kuwaona washitakiwa 52 walitenda kosa la kula njama isipokuwa mshitakiwa wa 48 (Waziri Omar Toli) hakutenda kosa hilo kwa sababu alikutwa akitoka kununua mabeseni, mahakama hii imewatia hatiani kwa kosa hilo kwani kwa mujibu wa vielelezo vilivyoletwa mahakamani yaani barua iliyoandikwa na Taasisi ya Jumuiya ya Maimamu kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam kuomba kibari cha maandamano na polisi wakawakataza ila wakaandamana, washitakiwa wengine walikamatwa na vipeperushi, mabango,vipaza sauti vinavyosema ‘Dpp ukristo utakuponza’:

“Kwa  vielelezo hivyo mahakama hii imeridhika kwamba walitenda kosa la kwanza, la pili na la tatu  na kosa la nne  ambalo ni la uchochezi mahakama hii imeona upande wa jamhuri umeshindwa kulithibitisha na kwasababu hiyo mahakama hii  imewatia hatiani kwa washitakiwa wote kwa makosa matatu isipokuwa mshitakiwa 48 ametiwa hatiani kwa kosa la tatu tu” alisema Hakimu Fimbo.

Akilichambua kosa la pili ambalo ni la kufanya mkusanyiko haramu, hakimu huyo alisema pia mahakama inamuachilia huru mshitakiwa wa 48 ,isipokuwa washitakiwa wengine wote wametiwa hatiani kwa kosa hilo kwasababu walikutwa katika maeneo tofauti wakitenda kosa hilo na katika utetezi wake walitoa walitoa ushahidi unaopishana ambao wengine walidai kuwa wa walikuwa wameenda kununua bidhaa,na walikuwa na fedha mfukoni lakini hata hivyo kiwango cha fedha walichokitaja polisi,na mahakamani ni tofauti ‘alisema hakimu Fimbo.

Hakimu huyo alisema kila kosa alilowatia nalo hatiani watalitumikia kifungo ha gerezani kwa mwaka mmoja,hivyo washitakiwa hao watatumikia adhabu ya mwaka mmoja jela.
Kabla ya hakimu kutoa adhabu, wakili wa serikali Komonya aliomba mahakama itoe adhabu kwa washitakiwa hao ili iwefundisho kwa wengine na kwamba upande wa jamhuri hauna rekodi zozote zinazoonyesha washitakiwa hao waliwai kushitakiwa kwa makosa ya jinai.
Kwa upande wake wakili wa utetezi Tibanyendera aliomba mahakama iwapatie adhabu ndogo washitakiwa hao kwani ni watu wanaotegemewa na familia zao na wengine tangu wakamatwe Februali 15 mwaka huu, wapo gerezani hadi leo hivyo muda wote waliokaa gerezani ni adhabu tosha na kwamba washitakiwa wengine ni wagonjwa na kwamba idadi ya washitakiwa ni kubwa na endapo ikipelekwa wote gerezani watakuwa wanatumia gharama kubwa za fedha za serikali kwaajili ya kuhudumiwa.
Kwa upande wake hakimu Fimbo alisema amezingatia maombi ya pande zote mbili na kwamba badala ya kuwahukumu kwenda jela miaka saba, anawahukumu kwenda gerezani mwaka mmoja na akasema yoyote ambaye ajaridhika na hukumu hiyo anaruhusiwa kwenda kukata rufaa mahakama ya juu.
Baada ya kumuliza kutoa hukumu hiyo, ndugu na jamaa wa washitakiwa hao waliigeuza mahakama na viunga vyake  ni sehemu ya msiba kwani walianza kuangua vilio kwa sauti ya juu.
Kesi hii ya kihistoria ilifunguliwa  rasmi Februali 18 mwaka huu na siku hiyo hiyo upande wa  jamhuri ukasema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na  Februali 19 mwaka huu,upande wa jamhuri uliwasomea maelezo ya awali washitakiwa hao na shahidi wa kwanza wa upande wa Jamhuri ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Hemed Msangi alianza kutoa ushahidi wake hadi Februali 26 mwaka huu, upande wa jamhuri ulipofunga ushahidi wake ,washitakiwa wakaanza kujitetea na Februali 19 mwaka huu, upande wa utetezi ulipofunga utetezi na jana mahakama ikatoa hukumu hiyo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Machi 22 mwaka 2013.

No comments:

Powered by Blogger.