Header Ads

WIZARA,NECTA ELIMU INAELEKEA WAPI?

Na Happiness Katabazi

SERIKALI kupitia Baraza lake lenye dhamana na mitihani (NECTA) imeshindwa kudhibiti uadilifu wa watendaji wake. Ithibati inajidhihirisha katika vitendo vilivyotamalaki vya uvujaji wa mitihani.

Pamoja na kwamba hiyo ni aibu na kashfa kwa kuwa uozo huo unahatarisha mfumo wa elimu na ubora wake kwa kuwaandaa watu mbumbumbu, hakuna hata mmoja aliyewajibika na anayeonekana kuwa na uelekeo wa kufanya hivyo, si Waziri mwenye dhamana wala viongozi wa NECTA, wote kimya, hali inayotoa uashirio kuwa mambo ni barabara.

Labda tujiulize, je, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, inaongozwa na mwanazuoni, Profesa Jumanne Maghembe, ambaye haoni wala kujua hatari ya kuvuja kwa mitihani?

Ingekuwa Tanzania ni taifa linaloendelea au linalotamani kupiga hatua kutoka katika hali yake ya sasa, Prof. Maghembe angelazimika kuwajibika pamoja na kufuatiwa kwa karibu zaidi na watendaji.

Lakini kwa kuwa Tanzania ni taifa limeamua kuishi gizani, waheshimiwa hao wanaendelea kupeta kwa kiburi kwa kuwa hata aliyewaitia kazi hiyo amenyamaza na hasemi jambo.

Sasa kana kwamba kashfa hiyo ya kuvuja kwa mitihani haitoshi, imeibuka kashfa nyingine kubwa zaidi na hadi sasa hakuna msimamo wala ufafanuzi wowote uliokwishatolewa.

Si nyingine, ni ile ya wahitimu wa kidato cha nne ambao walifaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza kutochaguliwa kuingia kidato cha tano katika shule za serikali kwa visingizio mbalimbali.

Kinachonishangaza zaidi ni kuona kuwa waliofauli kwa kiwango cha madaraja ya chini ya lile la kwanza (II na III) ndio wanaofanikiwa kupata shule hizo.

Viongozi wa wizara wamekuwa wakiwapatia wazazi wa wanafunzi hao majibu yasiyoridhisha, kwamba kuna awamu ya pili hivyo wametakiwa waandike barua kuomba nafasi za kuchaguliwa.

Sasa tatizo la jibu kama hili, linageuza kero kuwa kanuni. Mosi, hakuna tangazo lililotolewa nchini linalowataka wale ambao hawajachaguliwa waandike barua wizarani kuomba nafasi hizo.

Pili, utaratibu wa kujaza fomu za kuomba kuchaguliwa ‘selection form’ ambao umekuwa ukitumika, umetupwa, tumeamua kwamba watoto wawe wanaomba kuendelea na masomo kwa barua, tena shule za serikali, je huo ndio Utawala Bora ama Bora Utawala?

Hii njia iliyoamuliwa na Wakuu wa Baraza ni ya kifisadi na ni moja ya kero ya taifa katika awamu hii ya Rais Jakaya Kikwete. Iweje aliyefaulu daraja la kwanza alazimike kuomba kwa barua kuendelea na masomo licha ya kujaza selection form?

Wakati wenye daraja la pili, tatu na nne walichaguliwa kupitia selection form, iweje mtu akifaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza iwe tena ni adhabu, au ndiyo tumeamua kupalilia ujinga?

Hayo ni machache kati ya mengi yanayoashiria kuporomoka kwa kiwango cha elimu hapa nchini. Ni Wizara hiyo hiyo ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ndiyo inayosimamia mikopo ya wanafunzi, huko pia kuna vioja.

Mwanafunzi maskini ananyimwa mikopo wakati wale wanafunzi waliotoka kwenye familia tajiri wakipewa. Wakati huo huo wanafunzi ambao tayari maombi yao ya mikopo yameishadhibitiwa na kupewa mikopo mara moja, hujikuta wamekatwa na hawapelekewi tena mikopo bila maelezo yoyote.

Katika Bodi ya Mikopo ambapo fomu ya kuomba mikopo hutozwa fedha si chini ya sh 10,000-30,000, hivi hizo fedha wanalipa maskini au matajiri?

Tunaamini kuwa kutokana na matumizi yasiyo ya ulazima, kiasi kikubwa kinachotumiwa na bodi hiyo, kinaelekeza ndani ya bodi hiyo na kusahau maudhui ya kuundwa kwa chombo hicho.

Je, kwa aina hii ya matumuzi Watanzania tutafika?

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, April 29, 2009

No comments:

Powered by Blogger.